Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 34. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 34.

Siku Ya Harusi.

Naya aliondoka kwao na baba yake pamoja na Zayoni akawashusha na wenyewe kwenye saluni ili kukatwa nywele na kutengenezwa vizuri ili na wenyewe wajiwakilishe vizuri. Kisha akaondoka hapo akiimba taratibu tu akielekea saluni. Simu ya Joshua ikaingia. “Mama Kumu?” Naya akaanza kucheka. “Uwe unaniita ita hivyo mara kwa mara ili nizoee kabisa.” Joshua akaendelea kucheka. “Umeamka salama mpenzi wangu?” “Salama kabisa, na maandalizi ya kukabidhiwa mke na Mungu yameshaanza.” “Maandalizi gani?” “Acha haraka Naya. Usiku wa leo si unalala hapa?” Naya alicheka sana.

“Nataka ukiingia hapa, usitamani kutoka.” “Ndio maandalizi mazito hivyo!?” “Sana Naya. Nimesubiri kwa uaminifu wote, eti! Mpaka Mungu mwenyewe ameniheshimu! Acha nisimuangushe Mungu wangu, nimuonyeshe hajakosea, nipo tayari na wewe.” “Jamani Joshua wangu! Kwa hiyo tutakaa hapo mpaka lini ndio tunasafiri?” “Mimi nilikuomba usiku mmoja tu, Naya. Angalau safari yetu ya ndoa ianzie kwenye chumba chetu, kitanda chetu, ndipo tusafiri, twende mapumzikoni kwengine.” “Basi na wewe ujiandae kupata usiku mtulivu. Ni mimi na wewe tu. Bila...” Naya akiwa amesimama kwenye mataa, akisubiria taa zimruhusu huku akizungumza na Joshua asubuhi hiyo, akashangaa Malon anamgongea kioo cha dirisha ya gari.

“Malon!” “Bila Malon!?” Joshua upande wa pili wa simu akawa hajaelewa usiku huo mtulivu anaoahidiwa na Naya bila Malon, anahusika vipi tena! “Hapana Joshua. Malon kwenye kioo cha dirisha langu, asubuhi hii! Weka mute huko kwako asikusikie, mimi  namfungulia mlango nimsikilize.” “Naya!” Joshua akaita. “Tafadhali weka mute Joshua. Weka tu, niamini. Ili tumsikie.” Kwa kuwa walikuwa wakizungumza kutumia spika za gari hiyo ya kisasa ya Naya, Naya akajifanya kama amemaliza mazungumzo, akarudisha simu kwenye pochi kama kumuonyesha Malon ambaye bado alikuwa akimtizama nje ya dirisha la upande wa abiria, akitaka amfungulie mlango, kuwa amemalizana na mtu aliye kuwa akizungumza naye. Kumbe bado Joshua alikuwa hewani ameweka mute kama alivyoombwa na Naya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Naya akatoa loki ya mlango, akaingia. “Naona jamaa yako anahangika kweli kukuharibu akili. Anahakikisha anakupa mavitu ya bei nyingi, ili ujisahau kama wewe unajukumu la familia.” “Na naona kwenye hilo amefaulu. Kwa nini unanivizia mabarabarani Malon!? Nikusaidie nini?” “Mimi siye ninayetaka msaada wako Naya, ni  Bale. Unamuacha Bale anateseka hivihivi?” “Ndiyo.” Naya akamjibu, taa zikaruhusu. “Kweli Naya?! Umepatwa nini wewe?” “Haya ni mapenzi Malon, na msimamo kwenye malengo. Naolewa na Joshua. Tena leo. Ni baba peke yake ndio angesimamisha hii harusi, pengine na Joshua kama atabadili mawazo. Lakini mpaka sasa hivi tunavyoongea hapa, Joshua wangu anajiandaa kwa ajili yangu, na baba Naya anajiandaa kunitoa kwa baraka zote, RASIMI mbele za watu na Mungu, kunikabidhisha kwa Joshua. Upende, usipende. Umuadhibu Bale kwa hili au sisi kwa kutuficha Bale alipo, jua, leo nakwenda kulala kitandani kwa Joshua.”

“Acha kuniumiza kwa makusudi Naya!” “Pole sana, ila sina jinsi ya kukusaidia. Tafadhali acha kunivizia mabarabarani Malon.” “Umeamua kumtupa Bale kabisa sababu ya Joshua?” “Mimi na wewe wote, hata Bale anajua, Joshua si tatizo. Yeye mwenyewe na haraka zake, na ubishi yupo huko alipo. Na japokuwa unajitahidi sana kuwachonganisha Bale na Joshua, lakini Malon, Joshua wangu hajali. Hapa tunavyozungumza pesa yake inatumika kumsaka Bale huko Mbeya. Askari wawili wapo huko wakilipwa na Joshua kumsaka Bale.”

“Hawawezi kumpata Bale kwenye ule mji. Mimi nishatengeneza marafiki pale, najuana na watu, na wakubwa wa polisi mpaka magereza. Chochote kinachoendelea pale naambiwa. Wewe hushangai nimejuaje kama Bale amefungwa na hao askari wenu wanamuulizia kama mmoja wa wafanyakazi wangu?” “Mimi sijui Malon, na hayanihusu.” “Basi jua Bale hawezi kapatikana bila idhini yangu.” Naya akashituka sana. Akaanza kutafuta sehemu aegeshe gari. Akamwangalia akiwa amekunja uso kisha akarudisha macho barabarani.

“Wewe hushangai kwa mji kama ule mpaka leo askari wawili wameshindwa kupata fununu za mtu kama Bale, ila mimi nimejulishwa kila kitu?” “Unamaanisha nini Malon?” Naya akaegesha gari. “Namaanisha hamuwezi kumpata Bale bila mimi.” “Kwa kuwa wewe ni nani na unahusika vipi?” “Najua wewe ni mbishi Naya. Ila jiulize tu, kwa nini mpaka leo wameshindwa kujua alipo Bale?” Naya akatulia akifikiria. “Watu wanaishi kwa akili.” “Ukimaanisha wewe? Kwamba unaishi kwa akili kwa kumfungia Bale?” “Hata ukinidharau, lakini ndio ujue hamtampata Bale.”

“Sasa labda mimi nikuulize Joshua.” “Mimi sio Joshua, ni Malon. Acha dharau Naya, kujifanya gafla umenisahau mimi sababu ya mpuuzi uliyekutana naye jana tu! Hivi nyinyi watu mnakumbuka nilipowatoa kweli au mmesahau kabisa sababu ya huyu mpuuzi.” “Naona umeamua kurudia na yale matusi yako. Wokovu tena basi?” “Hayakuhusu Naya.” “Huyo mpuuzi anayekuumiza kichwa, anakuwa mume wangu Malon. Iwe kwa kupenda kwako au la. Vyovyote unavyomtambua wewe, Joshua ananioa Malon, sibadiliki. Halafu hakuna aliyesahau wema wako ila...” “Ila nini Naya? Ila nini? Baba yako ananifukuza mimi sababu ya Joshua! Hakika nitawakumbusha mimi ni nani?” “Kwa kumficha Bale?!” Naya akamuuliza kwa mshangao sana.

“Kwamba unamuadhibu Bale kwa sababu ya mimi kuolewa na Joshua?” “Na kukukumbusha ulipotoka Naya. Bila mimi usingekutana na Joshua. Pesa yangu ndio iliyokusomesha, na kukupa ajira. Narudia tena, bila mimi usingekutana hata na huyo Joshua.” “Kwani wewe ulinikuta barabarani?! Eti Malon? Maana ulinikuta nikisoma. Japo baba yangu alikuwa akikopakopa na kunyanyaswa akizalilishwa, lakini alihakikisha nipo shuleni. Na shule yangu haijawahi kusubiri. Baba alihakikisha nasoma bila ya kusimama. Tafadhali usije sahau hilo. Sikuwahi kufukuzwa shule sababu ya ada, eti wewe ndio ukanirudisha shule!” “Unasahau vipi Naya wewe! Unasahau vipi hali niliyokukuta nayo?” “Ilikuwa mbaya, wala sitasahau, lakini sikuwahi kushindwa kusoma, wala baba  yangu hakuwahi kushindwa kunisomesha. Mimi sijui ulikuwa ukizungumza nini na Bale. Sijui alikwambia nini, lakini Joshua.” “Mimi ni Malon. Acha..” “Unajua namaanisha wewe.” “Gafla unajidai hunijui Naya wewe!? Hakika mtanikumbuka, mtanitafuta na mtanisihi.” Naya akashangaa sana.

“Mbona unataka kuanzisha vita na mimi bila sababu Malo!? Ni nini nimekukosea wewe?” “Kunililia ukiwa na shida, na kunikimbia baada ya kufanikiwa. Hilo nitakulipa Naya. Nakuonya achana na Joshua, rudisha akili zako kule zilipokuwa. Sisi tulikuwa na malengo makubwa sana, mpaka majina ya watoto tulikuwa nayo! Leo unakwenda kujiingiza kwa mwanaume mwingine tena kwa kunitamkia wazi kuwa eti unakwenda kulala kwake!  Hakika nakuonya Naya.” Naya alibaki na mshangao lakini hofu ikaanza kumuingia.

“Labda nikuulize Malon. Hivi wewe ulitegemea nini kutoka kwangu kwa maisha yale?” “Kipi kigeni ambacho nilikianzisha na kushindwa kuendelea na mahusiano yetu Naya, kama sio ulikuwa ukinitumia tu?” “Malon! Umerudia bangi wewe?” “Wewe ulitaka niache wanawake, niokoke, nitulie na wewe. Nimefanya hayo yote. Nimehangaika, eti leo anatokea mwanaume mwingine baki tu, ndio unaniacha hivihivi! Hakika sikubali Naya. Nguvu ileile uliyotumia kuwa na mimi ukijidai unanivumilia kumbe ili utumie pesa yangu, ndio nguvu hiyohiyo uitumie kujirudi kwangu na tuendeleze familia yetu. Usinifanye mimi mjinga na mtoto.” Joshua naye alikuwa akisikiliza.

“Mimi nilijitoa sana kwako. Nimekupeleka mpaka kwa mama yangu. Ukawafahamu ndugu zangu, ukajidai mkwe, eti leo ndio unanikimbia! Hakika sitakuruhusu Naya. Mimi sio mjinga. Nishaona wasichana kama nyinyi wengi tu. Mnasaidiwa mpaka mnakuwa watu, kisha mnajidai kuwakimbia wanaume ambao wamewasaidia! Hakika sio mimi. Mimi sijinyongi wala sili sumu, lakini nitahakikisha unakumbuka nilipokutoa Naya.” “Malon, nahisi wewe bangi zimeanza kukuharibu kichwa mpaka unasahau unazungumza na nani!”

“Najua sana nazungumza na wewe?” “Sidhani Malon, na umekusudia kujiumiza na kunipa shutuma bila sababu, na hakika siumii Malon. Kama lengo lako ni kunishutumu uniumize, hakika sijali. Nilikufanyia yote. Nilikutaka ukiwa na pesa, na ulipokuwa huna pesa. Na nilikuomba utulie, hata kama hujasoma, mimi ningekutunza. Sikukwambia hivyo mimi ila ukaishia kunikataa na kunisukumia kwa wanaume wengine ukiamini sitapata mwanaume kama wewe? Hukutegemea mimi kama naweza kupata mwanaume kama Joshua, ndio maana ukajiamini kuniacha kila wakati na kurudi vile utakavyo. Sasa hivi umeona nimekomesha huo mchezo wako, ndio unajidai kunitisha!?” Naya na yeye akambadilikia.

“Sasa na mimi nakwambia Malon, hunitishi.” “Huijui jela Naya. Hujui anachofanyiwa kaka yako.” “Hakika sijali Malon.” “Kweli wewe katili Naya na sikutegemea! Yaani upo radhi ukalalwe na Joshua tu, halafu kaka yako, damu yako, aendelee kuteseka!” “Kama nimekuelewa sawasawa ni kuwa sharti la kutupa fununu za Bale,..” “Sio fununu, ni kumuweka huru.” Malon akamsahihisha. “Sawa. Kwa mimi kuachana na Joshua, si ndiyo?” “Yaani hii harusi ya leo isifungwe. Achana na Joshua, tuendelee.” Naya akacheka sana.

“Wewe ni katili Naya! Hakika sikukujua hivyo.” “Wewe nilikutoa jela Malon, bila msaada wako. Tutampata Bale, na tutamtoa jela. Naomba shuka kwenye gari langu. Usinitishe wala kuniwekea hukumu. Sijakutenda lililo baya, wala sikuwa na mpango wa mwanaume mwingine ila wewe tu. Wakati wote nilijua leo ndio ingekuwa siku yetu. Lakini uliishia kutothamini, ukinidharau. Amini unachoamini ili kujiridhisha, lakini kwako sitarudi Malon. Niite jina lolote litakalokufurahisha wewe, lakini kwako sirudi. Na nakushauri safari hii acha bangi kwa ajili yako mwenyewe si yangu, maana kwa jinsi nikikuangalia sasa hivi, umemrudisha yuleyule Malon aliyekuwa akiniliza mchana na usiku. Na mwisho wako sio mzuri Malon. Uliyatoa mapepo, ukayaumiza. Unayakaribisha sasa hivi kwa hasira ambayo ni uongo kabisa hata wewe unajua. Hali yako ya sasa hivi itakuwa mbaya kuliko ile ya mwanzoni. Rudi kwa Yesu, Malon.”

“Acha kunizungusha kwa maneno mengi, Naya. Nakuonya. Hakika nakuonya.” “Utanifanya nini Malon wewe? Kwa kutuficha Bale alipo?!” “Naya! Wewe unanijua vizuri sana. Nakuonya.” “Labda sasa hivi nitambulishe nazungumza na Malon yupi! Yule wa Morogoro, au huyu wa Dar aliyekiri wokovu au...” “Malon aliyejeruhiwa moyo na asiyekubali kushindwa.” “Haya shuka kwenye gari yangu haraka Malon. Naona umeshapandisha hasira, mikono inakutetemeka, utaishia kufanya fujo hapa na unanichelewesha naenda saluni.”

 “Naya!” “Naolewa na Joshua, Malon. Hilo ulikubali au ulikatae, jua nafsi yangu, akili na hiari yangu vimemchangua Joshua, na ndie mume wangu. Wewe nimemalizana na wewe Malon.” “Utarudi tu.” “Kwa namna yeyote unayopanga kunirudisha kwako, jua nampenda Joshua, na ndiye atakayepata kiapo changu cha hiari na dhati kuwa nitasimama naye mpaka kifo.”

“Na kuhusu Bale?” “Hayakuhusu tena. Shuka.” “Nyinyi familia ya ajabu kweli hata naanza kuona Bale yupo sahihi. Mnakwenda kushangilia, mwenzenu yupo matatizoni?” “Hata yeye ningemshauri aoe kama mimi nipo sehemu ambayo wanajua kwa wakati huo hawezi kunisaidia. Bale hajasahaulika. Anatafutwa na mimi naolewa. Ondoka Malon.” “Utakuja kujuta Naya, na hakika sitakuhurumia.” “Kwa sasa sihitaji huruma yako Malon. Nilishaiomba hiyo huruma na kuililia zaidi ya miaka mitano, ukashindwa kunipa kwa sababu hukuwahi kuwa nayo.” Simu ya Naya ikaanza kuita kwenye pochi na mlio kusikika kwenye gari. Malon akaangalia.

“Natafutwa Malon, naomba shuka.” “Utanifanya nini? Sishuki.” Malon akagoma kushuka kabisa, simu ya Naya ikaendelea kuita. “Nilikuwa dereva wako kwa zaidi ya miaka 5, nakuzungusha kwenye gari yangu, sasa hivi ndio unajidai kunifukuza! Sitoki sasa.” Malon akapiga ngumi ya nguvu kwenye gari ya Naya ila upande wa dashboard/pale mbele. Hofu ikamuingia Naya akiogopa asije akampiga maana Malon alikuwa mwepesi sana wa kupiga. Alijua anayo bangi tayari. Hayupo sawa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bado masaa machache harusi ya Naya ifungwe. Malon yupo garini amegoma kushuka na vitisho vingi tu. Nini kitaendelea na Malon amesema hakubali kushindwa!!??  Simu ya Naya ikakata na kuanza kuita tena. Naya akabonyeza sehemu ya kupokelea simu kwa haraka. “Bibi harusi wangu unachelewa bwana! Mimi nimemuahidi Joshua kumpelekea mke nyumbani kwake mapema. Mbona unaniangusha?” “Malon yupo kwenye gari yangu, anafanya fujo Nanaa. Naogopa, mwambie Joshua atakuwa ananiona nilipo.” Hapo hapo Nanaa akampigia simu Joshua. Joshua akapokea. “Mumeo yupo sekunde chache sana afike hapo. Nilishamtafuta, na mimi nina kuja nipo njiani.” Nanaa akaogopa akajua kumbe hali imeshakuwa mbaya.

Naya akabaki akitetemeka anamwangalia Malon akataka kushuka yeye akimbie, Malon akamgundua. “Ukishuka tu hapo, nakuitia mwizi. Watoto wa mjini wakupige mpaka wakuue.” Kioo cha Naya kikagongwa. Akageuka kwa haraka. “Geb!” Naya akataka kushuka kwa haraka, Malon akamrudisha ndani kwa nguvu kwa kumvuta gauni aliyokuwa amevaa.

“Acha kujidai mwehu, Naya.” Akaloki milango yote. Geb akaona. Akajaribu kufungua kwa nje mlango haukufunguka. Bado alikuwa kwenye simu na Joshua. “Yupo naye ndani, ameloki milango kwa ndani na anamzuia Naya kutoka. Nipo nikifikiria kitu chakufanya.” “Naya anahali gani?” Joshua akauliza akiendelea kukanyaga mafuta kwani na yeye alishatoka nyumbani tokea Malon anaingia kwenye gari ya Naya, kama aliyekwisha kuingiwa na wasiwasi kuwa, Malon amejuaje Naya alipo asubuhi hiyo na mapema mpaka kuweza kumpata barabarani! Alipoanza kusikia ukorofi wa Malon kwenye simu, ndipo akamtumia ujumbe Geb kwa haraka na eneo analomuona Naya yupo. Geb alikuwa kwenye ofisi zake, jengo la Magesa hapohapo Ubungo akisubiria muda aelekee nyumbani kwa Joshua tayari kwa harusi. Yeye na watoto wa kiume walishakatwa nywele, na wenyewe walikuwa wakisubiria muda waende nyumbani kwa Joshua ambako wangevaa hukohuko shuguli ianze.

Ndani ya dakika tano, Naya akiwa garini na Malon anamzuia kushuka, Geb amesimama nje ya mlango wa Naya akijaribu kumwambia Malon ashuke wazungumze, Joshua alifika hapo bila hata salamu, akagonga kioo cha dirisha la upande wa abiria wa mbele, alipokuwa amekaa Malon, akagonga na jiwe kwa nguvu sana kama mara mbili tu, kioo kikapasuka vibaya sana. Kabla taarifa hazijakwenda kichwani, akamvuta Malon kwa kupitia dirishani kwa nguvu. Kukaanza kuvutana. Malon anatoa damu, Joshua anatoa damu mikononi wanakovutana na Malon.

Naya akafungua mlango kwa haraka na kukimbilia nje, na Joshua na yeye kwa kutumia mkono mmoja akafungua mlango kwa nguvu, Malon akajivuta kwa haraka na yeye akatoka nje akimfuata Joshua. Kwa asili Malon ni mjenga misuli, mpenda ngumi. Alichokua akifanya Joshua ni kumkwepa na kumrushia ngumi. Geb akakimbia na kwenda kuwaamulia pamoja na mtu mwingine aliyekuwa karibu.

“Sasa nyinyi si mnajidai wajanja kwa kuwa mnayo pesa? Mimi nitawaonyesha kama mimi ni mtoto wa mjini. Hata mtoe mamilioni ya pesa kiasi gani, hamtakaa mkampata Bale.” “Tafadhali naomba nisaidie kurudisha gari ya Naya.” Joshua akamgeukia Geb bila kumjibu Malon. “Twende Naya.” Akaenda kumvuta Naya aliyekuwa amesimama kwa mbali kidogo.

“Hujaumia?” Joshua akauliza kwa kujali. “Wewe ndio unatokwa na damu Joshua! Pole.” “Nipo sawa. Twende.” Joshua akamshika mkono, wakawa wanaelekea alipokuwa ameacha gari yake. Malon akawakimbilia. “Sikubali umchukue Naya. Wakati mimi namtunza na kumsomesha, wewe ulikuwa wapi? Mimi nimehangaika naye, eti wewe sasahivi ndio unakwenda kumzalisha tu, hata hujahangaika naye kama mimi!” Malon akaendelea kuongea akiwa mbele ya Joshua. Alikuwa amebadilika Malon, anatisha kwa hasira.

“Unadai kiasi gani?” Joshua akamuuliza. “Naona hilo ndilo la msingi. Wewe piga mahesabu yako, tujulishe ulipwe.” “Nani amewaambia mnaweza kunilipa mimi!?” Akamgeukia na Geb aliyeongeza. “Mnaweza kunilipa muda na mapenzi niliyompa Naya, alipokuwa akipitia kipindi kigumu? Thamani yake ni nini?” Malon akauliza.

“Sina shida na pesa zenu. Sikuwekeza kwa Naya na familia yake ili waje wanilipe pesa! Naya ni mwanamke wangu, na tulikuwa sawa tu mpaka wewe ulipotokea. Matatizo kwenye wapenzi ni jambo la kawaida. Huwezi ukatokea tu eti na kumchukua akidhani malipo ni pesa! Nendeni kanunue malaya kibao huko mjini muoe. Acheni upuuzi na dharau.” Akataka kumsogelea Naya, Naya akakimbia kwa haraka mpaka kwenye gari la Joshua na kujifungia.

“Hawezi kujificha mjini. Nitamkamata tu. Asijidai sasa hivi mjanja. Alipokuwa na shida zake hakuwahi hata kuthubutu kuniacha. Muulizeni huyo. Hata alipokuwa akinifumania na wanawake, uchi kabisa, mbona alikuwa anarudi mwenyewe bila kumtafuta? Eti sasa hivi namwambia nimetulia na nimeokoka ndio ananiacha kama sio alikuwa akinitumia tu? Sasa kamwambie Naya, nitamkamata tu.”

“Acha kumtisha Naya. Utamfanya nini?” “Atakuja kusimulia nitakapo mkamata. Labda ahame dunia.” “Na ujue nakwenda kukushitaki. Nitaripoti vitisho vyote ulivyovitamka hapa.” “Nenda kasemelee polisi. Nani amekwambia mimi natishwa na polisi? Wewe unaijua polisi mapokezi, mimi najua mpaka ndani, kwa kuishi tokea mtoto. Uliza utaambiwa. Mimi polisi ndio maeneo yangu ya matembezi. Acha upumbavu wewe.” Malon akaondoka, Joshua akarudi kwenye gari na kuondoka. Walishajaza watu hapo. Geb naye akaita mtu ili aje achukue gari ya Naya. Akabaki amesimama akisubiria.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Naya alikuwa ametulia garini kwa mshituko, asiamini kama Malon amemgeuka kwa kiasi hicho! Kutoka kwenye kumbembeleza mpaka kumdai! Akapoa kama amemwagiwa maji. Hata hakuweza kujigeuza hapo kitini, wala kuuliza wanapokwenda. Wote kimya, Joshua akiendesha gari. Simu ya Joshua ikaanza kuita. Akaitizama, alikuwa Geb, akapokea. “Naya ameacha simu kwenye pochi yake hapa, inaita. Nanaa ameniambia ni yeye ndiye anayempigia, anasubiriwa saluni.” “Hapana Geb. Inavyoelekea Malon anamfuatilia Naya. Siwezi kumpeleka popote isipokuwa nyumbani ambako nina uhakika atakuwa salama. Hatatoka hapo leo wala kesho. Kama wanaweza kumfuata hapa wamtengeneze sawa, ikishindikana basi. Mwambie Nanaa wao wakimaliza, wamfuate hapa. Atakuwa sawa tu.” “Kama nimekuelewa vizuri ni kwamba maswala ya saluni kwa Naya tena basi.” Geb akataka uhakika ili arudishe majibu ya kueleweka kwa mkewe anayemsubiria bibi harusi huyo saluni.

“Kabisa. Tafadhali naomba mwambie Nanaa namshukuru, lakini Naya atakuwa sawa tu. Amjie na nguo zake, basi itoshe. Ila kama wakipata mtu wa saluni atakayeweza kuja nao hapa akamsaidia Naya, pia ni sawa. Nitalipia hata na ya usumbufu. Ikishindikana basi, Geb. Leo lazima nimuoe Naya. Sijali atakavyoonekana, ilimradi awe yeye, basi.” “Hata mimi nakubaliana na hilo. Tusije kujilaumu.” “Nashukuru Geb.” “Unahitaji kitu chochote sasa hivi?” “Naomba kama masaa mawili kuanzia sasa ili kuweza kujiweka sawa, mimi na Naya. Atulie kabisa, turudishe mawazo kwenye harusi. Hii siku isipoteze lengo.” Geb akaelewa ndio anaambiwa waachwe kabisa hata hayo mazungumzo yaishie hapo.

“Basi nitawacheki baada ya masaa mawili kuanzia sasa. Na Nanaa pia nitamwambia hivyohivyo. Ila nawasihi mtulie. Msiogope kabisa. Swala la ulinzi hapo lipo vizuri. Hilo nimehakikisha na nitampigia simu Gamba kuzungumza naye tena juu ya hiki alichozungumza Malon. Tujue anamaanisha nini anaposema hata tufanye nini hatutaweza kumpata Bale!” “Sijui Geb, lakini mimi kuna kitu nahisi hakipo sawa. Haiwezekani kwa askari wawili, wazoefu, na kwa magereza machache hivyo awe Bale anashindwa kupatikana!” “Unahisi nini?” “Siwezi kusema moja kwa moja, ila nataka tu kukwambia kuwa, kuna kitu hakipo sawa na yeye Malon ndiye anayejua. Na kama ulivyomsikia leo, ili asaidie ni Naya amrudie. Sasa sijui! Wazo la kuzungumza na Gamba naunga mkono. Naomba unijulishe.” “Sawasawa. Naya ananisikia?” Geb akauliza. Joshua akamgeukia Naya aliyekuwa ametulia sana.

“Upo Naya?” “Anakusikiliza.” Joshua akamjibia. “Najua upo kwenye mshituko na yote aliyoyafanya  na kuzungumza Malon. Naomba nitoe tu ushauri, tusubiri kwanza kumshirikisha baba Naya, iwe ni mpaka tumejua nini chakufanya, ili tusimuongezee wasiwasi usio na jibu. Na ashirikishwe endapo tu Naya unabadili mawazo juu ya harusi.” “Mimi naolewa na Joshua. Leo. Mengine nitajua mbele ya safari.” Akajibu Naya.

“Basi naomba tujipange kabla hatujaongeza sintofahamu kwa baba. Ameruhusiwa kwa masharti ya mapumziko ya siku mbili mfululizo. Nashauri ibakie hivyo. Atulie kabisa wakati sisi tukijipanga.” “Hata fujo alizofanya Malon hapa nisimwambie!?” “Hapana Naya.” Joshua na Geb wakajibu kwa pamoja. “Hana atakachofanya au kusaidia kwa sasa. Fujo zimeshatokea, ameondoka. Leo nashauri kama alivyosema Geb, tuache iishe hivyo. Haina sababu. Mzee bado hayupo sawa.” “Sawa. Maana hata leo asubuhi alikuwa akisema anaomba muujiza wa Bale atokee hata asubuhi hiyo. Kwa hiyo basi acha tu nimuache.”  Naya mwenyewe akaafiki.

“Wazo zuri. Acha niwaache mkatulie. Ila si tumekubaliana harusi bado ipo? Eti Naya?” Geb akaweka msisitizo wa swali kwa Naya kama ambaye anamjua Joshua vyakutosha na maamuzi yake. “Ipo Geb. Lakini!” Akajibu Naya na kuwatia wasiwasi kidogo. Joshua akamgeukia akiendelea kuendesha akielekea nyumbani kwake Goba akitokea Ubungo.

“Nini tena!?” Joshua akauliza kwa wasiwasi kidogo. “Nataka tu kusema mimi nampenda Joshua kwa dhati. Sijampendea pesa wala sijamuuacha Malon kwa sababu ya tamaa kwa Joshua. Mungu wangu nishahidi jamani. Mimi sijamkimbia Malon baada ya kunisaidia sana. Sikuwa nikimtumia hata yeye Malon anajua kuwa anadanganya na amekusudia kuniharibia tu kwa Joshua. Nakupenda Joshua. Na Malon nilikuwa nikimvumilia tu si ili kunufaika naye, ni kwa kuwa mimi nilijua kila mahusiano yapo na matatizo yake, nikawa nikivumilia. Ila ni kweli hakuwa akijua kujirudi, mimi ndiye niliyekuwa nikijirudi hata kama yeye ndiye aliyekosa. Pengine hilo ndilo kosa langu. Ila mimi sina tabia za tamaa. Na Mungu wangu ni shahidi.” Naya akaendelea akisikika kujitetea kwa hofu.

“Hata kama leo Joshua akifukuzwa kazi na kupoteza kila kitu, mimi nitamtunza Joshua wangu bila shida. Hata kama kwa kurudi kuanza kuishi naye kwa baba Naya wakati tukijipanga upya.” Mpaka Joshua mwenyewe akacheka kama Geb. “Kweli Joshua. Hakika sitakukimbia mimi. Hata uugue sasa hivi au uwe mlemavu wa kitandani tu huwezi hata kugeuka, ujue mimi nitabaki na wewe mpaka wewe mwenyewe uniache.” “Nashukuru Naya. Na naomba usilie. Achana na mambo ya Malon.” Joshua akaendelea.

“Ni jana usiku tu, Geb alinipigia baada ya kuachana pale na kunitahadharisha na maneno anayosema huyu Malon. Akanionya niwe nayo makini sana. Haswa kipindi hiki anachofanya juhudi zote kukurudisha kwake. Anaweza kuongea chochote ili tu kumwaga sumu ya chuki na hata kama ni kweli Bale alisema, mtu mwenye hekima, asingeweza kuzungumza. Angenyamazia tu. Anaongea waziwazi kusudi tu kutuvuruga. Usijali juu ya maneno ya Malon.” “Na pia si yakupuuza Joshua.” Akaongeza Geb na kuendelea.

“Katika kuropoka kwake akiwa na hasira amezungumza maneno mengi ambayo inabidi tukitulia na mambo ya harusi yakiisha, kama bado Bale hajapatikana, lazima kutafakari zaidi kujua jinsi ya kuendelea kuanzia hapo.” “Sawa Geb. Lakini lazima leo tufunge ndoa.” “Hilo limekaa sawa kaka. Tutakuja na watoto kama tulivyopanga na nitamwambia na Nanaa afanye hivyohivyo. Hata yeye walimpambia hotelini tu, chumbani kwake. Kwa hiyo nafikiri ni kitu kinachowezekana.” Wakakata simu baada ya kukubaliana. Joshua akaendelea kukanyaga mafuta. Wote kimya kila mmoja akiwaza lake.

Nyumbani Kwa Joshua.

Kukawa kimya mpaka alipofika nyumbani kwake mlinzi akamfungulia geti wote wakiwa kimya.  Joshua akavuta gari mpaka karibu na mlango, akashuka na kwenda kumfungulia Naya mlango na kwa kuwa Naya alishazoea kufunguliwa mlango, akasubiria kitini. Akamfungulia. Lakini kabla hajashuka, akageuka na kuanza. “Nakupenda Joshua. Nakupenda sana mpenzi wangu. Naomba Malon hata asikuharibu akili. Mimi sikupendei pesa na sikutumii. Nakupenda na ninakuhitaji. Naomba usiniache sababu yake kwa kuwa hata ukiniacha wewe, ujue hatanioa. Shida yake ni asinione mimi na mtu wa maana kama wewe. Alipokuwa akirudi na kunikuta na wanaume wa ajabu, hakuwahi kulalamika ila kufurahia kuwa utabiri wake umetimia. Sasa, sasahivi amenikuta na wewe, ndio anahangaika.” Naya akaendelea kujitetea akibembeleza.

“Haya yote aliyoyasema leo, ujue ni njia tu ya kuniharibia kwako baada ya kukuona upo na msimamo, na huna mpango wa kuniacha ndio maana amekuja kwa nguvu zote, maana hajawahi kuyasema haya hata mara moja na kwa mwanaume mwingine yeyote. Naomba uniamin...” “Achana na Malon. Naona anataka kukuharibu wewe akili. Usimfuatishe. Atakuharibia siku yako ya leo, naomba tulia. Mimi nimeshamuelewa ndio maana unaona hata sishindani naye kwa maneno wala ngumi. Najua ni mfa maji, hataacha kutapatapa. Ila kama nilivyokwambia, kukusikia hivi, kunazidi kunitia moyo.”

“Na kama nilivyosema, nahisi kuna kitu hakijakaa sawa Naya. Sitaki kusema moja kwa moja nisije nikaweka mawazo yasiyo sahihi kwenye mioyo ya watu kwa haraka, nakufanya wote tufikiri kama ninavyofikiri mimi halafu ikawa sio sahihi tukashindwa kupata mawazo tofautitofauti yakutusaidia. Ndio maana nakuwa kimya kila anapozungumza ili kumsikia yeye zaidi. Najua katika zungumza yake ya jazba naweza kuokoteza neno moja.” Naya akakaa akakunja uso.

“Sasa kama leo umeokota nini!?” “Acha niweke yote kwa pamoja.” “Kwa hiyo bado unanipenda?” Naya akauliza na tabasamu la penzi. “Ngoja nifikirie.” Naya akacheka sana. “Vile ulivyoniokoa kama ninja!” Joshua akacheka mpaka akainama. “Mimi nikajua ungepigana leo!” “Aniharibu muonekano wangu wakati leo nataka niweke kumbukumbu ya mpaka vitukuu!!” Naya alicheka sana. “Kwa hiyo hutaki ngumi!” “Mikono hii ya kalamu, mama Kumu! Najua mipaka yangu.” “Bora mpenzi wangu. Ila nakwambia ukweli kabisa, hivyo unavyomnyamazia ndio ujue unampandisha hasira.” “Nimemuona! Ndio maana anaropoka sana! Hajui mimi sitishwi hovyo.” Akajisifu Joshua na kumshika mkono Naya kama anayetaka kumshusha.

“Mkono unatoa damu Joshua. Twende nikakusafishe mpenzi wangu.” “Joshua Kumu anavyopendwa!” “Nakuhitajiwa pia.” Joshua akacheka sana wakiingia ndani. Walichofanya ni kusafisha mkono na kuhamia kochini, kukaanza kubembelezana na mabusu ya kina. Nanaa na timu yake wanaingia hapo, hawakuamini. “Mimi nilijua hali ni mbaya, tunakaribia kuahirisha harusi!” Nanaa aliingia bila hata hodi, akiwa na mizigo pamoja na mtu mmoja tu. “Bwana harusi wangu yupo tayari kunioa. Harusi ipo.” Wakaendelea na yao yakiwa yamebakia tu masaa machache ndoa yao ifungwe.

Kisasi.

Huku kwa Malon alijawa hasira, na ndipo alipoamua kuendelea na mipango yake ya kikatili. Alikwenda kwa Naya akiwa anampa nafasi ya mwisho kabisa. Alijiambia anakwenda kuzungumza naye kwa mara ya mwisho kuona kama anaweza kumbadilisha mawazo. Moyo wa Malon ulibadilika kabisa na kuanza chuki ya ajabu kwa familia hiyo baada ya mazungumzo yake ya mwisho na baba Naya usiku uliopita.

Wakati Joshua akisikiliza mazungumzo ya Malon na Naya garini na kuyarikodi kwa uthibitisho endapo chochote kikitokea, kumbe Malon naye aliingia garini akiwa anarikodi na yeye mazungumzo yake na Naya kwa kutumia simu yake kama alivyofanya siku iliyopita. Alianza kurikodi tokea anakwenda nyumbani kwa Joshua akiwataka ndugu wa Naya wazungumze pembeni na kukataa kumsikiliza na kwenda tena nyumbani kwao akitaka wazungumze, wakahitimisha na baba Naya kwa kumuaga rasmi kama anayemtoa kwenye familia yake. Malon alikuwa na mazungumzo yote hayo kwenye simu yake.

“Si wanajidai wajuaji na wamesoma! Sasa acha niwaingize shule ya mtaani niliyohitimu mimi.” Akaadhimia Malon. “Wanajidai wanavijihela hapa mjini, sasa acha niwaonyeshe na mimi pesa ninayo, sihitaji chechi zao ila kuwatia adabu wasiwe wanachukua wake za watu huku wakiwarubuni kwa mali. Wapuuzi wakubwa.” Malon akazidi kujipandisha hasira. Alichofanya akiwa na hasira, ni kutoa hiyo simu mara alipofika nyumbani kwake na kuanza kupakuwa mazungumzo ya siku hiyo yote kwenye kompyuta yake kama alivyokwisha pakua ya siku iliyopita.

Akaanza kuyatengeneza yale mazungumzo ya kwenye kompyuta akiwa ameyatengenezea faili jingine tena la kisasi. Hayo ya mara ya pili ya kisasi, akaanza kuyatengeneza atakavyo yeye. Akikata mazungumzo mengine na kubakisha mazungumzo yanayomuhusu Bale tu, tena majibu aliyoyataka yeye. Jinsi alivyokuwa akizungumza nao akiwaambia anayo jinsi yakumpata Bale, anachohitaji ni hiyo familia tu kujitenga pembeni na kusikiliza, lakini wakakataa kumtoa Joshua, wakataka na Joshua awepo. Akaweka na ya mara ya pili alipowafuata nyumbani, baada ya kutoka kwa Joshua.  Na bado akafukuzwa bila kutaka kumzungumzia tena Bale! Na mazungumzo yake na Naya pia asubuhi hiyo garini! Tena, akayatengeneza vizuri akitoa mengine mengi tu, na kubakisha aliyojua yanaweza kusikika vile atakavyo yeye, endapo akiongeza nguvu kidogo.

Kwa Bale.

Malon alichukua hatua ya haraka sana usiku mara baada ya kupiga simu ya Bale na kumkosa, usiku ule alipopigiwa simu na Naya akimuulizia Bale na kumwambia asubiri atampigia kwanza Bale, akikubali awape namba yake ndipo atawarudishia majibu na kupotea kabisa, siku tano zilizopita. Alichofanya Malon alipomkosa Bale akawazimia simu Naya na ndugu zake, akaanza yeye kumsaka Bale. Malon mtoto wa mjini akazipata habari za Bale kwa haraka sana. Akamtuma mmoja wa askari ambaye walitengeneza naye mahusiano hapohapo mjini Mbeya, kwa makusudi kabisa ili wamlinde yeye na chochote kitakachotokea. Akataka hao askari wawe upande wake.

Walichofanya Joshua na Geb siku nne zilizopita, yeye Malon alikifanya kwa haraka bila shida. Aliwajua askari kwa kuishi nao akiwa amefungwa jela. Aliielewa lugha yao kwa urahisi sana na kuweza kupanga nao mambo. Baba Naya anafika Tunduma kumsaka mwanae, askari wa Malon alishakuwa amepata habari kamili za Bale, na uzuri akawa Bale amerudishwa viwanja vya nyumbani, Mbeya kwenye makazi ya Malon. Malon akatoa pesa nyingi tu kutolewa kwa Bale. Isivyo kawaida, akahakikisha na jina lake linafutwa kabisa wala hakuonekana kama alipitishwa huko magerezani.

Baba Naya na kina Joshua wanatua jijini Dar wakiwa wametokea Mbeya na Tunduma, hawajui Bale alipo, kumbe Bale alihamishwa tu. Kutoka rumande, akapelekwa asipo pajua na asio wajua. Akaambiwa akae hapo asubirie maelekezo na akaagizwa asitoke lasivyo atarudishwa rumande ili akahukumiwe kwa makosa yake. Kwa kuwa amri hiyo alipewa na askari hao waliomtoa, tena wenye sare kabisa, Bale akatii bila shida. Tena akaona ni bora hapo alipohamishiwa kuliko rumande. Ikawa kama amefungiwa tena, lakini anatoka tu nje kama kawaida, akitaka mwenyewe, bila kulindwa, na yeye hakuwa akienda popote, na kurudi ndani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Malon akaandaa ushahidi wake, akasubiri kama ataweza kuingia nyumbani kwa Joshua siku hiyo jioni. Kama angekuwa hajafukuzwa kwa kina Naya, Kiluvya, angerudi na kuondoka na usafiri wa ndugu, kwenye kibasi. Lakini Malon alifukuzwa mbele ya bibi. Anarudije tena kuomba apande basi ya kwenda harusini na yeye hatakiwi! Akatulia akiwaza mpaka ilipofika mida ya harusi hiyo kufungwa akatoka hapo ili kwenda kujaribisha kama ataweza kuingia, lakini alishindwa kabisa. Kulikuwa na ulinzi mkali, tena askari wageni kabisa. Hata walinzi wa Joshua mwenyewe walikuwa wakipokea amri kutoka kwa askari hao waliokuwa wameletwa rasmi kuhakikisha Joshua anaoa jioni hiyo.

Hakuna magari yaliyoruhusiwa kuingia ndani ya ua. Kulikuwa na ulinzi haswa. Unaingia kwa kadi, unaachana na gari yako nje ya geti, askari maalumu ndio wanakwenda kukuegeshea gari yako. Jina lako lifanane na kwenye kadi. Hata ndugu ilikuwa hivyohivyo mpaka watoto. Asiyekuwa na kadi siku hiyo hakuruhusiwa, na picha za Malon zilikuwa getini askari wote walionyeshwa kuhakikisha haingii humo. Kwanza watu hawakuwa wengi. Joshua asiye na ndugu ila wafanyakazi wenzake, tena wachache tu na familia ya kina Magesa. Na ndipo wakaongezeka ndugu wa upande wa mama Naya. Upande wa baba Naya pia walikuwepo lakini wachache, kwa hakika watu walikuwa wachache sana.

Pakaandaliwa vizuri, kila kitu kilipangiliwa kwa ufanisi bila mwanya wa makosa. Geb muendesha shuguli nzima alishafikiria kila kosa na kutafutia ufumbuzi kabla ya muda wa harusi kufika. Hapakuwa na jambo lililoendeshwa kiholela. Halafu ni Joshua Kumu anayeoa! Pesa ipo, amekaa miaka yote akiiota hiyo siku atakayopewa mke! Hakutaka kosa litokee. Malon alisubiri nje ya geti mbali kidogo akisubiria kama kunaweza kupatikanika na mwaya aingie lakini hapakuwa na nafasi. Walioacha magari yao nao walipewa namba maalumu. Wakati wakutoka, unaonyesha namba yako, unaletewa gari yako nje ya geti, na kuondoka. Malon alipoona amebakia peke yake pale nje, akaona aondoke kabla askari hawajamfuata.

Naya Kumu.

Naya alipendeza haswa pamoja na wapambe wake wote mpaka watoto. Baba yake mwenyewe ndiye aliyemkabidhisha kwa Joshua mbele ya umati na mchungaji, wakatoa viapo vyao hapo, wakabarikiwa, Naya akawa Naya Kumu rasmi. Zikapigwa picha za kutosha ndipo Naya na Joshua wakaenda kubadilisha nguo wakati wageni wao wanaingia kwenye cocktailCocktail yenyewe iliandaliwa kwa umaridadi wa namna yake. Viliwekwa vitoweo vya kila namna, kwa pishi lake tena vizuri. Vikapambwa kwa kuvutia waalikwa walio bahatika kuingia harusini. Wakaachwa waalikwa wote wakila na kunywa, na mazungumzo ya hapa na pale, wakati kwa mara ya kwanza, maharusi hao wapya, wanapata faragha ya penzi kabla ya shuguli nzima ya sherehe iliyoandaliwa.

Kukiwa bado mapema tu, mida hiyo ya jioni, hata giza halijajaza dunia yao, maana ndoa yenyewe ilifungishwa ndani ya dakika 20 tu, hatimaye Joshua akajikuta na mwanamke chumbani kwake, tena wake wa baraka takatifu. Chumba hicho kiliandaliwa haswa, Naya akabaki akimshangaa Joshua. Kulijawa mishumaa kila mahali. Tena iliyopangiliwa kwa umaridadi, ikitoa harufu nzuri iliyojaza chumba kizima mpaka bafuni kwa kuwa iliwashwa muda mfupi tu wakati wanakaribia kuingia hapo. Kulikuwa na maua rosi yamemwagwa humo chumbani mpaka kitandani yaliwekwa kwa ustadi.


Bafuni mpaka kwenye sinki ya kuogea kulikuwa kukielea vimatawi vya maua rosi, yenye rangi nyekundu. Japokuwa chumba cha Joshua kilikuwa kizuri kabla ya yote hayo, lakini Naya mwenyewe aliweza kutambua hiyo juhudi ya makusudi ya siku hiyo.

Kitanda Cha Ndoa.

“Ndio maandalizi yote haya!” “Hiki chumba hakijawahi kuingia mwanamke Naya. Kitanda hiki hakijawahi kulaliwa na mtu mwingine isipokuwa mimi tu. Sijashika mwanamke, nikafanya naye mapenzi, kwa umri wa kumzidi Zayoni. Nilikuwa nasubiria kwa hamu mno. Haya yote nimeandaa kwa ajili yako Naya. Kukuonyesha natambua na kuhitaji uwepo wako hapa. Nakupenda sana Naya.” “Jamani Joshua wangu! Nakushukuru na asante kunithamini. Naamini tutakuwa na wakati mzuri wageni wakiondoka.” Naya akamsogelea ili ambusu.

“Hiyo cockail huko, imenigarimu zaidi, ili kufanya wageni wanisubirie angalau kwa lisaa na dakika 20, nipate na wewe muda hapa kitandani.” “Joshua!” Naya hakuamini. “Hakika nimemwambia Geb nahitaji huu muda na wewe tu. Yaani tukitoka hapa, tunakwenda kula nao huko chakula cha usiku, wewe ni mke wangu kabisa, nikamshukuru Mungu kwa yote.” Joshua alishamgeza akaanza kumbusu shingoni akimfungua gauni jeupe alilokuwa amevaa. Naya akaanza kucheka akifurahia. “Nikusaidie kutoa shela?” “Hiyo ni kazi yangu leo. Nilikuwa nikilala hapa, nafikiria huu wakati. Hatujasimama hapa kwa bahati mbaya, Naya.” Joshua akaanza bila papara.

Naya ambaye alikuwa hajawahi kumvulia mwanaume mwingine ila Malon. Asiyejua mikono ya mwanaume mwingine ila Malon. Ufanyaji wake wa mapenzi ulikuwa ukiendana na Malon, jioni hiyo akaonjeshwa mengine kwa kituo na utuli, penzi la Joshua. Joshua alikuwa mtulivu mno na alifanya kila kitu kwa hisia akimuuliza kama yupo sawa, na kuhakisha Naya yupo tayari kwa kila safari anayoanzisha. Joshua alifululiza mchezo kwa makini mno mpaka wakamaliza.

“Joshua wewe ni mtaalamu wa mapenzi kama uliyesomea bwana!” Joshua alicheka sana. “Kweli mapenzi ni sanaa ya ajabu! Natamani tusitoke wala kumaliza, Joshua! Tukae tu hapa kitandani. Unishike hivihivi.” Hapo Joshua akajisikia vizuri. “Nimefurahi kama umefurahia. Hujaumia kweli hata kidogo!?” “Aisee wewe upo makini Joshua, mpaka umenigusa moyo wangu! Unanijali mpaka kwenye mapenzi!” “Nywele zako zinasema tofauti Naya. Nanaa atanichukia.” Naya akajishika kwa haraka.

“Bwana Joshua!” “Hukuwa umeelewa nilipokwambia hali mbaya! Nilikuwa na uchu na wewe Naya! Hiyo shingo nilikuwa nikiitizama, nameza mate nisiamini kama ipo siku midomo yangu itafanikiwa kupita kama leo.” Naya akajifunika kwa haraka akicheka kwa aibu. “Joshua! Kumbe ulifika mbali hivyo!” “Leo pale kwenye kochi nilikuwa siwezi kusimama, bora alivyokuja Nanaa. Nilitamani uendelee kunilalia vilevile.” “Nilijua, na mimi nikaanza kuzidiwa pale.” Wakacheka.

“Nakupenda Joshua. Nakupenda sana. Naomba usije badilika. Unihitaji hivihivi.” “Mungu atanisaidia Naya. Naamini na nimekusudia kutorudia kosa la baba yangu. Namsihi Mungu wewe ndio uwe wa kwanza hapa ndani na wa mwisho, mpaka kifo.” “Na mimi.” Mapenzi mengine yakaanza tena. Naya hakujali nywele wala urembo tena. Joshua mpenda kuchezea nywele, kila wakati Naya alisikia mikono yake kichwani, zaidi alipokuwa akinyonya midomo yake. Hodi ya mlangoni ikawatoa katikati ya penzi.

“Naya anatakiwa kutengenezwa kidogo kabla ya tafrija.” Alikuwa Nanaa. Joshua akaangalia saa. Zilikuwa zimebaki dakika 6. “Mbona unanipunja muda wangu Nanaa!?” “Joshua wewe! Unakaba mpaka sekunde!?” Nanaa akalalamika nje ya mlango. “Usiku wa leo wote wako Joshua! Nipe Naya akatengenezwe bwana. Geb hataki kupoteza hata dakika moja ya ratiba. Mwishowe ataingia ukumbini akiwa hayupo nadhifu.” “Basi Nanaa, anakuja. Mpe dakika 3 tu.” “Naya, naomba usichelewe.” Akamsikia Naya akicheka ndani. 

Tafrija.

Wageni wote walikuwa wamekaa kwenye chumba hicho cha tafrija wakiwasubiria bwana na bibi harusi hao. Mwendesha ratiba akaomba watulie ili maharusi hao waingie. Mlio mzuri bila maneno ukaanza kusikika. Uliporudia mara ya pili, ikasikika sauti ya Joshua kwenye kipaza sauti akiimba vizuri sana. Watu kimya wakimtafuta, aliporudia kwa mara ya pili, Joshua akawa akiingia ukumbini na kipaza sauti akiimba. Watu wakaanza kupiga makofi lakini MC akaomba watulie kidogo, ndipo ikasikika sauti ya kike ikipokea. Alikuwa Naya Kumu.

Naya aliingia akiimba kwa sauti nzuri, akipandisha na kushusha kwa ustadi sana wimbo wa kwanza kabisa Joshua kumuimbia wakiwa botini. Watu wakashindwa kuvumilia, wakaanza kupiga makofi wakishangilia sana. Naya aliimba kama watu wawili tofauti. Ndipo akapokea Magesa. Akaimba kwa kujiamini na kuvutia wengi. Aliimba bila kukosea, bibi yake akasimama kumshangilia mpaka pale mbele na kumbusu kabisa akionekana amehamasika haswa. Joshua akampokea, akaja Naya, wakati Magesa anamalizia, Naya na Joshua wote wakawa wamefika pale mbele alipokuwa amesimama Magesa. Wakamsaidia kumalizia. Wakaimba wote watatu. Naya macho kwa baba yake kila wakati akiimba mpaka machozi kwa hisia zote wakimshukuru Mungu wao, na kuzitangaza rehema zake hapo ukumbini.

Hisia kwa wakati huo zilizokuwa zikiendelea hapo kwa Naya, ni kutamani mambo yaishe hapo kwa haraka, arudi kitandani na Joshua. Kila wakati alirudia kumnong’oneza sikioni akimwambia anampenda. Joshua akajua amemtendea haki kitandani, maana hata sauti yake sikioni ilisikika ya huba. Ukweli hata hapo kwenye tafrija Naya na Joshua pia walipendeza sana. Wenzie kwenye kitengo chao wote walikuwepo pamoja na viongozi wenzake Joshua. Tafrija ilikuwa fupi tu, hapakuwa na mambo mengi. Joshua na Naya wakasimama mlangoni wakiaga watu kwa kushika mkono mmoja mmoja. Joshua alikuwa na cheko huyo, ungejua ametulizwa. Hata usoni alionekana ametulia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mwishoni kabisa, kama kawaida yao, wakabaki wao tu. Yaani na kina Magesa na baba Naya wakipongezana na kumshukuru Mungu pamoja ndipo wakahitimisha siku hiyo. “Twende nikusindikize baba Naya.” Naya akamsogelea baba yake na kumshika mkono akitaka watoke naye, baada ya kuaga, akitaka akapumzike. Kila mtu alimuelewa, ni jana yake tu alikuwa hospitalini amelazwa. Alikuwepo hapo akijikaza tu, lakini ukweli alitakiwa bado awe amepumzika.

“Nashauri Joshua ufuate nyuma. Unaweza kushangaa mke yupo Kiluvya!” Ukazidi utani hapo, wakimtania Naya na baba yake. “Nikienda nitarudi. Nakwenda kuhakikisha ame...” Watu wakaanza kucheka. “Jamani kwani ni vibaya!” “Basi ndoa itakushinda au itabidi baba Naya ahamie hapa, au Joshua ahamie Kiluvya.” “Jamani mama! Si hata Joshua alisema nitakuwa nakwenda kutembea!” “Haya naomba msindikize baba, na Joshua anakuja kumuaga, urudi Naya. Usiniletee utani mimi. Na wewe Nanaa kusanya vifaranga vyako, weka kwenye gari, twendeni. Naya usitoke leo hapo getini.” “Sawa mama. Mimi namsindikiza tu baba Naya mpaka..” “Kwenye gari tu. Zayoni atakwenda kumpikia chai, na sisi kesho tutawapelekea chakula.” “Kweli mama?!” “Kabisa. Si anao wageni bado pale?” “Ndio maana nilikuwa na wasiwasi nani atamsaidia!” Naya akaongea akimwangalia baba yake.

“Naomba tuliza mawazo, Naya. Ratiba yao ya chakula yote imeandaliwa. Watakuwa wakipelekewa chakula mchana na usiku. Zayoni atasaidiwa mambo ya dukani. Mzee atapumzika. Nataka na nyinyi mpumzike kabisa. Usiwe na wasiwasi. Umesikia Naya mwanangu?” “Nashukuru mama yangu. Hapo nitatulia kabisaa. Ilimradi baba Naya anachakula! Anapata muda wa kupumzika, hapo sina neno. Na sasa hivi nakwenda kumchukulia chakula...” “Nimekwambia maswala ya chakula niachie Naya. Mbona hivyo!?” Wote wakaanza kucheka tena.

“Cha usiku huu tu! Hajala vizuri. Nimeona sahani yake wakati inatolewa pale ukumbini wakati wa sherehe. Hajala vizuri.” “Basi kazi ipo! Mimi nilijua tupo naye pale mbele kumbe akili ipo kwa baba Naya!” Nanaa akaongeza akimshangaa bibi harusi wake. “Baba anaumwa jamani!” “Naomba tulia Naya. Mimi mzima. Sikula sana sababu nilikula sana pale kwenye cocktail. Nilikutana na vitoweo vyangu ninavyovipenda, nikala kupitiliza. Tulia hapa na mwenzio.” Baba yake akamwambia. “Basi twende nikakuge. Kesho au kesho kutwa, nasafiri mwenzio.” Naya akamvuta mkono baba yake, wakawa wanaondoka, nakuacha wengine wakicheka.

“Ndio unaachwa hivyo!” Mama G akamchokoza Joshua. “Subutu! Nampa dakika 5 tu, na mimi nakwenda kumkumbusha ameolewa, na tunaaga wote, anatakiwa kurudi.” Wakaendelea kucheka wakitaniana. 

Kwa Malon&bale.

Wakati Joshua akifaidi penzi la mkewe, Malon anaumia akiona amesalitiwa na kudhulimiwa mwanamke wake. Hakuwa na mwingine wakumlaumu isipokuwa Naya na baba yake. Zayoni akawa amejiingiza yeye mwenyewe kwenye orodha ya wakosaji wa Malon, kwa kumuuliza swali mbele ya watu. Malon akahesabu kuwa, alimfedhehesha mbele ya umati. Malon alishindwa kulala wala kutulia usiku huo kila alipokumbuka Naya yupo na mwanaume mwingine usiku huo na si yeye tena! Kwamba yupo mwanaume mwingine anamgusa Naya kimapenzi! Alishindwa kabisa kulala. Usiku huohuo akakusanya vitu vyake akatoka jijini Dar, safari ya Mbeya ikaanza akiwa amejawa hasira haswa. Aliendesha usiku huo mpaka kesho yake mchana anafika Mbeya, bado hajachoka kwa hasira.

Akamtafuta askari aliyemuomba amtoe Bale rumande, akampeleka alikomficha Bale aliyekuwa amelala bado na uchovu wa kufungwa. Bale alishituka sana na kushangaa alipotoka usingizini na kumkuta Malon ndiye anayemuamsha. “Nini kinaendelea Malon!?” “Ni unyama na ukatili mtupu Bale! Mimi nimekuhurumia, nikaona nikusaidie tu. Japokuwa nilikuwa na mambo mengi Dar, lakini nikashindwa kuvumilia. Nikatumia pesa nyingi sana, kuhakikisha nakutoa jela na kukufutia makosa yako yote.” Malon akiwa na hasira akamwambia mengi ya kumuumiza sana Bale.

Jinsi alivyotupwa na ndugu zake. Hawamjali. Wanaendelea na maisha kama yeye sio mmoja wao. “Naya ameolewa jana. Na sherehe kubwa kabisa. Ndugu zako ni wakatili Bale, sijawahi ona! Nimewafuata zaidi ya mara mbili nikiwasihi tusaidiane kukutafuta, wamekataa na bibi yako pia alikuwepo ila akanyamazia na kukubali mambo yaendelee hivyohivyo, pamoja na wajomba zako! Eti baba yako anasema upo jela kwa kujitakia na unalipa garama.” Malon akamsikilizisha mazungumzo kati yake na ndugu wa Bale wakimjibu juu yake yeye Bale, yale tu aliyotaka yeye Malon, Bale ayasikie.

Mpaka Bale anamaliza kusikiliza, akaamini kile alichokuwa akikihisi na kumlalamikia Naya na baba yake siku chache kabla hajaondoka nyumbani kwao kuwa kweli baba yake amegawa nafasi yake kwa Joshua. “Kwamba wanamthamini Joshua kuliko mimi!” “Labda kwa vile ambavyo amembadilishia mzee maisha, akapagawa.” Malon akampandisha chuki na wivu zaidi kwa kumsimulia mapya na mageni aliyoyakuta nyumbani kwao. Mpaka aina ya gala ambalo baba Naya analo  hapo nyumbani kwao. “Mzee amenifukuza mimi niliyekuwa nikiwasaidia! Tena usiku! Hakika huwezi kumjua mwanadamu mpaka ashike pesa.” Malon akaongea mengi ya uchungu na ya kuumiza. Mpaka giza linaingia, na wao wakawa wametengeneza kundi lao.

Zikawa kambi mbili sasa. Malon amejishindia Bale. Tena Bale akamuheshimu zaidi kwa kumtoa jela. Akajisikia amebakiwa na Malon peke yake, na anao wajibu wakulipa fadhila kwa ndugu huyo. Akasahau dhambi zake zote. Akabaki akimsikiliza yeye. Na kambi ya pili sasa ni ya Joshua ambaye amejishindia mke, baba Naya, na Zayon wakiungwa mkono na kina Magesa. Wawili hao wakapandishana morari wakikumbushana upinzani mkali unaowakabili kutoka kwenye kambi ya kina Joshua. Joshua na Naya wakiwa fungate wanafurahia ndoa, Malon na Bale wanajipanga kuwaonyesha na wao ni wa muhimu na wanauwezo mkubwa. Bale anajipanga kuingia vitani kukomoa familia yake akidhani yupo ukurasa mmoja na Malon, kumbe mwenzie Malon anakadhalika tena yakutisha. Hawakuwa ukurasa mmoja kama alivyosikika Malon.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sababu ya janga la gonjwa la corona, lililokuwa likiendelea duniani, Naya na Joshua wakashindwa kutoka nchini kwa mapumziko yao ya fungate. Wakawepo tu mjini Bagamoyo, kwenye moja ya hoteli kubwa na ya kisasa, wakihudumiwa. Kazi yao ikawa kufurahia tu wakiridhishana bila kuchoka. Joshua alikuwa likizo kama Naya. Wakaamua kutumia siku 14 fungate. Walikuwa na wakati mzuri, tulivu, wa kwao tu wenyewe. Na simu wakakubaliana kuzima kabisa. Japokuwa walikwenda wenyewe, lakini Geb na Nanaa walijua maharusi hao walipo.

Zilishapita siku 7 wakiwa mapumzikoni. Naya akamuomba Joshua angalau asikie sauti ya baba yake. Likawa sio tatizo. Wakampigia kwa pamoja, wakawa wanazungumza wote wakiuliza hili na lile. Kwa kicheko kile, baba Naya akajua mwanae anawakati mzuri. “Bibi alishaondoka?” “Wapo. Naona safari hii nitakuwa naye. Ameamua kubaki anisaidie kulea.” “Baba wewe! Sasa anamlea nani hapo wakati Zayoni ameshakuwa mkubwa anakwenda sekondari!?” “Wewe ukirudi muulize bibi yako. Ila yupo, na amerithi chumba chako.” Naya akacheka kwa kuguna.

“Ila amefurahia kweli harusi yako. Kila wakati anamuita Zayoni amuonyeshe tena picha zenu.” Naya akacheka sana. “Na hapo ndio urafiki na Zayoni umekolea! Kila saa anamuita. Zayoni anamwambia anampendea picha tu.” Naya na Joshua wakacheka. Mzee akasikika yupo vizuri na Naya akaelewa kuwa ndio bibi amefika hapo nyumbani kwao. Wakazungumza kidogo ndipo wakaagana. 

SUKARI YAINGIA SHUBIRI.

Siku ya 14 asubuhi waliamka wakijua ndio wanakwenda kuanza sasa  rasmi maisha ya unyumba. Maana baada ya harusi, walikaa hapo ndani, nyumbani kwa Joshua kwa siku 4 mfululizo. Mpishi wa Joshua akifika jikoni, anapika, wakiamka wanakuta walishapikiwa. Wao ni kula na penzi. Jumba zima wao wawili tu, wakiwa huru kufanya mapenzi popote watakapo. Ikawa Joshua ameshatumia siku 18 za likizo, Naya siku 20 kwa kuwa yeye aliwahi kuchukua likizo. Ukweli walipumzika vyakutosha. Kutoka kwenye kufanya kazi mfululizo na shule, hatimae Joshua akapata mapumziko tena safari hii akiwa na mwanamke!

Walitoka hapo hotelini kurudi kwao  mida ya mchana. Alianza kuimba  Joshua. Alisikika mwenye furaha haswa. Naya akamsaidia kuimba kidogo. Akawa kama amekumbuka kitu. Joshua akamuona anatoa simu yake kwenye pochi na kuiwasha. Akajua anayetaka kupigiwa ni baba Naya tu. Yeye akaendelea kuimba wakati Naya akiweka simu yake sawa na kupiga. “Unasikika mwenye furaha, mama!” “Nimepumzika vizuri baba yangu. Nina amani na furaha.” Naya akaendelea kuzungumza na baba yake, Joshua na yeye akasalimia. Wakaomba wamsalimie na bibi pia. Akasikika bibi kufurahi kweli kwamba na yeye amepewa heshima kuzungumza na mume wa Naya. Naya akamtania hapo ndipo akaendelea kuzungumza na baba yake pamoja na Zayoni.

Wakaagana kwa makubaliano, jumapili baada ya ibada wote watakuwa hapo nyumbani kwa Naya kwa chakula cha mchana. Nalo hilo bibi akalipigia vigelegele. “Joshua mwenzio kapendwa baba.” Naya akamtania baba yake. “Mbona hilo nalijua!” Baba Naya akajibu taratibu bila shida, na kufanya wacheke. Wakaendelea kuzungumza kidogo kisha wakaagana.

 Walifika nyumbani kwao bado ilikuwa mapema tu, hata giza halijaingia. Lakini walikubaliana siku hiyo ni Naya aanze kuweka vitu vyake na yeye chumbani kwa Joshua, ili chumba kichukue sura ya chumba cha mke na mume. Mizigo yake yote ilishaletwa kutoka Kiluvya. Ilikuwa imefungiwa kwenye chumba kingine ila chini ya gorofa siko juu kilipokuwa chumba chao wao na vyumba ambavyo Joshua alivitenga maalumu akisema ni vya watoto wao watakao jaliwa na mungu.

Wakati Naya yupo kwenye hicho chumba akitizama mizigo yake, huku akichambua nguo zake na viatu vyakupandisha juu chumbani kwao, Joshua akaingia. Hamu ikampata Naya baada yakuona aina ya mavazi aliyovaa Joshua na rangi zake baada ya kubadili, akataka penzi kutoka kwa mumewe akilalamika amemfanyia kusudi kumtamanisha. Joshua naye hakutaka kusubiri. Hapohapo chumbani juu ya nguo za Naya, penzi la haja likachezwa, Naya akigugumia kwa furaha. Likaongezeka na jingine tena, penzi la haja lakuridhishana likatendewa haki. Wakaishia kulala hapohapo sakafuni mpaka usiku ndio wanashituka na kugundua walilala hapo.

Baada ya kujisafi, Joshua naye akasaidia kubeba vitu alivyochagua Naya alivyoona vitaendana na chumba cha mumewe. Takataka alizoona  hazitaendana na mama mwenye nyumba hiyo akabakiza kwenye mabegi. Wakasaidiana kupanga mpaka wakamaliza. Joshua akaridhika kwamba kimekuwa chumba chao, sio chake peke yake tena. Na hapo tena penzi jingine la kukaribishwa hapo chumbani likaanza tena. Wakamaliza, wakaanza kuongea taratibu kitandani wakibembelezana na mabusu ya hapa na pale mpaka wakapitiwa usingizi.

Wakiwa wamelala, wakasikia kengele inaita kama wana mgeni usiku huo. Joshua akafungua macho na kuangalia saa. Akashangaa kidogo baada yakuangalia muda. Naya aliyekuwa amekumbatiwa amelala kifuani akakaa baada ya kusikia kengele ikizidi kuita. Joshua akavaa kwa haraka akatoka hapo chumbani. Naya akamsikia akishuka ngazi kwa kukimbia kidogo.

Joshua akasogelea mlangoni. “Ni nini?” Joshua akauliza akijua wazi ni mlinzi huku akitaka kuchungulia kwa tundu maalumu la mlango kuona aliyepo nje akitaka uhakika na anayemgongea usiku huo. “Geb na Nanaa.” Joshua akashituka sana kusikia sauti ya Geb usiku huo. Akawafungulia kwa haraka. Wasiwasi ulimzidia baada yakuona sura zao, zaidi Nanaa mwenye maneno mengi. “Naya amelala?” “Wote tumeamka sababu yenu. Kwema!?” “Si kwema Joshua.” Geb akajibu wakaelekea subuleni.

“Ni nini!?” Geb akamsimulia kwa kifupi na kumshitua sana Joshua mpaka kusimama. “Mungu wangu uko wapi!?” “Naomba tulia Joshua. Tafuta jinsi ya kumtoa Naya hapa, tena kwa haraka.” Joshua akarudi juu akiwa anatetemeka asijue anamwambia nini Naya.

“Ni kina nani!?” Naya akamuwahi mumewe mara tu alipoingia. “Geb na Nanaa. Ila wanatusubiri hapo chini, wanataka tukazungumze.” Naya kajishika moyo. “Usiku huu! Mungu wangu, naomba isiwe ni baba Naya. Mungu nisaidie.” Joshua akamsikia Naya akiomba akiwa amejiinamia. “Vaa tukawasikilize.” Joshua mwenyewe alikuwa ameingiwa hofu ya ajabu. Ukweli ujio wa Geb na Nanaa usiku huo palikuwa hakuna kujifariji isipokuwa lipo jambo zito zaidi upande wake Naya. Geb asingemfuta Joshua hata iweje mida hiyo mpaka iwe ni jambo zito sana tena linalomuhitaji Naya wala si yeye. Joshua hana biashara, hana ndugu wakutolewa kwenye kitanda ambacho bado kina harufu ya fungate!

Moja kwa moja Naya alijua kabisa ni jambo linalomuhusu yeye. Tena wazo la kama ni Bale alilipinga, akajiambia kama ingekuwa Bale yupo matatizoni, baba yake angesubiri papambazuke ndipo aombe msaada kwa watu. Alimjua baba yake sio wakulia shida usiku wa manane. “Mungu nisaidie!” Naya akaendelea kumsihi Mungu akizidi kuingiwa hofu hapo kitandani na kushindwa hata kujisogeza.

Naya alikuwa mtupu kabisa hapo kitandani amekumbatiwa na Joshua, anapapaswa. “Twende mpenzi wangu.” Joshua akamsihi tena taratibu akimuhurumia. Akatoka na kuvaa harakaharaka. Wakatoka kwa pamoja. Vile alivyomuona tu Nanaa, akajua mambo si mazuri. “Ni baba Naya ndio amefariki?” Naya akauliza swali la moja kwa moja walipofika tu hapo sebuleni walipokuwa Geb na mkewe. “Mnajua nisingewasumbua kama si muhimu.” Joshua kimya mapigo ya moyo yakienda kasi. “Ni baba Naya?” Naya akarudia tena swali lake lakini safari hii akimwangalia Geb aliyekuwa akizungumza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati ikionekana ipo amani kubwa, ndipo na uharibifu unaponyemelea. Endelea kufuatilia kujua nini kinaendelea!!

 

 

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment