Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 32. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 32.

 Nguvu ya Pesa.

Zikiwa zimebaki siku 4 tu ndoa ya Naya na Joshua ifungwe, pesa yakutosha na kueleweka ikamtoka Joshua na Geb, wakisindikizwa na rafiki mmoja wa Geb anayefanya kazi Usalama wa Taifa mwenye uzoefu kwenye mambo ya upelelezi anayefahamika kwa jina la Gamba na askari kanzu mwingine mmoja, aliyechaguliwa na Gamba mwenyewe, kama rafiki yake na kusema anaweza kufanya naye kazi kirahisi popote kwani wameshirikiana naye kwenye mengi na kufanikiwa, wenzake walimtambua kwa jina la Chui kutokana na wajihi wake kikazi. Waliliacha jiji la Dar wakitumia usafiri wa ndege kuelekea walipokuwa wameelekezwa na James, alipoona mara ya mwisho baba Naya alikuwepo kwa kutumia simu ya baba Naya, ambako ni Tunduma. Nguvu ya pesa ilikuwa ikitembea kila mahali. Hapakuwa na kusubiri wala kuchelewa popote pale. Walishuka kwenye ndege wakakuta usafiri mzuri ukiwasubiria kuwafikisha Tunduma kabisa walipoelekezwa na James mtaalamu wa mambo ya kitekinologia.

Ule ushauri wa Joshua kumwambia baba Naya kuweka LocationOn, kulimsaidia kwa urahisi sana James kufuatilia akaweza kujua ile simu ilipo. Walifika kwenye huo mji wa Tunduma ikiwa mapema tu. Sehemu ilipoonekana bado ipo simu ya baba Naya, walipofuatilia ikawa kwenye ileile hoteli, lakini chini ya kitanda. Wakajua ilianguka wakati wa purukushani za kumchukua.

Muhudumu aliyekuwa zamu siku hiyo na yeye alijeruhiwa vibaya sana, akawa yupo amelazwa hospitalini. Wale askari wakasema nilazima kwenda kuzungumza naye. Wakaongozana mpaka hospitalini alipolazwa, akasema alivamiwa na watu waliokuwa wameficha sura zao kwa kujifunika kwa kuvaa soksi. Wakampiga mpaka akapoteza fahamu. Hajui kilichoendelea. Yule mtu wa usalama akamuamini. Akawaambia kina Geb waende moja kwa moja kwa huyo Mbabe bila kupoteza muda.

Wakakubaliana kwenda kuzungumza naye ana kwa ana. Wakatoka hapo mpaka kwenye maduka yake. Wakamkosa, wakataka apigiwe simu na kuambiwa ni lazima afike kituo cha polisi, anasubiriwa. Wakaelekea kituo cha polisi. Geb na Joshua wakaambiwa wasubirie ndani ya gari, wale askari ndio wakashuka kwenda kuzungumza na askari wenzao ambao ndio wenye mji.

Baada ya mazungumzo marefu, wakiwahakikishia wao hawataki kesi ila watu wao tu ndipo Mbabe akapigiwa simu sasa na mkuu wa kituo. Akafika hapo bila kuchelewa. Lakini yeye alikataa kabisa kuwa hausiki na utekwaji nyara wa baba Naya, na wala hajawahi kumsikia Bale. Ndio mara yake ya kwanza kumsikia hapo. Wale askari waliokuja na kina Joshua, wakasisitiza kusema kuwa hawataki kesi wanachotaka ni watu hao wawili. Hata kwa kutaja tu sehemu walipo, wao wataendelea kuanzia hapo. Mbabe akakataa kabisa.

“Labda niwaambie wote.” Akiwaangalia mpaka wale askari pale. “Watu wanaotafutwa, wanatafutwa na watu wakubwa sana hapa nchini. Mimi si askari, ni mtu wa Usalama, nimepewa amri kutoka juu, kuja kuulizia habari zao maana mara ya mwisho huyu mzee, ametuma kwa familia yake hizi picha na namba.” Akawaonyesha. “Huu ni uthibitisho kuwa, mji wenu umemshikilia si mtu mjinga, mtu mkubwa sana na mwenye akili ya kutosha. Asingetoa kwa familia yake habari kama hizi zinazoonekana si muhimu, lakini kumbe zina uzito mkubwa sana na zinazooonyesha ametekwa hapa.” Akaanza kuwatisha. “Usalama umeweza kuifuatilia simu yake, mpaka kuweza kuipata chini ya uvungu wa chumba cha hoteli.” Wale askari wenyeji wakaangaliana.

“Hiyo taarifa imeshafikishwa makao makuu uthibitisho kuwa ni kweli alikuwa kwenye hiyo hoteli na picha nyingi tu zimepigwa kuanzia pale tulipoikuta simu yake, mpaka jinsi ilivyokuwa. Wazi inaonyesha iliruka katika purukushani za kuchukuliwa kwa nguvu kama binti yake alivyoeleza alichosikia, wakati alipokuwa na baba yake kwenye simu akitekwa. Yule binti amehojiwa na maelezo yake yamehifadhiwa kwenye kabrasha kule Usalama na mimi nikapewa kusoma kabla sijaja huku.” Gamba akaendelea kwa vitisho.

“Mbaya zaidi, muhudumu wa pale naye alijeruhiwa. Yupo hospitalini. Japokuwa hakuwa na maelezo ya nini kilitokea, na kitabu cha wageni alichoandikisha huyu mzee hakipo pale, lakini zipo picha za kitabu alichosaini huyu mzee aliyetekwa. Hizi hapa.” Akaowaonyesha. “Usiku wa jana alipiga picha na kutumia familia yake, na huyu muhudumu aliyejeruhiwa, amekiri ni kweli huyu mzee alikuwepo pale usiku. Yeye ndiye aliyempokea na kumkabidhi funguo za chumba. Ni nini nataka kusema!” Gamba akawatizama wote kwa zamu. Akaona ni kama wameingiwa hofu.

“Iwe bwana Mbabe unahusika au la, jua jina lako lipo makao makuu ya usalama wa taifa kwa kuwa huyu mzee alikuja kukutafuta wewe, Mbabe. Ujue uchunguzi wa kina juu yako, kile unachokifanya, familia yako na wanao kuzunguka vitaanza kufanyiwa uchunguzi kwa kina. Hakuna jiwe ambalo halitapinduliwa kwenye huu mji mpaka huyu mzee apatikanike, ndipo lije sasa swala la kijana wake. Huyo kijana wake ametoroka tu nyumbani, lakini ni mtoto wa wenye nazo. Walioshika hii nchi. Mpaka sasa mimi nimeandika na kutuma ripoti pale nilipofikia. Natoa siku mbili mbele. Kama sitapata ushirikiano wowote ule, nitaondoka kwa amani kabisa. Ila natoa angalizo.” Wote kimya.

“Hatujui nani atatumwa baada ya sisi kuondoka na kupeleka ripoti kwamba tumeshindwa hata kupata ushirikiano wa polisi wa hapa.” “Mbona mimi ndio nimekuitia Mbabe!?” Mkuu wa kituo akajihami. “Kumuita si kutatua tatizo. Hakuna atakayetaka kujua hatua za kumtafuta huyu mzee ila matokeo ndio wanayotarajia. Na kwa bahati mbaya sana, habari zenu zipo na nasikitika kuwaambia si nzuri. Watu wanayajua mahusiano yenu na Mbabe.” Wakaangaliana.

“Huyu ni raia kama raia wengine na kwa kuwa ni mfanyabiashara mkubwa hapa, anasaidia jamii kwa kila hali, ndio maana pengine watu wanaona anapewa upendeleo! Lakini si vinginevyo.” Mkuu wa kituo akatetea. “Nasikitika kukuarifu sicho kilichofikishwa mbele ya chombo cha usalama. Habari za hapa zipo mbali sana.” “Lakini hawawezi kusikiliza majungu! Watu ni wanafiki na wambea sana. Wanaweza kuzungumza chochote kwa wivu tu.” “Na hilo nina uhakika kwa asilimia kubwa sana kuwa litazingatiwa kwenye uchunguzu utakao fuata baada ya hapa. Itajulikana kama ni uongo au la. Kwa uzito wa hili jambo lilivyo. Nawahakikishia ukweli utajulikana bila shida tena kwa haraka sana. Msiwe na wasiwasi, wanataka kuhakikisha huu mji ndio utakuwa mfano kwenye hii nchi, kukomesha unyanyasaji kwa raia, magendo, ubadhilifu wa mali za uma na kuweka sawa chombo cha usalama. Si mnajua sasa hivi wanaotaka madaraka lazima kujionyesha wanawajibika! Sasa jiwekeni sawa, ili fagio linapopita kusafisha, wenye uchu wa madaraka kujipatia sifa, nyinyi msiwe wahanga.” Gamba akaendelea kwa kujiamini zaidi maana walionekana ni kweli wametishika. {Na kilikuwa kipindi cha utawala wa awamu ya 5 nchini. Kuwajibika kwa kila kiongozi.}

“Kama nilivyotangulia kusema, hatuwezi kuondoka kesho, tutaonekana hatujasaka vyakutosha. Maana masikio na macho ya wakubwa yapo huku kwenye huu mji wenu sasa hivi, wakisubiria matokea. Wanafuatilia ripoti kila baada ya muda, wanataka ripoti kujua tulipofikia. Sasa sisi tunafunga siku ya kazi. Mahojiano ya muhudumu na ukiri kuwa huyu mzee alikuwa pale kwenye ile nyumba ya kulala wageni, tumeshatuma. Wote wamejiridhisha kuwa mzee ametekwa nyara akiwa kwenye chumba alicholipia, tena alikuwa akiomba na binti yake. Sasa sisi tutakuwa hotelini na siku ya kesho pia bado tutakuwa hapa. Kama mtapata fununu yeyote, maana tunaamini nyinyi ni wenyeji hapa. Mkifanikiwa, msichelewe kutufikishia taarifa zozote zitakazosaidia kupatikana kwa huyo mzee kwa haraka.” Gamba akaongeza kitisho.

“Mkishindwa, basi. Sisi tutaondoka na taarifa tulizokusanya tayari, tuwaachie mwenye nguvu waje kwenye mji wenu. Sasa wao ndio waje wapambane na majambazi wa huu mji wenu, na hapo ndipo itakuwa kutangazia umma kuwa mmeshindwa kazi. Jioni njema.” Akasimama. “Na wote sisi tuliokuwepo ndani ya hiki chumba, tuombe Mungu huyu mzee apatikanike akiwa salama. Lasivyo!” Gamba akawatizama mmoja baada ya mwingine, kisha akatoka akiwa amewatajia mpaka namba ya kesi waliyoifungua kina Joshua huko Dar, na kuwaambia wafuatilie wenyewe kujiridhisha juu ya hiyo kesi kuwa inafuatiliwa vilivyo. Yule askari kanzu aliyeongozana naye, Chui, naye akafuata nyuma. Wakatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakaingia garini walipokuwa wamewaacha Geb na Joshua. “Aisee umetumia akili sana! Maana bila hivyo, hakika tungegonga mwamba. Yule jamaa hafikiki!” Chui akaanza kumsifia Gamba mara baada ya Geb kuondoa gari hapo kituoni. “Halafu ana jeuri, haogopi kabisa! Anajibu kibabe mbele ya mkuu wa kituo!” Chui akaongeza. “Hata mimi nililiona hilo ndio maana ikanibidi niikuze hii kesi. Nafikiri anajua wale askari wote pale wapo upande wake, wanamlinda.” Gamba naye akaafiki. “Ila wametishika.” Chui akaongeza na kucheka. “Niliwaona.” Gamba akaafiki na Chui akaendelea. “Mwanzoni walianza kwa kutufukuza kibabe. Gamba alipowabadilikia, nikaona wamenywea.” Wakaanza kucheka ndipo ikabidi wawasimulie Joshua na Geb kilichoendelea wakiwa ndani, kituoni.

“Unashauri nini baada ya hapa?” Joshua akauliza. “Kama nilivyowaambia pale kituoni. Sisi turudini hotelini. Tutulie kabisa. Kwa hofu waliyoipata, hakika tutampata huyu mzee wenu. Awe hai au walishamdhuru. Wawe ni wao walimteka au la, tutampata tu. Tena tutampata kwa wao wenyewe kuhangaika ili usije fanyika upelelezi hapa, wakagunduliwa maovu yao. Naombeni tutulie kabisa. Najua ni ngumu lakini mjue na wao wanatuangalia. Tukianza kuchukua hatua za kupaniki tu, tutawaonyesha hatujui tunachofanya na ndipo wanaweza kumdhuru kabisa mzee ili kufuta ushahidi.” “Nafikiri sio wazo baya. Au unasemaje Joshua?” Geb akauliza. “Ni sawa.” Joshua akaafiki akiwa anafikiria.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          Walichukua vyumba katika moja ya hoteli ya hapohapo mjini kabisa, sehemu ya wazi tu. Wakatulia usiku huo wa kwanza. Asubuhi wakaenda kupata kifungua kinywa pamoja. Wakakaa hapo mgahawani kwa muda tu wakizungumza hili na lile. Wakaondoka, kila mtu akarudi chumbani kwake. Mchana tena wakakutana hapohapo. Hapakuwa na fununu yeyote ile ya baba Naya. Joshua akaanza kupatwa wasiwasi. Zimebaki siku 3 tu, harusi yao ifungwe. Baba mzaa chema hajulikani alipo wala kaka wa bwana harusi pia hajulikani alipo.

          “Mnafikiri vile vitisho vitafanya kazi jamani?” Joshua akauliza akisikika ameingiwa na wasiwasi. “Na wenyewe wanajiuliza swali kama lako. Hata hapa tulipo, wanatuangalia tu na kutufuatilia kila hatua tunayochukua. Nakuhakikishia, kosa dogo tu tutakalofanya, watathibitisha kuwa sisi ni hovyo tu. Nakuhakikishia pia sasa hivi tumewapa tumbo joto. Naomba muwe wavumilivu.”  Gamba mtaalamu wa mikasa kama hiyo akawahakikishia. Joshua anayetakiwa kutoa ripoti kwa Naya kila wakati ikabidi kutulia tu.

          Jioni wakati wakila tena hapohapo ujumbe ukaingia kwa Geb kutoka kwa askari aliyekuwa akiwaongoza nyuma ya pazia tokea walipokuwa Dar na kuwapa habari za Mbabe kwa kina ila kuhofia kuwa kimbembele. ‘Inaonekana mmetingisha mji. Matumbo joto! Tatizo ni jinsi yakujirudi. Wameingiwa hofu.’ Geb akasoma na kuuliza. ‘Kuna fununu zozote?’ ‘Nimesikia hapa kituoni wanashindwa jinsi ya kufikisha ujumbe kwenu.’ Geb akafikiria kwa haraka, akamjibu. ‘Wape wazo la kuandika alipo na kutupia chini ya mlango wa chumba cha mmoja wetu.’ ‘Acha nirushie hilo wazo, bado nipo kituoni. Kila mtu anajipanga na kujitetea wakijiandaa na huo ukaguzi mkuu endapo watu wa usalama wakija kwenye huu mji. Kila mmoja anasema lake.’ ‘Sisi shida yetu ni watu wetu tu. Wape hilo wazo. Sisi tutajichelewesha hapa.’ ‘Sawa. Pengine itasaidia.’ Akarudisha hayo majibu.

          Geb akarudisha simu mfukoni. Akatulia kwa muda. Akaangalia kulia na kushoto. Kulikuwa na wateja wengine hapo mgahawani. Kwa kuwa alikuwa mgeni pale, hakujua yupi mteja na yupi yupo pale kuwachunguza. Akatulia kabisa hata Joshua hakumuonyesha ujumbe kwa haraka. Uzuri ni mkimya. Hakuwa akichangia sana mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea pale. Hata alipotulia hakuna aliyemuhisi kuwa analo jambo.

Kila walipotaka kuondoka Geb aliwaomba wabaki kidogo. Baada ya muda Geb akatoa simu mfukoni ilipoashiria mtetemeko kuwa kuna ujumbe umeingia. ‘Chumba chako namba ngapi?’ Akasoma huo ujumbe. Kabla hajajibu, ujumbe mwingine ukaingia. ‘Nina ujumbe wako. Nimewaambia mimi najitoa muhanga kuleta kwenu. Wamekubali.’ ‘Nashukuru sana. Tumbukiza chini ya mlango, chumba namba,’  Akamtajia. Kimya. Baada ya muda kama dakika 10 hivi akapata ujumbe mwingine ‘Tayari.’ ‘Tutawasiliana. Nashukuru sana.’ ‘Karibu lakini hutanipata tena. Natoa kabisa hii namba hewani kwa muda.’ Geb hakujibu lakini akapata tumaini. Akasubiri kama dakika 20 mbeleni ndipo akawaambia wenzie waondoke pale.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakaondoka. Walipoingia tu garini akamkabidhi Joshua simu yake. “Nimepata habari njema ndio maana nilikuwa nikiwazuia tusiondoke. Sikuwaambia pale kwa kuwa nilijulishwa kuwa tunafuatiliwa.”  Shauku ya kusoma kwa Joshua ikaongezeka. “Nilijua tu.” “Hakika huu ni ulimwengu wako Gamba! Nimeambiwa kila kitu ulichobashiri.” Geb akampongeza.

“Haiwezekani!” Joshua akahamaki baada ya kumaliza kusoma. “Twendeni tukahakikishe kama nikweli.” Geb akaongeza. Ukimywa mkuu ukatanda humo garini. Roho mkononi hawajui karatasi walioachiwa imebeba ujumbe gani. Mawazo ya Joshua yakahamia kwa mchumba aliyemuacha akiwa na matumaini atamrejeshea baba yake. Swali likawa atakuwa kwenye hali gani! Yu mzima au la! Geb akaendelea kuendesha na yeye akiwaza.

“Naomba kila mtu aende chumbani mpaka nitakapo wapigia.” Geb akatoa mungozo wakati akigesha gari. “Ni kweli. Nivizuri tuendelee kama kawaida ili wasije kumuhisi huyo jamaa wa Geb, wakajua anawasiliana naye. Kwamba alishamwambia kuwa kuna ujumbe.” “Ni kweli.” Mpaka hapo Geb hakuwa amewatajia jina la huyo askari wa hapo. Maana hata kwenda kuwapokea, Geb alifikiria akaona sio sawa, ni kuhatarisha maisha yake. Kwa hiyo walipotua uwanja wa ndege, Geb akawa amewasiliana tena na mwenyeji mwingine wanaofahamiana kwenye mambo ya biashara na kuwapatia hilo gari. Kwa hiyo waliingia kwenye huo mji wakiwa wageni na hata hilo gari hawakuwa wakilijua.

Geb aliingia chumbani kwake na kweli akakuta karatasi ndani, kama iliyopitishwa chini ya mlango. Akaingia ndani, akafunga mlango, ndipo akaiokota. Hapohapo akampigia Joshua. “Vipi?” “Aisiee ipo. Sijafungua bado, naona uje kwanza ili ufungue mwenyewe.” “Nashukuru sana GM.” Joshua akatoka chumbani kwake kwa haraka kwani hakuwa hata amekaa.

Alipoingia tu, Geb akamkabidhi. Joshua akaipokea na kufungua kwa haraka. Akamuona anasoma mpaka mikono inatetemeka. Geb akabaki kimya akimtizama tu. “Mungu wangu saidia.” Akasikika Joshua, macho kwenye huo waraka. Akaenda kukaa kabisa kitandani kwa Geb, akaendelea kusoma. Ilikuwa ndefu na imechapishwa. “Naya anaweza kurukwa na akili. Mungu saidia!” Joshua akaongea na kumkabidhi Geb na yeye asome. “Lazima tuondoke sasa hivi Geb. Tafadhali sana. Tuanze na baba Naya kwa haraka. Huwezi jua tutaokoa nini! Maadamu tumeshajua Bale alipo, basi tutajua nini chakufanya naye, baada ya kumpata baba yake.” Joshua akaongeza wakati Geb naye akisoma.

Geb akasoma mpaka akamaliza. “Naona ni wazo zuri.” Akaafikiana na wazo la Joshua baada yakumaliza kusoma. Hata yeye alionekana ameingiwa hofu. Akawapigia simu wale askari waje na wao. Kama waliokuwa wakisubiri mahali, wakaingia wote kwa pamoja. Akamkabidhi Gamba. “Naomba uisome kwa sauti.” Geb akamkabidhi Gamba ile karatasi. Gamba akaanza kuisoma. Ilijawa kujihami kwingi ila huyo mwandishi alisema ni fununu wamepata kuwa kijana wa huyo mzee alikamatwa akiwa anavusha mali ya magendo huko mpakani. Mara ya mwisho yeye na vijana wengine wa kitanzania walikuwa jela ya mpakani mwa Zambia na Mbeya, lakini utaratibu wa kuhamishiwa jela ya Mbeya ulikuwa ukiendelea. Hakuna anayejua zaidi. Mwandishi alisema kuhusu mzee wake, kwa kuwa tokea afike hapo kwenye huo mji alianza kwa maswali na kutisha wenyeji, ndio maana hakuna aliyeweza kumpa hata fununu ila kuchukuliwa na kutolewa kwenye mji wao. Amesogezwa mji wa karibu na Mbeya ambako ni kama msaada wakumsogeza kwa kijana wake. Wakaelekezwa sehemu ziliposikika fununu kuwa alikwenda kuachwa.

“Sasa sisi huu mji hatuufahamu. Nashauri turudini palepale kituoni. Tuwaambie kiuungwana kwamba tumepata Msamaria mwema, ametupa sehemu ambayo huyu mzee anaweza kuwepo. Tuwaonyeshe hii karatasi na tuombe askari anayejua huu mji na vijiji vyake, zaidi anayejua hii sehemu iliyotajwa hapa, aongozane nasi.” Wote wakatulia. “Tukifanya haraka kuondoka hapa tukakimbilia sehemu tusiyoijua, kwanza tutapoteza muda, na kama tuna nafsi ndogo ya kuokoa, tutapoteza kwa sababu itatubidi turudi tena hapahapa endapo tukikwama huko. Au mnaonaje?” Geb akamtizama Joshua. “Naona wazo ni zuri. Nawashukuru sana.” Joshua akaafiki na kushukuru akionekana akili ilishaanza kuwaza kwingine zaidi.

Baada ya muda mfupi, kila mmoja akawa yupo garini na mizigo yake. Ndio wanaondoka hapo hotelini moja kwa moja. Geb akakanyaga mafuta kurudi kituoni. Safari hii wote walishuka wakijua hawana cha kujificha tena. Wanajulikana wapo wanne. Walipofika kituoni Gamba akawa muungwa. Akashukuru wakazi wa huo mji kwamba wametoa ushirikiano mzuri, wamewapa huo waraka. Akamkabidhi Mkuu wa kituo ambaye chakushangaza bado mida hiyo alikuwepo tu kituoni na askari wengine wengi tu kama waliokuwa wameitana. Na walipoingia hapo kituoni wakasababisha ukimya wa hali ya juu. Ila kwa kadiri Gamba alivyokuwa akizungumza nao, wakaanza kutulia.

Chakushangaza na ambacho hawakutegemea, askari watatu wa pale kituoni wakakubali kuongozana nao ili kusaidia, tena kwa usafiri wao wenyewe, wasitumie gari waliokuja nao kina Geb. “Ili msipate shida ya kuridi tena huku.” Kama waliokuwa wakiwafukuza kwenye mji wao. “Hata hapo mtakuwa mmetusaidia sana. Na sisi hatutawasahau. Huo wema wenu utakumbukwa hata kwa Wakubwa. Ila kabla hatujaondoka, nitachukua majina kamili na namba za utambulisho wa hao maaskari, na kuziripoti juu.” Gafla pakazuka ukimya tena.

Ila kwa Geb na Joshua wakapenda hilo wazo la Gamba isijekuwa ni njama ya kuwatoa hapo na kuja kuwageuka mbeleni. “Ni kwa usalama wao pia. Sisi tunajulikana kama tupo hapa. Huu waraka umeshatumwa kwa viongozi. Hiki mnachotaka kutusaidia, ni kujitoa kwa hali ya juu. Sasa lazima ijulikane ni nani yupo safari moja na sisi kwa chochote kitakachotokea.” “Basi tunaomba mtupishe, tujipange.” “Sawa Mkuu. Sisi tutakuwa garini tukiwasubiria.” Gamba akakubali bila shida na kuwaambia wenzie watoke.

Naya.

Simu kutoka kwa Naya ikaanza kuita. Joshua akafikiria ndipo akapokea. “Vipi?” “Naomba nivumilie Joshua. Nahisi nimejawa tu wasiwasi. Nikizungumza na wewe angalau napata utulivu.” “Naelewa kabisa. Tuendelee kuomba Mungu, kila kitu huku kinaendelea vizuri. Nipe masaa machache tena, pengine naweza kukueleza kinachoendelea kwa hakika.” “Mpaka sasa hamjasikia chochote?” “Wamejawa tu hofu. Na watu wenye hofu wanaweza kuzungumza chochote kile kujitetea. Sasa kusikia ni jambo moja, ila kutendea kazi tulichosikia na kufanikiwa, nafikiri hiyo ndio habari. Naomba ongeza subira tena kidogo. Sisi tupo macho mpaka sasa, tukimtafuta baba na Bale. Tuamini tu.” Joshua akawa makini na kila taarifa anayompa Naya.

 “Nawashukuru sana Joshua. Asante. Na namsihi Mungu pia anirudishie wewe salama. Naona Geb bado anaendelea na mipango ya harusi kama kawaida. Nanaa ameniambia Geb amesema chochote kisibadilike.” “Naona ameamua kuniweka mimi pembeni. Katika hilo hanihusishi kabisa. Tuache tuone mambo yanavyokwenda. Tusiwakatishe tamaa. Amini siku ya harusi, sisi tutafunga ndoa.” “Na baba atakuwepo, pengine na Bale kama hatakuwa ametuziria.”

“Iwe kama unavyonena. Naomba nikuache mpenzi. Kuna sehemu tunakwenda.” “Nakuombea.” “Sawa. Lakini naomba ulale, usisubiri.” “Siwezi Joshua. Mpaka na wewe ukiwa kitandani ndio nitajua hiyo siku tumeimaliza pamoja. Usiwe na wasiwasi. Sijachoka. Nipo tu hapa nyumbani. Na kesho ndio mambo ya saluni yanaanza. Mama G atakuja kunichukua, mida ya saa tano asubuhi. Kwa hiyo nipo sawa, hata nikichelewa kulala, nitachelewa kuamka. Usiache kunipigia. Ujue nakusubiria.” “Sawa.” Joshua akakata simu na kuingia garini wenzake walipokuwa wamekaa wakiwasubiria hao askari wenyeji.

Ikiwa Zimebaki Siku 3.

Zikiwa zimebaki siku tatu ndoa ya Naya na Joshua ifungwe, bado bwana harusi alikuwa Tunduma akimtafuta mkwewe, bibi harusi simu mkononi akisubiri taarifa za baba yake na akimfuatilia mchumba akiomba Mungu amrudishie salama. Wasimamizi wa harusi, kina Magesa, waliendelea na maandalizi ya harusi kama kawaida. Kwa kuwa walishakubaliana ndoa lazima ifungwe tu, ila aina ya sherehe ndio itategemea. Na kwa kuwa kina Magesa walishapata maelekezo kutoka kwa baba Naya kwamba harusi isisimame, basi wao wakaendelea kama kawaida.

Baada ya lisaa magari mawili yalikuwa yakiacha mji wa Tunduma kuelekea ambako waliambiwa baba Naya anaweza kuwepo. Geb alikuwa makini kulifuata hilo gari la polisi kwa nyuma. Geb na Joshua wao kimya, ila Gamba na Chui ndio waliendelea kuongea hili na lile mpaka mwisho na wenyewe wakaishiwa maneno. Wakaanza kusinzia, bado safari ilikuwa ikiendelea, tena kwa mwendo kasi bila kusimama wala kupunguza mwendao. Naye Geb hakutaka kuwapoteza, alihakikisha anaendesha kwa mwendo wao.

          “Nahisi tunarudi Mbeya.” Geb akamwambia Joshua ambae alikuwa kimya tu pembeni yake. Joshua akamgeukia. “Nimehisi kutokana na upande tunaoelekea.” “Sikuwa nimezingatia kabisa! Mawazo yapo mbali.” “Naamini kila kitu kitakwenda sawa. Acha tufuate tuone na wao watatufikisha wapi.” Geb akajaribu kama kumtuliza. Kimya kingine kikaendelea.

Kwa Naya.

Mkakati wa Kukomboa familia kabla ya harusi, unaendelea. Akamuona anatoa simu. Akajua anampigia Naya. “Joshua!” “Hujalala tu!?” Joshua akashangaa jinsi alivyopokea simu kwa haraka. “Siwezi. Nimekwambia mpaka wewe ukiwa kitandani unalala na mimi ndio nitahitimisha siku.” “Sasa unafanya nini?” “Nilikuwa naweka sawa mahesabu ya dukani kwa baba. Napitia bei zake. Mauzo kwa kila kipimo. Kwa kifupi kuelewa kwa undani hii biashara. Zayoni ataanza shule baada ya muda mfupi. Sitaki kujikuta...” Akamsikia amesita anaanza kulia.

          “Naomba usilie Naya.” “Naogopa Joshua. Naogopa sana. Iweje msimpate baba yangu? Au mumpate akiwa amekufa!” “Pole mpenzi wangu. Tuendelee kumuamini Mungu.” “Mungu hapotezi Joshua! Lakini sisi ndio tutapoteza. Pengo la baba haliwezi kuzibika kwetu kama la mama. Maisha yanaendelea, lakini pengo lake mpaka leo halijawahi kuzibika. Naogopa sana.” “Pole Naya. Ila sikutaka kukupa matumaini ambayo sina uhakika nayo. Lakini kuna fununu anaweza kuwa kwenye mji fulani hivi. Mpakani mwa Tunduma na Mbeya. Ndiko huko tunaelekea sasa hivi.” “Joshua!” Naya akahamaki. Ndipo Joshua akamuelezea kila kitu.

          “Nimepiga picha hii barua. Sikutaka kukutumia kwa haraka. Na nimepiga picha hiyo gari inayotupeleka huko. Sasa hivi tupo njiani, wao wanatuongoza. Majina ya askari wawili miongoni mwa hao wanne waliopo kwenye gari pia nimeandika. Sikutaka kukutumia kwa haraka. Ila acha nikutumie kama tulivyofanya kwa mzee, ikawa rahisi kutusogeza.” “Nina wazo.” Naya akaanza akisikika kusita kidogo.    

          “Ni nini?” Joshua akauliza. “Unakumbuka nilikueleza habari juu ya kaka Mati? Yule mwanasheria aliyenisaidia kumtafuta Malon!” Joshua akatulia. Naya akaendelea. “Nilikuwa sijui ni wapi au jela ipi Malo alifungwa. Ila tu mji. Kaka Mati akaenda kupeleleza mpaka akajua alifungwa wapi. Ilinigarimu, lakini alisaidia sana mpaka akamtoa na jela. Nashauri kama huna mtu unayemfikiria kwa haraka, basi tumtumie yeye. Anaonekana anao uzoefu na analeta matokea yakueleweka.” Joshua akatulia kama anayefikiria.

          “Naomba usiwe na wasiwasi. Ni mtumzima na anajiheshimu.” “Ni sawa. Sio wazo baya.” Joshua akaweka kituo akisikika kama kuna kitu angeweza kuongeza zaidi, lakini akasita kukisema. Wakatulia kwa muda. “Joshua?” “Nipo.” “Nashukuru sana mpenzi wangu na poleni. Mungu azidi kukubariki. Mfikishie Geb shukurani zangu za dhati. Najua ameacha familia yake huku na majukumu yake sasa hivi yuko huko maporini! Hakika Mungu amlipe zaidi na zaidi mpaka ajue amebarikiwa.” “Amina. Atasikia.” Geb akajua ametumiwa salamu tena.

          “Na taarifa pia za hilo gari mnalotumia sasa hivi hujanipa Joshua.” “Kweli. Acha basi nikutumie hizi nilizonazo kwanza, kisha nimuulizie Geb. Sijachukua namba za hili gari.” “Nawaombea.” “Amina. Ila hicho unachofanya ni sahihi kabisa. Hamisha hayo mawazo ya hofu, weka kwenye kitu cha msingi. Ili uwe ushuhuda wako siku moja. Huu usiku shetani alitaka autumie kwa hila, ila iwe kwa manufaa kwako. Usipoteze kabisa.” “Sawa. Usiache kuwasiliana kila wakati.” Joshua akacheka na kuafiki.

Aluta Kontinua.

          Baada ya mwendo mrefu wakutosha, giza nene maana walikuwa wakipita msituni wala si kwenye barabara kubwa yenye lami, ndipo wakafika kwenye kijiji. Waliweza kutambua mashamba na nyumba chache tu, kwa sababu ilikuwa usiku na hakuna taa. Simu ya Gamba ikaanza kuita. Akapokea kwa haraka. “Mliahidi hakuna kesi wala mjadala. Tumewasaidia na kuwafikisha mpaka hapa. Inavyosadikika mzee wenu ameachwa kwenye kituo kidogo cha magari ya abiria, yatokayo hapa kijijini. Mkifuata hii barabara kwa mwendo mfupi kidogo tu, mtaona kituo chenyewe. Kwa hali yeyote mtakayomkuta nayo huyo mzee, sisi hatuhusiki kabisa. Tumewasaidia kusaka habari zake mpaka kuwafikisha hapa. Kitakachoendelea baada ya hapa, sisi hatuhusiki. Tunaomba amani kwenye mji wetu.” Simu ikakatwa.

Wakati Gamba anawaambia juu ya hiyo simu, wakashangaa hiyo gari inakata kona. Geb kwa haraka akataka kuifuata lakini Gamba akamkataza. “Hao wanarudi Tunduma. Ameniambia sisi twende moja kwa moja mpaka tukute kituo kidogo tu cha mabasi.” Akamalizia kuwaambia ujumbe aliopewa kwa simu muda mfupi uliopita. “Maisha yameharibika sana. Watu tunaotegemea walinde raia ndio wanahusika kwenye kuwaangamiza!” Akalalamika Joshua. “Maana hawa waliotuleta mpaka hapa, inamaana mmoja wao au wawili wao wanahusika kumteka baba Naya. Kwa asilimia zote bila kupinga.” Akaongeza Geb.

“Lakini tuliwaahidi jamani! Naomba tusiwageuke. Haya mambo yapo halafu kuna leo na kesho, tunaweza kukutana nao mahali, tukahitaji msaada wao. Ni bora wao ndio wabakie tunao wadai, ili kuweka mazingira yakuja kuwatumia tena wakati mwingine, kuliko kutengeneza uadui.” Geb na Joshua wakanyamaza, wazi walitamani haki itendeke. Waadhibiwe waliofanya huo uovu. Lakini wakajirudi kwa hofu.

 Kwanza wakakumbuka wapo na askari kama hao wa Tunduma hapo garini. Wale askari hata kama iweje, wale ni wenzao tu. Pili hawakuwa wakijua kama kweli watamkuta huyo baba Naya! Wasije haribu, wakati hata baba Naya mwenyewe hawajampata. Kingine wanamlaumu nani? Bale si mtoto mdogo. Kwa hiyari yake, tokea anatoka kwa Malon huko Mbeya, alitahadharishwa madhara ya biashara atakayokwenda kufanya, lakini akakubali kwenda kufanya. Hata kama ni kwa kurubuniwa kwa ahadi za uongo, lakini alikubali kwenda. Wakawa wapole, Geb akiendelea kukanyaga mafuta. Safari hii kila mtu macho nje kuangalia kama wataona hicho kituo.

Baada ya kama dakika kumi hivi, wakipita kwenye barabara mbaya haswa, mashimo na vumbi jingi tu, ndipo wakaona eneo linalofanana kama kituo cha mabasi. Giza nene, hakuna hata taa. Geb akasogeza gari kabisa  mpaka karibu kabisa na hicho kituo. Kulikuwa na vibasi vidogo na pickup za mizigo, chache, zimeegeshwa. Wote wakatoka garini. Kila mmoja akawasha simu na kuanza kuzunguka huko na kule pengine watamuona baba Naya.

Mapigo ya moyo yakienda kasi kwa hofu. “Anatumia jina gani?” Gamba akauliza ili kuweza kumuita kwa sauti. “Sidhani hata kama yeye mwenyewe anakumbuka jina lake ila baba Naya. Kila mahali, kila mtu anamuita baba Naya, na yeye mwenyewe anajitambua hivyo.” Joshua akaongeza wakiendelea kumsaka wakitumia mwanga wa simu zao.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kazi ya kumsaka baba Naya inaendelea huku wakiwa hawana hakika alipo Bale, ila fununu tu. Je, yaliyoandikwa kwenye waraka waliokuta chini ya mlango, chumbani kwa Geb, ni ya kweli au wametolewa tu mjini Tunduma?

Itaendelea........

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment