“Tunavyofikiria
labda kulikuwa na gasi ilikuwa wazi pale ndani nyumbani! Maana mlinzi
anasema ilikuwa kama kibatari kimewashwa na kuzimwa. Ndivyo nyumba
inavyosemekana ilivyo teketea.” “Wakati huo baba, Zayoni na bibi na yule mjukuu
wake wakiume aliyekuja naye kutoka kijijini, Luka, walikuwa wapi?” Naya
akauliza tena swali la pili wakati hata la kwanza hakujibiwa. “Unajua leo ndio
mzee alikuwa akipokea mazao. Dereva anasema alimshushia mazao leo mida ya
jioni. Mlinzi anasema mzee alikuwa galani kwa muda mrefu sana. Yaani kama
aliyekuwa akisubiriwa hivi! Alipoingia tu ndani, na kufunga milango yote,
anasema hata dakika 20 hazikupita ndio huo moto ukatokea.” Naya akameza mate
akatulia kidogo. Kimya wote kama ambao hawajui wamwambie nini Naya.
“Naomba nisaidie Geb.” Akaanza Naya baada ya kutulia kwa muda
akionekana kama ambaye hapati majibu yake kwa waziwazi. “Nisaidie kuongea hicho
unachosita kukisema, maana unanitia wasiwasi zaidi. Baba Naya yuko wapi?
Zayoni, Luka na bibi yangu je?” “Baba Naya yupo hospitalini, Naya. Wote wapo
hospitalini. Hali sio nzuri, ndio maana mama ameona tuje tuwafuate, angalau
mkamuone mzee.” Naya akabaki ametulia kama ambaye bado hajaelewa vizuri na
akajua Geb hayupo tayari uzungumza zaidi ya hapo au hajui azungumze nini!
“Twende
Naya.” Akamgusa begani mkewe baada ya yeye pia kutoka kwenye butwaa maana wote
ni kama wakabaki wamepigwa na bumbuwazi, hawajui waseme nini kwa Naya, wakati wote
wanajua fika kilichotokea. Wajumbe na wafikishiwa habari, wote wakabaki kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Fungate
waliyokuwa wameambizana wanaihamishia nyumbani, ikaishia hapohapo. Wakaondoka
na kina Geb, kwenye gari yao. Joshua na mkewe wakawa wamekaa nyuma. Kama
kawaida Geb akawa dereva, mkewe amekaa pembeni. Kimya haswa. Naya akawa
amegeukia dirishani ametulia. Joshua akamwangalia baada ya kufikiria huko
mawazoni akimuhurumia sana mpenzi wake. “Niambie chochote unachofikiria sasa
hivi, Naya mke wangu.” Naya akamgeukia Joshua. “Naogopa sana. Nimeingiwa
na hofu ya ajabu Joshua! Hapa tumbo linauma nahisi kutapika na kama kuanza siku
zangu. Mikono inakufa ganzi.” Naya akajibu kwa sauti ya chini iliyosikika
ikitetemeka. “Pole sana. Pole.” Joshua akatamani aongee mengi ya kumfariji,
lakini hata yeye alikuwa kwenye mshituko. “Nishike mkono.” Naya akajisogeza
karibu na kumshika mkono vizuri, akajikunja kitini, akajiegemeza akimtizama
Joshua anavyosugua viganja vyake kama kuvitoa ganzi. Akapotelea mawazoni, kimya
hakuna aliyezungumza tena, na wote wakashukuru Mungu Naya hakuuliza swali
jingine. Geb akaendelea kukanyaga mafuta kuwatoa Goba, kwenda Kibaha hospitali.
Hospitalini.
Walimkuta
mama G peke yake akiwasubiria. “Pole Naya, mama. Pole sana.” “Naomba niambie
ukweli mama. Hali yangu ni mbaya, niambie tu ukweli nijue.” “Inavyoonekana ni
kama moto ulianza wakiwa wameshakwenda kulala na wamefunga milango yote, mpaka
mageti. Kwa hiyo wote walikutwa mlangoni kama waliokuwa wakijaribu kufungua
mlango wakalemewa na moshi, pengine na kuzirai kabla ya kuungua. Na wamesema
kuna mwili mwingine umepatikanika pale nyumbani unaonekana ni wa mtoto mdogo wa
kiume.” “Ni mjukuu wa bibi alimchukua baada ya bibi yake aliyekuwa akimlea
kufariki. Ni wa palepale kijijini anaitwa Luka.” Naya akaongea taratibu akiwaza
mpaka akawashangaza.
“Na baba
Naya?!” Akauliza tena taratibu. “Hali yake sio nzuri Naya. Mzee aliungua sana.”
Mama G akaendelea kwa tahadhali. “Nasikia kutapika, tumbo linanikata.” “Twende
chooni.” Joshua akataka kwenda naye yeye. “Acha mimi niende naye Joshua, ili
kuingia naye chooni kabisa.” Wakati Naya na Nanaa wanataka kuondoka, Naya
akaanza kutapika baada ya hatua chache sana wakiwahi chooni. Alitapika mpaka
Joshua akamshika mbavu. “Tumbo linauma sana. Kama nataka kujisaidia.” Nanaa
akakimbia naye chooni. “Nenda na wewe Joshua, uhakikishe anarudi kumuona baba
yake kabla hajachelewa.” “Ndio hali mbaya hivyo!?” “Sana. Ila tuliomba
awekwe kwenye chumba kizuri, apewe dawa ya kutuliza tu maumivu. Lakini hata
wewe ujiandae. Ameungua yule mzee, huwezi kumtambua.”
“Madaktari
wameshindwa kumsaidia kwa chochote kwa jinsi alivyoiva mwili mzima! Kuna nesi
amepita hapo, ametuambia eti tumruhusu, ili akapumzike. Ndio katika
kufikiria, tukasema labda anasubiri kumuaga Naya, ndio apumzike.” “Mungu wangu
uko wapi leo!?” Joshua akaweka mikono kichwani. “Aisee pole sana Joshua. Poleni
sana.” “Mungu wangu!” Joshua akarudia kumuita tena Mungu. Wakamuona Naya na
Nanaa wanarudi ametulia tu.
“Twendeni.
Uzuri kwenye chumba alipo baba Naya, kuna choo. Jikaze mama.” Mama G akamsaidia
Nanaa, akamshika yeye Naya, wakaelekea alipokuwa amewekwa baba Naya. Walitembea
kimyakimya mpaka walipokaribia mlangoni ikabidi mama G amuandae. “Naya!” Wote
wakasimama. “Baba ameungua sana, ni ngumu kumtambua.” “Amepewa dawa ya
maumivu?” Naya akauliza. “Ndiyo. Lakini kwa alipo na alivyo sasa hivi, nahisi anakuhitaji
tu wewe.” Mama G akaweka tena msisitizo akitamani Naya aelewe bila kuongea kwa
undani. “Nyinyi hamtaingia?” Naya akauliza akidhani wanamuaga. “Mimi nipo na
wewe Naya.” Joshua akajibu kwa haraka. “Nashukuru jamani. Asanteni.” Naya
akashukuru na kuingia.
Mwili wa
baba Naya ulikuwa umefunikwa, lakini hata mashuka yalionyesha damu. Ikawa kama
nyama mbichi iliyofunikwa na shuka jeupe. Naya hakuwa ameelewa alivyoambiwa
kama baba yake ameungua. Alikutana na kiumbe wa ajabu amelala kwenye hicho
chumba cha peke yake, kitanda kimoja tu, kuashiria huyo ndio baba yake.
Anatisha, hajawahi ona! Hana ngozi ile ya juu, mwekundu usoni alipoachwa wazi
mpaka kichwa ambacho nacho hakikuwa hata na nywele wala ngozi. Ila alikuwa
akihema kwa nguvu kwa kituo. Kila pumzi aliyovuta, aliivuta kwa nguvu zake
zote. Hapohapo Naya akaanguka na kuzimia. “Mimi nilijua tu.” Mama G
akaongea mikono kichwani.
Ikabidi
Joshua na Geb wamtoe nje. Akapewa huduma ya kwanza, akazinduka na kukaa kwa
haraka. Na hedhi nayo ikaanza. Naya akapatwa na kutapika mfululizo, akaanza na
kuharisha. Akakataa kulazwa. “Naombeni nirudisheni tena kwa baba.” “Unauhakika
Naya!? Umetapika mfululizo bila kupumzika!” “Kabisa. Ni mshituko tu, lakini
baba yangu sasa hivi ananihitaji, jamani! Lazima nirudi na mimi niwepo kwa
ajili yake. Amekuwa na mimi kila wakati, kila mahali, katika kila hali. Siwezi
kumuacha sasa hivi peke yake zaidi akiwa kwenye ile hali. Lazima na mimi niwepo
kwa ajili yake sasa hivi. Nitoeni haya madripu ya maji. Sihitaji. Ni mshituko
tu, ila nitakuwa sawa. Naomba nisindikize Joshua. Nataka kuwa na baba yangu.”
Joshua akaomba atolewe tu hapo alipokuwa akipewa huduma ya kwanza. Naya
akajikaza tofauti na walivyotarajia. Wakamsindikiza tena kurudi alipokuwa
amewekwa baba Naya.
Safari
hii walimkuta baba Naya hata ule upumuaji wa kwa nguvu umepungua. Anahema kwa
mbali sana. Naya akamsogelea pale alipokuwa amelala. Ukweli alikuwa akitisha.
“Pole baba. Pole sana.” Naya akabaki ameshika tumbo akimtizama machoni napo
akawa hatizamiki ila walibaki wakitizamana na baba yake. Naya akashindwa,
machozi yakaanza kumtoka kama baba yake. Baba Naya alikuwa akichuruzika
machozi. “Baba yangu mimi jamani!” Naya akasikika
akiongea taratibu. “Pole baba. Pole sana baba yangu.” Naya akarudia machozi
yakimtoka, akitizamana na baba yake. “Niite tena baba!” Naya
akaongea taratibu akimwangalia na kumsihi taratibu, akitamani kumsikia. Chumba
kizima kimya, machozi wote yakiwatoka.
Akamuona
kama anasogeza midomo. “Nimefurahi baba. Nimefurahi nimekuona. Pole
sana baba yangu. Na asante kwa kila kitu baba. Asante umesimama na mimi kwenye
kila hali mpaka umenifikisha kwa Joshua! Asante baba yangu.” Akamuona
anaendelea kutoa machozi. Hapakuwa na jinsi ya kumshika kwani kila aliposhikwa
hata na nguo, nyama ilitoka.
“Baba
Naya?” Mama G akamuita. “Pole. Pole sana. Funga
macho na wewe upumzike. Sisi tupo hapa na Naya, na atakuwa sawa kabisa. Usiwe
na wasiwasi. Hatakuwa peke yake. Tuko naye.” “Pole sana mzee wangu. Pole sana.” Joshua
akaongezea kwa mama G. Naya alikuwa akitetemeka kama amepigwa na baridi
kali. “Mimi nitakuwa sawa baba. Nipo na Joshua na kina Magesa, sasa
hivi. Nitafanya kama ulivyoniambia. Nakumbuka kila kitu na nakuahidi sitasahau.
Nakupenda baba yangu. Nakupenda sana.” Wakamsikia baba Naya
akihema kwa nguvu, kisha kimya. Wote wakajua ameshakata roho. Naya akabaki
ameduaa kama ambaye haamini. Hata machozi yakakoma. Ukazuka ukimya wa ajabu
hapo ndani.
Mwishoe
Geb akatoka kwenda kumuita nesi. Akaja kumuangalia. Akamfunika mpaka kichwani
ndipo taarifa zikaenda kichwani kwa Naya kuwa ule ndio mwisho wa safari
ya baba Naya hapa duniani. Joshua akamshika mkewe, wakatoka hapo.
Duniani Wote Tunapita. Unatokaje Hapa Duniani! Ni Fumbo Kwa Kila
Mwenye Mwili!
Baba Naya
alikuwa ameiva sana, kiasi ya kwamba ilikuwa lazima azikwe haraka. Naya alitoa
namba za simu za baba zake wakubwa ili kujulishwa kuwa itakuwa hata ngumu
kusafirishwa. Ila bibi yeye na Zayon pamoja na Luka ni kama walikaushwa kabisa.
Kwa hiyo Joshua na kina Magesa wakafanya taratibu za mazishi kwa haraka, baba
Naya na Zayoni wakazikwa siku hiyohiyo jioni karibu na alipokuwa amezikwa mama
Naya, safari yao hapa duniani ikawa imeishia hapo. Ndani ya masaa 24, walikuwa
wazima na mipango kamilifu. Umauti ukawakuta kiasi chakushindwa hata kuweka
msiba kwa masaa mengi mbeleni, wakarudi mavumbini siku hiyohiyo. Kwanza
waliagwa katika kanisa la hapohapo hospitalini hata hawakuonyeshwa, na
kupelekwa makaburini moja kwa moja.
Kesho
yake, safari ya kumsindikiza bibi na kijana aliyekuja naye kuwarudisha kijijini
na wenyewe kwa mazishi ikaanza. Ikawa hakuna kupumzika. Watoto wa bibi
wakasaidiana na kina Joshua. Wakafanya kwa ufanisi, wakakodi magari kwa kuwa ni
kama watoto wengi wa huyo mama na wajukuu walikuwa wamesambaa hapo jijini Dar.
Ndani ya huo mwezi wakawa wamekusanyika kwa harusi na msiba.
Kwa kuwa
Joshua alishajua dawa za Naya akiwa kwenye siku zake zaidi anapokuwa kwenye
hiyo hali ya mshituko, akabeba hizo dawa na soda zakutosha, ndipo safari ya
kuelekea kijijini kwa mazishi kwa mara ya pili, ikaanza. Kina Magesa wote mpaka
Grace na Man walikuja kwenda kuzika kijijini. Nako huko hawakukaa sana.
Walizika, siku inayofuata, baada ya mazishi, kina Magesa, Naya na mumewe
wakarudi jijini Dar. Naya alikuwa ametulia sana. Akiangalia sehemu, ni mpaka
umshitue.
Ila
ikawasaidia na kuwarahisishia sana kuendesha mambo kwa umakini, haraka bila
paniki ya kilio cha Naya kitu ambacho kila mmoja wao alitegemea iwe hivyo.
Lakini ikawa kinyume kabisa. Kwani Naya alikuwepo kama hayupo. Kimya tu. Joshua
akabaki kuweka mipango akizungumza na ndugu wa baba Naya, nao wakampa baraka zote
aendeshe mambo vile atakavyoweza. Ndipo sasa kina Magesa na marafiki wa karibu
wakaibebe hiyo shuguli nzima kwa wepesi, pesa ikitembea bila kuchelewesha
mambo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walirudi
wote mpaka nyumbani kwa Joshua na Naya, Naya akapitiliza juu chumbani kwao kama
anayewahi chooni, hata hakukaa sebuleni. Nanaa akataka kumfuata ili kumsaidia
huko chumbani, Joshua akawahi. “Nashukuru Nanaa. Acha nimfuate, pengine atataka
kuoga kabisa.” “Mimi nashauri tuwaache wapumzike jamani.” “Nafikiri ni wazo
zuri. Tumbo linamsumbua sana, acha nimsaidie alale.” Joshua akakubaliana na
wazo la mama G. “Tafadhali mtupigie muda na wakati wowote mkituhitaji.” “Kwa
niaba yangu na mkewe wangu, hakika nyinyi watu nawashukuru. Mungu wa
mbinguni awakumbuke kwa hili pia, na naomba anapowabariki kwenye hili awatendee
mpaka mjue ni katika hili amewalipa kwa kumsindikiza mtumishi wake
kwenye safari yake ya mwisho. Mmemtendea haki baba Naya. Mbarikiwe mpaka
mjue Mungu mwenyewe amewabariki.” “Amina Joshua.” Wote wakaitika na kama
wakapigwa tena na butwaa. Mwishoe Geb akawashitua, wakasimama na kuondoka bila
yakuongeza neno.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakabaki
Joshua na mkewe. Akamsaidia kuoga, akapanda kitandani. Joshua akiwa ameshaoga,
na yeye akapanda kitandani akaanza kumsugua tumbo na kiuno mpaka akalala bila
hata kuzungumza. Mapumziko ya Joshua yakahamia kwenye kuuguza tumbo la Naya.
Baada ya siku tatu mbeleni, tumbo likatulia, hedhi ikakoma ila bado Naya
alikuwa mtulivu sana hapo kitandani, hana maongezi kabisa. Siku ya 3 mbeleni
tena, Joshua akafuatwa na Jema mpaka nyumbani kuwa wanahitaji msaada wake
ofisini. Anasubiriwa. Ilikuwa mida ya mchana. Ikamlazimu kwenda tu na ahadi
yakutochelewa, chakula cha usiku watakuwa pamoja.
Naya
akasubiri mpaka ilipofika mida ya saa 10 jioni, Joshua akampigia simu kumwambia
mambo yamevuta kazini, atachelewa kidogo. Naya hakuona shida. Aliyajua majukumu
ya mumewe. Na yeye akaona atumie muda huo kwenda saluni angalau akaoshe nywele
alizotengenezwa sababu ya harusi karibia mwezi ulitaka kufika na zilishaanza
kutoa harufu. Pia alijua anakaribia kurudi kazini, maisha yanatakiwa yaendelea.
Ila mwili ndio ni kama ukawa umegoma. Akabaki amejilaza hapo kitandani akiwaza
na kushindwa kutoka kabisa.
Ni kama
kila kitu kilipoteza ladha na maana ya maisha kwa siku kadhaa, akawa amepigwa
ganzi ya namna yake. Akawa kama ameshushwa kwenye ulimwengu anaoutambua, ila
majibu ya maisha yake yote hapo duniani yakawa yametoweka. Hajui tena
chakufanya. Ila alijua wazi maisha nilazima yaendelee, nilazima atoke tu hapo
kitandani. Akamsikia baba yake akimwambia masikioni. ‘Tuliza akili usije
kuharibu kazi ya watu.’ Naya akakaa kwa haraka aliposikia usemi aliozoea
kuambiwa na baba yake.
Hapohapo
akampigia simu Joshua kumtaarifu anatoka kwenda saluni. Hilo likamfurahisha
sana Joshua, akajua angalau atachangamka kidogo. Na angalau siku hiyo
wakazungumza hata Joshua akahisi utofauti. Naya aliweza kuzungumza zaidi na
jibu alilozoea kumjibu tokea msiba wa baba yake, jibu la ‘sawa’, ‘ndiyo’ na
‘hapana’. Akamuahidi atamkuta nyumbani, asingechelewa. Wakaweka mipango ya
usiku huo, kidogo akasikika akicheka. Joshua akaridhika, akampongeza moyoni
mwake akijua anajikaza. Ni baba Naya! Alijua ameumia. Lakini akajua
kutoka hapo kitandani kutamsaidia. Wakazungumza kidogo ndipo wakaagana, Joshua
akaendelea kuwajibika.
Hakuna Msiba Usiokuwa Na Mwenzie.
Akiwa
ameshamaliza shuguli zake za saluni, ndio anatoka saluni kurudi kwenye gari
yake, akashangaa kumkuta Bale amesimama nje ya mlango wa gari yake. Giza
lilishaanza kuingia. Naya alishituka sana. “Bale!” Hakutegemea. “Naona maisha
yanaendelea bila mimi, hakuna anayenijali! Nafasi yangu amechukua mwanaume
wako. Maswali yanayotakiwa yajibiwe na mimi, yeye ndiye anaye ya jibu!” Naya
akabaki kimya akimshangaa Bale. “Hati ya nyumba ya Kiluvya iko wapi?” “Baba
alimpa Magesa kwa kuwa walifanya naye biashara. Akamwambia hiyo hati ndio
itakuwa kama dhamana, mpaka amalize deni lote ndipo amrudishie!” Naya alijibu
akiwa na mshangao mkubwa sana usoni. Bale aliyekuwa akitafutwa, amerudi na lawama,
hasira waziwazi usoni, halafu akiwa na swali ambalo Naya hakutegenea kabisa
zaidi kwa wakati huo wametoka kuzika!
Kwa aina
hiyo ya swali kwa haraka sana Naya akajua inamaana anajua kama baba yao
amefariki pamoja na Zayoni. Hakuonekana kujali kabisa. Na pia hakuonekana na
hali mbaya. Msafi tu. Hafananii kama aliyekuwa jela au kwenye matatizo! Akiwa
kwenye mshangao huo, akashangaa mtu nyuma yake anampiga kwa nguvu sana nyuma
eneo karibu na kichwa na shingoni, hapohapo akapoteza fahamu.
Kwa Joshua.
Joshua akiwa
ndio anajiandaa kutoka kazini arudishwe nyumbani, ujumbe kutoka kwa Naya
ukaingia. Ujumbe wa Naya huwa hausubiri. Akarudi kukaa na kusoma. ‘Joshua.
Naomba kukuaga rasmi. Nimeamua kuendelea na maisha yangu. Nimepoteza mengi sana
sababu ya kuwa na wewe. Naokoa kilichobaki kwenye maisha yangu na nafsi yangu
pia. Nilifanya makosa kuendelea kukung’ang’ania na kushindwa kuhesabu garama.
Nipo kwenye wakati mgumu, nahitaji kuendelea mbali na wewe. Funguo
za gari, zipo kwenye tairi ya mbele kushoto. Ndani utakuta pete zako pia.
Nimeamua kukuachia kila kitu nilichokipata kwako mpaka hii simu vyote utakuta
kwenye gari yako na gari nimeacha nje ya ile saluni waliyonisuka. Kila la
kheri, maisha mema.’ Joshua akahisi hajaelewa.
Tokea
wamzike baba yake, Naya hakurudia hali ya kawaida, lakini hapakuwa na dalili ya
kuachana! Akakumbuka kwa kituo mazungumzo yao ya mwisho! “Hapana.” Joshua
akahisi anamtania. Akajaribu kumpigia tena na tena, simu ikawa ikiita tu.
Akatoka kwa haraka kwenda alipoelekezwa ameliacha gari. Dereva alimpeleka mpaka
kwenye hiyo saluni. Akaangalia funguo kwenye hilo tairi aliloelekezwa, kweli
akaikuta hapo. Joshua akamwambia dereva aondoke tu.
Akafungua
mlango, ni kweli alikuta kila kitu cha Naya mpaka pochi! Akaangalia ndani ya
pochi, akakuta hata walet yake ipo na ina vitambulisho vyake vyote mpaka na
kadi za bima, benki pia zipo! Joshua akahisi kuna kitu hakipo sawa. “Naya
anaanzaje hayo maisha bila hata kitambulisho chake!” Joshua akawaza
akitumia tu akili zake kwa harakaharaka. Akajua kwa hakika alichoandikiwa
kupitia simu ya Naya, si Naya. Na huyo aliyefanya hayo yote kama si
mjinga sana, basi hakujipanga vizuri.
Hapohapo
akampigia simu Nanaa. “Umezungumza na Naya leo?” “Ndiyo. Jioni hii tu.
Alipokuwa saluni, mimi bado nilikuwa kazini. Tena alinipigia yeye mwenyewe
kunisalimia. Tukaachana akitaka azungumze na Magesa kipenzi chake. Nikaona wazo
zuri ili amchangamshe kidogo. Kwanza kwa nini unaniuliza? Kwema?” “Sijui
Nanaa! Mpo nyumbani?” “Wote tupo nyumbani.” “Basi nakuja.” Kabla
ya kuondoka, Joshua akaingia pale saluni kwanza. Akawaulizia kama Naya
alikuwepo hapo. “Alikuwepo hapa. Alikuja akitaka tu kuosha nywele, lakini
akaosha na miguu na kutengeneza kucha pia.” Akajibu dada aliyemuhudumia. “Kuna
mtu yeyote aliyemfuata hapa?” Joshua akaendelea kuhoji taratibu. Akafikiria
kidogo kama kuvuta kumbukumbu. “Hapana. Ila nilimuona akichati na kuzungumza na
simu tu. Mpaka mwisho alipotoka.” Joshua akafikiria akiwa amesimama hapo saluni
na wenyewe wanataka kufunga.
Mwishoe
akaona aondoke tu. Akatoa gari hapo kuelekea Tabata nyumbani kwa kina Magesa.
Njia nzima alikuwa akifikiria. “Haiwezekani!” Joshua
akapinga kabisa kwa sauti. Akaendelea kuwaza mpaka alipofika kwa kina Magesa,
akawaonyesha ujumbe. “Mmmh!” Nanaa akabaki akiwaza akivuta kumbukumbu ya
mazungumzo yake na Naya. “Alisikikaje kwenye simu?” “Hakuwa amechangamka,
lakini alikuwa akicheka maana nilikuwa nikimsimulia vituko vya Magesa. Sasa si
unamjua anavyompenda Magesa? Akawa anacheka huku akiuliza maswali. Mwishoe
akataka kumsikia Magesa mwenyewe. Nikampigia simu mama, nikamwambia amwambie
Magesa ampigie simu anti Naya, anahamu naye.” “Na walizungumza kwa muda
tu na Magesa, akimpa stori za shule.” Mama G akaongeza. Wote kimya.
“Najua
mnaweza msinielewe kutokana na huu ujumbe wake, lakini jamani kuna
linaloendelea na Naya hakuwa mtu wa kuniacha.” Kimya. “Najua mnaweza
msinisadiki pia, mkahisi ni kupaniki sababu nimeachwa, lakini hebu fikirieni
tu. Mtu anayekwenda kuanza maisha yake, ndio aache mpaka vitambulisho na kadi
za benki! Anakwenda kuanza vipi maisha na hana pakwenda? Nyumba iliungua moto,
tulikuwa na mpango wa kupajenga tena! Jamani huyu Naya anayeonekana amenitumia
huu ujumbe, anakwenda kuanza wapi na vipi!?” Joshua akauliza taratibu tu wote
wakiwaza.
“Nyumbani
kwenu je?” “Nimepiga simu pale getini, wameniambia aliyepita hapo baada ya Naya
kutoka, ni mpishi tu. Naye alishaondoka. Kwamba hakuna mtu mle ndani!” “Twende
Kiluvya.” Geb akasimama. Wakatoka. Walifika nyumbani kwa kina Naya, hakuwepo.
Walizunguka mpaka nyuma kwenye kuta zilizobakia za gala. Hapakuwa na mtu
yeyote. Wakaita, hapakuwa na dalili ya Naya.
Geb na
Joshua wakakumbuka maneno na vitisho vya Malon kwa Naya. Wakakumbuka Malon kuapa
kumsaka Naya mpaka kumpata tena akasema labda ahame dunia. Hapohapo wakaenda
kutoa taarifa polisi lakini wakawakatisha tamaa baada ya kusoma na ujumbe
kutoka kwa Naya mwenyewe. Naya hakuonekana yupo hatarini kwani hata gari
haikuvunjwa. Hapakukutwa hata tone la damu kuashiria pengine alivamiwa! Wakaona
ni visa tu vya mapenzi. Joshua amekimbiwa.
“Mkubwa
hapotei.” Likawa jibu la kwanza kutoka kwa maafande hao walio wakuta hapo
mapokezi mida hiyo ya usiku, baada ya kumsikiliza Joshua. Wazi waliashiria fika
kuwa Joshua ameachwa, na aanze kukubali matokeo na hapo hapakuwa na kesi.
Kwanza hata hivyo vitisho walivyosema Malon alimtishia Naya, hawakuwa
wameviripoti polisi. Ikakosa nguvu kabisa ikawa wanamsikiliza Joshua kama
anayetunga tu habari sababu ya kupaniki kwa kuachwa. “Moyo wa mtu msitu! Huwezi
jua lililokuwa likiendelea moyoni kwa mkeo.” “Na kweli! Pengine aliamua kurudia
makoloni yake! Inatokea.” Afande mwingine akamalizia hivyo kwa kebehi akimuunga
mkono mwenzie.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walipanga
wakimaliza fungate ndipo wakae kama familia walizungumzie hilo la vitisho vya
Malon, wakijua fika, Bale alirudi kwa Malon na kama mwanzoni, amegoma
kuwasiliana nao. Wakatulia wakiwa wameshajiridhisha hayupo jela na wala mwili
wake haupo chumba chochote cha maiti kwani na huko nako walitembelea mpaka Dar
pia Bale alitafutwa huko magerezani, mahospitalini mpaka vyumba vya maiti, ndipo
wakaamini yupo na Malon tena.
Kwa Naya.
Naya
aliamka akiwa na macho mazito sana. Akagundua yupo garini, tena mwendo kasi,
nje giza. Akataka kukaa maana alilazwa kiti cha nyuma kabisa. Akashindwa.
Palikuwa kimya, hakujua hata nani ni dereva. Akarudi kulala. Alikuja kushituka
nje kunapambazuka. Bado wapo safarini. Akatulia akijaribu kutafakari, napo
akapotelea usingizini mpaka akasikia kama anayeshushwa garini. Akafungua macho,
akakutana na Malon, pembeni yake Bale. Naya alishituka sana. Kila alipotaka
kujishika, mikono ikawa kama haina nguvu yakutosha. Akajihisi kama aliyelevya.
Malon
akambeba mpaka ndani. Akamuweka kitandani. “Una njaa?” Malon akamuuliza. Naya
akabaki akimwangalia pale alipokuwa amelala. “Acha jeuri Naya. Si unaulizwa
wewe?” Akageuza shingo kumuangalia Bale aliyekuwa amesimama mlangoni. Akasikia
maumivu ya shingo kidogo pale alipopigwa kabla hajapoteza fahamu. “Niko wapi?”
“Hana njaa huyu. Mrudishe tena kulala.” Bale akaongea na kutoka. Malon
akamchoma sindano iliyomfanya Naya ajisikie vizuri sana. Alijisikia utulivu wa
hali ya juu. Hata majonzi na simanzi moyoni vikaondoka gafla. Ule uchungu wote
moyoni nao ukaondoka kabisa. Hakuwa na maumivu popote pale. Si mwilini, si
rohoni. Akafurahia ile hali. “Nahitaji kutumia choo.” Akasimama Malon
akimwangalia. Hata usoni alionekana ametulia.
Malon
akamuelekeza. Ilikuwa nje ya hicho chumba. Akajaribu kutembea, akawa
anapepesuka. Mwili mwepesi mno! Akajicheka kilevi. “Nasikia kizunguzungu!”
Akalalamika akiwa na tabasamu. Malon akamsaidia kwenda chooni. “Hapa ni wapi?”
Akauliza tena, lakini safari hii sio kwa wasiwasi kama mwanzo. “Una wasiwasi
gani, wewe tulia. Upo na mimi.” Naya akafikishwa chooni akakaa. Wakati
akijisaidia, akili ikawa kama imemrudia.
“Joshua!”
Akaita kwa sauti. “Usiniudhi Naya!” Malon akageuka na huo mkwara. “Mume wangu
yuko wapi?” Malon alimpiga kibao mpaka akaanguka pembeni ya choo. “Nilikuonya.
Sitarudia Naya. Acha kulitaja hilo jina.” Naya alikuwa ameshikilia shavu pale
sakafuni akawa kama anayejaribu kuelewa. Malon akatoka na kumfungia mlango kwa
nje. Kwa kuwa alikuwa hana nguvu, akabaki amekaa hapo ndani chooni, tena sakafu
ikiwa na maji tu, akapotelea usingizini akiwa amekaa chini kabisa.
Kwa mbali
akasikia akivutwa kama anayetolewa pale. Tena kwa kuburuzwa kikatili. Akaenda
kuwekwa pembeni ya kitanda, akalala. Alikuja kuamka ikiwa imeshafika jioni.
Yupo peke yake sakafuni, anatetemeka baridi yakupita kiasi. Akajitahidi kutoka
hapo chumbani. Akajikokota mpaka nje kabisa alipoona mwanga wa mwezi na nyota angani,
akajikuta yupo katikati ya mashamba na mapori. Naya akashangaa sana. Hapakuwa
na nyumba isipokuwa hiyo tu. Giza nene isipokuwa huo mwanga wa angani.
Akajaribu kufikiria akivuta kumbukumbu alipo au ni ndoto tu! Lakini kumbukumbu
yakumuona Bale na kofi alilopigwa na Malon ikamjia. Akajishika shavu.
Mara
akaona gari ikija. Akabaki amesimama. Kumbe alikuwa Malon. Akafika hapo na
kuegesha gari yake akasubiri ashuke. “Huku ni wapi wewe Malon, na kwa nini nipo
hapa!?” “Unakumbuka nilikuonya usiolewe na Joshua, kwakuwa bado nakudai?”
“Unanidai nini!?” Naya akauliza kwa kumshangaa. “Muda na mapenzi. Sasa upo hapa
kulipa. Hutaondoka hapa, mpaka nikuruhusu mimi mweyewe. Huruhusiwi kwenda
popote, hapo uliposimama na nyuma ya hii nyumba ndio mwisho wako. Na ninakuonya,
usinijaribu Naya. Hakika nitakuumiza.” Naya akashangaa sana.
“Umechanganyikiwa
wewe Malon?!” “Wakati ukitumia pesa yangu na muda hukuona kama
nimechanganyikiwa. Ulinifuata kila mahali bila kukuita. Ulikula vyangu kwa
nguvu zote bila aibu. Nilikulisha na kukuvalisha kwa jasho langu, eti sasa hivi
ndio unataka kunikimbia! Huwezi Naya. Mimi nina akili ya kuzaliwa, ndio
maana hakuna aliyeweza kunifundisha darasani. Hapa umefika. Hutatoka
wala hakuna atakayekutoa hapa. Unalipa fadhila. Anza kuzoea mazingira.” Naya
akaangalia kulia na kushoto, akashindwa kujua alipo.
“Na hiyo
hali unayojisikia, dawa yake ninayo. Nitakuwa nikikuchoma sindano yake, pale
nitakapojisikia na utakaponifurahisha. Sasa kwa kuwa wewe ni jeuri, nakuacha
mpaka uje mwenyewe kuomba.” Malon akampita pale alipokuwa amesimama. Akasikia
harufu ya chakula. Akajua amerudi na chakula. “Ukichoka kusimama hapo nje, rudi
ndani, chakula tayari.” Hapakuwa na kubembelezwa tena. Kamasi zilikuwa
zikimtoka Naya, hana pakujifuta. Akashangaa na machozi yakimtoka huku
akitetemeka. Maumivu yake yote ya shingoni na moyoni yakarudi vilevile.
Akarudi
ndani maana baridi ilikuwa kali. “Hiyo baridi unayojisikia ni ya kutoka ndani
kwako. Hakuna baridi hapa.” Malon akamwambia kwa kumkejeli. Naya akaenda kukaa
kochini. Ilikuwa nyumba ya kawaida tu, lakini ilikuwa imekamilika. Naya akabaki
akitetemeka baridi amejikunja kwenye kochi. Jinsi anavyojisikia, haikuwa
kawaida. Akakimbilia chooni kutapika. Akatapika kwa muda, kisha akaamua kuoga
kabisa na kurudi kulala.
Akamuona
Malon amejiwekea chakula chake, anakula pale sebuleni. Akasimama na kufunga
mlango ili asiione sura yake. Akaendelea kutetemeka pale
kitandani hata usingizi ukawa mgumu kuja. Baada ya muda akamuona
Malon anaingia hapo chumbani na yeye anakwenda kuoga. Ila yeye alioga maji ya
moto. Alimuona akiyachemsha hayo maji kwa kutumia jiko la gesi, alimuona kwa
mwanga wa kurunzi kubwa aliyowasha mara baada ya kurudi. Alipomaliza kuoga,
Naya akashangaa anaingia hapohapo chumbani alipolala yeye akiwa na taulo tu.
Bila hata kuongea, Naya akashitukia anavuta shuka aliyokuwa amejifunika, kwa
nguvu, akalitupia sakafuni na kuanza kumtoa nguo kikatili kama aliyekusudia
kumuumiza. Akiwa amemuacha mtupu kabisa, anatetemeka baridi hapo kitandani,
amkandamiza kwa nguvu, akaanza kumbaka. Alifanya kila kitu mwilini kwa Naya,
kwa nguvu zake zote akimtizama bila kujali vile alivyokuwa akilia, mpaka
akamaliza.
Baada ya
muda akaamka na kwenda kutengeneza hiyo dawa. Akamuamuru Naya akaoge tena. Naya
akatoka hapo kitandani akilia. Malon akawa anamcheka. “Wakati ukitaka pesa
yangu, hata nilipokuwa nimekuudhi mpaka mwisho, ulipokea dhahabu zangu, na
penzi ulikuwa ukitoa bila shida, eti sasa hivi ndio unajidai kulia! Acha wizi
wewe!” Naya akajifungia chooni. Akaoga na kutoka akiwa na hali mbaya sana. Maumivu
ya kubakwa na mengineyo. Malon akarudi na kumchoma sindano. Taratibu Naya
akaanza kusikia furaha. Utulivu wa namna yake hata mawazo yakaanza kutulia.
Hapo napo Malon akapata mchezo mwingine. Tena safari hii bila ukinzani. Naya
alitulia tu wakati akibakwa. Aliyafanya yote atakayo mpaka akamaliza, Naya hana
habari.
Bahari Imechafuka.
Asubuhi
aliamka akiwa mchovu. Akabaki amejilaza tu hapo kitandani. Wazo likamjia
lakutoroka. Akatoka kwa haraka, hakukuta gari ya Malon ila kijana ambaye ni
mgeni kabisa kwake. Naya akamuwahi. “Naomba nisaidie simu nimpigie mume wangu.
Malon ameniteka nyara. Amenifungia hapa.” Huyo kijana akabaki kimya
akimwangalia vile kamasi zilivyokuwa zikimtoka Naya na akitetemeka baridi.
“Nisaidie kaka yangu. Mume wangu atakupa pesa yeyote utakayotaka, atakupa.”
Huyo kijana akatoa simu. Naya akafurahi sana akijua anampa yeye kumbe anampigia
Malon.
“Ameamka.
Ila anaomba simu ampigie mtu anayemsema kuwa ni mume wake, na amesema mumewe ni
tajiri, atanipa pesa ninayo..” Hapohapo Naya akakimbilia ndani na kujifungia.
Hazikupita dakika 10, Malon akawa anaegesha gari nje. Alikimbilia ndani kama
mwehu. “Fungua mlango Naya, nitakuua.” Baada ya vitisho vikali Malon akigonga
mlango kwa nguvu, Naya akafungua mlango wa chooni akilia kwa hofu. Alimvuta
kumtoa pale chooni na kuanza kumpiga. Kile kipigo alichoona na kusimuliwa huwa
anawapiga wafanyakazi wake, siku hiyo Naya alikipata. Alimpiga Naya kama mwizi.
Alimpiga bila kuchoka mpaka aliporidhika akamuacha. “Nilikuonya, na narudia
tena. USINIJARIBU. Maana wakati nahangaika na wewe, na Joshua naye alikuwepo
hapa duniani. Lakini sikumsikia. Narudia kukuonya Naya. Usinijaribu.”
Malon akatoka.
Naya
alishindwa hata kujigeuza pale sakafuni. Alikaa hapo baridi ya sakafu ikimpiga
siku nzima bila hata chakula mpaka usiku kabisa ndipo Malon akarudi. Hakumuona
tena Bale. Akashindwa kuelewa alipo kaka yake kwani ni kama walionekana wapo
pamoja. Malon alimpita hapo chini sakafuni. Akajitayarishia maji, akaenda kuoga
na kurudi kukaa sebuleni. Alianza kula bila kumuongelesha Naya. Naya akabaki
hapohapo sakafuni. Mpaka Malon akamaliza kula, akaenda kulala na kumuacha
hapohapo sakafuni akitetemeka, Naya asijue kama ni baridi au hali inayompata
mpaka apewe sindano. Kabaki hapo sakafuni akishindwa hata kusogea ila kugugumia
asiamini kinachomtokea.
Bale.
Mahusiano
ya Malon na Bale yalibadilika. Ni kama Malon akampandisha cheo Bale akawa
msimamizi badala yake na safari hii wafanyakazi wote wakajua kama Bale ni
msimamizi mkuu wa Malon. Hata safari hiyo aliyo mfanikishia kumletea Naya
nyumbani, alimpa safari ya kwenda Dubai kupokea mzigo waliokwisha safirisha
huko na akawa amemtambulisha kwa wenyeji huko nchini Dubai kuwa wamsaidie kama
yeye.
Bale
aliyekutana na Naya wa safari hii alikuwa mambo safi. Pesa ipo kwani
alishafundishwa biashara iliyomsaidia Malon kutoka kwa haraka, mwanzoni kabisa
wa maisha yake mpaka kuja kumfunga jela na Naya kumtoa. Kuuza bangi ila
sasa yeye Bale akajiongeza na mirungi pia. Malon akamfundisha
jinsi ya kuuza kwa akili bila kukamatwa kirahisi. Na kwa kuwa alionekana ni
jasiri na anao moyo wa kuthubutu, Malon akamtia moyo kuwa atafanikiwa kwa
haraka sana.
Bale
akaweka juhudi. Akayajua masoko yake kwa haraka. Na kweli ilikuwa ni biashara
inayolipa papo kwa hapo. Nipe bangi au mirungi, nikulipe. Ndani ya juma moja,
akaunti za Bale zikaanza kusoma namba zinazoeleweka. Hilo likamfurahisha sana
Bale kuona pesa imeweza kuingia kwa haraka kwa kiasi hicho! Ikamsogeza karibu
zaidi na Malon. Hapakuwa na kitu Malon anamwambia, Bale anakataa. Akaweka
heshima zaidi kwake. Na ni Malon huyohuyo kwa mara ya kwanza anamtoa
nchini, tena kibiashara! Hilo likamfurahisha zaidi Bale. Ujasiri wa
pesa ukachipuka ndani yake. Bale aliyekuwa na maono ya kuwa na pesa nyingi,
akaona tumaini jipya. Akaelekea nchini Dubai kwa biashara halali ya Malon huku
ile yale haramu, ikiendelea nchini.
Kwa Naya na Malon.
Wakati
kaka yake akifurahia mafanikio yake bila kujali lolote, huku kwa dada
yake fungate ya kibabe ikaendelezwa na Malon. Baada ya kile kipigo
kibaya na cha kikatili alichokipata bila huruma kutoka kwa Malon, Naya alibaki
pale sakafuni usiku huo mpaka kesho yake nakushindwa kutoka hapo kabisa.
Alijisikia mdhaifu wakupitiliza. Maumivu yakupita kiasi mwili mzima, akabaki
akigugumia peke yake. Asubuhi Malon aliamka na kumpita hapo kama hamuoni.
Akajitengenezea chai, akanywa peke yake, akamuacha Naya amelala palepale
sakafuni, hakumsemesha na Naya naye hakuwa amelala, ila tu akimsindikiza kwa
macho kila anapokwenda.
Alitoka
na kumuacha hapo sakafuni, Naya hakuomba dawa. Mchana napo akarudi
na chakula. Naya akafungua macho, akamuona anakula macho kwenye simu. Akala
alipokaribia mwisho akamuangalia Naya, akakuta ametulia tu amejikunyata hapo
sakafuni. “Kama unasubiri kubembelezwa, jua kipigo kingine kitakufuata
nikikukuta hapo jioni nikirudi.” “Sikuogopi Malon, na hunitishi.”
Naya akajibu akitetemeka sana. “Unasemaje Naya?” “SIKUOGOPI.” “Nitakuumiza
Naya!” “Huna uwezo wakuniumiza Malon. Huna. Na kama unahesabu
kunisulubisha huu mwili wangu ndio kuniumiza, basi nakuhurumia wewe.”
“Naya
utalia wewe!” “Mpuuzi tu wewe. Utamtisha nani? Huna akili ndio maana umekimbia
shule. Huna uwezo wakufundishika. Kichwa chako kimejaa maji matupu ndio maana
umeshindwa hata kukaa kanisani kujifunza neno la Mungu tu. Huna
uwanaume wa kweli kama Joshua wangu, ndio maana umerudi kutisha watu. Kwa kuwa
unajua bila...” Malon akasimama pale na kuanza kumpiga mateke. Safari hii Naya
akawa anamcheka huku akificha maeneo ya tumbo kwa kujikunja kabisa, magoti
mpaka kifuani. Mwishoe Malon akaondoka.
Kwa Bale.
Baada ya
safari yake ya Dubai, huku dada yake akitumikia kifungo cha Malon mchana na
usiku tena bila chakula cha kutosha, Naya akimvizia akiondoka ndipo ale makombo
kama yalibaki, Bale akamfuata Geb siku hiyo ofisini kwake. Akasubiria hapo nje
ya ofisi maana sekretari alimwambia yupo na mgeni. Baada ya muda wake aliopanga
yeye Bale wa kusubiria kupita, akahesabu anapuuzwa, na kudharauliwa. “Acheni
dharau jamani! Hata sisi tuna majukumu yetu na ofisi vilevile. Nimekaa hapa
muda wote, huyo Geb hatoki kwa lipi mno!” Bale akaanza kupayuka. Akaongeza
sauti kwa nguvu ili hata wa maofisini wasikie.
Askari
akaingia. “Kwema?” “Muulize huyo.” Bale akajibu. “Anataka kumuona Magesa.
Nimemwambia yupo na mgeni, asubiri. Hata dakika kumi hazijapita, anaanza
kelele!” “Kwani unayo miahadi.” “Sina. Nimekuja kumdai Magesa mali yetu. Aache dhuluma.
Anatuonea kwa sababu anaona mzee wetu hayupo..” Geb na Nanaa wote
wakatoka maofisini kwao kwa wakati mmoja.
Geb
akabaki akimtizama akiwa amekunja uso. “Nataka hati yetu ya nyumba yetu ya
Kiluvya.” Geb akamtizama kwa sekunde kadhaa, kisha akamuuliza. “Wewe unaidai
kama nani?” “Mrithi wa mzee.” “Wewe sio mrithi wa kile kiwanja cha
Kiluvya. Ila Naya. Baba yako aliacha kwa maandishi hapa kwangu, tena
mbele ya mwanasheria akiwepo.” “Kile kiwanja kilikuwa mali ya mama wala si
baba. Mama aliko..” “Tafadhali subiri nimalize. Usiniingilie ninapo zungumza.”
“Utanifanya nini?” “Nitakutoa hapa vibaya sana na hutaruhusiwa kurudi tena
hapa. Na siku nyingine unapokuja hapa, hakikisha unaongeza nidhamu kwa kila
unayemkuta hapa. Unanielewa Bale? Maana kama haupo tayari kunisikiliza mimi, sitaki
upoteze muda wangu. Unanielewa?” Geb akawa mkali kabisa.
“Wewe si
umesema na wewe unayo majukumu na ofisi, basi inamaana unaelewa juu ya uthamani
wa muda. Usirudi hapa bila Naya ambaye ndiye mwenye kiwanja kwa sasa.
Yeye ndiye atakayeidhinisha kupewa wewe hiyo hati na si vinginevyo.
Hujaridhika na hilo, nenda kashitaki popote maana mirathi ya baba yenu ipo
hapa. Na urudi na pesa yangu tasilimu kwa kuwa ndio yalikuwa makubaliano yangu
na baba yako, tena kwa maandishi. Kama hujaelewa, nikusaidie kwa kifupi. Mambo
mawili. Hati ni ya Naya. Sitatoa hati kwa mwingine yeyote isipokuwa Naya
mwenyewe awepo hapa na asaini mbele yangu na mwanasheria kuwa amekukabidhi wewe
hiyo hati. Na pesa yangu yote.” Akamtajia kiasi cha pesa anachomdai baba yao.
Bale akapoa.
“Kama
huna swali, askari huyo hapo atakusindikiza nje. Na kama unaswali uliza.”
Taratibu tu ila akiwa ameweka sura ya kazi. Akamkazia macho Bale. Nanaa kimya
akimtizama Bale. “Nitarudi.” Bale akajibu na kutoka.
Huku Kwa Naya Mwenye Mali.
Siku moja
jioni Malon akarudi akamkuta Naya amelala kitandani anatetemeka kupita kiasi.
Hali mbaya kwelikweli kama teja aliyezidiwa haswa kwa mwili kukosa madawa.
“Wewe si unajidai jeuri? Sasa sikupi dawa.” “Ni afadhali nife, kuliko kukuomba
wewe mshenzi tu. Nahisi unanipa madawa ya kulevya, unataka niwe teja
lako! Hakika bora kufa kuliko na mimi niwe kama wewe. Tena hata nikizidiwa,
nikakuomba, usinipe. Jichome mwenyewe madawa yako yakulevya. Tumia bangi na madawa,
vyote. Ila sio mimi. Hutanigeuza teja.” Malon akamcheka akimsogelea. “Kwa
taarifa yako tu, umeshakuwa teja ni vile hujajiona ulivyo sasa hivi. Mbovu
kuliko teja la mtaani! Unatokwa mikamasi na jasho kama teja tu. Sasa kaa na
hiyo hali ukijua nimekuweza. Na unakumbuka wakati ukikimbia siku ile
nilikuhakikishia nitakukamata tu, ukadhani mwanaume wako ataweza kukuficha
kwangu?” Akamuuliza kwa kumkejeli huku akivua nguo zake Naya akimwangalia.
“Yuko
wapi sasa hivi?” Naya kimya. “Nimebaki mimi kukutumia nitakavyo.” Akamvuta pale
kitandani akamvua nguo kwa nguvu, akaanza kumbaka huku amemshika kikatili. Naya
akaanza kumcheka. Malon hakujali mpaka akamaliza. Naya akakaa pembeni ya
kitanda akajifunika shuka bado akitetemeka, akaanza kumcheka tena.
“Huwa
nafikiria Malon.” Malon akamwangalia. “Usinipige kwanza. Nisikilize tu.” Naya
akawa anacheka kilevi. “Nafikiria kama Mungu angekupa wewe, nusu ya Joshua,
sijui ingekuaje!” Malon akamrushia teka. Naya akazidi kucheka. “Mwanamke mmoja
tu, mpaka ukanivutie bangi ndio uweze kunilala! Tena hata hujui unachofanya!
Unafanya fujo za kupitiliza hapa mpaka upate bao, upo hoi!” Malon akakaa kwa
hasira.
“Kama
hapo unajiandaa kunipiga kwa kuwa huna uwezo wa hoja, mshenzi na mjinga wewe.
Huna akili Malon ndio maana hata wewe mwenyewe unajijua huwezi kufanya kitu
bila bangi. Huwezi kumlala mwanamke bila bangi. Huwezi kuishi na watu una...”
Naya alishitukia kibao cha nguvu usoni akatema damu akicheka. “Mjinga tu wewe
Malon. Huna lolote na huwezi kumiliki chochote.” “Mbona nilikubikiri wewe?”
Naya akacheka sana.
“Nilikuwa
nikikuchezea nitakavyo!” “Ni wewe au bangi? Huna uwezo huo wewe na wote
tunajua. Si ulijaribu kuacha bangi ukashindwa kuwa kama wanaume wengine
wanaoishi na uwezo waliojaliwa na Mungu! Au akili yako ndogo imesahau wewe ni
nani!?” Naya akamuuliza akimkejeli. “Kaa na wanaume wenzio kama kina Joshua
wanaojua kumuweka mwanamke kitandani, wakufundishe. Anakuweka kitandani lisaa,
mchezo hauchoshi! Mwanaume hatokwi jasho! Hafanyi mazoezi kama wewe wala havuti
bangi na mchezo mrefu anauweza. Wewe ukitolewa bangi hapo, hamna kitu.
Unatukana mchana na usiku na kuhesabia watu vitu sababu huna akili. Na
hata ukirudi shule wewe, akili yako haina akili utafeli tu wewe, mpumbavu wa
mwisho. Fala wa mafala tu wewe Malon. Hata kanisani umeshindikana mtoto
wa shetani.” Malon alimrushia teke la nguvu lililomtoa Naya kitandani, akagonga
kichwa kwenye ubao wa kitanda, kisha akatua sakafuni, kimya. Malon akaondoka.
Bale Kwa Naya.
Huku kwa
Bale alipotoka tu ofisini kwa kina Magesa akaanza kuzungukia biashara yake
haramu hapo jijini. Akakusanya pesa na yeye akasaidia vijana wake hao wawili
wanao msaidia kuuza, akitaka apate pesa ya Magesa kwa haraka. Akafanya juma
zima mfululizo bila kupumzika, akafanikiwa kupata kiasi kikubwa tu cha pesa. Akawaongezea
mzigo vijana wake wanao mfanyia biashara, yeye akaondoka jijini kurudi alikomtelekeza
dada yake.
Aliadhimia
kujenga nyumba nzuri sana nyumbani kwao Kiluvya, yeye kama Bale akitaka kutoa
kumbukumbu ya baba yake kabisa pale, ubaki mji wake yeye. Kwa kuwa alikuwa na
moja ya gari la Malon, hakusimama hovyo njiani. Aliendesha mpaka usiku mwingi
sana. Akafikia hotelini kama kawaida yake. Hataki tena shida, Bale maisha
yamembadilikia. Akamtumia ujumbe Malon. ‘Nakuja kukuona kesho. Nataka
kuzungumza na Naya.’ Malon alipopata tu ujumbe, akatoka hapo baa usiku huo haraka
kurudi alipomuacha Naya.
Alichofanya
Malon baada yakumkuta anapumua pale sakafuni, ni kumvalisha tu nguo na
kumrudisha kitandani, akamfunika na kumuacha hapo. Akajilaza na yeye pembeni.
Asubuhi akaamka na kutengeza kifungua kinywa mpaka cha Naya. Akaona Naya
haamki. Akaenda kumtoa pale kitandani kwa nguvu na kumuweka sebuleni. Naya
akaamka, akamtizama kwa kumshangaa. “Kunywa chai.” Naya akamwangalia tu. “Wewe
Naya?” Malon akamuita kwa ukali kidogo. Kimya. “Nimekwambia kunywa chai, Naya,
acha kiburi!” Akawa kama anamtisha lakini akawa kama hamuelewi anachoongea.
Akaiangalia ile chai, akajirudisha nyuma ya kochi, akapandisha miguu
akajikunyata.
Bale naye
akawa anaingia. “Vipi huyu?” “Amegoma kula.” Bale akamwangalia pale
alipojikunyata. Akafikiria kidogo akaona asimpoteze malengo. “Naya, nataka hati
ya Kiluvya. Magesa anasema hawawezi kunipa mpaka wewe ukaidhinishe, na
niwalipe.” Malon akashituka sana kusikia Bale anazungumzia habari za kina
Magesa ambao ni kama Joshua! “Ati nini!?” Akauliza Malon kwa kuhamaki. “Nataka
hati ya kiwanja cha Kiluvya kwa jina langu mimi na si Naya. Kumbe mzee
alikopa pesa ya biashara kwa Magesa, akaweka kiwanja cha mama yangu
rehani mpaka alipie. Sasa mimi nataka nikilipie. Ila siwezi kulipia kiwanja
ambacho bado hakijawa changu! Twende tukaandikishane mbele ya huyo Magesa. Kuwa
nitamlipa mimi kwa awamu, na baada ya kumaliza pesa yote, kiwanja kinakuwa
changu sio cha Naya ambacho ni kama cha Joshua tu. Maana Joshua anaweza kuja
kukidai na kisheria yeye kama mume wake huyu kihalali, akashinda na kuchukua
jasho la mama yangu hivihivi! Hakika sikubali.” Naya kimya. Malon
akabaki akifikiria.
“We
Naya?” Bale akaita kwa ukali. Naya kimya amejiinamia. “Hakika tunakwenda Naya.
Kile kiwanja ni jasho la mama. Najua wazi mama angetaka mimi ndio
niendeleze ule mji sio uishie kwako ambapo itakuwa ni kama mama alimnunulia
Joshua! Hakika SIKUBALI. Baba na akili zake mbovu asizoweza kufikiria
mbali, anakukabidhi wewe kiholelaholela tu! Twende.” Akamvuta Naya kumtoa pale
kitini. Akaanza kulia maumivu kuwa anamuumiza. “Simama sasa!” Bale akamuamrisha
Naya.
“Subiri
kwanza Bale. Yaani unataka kuondoka naye sasa hivi!?” “Hili zege halilali.
Nakwenda kushugulikia haki yangu, nakurudishia mwanamke wako.” “Haiwezekani
Bale!” “Hakika INAWEZEKANA Malon. Na ninaondoka naye sasa hivi. Katika hili hakuna
mjadala. Kesho asubuhi kama leo nitakuwa nimefika Dar, nataka nikawekane sawa
na Geb. Kesho hiyohiyo namrudisha. Kwanza wala usiwe na wasiwasi. Jinsi nilivyokuta
hali kule, hakuna yeyote anayemtafuta huyu. Wote wanaendelea na maisha yao kama
kawaida. Hakuna anayemtaka tena. Kwanza yeye mwenyewe nikimwangalia ujanja wote
umemuishia!” Bale akaongea kwa kumkejeli dada yake. “Muone alivyo! Kwisha
habari yake! Huyu utakaa naye mpaka uchoke wewe, umfukuze. Wewe usiwe na
wasiwasi.” Bale akatoka na dada yake kwa hasira sana bila kutaka kutoa nafasi
ya mjadala kwa Malon. Akamuingiza kwenye gari, kiti cha nyuma, safari yakurudi
Dar tena ikaanza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya
alilia maumivu huko njiani mpaka akalala, bila hata kuongeleshwa na Bale. Ila
Bale alipokuwa akitaka kupiga simu zake alikuwa akimwambia apunguze sauti,
kisha kuendelea kuzungumza na simu zake bila kumjali, mpaka akalala.
Kilichomshangaza Bale ni pale alipomuamsha na kumwambia Naya ashuke
akajisaidie, Naya akawa hajui hata kama anaitwa Naya na hamtambui yeye ni nani
kabisa. Bale akaanza kwa ukali akidhania anamchezea akili, lakini akagundua pia
yupo kama teja!
Akampigia
simu Malon. “Ulikuwa ukimpa nini huyu, mbona amekuwa kama teja!?” “Janja yake tu
huyo, ili asikupe haki yako. Wewe humjui Naya nini! Anatumia kila njia
kujinufaisha. Akishapata anachokitaka ndio anaanza michezo yake hiyo. Sasa wewe
usipomkazania, ujue inakula kwako.” Malon akamkatia simu.
Bale
akamuacha hapo garini. Akaenda kula na kujisaidia akarudi garini, safari
ikaanza tena. Naya hakuwa amekula muda mrefu. Mwili unamuuma kwa njaa, maumivu
ya kupigwa na kubakwa mfululizo. Akalia tena mpaka akalala. Alikuja kuamshwa na
Bale usiku kuwa wamefika, ashuke garini. Naya akabaki anashangaa haelewi. Bale
akamvuta mpaka ndani. Ilikuwa nyumbani kwa Malon, Kunduchi. Bale alikuwa
akipatumia kila awapo hapo jijini Dar, kama kwake tu mpaka walinzi wote
walishamjua. Akamuingiza ndani na kumuacha, yeye akatoka kuzungukia dili zake
hapo mjini, usiku huo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa kuwa
yeye mtoto wa jiji, Bale alizaliwa jijini Dar, mtoto wa uswahilini tu. Akakua
akicheza na wajanja wa mtaani. Akasoma jijini pia. Basi hapakuwa na kona ya
jiji hilo asipofahamu. Akafanya biashara yake vizuri tu akifuata ule ushauri wa
Malon. Hata kama biashara itakuwa kubwa kwa namna gani, alimuonya asiongeze
wafanyakazi zaidi ya hao wawili tu, watakao mfahamu yeye. Wabakie hao wawili tu
wanao mfahamu yeye kama mwenye mali. Akamwambia kwanza itamsaidia kuwaongoza
vizuri na kwa urahisi, na pia kuepuka kukamatwa. Ila akamwambia kama wao
watatafuta watu wakufanya kazi chini yao, kusaidia kusogeza mzigo kwa haraka,
basi wasimjue yeye na yeye asiwafahamu. Iwe juu ya hao watu wake wawili. Hilo
likakaa sawa. Bale akawa bosi wa mabosi, vijana wa mtaani.
Na
japokuwa alikuwa ndio ameanza tu hana muda mrefu, ila ikawa ni biashara
inayomuingizia pesa hapo jijini na kuonyesha tumaini kubwa sana kwa Bale. Kwani
alifanya akiwa anatumia uzoefu mkubwa wa Malon. Kwa hiyo hapakuwa na makosa.
Harufu ya pesa ikawa inanukia mifukoni mwake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alirudi
usiku mwingi sana, dada yake bado akilia maumivu. “Vyovyote unavyotaka
kujiaminisha, mimi sijali. Uwe teja, mgonjwa, hiyo ni juu yako. Ila nakutaka
kesho uwe umetulia, ukazungumze kule kwa kina Magesa, nipewe haki yangu.” Bale
akalala bila kujali.
Mungu Hutumia Yeyote Na Chochote Kufanikisha Jambo Lake.
Asubuhi
na mapema, Bale akamtoa Naya hapo nyumbani. Tena kwa kumlazimisha achane nywele
na kuosha uso. Akamsukumia huko bafuni, akaona anampotezea muda kwani Naya
aliendelea kulia tu. Akatoka naye vilevile Naya akiwa na nywele zake zilezile
alizokuwa amesukwa sababu ya harusi. Alisukwa nywele ndogondogo. Ila alisukwa
chini tu, juu zikawa zimeachiwa. Kwa hiyo akawa na nywele ndefu ila hazikuwa
zimekaa vizuri, zimefungana sababu hazikuwa na matunzo hata ya kuchanwa tu tokea
atolewe saluni siku kaka yake amemfuata akiwa na Malon.
Njia
nzima Bale alikuwa akimwambia Naya kwa kurudiarudia kitu anachotakiwa kwenda
kuzungumza kwa kina Magesa. “Ukiharibu Naya wewe, utalia mara mbili ya hivyo.”
Bale akamtisha huku akiendesha mpaka kwa kina Magesa. Akamtaka ajifute uso na
nguo yake na akamwambia aache kulia. Baada ya kutulia kwa vitisho vingi ndipo
wakashuka garini akimkumbusha chakuzungumza na kumuonya asikosee. Safari hii
Bale alifika kwa kina Magesa bila ugomvi. Akaomba kuonana na Magesa mwenyewe.
Baada ya
muda akaambiwa aingie. Akaingia na Naya. Geb alishituka sana alipomuona Naya.
“Hujambo Naya?” Geb akamsalimia, lakini Naya kimya. Akabaki amekalia mikono
yake akifuta kamasi na jasho kwa mabega yake huku akitetemeka. Geb akashangaa
sana.
“Sitaki
kukupotezea muda. Nataka kulipa pesa yote unayomdai mzee. Ila kwa awamu tatu au
nne. Ila sitalipa mpaka tuandikishane kwamba nikilimaliza hilo deni, mimi ndio
utakayenikabidhi hiyo hati ya kiwanja changu.” “Ni cha Naya, na wakati mzee akizungumza
hivyo mbele yetu na wewe ulikuwepo Bale. Kwa nini unataka kufanya fujo sasa
hivi!?” “Mimi sifanyi fujo. Kiwanja ni cha mama yangu. Mimi
nimebeba jina la ukoo. Pale lazima nipaendeleze mimi mtoto wa kiume, hata mama
mwenyewe ndivyo angetaka hivyo. Tatizo la mzee hakuwa na uwezo mzuri wa
kufikiria. Anakwenda kumpa mtoto wa kike urithi wa famiia ili akiolewa huko
kikapotelee kwa mwanaume wake?!” “Naya alishaolewa na wala mumewe hajataka
kiwanja chake!” Geb akaongea akimshangaa sana Bale.
“Nisikilize
bwana Magesa. Mambo ya familia yetu wewe hayakuhusu. Uliniambia unamtaka Naya
aje akiri tena kwa maandishi kuwa kiwanja ananikabidhi mimi, nimemleta Naya
huyu hapa. Sijataka kesi ila kufuata ulichonishauri. Naomba tumalizane.
Nikulipe pesa awamu ya kwanza, nitamalizia zingine.” “Sawa. Subirini chumba cha
mkutano. Huyo dada hapo atawapeleka. Nataka kuandaa karatasi na kumuita
mwanasheria. Tusifanye mambo kiholela.” “Itachukua muda gani?” “Si mrefu.” Geb
akanyanyua simu nakumtaka sekretari wake aingie hapo.
“Naomba
waonyeshe chumba cha mkutano na uwahudumie chochote wanachotaka.” “Sawa.” Muda
wote huo Naya alikuwa kimya tu akitetemeka. “Twende sasa. Unatetemeka nini,
wakati nimekupa sweta?” Geb akabaki akimwangalia vile Bale anavyozungumza na
dada yake. “Wewe Naya?” Bale akamvuta kwa nguvu, Naya akaanza kulia. “Unaniumiza!” Naya
akalalamika akilia kama mtu asiye na akili vizuri. “Twende sasa.” Bale
akamsogezea kiti ili apite. Geb akashangaa sana ila akanyamaza mpaka
walipotoka.
Kwa Joshua.
Hapohapo akampigia
simu Joshua. “Kwema GM?” “Hapana. Hapa tunapozungumza, Bale na Naya wapo ofisini
kwangu.” Joshua akashituka sana. “Naya!?” “Ndiyo. Lakini si
Naya unayemfahamu wewe.” “Unamaamisha nini?” “Hayupo sawa. Na kwa jinsi
nilivyomwangalia na kumsoma kwa harakaharaka, sidhani kama anajitambua kama ni
Naya. Nikimaanisha hata kujua jina lake kama ni Naya, nadhani hajui,
kitu ambacho ninauhakika Bale hajajua kama dada yake hajitambui.”
“Sijaelewa GM!” Geb akamsimulia kwa vile alivyomuona Naya, na kwakuwa walishazungumza
tokea juzi yake juu ya ujio wa Bale pale ofisini kwake akiomba hati, Joshua
akaumia sana.
“Upo
Joshua?” “Nipo kaka. Nipo.” “Mimi naamini ulichosema ndicho kinachoendelea.
Japokuwa polisi walikukatalia juu ya kuandishisha kesi yake wakisema Naya hajatoroshwa
kwa kuwa aliaga kabisa, lakini mimi naamini. Hivi nilivyomuona, siye Naya
aliyekuandikia ujumbe. Ule ujumbe uliandikwa.” “Nisaidie GM, ndugu yangu.
Nisadie kaka. Nimekwama kila mahali! Nimemtafuta mke wangu nakaribia
kuchanganyikiwa!” “Hapa kuna mchezo nataka kumchezea Bale, hatajua. Subiri
nimpigie simu mwanasheria.” “Na mimi nakuja, japo nimuone kwa mbali tu.”
“Sawa.” Geb akamkubalia na kukata simu. Hapohapo Joshua akakimbilia
Ubungo zilipo ofisi za Magesa akitokea ofisini kwake bila hata kuaga.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya
nusu saa Geb, mwanasheria na kabrasha wakaingia hapo chumba cha mkutano. Naya
alikuwa ameegemea meza. “Naitwa Mangui, ni mwanasheria. Nipo hapa kumuwakilisha
Magesa, na bwana Denis ambaye ni marehemu. Ninayo hati ya eneo lake lilopo
Kiluvya, mirathi, na mkataba aliongia na bwana Magesa.” “Kwanza nashangaa ni
kipi kilichompelekea kumwachia Naya! Mimi amenishangaza sana! Lakini naomba
tuokoe muda. Naya aliyeachiwa huyu hapa, na yupo tayari kunikabidhi mimi. Wewe
Naya?” Bale akamuita, lakini Naya hakuitika. Akamtingisha. Naya akanyanyua
kichwa kamasi mpaka mdomoni.
“Jifute
wewe, acha ujinga!” Naya akabaki akimuangalia. “Nimekwambia futa kamasi.”
Akamsukuma kidogo, Naya akawa kama ameelewa kama ni yeye. Macho yalikuwa mekundu
sana. Bado anatetemeka. Akajifuta kwa mikono. “Ona lilivyo chafu! Sasa
utashikaje kalamu?” Akamsukuma kwa nguvu Naya akaanza kulia. “Unaniumiza!” “Ongea
sasa.” Bale akamuamrisha, lakini akawa kama hajaelewa. Akabaki akijifuta
machozi.
“We
Naya?” “Subiri kwanza bwana Bale. Naomba twende taratibu.” “Nina majukumu
yangu!” Akajibu kwa kiburi. “Basi rudi siku utakayokuwa na nafasi. Lakini mambo
lazima yaendeshwe kitaalamu ili hata kama ukitoka hapa hujaridhika, huko
utakapokwenda kushitaki uwe na habari kamili unazoelewa. Unanielewa?” Mungai
akamuuliza. “Basi changamka. Mimi nataka haki yangu leo. Sitaki dhuluma.” “Basi
tumeshakusikia. Naomba kuzungumza na Naya, mwenye mali.” “Mali ni ya mama
yangu.” Akakanusha Bale. “Ila kwa sasa ipo kwa jina la Naya.” Mungai akamsahihisha
Bale na kumgeukia Naya. Geb kimya akiwaangalia na kusikiliza.
“Naya?”
Akamuita lakini Naya akabaki kimya akijisafisha uso huku akilia taratibu.
Akajaribu kuita tena, ila safari hii kwa majina yake yote mpaka la baba yake,
lakini Naya hakuitika. “Una nini wewe Naya? Tulikubaliana nini!?” Bale
akamkaripia dada yake. Naya akamwangalia kwa hofu kubwa kama anayejihami
asimpige. “Nazungumza na wewe, na naomba umjibu huyu mwanasheria sijui, nani!
Mgeukie.” Naya akamgeukia akilia.
“Unaelewa
tunachozungumza?” Mungai akamuuliza Naya, lakini akabaki akimwangalia
akitetemeka. “Mjibu!” Bale akamuamrisha. Naya akatingisha kichwa kukubali.
“Nitajie majina yako yote matatu.” “Kunywa hayo maji mbele yako kwanza.” Geb
akamwambia taratibu. Naya akayaangalia, kisha akanyoosha mkono akitetemeka
sana. Akanywa yote kama aliyekuwa na kiu kali. Akamaliza. “Sasa tulia
uzungumze.” Bale akamuamuru tena.
“Nisawa
kama ukiacha mimi nikazungumza naye?” “Naona anajifanya mjinga wakati jeuri
kama yeye hakuna! Okoa muda Naya.” “Haya. Naomba majina yako yote matatu
yanayoonekana kwenye vitambulisho vyako.” Mungai akaongea akimwangalia yeye.
Naya akaonekana kufikiria kisha akasema. “Joshua.” Alitamka
akivuta kamasi huku akijifuta. “Hilo ndilo jina lako!?” Naya akatingisha kichwa
akikubali huku akijifuta. “HAA!” Bale akahamaki. “Kwamba leo wewe unaitwa
Joshua!?” Bale akamkaripia kwa nguvu Naya akamwangalia akiwa amekunja uso, kama
anayemshangaa yeye.
“Ujue
Naya wewe unanichezea akili na sikubali! Sema jina lako.” Naya akaanza
kulia. “Naomba nikazungumze naye, kisha tutarudi.” Mungai akataka kumkatalia,
Geb akasema wao ndio wawapishe pale. Wakaacha kila kitu mezani, wakatoka.
Walipotoka tu wakaanza kusikia makofi, Naya akaanza kulia kwa uchungu sana. “Unaniumiza
mimi. Unaniumiza.” “Wewe tokea lini unaitwa Joshua, kama si makusudi tu! Yaani
uitwe jina la mwanaume!? Bora ungetaja la kike! Hayo ni makusudi na sikubali.”
Akasikika ni kama anampiga tena, Geb akarudi kwa haraka. Kisha akaingia na yule
mwanasheria.
“Acha
kumuumiza dada yako sababu ya mali, Bale!” “Kama wewe unaona kitu kidogo mbona
hunipi, unanizungusha tangia juzi?” “Hata kama bwana Magesa atataka kukupa,
haitawezekana kwa sababu haya mambo baba yako hakutaka yaendeshwe kiholela. Alinilipa
kwa hili ninalofanya. Sasa kwa kifupi tu, endapo Naya atashindwa kunitajia
majina yake yote matatu niliyo nayo mimi na yanayoonekana kwenye kitaambulisho.
Na kueza kujibu maswali yangu yote nikaridhika, siwezi kuidhinisha
mkataba mwingine, kwakuwa tutakuwa tunaingia mkataba na mtu ambaye hayupo
kwenye fahamu zake sahihi. Yaani hana akili timamu, na kisheria sio sawa. Hairuhusiwi.
Anaweza kurudi kesho, akavunja mkataba kabisa akidai leo hakuwa kwenye akili
yake timamu, na kisheria akashinda.” “Hawezi kurudi huyu.” Bale akaongea
akimdharau dada yake.
“Hayo
unaongea wewe, sasa hivi kwa kuwa unaharaka, unataka mambo yaishe. Mimi sifanyi
kazi kiholela. Nendeni mkakae na kuzungumza tena, ndipo mnitafute. Kwa heri
bwana Magesa.” Naya alikuwa akiendelea kulia pale alipokuwa amekaa huku
anajificha uso.
“Naya una
roho ngumu wewe! Kweli unanikatalia haki yangu! Hakika utanipa tu. Twende.”
Akamuamuru, Geb akiwatizama. “Nimekwambia simama.” Akamnyanyua kwa nguvu sana.
Naya akazidi kulia. Akamsukuma kumtoa mlangoni. Naya mbele, kaka yake nyuma
akimsukuma kumtoa hapo. Alipomtoa tu kwenye hicho chumba akimsukuma kikatili,
Naya akajikojolea akilia. “Haa! Unajikojolea kama jinga wewe!?”
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment