Jumatatu.
Kama
kawaida ya siku nyingine zote za kazi, Naya aliamka akakuta baba yake
alishaamkaa na kumwandalia kifungua kinywa na maji ya kuoga. Akamsalimia na
yeye akaitika tu, hapakuwa na mengine. Akajitayarisha. Wakati akinywa chai Bale
naye akatoka kama anayejiandaa. Akasalimia, baba yake akaitika, akaendelea na
mambo yake, Naya kimya hata hakumtizama. Aliingia na kutoka bila kusemeshwa na
mtu. Na safari hii hakuazima chochote kutoka kwa baba yake. Kimya tu.
“Joshua
amefika baba. Nitakupigia baadaye.” “Sawa mama. Uwe na siku nzuri huko.
Ufanikiwe.” “Amina baba yangu.” Naya akachukua pochi yake, wakati anatoka Bale
akamuwahi. “Naya, hutanikuta ukirudi.” “Kuwa mwangalifu sana Bale. Usijekuta
unachokitafuta mbeleni, unakiacha nyuma na ndicho wenzio wote wamekuwa
akikitafuta.” “Wewe ulitegemea nikae hapa nikimsubiria huyo Joshua au
bahati inijie hapa ndani mpaka lini?” “Nitakupigia simu baadaye baba. Naomba
kama alivyokwambia Joshua na Geb, jana pale kwa kina Magesa msubirie yule fundi
akushauri vizuri na akusaidie ili wamalize mapema.” Bale akashangaa sana. Jana
wakati hayo yakizungumzwa yeye alikuwa nje akizungumza na Malon.
“Kwa hiyo
ndio mnaendesha mambo humu ndani bila mimi kujua!? Yaani mimi ndio nimekuwa mtu
wa nje tu, Joshua ndiye anayejua mambo ya humu ndani!? Mipango muhimu ya humu
ndani inaendelea bila mimi!?” “Jana pale nyumbani kwa kina Magesa, ulipotea kwa
muda mrefu sana Bale. Kwanza hukujua nini kinazungumziwa kwa kuwa katikati ya
mazungumzo yote wewe ulikuwa ukichati. Macho kwenye simu muda wote kisha
ukatoka kabisa. Na ndio maana nilikufuata nje. Haya yote yalizungumzwa wakati
wewe upo palepale na ulipotoka, Bale. Hapakuwa na usiri wowote. Yote
yalizungumziwa palepale mbele ya watu wote, Nanaa na mumuwe ndio waliokuwa
wakimshauri baba jinsi nzuri ya utunzwaji wa hayo mazao atakayokuwa akiletewa.
Palepale mbele ya watu wote na Joshua alisema ananyamaza kabisa akisema
wazi huo utaalamu yeye hana, na yeye anajifunza pale. Tena wote wakamcheka. Na
James kumtania kidogo kuwa amefikishwa uwanja wa ugenini, lugha ya kichina.
Yote hayo yaliendelea pale.”
“Haya,
tuliporudi hapa, mbele ya Joshua, kwenye siku yetu muhimu, ukaanza matusi.”
“Nimemtukana nani mimi?” Bale akauliza kwa ukali. “Muwahi mwenzio mama.
Usichelewe kazini. Na sitagusa chochote tena mpaka huyo fundi aje. Walishanipa
namba yake. Wamesema saa nne asubuhi atakuwa ameshafika kule kwenye lile duka
letu, Kibaha. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi. Nenda kafanye kazi.” “Asante baba.”
Naya akatoka.
Joshu&Naya.
Akamkuta
Joshua akimsubiria nje ya gari. “Samahani nimechelewa.” “Usijali. Twende.”
Baada ya kufunga mkanda na yeye, Joshua akaondoa gari. “Ulilala salama?”
“Nilitamani kukupigia lakini nikaona nikuache upumze kwanza.” “Nilijua
umenichukia, na mimi nikaona nikuache kwanza.” Naya akawa hajaelewa. “Kwa nini
nikuchukie tena Joshua!?” “Mimi najijua Naya. Kuna wakati na mambo mengine
nakuwa kama slow. Mchelewaji fulani hivi, kama ninayetakiwa kufanya jambo
fulani kwa haraka lakini nachelewa!” “Sivyo nikuonavyo Joshua. Kwa
nini ufikirie hivyo!?” Naya akamuuliza akijaribu kufikiria ni nini kinampelekea
Joshua kudhania hivyo.
“Nahisi
kama pengine nimechangia kwa asilimia fulani kwa Bale kuondoka nyumbani!” Naya
akashangaa kidogo. “Kivipi tena!?” “Basi. Nahisi labda nimejishuku tu.
Nilifikiri pengine ungenilaumu kwamba pengine ningemtafutia kazi mapema
asingefikiria kuondoka.” Naya akatulia kidogo kama anayefikiria, Joshua akahisi
amempa jambo ambalo hata hakuwa nalo kichwani. “Samahani. Nahisi
nimekupandikizia mambo ambayo hata hukuwa nayo!” “Umepatia kwa upande mmoja
lakini jiulize je, ungekuwa umemtafutia kazi. Halafu pengine isilingane na
ahadi alizompa Malon. Maana hatujui ni nini Malon amemuahidi. Kisha akatakiwa
aanze kazi leo. Au akawa ameanza kazi kwa mtu ambaye mnaheshimiana naye sana.
Kisha akaondoka kwa mtindo huuhuu. Kwako ingekuaje?” “Daah! Na
pengine ndio maana nilikuwa nikisita Naya.” Joshua akaongea
akisikika kupata aghueni ya utetezi.
“Naomba
niwe mkweli kwako Naya. Utakuwa mke wangu, nataka unielewe mapema. Ni mambo
machache sana ambayo siyafanyi bila kumshirikisha Mungu na kumuomba Roho wa
Mungu aniongoze. Nilimuomba Mungu juu ya jinsi ya kushirikiana na Bale, lakini
kwa hakika sikupata kibali. Sikujua jinsi ya nini chakufanya naye. Ndipo
nikaamua kumpa muda kumwangalia yeye ni mtu wa namna gani kabla sijamuwekea
dhamana popote.” “Na mimi nilimwambia hivyohivyo Bale. Tena wala si siku
nyingi. Jana tu. Nilimwambia uwezo wa kumtafutia kazi unao. Lakini
nimeishi na wewe kwa muda mfupi lakini nimekuona unapenda watu wanaojua ni nini
wanataka na kukisimamia. Nikamwambia pengine na wewe unamsubiria yeye. Lakini
acha nikwambie ukweli Joshua.” Naya akaendelea.
“Kwanza
sikulaumu kabisa. Haikuwa hata kwenye mawazo yangu ila jana nilijisikia tu
vibaya ndio maana nikashindwa hata kukupigia simu. Kile ulichokiona jana si
kigeni kwetu kwenye ile familia.” “Kipi sasa?” “Aina ile ya mazungumzo kwa
baba. Ila mara nyingi tulizoea kuona kutoka kwa mama. Tumekuwa tukiona vile.
Malalamiko yasiyoisha kwa baba. Sasa kwa kuwa Bale amekuwa mtoto wa mama tokea
anazaliwa. Hujui jinsi nyingine sahihi yakuzungumza na baba
isipokuwa ile aliyomuona mama akizungumza naye.” “Naya! Kwa nini kwa mzee
mkimya hivyo!?”
“Nafiri
hilo limechangia. Laukimya wakupitiliza ndipo anaonekana kama mzubaifu.
Asiyefikiria na mengine mengi. Halafu kwa kuwa yeye alikuwa mfanyabiashara,
hakuna inapoonyesha kipato chake kwa mwezi, pesa yake ikiingia ikawa ni ya
wote, haikai. Ila ya mama ikawa yakueleweka. Mshahara wa kila mwisho wa mwezi
wa uhakika wakupigia mahesabu ya kueleweka kwa vitu vya pale nyumbani.
Unapomsikia Bale akisema Malo amesaidia pale nyumbani, hakuongopa. Ni kweli
alisaidia kwa mali, kitu ambacho mama hakutaka kabisa. Kilikuwa kikimuuma sana,
nakuchukia mpaka ikabidi niache kuwashirikisha kama nalipa madeni kwa pesa ya
Malon, ila kazi nilizokuwa nikifanya mimi mwenyewe. Lakini ukweli madeni mengi
alitusaidia kulipa na alikuwa hata akitoa na pesa za matumizi kwa kina Bale,
bila hata kuombwa. Au kwa haraka kama ulivyomsikia Bale. Hakuwa akijua kusubiri
anaamua tu na kuwapa pesa za matumizi. Ndipo Malon akafanyika kama kaka kwao
mbali na mahusiano yetu sisi wawili.” Hapo Joshua akapoa.
“Lakini
ndipo linapokuja swala la mwisho ninalotaka kukwambia Joshua. Sijui kama
unakumbuka majibu uliyompa Malon?” Joshua akamwangalia na kuendelea kuendesha.
“Naamini ulimaanisha na hukuongea katika upande wa hasira.” “Japo nilikuwa
nimekasirika, lakini unanijua siwezi kuzungumza kitu kumfurahisha tu mtu.
Lakini nataka kujua ni upande upi unao zungumzia wewe!”
“Unakumbuka
ulimwambia Malon tupo kwenye kujenga msingi wetu? Kwamba itakuja kufikia
wakati na sisi tutaweza kusaidia nyumbani.” Joshua akatulia kidogo. “Naomba
tusimamie hapohapo. Tafadhali usiyumbishwe na Malon. Mimi namjua, kwa kuishi
naye. Na nilikuhakikishia atarudi tu. Tena na sababu ya kueleweka
kabisa.” “Aisee sikutegemea kama ingekuwa kwa haraka hivyo!” Naya akacheka kwa
kusikitika.
“Ni
kwanini anafanya hivyo!?” “Kwanza mimi nahisi ni muoga au hataki kujifunga
kwenye mahusino yatakayomfunga nakumfanya kuwajibika moja kwa moja. Nahisi
hivyo kama alivyosema baba yake. Ndio maana akiona ameanzisha jambo na mtu,
halafu huyo mtu akataka hatua nyingine ya kumfunga, anajitoa. Ndio baba yake
alisema watu wote tunataka kitu kimoja tu kwa Malon ambacho hana uwezo wakumpa
mtu yeyote yule. Ni bora atoe pesa nyingi, lakini si vinginevyo. Wote tunaishia
kuumia, lakini lazima kumuelewa Malon. Hana huo uwezo wa kujifunga kwa
mtu mmoja na hajui inakuaje kwa sababu Malon alikimbia malezi ya nyumbani na
kujiingiza mtaani. Akachagua fungu baya. Ndio maana baba alifurahia sana
aliposema ameokoka. Akamwambia amefanya jambo zuri. Hajachelewa hata kidogo.
Akamshauri atafute mazingira, tena akamwambia hata kwa kulazimishia, awe
kanisani. Awe mshirika kabisa anayejua mambo ya kanisani kama familia katika
mwili wa Kristo. Ili sasa akulie wokovu. Malon akamwambia aina ya biashara
aliyonayo inamfunga.”
“Baba
akamwambia Mungu yupo popote, hata huko Mbeya lazima atafute kanisa sio lazima
mpaka awepo huku Dar ndipo ahudhurie kanisani. Asisubiri miezi kwa miezi ndipo
arudi kanisani huku Dar. Akamwambia Mungu anamtaka yeye zaidi kuliko
pesa anayotoa kanisani kwao huku Dar. Maana ni kweli Malon anatoa pesa pale
kanisani kwao na kusaidia vijana. Zayoni alikuwa akienda huko. Au niseme kwa kifupi
ni mtoaji popote na kwa yeyote. Kwao pia yupo hivyohivyo kusaidia ndugu zake
sana. Amewainua sana kwenye maisha. Lakini hataki mahusiano na yeyote, na
usimwambie chochote. Zaidi kumkosoa kwa chochote. Hapo mtakosana. Kidogo
nilimuona anaweza kumsikiliza mama yake ila si mwingine yeyote. Bora akupe
pesa, muachane sio mumfuate nyuma.”
“Anyways, baba
akamshauri ajiingize kanisani, atulie kanisani ajifunze kwa upya. Hajachelewa.
Akamwambia ipo garama ya kulipa. Kugawa muda wake mchache, lakini lazima
alazimishie na kuwepo kanisani kama vile alivyoweka juhudi za makusudi kwenye
biashara yake na kufanikiwa sana, basi aweke juhudi atulie kanisani lasivyo
atapoteza kitu cha thamani sana alichopokea. Tena baba akamwambia lile andiko
la ‘I Pretro 5:8-9 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi
huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza’. Baba
akaongeza kwa kumuwekea msisitizo kwa ule msitari wa 9 kuwa Mungu
ameagiza ‘Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani’.” “Ambayo ni kweli.”
Joshua akaongeza.
“Basi,
baba akamwambia hawezi kumshinda shetani nje ya Yesu, lazima ajifunze pia ni
jinsi gani yakuishi kwenye imani. Hayo baba anazungumza naye wala hatukuwa
kwenye mahusiano naye ya kimapenzi, ila kama kijana wake tu au niseme kama Bale
vile. Tena ilikuwa kwenye mazungumzo tu, baba aliporudi kutoka Mbeya na baba
kuona vile alivyofanikiwa sana. Katika kuendelea kumpongeza na kumwambia
japokuwa anajituma sana, lakini kwa hakika na mkono wa Mungu uko juu yake ndipo
akamuuliza kama amefanikiwa kupata kanisa na kule Mbeya. Nimeongea mengi lakini
kujibu swali lako, sababu ya kwanza na kubwa ni hataki na hajui kujifunga
kwenye mahusiano na mtu. Kwangu yupo kwenye kusitasita kwa kuwa najua
amenipenda, ndipo inakuja sababu ya pili sasa.”
“Hakuna
jinsi Malon akaniona au kusikia nipo na mwanaume mwingine akatulia, Joshua. Na
amekuwa hivyo kila wakati. Anatoka akiamini sitapata mtu. Akisikia tu nina mtu,
anarudi kuchungulia. Sasa safari hii ameshindwa kuniingia tena. Mlango
wa kwa baba umefungwa, tena kwa kuufunga yeye mwenyewe. Ameshindwa kuutumia
kama alivyozoea siku zote. Kutoka na kuingia akijua baba huwa anampokea, halafu
mama ndiye aliyekuwa mbali naye. Sasa safari hii baba amemuacha kabisa.
Akiamini ameshamwambia yote aliyopaswa kusikia, anamuachia yeye mwenyewe
kuchukua hatua.”
“Unakumbuka
kuniona nasoma ujumbe siku ile ya kwanza uliponipa maua, tena tulikuwa
tunakaribia kufika nyumbani?” Joshua akatulia kidogo kama anayevuta kumbukumbu.
“Ukaniuliza nimesoma nini kwenye simu kilichotaka kunibadilisha furaha yangu,
nikakwambia ni ujumbe kutoka kwa Zayoni, ila hakuna kipya, nikarudi kwenye
kuimba?” “Oooh yeah! Tulikuwa tumekaribia sana nyumbani. Si ndivyo?” “Sawasawa.
Basi Zayoni alikuwa amenitumia ujumbe kuniambia Malon yupo pale nyumbani, baba
amemkaribisha ndani. Akampa chai aliyokuwa amejitengenezea yeye kwa kuwa
alikuwa amefunga. Akampa na Malon. Chakula kilipokuwa tayari akampa na chakula.
Ila akaniambia hajazungumza naye chochote amemuacha tu mpaka Bale alipokuja
ndio Bale akaendelea kuzungumza naye.”
“Sasa kwa
jinsi mambo yalivyokuwa, baba akijaribu kumkarimu na kuzungumza naye Malon kila
wakati na akitaka kumsikia kila akifika pale nyumbani, kitendo cha baba kumpa
tu chakula bila kuzungumza naye chochote, atakuwa amejua kabisa milango na kwa
baba imefungwa. Ndio sasa, sasahivi ameamua kuweka nguvu kwa kumtumia Bale,
asijue naye Bale anakaribia kufungiwa mlango na baba.” “Daaah! Ile ni mbaya
Naya! Mbaya sana.” “Ni kwa vile alizungumza mbele yako tu. Lakini ndivyo
anavyozungumza na baba wakati wote, zaidi anapokuwa na hasira. Na jana
nimekwambia nilizungumza naye. Nilimwambia juu ya hilohilo. Lakini najua
itachukua muda na maisha kumfunza mpaka aelewe jinsi ya kuzungumza na baba na
kuelewa nafasi ya baba. Mungu atamsaidia tu.” Joshua akafikiria kidogo akaona
aseme tu.
“Nikuulize
kitu Naya?” “Uliza tu.” “Katika amri ZOTE za Mungu. Namaanisha zooote
unazozijua hata kusikia tu, unakumbuka ni amri ipi yenye ahadi?” Naya
akatulia kufikiria, akakumbuka. “Amri ya 5 katika zile 10 za Mungu. ‘Waheshimu
baba yako na mama yako, upate baraka na uishi siku nyingi duniani.’ ”
“Sawasawa. Na unafikiri ni kwa nini ile tu ndio yenye ahadi? Wakati katika zote
hataYesu mwenyewe alisema wakati yule mwanasheria akimjaribu mbele ya
Mafarisayo na Masadukayo alipomuuliza amri kuu ni ipi, unakumbuka jibu la
Yesu?” Naya akatulia kufikiria tena, maana swali la kwanza alijibu kwa haraka
bila kufikiria.
Joshua
akatulia tu kumpa nafasi. “Yesu alisema amri iliyo kuu ni ‘Mpende
Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako
zote’.” Naya akajibu. “Lakini akamalizia kusema hivi, ‘Hii
ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Mstari wa 39 katika
kitabu cha Mathayo Yesu aliendelea kusema hivi, ‘Nayo ya
pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Akaongeza
kusema kuwa, ‘Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria yote na Manabii.’ Unakumbuka?”
Ikabidi Naya akae sawa akitaka kuelewa ni nini Joshua anataka kusema na aelewe
zaidi.
“Aisee
nimekumbuka!” “Sasa, katika zote na yote tokea mwanzo Mungu mwenyewe
anazungumza na Musa, akimpa hizo sheria mpaka Yesu anamjibu yule Mwanasheria,
umesikia ahadi yeyote nyingine Mungu kuahidi kumfanyia mwanadamu, au
baraka au zawadi atakayopata endapo atatimiza hiyo sheria mbali na amri ya
5?” Hapo Naya akatulia. “Fikiria tu na nikumbushe kwengine
palipoandikwa kwenye bibilia, kwenye amri aliyotoa Mungu kisha akaambatanisha
na ahadi/baraka au tuseme zawadi nyingine yeyote, hata hizo
sheria mbili Yesu alizosisema ni kuu, kisha akaweka msisitizo juu
yake kuwa ndizo msingi wa sheria zote na manabii wote
walisimamia hapo. Je, unakumbuka kama kuna ahadi nyingine
Mungu kuahidi kutoa kwa atakayetimiza hizo sheria hata ile ya kwanza na ya pili
inayomuhusu Mungu mwenyewe, umesikia ahadi yeyote ile mbali na ya 5?” “Aisee
hapana Joshua!” Naya akajibu akiwa na mshangao.
“Ulishafikiria
kwa nini? Yaani huyu Mungu aliyejitambulisha kwa Musa na kumwambia awaambie
watu kuwa yeye ni Mungu mwenye wivu, asiabudiwe mungu
mwingine yeyote ila yeye tu! Yaani asitoe ahadi hapo kwa watakao tii
kumuabudu yeye, eti aje atoe ahadi ya maisha marefu yenye baraka hapa duniani,
eti kwa kumuabudu baba na mama yako! Tena wanadamu aliyewaumba yeye mwenyewe!?”
Naya akatulia.
“Kwenye
kitabu cha Waefeso 6:2-3 hata Mtume Paulo amezungumzia hilo na kusema, ndiyo
amri ya kwanza na yenye ahadi! Nenda kasome vizuri wewe mwenyewe jinsi
hata Mtume Paulo alipoliona hilo. Yaani huyu Mungu mwenye enzi yooooote,
asitoe ahadi kwa yanayomuhusu Yeye, iwe mwanadamu! Inaingia akilini kweli?” “Kweli
umenifanya nifikirie, Joshua!” “Basi jua hapo ndipo kwenye siri kubwa na nzito.
Mungu akusaidie kuelewa.” Joshua akatulia kumpa nafasi Naya na yeye atafakari.
Kisha
akaendelea. “Unajua Naya. Kadiri tunavyokua. Au watoto wanavyokua, ndivyo
uelewa unavyopanuka. Na kwa kizazi hiki tumepata na neema ya elimu, ambayo
wazazi wamegharamia kwa uzima wao na uelewa wao, kwa kadiri Mungu
alivyowawezesha wao. Wengine hata kwa kukopa, halafu sasa tukawa na
tekinologia. Maisha na mambo yamerahisishwa mno. Ni rahisi sana kusimama na
kukosoa juhudi nzima za wazazi, bila kujua sisi tuna nguvu na uwezo wa kuona
yote hayo kwa sababu ya msingi walioweka wao. Ile kuona tu hili ni kosa,
haikutakiwa iwe hivyo kwanza ni neema ya ajabu, inamaana umelelewa sahihi kiasi
cha kutambua kisicho sawa, si sawa. Sijui kama unanielewa Naya?” Naya
kimya akisikiliza.
“Wapo
vijana wangapi wameridhika tu mtaani wakilalamikia maisha bila kuchukua hatua?
Wapo vijana wangapi wanaishi dhambini tu na hawasumbuliwi nafsi zao? Wewe
hudhani kujua hiki si sahihi, na ukapata akili ya kuchukua hatua, hudhani kuwa
ni neema na makuzi sahihi? Kule kujua natakiwa kusonga mbele, na nisibweteke.
Kukawa na mazingira ya kuita nyumbani, haijalishi pana sura gani, hudhani kuwa
ni juhudi fulani iliwekezwa kwa huyo mtu mpaka kufikia hapo?” Naya akatulia.
“Hakuna
msingi dhaifu uliowahi kutoa nyumba bora, Naya. Hata bibilia inathibitisha
hilo. Hakuna. Sikuwahi kulisema hili kwa mtu, lakini wewe unavyofikiria
Naya, mimi sikutambua makosa ya mama yangu? Niliyajua kwa hakika. Hata sasa
nikikaa na kutafakari najua kwa hakika mama hakuwa mjinga kiasi cha kutofikiria
au hata kuhisi anajiingiza kwenye mahusiano yasiyofaa na baba yangu ambaye
alikuwa mtumzima sana kwake. Haya, alikosea kwa baba yangu, akarudia tena kwa
aliyemuachia ugonjwa na ndio maana hata nyumbani kwao walikuwa wakimsimanga.
Kuwa aliishi maisha yasiyofaa. Lakini Naya, nilirudi kijijini, nikamlea mama
yangu mpaka kifo. Sikuwahi kumuuliza wala kumsimanga juu ya hilo kwa kuwa najua
na yeye alikuwa akijua alikosea kwingi tu, na pengine kujutia, ila mimi kama
mtoto haikuwa nafasi yangu.”
“Mungu
anaposema waheshimu wazazi, ni kwa kuwa anajua kuna wakati si rahisi
Naya. Ni ngumu kwa kuwa tunafika kipimo cha kupevuka akili, unagundua makosa
yao mengi. Ipo hekima ya kukabiliana na makosa yao, endapo Mungu akikupa hiyo
neema, ila kama hukujaliwa, ni bora ukae pembeni kwa kuwa na wao ni binadamu.
Wanaweza kukubali kosa, au wakakataa. Wengine wanakataa kwa kugomba waziwazi
kabisa kwa kukataa kukosolewa. Na wengine hubaki kusononeka tu.” Joshua
akaendelea.
“Hawa
mapacha wa mama G, hawa. Kwa kumuona Geb na Grace na watoto wao kama
unavyowaona. Wanaakili ile ambayo Geb huwa anasema wakati mwingine ni kama
laana. Hawasahau kitu.” “Kama Magesa?” “Hivyohivyo. Geb anasema hakumbuki
kukosa swali lolote kwenye mtihani kama alifundishwa na kusoma. Mama
yao anasema ni akili ya baba yao wala si yeye. Lakini Naya, wale watoto
wanamtii mama yao, hujawahi ona. Geb na mapesa yote yale, na Grace hivyohivyo,
mpaka leo, Grace huwa anasema jicho la mama yake linawanyanyua popote pale.
Anasema hata kama Geb amekasirika vipi au ametingwa kwa kiasi gani, lakini na
yeye akilipata hilo jicho, ananyanyuka bila swali.” “Sijaelewa.”
“Grace
anasema yeye na Geb wamekua wakimtizama mama yao. Kuna jinsi akiwaangalia bila
hata kusema, hata kama wapo katikati ya watu wanaelewa na kutii. Yule mama
harudii neno mara mbili kwa Geb wala Grace.” “Aisee kweli Joshua! Nilimuona
pale kanisani pia.” “Sawasawa. Mama yake aliposema asimame na atoke na familia
yake, ulimuona alichukua hata dakika?” “Daah! Kweli aisee.” “Basi na Grace huyo
dada yake yupo hivyohivyo. Hata Nanaa ulimuona ni kama alilalamika kidogo ndipo
akatoka.” “Tena alichukua muda kidogo, lakini si Geb.” Naya akaongeza akijaribu
kuvuta kumbukumbu.
“Basi
naona umenielewa sawasawa. Ndicho kingine kilichonivutia kwa yule jamaa.
Anapesa haswa. Lakini linapofika swala la kuwa mtoto, aisee utashangaa! Sasa
jiulize kwa akili kama ya aina ile ya watoto. Na mama kama mama G ambaye na
yeye alizaa na mume wa mtu. Wakapita kwingi na hata kwenye historia ya Nanaa na
Geb, Grace na yule mume wake wa kwanza pia yule mama kwa kumsikia yeye mwenyewe
anasema anayo majuto mpaka leo kama alichangia matatizo fulani hivi, tena
anasema makubwa mpaka kujilaumu vifo vya wajuu zake wawili, na kuwatenganisha
pia Nanaa na Geb kipindi fulani pamoja na watoto wao, mpaka Nanaa akaja
kusamehe.” “Ilikuaje? Maana ukiwaangalia wale huwezi amini kama walishapita
huko!”
“Wanahistoria
yao ngumu kweli. Utakuja kuwasikia wenyewe siku moja. Lakini katika yote hayo
yule mama aliyowatendea wanae, na kukosa kwingi, lakini hata kama Geb anaongea
na simu ya muhimu vipi, yule mama akimuita tu, aisee anaitika! Hata kama amekaa
chini, atasimama kwa haraka kama Grace tu, mpaka mimi nililiona hilo. Sasa wewe
jiulize kwa nini wale watoto bado wanatii? Kwa nini wamebaki kumuheshimu mama
yao ambaye ameshawaletea matatizo makubwa hivyo maishani? Kwamba si mama
mkamilifu pia. Ni kama wadamu wengine wowote wale. Lakini kwa nini abaki
kuheshimiwa vile?” “Mmmh!” Naya akaishia kuguna.
“Basi
ndio ujue kuna waliogundua siri. Wakakubali kutii hivyohivyo hata kama ni chungu
kumeza, wakakubali ndio wanaopata heri na maisha marefu hapa duniani. Wote
tunaishi, lakini kuna wenye heri Naya. Wapo. Na heri zao zinatoka kwenye
ahadi ya Mungu mwenyewe. Na wahenga wanasema, sikio halizidi kichwa. Hata
ufanye nini, haliwezi kuzidi kichwa. Hata kama unazo shahada tatu, mzee ni
mkulima yule aliyekuwa akiuza mahidi au pombe kilabuni ili usome, bado wanasema
huwezi kumzidi. Unafikiri kwa nini waseme hivyo?” Kimya, Naya akitafakari.
“Basi ujue na wenyewe waligundua siri.” “Mmmh!” Naya akapoa kabisa
na kubaki akitafakari.
Kisha
akaongeza. “Tatizo la Bale ni kama anamuona baba hana uwezo mkubwa wakufikiria,
ndio maana hatuna mamilioni ya pesa. Mimi nilishamuuliza kwa jinsi
alivyozunguka hapa nchini, kwani ameona ni wazazi wangapi wana uwezo mkubwa
sana mpaka baba aonekane yeye ndio hafai! Wengine wanashindwa hata kusomesha
watoto wao hata na kuwalisha au kuwatunza kwenye nyumba kama ile yetu tu,
wanaishia kwa wajomba na mashangazi! Nilipokuwa shuleni wala sikuwa peke yangu niliyekuwa
nikihangaika maswala ya ada! Wazazi wengi tu hawana uwezo, wakilia maisha
magumu kama sisi tu! Hapahapa nchini wala sio sehemu nyingine! Wazazi wenye
pesa ni wachache sana! Lakini asilimia kubwa sana ya watu wanaangukia kwenye
kundi letu, na wenyewe wazazi wao wamehangaika mpaka watoto wamekua!
Nilishamkumbusha hilo huyu Bale. Nikamwambia wengine wamekuwa mpaka mawaziri
kabisa, wazazi wakiwa mafukara tu! Au kwani wote walioko huko maofisini au
bungeni walitoka kwa wazazi mamilionea?”
“Si kweli
Naya. Utajiri wa mali upo kwenye mikono ya watu wachache sana. Wapo
waliochangamka, maneno mengi tu zaidi ya baba Naya na bado hawana pesa. Baba
yako au maisha yenu hayana tofauti na wananchi wengi hapa nchini. Geb mwenyewe
anasema amesomeshwa na mama yake kwa kukopa na kuuza mali zote alizokuwa
ameachiwa urithi na baba yao mpaka akapata shahada tatu! Yule mama alikuwa
akikopa, kufanya biashara ili tu wanae waishi. Geb alipofanikiwa ndipo
akamuinua tena mama yake pamoja na dada yake. Anasema walishaishi kwenye nyumba
ya kupanga, ila chumba kimoja.” “Joshua!” Naya akashangaa sana.
“Hakika
tena. Tena eti waliishi kwenye chumba kimoja, ndani ya nyumba ya wapangaji
wengi. Yaani wote wale watatu na mume wa kwanza wa Grace humohumo ndani.”
“Joshua wewe!” “Acha Naya wewe. Watu wanakufuru bwana! Nyinyi mnaishi kwenye
nyumba yenu, mpaka uzio! Nyumbani kwenu na kiwanja kinasubiri nyuma ya nyumba
halafu mnaona baba yenu hana akili ya maendeleo! Watu wanahistoria ngumu bwana!
Humuwezi nyinyi kujilinganisha hata na walipokuwa kina Magesa tu. Ukisimuliwa
habari zao wale, huwezi amini kule walikotoka. Lakini ona walipo sasahivi! Mali
walizonazo na bado wanamuheshimu sana mama yao!” Joshua akaongeza na kuuliza.
“Nifanyeje
Naya?” Akabadilisha mazungumzo na kurudi kwa yanayo wahusu. “Ukibadilika tu,
mimi ndiye utakayeniumiza. Tafadhali endelea kuwa Joshua
Kumu Mungu aliyekuleta kwangu, siye Joshua atakayechanganywa na
kutengenezwa na Malon. Wote tutakosa kimbilio, Joshua. Tafadhali usiyumbishwe.
Si na muonekano wake wa nje na wala aina ya utoaji wake. Fanya kama Joshua
Kumu, kama ulivyoanzana na baba na si vinginevyo.” “Ni kwa kuwa nimeona
kuwekeza kwa baba yako ni sehemu sahihi. Yupo tayari. Ni kama kumpa maji ya
kunywa mtu mwenye kiu sana. Hata Geb ameliona hilo ndio maana yupo tayari
kuwekeza kwake na kumpa fundi wa kampuni yake ili ajue jinsi ya kusaidia, tena
kwa haraka.”
“Basi
naomba usiyumbishwe. Tafadhali baki kuwa Joshua Kumu. Fanya maamuzi hata
unayoyaona ni magumu.” “Hutanikimbia?” “Siku nitakayokuapia kuwa nitakuwa na wewe
mpaka kufa, au siku nilipokwambia nitakuwa na wewe, ujue mpaka wewe mwenyewe
utanihurumia.” “Basi nakushukuru kusimama na mimi Naya. Asante kunitia moyo.
Jana nilikuwa na hali mbaya! Mpaka nikashindwa kitu cha kukwambia.” Naya
akacheka.
“Nini?”
“Sikutishi Joshua. Lakini jua Malon atarudi. Atarudi tena. Na kama
hatashindwana na Bale, ujue atarudi safari hii Bale akiwa upande wake. Atafanya
nini, na akitumia sababu gani, sijui. Ila usiruhusu kutishwa naye.
Simama mbele yake kama ulivyosimama siku ile mpaka ukafanikiwa. Hajazoea hivyo.
Wewe umemtisha. Na baba kuonekana kukukubali wewe waziwazi vile, ndio maana
nahisi amerudi kwa haraka. Hakuchukua muda mrefu. Kwa hiyo naomba tutengeneze
msingi wetu ambao tutasimamia bila kuyumbishwa hata na mambo ya familia yangu.
Usikubali kuyumbishwa.” Hapo Kumu akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha
taratibu kama aliyetua mzigo.
“Apatae
mke, apata kitu chema. Naye, anajipatia kibali kwa Bwana.” Naya alicheka sana.
“Mimi Kumu, nimepata kitu chema na nimepata kibali kutoka kwa Bwana.
Nakushukuru kwa kuniamini na kuamua kuongozana na hiki kichwa changu. Umeifanya
siku ya leo iende vizuri, na kunirudishia ujasiri.” “Karibu. Sasa turudi kwenye
mipango yetu.” Angalau wakaanza kuzungumza mengine na kucheka mpaka walipofika
kazini kila mtu akiwa ametulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alimsindikiza
ofisini kwake, akamuacha hapo akifanya kazi kwa makubaliano mida ya chakula cha
mchana watoke wakatengeneze pete kufanya ienee kidoleni kwa Naya. Na jioni
wakitoka, wakutane na kina Magesa kwa chakula cha jioni wao tu wanne bila
watoto. Geb, Nanaa, Naya na Joshua. Hilo likakaa sawa. Naya akahamisha akili
kazini kama kawaida yake. Akapangia kila mtu kazi, kisha akaanza kufanya kazi
nyingine mpaka mida ya saa mbili kasoro, wenzake walipoanza kuingia hapo, Naya
asijue picha zake akichumbiwa zilienea kampuni nzima. Jamali akaanzisha kikao
kwa kuanza kumpongeza Naya. Naya akacheka akionyesha hakuwa ametarajia hilo.
“Asante bosi wangu.” Akashukuru.
Ndipo
akaweka msisitizo wa kazi. “Mama Kumu, si na leo utasaidia kama siku ile? Ule
mtindo wako naona utanifaa sana hapa.” “Nishaandaa kila kitu kutokana na kazi
nilizokuta hapa.” “Daah! Naona mwaka huu kama kitengo chetu hakitashinda, mimi
nitajua kuna mkono wa mtu tu.” Jamal akaongea kwa furaha kama kawaida yake
kupenda kufanyiwa kazi. Wakati akimalizia kikao, akaja yule msaidizi wa CEO na
Joshua. Wakasubiri ili Jamal amalize. Na yeye hakutaka mengi, hapohapo akafunga
kikao.
“Mbona
kama Jamal anatukimbia?” Akauliza msaidizi wa CEO aliyekuja na Joshua. “Hataki
siri za kitengo chake zisikike.” Joshua akawa kama anamtetea Jamal. “Nimemaliza
viongozi.” Akajibu Jamal na cheko akisikika kupaniki kidogo. “Mimi
nipo hapa kibinafsi kumpongeza Naya. Nilikuwa safarini juzi,
nikashindwa kuhudhuria tafrija.” Akamsogelea Naya pale mezani, Naya akasimama
na cheko akimtizama Joshua. “Hongereni sana.” “Asante. Tunashukuru.” “Tuone
pete aliyokupa Kumu. Asitutie aibu hapa mjini.” Joshua alicheka sana, wawili
hao walionekana kufahamiana kwa karibu. Alikuwa mtumzima, mkubwa kwa umri
kumlinganisha na Joshua. Alionekana kushiba mamlaka kama Joshua tu. Msafi na
suti yake pamoja na tai.
“Sijawaangusha
bwana!” Kumu akajitetea akicheka sana. “Acha mimi ndio niwe muamuzi wa hili,
Kumu. Tusije wote tukaonekana hovyo huko mtaani. Hakuna maandalizi mazuri.”
Wote wakaendelea kucheka. Naya akanyanyua mkono, akaupokea kuangalia hiyo pete.
Wote wakamuona anacheka. “Vipi?” “Heshima yako Kumu.” Joshua alicheka sana.
“Kuoa ruksa?” Joshua akauliza. “Kabisa. Tunakukaribisha chamani. Unaonekana
utamudu majukumu, hutatuangusha.” Walikuwa viongozi wao wakubwa sana hapo
kwenye kampuni wakifanyiana utani mbele ya Naya. “Hongera sana Naya.”
“Nashukuru, asante.” Hilo tu ndilo alilomudu kusema Naya. Hakujua azungumze
nini tena mbele ya bosi zake. Wapo kazini.
Wakatoka
wakitaniana. “Harusi lini?” Wakamsikia akimuuliza Kumu huko koridoni. “Aisee
nasubiri taratibu za kanisani zikamilike, nioe. Sina sababu yakusubiri tena.”
“Ndio haraka hivyo!?” “Kabisa. Ndani ya majuma machache sana, nitakuwa na hili
nimefunga.” “Hongera sana Kumu. Unastahili aisee! Mimi mpaka nikaingiwa na
wasiwasi! Ukimya ulikuwa mzito mno! Hapakuwa hata na fununu kokote hata za
mtaani tu!” Wakasikika wakiendelea kucheka, sauti zikiishia koridoni. Naya
akarudisha akili kazini.
Wakapita
tena viongozi wengine wa hiyo idara yao ya masoko wakimpongeza. Wao walikuwa na
vyeo kama vya Jamal ambao Naya alikuwa akiwaona tu na kumpita, siku hiyo
walifika kumpongeza. Na walikuwepo siku ya jumamosi nyumbani kwa Kumu
akichumbiwa, wakamuomba kupiga naye picha. Nao Naya akawachangamkia tu na
kupokea pongezi. Akawashukuru wote kwa kuhudhuria. Kweye hiyo idara yao ni
Jamal peke yake ndiye aliyekuwepo siku hiyo yakuchumbiwa kwake, wengine
walisikia tu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mida ya
chakula cha mchana Joshua akarudi. “Mimi nipo tayari na nimekuombea ruhusa kwa
Jamal, maana tunaweza kuchelewa kurudi.” “Nashukuru. Hata mimi nimemaliza.
Tunaweza kutoka.” Naya akachukua pochi yake na kutoka akiongozana na Joshua.
“Mbona unacheka?” “Nimefurahi Joshua! Bado siamini.” Joshua akacheka wakati
anaondoa gari. “Nimefurahi kama na wewe umefurahia. Na mimi ninafuraha sana.
Ilitaka kuharibika jana, lakini umenifariji asubuhi, imerudi.” “Namuhurumia
Bale! Hakika namuhurumia sana.” “Umejua amefikia wapi?” “Wakati
Zayoni na baba wakiwa wanaelekea Kibaha kumsubiria fundi wa wakina Magesa,
amenitumia ujumbe kunitaarifu na kuniambia Bale aliondoka kwenye mida ya saa 12
asubuhi.”
“Nashauri
umtafute Bale, kujua amefikia wapi.” “Joshua!” “Hakika Naya. Wewe ndiye dada
yao. Wewe ndiye uliyewaletea Malon pale nyumbani. Na wewe ndiye unayejua nguvu
ya Malon kwa ukaribu sana.” “Joshua jamani!” “Hutaki Bale apotee, si ndivyo?”
“Lakini ameniumiza sana! Anafanya fujo mbele yako, tena siku muhimu sana
kwangu! Na bado eti mimi ndio nimtafute!” Naya akalalamika.
“Unawajibika
kwa asilimia 100, Naya wangu. Wewe kama dada yake na uliyemtambulisha Malon
kwao. Tafadhali anza kuishi hivyo. Wala usishindane naye, kwa kuwa na yeye
anakutegemea umzirie kama alivyozoea siku zote.” “Siku ile yenyewe uliponituma
kwake nikatengeneze naye na hata kumsaidia pesa, hakutegemea. Maana nilimtamkia
maneno mabaya sana kama kawaida yetu tunavyokuwa tukigombana.” “Basi naomba
badilika Naya. Kuwa dada kwelikweli. Na wenyewe waone mabadiliko. Watakuheshimu
tu.” Naya akatoa simu yake.
Damu nzito kuliko maji.
Naya
akampigia, Bale akapokea. “Umefikia wapi?” Bale akashangaa sana.
Akamsikia akicheka. “Sasa unacheka nini, hunijibu?” “Sikutegemea kukusikia hivi
karibuni. Nilijua mmenichukia, hamtaki hata kuniona! Nikajiambia nikahangaike
kivyangu mpaka nifanikiwe ndipo nirudi.” Naya akamwangalia
Joshua kama kumwambia alichofikiria ni kweli. “Hata
usipofanikiwa, unajaribu tena na tena.” Bale akashangaa
sana. “Kwamba hutanicheka wewe!?” “Kwa nini nicheke juhudi zako Bale? Mimi
naamini tutakuja kufanikiwa sana, kwa kuwa nia tunayo na ndoto zetu hazijafa.
Sema ni vile hatujajua njia ipi ni sahihi ya kufikia. Mungu atatusaidia tu.
Tutembee kwa imani.” “Naya! Wewe umeingiwa na nini!?” “Mimi nataka tusipotezane
Bale. Tumekuwa wote kwenye shida na raha. Tumeteteana katika mengi hata
yale ambayo wazazi walikuwa kinyume yetu! Naomba tusitengane sasa hivi.
Ukikwama kwenye lolote lile. Hata ushauri, tafadhali usijifungie mwenyewe. Bado
ukumbuke tunayo hii kazi ya Coca, tunapo pakuishi, na sisi tupo. Usiishi huko
mpweke ukitaabika peke yako.” Bale alihisi anaongea na mtu mwingine na
si Naya.
Ikamgusa
sana. “Daah! Nashukuru Naya. Asante. Na naomba unisamehe. Nahisi
niliomba ruhusa ya kujihami ndio maana nikawa mkali bila sababu. Nikawa ni kama
najitetea tu. Ila tuyaache hayo. Nashukuru kwa kunipigia.” “Utanijulisha kama
utafika salama?” Naya akamuuliza. “Sawa. Nitafanya hivyo.” Bale
akakubali bila shida. Naya akakata.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Daah!
Kumbe kweli Joshua! Alitegemea tumchukie!” “Mungu amekuweka kuwa dada wa
familia, ujue ni dhamana. Mengi itabidi kujikana tu, ili kuweza kuwa dada yao.”
“Ni ngumu, hakika ni ngumu! Ila basi tu. Naomba Mungu aingilie kati. Ila
sikutamani tuje turudi kwenye maisha ya Malon.” “Kama ulivyosema, Mungu
atatutetea lakini pia ni kukusudia kabisa isiwe hivyo kwa kuwa kunakujaribiwa
na yeye anaweza kukujaribu kujua msimamo wako kwa sasa. Umeamua kumuacha kweli
au ni kama alivyozoea kutoka na akirudi unampokea! Na atataka kukuhakiki zaidi
kujua kusudio la safari hii kama ni kweli au ni hasira tu kwamba utakuja
kumkumbuka na kugundua unafanya kosa? Hayo yote atakujaribu tu.” Naya
akanyamaza.
Walifika
kwa sonara wakafanyiwa marekebisho ya haraka kama alivyolipia Joshua. Hakutaka
Naya atoke hapo bila hiyo pete kidoleni. Simu ziliwafanya warudi ofisini na
kushindwa kukaa mahali na kupata chakula cha mchana pamoja. Joshua alipata simu
nyingine tena kutoka kwa Jema akisisitiza kuhitajika yeye mwenyewe ofisini. Ila
alimnunulia chakula Naya na kurudi ofisini. Njiani alimsikia Joshua akijibu
simu alizokuwa akiunganishwa na Jema, Naya akabaki tu kimya kitini akipanga
vidole vyake vya upande wa kushoto akichezea pete yake akiwa bado haamini kama
yamekuwa na kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa kuwa
jioni alijua wanakutana na kina Magesa, na lazima kurudi nyumbani kwao Kiluvya
kujiandaa kisha kurudi tena mjini, Naya akajiandaa kutoka kwa wakati.
Alipomaliza tu kuweka vitu sawa, akawa anaingia Jema na Joshua. Jema akiongea
kwa kusoma kitu kwenye tablet yake, Joshua akimsikiliza. “Twende Naya,
tusichelewe.” Naya akanyanyuka na kumfuata. Jema akawa anaendelea kusoma.
“Unaionaje?” Akamuuliza Joshua wakati wanataka kutoka kabisa kwenye hilo jengo.
“Excellent.” Akajibu Joshua. Jema akageuza njia palepale Naya akamsikia
akicheka kwa kushangilia kwa sauti ya chini nyuma yao akiondoka. Naya
akamtizama Joshua, wakaendelea kutembea wakielekea alipoegesha gari Joshua.
“Sasa si
tutachelewa! Kwa nini wewe usiende kwako, mimi nikachukua usafiri hapa
wakunirudisha nyumbani kisha unifuate nikiwa tayari?” Naya akatoa wazo kabla
Joshua hajatoa gari getini. Akasimama akifikiria. “Wazo zuri.” Akafikiria tena
kidogo, kisha akamuona anatoa gari nje ya geti na kuegesha pembeni. “Wewe nenda
na hii gari nyumbani, nitakufuata nikiwa tayari.” Naya akashangaa. “Unakumbuka
nina magari mawili na nina dereva hapa kazini?” Naya akacheka na kushuka garini
ili aende upande wa dereva. “Nakushukuru Joshua wangu. Hutaki nipate shida! Ila
mwenzio hata daladala ningepanda tu.” “Usijali.” Naya akaondoka na gari ya
Joshua, na kumuacha Joshua akirudi ndani akitembea.
Zayoni Naye.
Ilipofika
mida ya saa moja kasoro kama 10 hivi Joshua akawa anagonga mlangoni.
“Umependeza!” Naya akiwa chumbani akamsikia Zayoni akimsifia Joshua, na Joshua
kucheka. “Asante Zayoni. Hujambo?” “Mimi sijambo. Lakini baba ameniambia endapo
napokea simu za Malon nisimwambie mambo yanayoendelea hapa nyumbani, ila salamu
tu.” Joshua akabaki ameduaa asijue nani anawasikiliza. “Baba anasema hayamuhusu
tena. Lakini unajua mimi nimeamua nini?” Naya akabaki akisikiliza, mkono
umeshikilia moyo kama utatoka kupitia kwenye kifua, udondoke. “Sijui Zayoni.”
Joshua akajibu kwa utulivu. “Japokuwa Malon alikuwa akitupenda sana, lakini
mimi naona nisipokee kabisa simu zake. Niepuke kabisa ili wasinitege kwa
maswali. Si unafikiri ni sawa?” “Nafikiri baba anayo sababu ya msingi kukwambia
hivyo, Zayoni. Wakati mwingine kutii ni bora kuliko chochote kile.”
Ikabidi Joshua kutumia akili ya haraka na kujibu kwa hekima.
“Hata
mimi nimeona hivyo. Ujue mwanzoni walipanga mipango vizuri na Bale, hata
wakamshirikisha na baba. Baba akamshukuru kabisa Malon kwa kukubali kumpa kazi
Bale. Ujue Malon alimuacha Bale bila taarifa yeyote ile?” “Nakumbuka kusikia.”
“Basi sasa hivi amemchukua tena bila kumtaarifu tena baba! Yaani kimyakimya.”
Joshua kimya. “Sijui umeelewa? Yaani kama hivi wewe unavyoomba ruhusa kwa baba
kumchukua Naya, yeye hajamuombea ruhusa Bale wala kuwasiliana na mtu mwingine
yeyote kusema safari hii amerudi tena, halafu anamchukua Bale, Bale atakuwa
kwake kama walivyoanza kwa utaratibu pale mwanzo kabla hajamuacha.” Joshua
kimya akisikiliza. Zayoni akaendelea.
“Hivi
unajua alimkimbia Bale kabisa, akawa hapokei simu zake? Yaani Bale alikuwa
anakesha akimpigia simu kila wakati, akimsihi amchukue. Niliamka siku moja
nikamkuta anampigia Malon, usiku. Ila akaniambia nisimwambie Naya na baba kama
bado anamtafuta Malon.” Joshua hakujua ajibu nini. Naya naye kimya huko ndani.
“Ile siku
ya jumapili, juzi, ujue alimtumia tena ujumbe kama kumjaribisha tu. Maana Malon
alimfungia simu zake, akawa hampati tena na jumbe hajibu japo alikuwa akiona
zinafika. Sasa siku ile ya jumapili tulipotoka kanisani ndipo akajibu ule
ujumbe aliomwandikia kama kumjaribisha tu, kumwambia kama wewe umemchumbia
Naya. Ujue Bale alifurahi sana?” Joshua kimya.
“Nilivyomsimulia
baba leo, baada ya Bale kuondoka, ndio amenionya mimi nisifanye hivyo tena.
Kutoa mambo ya humu ndani. Ndio naona bora nisipokee tu hata simu zake.
Nilishaharibu kipindi fulani alipiga, sasa mimi kwa nia njema tu
nikamwambia Naya alipo. Baba hakufurahia kabisa. Amenionya nisirudie tena.
Lakini mimi sikujua kama angemfuata Naya, na Naya hamtaki tena kwa hakika. Kwa
kuwa mara zote wanakuaga hivi. Naya anakuwa analia sana, lakini baadaye
wanapatana tena. Mimi nikajua na safari ile ninakuwa nawasaidia, kumbe
niliharibu!” Naya akaishiwa nguvu na kukaa kitandani taratibu.
“Malon ni
mzuri sana wakujirudi. Na mama alikuwa akimchukia anasema anampotezea muda
Naya, Malon si mtu wa msimamo. Ila Naya mwenyewe alikuwa akimsamehe. Unajua
mama alimfukuzaga Malon?” Bado Joshua na Zayoni walikuwa wamesimama hata
hajakaribishwa kiti. Zayoni ananong’ona kwa sauti ya kusikika tu. Akaendelea.
“Ila Naya akawa analia sana. Mimi na Bale tukasema atakuwa anamlilia Malon tu.
Ndio Malon alipopiga nikampa...” Naya akatoka kwa haraka. “Mimi nipo tayari.”
Zayoni akajisogeza pembeni kwa haraka kama aliyeshituka.
Naya
akamgeukia. “Baba amesisitiza usitoke Zayoni. Anarudi sasa hivi. Unasikia?”
“Nikiogopa?” “Huwezi kuogopa. Funga milango na uwashe tv.” Akarudi kukaa kwa
upole. “Au tumsubirie baba mpaka arudi? Tusimuache peke yake.” Joshua akatoa
wazo. “Baba yupo njiani, anarudi hapa sasa hivi. Ameniambia hayo kama dakika 10
zimepita. Kwa hiyo atakuwa hapa muda mfupi sana, hatachelewa. Twende
tusiwachelewe kina Magesa.” Joshua akamwangalia Zayoni pale alipokuwa amekaa.
“Utakuwa sawa Zayoni. Na baada ya dakika 10, Naya atakupigia simu kuhakikisha
upo sawa.” “Sawa. Ila usisahau Naya. Mimi nitaogopa tu. Najua.” “Nitakupigia.
Na wewe baba akija unijulishe.” “Nishaanza kuogopa.” “Jamani Zayoni!” “Kweli
Naya. Mimi naogopa tayari.” “Nashauri tumsubirie baba mpaka arudi.
Hatutachelewa.” Joshua akakaa kabisa.
“Mimi
siwezi kuwa peke yangu. Nilikuwa na mama kila wakati.” Zayoni akaanza. “Mama
hakuwa akiniacha mimi peke yangu. Hakuwa akifanya hivyo.” “Basi Zayoni. Na mimi
sitakuacha. Tumsubirie baba.” Naya akakaa na yeye. “Unataka kuangalia nini?”
“Mimi sijui tena, Naya!” “Sasa kwa nini unataka kulia tena wakati tunabaki wote?
Sikuachi Zayoni.” “Bale alisema haondoki tena, atabaki hapahapa atafute
kazi. Leo asubuhi ameondoka bila hata kuniaga! Na wewe ulikuwa unaondoka
nakuniacha Naya! Mama aliniahidi mtakuwa mnanikumbuka. Ila mnanisahau! Mama
hakuwa akinisahau hata siku moja! Ila nyinyi mnanisahau.” “Basi
samahani Zayoni. Nitaongeza umakini nafikiri sababu ya haraka nikakusahau mdogo
wangu. Ila siku nyingine sitafanya hivyo. Mpaka uzoee kubaki peke yako. Si ni
sawa?” Joshua akawa ametulia kimya akisikiliza. “Kwa
hiyo nikizoea ndio mtakuwa mkiniacha peke yangu!?” Hapo
Naya akatulia kidogo.
“Hujui!?” “Nafikiri
tuongeze kuzungumza. Tuwe tunazungumza. Chochote unachoona najisahau,
nikumbushe. Au hata kama kitu hujapenda, wewe niambie jinsi sahihi. Au
unaonaje?” “Hapo sawa.” “Na ninakuahidi nitakuwa nikikusikiliza na
kuongeza umakini.” Hapo akamuona ametulia. Na baba yao akawa anaingia
malangoni. “Wewe bado upo tu?” “Nilikuwa nakusubiria baba. Umefanikiwa?”
“Maneno matupu! Hamna lolote.” Joshua akasimama ili asalimie. “Naya aliniambia
mnawahi kukutana na kina Magesa!” “Bado muda mzuri kabisa. Pole na majukumu.”
Wakasalimiana na kutoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Kweli
inabidi kuongeza umakini kwa Zayoni!” Naya akawaza kwa sauti na kuongeza,
akijitetea mawazoni. “Ila mimi nilijua ameshazoea!” “Ila nimependa hitimisho
lenu. Jinsi ulivyomwambia.” “Kweli?” “Kabisa, ila tu hakikisha unazingatia
ulichomwambia ili asione umemdanganya.” Naya akatulia. “Umependeza sana.”
Akamrudisha pale kimawazo, angalau Naya akacheka na kuondoa hofu ya
alichokisikia Zayoni akimwambia.
Naya, Nanaa, Joshua na Geb.
Walifika
na kuwakuta Nanaa na Geb wakiwasubiria garini, Nanaa akicheka sana, mumewe
taratibu tu. Joshua akagonga kioo. Wakatoka. “Leo Magesa mwanangu, kamuweza
baba yake, ndio nilikuwa nikimcheka Geb. Kampigia mahesabu, yaani Geb mwenyewe
akaingia mtegoni. Anakuja kumaliza ndio akagundua Magesa amemchezea akili.”
“Ila mimi nimempongeza! Sijapata kichwa chakunizidi mahesabu ila yeye! Inabidi
kuongeza umakini. Sijazeeka kiasi chakumuachia kiti kirahisi hivyo!” “Mimi
sidhani kama uamuzzi ni wako GM. Ukizidiwa, huwa unazidiwa tu.” Geb akatingisha
kichwa kwa masikitiko huku akicheka.
“Bibi
harusi wangu amependeza sana. Na wewe pia Joshua. Wote mmependeza.” “Asante
Nanaa, na nyinyi mmependeza.” “Asante, ila sisi ni kawaida yetu.” Wote
wakacheka sana. “Nanaa!” “Mimi namfundisha bibi harusi wangu abakie waviwango.
Mwenzie nilifundishwa na wifi yangu Grace. Usafi na kupendeza mpaka usiku
ukilala. Kwa hiyo leo sisi hatujapendeza kwa bahati mbaya, nilipania. Na
wifi yangu na leo alihakikisha yupo na mimi muda wote, sijikosei.” “Nitaiga
mama matron wangu.” “Hayo ndio maneno. Sasa twendeni tukale, maana chakula cha
hapa mimi huwa kinanichanganya akili. Nakipenda sana.” Wakaongozana huku
vicheko vikiendelea, Nanaa ndio mzungumzaji mkubwa akionekana amezoeana vizuri
tu na Joshua. Wakabakia wao wawili wakipokezana maneno na kuwaacha Naya na Geb
wasikilizaji nyuma yao.
“Niambie
Naya! Unaendeleaje?” Naya akamwangalia Geb aliyejua si mzungumzaji. “Naendelea
vizuri kabisa. Mama anaendeleaje?” “Amekusalimu. Hivi Nanaa atakuwa anasalamu
zako, kama hajasahau.” Joshua na Nanaa walikuwa wametangulia mbele kidogo
wakicheka kwa sauti za juu tu. Ila ni kweli macho ya Geb yalikuwa kwa mkewe
kila wakati. Akamuona anacheka kama aliyesikia kitu alichozungumza mkewe akiwa
mbele yao na Joshua. Naya akabaki kuwatizama wote watatu.
Walifika
sehemu ya kukaa ndani ya hoteli. Ukweli palionekana ni pahadhi yao. Naya na
yeye akaagiza kinywaji, vyote vikaletwa kwenye glasi nzuri haswa.
Wote walitaka juisi. Akaamua kuuliza. “Kwani nyinyi mlikutana wapi? Na kwani
mnaishi na Grace, dada yake Geb? Maana ni kama nilimsikia mama akisema, Grace
na familia yake wanaishi Arusha!” “Ni kama tunaishi na Grace humo ndani.
Kuanzia asubuhi tukiamka mpaka tunakwenda kulala tunakuwa naye kwenye simu.
Ndiye aliyenisimamia harusi.” Naya akashangaa. “Yaani mlisimamiwa harusi na
pacha mwenzie!” “Wewe mwenyewe ungemuona, ungeniibia tu! Muulize Joshua. Ni
dada mzuri sana. Na alinipenda tokea zamani hata sijaolewa na Geb.” Akamuelezea
kwa kifupi juu yake na Grace, na kumfanya Naya kuzidi kuvutiwa.
“Niwaulize
swali jingine? Ni katika kujifunza tu. Ni sawa Joshua?” “Uliza tu na sisi
tujifunze.” “Matatizo gani nyinyi mnayo kutana nayo kwenye mahusiano yenu?”
Nanaa akamwangalia Geb. “Labda niseme yale tuliyokumbana nayo.” Geb akaanza
yeye. “Kwa asilimia kubwa sana, sasa hivi ni kama tupo sawa, ila ni baada ya
kukosea sana.” Nanaa akacheka kidogo na kuinama. Wakatulia kidogo kama
waliokumbuka mengi ya nyuma. “Mbona mnatutisha?” “Hapana. Msitishike. Lakini
makosa mengi ndiyo yamefanya ndoa yetu iwe hivi ilivyo sasa.” Geb akafikiria
kidogo na kuendelea.
“Labda
kwa kuwa tunawasimamia harusi pengine niongeze uwazi kidogo. Tumepita pagumu
sana na Nanaa, mpaka kuwa hivi leo. Ilitugharimu mno mpaka kuumiza watoto
wetu.” “Ni kama kila mmoja wetu akakubali hakuna maisha bila mwenzie ndipo
ikabidi kurekebisha mapungufu yetu kwa lazima na kwa haraka ili kujiponya nafsi
zetu.” Akaongeza Nanaa.
“Kikubwa
na cha muhimu nafikiri kabla ya kuingia kwenye ndoa, nilazima kila mmoja wenu
bila unafiki kujiridhisha kuwa anataka kufanya hivyo. Kwanza kwa ajili binafsi
kisha mwenza. Hapo itawarahisishia sana. Msiingie kwenye ndoa kwa sababu ingine
yeyote isipokuwa kutaka kwa kibinafsi, mengine ndipo yafuate.” Geb akaongeza.
“Na sisi
kitu kilichotugarimu zaidi ni siri.” Nanaa akaongeza na kumwangalia Geb. “Geb
hawezi kabisa mambo ya vificho. Hata kama jambo ni baya kiasi gani, ni bora
umwambie tu, kuliko kumficha.” “Nafikiri hata mimi nipo hivyo aisee.” Akaongeza
Joshua.
“Sasa
hapo, kwenye hilo, ilitugarimu sana. Mno. Ndipo nikajifunza kuzungumza na Geb
na kuwa mkweli na muwazi kwake.” “Na nafikiri kuanzia hapo, tulipoanza
kuzungumza kwa wazi, ndipo tulipofunguliwa kwenye mengi mno.” Akaongeza Geb.
“Labda niwasimulie kwa kifupi tu mkasa fulani. Kama Geb ataruhusu.” “Nini?” Geb
akamuuliza mkewe. “Juu ya Malii.” “Kama ukiona sawa, ni sawa. Pengine
watasaidika wasipite tulikopita sisi.” Geb akaridhia.
“Okay.
Huyu Geb alikuwa na kundi la marafiki zake ambao walisoma na kaka tokea
sekondari.” Nanaa akawasimulia mpaka mkasa wa Malii na kumbaka. Naya alishituka
sana. “Hatujawahi kupita kwenye kipindi kigumu cha mahusiano kama hicho, na kwa
hakika tulijua ndio ungekuwa mwisho wetu. Geb alinirudia nikiwa na mimba ya
huyu Jimmy, tukijua ni mtoto wa Malii.” “What!?” Joshua akashangaa sana,
asiamini Geb aliwezaje! “Nilikuwa sina jinsi, Joshua. Ilikuwa ni eidha nimkose
Nanaa, au nimchukue vile alivyo! Na garama ya kuishi bila Nanaa ikawa kubwa
kuliko kumchua vile alivyo na mtoto niliyedhania ni wa Malii.” “Na tulifunga
ndoa nikiwa na mimba yakukaribia kujifungua huyu Jimmy, bado tukijua ni mtoto
wa Malii, ambaye alipatikanika kwenye ule ubakwaji.” “Daah! Heshima yako Mkuu!”
Mpaka Joshua akasimama na kumpa mkono. Wakacheka.
“Hakika
ni mapenzi makubwa sana. Mimi sijawahi kusikia. Kumbe nyinyi watu mnahistoria
ngumu hivyo!” “Nilimficha Geb nikijua naokoa kumbe ndio niliharibu haswa.”
Wakamuona Naya anatoa simu kwenye pochi akafungua na kumkabidhi Joshua.
Pakatulia kabisa pale wasielewe Joshua amepewa nini asome kwenye simu ya Naya.
Akasoma,
wakamuona amebadilika ila akacheka kwa masikitiko. “Ila mimi sijamjibu.”
Wakamsikia Naya akijitetea, Geb na Nanaa kimya. “Umejua sasa kama Bale amefika
salama?” “Nimeshindwa Joshua. Alinipigia nikiwa najiandaa, kabla hajazungumza
kitu cha maana simu ikakata. Nimempigia zaidi ya mara tatu, simu yake haipo
hewani. Moyo wangu umesita kumpigia Malo sababu ya huo ujumbe alionitumia jioni
ya leo, muda mfupi hata kabla ya Bale kunipigia. Niliogopa hata kukwambia tena
kwa yale aliyokuwa akikwambia Zayoni. Nilijua nitakuchanganya zaidi.” “Sasa kwa
kuficha jumbe za namna hii ndio utanichanganya zaidi, Naya.” “Ndio nimejifunza
leo, Joshua. Na nimekusikia kwamba ni bora ujue tu.” Nanaa na mumewe kimya.
Joshua akatulia
kidogo kama anayefikiria. “Naomba usikasirike Joshua.” “Sasa umejua kama Bale
amefika salama au la!” Joshua akarudia tena swali. “Hapana Joshua. Mimi
ninamjua Malo. Usifikiri kumchukua Bale ni kwa ajili yakumsaidia Bale! Ni kama
hivi. Kwamba nikimkosa Bale, basi nimpigie yeye.” “Basi acha mimi nikampigie.”
“Nakushukuru Joshua. Na samahani. Najua nakuingiza kwenye kero.” “Usijali.”
Joshua akambusu na kutoka. Akawaacha wao watatu hapo. “Samahanini jamani. Hiyo
stori yenu imeniogopesha sana.” “Usijali.” Akajibu Geb na kutulia.
Nanaa
akamwangalia mumewe. Naya akashangaa Geb anacheka na kutingisha kichwa.
“Nanaa!” “Sio kwa undani sana!” Nanaa akawa kama anajitetea kwa mumewe
aliyekuwa akimwangalia tu, Naya akawa hajawaelewa maana akili zilikuwa nje kwa
Joshua. “Natamani nikamuangalie Joshua, lakini naona bora nimuache tu. Malon ni
mkorofi sana. Atatutibua wote wawili usiku huu, kusiwepo hata wakumliwaza
mwenzie. Acha tu nimuache apambane naye.” “Kwani ni nani?” Akawahi Nanaa
kutupia swali alilotaka kuuliza tokea mwanzo, mumewe akimwangalia. Alimjua
mkewe kwa kupenda stori, asingeweza kuacha apitwe.
“Tulikuwa
kwenye mahusiano naye kuanzia nipo sekondari kidato cha nne, mpaka nikamaliza
chuo.” “Kumbe ni mtu mliyekuwa naye kwa muda mrefu hivyo! Kwa nini ulimuacha
sasa au ni kwa sababu ya Joshua?” “Ndivyo na yeye pamoja na wadogo zangu au
kaka zangu wanavyodhani. Mahusiano yalishaisha muda tu, na wote wanajua. Lakini
tulikuwa na mtindo wa kuachana na kurudiana. Au niseme matatizo kwenye
mahusiano yetu lilikuwa jambo la kawaida. Leo asubuhi tunakuwa tumeachana,
jioni au hata baada ya mwezi tunakuwa tumerudiana. Kwa hiyo safari hii
wanalalamika wanasema nashindwa kumrudia au kumsamehe sababu ya Joshua.”
“Ambayo ni kweli?” Akauliza Geb.
“Najua
hamnifahamu na ninaweza nisiwe na ushahidi wa kutosha hata kwa Joshua, maana na
yeye haya ninayowaambia yakugombana na kurudiana, na yeye amethibitishiwa leo
na Zayoni, yule mdogo wangu wa mwisho. Lakini kwa Malo nilifika mwisho hata
kabla ya Joshua. Siku chache kabla ya kuanzana na Joshua, alikuja nyumbani na
pete yake akitaka kunichumbia. Hakika nilimkatalia na kumwambia yeye hatakuwa
mwanaume atakayenitoa kwa baba Naya. Sasa leo kati ya mengi aliyoniandikia ndio
ananiambia, yeye ndiye atakuwa mwanaume wa kunitoa kwa Joshua, kwa
sababu nilishatoka kwa baba Naya na mengine mengi.” “Hee!” “Subiri kwanza
Nanaa.” Geb akataka kumtuliza.
“Ni kwa
nini ulikataa kuolewa naye.” “Geb, hiyo pete aliyonipa usiku ule niliililia kwa
miaka mingi sana mpaka hata kwa wazazi wake.” “Naya!” Nanaa akashangaa. “Kweli
tena. Yalikuwa ni mahusiano ya kudhalilishwa kupita kiasi, hamna tofauti na huo
umalaya wa huyo Malii mliyetusimulia, sema sisi tulifika umbali wa kuishi
pamoja. Kuanzia tunaanzana mpaka karibu na mwisho. Tuliishi kama mke na mume
kabisa. Umalaya aliokuwa akiufanya na kusingizia ni bangi, halikuwa jambo geni
na la siri. Kila mtu alimjua jinsi alivyokuwa akilala na wanawake, tena mpaka
wa karibu yangu mimi. Nanaa, hapakuwa na sehemu tunakwenda mimi na yeye Malon,
kusiwepo na wanawake amekwisha lala nao.” “Naya!”
“Kweli
Nanaa. Ilikuwa fedheha ya hali ya juu. Maisha ya aibu na manyanyaso mabaya
sana. Baba yake mzazi alituambia tukiwa na baba, wakati nikikusanya pesa za
kumtoa jela, aka..” “Naya! Jela tena!?” Na yeye akapata moyo wa kuwasimulia
baada ya Nanaa na yeye kujifunua kwao mpaka kusema alibakwa na rafiki ya mumewe
pamoja na kaka yake. Naya naye akawasimulia kwa kifupi habari zake na Malon.
Wote wakabaki wanamshangaa.
“Sasa kwa
nini ulikuwa ukiyafanya yote hayo Naya!?” “Kwanza ndiye aliyekuwa mwanaume
wangu wa kwanza. Halafu kwa ukweli Malon ana jinsi fulani hivi, akiwa na mimi,
utatamani masaa yasisogee. Kila mtu alijua mimi ni mwanamke wake, na akiwa na
mimi popote, atatulia mno na heshima. Watu wanajua nipo kwenye hiyo sehemu kwa
utulivu anaokuwa nao, hata fujo hawezi kufanya. Alinipumbaza kwa mengi nikawa
nikijiambia pengine atakuja kubadilika. Na kingine nafikiri kikubwa ni kama
akawa aliweka deni kubwa sana moyoni, kwa misaada ya kiuchumi aliyonisaidia
tokea tunaanzana. Alisaidia sana. Kwa hiyo nikawa kama nipo naye kumthibitishia
kuwa sikuwahi kumpendea pesa zake ila yeye. Nilikuwa nikimlilia, nikimsihi
atulie tu anichague mimi, nibakie peke yangu, lakini haikuwahi kubadilika.
Nilifanya kila kitu mpaka nilipomtoa jela na bado hakunichagua! Pale ndipo
nilipojiridhisha kuwa Malon hakuandikiwa kuwa mume wangu, na hatakaa awe wangu,
napoteza tu muda. Na umri unazidi kwenda, historia yetu itaendelea kujirudia
vilevile. Kuachana na kurudiana kila kukicha kwa kila sababu anazochagua yeye
kwa wakati huo.” “Inawezekana alikuwa ni daraja tu. La kukuvusha sehemu
moja kwenda nyingine ila wewe ukang’angania darajani, hutaki kuvuka. Ndio maana
hukufika popote. Huwezi kujua Naya!” Nanaa akaongeza akisikika na yeye akiwaza.
Kisha
akawa kama amekumbuka kitu. “Naomba nikwambie kitu Naya. Kwa ufupi tu bila
kukupoteza, ila kutaka ufikirie.” “Niambie tu.” Naya akakubali na kuangalia
mlangoni kuona kama Joshua ataingia hapo. “Kuna mambo mimi nimejifunza
kibinafsi kwenye haya maisha na kule tulikopitishwa na makosa mengi
tuliyofanya, sababu ya kung’ang’ania watu na vitu vilivyotakiwa kupita kwenye
maisha.” Nanaa akaendelea.
“Wapo
watu Mungu huwatuma kwenye maisha yetu kutimiza kusudi fulani, na wakimaliza
hilo kusudi wanatakiwa kuondoka kwa kuwa wameshatimiza kusudi lao. Liwe kubwa
sana au dogo sana. Wakati wao ukiisha, wanatakiwa kuondoka. Iwe kusimama na
wewe kwenye msiba, au shuguli fulani maalaamu hata ya kimungu. Wakishatimiza
kusudi, wanatakiwa kuondoka. Ukiwang’ania wabaki, huwa wanaweza kuleta madhara kwako
binafsi au kwenye lile kusudi zima waliloitiwa na kulisimamisha. Kwa kuwa
hawakupewa uwezo wa kubeba lile jambo ila kulianzisha au kulisogeza sehemu moja
kwenda nyingine. Chukulia mfano wa nabii Elia. Alipokimbilia pangoni, akiogopa
kuuwawa na Malikia Yezebeli. Unakumbuka habari zao kwenye kitabu cha 1 wafame 18?” Naya
akatulia akisikiliza kwa makini.
“Nenda
kasome vizuri. Kote alikopita nabii Elia. Yote MAKUBWA aliyofanya mpaka kufikia
kwenye kujificha pangoni, njaa ikimuuma, akimuomba Mungu kufa tu, kwa kuwa
alifika mwisho kwenye maisha, anaogopa kuuwawa na malikia tu. Tena mpagani,
hata hamjui Mungu wake aliyetenda miujiza mbele za watu wote wakishuhudia! Yeye
mwenyewe nabii Elia alifanya mambo makubwa yaliyojulikana sana mpaka Mfalume,
mumewe Yezebeli akawa anamtafuta kwa makubwa aliyoyatenda. Kuzuia mvua
isinyeshe. Haya, akaja kuita moto kutoka mbinguni, Mungu akafanya yote hayo
kujidhihirisha kwake na mbele ya wote kwamba yeye ni Mungu mwenye nguvu. Lakini
utisho tu wa maneno matupu ya malikia Yezebeli, akakimbia akaenda kujificha
pangoni. Hana chakula, hana malazi anaomba kifo! Unakumbuka Mungu alimtumia
kunguru ili amlishe?” Naya na Geb kimya wakisikiliza wakitaka kusikia
analinganisha nini na ya Naya.
“Kwani
yule kunguru aliendelea kumlisha mpaka mwisho wa maisha yake yote?” Nanaa
akauliza na kuendelea. “Wewe unafikiri kama Elia angemng’ang’ania kunguru
amlishe, na kukataa kumtii Mungu ili atoke pale, unafikiri aliyotenda yote
baada ya pale mpaka kuandikwa kwenye bibilia yangetokea?” “Asingeweza kufanikisha.”
“Sasa? Wakati mwingine Mungu huwa anatuambia kwa njia nyingi sana mpaka kwa
matukio fulani fulani akitaka tuendelee kwenye maisha lakini tunakuwa wagumu
kukubali, kuchukua hatua. Kwa hofu au kwa sababu ya kuona tulipo ni bora kuliko
kukubali kukabili adha ya mbeleni. Tunaridhika palepale kwa sababu za
kibinadamu na kuishia na vile tunavyodhani vinatustahili kumbe Mungu anakusudia
makubwa zaidi juu yetu. Na Hawezi kuweka divai mpya kwenye kiriba cha
zamani, kilichochakaa. Sasa wewe akili kumkichwa. Endelea,
nisikuchanganye na mengi.” Nanaa akaona amuache aendelee tu.
“Inawezekana
upo sahihi Nanaa! Inawezekana kabisa. Ila ukweli alijua nimetulia,
nimejifunga kwake na ni mwaminifu sana tu. Nikimsubiria yeye achukue hatua
ingine. Hilo alikuwa akilijua na ndilo anang’ang’ania mpaka leo hata kwenye huo
ujumbe akiniomba msamaha, anasema hatuko pamoja kwa sababu yake yeye mwenyewe
kushindwa kusimama kwenye nafasi yake, ila sasa hivi yupo tayari akiujua
moyo wangu, kuwa nipo namsubiria tu yeye achukue hatua ya msingi. Hakuwahi
kutegemea mimi kuja kumwambia nimefika mwisho na sitabadilika tena. Hii mara ya
mwisho ndiyo amejua ni kweli nimemaanisha kwa kuwa pia ameniona nimetulia na
Joshua, kitu ambacho hakutegemea mimi kuja kupata mwanaume kama Joshua. Aliyetulia
na akili za kiutu uzima hivi.”
“Maana
alishanitoa kwa wanaume wawili ambao wao walikuwa wababaishaji tu na hilo pia
amenikumbusha kwenye huo ujumbe niliompa Joshua asome. Mmoja alinikuta naye
kijana tuliyekuwa naye kanisani. Kila mtu alijua angenioa, kama hivi Joshua.
Mpaka wazazi na mama walimpenda sana. Lakini niliachana naye nikaanza mahusiano
na yeye Malon. Lakini huyu kijana wa kwanza mimi sikuwahi kumkubali na ndio
ukawa ugomvi wangu na mama, na ndio maana mama hakumpenda Malon akahisi ananipotosha.
Ila sio kwamba nilikuwa kwenye mahusiano mazuri na Ino ndipo nikamuacha sababu
ya Malo! Hapo Malo hajasema ukweli. Hata bila yeye Ino asingenioa!” Hapo napo
Naya akawasimulia kwa ufupi kama akijitetea kwa ujumbe aliotuma Malon na kumpa
na Joshua asome.
Huku kwa Joshua.
Joshua
akaanza kwa kumpigia Bale. Haikuwa hewani. Akarudia tena na tena, hakumpata.
Ndipo akajaribu kumpigia Malon akitumia simu ya Naya. Akapokea kwa
haraka. “Naya, mama!” “Ni mimi Joshua.” Joshua
akamuwahi. “Umempokonya na simu yake?” Malon akamuuliza kwa
kejeli. “Tulitaka kujua kama Bale alifika salama.” “Wewe kama nani?” Malon
akamuuliza tena. “Kama mpenzi wa Naya, mume mtarajiwa na shemeji yake Bale.” Malon
akacheka kwa kejeli. “Ndivyo unavyojiaminisha hivyo? Hujui walipita watu kama wewe
kwa Naya, uliza wapo wapi sasa hivi!” “Tunataka
kujua tu kama Bale amefika salama.” “Kama unayejali vile! Si wewe aliyekuomba
kazi ukamkatalia? Si niliwaachia Bale ili muweze kuyatengeneza ya familia,
ukashindwa? Ule ulikuwa mtihani kwako, lakini ulishindwa vibaya sana kama
wanaume wengi tu waliopita kwa Naya na kushindwa kama wewe. Mimi nimeweza kuwa
na Naya pamoja na familia yake, tukatengeneza familia yakueleweka. Lakini wewe
ni mbinafsi, mtu unayejiangalia wewe tu, na ni hatari kwa familia ya kina Naya,
na sitakuruhusu.” Joshua kimya akisikiliza.
“Walipita
wenzio kama wewe, wakakubaliwa na kujulikana mpaka kanisani, nikifikiri
watamfanya Naya awe na furaha, lakini wamekuwa wapuuzi tu kama wewe, pamoja na
elimu zao kama wewe, nikaishia kumchukua Naya wangu. Na yupo mwenzio
alimchumbia kabisa Naya, kama hivyo wewe, kanisani kabisa, Naya alimuacha kwa
ajili yangu. Sembuse wewe hata ndugu zake tu hawakutaki! Kwanza wameshakuona
wewe ni mnyanyasaji tu. Umeingia kwenye maisha ya Naya umekuwa mtu wakuchukua
tu bila kujali furaha ya Naya mwenyewe na ndugu zake! Masharti mengi ya kiwivu
tu na kumbana tu Naya. Sasa kama unafikiri kukubaliwa na baba yake Naya ndio
kila kitu, uliza historia yangu mimi na Naya. Hata mimi huyo mzee alinikubali
sana tu. Amehangaika kunitoa jela na mengine mengi.” Malon
akaendelea.
“Upo na
Naya kwa sababu mimi niliruhusu. Naya ananipenda mimi. Hajawahi na wala
hatakaa akampenda mwanaume mwingine, kama anavyonipenda mimi. Hilo ukae na
uelewe, ili usijipotezee muda. Ilikuwa ni mimi tu sikuwa tayari, nikitaka
nijijenge kwanza ili Naya asije ishi kwenye mazingira mabaya. Ila sasa hivi
nipo tayari na Naya wangu, narudi. Tena narudi na kumchukua mwanamke wangu moja
kwa moja. Siwezi kumuacha Naya kwa mwanaume mpuuzi, mbinafsi na mchoyo kama
wewe!” “Kama umemaliza kuzungumza hicho unachoamini kipo sahihi kichwani mwako tafadhali
tujulishe tu kama Bale alifika salama na upo naye.” Joshua
akarudi kwenye swali lake.
“Kwani
unajali nini au unafiki tu? Unataka kumdanganya nani ambaye ameshindwa kukusoma
wewe? Hata Bale mwenyewe anakujua tabia zako. Hana mpango hata wakuwa karibu na
wewe. Kwa hiyo acha unafiki, usimtafute. Umejawa sifa tu kujitangaza utajiri
unaonufaika nao wewe mwenyewe, lakini huna chochote! Acha kumbana Naya,
mrudishie simu yake. Na ukiendelea hivyo nitamnunulia simu ingine. Uache
manyanyaso.” Simu ikakatwa.
Japokuwa
alijaribu kutulia, lakini kwa hakika Joshua alikuwa ametibuka moyo na akili
vibaya sana. Akashindwa hata kurudi ndani, kwa kuwa hakuwa na jibu la kurudisha
juu ya Bale ila kashfa tupu. Akabaki amesimama hapo nje akijaribu kutulia.
Mengi aliyoyasema Malon, hayakutofautiana na ujumbe mrefu aliokuwa amemuandikia
Naya. Akimkumbusha walipotoka, waliyopitia, waliopita kwenye mahusiano yao, na
ahadi nyingi tu na nzuri kwa Naya pindi watakapoendeleza mahusiano yao ambayo
hayakuwahi kubadilika. Joshua alibaki palepale amesimama, na kushindwa hata
kujisogeza. Maneno ya Zayoni nayo yakajirudia kama kumthibitishia kuwa ni kweli
Naya na Malon huwakuwahi kuachana moja kwa moja. Wakati wote hurudiana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Kwa hiyo
huyo Ino sio kwamba kweli alikuwa amekuchumbia kisha kumuacha sababu yake?”
“Hapana Geb! Hapo Malo hajasema kweli. Ni ile kudhania kwa watu au wazazi
kutamani itokee hivyo kwa kuwa tulikuwa pamoja. Sikatai kama tulijaribu. Lakini
Geb, hata baba na Bale walikuwa wakijua nitaishia pabaya sana endapo nitakubali
kuolewa naye. Na nikawa muwazi kwake na mama pia. Nikamkataa mbele ya mchungaji
na mama. Ikaisha hiyo. Tukaanzana na kuendelea na Malon.” Naya akawasimulia
mpaka mambo ya Joshua, ila kwa kifupi tu. Mpaka hapo Joshua akawa hajarudi.
“Sikuwahi
kuacha kulia na kumbembeleza Malon anioe. Nilijifunga kwake nikiamini
anachosema mimi ndio mwanamke pekee amewahi kunipenda na hataruhusu mwanaume
mwingine awe na mimi. Nilisubiria hiyo ndoa, bila kuchoka mpaka niliposalimu
amri na kusadiki Mungu hakukusudia mimi niwe na Malo.” “Kweli Naya ungekubali
kuolewa na mtu wa namna hiyo!?” “Angewahi kabla ya mkasa wa Ritha na kifo cha
mama, hakika ningekubali Nanaa. Hata baba aliniuliza swali kama hilo.
Nikamwambia nisingejali hata kama kipato chetu kingeishia kumtoa yeye jela tu,
nilikuwa tayari kuwa naye. Na yeye anajua hilo na anajiaminisha nalo mpaka
sasa. Baba alikuwa akiumia sana. Alikuwa akiniombea kupita kiasi, nafikiri
mpaka Mungu akaamua kuingilia kati kunikomboa kwenye hicho kifungo.” Joshua
akarudi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ukweli
alionekana kubadilika kabisa usoni. Akakaa kama ambaye hajui azungumze nini
tena. “Tafadhali usimsikilize Malon, Joshua. Usikubali akakutibua moyo, kwa
kuwa mimi namfahamu Malon. Naomba tulia mpenzi wangu. Tuangalie ya kwetu tu.”
“Umefanikiwa kujua kama dogo amefika salama?” Geb akauliza kwa kujali. Joshua
akajicheka. Wote wakatulia wakimwangalia akiwa ameinama akiitizama simu ya Naya
mkononi mwake.
“Mimi
ngoja niwashauri Joshua. Nimemsikiliza kwa makini sana Naya. Na nashukuru
amekubali kuwa muwazi kwetu. Ninachotaka kuwahakikishia ni hiki, mnakopita
nyinyi si pageni wala si pahatari kama inavyoweza kuhisika sasa hivi, kipindi
hiki mnachopitia. Na sisi tulipita hapo. Mimi na Nanaa, tena kwa garama kubwa
sana, nafikiri Joshua nilikusimulia kwa sehemu. Ambacho sikukwambia au kuweka
msisitizo ni kwamba, kote tulikopita, tulipita kila mtu akiwa kinyume na mimi
kumuoa Nanaa isipokuwa James na mama, pamoja na Grace tu.”
“Watu
wakaribu yetu walijaribu kupinga si kwa maneno haya ya kashfa tu, hapana.
Walikwenda umbali wa mpaka kutoa uthibitisho kanisani wakipinga nisimuoe Nanaa.
Mmoja wao alisema na kutoa uthibitisho akipinga hiyo ndoa kuwa alishamuoa
Nanaa, nchini Nairobi. Kwamba Nanaa ni mke wake kihalali.” “Haiwezekani!”
“Kweli Joshua. Na mbaya zaidi, yule mama mkubwa niliyekusimulia alinilea,
ali...” “Mama yake James?” Joshua akauliza. “Ewaa! Alithibitisha ni kweli kuwa
alipokea mahari ya Zinda, rafiki ya Geb na kaka James, na alinioa.”
“Haiwezekani Nanaa!” “Wewe msikilize Geb.” Nanaa akataka mumewe aendelee.
Walishaagiza
chakula. Kikaletwa. “Naombeni tumshukuru Mungu kwa chakula kabla
hatujaendelea.” Nanaa akaomba. Ndipo yeye mwenyewe Nanaa akaanza kula kama
kawaida yake. Chakula hakisubiri kwenye sahani. Naya na Joshua wakataka
kumsikia Geb ambaye yeye aliomba tu Samaki wakuchomwa na tango pamoja na
nyanya, basi.
“Haikuwa
rahisi kama hivi mnavyotuona sasa hivi. Rafiki wote waliokuwa kama familia.
Wakila na kunywa alivyotayarisha mama G, baadaye akaja Nanaa aliyekuwa
akiwakarimu nyumbani kwetu. Maana sisi tulianza kuishi pamoja, sio kama nyinyi.
Maisha ya ndoa yalianza ndipo tukaja kubariki ndoa. Anyways.” Geb
akaendelea. “Kila mtu alitugeuka. Nilikuwa nikichafuliwa mno kwenye kundi letu
la hao marafiki. Walituwekea mitego mpaka ushirikina wakitaka kumdhuru Nanaa,
akaharibiwa miguu ikawa kama matende lakini yaliyojaa malengelenge.” “Nakumbuka
kumsikia Nanaa kusema hivyo kwa baba Naya, siku ile ya mahari ya Naya! Aisee!”
Joshua akahamaki. Geb akacheka.
“Acha
kaka. Na usiombe akurudi mtu wa karibu yako, anayekujua vizuri
mpaka madhaifu yako. Anahakikisha anakupiga pale anapojua utaumia
haswa.” “Ndivyo anavyotaka kunifanyia Malon.” Akalalamika Naya. “Sasa nyinyi
nguzo yenu iwe umoja.” “Sawasawa Nanaa. Hicho anachowaambia Nanaa, ndio kitu
pekee kilichotufanya mnatuona hapa na furaha na watoto wetu wanakuwa vizuri.
Walituvuruga, kiasi ya kwamba kama si Nanaa, mke wangu kukubali yaishe na
kujenga familia hii unayoiona na kumsikia Grace akimtaja kila mara, tusingekuwa
hivi. Na wanangu wasingekuwa vile. Ndio maana mama anamchukulia Nanaa si mkwe,
ni mziwanda wake aliyechukua nafasi yangu.” “Geb linamuuma hilo! Wewe kubali
yaishe.” Nanaa akaongeza wakacheka.
“Mimi
nilishazoa kuwa kiziwanda! Lakini sijawahi pewa mapenzi anayopewa Nanaa na
mama.” “Basi kilio hicho cha Geb, hata Grace anacho.” Nanaa akaongeza
akiendelea kula. Angalau wakacheka. “Hata Joshua aliniambia hata kabla
sijawaona aisee. Alivutiwa sana jinsi mama G anavyokupenda. Alisimulia mpaka
nyumbani!” “Na si kwa unafiki Naya. Yule mama ananipenda haswa. Mimi nimeyajua
mapenzi ya mama, nikiwa mkubwani hivi, kwa kupitia mama G. Ila niweke msisitizo
hapo kwa Geb, kwenu Joshua na Naya, majaribu yenu yatakuwa mepesi sana mpaka
watawashangaa kama mtasimama pamoja bila usiri. Sisi tuliwaziba midomo, mpaka
leo hawaamini.” Nanaa akaongeza.
“Nikuulize
Nanaa, sasa Malii alitoka jela?” “Geb alihakikisha anaweka fundisho kupitia
Malii, Gozi na Zinda. Hakuna anayetusogelea. Kesi zao zilinguruma, na Geb
alihakikisha anatumia pesa, haki ifuate mkondo. Yupo dada mzuri sana, anaitwa
Sonia, mtoto wa Tambo. Yule aliyekuwa jaji mkuu kipindi cha awamu ya tatu ya
uraisi.” “Namkumbuka yule jaji, na yeye alipataga hekaheka ya familia kweli!”
“Ewaa! Alikuja kutusimulia Sonia mwenyewe kipindi fulani baada ya kesi kuisha,
mama alimualika nyumbani kama kumshukuru. Akaja na familia yake. Tukayazungumza
hayo. Na yeye anahistoria ngumu! Nitakuja kukukutanisha naye. Ni dada mzuri tu.
Na hata kwenye harusi nitawaomba tumualike. Sio dada mbaya, hana mambo mengi.”
{Simulizi juu
ya Sonia Tambo ipo kwenye Simulizi ya “Zaidi ya Kutamka”. }
“Ila
kujibu swali lako, Malii yupo jela.” “Na hatakaa akatoka.” Akamalizia Geb.
“Kweli!?” “Oooh yeah! Kosa la ubakaji na vitisho alivyofanya mpaka kutupiga na
kuwalevya walinzi wangu, kutuvamia na silaha, ni kusudio la kutaka kuua!” Geb
akaongeza. “Daah! Na hao wenzie.” Nanaa akacheka.
“Bwana
Geb aliwatenda wale watu, hawatakaa kutusahau!” Nanaa akaongeza. “Siku
wanakamatwa Gozi na Zinda, kwanza alikuwepo mwanasheria wa kwanza kabisa ambaye
ndiye aliyetutambulisha kwa Sonia baada ya yeye kuugua sana. Siku hiyo
tuliwatega Gozi na Zinda mpaka wakakiri wakitaka kumuumiza Geb, mbele ya wazazi
wa Malii waliokuwa wamewaleta kwa makusudi mjini, kutokea migombani, kuja kwa
Geb kudai mtoto wa Malii, ambaye naye tayari tulishamfungulia kesi ya ubakaji
ila hajulikani alipo.” “Nyinyi jamani! Mtu akiwaona hivyo hawezi kudhania kama
mlipita huko!” Naya akashangaa.
“Nakiri
hayo yote ndiyo yaliyotusogeza pamoja, na kuongeza mapenzi kwetu, na
kushikamana. Sisi majaribu yalituweka pamoja zaidi.” “Naomba nisimulie kidogo
Nanaa juu ya usiku huo mpaka kuwaweka jela.” Joshua akataka kusikia. “Kuleni
sasa. Usiku huu tumekubaliana na Geb tuwe kwa ajili yenu tu. Uzuri wa Geb huwa
si mwepesi wakusema ‘ndiyo’ kwa watu. Ila akikukubalia, ujue atasimama na wewe.
Ndio uzuri wa mume wangu. Na hana ‘ndiyo’ za hovyo au niseme nyingi
kumfurahisha mtu.” “Nimemuona leo mpaka ameongea yote haya! Nikashangazwa na
kumshukuru Mungu wangu! Hakika alijua nitawahitaji. Malon amenisema maneno
mabaya sana, yanayoendana na ukweli. Nikaingiwa hofu kwa kuwa amefanikiwa kumvuta
Bale upande wake!” “Lakini sio mimi, Joshua! Mimi nipo na wewe na ndio maana
Malon anahangaika. Alitegemea ingekuwa rahisi kama alivyozoea kurudi na
kunichukua kama mzigo anaokuwa ameacha mahali. Lakini amejua amenikuta kwenye
mikono sahihi, ni wewe.” Naya akamgeukia vizuri Joshua.
“Anachojaribu
kukifanya ni kukutingisha mpaka utingishike, kama siku ile mbele ya baba juu ya
maswala ya gari! Unakumbuka?” “Nakumbuka Naya.” “Sasa ataendelea kukujaribu
sana ili tu ushindwe, kwa sababu kwanza umeshamtisha na Malo hapendi
kushindwa.” “Kumbe afadhali sikumjibu.” “Tena kama hukumjibu ndio umemuumiza
zaidi. Malon mtoto wa mtaani na mtu wa ugomvi. Ungemjibu ndio ungejishusha
kwenye hadhi yake. Tafadhali tusigombane sababu ya Malon au Bale.” “Na hilo mlikumbuke
aisee. Si kwa leo tu, hata baadaye kwa sababu majaribu yanaendelea kuwafuata.
Mwanamke wako ni mzuri Joshua! Yupo kama mwanamitindo! Anavutia kwa macho.
Watawasumbua sana.” Wote wakacheka.
“Mimi
nawaambia kweli. Muulizeni Geb kama changamoto zimeisha.” “Wanamtaka Nanaa
wangu mpaka leo. Ila sema sasa hivi wanao msumbua sio watu wa ngazi ya chini,
wenye kipato cha juu kama sisi, tunaokutana nao kwenye biashara na maisha.”
Naya akajikonyeza kuwa Geb anajitambua anayo pesa! “Sasa mnafanyaje?” Joshua
akauliza. “Kwanza mimi mwenyewe nampenda Geb wangu. Sithubutu kujijaribu wala
kujaribiwa.” Wakacheka sana. “Kweli Joshua. Shetani mjanja na hila zake nyingi
kwa kuwa na yeye anatufahamu kwa kipimo karibu na Mungu. Kumbukeni habari za
Ayubu kwenye bibilia. Alimjaribu Ayubu kwa vile alivyomfahamu hata kumwambia
Mungu! Hawezi kukujaribu kitoto. Anakujaribu haswa akijua lazima atakupata tu.”
“Yeye mwenyewe Nanaa akaanzisha siku ambazo ananiachia simu yake.” Wakacheka
sana.
“Haiwezekani!”
“Kweli kabisa. Hata tukiwa ofisini, anakuja kuniletea. Jumbe na simu zake
napokea na kujibu zile ninazoona hazimuhitaji yeye. Wanaume ninaoona hawana
heshima, ila nataka pesa yao na wao wanataka huduma yangu, nimehakikisha
wanaelewa kumsogelea Nanaa ni kosa ambalo siwezi kusamehe haswa kujua ni
mke wangu na mama watoto wangu!” “Na hapo Geb hana aibu jamani! Anamuweka sawa
huyo mtu mapema tena kwa wazi kabisa.”
“Kingine,
tunapendana kiasi ya kwamba watu wanatujua. Hata mimi nilimuomba Nanaa anilinde
kabisa. Akihisi hatari, asiache kuniambia na kuomba kwa ajili yangu. Hakuna
safari nakwenda bila mke wangu. Nikitoka hivi lazima awe kama hivi pembeni
yangu. Nipo naye kila mahali na narudia tena. Sisi tunaomba.
Tulishajijua sisi ni waharibifu mno, bila Mungu. Hakuna kipindi tulimuacha
Mungu tukabaki salama. Muulizeni mama au huyu Nanaa. Na huwa tunaharibu haswa.
Kwa hiyo kwa upande fulani sisi kwetu maombi tumefanya ni dini kabisa. Wala
tusidanganye. Linapofika swala la kuomba, hata kama hatujisikii, tumetoka
kufanya ibada ya familia, tumechoka na siku ya kazi pengine ilikuwa ngumu, sisi
wawili, lazima tukifika chumbani tupige magoti na kuomba. Hata maneno machache
tu. Na tunajua kabisa, wakati mwingine hatumaanishi sababu ya uchovu, lakini
katika hilo tulikubaliana tufanye tu. Kujihudhurisha mbele za Mungu sisi
wawili, kwa pamoja.”
“Tena
hata kama tumeudhiana. Kwa sababu maudhi yapo wala tusiwadanganye.
Wakati mwingine hata kama Geb au mimi nimekasirika, lakini tutapiga magoti tu
hata tukiwa tumenuniana.” Naya na Joshua wakacheka. “Tuliwaambia katika hilo
tulikubaliana iwe kama dini tu.” Geb akaongeza na kuendelea.
“Joshua
ulitaka kujua juu ya Malii, Zinda na Gozi.” “Aisee kweli Geb husahau kama
mwanao Magesa!” Walicheka sana walipomkumbuka Magesa. “Na wale wengine wapo
vilevile, sema mwanangu Magesa yeye mdomo huwa unamponza! Hawezi kunyamaza
Magesa mwanangu, kama mama yake!” Walicheka sana.
“Anyways.
Kwa ushahidi wa kukiri usiku ule mbele ya wazazi wa Malii, yule
mwanasheria pamoja na sisi wote wakisema wanajua kama Malii alinibaka, moja kwa
moja wakageuka mashahidi wangu. Na Geb akakusanya ushahidi wa jumbe walizokuwa
wakitumiana kabla na siku yenyewe niliyobakwa kwenye sherehe
nyumbani kwetu kumtaarifu Malii kama ni muda mzuri wa kuja au la ili aje afanye
uchafu wake!” “Haiwezekani Nanaa!” “Kweli Joshua. Geb anapokwambi ogopa
kupigwa na watu wa karibu yako wanao kufahamu, hakika ogopa.” Nanaa
akaongea kwa unyonge.
“Kaka
aliumia sana kwa walichonitendea marafiki zake. Na yeye alisomea mambo kama
Geb.” “Yeah, si mlisema wote walikuwa darasa moja?” “Ewaa! Ila sema Geb
alikwenda kumalizia shule yake nje ya nchi, wao wakamaliza hapo chuo kikuu cha
Mlimani pamoja, wakawa kama familia. Kwa hiyo kaka bila kumwambia mtu akaanza
uchunguzi kujua Malii alijuaje kama ule ndio ulikuwa muda sahihi wa yeye na
majambazi wenzake kuja na kuweza kufanya uharamia! Ndipo akagundua siku ile Gozi
alikuwa akisaidiana na Malii. Anamwambia kila kitu kinachoendelea pale, na
akaanza kufukuza wageni kwa utani akiwaambia watu waondoke ili nipumzike, kumbe
ilikuwa ili tubaki peke yetu, Malii aje na majambazi yake.” Nanaa akawasimulia
kwa uchungu kama aliyekumbushwa machungu.
“James
aliponiambia tu hivyo. Nilihakikisha Gozi anahukumiwa kama Malii. Akae ndani
ili asije kumdhuru mtu mwingine. Hakika nilihakikisha, na Sonia alinisaidia
vizuri sana. Na yeye akahukumiwa kwa kosa la kushiriki ubakaji na
mauaji. Zinda yeye hatakaa akatoka japo mwanzoni alihukumiwa muda mfupi kwa
kosa la kukiuka restraining order lakini nilimsaidia Grace. Zinda akiwa
jela kwa kosa la kwanza, tukamshitaki kwa kosa jingine, alihusika na vifo vya
watoto wa Grace, hiyo nayo ni habari ingine lakini kwa upande wa kiushirikina. Ilinigarimu
sana mpaka nikapata ushahidi wa kuhakikishia mahakama kuwa anahusika na
vifo vyao. Tulinyaka mazungumzo kati yake na mama yake walivyokuwa wakipanga
njama ya kutoa kafara familia ya Grace ili yeye Zinda akombolewe kiushirikina.”
“What?!” Joshua akahamaki.
“Kwamba
ilikuaje?” Ndipo Geb akawaeleza kwa ufupi historia ya Grace na Danny, mpaka vifo
vya mapacha wao. {Simulizi nzima ipo kwenye naomisimulizi.com katika Simulizi
ya “Ni Wangu!”} “Nyie shetani jamani?” “Acha Naya. Wale marafiki walitugeuka
vibaya sana. Zinda amefungwa na mama yake.” Nanaa akaongeza. “Nilihakikisha
natafuta ushahidi mpaka akaongezewa hukumu ingine ya kifungo cha maisha,
mama yake naye alikamatwa na kuhukumiwa kama mwanae, pamoja na mganga
wao pia nilihakikisha anakaa ndani ili asije dhuru familia ingine.” Geb
akamaliza na kutulia kabisa.
“Aisee
walishika adabu. Hakuna mwenye hamu ya Geb. Na hapo mkumbuke mwanzoni kabisa Geb
aliwaonya mpaka kwa kupitia mwanasheria. Wasiwahi kurudi nyumbani kwetu.
Waliwekewa restraining order.” “Na ndilo lilisaidia kumuweka ndani
Zinda wakati nikitafuta ushahidi wa vifo vya watoto wetu.” “Sasa kipi
kiliwapelekea kuwawekea hiyo restraining order tokea mwanzo?” “Katikati
ya machafuko ya mwanzoni, wake zao walikwenda kumfanyia mama fujo, akiwa
kazini kwake.” Geb akawasimulia tena kwa kwa ufupi. “Ndipo waliporudi nyumbani
tena...” “Ikawa wamekiuka agizo la kisheria!” Akamalizia Naya.
“Sawasawa.
Ndipo Zinda alipowekwa ndani kwa kosa hilo la kukiuka restraining
order, nikiwa sina ushahidi wa kutosha wa mauaji waliyoyafanya kiushirikina.
Na Sonia aliniambia kosa la ushirikina ni kesi ngumu sana. Mpaka ushahidi wa
kueleweka kweli uwepo ndipo kesi zake zinaweza kushinda. Sasa kwa kuwa
nilikusudia haki itendeke kwa watoto wa Grace waliokuwa wameuwawa kikatili, Zinda
akiwa ndani ndipo nilipopata sasa nafasi kumfanyia uchunguzi wa kutosha wa hayo
mauji ya kishirikina waliyofanya kwa hao mapacha wetu. Nilifunga nakuomba
nikimlilia Mungu kilichotokea kwa watoto wa Grace, wasije weza kukifanya
kwa watoto wa mtu mwingine. Nikamsihi Mungu anipe uwezo na aniinulie
watu watakao nisaidia kuwakamata na wahukumiwe kwa haki. Basi Mungu akasadia. Huyohuyo
Sonia akapata taarifa kamili. Nafikiri ni kutoka Usalama wa Taifa, yeye
mwenyewe hakukiri, ila nahisi tu kwa kuwa anatoka kwenye familia ya watu
wanaofanya kazi huko Usalama wa Taifa kwa miaka mingi tu. Aliweza kunyaka
mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kati ya Zinda na mama yake. Na jumbe zao zote
walizokuwa wakiandikiana wakiwekeana mipango ya kuwaita huko kwao Tabora na
kumwaga damu yao njiani.” Geb akawasimulia mengi waliyoyafanya na kuwaacha hoi.
“Daah!
Kumbe afadhali tumezungumza. Binafsi mmenijenga sana. Nilifikishwa sehemu
nikawa nimehisi nimebanwa!” “Usitishwe na maneno hata kidogo. Na wewe Naya
hivyohivyo. Wanaweza kukuletea maneno yanayofanana na kweli tupu juu ya Joshua,
tena hukohuko ofisini kwenu.” “Mbona tayari! Natamani ningewafahamu mapema.”
“Huu ndio wakati wa bwana. Tushukuru hatujachelewa.” Joshua akaongeza kwa Naya.
“Aisee tunawashukuru sana.”
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakaanza
kula. “Sasa mbona wewe huli? Au kimeshapoa?” Nanaa akamwangalia Geb, na kuanza
kucheka. “Naya anakuuliza.” Geb akacheka huku anaangalia yule samaki mzuri
kwenye sahani. “Anavutia!” Naya akasifia jinsi alivyowekwa kwa ustadi pale kwenye
sahani, akiwa na rangi nzuri ya kuokwa. “Sio machoni kwa Geb. Hapo
ameshamtoa kasoro huyo samaki, na hatakwambia hizo kasoro wewe kwa kuwa sio
mama au mimi. Alivyoletwa tu hapa, mimi nilipomuona tu na kumwangalia Geb,
nikajua hatamla.” “Kwa nini!?” Naya akauliza akishangaa asione tatizo. “Wewe
jiachie tu. Huyu kwenye swala la chakula hutamuelewa. Nasubiri mimi
nishibe, niombe wanifungashie huyo samaki, nimpelekee mama yangu, akale wakati
nampigisha stori.” Akarudi kuendelea kula. Geb akabaki akimwangalia Nanaa
alivyokuwa akila kama ametoka jangwani kusikokuwa na chakula. Akamuita muhudumu
achukue kile chakula chake akakifunge. Nanaa akamwambia akaongezee na ndizi
tatu za kuchoma.
Naya
akawa hajaelewa. Nanaa akaona amsaidie asibaki anashangaa. “Geb ni mvivu
wakula. Na anashida ya kula kama yule mwanae Liv, ndio maana unamuona Liv wangu
hana mwili kama wa Magesa. Ila angalau kidogo Jimmy kuna vitu vyake ukimpikia
anakula. Ila hawa wawili ni shida ya familia. Kwa hiyo kabla sijatoka
naye huyu kwenda popote, nahakikisha anakula na kushiba, ndipo tunatoka.
Lasivyo analala na njaa, na haimsumbui hata kidogo.” “Sasa hivi tunavyokula,
hatamani?” “Hata kidogo.” Akajibu Geb mwenyewe. Wakacheka.
“Na
usifikiri anakutania. Adhabu yakumnyima Geb chakula sio adhabu kwake. Ni nafuu
kubwa, kwanza atashukuru hata usipompa tena chakula, endapo amepata hata mlo
mmoja wa siku. Wewe kula tu muache huyu.” “Lakini umenifanya nifikirie, ni
kweli sijawahi kumuona Geb akila.” Joshua akajaribu kuvuta kumbukumbu.
“Sina
shida mbaya kwa kiasi hicho bwana, Joshua! Wewe utakuwa umesahau tu. Ukija
nyumbani huwa na kula, labda inaweza kuwa isiwe chakula mnachokulaga nyinyi
wote, au muda wenu nyinyi wakati mkila, ila nakula bwana!” Akawasogelea mtu
ambaye alimfanya Nanaa kushituka mpaka Geb akageuka, na yeye akabaki ameduaa.
Asiyesikia la Mkuu.
“Huwa
napenda juisi ya hapa.” Danny akaanza. Kimya. Naya akashangaa Nanaa wa maneno
mengi na Geb kimya wanamwangalia. “Najua nimebadilika sana, ni kwa sababu ya
kuugua. Niliugua sana.” Kimya. “Halafu bwana Nanaa ulikuwa sahihi, yule Sara
hakuwa ametulia, yupo kama mwehu! Kanisababishia matatizo na kuniacha na
gonjwa! Mimi nilijua tu atakuwa ni yeye kwa sababu mimi na Grace tulikuwa
tumetulia sana. Sasa nilipopatwa mkanda wa jeshi, homa kuwa kali sana, nikahisi
tu. Eti yule mtoto nampigia simu, ananiambia kama jambo la kawaida vile! Eti
niache kupaniki, UKIMWI ni jambo la kawaida sana siku hizi, wala si jambo la
ajabu. Watu wanakufa na maradhi kibao na kuwaacha wenye UKIMWI, mimi natakiwa
tu kuwahi dawa, yeye amekuwa akitumia dawa muda tu na yupo sawa. Ndio ikabidi
kwenda hospitalini wakaniambia ni kweli, nikaanzishiwa matibabu, hivi hapa
ninanafuu sana.” Kimya.
Naya
akawatizama Geb na Nanaa, waliokuwa wamemgeukiwa Danny. Kisha Danny akawageukia
na wao. “Samahanini sikutaka kuwaingilia, nilikuwa naingia hapa kufuata juisi,
nilipowaona nikaona nisiwapite tu, si uungwana.” “Hichi unachokifanya hapa sasa
hivi, ndio sio uungwana.” Akajibu Geb. “Mimi sitaki ugomvi Geb. Ni salama tu.
Vipi Fili?” “Nakuonya, si kwa kukutisha Danny, usinijaribu.” “Si kwa
ugomvi Geb, nataka kujua hali yake na angalau kumuona sijui mwisho wangu ni
upi! Tafadhali Geb.”
“Huko
ni kunijaribu ambako nakuonya Danny!” “Mimi ni baba yake. Na wewe ni baba Geb,
kweli unataka kuniadhibu mpaka kifo changu nisimuone mwanangu!? Najua
nimekosa, na ninawaomba msamaha. Tafadhali naomba kumuona mtoto wangu.” “Kama
Mungu wangu aishivyo, nakuhakikishia hutamuona Fili, mpaka Fili aje
akutafute yeye mwenyewe ambayo sijui ni lini.” “Hivi unajua pesa iliyotumika
kumrudisha Fili kuwa mtoto wa kawaida, sababu yako wewe Danny?” Nanaa naye
akaongeza.
“Fili
alikuwa kama amechanganyikiwa kwa ajili yako na Sara! Mtoto hakuwa akilala!
Tunashukuru Mungu mume wa Grace alimchukua yule mtoto kama wake na kuhangaika
naye sana akisaidiana na Geb mpaka Fili akaweza kurudi kuwa kama mtoto wa
kawaida, japo umembadili Fili na kumfanya kama bubu! Mtoto ameingiwa
hofu ya kuzungumza wakati Fili alikuwa mtoto mzungumzaji, mzuri tu! Umembadili
kabisa Fili! Halafu eti sasa hivi unarudi tena na kutaka kuanza machafuko
tena!” “Na sitakuruhusu.” Geb akaongeza.
“Nimebadilika.”
“Kama kweli umebadilika Danny, anza kwa kumfikiria yule mtoto. Wewe ni baba wa
namna gani ambaye unajua kuua tu, hujui kutengeneza!?” Geb akamuuliza
akimshangaa kabisa. “Kwanza Fili mwenyewe hataki hata kukuona. Akisikia jina
lako yule mtoto anatetemeka mpaka anajikojolea! Imebidi wote tujifunze
kutotamka jina Danny, akiwepo Fili! Haya, usiku mtoto alikuwa akiamka anakimbia
mpaka nje akimtafuta mama yake, analia asirudishwe ndani akidhani wewe na Sara
mpo ndani! Hakubali kuingia ndani mpaka Grace mwenyewe atoke na aamini wewe na
Sara hampo ndani!” Nanaa akaongezea kwa mumewe na kuendelea.
“Muulize
kaka atakwambia jinsi alivyokuwa akimlilia Geb asirudishwe kwako! Anamlilia Geb
mpaka anapiga magoti, anasihi asije akarudishwa kwako na Sara, msije
mkamkatakata na kumponda kichwa kama wadogo zake! Eti bila aibu unarudi kumdai
na Fili naye! Unawazimu wewe!” Nanaa akawa mkali kabisa.
“Uuwe
watoto wa Grace wawili halafu urudi tena utake kummalizia aliyebaki!
Hivi unajua Grace amebarikiwa watoto wengine wawili lakini bado analia
msiba wa Fillius na ndugu yake mpaka jana? Umeharibu vibaya sana maisha ya
Grace na Fili, halafu eti unarudi unasema nini!? Nahisi huo ugonjwa umeanza
kukula ubongo wako, si kawaida. Twendeni Geb.” Nanaa akasimama na kuchukua
pochi yake.
Bila
kuzungumza neno Naya naye akasimama na Joshua. “Sitarudia kukuonya tena Danny.
Usiwahi hata kutaja jina la Fili, kwangu, Grace, mama, Nanaa na watoto wangu.
Sikutishi, lakini jua sikutanii. Na kukuthibitishia hili, kwa kuwa
umenianza, utapokea mashitaka yangu kutoka kwa mwanasheria wangu.” “Hapana Geb.
Tafadhali naomba yaishe. Sikutaka...” “Twende Nanaa.” “Samahanini sana jamani!
Tafadhali naomba tusifike mbali. Naahidi sitorudia tena.” “Na nitahakikisha hilo
hutakaa ukasahau mpaka kifo chako.” Geb akamuhakikishia. Akabeba samaki na hizo
ndizi vilivyokuwa vimefungwa vizuri kwenye boksi, wakaondoka pale. Geb
akapitiliza kwenda kulipia. Hakutaka kumsubiria muhudumu ndipo amlipe pale,
wakamsubiria wote hiyo sehemu ya kulipia, ndipo wakatoka nje kwa pamoja wala
Joshua na Naya hawakuwa wamemaliza chakula chao.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mambo Juu Ya Mambo. Ni nini kitaendelea?
Endelea kufuatilia.
0 Comments:
Post a Comment