Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 30. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 30.

Waliongozana moja kwa moja mpaka sehemu waliyoegesha magari yao bila kuongeleshana. Walipofika Geb akageuka. “Tutapanga ili kupata muda zaidi ila nafikiri inabidi kuombea kila kitu zaidi maandalizi ya harusi.” “Nashukuru sana Geb, na poleni. Inawezekana jioni yenu haikuisha kama mlivyotarajia, lakini kwa hakika nyinyi mmefanyika baraka kwetu. Mungu alijua kwa hakika tungewahitaji. Asanteni kwa kutoa muda wenu.” “Karibu Joshua. Tupo pamoja. Muda na wakati wowote kukiwa na swali, muwe huru kutupigia. Tukishindwa kwa ushauri basi tutaomba pamoja.” “Asante. Lakini..” Naya naye akashukuru na kutaka kuongeza akasita. Wote wakamwangalia sasa yeye kumuonyesha wanamsikiliza.

“Pengine inaweza isiwe wakati muafaka sasa hivi, lakini nilitaka kuwashukuru. Geb na mkeo, pamoja na Joshua pia.” Wote wakaongeza umakini kama ambao wanataka kusikia zaidi. “Baba ameniambia yale fundi wenu anafanya kule na nguvu nyingine ya watu mliyomuongezea ili kukamilisha vizuri na kwa haraka. Nashukuru. Najua nimeshamshukuru Joshua tena na tena, lakini na nyinyi nawashukuru sana. Imemchangamsha sana baba na amepata tumaini la ajabu! Alikuwa akinimbia kwa hakika upo wakati wa Mungu na ukifika, huwa Mungu mwenyewe anasimama kwelikweli ili kuhakikisha alilokusudia linatimia. Anasema alikuwa akiomba bila kuchoka, huku akisubiri lakini hakujua kwa hakika, Mungu atatenda vipi ili kukamilisha makubwa aliyokuwa akimuomba. Ila ameamini huwa anatumia yeyote ili kukamilisha jambo lake.”

“Anasema hakuwahi kufiri kwa umbali huo mpaka alipomuona akitembea kwake akiwatumia nyinyi watu baki tu. Joshua aliposikia tu wazo lake, anasema ikawa ni kama amelizungumza kwa upya kwenye sikio la Mungu moja kwa moja, na kuwatuma nyinyi wote kusimama na yeye. Baba yangu ni mkimya sana. Mnaweza msiyasikie haya yote kutoka kwake mwenyewe, na mkaelewa furaha yake ndio maana nikoana niwafikishie shukurani zake na zangu. Asanteni sana. Nawashukuru sana. Baba yangu anaimani ile inayowakera wengi na wakati mwingine anadharauliwa kwa hiyo imani yake mpaka kuonekana ni kama hajui anachoongea na pengine mzubaifu. Lakini kwa mara ya kwanza, nimeona nyinyi mliweza kumsikiliza  na kuamini mawazo yake mkaweza kusimama naye. Ndio maana nimeona nisiache huu wakati upite tu, niwashukuru.” Wakamsikia Nanaa anacheka.

“Kwanza karibu Naya. Ila sisi wenyewe na mama tulikuwa tukimsengenya Geb. Tukasema amempenda baba Naya, na kumuheshimu sana Joshua. Geb sio mtu wakupigia simu mafundi akiwa nyumbani au tuseme kuzungumzia mambo a kazi nyumbani zaidi anapokuwa na wanae, labda iwe dharula napo hapokei simu mpaka kule kazini wanamjua. Ikifika jioni au akitoka kazini, simu zote zinahamia kwangu. Sasa kuja kumuona anahangaika na mafundi na kuwaeleza nini chakufanya kule kwenye sehemu ya baba Naya! Tena mpaka usiku! Mama mwenyewe alikuwa akishangaa ila akasema tumuache tu.” “Ni kwa kuwa ni mtu anayeonekana anajua nini anataka. Mtulivu, yupo tayari kujifunza halafu...” Wakamuona Geb kama amesita hivi akifikiria.

Anyways, ni mtu mzuri.” Nanaa akacheka. “Wewe umempenda tu. Si useme!” Geb akacheka kama anayefikiria. “Nafikiri kuna namna Mungu amefanya mioyo yetu ipatane tu. Nikizungumza naye sioni ugumu wa kufikia moyo wake au mawazo yake na akili. Sijui kama mnanielewa?” Geb akauliza na kuendelea. “Kuna mtu unapata naye muda, hata kama ni lisaa kwa muzungumzo tu. Kila anachozungumza, unaona kabisa sicho kilichopo moyoni mwake. Hupati kile kitu sahihi. Na si kuwa anakudanganya, ila inakuwa ngumu ku..” “Inamaana baba Naya hana hila?” Nanaa akamsaidia kwa kifupi.

“Ewaa! Unaweza kusema hivyo, lakini pia anacho kitu cha tofauti, nimeshindwa kukisema ila ni mtu ambaye...” Akasita tena. Wote wakacheka. “Hana hila aisee, halafu mnyenyekevu mno. Huo uzubaifu unaosema Naya, kwangu naona ni unyenyekevu tu. Baba yako anao uelewa wa mambo! Sana. Ukiwa tayari kusikiliza, anayo machache, lakini anao uelewa. Si mjinga. Ila ni..” “Hekima?” “Sawasawa Joshua. Ni mtu niseme kwa jinsi nilivyomsoma kwa haraka, anahekima hii ya duniani. Ya kawaida tu. Anaweza kuishi na yeyote, na popote. Awe huyo mtu yupo juu sana. Kifedha, elimu au hata maneno mengi ya kujifanya yupo juu sana kuzidi yeyote yule, lakini baba Naya hatahadaiki na kupoteza dira atabaki mtulivu tu. Halafu akiwa na mtu wa chini, pia, atajua jinsi ya kuwa naye. Anajua ni wakati gani wakuzungumza na yeyote. Hata kubaki kimya kwake, ukiwa makini naye, utagundua ni jibu pia.” Geb akaendelea.

“Anasikiliza na anakubali mabadiliko ndio maana nimemuona itakuwa rahisi kukimbia naye kufika mwendo mrefu kwa urahisi kuliko kuanza na mtu ambaye kwanza mbishi. Mjuaji. Hana nia. Inachukua muda mrefu sana kwanza kumfikia yeye mwenyewe ndipo ije maswala ya biashara. Inachelewesha. Nafikiri mmenielewa.” “Tumekuelewa mpenzi wangu. Kwa kweli baba Naya kapendwa. Sifa zote hizo ni zake tu, na zinatoka kwako Geb, mume wangu!?” Wakacheka sana.

“Lakini ni kweli. Pengine iwe nimemsoma vibaya tu. Ila ndivyo alivyo. Ni watofauti.” “Naenda kumwambia mama!” “Sasa unaenda kumwambia nini!? Mimi sijasema kitu cha ajabu.” “Ushawahi kuyasema yote hayo kwa nani, Geb wewe!? Huwa unabaki kutizama tu mtu, na kunyamaza.” Geb akacheka na kutingisha kichwa. “Nitakupigia kesho, Naya. Muwe na usiku mwema. Kila kitu kitakwenda vizuri kabisa, wala msiogope.” “Asanteni.” Wote wakashukuru kwa pamoja. Kina Magesa wakaondoka. Angalau wakaagana wakicheka sio kama walivyotaka kuondoka kabla. 

Naya&Joshua

Naya akamshika mkono Joshua na kumvuta mpaka kwenye gari yake akiwa anamuongoza njia. “Ulisema kuachana sio chaguzi tena. Acha kutishwa na Malon. Maneno ya Zayoni pamoja na Bale au hata mimi mwenyewe. Yaani kutishwa kwa jinsi nilivyoishi na Malon. Usitishwe. Nimeishi vile na Malon kwa kuwa sikuwa najua kama naweza kupata mtu bora kama wewe na pia kwa ukweli kwangu hakuwa mkatili, kasoro yake ilikuwa moja tu, umalaya. Vinginevyo alikuwa mtu mzuri ndio maana nilikuwa najikuta narudi kwake. Ninachotaka kukuhakikishia Joshua ni kuwa nakupenda na sitakusaliti sababu ya Malon. Kwa kuwa nilishaamua kumuacha hata kabla yako. Wewe ni muujiza wangu Joshua. Mungu alikuleta akijua nakuhitaji. Siwezi kurudi nyuma. Naomba usitishwe. Simama na Naya huyu aliyekushika hapa.” Joshua akavuta pumzi kwa nguvu na kubaki akifikiria bila kujibu.

“Hakika utanioa Joshua.” Ikabidi tu Joshua acheke. “Kwa lazima?” “Hakika tena. Mimi nimechoka hii michezo yakuanza kila wakati. Mwenzio napenda maisha kama hivi Nanaa. Kuolewa na kuwa na watoto wake. Akatulia nyumbani kwake na mume anayesema anampenda na yeye anampenda. Hayo maisha nayatamani Joshua, wala sitaona haya kusema. Na nakutaka wewe Joshua Kumu.” “Wala sina mpango wa kukuacha Naya. Ila napata ujasiri zaidi kukusikia ukisema hivyo. Wewe Naya. Hapo unanipa ujasiri.” “Basi mimi ni wako Joshua Kumu. Wala usiwe na wasiwasi, tuombe Mungu atufanikishe kwenye mipango yetu tu. Mengine tuachane nayo. Mimi nakupenda mpenzi wangu.” Naya akaongea kwa kubembeleza. Yakaanza mabusu hapo sehemu ya kuegeshea magari. Yakaendelea yakutosha tu mpaka akamuona ametulia kabisa, ndipo safari yakurudi Kiluvya ikaanza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          Walifika nyumbani wakamkuta baba Naya sebuleni. “Mmekuwa na wakati mzuri huko?” “Mambo yalitaka kuharibika kidogo, baba.” Naya akamsimulia baba yake. “Nisikilize Naya. Kwa jinsi alivyonisimulia Zayoni na shauku aliyokuwa nayo Bale juu ya hii safari, kwa hakika sasa hivi yupo sehemu sahihi kwake. Na mimi si mtu sahihi kabisa hata kumtafuta kwa sasa tena kwa haraka, sababu yupo  kwenye kurekebisha makosa yangu yote anayojua nimefanya maishani ili asije kuwa kama mimi. Mwache kabisa. Akitaka kututafuta, atatutafuta tu. Lakini acha kuwaingilia. Kaa pembeni ” Naya akatulia.

          “Na Joshua na wewe usihangaike na familia yangu. Angalia ya kwako Mungu anayotaka kukupa. Jenga kwako, lasivyo utajikuta unawekwa njia panda na kushindwa kuwa mwaminifu kwa Mungu kwa atakachokukabidhi. Sijui kama unanielewa?” “Nakusikiliza mzee wangu.” “Yapo mengi sana yanaendelea hapa ndani, na sitaki uchanganywe na kujikuta unapoteza dira. Sikutegemei kwa chochote hapa nyumbani kwangu. Sitegemei utukomboe kwa chochote kile. Au sikutegemei eti ndio uanze kufanya mambo humu ndani kwetu. Tafadhali endelea kujenga kwako bila kuyumbishwa ukimtegemea Mungu. Na uache kujilaumu juu ya Bale. Hawa wawili wana maelewano yao, hata wewe usingeweza kuingilia. Malon ni mfano wa kuigwa kwa Bale. Hakuna yeyote kati yetu ambaye angeweza kumtuliza Bale ila Malon. Ungeweza kumatafutia kazi, kisha kuja kuiacha katikati na kumkimbilia Malon. Hudhani huko nako ungeharibu?” “Na mimi nimemwambia hivyohivyo.” Naya akadakia.

“Kabisa. Mwacheni kabisa Bale. Mimi mwenyewe ndio nitajaribu kwa ujumbe kumuuliza kama alifika salama. Akijibu sawa. Asipojibu nitabaki kumuombea. Basi. Nyinyi  msijihusishe nao kabisa.”  “Nimeelewa mzee wangu. Na ninaamini kila kitu kitakwenda sawa kabisa. Tuendelee kumwamini Mungu pamoja. Najua sijakuwa kwenye familia kwa muda mrefu tokea mama aliponiacha. Lakini ninauelewa na mambo ya familia. Familia ya Naya itakuwa familia yangu. Ni Mungu mwenyewe ameniweka hapa, sina chakukwepa na siwezi kuepuka chochote. Tafadhali kama kuna uwezekano wa kunishirikisha chochote bila kificho msisite na msione ni usumbufu. Sisi ni familia sasa. Muwe huru na amani. Unapoona anahitajika Naya, naomba ujue ni mimi pia, kwa hiyo usiwe na shaka, tafadhali nishirikishe tu mzee wangu.” Baba Naya akanyamaza. Wakatulia.

“Nashukuru sana kwa kunitambulisha kwa kina Magesa. Naona amekusudia kwelikweli kusaidia.” Baba Naya akavunja ukimya, nakufanya Naya na Joshua kucheka kidogo wakamkumbuka Nanaa. “Amefanya nini tena?” “Kuna sehemu kuna mtu alikubali mwanzoni kunikodisha ili kuweza kuhifadhi bidhaa. Nilipokwenda kuzungumza naye jioni hii kabla hamjaondoka, naona amepatwa tamaa, ameamua kumkodisha mtu mwingine kwa bei ya juu kidogo. Sasa Geb alitaka fundi wake akapaangalie kama patafaa kuwekea bidhaa kabla hatujaanza. Sasa nikamjulisha kumwambia kama hilo eneo sijafanikiwa. Nafikiri atakuwa amemwambia Magesa mwenyewe. Mlipoondoka tu, Geb mwenyewe amenipigia. Baada ya kuuliza maswali mengi ameomba kama kesho mida ya saa 6 mchana kama wanaweza kuja hapa na kupaangalia huko nyuma nilikokuwa nikifuga ng’ombe.” Naya akashangaa.

“Baba, kwamba uweke huko nyuma!?” “Sijui mama! Lakini Geb anasema Yesu alitema mate kwenye udongo, akatengeneza tope na kumpaka kipofu, akaweza kuona. Anasema Mungu anauwezo wa kutoa chochote kutoka udongoni na kukipa uhai, kikawa kitu cha ajabu sana. Anasema ilimradi kuwe na aridhi, popote, basi chochote kinaweza kutokea hapo. Anasema ipo nguvu kwenye kile alichosema Mungu kuwa popote unapokanyaga, amekupa. Amesema anataka kuja kuona nilipokanyaga, na kile Mungu anataka kunipa.” Wakamsikia Joshua akicheka taratibu.

“Geb mwenyewe!?” Naya akauliza akishangaa. “Yeye mwenyewe amesema anakuja kesho saa sita mchana kama nitakuwepo.” “Kweli amekupenda! Mkewe anasema si kawaida yake. Mzito sana kwa watu.” “Na ana mambo mengi mpaka amenishangaza!” “Wakati wa Mungu umefika kwako baba yangu. Maombi yako yamefika mbele ya kiti cha enzi, ndipo anakuinulia watu sahihi kutimiza kusudi lake. Geb ana mambo mengi sana. Si mtu wakuyafanya yote hayo, ila ni Mungu tu.” Joshua akaongeza.

“Ila nahofia sana pesa. Kwa mtu kama yule mawazo yake hayawezi yakawa ni ya pesa ndogo! Sitaki kumkatisha tamaa.” “Maji yameshatibuliwa mzee wangu. Ni wewe kuingia tu. Usiogope. Geb anajua nini anafanya. Akiwa anakujua wewe ni nani. Hawezi kuanzisha jambo akashindwa kulimaliza. Acha tuone anakushauri nini, kisha tuzungumze kuanzia hapo.” “Ila Joshua, hakika nakushukuru sana.” “Ni Mungu, mzee wangu. Wala si mimi. Amenitumia tu. Na nisingefanya mimi, basi angekuinulia mtu mwingine. Tumshukuru Mungu.” “Hata na wewe nakushukuru kwa kukubali kutumika. Asante. Haya yote nahisi pia anafanya kwa heshima yako. Jinsi mnavyoishi huko. Nashukuru.” “Karibu sana mzee wangu.” Angalau mazungumzo yakabadilika. Joshua na yeye akaomba kwenda kuona huko nyuma ya nyumba ya kina Naya. Wakatoka kwenda kuzunguka usiku huohuo nyuma ya hiyo nyumba.

“Kumbe una eneo kubwa hivi!” “Ni pakubwa ila nilishindwa tu kupaendeleza. Na mke wangu alipofariki ndio kila kitu kikakosa maana. Hata mifugo ikanishinda.” “Pole sana.” “Asante. Lakini najua sikutakiwa kufanya hivyo. Ni moja ya makosa ninayojutia. Haikuwa biashara kubwa lakini si sawa na kukaa bure na kuanza upya.” Hapo Joshua hakuongeza akanyamaza.

“Hapa lazima Geb atatoa kitu kizuri sana, acha atushauri hiyo kesho. Anaakili ya ajabu sana yule kiumbe. Hafikirii vitu vidogo na dhaifu. Halafu haogopi kuthubutu. Acha tuone na hapa nako Simba wa kabila la Yuda anataka kutoa nini!” Joshua akaongea kwa kuhamasika mpaka Naya na baba yake wakacheka. “Kweli kabisa. Huyu Mungu ana mtindo wake wakustahilisha watu wanao onekana dhaifu, wasiostahili kwenye macho ya wenye hekima hii ya duniani, kwa makusudi tu. Ili wanaosikia masikio yao yawashe, na wanao ona wasiamini mpaka wajue na hapo napo Mungu ametembea na kujibu kwa moto. Acha atembee aweke mambo sawa na sisi tushuhudie ukuu wake kwa mara nyingine tena.” Joshua akaendelea.

“Wakati nikilala mtaani. Nikihangaika sina jinsi ya kibinadamu ya kunitoa pale, kipo kipindi nilikuwa nikimuomba Mungu kama kutimiza wajibu tu, maana ni kweli kwa akili zangu nilijua fika naomba yasiyowezekana. Nikaendelea hivyo mpaka yeye mwenyewe Mungu akanihurumia akijua nimeshakata tamaa, ndipo akanikutanisha na like andiko la (Waphilipi 4:19.)” Wakamuona baba Naya anacheka. “Hata mimi ndio mstari pekee unaoendelea kunitia moyo kubaki magotini. Maana kwa namna ya kibinadamu mimi kama mimi nimeshafilisika mpaka mwisho. Nimejaribu mengi bila mafanikio. Nimekosea kwingi mpaka nikakosa tumaini. Kwa namna ya kibinadamu, mwingine angenishauri tu nisiendelee kuomba. Niache tu, sistahili. Lakini kila nikikumbuka hapo, ni kwa kadiri ya utajiri wake Mungu si mimi na mazingira yanayonizunguka, narudi kuomba na nakuwa radhi kusubiri.”

“Sawasawa. Kumbe na wewe upo hivyohivyo! Yaani mimi mzee wangu, huo mstari huo, ndio unanipa ujasiri wakusimama hata mbele ya wakuu. Bila kujali rangi zao wala vyeo vyao na vile wanavyovimiliki. Hakuna mlango amewahi kufungua Mungu nikaogopa kuingia, sababu ya huo mstari nikijua atanipa hata hekima kwa kadiri ya utajiri wake, si wangu.” “Bwana mbona mnashangilia tu wenyewe mimi mstari wenyewe hata siujui!” Naya akalalamika nakufanya Joshua na baba Naya wamgeukie na kucheka.

Walishahamasishana hapo! Baba Naya alipenda sana neno la Mungu. Mkimya, lakini ikifika kwenye maandiko huchangamka kwelikweli. Hapo akawa amefikishwa kwenye eneo lake. Akafurahia mpaka ungeona moyo wake. “Baba jamani! Na wewe Joshua acha kunicheka.” “Unaujua sana mama yangu mzazi! Ni vile haujaushika tu kichwani. Ila huwa nakukumbusha sana na wewe. ‘Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji, kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu’. Umekumbuka sasa?” “Huo naujua. Ulikuwa hata ukimwambia mama.” “Basi na mimi huwa na usimamia kwenye maeneo mengi sana.” Joshua akaongeza. “Ni kwa kuwa unafaaa katika kila eneo la maisha ya mwanadamu. Pale hekima ya mwanadamu inapopungua, ukidhani umefika mwisho, basi Mungu anakukumbusha ni kwa kadiri ya utajiri wake. Mungu tu. Anakushusha na kukufanya umtizame yeye peke yake kama mfamle Daudi alipofikishwa mahali akatambua kuwa msaada wake ukatika Bwana, aliyeziumba mbingu na nchi. Wala si ufalume wake na mengi ya thamani yanayomzunguka ila Mungu tu. Acha nikuache Joshua ukapumzike maana sitamaliza juu ya huyu Mungu.” Wakacheka.

“Lakini upo na eneo zuri sana. Huna haja yakukodi popote. Na uzuri kampuni yake inamafundi kabisa, tutamuomba atupe haohao mafundi wake. Huu msitu ukikatwa vizuri na eneo lake likachanganywa na hayo mabanda yaliyokuwa ya ng’ombe, kutapatikana gala zuri tu. Tusubiri tuone.” “Asante Joshua.” Naya naye akashukuru.  Joshua akacheka na kumwangalia Naya. “Karibu.” Wakazungumza wakiwa hapohapo nyuma ya nyumba, ndipo Joshua akaondoka.

Jumatatu.

Kama kawaida Joshua akaenda kumchukua kwenda kazini. “Nilishakwambia asante kwa kuja mbali kote huku kunifuata?” “Zaidi ya mara 10.” Naya akacheka. “Wewe ni mchumba mzuri sana.” “Usizoee. Gari yako imeshafika. Kesho unatakiwa kwenda kukamilisha kuisajili.” “Joshua!” “Sikutanii. Walikuwa wanahangaikia kuitoa bandarini na ukaguzi kuhakikisha kila kitu kipo kama nilivyoona kwenye picha. Hakujaibiwa kitu, ndipo wanataka kutukabidhi.” Simu ya Naya ikaanza kunguruma kwenye pochi yake. Akashangaa asubuhi hiyo ni nani awe anampigia.

Wazo likamjia. “Bale.” Akachangamka kutafuta simu yake. Alipotoa akakuta ni simu ya Malon. Akapoa gafla kama aliyemwagiwa maji. Joshua akamuona. “Nani?” “Mimi sijui.” “Hamna jina!?” Naya akanyamaza akiitizama ile simu ikiita mkononi mpaka ikakata. Joshua akahisi. “Ni Malon tena?” Kabla ya Naya kujibu ikaanza kuita tena. Ikaita mpaka ikakata tena. Kisha ukaingia ujumbe. ‘Ni mimi Bale. Nilitaka kukutaarifu nilifika salama.’ ‘Kwani simu yako imepatwa na nini?’ Joshua akamuona anaandika ujumbe bila ya kujibiwa swali lake. ‘Imekorofisha. Sasa kwa nini hutaki kupokea simu yangu?!’ ‘Hiyo sio simu yako ni ya Malon. Nipigie kwa simu yako.’ ‘Nimekwambia imekorofisha, Naya!’ Naya akahisi anamdanganya.

Simu ikaanza kuita tena. Ikaita na kuita. Joshua kimya. ‘Ni nini Naya?’ Ujumbe mwingine ukaingia. Naya hakujibu. ‘Inamaana hatutawasiliana tena!?’ Naya akafikiria kwa haraka kisha akamjibu. ‘Leo nitakutumia simu ingine, Bale. Ili tuwasiliane ila si kwa kutumia simu ya Malo.’ ‘Unanitumia simu ingine wapi na wewe hutaki tuongee?’ ‘Usiwe na wasiwasi.’ Naya akamjibu hivyo na kumpigia simu yake mwenyewe Bale. Kweli haikuwa hewani. Akaona ampigie simu baba yake.

“Mama mzazi?” “Kwani ulirudi kulala?” “Hapana. Kwema?” “Mbona sasa sauti yako ipo kama ulirudi kulala?” Akamsikia kama anahasira. “Nilikuwa nikiomba mama! Vipi?” Naya akatulia kidogo. “Eti mama, vipi?” “Bale amenipigia kwa simu ya Malon. Anasema eti simu yake imekorofisha.” “Inamaana gani?” “Mimi sijui baba. Ila namuhisi vibaya. Bale ameondoka hapa nyumbani simu yake haina shida kabisa! Naomba ukamnunulie simu kisha umtumie.” Baba yake akatulia. “Mimi nitakurushia pesa.” “Acha nizungumze nao wote wawili kwanza.” Naya akanyamaza. “Na Naya.” “Mimi nipo lakini...” Naya akasita. “Naomba ukatulize akili kazini. Umenielewa?” “Nahisi nimeshaanza kukasirika baba! Bale ananifanyia makusudi.” “Wewe usiwe na wasiwasi na Bale. Mimi nitazungumza naye. Na kama kuna uhitaji kweli wa simu, mimi nitakwenda kumnunulia na nimtumie. Uwe na siku njema. Usiende kuharibu kazi za watu huko. Katulize akili ili ufanye kazi vizuri.” “Asante baba.” Naya akakata.

“Samahani Joshua. Nilikasirika ndio maana niliona nimpigie tu simu baba.” “Mimi nisingekufanyia hivyo Naya. Siwezi nikakupuuza wewe hata iweje.” Naya akafunga macho. Hakujua kama Joshua angechukulia hivyo. “Samahani Joshua. Sikuwa nikikupuuza.” “Ila ni nini Naya? Nakuuliza, hunijibu, unaendelea kuchat, kisha unampigia simu baba na kuniacha mimi hapahapa!” “Nahisi napaniki Joshua.” “Unapaniki nini!?”  “Nahisi nimeingiwa na hofu mimi mwenyewe. Sitaki chochote kitokee.” “Sikuelewi!” “Sitaki chochote kitokee kati yetu sisi, halafu ukaniacha. Napaniki.” Joshua akatulia kidogo kama anayefikiria.

“Huyu ni Bale akinitafuta kwa kutumia simu ya Malon, anasema simu yake imekorofisha.” Kimya. “Samahani Joshua. Sijakupuuza.” “Kwanza nahisi hujaelewa Naya. Sipo na wewe kubahatisha. Sipo kwenye majaribio kwamba najaribu nikiona vinashindikana nakuacha!” “Kweli Joshua? Sio kwamba...” “Naya, kama wewe ni mke aliyenipa Mungu, hakuna atakayekutoa kwangu. Vya kwangu huwa Mungu ananipa nguvu yakuvitunza. Nilikwambia huwa nina vitu vichache na Mungu huwa ananipa uwezo wa kuvitunza. Nahisi bado hujanijua na kunielewa. Malon hanitishi mimi, Naya! Hata kidogo. Hata nikimsikia namsikia kwenye upande wa vitisho tu, kama aliyeshindwa. Wasiwasi wangu ni wewe Naya. Naona umempa nguvu kubwa sana zaidi hata anavyojua yeye. Yeye mwenyewe anajua amepoteza nguvu kwako ila wewe huonekaniki hivyo Naya.” “Mimi napaniki kwa ajili yako Joshua! Sitaki kukupoteza.”

“Hutanipoteza.” “Unauhakika Joshua?” “Kabisa. Ni vile hunifahamu Naya. Nisingekuwa hapa nilipo kama ningekuwa mtu wa kuyumbishwa yumbishwa. Naishi kwa vitisho kila siku. Kazi yangu yenyewe tu ni vitisho tupu. Natishwa na soko la dunia. Natishwa na soko la hapa ndani ya nchi. Lakini nipo hapa nilipo, na bado nimesimama nikiongoza kampuni kama ile! Unafikiri ni kwa nguvu zangu?” “Sijui Joshua! Mimi nimechoka na michezo isiyoisha.” “Basi usicheze.” Naya akawa hajaelewa.

“Mimi ni wako na nimekuhakikishia kuwa sina pakwenda. Nipo na wewe. Ishi hivyo. Acha kutishwa na jumbe.” “Naomba unihakikishie hutaniacha nikapotea na kuniacha nirudi tena kwa Malon, Joshua.” “Hata kama ukitaka mwenyewe?” “Joshua! Hata kama leo nikaamua kurudi kwa Malon ujue hakuna mwendelezo wangu na Malon. Ukiniacha leo, ujue ukija kuniona mwakani, nitakuwa Naya huyuhuyu, sina ndoa ila nimerudi kuwa mpweke zaidi. Mimi namjua Malon, Joshua. Kile umeona amemfanyia Bale, ndio mchezo wake hata kwangu. Hakujawahi kuwa na muendelezo. Tunaanza na mipango inayosikika vizuri lakini haijawahi kutimia. Ndio maana naogopa usije ukachoka na kuniacha kwa sababu yake ukadhani ni mpinzani wako. Mimi ndio nitabakia kuumia na kubaki mpweke mpenzi wangu. Natamani maisha kama yale ya Nanaa! Nataka kutulia na mtu wangu. Nakutaka wewe Joshua, ndio maana unaona napaniki. Sitaki kurudia ule upweke ulionikuta nao. Umebadili maisha yangu, Joshua! Umeleta tumaini ambalo hata sikujua kama lipo! Sitaki kukupoteza.” “Hutanipoteza. Nimekusudia kuwa na wewe.” “Kwa hiyo utanigombania hata iweje?” Hilo swali likamfanya Joshua acheke.

“Usicheke bwana! Mimi ndio kilio changu kilikuwa kwa Malon. Anichague mimi zaidi ya tamaa zake na kila kitu, nibakie mimi tu.” “Basi Naya, nitakupigania.” “Kweli Joshua? Mimi sikutanii. Usije kunibadilikia bwana!” “Nakuahidi Naya.” “Mpaka kifo?” Joshua akacheka na kutulia mpaka walipofika kazini maana walikuwa wamekaribia. Akaegesha gari na kumgeukia Naya. “Nitakulinda, na kukupigania mpaka kifo changu. Wewe ni wangu. Na hutarudi kwa Malon.” Naya akacheka kwa furaha. “Muone!” “Nimechoka mwenzio! Mimi nakutaka wewe kwa hali na mali. Sitaki eti ije itokee siku eti wewe upo na mwanamke mwingine sio mimi!” Joshua akacheka sana. “Kweli tena. Uning’ang’anie mpaka kifo changu.” “Sawa Naya Kumu. Naahidi. Naapa. Na Mungu anisaidie.” Wakatulia. Akamsikia Joshua anacheka kidogo.

“Nini?” “Sikujua kama na wewe unanihitaji kwa kiasi hicho! Kila nikipata huo uhakika, napata moyo. Nakupenda Naya. Na hata mimi sitaona haya kusema nakuhitaji. Nataka alichonacho Geb. Familia na mke anayemtaka na kumlinda akihakikisha anabakia kuwa wake daima. Nataka kutulia, nifunge hiki kipengele. Sasa kwa kuwa wewe umenihakikishia tena, tena kwa umbali huo, moyo wangu umetulia. Twende tukaanze siku yetu tukijua tulichonacho kinawindwa, na sisi tupo kukitetea mpaka kifo. Si ndivyo?” “Hivyo viapo vingesindikizwa na mabusu mazito.” Joshua alicheka mpaka  machozi. “Nakupenda Joshua. Nakupenda sana na ninakuhitaji. Mungu asaidie chochote kisitokee kati yetu.” Joshua akajivuta kidogo pale kitini na kweli akalitendea haki hilo busu alilotaka Naya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Huku kwa baba Naya akaamua kuanza kumpigia simu Bale. Chakushangaza yake ikaita kisha ikakatwa. Naya hakuwa akimpata kaka yake, lakini simu za baba Naya ziliingia na kukatwa mwisho ikawa haipatikaniki kabisa. Akaamua kumpigia Malon. Ikawa ikiita bila kupokelewa. ‘Mimi ni baba yake Bale, naomba kuzungumza na Bale kama upo naye karibu.’ Akatuma huo ujumbe na kusubiri bila mafanikio. Akapiga tena, safari hii simu ya Malon nayo ikawa haipo hewani. Akatuma ujumbe kwa wote wawili. ‘Tafadhali naomba Bale anipigie. Nawatakia siku njema.’ Akatuma huo ujumbe lakini hapakuwa na majibu wala hakuna aliyempigia. Mpaka wanakwenda kulala usiku huo hawakumsikia tena Bale, wala Malon na wote simu zao hazikuwa zikipatikana tena. 

Kwa Bale.

Wakati mapenzi yamepamba moto kati ya Naya na Joshua, wote wamehakikishiana kifungo cha mpaka kifo, huku kwa Bale naye akakusudia kutulia na kuwatafuta pindi atakapofanikiwa sana ili kuja kuwasuta. Na kweli akakusudia kurekebisha makosa ya baba yake akikumbuka yote aliyokuwa akilalamikia mama yao. Bale akakusudia kutokuja kuwa kama baba yake. Akajituma haswa huko Mbeya akiwa kwa Malon. Lengo ni kufanikiwa sana. Na Malon akipiga mahesabu jinsi ya kumrudisha Naya kwenye hemaya yake, ila akihisi kushindwa na Bale anashindwa kuwa msaada kama alivyotarajia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Geb alifika nyumbani kwa baba Naya na kustaajabu sana. “Ni vile ni wewe mzee wangu. Ningekupa pesa ya kukufanya unipe hili eneo bila kufikiria mara mbili.” Vijana wake Geb wakacheka taratibu. “Hili eneo ni zuri sana. Hapa tumesimama kwenye ardhi ambayo inaweza kukupa majibu ya mambo mengi sana.” “Kama nini?” Akauliza baba Naya akitaka kumsikia Geb. Akamuona anafikiria huku akiangalia lile eneo. “Kuna aina fulani ya nyumba huwa najenga.” Akamuona ametulia akifikiria. Akaangaza macho kulia kuchoto, mbele na nyuma. “Kwa vipimo,” Akaanza kutaja namba za ukumbwa wa eneo. “Kwa kutoa gala na sehemu ndogo ya kuhifadhia vifaa na ukapata ofisi ndogo tu kwa kutunza kumbukumbu zako, tutahitaji eneo la ukubwa...” Akafikiria na kutaja huku akiendelea kuangalia.

“Na kwa harakahara nikiangalia hapa. Hutamaliza eneo lote. Upande ule wenye ule msitu pale ambako ndipo kunakopokea upepo, naona patafaa. Lazima kujengwa kwenye sehemu ya juu kidogo kuepuka maji ya mvua yasiingie ndani na kupokea upepo kwa wingi mazao yabaki makavu. Jengo lenyewe lijengwe kwa muundo wa...” Akawa akiongea huku akifikiria. Akamuona anafikiria kwa mikono yake sasa kama anayefanya vipimo. “Hapana. Hiyo inazuia kuweza kuongezeka kwa jengo jingine biashara ikipanuka zaidi.” Akajipinga mwenyewe akiendelea kuzungumza wote wakimsikiliza.

Kisha akamgeukia baba Naya. “Unamjua jirani yako upande huu?” “Namfahamu. Ana eneo kubwa, nyumba yao ndio ipo mbali na hapa. Hapo amepaacha tu.” “Safi sana. Sasa nashauri ukamtembelee umuombe akuuzie sehemu ya eneo lake linalopakana na eneo lako kwenye upande wa huu msitu ili huku kwengine usibomoe, uache kwa baadaye kama endapo utataka kupaendeleza. Mtajie pesa unayojua itamuhadaa nakumfanya akubali kwa haraka. Usimtajie pesa atakayokutaka afikirie kwanza ndipo aje akupe jibu. Hapo utafungua jibu la hapana au kurudi kwako na bei kubwa zaidi.” Baba Naya akapoa. Alichokihisi kwa Geb kinatimia. Akili yake ni ya kufikiria makuu na yeye pesa hana.

“Ipo hivi mzee wangu.” Akamuomba wasogee pembeni. “Naomba nipate vipimo kuzunguka huo msiti hapo.” Akawaambia vijana wake ili abakie na baba Naya peke yao. Aliporidhika wapo peke yao akamgeukia. “Pesa unaweza kukopa popote na kwa yeyote, ila si ardhi. Sijui kama unanielewa?” Akaanza Geb. “Wengi wanaweza kuwa na pesa ila hawana ardhi. Ardhi ni utajiri ambao hubadilika thamani kwa kuongezeka, ila pesa hubadilika thamani kwa kushuka.” Baba Naya akacheka. “Aliyeshika ardhi, si sawa na aliyeshika pesa. Nikiwa na milioni 100 leo, mwakani thamani yake inaweza kushuka, nikajikuta hiyo milioni 100 haina uwezo kama wewe uliyekuwa na heka 100 mwaka jana na juzi. Wewe thamani yako itaongezeka, mimi nitapungua. Ndio maana tunakopa pesa kununua ardhi. Wasio na uelewa ambao wanatusaidia sisi, ni wale wanao uza ardhi kupata pesa wakiwa na shida. Hiyo ni siri alinipa baba yangu, na wewe nakuibia. Usiogope kununua ardhi kwa kuwa hupotezi.” Geb akaendelea.

“Walipokonya mali za baba yangu sababu ya baba kuja kuwa na mama yangu. Hapo maeneo ya Kibaha. Lakini mzee wangu, nilihakikisha narudisha mali ya baba yangu yote bila wao kujua.” “Geb!” “Kabisa mzee wangu. Walimuadhibu kwa kosa la kutoka nje ya ndoa, japo hakumuacha mkewe ila ile tu kuwa na mama pia. Matokeo ya hayo makosa ni mimi na dada yangu Grace. Wakampokonya jasho lake kwa kuwa yeye ndio alikosa kwenye ndoa! Akaachwa hana mali. Ni miaka mingi sana, alikufa akiwa hana kitu kabisa. Ila akahangaika sana akabahatika mali chache ambazo alikusudia akifa amuachie mama. Na kweli ikawa hivyo lakini naye mama aliuza ili nisome. Nilihakikisha namrudishia mama ardhi yake kama vile alivyopewa na baba, na kurudisha mali zote za baba. Zimerudi kuwa ni za Magesa tena. Sio Magesa yule wa kwanza, ila Magesa mimi na Magesa wajao. Ndugu wa mke wa kwanza waligawana na kuuza hovyohovyo, nimerudisha zote. Ukiwauliza wao, pesa wamemaliza, ila mimi nimebakiwa na ardhi ya baba yangu. Sijapoteza. Na inazidi kuongeza thamani na kuleta utajiri.”

“Ninachotaka kukwambia ni nini! Ni kwamba unachohitaji ni ‘ndiyo’ ya mwenye ardhi. Hiyo tu. Ukishapata ‘ndiyo’ yake, unamkabidhi pesa, unatunza ardhi. Halafu itamkie kitu ile ardhi, jipe muda kama Mungu alivyomtoa mwanadamu kwenye ardhi. Akamfinyanga kwa makini na ustadi, uone kama hujatawala hili eneo na kila atakayekuona atakuita heri kwa  kuwa umeijua siri! Utakuwa umejiunganisha na siri ya kiMungu. Ardhi haijawahi kumtupa mwanadamu, mzee wangu.” Mpaka hapo baba Naya akawa amehamasika.

“Usiogope madeni. Chukua pesa mfukoni mwa walionazo, kisha fanyia makubwa. Wapo wenye pesa wanatapanya kwa kuwa hawajui nini chakufanya, kwa hiyo wanapoteza. Wewe unalo wazo, fikia malengo kwa kutumia pesa zao.” “Nakushukuru sana Geb. Nitakwenda kisha nitajua ni kiasi gani.” “Hapana mzee wangu. Sasa hivi unahangaikia ‘ndiyo’ ya mwenye ardhi. Usiweke pesa mbele. Akishasema ‘ndiyo’ tu, hakuna kulalika mpaka umepabadili pamekuwa kwa jina lako wewe. Usiogope pesa, ogopa HAPANA ya kuuziwa. Ombi lako ukiwa unaenda kwake ni Mungu akupe kibali, akubali kukuuzia. Nenda ukitaka ardhi sio ukiwa unaogopa bei. Utashangaa jinsi mazungumzo yenu yatakavyokuwa marahisi. Hutakuwa na hofu, ila ujasiri na atakuuzia tu.” “Nimeelewa.” Baba Naya akakubali.

“Baba yangu alikuwa akisema, ‘linalowezekana leo, lisingoje kesho.’ Sijui kama umeelewa?” “Nimeelewa.” “Basi, sasa naomba mimi nikuache. Tutawasiliana ukishatoka kuzungumza na mwenye shamba.” Geb akawapa maelekezo wale mafundi wake zaidi kiongozi wao kwamba apime kisha amtumie vipimo kamili kwenye eneo aliloona, kisha akaondoka na kumuacha baba Naya na mawazo ya hofu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akaona ampigie simu Naya. Akamuelezea kwa ufupi mazungumzo yake na Geb na hofu yake. “Sitaki hawa watu wanione kama mzigo, mama. Au wasije niona mzubaifu. Maana hata kama tukipewa hilo shamba hapo nyuma, tunapata wapi pesa? Nani wakunikopa? Sitaki mahusiano yakujengwa kwenye misaada, mama. Sitaki aina hiyo ya mahusiano. Sitaki ujikute unafungwa tena kwenye mahusiano ya pesa, ukabaki ukilipa fadhila.”

 “Kwa jinsi nilivyowasoma hawa watu baba, ni watu wa umoja. Wakisha kufahamu na kukupokea, unakuwa mmoja wao. Mimi mwenyewe mpaka imebidi kuzungumza na Joshua. Wanagawana vitu vyangu vya harusi bila kujali bei. Tena mama yao ndio anavigawa. Hawawazi bei ila kufanikisha jambo. Nimetoka kuzungumza na huyo Grace muda si mrefu akiwa na Nanaa kwenye simu. Yaani baba, mimi mpaka nimewashangaa! Shuguli yangu wameibeba kama yao na kwa moyo mmoja mpaka wamenishangaza! Wote wanaongea lugha moja na mama yao ndio anawasisitiza hataki wamuharibie harusi.” “Hiyo harusi yenu!?” Baba Naya akauliza kwa kushangaa.

“Harusi yetu baba! Mpaka ananishangaza. Amegawa majukumu na anasisitiza anataka aletewe vitu vizuri, kama mimi naishi pale kwao! Kwa hiyo usiogope baba. Umekuwa ukiomba sana. Inawezekana huu ndio wakati wa Mungu kwako. Usirudi nyuma, songa mbele. Nenda kazungumze naye. Mzee Kwayu haonekani kama anampango na hilo eneo. Hana pesa, ukimwambia unampa pesa hata kesho, hawezi kukataa.” “Sasa huo ndio wasiwasi wangu mama. Hiyo kesho pesa naipata wapi, mama!?” “Nenda kisha tutajua. Naomba usiogope.” Akavuta pumzi  kwa nguvu na kumuaga mwanae.

‘Joshua!’ Naya akamtumia huo ujumbe. ‘Nipo kwenye simu na GM, nitaitika mama Kumu.’ Naya akacheka baada ya kusoma huo ujumbe, lakini akajua Geb anamtaarifu kilichoendelea. Akatulia. Mipango ikaendelea. 

Kimeumana.

Huku kwa Bale bado hakuwa amewasiliana na mtu yeyote yule wa nyumbani kwao. Juma la kwanza likapita, na la pili akiwa kwa Malon. Kula kulala, na uwepo wa kila mmoja kwa mwenzie kuanzia asubuhi mpaka jioni, uhalisia ukaanza kuchukua sura yake. Akamfahamu Malon ambaye Naya hakuwahi kumfunua kwao. Siye waliyekuwa wakikutana kwa  mazungumzo ya dakika chake kisha kuagana. Sio Malon anayetaka kuonekana bora zaidi ya wanaume wote wa Naya. Hapana. Malon halisi ambaye yupo kazini. Anayepambana kwenye maisha. Kwanza anayechukia umasikini kwa vitendo, pili anayewahakikishia watu shule si kila kitu, na yeye hakukosea kukataa shule. Hakutaka chochote kitokee kwenye biashara zake, na hakutaka kugawana utukufu na yeyote yule kwenye mafanikio yake. Kwa hiyo hakukaribisha akili ya mwingine yeyote yule ili wasije jipatia utukufu kwenye mafanikio yake. Alitaka mafanikio yake yawe yeye kama Malon, sio mtu mwingine.

Sasa akakutana na Bale na yeye anao moto wa maendeleo. Afanikiwe na kufedhehesha watu wa nyumbani kwao. Akitaka kuwa kile mama yake alimsikia akilalamikia. Kufikiri kwa haraka na kutenda. Kipaji chake cha uongozi, elimu aliyo nayo, sasa amewekwa kwenye eneo la kazi. Akachangamka kwelikweli akitaka kuwa kama Malon, asijue anachangamkia sehemu iliyobeba hatima na malengo makubwa sana ya Malon. Vikaanza kuumana.

 “Kabla hatujakwenda mbali naomba nikuweke sawa, Bale.” Malon akamfuata akiwa katikati ya wafanyakazi wengine, Bale akijua yeye ni kiongozi wao. “Nataka utambue nafasi yako hapa. Na hilo sitaacha kuliweka wazi. Si kwako tu, ni kwa kila mtu anayekuja kunifanyia kazi. Kwa baba yako sikulazimika kwa kuwa alionekana anajua nafasi yake.” Malon akaanza na kumshitua kidogo Bale.

“Hichi unachokiona hapa, nimeanza kuanzia chini kabisa nikiwa najijua mimi ni nani, nafasi yangu na ninakwenda wapi. Hapakuwa na sayansi iliyotumika hapa wala elimu ya chuo Kikuu ile mnayokaaga nyinyi darasani, wanaume wenzenu wakiwadanganya juu ya mambo ambayo hata wao hawayajui na yameshindwa kuwaweka mjini, kama hivyo wewe. Wakishamaliza kuwadanganya huko darasani, wanarudia dhiki zao na kuwafanya nyinyi wafuasi wao. Mnakaa huko vyuoni miaka mingii mkifundishwa ujinga ambao unashindwa hata kuweka chakula mezani. Mnarudi mtaani kuombaomba walewale ambao mliwaacha, mkajidai nyinyi ndio wasomi.” “Mbona unaanza matusi Malon!?” Bale akashangaa sana. Akahisi Malon hayupo sawa, kama ambaye ameshavuta bangi inayomzungusha kichwa anaongea tu.

“Ninapoongea sitaki uniingilie Bale. Mimi sio Naya au baba yako unayemjibu utakavyo. Upo kwenye himaya yangu nataka heshima. Unanisikia Bale? Sitaki ujinga na sitaki ujuaji kwa kuwa huna unachojua.” Bale hakutegemea. “Acha kutoa macho ukishangaa. Mimi nakuwa muwazi kwa kuwa sitaki unirudishe chini. Unanielewa Bale? Sitaki uniharibie hapa. Sitaki ujuaji. Usilete elimu yako ya darasani kwenye biashara yangu kwa kuwa mimi nakujua wewe na unakotoka. Huo ujuaji unaotaka kuwaonyesha wafanyakazi wangu, kama kweli wewe ni mjuaji kama unavyojionyesha kwao, si ungekusaidia wewe mwenyewe na baba yako?” “Acha kumtukana baba yangu Malon. Hausiki hapa!” Bale akasikia kuumia.

“Haa! Anayemtukanaga baba Naya hapa ni nani kama si wewe?!” Malon akamuuliza kwa ukali kabisa. “Ushawahi kunisikia mimi nikisema vibaya wazazi wangu hata siku moja? Muulize Naya. Mimi nilikataa ushauri wao. Sikufuata walichokuwa wakitaka, lakini sikuwahi kuwatukana hata mara moja. Nilichokuwa nikifanya ni kusikiliza, sijibu na kuondoka. Mimi huwa nabishana na watu wengine lakini hutanisikia nikijibishana na wazazi wangu hata mara moja. Ndio maana mimi mzee alikuwa akinipiga karibu kuniua, lakini sikuwa na mjibu na nilikuwa sifanyi anachotaka nifanye. Piga simu hii hapa muulize Naya kama katika mabaya yangu yote kama alishawahi kunisikia au hata kusikia fununu kama mimi nilikuwa nikibishana na wazazi wangu kama hivyo wewe ulivyokuwa ukimjibu baba yako kama hana akili nzuri! Uliza.” Bale kimya.

“Wewe ndiye unayemtukana kila leo na kusema amezubaa, hana uwezo wa kufikiria! Lakini baba yako alikuja hapa na shida zake, akaelewa nafasi yake, akatumika na kuondoka bila tatizo. Uliza wote hao wanamfahamu na kumuheshimu yule mzee, kwa kuwa walimuona akitumika hapa bila maneno mengi ila kazi tu mpaka siku anaondoka hapa, wanahuzunika. Mpaka leo wanamuulizia baba yako unayemdharau na kumsema vibaya!”

“Sasa wewe umekuja tu na kuanza kutawala wenzio! Unawafoka na kuwapanga utakavyo! Unaweka mashariti na mipango yako bila kuniuliza!?” “Nia ni kutaka kusaidia Malon! Kitu kisiharibike.” “Ushajiuliza wakati wewe upo darasani nani alikuwa akiwaongoza hawa?” Bale kimya.

“Acha ujuaji wa kijinga. Hawa hawajasoma lakini wanaijua hii kazi kuliko wewe uliyekaa darasani miaka yote hiyo! Wanakucheka tu hao na kukudharau wakikusema kwa kilugha chao, wameshakusoma na wanaambizana kuwa unajidai ni mjuaji wakati hujui chochote! Wanakukebehi tu. Na ujue wazi unajidhalilisha tu hapa. Wanajua mambo hao, zaidi yako. Nimekaa nao hao waulize kama kuna nilipokosana nao. Japokuwa unawaona hawana shule kichwani lakini mashine zote hizo wanajua kuzitumia. Nikiwa Dar, wao ndio nawaachia kila kitu! Hatujawahi kupishana nao hata mara moja. Nawaheshimu sana hao wote, maana ndio wanaoshika hatima ya biashara yangu! Halafu wewe unakuja kuwafoka wanaume wazima hao na familia zao! Nipo ndani huko nakusikia ukiwapanga kwa ukali, halafu sasa hujui ni nini unazungumzia! Acha kabisa Bale. SITAKI ujuaji. Hapo tutakosana na sina utani, muulize Naya. Huwa ananijua na kila anayenifanyia kazi ananitambua. Linapofika swala la biashara zangu sitaki utani na sitaki ujuaji. Mimi ndiye najua nini kifanyike, nani akifanye na kwa muda gani.”

“Umeletwa na shida ya kazi, fanya majukumu yako, heshimu wengine, kaa pembeni. Unanielewa Bale?” Kimya. “Wakati nyinyi mnafundishwa zile hesabu zenu walizochanganya namba na herufi, wenzenu tulikuwa mtaani tukisaka pesa. Washamaliza kuwadanganya huko darasani eti ndio unataka kuja kunitibulia hapa kwangu! Sitakuruhusu Bale. Washa simu yako mpigie dada yako atakwambia ninavyokuwa linapofika kwenye swala la biashara zangu. Sina udugu, sina mchezo. Naya mwenyewe alikuwa akijua kutumia tu, hajui nilikokuwa nikitoa pesa.” “Ni nini Malon? Kweli ndio unamsema vibaya Naya kwa namna hiyo! Sio wewe ulikuwa ukimsifia na kipaji cha ajabu!” Bale akashangaa sana.

“Unakosa pointi ya muhimu sana Bale. Swala la kipaji cha Naya na matumizi ya pesa yangu na upatikanaji wa pesa yangu ni vitu tofauti kabisa. Kipaji cha Naya kilijulikana sababu ya heshima yake kwenye biashara zangu, ndipo akaweza kufikia pesa yangu. Na hakuna mwanaume ataweza kumuinua Naya kama mimi. Na ndio maana unaona vipaji vyote vimekufa alipoamua kuniacha mimi. Katika harakati zake zote za kunufaika na pesa yangu, mwenzio alijua kuniheshimu mimi na mipango yangu. Hakuwa bosi wangu. Alijua hayamuhusu, kazi yake ikabaki kutumia tu akiwasaidia nyinyi wote. Ninachotaka kukwambia Bale, jua, tambua na elewa nafasi yako. Wewe ni mfanyakazi kama wafanyakazi wengine wote hapa. Wote mnafuata maelekezo yangu. Vikikushinda ondoka. Kabla hujaona upande wangu mwingine ambao ujue hutaupenda na sikutanii. Muulize Naya. Tabia zako za ubishi na ujuaji, tafadhali hapa si sehemu yake. Kuwa makini.” Malon akaondoka.

Wafanyakazi wengine wakaanza kucheka waziwazi na kubadili kilugha. Bale alijua wazi wanamsema yeye huku wakimcheka. Akaumia sana asiamini alichokifanya Malon. “Ameshindwa vipi kuniita pembeni na kuzungumza na mimi!?” Akajiuliza Bale akiwa hajui chakufanya tena. Aondoke au abaki hapo!

Maamuzi Magumu Kwa Bale.

Yalikuwa mazingira magumu kwa Bale kuwepo katikati yao tena. Akaamua kutoka hapo kabisa eneo hilo la shambani ili akajitulize mjini. Hapo walipokuwepo kwenye ghala za Malon na mjini palikuwa na umbali wa kutosha tu. Lakini hasira na fedheha ikamsaidia kutembea bila kuchoka katika jua hilo mpaka mjini. Akaenda kukaa kwenye moja ya mgahawa akiwa anatokwa jasho kwelikweli. Akaagiza kinywaji na kubaki hapo akitafakari maneno ya Malon na kushindwa hata kunywa. Chupa ya soda ikabaki mbele yake ikiwa vilevile hata hajagusa japo alishafunguliwa, akabaki akitafakari. Akasikia kuumia sana, hakujua nani wa kumlaumu.

Akatamani kuwasiliana na nyumbani kwao, akakumbuka yameshapita majuma mawili tokea atoke nyumbani kwao, na kugoma kuwasiliana nao kabisa. Mwanzoni alianza kwa kuzima simu yake, mwishoe akamuomba Malon amtafutie line nyigine, akabadili namba yake kabisa na kumuonya Malon asije pokea simu zao, ndipo wakakubaliana wazifungie kabisa. Ndipo hata Malon akawa hapatikaniki na baba Naya pamoja na Zayoni. Ila hakufungia simu za Naya, hapo Malon alikataa. Bale akalikumbuka hilo. Akapoa. Aliondoka akiwa amejawa tumaini akijua atarudi akiwa amefanikiwa sana. Siku hiyo tumaini zima lilimuishia. Malon alimtoa juu sana na kumrudisha chini, akajiona mjinga kupita kiasi.

Akabaki hapo akiwaza. Akapotelea mawazoni kabisa. Mawazo yakamrudisha kwa mama yake. Akatamani kama mama yake angekuwa hai angekuwa na kwa kurudia. Akapotelea mawazoni akiwa amejawa uchungu wa kupitiliza.

Yaliyo Sirini, Mwangani.

Wakati amepotelea mawazoni akaona gari ya Malon imesogea mpaka kwenye nyumba za kulala wageni iliyokuwepo karibu na alipokuwa amekaa. Malon akashuka na kuingia ndani. Akajiweka sawa. Baada ya kama dakika saba tu, akaona gari ingine imesimama hapo. Akashuka mdada mrembo tu, akaingia ndani. “Nisimfikirie Malon vibaya. Amenihakikishia ameokoka na ameacha tabia za wanawake.” Akamtetea moyoni mwake kwa hofu. Akakumbuka tabia za Malon za kupenda wanawake. “Ila ile ilikuwa ni kwa sababu ya bangi. Malon ameokoka na ameacha bangi. Sijasikia hata harifu ya bangi! Wanao vuta ni wale vijana tu si...” Akasita Bale na kujikuta akitetemeka kwa hofu huku akiomba Mungu asiwe amekosea kwa kiasi hicho. “Haiwezekani!” Akapinga na kujikuta macho yamegomea kwenye nyumba ya kulala wageni. Akikumbuka hali ya Malon asubuhi hiyo wakati akimfoka kama aliyepagawa.

Alikaa hapo mpaka giza likaanza kuingia hata asijue kama ulishapita muda mrefu kiasi hicho. Baada ya muda akawaona Malon  na yule dada wakitoka pamoja. Safari hii wakaondoka na gari ya Malon. Bale akaanza kusikia jasho likimtoka mida hiyo ya jioni, mjini Mbeya ambako baridi ilishaingia. “Mungu wangu nimefanya haraka kumuamini M..”  Akasita na kubaki akisindikiza gari ya Malon kwa macho.

Alikaa hapo mpaka usiku kabisa. Alikuja kushituliwa na muhudumu kuwa wanafunga. “Kwani sasa hivi ni saa ngapi?” “Inakwenda saa sita kaka yangu. Mpaka jikoni wamefunga.” Bale akatoka hapo hata hamu ya kurudi kwa Malon ilikuwa imemuisha. Akatembea taratibu kurudi mpaka nyumbani kwa Malon. Alikuta gari yake kuashiria alisharudi. Alichofanya ni kuingia kwenye chumba alichopewa akitumie na mwenzie Mpoki, akakusanya vitu vyake vichache akaondoka akiwa amemuaga Mpoki. “Naomba mwambie kama kuna malipo yeyote anayoona nastahili, anirushie kwenye simu yangu, namba ambayo alininulia yeye mwenywe.” Usiku huohuo Bale akaondoka nyumbani kwa Malon.

Naya&Joshua.

Huku kwa kina Naya mambo yalikuwa yamepamba moto. Mapenzi mazito. Joshua na Naya wakiwa wanakaribia ndoa yao. Amani na furaha vikawa vimetawala. Naya akiwa katikati ya familia ya kina Magesa kama mmoja wao. Nguo nzuri ya harusi kwa Naya ikawa imeshapatikana. Zikawa zimebaki siku chache tu harusi yao ifungwe. Nanaa na mama Magesa walimuandalia Naya kichen Party nzuri sana. Watu wachache tu tena wakaribu. Wakakodi ukumbi mdogo tu wakutoshea wageni wao, na kualika wanawake wa kanisani kwao pia. Wengi waliokuwa na mama Naya tokea Naya ni mtoto mdogo akikua hapo kanisani. Naya alikuwa amejawa furaha ya kupitiliza asiamini yote hayo anafanyiwa yeye tu! Alijawa furaha ya ajabu.

Mambo yalikwenda vizuri kina Geb nao walimfanyia Joshua Bachelor party. Wakakutana wenye pesa zao na kusheherekea Joshua kuuacha ukapela. Ukawa wakati mzuri sana jioni hiyo, baba Naya akiwa kwenye shuguli zake. Mambo yakibiashara ndio yalikuwa machanga, akawa busy akihakikisha kitu hakiharibiki kwenye biashara zake.

Baada ya kila kitu Joshua akaenda kumchukua Naya ili amrudishe mwenyewe nyumbani. “Mimi Joshua Kumu, nimepata kitu chema! Umependeza sana Naya na onaonekana unafuraha!” “Sana!” “Nimefurahi kukuona hivyo.” “Hii furaha itakamilika nikishavaa ile shela, na pete ya ndoa. Ndio nitafurahi zaidi.” “Zimebaki siku chache sana furaha yetu ikamilike. Twende ukapumzike. Maana mama amenisisitiza nikurudishe nyumbani moja kwa moja asisikie unazurula mtaani.” “Mama G!” Naya akakumbuka na kuanza kucheka wakati mzuri alioupata usiku huo. Akaongeza. “Hata mimi amenisisitiza.” Wakacheka wakiwa njiani wanarudi Kiluvya kwa baba Naya. Wakaanza kuimba wakipokezana mpaka walipofika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakamkuta baba Naya amekaa sebuleni. “Umejawa na furaha mama!” “Sana. Tumecheza sana ukumbini, tukawa tunacheka mno. Hakika nimekuwa na wakati mzuri baba yangu. Hivi zawadi zinakuja nyuma. Nimeacha wakipakia kwenye gari ya kina Magesa ili dereva alete. Ila nimefurahi.” Baba Naya akacheka kidogo wakamuona ameinama. Naya akahisi anajambo akamkonyeza Joshua kama akae.

Akaenda kukaa pembeni yake. Joshua naye akakaa. “Umekula vizuri, baba Naya?” Naya akaanza. “Sitaki kukuharibia wakati wako, lakini..” Akasita. “Nini?” “Kuna kitu hakipo sawa kwa Bale, Naya. Naweza nikakosa lugha yakueleza lakini moyoni mwangu najua kwa hakika lipo jambo. Hii ni siku ya pili moyo wangu unauma, nashindwa kutulia juu yake. Nimeomba na  kushindwa kula tokea jana, lakini nimeshindwa kabisa kupata amani. Tokea juzi najaribisha simu yake, haipo hewani. Na Malon hivyohivyo.” “Lakini si umekuwa ukiwapigia na mara zote unakuwa ukisema huwapati? Mwache tu baba pengine hataki mawasiliano na sisi.” Wakamuona anatingisha kichwa anakataa.

“Hapana Naya. Kuna kitu hakijakaa sawa. Nimeomba Mungu hata anionyeshe kwenye ndoto, lakini haijatokea. Moyo umejawa hofu ya ajabu! Tafadhali mpigie wewe Malon.” “Baba!?” “Tafadhali mama. Nisaidie tu ili moyo wangu utulie. Mwambie nataka tu kujua kama yupo mzima, basi. Hilo tu.” Naya akamwangalia Joshua. “Mimi mwenyewe nilitumia simu ya GM kumpigia sikumpata. Sijui kwa nini, tokea wakati ule, kwa mara ya kwanza na mimi leo nilimkumbuka Bale, na kumuomba GM anipe simu yake nimjaribu nikijua simu zangu amezuia. Lakini hata ya GM haikwenda! Nashauri kweli tumpigie Malon ili kujua.” “Mimi leo nilikuwa na furaha sana jamani, sitaki kutibuliwa!” Naya akalalamika. Joshua akamtizama kama anayemkumbusha kitu. Naya akatoa simu yake kwenye pochi.

Mtaka Cha Mvunguni, Sharti Ainame.

Naya akampigia Malon hata bila hata kuitafuta namba yake. Ilikuwa tu vidoleni kwake hakuhitaji kukumbushwa. Bado ilikuwa imebaki kichwani mwake hata vidole havikuomba msaada. Akapiga na kubonyeza spika ili wote wasikie. Iliita mara moja tu akapokea usiku huo mpaka Naya akashangaa. “Naya mama, umenikumbuka?” “Samahani nimekupigia mida mibaya, lakini nilikuwa ninas hida  na Bale. Baba hampati kwa simu, naomba tuzungumze naye.” “Mimi nilijua yupo huko!” Naya akamtizama baba yake kwa wasiwasi. “Nasikiliza. Muulize aliondoka lini?” Malon akawa ni kama amemsikia baba yake akajibu. “Nafikiri siku kama nane zimepita sasa au kumi! Bado hajawatafuta tu?” “Hivi Malon wewe kichwa chako kikoje jamani!? Kwa nini unakuwa na mtoto wa mtu unashindwa kuwasiliana.” “Heee! Naya! Bale si mtoto mdogo. Anaposema hataki kuwasikia nyinyi kabisa, mimi nilitakiwa kufanya nini?!” Malon akamuuliza kwa kumshangaa.

          “Ni kwa nini wewe uliondoka naye bila kuzungumza na yeyote?” “Pengine wewe hujui, lakini baba yenu alikuwa akijua na kunishukuru kabisa kwa kumpa nafasi ya kazi huyo Bale!” “Hiyo ilikuwa mara ya kwanza Malon! Kukawa na maelewano mazuri mpaka ukamkimbia, ndipo...” “Subiri kwanza Naya. Naona mnatafuta mtu wakumlaumu kwa mambo yenu ya kifamilia! Sijui ni nini kinaendelea huko, mnashindwa kuweka mambo yenu sawa, naona mnataka kuniingiza na mimi! Ulinikataa, nikaamua kuwaacha kabisa. Safari hii nikaheshimu maneno yako. Lakini Bale akawa ananisumbua siwezi kulala na siwezi kubadili namba, kwa kuwa alikuwa akizijua namba zangu zote na akawa anatumia zaidi ile ya biashara ambayo wateja wangu wote wanayo.”

“Malalamiko juu yenu zaidi mwanaume wako yalikuwa hayaishi! Analalamika kuchoshwa na umasikini wa nyumbani kwenu ambao hauishi, anaomba msaada. Ninazo jumbe zake mpaka leo, naweza kuwatumia muone.” “Haina haja.” Naya akajibu.

          “Bale hana maadili kabisa. Amekuja hapa mkorofi na mjuaji anataka kutawala biashara zangu wakati hajui misingi yangu! Anataka kuwa kiongozi wa watu aliowakuta kazini, wanaojua kazi zangu kuliko hata yeye na shule yake ambayo amekuwa akijisifia nayo hapa kijijini! Haambiliki. Nimezungumza naye, kama kawaida yake, hawezi kusikiliza mtu, yeye ndio yupo sahihi wakati wote, anataka kujibishana! Mimi sina muda wa kijinga Naya. Na unanijua nilivyo makini na biashara zangu. Siwezi kuruhusu mtoto aliyekuja leo tu, hajui hata maisha ni nini, aniharibie mimi! Hapana. Nilipojaribu kuzungumza naye, amekasirika na kuondoka siku ileile niliyomuonya aache kufoka wafanyakazi wangu na kumtaka awe na heshima. Kwanza wengi wao hapa wamemzidi hata kwa umri! Watu na familia zao, wenye wake na watoto, eti yeye anawafanya wajinga na kuwafoka hovyo! Nilishindwa kuvumilia, Naya.” Malon akaendelea.

          “Alivyo mtu wa ajabu, aliamua kuondoka bila kuniaga. Tena muda, anamuaga mfanyakazi wangu ambaye anatumia naye chumba sio kwamba mimi nilikuwa mbali!  Hapana. Nipo chumba cha pili tu. Ameondoka na kumtuma mfanyakazi wangu eti anataka nimlipe pesa yake kwa kumrushia kwenye simu yake!” “Namba gani ya simu uliyomrushia pesa?” Naya akauliza. “Siwezi kukupa hiyo namba kwakuwa alinionya kabisa nisikupe wewe wala mwanaume wako anayemsema ni mnyanyasaji. Anapenda yeye tu ndio awe nacho si..” “Malon, tafadhali naomba namba ya Bale hiyo unayoifahamu. Bale hayupo hapa nyumbani, na hajulikani alipo. Tafadhali Malon.” Naya akamkatisha akimsihi.

Kidogo akatulia. “Basi acha nimpigie kwanza yeye mwenyewe nimuulize. Akikubali ndipo nitakutumia.” “Tafadhali mwambie baba anawasiwasi sana. Anaomba apokee simu yangu. Ilimradi tu tujue kama yupo salama, hatutamsumbua. Ni salamu tu.” “Nitafikisha ujumbe.” “Na naomba ukumbuke nakusubiria Malo. Usipotee.” “Mimi nipo Naya, ila wewe ndio nakushangaa unataka kujiingiza kwenye matatizo! Unataka nini Naya, mpenzi wangu? Tulipokuwa pamoja na familia ilikuwa pamoja. Amani, utulivu na heshima. Sasa kwa nini unataka kuharibu tulichonacho na kujiingiza kwenye ndoa ambayo...” “Nasubiria namba ya simu ya Bale, Malon. Tafadhali sana.” Naya akakata.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          Wote walikuwa wakisikiliza, wakabaki kimya kila mtu akiwaza lake wakimsubiria Malon. “Nikuletee chai, baba?” “Nashukuru mama, ila acha tu.” “Bale ni mzima baba, usiwe na wasiw...” Kisha akasita. “Naamini atakuwa mzima. Atakuwa amepata kazi sehemu ingin...” Akasita tena akipingana na mawazo yake mwenyewe. Bale hakuwa mwenyeji huko mjini Mbeya. Hawakuwa watoto waliokuzwa mbali na hilo jiji la Dar. Bale ameondoka hapo kumfuata Malon ndio mara yake ya kwanza kusafiri kwenda mikoani tena peke yake. Akaanza kuingiwa na yeye na hofu.  Akaona anyamaze na yeye asubirie.

          Furaha yote ikaisha, wakabaki na wasiwasi. Tumaini likabaki kwa Malon pekee anayeweza kuwasiliana na Bale. Wakasubiri zaidi ya dakika kumi na tano, Malon akawa hajarudisha bado simu aliyoahidi kurudisha. Akaenda kubadili nguo za shuguli alizokuwa amevaa na kuvaa nguo za kawaida tu kisha akarudi kukaa hapo sebuleni wakisubiria simu ya Malon. Baada ya lisaa Naya akaamua kumpigia yeye, simu yake na yeye ikawa haipo hewani. “Haiwezekani!” Naya hakuamini. Akaamua kumpigia tena Malon, hakumpata. “Hakika siamini!” “Nipe na mimi namba yake, nimjaribishe kwenye simu yangu.” Joshua naye akaanza kumpigia bila mafanikio.

Naya akamwangalia baba yake. “Sio mwenyeji sana kule Mbeya, lakini itabidi kesho niende.” “Kweli baba!?” “Kabisa mama. Sina jinsi. Wale vijana wote wa Malon nafahamiana nao na walitokea kuniheshimu sana. Nitaanzia kwao. Angalau kujua kama kuna ambaye alikuwa karibu na Bale pengine alimsikia hata akiweka mipango fulani. Nimtafute mpaka nimpate. Nikimuona na nikaridhika yupo sawa ni kwamba hataki tu kutuona, nitamuacha na kumuomba angalau awe anatuma ujumbe hata mara moja kwa juma tu. Basi. Nitamwambia hana sababu ya kuwa akipiga ila salamu tu basi tuwe tunajua yupo mzima.” Naya akapoa kabisa.

          “Lazima niende mama, lasivyo sitaweza kufikiria. Nina hali mbaya sana ndani ya moyo wangu. Naugua kiasi cha kushindwa kutulia.” “Natamani kukusindikiza!” “Hatuwezi wote kukwama kwenye jambo moja. Acha mimi niende tutakuwa tukiwasiliana.” “Naomba uwe unanikumbuka na mimi, baba. Sitaolewa bila wewe na siku zimebaki chache.” “Nitarudi mama. Nitarudi. Niombee nifanikiwe mapema.” “Ungehitaji msaada wowote, mzee wangu?” “Maombi tafadhali. Kule macho yangu yasipofika, basi Mungu amtizame na kumlinda.” “Tutakuombea. Ulikuwa ukifikiria kuondoka na usafiri gani?” “Basi tu. Nitatumia basi ndio itakuwa rahisi kufika huko kwake. Nikianzia stendi ya mabasi, naweza kufika huko. Pana umbali kidogo na mjini lakini napakumbuka. Nitafika tu.” “Nilifikiri kwa usafiri kwa ndege utafika haraka ukiwa hujachoka!” “Labda wakati wa kurudi. Lakini kwenda, acha nitumie tu basi. Itaniwia rahisi. Nashukuru.” “Acha nikamwandalie sanduku la safari. Mbeya huwa kunakuwa na baridi.” Naya akaongea kwa unyonge akianza kuona dalili mbaya juu ya harusi yake.

          “Usiku mwema Joshua. Tutawasiliana.” “Ni sawa tukiomba pamoja?” Akauliza Joshua. “Tumuombee Bale na safari yako mzee wangu. Tumsihi Mungu awe na wewe katika yote. Arahisishe mambo yote na akulinde. Njoo Naya.” Wakasimama na kushikana mikono. Joshua akaanza kuomba kwa kutubu. Yeye mwenyewe na kuwatubia wote mpaka Bale. Akatubu kwa popote pale walipomkosea Mungu na kumsihi Mungu awasamehe na kuwarehemu. Aliomba Joshua mpaka baba Naya akapokea. Ukawa usiku wa maombi ya namna yake. Wakaomba amani na utulivu katikati yao, ndipo Joshua akaondoka.  

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bale Yuko Wapi? Ni nini kitaendelea kwa familia hiyo?

Harusi ipo?

 

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment