Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 36. - Naomi Simulizi

MAPENZI&PESA! – SEHEMU YA 36.

 Wakati Bale anamgombesha pale nje ya mlango, Nanaa na Joshua wakatoka kwenye chumba cha pembeni. “Acha kumfanya hivyo.” Joshua akaingilia kwa ukali sana. Naya akaendelea kulia kamasi zikimtoka kama kondoo. “Hayakuhusu.” “Yananihusu kwa kuwa mimi  ni mume wake.” “Inamaana hukupata ujumbe aliokuandikia Naya, wa kukuacha?” Bale akamuhoji  Joshua. “Naya hakuniandikia mimi ujumbe. Ni mke wangu na alipotea kwenye mazingira ya kutatanisha. Anatafutwa na polisi kila mahali.” Wakamuona Bale ameingiwa na hofu.

          Kwa haraka Geb akatumia akili akitumia hofu ya Bale. “Sera. Niitie askari polisi hapo nje ili awasaidie hawa.” “Nisikilizeni. Sitaki kesi, nataka haki yangu.” “Ndio hiyo unataka kupewa. Sera, mwite askari.” “Sasa mnaniitia askari wa nini!?” “Kwanza upo na mke wa mtu kimakosa. Yupo na wewe akionekana kabisa si kwa matakwa yake na hayupo kwenye akili zake timamu. Anaonekana ni mgonjwa na anahitaji msaada wa haraka ambao wewe huonekani kama upo hata na mpango wa kumsaidia ila kutaka yeye asiye na akili timamu, ndio akusaidie.” Geb akazidi kumtia hofu.

          “Anaakili timamu sana tu! Mbona wakati yeye na baba wakinitenga kwenye familia mbona Naya alisikika vizuri sana?” Bale akajibu kwa uchungu sana akionekana na hasira. “Hivi wewe Bale unajua kama baba yako alikufa mgojwa kwa sababu yako?” Bale akamgeukia Nanaa kwa hasira na wasiwasi kidogo. “Baba yako amekufa akikutafuta Bale.” “Huo ni unafiki kabisa. Nimeyasikia majibu yake yote alipokuwa akiambiwa jinsi ya kunipata, na kukataa! Alinitoa kwenye familia yake kabla hajafa! Amekufa kwa yake mwenyewe.” Bale akajibu kibabe.

 “Basi kwa taarifa yako na sisi tunajua sana kama aliuwawa wala hajafa kwa yake kama unavyosema. Joshua amefanya uchunguzu, ametafuta watu wakafanya uchunguzi kwa kina kujua chanzo cha moto uliosababisha kifo chao. Maana ile nyumba ilitengenezwa upya umeme na mafundi wa hapa kwenye hii kampuni yetu. Hapakuwa na shida ya umeme ila mtu alianzisha moto kwa kurushia chupa iliyokuwa na dizeli ndani, kisha ikawashwa moto na kurushiwa kwenye nyumba waliyokuwa wamelala wao. Chupa imeokotwa na ushahidi upo polisi. Uchunguzi unaendelea. Baba yenu, mdogo wenu, bibi na mjukuu wake wameuwawa kikatili sana na mtu ambaye anaonekana alikusudia kulipa kisasi kwao. Aliyefanya au kutengeneza huo mpango, alionekana kufanya kwa makusudi kabisa.  Waliwasubiria wakiwa wamelala kabisa wakijua hawatawahi hutoka ndani kwa kuwa walishafunga na milango yote.” Bale akapoa kabisa akaonekana kuna kitu kimemuingia.

Nanaa akaendelea. “Mimi sijui umesikia nini na wapi! Sijui unakotolea taarifa zako. Lakini kabla ya siku kama 4 hivi za harusi ya Naya, baba yako alikufuata mpaka Mbeya! Akaambiwa ulikwenda Tunduma. Yule mzee akiwa amefunga, na kila mahali akisikia jinsi ulivyoacha sifa zake mbaya kama hivi hapa unavyomtukana kama hana akili ya kufikiria. Akiwa hali wala kunywa, alikufuata Bale. Tena alitoa amri Naya aolewe asimsubiri yeye maana alisema yeye hatarudi bila wewe.” “Uongo huo. Sio kweli. Baba alikubali maisha yaendelee bila mimi.” Bale akabisha.

“Wewe amini vile unavyotaka kuamini. Ila baba yako alikwenda mpaka Tunduma ilikosemekana umekwenda kufanya biashara, tena haramu. Kabla hajakupata akatekwa nyara sababu alikuwa akikutafuta kupitia mtu hatari sana aliyesikia wewe mwenyewe, kwa tamaa zako ulimfuata huko Tunduma ukijua aina ya biashara unayokwenda kufanya. Lakini baba yako alikufuata Bale akitaka angalau ajiridhishe upo salama kwa kuwa alipata ujumbe wako kuwa humtaki yeye ni mjinga, hana akili ya kufikiria.” Nanaa akaendelea kwa jazba.

“Watu wakamkatisha tamaa hata asikufute huko Tunduma, kwa kuwa huyo mtu ni hatari lakini alikwenda. Na alipofika huko nako wakamtisha kwa kumpa habari za kweli juu ya huyo mtu kuwa ni kweli ni hatari na analindwa mpaka na askari waovu, lakini baba Naya alikataa kurudi nyuma, akasema hataogopa wala kurudi mpaka akutane na huyo mtu aliyesikia anajua ulipo. Tena huyo mtu anaitwa..” Nanaa akawa kama amesahau.

“Mbabe.” Geb akamsaidia mkewe maana Joshua yeye akili zilishahama pale kwa Bale, akawa ameshamsogelea Naya na kujaribu kumtuliza lakini akawa anamkwepa. “Usinipige kichwani. Naumwa sana kichwa. Nipige huku kwingine.” Naya akasikika akilalamika akijikinga kichwa. “Sikupigi Naya. Nataka kukusaidia kukufuta machozi.” “Usinishike kichwa. Kinauma sana.” Naya akaendelea kulia taratibu akijaribu kusogea mbali kidogo ya Joshua.

Umelaaniwa Bale. Unapiga dada yako mpaka anakuwa tahira sababu ya mali alizoacha baba yenu, aliyekuwa akikupenda hivyo! Tena wala baba Naya hakusema Naya awafukuze pale. Muulize Joshua huyo aliyeachiwa maagizo yote na baba Naya. Baba yenu alitaka nyinyi watoto wa kiume mtambue pale ni kwa Naya pia. Ili vikishindikana huko, basi mumfungulie mlango dada yenu! Hakutaka wake zenu na watoto wenu waje kumfukuza Naya! Alitaka na yeye Naya awe na sehemu ya kudumu, kimbilio wakati akihitaji! Lakini si kwa kuwa alikuwa akikuwazia wewe au Zayoni mabaya kuliko Naya! Yule mzee alikuwa radhi akose sherehe ya Naya akutafute wewe mpaka akupate bila kujali matusi yako, au vile ulivyokuwa hutaki mahusiano naye tena ukisema waziwazi humtaki. Baba yako hakujali akasema ni mpaka akupate ili kujiridhisha tu upo salama. Ila ndio watu wa Mbabe wakamteka nyara baba yako kabla hajakupata tena akiwa hotelini Tunduma, amepiga magoti akikuombea kwa simu na huyu Naya unayempiga.” Nanaa akaendelea ila wakashangaa utulivu wa Bale. Ni kama alitulia kabisa akisikiliza kama anayetafuta kuelewa.

“Wakampiga sana mpaka Geb na Joshua walipokwenda huko kumtafuta maana kama nilivyokwambia, alitekwa nyara kwa kuvamiwa hotelini, ndani ya chumba alichokuwa amefikia, akiwa amepiga magoti yupo kwenye simu na Naya, tena alianza kwa kumuhusia tena Naya, maana sisi wote alishatuaga hapa kuwa mambo ya harusi ya endelee hata kama yeye hayupo maana alisema hatarudi bila wewe. Akarudia tena kumwambia Naya kabla hawajaanza kuomba kuwa yeye maisha yake yaendelee bila yeye kwa kuwa yeye hatarudi bila wewe! Na vile baba yenu alivyowapenda nyinyi watoto, akatuambia wote, kwamba hata kama atauwawa huko alikokwenda kukutafuta, maiti yake ifungiwe chumba cha maiti, Naya aendelee na ndoa yake. Hakutaka hata mmoja wenu aharibikiwe zaidi kwa ajili yake.”

“Baba yenu alikuwa akilalamika na kujutia sana kuwa amefanya makosa mengi, hakubahatika kufanikiwa kama wazazi wengine, ndio maana hataki tena kuendelea kuwachelewesha. Tena hayo alimwambia mama kwa simu, maana ilibidi mama kumtafuta na kuzungumza naye kwa undani akimwambia wosia anaoacha kwetu, sio picha nzuri kwa jamii endapo kweli lolote baya likimtokea, halafu sisi tuonekane bado tunaendeleza sherehe ya Naya! Akamwambia anaomba afute hiyo kauli, wosia wake ni mzito. Baba yenu alikataa akasimamia hapohapo, Naya huyu akimlilia lakini akakubali kumuacha Naya hapa, yeye akawepo Tunduma akikutafuta!” Nanaa akamsimulia kila kitu Bale, na kumuacha Bale anatamani kulia.

“Baba yako amerudishwa hapa jijini na kina Joshua, akiwa mgonjwa, anaanguka kifafa sababu ya kupigwa kichwani huko kwa kina Mbabe, akikutafuta wewe, leo unamfanyia hayohayo dada yako! Umelaaniwa Bale. Mungu hatakuacha wewe.” Bale kimya akabaki akifikiria. Maana kweli Mbabe anamjua.

“Tena nikwambie kabisa, baba yako hakuacha kukutafuta Bale. Aliomba watu wamsaidie kuzunguka mahospitalini na vyumba vya maiti, baada ya kushindwa kupatikana huko magerezani.” “Tena kwa pesa zake mwenyewe, aliniomba nisubiri malipo yangu, awe ananilipa kiasi cha chini ya pesa tuliyokuwa tumekubaliana, ili hiyo pesa ya kukutafuta wewe ailipe mwenyewe wala si Joshua tena aliyekuwa akilipa watu waliokuwa wakikutafuta. Ndio chanzo cha kuja kuacha hapa hati yake akitaka kuniaminisha sio kwamba anakwepa kunilipa pesa ya biashara tuliyokuwa tukifanya naye. Ila akanisihi nimvumilie akinihakikishia lazima atamaliza pesa yote akiweza kukupata au kujiridhisha upo salama sehemu, yaani haupo matatizoni. Na hayo yote yalimgarimu pesa ya kutosha tu.” Geb akaongezea kwa mkewe.

“Sasa hapa huondoki na Naya. Askari yule pale. Ukimgusa tu Naya, nakuitia mwizi hapa, wakupige kisha nakupeleka jela. Haya mlango huo hapo, toka na uchu wako za mali. Kijana mzima unapigania mali za kurithi na si kutafuta mwenyewe kiwanja chako ujijenge kama wanaume wenzio, unalilia mali za mama yako! Huna aibu wewe! Na kama sio umeanza kuvuta bangi ni nini wewe uliyeshindwa kukanusha mbele ya baba yako siku ile, mbele za watu wote, tena akasema alishazungumza hata na mama yenu! Unakuja hapa unamtukana mume wangu eti anataka kuwadhulumu! Tena toka kabla hujaniudhi zaidi.” Nanaa akazidi kukasirika, akiongea kwa sauti.

“Na ukamwambie huyo mwalimu wako anayekufundisha kuvuta bangi, tumemchukua Naya, na tunakwenda kumuonyesha ustawi wa jamii na polisi ili muanze kuchunguzwa huko mlikokuwa mmemficha Naya.” “Mimi sitaki kesi ndio maana nilikuja na Naya, tuyamalize.” “Kwa kumpiga dada yako?” Nanaa akamuuliza kwa ukali.

“Naombeni nimpeleke Naya hospitalini jamani! Hayupo sawa. Anatetemeka baridi ya ajabu, kichwa kinamuua mpaka namuona anaogopa kujishika kichwani yeye mwenyewe! Hata machozi anaogopa kujifuta! Naya hayupo sawa. Naombeni mimi niende.” “Naweza kukusaidia.” Bale akajirudi. “HATUTAKI. Toka hapa na bangi zako. Na tusikuone tena. Twende mwaya Joshua.” Kazi ya Nanaa nayo ikaishia hapohapo. Mama bosi huyo akaingia ndani, akabeba pochi yake akawa amemaliza siku yake ya kazi bila kuaga, asubuhi na mapema hiyo, siku ikiwa ndio imeanza, na majukumu yake mengi kuliko yeyote kwenye ofisi hiyo. Lakini hakujali, akatoka kama ni jioni vile, amemaliza siku ya kazi! Geb akabaki akimwangalia mkewe jinsi alivyonunua ugomvi. Ila akafurahi kuwa amemuweza Bale.

“Usinishike mimi. Naumwa!” Naya akalalamika akilia taratibu. “Nataka kukupeleka hospitalini, Naya. Si unaumwa?” Joshua akamuuliza taratibu, akatingisha kichwa taratibu sana, akikubali. “Unataka nikusaidie kukushika mkono?” Akakataa. “Mkono nao unauma?” Joshua akaendelea kumuhoji kwa kujali. Akakubali akijifuta machozi na kamasi kwa hofu sana kama anayeogopa kujitonesha ila nazo zimemzidi zikiingia mpaka mdomoni. “Wewe Bale, kwa nini Naya yupo hivi!? Mlikuwa mkimpa nini?” “Mimi sijui.” Bale akajibu hivyo na kuondoka kwa haraka.

“Basi sitakushika. Twende hospitalini. Tupitie mlango huo.” Akaanza kutoka akiwa amejikojolea. Nguo mbichi! Mbali na mkojo, Naya alikuwa akinuka. Alitoa harufu kama aliyemchafu, hajisafishi vizuri. “Pole Naya.” Nanaa akajaribu kumsemesha. Naya kimya akitembea kutoka mlangoni. “Joshua. Nendeni na Nanaa, mimi nitawafuata baadaye.” “Wewe piga kazi GM. Tutawasiliana.” “Basi kukiwa na kitu chochote tafadhali mnijulishe.” Nanaa alishatoka bila hata kumuaga mumewe, macho kwa Naya.

Ikawa shuguli kuingia kwenye gari, Naya analia maumivu hawezi kunyanyua mguu kupanda kwenye gari ndefu ya Joshua! Hataki tena kwenda. Kazi ya kumsihi apande garini apelekwe hospitalini ikaanza. “Naumia mimi!” Alipoona wanamkera, akaanza kuondoka pale taratibu. Joshua akamkimbilia akikumbuka maneno Naya aliyomwambia siku ya harusi yao, masaa machache kabla yakufunga ndoa akiwa amemuokoa kutoka kwenye gari yake Malon alipomzuia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Naya alimwambia maneno yaliyokuwa yamebaki moyoni mwake, japokuwa alitaka kumkasirikia kwa nini alimfungulia Malon mlango wa gari, lakini Joshua akabaki akimtetea nakusema Mungu aliruhusu lile kosa alilofanya Naya, kwa ajili yake yeye mwenyewe Joshua, ili tu kumsikia Naya akitoa moyoni mwake jambo alilotamani kulisikia kwa mwanamke yeyote atakayemuoa wakati huo akiwa amefanikiwa sana. Joshua alitamani sana mapenzi ya dhati. Alimpokea Naya na kukubali amuoe kwa imani tu, akiamini kuwa, hatua za mwenye haki huongozwa na Bwana, akampokea Naya kwa shukurani bila uhakika kama Naya huyu kama kweli angemkubali akiwa na dhiki!

Lakini katikati ya fujo ile, Joshua akapokea yale maneno kwa furaha akiamini Mungu amezungumza naye kwa kumtoa hofu au kujibu swali kubwa alilokuwa nalo ila kushindwa kuliuliza kwa yeyote hata kwa Naya mwenyewe. Akiwa ameingiwa hofu, Naya akaongea akiwa wala hajajipanga azungumze hayo, akamsikia Naya akimuapia wakiwa na Geb kwenye simu kuwa hatamuacha hata kama atafilisika na kupoteza kila kitu, atamchukua na kwenda kuishi naye kwa baba Naya wakijipanga upya. Tena akaongeza hata akiwa mgonjwa mahututi wakugeuza kitandani, basi Naya akaahidi atabaki naye kumuuguza mpaka kifo. Hatamkimbia. Naya anajitetea kwao kwa hofu akijua ameharibu na Malon ameongea maneno yanayofanana na ukweli, huko moyoni Joshua alikuwa akimshukuru Mungu wake kwa kumpa wakusimama naye mpaka kifo. Ndio maana walipofika nyumbani, Joshua akalemewa katikati ya mabusu mazito akiwa amejihakikishia kwa hakika Naya ni wake, akatamani amalize hapohapo mpaka Nanaa akatokea.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Joshua akaongeza mwendo na kwenda kusimama mbele ya Naya aliyekuwa ameshafika mbali kidogo ya alipoegesha gari yake. “Nakuahidi nitakuwa mwangalifu wakati wakupanda garini, hutaumia. Twende watakupa dawa ya kutoa hayo maumivu.” Ndipo akakubali na kurudi garini, wakielekea hospitalini. Njiani Nanaa akampigia simu Sonia Tambo, mwanasheria anayewasaidia ushauri mwingi wa kisheria ambaye naye alikuwepo kwenye kitchen party na harusi ya Naya pia. Akamtaarifu kurudi kwa Naya na hali aliyokuwa  nayo kwa wakati huo. Akawashauri lazima waanzie polisi kuripoti lasivyo kila jambo baya atakalokutwa nalo Naya huko hospitalini litakuwa kwao. 

Naya/Joshua.

Japokuwa Joshua aliona nikupoteza muda, lakini akakubaliana nao. Wakaanzia kituo cha polisi kuandikisha kesi na kupata RB, jina alilokuwa akilijua Naya, ni Joshua tu. Akakazania kwamba hilo ndilo jina lake hata hospitalini akajitambulisha kwa daktari kama anaitwa Joshua. “Kabla ya kukimbilia kuwa ni tatizo la akili, naomba apimwe kwanza kichwa. Analalamika kinamuuma. Na hawezi hata kusoma. Kama kweli alikuwa akipigwa, inawezekana wamegusa sehemu ya ubongo.” “Na pia tusubiri majibu yake ya damu na mkojo. Inavyoonekana alikuwa akitumia madawa ya kulevya. Hiyo hali ni ya mateja. Akipewa unga hapo, atatulia kabisa.” Daktari akaongeza akiwa ameshapata muda wakutosha wakumchunguza Naya. Joshua akaumia sana. Naya hakuwa akielewa wala kutambua chochote.

Vipimo vya kina na vya haraka vikaanza kwa mke wa Joshua Kumu, mfanyakazi na kiongozi wa ngazi ya juu sana wa kampuni ya Coca. Mbali ya kuwa bado alikuwa ni kama mfanyakazi, japo Joshua alimchukulia likizo bila malipo, lakini Naya alikuwa kwenye hospitali hiyo ya wenye nazo akilipiwa matibabu hayo ya garama za juu sana na kampuni, kama mke wa Kumu. Huduma zilikuwa ni za haraka, na za kisasa, halafu na madaktari walikuwepo wakutosha kumuhudumia Naya kwa kadiri ya uhitaji wake.

Baada ya yote, vipimo vikaonyesha damu ipo na madawa ya kulevya, kwamba ni kweli alikuwa akitumia madawa ya kulevya. Na majibu ya vipimo vya CT scan yalionyesha Naya ana uvimbe kwenye ubongo. Jambo lililopunguza wasiwasi mkubwa kwa Joshua ni pale daktari alipoeleza kuwa haukuwa uvimbe kama mwenye kansa ila ni uvimbe mdogo tu wa kama aliyekuwa amegonga kichwa sehemu inayohusika na kumbukumbu, na ndio ikamsababishia kupoteza kumbukumbu. Na wakaambiwa kwa matibabu, utakuja kuisha tu. Hilo likawa faraja. Alipoulizwa ilikuaje, Naya hakuwa akikumbuka chochote.

Matibabu yakaanza akiwa ameshatolewa nguo za mikojo, na kupewa mavazi ya hospitalini. Napo walishangaa ila wakaelewa ni kwa nini alikuwa pia hataki kuguswa hata mkono. Naya alikuwa amevilia damu kila mahali kama aliyekuwa akipigwa sana. Joshua akazidi kuumia na kushindwa kuelewa nini alipitia huko alipokuwa.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Maisha ya Joshua yakahamia hapo hospitalini akimuuguza mkewe. Japokuwa Naya hakuwa akimtambua kabisa, lakini hakuacha kuwa naye mchana na usiku. Siku ya kwanza anajua Naya analazwa, alikwenda kufungasha vitu vyake akiwa amemuacha hapo Nanaa, na ombi asije akaondoka hapo kabla hajarudi. Na kweli alifanya haraka, akakusanya vitu vyake muhimu na vitu vya Naya, akarudi hospitalini kwa haraka. Akawa kama amehamia hapo hospitalini hata asitoke. Kama ni simu za kiofisi, alizungumza nje akiwa anaona mlango wa kuingilia chumba alicholazwa Naya peke yake bila mgonjwa mwingine, akihofia wasije kuja kumchukua tena. Naya alikuwa akimka, anamtizama kwa muda mrefu ila hamuongeleshi kisha anarudi kulala.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya siku tatu ngumu wakijitahidi kusafisha damu yake, akitapika na kulia maumivu kila wakati huku madaktari wakimkatalia kumpa madawa makali, usiku huo kidogo akalala akionekana ametulia. Sio kama alivyotapika siku mbili mfululizo akionekana kama teja. “Vipi sasa hivi kichwa?” Joshua akamuuliza baada ya kutoa macho kwenye laptop yake na  kukuta Naya akiwa ametulia akimtizama. Akamuona anavuta pumzi kwa nguvu kisha akatulia. Ila akaacha kumuangalia.

“Pole.” Akageuka na kumtizama tena Joshua. “Ninaumwa nini?” Naya akauliza taratibu. “Kichwa. Unakumbuka nini kilitokea?” Akafikiria kisha akamuona anatingisha kichwa akikataa. “Sasa hivi upo na maumivu yeyote?” “Hapana. Wewe ni nani?” Naya akamuliza taratibu tu. “Joshua.” Naya akabaki akimtizama. Ila Joshua akaumia sana.

Akasimama. “Umenikumbuka?” Joshua akamuuliza. “Nakufahamu?” Naya akamuuliza taratibu akionyesha kushangaa ila na wasiwasi kidogo. “Ndiyo.” Naya akamtizama kwa muda. Akamuona anafunga macho. “Usijali. Jipe muda. Utakumbuka tu.” Akamwangalia na kubaki akimwangalia kama anayejitahidi kufikiria zaidi. Joshua akatamani amwambie mengi ila akaogopa kumchanganya. Akamsaidia kumfunika vizuri, ila kwa tahadhari, kisha akasogea pembeni kidogo. Wakatulia.

“Hapa ni wapi?” Naya akauliza tena. “Ni hospitalini. Ulikuja ukiwa unaumwa.” “Sasa hivi nimepona?” “Kesho asubuhi unafanyiwa kipimo kingine tena, ndipo daktari atatujulisha. Ila wanajitahidi kukupa dawa ya kupunguza maumivu, ili usipatwe na maumivu makali kama  mwanzo.” “Kweli kichwa kilikuwa kikiniuma sana.” Akaongea akifikiria. “Pumzika.” Akamuona analala. Akafungua macho kabisa.

Kisha akafungua macho na kukuta bado Joshua amesimama akimtizama. “Ulisema unaitwa Joshua?” Akawa kama anataka uhakika. Joshua akatoa tabasabu la kufariji akimwangalia kwa kuwa bado alikuwa amesimama pembeni ya kitanda chake. “Ndiyo naitwa Joshua.” Akatulia akimwangalia, kisha akamuona anasinzia tena. Usiku huo akalala, akiwa ndio kwa mara ya kwanza kuzungumza kwa muda mrefu. Kipimo kingine cha kichwa, MRI kilionyesha uvimbe unanywea. Wakaruhusiwa Naya akiwa anamwangalia sana Joshua.

Baada ya Kuruhusiwa Hospitalini.

Naya alielewa kuwa ndio ameruhusiwa kutoka pale hospitalini. Madaktari walipotoka tu, akamgeuki Joshua. “Asante. Lakini mimi naondoka.” Joshua akashituka sana moyoni ila akajikaza. “Unakwenda wapi?” Hapo akatulia kama anayefikiria. “Ni kama nimeruhusiwa!” “Ndiyo. Ila unatakiwa kuendelea kutumia dawa na kuhakikisha hurudii tena kutumia madawa mabaya.” Hapo Naya akawa hajaelewa, akabaki akitafakari. “Hujanijibu Naya. Unataka kwenda wapi?” “Samahani lakini. Ni kama hata nimesahau mimi ni nani! Kwani nilitakiwa kwenda wapi baada ya hapa?” “Turudi wote nyumabani kwetu.” “Unamaanisha nini!?” Naya akauliza akionekana kwa hakika haelewi.

“Kwani wewe ni nani?” “Joshua Kumu, mumeo.” Naya akashangaa sana. Akabaki akimwangalia. “Hukumbuki?” “Hapana! Hata kidogo. Kwani kama sio kwenda na wewe, ningetakiwa kwenda wapi?” Naya akauliza akionyesha kutoridhia kabisa kuondoka na Joshua. Joshua akatulia kidogo akifikiria. “Siwezi kwenda na mtu nisie mfahamu. Samahani. Unaonekana wewe ni mtu mzuri, ila sikufahamu kabisa. Naogopa sana.” “Unakumbuka kuniona hapa muda wote?” “Ndiyo ila sijui ni kwa nini ulikuwa hapa!” “Ili kukuuguza, wewe.” Naya akabaki akimtizama kama asiyemuelewa kabisa. Akajua anamkatalia, ikabidi aongeze ushawishi asipokonywe tonge mdomoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bado Joshua alikuwa akitaniwa juu ya ndoa changa na watu wa karibu, ila mke hayupo nyumbani! Akabaki kupokea pongezi za ndoa tu. Akamchukulia Naya likizo bila malipo huko kazini ili asije poteza kazi, akiamini tu, Mungu hajawahi kumpokonya vitu ampavyo. Akabaki akiomba huku akimsaka Naya kwa udi na uvumba. Na bado aliendelea kufanyia uchunguzi chanzo cha moto uliomuua baba Naya na ndugu zake mkewe. Akiwa hajui kama Bale yu hai au la, kwa sababu ni kama habari zake hazikuwa zikieleweka vizuri, ndipo akapigiwa simu na Geb kuwa Bale yumzima, ametokea ofisini kwake akidai kiwanja.

Ile Geb kumkatalia na kumwambia lazima awepo Naya, na Bale hakuonyesha hilo ni tatizo, moja kwa moja Geb akamwambia Joshua, kuwa Bale anajua Naya alipo. Joshua akaumia kuona kwamba walishindwa kumfuatilia Bale kujua Naya alipo ili kama kuhitimisha ndoa, basi ahitimishe Naya mwenyewe kwa mdomo wake, tena mbele ya Joshua mwenyewe.

Lakini Geb akamtuliza. Akamwambia uchu aliouona kwa Bale, atarudi tu, tena atarudi kwa haraka na hapo ndipo wambane mpaka aseme Naya alipo. Tangia asikie hivyo, Joshua akatembeza mfungo akimsihi Mungu na kumkumbusha ahadi zake mpaka alipompata Naya na ndipo akabaki akishukuru Mungu kuwa amemrudishia mke, na safari hii akaaga kwa ujasiri kazini kuwa mkewe anaumwa, amelazwa, anamuuguza. Kazi zote atafanya akiwa hospitalini. Leo Naya anamuaga kwamba hamtambui! Joshua akaona ang’ang’anie muujiza wake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 “Nikuulize kitu Naya?” Naya akabaki kimya. “Unakumbuka daktari kukukumbusha kwamba wewe unaitwa Naya?” “Aliniambia mimi siitwi Joshua ila Naya. Ila sikumbuki kabisa!” “Umebakia na jina langu moyoni, Naya. Mimi ni  mumeo. Naomba uniamini ujue sina sababu ya kukudanganya.” Naya akanyamaza. “Unakumbuka kuniona nipo hapa, nikikusumbua?” Naya akatingisha kichwa taratibu akikataa, huku akimwangalia. “Ndivyo itakavyokuwa nyumbani. Nitakupa chumba chako. Utulie hapo, mpaka utakaponikumbuka. Ni sawa?” “Hujanijibu swali!” “Kwamba kama sio kwangu ungetakiwa kwenda wapi?” “Ndiyo.” “Huna pakwenda Naya, ila ni nyumbani kwetu, mimi na wewe.” Naya akakunja uso kama anayeshangaa.

“Daktari alishauri tusikwambie mambo mengi kwa wakati mmoja ili tusikuchanganye. Ila mimi na wewe tuliona, na wote hatuna wazazi ila marafiki tuliojitengenezea ukubwani wakawa kama ndugu. Unamkumbuka Nanaa?  Hata asubuhi hii alikuwa hapa akakupeleka bafuni kuosha uso?” “Namkumbuka pamoja na mumewe na mama yake. Si wote wanakuja hapa kila wakati?” “Ewaa! Basi hao ni baadhi ya watu wetu wa karibu sana. Wanakuja hapa asubuhi na jioni kukuona wewe. Wanatupenda sana na wamekuwa kama ndugu.” Joshua akaendelea taratibu.

“Nanaa na Geb walitusimamia harusi yetu. Tukaenda mapumzikoni. Tukawa na wakati mzuri sana.” Akamuoana anaanza kukosa raha. Akajipandisha kitandani vizuri. “Kwa nini sikumbuki hayo yote?” “Naomba usilie. Ila naomba jipe muda. Ulipotea Naya. Ndio nimekupata tu! Tafahali amini sikudanganyi.” “Nilipotea!?” “Ndiyo. Ila umerudi ukiwa hujitambui, ndio maana naogopa usije ukaondoka hapa, ukapotea tena.” “Kwa nini sikumbuki hayo yote!” “Naomba tulia kabisa. Usilie. Taratibu utakumbuka. Na hata kama hutakumbuka, una maisha marefu sana yakuishi, utaendelea kuanzia utakapokumbuka.” Akamuona anajifuta machozi na kujaribu kutulia.

“Nikupe maji ya kunywa?” Akakataa. Muuguzi akaingia na karatasi za kuruhusiwa na dawa alizoandikiwa Naya. “Hata akilalamika maumivu vipi, usimpe dawa mbali ya hizi ili kuhakikisha madawa makali hayarudi mwilini mwake.” Naya akamsikia Joshua akipewa maelekezo. “Nimeelewa.” “Poleni sana, na nawatakia kila la kheri.” Muuguzi akatoka. Akamsogelea Naya. “Kwa hiyo tunakwenda wote?” Joshua akamuuliza taratibu. “Utapata wakati mtulivu, bila muingiliano wowote. Nitakupa chumba chako tu. Twende Naya.” Akakubali.

Geb na Nanaa nao wakaingia. “Vipi Naya?” Geb akamsalimia lakini akanyamaza akimtizama huku ni kama akisinzia. “Unajisikiaje?” Nanaa akaongeza swali. “Vizuri.” Akajibu na kunyamaza. Pakatulia kwa muda. “Naona sisi tupo tayari kuondoka.” Joshua akavunja ukimya akimwangalia Geb. “Basi acha mimi nibebe mizigo, ndio tutoke pamoja.” Geb akanyanyua kila kifurushi hapo chumbani kama mzoefu wa kulazwa hospitalini. Mkewe akamsaidia kubeba baadhi, wakatoka. “Twende Naya.” Maana alibaki ametulia hapo kitandani. “Nikusaidie?” Joshua akauliza kwa kujali, ila kwa tahadhari asije muudhi na kubadili mawazo. “Hapana.” Akatoka kitandani akabaki amesimama. Joshua akamfungulia mlango kama kumuashiria atoke. Akatoka taratibu.

“Niambie unavyojisikia.” Joshua akabembeleza. “Kizunguzungu halafu nachanganyikiwa. Sielewi tena! Kidogo nilicho nacho kichwani, naambiwa pia sicho! Sielewi.” “Kama jina?” “Najua mimi naitwa Joshua. Ila kila mtu ananiita Nay..” Akasita. “Naya.” Joshua akamsaidia kumalizia kisha akaendelea kumfariji. “Lakini usijali. Jipe muda.” “Itakuaje nisipokuja kukumbuka tena?” “Kama nilivyokwambia. Jipe muda. Kama usipokumbuka, ishi kutokana na vile utakavyokuwa unaelewa na kuweza. Hakuna mtu anakutegemea kwa chochote. Tulia tu. Sawa?” “Sawa.” Wakatoka hapo kurudi nyumbani, wakisindikizwa na kina Magesa. 

BALE.

Kisasi.

Bale aliondoka pale ofisi za Magesa akiwa ameumia sana. Hakujua ukweli wote kwa hakika kama ulivyo. Ili kupata uhakika wa kile alichokisikia kutoka kwa Nanaa, akaamua aanzie Tunduma. Kuhakiki kama kweli baba yake alikwenda huko. Kwa kuwa alimjua Mbabe mtu wa madili na mpenda pesa sana, akakanyaga mafuta mpaka Tunduma huku akijipanga. Alishayajua yale mazingira mpaka na watu wake. Akajua wapi aanzie. Aliendesha kwa muda mrefu sana na hakutaka kupokea simu za Malon. Ila alimtumia ujumbe kuwa atarudi baada ya siku 4. Akamzimia kabisa simu.

Alifika majira ya jioni, akatafuta sehemu akaegesha gari na kulala kabisa mpaka aliposikia mji umetulia kabisa, ndipo akatoka sasa kumtafuta Mbabe. Alijua atamkuta kwenye moja ya baa anazopenda kunywa. Hakuingia ila akamtuma muhudumu na pesa. Akamwambia amuite, amwambie ni dili ya pesa nyingi. Kama jina lake lilivyo, akatoka akiwa anajisifia akijua mji huo hakuna atakayemfanya chochote. Akamkuta Bale garini, akashituka kidogo akikumbuka unyama aliomfanyia Bale.

Akiwa yeye ndiye mwenye mali hizo za magendo, akimuahidi atamlipa asilimia 50 ya mauzo yote endapo atafanikiwa kuutoa. Lakini walipo kamatwa, akamsingizia Bale kila kitu. Akamtupia lawama zote. Akatolewa yeye jela akamwacha Bale bila kugeuka nyuma. “Mimi sijui walikwambia nini wale askari wa mpakani, lakini hivi hapa nilikuwa nikijipanga, nikutoe.” “Acha woga wewe. Twende nikakupe dili la ukweli. Pesa ya ukweli bila jasho.” “Kweli?” “Sasa unafikiri mimi ningefanikiwa vipi kwa haraka kama sio hivyo? Twende.” “Hamna mambo ya visasi?” “Mimi  naelewa biashara na ulishanipa madhara yake kabla, nikakubali mwenyewe. Twende nikupe dili za kiutuuzima.” Bale akasikika mwenye mamlaka sio kama mwanzoni alipokutana naye. Bale akionekana mgeni wa mambo.

Mbabe akapanda garini. “Kwanza kwa nini kama umefanikiwa, umenitafuta mimi?” Akawa kama bado anao wasiwasi. “Napanua soko langu la bangi na mirungi. Sasa kwa kuwa wewe mjanja, na umezoeana na askari mpaka wamipakani, naona soko litakuwa zuri huku.” Mbabe akaanza kushawishika. “Maana mimi nauza bangi daraja la kwanza.” Bale akaendelea kumvutia akiwa anaondoa gari hapo kwenye hayo maeneo. “Unatoa wapi?” “Sasa nikwambie halafu iweje!? Wewe mbona kama unakuwa mgeni wa biashara tena!?” Mbabe akacheka kwa heshima kidogo akijua anaongea na mtu wa maana.

Bale akaendesha kama anayemtoa mjini. “Tunaenda wapi sasa!?” “Acha wasiwasi wewe! Mbona unakuwa kama sio wewe? Umeanza lini woga, Mbabe?” Akacheka na kutulia. Hakumpeleka mbali sana. Giza lilikuwa jingi tu, akaacha njia kuu na kuingia njia ya vumbi, aliporidhika hakuna mtu huko akasimamisha gari. “Mbona hakuna mtu hapa?” “Ndio penyewe, sasa wewe unataka na mashahidi tena!?” Akamuuliza akicheka kama anayemsanifu.

“Shuka.” Mbabe akiwa na sitofahamu kubwa mpaka usoni mwake, akafungua mlango na yeye Bale akafungua mlango wake na kutoka garini. Akazunguka kwenye mlango wa nyuma akatoa gongo akawa amelishika kwa nyuma, akamfuata Mbabe mpaka pale aliposimama akishangaa. “Unaona kule?” Mbabe akageuka ili kuangalia anapoonyeshwa, Bale alimpiga gongo la shingoni sehemu aliyojua atapoteza fahamu kama alivyomuona Malon akimfanyia Naya na kweli akaanguka na kupoteza fahamu hapohapo bila hata kutingishika. Alishajiandaa kwa kila kitu.

Wakati yupo chini hajitambui, akamvua nguo zote. Akamfunga kamba ambayo tayari alishanunua ilikuwa kwenye gari. Akamfunga vizuri mikono na miguu na kuikutanisha kwa nyuma. Akachana shati lake na kumuingizia baadhi mdomoni ili asiweze kupiga kelele. Taa za gari zilikuwa zikimulika pale mbele alipomvuta. Giza kila mahali. Halafu kulikuwa na hali ya baridi na Mbabe alikuwa mtupu kabisa kama alivyozaliwa.

Bale aliporidhika amemfunga vizuri, akachukua tena maji aliyokuwa ameyahifadhi kwenye dumu, nyuma kabisa ya gari. Akammwagia, Mbabe akaamka. Alipangilia kila tukio atakalomfanyia Mbabe, akiwa njiani na akahakikisha hakosei hata kitu kimoja. Akaanza kuhangaika akitaka kupiga kelele. Bale akampiga mateke kumtuliza. “Nisikilize Mbabe. Nina maswali nataka kukuliza. Ukinijibu, nakuachia. Ukipiga kelele nitakapotoa hilo shati mdomoni, ujue nitakuumiza kwa kuwa utakuwa ukinipotezea muda. Kama umenielewa kubali kwa kichwa.” Mbabe akakubali akitetemeka.

“Kama mwezi sasa umepita. Nilipokuwa jela, kuna mzee alikuja kunitafuta mimi kama Bale. Unakumbuka? Jibu ndiyo au hapana kwa kichwa.” Akakubali. “Sasa nakutoa shati mdomoni, ili unielezee ilikuaje. Nakuonya usinipotezee muda kwa kuwa hapa tulipo hakuna atakayekusikia. Acha kupoteza muda, uongee. Sawa?” Akakubali. Bale akamtoa kipande cha shati lake mdomoni. Mbambe akaanza kupiga kelele. Bale akachukua mkanda wa suruali yake na kuanza kumtandika nao kila mahali bila huruma, tena kikatili sana. “Nitaacha, utakapoacha kupiga kelele.” Mbabe akanyamaza.

Bale akampiga teke la tumbo. “Tuanze tena. Eleza kilichotokea kwa mzee wangu alipokuja kunitafuta.” “Mimi sikujua kama ni mzee wako. Nikajua ni watu wa usalama wamekuja kunichunguza. Nikawaambia vijana wangu wamchukue, wakamtoe ukweli. Sasa walichomfanya huko, hawakuniambia.” “Ila mimi na wewe tunajua walichomfanya ili kumtoa ukweli, na bado hamkumsadiki!” “Wewe unayajua maisha Bale na umepita nilikopitishwa mimi. Huwezi kuamini maneno tu! Mpaka walipokuja wale vijana wawili na maaskari wakasema hawataki kesi ila kumtaka tu yeye, ndipo akaenda kutolewa.” “Kutolewa wapi!?” “Alikuwa amefungiwa Bale! Si nilisha kwambia?” Bale akaumia sana.

“Sasa nipo hapa kulipiza kisasi. Si kwa uliyonitendea, ila uliyomtendea baba yangu. Kwa kuwa yeye hayupo, mimi nitakulipiza kisasi ikawe fundisho. Na sitakuweka kitambaa mdomoni. Nakuadhibu ili ulie sana, nataka masikio yangu yasikie kilio chako. Ukome.” Bale akaanza kumpiga kama mwizi. Safari hii alimpiga na gongo kila mahali, bila huruma kama aliyepagawa. Akampiga viwiko vya miguu kama anayetaka asije tembea tena. Akampiga magoti. Kiunoni ndio zaidi. “Hapa ndio kutakusaidia usiwahi kuja kulala na mwanamke tena.” Akampiga hapo tena na tena. Akarudia mikononi. Bangi ilimsaidia kuhakikisha anampiga mpaka anasikia sauti ya mifupa kuvunjika bila huruma. Akatulia akimwangalia.

“Sasa nimeridhika. Uso na mdomo nakuachia ili ukawasimulie wale askari na vijana wako. Kawaambie Bale amenilipiza kisasi kwa niaba yenu wote kwa kile mlichomtendea baba yangu. Waambie nikirudi tena kwenye huu mji, wajue nilibadili mawazo, nimeona wewe hutoshi, nitakuwa nimerudi kuwalipiza na wao. Na atakayenifuata, nitamrudisha maiti.” Bale mwenyewe alikuwa akihema.

Akamuingiza tena Mbabe kwenye gari. Akamrudisha mpaka njia kuu. Akamuacha sehemu ya wazi kabisa, akilia kama mtoto mdogo. Yeye akaondoka kurudi kwa Malon akimjua Malon jinsi alivyo mkorofi. Akaanza kujipanga sasa kumkabili Malon.

Kwa Malon.

Alikwenda alikojua atamkuta Malon huku moyo wake ukimuuma sana akiwa ameamini alichoambiwa na Nanaa. Akajiuliza mengi juu ya Malon huku akijilaumu akiumia. Alikuwa akielekea sio sehemu ambayo Malon alikokuwa amejificha na Naya. Alijua mida hiyo anakusanya mazao kwenye mashamba yake na kuyaweka kwenye gala kuu la huko Mbeya. Sehemu aliyofikia yeye mwanzo kabisa. Alifika alfajiri tu na mapema, kila mtu amelala. Akaamua kulala garini nje ya gala.

Akiwa amepotelea usingizini akasikia kioo kikigongwa. Akafungua macho alikuwa Malon. “Naya yuko wapi?” Bale akatoka garini. “Kwanza wewe ulikuwa ukimpa nini?” “Acha kunihoji wewe! Nijibu.” Bale akachukua kibegi chake garini. “Naya yupo Dar mgonjwa na hajitambui kabisa. Hata jina lake hajui ni nani?” “Hiyo ni janja yake tu ili kukukwepa. Naya tapeli sana.” “Wewe achana na maswala yangu.” Bale akampita kama aliyemaliza. “Unamaanisha nini wewe? Kwa nini hujarudi na Naya!? Tulipanga nini na unafanya nini?” Bale akasimama kwa hasira.

“Hivi unasikia chochote ninachokwambia Malon?! Nakwambia Naya ni mgonjwa, hajitambui! Wewe niliyekuwa nimekuacha naye hapa, hukujua kama nimgonjwa?!” “Ningejuaje mimi?” “Naya tuliyemchukua majuma machache yaliyopita sie huyu! Amekua kama teja! Nakuuliza umekuwa ukimpa nini, hunijibu! Sasa unamuulizia wa nini?” “Kwamba yupo anapewa matibabu?” “Matibabu gani, wakati ndio nakuuliza ili kuweza kumsaidia, hunijibu! Labda nirudie tena, Naya umekuwa ukimpa nini, mbali na zile dawa ulizoniambia mimi ni za usingizi, ulimpa nini?” “Ni zilezile. Labda kwakuwa hakuwa akinywa pombe au hajawahi kuweka kileo chochote kile mwilini ndio maana imemchukua vile. Haya nimekujibu, na wewe nijibu yuko wapi?” “Subiri kwanza Malon. Naya analalamika sana maumivu. Ulikuwa ukimpiga?” “Maswali gani hayo Bale kutaka kunifanya mimi mtoto mdogo? Acha ujinga wewe.” Bale akaondoka pale akitaka kuelekea kwenye nyumba wanayoishi.

Siri Mwangani.

“Umekua na vijisenti, ndio unaanza jeuri Bale wewe mimi ndio nakufundisha biashara! Hukuwa na kitu, umekua mtu, unaaza dharau kama ndugu zako!? Kweli nyinyi wote hamkujaliwa shukurani! Mnapenda kutumia tu watu!” “Ndio maana umemchoma moto baba yangu na mdogo wangu!?” Bale akamuuliza swali la moja kwa moja kama ambaye hakuwa amepanga hivyo au silo lililompeleka pale kumbe lengo lilikuwa na hilo swali pia, kujiridhisha akimtetea Malon kuwa hata kama ni mnyama kiasi gani, hawezi kuwa alifanya unyama ule kwa familia yake!

Malon akababaika kidogo. “Eti Malon? Uliamua kuwalipa ndugu zangu vibaya kiasi hicho ukaamua uwachome kabisa!?” “Kweli Bale huna shukurani kama ndugu zako! Walikutelekeza jela, mimi nikaja kukutoa, leo unaniambia hivyo!” “Labda nikuulize Malon, wewe ulijua kama baba alikwenda Mbeya kunitafuta akaishia kutekwa nyara, wakampiga vibaya sana mpaka Joshua na Geb kwenda kumuokoa huko, na bado alikusudia kurudi tena kunitafuta!?” “Wameshakudanganya huko Dar, wamekujaza uongo, unarudi kwangu kwa kiburi! Sio wewe nilikusikilizisha maneno waliyonijibu juu yako?” Malon akamuuliza kwa ukali kabisa.

“Ulinisikilizisha ulichotaka wewe, na mimi nikaamini kutokana na nilichotaka kusikia kwa wakati ule nilipokuwa na hasira, tena hasira ulizosababisha wewe.” “Mpuuzi wewe Bale na huna shukurani! Kweli wewe unaniambia hivyo mimi!?” “Acha kupaniki, nipe simu yako tujue leo nani ni muongo.” “SIKUPI.” “Kwa kuwa unajua nitakutana na rikodi za ukweli. Wewe ulitengeneza mazungumzo Malon.” “Mjinga tu wewe, Bale.”

“Nahisi Naya yupo sahihi. Na nahisi ni bangi imekuharibu kichwa mpaka huamini mtu anaweza kukupenda wewe kama Malon, mpaka uwe na kitu. Ndio maana unatumia nguvu nyingi sana kuvuta watu kwako. Lakini usingemuua baba yangu Malon. Mzee alikupenda sana japo mama alikukataa, ila baba alisimama na wewe mpaka wewe mwenyewe uliposhindwa kuendeleza uongo wako ndipo akaamua aachane na wewe, na Naya aamue mwenyewe! Naya anaolewa na Joshua, bado mzee akabaki kuwa mkarimu kwako, akikufungulia milango mpaka ukashindwa mwenyewe! Kweli unamchoma mzee wangu kwa wewe mwenyewe kushindwa kuwa mwanaume!?”

“Wewe bangi zinakuchanganya Bale. Sio wewe tuliweka wote mipango hapa, ili kuwaadabisha na kuwakumbusha wao ni kina nani? Kuwatoa pale walipofikishwa na kina Joshua, na kuwarudisha chini kabisa! Leo imetokea ajali kazini, unarudi kunilaumu mimi!?” “Acha kujidai mjanja Malon. Tulikubaliana tuchome lile gala mida tunayojua kabisa watu hawapo pale nyumbani. Nyinyi mkawasha moto nyumbani na wala si galani, tena mkijua wamelala!” “Wewe kama unasumbuliwa na kuuwa ndugu zako wewe mwenyewe, ni juu yako Bale. Wakati moto unawashwa tulikuwa wote huku. Iweje leo uje unitupie mimi lawama! Ushanisikia mimi hata siku moja nataka nikawachomee moto wazazi wangu mali zao au kuwadhuru kwa namna yeyote ile?” Malon akamuuliza akimsuta na kumuumiza sana Bale akijiona mjinga.

“Hata siku moja! Wewe mwenyewe ulikubali. Tukaweka mipango. Kwa kuwa wengine hatujui kuwa vigeugeu, mambo yamefanyika, sasa hivi unakuja kulaumu! Nani amekwambia kuua mzazi wako au kumwaga damu ya mtu ni jambo rahisi!? Mimi na uovu wangu wote huu, sijawahi ua. Wewe umemwaga damu ya watu wanne, tena ndugu zako!”  “Kwamba sasa hivi mimi ndio nimeua!?” Bale akashangaa sana.

“Twende tukajieleze polisi, tuone wataamua vipi hii kesi. Acha kujifanya umechanganywa na bangi ulizokutana nazo ukubwani wewe! Na ninamtaka Naya, kama tulivyokubaliana. Kama wewe umeshindwa kusimamia mipango yako, mimi sijashindwa. Namtaka Naya, bado sijamalizana naye. Umenisikia Bale? Nenda kamlete Naya kabla hujaniudhi zaidi na haya mambo yakaenda mbali nikakurudisha jela, na nikuongezee na kosa la uuaji.” Bale akarudi ndani ya gari.

“Nitamrudisha.  Ila naomba nikukute hapahapa sio kule.” “Unafikiri mimi nipo kama wewe! Utanikuta hapahapa nikimsubiri. Sijamalizana naye na kama ukishindwa kumleta, jua unarudi jela, na Naya nitampata tu. Hakuna mwanaume wakumficha Naya kwangu, nisimpate.” Bale akaondoka akiwa ameumia sana ila Malon akafurahia kuwa amemtisha mpaka ameenda kumchukua Naya.

Kwa Naya.

Naya alifikishwa nyumbani kwa Joshua, hata wao waliamiani hajui alipo. Alishangaa mpaka uso ukaonekana ameshangaa. “Karibu nyumbani Naya.” Joshua akavunja kimya maana Nanaa na mumewe walibaki wakimtizama. Akaonekana kukosa raha kabisa. Joshua akamsogelea. “Unakumbuka tulichozungumza hospitalini?” Naya akamwangalia. “Nitakupa chumba chako wewe mwenyewe, hakuna mtu atakusumbua huko. Kwa hiyo usiogope.” “Na hapa pako salama Naya. Hakuna mtu atakuingilia au kukusumbua.” Nanaa akaongeza. Akatulia. “Twende nikakuonyeshe chumba chenyewe.” Akamsihi kwa tahadhari. Wakaongozana.

Alimkabidhi tu chumba cha chini. Kilikuwa na kila kitu humohumo ndani. Alichofanya Joshua nikumuhamishia baadhi ya vitu vyake humo ndani. Hakutaka kutoka tena. “Unataka tukawaage kina Magesa pamoja?” Akakataa. “Hamna shida, basi nitarudi.” Baada ya kutoka kuwasindikiza kina Magesa, Joshua aliporudi akakuta mlango umefungwa kabisa. Akajaribisha tena kufungua, lakini ukawa umefungwa kabisa na funguo kwa  ndani. Akaona asimsumbue amuache kama alivyomuahidi. Joshua akaondoka akizidi kusononeka moyoni.

 Akamuacha mpaka jioni, akaenda kumgongea. “Naya!” Akamsikia ametoka kitandani na kusogelea mpaka mlangoni lakini hakufungua. “Chakula kipo tayari. Twende ukale ili unywe dawa.” Kimya. “Naya!” Akamuita tena, lakini ikawa kimya. “Unataka nikuletee humu ndani?” Kimya. “Naomba unijibu Naya, tafadhali.” “Sitakula.” Akamsikia kwa sauti ya chini. “Unataka nini?” “Nilale. Sijisikii vizuri. Nataka tu kulala.” “Unatakiwa kunywa dawa. Lakini lazima ule kwanza.” Kimya.

“Naomba uniambie ni nini kinauma.” Akamsikia akianza kulia ndani. “Mimi nipo na wewe Naya. Naomba niruhusu nikuhudumie.” “Mimi sitaki kula. Nasikia kutapika na kichwa kimeanza kuuma.” “Hiyo hali wamesema itachukua muda kidogo, lakini wemesema itaisha. Pole sana. Nitarudi tena na juisi, tafadhali naomba nikirudi unifungulie ili nikupe na dawa.” Joshua akasubiri ajibiwe, lakini kimya. Akaondoka kwenda kufuata juisi aliyojua anaipenda sana na alikuwa akiomba apelekewe hata ofisini. Mpishi wa Joshua ndiye aliyekuwa kiitengeneza.

Aliporudi akakuta mlango upo wazi kabisa, akajua anaelewa vizuri tu. Akaingia nakumkuta bafuni akijaribu kutapika. Joshua akamsaidia na kutoka naye. Hakuwa amepewa dawa kali sababu ya madawa ya kulevya yaliyoluwa yamekutwa mwilini. “Naomba jaribu kunywa hiyo juisi, ni nzuri sana na ulikuwa ukiomba uletewe hata kazini. Jaribu.” Akajifuta machozi na uso vizuri akakaa sawa na kuipokea kutoka kwa Joshua. Akaanza kuinywa. Alipomuona anakunywa mfululizo, akajua ameipenda. Akaimaliza. “Nzuri. Asante.” “Karibu.” Akampa na dawa.

“Sasa kuna jinsi ambayo tulikuwa tukifanya unapoumwa na tumbo. Unataka nijaribu?” Naya akafikiria, akakataa kwa kutingisha kichwa. “Ila nataka kulala.” Joshua akajua ndio anatakiwa kutoka. “Sawa. Lakini naomba usifunge mlango ili nije kukuangalia baadaye bila kukugongea.” Hakujibu ila akapanda kitandani. Kimya. Akamfunika vizuri, akamuona anafunga macho. Akatoka.

Joshua alikuwa amenyongea  mno. Moyo ulikuwa ukimuuma akitamani kama Naya angemkumbuka. Akaamua arudi kwenye kuimba. Akafungua kinanda chake kikubwa, tena maridani kilichoonyesha ni cha mahela mengi. Akaanza kupiga taratibu huku akiimba
sauti ya chini lakini nzuri iliyokuwa imetulia. Akaimba sana mbele za Mungu wake mpaka machozi yakawa yakimtoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ø  Malon bado anamtaka Naya. Bale Majutoni kukubali hasira, wivu na haraka ya maendeleo kusababisha kumwaga damu ya ndugu zake, zaidi baba mzazi na mdogo wake asiye kuwa na hatia. Alikuwa akikubali kila kitu anachoambiwa na Malon, je safari hii akiwa amejua ukweli kwa asilimia kubwa sana, atamfanikishia Malon kumpata tena Naya kuepuka kurudi jela!?

Ø   Je kisasi kimeishia kwa Mbabe tu?

Ø  Akiwa mke hamkumbuki kabisa, Joshua machozini mbele ya Mungu anayeamini kumpa Naya, je, atakuja kupata happily, ever after? Kuishia kwenye furaha na mkewe?

Ø  Usikose muendelezo juu ya simulizi hii ya Mapenzi yaliyochanganywa na Pesa kujua mwisho wake.

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment