Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 28. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 28.

Ahadi tu.” Hiyo ndio ikawa mahari anayohitaji kwa binti yake. Kisha akaendelea. “Ahadi kutoka kwa Joshua kuwa atakuwa mwaminifu kwa Naya. Lakini, ikitokea macho yake yameona mwanamke mwingine, au akagundua hataweza kuishi tena na Naya, amepata mtu bora zaidi ya Naya, kabla hajaanzana na mwingine, tafadhali hitimisha na Naya kwanza. Ukiwa huna haraka ya kuanza kwengine, ukawa na nafasi, ningeshukuru kama utafanya kama hivi ulivyofanya leo, kuja kumchukua nyumbani, tukakabidhiana kwa amani, basi mrudishe kwa maelezo ya wazi utakayochagua wewe, tuagane kwa amani tu. Na wala usijifunge. Iwe ni kesho yake baada ya harusi au baada ya miaka 20, kumbuka kufanya hivyo. Jua Naya ni binti ya mtu. Anapo pakwenda. Pale Kiluvya ni nyumbani kwa Naya tena pako kwa maandishi kabisa.” Watoto wake wakiume wakashangaa na kumwangalia baba yao. “Hilo nilimuomba mama yao tokea yupo hai. Alipoanza tu kuugua. Tukakubaliana iwe hivyo. Ile nyumba ni ya Naya.” Bale akamtizama baba yake kwa mshangao zaidi. Ila hakuwa na chakusema.

Baba yao akaendelea. “Muda na wakati wowote uwe huru kumrudisha au hitimisha naye kwanza bila ugomvi au kumchanganya akili ndipo uje umuache. Au zile tabia za kurudiarudia habari za kuomba msamaha kila wakati, ukirudia jambo hilohilo, kisha ndio unamuacha na kuamua kuanzana au kuendelea na mwanamke mwingine! Hapana Joshua. Niwe hai au nimekufa, naomba Joshua, mrudishe binti yangu nyumbani kwa heshima tu au hitimisha naye kwanza. Niahidi hutaanzana na mwanamke mwingine yeyote, kabla hujamrudisha mwanangu nyumbani au niseme kuhitimisha naye rasmi. Usimzungushe katikati ya michezo ya ajabuajabu, itakayo eleweka kichwani kwako, na kuanza kumvuruga kwenye njia zisizofaa. Halafu yeye akabaki amevurugukiwa hapo katikati wakati wewe ukiendelea na chaguzi za maisha yako kwa furaha. Hitimisha naye. Muweke sawa. Ndipo uendelee na utakachokuwa umeamua. Ni hilo tu.” Palizuka ukimya mkubwa huo, kila mtu akabaki akitafakari.

“Hiyo ndio mahari ya Naya. Ahadi tu. Sitataka mali. Na kama utataka muda wakufikiria juu ya hilo, utakapokuwa tayari, karibuni nyumbani. Maana siku utakapokubali hili, ujue ni ahadi, na nadhiri uliyoingia kwa hiyari yako wewe mwenyewe mbele za Mungu na sisi tutakuwa mashahidi. Ujue Mungu hatakuacha, atakutizama ili akupatilize sawasawa na ahadi utakayoahidi juu ya hili. Maana nimemuomba kwa kufunga na kuomba asimame na mimi kwenye hili, na anisaidie kusimamia hili hata pale ambapo macho ya Naya na wengine yasipofika, yeye aonaye sirini, asimame na hili. Sitaki mali yeyote ile, ila ahadi tu.” Akajirudisha nyuma kabisa na yeye akatulia.

Mzee hajasoma wala hana mali nyingi kama wao, halafu mtulivu. Mkimya, akisikiliza kuliko kuongea. Lakini anacho kitu cha thamani wanachotaka. Na Naya mwenyewe akaongeza uthamani wa huyo mzee, hata kama hakubeba sura ya kitajiri kama wao, lakini usiku huo wote kimya, heshima, macho kwake. Mkimya. Ila siku hiyo akaongea kifasaha, akafikisha ujumbe wake. Hata kama haukuleta umaana kwa wengine, lakini yeye ndiye mwenye mali wanayo itaka, Naya. Akarudia ukimya wake, akimpa nafasi Joshua atafakari na aamue akiwa anaelewa anachotaka. Hata bibilia imeandika katika {Mithali 17: 27) Asiyesema sana ana maarifa. Mtu mtulivu ni mwenye busara. 28) Hata mpumbavu akinyamaza huonekana mwenye hekima. Akifunga mdomo wake huonekana kuwa mwenye akili.}

Umaana wake ukaongezeka katikati wa wasomi na matajiri hao. Joshua, Geb, baba Nanaa ambaye na yeye ni daktari na James. Halafu uje mama G. Mama mpambanaji. Anayejua kuzisaka pesa na zenyewe zikatii amri kwenye mifuko yake. Naye yupo hapo usiku huo mbele ya baba Naya, akimsindikiza Joshua kama mwanae akitaka kuoa binti yake. Wote mbele ya baba Naya wakitaka baraka zake katika hilo. Wakiwa wamejiandaa ipasavyo kutoa mali, chochote atakachotaka mzee huyo, walijua watammudu tu. Mzee wa Kiluvya! Walijua watamalizama tu, hawatashindwana. Lakini mzee hataki mali, ahadi tu. Wakatulia wakijua hata wao wapambe katika hilo hawana nafasi tena. Kazi kwa Joshua.

Kwa aina ya maisha aliyonayo huyo baba Naya, na vile anavyomjua na kumuona Joshua alivyofanikiwa, pamoja na hali nzuri za maisha za hao  watu wanao mzunguka huyo Joshua, ungeweza kufikiri hapo ndipo angeponea. Kwamba ataje mahari kubwa sana, alipwe na kuanza biashara yake, lakini bado mzee amesimamia masilahi ya mwanae. Hakutaka aje atendwe tena kama alivyoishi na Malon akimuona akilia kila wakati sababu ya usaliti. Akaona aweke dhiki zake pembeni, mtaji wa biashara anayotaka kuanza, usubiri kwanza, mwanae kwanza.  Hata wao walimuheshimu, hawakutegemea.

Geb, mama G, Nanaa na James wakakumbuka hekaheka ya mahari ya Nanaa iliyosababisha vurugu, na pesa nyingi sana kumtoka Geb mpaka kumuoa Nanaa. Nanaa akainama kabisa akiumia jinsi yeye alivyoozwa kwa mapesa mengi tena kwa kudaiwa kwa aibu kabisa! Akabaki ameinama tu akimtafakari mama yake mkubwa na kuanza kuona bahati aliyoipata Naya yakupata mzazi anayesimama naye mpaka na utu uzima huo! Geb akamuona vile alivyojiinamia. “Hata wakitaka mahari nyingine tena, mimi nitalipa tu, ilimradi ubaki kuwa wangu.” Akasikia Geb akimnonng’oneza sikioni. Nanaa akajua Geb amemgundua. Akamwangalia na kutoa tu tabasamu, akarudi kujiinamia. Geb akamvuta karibu. Wote wakawagekia wao, walikuwa wamekaa kochi moja. “Samahanini.” Geb aliyesababisha hilo akaomba radhi kwa sauti ya chini. Wakatulia.

  Joshua akaanza. “Sababu kubwa ya kuomba Geb na Nanaa wawe karibu na sisi nikimaanisha mimi na Naya, japokuwa Naya hawafahamu vizuri ni vile walivyoweka uthamani wa ndoa. Nimejifunza kutoka kwao kuwa ndoa ni zaidi ya hisia.” Joshua akaanza. “Sikuwa nikimjua Naya. Sikumfuata Naya kwa tamaa ya urembo wake au uzuri wake tu, ila ni zawadi Mungu amenipa. Na ninashukuru Mungu kunipa mwanamke ambaye mpaka sasa kwangu Naya ameendana zaidi na kile nilichofikiri nahitaji kwa mwanamke, lakini Mungu amenipa na zaidi.”  Joshua akaendelea.

“Nakuahidi mzee wangu, Naya atarudi nyumbani kutembea tu. Hapa ni nyumbani kwa Naya na watoto Mungu atakao tujalia.” “Wao!” Nanaa akasikika kuhamasika mpaka akanyanyua na kichwa. “Nakuahidi nitamuheshimu Naya. Si kwa ajili yake tu, hata yangu mwenyewe. Siwezi kuchezea kitu alichonipa Mungu kwa heshima kiasi hiki! Hapana, sio mimi. Najua vitu anavyonipaga Mungu mwenyewe, na huwa ananipa uwezo wa kuvitunza. Nitampenda Naya, kama nafsi yangu. Akirudi nyumbani, basi ujue ni kwa muda tu, na mimi nitakuwa nikimsubiria nyumbani, kama sitakuwa naye.” Mama G akapiga kigelegele kidogo kisha akanyamaza. Wakacheka.

“Sina tamaa za wanawake. Nimejawa hofu na kiumbe mwanadamu, kwa jinsia yeyote ile, ni mpaka Mungu aniruhusu niwe naye karibu ndipo nafanya mahusiano naye. Imekuwa hivyo na sitabadilika kwa Naya. Kwa hiyo nakuahidi mzee wangu, Naya atabaki peke yake kwangu, mpaka kifo changu na Mungu anisaidie.” “Kutoka kwenye midomo yako mwenyewe, mpaka kwenye sikio la Mungu.” Baba Naya akaongeza na kuendelea. “Nakukabidhi Naya.” Akamalizia hivyo tu baba Naya. Joshua akanyanyuka na kumpa mkono kwa heshima sana akimshukuru. Hapo hata Nanaa akapiga kigelele akisaidiana na mama G. “Tunashukuru Mzee wetu.” Wote wakampa mkono baba Naya kama kumshukuru.

“Kwa baraka hizo mzee wangu, basi mipango ya harusi inaanza rasmi. Ili kukamilisha hili.” Akaongea Geb. Wakaelewa ndiye anayesimamia hilo jambo. Wakati wakipeana mikono, Joshua akatoka hapo kwa haraka na kurudi na champaign mkononi pamoja na glasi nzuri nyembamba katikati ya vidole vyake akiwa amezipishanisha mkiani ili zisianguke. Naya akasimama kwa haraka kumpokea zile glasi. “Asante.” Akamshukuru Naya akimkabidhi. “Naombeni tumshukuru Mungu wangu kwa hili jamani. Hii champaign ni moja ya champaign nilizonunua miaka mingi nikitafutia sababu ya kunywa. Maadamu mpaka sasa naona mkono na baraka za Mungu juu yangu katika hili, naomba tunywe rasmi na kufurahi tukimshukuru Mungu wangu kwa kutenda kwake kwa muujiza.” Naya akaanza kugawa zile glasi kwa kila mmoja pale wakati Joshua akifungua ile chupa ya champaign. “Jamani huyu Mungu, humpa amtakaye na wala hakuna wakumuuliza kwa nini!” Joshua akamalizia akionekana kufurahia kweli! Akawamiminia kila mtu kwenye glasi, wakicheka na kupongezana. Wakagonganisha glass zao kwa furaha. 

Nanaa kwa Baba Naya.

Wakashangaa Nanaa anaenda kupiga goti mbele ya baba Naya na kumpa mkono pale alipokuwa amekaa. Naaa akaona goti moja halitoshi, akapiga yote mawili. “Hakika nimekuheshimu baba Naya. Na nikakupenda zaidi.” “Kwa nini Nanaa, binti yangu?” “Natamani na mimi ningepata nafasi kama aliyonayo Naya, kuwa na baba aliyenilea kama wewe, na kunitoa kwa heshima kubwa namna hii! Hakika nimeona wivu.” Wote kimya. “Kama Mungu hakuwa ameniandikia Geb, mwanaume anayejua anachokitaka, na kukipigania, pengine mpaka leo ningekuwa kwa kaka James, sijaolewa. Lakini Geb, kaka James na huyu mama ambaye ni mama Mungu aliyenipa, walipigana mpaka leo na mimi nina ndoa. Kwa hakika umenigusa baba Naya.” Nanaa akaendelea.

“Kwa kutokujua kwangu nikifikiri ni kawaida au watu na mambo yanafanana, nilikuwa nikimtania Joshua nikimwambia aandae hundi nzito kwa mahari kwa vile alivyokuwa akimsifia Naya kwetu, nikamwambia baba yake hawezi kumtoa kwa pesa ndogo kama kweli sifa hizo zote anazo na ni mtoto wa baba kama hivi Liv kwa Geb. Nikamwambia ajiandae haswa. Tena Geb akasema wazi kabisa kuwa, hakuna mwanaume hapa duniani anaweza kuwa na pesa yakuja kumlipia Liv kwake. Tukacheka, tusielewe tukijua ni mapenzi tu ya Geb kwa Liv, lakini kwa hiki ulichokifanya sasa hivi wewe, ndio nimeelewa Geb wangu alikuwa akimaanisha nini. Lakini mimi nilikuwa nikimwambia Joshua nikijifananisha na Naya,  kule mimi nilikopitishwa kipindi kama hiki nikitaka kuolewa, na uwezo alio nao Joshua! Kweli wewe huna tamaa, baba Naya! Na Mungu wa mbinguni hatakupungukia. Ni heshima kubwa sana umempa Naya. Pengine yeye anaweza asione, lakini mimi imenigusa sana.” “Naona Nanaa.” Naya akajibu taratibu.

“Basi Mungu akusaidie usisahau Naya. Mimi niliuzwa, baba Naya! Niliuzwa kama mtumwa! Tena kwa thamani ya magari zaidi ya mawili au matatu kama ni haya ya kawaida. Nikafanyiwa mengi mno. Uchawi, ndoa kuwekewa vipingamizi, ili tu Geb alipe pesa zaidi, na mengine mengi. Halafu sasa, mahari hiyo ya mamilioni inadaiwa, ilipwe TENA, baada ya mahari ya kwanza, mimi nipo hospitalini wameniloga na kunipa ugonjwa wa matende ambao haujawahi kuonekana hapa duniani.” “Pole.” “Baba Naya, wanamdai pesa Geb. Niseme mamilioni ya pesa, nikiwa navuja maji laliyochanganyikana na usaha, miguu inamalengelenge kama niliyeungua, lakini ikavimba, mimi mwenyewe nilikuwa siwezi kuitizama. Geb alishakuwa amenizalisha mtoto mmoja, huyu Liv. Kwa kifupi sikuwa na thamani ya mapesa yote hayo waliyokuwa wakimdai Geb.” “Kwangu ulikuwa na hiyo thamani na zaidi Nanaa. Usiseme hivyo hata kidogo! Ile pesa ni thamani ndogo sana waliyokuwa wameiweka kwako. Hulinganishwi hata kidogo na ile pesa.” Akaongeza Geb. Nanaa akaanza kulia.

Mimi sikupenda Geb. Natamani heshima hii anayopata Naya na mimi ningepata, sio kupata heshima kutoka kwa watu baki kama wewe, mama hapa na kina Grace! Walimzungusha kaka kwenye swala la mahari mpaka kaka akakonda kwa mawazo! Nipo hospitalini nikiwa sijulikani hata tiba gani nipewe, huku kaka anapambana na maswala ya mahari!” “Basi hapo sasa Nanaa wanao wote wataamka bwana waje waanze kulia na wewe hapa! Ni nini lakini? Umeanza vizuri, unataka kuniamshia watoto sasahivi!” Mama G akalalamika Nanaa akaanza kucheka huku akifuta machozi.

“Pole mama. Pole sana.” Baba Naya naye akamtuliza. “Mimi ninachotaka kusema nimekupenda na kukuheshimu baba NayaNakuombea baraka baba yangu, Mungu wetu wa mbinguni asikupungukie.” “Amina mama.” Akapokea baba Naya. Baba mzazi wa Nanaa kimya kama James.

“Wala Nanaa hajakosea. Kuna mwenzio amejengewa nyumba kabisa kwa ajili ya huyuhuyo Nanaa. Ana biashara mpaka leo, na zinaendelea vizuri tu hapa mjini kwa ajili ya huyuhuyu Nanaa. Hata mimi umenishangaza baba Naya. Kama anavyosema Nanaa, Mungu akubariki. Hapa nilikuwa nimeshajiandaa na kumwandaa Grace, pacha mwenzake huyu Geb, yeye yupo Arusha na familia yake. Hivi leo tu ameshindwa kuja sababu mtoto mgonjwa. Ila nilishamwandaa kwa ajili ya mahari yake huyo Naya. Nishampa orodha ya vitu vile ninavyojua havikosekani kwenye mahari za makabila mengi hapa Tanzania. Nikamwambia atusaidie kuanza kununu wakati sisi tukijiandaa kwa vikubwa. Halafu Joshua na huyu mwenzie Geb wao pesa. Nilimwambia Geb na Joshua wajiandae kipesa haswa, ili tena wasitukwamishe. Ukitaja tu pesa unayotaka kwa mahari, tukupe bila kukuchelewesha. Muulize Joshua huyo.” “Ni kweli tulijiandaa kwa pesa nyingi tu.” Akaongeza Joshua.

“Sio kwa Naya. Nimeshaona madhara ya pesa zikichanganywa na mapenzi hapo! Zinakuwa chungu kwelikweli. Unashindwa kujua kama zimekuwa msaada au laana! Hata chakula kilichonunuliwa na hizo pesa kinakuwa si kitamu, unaishia kufunga tu, na hujui umwambie nini Mungu! Hapana. Si kwa Naya. Naomba hiyo thamani ya pesa muibadili kwa kumpenda binti yangu. Kwa muda mfupi nimekuwa na nyinyi hapa, nimeshaona umoja mlio nao. Upo na nguvu mno. Mumpokee Naya kwa heshima tu, na mumvumilie kwa madogo mtakayokutana nayo kwake. Mkumbuke na yeye ni binadamu. Kama hivi mama G ulivyompokea Nanaa, basi mpokee na binti yangu. Mumsaidie kama hivi leo mlivyofanya hapa kutengeneza mazingira mpaka akafanikisha kukarimu wageni kwa ustadi. Najua itamsaidia na Joshua kuweza kuwa katikati yenu vizuri.” “Kwa nilivyomuona Naya na kumsikia, huyo mbona ameshakuwa wetu, wala usijali baba Naya. Ukimsikia analia sababu ya mama G, ujue ni kwa wema.” Nanaa akaanza kucheka.

“Na ujiandae Naya. Mama hajui kuficha. Atakwambia tu. Tena atakwambia bila kukuficha. Mimi nalia na kununa, lakini sina jinsi.” Angalau watu wakaanza kucheka na kutaniana. Mpaka kina Magesa, James ambaye ni kaka yake Nanaa na ndiye aliyemlea tokea kachanga, aliyekuwa kimya tu muda wote maana mama yeke ndiye huyo aliyekuwa akizungumziwa hapo. Aliyechukua mapesa mengi na kuzuia ndoa ya Nanaa. Na baba yake mzazi Nanaa ambaye alikuja utuuzimani baada ya kukataa mimba ya mama Nanaa alipokuwa binti mdogo, wote wanafunzi, walipoondoka.

Mpaka wanaachana hapo, tayari Naya alishawazoea na kupanga nao mipango mingi tu yakuja kukutana tena siku za karibuni na kubadilishana namba za simu. Naya na Nanaa wakawa wametengeneza ukaribu kwa urahisi sana kitu kilichomfurahisha sana Joshua kuona Naya naye amewakubali na kuwafungulia moyo kwa kiasi hicho.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Waliwaacha familia ya Naya hapo nyumbani kwa Joshua. “Naona leo nimepata mambo mawili kwa wakati mmoja.” Naya akaanza waliporudi tu ndani baada yakuwasindikiza. “Umenivalisha pete. Na kunipa familia nzuri ya kina Magesa. Hakika nimewapenda.” “Nimekuona.” “Nimefurahi sana. Ukiwa na wale watu, huwezi kuwa mpweke. Wanaleta uwepo fulani hivi, hujisikii kupungukiwa. Kukiwa na tatizo wanasema letu na hapohapo wanatafuta suluhu! Mpaka wamenishangaza wakati nipo nao kule ukumbini! Yule mama mwepesi na akili yake ipo haraka kufanya mambo!” “Unafikiri hata swala la kuoa nimepata shida kuwaomba! Nilipomwambia tu nimepata mchumba. Akalibeba hilo jambo kama mimi ni mtoto wake wakunizaa. Na usimuone vile. Anakauli sana kwa wanae. Huyo Geb na Grace!” “Eeh?” “Wanamsikiliza sana. Akisema jambo, wanatekeleza tena kwa pamoja. Sasa mume wa Grace naye amekuwa kama Nanaa, akaweza kuingia katikati yao, utapenda kuwa nao. Nanaa na Man, mume wa Grace ndio watundu kuliko watoto wa mama G.” “Kwamba na Grace ni mpole kama Geb!?” “Hivyohivyo. Ongea yake kama hivyo Liv. Mtulivu sana. Ila mumewe, ndio mtacheka mpaka machozi. Mtundu sana. Maneno yake ya utundu mno. Ila sasa Grace yeye hakubahatika mtoto muongeaji kama Magesa.” Wote wakacheka walipomkumbuka Magesa.

“Ukweli ni watu wazuri sana. Wanaonekana kukubeba, kama mtoto aliyezaliwa na mama G!” Akasifia baba Naya. “Na ndivyo anavyonichukulia huyo mama, mpaka najisikia vizuri.” “Mimi nimewapenda sana. Na nimewafurahia. Asante Joshua.” Naya akaongeza. “Karibu. Sasa kabla hamjaondoka, naomba ni mzungushe rasmi Naya kwenye hii nyumba. Najua mmechoka, ila naomba mnivumilie tu. Ni sawa baba yangu?” “Bila shida.” Akajibu baba Naya. Joshua akamshika mkono Naya akimuongoza. Zayoni akaomba na yeye azunguke aangalie. Joshua akawakaribisha wote kama wangependa. “Najua mmechoka. Ila atakayependa kuongozana nasi, karibu.” Wote wakawa wamehamasika, hakuna aliyelalamika kuchoka. Wakaongozana pamoja. Joshua akawazungusha mpaka juu vyumbani nakuwaacha wakishangazwa na maendeleo yake.

“Kuna sehemu ya mwisho naomba Naya aiangalie.” Naya akakunja uso akicheka. “Nilifikiri umetuzungusha kila mahali!” “Bado. Sehemu hiyo nimeiacha maalumu kwa sababu nataka kukuomba kitu.” “Nini tena?!” “Twende.” Akamshika mkono wengine wakafuata nyuma mpaka nje. Wakatokea mlango wa ukumbini. Wakajikuta nyuma ya hiyo nyumba. Napo pakawatoa macho zaidi. Palijengwa  vizuri sana.

“Hakika umejenga hii nyumba kwa hali ya juu Joshua!” “Nashukukuru mzee wangu. Nilitaka kumuomba rasmi Naya kama atakubaliana na ombi langu kuwa harusi yetu tufunge hapa. Najua leo nimemshitukiza na mambo mengi mpaka na wasimamizi wa harusi kabisa, lakini kuanzia sasa, hakutakuwa tena na suprise juu ya harusi yetu. Nitakushirikisha.” “Suprise zote mpaka sasa nimezipenda. Nimempenda Nanaa. Hujakosea hata moja.” Joshua akacheka kwa kuridhika.

“Unafikiri nakutania Joshua? Na kama Nanaa ndiye atanisimamia harusi, sina malalamiko kabisa. Nitakuwa na mfano mzuri sana wakuiga. Aisee ni kweli wanapendana wale watu. Geb na Nanaa! Aisee mwisho. Mimi nilikuwa nikiwaangalia  kwa kujiiba! Mpaka nikawa nawafurahia.” “Nilijua tu ungewapenda.” “Haya turudi kwenye suprise ulizonifanyia. Pete yangu nzuri, tena sana. Japo inatakiwa kubanwa kidogo. Inanipwaya.” “Hilo ni jambo la kwanza siku ya jumatatu.” Akajibu Joshua. “Basi ujue hujakosea suprise hata moja. Zote ni nzuri na ninakushukuru sana.” Joshua akacheka, wengine kimya wakiendelea kuangaza macho.

“Na kuhusu hapa? Maana nataka kuacha historia hata kwa watoto wetu na vijukuu waone sehemu tuliyoweka historia. Maana haya makumbi huwa wanabomoa na kubadilisha majina, ila hapa patabakia kwa muda mrefu. Silazimishii. Kama kuna mahali ulishakuwa na ndoto za kuja kufungia ndoa, sitapinga.” Naya akajisikia vizuri. Ndugu zake wote wakabaki kimya wakiendelea kuangaza macho, huku wakisikiliza. “Sizani kama tutapata sehemu nzuri kama hii Joshua! Hapa ni pazuri sana na sababu uliyotoa ni kweli na ya msingi. Tufanyie tu hapahapa. Ila mwenzio bado nipo kwenye mshituko kwa yote yaliyotokea leo! Bado siamini!” Naya akajiangalia kidoleni tena.

“Umeipenda?” “Sana. Na zaidi ni kwakuwa inatoka kwako Joshua! Sikutegemea! Maana ni kama hukua tayari!” “Hapana Naya. Wewe siku ile ulikaribia kuniharibia suprise yangu. Ila nikashukuru ukatulia.” Naya akacheka. “Ila ungeendelea vile siku ile, nilijiambia nisingekuacha umepoa vile. Ingebidi kukwambia tu. Lakini nilipoona umekubali ninyamazie tu lile, nikamshukuru Mungu. Maana siku ile niliingia nchini mapema zaidi ya muda ule uliponiona pale ofisini. Nilimuomba mzee hapa tukutane mbali na nyumbani tuzungumze. Ndipo nikamuomba kama ataniruhusu nikuoe. Tukazungumza vizuri. Tukawekana sawa, mpaka tukapata na muda, akaniombea mimi kama Joshua! Ndipo nikaja kukuchukua kazini.” “HAIWEZEKANI Joshua!” “Muulize mzee hapa. Ni nyinyi tu ndio mlikuwa hamjui kinachoendelea ila nilimuomba asiwaambie wote nyinyi.” Naya akamwangalia baba yake.

“Nini?” Baba yake akamuuliza. “Mimi nilijua hunifichi kitu!” Naya akaongea akilalamika kidogo kwa baba yake. “Ni kwa uzuri mama. Huoni jinsi ulivyofurahia?” “Sana. Nimefurahi sana baba. Nampenda Joshua.” Wakacheka. “Hata mimi nakupenda Naya. Naamini tutakuwa na ndoa nzuri sana. Umetulia na umejawa shukurani. Huna makuu. Namshukuru Mungu kwa ajili yako.” “Asante kwa heshima kubwa uliyonipa leo! Mbele ya watu wote wale! Zaidi kwa baba yangu! Unamuheshimu sana baba yangu mpaka nafurahi. Hakika sikutegemea kila kitu ulichofanya! Nashukuru.” Naya akajisogeza karibu akataka kusahau kama baba yake yupo hapo. Joshua akacheka akimwangalia kama anayemkumbusha. Naya akaelewa akaishia kumkumbatia kwa pembeni. “Naoana sisi utusaidie usafiri wa kurudi tu, Joshua. Naona usiku umeendelea sana.” Naya akacheka akajua amekamatwa. Na Joshua akacheka. “Bila shaka mzee wangu. Nakushukuru sana kwa kuniamini na Naya. Asante sana.” “Nawaombea.” “Asante baba.” Na Naya naye akashukuru.

Akawagekia Bale na Zayoni. “Na nyinyi nawashukuru sana kusimama na sisi leo kufanikisha hili. Mmejituma vyakupitiliza. Asanteni sana.” “Mimi nimefurahi Joshua. Na nimepiga picha nyingi sana.” Akadakia Zayoni. “Nimekuona. Nashukuru sana Zayoni. Ujue uwepo wako hapa ni muhimu sana.” “Kweli?” “Kabisa. Unafikiri Naya angejisikiaje yote haya yanaendelea kwenye maisha yake halafu wewe haupo hapa?” “Kweli isingekuwa vizuri.” Wakacheka.

“Kama tulivyozungumza na baba, kesho wote na kina Magesa tutakuwa kanisani kwenu kujitambulisha kwa mchungaji, kisha nyumbani kwa kina Magesa. Angalau na nyinyi mpafahamu kwao kama walivyoomba.” “Yaani yote hayo mmepanga na baba!?” Naya hakuwa akiamini. “Kabisa. Baba amenisaidia sana. Majukumu yote yakuzungumza na mchungaji, kumwambia kesho nakwenda kukuchumbia kanisani ameyachukua yeye, amesema atanisaidia huko ili mimi akili itulie hapa.” Naya akatulia kama anayetafakari. Wakamuona anacheka.

 “Nini sasa?” “Siamini kama kwenye lile kanisa na kwenyewe watashuhudia kitu kizuri kinatokea kwenye familia yetu!” Wote wakacheka. “Nakushukuru Joshua. Hakika nashukuru kwa hii heshima. Mungu akubariki mpenzi wangu.” “Sisi sote. Naamini tutamaliza mambo yote salama.” Wakazungumza kidogo. Wakakubaliana kwa hili na lile na kutoka wakikubaliana hata Bale atawasaidia kuimba ule wimbo siku ya harusi yao. Kwamba waimbe wao watatu. Joshua, Naya na Bale. 

Busu la Uchumba

Wakaingia kwenye gari, Joshua akawasha gari kabisa akawa ni kama amesahau kitu. “Naya?” Akageuka. “Naomba tushuke mara moja, kuna kitu nataka tuzungumze ndani. Sitakawia mzee wangu.” “Bila shaka.” Akaafiki baba Naya bila shida. Naya akashuka mara baada ya baba yake kuridhia. Joshua akaenda kumfuata na kumshika mkono. “Twende.” “Umesahau nini!?” Joshua akamwangalia na kucheka kidogo. Wakarudi mpaka ndani. Akamuongoza kupandisha ngazi mpaka juu kabisa chumbani kwake na kufunga mlango kabisa.

“Ni nini?” Naya akauliza na cheko kidogo. “Nimetafuta nafasi ya kupata busu, nimekosa. Kila wakati kumekuwa na mwingiliano. Leo ni siku yetu Naya. Mwenzio kwa mara ya kwanza, rasmi na baraka za wazazi ninajulikana na watu nina mwanamke wangu! Siwezi kuacha siku kama hii Mungu aliyoniandikia historia ipite hivihivi  bila kupata busu kutoka kwako!” Naya akacheka na kumsogelea.  “Yaani unamsubirisha baba Naya garini kwa busu tu!?” “Nimeomba anipe muda kidodgo, nipate hii nafasi ya pekee.” Akampokea vizuri kwa kumshika kiunoni. Safari hii hata Naya aliona utofauti wa jinsi alivyomshika. Alihakikisha amemkumbatia mpaka mikono yake imeelewa kuwa imegusa mwili wa Naya. Akampa mabusu mazito mpaka Naya akayasikia. Kisha akawa na kiasi, akamwachia. “Angalau moyo wangu umeridhika. Nimepata nilichokuwa nikikitamani.” Akaongea Joshua akijaribu kuweka sawa nywele za Naya.

“Napenda hivyo unavyonichezea nywele huku ukinibusu! Nasikia raha.” Joshua akacheka na kumbusu shavuni. “Twende tusimuweke mzee muda mrefu zaidi. Umesema unaamini Mungu atatujalia ipo siku na sisi tutakuwa na usiku wote sisi wenyewe bila muingiliano wowote?” “Naamini hivyo Joshua, na asante, tena na tena kwa heshima uliyonipa. Nimefurahi sana.” “Na mimi nashukuru sana kwa kunikubalia kukuoa, maana ilikuwa hatua ya imani tu. Ungeweza kusema hapana, au unaomba muda lakini ulikubali bila kujiandaa! Nashukuru.” Wakapeana mabusu tena ndipo wakatoka.

 

Jumapili Baada ya Kuchumbiwa.

Nyumbani.

Naya aliamka asubuhi akadhani yaliyotokea usiku uliopita ilikuwa ni ndoto tu. Akakimbilia kidoleni na kujikuta akicheka peke yake. Alikaa pale akitafakari hili  na lile masaa yakizidi kusogea asiamini na yeye siku hiyo anakwenda kutambulisha mchumba kanisani kwao! Tena Joshua! Mwanaume wa maana wakuvutia! Anasindikizwa na kina Magesa! Furaha na shauku ya kufika kanisani siku hiyo ikaongezeka. Akabaki akitafakari pale kitandani. Bale akagonga. “Naya!” “Ingia tu.” Akaingia mpaka ndani.

“Toka sasa kwenye neti!” “Wewe zungumza.” Bale akatoa chandarua na kukifunga. “Hujisikii raha mpaka unikere! Unataka nini?” “Jana nimeona aina ya watu waliokuja kwenye ile shughuli yenu. Ukweli Joshua anafahamiana na watu wa maana sana! Ni kiasi cha kunyanyua simu tu na kuzungumza na mtu, mimi nikapata kazi. Huu ukimya wa mpaka sasa unaniashiria pengine nilisha mboa tokea mwanzo.” “Bale!” “Kweli Naya. Huyu mtu kumbuka alikuja hapa na ukayaona mahusiano yetu, kama wewe mwenyewe ulivyosema. Nilimkumbatia Malon nikimpuuza yeye. Pengine nilishamtoka moyoni. Unadhani ni sawa nikimuomba msamaha?” Naya akakaa.

“Tunashida Bale, lakini si yanamna hiyo!” Naya akaongea kwa kujiamini sana akiweka msisitizo. “Hutakuwa mtu wa kupenda watu kwa sababu wana vitu unavyohitaji Bale! Hata Joshua atakushitukia. Mahusiano hujengwa si kwa kutumia watu. Usimtake mahusiano Joshua kwa kuwa unadhani anao uwezo wa kukusaidia. Muweke karibu kwa kuwa unaona ni mtu mzuri anafaa kuwa karibu na wewe. Tafadhali hilo ukumbuke Bale. Kwa sababu zifuatazo. Mimi nakuamini wewe ni mtu mzuri, unayo maamuzi sahihi kwenye kuchagua watu sahihi wakuwaweka karibu yako. Sikutegemei umkimbilie tu Joshua na kuwa naye karibu kwa kuwa mimi nimemchagua. Na pia sikutegea pia umfungie mlango kwa sababu unataka kuwa upande wa Malon kujinufaisha naye!” Bale akabaki kimya. Naya kajua ni kweli.

“Nilitegemea ungekuwa mtu wa haki na kutambua nani ni nani na wote kujua jinsi yakuishi nao!” Kimya. “Sasa kwa kuwa umeshakosea Bale, ndipo nakuja kwenye sababu ya pili. “Joshua ni mwangalifu sana na anajua kusoma watu. Utakapolazimishia mahusiano sasa hivi ujue utaharibu zaidi mahusiano yenu yote yaliyobaki. Atajua unataka kumtumia, kitu anachojua wengi wanamtaka sasa hivi sababu anacho. Sababu ya tatu na ya mwisho pia mimi mwenyewe sitakuruhusu mfanyie hivyo Joshua mtu mwenye moyo mzuri na hana hila ila kutuomba undungu tu tokea siku ya kwanza anakuja hapa wewe ukamkataa. Sitakubali umtumie vibaya. Hapo naomba uelewe Bale.” Naya akaendelea.

“Hata akikutafutia kazi kesho na bado ukaona siye mtu unayetaka awe karibu yako, mimi nitakuelewa kabisa. Usirudi kwa Joshua sababu ya kutaka kitu kwake ila kutambua umuhimu wake kwanza kwangu mimi kama ndugu yako na pili iwe kwako. Hata kama kwako haleti maana, ningetarajia angalau umkubali kwa kuwa ni mtu wangu mimi! Napo silazimishii Bale. Ila kwa jinsi nilivyoishi na Joshua kwa muda mfupi, nimemgundua ni mtu wa maneno yake. Haongei tu jambo ili kumfurahisha mtu. Pengine huu ukimya tunao uona inawezekana anakusubiria wewe.” Bale akashangaa kidogo.

“Kivipi tena!?” “Anataka kujua upo serious kwa namna gani. Hiki kitu unakitaka kwa kumaanisha au ni kitu tu cha kupoteza muda ukishapata kingine uache halafu unakuwa umemuharibia yeye mahusiano na huko alikokuwa amekutafutia hiyo kazi! Sijui kama unanielewa?” “Kwamba anahisi Malon anaweza kurudi akani...” “Sio kuhisi, mimi nimemuhakikishia kuwa Malo lazima arudi.” “Naya!” “Wewe humjui Malo kwa kuwa nimemfungua kwenu kwa upande niliotaka nyinyi mumfahamu. Hili alilokufanyia wewe si geni kwakwe hata kidogo.” “Hawezi kurudi!” “Basi ndipo utakapomjua Malon kwa uhalisia wake. Atarudi na sababu nzuri tu tena ya kueleweka.”

“Na mwanzoni kabisa, nilishamsikia Joshua akisema hivi, mwanadamu akiwa na shida yake na akijua wewe unao uwezo wa kumpa hicho kitu, huwa anaongea chochote ili akipate kile kitu.” “Naya!” “Sikudanganyi Bale. Na ndio maana yeye anasemaga alishakataa kujiingiza kwenye usahili. Hafanyagi interview pale kazini. Wanamjua. Mzito sana kuamini watu ni mpaka awe anataka mtu wake yeye mwenyewe, lakini sio vinginevyo.” “Daah!” Bale akaishiwa nguvu kabisa.

“Ndio maana mimi nakushauri utulie na umuonyeshe kwa vitendo, ulichomwambia unataka, unamaanisha. Kwamba hata ikitokea anakupatia kazi sehemu basi hata ukipata fulsa nyingine, utabaki kufanya kazi aliyokutafutia. Vile unavyomuona Joshua hana watu wengi sio kwa sababu nyingine yeyote ile, ila amekusudia kabisa kwa kuwa yupo makini sana na watu. Sasa naomba na wewe usiingie kwenye kundi la watu wanaomlazimu kuwakwepa, maana Joshua atakuwa mume wangu. Mungu akijalia ni mpaka kifo. Sasa sitaki uniweke kwenye wakati wakutafuta suluhu kati yenu wakati mimi najua ni muda tu Bale. Iwe kwa kupitia yeye au la, utapata tu kazi. Mimi sikutafutiwa kazi na Joshua, lakini nipo hapa. Naomba utulie ukijua hujachelewa kama mwenyewe alivyokwambia. Tafakari maneno yake kwa sababu huwa Joshua si mropokaji.” “Nimemuona.” “Basi tulia Bale, mimi nakushauri tu.” Naya akaweka msisitizo.

“Na pia naomba kukushauri kitu kingine, kuwa makini sana na jinsi unavyoshirikiana na baba.” Bale akapoa. “Chunga maneno yako hata jinsi unavyomjibu hata akikukera, kuwa makini. Baba anatuombea sana. Kwa kufunga na kuomba na anaamini Mungu atatutendea mambo makubwa sana.” “Kama wewe?” Naya akacheka. “Na zaidi. Jinyenyekeze tu kwake na kwa Mungu. Hata kama unaona unao uelewa mkubwa wa mambo fulani fulani kuliko yeye, tafadhali tafuta hekima yakuzungumza naye sio kumrushia tu maneno! Huwa inaniuma sana, na kwa kuwa huwa hakujibu, wewe hujui. Lakini inamadhara makubwa sana, Bale. Kuwa makini jinsi unavyozungumza naye. Usimchukulie kama vile mama alivyokuwa akimsema vibaya kwetu kwamba hana akili ya maendeleo ndio maana mambo yake hayaendi.” “Simchukulii hivyo.” Bale akapinga.

“Ndivyo unavyoishi naye Bale. Hata jinsi unavyomkosoa jambo si kwa heshima na yeye huwa ananyamaza tu. Nipo hapa nilipo na yote niliyonayo mimi, kwa sababu ya ushauri anaonipa baba. Jumla yangu yote unayoniona nayo ni kwa sababu ya baba. Hata huyo Joshua, nisingekuwa naye isingekuwa baba. Nazungumza na baba kuliko hata Mungu. Mchana na usiku natumia hekima zake bila kukoma. Nikiwa hata kazini jambo linapokuwa gumu nampigia baba, ananishauri na kunifanya niendelee. Mimi niligundua mengi aliyokuwa akilalamikia mama ni kushindwa kwake yeye mwenyewe kufikia ndoto zake wala haikuwa sababu ya baba. Kwani kuna wanawake wangapi hapa duniani ni mamilionea! Wengine wameajiriwa na bado wanafanya biashara. Yeye alishindwa nini kuyafanya yote hayo kama kweli alikuwa anataka vingi! Kwa nini yeye alazimishie umilionea ni lazima utoke kwa baba tu!” Bale kimya. “Kwa hiyo kuwa makini sana, usije jifungia baraka zako au ukajichelewesha.” “Nimeelewa Naya.” Bale akatoka, Naya akafurahia hiyo nafasi ya kuweza kuzungumza na Bale na akamsikiliza. Hakuwa akipenda jinsi anavyozungumza na baba yao ilikuwa ni kama amechukua nafasi ya mama yake hapo ndani, kuzungumza vibaya na baba yao. 

Kanisani.

Joshua aliwahi hapo nyumbani kwao kama kawaida yake bila ya kuchelewa. “Mama umepania!” Naya akacheka sana kwa aibu. “Na wewe umependeza, mchumba wangu.” Joshua akacheka sana. “Hapo umeifanya siku yangu kuwa nzuri zaidi.” “Hata mimi bado siamini! Nimebaki nikijikumbusha tu.” Walikuwa wakizungumza Naya na Joshua nje ya mlango alipoenda kumfungulia, maana Naya alikimbilia mlangoni. “Acha nisalimie ndani kwanza.” “Ila asante kwa nguo. Si umeona ilivyonikaa vizuri?” “Nimeipenda mwilini mwako zaidi kuliko ilipokuwa dukani.” Naya akacheka zaidi. “Tunafanana rangi.” “Ndio lengo zima, si ndivyo?” “Kabisa. Acha nijimalizie kidogo ndipo tuondoke.” “Utaharibu sasa Naya! Umependeza, hapo inatosha.” “Kidogo tu.” Wakacheka na kuingia ndani, baba Naya alikuwa akiwasikiliza ndani. Kimya kama kawaida yake kochini.

Joshua akasalimia. “Nimeshazungumza na viongozi wa kanisa, nimewaambia juu ya kuchumbiwa kwa Naya, na ugeni wenu leo.” “Nashukuru sana mzee wangu. Naomba uniombee huko kanisani mambo yasivute ili tumalize hili swala mapema. Tufunge ndoa yetu mapema.” “Naamini itakuwa hivyo, sioni sababu ya kuwachelewesha. Ila pia nitajitahidi kuweka msisitizo kwenye hilo.” “Nashukuru sana mzee wangu.” Joshua amehakikishiwa na baba mkwe, furaha ikazidi kuongezeka.

Naya na familia yake wakatoka kuelekea kanisani bila ya kuchelewa. Joshua akiwa ndio dereva, na baba Naya akiwa amekaa mbele, Naya kiti cha nyuma ya dereva, Joshua, akiwa na pamoja na kaka zake.

Walifika kanisani na kubaki nje wakiwasubiria kina Magesa. Nao hawakuchelewa. “Mimi namkubali sana bibi harusi wangu. Upo wa viwango mno!” Nanaa akashuka garini na hizo sifa. “Nanaa kwa ushabiki! Sasa hapo umeacha watoto wote ndani ya gari umemkimbilia Naya!” “Kapendeza sana bwana! Wewe ungemsaidia Geb kushusha watoto!” “Hata mimi nataka kuwahi kutoa sifa.” Mama G na Nanaa wakaanza kucheka wao wenyewe na kufanya wengine wacheke. “Na nyinyi mmependeza sana.” “Mimi na bibi harusi wangu tutakuwa gumzo!” Nanaa akaendelea kusifia. “Si umetuona baba Naya?” “Nakuona Nanaa, binti yangu. Umependeza sana.” “Asante baba Naya. Ila ujue nimepania.” Wote wakacheka.

“Na watoto pia hutaki tena?” Joshua akacheka akimuuliza. “Nimeona nimuwahi Magesa. Akija hapa atataka kutawala mazungumzo yote! Umependeza bwana harusi.” “Nashukuru Nanaa. Na wewe umependeza sana.” “Na mimi nimependeza anko. Niangalie.” “Sana Magesa. Hujambo?” Magesa alishushwa garini na baba yake na kukimbilia hapo. “Sijambo. Mimi napenda miti mirefuuuu!” “Hapana Magesa.” Baba yake akamuwahi akiwa bado garini akimshusha mdogo wake. Alimsikia. “Na mti huu ni hatari?” Akauliza taratibu akisogelea mti. “Mti si hatari, lakini sitaki wewe upande hapo. Kwanza utajichafua, pili utaanguka.” Baba yake akamjibu.

“Mtu akipanda na viatu lazima aanguke. Lakini mimi mtoto mzuri, nitavua viatu.” “Dad ameshakwambia hapana Magesa. Tulia.” Liv akamuwahi kaka yake akimuonya. “Mimi nitakuwa mwangalifu na mami atakuwa na mimi akiniangalia nisianguke, au wewe anko mwambie dad utahakikisha sitaanguka.” “Kwa kupenda kuuza kesi wewe! Unataka anko ndio apambane na dad wako?” “Kwani wewe bibi unajua kule juu kuna nini?” Magesa akauliza. Nanaa akazidi kucheka.

“Uje umuulize baba yako aliyekukatalia kupanda. Usianze kunitesa kwa maswali mimi.” Bibi yake akamkatalia. Magesa akabaki akiangalia juu ya mti. “Nanaa una watoto wazuri!” Naya akasifia. Nanaa akaanza kucheka akiangalia wanae. “Asante mwaya. Nashukuru Mungu. Wote ni wa miujiza hao. Upatikanaji wao ni wa kufa, kupona, mpaka tukaamua kuweka kikomo.” “Kwani dad wewe unajua kule juu kabisa kuna nini?” Magesa akamuwahi baba yake mara aliposogea na Jimmy. Wote wakacheka walipomsikia bado anahabari ya mti tu! “Mimi nilifikiri kasahau!” “Hawezi hata kidogo. Atang’ang’ania mpaka kesho atakumbuka.” “Nisikilize Magesa. Mbali ya yale matawi tunayoyaona sisi wote hapa chini, hakuna kitu kingine kule juu.” “Ume...” “Kabla hujaniuliza swali la pili kama nimejuaje, najua aina hii ya miti. Haina matunda na hakuna kitu kingine juu ya huu mti.” “Labda nikaangalie, leo inaweza kuwa kuna kitu.” Magesa akakazana kwa sauti yake ya tahadhari kama asiyetaka kuharibu, wote wakazidi kucheka.

“Haiwezekani Nanaa!” Naya akashangaa sana. “Hajamaliza hapo! Na usifikiri ni yeye peke yake. Wote wapo hivyohivyo ila wengine wao huwa hawaongei ni kwa vitendo tu. Sasa mimi na bibi yao huwa wanatuonea. Baba yao ndio kiboko yao. Anayajua majibu ya maswali yao yote kabla na baada ya kuyauliza, na kuwajibu mpaka wanatulia. Haya njoo mwanangu, maana huo mti hutapanda.” “Wewe mama hutaki kujua kule juu kuna nini?” “Hapana Magesa, mwanangu.” Wakazidi kucheka vile Nanaa alivyomjibu. “Mimi nataka tu kuingia mle ndani kanisani, nikaimbe na kucheza. Si nimekwambia kwa nini tupo hapa leo?” Nanaa akamuuliza Magesa. “Sababu anko anataka kutambulishwa hapa kama yeye ndio mchumba wa anti, ili wasije kumuiba mchumba wake.” Magesa alijibu kwa ufasaha nakufanya watu wote wazidi kucheka.

“Wewe Nanaa!” “Lakini si amepatia, mama jamani!” Geb akabaki akimwangalia mwanae. “Haya twende tukaimbe ndani kanisani, acha mawazo yakupanda kwenye miti.” Bibi yake akaongeza. “Wataimba wimbo wangu mzuri, bibi?” “Utamuomba mchungaji. Haya ongoza njia.” “Ila nikiingia nisishike kitu labda...” “Hata kinanda usiguse, Magesa.” Baba yake akamuwahi. “Labda kama nikiomba halafu wakaniruhusu?” Wakaanza kucheka upya. “Sasa wewe Nanaa unaishije nao hawa watoto.” “Rahisi sana. Ningekuwa naye mimi, ningeenda huko ndani kanisani na kumuombea apige kidogo, roho imtulie na mimi nitulie.” “Haya tangulia Magesa.” Baba yake akamkumbusha. “Lakini nisiguse chochote hata kama wakinikaribisha?” “Usiwe na wasiwasi, hakuna atakaye kukaribisha.” Walicheka sana jinsi baba yake alivyomjibu kwa haraka tena vizuri tu. Kweli akaondoka taratibu. “Huyo ndio Magesa mwenyewe!” Nanaa akaongeza.

Geb akasalimia wote kwa kuwapa mkono. “Nisalimie Jimmy.” Joshua akamwambia Jimmy aliyekuwa akimwangalia Magesa akielekea kanisani. “Kwani huyu mtoto anaongea kabisa, yaani kama vile Magesa?” Naya akauliza. “Subiri uone.” Nanaa akamtuliza Naya. “Jimmy? Niangalie.” Baba yake akamuita. Akamwangalia. “Umemsikia anko?” Akarudi kumwangalia Joshua. Akamsalimia vizuri tu. “Shikamoo anko Joshua.” “Nanaa!” Naya akashangaa. “Nilikwambia nini ukiona watu?” Akamwangalia baba yake, kisha akamgeukia tena Joshua. Akarudia tena kumsalimia ila safari hii akampa na mkono. Akafanya kwa wote kisha akamwangalia baba yake. “Sasa hivi ndio unaweza kumfuata Magesa.” Wakamuona akiondoka taratibu, Magesa naye akawa anarudi akikimbia.

“Utaanguka bwana Magesa, halafu ujichafue! Ni nini tena?” Mama yake akamuuliza. “Nilitaka kumsahau mtoto!” Akawa amemfikia Jimmy. “Sijakusahau Jimmy, mtoto mzuri. Nimekuja kukuchukua. Umesikia?” Wakamsikia akimuongelesha Jimmy kwa upendo akamshika mkono kabisa akimuongoza kurudi ndani kanisani. “Ulifikiri nitakuacha?” “Nilijua tu utarudi kuja kunichukua.” Wakamsikia Jimmy akimjibu kaka yake huku wakielekea ndani kanisani. “Wewe Nanaa, kumbe anaelewa na kuzungumza kabisa!?” “Sana.” Bibi yake akadakia. “Na anampenda sana yule mwenye maneno mengi. Hasikii raha asipomuona, ndio maana macho yake wakati wote yalikuwa kwake, na Magesa anampenda sana mdogo wake. Hataki alie.” Bibi yake akaongeza.

“Mimi nilishasalimia, dad.” “Nilikusikia Liv. Wewe mtoto mzuri sana.” Akamuona Nanaa na mama G, wakikonyezana. Geb akawaona akacheka akitingisha kichwa. Wakajua huyo ndio kipenzi cha Geb kwa hakika. “Baba Naya na Naya.” Nanaa akasengenya akimteta Geb na Liv, wakacheka wote na kuelekea kanisani. 

Uchumba Wa Naya Na Joshua Kanisani.

Ukatangazwa uchumba wa Naya na Joshua na siku hiyohiyo likatoka tangazo la kwanza la ndoa yao kama alivyoomba Joshua. Naya alijawa furaha na fahari ya aina yake. Wakaitwa pale mbele ili kuombewa, Nanaa na Geb nao wakaenda ili kuungana nao kwenye maombi. Joshua akataka tena kumvalisha ile pete pale kanisani. Naya alishamvulia kabla hawajaitwa pale mbele, kwa hiyo Joshua alikuwa nayo mfukoni. Akaruhusiwa. Akarudia tena kama usiku uliopita, tena na goti kabisa. Safari hii Naya alikubali na cheko kubwa ila akambusu tena kiganja cha mkono ule uliokuwa umemshika yeye Naya, alipopiga goti akimuomba amuoe, kama usiku uliopita. “Nakupenda Joshua.” “Na mimi nakupenda Naya.” Ndipo akamvalisha. Watu wakaimba na kushangilia wakimtukuza Mungu.

Lakini gafla ukapita wakati wa ajabu ndani ya moyo wa Naya wakati yeye na Joshua wamepiga magoti pale mbele kanisani ili waombewe. Akatamani sana hiyo siku mama yake angekuwepo na yeye ashuhudie kinachoendelea kwa wakati huo kina mama wengine wakipiga vigelegele wakishangilia. Akakumbuka  jinsi mama yake alivyokuwa akitamani aishie kuwa na mwanaume kama Joshua! Heshima iliyowekwa pale kanisani na kina Magesa na huyo mchumba mwenyewe Joshua! Akajikuta machozi yakimtoka na kuhisi kuna kitu hakijakamilika siku hiyo. Ile simanzi ikataka kuiba ile furaha yote aliyoianzisha Joshua siku iliyopita. Joshua akamuona wakiwa wamepiga magoti. Akamwangalia vizuri kwa kuinama akimchungulia usoni, akagundua yale sio machozi ya furaha.

Akajisogeza karibu zaidi. “Vipi?” “Natamani mama angekuwepo Joshua! Naumia kuona haya yote yananitokea halafu ameshindwa kushuhudia! It’s not fare.” Akasikia kuumia zaidi. Joshua akakumbuka kusimuliwa habari za mama Naya jinsi alivyokuwa akihangaika kumlazimishia wachumba walioonekana wamejijenga kitaaluma. “Pole sana Naya. Pole. Ila tumuenzi kwa kuhakikisha hili tuliloanza, tunalikamilisha kwa heshima.” Joshua akajisahau kama wapo madhabahuni, akamuwekea mkono juu ya mabega akamvuta karibu ubavuni. Akimsugua pembeni ya mabega taratibu. Naya akajilaza hapo ubavuni vizuri. “Tutakuwa sawa tu. Tuamini Mungu tutakuwa kile mama alitamani kukiona kwako.” Joshua akamnong’oneza sikioni, wakati watu wakiendelea kutulia wakirudi kwenye viti vyao ili waombewe baada ya kuvalishana pete tena. Wakabaki wachungaji, wazee wakanisa na hao wasimamizi wao kina Magesa. Watu walipotulia ndipo wakaombewa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ndipo mchungaji akaanza mahubiri akisoma habari ya Yesu kutembea juu ya maji,  na Petro kutaka na yeye atembee, akamuomba Yesu amuamuru atembee juu ya maji kama yeye. Kila mtu alikuwa ametulia kabisa, wakisikiliza. Wakashitukia Magesa anaanza kuongea. “Mama yangu alinisomea kutoka kwenye bibilia. Kitabu cha Mathayo 14, mstari wa 22 kuanzia pale.” Watu wote wakamgeukia Magesa.

Wazazi wake walibaki wamepigwa na butwaa. Watu wakampigia makofi, Magesa akapata moyo akasimama kabisa juu ya kiti alichokuwa amekalia ili awaone watu wote. “Ila nilimwambia mama, Petro alizama sio sababu ya kukosa tu imani. Alikuwa hajaamua kwa moyo wake wote kutembea juu ya maji. Ukitaka kufanya jambo lako, ukiamua, unakusudia, halafu unafanya kwa moyo wako wote, utashangaa huogopi na huzami.” “Watajuta kutukaribisha hapa!” Bibi yake akaongea na kufanya watu wacheke.

“Kweli tena. Mimi sisemi uongo. Si ni kweli mama?” “Kweli huwa husemi uongo, baba mzazi. Haya shuka basi hapo juu.” “Mmemsikia mama yangu? Kwa hiyo ukitaka kufanya jambo, kusudia kutoka moyoni na ufanye. Hata kama unataka kupanda kwenye mti mrefu sana, usiogope.” Ilibidi mpaka baba yake acheke na kutingisha kichwa. “Nilijua tu hayajaisha! Magesa mwanangu wewe! Jambo la kupanda mti mpaka sasa hivi unalo tu? Shuka baba.” Nanaa akamsihi mwanae taratibu, watu walikuwa wakicheka sana na kumpigia makofi.

“Haya, naomba ushuke hapo kwenye kiti Magesa, na uje ukae hapa.” Baba yake akaamuru. “Nisiombe tena ule wimbo wangu aliosema bibi nimuombe mchungaji?” Akauliza na kufanya watu wazidi kucheka. “Umeona mama wewe!?” “Mimi nilitaka atulie bwana. Sikujua kama kweli mwenzangu atayabeba tena mpaka huku kanisani!” Mama G, akajibu akicheka. “Magesa, sitaki kurudia mara ya pili.” Baba yake akaweka msisitizo. Magesa akapoa gafla  baada yakuona sura ya baba yake. “Au labda nikae hapahapa pembeni ya mama yangu, ila nisiongee tena?” Watu wakazidi kucheka. Baba yake alivyomtizama bila kujibu, akashuka taratibu. “Labda mama ananitaka mimi?” Akamuuliza baba yake kwa sauti ya wasiwasi. “Wewe hutanyamaza mpaka ukae karibu na dad, Magesa. Kila mtu anakujua. Hapo utaongea tena wakati ulishaambiwa na dad tokea zamani, mchungaji akiongea kanisani, usiingilie.” Liv akamwambia kaka yake taratibu kwa sauti yake ya chini.

“Wewe mama unanitaka nibaki hapa?” Akamuuliza mama yake kwa upendo akionyesha ameshaingiwa hofu. “Sasa hapo na nyinyi mnaanzisha ibada yenu, na kumfanya mchungaji ashindwe kuendelea.” Mama G akawashitua. “Muahidi dad hutaongea tena, mpaka ibada iishe, halafu ndio nikuombee urudi ukae hapa.” Mama yake akamwambia watu wote wakiwasikiliza. “Mimi sitaomba hata ule wimbo. Nanyamaza kabisa.” Akaongea kwa upole akimtizama baba yake na sura ikawa kama Jimmy vile na macho yao ya upole na ya kurembua kama baba yao.

“Mimi naona nikae tu hapa na mami. Si sawa dad?” Akiishaita ‘mami’, wanajua ameogopa. “Mjibu bwana Geb, ataanza kulia sasa hivi, wote ibada ituishie hapahapa!” Nanaa akamsihi. “Lakini mtoto amemaliza ibada nzima na ameongea vizuri sana.” Akaingilia mchungaji kama kumtetea. “Mimi naitwa Magesa.” “Umeona mama? Huyo hawezi kunyamaza mpaka akae karibu na dad.” Liv akadakia “Kwani mimi si nimejitambulisha tu?” “Hakuna hata aliyekuuliza jina lako Magesa! Umemuingilia tena mchungaji.” Liv akaongeza kwa sauti yake ya chini. “Magesa?” Baba yake akaweka msisitizo. Akaanza kulia huku akimsogelea baba yake macho kwa mama yake. 

“Mimi nishakuwa mtoto mbaya, mami?” “Mimi nilijua tu jamani! Na hili kanisa nalo mpaka litatujua! Nyamaza Magesa mwanangu. Wewe usilie.” Nanaa akalalamika kwa sauti ya chini. “Mimi nimeshaharibu natakiwa kuwajibika tu?” Magesa akauliza na kilio juu, watu wakazidi kucheka.  

“Si niliwaambia mimi? Hapo mshaanzisha ibada yenu ya vilio, kinachofuata ni kutapikia watu hapa, wote turudi nyumbani.” Mama G naye akalalamika. “Haya Geb na familia yako simama.” Mama G akaongeza. Geb akasimama akijua ndio anaambiwa na mama yake watoke. “Twende Magesa.” “Bila mami wangu, mimi!?” Akamuuliza baba yake akilia sana. “Mimi nashauri niende tu na mami wangu jamani!” Magesa akazidi kulia. “Haya, Nanaa na wanao tokeni mtupishe humu, ibada iendelee.” “Mama jamani! Si Geb anatoka naye?” “Nenda bwana Nanaa! Wewe unajua mwisho wa yote utakuja tu kuitwa, ametapika na bado analia. Naombeni tokeni. Haya Geb ongoza njia, mkeo na watoto wanakufuata nyuma. Mkaendeleze ibada yenu huko nje, na sisi tuendelee na ya humu ndani. Haya tangulia.” Geb, Liv na Jimmy wakatoka. Kanisa lenyewe lilikuwa dogo tu, kama darasa kubwa tu, hata hapakuwa pakubwa sana.

“Mimi nimeshaharibu mimi! Nimekuwa mtoto mbaya.” “Wewe sio mtoto mbaya, Magesa mwanangu.” “Bado mimi ni mtoto mzuri, unamshukuru Mungu amekupa mimi?” Watu wakazidi kucheka, Magesa anauliza huku akilia, mama yake anakusanya mizigo yao watoke. “Ndiyo Magesa, mwanangu. Nyamaza sasa.” “Nikiendelea kulia ndio naharibu zaidi, Mami?” “Nanaa na mwanao naombeni mtoke. Wenzenu washatangulia nje, bado nyinyi wawili tu. Kinachokufanya hutoki ni nini bwana!” “Nakusanya mizigo yetu yote maana tunaweza tusirudi tena humu ndani. Ila sasa sioni tai yake huyu si unamuona anavyolia na kuvua shati kirahisi tu? Hana tai ndio maana.” Bibi yake akamtizama pale aliposimama Magesa akilia huku akikunja shati lake mpaka kifuani akilifungasha kama kifurushi.

“Tai iko wapi Magesa?” Bibi yake akamuuliza. “Nimeweka kwenye kapu la sadaka.” Watu walianza kucheka tena. Nanaa aliposikia hivyo akasimama wima kama mshale kwa mshituko na kuweka kila kitu chini. Magesa akamuona vile mama yake alivyoshituka. “Nisingetoa na saa yangu sadaka pia, Mami? Nimezidi kuharibu?” “Jamani Magesa!? Na saa pia umetoa sadaka!?” Watu wakazidi kucheka. “Kama yule mama mjane Yesu alimsifia ametoa vyote alivyonavyo! Unamkumbuka mami?” Nanaa akabaki akimwangalia kwa mshangao. Mpaka bibi yake alikuwa akicheka.

“Umemsahau tu mami. Hata Yesu alimsifia akasema yeye ndio ametoa nyingi zaidi kuliko wote kwa kuwa ametoa vyote alivyo navyo. Kwenye kitabu cha Marko 12 mstari wa...” “Nakumbuka Magesa mwanangu!” “Ila leo nimeharibu zaidi sikutakiwa kuwa kama yule mwanamke mjane, tena masikini?” Watu wakazidi kucheka ila kushangazwa naye jinsi anavyokumbuka maandiko.

“Leo sikutakiwa kulitendea neno kazi?” Magesa akazidi kumuhoji mama yake aliyekuwa ameduaa akimwangalia. Watu wakizidi kucheka. Yeye mwenyewe akilia sana huku akiuliza na kukusanya shati lake kifuani, alishalichomoa kwenye suruali. “Mnachelewesha ibada bwana!” “Sababu yangu mimi, bibi? Mungu hataki saa kwa sababu anajua muda na wakati. Mimi ndio natakiwa kujua  muda?” “Kumbe unakumbuka ulivyoambiwa na baba yako mara ya mwisho ulipotoa saa yako sadaka? Sasa leo upo matatizoni zaidi. Wewe hufanyii kazi mafundisho ya wazazi, unataka kuyafanyia kazi yale ya kwenye bibilia tu, tena unayoyapenda na kuyachagua wewe. Sasa leo upo matatizoni.” Akazidi kulia kwa hofu.

“Jamani mimi nipo matatizoni!” Watu wakazidi kucheka. Baba yake akarudi na kumbemba pale alipokuwa amesimama akilia huku akimtizama mama yake kama akimtaka amuhurumie. Geb akamtoa hapo ndani juujuu akilia. “Ningemsubiri tu mami wangu jamani!” Magesa akasikika huko nje akilia kwa sauti. “Sasa na wewe uwahi, maana kinachofuata hapo nje ni kutapika, halafu njaa, anataka kula, safari ya kurudi nyumbani inaanza tena wakati ibada ndio ipo katikati.” Mama G akaweka msisitizo, Nanaa akarudi kunyanyua vitu vyake na watoto wake alivyokuwa amekusanya na kuvitupa tena chini baada ya Magesa kusema ametoa sadaka tai na saa yake.

 “Samahanini sana jamani.” Nanaa akaomba msamaha akitoka. “Lakini hakukosa. Aliongea vizuri sana.” Mchungaji akasifia kama akituliza hasira za wazazi na yeye alikuwa akicheka. “Bora tu watoke baba. Huyo mtoto kukihubiriwa kitu anachokijua, hawezi kunyamaza. Mahubiri yote atakuwa ni yeye tu akichangia, hutaongea ujumbe wako. Makanisa yote wanatujua. Waache tu watoke. Watarudi mwishoni kabisa, tuimbe nao kama hawatalemewa huko nje na kuondoka moja kwa moja.” Watu wakazidi kucheka. “Mama naye kutusemelea mpaka kwa mchungaji mpya jamani!” Nanaa akaongea akitoka.

Naya akamfuata. “Wewe rudi tu ndani. Leo siku yako. Hii fujo niachie tu mimi mwenyewe. Nishazoea.” “Au tumpeleke kwa watoto?” “Huko ndio baba yake atalala jela leo. Hajuagi kutulia Magesa mwanangu. Akifika huko atapanda kila mahali huku akitaka aongee yeye kila kitu. Na mwili wake ule anaweza akaangukia mtoto wa watu, akamvunja hata shingo.” “Nanaa!” “Nakwambia kila kanisa tulilowahi kwenda tunajulikana kwa majina yetu wote sisi! Ndio maana unawaona wote tunakuwa nao ibadani kama watu wazima, sababu yake huyo.” “Anatapika!” Wakamsikia akitapika huku akilia sana.

 “Ndio kazi yake huyo. Mtundu, maneno mengi, lakini muoga kupitiliza. Sasa hapo yupo na baba yake mimi sipo ndio hofu inamzidi. Acha niende ndipo atatulia, tutarudi.” “Kwani huwa anamchapa?” “Chakushangaza, mimi na bibi yake ndio huwa tunamchapa, lakini haniogopi hata. Baba yake hajawahi kumchapa hata mara moja, ila akimuita tu, kama amekosa, ndio kilio kama hivyo.” Naya akazidi kucheka.

 Joshua naye akatoka. “Tuwasaidie?” “Wala msijali. Ndio nilikuwa nikimwambia Naya, arudi tu ndani, na sisi tutarudi baadaye kidogo akitulia. Kwanza hana muda mrefu, atachangamka sasa hivi, tutarudi. Acha nimuwahi.” Wakacheka, Nanaa akaondoka na mabegi yake. Naya na Joshua wakarudi ndani.

Baaada ya kama dakika 15 hivi, Geb na familia yake wakarudi tena, Magesa akiongoza njia. Mama G akaanza kucheka kimyakimya. “Sasa hivi siongei tena, bibi.” Magesa akanong’ona kwa sauti ya juu akimwambia bibi yake huku akimsogelea. “Hapo mbona unaongea?” Bibi yake akamuuliza. Akafunga mdomo na mikono yake yote miwili kwa haraka na kumgeukia baba yake akamkuta akimtizama. Akatingisha kichwa akiashiria kukataa. Alikuwa amebadilishwa mpaka nguo. Yeye peke yake, akiashiria alijitapikia.

Walipokaa, Joshua akamwangalia na kumuonyeshea ishara aende kwake. Akamgeukia baba yake kama anayemuomba ruhusa, akamkubalia akanyanyuka kwa haraka na kumfuata Joshua pale alipokuwa amekaa. “Sasa hivi siongei tena anko. Lasivyo tunarudi nyumbani wote. Inakuwa namuingiza na mama yangu matatizoni pia. Hamsikilizi mchungaji, tunafukuzwa naye makanisani.” Magesa akanong’ona kwa sauti ya juu tena, nakufanya watu wacheke tena. Baba yake akatingisha kichwa kwa masikitiko. “Huku pia tunakusikia wewe Magesa.” Bibi yake akaongeza kwa sauti ya chini, Magesa akafunika mdomo wake tena kwa haraka na mikono yake yote miwili. Akamgeukia mama yake wa kwanza kisha baba yake, akakuta wote wakimtizama. Akaanza kutingisha kichwa tena akiashiria ishara ya kukataa huku akiwatizama wazazi wake na mdomo kafunga, ndugu zake kimya wakimtizama.

Baada ya ibada kuisha, Joshua alikuwa amemwandikia mchungaji kikaratasi akiomba mwishoni kabisa tai ya Magesa na saa aliyotoa sadaka vipigwe mnada na aimbe. Na kweli, baada ya kufunga ibada mchungaji akatangaza kutakuwa na mnada wa tai na saa ya Magesa. Watu wakashangilia sana, na kuhamsika na ndipo alipomkaribisha Joshua. Wakashangaa anakwenda na Magesa pale mbele. Joshua akachukua gitaa la bezi, akasimama kwenye kipaza sauti, Naya akamkabidhi Magesa kipaza sauti kingine na yeye akachukua chake. Bale akaenda kwenye kinanda.

“Upo tayari Magesa?” Joshua akamuuliza. “Si umesema tutaimba wote?” “Ila wewe unaanza, halafu anafuata anti Naya, mimi halafu anko Bale. Ila tunataka wewe ndio utuanzishie wimbo wako.” Magesa akafurahia sana. “Mama utacheza?” “Mimi naona ungeanza tu kuimba mwanangu.” “Au uje hapa?” “Mama yako hajui kuimba bwana, wee! Acha kupoteza muda.” “Mama wewe! Ujue mimi nimwimbaji sana!” Nanaa akashangaa kwa sauti akijitetea. “Mmmmh!” Mama G akaguna. Watu wakacheka, hakuna aliyetoka. Bale akaanza kupiga kinanda, Joshua akapokea. Na mpiga ngoma hakuwa ametoka kwenye kupiga ngoma. Akawapokea wimbo wa, ‘Hakuna Mungu kama wewe, Hakuna Mungu kama wewe. Hakuna Mungu kama wewe, hakuna na hatakuwepo.’ Akaanza Magesa vizuri tu akionekana kweli ni wimbo wake na huwa anaupenda sana. Kisha akapokea Naya, alipokuja Joshua, ndipo kila mtu akashangilia sana. Aliimba  kwa hisia zote, tena kwa sauti tofauti tofauti. Magesa alikuwa akicheza sana. Akaja kupokea kuimbisha Bale, akarudia Joshua akipiga gitaa vizuri na kwa ustadi, wakaimba wote mpaka wakamaliza. Watu walishangilia sana kwani waliimba vizuri kama waliokuwa wamejiandaa kwa huo wimbo siku hiyo.

Ilipokuja swala la mnada wa tai pamoja na saa, Mchungaji akawaambia anayetaka upako wa Magesa anakaribishwa kushiriki. Wengi walianza kwa kutaja bei, wakaishia mwanzoni kabisa kwani wakabaki Joshua na Geb wakishindana mpaka kufika mamilioni. “Hakika Geb lazima uniachie. Mimi na Naya tunataka huo upako wa Magesa nyumbani kwetu.” “Lakini ni nini Joshua! Mimi nimehangaika kutafuta aina hiyo ya tai, muulize bibi yake ndio maana umeona wote, yeye na Geb wananisaidia kuweka pesa nyingi ili virudi nyumbani! Nimefanya kazi ya kuagiza, Joshua bwana! Hiyo tai ni ya tofauti, inafanana na mkanda wake pamoja na viatu vyake. Acha bwana!” Nanaa akalalamika. “Nashauri huko ulikotoa hii, ukaagize nyingine. Hii inakwenda kwetu.” Joshua na Nanaa wakabishana tena. Joshua akaongeza pesa. Geb na yeye akaongeza. Watu wakazidi kucheka. Maana yeye Geb alikuwa akitaja tu pesa, Nanaa na Joshua wao ndio wanabishana.

“Hakika tutakesha hapa.” Joshua akaweka angalizo. “Tukifika nyumbani nitawapa tai nyingine hata na saa yake nyingine hivyo niachie Joshua bwana!” Nanaa akabembeleza. “Sisi tunataka hivi alivyomtolea Mungu sadaka.” “Mama alishasema mimi ni mtoto mzuri.” Magesa akakumbushia alivyoona mama yake akihangaikia kurudisha hivyo vitu vyake kama ishara ya kumkumbusha asije kumgeuka wakirudi nyumbani. Watu wakacheka.

“Wewe ni mtoto mzuri Magesa.” “Kwa hiyo unataka upako wangu, anko?” “Ndiyo Magesa.” Akajibu Joshua na kuongeza pesa. Geb akacheka na kutingisha kichwa. “Basi Joshua. Naona kweli umekusudia.” “Geb jamani!” Nanaa akalalamika. “Ni siku yao leo.” Watu wakashangilia sana. Joshua akaandika hundi na kumkabidhi aliyekuwa akifanya mnada huo, akachukua tai na saa ya Magesa. Watu wakashangilia sana na kushangazwa na hiyo pesa iliyopatikana sababu ya hivyo vitu viwili tu. Mchungaji akashukuru, wakaondoka. 

Nyumbani Kwa Magesa.

Walikaribishwa vizuri sana nyumbani kwa kina Magesa. Baba yake Nanaa naye alifika hapo pamoja na James kwa ajili ya chakula cha mchana pamoja. Zikaanza stori na vicheko. “Leo Magesa amefanya nini tena? Mbona yupo tena kwenye kona yake ya adhabu? Leo anahesabu mpaka ngapi?” James akauliza akicheka huku akimwangalia Magesa pale alipokaa akihesabu, Jimmy akimsubiria pembeni yake ili amalize, aruhusiwe, wakacheze. Kina Naya ndio wakaelewa ndio adhabu yake kila wakati. “Na leo kamuingilia tena mchungaji kanisani. Ndio ameambiwa asinyanyuke pale, wala asiguse kitu chochote kile, hata akimaliza kuhesabu atulie kimya. Akiongea tu, au akisogea pale bila kuruhusiwa, anaanza kuhesabu upya.” Bibi yake akajibu nakufanya wote wazidi kucheka. Geb akarudisha macho kwa Magesa. “Leo anahesabu mpaka ngapi?” James akauliza akizidi kucheka. “Dad amemwambia ahesabu mpaka elfu moja.” Akajibu Jimmy akimwangalia kaka yake. “Hapo anatamani achapwe, yaishe, aendelee na shuguli zake kuliko kuwekwa hapo chini akihesabu.” James akaongeza. Wakazidi kucheka wakimwangalia vile alivyopoa usoni huku akiendelea kuhesabu taratibu.

Ukweli Nanaa alikuwa mkarimu sana na walionekana kumkumbali pia Naya. Akamuonyesha picha zake za harusi, Naya akagundua wao walifunga ndoa wakiwa na watoto wawili tayari na Nanaa alikuwa mjamzito wa Jimmy. Akatulia akitafakari akakumbuka kisa Nanaa alichomwambia baba yake usiku uliopita nyumbani kwa Joshua, juu ya vipingamizi walivyopitia kabla ya hiyo ndoa. Akatamani kumfahamu zaidi Nanaa na historia yake binafsi mpaka kubahatika mwanaume kama Geb! Akajaribu kujiweka kwenye nafasi ya Nanaa. Akafikiria ndio angekuwa yeye amezalishwa hao watoto watatu na Malon! Hofu ikamuingia kidogo akitafakari mwisho wao ungekuwaje! “Wala sisi tusingeweza kuishia kama hivi Nanaa na Geb. Sasa hivi ningekuwa na wanangu wote, Kiluvya kwa baba Naya, tunamsubiri Malon akili imrudie, tuanze tena!” Naya akawaza kwa hofu. Akamshukuru Mungu alitoka peke yake kwa Malon, sio na msururu wa watoto.

Walikuwa wamewaandalia haswa ni kama waliacha  vyakula vingine wakiwa wameshapika. Wakasaidiana na msichana wakazi kuweka vyakula mezani wakati wakiendelea kuzungumza na Naya kuangalia album za picha kuijua hiyo familia zaidi.

Kweli aligundua Geb ni mkimya sana. Na ukimya wake ukaongezwa zaidi alipokuja James ambaye alimtambulisha Joshua kwao, kina Magesa. James yeye alisema hata kanisani hakwenda, ametokea kazini siku hiyo kulikuwa na dharula. Akaongezeka na baba yake Naya, naye mcheshi kama mwanae Nanaa. Wakaanza mazungumzo wakicheka na utani mwingi kwa mama G, hapo ndipo Geb alinyamaza kabisa akicheka hapa na pale ila kusikiliza kwa kila anayechangia.

Naya alishamuona Bale akituma jumbe kwa muda mrefu tu nakushindwa kuwepo pale kimawazo. Hakuchangia lolote muda wote macho kwenye simu akisoma na kurudisha majibu. Akawa kama anachati na mtu kwa muda tu, kitu ambacho si kawaida yake. Naya akamwangalia baba yake, akagundua na yeye anamtizama Bale. Wakamuacha. Kwa kuwa alikuwa katikati ya watu, lakini akituma jumbe zake tu kama hayupo pale au amepuuza kinachoendelea pale. Kisha wakamuona anatoka nje kwa haraka. Hakurudi mpaka walipohamia  mezani. Ikabidi Naya amfuate nje. Alipomuona ni kama akakata simu kwa haraka na kuirudisha mfukoni. “Vipi?” Naya akamuuliza. “Ndio nilikuwa nataka kurudi ndani. Akamsogelea na kumpita Naya aliyekuwa akimfuata pale nje. Naya akashangazwa kidogo, ila akamuacha tu.

Wakapata wakati mzuri sana kwa kina Magesa, mipango ya wapi kutafuta nguo za harusi na wasimamizi ikaanza. Nanaa akiwa amechangamkia kweli hiyo harusi, mumewe akimtizama tu anavyoweka mipango na Naya. Mpaka wanaondoka pale, Naya akawa ameshapatwa na hamu ya harusi.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Safari ya kurudi Kiluvya ikaanza. Lakini Naya akagundua Bale yupo kimya na kama mwenye wasiwasi hata na kutizama simu yake pale mbele yao. Akarudisha mawazo kwa Joshua. Wakaanza kukumbuka vituko vya Magesa, mpaka baba Naya alikuwa akicheka sana. “Halafu huwezi kumuelewa Magesa! Ni kama mpole sana, asiye na hatia kabisa. Lakini...” Baba Naya akaongeza nakufanya wazidi kucheka kila wakikumbushana hili na lile la Magesa.

Walifika nyumbani ikiwa imeshafika saa moja usiku. “Ni sawa nikibaki kidogo, au unafikiri niwaache tu mpumzike?” Akamuuliza Naya walipobakia peke yao nje wengine wakiwa wameshaingia ndani. “Jamani Joshua! Naomba ukiwa hapa uwe huru bwana. Pafanye hapa kama nyumbani.” “Unafikiri iwe wakati huu au angalau tukishaoana?” “Baba anakupenda na kukuheshimu sana Joshua. Tafadhali kuwa huru. Mimi pia nataka tubaki wote.” “Kama ndio hivyo sawa.” Wakapeana mabusu ya wizi ya harakaharaka hapo nje ndipo wakaingia ndani.

“Acha nitayarishe basi hata chai kama wote mnasema mmeshiba.” Naya akaingia jikoni baada ya kubadili nguo, Joshua amekaa na baba yao hapo sebuleni. “Nikusaidie?” Joshua akauliza. “Napika chai ya rangi tu, wala sitachukua muda mrefu. Nisubiri tu nakuja.” Wakatulia pale sebuleni, Bale mezani kimya. Naya alitengeneza chai ya tangawizi nzuri ikawa inanukia na hiliki, akaanza  kuwagawia.

Bale.

“Mimi naomba niwaage jamani.” Kila mmoja akamgekia Bale pale mezani. “Naona milango imefunguka, nakwenda Mbeya.” “Kwa Malon!?” Naya akamuuliza kwa mshangao sana. “Sio kwa Malon, ila kufanya kazi kwenye kampuni yake. Amenieleza sababu ya kuniacha. Ameniambia alikuwa na nia nzuri tu ili nitengeneze mambo ya hapa nyumbani kwanza. Hakutaka kunichukua wakati ule, katikati ya kutoelewana na familia.” “Bale!” “Subiri kwanza Naya. Maana mimi sio mjinga. Nina akili zangu timamu, sio mtoto mdogo.” Hapo Bale akawa mkali.

“Ameniuliza kama niliweza kusuluhisha na tukapatana.” “Leo hiyo!?” Naya akamuuliza kwa mshangao. “Ndiyo. Pale tulipokuwa kwa kina Magesa na ndipo nikatoka kuzungumza naye. Malon anasema yeye alikosa nafasi ya kuwa na familia kama hivi mimi, hataki aone mimi naangamia ndio maana aliniacha ili nitengeneze kwanza. Akataka kujua kama ipo amani. Nilipomwambia hata wewe ulinisamehe na kunipa baraka zako juu ya kwenda naye tena siku ileile, na ukanisaidia mpaka kufungasha kabisa. Na nikamwambia kwa wakati ule tulikuwa wote kwa kina Magesa, ulichumbiwa jana yake na siku hiyo kanisani pia na tukaimba pamoja, ndipo akasema kama ndio imekuwa hivyo basi ni sawa. Anasema yeye bado yupo tayari kusimama na mimi.” “Bale?” Naya akamuita taratibu tu.

“Sasa mbona husubiri nimalize? Au wewe unaona ni sawa hivi ninavyokaa tu nyumbani wenzangu wote wanakazi na kutengeneza pesa? Angalia wale vijana wenzangu pale kanisani! Wote wanakazi zakueleweka.” “Sasa wale kina Ino si walitutangulia shule! Unawezaje kujiling..” Naya akamwambia, kabla hajamalizia baba yake akadakia. “Kwanza hujalingana na Ino wewe. Maana najua ndiye anayekuumiza kichwa.” Baba yake akaongeza.

“Mimi sijaelewa jamani! Mnataka nini kwangu? Mnataka tu nikae hapa nyumbani niendelee kulia shida au nichukue hatua? Maana kama mlango umefunguka, ni kwanini mimi nisichukue hatua?” Joshua kimya kama Zayoni. “Angekuwa ni Naya, najua kwa hakika ungemkubalia na kumuunga mkono. Lakini mimi unanipinga, na sijui ni kwanini, baba?” Bale akafoka kwa ukali kabisa. “Punguza hasira Bale!” “Hapana Naya. Kunakuwa kama kuna upendeleo hivi! Wewe ulianza kufanya kazi tokea upo kidato cha tano, sijui! Lakini mbona uliruhusiwa? Tena ulikuwa ukifanya mpaka kazi za usiku! Hatukuwa hata tukimjua mwajiri wako! Mimi mtoto wa kiume nataka kufanya kazi, tena kwa mtu ambaye wote tunamfahamu, ni Malon. Na wewe baba ulienda ukafanya kazi huko, ukasema yapo mazingira mazuri sana. Ukamsifia sana Malon.  Sasa kwa nini leo mimi ndio naonekana sistahili! Au wewe baba unanionaje mimi!? Kwamba Naya ndiye mwenye uwezo wakuhimili mambo fulani fulani lakini si mimi?” Bale akamuhoji baba yake akiwa anawakwa hasira kabisa bila hata kumjali Joshua. Kimya.

“Wakati mwingine mpaka natamani mama angekuwa hai, pengine na mimi ningepata mtu wakunitetea na angeelewa nia yangu ya maendeleo.” “Ni nini Bale!?” “Hapana Naya. Huku ni kunidharau! Kwamba wewe mtoto wa kike unao uwezo mkubwa kunizidi mimi! Wewe umefanya kazi na Malon kwa muda gani na wazazi wakijua, na mbona wasikukatalie? Kama kweli Malon alikuwa mbaya sana wa kiasi hicho, mbona wewe usikatazwe kufanya naye kazi mimi ndio nikatazwe!?” “Unagomba bure bila sababu! Nani amekukataza hapa?” Naya akamuuliza taratibu tu.

“Umeanza kuzungumza mwenyewe na kuongea mengi wewe peke yako, ukitufoka!” “Kwa sababu naona mnataka kuniambia mambo nisiyoelewa! Kwa nini kunilinganisha na Ino, na si wewe uliyeanza kazi ukiwa bado shuleni? Mimi nimevumilia. Sijachanganya masomo na mapenzi, wala kazi au niseme starehe yeyote ile! Leo nimemaliza chuo, pia natakiwa kuomba ruhusa kwa kutaka maendeleo jamani!” Wote kimya.

 “Malon amekuwa msaada sana humu ndani na anatujali. Akisikia tu tunauhitaji wowote ule, anaacha kila kitu, anakuja kutusaidia kwa haraka bila mashariti mengi au kusimanga mtu, akijishusha.” Joshua akajua anamsema na yeye, lakini akanyamaza tu. “Amenitumia pesa nyingi tu na nauli juu kwamba nikiwa tayari nimfuate, atanisubiria kituo cha mabasi ili nisipotee. Jamani, tunataka nini tena? Au mnataka kuniona nabaki tu hapa nyumbani na kuendelea kuwapikia tu?” “Unapokwenda huko Bale, unaharibu.” “Wala siharibu. Naongea ukweli. Labda uwe unakuuma kwa sababu ni kweli.” “Labda Bale, pale ulipoanza ungeishia tu kwenye kuomba ruhusa, basi.” Mpaka Zayoni akaongea ila kwa kujihami.

“Asante sana Zayoni. Maana umeongea mengi ambayo wala hayakuhitajika hapa, zaidi mbele ya Joshua!” “Mimi naomba kabla sijaingia kwenda kulala nikwambie hivi Bale, ukiwa unatoka hapa, iwe ni kwa ajili yako tu. Isiwe..” “Sasa mbona ulikuwa ukimuunga  mkono Naya, mimi unashindwa nini baba?” “Mwache baba amalizie, Bale! Umepatwa na nini wewe!?” “Nahisi kama naonewa kwa sababu mama hayupo!” Naya akabaki akimshangaa sana Bale.

“Unapotoka hapa kwenda kufanya kazi, iwe ni kwa ajili yako tu Bale. Usije toka hapa kwa kusema unakwenda kuhangaikia familia yangu. Hapana.” “Naya mbona analeta pesa hapa na tunazitumia pamoja, kwa nini mimi unikatalie.” “Usikimbilie Mbeya kwenda kukusanya mazao ukitaka kuniletea mimi. Hapana. Kwa kuwa wewe umefika umri au hatua yakujijenga, basi, nenda kakusanye mazao, tafuta na masoko, uzo ili uanze kujijenga usiwe kama mimi.” “Sijasema hivyo baba!” “Leo na sasa hivi ndio hujatamka maneno kama hayo, lakini ndivyo umekuwa ukiishi na mimi hivyo na kunionyesha kwa waziwazi kabisa. Mungu akusaidie na kukufanikisha uzishike hizo pesa unazozitaka na ufikie hayo maendeleo unayoyatamani. Lakini ongeza umakini. Ni hilo tu. Usiku mwema.” Baba yao akaingia chumbani kwake.

“Na wewe acha kuniangalia hivyo!” Bale akamgeukia Zayoni. “Ungemuaga tu baba kwa vizuri Bale. Ona mpaka amekubariki!” Zayoni akaongea kwa upole tu. “Kwa kuwa ameona nimemkumbusha juu ya Naya. Mimi sijui natakiwa kufanya nini jamani! Nahisi nimekuwa mtoto mzuri tu humu ndani ambaye ni mama tu ndiye aliyekuwa akiniona hivyo. Sasa hivi naishia kuomba msamaha mpaka kwa kuomba maendeleo!” “Joshua, nenda kapumzike na mimi nifunge mlango. Nitakupigia nikiwa kitandani.” “Sawa.” Joshua akasimama kwa haraka bila yakubisha. Wakatoka hapo. Ni kama wote wakabaki hawajui tena ni kitu gani chakuongea. Sivyo walivyoingia humo ndani. Bale alibadili hali ya hewa hata chai aliyopika Naya haikunywewa. “Usiku mwema Naya.” “Na wewe.” Joshua akaondoka hapo kama aliyepatwa na mshituko na kushindwa kuzungumza. Usiku huo hakuna hata aliyempigia mwenzie simu. Wakawa kama wasiojua muendelezo. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Katikati ya Furaha ya familia, Malon amerudi akiwa na SABABU NZURI SANA NA YA KUELEWEKA.

Usikose kufuatilia muendelezo KWENYE kurudi kwake. Nia ya Safari hii ni nini?

 .

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment