Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 33. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 33.

Geb akarudi garini ili kusogeza gari karibu zaidi kumulika vibandani, waweze kutumia mwanga wa gari huku wale polisi wakimuita baba Naya. Joshua akaingia kwenye moja ya kibanda. Akamkuta amelala chini kabisa. “YUKO HAPA.” Akapiga kelele kwa sauti, Gamba akawa wakwanza kufika. Akamwangalia na kumshika. “Ni wa moto kabisa, na anamapigo ya moyo. Yupo hai.” Geb akasogeza gari. Baba Naya alikuwa akinuka sana mikojo, kama aliyejikojolea.

Gamba akaanza kumtingisha akimuita. “Nashauri tutokeni hapa, tukatafute hata dispensary, aweze kupewa huduma ya kwanza.” Joshua akatoa hilo wazo baada ya kuitwa mara kadhaa asiitike. Wakatoka hapo, hawajui waendako wala walipo. Ila Geb akasema alielewa upande waliokuwa wakipelekwa mpaka kufika hapo, na upande upi ni Mbeya kutokana na alivyoendesha tokea wanashuka uwanja wa  ndege mpaka Tunduma. Wakamuacha aendeshe kwa vile anavyojua. Kila mtu kimya.

Joshua akakumbuka kumpigia simu Naya kumpa habari njema. Akampigia. “Tupo na Mzee hapa.” Naya akaanza kulia. “Nipe nizungumze naye.” “Hajazungumza chochote. Hapa yupo dirishani, tumemfungulia dirisha ili apate hewa. Tunatafuta hospitali.” “Amefungua hata macho?” Naya akauliza akijaribu kutulia. “Kulikuwa giza sana. Hiki kijiji chenyewe ni giza, hakuna hata umeme! Hatuonani.” “Cha kwanza baba hajala. Alikuwa amefunga. Na nina uhakika huko alipokuwa amefungwa, hawajampa chakula. Inawezekana amechoshwa na njaa pia, japo hatujui ni mazingira ya namna gani alikuwepo. Naomba muweke simu sikioni. Tafadhali Joshua.” “Haongei Naya.” “Wewe weka tu simu sikioni kwake na uongeze sauti.” Joshua akafanya kama alivyoomba Naya.

“Ongea Naya.” “Huyo ndio Naya wa baba Naya?” Akauliza Chui. “Ndiye huyo.” “Baba!” Naya akanza kuita. “Baba Naya?” Naya akaita tena akijaribu kutulia kutoa sauti ya kilio. “Pole baba yangu, pole sana. Una maumivu kokote?” “Nimehisi kama ametingishika!” Gamba aliyekuwa amekaa pembeni yake, akahamaki. “Joshua, washa taa ya juu ili tumuone.” Geb akatoa wazo.

Wakawasha. “Haya, Naya, muulize tena.” Joshua akamwambia Naya. “Baba! Baba Naya? Unanisikia?” Naya akarudia. Akatingisha kichwa kukubali. “Ameitika.” Wote walikuwa wakimwangalia yeye kasoro Geb aliyekuwa akiendesha. “Muulize tena kama yupo na maumivu.” Joshua akataka Naya ndio aulize huku akimwangalia baba Naya, lakini akatingisha kichwa kabla Naya hajamuuliza. Hapo Joshua akaridhika. “Pole mzee wangu.” “Asante. Asanteni.” Akaongea kwa sauti ya chini lakini wakasikia. “Maumivu yapo wapi?” Joshua akauliza. “Nyuma ya kichwa. Nahisi walinipiga hapo kwa nguvu. Ila njaa ndio inanisumbua. Sijala kwa siku nyingi.” “Pole baba.” Naya akawa amesikia.

“Nina wazo.” Akasikika Gamba. “Tutafuteni nyumba yeyote ile, tuombeni chai ya rangi. Mzee haonekaniki kama ni mgonjwa wa kukimbiza hospitalini kwa haraka ila anahitaji chakula. Tunaweza kukimbilia hospitalini, tukajikuta tunawekwa hapo kwa muda mrefu halafu na bado tusipate msaada kwa haraka. Ila mzee akipata chai ya rangi, akaja kupata chakula, ndipo akapelekwa hospitalini kwa uchunguzi, hata wakituweka hapo kwa muda mrefu, haitakuwa shida.” “Wazo zuri.” Joshua na Geb wakajikuta wamekubaliana kwa pamoja.

Walishatoka kwenye kile kijiji walichompata baba Naya, wakaona wasirudi nyuma waendelee mbele. Bado Naya alikuwa kwenye simu. “Joshua?” “Nakusikia Naya.” “Nawashukuru sana. Naomba waambie wote nawashukuru halafu muwekee simu tena baba.” “Jamani! Naya anawashukuruni sana.” “Karibu Naya wa baba Naya.” Chui akaitika yeye wakwanza nakufanya wengine wacheke kidogo. “Naweka simu sikioni kwa baba, japo amechoka sana.” “Naongea naye kidogo tu, na Zayoni anataka kumsalimia halafu tutamuacha apumzike mpaka ale.” “Haya, naweka simu masikioni kwake.” “Baba? Nimefurahi sana. Nilikuwa nakuombea.” “Asante mama.” “Na mimi baba, ila mimi nilikuwa naogopa. Nilijua hutarudi tena. Unaumwa?” “Kidogo tu. Njaa zaidi.” “Joshua atakupa chakula. Pole baba.” Zayoni akafanya mle garini wacheke. “Asante Zayoni.” Akaitika baba yao. “Usilie Zayoni. Tutamtafutia chakula, atakula. Tukiona asubuhi yupo salama, tutarudi naye wakamwangalie hali yake hukohuko Dar hospitalini.” “Yesss!” Wakamsikia Naya akichangilia pembeni. “Na mimi nilikuwa nikifikiria hivyohivyo. Endapo atakula nakujisikia vizuri, tuondokeni. Matibabu yakaendelee kwenye hospitali tunazozijua.” Geb akaongeza. Wakakubaliana hivyo, ndipo kukaanza kazi ya kusakwa nyumba yeyote ile waingie na kuomba msaada.

Geb aliendesha kama baada ya lisaa ndipo wakaona tena kijiji kingine, lakini kila mtu alimpongeza kwa uwezo wakuweza kuwatoa maporini na kuwafikisha barabara kubwa ya lami. Na hilo eneo lilionekana ni kama kijiji chenye maendeleo kwani kulikuwa hata na umeme. Geb akasogea mpaka kwenye nyumba ambayo ilikuwa karibu kabisa na barabara. “Nashauri sisi ndio tukagonge.” Akashauri Chui. Akimaanisha wao askari. Wakakubaliana, wao wawili wakashuka.

“Nasikia baridi sana.” Wakamsikia baba Naya akiongea kwa sauti ya chini. “Nafikiri nina koti zito kwenye begi langu. Joshua akashuka kwa haraka. Akashangaa na Geb anashuka. “Ukimpa mzee koti, tuzungumze kidogo.” “Sawa.” Akalipata koti lake kwa urahisi tu ndani ya begi lake, nyuma ya gari. Akaenda kumvalisha, wakapandisha kidogo kioo, ndipo wakajitenga ili wazungumze wakati kina Gamba na wenzie wakigonga kuomba msaada.

“Nimefikiria. Kwa kuwa ni kama tumepata fununu za Bale, nashauri huyu askari kanzu, Chui, tumuombe yeye arudi huko mpakani kunakosemekana anaweza akawa amefungwa huko Bale. Wakusanye taarifa zozote zile juu yake ndipo tujue nini chakufanya kuanzia hapo.” “Wazo zuri, lakini naomba zungumza na Gamba, kama anaweza kuongozana naye. Anaonekana anao uelewa mkubwa sana wa haya mambo.” “Sidhani kama itawezekana, kwakuwa ni kama Gamba ametingwa na majukumu mengi mno. Hapa yupo kwa kulipa fadhila tu. Ila aliniambia wazi yupo na majukumu mengi sana. Isingekuwa ni mimi, hiki sio kipindi angesafiri, kuwepo nje ya ofisi.” Geb akafikiria kwa haraka.

“Naweza kumuomba amsimamie Chui kwa simu bila yeye kuwepo huko. Awe ni mtu ambaye anamuongoza kwa karibu na  awe anaripoti kweke kwa simu.” “Sio wazo baya. Ila Geb, nakushukuru sana. Asante sana.” “Tupo pamoja na ndio mambo ya familia yalivyo. Mimi nimeshazoea kwa sababu nimekuwa nikizungukwa na familia wakati wote. Inachukua muda sana kuiweka familia pamoja, ila nikwambie kabisa, ndio maana nzima ya maisha. Baada ya hili, utakuja kuniambia, hawawezi kukutizama kama Joshua anayeoa kwao. Ila Joshua wanayemtegemea kwa karibu sana. Hakuna litakaloendelea kwenye familia yao bila baraka zako. Si kwa pesa, ila kwa umbali uliokwenda kwa ajili yao. Na ndivyo Mungu anavyofanya. Hakupi kitu  kikubwa kabla hajakujaribisha na kuona kama unao uwezo wa kukimiliki.” “Yaani na mimi nilifikiri hivyohivyo aisee! Ila kwangu huyu Mungu amezidisha jamani!” Geb akacheka.

“Kweli Geb! Mimi mpaka huwa namwambia, ni kwa nini anapenda kunijaribu katika kila hatua au ngazi anayonipandisha? Mbona ni kama nishamuonyesha kuwa nina uwezo!!” “Njia zake si zetu. Na mimi huwa ananijaribu hivyohivyo, namwambiaga Nanaa kabisa. Hili ni jaribu langu kwa sababu nimemuomba Mungu kitu. Nilishamjua. Huwa ananipitishaga sehemu mpaka huwa nabaki kucheka tu, na kwa kuwa najua ni yeye, huwa namuomba hekima na uwezo.” Wakasikia mwenyeji mwanaume akizungumza na kina Gamba. Wakasogea na wao. Wakakaribishwa ndani, na mkewe naye akaamka.

Uzuri walikuwa na jiko la mafuta ya taa. Mama huyo akaliwasha kwa haraka. Geb na Joshua wakaenda kumchukua baba Naya. Wakamuweka kitini na kumfunika. “Samahani kwa usumbufu aisee.” “Msijali kabisa.” “Baada ya chai, kama tungeweza kupata na maji moto ili kumsafisha kidogo, ingekuwa msaada sana.” “Bila shida.” Akaitika mkewe huko jikoni. Wakakaa hapo sebuleni. Sebule yenyewe ilikuwa ya kawaida sana, lakini ikaongezwa umaana na ule ukarimu wao. Geb na Gamba wakaanza kuzungumza. Wakaweka mipango hapo. Chui akakubali kwa haraka sana. Akajua kwake ni kuongeza pesa. Lakini wawili hao wakakubaliana wajipe siku mbili mbeleni ndipo warudi Dar pamoja. Wakamwambia Geb walishazoea kufanya kazi pamoja na wakati wote wakiwa pamoja hufanya kazi kwa haraka. Hilo likamfurahisha Joshua zaidi ambaye aliamini zaidi akili ya Gamba. Ndipo wakamgeukia mwenyeji wao kuulizi magari yaendayo mpakani. Mpaka baba Naya anawekewa chai, mipango ya kuanza kumsaka Bale ilishakuwa imekamilika.

Joshua akamsogelea. “Nikusaidie kukunywesha?” Baba Naya akafungua macho. “Asante, lakini nafikiri nitaweza tu. Acha nijaribu.” Joshua akamsogezea ile chai karibu. Akaanza kunywa taratibu tu. Alipomaliza Joshua akamuuliza. “Unajisikiaje?” “Maumivu tu hapo kichwani na huu mkono. Walinipiga ule usiku walionichukua wakitaka kunitoa taarifa kama kunitisha tu. Hakikuwa kipigo kibaya sana. Ila nahisi huu mkono, zaidi bega ndio limedhurika na hapo kichwani.” “Pole sana.” “Ila nashukuru sana. Nahisi mmewahi kuniokoa. Lasivyo wangenidhuru zaidi kama kupoteza ushahidi.” Wote wakasogea karibu kusikiliza.

“Sina mengi sana yakueleza maana walinifungia sehemu ambayo ilikuwa giza. Sikujua nilipo ila sauti tu nje wakishauriana kitu chakufanya na mimi. Walinipiga siku ya kwanza tu. Wakitaka kunifahamu. Ila baada ya hapo ndipo ikawa kushauriana, ila nafikiri walikuwa wakipokea maagizo kutoka kwa Mbabe. Nilisikia wakimtaja na wakiambiana inabidi kumuuliza nini chakufanya na mimi baada yakujiridhisha mimi sio askari mpelelezi. Inavyoonekana Mbabe hapendi au hataki kuua. Anakanuni yake inayosema damu ya mtu mkononi mwake ni mkosi na hataki afuatwe na damu ya mtu ila pesa tu. Kwa hiyo nafikiri waliafikiana wakanitupe porini, mimi mwenyewe ndio nitafute njia yakutoka au kama kuna baya litanipata, sio juu yake.” Baba Naya akaongea taratibu tu.

“Ila sasa wakati nimelala, nikasikia wakiogopeshana nje kuwa mtoto wangu amekuja na watu wa usalama, na wakuu wa nchi wananitafuta. Mbabe ameshauriwa na polisi lazima anitoe. Ndipo sasa nikaja kuachwa pale mliponikuta.” “Pole sana.” Wote wakampa pole. “Katika mazungumzo yao, umesikia wakisema chochote juu ya  Bale?” Joshua akauliza. “Ni kama waliokuwa wamejionya juu ya hilo. Walikataa hata kumtambua.” Akajibu baba Naya. “Sisi tumepata habari zake kwa sehemu.” Joshua akamsimulia baba Naya juu ya Bale kutokana na ujumbe walioachiwa chini ya mlango wa Geb, hotelini.

“Ndio nimesikia mkiweka mipango hapo?” Geb na Joshua wakaangaliana. Hawakujua kama alikuwa akiwasikiliza, alikuwa amefunga macho muda wote. “Samahani mzee wangu. Naona tumeweka mipango bila kukushirikisha.” “Hata kidogo. Nyinyi endeleeni tu. Ila mjue nawashukuru sana.” Hilo likapunguza wasiwasi. “Karibu.” Geb naye akaitika. Maji yakawa tayari bafuni. Joshua akatafuta hekima yakumwambia baba mkwe aende akaoge abadilishe nguo zinazonuka.

“Wakati anaoga, nitatengeneza uji.” Huyo mama akawa mkarimu zaidi ya walivyoomba. “Tunashukuru sana.” Geb akaongeza. “Ungependa nikusaidie?” Joshua akauliza. “Labda kunisindikiza mpaka bafuni. Bado nahisi kizunguzungu.” Joshua na Geb wakamsaidia kusimama. “Mkono huo wa kushoto upo na maumivu makali sana.” “Basi kitakushika upinde wa suruali.” Baba mwenye nyumba akamuwekea kiti huko bafuni. Baba Naya akajisafi akisaidiwa na Chui, Geb alimnong’oneza akimuomba yeye ndio aingie bafuni amsaidie kwa kuwa wao ni kama wakwe. Joshua alimpa suruali yake. Akatoka akiwa angalau msafi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Waliwaombea hao askari wawili wabakie hapo ili wasubiri kukipambazuka, waweze kuchukua usafiri wakuelekea mpakani mwa Zambia na Mbeya. Wao wakaendelea na safari kurudi Mbeya mjini, usiku huohuo, wasogee karibu na uwanja wa  ndege. Baba Naya alishakunywa uji na dawa ya maumivu, akapotelea usingizini akiwa amevaa suruali ya Joshua. Simu ya Naya ikaingia. “Umenisahau mpenzi wangu!” “Hapana. Ila nimeona mzee amechoka na alikuwa na maumivu. Amelala.” “Ameweza kuzungumza?” “Ameongea. Kilichokuwa kikimsumbua zaidi ni njaa. Ila tunarudi naye ili aje aangaliwe hukohuko. Naomba ulale Naya.” “Basi nionyeshe hata kwa video tu nimuone.” Naya akasihi akimbembeleza.

“Ni giza, na amelala nyuma! Tunakopita ni giza, hata kwa video hutamuona, Naya. Naomba ulale kesho mapema tu tutakuwa Dar.” “Acha nizungumze naye, ili atulie.” Wakamsikia baba Naya akiongea. “Basi nakupa baba, ameamka.” “Asante Joshua, na samahani kwa usumbufu.” “Usijali. Mimi ndio nilikuwa nikikuhurumia wewe. Nakupa baba.” Akamkabidhi. “Baba Naya?” “Nipo mama mzazi. Nimekula, najisikia vizuri. Usiwe na wasiwasi.” “Maumivu ni ya wapi?” “Naona waliniumiza mkono huu wa kushoto na nyuma ya kichwa. Ila vinginevyo nipo mzima kabisa. Hapa nilikuwa nimelala, mpaka nilipokusikia ndio nimeamka.” “Pole baba.” “Acha kulia. Si uliniombea nirudi nyumbani?” Kimya, Naya akiendelea kulia.

“Ndio narudi nyumbani.” “Pole baba.” “Mimi nipo sawa. Mambo yote yakienda sawa, nitakuona hivi karibuni.” “Nitakuwa nakusubiria uwanja wa ndege. Mimi na Zayoni.” “Kumbe una mipango mizuri tayari! Basi ulale ili ukiamka uwe na akili iliyotulia.” Akamsikia akicheka taratibu. “Ujue nakusubiria!” “Najua mama. Najua. Zayoni yuko wapi?” “Mwanao muoga huyo! Amelala hapo chumbani kwangu. Imenibidi kutoka, ili nizungumze na wewe. Alikuwa hapo kitandani kwangu. Itabidi nikalale kwenye kitanda cha Bale.” “Bora ukalale kitandani kwa Bale si kwake, ili usimchafulie mashuka yake.” Wakacheka maana Zayoni hutandika mashuka meupe kitandani kwake. Kidogo wakacheka.

“Wewe ukiamka nipigie.” “Naomba ulale Naya.” “Nimesema ukiamka baba jamani!” “Hapana. Wewe ukitulia huko ujue na mimi huku nitalala. Naomba acha wasiwasi. Si umenisikia mimi ni mzima?” “Basi nalala, baba. Ila nikiamka nitapiga tena.” “Najua hutalala Naya. Utatulia masaa mawili kisha utapiga tena. Naomba ulale kabisa, upumzike. Nataka ulale, utulie. Au hauhesabu tena siku?” “Nilipoteza mahesabu walivyokuchukua. Ila sasa hivi naanza tena. Naolewa na Joshua, mwenzio.” Wakamsikia baba Naya akicheka.

“Na leo ulijaribisha gauni?” “Nanaa amekuja kulichukua mwaya! Anasema nitalichafua, niache mtindo wakulivaa kila saa!” Mpaka Geb akacheka, ndipo wakajua wanasikiliza. “Nimelimisi gauni langu!” “Yamebaki masaa mangapi ulivae rasmi?” “Kesho ukija nitakupa mpaka dakika. Acha nilale nitulize akili. Nilikuwa nalia mwenzio. Nalia kila saa.” “Nakujua.” Naya akasikika akicheka. Wakaongea kidogo na baba yake akasikika kutulia. Akamrudishia simu Joshua.

“Sasa hivi hata ukiniambia nilale, nitalala kama mtoto mchanga.” “Nimekusikia.” “Nimefurahi sana. Nimeongea na baba Naya, mwenzio! Siamini!” Joshua akacheka. “Kwa hiyo na leo nitegemee kukoroma.” Naya alicheka sana. Akasikika amefunguka kabisa. “Nakuweka mute, Joshua.” “Ili nipitwe!” “Bwana Joshua!” “Wewe koroma tu.” “Kwanza nishasahu siku hizi huwa watu wanakoromaje.” Joshua alicheka sana mpaka akajisahau kama yupo na watu karibu

“Mwenyewe Naya huyo!” “Oooh kabisa. Naya huyu huwa hakoromagi.” “Basi usiweke mute.” Naya akacheka sana. “Umejuaje?” “Najua janja yako. Unaweza ukaweka mute, nikasema hujakoroma, kumbe huko Zayoni anakesha!” Naya alicheka sana. Angalau Naya akatulia na kweli akalala, Joshua akimsikiliza. Huku ameweka na yeye mute ili asiwasikie pale garini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Geb aliendesha mpaka wote wakapotelea usingizini, wakamuacha yeye peke yake. Yeye ndio alizijua hizo pande za dunia alizokuwa akizifuata. Hakuna aliyemuelewa wala kujua hapo ni mashariki au magharibi. Lakini yeye alionekana kuelewa. Wakati akiendesha simu yake ikaanza kuita. Ilionyesha Nanaa. Akakunja uso, hakumtegemea muda huo. Akapokea kwa haraka. “Vipi?” “Mimi nalia dad!” Alikuwa Magesa. “Kwa nini tena unalia usiku huu wewe niliyekuachia familia yangu?” “Mbona hurudi sasa? Kwani ‘muda si mrefu’ ni masaa mangapi? Maana sasa hivi ni masaa.” Akamtajia mpaka na dakika baba yake alizoondoka nyumbani. Geb akajua ameamka usingizini, mida hiyo ya alfajiri lazima aamke ale ndipo aendelee kulala, akaangalia saa akagundua ni mapema zaidi ya muda wake.

“Muda si mrefu, inategemea Magesa.” “Na nini?” Akauliza. “Na umbali au kitu au jambo. Wakati mwingine ni ngumu kutabiri muda kamili.” “Mimi nalia dad. Muda si mrefu, haufiki!” “Pole Magesa. Mimi nipo njiani. Si unajua kila nikikanyaga mafuta na kila nikiendesha huwa...” “Unakuwa unakuja au lengo ni kurudi nyumbani kwa mami, bibi, Magesa, Liv na Jimmy. Hata kama ndio unatoka hapo getini lengo ni kuwahi kurdi nyumbani kwa ajili yetu.” Akamalizia Mgesa mwenyewe. “Ewaaa! Basi ujue sasa hivi naendesha haraka, ila kwa makini sana kwa kuwa nakuja kwenu. Mami amekupa maziwa?” “Amekataa huyo. Ameamka na kukuulizia. Amekuja huku akilia. Anakutaka wewe, ndio nikaona nikupigie, mzungumze kwanza. Nahisi amekuota.” Akamsikia Nanaa akimjibu.

“Eti Magesa? Kunywa maziwa, halafu urudi kulala. Nikipata ndege ya mapema, ukimka wewe na ukienda shule na kurudi, mimi nitakuwa nimeshafika nyumbani.” “Muda si mrefu utakuwa umeshafika?” “Naamini Mungu, utakuwa umeshafika. Halafu nikiwahi mapema, nafikiria mimi ndio nije kuwachukua shule.” “Ukija kutuchukua wewe ndio nitakuwa nafurahi sana.” “Basi kunywa maziwa, rudi kulala. Nitamwambia Jerry, leo mimi ndio nitakuwa dereva wa wakina Magesa.” Akamsikia akicheka. Akamuaga baba yake vizuri, akamkabidhi simu mama yake.

“Karibu aamshe ndugu zake, ndio bibi yake akamwambia eti aje alilie huku chumbani kwetu mpaka apate majibu yake yote. Yaani mama jamani!” Geb na Nanaa wakaanza kucheka. “Hapo atakua amemuuliza maswali akaona anamtoa usingizi wake wote, akaona aje anitoe mimi usingizi!” “Muda si mrefu ndio masaa mangapi?” Geb akarudia swali la Magesa kwa sauti ya chini, Nanaa akazidi kucheka.

“Mimi sikujua kama wewe uliwaaga na kuwaambia utarudi ‘muda si mrefu’.” “Huyohuyo Magesa alitaka nimpe masaa maalumu ili aanze kuyahesabu. Sasa nikajua nikimtajia masaa, yakiisha kabla sijarudi, wote wataanza kungiwa na wasiwasi na vilio kama hivyo kwa wote. Wakati naongea na Liv jioni hii yeye alikuwa ameshalala. Mwenzie nikamuongezea muda si mrefu na Jimmy. Yeye hakuwepo.” Wakazidi kucheka. “Alilala mapema leo. Liv alisema alimuona akicheza sana kwenye kuogelea. Akamfuata na kumwambia eti atulie kabla hajaumia, akashindwa kuimba kwenye harusi ya anko, ndio akatulia. Lakini anasema alimuona anarukaruka sana kwenye pool, halafu eti anamwagia wenzie maji mkusudi, ndio akaenda kumtuliza.” Naya na Geb wakazidi kucheka.

“Kama leo ilikuwa siku ya kuogela, basi ndio maana ameota. Atakuwa aliwafanyia sana fujo huko, ndio fujo zote zinarudi usingizini.” “Yaani Magesa mwanangu! Acha nikamwangalie huko anakopewa maziwa.” “Muda huu akatakuwa alishamaliza muda mrefu sana. Magesa hawezi kukiweka chakula muda mrefu hivyo.” “Naomba muache mwanangu, Geb.” Wakazidi kucheka maana Magesa na chakulani kama mama yake tu. Wakaagana na kukata.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Magesa huyo?” Joshua akaamka na kuuliza. “Ndiye mwenyewe huyo. Niliwaaga nikawaambia nitarudi baada ya muda si mrefu. Sasa kumbe yeye anahesabu masaa. Naona yameshakuwa mengi mpaka huko usingizini kwake, naona ameamka.” “Aisee pole Geb, na samahani. Ila ujue nilikuwa nakuhitaji sana. Umerahisisha sana mambo.” “Lakini Joshua, kwa hakika ulijipanga sana mpaka nahisi ungefanikiwa tu bila mimi. Ile akili yakuchukua taarifa za mzee! Mpaka sasa hivi nafikiria, najiuliza ulifikiria nini?!” “Nahisi ni Mungu tu wala si akili zangu. Halafu sikutaka turudie kosa kama tulilofanya kwa Bale.  Sikutaka tuje tujikute wote hatujui chochote kama tuliokuwa hatujajipanga! Anyways, naomba upokee shukurani zangu sana. Nanaa nishazungumza naye na kumshukuru kwa kukuruhusu uje.” “Usijali Joshua. Kwa hakika ujue tupo pamoja. Na tunamaanisha. Ni katika kila kitu.” “Hilo nimelithibitisha aisee. Asante.” Wakaendelea kuzungumza Geb akiendesha mpaka pakaanza kupambazuka ndipo Joshua naye akampigia simu Jema ili kuwaangalizia ndege yakuwatoa hapo Mbeya kuwarudisha Dar.

Baada ya kuendesha mwendo wakutosha, wakatokea uwanja wa ndege. Kila mtu akamshangaa Geb. “Haiwezekani Geb!” Geb akawa akicheka. “Ngoja nikupe siri yangu. Biashara ya kukusanya mazao mashambani, nikilazimika kulala maporini hata kwa watu nisio wajua, kulinisaidia sana kujua kusoma ramani. Sasa hivi imekuwa kama kasumba tu. Nikisafiri kokote lazima nijue nimesimama wapi, nimetokea pande ipi. Kwa ufupi lazima nijue mashariki, magharibu, kusini na kaskazini ni wapi. Hilo ni lazima nijue.” Wakazungumza hapo kidogo wakisubiria muda wakuondoka hapo ufike. Baba Naya alikuwa ametulia sana. Ila wakajua ni kawaidia yake. Mara kadhaa Joshua alijaribu kumuuliza anavyojisikia. Naya alishapiga simu mara kadhaa, akawa ni kama yupo nao hapo wakisubiria waondoke.

Muda ulipofika, wakamsadia kuingia kwenye ndege na kuacha viwanja vya ndege vya mji wa Mbeya wakielekea Dar. Naya na Zayoni walishafika uwanja wa ndege wakimsubiria baba yao. Baada ya muda mama G naye akafika hapo akiwa anatokea kwenye shuguli zake, na Nanaa naye akafika hapo akitokea kazini. Bado ilikuwa mapema tu.

Jijini! 

Zikiwa zimebaki siku 2 tu ndoa ya Naya na Joshua kufungwa, ndege hiyo iliyokuwa imembeba baba Naya, bwana harusi na msimamizi wake pia, Geb, ikatua kwenye viwanja vya ndege vya jijini Dar bado ikiwa mapema tu. Naya akawa wa kwanza kusimama kwenda kumpokea baba yake. Ila akashangaa anatoka akiwa anasukumwa kwenye kigari. Akamkimbilia pale kwenye whealchair. “Unajisikiaje?” “Kizunguzungu tu, na maumivu.” “Pole baba. Ila nimefurahi kukuona.” Akamuona anafunga macho. Akamwangalia Joshua. “Tunaelekea hospitalini ili tujue ni kwa nini. Ameanza kusema anaona giza.” “Naombeni haya mazungumzo yakaendelee hospitalini. Unanisikia Geb?” “Sawa mama.” Wakatoka hapo sehemu yakupokea abiria, baba Naya akisukumwa, amefunga macho.

“Pole baba.” Zayoni akamsogelea kwa karibu wakati Joshua akimsukuma. “Asante Zayoni. Unaendeleaje?” “Nyumbani kuna kelele, bora umerudi. Tumewaacha kina mamdogo wote ndio wameingia na bibi. Wakamkatalia Naya kutoka, ila Naya akawaambia lazima aje. Wanakelele! Na wameshaanza kugombana.” “Kwa hiyo hali yako baba, pale hutaweza. Fujo zimeshaanza kama anavyokwambia Zayoni. Bora hivi tunavyokwenda hospitalini kwanza, ukapumzike.” Naya akaongeza.

“Na kweli anahitaji mapumziko. Hata safari yenyewe haikuwa tulivu. Na kama walimpiga kichwani, na barabara tulizokuwa tukipita usiku kuchwa! Sio nzuri kabisa nafikiri ndio maana hata yeye anasikia kizunguzungu zaidi. Hajapumzika kabisa. Tutaona daktari atakavyotushauri lakini anahitaji mapumziko kwa hakika.” Joshua akaongeza, kina Magesa kimya wakifuata kwa nyuma. Tayari Nanaa kwapani kwa mumewe. Kimya wasafiri wote wakionekana wamechoka. Yalikuwa masaa machache tokea watoke hapo jijini lakini yakuchosha haswa na hekaheka mpaka wanarudi hapo.

Walipofikia gari ya Naya wakati wanamsaidia baba Naya kusimama, huyo mzee alianguka chini gafla, nakuanza kutetemeka kwa ngvu kama mwenye degedege. Naya aliona hilo, alianza kupiga kelele akilia kwa sauti. Zayoni naye alishituka sana. Joshua na Geb walipotaka kumshika, mama G akawaambia wasimguse wamuache kwanza na wampe nafasi apate hewa. Aliendelea kwenye hiyo hali kama degedege kwa muda mpaka akajikojolea kabisa ndipo akatulia. Naya alilia sana. “Sasa hivi mnaweza kumsaidia kusimama sasa.” Mama G akawashitua maana wanaume hao wawili na wenyewe walibaki wamepigwa na butwaa.

Wakamuingiza kwenye gari ya Naya, safari ya kumkimbiza hospitalini ikaanza. Walihakikisha wanampeleka kwenye hospitali waliyojua atapewa huduma kwa haraka. Na kweli. Baba Naya alipokelewa na kuanza kupewa huduma ya kwanza ikiwemo na kubadilishwa pia. Alipofanyiwa CT scan, kila kitu kilikuwa sawa huko kichwani, ndipo daktari aliwaambia inawezekana walimgonga sana, amepatwa Concussion. Kutingishika kidogo kwa ubongo wake. Lakini daktari akawafariji kwa kuwaambia kwa vipimo alivyofanyiwa, hakuna kitu cha hatari. Anahitaji mapumziko mazuri ya siku moja au mbili tu, kisha arudi kwenye shuguli zake za kawaida, ili kurudisha ubongo kufanya kazi kama kawaida bila kumpa matatizo ya kudumu.

Akatolewa sehemu aliyokuwa amewekwa kwa muda akipewa huduma ya kwanza na kupelekwa atakapolazwa. Alishaamka ila wakaambizana watulie kabisa ili wamfanye  na yeye atulie na kupumzika. Alipofikishwa wodini, Joshua akawa muugwana. “Naomba ukapumzike Geb. Umekuwa ukiendesha usiku kuchwa. Tukiwahitaji, tutawapigia.” “Unauhakika?” “Kabisa Geb. Nanaa, nakushukuru sana. lakini huyu anahitaji kupumzika.” Nanaa akamwangalia mumewe. “Naona kweli akalale, turudi jioni au usiku akishaongea na Magesa.” “Nitawaambia kama mrudi au la. Nafikiri lengo zima ni mzee apumzike.” “Lakini kweli. Maana tena sio tuje tujazane hapa, zianze stori, hata ashindwe kupumzika! Naona wazo la Joshua ni zuri. Tumuache kabisa. Ila kukitokea mabadiliko yeyote yale, tafadhali tupigie Joshua.” “Bila shaka mama.” Joshua akaafiki kwa mama G.

Wakamwangalia Naya pale alipokuwa amekaa karibu na kitanda cha baba yake. Joshua akawafanyia ishara watoke. Wote wakatoka kasoro Naya na Zayoni. Mama G akauliza mara walipotoka nje. “Unafikiri atakubali tena kwenda saluni kwa masaji? Maana ndio miahadi ilikuwa leo. Maandalizi ya harusi. Leo awekwe kwenye sauna na masaji.” “Hawezi kukubali, mama. Ameshituka sana kumuona baba yake kwenye ile hali. Hawezi kukubali kutoka hapa sasa hivi. Naomba tumuache kwa leo. Akikaa hapo akaridhika baba yake anaendelea vizuri, kesho hata tukimwambia aende saluni atakubali. Lakini si leo. Nyinyi nendeni mkapumzike tu. Na kwakuwa na chakula watampa hapahapa, msihangaike.”

“Basi akitulia, mwambie aje alale Tabata, asirudi huko Kiluvya kwenye kelele.” Mama G akatoa wazo. “Hawezi kumuacha Zayoni na hao ndugu za mama yao. Naya anasema ni wakorofi sana.” “Pale kwetu ni pakubwa sana. Kuna vyumba ambavyo hata havitumiwi! Waje tu, ili atulie. Akili ibakiwe kwenye harusi yake na baba yake.” Akaongeza Nanaa. “Nitamjaribisha. Akikubali, nitawaleta. Nawashukuru sana.” Wakaagana ndipo wakaondoka.

Baba Naya alilala muda mrefu, akaamshwa ale, akala vizuri tu akarudi kulala tena. Akaamka tena usiku. “Nendeni mkapumzike. Mimi nipo sawa. Nasikia hata kichwa kimetulia vizuri. Mpaka kesho nitakuwa mzima kabisa.” “Nataka kubaki na wewe kidogo.” “Nataka kulala mama. Nikirudi kulala sasa hivi, ndio mpaka asubuhi. Naomba usiwe na wasiwasi. Nenda ili na mwenzio akalale. Hajalala huyo usiku kuchwa.” “Basi asubuhi nitakuwa hapa.” “Sasa tena isiwe alfajiri.” “Jamani baba!” Naya akalalamika. Kidogo wakacheka.

“Itakuwa hamna maana ya mimi kuwepo hapa. Wewe nenda katulize ile fujo ya mama zako kule. Wewe unawawezea.” Naya akacheka sana. “Mimi siku hizi sipendi ugomvi na mtu. Nakuwa mke wa mtu, sina muda huo.” “Kwa ninavyowajua wale, watakutafutia tu muda.” “Walitaka waanze, nikamwambia bibi, mimi sina muda wa ugomvi, nakuja kukupokea.” “Bibi akalalamika eti tunatumia pesa za mwanae kupanda ndege.” Zayoni akaongeza. “Yaani hizo pesa za mama Naya bado tu hazijaisha mpaka leo!?” Baba yao akaongeza akijiweka sawa hapo kitandani. “Wenzio wanasema ndio umezichukua zote ukajenga lile ghala na kununua vitu vya ndani, halafu yeye bibi hajapata urithi wa mwanae.” “Nashauri tumuache baba apumzike kwa leo.” Joshua akaingilia kwa Zayoni, ili wasiendelee kumchosha.

“Joshua!” Baba Naya akaita wakati wanataka kutoka. Naya akarudi haraka kama yeye ndio Joshua. “Hujui ni kwa kiasi gani namshukuru Mungu kwa ajili yako Joshua. Mungu alikuleta kipindi maalumu akijua tutakuhitaji. Najua unalipa garama kubwa sana kwetu. Pengine muda uliotumia kunitafuta ungekuwa ukifanya kazi yako, lakini umehangaika mpaka umenirudisha kwa wanangu na bado unamuhangaikia Bale japo umejua kabisa, hakukubali! Hakika Mungu akukumbuke na wewe. Asante sana Joshua.” “Karibu sana mzee wangu. Lakini nakumbuka ulishanikaribisha kwenye familia. Nahesabu na mimi ni mmoja wenu. Kinachomuhusu Naya, na mimi kinanihusu, na Mungu ameniweka katikati yenu akijua nitaweza tu. Kwa hiyo naomba muwe na amani kabisa. Chochote mnachoona naweza kufanya, msisite kabisa kunishirikisha.” Wakazungumza kidogo na kutoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Twende ukalale mchumba wangu. Bwana harusi.” Joshua akacheka. “Harusi kumbe bado ipo!” “Lazima. Hapo tushakubaliana. Haturudi nyuma. Ila sherehe ndio inategemea. Sasa twende ukapumzike na mimi nirudi kwenye zile kelele nyumbani.” “Mama G anawazo la tofauti.” “Nini tena?” Joshua na Naya pamoja na Zayoni wakaendelea kuzungumza wakitoka hapo hospitalini. “Anataka ukapumzike kwao mpaka kesho.” Naya akacheka. “Wazo zuri lakini ile fujo pale, siwezi kuicha siku nzima eti na usiku bila sisi kuwepo! Haiwezekani.” “Ndio mbaya hivyo!” “Hujawahi ona ndugu wa aina ile. Baba yeye anawawezea kwa sababu haongei. Ananyamazaga kimya. Wanaongea mpaka wanamaliza yote, yeye kimya. Malalamishi yao hayaishi. Kama kulalamikia kwamba mama alipokuwa hai ni kwa nini alikubali kuolewa na baba! Haya, alipokufa na wao wakataka urithi wengine wakamsema baba eti amemuua kwa shida zake. Haya leo wamekuja bibi analalamika kuwa mafao ya mwanae ndio baba anayatumia sasa hivi kujijenga! Wadogo zake wanasema eti baba alimtoa kafara ndio amefanikiwa sababu ya kifo cha ndugu yao! Ni fujo na niwazungumzaji haswa.”

“Sasa hudhani ndio unasababu ya kwenda kupumzika kwa kina Magesa?” “Mimi nimeshawazoea. Hawanisumbui. Halafu nimemuahidi bibi nitalala naye usiku nimpe habari zako kwa undani.” Naya akaanza kucheka mwenyewe. “Sijaelewa Naya!” “Alikuwa akinikatalia kutoka akitaka kujua naolewa na mwanaume wa namna gani! Tajiri au masikini! Anayo nyumba au ananipeleka kwenye nyumba ya kupanga halafu nianze kumlisha! Mzuri au naolewa na mwanaume mbaya ambaye atasababisha nizae watoto wenye sura mbaya!” “Naya!” “Wewe acha tu niende nikawatulize ili baba akija wawe wametulia.” “Unataka nikusindikize?” Naya akaanza kucheka huku akimtizama Joshua.

“Acha bwana! Watanila nikiwa hai?” “Nakwambia wakiwa wanakutizama hivi! Kuna watakao kuomba hela. Kuna watakao taka kujua mshahara wako kwa mwezi. Ushakuwa na wanawake wangapi. Kama ulishazaa. Habari za mama yako na baba yako na mengine mengi. Wakija kukuachia hapo, huna hamu ya ndoa.” Joshua akacheka sana. “Nenda kalale upumzike. Achana na ndugu wa mama Naya.” Wakakubaliana Joshua aende akapumzike. Naya akamrudisha nyumbani kwake wao wakaanza safari yakurudi kwao Kiluvya.

Siku Moja Kabla Ya Harusi.

Ilikuwa imebaki siku moja tu harusi ya Naya na Joshua ifungwe. Baba Naya bado alikuwa hospitalini na Bale bado hajulikani alipo. Usiku uliopita Joshua alilala kama aliyekufa, akaamka alfajiri na mapema kwenda kazini, angalau kuweka mambo sawa kabla ya harusi ambayo alijua maadamu Naya anaishi, basi hiyo harusi lazima kufungwa ila hakujua aina ya sherehe.

Katikati ya kikao simu ya Geb ikaingia. Akaomba udhuru na kutoka. “Samahani najua unaweza kuwa sio muda mzuri. Lakini nimetoka kuzungumza na kina Gamba ni kama wamegonga mwamba huko walikokuwa wakimsaka Bale. Wanasema wengi wanakuwa na majina ya uongo au wanakuwa hawana vitambulisho wala hati za kusafiria ndio maana wanatumia njia za panya tu. Kwa hiyo kwa jina hilo la Bale hawajafanikiwa kupata, na pale mpakani ni kama mahabusu tu. Wakikamatwa hapo wanashikiliwa kwa muda na ndipo wanasambazwa.” “Wapi?” Joshua akauliza.

“Hapo ndipo ulipo ugumu. Haijulikani kwa hakika. Wengine huhamishiwa magereza ya Tunduma. Magereza yakiwa yamejaa na wafungwa wengine wakisema wanatokea Mbeya, wanapelekwa magereza ya huko. Sasa basi, walianzia magereza ya palepale Mbeya tulipokuwa tumewaacha, wamezunguka tokea jana na leo lakini hawajafanikiwa kumpata. Ndio nimewaomba tena, leo warudi tena Tunduma wajaribu kumuulizia tena kwenye kila magereza.”

“Nakushukuru sana Geb. Aisee ni muhimu sana. Salamu ya yule mzee asubuhi hii si kuhusu afya yake ila Bale. Naya naye ni hivyohivyo, mpaka anafikiria pengine baada tu ya kufunga harusi, yeye mwenyewe ajaribu kwenda huko akasaidie kumtafuta.” “Sio fungate tena!?” Geb akashangaa. “Akili yake haipo huko kabisa. Anasema atatulia kama akirudisha familia yao pamoja, hapo ndio hata akili ya mapumziko itakuwepo.” “Daah! Basi acha niwaambie waongeze juhudi.” “Nashukuru Geb. Basi tutazungumza baadaye.” Joshua akakata simu.

Reheasal Dinner.

Jioni hiyo anatoka baba Naya hospitalini, anakutana na ratiba za harusi ya binti yake, zikiendelea kama alivyoomba mwenyewe jambo lisisimame hata kama ni yeye mwenyewe asizuie harusi ya binti yake kufungwa. Walikuwa na mpango wa kufanya reheasal dinner, nyumbani kwa Joshua. Ili kufanyia mazoezi kila kitu kitakachoendelea kesho yake siku ya harusi. Jinsi watakavyoingia hapo ukumbini, wakati wa kufunga ndoa na wakati wa sherehe yenyewe. Nani anasimama wapi na kufanya nini kwa hao walengwa. Bibi harusi, bwana harusi, wasimamizi wote kujipanga vizuri. Na ndugu pande zote mbili kufahamiana kwa karibu siku  hiyo kabla ya siku yenyewe ya harusi.

Kwa kuwa Naya alikuwa akitokea saluni, Joshua akaenda kumchukua baba Naya hospitalini, dereva akatumwa kwenda kuchukua ndugu wa Naya ili na wenyewe wahudhudhurie kwenye reheasal dinner kama na wenyewe walengwa wakubwa wa hiyo shuguli kuja kukutana na bwana harusi rasmi pamoja  na ndugu zake ambao ndio kina Magesa.

Naya alikuwa saluni na mama G, Nanaa, Liv, Grace na mtoto wake wa kike wakianza kutengenezwa. Kwa hiyo baada ya saluni, muda ulipofika wakaongozana nyumbani kwa Joshua. Baba Naya alishapelekewa hospitalini nguo safi na Naya wakati akielekea saluni. Akaoga hapohapo hospitalini na kubadili akabaki akimsubiria Joshua. Na wao ndio wakawahi kufika nyumbani kwa Joshua. Akaingia Man, mume wa Grace, Geb na watoto wao wakiume na dada yao wa kuwasaidia kazi. Wakiwa wanazungumza tu hapo sebuleni Joshua, baba Naya, Geb wakawa wanaingia mama G na kundi lake la kina Nanaa, pamoja na bibi harusi wao. Vicheko na stori wakicheka kuanzia huko nje vilisikika ndani walipokuwa wamekaa hao wanaume. Hawakupishana sana na James. Kundi likakamilika ndani, vicheko na utani vikaendelea wakati wakiwasubiria ndugu wa kina Naya ambao walishafika Kiluvya, ndio wanaletwa hapo.

Magesa akaomba wote watulie wamsikilize aimbe. “Naombeni mumsikilize baba mzazi jamani! Ameweka juhudi kweli kujifunza na kushika maneno.” Nanaa akamuombea mwanae. “Mama yangu amesema mimi ni mtoto mzuri, nikikubali kufanya jambo naweka nidhamu mpaka nahakikisha nafanikiwa.” “Kweli Magesa wewe ni mtoto mzuri sana.” “Asante dad, kwa hiyo watanisikiliza na leo pia?” “Na mimi pia nitakusindikiza, pamoja na anti Naya. Tutaimba pamoja.” “Ila mimi ni mpaka nisimame.” “Basi pumu imepata mkohozi. Kwani wewe huwezi kuimba mpaka usimame bwana Magesa!?” “Hamuwezi kunisikia vizuri na kuniona, bibi.” Wakaanza kucheka. “Haya baba.” Bibi yake akamalizia huku akicheka akitingisha kichwa.

“Basi mtu anikaribishe. Eti dad?” Watu walicheka mpaka machozi. “Jamani mkaribisheni mwanangu aanze kuimba!” Nanaa akajaribu kumtetea mwanae. Watu wakazidi kucheka. Mara wakasikia geti linafunguliwa na gari kubwa lililobeba ndugu wa Naya wanaingia wakiimba. Naya akamwangalia baba yake. “Naona wenzetu wamechangamka kwelikweli! Wanaingia na vigelegele.” “Hayo ndio mambo.” Akaongeza Grace kwa mama yake. “Basi hao mtawachoka.” Naya akasimama ili kwenda kuwakaribisha.

Joshua akataka kumfuata, akasimama kabisa. “Naomba kwanza mimi nikawakaribishe halafu ndio uje na wewe.” Naya akaongea akicheka na kumtizama baba yake pia. Joshua akawa hajaelewa. “Sio wote ndio twende tukawapokee kwa shangwe kama walivyoingia!” Mama G na yeye akasimama kama kumsindikiza Naya, akafuata na Grace. Ikawa kama Naya ameshindwa awaambie nini akabaki amesimama akimwangalia baba yake, ikabidi baba Naya amsaidie. “Ana maana yake huyo. Acha kwanza yeye atangulie kukaribisha mama zake, kisha sisi ndio twende.” Akaongeza baba Naya. Wakaangaliana, Naya akazidi kucheka. “Naombeni mimi nitangulie kwanza jamani. Kisha mtakuja na baba.” Naya akatoka kwa haraka bila kuongeza zaidi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akakuta mama zake wadogo, bibi yake, wajomba zake wawili na wake zao pamoja na watoto wanashuka kwenye hiyo hiace, kibasi kidogo. “Naombeni tuzungumze kwanza kabla hamjaingia ndani.” “Naya naye! Mbona unataka kutunyima raha na maonyo yasiyoisha.” “Hapana mama mdogo. Nataka tu kuweka msisitizo ili leo paishe vizuri.” “Sasa kwani..” “Mnaona wale askari pale?” Naya akaendelea, wote wakageuka. “Mbwa wamefungiwa ndani kwa sababu yenu tu. Jamani ndugu zangu, hii nyumba ina kamera kila kona. Hapa tuliposimama hapa, mwenye nyumba anatuona kwa kupitia simu yake pale alipokaa.” “Mpaka vyooni!? Tutajisaidiaje sasa?” Akaanza mmoja wa mama yake mdogo.

“Humo ndani, kila kona, jikoni, sebuleni, vyumbani pia anazo kamera ila anazima kukiwa na mgeni analala kwenye hicho chumba.” Naya akaendelea taratibu tu. Akashangaa wote kimya. Hakuna hata shangwe tena. Akatoka Zayoni. “Kujibu swali lako mama yangu mdogo, ndani ya vyoo hakuna kamera ila nje ya kila mlango kwenye hii nyumba, ndani na nje ya nyumba, kuna kamera. Sasa hivi ndivyo zinavyofanya kazi.” Wote kimya. Naya akaendelea akiwatizama wote.

“Mlango wowote ukifunguliwa ndani ya hii nyumba, kuna mlio unaingia kwenye simu ya Joshua. Ambaye ndiye mwenye nyumba na kumfanya aangalie. Anaweza kuzungumza na huyo mtu akiwa popote hapa nchini, ila akiwa nje ya nchi, walinzi wake macho yao yapo mpaka ndani.” Kimya wote wakisikiliza kwa makini. “Mbona shangwe zote zimeisha huko nje?” Akauliza mama G. “Naya huwa anaweza kuzungumza lugha wanayoelewa wao tu. Kuna anachowaambia tu, ndio maana unawasikia wametulia. Ila utawasikia tena.” Akajibu baba Naya taratibu tu.

“Kwa nini nimewaambia haya yote!” “Msiibe.” Naya akataka kuendelea lakini Zayoni akamuwahi. “Ewaa! Zile tabia zakuchukua vijiko, vikombe na kuingia vyumbani mnaiba na kufichwa vitu mpaka kwenye sidiria, hapa si mahali pake ndugu zangu. Tafadhali mjihadhari.” “Muache tamaa.” Akaongeza Zayoni. “Huyu naye jeuri kama baba yake! Sasa aliyekwambia kuna mwenye tamaa hapa nani?” “Usimpandishie mtoto, kwa kuwa wote sisi tunajuana tabia zetu. Nimewawahi ili msije ingia aibu. Kitu kikiibiwa hapa, itajulikana. Ukitoka nacho nje ya hilo geti, mbwa watapata harufu, ndipo mtaanza kusachiwa pale getini. Kwa kifupi tu, mali ya humu ndani haitoki bila ruhusa ya mwenyewe.” “Kwa hiyo kuomba ni sawa si kuchukua tu?” Akauliza mmoja wao.

Zayoni akaanza kucheka. “Ndipo linapokuja swala jingine kabla na la mwisho. Siku ya leo, kesho kwenye harusi yangu, mtu yeyote kati yenu, haruhusiwi kumuomba Joshua chochote. Hata pesa na yale matatizo ya pesa ya ada za watoto shule na pango, hamruhusiwi.” “Mashariti mengi mpaka nishachoka!” “Kama umechoka bibi, dereva huyo hapo, anaweza akakurudisha nyumbani ukapumzike, mimi nitakuja kukusimulia jinsi mambo yalivyokwenda hapa maana na leo tunalala kitanda kimoja bibi yangu. Tupige stori kama jana usiku.” “Nitaondoka vipi mama yako hayupo? Mimi ndio mwakilishi wake.” “Basi jikaze. Maana mambo ndio yanaanza, mwakilishi wa mama Naya.” Naya akaongea akicheka kidogo ila walimjua ni mkali kama mama yake.

“Jamani kuna mwenye swali? Au mtu hajaelewa chochote hapa?” “Na hivi tunavyoshangilia ni sawa au napo kamera zinatuangalia?” Akauliza kishari akilalamika. “Wewe mama yangu mdogo shangilia kwa kadiri ya uwezo wako,  mimi mwenyewe nitawasaidia vigelegele.” Wote wakawa wameshapoa kabisa, kama morari iliwaisha.

“Cha mwisho na cha msingi, nakumbushia tu. Inawezekana jana wakati nawaambia hili mjomba na mama mdogo mlikuwa mmelewa sana.” “Nini tena!?” “Hapa tuliposimama sasa hivi, na yeyote mtakayekutana naye kuanzia sasa upande wa Joshua, wanamuheshimu sana baba.” “Tena sana.” Zayoni akaongeza. “Mmemsikia Zayoni. Baba mliyezoea kumtukana na kumbeza kila wakati, hapa anaheshimiwa mno. SITARUHUSU. Narudia tena. Sitaruhusu, hata kwa bahati mbaya, au kuropoka yale maneno yenu ya kejeli kwa baba. Nikikusikia tu, hapa unaondoka. Ukiona huwezi kumuheshimu baba Naya, basi ondoka, tutakuja kukuonyesha picha ya kitakachokuwa kimeendelea wakati haupo.” Kimya, Zayoni akaanza kucheka.

“Hapo wenzio wanataka kuondoka wote.” Zayoni akaongea akicheka. “Basi nitawaonyesha video, gari hiyo hapo, dereva yupo, mambo yafamilia yetu tunayoshindwa kumaliza kifamilia, tukaendeleze kwetu sio hapa kwa watu.” “Si na wewe patakuwa kwako, lazima ajifunze kuishi na watu huyo Joshua!” “Sawasawa. Lakini bado hapajakuwa kwangu. Hajanioa. Akishanioa, ndio tuanze zile fujo zetu hata mbele yake, atajifunza tu na itabidi ajue jinsi yakuishi na nyinyi. Ila kabla hajanioa, hapana.” Kimya. Na yeye Naya akanyamaza.

“Mambo yataenda sawa Naya mjukuu wangu, wala usiwe na wasiwasi.” “Asante bibi yangu. Kesho na mimi niolewe, niwe mke wa Joshua.” “Unavyojidai!” “Ndio maana ulikuwa unajishaua na huyo Joshua! Kumbe sababu mambo yake safi!” “Kumbe! Sasa hamjamuona Joshua wangu. Nyinyi acheni fujo, aje mumsalimie tu. Sio muanze kumuuliza yale maswali yenu. Au mnasemaje ndugu wa mama Naya?” Kidogo wakaanza kucheka na vigelegele.

“Hapo sasa tunaweza kutoka.” Baba Naya akasimama, wengine nao wakamfuata nyuma. “Kapendeza baba Naya! Kama sio yeye!” “Na wala si mafao ya mama Naya. Mwacheni baba Naya.” Naya akajibu kwa haraka, vigelegele vikaendelea. Kina mama G nao ikabidi wachangake, wakawapokea hapo na vigelegele.

Katikati Ya Msafara Wa Mamba,

Kenge Nao Wamo!

Kabla hawajataka kusalimiana baada ya vigelegele na shangwe, wakashangaa Malon anatoka kwenye hilo basi lililoleta ndugu wa Naya. Naya akamuona wakwanza. Akashangaa mpaka ikabidi na Joshua ageuke. Wote wakageuka, kimya. “Huyo kijana aliomba lifti baada ya mjomba wako kumwambia hawezi kuongozana na sisi akiwa kwenye gari yake, wewe ulisema wote mje na usafiri mmoja ili kuepuka kuchanganya askari getini. Kwamba ni hiki kibasi tu ndicho kitafunguliwa geti na kuruhusiwa kuingia humu. Ndio ameacha gari yake nyumbani na kuongozana na sisi, anasema anashida sana na wewe, mnafahamiana.” “Kabla yakumpandisha kwenye gari ungenipigia mimi simu bibi au mjomba!” “Shuguli ni watu mama.” Akajibu bibi yake bila hila moyoni. “Sie huyo, bibi.” Naya akamalizia.

Malon akacheka akitingisha kichwa. “Nipo hapahapa nakusikia mimi mwenyewe Naya! Na nimekuja na habari njema.” Wote kimya wakimtizama wakimsikiliza Malon. “Najua Bale alipofungwa na naweza kusaidia.” “Sasa mbona umesimama hapa?” Akauliza Zayoni. “Asante sana Zayoni.” “Subiri kwanza Naya. Kwamba sisi tunashangilia hapa, kumbe Bale amefungwa jela!?” Akaanza bibi mtu. Kimya.

“Nilikwambia bibi, Bale atarudi. Na inawezekana akarudi kabla ya harusi.” “Kweli Naya wewe!? Kaka yako amefungwa jela unashangilia! Kweli Denis wewe, mkeo amekufa juzi tu nyumba inakushinda mpaka watoto wanafungwa jela! Upo hapa unashangilia harusi ya Naya, mtoto hajulikani alipo!” Bibi akaanza kulia, wakaja kina mama wadogo. “Dada atakuwa anageuka huko kaburini!” Mdogo mtu akaongeza na kuzidi kulia. “Kweli wewe huna nafsi baba Naya. Umetulia ndani kwenye majumba haya yenye mageti makubwa hujali mtoto alipo?” Wakazidi kulia. Nguvu ileile waliyotumia kushangilia, ikageuka kilio. Baba Naya kimya.

“Labda tungewakaribisha wageni kwanza, angalau wapumzike.” Akatoa wazo mama G. Kila mtu akawa kama amepigwa na butwaa. “Twendeni jamani. Poleni sana. kuna mahali maalumu kumeandaliwa kwa ajili yenu. Twendeni mkatulie kwanza, halafu tutapata muda wa mazungumzo.” Mama G na Grace wakawatoa hapo. “Nani amefungwa jela mami? Mimi naogopa polisi!” Mama G akageuka haraka. “Haya njooni. Twendeni na wageni.” “Wana polisi?” “Hapana Magesa. Usiogope, hakuna polisi.” Baba yake akamtuliza na kuongeza. “Samahani Joshua. Ni sawa dada yao akiwachukua awapeleke ndani kwenye chumba cha tv, wasiende huko mpaka nitakapokwenda kuwachukua?” Geb akaweka ombi ambalo halikuwa na jibu la hapana. Anataka watoto wake wakafungiwe mahali mpaka yeye akawachukue. “Bila shaka.” Dada akaondoka na  watoto.

Naya akamgeukia Malon kama ammeze. “Sijakusudia kuharibu Naya, nimetaka kusaidia.” “Labda mimi niulize swali kama alilouliza Zayoni. Samahani lakini. Ni kwa nini sasa upo hapa? Maana ni kama nimesikia umesema unajua alipo na unaweza kusaidia!” Akaongeza Geb na swali. “Nisingeweza kufanya bila kuwasiliana na familia yake kwanza.” “Pengine ufafanue zaidi. Tafadhali, Malon. Maana Bale yupo matatizoni. Anatafutwa sana. Muda si mrefu tumetoka kuzungumza na askari wanao mtafuta, bado Bale hajulikani alipo.” “Hawawezi kumpata.” Malon akamjibu Joshua kwa kujiamini.

Wote kimya. “Labda mimi niulize japo nimesikia habari hii kwa juu juu wakati Geb akizungumza na hao askari wanaomtafuta Bale. Mimi naitwa Man, shemeji yake Geb. Sijui wewe ni nani?” “Wewe uliza swali lako.” Malon akamjibu kijeuri. “Samahani Man. Anaitwa Malon. Tulikuwa kwenye mahusiano naye kabla ya Joshua. Ni kweli anafahamiana na familia yetu. Hata Bale amepotelea kwake. Akiwa ametoka nyumbani kwenda kwake kufanya kazi.” “Bale hajapotelea kwangu, hilo moja. Na pili mimi siye niliyesababisha Bale aondoke kwangu. Ni ujuaje wake.” “Kama tazizo ni Bale, na mimi imekuaje niliondoka kwako? Maana wote tunajua tatizo si Joshua.” “Tatizo ni Joshua. Hata kama ukikataa Naya. Matatizo kwetu ni kawaida, na tulikuwa tukiyamaliza.” Wakaanza Naya na Malon.

“Wewe hujui mahusiano Malon. Hujui kuishi na watu. Hutaki majukumu. Kila mtu anayo mapungufu yake, watu wote wanajua, na watu wanaishi pamoja kwa kuwa wanajua jinsi yakuchukuliana.” “Sasa hapo kosa linakuaje ni langu tena? Yeye ndiye aliyeondoka na kwenda kujiingiza kwenye matatizo akitaka kufanikiwa kwa haraka!” “Man samahani. Naomba uliza swali lako.” “Sitakwenda mbali na Zayoni, kwenye swali lake la kwa nini upo hapa. Ila mimi nitabadilisha kidogo, kwamba, unataka nini kwa familia ili kusaidia kumpata Bale?” Man akauliza.

“Cha kwanza nyinyi wote hapa si familia ya Bale. Siwezi kuzungumza chochote na nyinyi ila familia ya Bale. Na nikisema familia ya Bale, sio tena na Joshua. Bale hamtaki kabisa Joshua.” “Unakumbuka mara ya mwisho Naya kukupigia simu usiku kukuomba namba ya simu ya Bale?” Baba Naya akauliza. “Sikumtafuta tena kwa...” “Sasa hapo Joshua sikiliza zile sababu zake. Moja nzuri sana inakuja.” “Acha kunikejeli Naya.” “Mimi  sikukejeli Malo. Hata huyu Bale unayemzungumzia hapa ukitaka kumuumiza Joshua wangu kuwa eti hampendi, naye nilimwambia hakunisadiki. Nilimwambia huwa hukosi sababu ya kukufanya upotee.” “Sasa ningerudi vipi na taarifa nusunusu?” “Ingekugarimu nini kurudisha ujumbe kuwa hujapata taarifa kamili, unashugulikia kupata taarifa kamili kisha utatutafuta?” Joshua akamuuliza. “Hayakuhusu Joshua.” “Umechelewa Malon. Yananihusu sana.” “Mimi sidhani kama kweli unazo taarifa za kusaidia bwana Malon.” Akadakia Man. Grace akamvuta. Alisharudi na kusimama nyuma yake.

“Subiri kwanza Grace. Mimi naongea kwa vile ninavyomfahamu mwanadamu, pengine wewe uwe tofauti. Huyu kijana amepotelea kwako. Akiwa mikononi mwako!” “Mtu mzima vile ameamua kuondoka, unafanyaje wakati hata kwao tu aliondoka bila maelewano na ndugu zake!?” “Kwa sababu yeyote ile iliyosababisha kuondoka kwako. Kwa staili yeyote ile aliyoondokea kwako, kama kweli wewe ungekuwa mtu wa kutaka kusaidia, ungetaarifu familia yake mapema sana pale tu ulipogundua asubuhi yake kuwa hayupo. Kutoa tu taarifa kuwa, Bale ameondoka kwangu. Hivyo tu.” “Asante sana Man.” Naya akashukuru.

“Hapo aliposimama Naya, yupo sehemu sahihi, Malon. Inawezekana si pale ungetamani kupaona au sivyo yeyote yule kati yetu angefurahia, lakini ni uchaguzi na matakwa ya Naya. Mimi kama baba yake nimeliheshimu hilo kama nilivyoheshimu alipokuwa na wewe. Anza kuelewa hilo na kulikubali ili wakati mwingine wowote unapotaka kuzungumza naye, ujue Naya uliyemzoea wewe siye wa sasa hivi. Naya ataolewa na Joshua, kesho. Iwe isiwe, ataolewa. Mimi niwepo, nisiwepo, Naya anaolewa na Joshua, KESHO. Chochote unachotaka kuzungumza juu ya familia hii, huwezi kumtoa tena Joshua. Amejithibitisha ni mmoja wa familia hii kwa vitendo.” Akaongea baba Naya.

“Ninachotaka kukuhakikishia Malon, Bale tutampata tu. Labda kama Mungu hayupo. Ila kama Mungu yupo, basi yeye aliyenipa Bale, atanirudishia. Hata kama nilifanya kosa, nimemsihi Mungu anisamehe, anirudishie Bale. Sasa Mungu atamtumia nani kumrudisha Bale, sijui. Kama unazo taarifa, na unataka kuzungumza na familia. Wote wataondoka ila ujue Joshua hataondoka. Uwamuzi ni wako. Utasaidia au unaondoka?” “Siwezi kukiuka matakwa ya Bale mwenyewe. Mambo yake hakutaka Joshua ayajue, basi itabaki hivyo.” Malon akaweka ngumu.

“Jamani, acheni tu mimi niondoke. Lengo ni kumpata Bale. Acha mimi niondoke tu kuwapa nafasi.” “Nakwambia ukweli Joshua. Leo ukitolewa kwa hili, kesho utatolewa kwa jingine. Tena litakalosikika la muhimu sana, kisha watafanikiwa kuja kuwatenganisha kabisa. Kama Malon hawezi kuzungumza mbele yako, basi.” “Nikuheshimu matakwa tu ya Bale.” “Basi hilo ndilo litamgarimu Bale huko alipo, itambidi asubiri. Lakini hutamtoa Joshua kwenye hii familia, labda aamue mwenyewe Joshua au Naya.” “Mimi hapa niliposhika ni mpaka kifo baba yangu.” Naya akajibu kwa haraka bila yakufikiria. Ujasiri kwa Joshua ukaongezeka. Akaushika mkono wa Naya kwa nguvu zaidi.

“Basi twendeni.” Baba Naya akageuka na kuanza kuondoka. “Twende Joshua.” Naya akamtingisha mkono waliokuwa wameshikana. Joshua akamwangalia na kurudisha macho kwa Malon. “Mlinzi atafunga geti ukitoka.” Joshua akamalizia kama anayemwambia anaweza kwenda sasa.

“Kweli Naya unakubali kaka yako akae jela sababu ya mtu baki!?” “Joshua si mtu baki. Na kukutoa tu wasiwasi Malon. Wakati wewe umefungwa. Wala sikuwa nikijua umefungwa jela ipi! Nikiwa sina hata pesa, mimi mwenyewe na kwa maombi ya baba Naya, niliweza kukutafuta mpaka nikakupata. Nikakuwekea dhamana ya mamilioni ya pesa, ukatolewa jela, tena ukawekwa huru bila kosa lolote. Mungu akakufutia makosa yote na kukupa nafasi ya pili. Sasa Mungu huyohuyo wa nafasi ya pili, atampa na Bale.”

“Na sisi pia kama ulivyosema, familia yetu ina matatizo. Mungu atatusamehe na atatusaidia. Kama alitenda kwako, hatashindwa na kwa Bale. Kokote alipo, tutampata tu. Wala usijali Malon. Uwe na usiku mwema. Twende Joshua.” “Ungependa kurudishwa mpaka Kiluvya ulipoacha gari yako?” Joshua akawa muungwana, akajirudi. “Sawa.” Malon akajibu hivyo tu na kuondoka hapo akawa anatoka getini. Joshua akampigia simu dereva amfuate na kumrudisha Kiluvya. Malon akaondoka bila kusema alipo Bale.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Mimi naomba nimfuate baba kule kwa kina bibi. Wameshaanza kumlaumu na baba hajisikii vizuri. Asije akaanguka tena.” “Twene wote.” Bado Joshua alikuwa ameshika mkono wa Naya. “Acha na mimi nije. Au unasemaje?” Mama G akaongeza. “Twende tu mama yangu. Si unasikia vilio hivyo?” “Sasa utafanyaje Naya!?” Nanaa akauliza. “Baba alikuwa akiniambia leo asubuhi nilipomfuata hospitalini. Hatutakuwa na majibu yote kwa wakati mmoja. Kama hili la Malon na msiba huu alioanzisha hapa sasa hivi, hatukuwa tumejiandaa nao. Akasema tutembee kwa hatua. Tukabiliane na kila hali tutakayokutana nayo. Lakini hakuna mpango wakurudi nyuma. Amekataa na amesema lazima kuendelea, iwe tu mimi nimebadili mawazo nimeamua sitaki tena kuolewa na Joshua, au Joshua mwenyewe hataki tena. Ila kama sisi tupo tayari, amesema hata kama itatugarimu kuwepo sisi tu wawili, tusiahirishe.” Naya akaendelea.

“Kama ulivyomsikia hapa. Anasema tukija kuahirisha tu kwa moja, kesho litatokea jingine na jingine na ndivyo maisha yalivyo. Si wakati wote yanatoa fulsa sawa kwa wote. Anasema wengine hawajajaliwa kutokuwa na vipingamizi kila wakati. Wengine nilazima kulazimishia ili mambo fulanifulani yatokee.” “Hata mimi namuunga mkono mzee.” “Man mume wangu wewe jamani!” Grace akashituka kabisa. “Mimi nasema kweli. Kuna mambo mengine Grace, yanayopatikana kwa nguvu. Si Mungu mwenyewe amesema, ufalme wa Mungu unapatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu watauteka! Mathayo 11:12. Sasa kama mpaka ufalme wa Mungu ni kwa kutumia nguvu, je huu wetu! Simama hapohapo Naya, mpaka upate mume.” Wakaanza kucheka.

“Basi hapo Man amepata shuguli!” “Wanangu wamejiandaa kusimamia harusi, halafu wanataka kuniletea mahairisho! Usinitanie mimi.” Wote walicheka kwa sauti. “Yaani Man wewe jamani!  Kumbe maandiko yote hayo ni ili wanao wasimamie harusi!?” “Vyote bwana Grace. Eti Joshua, kwani uongo?” “Kabisa Man.” Joshua akajibu akicheka. “Mimi naungana mkono na baba Naya. Lakini si kwa ajili ya Magesa aimbe!” Geb akafanya wazidi kucheka huku wakielekea walipo ndugu wanao lia.

Kisha Geb akaendelea. “Ishini kwa kumuenzi mama. Ndoa takatifu ni heshima kwa mzazi yeyote yule. Msiache kufunga ndoa. Mengine mtajua mbele ya safari.” “Tunashukuru kwa kutuunga mkono jamani. Uwepo wenu hapa ni muhimu sana. Hakika tunawahitaji.” “Tupo pamoja Joshua.” Hapo mpaka James akaongeza. Wakaendelea kutembea. Kadiri walivyosogelea walipokuwepo hao wageni, sauti ya vilio ikaongeza simanzi na kuwafanya waaache kucheka.

Kabla hawajaingia ndani, maana wageni hao walipitishiwa mlango wa nyuma, Joshua akamvuta Naya, kidogo akageuka. “Nimevumilia nimeona tu nikwambie. Umependeza sana.” “Sasa hapa bado.” Ilibidi Joshua acheke. “Naya!” “Mimi nakwambia ukweli. Usifikiri eti hapa ndio nimependeza mpaka mwisho! Subiri sasa kesho. Ndio utasimamisha kabisa harusi.” “Kwa jinsi utakavyokuwa umependeza?” “Hutaamini kama ni Naya Kumu.” Joshua alicheka mpaka akapiga makofi. Wakawageukia wao.

“Hivi wewe Joshua unajua kama wakwe zako wanalia!?” Nanaa akamuuliza akimshangaa. “Si Naya huyu! Anataka kuniponza ukweni.” “Sasa twendeni tukamsikilize baba Naya,  na wakwe zake.” “Mbona sasa hatumsikii akiongea?” “Huwa anawaacha kwanza wafanye yao mpaka wakimaliza ndipo anaongea. Akiona hawapo tayari kumsikiliza basi anawaacha tu. Anabaki kimya.” Wakacheka kwa sauti ya chini. “Acha mimi nianze kuingia, nikambembeleze bibi kwanza.” Mama G akatungulia ndipo wengine wakafuata.

Walilia hapo wakimkumbuka mama Naya. Wakalalamika kwa hili na lile wakimlaumu baba Naya, baba Naya mwenyewe akawa amebaki tu kimya. Upande wa kina Geb wakabaki wamesimama hawajui wafanye nini! Muda ukazidi kwenda bado hawanyamazi. Naya akaona asaidie.

“Mimi nashauri mnyamaze, tumsikilize baba kwanza.” “Nilimuonya mama yako kuolewa na Denis. Nilijua hata...” “Unakaribia kuharibu bibi. Maana hapa mama hayupo, aliyebaki ni baba. Nashauri mtulie tuzungumze hapa, au tubebe tena huu msiba, tukaanzishe tena kule Kiluvya! Hapa kuna ratiba inayohusu mpaka watoto. Lazima tufanye mazoezi kabla hawajaenda kulala.” “Kwa hiyo kweli Naya wewe utaolewa wakati kaka yako hayupo?” “Ndiyo bibi. Tena kesho. Ndio maana nashauri hiki kilio tukihamishie kwetu, tuache nyumba ya watu na ratiba zao. Sasa kwa kuwa bado hampo tayari kumsikiliza baba, nashauri tuhamishe kikao chetu cha familia kule kwetu Kiluvya. Dereva awarudishe. Mimi na baba pamoja na Zayoni tutakuja hukohuko. Tena hatutachelewa.” “Labda wangekula kwanza.” Joshua akatoa wazi.

“Wapo na kuomboleza, sijui kama wataweza kula. Eti bibi yangu? Mtajikaza mle kidogo ili msilale na njaa. Tena wenyewe tunafanana na bibi yangu. Au huoni Joshua?” Naya akamchokoza. “Ila huo moyo ni wa baba yako. Mimi moyo wangu si mgumu hivyo! Wangu wa nyama.” Naya akaanza kucheka. “Sasa bibi na wewe unataka tufanane kila kitu? Acha bwana kulia. Tule, tumshukuru Mungu, mengine tutaendelea nayo. Au unasemaje?” “Mbona sasa mimi nilifichwa?” Bibi akalalamika. “Kwa kuhofia mambo kama haya bibi. Hata hapa usingekuja, kwa kilio. Halafu wanae mpishi mzuri huyo! Chakula chake sitaki kikupite bibi yangu. Na wamekutayarishia yale mambo yako. Acha kulia bwana.” “Basi mwambie baba yako anijibu maswali yangu.” Angalau akasikika ametulia na wanae pia wakatulia.

“Nyinyi mnamjua baba Naya. Kelele hawezi. Mkitulia hivyo, na yeye atatulia na atawajibu. Mkianza kelele ndio mnamfunga mdomo kabisa. Haya anza swali lako bibi yangu.” “Kwanza nataka kujua habari za Bale. Mtoto yule alikuwa mzuri. Mama yake alimuacha mtoto mwenye maana! Na yupo chuo kikuu! Leo mama yake tu ameondoka mnamfunga jela! Nilikwambia mimi baba Naya, hawa watoto wewe hutawaweza bila mkeo, nibaki mimi nikusaidie kuwalea, ukakataa tena kwa jeuri kabisa! Umeona sasa kilichotokea? Maana..” “Huko unakoelekea bibi unaharibi na baba hatakujibu tena.” Zayoni akaingilia.

“Na wewe si jeuri tu kama...” “Naomba tufupishe hiki kinachoendelea.” Akaanza baba Naya. “Bale yupo jela na hajulikani yupo jela gani na tutampata lini. Wapo polisi wanamtafuta Bale angalau kujua alipo ndipo taratibu za kumtoa zianze. Naya anaolewa kesho. Hata yeye nimetoka kumwambia pale hospitalini leo alipokuja kuniona. Nilimwambia hivi, kesho ataolewa. Ndoa yake haitasimamishwa kwa sababu yeyote ile, isipokuwa yeye mwenyewe amaeona hamtaki tena mchumba wake au mchumba wake mwenyewe amebadili mawazo. Nikamwambia jambo ambalo na yeye hakutaka kusikia. Hata nikifa mimi leo. Wakaweke mwili wangu chumba cha maiti, harusi ifungwe.” “Haa!” “Sijamaliza.” Baba Naya akaendelea.

“Harusi ya Naya ipo kwenye mpango wa Mungu, tumeomba na tumemuamini Mungu kuwa ni siku yenyewe, mengine tunakutana nayo kama hivi nyinyi mlivyokuja mkiwa na shangwe, kisha kugeuza hapa kilio, ni yatakayojitokeza mbeleni, hayatabadilisha lengo kubwa la kesho.”

“Kama nilivyotangulia kusema. Hata kifo changu hakitabadilisha kuolewa kwa Naya kwa kuwa hata nikifa leo, na kesho nitakuwa nimekufa, mwezi ujao nitakuwa nimekufa, na mwakani hivyohivyo hakuna kitakachokuwa kimebadilika ila ndoa ya mwanangu. Kufupisha hili, au kwa kumalizia hili bila mjadala kwa kuwa mimi na nyinyi hatukuwahi kukubaliana kwenye chochote kile, kubwa na dogo. Sasa nani anabaki hapa, nani anaondoka sasa hivi kurudi Kiluvya?” Kimya.

“Narudia tena. Hapatakuwa na mjadala wa Bale tena kwa sababu kati yenu hakuna atakayesaidia chochote kile ila kutaka kumchanganya tu Naya. Hakuna msiba tena wa mama Naya hapa. Anayejisikia kuendelea kulia, basi hapa si mahali pake. Tafadhali tuheshimu ratiba na mipango ya watu. Sasa nani anabaki nani anakwenda?” “Tutakuwa hatumtendei haki dada kama kipindi kama hichi yeye hayupo na sisi tusiwepo! Itakuwa sio sawa shemeji.” Akajibu mjomba. “Basi naomba tutulie, tupate muongozo.” Baba Naya akamaliza na kunyamaza.

“Karibuni sana jamani, na poleni kwa matatizo. Ila nataka kuwahakikishia tu, hakuna aliyetulia kati yetu, Bale anatafutwa na pengo lake lipo bayana. Tunaamini muujiza wowote ule unaweza kutokea, hata Bale kuwepo kwenye harusi kesho. Kwa hiyo tunaomba muungane nasi  kwenye kumuamini Mungu, na tuendelee na kile tunachoweza kufanya. Mezani hapo kuna vinywaji. Mnaweza tu kuendelea wakati wakiwahudumia vitafunwa vidogovidogo wakati tukifanya mazoezi na watoto kabla chakula cha pamoja ndipo tuagane tukapumzike kwa usiku huu. Karibuni sana.” Joshua akawakaribisha.

Wakafanya mazoezi hapo, kila mmoja akajua nini chakufanya kesho yake siku ya jumamosi. Harusi hiyo ilikuwa ikifungwa saa kumi jioni hapohapo nyumbani kwa Joshua na kushiriki chakula cha jioni pamoja kumshukuru Mungu kwa harusi hiyo. Kwa hakika kuliandaliwa. Huyo mpambaji aliyekuwa akipamba hilo eneo, alipatendea haki. Siku hiyo jioni, kilichokosekana ni maua tu ambayo yalikuwa yawekwe siku ya harusi yenyewe ili yabakie bado fresh na harufu nzuri. Kwa hakika palionyesha mwenye pesa anaoa! Maneja masoko huyo aliweka pesa yake yakutosha kwenye hiyo harusi, akisaidiwa na marafiki wenye pesa kama yeye.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Waliagana, ikawa Naya anatakiwa kwenda kulala kwa kina Nanaa ili asubuhi wawahi saluni pamoja na wasimamizi wote. “Naomba unisamehe Nanaa. Sitaweza kwenda kulala, wakati najua baba hajisikii vizuri halafu namuacha peke yake kule! Hakika sitaweza jamani. Acheni nikalale tu nyumbani, asubuhi na mapema nikishahakikisha amekula, amekunywa na dawa, ndipo nimuache akiwa anakwenda saluni na mimi ndio nije.” “Naya wewe!” Nanaa akaishiwa nguvu kabisa. Joshua na Geb wakawasikia, wakasogea.

“Kweli Nanaa. Hakuna kipodozi kitawekwa kwenye huu uso kesho, kikakubali bila leo kuondoka hapa na baba.” Bila kuuliza wakawa wamepata jibu. “Nimekuandalia mpaka chumba!” Nanaa akalalamika. “Samahani Nanaa. Samahani sana. Lakini naomba mimi ndio nimrudishe baba Naya nyumbani. Hakika sitaweza kulala na kesho nitaamka nimechoka zaidi, hutanipenda.” “Mwezio amejiandaa kweli kwa ajili yako!” Mama G akaongeza, Naya akaishiwa nguvu akabaki kimya, akamgeukia Joshua.

“Sasa wewe ndoa utaiweza wewe!” Naya akaanza kucheka. “Kesho utamuacha mume, uende kwa baba Naya tena?” “Nikienda kwa baba Naya, nambeba na Joshua wangu. Usiwe na wasiwasi mama.” Wakacheka. “Nanaa usiumie bwana! Naomba unielewe. Ile picha ya baba kuanguka ile jana pale uwanja wa ndege, inanisumbua kweli, sasa nafikiria hiyo hali impate usiku akiwa na hii fujo yote hii! Watamuua baba yangu jamani.” “Kwani hapo bado hayajaisha!?” “Mama! Wewe acha tu. Undugu kazi mama yangu, acha tu. Hawa watu hawajui kumaliza jambo. Wewe si umesikia bado bibi analalamikia mama aliyekufa, kuolewa na baba?” “Jamani!” “Basi ndio hivyo. Na wakijua tu sitakuwepo huko, watampandisha pressure. Hiki kilio kitakuwa cha usiku kuchwa, alilotabiri baba litatimia. Ndoa yangu ifungwe, yeye asiwepo. Sitaki kumpa shetani nafasi. Naombeni mniruhusu tu. Naahidi sitachelewa saluni.” “Sawa.” Na wenyewe wakaafiki. Lakini walimaliza vizuri tu mpaka wakacheza pamoja na vigelegele viliendelea na ndugu wa mama Naya pia walisherehekea.

Usiku Baada ya Rehearsal Dinner.

Waliondoka ndugu wa Naya, nahilo gari. Wakabaki wao kumalizia na maombi wakiikabidhi siku ya kesho mikononi mwa Mungu, wakamuombea na Bale ndipo Naya na baba yake pamoja na Zayoni wakaondoka. Walipofika nyumbani wakakuta gari ya Malon bado ipo. “Hivi nifanyaje baba jamani!? Huyu mtu anataka kuniharibia baba! Mimi namjua Malon.” “Hakika sitamruhusu. Wewe tulia tu.” Wakashuka na kuingia ndani, wakamkuta Malon akizungumza na bibi. “Baba Naya huhitaji chai?” Naya akamuwahi kabla hata ya salamu. “Nitashukuru mama. Naona nina kiu nayo kweli.” “Basi dakika chache tu, nakuletea.” Baba Naya akakaa kochini, Naya akapitiliza chumbani kwake anakolala na bibi yake, wengi wa ndugu walishaondoka kwenda kulala makwao kasoro waliotokea kijijini na bibi. Baada ya dakika chache akapitiliza jikoni kutengeneza chai ya baba yake.

          “Malon!” Baba Naya akaita. “Naam!” “Ulipokuja nyumbani kwangu kwa mara ya kwanza, unakumbuka jinsi tulivyokupokea?” “Nakumbuka mzee wangu.” “Nikakufanya mmoja wa familia bila kukubagua, ukawa kama Bale tu. Ndivyo ninavyofanya kwa vijana wote wanao jisogeza kwenye hii familia bila kujali dini wala kabila. Uwezo wala muonekano. Ndivyo nilivyo.” Akaendelea.

          “Lakini wewe unataka kuweka tabaka ndani ya familia yangu, na SITAKURUHUSU.” Mpaka Naya akashangaa nakusimama huko jikoni. “Joshua ni mmoja wa familia hii. Hilo halitakaa likabadilika tena, na kesho atakuwa mume wa Naya. Sasa basi, kwa kuwa wewe umeshindwa kumpokea kama wewe ulivyopokelewa hapa ndani bila kubaguliwa ila kusambaza sumu kati yake na Bale.” “Mimi nimeongea alichosema Bale.” “Nilishawahi kukwambia alichokuwa akikisema mama Naya juu yako?” “Hapana.” Malon akajibu. “Nilinyamaza mpaka wewe mwenyewe ulipopambana naye. Lakini bado nilipokuwa nikikutana na wewe nilikuheshimu, lakini wewe umeshindwa kuwa muungwana! Unasambaza chuki waziwazi.” Baba Naya akaendelea akimtizama machoni kabisa, bila kukwepesha macho.

“Hivyo basi, hutakuwa tena mmoja wa hii familia. Na hukaribishwi tena hapa.” “Haiwezekani! Yaani unaniadhibu kwa kosa la Bale?” “Labda nikuulize Malon, undugu huo unao utaka hapa ni kwa nani na kwa nini? Maana ulianzana na Naya, ikashindikana. Ukaja kwa Bale. Naye pia umeeleza mapungufu yake mengi tu mpaka amepotea akiwa kwako, kwa sababu ya mapungufu yake kuwa mengi na kukukera sana, ulishindwa hata kumfuatilia tena. Haya, Joshua naye humtaki. Sasa ukisema unaendelea kuja hapa na kuendelea na hii familia unayotangaza ina matatizo, ni kwa manufaa ya nani? Au utanufaika na nini au nani sasa?” “Siamini!” “Labda niambie ni nini unataka kuendeleza hapa, Malon! Ni nini? Au unataka nini? Bale mwenyewe ambae yupo matatizoni, ambaye alikuamini sana, unashindwa  kumsaidia, upo hapa. Unataka nini Malon?”

“Daah! Siamini!” Bado Malon akasikika kama hajaridhika, haamini. “Labda sasa wewe ndio uzungumze Malon. Mimi nikusikilize aina ya mahusiano unayofikiria utakuwa nayo kwenye aina ya watu wa hii familia!” “Basi bwana.” “Usiku mwema.” Baba Naya akasimama kabisa nakumfungulia mlango. Malon akacheka na kutingisha kichwa. Kisha akasimama na kutoka. Naya mwenyewe hakuamini kama ni baba yake.

“Sasa unamfukuza mtu pekee mwenye taarifa za Bale! Utampataje huyo Bale?” “Tutampata tu, usiwe na wasiwasi. Kila uamuzi hapa duniani una jinsi ya kuwajibisha. Bale yupo kwenye kuwajibika kwa maamuzi yake. Nimemuombea rehema, Mungu atamrehemu tu. Ningetamani iwe tofauti na kukupa majibu ya kukufurahisha lakini sina jinsi. Nafanya kwa kadiri ya uwezo wangu kumpata. Na tutampata kwa njia sahihi lakini si kwa kumuharibia Naya. Usiku mwema.” Baba Naya akaingia chumbani kwake na kuwaacha wote kimya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bado Malon Hakubali Kushindwa. Yupo Na Taarifa Za Bale Zenye Mashariti Yaliyokataliwa Na Baba Naya.

Hajui Kukubali Kushindwa.

Na Ameondoka Akisikika Hajaridhika.

Nini Kitaendelea?

Bale Yuko Wapi?

Harusi Ya Naya Na Joshua Bado Ipo?

Inaendelea.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment