Akaendelea
kupiga kinanda chake kwa muda, akahisi mtu anamchungulia koridoni. Hakugeuka
kwa haraka, kwa kuwa alijua ni Naya. Akamuona kwa jicho la pembeni ni kama
anakaa kabisa chini, ila kwa kujificha akimchungulia. Joshua akaimba kwa muda
mrefu mpaka akamaliza. Akageuka, akamkuta ni yeye ila amekaa kwa mbali sana
kama asiyetaka amuone. Na yeye alipomuona Joshua amegeuka, akatambaa taratibu
kurudi chumbani kwake, Joshua akimwangalia.
Asubuhi
yake Joshua alifanya hivyohivyo. Asubuhi na mapema kama kawaida yake, kabla
hata hajaoga ndivyo alivyokuwa akifanya mara kwa mara. Akiamka tu, anapata nusu
saa ya kuimba, anamuabudu Mungu wake, kisha anaomba ndipo siku inaanza. Na
walinzi wake walijua mwenye nyumba wao ameamka kwa kuimba kwake. Akaanza tena
kuimba. Kwa sauti ya chini vilevile ili asimsumbue Naya kama amelala. Kwa kuwa
hakuwa akienda kazini na siku hiyo akaimba kwa muda mrefu sana, sauti nzuri ya
chini huku akipiga kinanda. Akahisi tena mtu kwa nyuma yake. Akajua ni Naya
tena ameamka. Akafanya kama jana yake. Akakaa kabisa chini akimsikiliza.
Akaimba Joshua kwa muda mrefu sana. Kuja kugeuka, akamuona amekaa amejiegemeza
ukutani kama aliyelala. Akaacha kinanda kikiendelea kupiga mziki wa taratibu.
Akamsogelea pale. Akawa kweli amelala. Akambemba kumrudisha chumbani.
Akamfunika na kumuacha hapo.
Akarudi
kama mida ya saa nne asubuhi. Akamkuta amekaa tu kitandani akiwaza.
“Upo tayari kwa kifungua kinywa?” Akakubali. “Unajua unaweza kutoka nje na
kuzunguka kidogo?” Kimya. “Ukijisikia vizuri. Utoke kabisa nje ukazunguke
kidogo. Na kuna sehemu nzuri tu za kukaa.” Naya hakujibu. Ila akajua
amemuelewa. Akapata kifungua kinywa akarudi kulala. Mchana ikawa hivyohivyo.
Kula na kurudi kulala ila akagundua anamwangalia sana kwa kujiiba.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mida ya
jioni, Joshua alipokuwa ofisini kwake hapohapo ndani nyumbani kwake, simu yake
ikaonyesha mtu ameshika mlango wa mbele. Akaangalia, akagundua ni Naya anataka
kutoka. Akamsaidia kutoa loki. Akabaki akimwangalia. Akatoka. Alionekana ni
kama aliyeoga vizuri tu, ila nywele vilevile kama ambazo hazijaguswa kwa muda
mrefu na tokea hospitalini alikataa kabisa kuguswa kichwa. Alikuwa akilia
maumivu wakati wote. Akajua hata hapo ameoga ila hajagusa kichwa. Akawa
akimfuatilia. Akamuona kweli amezunguka na kwenda kukaa nyuma kabisa ya nyumba.
Akatulia.
Alimpa
kama dakika 5 hivi, akamuona kwa kupitia simu yake amekaa vilevile anaangalia
sehemu moja tu bila hata kusogea. Akaamua amfuate. Akamkuta bado ameduaa tu.
Akaingiwa na hofu, ikawa ni kama vile alivyofanya baada ya kumzika baba yake.
“Naweza kukaa?” Naya akamgeukia. Akasogea pembeni kidogo kama anayempisha akae
pembeni yake. Joshua akakaa. Kimya kikapita kwa muda.
“Kwa hiyo
wewe ndio Joshua, mimi sio Joshua?” Joshua akatoa tabasamu kidogo. “Ndiyo.”
Akamuona anavuta pumzi kwa nguvu, akatulia. Akamgeukia tena baada ya muda na
kuuliza. “Ulisema tulikuwa tukiishi pamoja?” “Ndiyo, Naya. Wewe ni mke wangu
kabisa. Na hapa ni kwetu. Hukumbuki kabisa!?” Akatingisha kichwa kukataa na
machozi yakamtoka. “Sikumbuki kabisa. Najitahidi lakini sikumbuki!” “Usiwe
na wasiwasi. Huna haraka.” “Itakuaje nisipo kuja
kukumbuka tena?” “Labda nikueleze juu ya Naya niliyetambulishwa mimi na
Mungu. Nikampa muda wa kumfahamu na nikampenda zaidi. Labda na wewe itakusaidia
kukutoa wasiwasi na kujijua. Ni sawa?” Joshua akauliza kiustaarabu.
“Hata
mimi nilikuwa natamani kujijua mimi ni nani!” “Acha nianze kwa
kukuonyesha picha zetu.” Akamtolea simu yake akaanza kumuonyesha picha. Naya
akaonekana kushangaa sana. “Unauhakika huyu ni mimi kabisa!?” “Nakufahamu wewe
Naya, kwa mapigo ya moyo wangu. Ulipo popote, hata wakiwa wamekufunika, nitajua
upo hiyo sehemu.” Naya akashangaa sana kusikia hivyo mpaka akatoa macho kwenye
simu na kumtizama Joshua.
“Mungu
alikuleta kwenye maisha yangu akijua nakuhitaji sana. Ukaja na kuenea vizuri
mno.” “Hapa unaonekana unanipenda sana, hata kwa jinsi unavyoniangalia! Kila
picha ninayoangalia hapa, nakuona jinsi ulivyokuwa ukinitizama!” Joshua
akacheka na kurudisha macho kwenye simu yake. “Hizo ni picha zetu tulipokuwa
fungate. Tulikuwa na wakati mzuri mno. Sana. Unaona hivyo unavyocheka?”
Naya akabaki akijiangalia. “Ndivyo ilivyokuwa. Kulikuwa na hali ambayo, Naya!”
Naya akamtizama.
Joshua
akawa kama anayevuta kumbukumbu na tabasamu. “Sijawahi pata hiyo hali kwa muda
mrefu sana. Pengine tokea mdogo.” “Hali gani?” “Usalama wa moyo. Utulivu kwenye
hii dunia, na uhakika wa maisha kama hayo, mpaka kifo changu, kwa sababu wewe
Naya uliniahidi. Ukaniapia na ukasema ni mpaka kifo.” Naya akamtizama Joshua
kama ambaye hakumbuki kabisa, na kurudisha macho kwenye hizo picha. Akaendelea
kuangalia hizo picha. Na Joshua alihakikisha baba Naya hayupo kabisa kwenye
hizo picha. Alimuonyesha zile alizoziandaa maalumu kwa kuja kumuonyesha siku
moja, wakati akiwa ametulia kama hivyo.
Naya
akaangalia mpaka akamaliza, Joshua akimwangalia tu. Akamuona anarudia tena.
Akatulia. “Usiwe na haraka na wala sikutegemei ufanye au uwe chochote kile.
Nimekwambia kukusaidia tu. Ila nilitaka kukwambia juu ya Naya huyu
uliyemsahau.” Naya akamgeukia vizuri. “Kwanza ni mvumilivu. Ana upendo
mno kwa watu na anajali. Mchapakazi asiyejua kutegea. Mungu
alikujalia kipaji cha ajabu sana cha ubunifu. Katika moja ya vitu vyako
vilivyopo ndani, kuna kitabu maalumu. Ulikuwa ukichora wewe mwenyewe, mavazi
unayobuni. Ukachagua moja ya chumba humu ndani, tukakubaliana kuwa kitakuwa
chako cha mambo yako ya ubunifu. Zipo picha tulishauriana tuzitoe kabisa kwa
kuzi print na kuziweka ukutani. Kwa hiyo zipo kwenye hicho
chumba chako. Naya huyo uliyemsahau, alimpenda na kumchagua
Joshua. Akasimama naye kwenye kila hali na wakati. Huyo ndio Naya wangu,
kwa kifupi tu.” Naya alikuwa akimsikiliza kwa makini sana.
“Kwa hiyo
usiwahi kujitilia mashaka. Wewe ni zaidi ya hapo akili zako zinapogota. Zaidi
ya hivyo unavyojisikia sasa. Huo uvimbe ukiisha kabisa huko kwenye ubongo,
daktari amesema unaweza, kurudisha kumbukumbu. Lakini mimi nataka nikwambie
hivi, hata kama hutakumbuka kitu, sina wasiwasi na hilo. Naya ninayemjua mimi,
ni mkubwa mno. Anaweza kuanzisha chochote na kikawa.” “Unajuaje? Pengine
huo uwezo utakuwa umepotea kama kumbukumbu!” “Nisikilize na uniamini Naya. Upo
uwezo wa ajabu sana Mungu ameweka ndani ya kila mwanadamu. Kutawala mazingira
yake. Utashangaa sana. Unajiona hivyo ulivyo sasahivi?” Naya akajiangalia.
“Unaweza
kukatwa mikono yako yote, ukiwa mkubwa hivyohivyo. Itakuchukua muda mfupi sana
kuja kuweza kurudi kama kawaida. Ukaweza kula na kunywa kama wanadamu
wengine." Naya akakunja uso kama asiyesadiki. "Nayaongea haya kwa
kuona. Yupo binti au mwanamke ambaye hana mikono kabisa, lakini anaendesha
ndege na kuyafanya yote ya mikono kwa miguu.” Naya akashangaa sana.
“Mimi na
wewe hatuyafanyi hayo kwa kuwa tunayo mikono. Na wapo ambao wana mikono na
uwezo wa kuendesha hata baiskeli, lakini hawataki tu. Ninachotaka kukwambia ni
kuwa, mwanadamua anao uwezo mkubwa sana ila yeye tu hajajipa muda wa
kujichunguza na kutaka kutumia. Hata mimi najua kwa hakika, pengine sijafika
hata nusu ya uwezo ambao Mungu ameweka ndani yangu. Na sijapoteza kumbukumbu.
Nikiamua kutulia na kutafuta zaidi uwezo mwingine, nikawekeza muda wakutosha,
unaweza kushangaa nakuwa Joshua mwingine kabisa na huyu unaye muona
hapa, na nikawa pengine bora zaidi. Ila sioni sababu ya kufanya hivyo kwa sasa
kwa sababu hichi nilichonacho, Mungu amekiwekea mkono wake, na nimeamua
kumuonyesha ninastahili ili asione sifai akampa mwingine.” Naya akaonekana
kuanza kutulia.
“Ndio
maana nakwambia usiogope kabisa na wala usihangaike ukijitafuta kule
nyuma. Huyu Naya uliye naye sasa hivi, basi mtumie vilivyo. Mimi naamini Mungu
analo kusudi lake. Ukiwa tayari, na akiona unahitaji ya nyuma, basi jua
atayarudisha tu. Yaani jihesabu hivi, huyu Mungu, amekuumbia Naya mpya,
akakukabidhi, ni wewe tu kutafuta kumjua. Hilo moja. Uwezo Mungu aliouweka
ndani yake huyu Naya, msome. Wewe mwenyewe jifunze kuzitumia hizo karama ndani
yako. Yaani inakuwa kama umenunua tv, au simu au pengine kifaa kizuri ambacho
hujui jinsi ya kukitumia, ila aliyekuuzia, amekupa na kijitabu cha jinsi ya kutumia
hicho kifaa. Ndio ulivyopewa huyu Naya mpya. Usiwe na haraka. Jisome.
Jichunguze. Kile unachokipenda sana. Kifanyie mazoezi bila kuchoka. Jua
ndicho ulichowekewa ndani yako. Fanyia juhudi mpaka ukiwezee. Utaona maisha
yanaendelea bila shida.” “Wewe ni mwema Joshua! Asante. Nilikuwa nimejawa hofu
sijui chakufanya!” Joshua akacheka.
“Asante.
Utanifanya nitulie. Na nitaacha kutumia jina lako.” Joshua alicheka sana.
“Hutaki tena kuitwa Joshua?” Naya akapandisha mabega akikataa na tabasamu
usoni. “Basi turudi kwa Naya.” Akakubali akicheka kama anayetafakari. “Utakuwa
sawa Naya. Na sijui kwa nini, ila naamini utafanya makubwa na mazuri zaidi.”
“Asante.” Wakiwa kwenye ule wakati mtulivu, Nanaa na familia yake wakawa
wanaingia getini.
Joshua
akaangalia kwenye simu yake. “Nanaa na familia yake waliomba leo waje kula
chakula cha usiku pamoja na sisi. Niliwakubalia. Lakini kama bado hujisikii
kuwa karibu na watu wengi ambao bado huwakumbuki, basi unaweza kuendelea kuwa
hapa au ukarudi chumbani ukapumzike tu.” “Sawa.” Joshua hakuelewa hiyo sawa
inamaana gani! Kwamba amechagua kipi! Ila akaamua kumuacha tu. Akambusu begani,
upande ule aliokuwa amekaa karibu yake, akasimama. “Asante.” Naya akashukuru.
Joshua akacheka taratibu akitamani aulize ni ya nini! Ila akaona amuache tu.
“Acha nikawapokee.” Naya akageuka pembeni, akamwangalia kidogo kisha akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Joshua
akawapokea kina Magesa. Walikuwa familia nzima. Akawapa maendeleo ya Naya mpaka
hapo. “Ameanza kukubali jina lake na kuamini yeye si Joshua. Ametulia, ila bado
naomba tumchukulie taratibu. Naona lipo tumaini. Leo kwa mara ya kwanza ametoka
mpaka nje. Amezungumza na kuuliza maswali.” “Ulimuonyesha zile picha?” Geb
akauliza. “Ameangalia, tena kwa kurudia rudia, hajakumbuka kitu.” “Bado
hajamuulizia baba yake?” “Yaani ndicho namshukuru Mungu mpaka sasa, mama. Na
nilipomwambia sisi tuliona na wote ni yatima, hakuonekana kujali.” “Mungu naye
anasiri zake jamani!” “Acha mama. Lakini katika hilo namshukuru. Afadhali aje
akumbuke taratibu na ameridhia pia hata asipokumbuka ataanza upya.” “Bora.”
Wakaingia ndani. Mpishi wa Joshua alishapika na alishaandaa meza. Ila wakabaki
tu sebuleni.
“Tufanyie
mazoezi wimbo.” Magesa akaanza. “Kumekucha! Sasa unafanyia mazoezi mara
ngapi!?” “Nilikwambia bibi, anko mwenyewe alisema ukitaka kuwa mzuri kwenye
kitu lazima ukirudie tena na tena.” “Basi sasa sio umsumbue mwenzio.” “Kwani
eti Liv mimi nakusumbua?” “Ndiyo.” Liv akakubali kwa haraka. Magesa akapoa,
akamtizama baba yake akakuta akimwangalia. “Mimi siwezi kuimba mpaka Liv
ninayemuimbia anisikilize.” Akamlalamikia baba yake kama anayetaka amlazimishe
Liv. “Mimi nakusikiliza. Wewe imba. Halafu kesho kwenye birthday,
ndio atakusikiliza.” “Na mimi nakusikiliza baba mzazi. Imba mwanangu.” Nanaa
akaongeza kwa mumewe. Magesa akafurahi sana. “Na kwakuwa simsumbui na bibi, na
yeye atanisikiliza.” Wote wakacheka. “Anapenda kunipanga huyu! Hata haniulizi!”
Bibi yake akalalamika.
Joshua
akahamia upande wa kinanda chake, wote wakasogea. Akaanza kupiga wimbo wa
birthday. “Sasa nyinyi msiitikie mpaka niwape ishara.” “Magesa kupenda kuongoza
mambo wewe!” “Sitaki msahau bibi!” “Tunakumbuka sana. Kila saa onyo ni
hilohilo! We imba bwana.” Naya akaingia taratibu kama mwenye wasiwasi. Wote
wakageuka kumuangalia kule alipokuwa akiingilia.
Akawatizama
wote kwa zamu, akarudisha macho kwa Joshua. “Anti Naya! Kesho
birthday yangu mimi na Liv. Sisi tulizaliwa siku moja. Sasa
unakumbuka nilivyowaimbia kwenye harusi yenu?” Naya kimya akimwangalia huyo
mtoto anayeonekana kumfahamu ila yeye hamkumbuki. “Sasa kesho pia nitamuimbia
na Liv. Mimi mwenyewe. Halafu nikimaliza, nawapa ishara, ndipo na nyinyi
mnaimba. Ila nikiimba mimi, nyinyi msiniingilie.” Ilibidi kila mtu acheke.
“Kazi
ipo!” “Njoo unisikilize. Mimi mwimbaji mzuri sana. Ila Liv yeye hataki kuimba.
Anasema kichwa kitamuuma. Mimi kichwa huwa hakiniumi hata nikiimba sana.” Naya
akabaki kimya palepale sebuleni mbali na walipo. Akabaki amesimama. Joshua
akasimama na kumfuata. “Unataka kukaa hapa, au unajisikia kwenda kupumzika
chumbani?” “Nitakaa kidogo ndipo nikalale.” “Njoo usalimie.
Nitakutambulisha kwao.” “Nimemkumbuka yule mama. Si ndiye aliyekuwa akija
hospitalini?” “Sawasawa. Sasa Nanaa na Geb ndio watoto wake, hao ni wajukuu.”
Joshua akawa akiwaonyeshea maana Naya alionekana kama asiyetaka kwenda kule
walikokuwa wamekaa wote.
“Anti
Naya, na mimi ni rafiki yako. Unanipenda sana kuliko wote!” Wakacheka kule
walikokuwa. “Magesa kwa kupenda kupendwa yeye! Sasa aliyekwambia anti anakupenda
wewe zaidi ni nani?” “Mimi najua. Alikuwa akiimba na mimi huku akinifundisha
jinsi ya kutawala pumzi zangu wakati wa kuimba, halafu ananipigia simu kila
siku na kuniambia nimsimulie mambo ya shule. Au umesahau anti!?” “Bwana wee!
Acha kumchosha anti kwa maswali. Wewe anza kuimba.” Bibi yake akataka amuache
Naya. Joshua akamgeukia Naya akijua ameshakataa kwenda kujumuika nao kule
walipokaa.
“Basi kaa
hapa.” Akakaa taratibu. Joshua akaondoka. Akaona bado wakimwangalia. Akainama
kwa muda kisha wakamuona ananyanyuka. Akaenda chumbani. Nanaa akamfauta.
“Nimekuletea vitu vyakuoshea nywele. Tujaribu kuosha leo ili angalau zikae
sawa. Au bado kichwa kinauma sana?” Nanaa aliingia na kumwambia hivyo moja kwa
moja. “Hakiumi sana. Ila wewe ni mtu mzuri. Umenisaidia sana tokea
hospitalini.” Nanaa akacheka akimuhurumia. “Pole Naya. Ni vile hukumbuki.
Lakini sisi ni marafiki sana.” “Sikumbuki kabisa!” “Usijali. Sisi wote
tunakupenda Naya. Na tupo kwa ajili yako. Hata leo tumekuja kwa chakula cha
usiku hapa ili tuwe na wewe. Twende tukaoshe nywele, halafu ukamsalimie mama.”
Akakubali.
Akamsaidia
kuosha hizo nywele ambazo hazikuwa hazijaoshwa zaidi hata ya mwezi. Zilikuwa
zikinuka maana huyo Naya alishalazwa chooni na Malon. Na kwa kuwa zilikuwa
zimesukwa chini, Nanaa alitumia muda mrefu sana kuziosha mpaka kutakata na
kuzichana bila kumuumiza sana. “Najisikia vizuri. Acha nioge tena.” Akampisha
hapo bafuni. Akaoga, akabadili, Nanaa akimsubiria tu. Akamchana tena vizuri.
“Vaa na hereni, Naya. Nataka upendeze, utoe hali ya ugonjwa. Hata mumeo
akikuona, afurahie.” “Simkumbuki kabisa!” Naya akalalamika na kuongeza. “Ila
anaonekana mtu mzuri sana, na yeye mwenyewe mzuri kweli! Halafu msafi!”
Nanaa alicheka mpaka akakaa.
“Usicheke
kwa sauti, Nanaa!” “Basi na yeye huwa anakusifia hivyohivyo!” “Kwani eti
tulikuwa na mahusiano ya aina gani?” “Mazuri sana. Natamani ukumbuke kidogo.
Joshua anakupenda kupita nitakavyokwambia.” “Nimemuona! Ila sijui nifanyeje!”
“Taratibu tu. Usiwe na haraka. Fungua moyo. Jipe muda. Kwa kuwa anakupenda kwa
hakika, utakuja tu kujisikia upendo.” Naya akacheka kidogo na kunyamaza. Nanaa
akamuona. “Ushaanza kumpenda nini!?” “Sijui!” Nanaa akazidi kucheka vile Naya
alivyojibu kwa aibu kidogo akicheka kwa kujificha.
“Na mimi
nataka kucheka na wewe, mama.” Magesa akaingia bila hodi. “Magesa mwanangu
wewe! Umeshaimba sasa?” “Nimemwambia anko siwezi kuimba mpaka mama
yangu awepo, anisikilize.” “Jamani Magesa!” “Kwani wewe umechoka kunisifia
tena?” Mpaka Naya akacheka. “Sijachoka mwanangu. Twende baba, ukaimbe.” “Na
anti naye atakuwepo?” “Anakuja.” “Ila ujue anti sasa hivi umependeza sana.”
Nanaa akazidi kucheka. “Magesa kwa kupenda vitu vizuri wewe mwanangu! Macho
yako yanavutwa na vizuri tu!” Akacheka Magesa. “Twende sasa ukamsalimie vizuri mama
yetu. Tunae mama mmoja tu hapa mjini.” Wakatoka na Naya wa tofauti na
alivyoingia hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mrembo
wa Joshua huyo!” Naya akacheka na kujifunika uso. Maana mama G alimuwahi tu
alipowasogelea. Naya akamwangalia Joshua na kumsogelea mama G akicheka kwa
aibu. “Mimi nilijua mimi ndio Joshua!” Walianza kucheka hapo mpaka machozi.
“Msinicheke.” Naya akalalamika akicheka taratibu. “Mimi naomba hili swala
tulizungumze vizuri.” Akaanza Nanaa. “Nanaa akanipigia simu, ananiambia tupo na
Naya, lakini sasa hivi haitwi tena Naya, anaitwa Joshua.” Wakazidi kucheka,
Naya akajifunika na mto.
“Sasa
mimi namjua Nanaa yupo kama mwanae Magesa. Nikasema acha mimi nije, nijionee
mwenyewe.” Mama G akaendelea. “Sasa Mungu naye alivyo, nafika pale nakutana na
daktari wa akili. Anakuuliza unaitwa nani, nasikia Joshua!” Watu wakazidi
kucheka. “Nikasema mwanangu Joshua kweli kapendwa! Mke kaamua achukue
mpaka jina lake kabisa!” Naya akazidi kucheka huku amejifunika mto usoni. Ila
Joshua alijisikia vizuri sana.
“Kila ukiambiwa
wewe ni Naya, mwanangu unalia, unataka uitwe Joshua!” “Mimi sijui bwana! Ndio
neno hilo tu lilikuwa limebaki kichwani kwangu.” “Kwa hiyo mpaka sasa hivi
hukumbuki?” “Ni vile Joshua amenieleza kwa kituo na kunionyesha picha, ndio
nimeamini. Lakini nilikuwa naogopa kukubali halafu nipoteze kitu kimoja tu
ambacho nina uhakika nacho!” “Basi Naya mama. Wewe usiwe na haraka. Pengine
Mungu ameona hataki ukumbuke ya nyuma. Anataka akupumzishe. Usijisumbue na ya
nyuma, wewe songa mbele.” “Ila mimi bado sijaimba, nilikuwa namsubiria mama
yangu.” “Haya baba. Imba. Na umekuwa mvumilivu kweli!” “Si hata wewe bibi
umeona eeh!” “Nimeona baba. Tena sasa hivi ndio nina hamu kweli ya
kukusikiliza.” Magesa akafurahia.
Akaanza
kuimba, akimuimbia dada yake. Akaimba tena mara mbili ndipo akawapa ishara
wampokee. Wakaimba hapo mpaka mwenyewe akaridhika. “Umeimba vizuri sana
Magesa. I am so proud of you, son!” Magesa akafurahi san. “Asante
dad.” “Mwanangu muimbaji huyo!” “Mpaka unajivunia mimi, mama?” “Kabisa baba
mzazi.” “Asante mami wangu. Na asante bibi kwa kunipigia vigelegele. Na anko
kwa kunipigia kinanda na makofi. Wewe anti hukupenda?” Akamgeukia Naya. Akawa
kama amemtoa kwenye mawazo. “Nimependa sana. Umeimba vizuri.” Akacheka kwa
furaha.
Joshua
akamuona amebadilika kidogo. Akasimama nakumuita pembeni. “Niambie
unachojisikia.” “Kichwa kinaanza kuuma.” “Pole.” Akaweka mkono wake kwenye hiyo
shingo ndefu ya Naya. Akamshika vizuri na kumsogelea karibu. “Upande upi unauma
zaidi?” Akamuonyesha. Joshua akamshika na kumsugua kidogo kisha akambusu hapo.
“Pole sana.” “Asante.” Akamkumbatia vizuri, taratibu kwa tahadhari. “Umependeza
sana Naya!” Akamnong’onoza sikioni. Akamsikia akicheka taratibu. “Nywele
zinanukia vizuri!” “Nanaa ameziosha. Ni sawa nikienda kupumzika?” “Hutataka
kula na kina Magesa?” Akanyamaza.
“Wamekuja
hapa kwa ajili yako. Naweza kuwaambia tule sasa hivi ili ukapumzike. Au
umechoka sana?” “Kwani muda wa dawa bado?” Joshua akaangalia saa. “Bado Naya.
Pole. Naomba ujikaze tena kidogo.” Akakubali. Wakarudi akiwa amemshika vizuri.
“Naya anataka akapumzike, lakini nimemuomba tule pamoja. Tupate muda wa
kumshukuru Mungu pamoja.” “Ndio wote sasa tusimame na twendeni mezani moja kwa
moja, tule ili akalale.” Akasisitiza mama G. Wakahamia mezani.
Wakala
kwa pamoja, Joshua akamletea dawa palepale mezani alipokuwa ametulia kabisa,
akila taratibu macho kwenye sahani yake tu kama hayupo pale. “Muda umefika?”
Akamuuliza taratibu. “Ndiyo. Kunywa kitatulia.” Akameza na kutulia tu palepale
mezani. Na kina Magesa wakaona huo ndio wakati wakuaga ili wamuache akapumzike.
Wakaondoka.
Joshua & Naya.
Wakabakia
wao wawili. “Twende nikusindikize chumbani.” Wakaongozana. “Ni sawa
nikikusubiri mpaka ulale?” Joshua akauliza kwa tahadhari lakini akionyesha
kujali. “Wewe ni mtu mzuri Joshua! Upo mwema.” Joshua akacheka taratibu
akimuangalia. “Naomba tu ukampumzike. Kwa kuwa umenipa dawa, naamini nitalala
tu.” “Nikwambie ukweli Naya?” Akatingisha kichwa kukubali.
“Bora
vile ulivyokuwa hospitalini, kuliko hapa!” Naya akawa hajaelewa. “Unalala
kitandani nikikuona. Lakini hapa nakuwa kule juu chumbani kwetu, wewe
uko huku kwenye vyumba vya ziada! Nakuwa sijui umelalaje! Sijui unaendeleaje!
Nakuwa na wasiwasi, siwezi kulala mke wangu. Nakuwa nina kazi ya kukufuata tu
huku kukuchungulia kujua kwanza kama bado upo hapa, hujaondoka tena. Na pia
kama upo mzima!” “Pole Joshua. Na samahani.” “Huna haja yakuomba msamaha. Ila
tafadhali niruhusu hata nilale kwenye hilo kochi. Angalau usiku wa leo na mimi
nilale nikiwa najua nipo karibu nawewe.” Ikamgusa sana Naya.
“Sawa.”
Akakubali. “Basi acha nikasafishe kinywa kabisa na nakuvaa nguo za kulalia
halafu nakuja. Nikirudi umelala, sitakusumbua.” “Nitakusubiri.” Joshua
akafurahia hilo. Akatoka hapo kama akimbie. Akakimbilia bafuni, akasafisha
kinywa haraka. Akaona aoge kabisa. Akayafanya hayo kwa haraka, akarudi
alipomuacha Naya. Akamkuta ameshapanda kitandani amejifunika. Akaenda kukaa
pembeni ya kitanda na kumshika kichwani akimpapasa taratibu.
“Kinatulia?”
Akamuuliza akimbembeleza. “Natamani dawa zaidi.” “Unajua hatuwezi Naya. Pole.”
“Hivi walisema ni kwa nini?” “Ila naomba usiogope.” Joshua akamtahadharisha.
“Ni nini?” “Walikuta madawa ya kulevya kwenye damu yako. Niliwaomba
wakusafishe. Nikawahakikishia wewe si mtumiaji. Hata pombe hujawahi kutia mdomoni.
Kwa hiyo nikawahakikishia hutarudia tena. Ndio wakakubali na hilo sharti kuwa
hata madawa ya kupunguza maumivu, hayawezi kuwa makali na lazima iwe kwa masaa
maalumu.” “Ni nini kilitokea kwangu!?” “Hakuna anayejua mpenzi wangu. Hakuna.
Nilitegemea ungekuja kuniambia ni nini kilitokea. Maana..” Joshua akamsimulia
ilivyotokea mpaka mwenyewe machozi yalikuwa yakimtoka.
“Pole
Joshua. Pole sana.” Joshua akaingia chooni. Akasafisha uso ndipo akatoka
akionekana ametulia, akamkuta Naya akimsubiria. “Lala tu. Mimi nitakuwa hapa.”
Naya akajilaza vizuri kitandani, wakati akijifunika Joshua akasogea kumsaidia.
Kisha akakaa pembeni yake akimtizama. “Usilale kwenye kochi, Joshua.” “Unataka
nirudi chumbani kwangu!?” Akajaribisha kwa swali. “Hapana, tunaweza kulala hapa.
Hiki kitanda ni kikubwa sana, tutatoshea kabisa. Njoo.” Joshua akahisi anapewa
ulimwengu. Akajipandisha kwa haraka , kama anayeogopa asibadili mawazo.
Ila akawa
naye makini asianzishe jambo maana bado hakuwa ameusoma moyo wake kujua alipo.
Akajiweka pembeni, ila akiwa anamfunika zaidi yeye. Wakatulia. Baada ya muda
akamuhisi yeye mwenyewe anamsogolea. Akatulia tu kuona anachotaka kufanya.
Akajisogeza karibu kabisa ndipo akamuwekea mkono kwa juu kama anayemkumbatia.
Wakatulia kidogo.
“Joshua!”
Akamsikia akimuita taratibu. Akamkumbatia zaidi. “Sijui tulikuwa tukiishije
mpaka nikaondoka mara ya kwanza. Au sijui nini kilitokea, ila kwa jinsi ulivyo
sasa, naona ni afadhali kuwa na wewe.” Ikamgusa sana Joshua. “Wewe ni mtu mzuri
Joshua, ningetamani niwe na wewe tu, nibaki kwako. Nisiondoke.” “Ndivyo
ilivyokuwa tokea mwanzo Naya. Tulikuwa na utulivu wa aina yake, na ukaniapia
kubaki na mimi mpaka kifo. Hatukuwa na tatizo! Na siku nimepokea ujumbe wako
kuwa umeamua kuondoka, tuliachana vizuri tena ukiwa umeniahidi usiku mzuri
sana. Tuliagana kwa penzi fupi lakini lilikuwa zuri.” Akamsikia Naya akicheka,
na kujificha.
“Kweli
Naya. Tulikuwa tukifanya mapenzi hapa, bila kutosheka. Kila mahali kwenye hii
nyumba kasoro tu hivi vyumba vya huku. Ulikuwa muda mfupi tulioishi hapa
pamoja, lakini ulikuwa wakati mzuri sana uliotutoa wote majonzi na simanzi.
Tukaomba Mungu pamoja kuwa hii itakuwa nyumba ya faraja. Eti baada ya muda
mfupi napata ujumbe kutoka kwenye simu yako kuwa unaniacha! Nilimkatalia
kila mtu. Japokuwa kule polisi walikuwa wakiniona nimepaniki tu sababu ya
kuachwa, na kushindwa kunipa msaada, lakini Naya, sikuacha kukutafuta na
kukufanyia uchunguzi bila kuchoka. Sema tu kuna mambo fulanifulani ya msingi
nayo yalikuwa yakinikwamisha. Halafu sasa, kukawa hakuna hata funununu au
dalili ya wapi upo.” Joshua akaendelea.
“Nilikufuata
mpaka Mbeya kwenye sehemu nilizohisi pengine unaweza kuwepo. Nikisindikizwa na
Geb. Lakini wakaniambia hawajawahi kukuona huko. Nikawa kama nimegonga mwamba.
Lakini nikabaki kumuomba Mungu yeye aonaye sirini. Nilikuwa nikifanya mikesha
hapa! Ijumaa kuamkia jumamosi nilikuwa nikikesha nikiomba mpaka saa sita usiku
na kunilazimu kulala kwa sababu ya kazi asubuhi. Ila jumamosi kuamkia asubuhi
ya jumapili, nilikuwa nikikesha nikimuita Mungu ambaye hakuwahi
kunipokonya vitu anipavyo. Wakati mwingine familia ya kina Magesa
walikuwa wakija kuomba na mimi. Mkesha kabisa, tukiimba na kumsihi Mungu
anitendee muujiza.” “Jamani Joshua! Pole.” Naya akajisogeza kwa karibu zaidi
tena safari hii akamsogelea mpaka usoni.
Akaweka
mkono kifuani akaanza kumpapasa nywele za kifua taratibu. “Umesema sina ndugu?
Pengine alijua nilipo.” “Ndipo huko uliashiria unakwenda. Ila pia huyo ndugu
yako sikuwa nikijua jinsi ya kumpata. Kwanza ni kama alipotea, tukawa tukimtafuta
wote na wewe pia hata kabla hujapotea. Kingine hakuwahi kunipenda
kabisa.” “Simkumbuki. Sina kumbukumbu naye kabisa! Kwa nini hakuwa akikupenda?”
“Yeye aliona sikustahili. Ni kwa kukupenda tu na kukutakia mema. Alitamani
uolewe na mwanaume mwingine sio mimi.” Naya akabaki akifikiria.
“Kwa hiyo
hajawahi kupatikanika mpaka sasa?” Joshua akafikiria kidogo akisita, lakini
akaamua kumwambia. “Sijui kumbukumbu zako zinakurudisha mpaka wapi!” Naya
akabaki kimya akifikiria. “Unakumbuka kufika ofisini kwa kina Magesa, ukatakiwa
useme jina lako kamili?” Naya akabaki akifikiria. “Ulikuwa ukiumwa sana sijui
kama utakuwa ukikumbuka! Ila kwenye hicho chumba kulikuwa na wanaume watatu na
wewe wa nne.” “Mume wa Nanaa alikuwepo?” Naya akauliza kama anayeanza kujiwa na
kumbukumbu.
“Ndiyo.”
“Kuna mtu mwingine alikuwa mkali, akaanza kunipiga akisema mimi sio Joshua!
Akawa akinipiga akinielewesha jina langu ila sio kama vile wewe ulivyonielekeza
kwa utaratibu mpaka nikakubali japo bado mimi naamini ndilo jina langu!” Joshua
akacheka kidogo akijaribu kumpoteza ili asimkumbuke Bale kwa jinsi ile. Joshua
mwenyewe siku ile ni kama alikuwa tu kwenye kile chumba cha mkutano na kina
Mungai, Geb, Naya na Bale. Kwani muda wote ule alikuwa akisikiliza kila kitu
kinachoendelea pale kwenye kile chumba cha mkutano kwa kupitia simu ya
Geb. Geb alimpigia simu Joshua na kumuweka kwenye mute.
Geb alitegesha simu yake vizuri ili Joshua aweze kusikia chumba cha jirani kwa
kuweka simu yake mezani.
“Mmoja
alikuwa akiongea mara chache. Ila yule tuliyekuwa tumekaa naye karibu alikuwa
mkali! Tena nakumbuka alinipiga makofi wakati nilimwambia kichwa kinaniuma.
Nakumbuka japo si vizuri. Kichwa kilikuwa kikiuma sana nashindwa hata
kuangalia! Alikuwa nani yule! Mkali!” “Anaitwa Bale.” Naya akatulia. “Umemkumbuka?”
“Hapana.” Naya akawa hakumbuki ila akaingiwa hofu. “Akija kunichukua tena?”
“Hawezi kwa kuwa nimemdhibiti kisheria na nimemwambia kuwa nilikukuta na yeye
ukiwa na hali mbaya, kwa hiyo haruhusiwi tena kuwa na wewe mkiwa peke yenu
mpaka mimi niwepo.” Mawazo ya Naya yakawa yamechanganyika tayari, hofu imemjaa
hajui aulize nini, aache nini.
“Sasa kwa
nini alikuwa akinipiga!? Kwa sababu nakumbuka hakuwa ameanzia hapo.” Naya akawa
kama anavuta kumbukumbu. “Alinichukua sehemu. Mbali. Tukasafiri kwa muda mrefu
tu. Nikawa nikimwambia nina maumivu, lakini akawa hajali. Akaenda kunifungia au
kuniacha sehemu ingine. Akawa ananifundisha kitu nikawa sielewi. Akawa
ananipiga. Ila nikamwambia ni kwa sababu kichwa kinauma. Akaendelea kunipiga
tu. Kwani alikuwa akitaka nini!?” “Kwanza naomba usilie.
Tulia ndipo tuzungumze na usiogope Naya. Sasa hivi hakuna atakayekuchukua tena.
Niambie kama unakumbuka popote ulipokuwa. Hata mazingira tu. Na hata kama si
kwa hakika, hata tu kidogo pengine nitajua ulikuwa wapi au kwa nini ulipotea.”
Naya akajaribu kukumbuka lakini akashindwa.
“Sikumbuki
Joshua! Sijui nilikuwa wapi mpaka pale hospitalini tena kwa sababu ulikuwa
ukiniambia kila wakati kitu gani wanataka kunifanyia kabla wauguzi wenyewe
hawajazungumza na mimi kunihudumia. Hapo ndipo nikajua nipo hospitalini.” “Sura
je? Mbali na yule unayemkumbuka mliyekuwa naye siku ile, yupo mtu mwingine
unamkumbuka kumuona?” Naya akajaribu kufikiria.
“Kuna
mtu.” Naya akawa kama anayekumbuka. “Niambie zaidi.” Naya akakaa kabisa. “Ni
kama ndiko alikonitoa huyu wa pili.” “Anaitwa Bale.” “Huyu aliyenipiga?”
“Ndiyo.” “Basi Bale ndiye aliyenitoa kwa huyo mtu mwingine.” Naya akatulia.
“Unaweza kunieleza zaidi jinsi alivyo?” Akaendelea kumdodosa zaidi. “Ni kama na
yeye hakutaka huyo Bale anichukue, nafikiri. Wakawa kama wanabishana.”
“Wanabishana nini?” Naya akakunja uso akionekana anajaribu kukumbuka kwa juhudi
zote. “Huyu Bale ndio alikuja kunichukua, nafikiri. Sasa huyu mwingine akawa
anakataa kama asinichukue. Naye alikuwa na hasira na mimi. Ila sikumbuki
alikuwa akiniambia nini! Ila uso wake ulijawa hasira! Akawa na yeye
akinielekeza au kuniambia kitu kwa ukali lakini sikuwa nikisikia vizuri au
kuelewa. Ndio akaja sasa huyo Bale kunichukua hapo, akawa kama
anakataa lakini sikujua ni kwa nini kwa kuwa sikuwa nikisikia au kuelewa.
Nilikuwa naumwa Joshua!” “Pole. Pole sana. Lakini naomba jitahidi kunielekeza
huyo mwingine Naya. Tafadhali mpenzi wangu. Itanisaidia kujua nakukinga
dhidi ya nani.” Naya akamuelekeza taratibu mpaka akajua kama ni
Malon.
Joshua
akaumia sana kuona Bale na Malon wapo pamoja. Kwamba kwa kumchukia yeye ndio
Bale amekwenda umbali wote huo! Akaona anyamaze tu hata asimwambie kama ni kaka
yake mpaka yatokee mazingira mazuri. “Njoo ulale ili kichwa kisianze kuuma na
kushindwa kunywa dawa, maana muda bado.” Naya akarudi kujilaza.
Akatulia
kidogo akamuita. “Joshua!” “Nipo macho bado. Nilikuwa nikiwaza.” “Umeshajua
jinsi ya kunilinda lakini? Ili wasinichukue tena.” “Ndiyo Naya. Hutatoka peke
yako tena kwa muda mpaka upone kabisa wakati huo nikitafuta jinsi ya
kuwadhibiti waliokuchua.” “Umeshawajua?” “Ndiyo. Mmoja anaitwa Bale na mwingine
Malon. Popote utakapowaona uniambie.” “Sawa.” Naya akakubali.
“Na
wakikwambia uende nao popote kule, usikubali.” “Nitakwambia pia. Ila usikubali
ikatokea nakutana nao tena. Sawa Joshua?” “Nitajitahidi na hata
ikitokea wanakusogelea, nitahakikisha hakuna wakukuumiza tena, sawa?” “Sawa.”
Naya akaridhika.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walilala
usiku huo Joshua akimbembeleza kwa kuwa kichwa kilikuwa bado kikimuuma ila sio
sana. Akalala akikumbatiwa na kubembelezwa. Asubuhi aliamka mapema tu ndio
ilikuwa siku ya birthday ya watoto wawili wa Nanaa. Walizungumza wao wawili
Nanaa na Joshua, hawakumwambia Naya. Nanaa akafika hapo asubuhi kumchukua,
aliwakuta wakipata kifungua kinywa.
“Nimekuja
kukuchukua Naya. Twende wote nyumbani. Tukaandae sherehe ya watoto. Itakusaidia
kuchangamka.” Naya akamwangalia Joshua kwa wasiwasi. “Utakuwa sawa, usiogope.”
“Tunakwenda wote!?” Naya akamuuliza kwa wasiwasi kama ambaye hataki. “Nakwenda
kazini kwa masaa machache kisha nitakuja na mimi.” “Kwa hiyo sasa hivi
tunakwenda bila wewe!?” Nanaa akajua kazi itakuwepo, akavuta kiti akakaa karibu
yake. Akaanza kumueleza uzuri wakutoka hapo na kuweka akili kwenye shughuli
mbalimbali. “Lakini sio na Joshua?” Akawa kama bado hajaridhika. “Joshua
atakuja baada ya kutoka kazini.” Naya akatulia kidogo na wasiwasi mwingi usoni.
Joshua akamuhurumia.
“Naomba
nikazungumze naye. Nitarudi Nanaa. Twende Naya.” Akamshika mkono kumsaidia
kusimama. “Umesema hatuendi wote?!” “Mimi nitakuja, na sitakawia.”
“Uliniambia utahakikisha wale watu hawanisogelei Joshua! Wakinifuata
wewe haupo, si watanichukua tena? Naona mimi nibaki tu hapa ndani
wakati wewe ukienda kazini. Nisitoke. Tafadhali Joshua. Sitaki kuumwa tena.” “Naomba
usilie. Nanaa anawafahamu na anakupenda. Atakulinda. Kwa sasa sitamuamini
yeyote yule na wewe isipokuwa Nanaa, Geb na mama G. Ni hao tu kwa sasa. Ukiwa
nao hao sitakuwa na hofu kwa kuwa najua utakuwa salama. Na ninakuahidi
sitachelewa. Nitakuja hukohuko ili tuwe wote. Nahitajika sana kazini ndio maana
inanilazimu niende, na mama naye ameomba upelekwe, ili utoke ukawe na wenzio,
ukawasaidie kupanga mambo. Itakusaidia.” Ikabidi Naya akubali.
Nanaa
akaenda kumsaidia kuchukua nguo aliyojua atavaa baadaye kwenye shuguli
akambebea vitu baadhi, wakawa wanatoka. “Joshua amesema hatachelewa.” Akawa
anaongea kama anayejifariji. “Utakuwa sawa Naya. Usiogope.” “Hata Joshua
ameniambia hivyohivyo.” Akageuka, akakuta Joshua akiwasindikiza kwa macho na
yeye kama asiyekuwa ameridhia tena. “Si unakwenda kazini, halafu utakuja na
wewe?” Akawa kama anayetaka uhakika tena akionyesha wasiwasi mkubwa. “Nitakuja
Naya, na sitachelewa. Nenda ukafurahie na Nanaa pamoja na wengine.” Wakatoka.
Njiani Nanaa akamuona ametulia sana. Amejawa wasiwasi. Kila alipomuongelesha
akawa kama haelewi tena au hasikii. Akaona amuache tu na waende hivyohivyo
kwani walikusudia kumtoa ndani.
Kwa Kina Magesa.
Walifika
nyumbani wakawakuta mpaka Grace na wanae wote wameshafika hapo na watoto wake.
Kukawa na shamra shamra hapo, Naya amepoa akiangalia tu. Akakataa kula kitu
chochote hata maji, akabaki kimya tu. Nanaa akamfundisha kufunga zawadi
akaelewa. Akaanza kufunga ila hazungumzi na akili kama hazipo hapo. Baada ya
muda akamuita Nanaa. “Joshua alisema atakuja. Alimaanisha hapa au nirudi kule
nikamsubirie? Asije kurudi kule akanikosa.” “Joshua atakuja hapa Naya. Naomba
uwe na amani. Hapa hakuna mtu atakuja kuingia na kukuchukua. Umesikia?” Nanaa
akajaribu kumtuliza. Akaonekana kama hajaridhika. “Au nimpigie simu uzungumze
naye?” “Hapana, amesema yupo na kazi.” Akajirudi na kutulia kabisa.
Mambo
yakaendelea yeye akiwa ametulia. Hata walipomteta hakuwa hata akielewa. Kila
aliyeingia mlangoni na kutoka, alidhani ni Joshua. Macho yakawa mlangoni wakati
wote. Wakahamia kuweka sawa nje sehemu ya maua ambapo watu watakutania kwa
shuguli hiyo nzima ya birthday ya watoto hao wawili wa Magesa. Mama G akampa
kazi kumfanya asifikirie zaidi ila kazi aliyokuwa akifanya.
Atafutaye Hachoki.
Naya
akajikuta amebaki yeye peke yake hapo nje na watoto wakicheza. Akakaa tu
akiangalia watoto lakini akili kwa Joshua akiangalia getini. Mlinzi
akamsogelea. “Unaitwa na mume wako hapo nje.” Naya kwa haraka
akasimama kama akimbie. Kutoka hakumuona Joshua. Akasogea mbele zaidi
kumtafuta. Akamuona Malon. Naya akashituka sana, maana alimkumbuka kuwa ndiye
aliyekuwa naye kabla ya Bale kumchukua. Akakumbuka alikuwa akimzungumzisha kwa
hasira. Akaanza kurudi nyuma taratibu akitetemeka. “Nitakuumiza Naya, njoo.”
Naya akataka kama ageuke, akimbie. Malon akamgundua na kumuwahi kumtisha.
“Ukisogea hata hatua moja nyuma nakuhakikishia nitakuumiza, Naya.” Naya
akasimama akitetemeka, akaanza kulia.
Naya huyu
amekuwa kama asiye na akili nzuri. “Unanielewa?” Naya akatingisha kichwa
kukubali akilia. “Haya njoo.” Naya akajifunika uso akaanza kulia palepale aliposimama
bila kuweza hata kusogea. Malon akamsogelea akamshika mkono kwa nguvu akaanza
kumvuta akirudi naye garini kwake.
0 Comments:
Post a Comment