Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 31. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 31.

 Baba Naya Mjini Mbeya.

Joshua alifika hapo mapema sana siku hiyo mpaka akawashangaza. “Kwema?” akauliza baba Naya wakati akimfungulia. “Nilitaka kuja ili tukusindikize na Naya. Angalau tuwe pamoja, Naya asijikute amebaki peke yake pale kituo cha mabasi.” “Hapo umefanya vizuri, nashukuru sana.” Akaingia ndani na kumkuta Naya akiwa ameshamaliza kuandaa sanduku la baba yake.

          “Karibu Joshua, na asante kwa kuja.” “Karibu. Nisaidie nini?” “Kuweka hili sanduku kwenye gari ndipo tutoke moja kwa moja, awahi.” Joshua akatoa sanduku, baada ya muda mfupi sana wote wakajikuta kimya, ndani ya gari ya Joshua wakielekea kituo cha mabasi makubwa yaendayo mjini Mbeya. “Unipigie simu kila wakati, baba.” “Nitafanya hivyo.” “Ukichelewa ujue nitakufuata.” “Tutawasiliana. Usiwe na wasiwasi. Naomba tulia kazini mama. Tusiharibu kila mahali. Ila naomba usisahau kupita kule dukani jioni ili uwasaidie kufunga mahesabu.” “Nitakwenda. Wewe usiwe na wasiwasi na huku. Ila kuwahai kurudi kwako baba. Mimi nataka kuolewa. Na siwezi bila wewe kuwepo.” Baba yake akanyamaza.

Baba Naya Mjini Mbeya.

Baba Naya alifika mjini Mbeya bado ilikuwa mapema tu. Akachukua pikipiki mpaka kwa Malon. Akamkuta kijana ambaye anaishi hapo na wanafahamiana sana tu kwani naye alikuwepo kipindi akifanya kazi hapo, Mpoki. “Bosi hayupo. Aliondoka na mzigo siku tatu zimepita sasa.” Akamwambia baba Naya. Ndipo akajua walikuwa wakizungumza na Malon akiwa Dar. “Unakumbuka kumsikia Bale akiweka mipango yeyote ya baada yakutoka hapa?” “Bale ana mipango mingi mzee wangu! Halafu mbishi. Ameondoka hapa akiwa amekosana na kila mtu.” “Mpaka wewe!?” “Mimi alikuwa akinidharau na kuniona nimezubaa. Ila usiku alipokuja kuchukua mizigo yake hapa, ali...” Akasita.

          “Naomba nisaidie hata kujua pengine ni wapi hata alitamka anafikiria kwenda. Sio lazima ikawa kwa hakika. Hata kutamka tu.” “Nina shemeji yangu aliyemuoa dada yangu tunayefuatana. Wao wanaishi mjini. Alikuja hapa siku moja, wakati tukizungumza, Bale akanifuata na kuanza kugomba kwamba naongea tu badala ya kufanya kazi. Ndipo shemeji akamwambia alikuwa akinipa dili nzuri itakayonitoa haraka kimaisha. Bale akavutiwa nakutaka kujua nini maana mimi nilikataa.” “Ni biashara gani?” Baba Naya akataka kujua.

          “Shemeji anaingiza nguo kutoka Zambia. Zaidi vitenge. Wanaduka hapo mjini. Sasa akamwambia hiyo biashara inalipa sana, lakini amesikia au sijui kuna mtu  amempa dili nyingine kuwa huwa wanaingiza na kutoa mirungi. Wanaficha kwenye mizigo ya nguo wanapitisha pale mpakani, inalipa sana. Mimi nilikataa. Na Bale ni kama alikataa siku hiyo. Ila usiku alipokuja hapa, aliomba namba ya simu ya shemeji, akasema atamtafuta ili kumuulizia zaidi. Sasa sijui!” “Nashukuru sana, Mpoki. Unaweza kunisaidia namba ya simu ya Bale pamoja na shemeji yako?” “Ya Bale sina. Ila naweza kukupa ya shemeji na ya huyo dada yangu. Ni watu wakarimu sana. Hawana shida.” Baba Naya akachukua namba na kutoka kwa haraka akiwa ameacha mizigo yake yote hapo.

          Akiwa anatembea kwa haraka akirudi mjini Naya akampigia. “Pole baba.” “Asante mama. Ila nawahi kurudi mjini kukutana na mtu ambaye pengine anajua atakapokuwa ameelekea Bale.” “Nakuombea baba yangu. Ila naomba unywe hata maji.” “Mpoki amenipa chai ya rangi hapo, nimekunywa ndipo nimetoka. Kwa hiyo nipo sawa. Hapa natembea kuwahi mjini.” “Pole baba yangu. Nakuombea ufike salama. Nitakupigia tena. Acha niweke sawa haya mambo ya hapa dukani kwako. Nanaa naye kuna kitu alikuwa akinifundisha hapa, ukija nitakwambia na wewe. Naona itakurahisishia.” “Nashukuru mama. Sasa mwenzio umemuacha wapi?” “Nimemuacha kazini, nimekuja huku kwenye duka lako na gari yake. Atanifuata nyumbani akitoka kazini. Alikuwa na mambo mengi leo nikajua nikimsubiria sitaweza kuwahi huku Kibaha na hizi foleni. Tumekubaliana aje nyumbani baadaye. Atamtumia dereva wake na gari ya ofisi kumleta.” “Na Zayoni?” “Nilimkuta hapa. Yupo mzima tu. Naona anasaidia kweli! Wanamsifia.” “Nimemuona jinsi alivyoweka juhudi. Sasa huyo  ndio wakumfundisha, ili aje anifundishe na mimi.” Naya akacheka.

“Naona ameshajua zaidi yangu. Nanaa alikuwa akinielekeza kwa kupitia yeye maana ndiye aliyekuwa akijua vizuri mambo ya hapa kuliko hata mimi. Ni mambo ya bidhaa za hapa, bei na mahesabu yake kwa kutumia kompyuta, ili kwamba hata nikiwa kazini niwe najua ni nini wameuza, nini wameishiwa au kupungua, ili niweze kuagiza kwa haraka. Sasa Zayoni naona bei zote zipo kichwani na kumbe anajua unapoandika vitu vilivyopo stoo! Basi amemrahisishia kweli Nanaa.” “Basi huyo atakufaa. Acha niwahi mama.” Wakaagana, baba Naya akijua akili ya Naya ikitulia, ataweza kuongoza hapo vizuri, hapata haribika jambo. Hilo likampa moyo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          Baba Naya akamkuta dada yake Mpoki na kumwambia mumewe hayupo, amekwenda kusambaza mzigo. “Unajua chochote juu ya Bale?” “Mpoki amenipigia simu muda si mrefu na kuniambia unakuja, wewe ni baba yake Bale. Lakini hata hamfanani!” “Wanafanana na mama yao. Unajua alipo?” “Alikuja nyumbani usiku usiku, akaomba hifadhi, ila kesho yake akaondoka. Baba Tupo, ndiye aliyemsindikiza mpaka kituo cha mabasi akielekea kwa rafiki yake ambaye alikuwa amsubirie, waende huko Zambia. Nimempigia baba Tupo kumuulizia baada ya kuagana na Mpoki, akasema hajawasiliana nao tena. Hajui kinachoendelea huko lakini anasema kijana wako ni mchangamfu, yupo tayari kupambana. Atafanikiwa tu, usiwe na wasiwasi.” Akampa moyo asijue bado hata hajamsogeza karibu na mwanae! Bado kumpata Bale kukawa ni msururu wa watu hapo katikati na bado wote hawana taarifa kamili za Bale.

“Nashukuru mama. Sasa unaweza kunisaidia namba yake ya simu?” “Ya baba Tupo?” “Na ya huyo ambaye Bale aliyekwenda kwake.” “Acha tumuulize baba Tupo, maana si kwamba ni watu wenye mahusiano! Ni mtu tu waliyekutana kwenye biashara. Akampa hilo wazo. Akataka kushawishika hapa ili akafanye na hiyo biashara ya mirungi, lakini mimi nilimkataza kabisa.” Moyo wa baba Naya ukazidi kuumia kila akisikia aina hiyo ya biashara mwanae aliyokimbilia.

          “Watoto wetu wadogo. Akija kukamatwa huko Zambia! Si ndio maisha tena basi! Nimemuonya na kumuapisha asijejaribu. Bora turidhike na kidogo tunachopata.” “Ni kweli mama. Umetumia hekima.” “Acha nimpigie, akurushie namba ya huyo mtu.” “Niombee na yake tafadhali ili nikikwama huko, nipate mtu wa kumuuliza.” Akampa namba ya simu ya mumewe, huyo baba Tupo, kisha akapiga simu na kumpa baba Naya mwenyewe azungumze naye. “Ongea naye tu ili umuulize maswali yote unayotaka.” “Nashukuru mama.” Akapokea simu.

          “Shikamoo mzee wangu.” Akamsalimia kwa heshima. Baba Naya alipoitika akaendelea. “Nimempigia simu jamaa mwenyewe, hapatikaniki. Atakuwa bado yupo Zambia. Yeye anabiashara kubwa kuliko hii yetu. Anasambaza vitenge mpaka mikoani, na hapo ndipo nilipojua siri ya mafanikio yake kuwa kumbe huwa anachanganya na hiyo mirungi. Amesifia sana. Na hata alipozungumza na Bale alimwambia wasizungumze kwa simu, aende hukohuko akajionee kwa macho. Ndipo Bale akaondoka hapa. Sikuwafuatilia tena kwa kuwa wote si watu ninaofahamiana nao kwa karibu. Bale nilikutana naye akiwa anamfoka shemeji, na huyo jamaa nilikutana naye madukani huko Zambia na kugundua kuwa na yeye ni Mtanzania. Ndipo tukapata muda, akanishirikisha siri ya mafanikio yake. Nilipokuja kumwambia mke wangu alinikatalia kabisa na kuniapisha nisiwahi hata kuja kumtafuta tena asije akafanikiwa kunishawishi. Kwa hiyo tokea kijana wako aondoke hapa na kuwa na uhakika wamewasiliana na atampokea, basi sijamtafuta tena mpaka hii leo na sikufanikiwa kumpata.”

          “Unajua anapoishi?” “Sifahamu. Ila nakumbuka aliniambia maduka yake yapo karibu na mpakani mwa Tunduma.” “Kwa hiyo hata Bale alikwenda huko Tunduma?” “Sina uhakika sana. Nilichofanya mimi  ni kumpigia simu. Bale akaomba kuzungumza naye mwenyewe. Wakapanga mpaka aina ya mabasi yakupanda na wapi ashuke. Nikamsindikiza kituo cha mabasi, nikamuacha hapo. Sikujua kilichoendelea. Ila tulipokutana Zambia, katika mazungumzo yetu, nakumbuka kumsikia akisema hivyo.” “Nakushukuru sana. Asante. Nakutumia na namba yangu ili ukiiona inaingia kwenye simu yako, tafadhali pokea. Pengine nitakuwa nikihitaji maelekezo huko.” “Kwamba unakwenda!?” Akauliza kwa mshangao kidogo.

          “Ndiyo. Naona nikaanzie huko Tunduma.” “Kwani huwa hamuwasiliani na kijana wako?” “Hapana. Ndio maana naona nikamtafute ili nijue hali yake.” “Kwa nini usisubiri mpaka jamaa atakapopokea simu?” “Asipopokea? Iweje iwe alikusudia kubadili namba ya simu?” “Kweli.” Akaafikiana naye. “Acha nirudi kwa Mpoki, nilale mpaka kesho na mimi niwahi mabasi ya kwenda Tunduma.” “Basi nitakuja kukuchukua mzee wangu, nikusindikize. Mimi ninao usafiri. Usihangaike usiku wakati vijana wako tupo.” “Nashukuru sana.” Baba Naya akashukuru na kurudisha simu ya mama Tupo, dada yake Mpoki. Akatoka hapo kurudi kwenye makazi ya Malon, alipoacha mizigo yake kwa Mpoki.

Safari Moja Yaanzisha Ingine.

Akiwa njiani akiwaza na kupanga hili na lile na maombi akimsihi Mungu ulinzi kwa Bale huko alipo, akakumbuka jinsi maisha yalivyo ya ajabu. Akakumbuka alipo kwa wakati ule na alikotoka. Akavuta pumzi kwa nguvu akitafakari. Akiwa hana uwezo kama alionao wakati huo alikuwa na familia. Mke na watoto. “Mama Naya!” Akamkumbuka mkewe kwa kuumia sana. Akakumbuka alikopita na mkewe akilalamikia mali mchana na usiku! Sasa Mungu wake ndio amemjibu. Tena huyo Mungu amejibu kwa moto. Akacheka na kutingisha kichwa kwa masikitiko. Hata majirani walishuhudia Mungu alichomtendea kwa jinsi nyumbani kwake tu palivyo badilika. Duka alilonalo mjini Kibaha!  Lakini familia haipo kama mwanzo. Mkewe amefariki mambo yakiwa ndio yanakaribia kubadilika, na Bale kaondoka nyumbani akipishana na mafanikio mlangoni kwao!

Alilokwenda kutafuta huko nje kwa shida na matusi akisimangwa na kuhatarisha maisha yake amepishana navyo mlangoni kwao. Wakati mafanikio ndio yanaingia kwao, yeye ndio anatoka! Baba Naya akaumia sana. Yote aliyokuwa akimuomba Mungu miaka yote akifunga na kuomba, eti ndio anajibiwa wakati huo! Tumaini la pesa limechupua. Baba Naya tayari anayo miradi ya kueleweka tena ya uhakika akiwa ameshikwa mkono na Geb Magesa anayeijua hiyo biashara haswa. Kila alilomshauri limekamilika tena limekamilika kwa kiwango cha juu. Mambo yake yamekaa vizuri. Akazidi kuumia kila akifikiria alichoacha nyumbani kwake lakini watu muhimu kwake wanapungua!

Akakumbuka ahadi za Mungu kwa mwanadamu. “Ibrahimu aliahidiwa uzao mkubwa, akaamini mpaka kuitwa baba wa imani, lakini alikufa bila kuushuhudia huo uzao mkubwa zaidi ya hao watoto wawili tu!” Akawaza baba Naya na kuendelea kukumbuka. “Musa naye alihangaika kuwatoa wana wa Israeli huko Misri ili kuwapeleka mji wa ahadi, lakini yeye mwenyewe hakuingia mji wa ahadi japo Mungu alimuonyesha kwa mbali.” Akazidi kusononeka kila huo ukweli ulipokuwa ukiendelea kufunguka moyoni mwake. “Lazima nimpate Bale. Sitarudi nyumbani mpaka nimpate Bale.” Akaazimia moyoni mwake.

Lakini anakopanga kwenda, hapajui! Naya naye anamuhitaji. Furaha aliyokuwa nayo Naya akiisubiria hiyo ndoa! Baba Naya akavuta pumzi kwa nguvu akitembea. Naya alikuwa akimuhesabia baba yake siku zilizobaki ili aolewe na Joshua. Kila siku akiamka lazima amwambie baba yake siku zilizobaki awe mke wa Joshua. Akamuhurumia endapo chochote kikitokea kwake. “Lakini ni lazima nimpate Bale. Nitajua hukohuko niendapo. Hata kama itanigarimu pumzi yangu ya mwisho. Lazima nimpate Bale.” 

Wasiwasi ukaanza kumuingia kila alipokumbuka umbali mwanadamu anaoweza kwenda akitaka jambo lake. Akamfikiria vile Bale alivyoanza akiwa na haraka ya kufanikiwa, akajua wanaweza kumtumia vyovyote ili kujinufaisha na kijana wake. “Mungu wangu turehemu. Najua nimekosa sana na sistahili hata rehema zako, lakini Mungu wangu, nakusihi nirehemu tena. Nitazame mimi na wanangu tena, tena kwa upya.” Baba Naya akamsihi Mungu kwa hofu akitembea kurudi kwenye makazi ya Malon. Hakutaka hata kuchukua usafiri umrudishe.

Mawazo yakamrudisha na kwa Zayoni. Akamuhurumia ambavyo alivyo mdogo. Bado anaomboleza msiba wa mama yake. Bado baba Naya hakuwa akijua atakachokabaliana nacho huko mbeleni. Hakujua huyo mwenyeji wa Bale ni mtu wa namna gani kwa hakika. Ila kwa kusikia kwamba ni mfanyabiashara mkubwa na mzoefu wa biashara haramu, akajua hatakubali kuangamia kirahisi endapo kama amemuingiza kijana wake kwenye matatizo au kama yeye ndiye anayenufaika na kijana wake. “Umbali gani atakwenda kuficha maovu yake?” Akajiuliza. “Lakini lazima nikamkabili kwa namna yeyote ile. Liwalo na liwe, nitajua mbele ya safari.”

Nani wa kumuachia mji wake ambao kwa muda mfupi sana umebadilika haswa! Jengo jipya na zuri lipo nyuma ya nyumba yao ya kawaida tu. Kulitengenezewa uzio mzuri kama alivyoshauri Geb kuepusha wezi kuweza kuingia hapo galani kiurahisi. Geb alishauri hata aridhi ya kutembelea hapo isibakie mchanga tu. Ifunikwe na vitofali na kutengenezwe mifereji maalumu kuelekeza maji ya mvua sehemu ingine yasije kuja kuingia galani. Yote hayo yalifanyika kwa muda mfupi bila kutarajia. Ikawa kama alivyotamka Mungu na mambo kutokea hapohapo! Kama mama Naya angefufuka na kurudishwa nyumbani kwake, asingeamini. Kuanzia getini mpaka kuzunguka nyumba, kukawa kumepangiliwa kwa ustadi mpaka njia maalumu pembeni ya hiyo nyumba, nzuri maalumu kwa malori kuingia kwa urahisi kushusha mazao galani, na majunia ya mkaa sehemu yake. Akacheka baada ya kukumbuka nguvu ya pesa.

Wewe ni Mungu, na zaidi yako hakuna mwingine.” Akajikuta akiutambua mkono wa Mungu akimshangaa pale anapoamua kutenda jambo lake. Hata gari ya Naya aliyopewa na Joshua iliweza kuhifadhiwa hapo nyumbani kwao kwa sababu ya mazingira mazuri na ulinzi mzuri. Kila alichoshauri Geb, alihakikisha kinafanyika tena kwa kusimamia yeye mwenyewe na mafundi wake. Kwa vipimo sahihi alivyotaka Geb  mpaka akatoa kitu kizuri sana tena chathamani! Pesa yote aliyokuwa akiwekeza hapo alikuwa akiwaandikia kisha kumkabidhi baba Naya mwenyewe na Joshua, kwa makubaliano atakuwa akimkata tararibu kwenye biashara watakayokuwa wakifanya pamoja. Ikawa unafuu sana kwa baba Naya. Hakuanza kwa aibu ya kukopakopa wakwe bila ujasiri wa kurudisha au kupewa bure. Ilikuwa kwenye mkataba wao wa biashara. Kumlipa Geb kwa kadiri watakavyoendelea. Hapo napo Geb akawa amewekeza kupitia baba Naya. Ameongeza soko la uhakika na ni kama ametunza pesa yake.

Akajikuta akimshukuru mkewe kwa kusaidia kulipia hilo eneo ambalo limekuja kuwa msaada mkubwa sana. Akajua na yeye anajukumu la kuwaacha wanae sehemu nzuri na kuendelea hapo alipowaacha endapo hatakuwepo, sio kuwaacha hapo na kujikuta wanarudi chini kabisa.

Akafikiria nani wakumuachia majukumu yake. Baba Naya akajaribu kuwatafakari ndugu zake mmoja hadi mwingine, wakajua wote watasumbua sana watoto wake. Akajua hawatashindwa kuwapokonya mali zote endapo ataacha chini ya usimamizi wao. Ndugu wa mkewe ndio kabisa. Kwanza hawakuwa wakimpenda baba Naya kwani wote hawakutaka ndugu yao aolewe naye. Walimpinga sana, lakini mwishoe mama Naya akaolewa tu. Na kadiri mambo yalivyokuwa yakiwaendea vibaya, hawakuacha kumkubusha na kumwambia, ‘Tulikwambia sisi!’ Akaona hao sio wakuwagusa kabisa. Na baada ya kumzika mkewe, wote walitaka vitu vya dada yao kana kwamba hakuwa na watoto. Na pia kudai pesa zaidi, wakisema wanataka akiba yake yote na watakayolipwa serikalini kwa ajili ya ndugu yao pia wapewe. Ukatokea ugomvi hata kati yao wenyewe lakini mwishoe baba Naya akakubaliana nao, nakuwapa alivyoweza. Akabaki akitafakari akimtafuta mtu sahihi wakumuachia maagizo/wosia endapo chochote kitamtokea huko anakokwenda kumsaka mwanae, na asirudi.

Baba Naya kwa Joshua.

Akajikuta anampigia simu Joshua. Akapokea kwa haraka sana. “Samahani kwa usumbufu Joshua.” “Bila shaka mzee wangu. Vipi huko?” “Ndio nimepiga angalau nikupe maendeleo ya huku.” Hilo likamfurahisha sana Joshua kuona amekumbukwa na kuthaminiwa. Baba Naya akamueleza yote bila kumficha. “Kesho nitaelekea Tunduma, nikaanze kumsaka. Nimepewa jina moja tu la huyo mwenyeji wake huko, inavyoonekana ni mtu mashuhuri huko. Naamini nitampata tu ili anisaidie kunisogeza kwa Bale. Lakini Joshua?” “Nakusikiliza mzee wangu.” “Kuna kitu hakipo sawa. Nakwambia haya ili kukuomba unisaidie kuwa karibu na huyo mama mzazi pamoja na mdogo wake. Sitarudi mpaka nimpate Bale. Ambayo sijui ni lini na nini kitatokea huko. Lakini nimekusudia kupambana kufa na kupona, mpaka nimpate Bale.” “Tunakuombea kila kitu kiende sawa.” Joshua akajaribu kumtia moyo asielewe undani wa hiyo simu ya baba Naya.

“Nashukuru lakini kufa kwangu mimi ni faida. Sitapoteza. Hilo siogopi, ila nafikiria wanangu.” Hapo Joshua akaongeza umakini akiwa ameshituka kidogo. Baba Naya akaendelea. “Sina ndugu wakaribu wa kunisaidia kwa umbali mrefu kusema chochote kikitokea kwangu, wanaweza kusimama na watoto wangu. Nimeona alipougua mke wangu mpaka kifo chake. Tulipata ushirikiano mdogo sana kutoka kwa ndugu. Sasa kila nikiwawaza wanangu endapo mimi sipo, zaidi Zayoni, nawahurumia sana.” “Naomba usiwe na wasiwasi mzee wangu. Kila kitu kitaenda sawa.” “Naelewa kabisa Joshua. Hata kuondoka kwangu hapa duniani ni kwenda sawa. Mama Naya hajapoteza hata kidogo. Tuliobaki ndio tumepoteza. Inaweza ikawa hivyohivyo na kwangu. Mimi nisipoteze ila wanangu. Naomba nisikilize tu tafadhali.” “Sawasawa.” Hapo Joshua akajua amepigiwa kuachiwa wosia. Akatulia kabisa akimfikiria Naya.

Mungu saidia chochote kisitokee.” Akajikuta na yeye akiomba baada ya kufikiria endapo huyo baba akifa huko. Akajua ndio atampoteza na Naya kabisa. “Zayoni ni muoga sana. Asubuhi leo alipoamka na kujikuta peke yake na hata mlinzi hayupo, alinipigia simu akilia sana.” “Mlinzi alikwenda wapi tena!?” Joshua akauliza akionyesha kujali na kushangazwa kwani hata yeye aliyajua makubaliano kati ya baba Naya na hiyo kampuni ndogo ya ulinzi inayolinda nyumbani kwake. “Nafikiri aliondoka kabla ya mwenzie wakulinda kutwa hajaja kumpokea. Sasa hiyo imemuogopesha sana Zayoni, ilimbidi aondoke hapo aende kukaa na mlinzi wa kwenye duka la Kibaha.” “Nitakwenda kuzungumza na walinzi leo. Hivi  hapa  ndio nakwenda kuwaona. Nilikuwa na vikao mpaka mida hii. Naya aliondoka na gari yangu kwa kuwa asubuhi unakumbuka mimi ndiye niliyekuja kuwachukua?” “Ameniambia nilipozungumza naye jioni hii.” “Basi nipo njiani. Nitakwenda kuliweka hilo sawa kuhakikisha mlinzi wa usiku hatoki mpaka wa kutwa awe amefika.” Joshua akamuhakikishia.

“Nitashukuru sana. Na huyo wa usiku zungumza naye juu ya gari ya Naya. Huwa nikiwepo mwenyewe nazunguka usiku mpaka kule kwenye ghala. Na mara zote anakuwa amelala. Sasa mwambie sipo, lazima aongeze umakini.” Baba Naya akaendelea. “Zayoni hayupo kama watoto au vijana wengine wanavyotakiwa wawe. Nalo hilo ni moja ya makosa niliyoyafanya kwenye malezi yao hao. Alikuwa karibu sana na mama yake. Yaani sasa hivi ndio kama anawekwa kwenye ulimwengu mgeni sana kwake. Yupo kwenye kujifunza maisha kama mtoto mchanga. Alibebwa na mama yake akimfanyia kila kitu mpaka kumsaidia kufikiria. Itachukua muda, lakini namuona yupo tayari kujifunza. Ila kwa sasa tafadhali usimsahau. Ataharibikiwa kabisa akijikuta yupo kwenye huu ulimwengu peke yake, akitakiwa kufanya maamuzi na kuchukua hatua yeyote ile akiwa peke yake.” “Nitahakikisha yupo salama. Nimeweza kumsoma, uzuri yupo tayari kujifunza.” “Nashukuru sana.” Akaendelea.

“Tafadhali swala la ulinzi hapo usisahau Joshua. Panaonekana pako shamba kidogo lakini si salama. Nimeacha mwanangu hapo, wasije kuwaingilia usiku endapo wakijua mwenyewe sipo.” Joshua akajua anayezungumziwa hapo ni Naya tu. “Nitaweka msisitizo mzee wangu. Hilo usiwe na wasiwasi nalo kabisa. Nitahakikisha leo hilo linakaa vizuri.” Hapo napo Joshua akaahidi.

“Nashukuru. Kingine na cha mwisho. Najua nilikuapisha juu ya Naya. Naomba niongeze ombi hapo.” “Karibu.” Joshua alikuwa akiendeshwa na gari ya kazini kwao akipelekwa Kiluvya kwa kina Naya na si nyumbani kwake. “Naya ni mtoto niliyelea mimi mwenyewe kuanzia ni mdogo sana. Aliugua sana wakati yupo mdogo mpaka tulifikiri pengine tungempoteza. Akiwa kwenye hiyo hali mama yake akashika mimba ya Bale iliyokuwa na yenyewe akimsumbua sana mama Naya. Kutwa yupo hospitalini kwa hili au lile juu ya huo ujauzito. Kwa kuwa kulikuwa hakuna matumaini ya kuishi kwa Naya, mama yake akaweka tumaini kwenye mtoto aliyekuwa amebeba, hiyo mimba, ambaye ndio Bale, wakati akijiuguza, mimi nikihangaika na Naya.” Akaendelea.

“Katika miujiza ambayo imenifanya nibakiwe na Mungu, hata kama mazingira na watu wakinikatisha tamaa, ni Naya. Ipo siku aliugua. Akabanwa akawa anashindwa kuhema kabisa. Ilikuwa ni usiku, mama yake ndio amejifungua Bale. Nilikimbia na Naya hospitalini, wakati tupo mapokezi nikisubiria ahudumiwe, akaacha kuhema kabisa, mwili wake ukaanza kupatwa baridi kama aliyekufa. Bado nilikuwa nimempakata tu, na hakuna aliyenipa hata huduma ya kwanza. Nilijua wazi amekufa na ndivyo hata mama yake alijua tusingefika mbali kwa ile hali aliyoipata usiku ule. Nikajua wangemchukua mtoto wangu na kwenda kumtupa chumba cha maiti kwa haraka, wakati walishindwa kumuhudumia kabisa.” Joshua kimya akisikiliza.

“Nilitoka naye pale mapokezi, nikaenda kukaa naye nje, nikiwa nimempakata tu. Ila nilijiwa  na uchungu wa ajabu sana. Sikuwahi kuomba maishani kama ule usiku nikiwa peke yangu. Pengine niliomba kama nilivyomuombea mama yao kipindi hiki mgonjwa mpaka akafariki. Niliomba Joshua, mpaka nikaanza kusikia mwili wa Naya unaanza kupatwa joto.” “Waw!” Joshua akashangaa akisikia mwili kusisimkwa.

“Kufupisha habari, kuanzia siku hiyo ndipo nilipogundua Mungu yupo, ila yeye ndiye atendaye wala si mwadamu. Ikaniongezea ujasiri wa kuombea watu hata nikiwakuta na hali mbaya ya namna gani huwa siogopi kuomba kwa kuwa nilishakutana na Mungu aliyenitendea. Naya ni muujiza wangu ambao nashindwa kuutangaza kwa wengine kwa kuwa hakuna aliyeshuhudia usiku ule nikiwa nimempoteza na kurudishiwa. Natamani wangempima kisha akaonekana alikufa na Mungu kumrudisha, lakini Mungu alinitendea mimi tu, nikatambua nguvu na uweza wake, basi.” Joshua akabaki akimshangaa Mungu.

“Naya huyo amekua mikononi mwangu si kwa mama yake, kwa sababu ya kupishana kidogo tu na Bale. Mama yake alikuwa karibu sana na Bale tokea anazaliwa, nikaona Naya anakua kama mtoto ambaye hatukuwa tumejiandaa kuleta mdogo wake, ndipo ikabidi sasa mimi kuongeza umakini kwa Naya asijisikie mtoto wa nje ya familia. Kama aliyesahauliwa au haiitajiki. Wakakua pamoja na wote nikiwatizama tabia zao.” Akaendelea. 

“Katika watoto wangu wote, ni Bale peke yake ndiye mwenye uwezo mkubwa sana wa kuthubutu mambo magumu hata kama wote wakimpinga. Hilo nililiona tokea mdogo. Anayo karama na kipaji kikubwa sana ambacho Mungu alimjalia, na shetani amejua hilo ndio anataka kumtumia vibaya. Lakini Naya hakuumbwa hivyo hata kidogo. Bila mtu kumshika mkono, hana uwezo wa kwenda mbali na ndio maana unaniona nipo naye karibu sana.”

“Popote unaweza kumuweka Bale, akaweza kujiongoza na kuishi lakini si Naya. Naya akikuamini wewe, basi unaweza kumfanya mateka wako kirahisi sana. Ukimuongoza vizuri, na kumtia moyo, ujue atafuata na kufanya vizuri sana. Lakini mtu huyohuyo akatokea kumyumbisha kwa maneno au kwa matendo kidogo sana, anarudi chini kabisa na kupoteza dira. Hiyo ndio siri na udhaifu wa Naya. Yupo hapo alipo kwa kusimama naye kwa maombi haswa maana alikubali kujiingiza kwenye mahusiano ambayo hayakuwa na msimamo. Kwa hiyo kila yalipoyumba, basi na yeye aliyumba.”

“Hili lililompata Bale, ingekuwa ni Naya, angesharudi nyumbani kwa haraka sana na angekuwa amepoteza dira kabisa, sio kama hivi Bale alivyokusudia kuendelea kupambana mpaka kufikia lengo. Nilipogundua huo udhaifu wa Naya, ilinibidi mimi nivae sura ya umama ili kumfikisha hapo alipo. Hana kimbilio ila mimi, na sasa hivi afadhali namuona ameweza kuegemea kwako. Ndio maana kauli ya kwamba, ‘sitaolewa mpaka wewe uwepo,’ zipo nyingi sana kwake na ametoka kunitumia tena ujumbe kama huo, sasa hivi.” “Kweli!?” Joshua akashangaa.

“Kabisa. Na usifikiri anatania! Kwa kuwa kwake kuingia kwenye hiyo ndoa, anajua nitaingia naye huko. Kwamba ugumu wowote atakaokumbana nao huko, anajua nitakuwepo naye. Kwa hiyo hicho anachokisema ni zaidi ya maneno tu. Anamaanisha kabisa. Haamini kama anaweza kukaa huko sawa bila mimi kuwepo. Chochote kikitokea kwangu ujue atachanganyikiwa na kuharibikiwa kabisaa. Na akiharibikiwa Naya ujue na Zayoni hivyohivyo. Zayoni hayupo kama Naya, japo kwa haraka haraka unaweza fikiri wanafanana. Zayoni yeye anatakiwa kujua maisha tu kwa uhalisia, basi. Anaweza kuishi kwenye mazingira yeyote lakini anaweza asimfikie Bale, ila haitaji sana kushikwa mkono kama Naya ambaye Zayoni anamtizama kama mama wa pili.”

“Ninachotaka kukuomba ni hiki. Japokuwa kiapo chetu kiliishia ni umrudishe Naya nyumbani pindi mkishindwa,...” “Haitatokea mzee wangu. Nilikuahidi na ninaahidi tena.” “Hapana Joshua. Naomba unisikilize tu. Hakuna anayeingia kwenye ndoa akiwa anategemea talaka. Talaka ni moja ya ajali mbaya sana za ndoa. Wengi huwa hawapangi. Lakini huwa zinatokea. Ikitokea kwenu, kwa kuwa mimi nimekusoma na nimekuona si myumbishwaji. Unao msimamo wako. Unaaminika kwenye maeneo mengi niliyokufahamu mimi, basi usiache kuwa karibu na Naya. Mahusiano hayo ya kimapenzi yakiisha, ubaki undugu kati yenu. Simama naye ili asiyumbe tena.”

“Kama si kuzembea kwetu sisi wenyewe kwenye maeneo fulanifulani na kumsababisha Naya kujiingiza kwenye aina hiyo aliyojiingiza kwenye mahusino yanayotugarimu mpaka sasa, nina uhakika Naya angekuwa mbali sana. Kumekuwa na kuyumbishwa yumbishwa sana ndio maana unamuona ni kama yupo anaanza. Lakini anao utajiri mkubwa sana ndani yake. Lakini kama binadamu wengine wote, akawa nahuo udhaifu. Hapo ulipomfikisha na kumfanya anaweza kufikiria na kutenda, tafadhali pasiyumbe tena. Simama naye tu. Anakupenda na anakuheshimu wewe. Hata akiwa amekasirika najua atakusikiliza tu.” Akaendelea.

“Nimehangaika sana kwa  maombi na juhudi kufika hapo mliponisaidia wewe na mwenzio kufika. Naomba wanangu wasije kuanza tena chini. Naomba simama kama kaka yao. Hayo mengine Mungu akijalia, basi tutashukuru. Ni hilo tu. Nimeona nikwambia kwa kifupi ili uelewe na nisiwaache wanangu bila muelekeo endapo chochote kitatokea kwangu.” Baba Naya akahitimisha.

Japokuwa naamini utakuwepo. Na Mungu atakurudisha kwetu salama. Naamini utaona utuuzima wangu na Naya. Nakuahidi sitamuacha Naya, hata iweje. Kwanza nahisi mimi ndio namuhitaji sana Naya kuliko anavyonihitaji mimi. Halafu, kwa kuwa nimepata baraka zako, basi na mimi nakuahidi kusimama nao kama kaka kwelikweli. Naona ni bahati mzee wangu. Sikujaliwa familia, naona Mungu ameamua kunikabidhi nikiwa na umri huu, akijua nipo tayari na ninaweza. Basi naamini Mungu atanisaidia.” “Nashukuru Joshua. Basi acha nikuage kwa sasa. Mtanipigia mkiwa pamoja. Na kama kuna maswali wewe nipigie tu, nitapokea. Na kama sitapokea basi nitarudisha simu yako.” “Bila shaka.” Hapo baba Naya akapata amani kabisa. Akili ikahamia kwa Bale.

Baba Naya, Tunduma.

Alifika mida hiyo akiwa amekusudia kutafuta nyumba za kulala wageni ndipo aanze kumtafuta huyo mtu aliyepewa jina moja tu la Mbabe. Aliposhuka tu akatafuta taksii na kuomba impeleke kwenye nyumba za kulala wageni. Aliyemchukua kwenye gari yake akawa mcheshi kwelikweli mpaka akamfanya baba Naya amuulize. “Unamfahamu Mbabe?” “Sana tu. Mpaka kwake napafahamu. Walimuweka ndani huko mpakani, ametolewa kwa dhamana. Anajuana na wengi yule! Akiwa ndani, wengi watakufa njaa. Macho ya wengi yanamwangalia. Kwa kifupi Mbabe ni ulaji wa wengi wenye vyeo na mamlaka. Huwezi kumgusa yule! Yaani waliposikia amekamatwa mpakani, bila kuomba msaada unaambiwa watu wenyewe wakaenda kumtoa!” Akaongea kishabiki bila kufikiria anazungumza na nani.

 “Walimuweka ndani kwa kosa gani?” Hilo swali likamfanya mpaka dereva amgeukie. “Vipi?” Baba Naya akamuuliza. “Kwani wewe nani?” Akamuuliza kwa wasiwasi kidogo na kumfanya baba Naya afikirie kwa haraka ili asije haribu. “Kwa nini unamuulizia Mbabe halafu kumbe humjui yeye mwenyewe wala habari zake!?” “Nimepewa namba yake tokea mbali. Nina shida ambayo nimeambiwa ni yeye tu ndiye anayeweza kunisaidia.” “Kwa hiyo nikupeleke kwake moja kwa moja?” “Hapana. Nipeleke kwanza hotelini kisha nitamtafuta kuanzia hapo.” Akashangaa yule dereva ananyamaza kabisa hata uchangamfu ukamuisha. Baba Naya akamtizama. “Vipi bwana?” “Mimi sitaki kupelelezwa. Ni hilo tu.” Akanyamaza na kumshangaza baba Naya. Naye akanyamaza. Akamfikisha hotelini, akamuacha nje kabisa kama anayemkimbia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baba Naya akachukua chumba na kuingia ndani baada ya kuandikisha jina lake. Giza lilikuwa limeshaingia. Akaonelea ampigie simu Naya kisha Joshua ili kuwataarifu kama amefika salama. “Nipo na Joshua hapa. Naweza kuweka spika.” “Afadhali. Itarahisisha.” Akakubali baba Naya. “Pole na safari.” Akamsikia Joshua. “Asante lakini ilikuwa safari nzuri na huyo mtu, ni kweli anafahamika. Dereva taksii aliyenibeba alionekana kumfahamu vizuri ila ni kama mtu anayeogopewa sana hapa kwenye huu mji. Na kuna kitu ambacho aliniambia kimenitia wasiwasi.” “Ni nini baba?” “Alisema kuwa alikuwa amekamatwa. Akawekwa jela, ila ametoka kwa dhamana. Nilipomuuliza alifungwa kwa kosa gani, akabadilika kabisa. Ni kama mtu aliyeingiwa hofu!” “Isijekuwa ni mtu hatari baba!” Naya akatahadharisha.

“Inavyoonekana ni hatari. Lakini yeye ndio mwenye jibu la mtoto wangu! Siwezi nikaishia njiani. Hata kama analindwa na askari wote wa huu mji, lazima nikutane naye tu, anipe majibu yakueleweka.” “Mimi naomba kuwa mwangalifu baba Naya. Mwenzio bado nakuhitaji. Maisha yang..” “Naomba utulie Naya. Tumeomba, amini kila kitu kitakuwa sawa.” “Hapana Joshua. Mama tulimuombea sana, lakini akatuacha. Mungu hapotezi ila sisi ndio tunapoteza. Mimi naomba uwe makini baba Naya. Tafadhali sana. Ujue umebaki peke yako kwenye maisha yetu. Hatuna kimbilio. Umeona ndugu zenu jinsi walivyo! Naomba uhakikishe unarudi nyumbani.” “Naya!”

“Naogopa Joshua. Naogopa sana. Zimebaki siku 5 tu, tufunge ndoa. Mimi bila baba sitawezaUnafanya kitu kizuri sana na mimi nakuunga mkono baba. Lakini naomba usiyatupilie maisha yako kabisa. Ukiona kumekuwa kugumu na hatari, rudi tuanze kutafuta ushauri kwa wataalamu wa mambo ya sheria, watushauri pakuanzia kuliko kuwa tu huko ukihatarisha maisha yako huku hujui kama Bale ni kweli kwa hakika yupo matatizoni au amechagua kuendeleza maisha yake bila sisi. Halafu ikatugarimu maisha ya baba wakati mwenzetu yeye kumbe hana anachopoteza! Hapana baba. Mimi na Zayoni tunakuhitaji. Kama yeye Bale hatutaki sisi tu..” “Naomba tulia Naya, mama. Ndio nimefika tu.” Baba yake akamtuliza.

“Acha niulize kwa amani tu. Nikiona ipo hatari, basi nitarudi tuanze upya kiutaalamu nikiwa nina angalau taarifa za kuwapa chombo cha usalama, wajue pakuanzia. Nitakuwa mwangalifu. Na nikiona mambo yanachukua muda mrefu na hayana sura ya kueleweka, pia nitarudi kuomba msaada wa kisheria. Sitaki muahirishe harusi yenu kwa ajili ya hili.” “Hapo sawa.” Naya akaitika. Hapana Naya. Umejibu bila kufikiria na kuelewa ni nini nimekwambia.” Naya akatulia kidogo na kufikiria.

“Nimekwambia sitaki uharishe harusi yenu. Tarehe hiyo iliyopangwa, tuliomba kwa Mungu na imepata kibali.” “Sijaelewa.” Hapo Naya akakaa sawa. “Kwamba unasema nifunge harusi aidha wewe upo au haupo?!” Naya akauliza kwa mshangao kana kwamba anahisi hajamuelewa vizuri baba yake. “Unanisikia Joshua?” Baba Naya akamuuliza na Joshua akiashiria Naya ameelewa. “Nakusikiliza mzee wangu.” Joshua akaitika. “Shetani ni mvurugaji, na hajawahi kupenda ndoa tokea kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu. Alipoona Adamu na Hawa wanaamani na mipango yao inaendelea vizuri pale bustanini na Mungu yupo katikati yao, akaingia kwa hila katikati yao. Akaanza kwa kumvuruga Hawa akijua mbegu yake ya uharibifu haitaishia kwa wao wawili tu ni mpaka kwa watoto wao. Nafikiri mnakumbuka kilichotokea kwao na mpaka watoto wao kuja kuharibikiwa mpaka kaka mtu kumuua mdogo wake.” “Mimi nakumbuka.” Joshua akaitika Naya alishaanza kulia.

“Ukimpa nafasi shetani kidogo tu, hana mipaka. Ataingia na kuwavuruga mno. Lazima kazi zake tuzidhibiti na tuzikomeshe kwa maneno na vitendo. Unanisikia Naya?” Kimya. “Safari hii hutaanza, hutasita njiani wala hutayumbishwa hata na mimi. Mnazo baraka zangu tayari. Tumefunga tukimuomba Mungu sisi wote na kina Magesa. Tukaikabidhi siku hiyo mbele ya Mungu. Mungu ameikubali na mambo yote yapo sawa, sasa hakuna kurudi nyuma. Unanisikia Naya?” “Naamini utarudi mapema baba. Hakika Mungu aingilie kati jamani! Haitakuwa sawa kwangu. Mama asiwepo na wewe pia baba jamani! Sidhani kama Joshua atajali kuahirisha kwa siku chache tukusubirie.” “Hapana Naya. Unakumbuka ni kwa muda gani umekuwa ukisubiri hiyo siku?” “Muda mrefu baba.” Naya akajibu akilia sana.

“Basi nataka usiahirishe. Jua nipo na wewe kwa maombi. Kabla, wakati na baada ya hiyo harusi yako. Shetani ni kama simba aungurumae. Anazunguka zunguka akitafuta mtu wakumrarua. Hila zake ni dhahiri kabisa. Anayo mitego kila iitwayo leo. Hasinzii wala halali. Huwezi jua tukiahirisha kwa hili, kesho atarudi kwa lipi! Unanielewa Naya?” Naya akaendelea kulia.

“Na kuliko kuendelea kukwama kwenye hili, ukilia usiku kuchwa, nakuomba ukumbuke kwenda kushugulikia maswala ya shule ya mtoto. Hataki kukaa bweni, lakini kwa muhula wa kwanza lazima aende wakati tukijipanga upya. Nimezungumza naye sana tu.” “Hataki baba. Mimi nikiongea naye anaishia kulia. Asijeona tunamtupa sababu mama hayupo! Naomba tumuache tu, baba. Mimi nitakuwa naye na nitajua chakufanya shule zikifungua. Asije akafeli akiwa huko shuleni ikawa haina maana tena ya yeye kuwepo shuleni. Nilimuahidi mama, nitakuwa naye tu. Usiwe na wasiwasi.” Naya aliongea akijaribu kumtuliza baba yake lakini na machozi mengi yakitoka kama mvua.

“Hapo utakuwa umefanya vizuri. Lazima Zayoni asome. Asiishie kwenye biashara kabla ya kupata shahada hata moja. Mama yake amesisitiza hilo. Ametaka asome.” “Atasoma mzee wangu. Na mimi nitahakikisha anasoma. Usiwe na wasiwasi. Sisi tunakuombea huko mambo yaende vizuri, na urudi salama.” “Nashukuru Joshua. Acha nikapate muda wa maombi, kisha nipumzike. Nianze siku ya kesho nikiwa nina mawazo yaliyotulia.” “Usiku mwema.” Joshua akaaga.

“Naya mama mzazi?” “Mimi nipo baba, nitakupigia wakati nalala.” “Naomba upunguze wasiwasi. Na muamini Mungu kila kitu kitaenda sawa.” “Nitakupigia baba. Naomba usiache kupokea, lasivyo nitakuwa na wasiwasi.” “Basi sitalala mpaka nikusikie.” “Hapo sawa.” “Si na asubuhi tena ni hivyohivyo?” Naya akacheka akifuata machozi. “Mimi sitanii bwana!” “Mbona hilo nalijua mama! Asubuhi nayo nihakikishe napokea simu bila yakuchelewa.” “Hapo sawa.”  Kidogo wakacheka.

“Naomba kabla hatujaagana mzee wangu, naomba uende mapokezi. Omba jina kamili la hiyo hoteli, namba zake za simu na huyo muhudumu aliyekuwepo hapo sasa hivi.” Joshua akafanya wote watulie. “Ni kwa nia nzuri tu. Sijui kwa nini nimejisikia hivyo. Ila naona si wazo baya na sisi tujue ulipo. Naomba tusikate simu. Uliza halafu Naya atakuwa akiandika. Ikiwezekana omba mpaka kuona kitambulisho chake. Tusirudie kosa tulilofanya kwa Bale. Aliondoka, hakuna aliyefuatilia alipo na kwa nini hakuwa akipokea simu zetu. Ilitupasa kufanya kama hichi unachokifanya mzee wangu sasa hivi. Sasa hivi tunalipa garama ambayo tungeweza kuepuka kabisa.” Joshua akafanya wote wajifikirie. Baba Naya akatoka hapo chumbani kwake na kwenda mapokezi bila kubisha.

Wakamsikia muhudumu ni kama anakataa kutoa kitambulisho chake baada ya baba Naya kuomba. Lakini Naya akamwambia baba yake basi ampe namba ya hapo na jina la hapo. Kisha apige simu akiwa hapohapo na ahakikishe anapokea kujiridhisha hajampa namba za simu za uongo na baba yake apige picha kitabu cha wageni kwa nje na ndani aliposainisha yeye baba Naya. Baada ya ubishi wa muda mrefu kidogo, wakafanikiwa bila kitambulisho cha huyo muhudumu wa zamu. Naya akaandika. Na baba Naya akawatumia hizo picha alizopiga za hicho kitabu na akatoka nje kabisa, akapiga picha na hilo  jengo na kuwatumia. 

“Jambo la mwisho kabisa. Ila usione ni usumbufu mzee wangu.” “Bila shida.” Baba Naya akaafiki kwa haraka. “Kwenye simu yako naomba nenda kwenye Settings, kisha bonyeza Location, ili kuweka On. Hiyo itatusaidia kujua popote ulipo.” Mpaka Naya akashangaa.

Kimya kidogo. “Umefanikiwa baba? Au unataka arudie?” Naya akamuuliza. “Au mtumie hayo maelekezo kwa ujumbe na afanye sasa hivi kabla hatujakata simu.” “Nimeshafanikiwa. Si kinachotakiwa ni pale ndani ya Location kwenye On kuwe na rangi ya bluu?” “Ewaaa! Hapo sawasawa kabisa.” Hapo Joshua akaridhika ndipo wakaagana.

Naya Kwa Joshua.

Naya akamgeukia Joshua. “Kwani wewe utakubali kufunga ndoa bila baba Naya?” “Unataka jibu la ukweli au la uongo?” “Nataka jibu la kwamba tutafunga ndoa baba Naya akiwepo.” “Sawa. Tutasubiri. Ila na yeye  ameongea kitu cha msingi sana na ukweli mgumu pia. Sasa na mimi nataka kujua Naya. Utakuwa tayari kusubiri mpaka lini? Je, ikatokea baba harudi pengine mpaka mwezi, hajampata Bale, na yeye amesema nilazima ampate Bale.” “Siku zikikaribia bado hajampata, nitamkatia tiketi ya ndege. Aje awepo kwenye harusi yangu kisha arudi kuendelea kumtafuta Bale.” “Unakimbia kunijibu swali langu Naya, na wewe unajua.” “Wewe usiwe na wasiwasi, tutafunga ndoa yetu  siku tuliyopanga.” “Sawa.” “Na baba Naya akiwepo.” Naya akaongeza. Joshua akamwangalia na kunyamaza. 

Hakuna Msiba Usiokuwa na Mwenzie.

Usiku alipoondoka tu Joshua baada ya kula pamoja hapo nyumbani kwao, na kuhakikisha kila kitu kipo sawa, akazungumza na walinzi ndipo akaondoka, Naya akakimbilia kumpigia simu baba yake. “Baba Naya?” “Nipo mama. Umenikuta nimepiga magoti, ndio namalizia kuomba.” “Basi omba na mimi baba. Nimeingiwa hofu, sina amani!” “Sababu ya wasiwasi wakufikiri sitakuwepo kwenye harusi yako?” “Kumbuka tulivyoomba pamoja baba! Kweli usishuhudie? Hakika omba na mimi baba. Umpate Bale akiwa salama ila tu anahangaika kutafuta pesa, wewe urudi salama. Mwambie Mungu asinijaribu kupita uwezo wangu. Hakuna mlango utanitoa hapo nikatoka salama.” “Naomba tulia tuombe. Na wewe mwambie Mungu wako hayo uliyoniambia sasa hivi. Ila sio kwa kilio hivyo na kumtisha Mungu. Wewe msihi. Mungu anatuwazia mema.” “Na mimi nimepiga magoti.” Baba Naya akaanza.

Kabla hajafika mbali Naya akiwa anamsikiliza baba yake akiomba, akasikia kishindo kama mtu anamgongea kwa nguvu. Wakatulia. “Ni nini baba?” “Kama wananivunjia mlango wangu!” Naya akashituka sana. “Piga kelele baba. Piga kelele kwa sauti ya juu.” Naya akaanza yeye kupiga kelele. Akasikia mshindo unaongezeka. “Ni kina nani nyinyi na kwa nini mnavunja mlango wangu, badala ya kugonga tu taratibu?” Naya akamsikia baba yake akiuliza kwa sauti ya juu akishindana na ile kelele.

 Mwishoe akasikia mshindo mkubwa, mlango ukijigonga ukutani kama uliokwisha vunjwa, baba Naya akasikika akipiga kelele kidogo, mshindo mzito. Kimya. Hakumsikia tena baba yake. “Mbembeni, ameshazimia huyo.” Naya akafunga mdomo kwa nguvu ili aweze kusikia yeye asisikike kule kwenye simu ya baba yake. Kwa mbali akasikia vishindo. Kisha kimya. Alishituka Naya, akabaki amepiga magoti akitetemeka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Zayoni akaingia. “Kuna nini Naya!? Umepiga kelele kwa sauti mlinzi amekuja kunigongea!” “Wamemchukua baba kutoka hotelini. Wamemteka nyara. Nimesikia Zayoni, nilikuwa nikiomba na baba.” “Mimi naogopa Naya.” Hapohapo Naya akampigia Joshua. “Vipi, nilijua upo na baba!?” Joshua akapokea na kuuliza swali. “Wamemchukua Joshua. Wamemvunjia mlango wakati tunaomba naye. Wakampiga nikisikia, akapoteza fahamu ndio nikasikia mmoja anamwambia mwenzie wambebe.” “Naomba usilie, fikiria. Wakati mimi napiga simu ya pale alipochukua chumba.” Joshua akakata, akageuza kurudi Kiluvya akiwa amechoka na amekaribia sana nyumbani kwake akapumzike.

Baada ya muda Joshua akampigia tena Naya. “Naya?” Joshua akaita baada ya Naya kupokea ahijua kwa hakika atakua akilia sana. “Nipo Joshua. Najaribu kufikiria.” “Safi sana. Hapo sawa, kuliko kulia, tutashindwa kufikiria.” Joshua hakutegemea, hapo kidogo akampongeza. “Sasa ile simu ya pale uliyopiga akapokea yule muhudumu sasa hivi haipatikaniki ila ya baba inaita tu. Nimefikiria kwa haraka. Kama kweli waliingia kwa mshindo, inawezekana ile simu imeruka chini ya kitanda au baba ametoa sauti akaiweka mfukoni kwa haraka wakati wakimvamia, kuendelea kuipiga, cha kwanza, kama ipo chini ya kitanda ni kuimaliza charge ambapo tutashindwa kuifuatilia mtandaoni. Nitampigia sasa hivi James, anisaidie kuniambia inaonyesha simu ipo wapi. Na cha pili sasa, kama yupo na hao watu wabaya, kuendelea kumpigia bila sisi kujipanga, itasababisha wajue anayo simu na kuitupa njiani tusijue wanapompeleka.” Naya alikuwa kimya muda wote akisikiliza tu.

“Unanisikiliza mpenzi wangu?” “Nasikiliza. Ila Joshua?” Naya akamuita kabla hajakata. “Nipo Naya, wangu.” “Nilazima nimpate baba.” “Najua mpenzi wangu. Najua.”  Joshua akaafiki na kukata simu.

Naya akanyanyuka kwa haraka kama anayekomboa wakati. “Unafanya nini, Naya?” “Lazima nikamtafute baba, Zayoni. Naondoka kesho asubuhi.” Naya akajibu akikomboa wakati. “Unataka kuniacha peke yangu!?” Zayoni akashangaa sana, akawa kama amemkumbusha Naya. Akaweka kila kitu chini. Akatulia akifikiria anafanyaje na huyo kijana wa kiume aliyelelewa naye humohumo ndani ya nyumba lakini hakuwa akimfahamu kwa umbali huo. “Lazima nikamtafute baba. Nina uhakika kuna kitu kinachomuhusu Bale, wanaficha. Tukimpata baba tutajua juu ya Bale pia.” “Basi twende wote. Siwezi kubaki peke yangu.” Naya akafikiria akijua kabisa kwenda naye ni kuongeza mzigo, ila jinsi ya kumkatalia.

“Tumsubiri Joshua tujipange kwa pamoja. Ni kama baba ametuacha wote kwenye uangalizi wake.” “Hata mimi baba alinipigia simu alipokuwa Mbeya, akasema nimsikilize na kutii kila kitu atakachoniambia Joshua. Anaonekana anamsimamo na anauwezo mkubwa sana ndani yake. Nikimfuatisha sitakuwa kama nilivyo. Akasema amemuona ‘ndiyo’ yake huwa inabaki kuwa ‘ndiyo’. Hayumbishwi. Akaniambia nahitaji mtu kama huyo ili kufika mbali. Nisiwe mbishi.” Naya akaingiwa na wasiwasi.

Akajaribu kufikiria ndipo akagundua ni kama baba yao alikuwa kama akiacha wosia. “Mungu tusaidie!” Naya akaanza kulia. “Unafikiri na yeye atakufa?” Zayoni naye akauliza akianza kulia tena. “Sijui, Zayoni. Lakini Mungu aingilie kati kwakweli.” Wawili hao wakaanza kulia hakuna wakumbembeleza mwenzie. Wakajaribu tena kumpigia Bale kwani Joshua aliwaonya kutompigia simu tena baba yao. Simu ya Bale haikuwa hewani. Akataka kumpigia tena Malon lakini akasita na kuacha. Wakabaki kumsubiria Joshua.

Baada ya muda Joshua akaingia akisikika akizungumza na simu. Simu ya Naya ikaanza kuita chumbani. Akaikimbilia akidhani pengine ni baba yao, lakini alikuwa ni Nanaa. “Tupo njiani. Pole sana.” “Asante.” “Unahitaji kitu chochote tukujie nacho?” “Maombi tafadhali. Naombeni mumuombee baba yangu jamani.” “Usilie. Naona kaka James anahangaika huko, atafanikiwa tu. Tunakuja.” Naya akakata simu na kutoka chumbani kwake. Akamkuta na Joshua naye amemaliza kuzungumza na simu.

“Nataka kukipambazuka, niende kumfuata baba. Nitumie maelekezo na picha alizotutumia, mpaka pale hotelini.” “Naomba kwanza utulie Naya.” “Siwezi Joshua. Ninachoomba ni unisaidie kubaki na Zayoni kwa muda huo nitakapokuwa safarini halafu na mambo ya harusi yaendelee kama alivyosema baba. Mpaka siku ya karibu na harusi kama sijampata nitarudi tufunge ndoa, kisha nirudi niendelee.” “Naomba ukae.” Akamvuta mkono mpaka kwenye kochi.

“Cha kwanza, hatuwezi kwenda tukiwa hatujui tunakabiliana na watu wa namna gani. Tukienda bila kujipanga, kilichompata baba kitatupata na sisi, kisha wote kuishia mateka. James anafuatilia simu ya baba kujua alipo. Huyu niliyekuwa nikizungumza naye ni GM. Anakuja hapa. Lakini pia anaye mtu anafahamiana naye kwa karibu huko Tunduma. Amempigia simu. Anaonekana anaweza kutusaidia. Anamfahamu huyo mtu baba aliyekwenda kumtafuta ili kupata habari za Bale. Na kumbe ni tabia zake kutumia vijana wadogo kumfanyia biashara zake za magendo, na mengine mengi GM anakuja kutueleza kwa undani. Kuanzia hapo ndipo tutajua chakufanya. Vile nilivyokupigia simu nikakukuta umetulia, naomba endelea hivyohivyo. Ukitulia tunaweza kufikiria.” “Nashukuru Jos..” Simu ya Joshua ikaanza kuita tena.

Enzi Zarudi!

Joshua akaitoa mfukoni kwa haraka. Kisha Naya akamuona amekunja uso. Akabaki akiitizama simu yake. “Haiwezekani!!” “Ni nani!?” Naya akauliza baada yakuona sura ya Joshua ni kama hakuwa kiitarajia hiyo simu. Ikaita mpaka ikakata Joshua bado akiwa anaitizama na mshangao mkubwa sana usoni mwake. “Ni nani!?” Naya akauliza kwa wasiwasi zaidi. “Benadina!!” Hapo Naya akanyong’onyea maana kwa ule mshangao wa Joshua, kumbukumbu haikuchukua muda mrefu kumrudia.

Swali likabaki kwa Naya kama bado walikuwa wakiwasiliana! Na kwa nini bado Joshua anayo namba yake mpaka siku hiyo! Na huyo Benadina anaujasiri gani wa kumpigia Joshua mida hiyo! Naya akainama akifikiria akiwa na wasiwsi zaidi. “Kumbe bado Benadina yupo kwenye picha! Na matatizo yangu haya ya familia yasiyoisha, huyu Benadina anayepiga simu usiku kwa uhuru wote huu, si atafanikiwa kwenye moyo wa Joshua!” Wivu ukaanza kumsumbua Naya. Lakini akajirudi baada ya kukumbuka hata yeye anayo namba ya simu ya Malon na bado wanawasiliana. Hofu ikaanza kuongezeka. “Nitampoteza baba na Joshua! Mungu nisaidie.” Akawaza Naya, kisha akajifuta machozi akiwa amejiinamia. Simu ya Joshua ikaanza kuita tena.

Safari hii Joshua akapokea. “Kumu, anaongea.” Akaanza hivyo Joshua baada ya kupokea. “Ni mimi Benadina!” “Okay?” Joshua akaitika hivyo kama anayemwambia kwa hiyo! Kidogo Naya akapata faraja. “Nimekuwa nikikupigia ila ukawa hupokei, ndio ikabidi kutumia hii namba ambayo najua unaifahamu siku zote.” “Huyo aliyekupa namba yangu, alisahau kukwambia huwa sipokei namba nisizozifahamu.” “Ndio maana imenibidi kuhangaika mpaka kupata namba yangu ya zamani. Tena nimeinunua kwa mtu na kwenda kuandikishana naye polisi kwamba nimeichukua mimi na sitafanya uhalifu wasije kumkamata yeye.” Joshua kimya akisikiliza.

“Nimehangaika hivi kwa kuwa nina shida na wewe.” “Nakusikiliza.” Joshua akaongeza. “Naomba isiwe kwenye simu Jo. Tafadhali sana. Naomba tukutane na nimuhimu sana.” “Kwanza umepiga wakati mbaya sana ambao umenishangaza. Huu ni usiku sana. Unapata wapi ujasiri wakunipigia simu mida hii ya usiku hivi?” “Ni kwa sababu nina shida sana.” “Sidhani kama shida ndiyo imekufanya upige  mida hii, ila dharau.” Naya akashukuru Mungu.

“Hapana Jo, naomba usikasirike na ku…” “Niite Joshua.” Joshua akamkatisha na kuendelea. “Mbali na kuwa huu ni muda mbaya, unaonyesha dharau zako kwa wazi kwangu, pia sio kipindi sahihi ambacho naweza kukusaidia kwa lolote.” “Kabla hujasikiliza jamani!?” “Ni kwa kuwa mimi nakufahamu. Na nina uhakika na uwezo wangu. Mimi sitakuwa msaada kwako. Umeendelea na maisha yako zaidi ya miaka 15 sasa, na..” “Ni miaka 21 na miezi..” “Naomba nimalizie. Nisingependa kukukatia simu, tafadhali nisikilize. Kwa kipindi hicho chote umeweza kuwa salama bila mimi, naamini utakuwa sawa tu. Tafuta msaada kwengine ila si kwangu. Kwaheri.” Mpaka Naya akashangaa na kumwangalia.

“Na kitu kingine cha mwisho, tafadhali USINIJARIBU.” “Sikuwa na nia ya kukuudhi Joshua.” “Na ninakuonya, usirudie kunipigia tena simu. Mchezo wowote unaotaka kuucheza, sipo tayari na sina muda. Nimekuwa muwazi kwako, na kwa heshima tu. Tafadhali kuwa muungwana.” Joshua akakata simu, na kutoka kabisa pale. Akamuacha Naya na mshangao wa muda mpaka akasahau kama amepoteza baba.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda wakasikia mlinzi akifungua tena geti, wakajua ni kina Magesa. Baada ya kuegesha gari, wakamsikia Joshua akimsalimia mama G, Naya akajua wamefika wote kwa pamoja. “Poleni sana.” “Asante mama, na poleni na nyinyi kwa usumbufu, najua usiku umeendelea!” “Hata kidogo. Bado hatukuwa tumelala. Naya anaendeleaje?” Wakasikia majibizano yakisogelea mlangoni, Naya akasimama na kwenda kuwafungulia mlango.

“Karibuni.” “Pole bibi harusi wangu.” “Asante. Ila nina tumaini. Nashukuru Mungu Joshua alitumia akili, akachukua habari nyingi na majina ya alipokuwepo baba. Nina imani tutampata tu.” “Hata mimi nimemwambia, alifanya vizuri sana. Imekuwa rahisi mno.” Akaongeza Geb. “Kweli?!” Naya akauliza kwa wasiwasi tena. “Ooh yeah.” “Karibuni ndani ndipo tuzungumze vizuri.” Joshua akaingilia nakuwakaribisha. “Samahanini jamani, nimeshindwa hata kuwakaribisha! Nimeingiwa hofu, mara tumaini linanijia! Basi imekuwa mvurugano tu.” “Tunaelewa wala usijali.” Akajibu mama G.

 “Vipi Zayoni?” Geb akamsalimia. “Mimi naogopa.” Akajibu Zayoni akitetemeka midomo. “Pole. Lakini nina imani kubwa kwamba tutampata baba. Kwa muda mfupi sana, tumefika pazuri.” Geb akamtuliza. “Huyo jamaa, Mbabe kama anavyojiita, ni jina la mtaani tu. Nimetumiwa jina lake kamili. Na ni kweli anayo pesa kulingana na huo mji wake na analindwa na wale askari walioharibika kwa kupenda hongo. Anasema ni ngumu kumfikia, lakini anasema palepale wapo askari ambao wamechoshwa na tabia zake. Hiyo ndio itakuwa nguvu yetu.”

“Na kutokana na taarifa pamoja na picha ambazo Joshua amenitumia, nikamuuliza. Ni kweli ile nyumba ya kulala wageni ipo na jina ni sahihi. Sio mbali na kituo cha mabasi, kitu kinachofanya wahuni wengi kupapeda hapo kwa kuwa panafikika kwa urahisi na ipo mjini. Amenipa namba ya simu ya askari ambaye anamuamini sana, amesema yeye anaweza kutusaidia kwa karibu. Na yeye hatamwambia mtu haya tunayoyajua sisi juu ya baba Naya.” Geb akaendelea.

“Ndio nasubiria azungumze naye. Atutambulishe kwake, ndipo na sisi tumpigie.” “Lini?” Naya akauliza kwa haraka. “Nimemwambia huyu jamaa yangu, atusaidie iwe leo kabla hapajapoa. Najua usiku umeendelea sana. Lakini nimemuomba ampigie simu huyo askari na kumwambia tunamsubiria yeye tu. Akitoa baraka zake, na sisi tumpigie. Wakati James anafanya uchunguzi wake, basi na sisi tupate mwenyeji huko wa uhakika.” “Samahani Geb. Sijui kama nikuchanganyikiwa! Sijaelewa.” Naya akaongea kwa wasiwasi.

“Chakwanza naomba utulie Naya. Najua ni hali ngumu, lakini tulia na kuendelea kuomba. Shetani ni mvurugaji mno. Na furaha yake ni kuona anapoharibu, kunatoa mafanikio mazuri. Kila wakati jambo zuri linapotaka kutokea, ambalo haliendani na mipango yake, huwa anamtindo wa kutupia jambo hapo. Akijua ameshindwa kabisa, ila tu nia ni kuwavuruga, zaidi akili. Nguvu yako itakuwa ni kuzitambua hila zake na kubaki umesimama imara.” “Kama alivyosema mfamle Daudi kwenye bibilia Zaburi 23:4. Kwamba, ‘nijapopita kwenye bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya,’  si unakumbuka ni kwa nini alisema hivyo?” Mama G akamuuliza.

“Alijua Mungu yupo naye.” Naya akajibu taratibu. “Ewaaa! Basi amini hata hapa, sasa hivi, na kule baba alipo, Mungu wetu yupo naye. Tena inawezekana akatoka huko akiwa na jambo zuri, hiki kilichompata, kikawa faida wala si hasara. Tulia kabisa uuone na wewe mkono wa Mungu.” “Amina.” Naya akajibu na kuinama kama anayefikiria hapo kitini. Joshua akamvuta mkono. “Naomba usiogope Naya.” “Naogopa mambo mengi Joshua! Naogopa sana. Kumbuka hatuna mama. Bado Bale hatujui alipo! Baba naye hatujui alipo! Harusi imekaribia. Sijui tukiahirisha kwa hili, inakuwa mpaka lini!” Naya akaanza kulia.

“Natamani isingekuwa wakati huu jamani! Zimebaki siku 5 tu na mimi natakiwa niwe nimeolewa! Halafu haya yote yanatokea!” “Baba yako alinipigia simu jana jioni, Naya. Mimi sijui ni kwa nini! Sijui Mungu wake alimuonyesha nini! Lakini alinisihi sana tarehe tuliyopanga harusi ifungwe, nihakikisha ndoa inafungwa.” Naya akazidi kulia. “Na mimi pia alinipigia mida ya mchana hivi. Akaniachia maagizo hayohayo. Nilishangaa kidogo mpaka mikampigia mama, nikamwambia maagizo yote aliyoniachia baba Naya. Tena mimi alinipigia akiwa njiani akielekea huko.” Geb akaongeza kwa mama yake. “Ni kama aliyejua kama kuna jambo baya linaweza kumpata!” Nanaa akaongeza. Naya akaendelea kulia.

Joshua akamvuta tena mkono kama kumrudisha hapo. “Kesho tunakwenda mimi na GM.” Naya akashituka sana na kumwangalia Joshua kisha Geb. “Ndicho nilichokuwa nikikwambia. Tutatumia msaada huo wa James na huyo polisi wa huko. Kuna jamaa yetu wa usalama naye nimemuomba anitafutie askari ambaye atakubali kuongozana na sisi kesho. Tutaondoka hapa sisi wanne, na ndege ya asubuhi kama tukifanikiwa kuipata. Ili itusogeze karibu na huo mji, kisha nimemuomba huyo jamaa yangu aje atupokee. Kesho hiyohiyo tutahangaika kwenye huo mji, mpaka tumpate baba Naya na kujua maswala ya Bale kwa hakika. Nashauri  tutulie.” Akaongeza Geb.

“Zayoni na Naya, tunafanya kila tuliwezalo, kumpata baba na Bale. Hatutakubali kushindwa kirahisi hivi. Pateni muda wa kupumzika, na sisi acha tuondoke tukajipange vizuri.” Naya alifurahi sana mpaka akajikuta anapiga magoti. “Jamani nawashukuruni sana. Asante Joshua mpenzi wangu. Geb, asante sana. Wewe Nanaa ndio naogopa utanichoka!” “Sio rahisi kiasi hicho na shetani anajua. Amekutana na sisi, atahangaika mpaka aelewe safari hii amecheza pabaya. Aache utani!” Nanaa akajibu.

“Mama G, nakushukuru mama yangu.” “Wewe usilie na usipige magoti. Kila kitu kitakwenda sawa na mapenzi ya Mungu wala si michezo ya shetani yatatumia kwa wakati. Sisi tumeshamtambua na hila zake. Huwa akipita sehemu tunamjua kabisa na kumshugulikia. Usiogope. Tulia. Jua ndoa ipo na kesho tutapata majibu ya baba pamoja na Bale.” Joshua akamsaidia kukaa.

“Pole Naya. Pole sana. Naamini kila kitu kitaenda sawa.” “Sasa hivi na mimi nimepata amani.” Yakaanza maombi hapo. Wakamsihi Mungu kwa kutubu na kujitakasa. Wakamuombea baba Naya huko alipo pamoja na Bale ambaye sasa habari yake ikawa imebadilika. Hofu yakuwa pengine yupo hatarini na yeye ikawa bayana. Wakamuombea. Kisha wakakabidhi mipango yote kwa Mungu, mama G akiwa ndio kiongozi wao. Mpaka wanamaliza wakawa wameongeza kiwango cha ujasiri si woga tena.

Simu ya Geb ikaanza kuita, akaipokea kwa haraka. “Naomba nikuweke kwenye spika, nipo na yule ndugu yangu niliyekwambia tutakuwa naye huko.” “Hamna shida.” Mtu wa upande wa pili akajibu. Geb na Joshua wakatoka nje kuzungumza na huyo mwenyeji wao wa huko Tunduma. Wakapata na namba ya huyo polisi, naye akakubali kuzungumza nao. Wakampigia. Wakamueleza kwa kifupi habari nzima juu ya baba Naya na sababu iliyompeleka huko kuwa ni kumtafuta Bale na amechukuliwa akiwa anazungumza na binti yake.

“Mbabe ni jeuri kweli sababu ya watu wanao mzunguka. Na huwa kuna mambo anafanya ya udhalilishaji kabisa akijua hakuna wakumgusa, ila uuaji sio asili yake labda awe ameanza sasa. Kwa nilivyowasikia, itakuwa amemchukua kwenda kumtisha tu ili aogope na kuondoka kwa sababu ni kweli biashara zake anategemea vijana. Sasa nina habari ingine inaweza kuwashitua kidogo lakini msikate tamaa.” “Ni nini tena!?” Akauliza Joshua.

“Siku chache zilizopita, alikuwa amekamatwa huko Zambia. Wakamfunga. Ikasikika alikuwa na vijana wake wengine wawili, ambao huwa wanamsaidia kupitisha mizigo yake mpakani. Kilichoniudhi na kuniumiza zaidi ni vile alivyotolewa yeye tu dhamana. Akatoka rumande, na nasikia ni kama amekana kabisa kuwa hakuwa pamoja na hao vijana! Eti anasema hao vijana walikwenda kwa mipango yao binafsi yeye alifanya kuwaonyesha tu njia na alishawapa madhara kabla ya kwenda lakini eti wao vijana walikubali kwenda naye. Lakini inavyosemekana, na mtu wake wa karibu kabisa ni kwamba alivuka nao mpaka, au alikwenda nao ili kumsaidia kupitisha mali zake, akiwa amewaahidi eti wakifanikiwa, atawalipa asilimia fulani ya hiyo mizigo. Sasa walipokamatwa ndipo amewakana ili asije akawajibishwa!” Joshua na Geb wakaumia sana.

“Sasa hakuna wakumwajibisha?” “Kwenye huu mji ameweza kushika wakubwa wengi. Anakula nao, na wengine wanasema ni kama anawafanyia wengi wa hao wakubwa biashara, kisha wanalipana humo kwa humo. Kwa hiyo kuwekwa kwake ndani ni kukwamisha wengi, kitu ambacho hawawezi kukubali. Sijui kama mnanielewa?” “Sisi hatutaki matatizo na yeye. Tunachotaka ni watu wetu, basi. Ila akijidai mjuaji, hapo na sisi hatutakubali.” Joshua akatahadharisha. “Kabisa. Hapo hatutanyamaza wala kutulia. Kesho tutakuja na watu wa usalama. Tunaomba na wewe uungane na sisi.” Akaongeza Geb.

“Mimi bado ni mkazi wa hapa, jamani. Baada ya yote haya nitabaki huku. Naomba niwasaidie kuwapa muongozo tu lakini sio kuwa kimbelembele.” Joshua na Geb wakaangaliana. “Hata mpaka sasa umeshakuwa msaada wa kutosha. Tunashukuru. Hiyo kesho tukija..” Wakaweka mipango yakueleweka ndipo wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakarudi ndani kuwaambia mipango yote na kile walichosikia kutoka kwa huyo afande. Nalo hilo likawa jambo jema. Wakazungumza mambo mawili matatu, kina Magesa wakaondoka, akabaki Joshua na kina Naya. “Nashauri Zayoni akapumzike. Amelia muda mrefu sana.” “Kichwa kinaniuma.” Akalalamika. Naya akampa dawa za maumivu, akaenda kupumzika, ndipo wakabaki wao wawili.

“Nikuulize swali Joshua?” “Juu ya Benadina?” “Hapana. Baba kwanza. Unafikiri alijua kama kuna baya litampata ndio maana alikuwa akiacha ujumbe kwa kila mtu?” “Sijui Naya. Pengine ule wasiwasi alikuwa nao juu ya Bale na habari za huyo mwenyeji wake huko zilishamuogopesha lakini kwa kuwa alishakusudia kwenda, akakubali liwalo na liwe, ila sasa akawa na wasiwasi, na hakutaka awaache pabaya. Si lazima ikawa alipata maono ya nini kitamtokea! Naomba usiwe na wasiwasi Naya. Tutembee kwa hatua. Tutakubaliana na hatari ya kesho, kesho yenyewe. Leo baba ametekwa akiwa mzima na katikati ya maombi. Kwa sehemu tumejua mtekaji si muuaji ni mtishaji tu. Tumemuomba Mungu amlinde huko alipo. Naomba tuwe na imani.” “Nakushukuru kwa kusimama na mimi Joshua. Asante.” Joshua akamuhurumia.

Naya akafikiria. “Kwa hakika kama isingekuwa wewe, nahisi sasa hivi ningekuwa nimechanganyikiwa. Fikiria ndio hii hali ingenikuta na mchumba ni Malon! Ndio yupo kwenye kile kipindi chake cha kupotea na mimi ndio nipo hivi!” “Hajakutafuta tena?!” “Hapana Joshua. Sasa fikiria haya ndio maisha niliyokuwa nayo na yeye. Anakuacha katikati ya hali kama ile niliyompigia na kumwambia kabisa nina shida! Amepotea. Atakuja kurudi wakati mwingine tena, akiwa na mipango yake. Lakini Joshua, Mungu amekuleta kwangu, naomba Benadina asinipokonye.” Joshua akafikiria kidogo.

“Nini?” Ikabidi Naya aulize baada yakumuona amekunja uso na kutingisha kichwa. “Sijui Naya! Lakini kuna kitu hakipo sawa juu ya Benadina.” Joshua akanyamaza tena kama anayefikiria tena. “Sijui ni kwa nini, lakini nahisi kuna jambo zaidi ya hiyo simu. Tuache tu, lakini naomba usitishwe na Benadina. Huyo mtu sijamsikia kwa muda mrefu sana. Sana. Eti leo, nikiwa nataka kuoa, yeye alishaolewa na ana watoto juu, ndipo anitafute kuwa anataka msaada wangu! Hapana Naya. Kuna kitu kinachoendelea. Ila tuyaache tu. Na wewe naomba utulie. Nitarudi, tutafunga ndoa yetu, changamoto nyingine tutaendelea kupambana nazo tukiwa ndani ya ndoa.” “Kwa hiyo umekubali na wewe tuendelee!?” Naya akauliza kwa unyonge kama anayetamani jibu jingine.

“Kabisa. Sio lazima ikawa sherehe, ila ndoa lazima Naya. Tunastahili kuishi pamoja. Sitajali hata kama tutakuwa sisi tu kama tulivyokuwa hapa na kina Magesa, tukala viapo vyetu vya ndoa, kisha tukaja kufanya sherehe wakati mwingine. Hilo naomba ulifikirie na ukubali tu. Ona huku unakoishi, na kule ninakoishi mimi, halafu kipindi kama hiki! Vita yetu itakuwa rahisi tukiishi pamoja, karibu, kama mke na mume! Itaturahisishia. Au unaonaje?” “Ni kweli. Hata mimi natamani Joshua. Ukweli najiona kabisa nipo tayari kuishi na wewe. Wala sioni haya kusema.” “Hapo nashukuru. Basi tuombe Mungu kila kitu kiende sawa. Kitakachobadilika ni aina ya harusi tu, lakini sisi tunaendelea na ndoa yetu.” “Sawa.” Wakakubaliana. Naya akahamia kwenye kochi alilokuwa amekaa Joshua. Kochi dogo tu, lakini linaweza kukaa watu wawili. Akajisogeza karibu, akapitisha mikono kama kumkumbatia kwa nguvu juu ya kiuno karibu na mbavuni, akamlalia Joshua kwa upendo.

“Namshukuru Mungu kwa ajili yako Joshua. Wewe ni wa kuaminika. Hata baba ameliona hilo. Amemwambia na Zayoni, akusikilize.” “Kweli Naya?!” Joshua hakutegemea. Akamshungulia pale alipokuwa amejiegemeza. “Ndivyo alivyoniambia Zayoni usiku huu ulipoondoka. Binafsi mimi nishahidi wa hili. Najua umechoka, lakini ona ulivyofikisha hili jambo mbali kama uliyekuwa umejipanga! Umetafuta watu sahihi wakutusaidia na kusimama na sisi. Umelibeba hili jambo kama baba Naya ni baba yako!” “Ni baba yangu, Naya.” “Hapana Joshua. Najua unajua ninachomaanisha. Heshima uliyompa baba imefanya mpaka hata kina Geb wanamuheshimu sana. Mpaka najisikia vizuri nikimuona mtu kama Geb jinsi anavyozungumza na baba! Najua yote ni kwaajili yako. Heshima na thamani uliyompa, ndio imefanya na wengine wamchukulie hivyo. Hata yeye baba ameliona hilo na akaniambia. Nashukuru mpenzi wangu. Asante.” “Karibu, na naomba usilie. Twende ukalale.” “Hapana Joshua wewe ondoka, nitakuwa na wewe kwenye simu mpaka ufike, ukilala na mimi ndio nilale. Sasa hivi hofu imepungua kwa asilimia kubwa, nenda tu kapumzike.” “Basi nitakupigia na asubuhi. Nitaanzia ofisini. Nikafanye vikao vya asubuhi, niweke mambo sawa, ndipo niondoke.” Joshua akaondoka baada ya kuagana na Naya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usikose Muendelezo kujua kitakachoendelea kwa baba Naya, na Bale. Wote wapo wapi? Nani anahusika na kumteka nyara baba Naya? Benadina naye anatokea wapi tena? Nani amempa namba ya Joshua? Kwa nini iwe sasa hivi?

Usikose Muendelezo.

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment