Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com SOULMATE. - Naomi Simulizi

SOULMATE.

  
 

Hadithi hii ni kazi ya utunzi tu. Majina, sehemu na matukio yote yaliyotumika kwenye hadithi hii ni mawazo ya mtunzi wa hadithi hii.  Tutangulie kuomba radhi kwa jina au mahali husika, litakalokugusa moja kwa moja.

Hadithi hii imeanza kuandikwa kuanzia 11/24/2015 - 5/27/2016

Hakimiliki ©2018 Naomi Mwakanyamale Ngimba.

ISBN: 978-9976-5447-01

E-mail: naomisimulizi@gmail.com

Blog: naomisimulizi.com


Haki zote zimehifadhiwa, hakuna sehemu ya kitabu hiki au machapisho haya inayoweza kuchapishwa kwa mara ya pili au kuhamishwa au kusambazwa katika namna tofauti bila idhini ya mchapishaji ambaye ni 

Naomi Ng’imba Mwakanyamale.


DEDICATION

For the wonderful memory of my  loving father.

Abel Edson Mwakanyamale

Born 01/01 1928

Died 03/10/2017

Baba!

Milele tutakukumbuka.

Though you are no longer with us, but your Smile, Love, Thought and Wisdom will live with us forever.

Amen!


Katika kipindi hichi kigumu katika maisha yangu, nikiwa kwenye uchungu mkubwa wakuondokea na baba yetu. Mwanaume aliyetupenda na kututhamini kuliko mtu ambavyo angeweza kueleza. Alitoa vyote kutupa sisi. Nikiwa kwenye majonzi mazito nikimlilia Mungu na kumuuliza ni kwa nini, ndipo Roho wa Mungu aliponiwezesha huhamisha akili zangu na kuweza kuandika hadithi hii na nyingine nyingi kama  Endless Love, My Past!, Pacha Wangu!, Ni Wangu!, Nilipotea!, Zaidi Ya Kutamka, Mapenzi & Napesa!.


Utukufu na heshima ni kwake yeye awezaye kutenda zaidi ya tuombavyo na tufikiriavyo.

    

Sehemu ya 1.

                     

K

enny alishindwa kabisa kutulia. Alijawa furaha kama fukara aliyeokota mkoba wa mamilioni ya pesa za kimarekani. “Anaitwa Naih.”  Kenny alijibu. “Unajua maana yake?” Alimuuliza baba yake huku akionyesha uso wa furaha, akitaka yeye ndio asikilizwe akitoa maana ya jina la mtoto huyo wa kike, aliyekuwa na siku kumi tu tokea kuzaliwa kwake. “Hapana. Kwani ina maana gani?” Mzee Olendekai, baba yake Kenny alikuwa akijua maana, kwani lilikuwa ni jina lenye asili ya nyumbani kwao, masaini. Alitaka tu Kenny ajibu. “Kubembelezwa!” Kenny alijibu huku macho yake yakiwa bado kwa mtoto huyo mchanga.

“Kwa hiyo Naih maana yake ni Kubembelezwa?” “Yes dad.” Kenny alijibu kwa kujiamini mbele ya wazazi wake. “Naona tokea ajue maana ya hilo jina, amegoma hata kurudi nyumbani! Kuanzia asubuhi yupo huku kwa mtoto. Anambembeleza huyo mtoto hata kama hajalia.” Wote wakacheka. “Naweza kumbeba na kumbusu.” Kenny aliendelea kujisifia kwa baba yake aliyekuwa ametoka safari, nakuamua kwenda kumuona mtoto huyo wa mlinzi wa nyumba yao aliyekuwa amezaliwa akiwa safarini. “Kila saa anambusu huyo mtoto. Hachoki!” Mama yake Kenny aliongeza tena. “Unataka nikuonyeshe ninavyombeba mtoto?” “Utanionyesha wakati mwingine. Muache mtoto alale.” Kenny alionyesha uso wakutoridhika. “Twende nikakuonyeshe zawadi nilizokuletea.” “Baadaye dad. Nataka kukaa na mtoto.” “Sasa hivi amelala. Tunakwenda mara moja tu, utarudi.” “Nenda na mama, ukampe hiyo zawadi aniletee huku huku.” Kenny alijibu huku macho yake yakiendelea kumwangalia yule mtoto, akionyesha kutotaka kuondoka kabisa pale.

“Si nilikwambia? Huwezi kumtoa hapo mpaka alale. Chakula kinamfuata hapohapo alipo. Anaogeshwa hukuhuku. Akiamka tu na kujikuta chumbani kwake, analia arudishwe huku. Ukitaka mgombane hapo mlazimishe kurudi nyumbani. Atalia mpaka atatapika.” Mama yake Kenny ilibidi kumwambia mumewe baada ya kutumia kila njia kumtoa mwanae hapo na kushindwa. “Mwache tu. Atazoea, ataona ni kitu cha kawaida. Alikuwa akimsubiria mdogo wake kwa hamu sana. Sasa amekuja huyu, naona na usumbufu wa kumuulizia mdogo wake utapungua.” Walitoka pale kurudi nyumbani kwao na kumuacha Kenny amekaa pembeni ya mtoto akiendelea kumwangalia.

************************

Naih alizaliwa kwenye mtaa wa kitajiri. Akizungukwa na matajiri, wasomi wenye majumba ya  kifahari, yeye akiwa mtoto wa mlinzi wa jumba hilo la wasomi na mamilionea kina Olendekai waliokuwa na mtoto mmoja tu, Kenny. Baba yake Naih alilinda jumba hilo kwa uwaminifu na kwa muda mrefu sana, tokea anatua jijini Dar, kutokea kwao Oldonyo Sambu, kabla hata Kenny hajazaliwa. Aliajiriwa na wazazi wake Kenny, Mmasai mwenzake, Olendekai, wakiwa ndio wametoka kuona tu na mama Kenny, Rita. Alilinda hapo karibu miaka 6, ndipo alipozaliwa Kenny. Akiwa ni mtoto aliyetafutwa sana na wazazi wake. Walishatumia njia kadhaa kumpata mtoto huyo mpaka walipokata tamaa ndipo mwishowe mama yake akajigundua ni mjamzito wa Kenny. Walimlea kama yai, huku wakiwa hawana tumaini la mtoto mwingine tena.

************************

Masai, kama walivyozoea kumwita baba yake Naih, alizaa na msichana ambaye na yeye alikuwa akifanya kazi za ndani kwa wazazi wake Kenny. Masai alitupilia mbali wazo la binti aliyekuwa amemuacha kijijini na kuamua kuanza kuishi na mama yake Naih mara baada ya kupata ujauzito. Mama yake Kenny alikasirika sana, kwani mama yake Naih, Atu, ndiye binti aliyekuwa akimlea Kenny vizuri, tokea anazaliwa. Aliweza kusafiri kikazi na kumuacha naye Kenny bila hata kuwa na wasiwasi. Kenny alipofikisha miaka 4, ndipo Atu, msichana huyo wa kazi, alipopata ujauzito.

Ilimsumbua sana mama Kenny ambaye alikuwa busy na kazi zake, hakuwa na muda wa kukaa nyumbani. Kwanza alikuwa akisafiri safiri sana. Asingekuwa na muda wakutafuta msichana wa kazi mwingine, akaweza kumchunguza vizuri na kujiridhisha kama anaweza kumtunza mtoto huyo wa pekee. Atu alikuwa msaada mkubwa sana. Hakuwa akimpa maelekezo mengi zaidi yakumwachia tu pesa. Atu alijua nini chakufanya na huyo Kenny na nyumba yake bila maswali mengi kwa mama Ole. Hapakuwa na simu za maswali. Alirudi kwenye nyumba safi na mtoto wake alimkuta salama wakati wote.

************************

          Atu alijaliwa umbile lililomfanya si Masai tu kutupia mbali mila na desturi za kwao, alishawaingiza wengi matatizoni. Wazee kwa vijana, waliooa na ambao hawakuwa hata na mpango wa kuoa, walimtolea mate Atu. Na yeye hakuwa mchoyo kwa yeyote aliyemsogelea. Aligawa penzi kwa kadiri ya nafasi yake. Mchana na usiku, bila shida wala kinyongo. Alipojigundua ni mjamzito, ilimbidi Atu aondoke pale kazini. Lilikuwa jaribu ambalo Masai alishindwa kulistahimili.

Atu alikuwa akimgawia penzi Masai kwa nafasi. Kwani walikuwa wakiachiwa nyumba hiyo wao wawili. Kazi ya Masai ilikuwa usiku tu. Mchana alikuwa huru kupumzika au kujitafutia riziki sehemu nyingine kama akitaka. Sasa hapo ndipo alipokuwa akimfaidi Atu ambaye hakuwa na garama au hakuwa akimdharau Masai kama wanawake wa nje. Haikuwa ikimgarimu sana kwa Atu, alimpa pesa kama akipenda, na Atu naye hakujaliwa kinyaa wala dharau kwenye mapenzi. Kwanza hakuwa akijivunga hata kidogo linapofika swala la kutoa mwili wake. Alifanya kama mchezo tu kujiridhisha tamaa za mwili. Hakuona tatizo kumvulia nguo yeyote. Damu ilikuwa ikimchemka Atu, alikuwa tayari muda na wakati wowote akipata nafasi. Masai alinogewa na penzi hilo la bure alilokuwa akipewa yeye zaidi ya wengine. Kila alipomtaka Atu, alikuwa tayari bila kuzungushwa.

Atu alipoondoka,  Masai alimfuata nakumtaka akaishi naye palepale kwa Mzee Ole,  kama mkewe si mfanyakazi tena. Na alimwambia yeye yupo tayari kulea mtoto. Ilibidi sasa Masai kutafuta kazi za mchana kuzisaka pesa ili Atu aishi vizuri mjini.

Wakati huo Masai akihangaika kumtunza Atu aliyekuwa mjamzito, na Mama yake Kenny naye alikuwa akihangaika  na wasichana wa kazi. Mwishowe akaamua kumrudisha Atu kazini akiwa hivyohivyo mjamzito, ili aweze kumlea Kenny. Hasa yeye anapokuwa kwenye safari zake za kikazi. Hakumrudisha tena kuishi pale ndani. Kwani tayari alikuwa akiishi na Masai kama mke na mume kwenye kanyumba hako kadogo, nyuma ya jumba hilo kubwa la Mzee Ole. Masai kama mlinzi na Atu kama mfanyakazi wa ndani. Alitafutwa msichana mwingine wa kazi, Atu akawa akisimamia tu mambo ya pale ndani na kumlea Kenny ambaye alikwisha mzoea Atu kama mama yake.

Kenny alikuwa na Atu kila mahali. Hakutaka mtu mwingine amguse ila Atu tu. Hilo liliwasaidia wazazi wa Kenny kutulia na majukumu yao kwani muda mwingi Kenny alitumia na Atu. Siku chupa ya uchungu inapasuka, Atu alikuwa akimuogesha Kenny. Alijitahi kumbembeleza alale ndipo alipomjulisha Mama yake Kenny kuwa ana uchungu, dereva akamkimbiza hospitalini kwenda kujifungua. Tokea anarudi na Naih nyumbani, Kenny naye akahamia kwenye nyumba hiyo ndogo iliyokuwa na vyumba viwili tu, tena vyumba vya kawaida sana.

Ni kweli Kenny alihamia hapo. Alirudishwa kwao akiwa ameshalala, na kila alipoamka na kujikuta chumbani kwake, alikimbilia kwa Atu. Japokuwa alikuwa amejifungua, lakini aliendelea na ulezi wa watoto wote wawili, Naih na Kenny. Masai alikuwa akimsaidia mkewe kila anapoweza lakini mara nyingi ilimlazimu kutafuta vibarua mida ya mchana ili kuongeza kipato na hapo ndipo Atu alipokuwa huru na wanaume wengine mbali na Masai.

Naih

N

aih alipewa nguo zote za thamani za mtoto wa kike aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu na wazazi wake Kenny, lakini mtoto huyo alifariki muda mfupi sana mara baada ya kuzaliwa. Mama yake Kenny alizifunga nguo hizo kwenye maboksi asijue ni nani wakumpa mpaka alipozaliwa Naih. Alivaa mavazi hayo ya thamani, na kupewa kila kitu cha marehemu mdogo wake Kenny. Atu hakuwahi kununua nguo, akaishia kutumia vitu hivyo. Thamani yote ya chumba cha marehemu mtoto huyo wa kike wa Ole, ilihamishiwa kwenye chumba cha pembeni kwenye nyumba hiyo ndogo aliyokuwa akiishi Masai na Atu. Ilibidi kitengenezwe kwa haraka, na kwa hadhi nzuri zaidi, ili kumfanya Kenny akiwa kwa kina Naih akae kwenye chumba hicho kizuri.

Mama yake Kenny ni kama alihamisha kiu yake ya mtoto wa kike kwenye chumba hicho. Alikitengeneza chumba hicho kikawa nadhifu sana. Alitafuta mtu wa kuchora michoro


mizuri huko ukutani. Kikawa na rangi nzuri zilizotulia. Zile thamani zote alizokuwa amenunua na kupewa zawadi na marafiki zake, kwa ajili ya marehemu binti yake, zilipangwa humo kiutalamu. Kilikuwepo kitanda hicho cha thamani, makabati yake mazuri na zulia nzuri za thamani zilizokuwa zimetandikwa hapo chini. Ili Kenny mtoto  huyo wa pekee aliyeamua kuhamia hapo kumlea Naih awe kwenye mazingira mazuri zaidi anapokuwepo huko, ilibidi kuwekwe na  ‘air condition’.  Yote hiyo ni kwa ajili ya Kenny tu.

Ilikuwa ukiingia ndani ya hicho chumba, usingeweza kudhania kama upo kwenye hicho kijumba kidogo tu cha uwani. Ndani palivutia sana. Atu alikabidhiwa rasmi hicho chumba kwa ajili ya Kenny na Naih. Kwa hiyo yakawa makao makuu ya Naih na Kenny.  Kenny alicheza michezo yake hapohapo ndani chumbani, na alipokuwa akichoka, alipanda kulala kitandani alipolazwa mtoto. Hakuthubutu kutoka. Hata rafiki zake walipokuwa wakija kumtembelea nyumbani kwao, walimfuata humo ndani.

Naih&Kenny.

K

enny na Naih walikuwa pamoja kama mapacha. Kenny akimtambua Naih kama nusu yake. Tangia wapo watoto, Kenny alisema Naih ndio yeye. Hakuwa na namna nyingine yakumuelezea mtu. Kila alipoulizwa mtoto ni nani, alisema ni mimi. Alipokuwa mtoto lilikuwa jambo la kufurahisha na watu walizoea hivyo kuwa Naih ni ‘mimi wa Kenny’ na Kenny akaendelea kumuelezea hivyo kila mahali. Kadiri walivyoendelea kukua, ikaanza kusikika tofauti kwa  mama Ole. Akajaribu kumfundisha Kenny kuwa amtambulishe Naih kama mdogo wake tu, lakini Kenny aliendelea kusisitiza kuwa Naih ni ‘mimi wangu’. Ilibidi Naih kuendelea kuvalishwa vizuri kama mtoto wa tajiri, kwani alikuwa akiongozana na Kenny kila mahali.

Kadiri walivyoendelea kukuwa ndivyo walivyojikuta wakifanya mambo mengi pamoja. Kucheza na mara nyingi walijikuta wakilala pamoja. Kenny akawa amepata rafiki wa kwanza na wakaribu kabisa, Naih. Kwenye jumba hilo la kifahari, Naih aliingia bila kubisha hodi, kadhalika na nyumbani kwa kina Naih pia. Kenny hakuhitaji kugonga chumbani kwa Naih, wala kuaga. Aliingia na kutoka atakavyo. Haikujulikana wanalala wapi kwa hakika, ilikuwa inategemea usiku utawakuta wapi. Na kwa kuwa wote walihudumiwa na Atu, haikusumbua chochote. Mama yake Kenny alimuacha Atu afanye vile anavyotaka yeye na hao watoto. Ilimradi Kenny awe na furaha tu. Tatizo la wazazi hao ni kuona Kenny anatoa machozi, au awe hana furaha.

************************

Nai kama walivyoanza kumwita pale kwao, alizaliwa wakati Kenny akiwa ametimiza umri wa miaka 4. Alikuwa na  weusi ule wa kung’aa na urefu wa kimasai. Mama yake Kenny alizaliwa na mama mwenye asili ya kijerumani. Yeye mwenyewe hakubeba asili hiyo, lakini Kenny ndiye aliyekuwa amebeba damu ya kijerumani kabisa. Alishangaza kila mtu wakati amezaliwa na kuwa kama mtoto wa kizungu wakati baba ni Mmasai tena mweusi haswa na mama alikuwa mweupe tu. Utata ulipungua pale walipokuja kujitokeza baadhi ya ndugu upande wa mama, tena wa ukoo. Ndipo angalau watu na marafiki wakaribu walifungwa midomo. Lakini kabla ya hapo wengi walisema mama huyo ameumbuka baada ya kupewa mimba na mzungu.

************************

Naih alipofikisha miaka 3, kwa mara ya kwanza baba yake alikwenda umasaini kusalimia na hakuwahi kurudi tena. Atu hakuwa akijua linaloendelea na wala hakujua ni wapi pakumtafuta Masai. Hakupafahamu kijijini kwao wala ndugu zake. Baada ya Masai kuondoka, wazazi wa Kenny walitafuta kampuni ya ulinzi kulinda nyumba yao. Hawakutaka kuajiri tena mlinzi wakawaida. Wakaingia mkataba na kampuni kubwa sana ya ulinzi hapo jijini. Walianza kufika walinzi tofauti tofauti kulinda nyumba hiyo, na wote waliomtaka Atu aliwapa uroda bila shida. Alilala na kila mlinzi aliyemtongoza. Wazee kwa vijana walipishana kwenye chumba hicho cha Atu, usiku walipokuwa wakija kulinda.

Baada ya Nai kufikisha miaka 4, mama yake alijifungua mtoto mwingine wa kike, akiwa hajulikani baba yake, kwani alikuwa na mahusiano na wanaume wengi kwa wakati mmoja. Kuanzia mtunza maua wa nyumba hiyo ya Mzee Olendekai, aliyekuwa akipewa penzi mchana, mpaka hao walinzi waliokuwa wakibadilishwa mara kwa mara mida ya usiku wanapokuwa kazini.

************************

Kenny alianza shule katika moja ya shule za watoto wa mamilionea wa pale jijini, na Naih alipofikisha umri wa kuanza shule, Atu alimtafutia shule zakawaida tu za serikali. Naih alipotimiza umri wa miaka 5, mama yake alikuwa tayari na mtoto mwingine, Zai, wa umri wa mwaka mmoja na mimba nyingine tena. Alipojigundua ana mimba ya mtoto wa tatu, akajaribu kutoa mimba. Alikaribia kufa kwa matatizo, mwishowe mama Ole akashauri afungwe tu kizazi ili asishike tena mimba.

Kwa kuwa bado alikuwa akimtunza Kenny, na kufanya kazi ndani ya jumba hilo la kina Kenny, Atu na wanae hawakufukunzwa kwenye kinyumba hicho cha nje. Kwa hiyo angalau Atu alipata pakuishi yeye na watoto wake, bila mwanaume yeyote kujitokeza kama baba wa wale watoto wawili, wala kutoa matunzo. Kwa asili Atu alikuwa mchapa kazi kitu ambacho Mama yake Kenny hakukipata kutoka kwa mfanyakazi mwingine yeyote ila Atu. Atu aliijulia ile nyumba. Alijua nini chakufanywa na kwa wakati husika. Yeye ndio alisimamia mambo ya nje na ndani ya hiyo nyumba, na kumtunza Kenny bila tatizo. Aliendelea kuwatunza watoto wake huku wakila na kuvaa kutoka kwenye jumba hilo. Na kwakuwa mama yake Kenny alikuwa akiwa na shuguli nyingi sana za kikazi na mumewe hivyohivyo, Atu hakuhangaika sana kuwalea wanae. Alichokuwa akila Kenny, ndicho walichokuwa wakila Naih na wadogo zake.

************************

Lakini katika watoto hao watatu wa Atu, ni Naih tu ndiye aliyekuwa akinunuliwa nguo nzuri na mama yake Kenny, kwani kila alipokuwa akienda Kenny, ilikuwa lazima aongozane na Naih, lasivyo hakukubali kwenda popote na kumuacha Naih. Ikamlazimu mama Kenny kuendelea kumvalisha vizuri Naih ili alingane na sehemu anazokuwa akienda Kenny. Waliendelea kufuatana katika umri wao wote. Wakati wote Naih ndiye aliyekuwa akiwahi kutoka shule, kwa hiyo kila anaporudi Kenny kutoka shuleni, ilikuwa nilazima amtafute Naih alipo ili awe naye. Kama siku hiyo alikuwa na mwalimu anayefika nyumbani kumfundisha kitu chochote, iwe masoma au kutumia vyombo vya mziki, lazima Naih awepo na ajifunze naye.

Kwa hiyo Naih alikuwa akijua mambo mengi anayoyajua Kenny. Alijua kutumia kinanda, gitaa na kusoma mziki kama Kenny. Japokuwa hakusoma shule za kimataifa au wanazosoma kwa lugha ya kingereza kitupu, lakini Naih alijua kuzungumza kingereza kama Kenny, kwani muda mwingi alikuwa na Kenny na marafiki zake Kenny pia walitumia lugha hiyo ya kingereza mara nyingi kwa mawasiliano hata kwa wazazi wao. Kwa hiyo mara nyingi lugha aliyotumia Kenny kwa mawasiliano, isipokuwa kwa Atu na dereva wake tu, ilikuwa ni lugha ya kingereza. Kila alipokuwepo Kenny ndipo alipokuwepo Naih. Na wote walimjua Naih kama Kenny, au kama ‘mimi wa Kenny’. Mtoto huyo wa kitajiri, tena wa pekee, hakufanya kitu bila Naih.

Kenny.

Kutokana na asili yake ya mchanganyiko wa Kitanzania na Mjerumani, tokea akianza shule ya chekechea, watoto wa kike walimpenda sana. Alifuatwa na mabinti mbalimbali wakitaka ukaribu naye. Alipofika umri wa miaka 14 Kenny alianza kuwa na mahusiano na wasichana mbali mbali. Alilala na kila msichana aliyemsogelea. Na kwa kuwa alikuwa na pesa na mzuri sana wa sura, mabinti wengi waliona fahari kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Kenny. Wazazi wake walifahamu tabia yake hiyo lakini kila kitu alichokuwa akifanya Kenny, ilikuwa ni sifa kwa wazazi wake. Walijivunia. “Amekuwa siku hizi!” Wazazi wake walikuwa wakiongea kana kwamba ni jambo la fahari.

************************

Baada ya kuzaliwa Kenny na mama yake kuhangaika swala la watoto na kushindwa, hakuna aliyejua ni nini kilitokea kati ya wazazi hao. Ndoa yao ilibadilika kabisa. Ikaanza kutoeleweka. Walikuwa wakiishi pamoja, lakini hapakuwa na maisha ya ndoa kati ya wazazi wake. Kenny ni kama alirithi tabia ya uhuni kutoka kwa baba yake. Mzee huyo alitembea na kila mwanamke aliyemtaka yeye. Ilikuwa ili ufanye kazi kwenye kampuni zake, nilazima uwe umemridhisha kitandani. Na wanawake wengi walijituma kwa Mzee huyo kwa pesa aliyokuwa akihonga. Hakuwa mchoyo, ilimradi umtimizie haja zake basi utafaidi pesa yake. Iwe ofisini au kwenye nyumba za kulala wageni, anapokutaka yeye, basi umridhishe. Alisafiri nchi na mikoa tofauti tofauti hapa nchini, na wanawake tofauti tofauti. Mama yake Kenny yeye alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mume wa mtu, yaliyodumu kwa muda mrefu sana, akatulia hapo.

************************

Naih alizungukwa na mifano mibaya sana ya mapenzi. Alikuwa huku akimuona vile mama yake anavyolala na wanaume tofauti tofauti. Kenny naye ambaye ndiye alikuwa rafiki yake kipenzi, ndiye alilala na kila binti. Na kwa kuwa alimpenda sana Naih, na ndiye aliyekuwa msiri wake, hakuacha kumsimulia mambo anayoyafanya na mabinti hao. Kila siku Kenny alimjia Naih na habari za mabinti aliokuwa akilala nao huko shuleni.

“Mnalala chooni sakafuni!?” Naih aliuliza kwa upole huku akiwa anamshangaa Kenny. “Hapana Nai! Tukilala chini sakafuni, wanafunzi wengine wakiume wanaongia kujisaidia chooni watatuona.” “Mnafanyaje sasa!?”  Naih aliendelea kuhoji mara baada ya Kenny kumletea habari aliyoiona njema kuwa ameshalala na mabinti karibia wote wa darasani kwao. “Ni rahisi sana. Kwanza wao wenyewe ndio wanataka. Kwa hiyo wakati wamapumziko au wakati wengine wapo darasani nawaambia tuingie nao chooni kwetu, tunajifungia kwenye moja ya choo, basi.” Naih alibaki akimtizama Kenny.

“Lakini wewe usifanye hivyo Nai. Umesikia?” “Kwa nini?” Naih akauliza. “Sitaki wewe ufanye hivyo.” “Mbona namuona mama anafanya. Halafu unakumbuka siku ile tulimkuta baba yako anafanya hivyo na yule dada anayekuja kusafisha, na wewe pia kila siku unanisimulia kuwa unafanya hivyo! Sasa kwa nini na mimi nisifanye?” Naih alimuona vile Kenny alivyobadilika sura na kuwa mwekundu. “Nataka wewe usifanye.” “Kwa nini?” Naih aliendelea kumuhoji wakati wapo chumbani kwa Kenny. “Just don’t do it. Okay?” Kenny aliongea kwa ukali. “Usikasirike Kenny. Sitafanya hivyo. Nilikuwa nakuuliza tu.” “Afadhali. Sitaki wewe ufanye hivyo, sawa?” “Sawa. Usikasirike sasa!” “Umeniogopesha.” Naih akacheka kidogo. “Pole. Nilikuwa natania tu.” Hapo tayari Kenny alikuwa kidato cha tatu, wakati Naih ndio anakaribia kumaliza darasa la saba.

Naih.

Naih aliendelea kukuwa akiwa na muonekano wa kimasai. Mweusi aliyekamilika, mtulivu sana, tofauti na wadogo zake wawili waliomfuata. Wote wawili walifanana maumbile na mama yao kama mapacha. Wadogo zake walizaliwa wakiwa maji ya kunde. Bila shaka baba zao walikuwa weupe sio kama Masai. Wadogo zake hao walijaliwa mvuto wa haraka machoni mwa watu, zaidi wanaume tofauti na Naih, aliyekuwa akivalishwa nadhifu na kutembea na Kenny kila mahali lakini hakujaliwa mvuto kama wadogo zake.

Watu wengi walimtizama na kutafuta kile anachovutiwa nacho Kenny bila kupata jibu. Kila mahali alipokuwa akitokea Kenny, akiwa na Naih, ndipo watu wengi ilibidi kumtizama Naih kwa vile alivyokuwa akisifiwa na Kenny. Kenny hakuacha kumtambulisha hata kwa wasichana zake kama ni ‘mimi wake’. Ukitaka urafiki na Kenny, umpende Naih. Hata kama ni msichana alitaka kulala na wewe, ukitokea kumchukia Naih, mahusiano yanakufa hapohapo. Na aliweza kumsoma kila mtu kwa kumwangalia machoni pale anapomtambulisha Naih. Ni heri uonyeshe tabasamu wakati anaongelea habari za Naih, kuliko kumkashifu kwa chochote, ‘mimi wake’. Hata kama ni rafiki wa kiume, ukimchukia Naih, Kenny alihesabu unamchukia yeye.

************************

Hakuwa akifanya mapenzi na msichana yeyote kama Naih yupo sehemu hiyo. Ni heri apange na huyo binti wakutane siku nyingine akiwa peke yake bila Naih kuwepo. Lakini pia hakuna msichana aliyelala naye bila kuja kumsimulia Naih. Hakujali mapenzi hayo mtafanyia wapi, ilimradi isiwe eneo alipo Naih. Alipofikisha miaka 16, Kenny alipewa gari nzuri sana, na ndipo hapo alipopata sehemu ya kulala na wasichana wote waliomtaka. Na hakuwa akichagua. Uwe mweusi au mweupe, mnene au mwembamba, ilimradi uwe na jinsia ya kike na utake kulala naye, Kenny hakuwaza mara mbili.

Alikuwa akiwapa muda atakao kuwa na nafasi, ukikubali, atakupeleka kwenye gari yake, ukimalizana naye, anakupa pesa ya taksii, mnaachana. Atarudi nyumbani kuoga kwanza, ndipo amtafute Naih alipo na kukaa naye. Hakuwahi kuchelewa kurudi nyumbani. Alihakikisha kabla Naih hajalala, anamuona na kumsimulia siku yake iliendaje. Alilala na nani na wapi. Akichelewa kurudi, nakumkuta ameshapanda kitandani, na yeye atapanda kwenye hicho kitanda na kuanza kuzungumza naye.

************************

“Sitaki kuongea sasa hivi, Kenny. Niache.” “Kwa nini!?” “Nina usingizi.” “Just open your eyes and look at me. Please. You don’t have to say anything.” “Sitaki.” “Umenikasirikia?” “Kwa nini umechelewa kurudi nyumbani?” “Twende ukalale chumbani kwangu, nitakwambia kwa nini.” “Sitaki.” “Naih please!” Hakuweza kulala bila kumuona Naih. Na hawakujulikana wanalala wapi. Ikitokea Naih anamgomea kabisa, basi Kenny atalala hapohapo pembeni yake mpaka asubuhi. Na wakati mwingine akikubali, wanaenda kulala chumbani kwa Kenny. Hawakujulikana siku hiyo wanaamkia nyumba ipi, na ndio maana mama yake Kenny alihakikisha chumba cha Naih kinafanyiwa marekebisho ya mara kwa mara kwa kuwa ni kama mtoto wake aliishi huko.

 Na hakutaka mtu mwingine chumbani hapo isipokuwa Naih peke yake. Kwa hiyo Atu alilala na watoto wake hao wawili, na Naih alikuwa akilala kwenye chumba chake peke yake. Kiliendelea kubadilishwa vitu vya thamani na mama Ole kwa kadiri Kenny na Naih walivyoendelea kukua. Mwanzoni Atu hakuwa hata akiwaza juu ya nguo za wanae. Kwani Naih alivalishwa na mama yake Kenny na Kenny mwenyewe, na nguo hizohizo zilipokuwa ndogo kwa Naih, Atu aliwavalisha watoto wake wadogo mpaka walipokuwa wakubwa na kutofautiana maumbile. Naih mwembamba, wadogo zake wapana chini.

************************

Waliendelea hivyo kukua pamoja, na Kenny akimsaidia mara kwa mara Naih katika swala la usafiri. Alipomaliza darasa la saba, Naih alifeli. Ikabidi Atu amtafutie nafasi katika shule ya Sekondari ya Shabani Robati, iliyokuwepo hapohapo jijini. Wakati anaanza kidato cha kwanza katika shule hiyo, Kenny ndiye aliyekuwa akimpeleka shuleni kila siku asubuhi, na kama atashindwa kwenda kumchukua, basi alimtuma dereva wao kumfuata Naih. Japokuwa hakuwa na akili nzuri za darasani kama Kenny, lakini hakumsumbua mama yake hata kidogo. Alikuwa mwanafunzi wa kawaida sana darasani na tabia za utulivu. Atu hakuwahi kuitwa shuleni kwa kina Naih sababu ya kosa lolote lile.

Maisha yake yalijaa Kenny tu. Walifuatana hapo nyumbani kuanzia asubuhi mpaka usiku, kama Kenny hatatoka. Au wakati mwingine alitoka na Naih. Isipokuwa safari za usiku, Atu alikataa kabisa asitoke na Naih. Atu alikuwa mama mkali sana kwa binti huyo.  Kuna mambo mengine aliona ni heri afukuzwe kazi kuliko kuyaruhusu kwa Naih ili kumfurahisha Kenny. Ilikuwa lazima saa 12 jioni, awe amemrudisha Naih nyumbani. Naih alipoanza kukua, aliacha kuwaogesha pamoja na kumwambia Kenny hawezi kuoga tena pamoja na Naih na wala asiwe anamwangalia Naih akiwa anavaa. Afunge macho au atoke nje ampishe wakati anavaa. Na mambo ya msingi yakumfanya Kenny asicheze na mwili wa mwanae. Walipojua mambo gani hataki kwa mtoto wake, wazazi wa Kenny na Kenny mwenyewe waliridhia na kuendelea kuishi nao kwa sheria za Atu na mipaka aliyoweka kwa mwanae. Na kwa kuwa Naih mwenyewe alikuwa mtulivu, hapakuwa na tatizo.

************************

Napo kwenye shule hiyo ya Shabani Robati, Kenny alianza mahusiano ya kimapenzi na kila rafiki wa Naih. Kila aliyekuwa akimuona Kenny, alimfuata Naih na kutaka kumjua vizuri Kenny. Naye Naih hakuwa na shida aliwaelekeza. “Unataka kulala naye?” Naih alikuwa akiwauliza kwa upole, akionyesha kutokuwa na wasiwasi wowote. “Unafikiri atanikubali?” “Kenny hana shida ya kulala na msichana yeyote yule. Akija kunichukua leo, wewe tangulia ukazungumze naye.” Huo ndio ulikuwa ni ushauri wa Naih kwa kila aliyekuwa akichanganyikiwa wakimuona mtoto huyo mwenye asili ya Kijerumani, akifika pale shuleni kumshusha au kumchukua Naih. “Nitamwambia nini sasa?” “Sijui. Labda kama hivi unavyoniambia mimi. Hana shida kabisa.” “Kwani analala na kila msichana?” “Ndiyo.” Naih huwajibu bila kusita, wala kuonyesha kama ni jambo la ajabu.

Mpaka Naih anafika kidato cha pili, Kenny alishalala na wanafunzi wengi sana wa shuleni hapo. Ukabaki ugomvi tu kwa mabinti hao, wakimgombaniana Kenny. “Kenny huwa hana mwanamke wa muda mrefu. Anasema huwa hawezi, anakinahiwa.” Naih alikuwa akiwaambia kwa sauti yake tulivu, kutaka wasigombane bure. Aliwahakikishia kuwa Kenny huwa anasema hajawahi kumpenda msichana yeyote ila tu anafurahia kile anachokifanya nao. Na asirudie na msichana huyohuyo mara nyingi.

“Anasema hataki mambo yakufuatana nyuma. Hana muda na watu wengine.” Naih aliongeza. “Ila wewe?” Naih alibaki akifikiria. “Labda. Ukikutana naye, muulize.” Naih hujibu huku akifikiria. “Hapokei simu zangu wala hajibu jumbe zangu!” Hulalamika. “Basi atakuwa hakutaki tena. Kenny hawezi hayo maisha ya kupigiana simu.” “Mbona sasa wewe anakupigia?” “Mimi nitofauti kwa Kenny.” Naih hujibu na tabasamu. “Tofauti gani sasa? Au ndio upo bora kuliko sisi?” Wengine walikuwa wakijaribu kumkejeli Naih, kwani wengi wao walionekana na mvuto kuliko hata Naih mwenyewe.

Hata Naih mwenyewe hakuwa akijua awajibu nini au aeleze nini juu yake na Kenny. Ila alijua Kenny anampenda kuliko kitu chochote duniani. Na hata wakilala naye, alitaka awe anamgeukia na taa iwe inawaka awe akimtizama tu mpaka apitiwe na usingizi. Walijuana kwa kuangaliana tu. Walipendana bila hata sababu. “I love you for free, Naih.” Ndio usemi wa Kenny kwa Naih kila wakati na kumfanya Naih naye kuiga bila kujua maana. “I love you for free too, Kenny.”

************************

Maisha yao yaliendelea kuwa ya furaha na amani, mpaka pale Kenny alipomaliza chuo kikuu. Hakutaka kusoma nchi yeyote mbali na Tanzania. Tabia hiyo ya kulala na kila mwanamke ikaanza kumtia hofu mama yake. Alihofia atakufa mapema sana, tena mtoto mwenyewe mmoja tu! Akaonelea asiendelee na shahada ya pili, ni heri aoe kwanza, labda angetulia.

Mama yake alishastaafu kwenye wizara ya fedha ambapo alifanya kazi hiyo kwa muda mrefu sana. Alishashika nyadhifa nyingi, tena mbali mbali katika wizara hiyo ya fedha. Mpaka anastaafu alikuwa kwenye ngazi ya naibu wa fedha. Alifungua kampuni yake ya fedha. Akitoa ushauri kwenye makampuni binafsi juu ya mipangilio ya pesa, kuwatengenezea budget, na mambo mengi yafananayo na matumizi ya pesa kwenye makampuni ili kufanya makampuni hayo kuongeza faida.

Akiwa amemaliza tu chuo, mama yake alitaka ajiunge na kampuni yake, wafanye naye kazi wakati akisubiria matokeo yake ya chuo kikuu. Kama kawaida ya Kenny, hakuwa mbishi kwa lolote. Akaanza kazi kwenye kampuni hiyo ya mama yake akiwa amemuweka kwenye kitengo cha masoko. Kutafuta wateja. Kwa uzuri wa sura na maneno ya mwanae, aliweza kumletea mama yake wateja, bila shida. Lakini napo pia kwenye ofisi hiyo ya mama yake, alishalala na kila mfanyakazi. Kasoro kwenye ofisi za baba yake. Hapo alishindwa hata kutongoza kwa kuwa wote walishalala na baba yake.

************************

Kipingamizi pekee kitakachomfanya Kenny asilale na mwanamke yeyote yule, ni kama ulishalala na baba yake, rafiki zake au ni mke wa mtu, basi. Na katika hilo hata marafiki zake walimuheshimu. Hakuthubutu kupita walikopita watu anao wafahamu. Alijaliwa moyo mzuri wa kupenda na kujali. Hakuwa na dharau hata kidogo. Tabasamu usoni mwake ndilo lilokuwa likivutia wanawake nakutaka awavue nguo kwa haraka. Pia hakuwa mchoyo. Rafiki zake walimjua kama ni mtu anayependa kusaidia.

************************

Kila msichana aliyekuwa akiletewa na mama yake kwa ajili ya kuoa kulikuwa na tatizo. Kama hakuwa ameshalala na Kenny, basi ni wale kina dada wanaojiheshimu, wanaotaka mume wa kweli kwenye maisha, na wanapokutana na Kenny, wanashindwa na tabia zake za kulala na kila mwanamke, na kwake hakuonyesha kama kuna tatizo. Waliojikaza na kuamini atabadilika, walikutana na kipingamizi Naih ambaye huyo ndio alianza kumuumiza kichwa Mama Kenny. Hakuwa na shida ya kukataa wanawake aliokuwa akiletewa na mama yake. Hakuwahi kusema wanatatizo, lakini wengi akishatambulishwa kwao, siku inayofuata atalala nao, na kumwambia mama yake hamtaki tena huyo msichana. Mama yake alijaribu kuzungumza naye akijaribu kujua ni nini hasa anatafuta kwa hao mabinti wote na hajapata kutoka hata kwa mmoja wao, jibu lake lilikuwa hata akimwambia mama yake, asingeelewa. 

Nora.

M

iaka ikasogea Kenny akifanya kazi kwa juhudi sana kwenye kampuni hiyo ya mama yake. Aliweka juhudi na alikuwa na nidhamu ya kazi kitu kilichokuwa kikimfurahisha mama yake. Kuna kipindi alibahatika kumpatia mama yake kazi au tender kubwa kutoka kwa mfanyabiashara mmoja mkubwa sana jijini Mwanza. Alikuwa amejenga Super makert kubwa sana jijini hapo, na alikuwa na mpango wakuendelea kuzifungua hizo Super Makert katika kila mkoa nchini Tanzania. Akampa kazi ya kufundisha wafanyakazi wake wa ngazi za juu wanaohusika na mambo ya fedha, au anaowaandaa kuwapeleka kwenye mikoa anayotarajia kufungua super makert hizo.

Kiongozi mkubwa wa upande wa fedha wa kampuni hiyo alikuwa ni binti wa huyo mfanyabiashara, Nora. Na kwa kuwa makao makuu ya mfanyabiashara huyo yalikuwa ni Mwanza, ilimbidi Mama Kenny awe akisafiri mara kwa mara kwenda jijini huko kutoa elimu. Ikatokea Mama Kenny akapatana sana na Nora. Alimpenda sana binti huyo, akaona ni binti atakayemfaa mwanae. Alijielewa, alikuwa na msimamo, na alijaliwa uzuri wa aina yake.

Binti huyo wa kisukuma akisimama mbele yako, utatamani kumtizama tu. Kuanzia utosi mpaka mguu wake alijaliwa uzuri. Hukuhitaji kumtizama kwa muda mrefu kugundua kama Mungu alichukua muda wa kutosha kumtengeneza kwa makini ili kuonyesha ujuzi wake kwa wanadamu. Alijaliwa weusi wa maji ya kunde, usio hata na doa. Rangi yake moja, juu mpaka chini. Kwa ufupi Nora alikuwa mzuri. Na yeye alijijua hivyo. Zaidi alipewa akili nzuri na alikuwa msichana mtulivu.

Alifanya kazi kwa karibu sana na Mama Kenny, mwishowe akamkaribisha jijini Dar kutembelea kampuni yake. Kwa kuwa walianza kujenga mahusiano ya kirafiki na mama Kenny, Nora alifanya kila awezalo, kupanga ratiba yake iliyokuwa imejaa kila wakati, ili kupata muda wa kufika jijini Dar kumtembelea mama huyo. Kwa kuwa Kenny ndiye aliyekuwa akibakishwa ofisi endapo mama yake akisafiri, hakuwahi kuonana na Nora. Kwa hiyo Mama Kenny alimuandaa Kenny kuwa watakuwa na mgeni siku hiyo ya ijumaa pale ofisini kisha atakuwa nao kwenye chakula cha usiku. Bila shida Kenny hakubisha, akamwambia atajitahidi awepo kwa chakula cha usiku wa siku hiyo.

Mama Kenny akampa maelekezo yakutosha Atu juu ya chakula gani kipikwe na muda wa kuwa tayari, na kusisitiza jambo lolote lisiharibike kwa kuwa atafika hapo na mgeni muhimu sana. Atu alishakuwa mtu mzima, hata utendaji kazi wake ulibadilika, msaada mwingi aliupata kutoka kwa Naih na wadogo zake. Naih ndiye aliyekuwa akimsaidia sana mama yake kazi kwenye jumba hilo kuliko wadogo zake. Alijua kugawa muda wake wa shule na kufanya kazi za ndani kwa kina Kenny. Kama kupika na mambo mengine mengi. Mwanzoni haikumsumbua Mama Kenny, kwanza aliona inampunguzia garama ya kuajiri wafanyakazi wengine mle ndani ambao hawakuwa waaminifu. Naih na Atu walikuwa waaminifu sana. Hata Mama Kenny aache vitu vyake vya thamamani juu ya meza au popote pale, atavikuta tu. Kwa hiyo hawakuwa na mipaka kwenye nyumba hiyo. Alimuongezea mshahara Atu, akawa anafanya kazi zote yeye na wanae watatu.

Kilikuwa kipindi Naih amemaliza kidato cha sita, yupo nyumbani anasubiri majibu ya matokeo yake ili ajiunge na chuo. Siku hiyo mama yao aliwagawia kazi wote watatu yeye na wadogo zake. Naih alipewa jukumu la usafi. Akaanza usafi kwenye jumba hilo kuanzia asubuhi, huku mama yake na wadogo zake wakihangaikia matayarisho ya ugeni jioni hiyo. Kenny na wazazi wake walikuwa wakitoka kwenda kazini kuanzia asubuhi nakurudi jioni.

************************

Lakini kila asubuhi kabla yakutoka nyumbani, lazima Kenny aende akamuone Naih. Na kwa kuwa alikuwa akitoka mapema, Naih alikuwa akishtukia Kenny ameingia kwenye chandarua kitandani kwake. Analala naye pale akizungumza hili au lile, mpaka muda wake wa kwenda kazini ukifika, ndipo anaondoka na kumuacha Naih kitandani hapo.  Na usiku lazima amuone kabla ya kulala, ndipo atoke tena. Kwa hiyo kila akitoka kazini, alikimbilia nyumbani kumuona Naih. Watakaa naye kwa muda. Kama akimkuta anakazi, anazunguka naye humo ndani, Naih akifanya shuguli zake, yeye anaongea. Anakuwa mgongoni mwake muda wote. Hata kama anaingia kuoga, atakaa nje ya mlango akimsimulia Naih hili au lile, mpaka Naih anamaliza kuoga, anatoka bafuni bado anakuwa anamfuata, mpaka muda wake wakutoka, kama anataka kutoka ndipo ataondoka kwenda kwa rafiki zake, kama anatoka na Naih au wanaachana kwenda kulala. 

Na wakati wote Naih anakuwa anajua alipo Kenny. Kenny alitaka kuongea na Naih kila wakati. Na kama yupo sehemu mbali na Naih, alimpigia simu au kutuma ujumbe, kumueleza kinachoendelea huko alipo mpaka anaporudi nyumbani. Wengi waliomfahamu walishajua kuwa Naih ni nusu ya Kenny. Walishazoea kumuona wakiwa katikati ya starehe akitoka kupiga simu kuzungumza na Naih kwa muda mrefu, na wakati mwingine kurudi kuendeleza starehe huku akiendelea kuchati naye au kurudi kuwaaga akiwaambia anamuwahi Naih nyumbani.

************************

Mpaka inafika muda wa mgeni na wenyeji wake kufika nyumbani, Atu na wanae wote walikuwa hoi kwa matayarisho. Meza ilitayarishwa vizuri, ilijazwa vyakula na vinywaji. Atu na wanae wakabakia jikoni wakisubiri waitwe, kama kuna kitu kinahitajika. Naih alikuwa anamalizia kusafisha pale jikoni na kuosha vyombo ambavyo mama yake alitumia kupikia, ndipo Kenny, wazazi wake na mgeni wakaingia. “Naenda kumuangalia Naih. Nitarudi muda sio mrefu. Nyinyi endeleeni tu.” Walimsikia Kenny akiaga. “Nai yupo huku jikoni anaosha vyombo.” Atu alitoka jikoni na kumuwahi Kenny kabla hajatoka mlangoni.

“Nai!” Kenny aliita huku akielekea jikoni wakati mama yake akimkaribisha Nora sebleni. “Nai!” Alirudia kuita. “Nipo huku Kenny. Njoo na uache kelele.” “Mbona unaninyamazia sasa!?”  Kenny akaingia hapo jikoni. “Nimeitika Kenny!” “Basi sikukusikia.” Kenny akarukia juu ya kibambaza, pembeni ya sinki analooshea vyombo Naih na kukaa, huku akimwamgalia.

“Mbona huniangalii sasa!?” “Nimechoka Kenny. Nataka nimalize hapa, nikapumzike.” “Nikusaidie?” “Nimeshamaliza.” “Niangalie basi kidogo.” Naih akacheka na kumwangalia. “Kweli unaonekana umechoka. Ukimaliza hapo nitakusindikiza ukaoge, halafu ulale. Umekula?” “Nimekula wa kwanza. Nilikuwa sijala tokea asubuhi.” Naih aliendelea kuzungumza na Kenny huku akiosha vyombo, Atu na wanae wote walikuwa wameinamia simu zao, kila mmoja kimya. Kasoro Kenny ndiye aliyeendeleza maongezi.

“Futa hizo kaunta wakati unaongea.” Naih akamtuma Kenny. Bila ubishi akachukua kitaulo na kuanza kufuta kaunta za pale jikoni huku akiendelea kuongea. Naih alimaliza na kutaka kutoka, akamuona Kenny naye anamfuata. “Unaenda wapi!?” Naih akamuuliza kwa mshangao. “Nakusindikiza.” “Si kuna mgeni? Baki mpaka atakapoondoka halafu ndio uje.” “Ni mgeni wa mama.” “Unauhakika? Sitaki mama yako aje aanze kugomba baadaye anilaumu kuwa nakufanya hutimizi majukumu yako.” Kenny alitoka pale bila kujibu kitu, akampita Naih mwenyewe na kuelekea kwenye chumba cha Naih, Naih akamfuata nyuma. Badala yakuingia kuoga, akabaki chumbani kwake akicheka na Kenny, nakujisahau kabisa.

Mdogo wake Naih akaingia pale chumbani kwa Naih, kumwita Kenny. “Mama yako anakuita.” “Anataka nini!?” Kenny akauliza kama asiyetaka kusumbuliwa. “Atajuaje bwana!? Wewe nenda, acha kuuliza maswali.” Naih akaingilia. “Usiwahi kulala, Nai. Nikikukuta umelala nakuamsha.” Kenny akasimama pale alipokuwa amejilaza kitandani kwa Naih. “Umenisikia Nai?” “Bwana wewe nenda.” “Usilale.” Kenny akasisitiza, wakashangaa Mama Kenny ameingia. “Nitabia gani hii? Wewe Nai! Hukujua kama leo Kenny ana mgeni hapa nyumbani?” Kama kawaida ya Mama Kenny kumlaumu Naih kwa kila kosa la Kenny.

“Ngoja kwanza mama. Kwa nini hukuniambia kama ni mgeni wangu!? Wewe umeniambia ni mteja wetu, mmekuwa marafiki ndio maana umemkaribisha nyumbani. Mimi nimewapisha ili mzungumze!” “Hapana Kenny. Nimemleta kwa ajili yako.” “Ili iweje!?” “Ni binti mzuri wakumfanya mke.” “Mama naye kwa kuzunguka! Sasa siungeniambia mapema nimchangamkie?” Kenny akacheka. “Narudi sasa hivi Nai, ngoja nikamuone mke wa Kenny mtarajiwa.” “Lakini Kenny!” Mama yake akamuita kabla hajatoka.

“Nini?” Kenny akageuka. “Naomba heshima.” Kenny akacheka. “Hivi ushawahi kusikia mtu anakulalamikia hata mara moja kuwa mwanao Kenny hana heshima?” “Najua unanielewa Kenny. Zile tabia zako, naomba uache.” “Hapo ndipo unanichanganya! Umeniambia ni mke wangu. Si ndio unataka nimuoe?” “Ndiyo Kenny.” “Basi wewe usiwe na wasiwasi na hilo. Wewe si umeridhika naye?” “Ndiyo, lakini…” “Wewe usiwe na wasiwasi na mimi. Nitarekebisha kila kitu.” “Huyu binti anaonekana anajiheshimu sana. Na anaonekana yupo tayari kuolewa na kutulia. Nimezungumza naye kwa muda mrefu, nilimuonyesha picha zako, akaonekana amevutiwa na wewe. Naomba usiharibu na kwa huyu tena. Acha yale mambo yako ya..” “Ngoja kwanza mama. Wewe umenitafutia mchumba, unasema anaonekana amevutiwa na mimi na mimi sijakataa. Sasa tatizo tena liko wapi!?”

 “Huwa unaharibu mapema sana Kenny.” “Basi safari hii sitaharibu mama yangu. Twende tukarekebishe, tumuweke sawa. Kenny nipate mke.” Naih alikuwa akiwasikiliza tu. “Na ninakuomba uwe unamaanisha Kenny. Nataka kukuona angalau huyu unamfikisha kanisani.” “Usijali mama yangu. Twende kabla mchumba hajakasirika.” Alitoka na mama yake na kumuacha Naih akicheka moyoni huku akitingisha kichwa. “Simuoni muoaji hapa!” Naih alijisemea moyoni, akatoka kwenda kuoga.

************************

“Pole tulikuacha peke yako.” Kenny aliingia na kumrushia Nora neno. “Nilikuwa na baba. Ameingia ndani sasa hivi. Hakuna shida.” Nora alijibu kiungwana. Mama Kenny akawakaribisha wote mezani mara baada ya baba yake Kenny kutoka. “Yaani chakula alichopika Mama Nai, utakijua tu.” Kenny alianza kusifia. “Kweli kinanukia vizuri.” “Basi hata ladha yake utaipenda. Mama Nai ndio amenilea mimi tokea mtoto.” Kenny akaanza. “Ooh! Mnaishi naye hapa?” Nora aliuliza wakati anapakua. “Anaishi nyumba ya hapo nyuma. Ana watoto watatu, wakike. Mkubwa anaitwa Naih. Naih ndio Kenny.” Nora akakunja uso kidogo, na mama yake Kenny akaona. “Naih ndio Kenny!?” Nora akauliza kwa mshangao.

“Yaani Naih alizaliwa wakati Kenny anatamani sana mdogo wake. Sikubahatika kuzaa tena, kwa hiyo Naih wakati anazaliwa, Kenny alimuona kama mdogo wake. Wamekuwa pamoja.” Mama Kenny akajaribu kusawazisha. “Hapana bwana. Nai sio kama mdogo wangu. Nai ni ‘mimi wangu’. Nusu yangu mimi ni Naih. Yaani si unaniona mimi hivi? Upande wa kushoto ni Kenny, wa kulia ni Naih. Sijui umenielewa?” Wote walibaki wakimsikiliza vile Kenny anavyoongea kwa urahisi.

Walibaki wamemkodolea macho. Kenny akashangaa. “Come on guys! It’s so understandable. Nini kigumu hapo? Mbona inaeleweka kabisa! Yaani, Kenny/Naih. THERE! Ni rahisi hivyo.” Mama yake akajimiminia maji kwenye glasi bila ya kuongeza kwa mwanae na kumgeukia Nora. “Ungependa nikuwekee maji na wewe?” “Nitashukuru Mama.” Akammiminia kwenye glasi yake na kumsogezea Nora karibu.

Kenny alitoa simu yake mfukoni akaanza kutuma ujumbe. Alikuwa akila huku akituma ujumbe. Macho na akili zake, vyote vilikuwa kwenye simu. Baba yake alikuwa kimya, alishaonywa sana na mkewe. Aache tamaa au asijaribu hata kumuwaza Nora, ambaye amemkaribisha pale maalumu kwa ajili ya Kenny. Alimwambia mumewe Nora ndio atakuwa mke wa mtoto wao. Hataki aharibu chochote kwa tamaa zake za wanawake. Aliambiwa awe msikilizaji tu. Asiongee neno lolote. Basi na yeye hakutaka shida na mtu. Muda aliotakiwa kufika nyumbani ulipofika, na yeye akarudi nyumbani kama alivyoamrishwa na mkewe, akatulia kimya. Alipojiona amebaki yeye na yule binti tu pale sebuleni, akaamua kuingia chumbani, asizue matatizo.

Kwa hiyo na yeye alibaki pale mezani akitazama mambo yanavyokwenda. “Unaonekana unatumia muda mwingi sana na Naih!” Nora akaongeza kama kitu ambacho bado kilikuwa kichwani mwake. “Labda hujaelewa.” Kenny akatoa tabasamu lake lililokosha mioyo ya watu wengi waliobahatika kumfahamu. “Naih ni mimi wangu. Hakuna kitu kinaendelea maishani mwangu bila Naih kujua. Yeye ndio mimi na mimi ndio yeye. Ni mzuri wa kila kitu. Ananisikiliza. Nikiwa na matatizo yeyote yale, yeye ndio kimbilio langu.” Kenny akaendelea akisikika kuhamasika.

“Zamani alikuwa mama yake. Mama yake amenilea, na ndio nilikuwa naye muda mrefu kwenye maisha yangu. Hata nilipokuwa nikiumwa wakati wazazi wangu hawapo, Atu, ambaye ni mama yake Nai ndio alikuwa akiniuguza. Amenifundisha vitu vingi sana maishani, kwa kuwa muda mwingi nilikuwa naye tu.” Kenny aliongea kifasaha bila shida wala wasiwasi.

“Si unajua haya mambo ya kazi? Unakuwa labda upo kwenye vikao vya Bunge kwa muda mrefu, kutetea bajeti. Sasa Atu huyo msichana wangu wa kazi, ndio nilikuwa nikimlipa anilele Kenny. Sasa kama unavyojua kuna watu wengine sio waaminifu. Kwa kuwa alikuwa peke yake kwenye jumba lote hili akakosa uaminifu. Akawa na mahusiano na kila mlinzi aliyekuwa akilinda humu ndani. Hata huyo Nai mwenyewe alimzaa na Mmasai aliyekuwa mlinzi wetu. ” Mama Kenny alianza kuongea mambo mengi.

“Ukisema Mmasai unamaanisha jina?” Nora akauliza. “Mmasi jina na ni yule walubega kabisa. Alipomuona mama yake Nai hajatulia anahangaika na wanaume wengine, huyo Masai akamkimbia. Akaishia kuzalishwa watoto wengine wawili ambao hawajui hata baba zao! Sasa nilipoona anazidi kuzaa tu, na mimi nikamuona anamfaa Kenny, nikaamua kwenda kumfunga kizazi. Ujauzito wa mwisho ulimsumbua karibu afe. Alitaka kumtoa huyo mtoto, akanywa madawa yakutoa mimba, akakaribia kufa ikabidi kumkumbiza hospitalini ndio..” “Mama! Hizo ni habari nyingi sana kwa mtu ambaye wala hatumfahamu!” Kenny alishakasirika.

“Namweleza aelewe. Asije akafikiria vinginevyo kati yako wewe na Naih. Akajua ni kama watu fulani. Akafikiri, yaani akadhani, au kwa kifupi ajue ni watu tuliokuwa tukiwasaidia tu.” Kenny alishakuwa mwekundu.

“Inawezekana kwako walikuwa wafanyakazi tu, lakini kwangu Atu alikuwa mama. Naih anaweza kuwa kwako ni mtoto aliyezaliwa kwa umalaya, lakini kwangu ni kama nililetewa nusu yangu iliyokuwa imefichwa mahali. Wale watu wananipenda na kunisikiliza kuliko nyinyi wote wawili.” “Si kwa kuwa nawalipa!? Yote hayo wanayokufanyia yapo kwenye moja ya majukumu ninayowalipa!” Mama Kenny alijibu na yeye kwa hasira.

“Unafikiri kwa nini wapo hapa mpaka sasa? Tena yupo Atu na wanae wote! Umeshawahi kuona wapi eti mfanyakazi wa ndani analipwa mshahara na kupewa nyumba ya kuishi yeye na watoto wake? Kwa kuwa nimeona yeye ndio mfanyakazi anayeweza kufanya yale ninayomtuma afanye.” Kenny akasukuma sahani, akasimama. “Naenda kumuona Nai kabla hajalala.” Akatoka, nakuwaacha wote wamekaa palepale mezani. Atu na wanae wawili walikuwa wakisikiliza kila kitu wakiwa jikoni.

Alimkuta Naih alishapanda kitandani. Alivua viatu na yeye akapanda. “Nigeukie Nai.” “Nimechoka kulala upande huu, Kenny. Nimegeuka sasa hivi.” Kenny akaruka upande aliokuwa amegeuka Naih. Akashangaa kuona amenyamaza hamsumbui tena, wala hamuombi amtizame, kama kawaida yake. Naih akafungua macho taratibu macho yao yakagongana. “Nani amekuudhi?” Naih akamuuliza baada yakumwangalia tu. Kenny akabaki kimya.

“Hujampenda mchumba?” Kimya. Naih akabaki akimtizama na yeye. Walikaa pale kitandani kwa muda, akamuona anasinzia. Akavuta kwa nguvu shuka alilokuwa amelilalia, akamfunika nalo. “Asante.” Kenny akashukuru, akafunga macho na kulala. Naih akabaki akimtizama, akajua mambo hayakwenda kama alivyotarajia.

************************

Zilipita siku tatu za ajabu kwa Naih akabaki akijitizamia kama kawaida yake. Kenny akionekana hana furaha, na ni kama alikuwa akimkwepa mama yake. Alilala chumbani kwa Naih tu. Alirudi kutoka kazini akiwa na movies nyingi, akawa anaangalia chumbani kwa Naih mpaka analala, na kwa kuwa alishamuuliza hakutaka kujibu, Naih hakuuliza tena. Atu naye ni kama akawa amemkasirikia Mama Kenny. Kazi zake zote alizotakiwa akafanye nyumbani kwa kina Kenny, alimtuma Naih akafanye. Kwa hiyo tangia asubuhi anapoagana na Kenny akienda kazini, yeye anaingia kwenye jumba hilo kufanya kazi mpaka jioni,  akimaliza anarudi chumbani kwake na Kenny naye anakuwa ametoka kazini. Ataangalia movie zake wakati Naih analala.

Siku ya tatu wakati amerudi chumbani kwake baada ya siku ndefu ya kazi nyumbani kwa kina Kenny, aliamua kuoga na kujitupa kitandani. Kenny aliingia na chakula alichosema alipitia sehemu akanunua, akamwamsha, wakala, Naih akajirudisha kulala ukutani kabisa wakati Kenny anaangalia movie zake. Akiwa amejifunika, alimsikia Mama Kenny anaingia, akakaa kwenye kiti na kuanza kumuomba mtoto wake msamaha. Naih akajifanya amelala lakini alikuwa akiwasikiliza.

“Atu is like a mother to me.” Kenny akalalamika akisema Atu ni kama mama yake. “Huwezi kumzungumza vibaya wakati mimi nipo! Alikuwepo kwenye maisha yangu wakati wewe na baba mlishindwa. Hata kama ulikuwa mkimlipa, lakini Atu ananipenda. Kwani ni wangapi walipita hapa nyumbani kwetu, na mlikuwa mkiwalipa kama Atu, na wakashindwa kuwa na mimi? Atu loves me. Yeye ni binadamu, anamapungufu yake, lakini amefanya yale uliyoshindwa kufanya wewe. Lazima umuheshimu.” Kenny alisisitiza kwa mama yake.

“Sijawahi kushindwa kukulea, Kenny.” “Sasa ulikuwa wapi wakati nakua? Nilikuwa nikimuona Atu tu!” “Nilikuwa nahangaikia pesa ili uishi vizuri.” “Nashukuru kwa hilo na Atu naye alikuwa akihangaika kunilea mimi. Naumia nikisikia unamsema vibaya.”  “Siku ile nilijisahau Kenny. Naomba unisamehe.” Kenny akatulia kidogo. “Itakuaje kama siku ile alikusikia?” Kenny akamuuliza mama yake.  “Nina uhakika hajasikia kitu chochote.” “Kama alisikia nilazima umuombe msamaha.” “Sawa nitafanya hivyo. Kwa hiyo na wewe umenisamehe?” Kenny akacheka kidogo. “Yameisha, mama.” Walizungumza maneno mawili matatu, wakaanza kutaniana huku wakicheka.

“Ulimuonaje Nora?” Mama yake akauliza. “She is okay.” “Just okay?” “Yeah.” Kenny akajibu. “Yule binti ni mzuri sana, Kenny. Ameumbwa na umbile zuri sana.” “Kila mwanamke ni mzuri mama.” “Sawa Kenny. Lakini tunatofautiana. Yule amejaliwa umbile zuri, anaakili, ametulia, watu wengi wanampenda.” Kenny akanyamaza. “Kenny!” “Nafikiria mama!” “Unafikiria nini wakati yule ni binti mzuri?” “Unajuaje kama atanifaa mimi?” “Mpe nafasi muwe naye kwa muda, najua ukimfahamu utampenda tu.” “Sawa.” Kenny hakuwa mbishi kwa mama yake.

“Wametualika nyumbani kwao Mwanza.” Kenny akakunja uso. “Lini!?” “Jumamosi hii inayokuja.” “Siwezi kwenda, nampeleka Naih sehemu.” “Kwa nini usimpeleke Naih siku nyingine.” “Nimemuahidi tutatoka naye jumamosi, siwezi kubadilisha.” “Basi tupange ile jumamosi ijayo.” “Jumamosi ijayo ni birthday ya Nai.” Mama Kenny akatulia kidogo, wakati Kenny akiendelea kubonyeza remote.

“Basi twende Mwanza asubuhi halafu tutawahi kurudi.” “Lini sasa?” Kenny akamtizama mama yake. “Jumamosi ijayo.” Mama Kenny akajibu. “Si nimekwambia ni birthaday ya Nai!?” Kenny alishabadilika, akamgeukia mama yake na kumuuliza kwa ukali kidogo kama anayemshangaa. “Unafikiri lini twende?” Mama Kenny akajirudi kwa upole. “Sijui. Labda ijumaa.” “Ijumaa nina kazi ambayo siwezi kuacha, Kenny.” Kenny alibaki amemkodolea macho mama yake. “Ndio maana niliona tusafiri asubuhi, halafu tutawahi kurudi, uendelee na ratiba zako na Nai.”  “Nimekwambia nilishamuahidi Nai. Siwezi kubadilisha. Watasubiri mpaka utakapo pata nafasi.” “Basi tuondoke na ndege ya ijumaa jioni, na kurudi na ndege ya jumamosi asubuhi, ya juma lijalo. Unaweza kuondoka na ndege ya kwanza ya kutoka Mwanza kurudi huku, ukamkuta hata Nai hajaamka.” Kenny akanyamaza. “Kenny!” “Nitafikiria.” “Nataka unijibu ili niwataarifu kina Nora.” “Kina Nora!?” Kenny akashangaa kidogo. “Na wazazi wake.” “Sawa.” Kenny akakubali. Mama yake akatoka.

************************

Jumamosi hiyo ambayo Kenny alisema alimwahidi Naih watatoka, ilijaa hekaheka nusura Atu na wanae wafungwe jela. Naih aliamka na kwenda kutaarisha kifungua kinywa cha nyumbani kwa kina Kenny, ili ajiandae atoke na Kenny. Mama yake alimwambia kabla ya kutoka na Kenny, lazima amalize kazi zote. Wadogo zake Naih walikuwa wavivu na wabishi sana. Hawatumiki. Ilikuwa rahisi kumtuma Naih kwa kuwa hakuwa mbishi na kwa asili alikuwa mchapa kazi.  Wakati anamalizia kazi, Mama yake Kenny alitoka akiwa amekasirika kuwa ameibiwa mkufu wake wa pesa nyingi sana, na Naih pekee ndiye aliyekuwa ameingia hapo asubuhi hiyo.

Kenny aliposikia shutuma hizo, alitoka chumbani kwake kama mshale na kwenda kuuliza kulikoni. Naih alikuwa akilia tu. Mama yake akaingia na yeye akaelezewa kisa chote. “Lakini Mama Kenny, Nai amekuwa akikufanyia kazi siku zote, hajawahi kuiba hata mara moja! Inawezekana hujaangalia vizuri.” Atu alitetea akionekana kama anamaumivu makali. “Naomba turudi chumbani kwako tukaangalie tena mama.” Kenny akajaribu kutuliza. “Usilie Nai. Tutaupata tu.” Kenny alienda kutafuta huo mkufu na mama yake bila mafanikio.

Mlinzi alipigiwa simu na kuambiwa asiruhusu watoto wa Atu watoke hapo getini, na awaite wote pale ndani. Atu alibaki amekaa na binti zake pale sebuleni. Mkufu ulipokosekanika chumbani kwa Mama Kenny, wakahamia chumbani kwa Naih aliyekuwa akilala peke yake na Kenny wakati mwingine. Mlinzi alisaidia kupekua kila mahali bila mafanikio, ndipo wakaenda chumba alichokuwa akilala Atu na watoto wake hao wawili. Walianza kutafuta kwenye mabegi yao, na kukuta mkufu huo kwenye begi la mdogo wake anayemfuata Naih, ambaye ni Zai.

Waliitwa wote kwenye kile chumba na kuonyeshwa ulipokuwa umefichwa ule mkufu. Atu aliumia sana. Atu na Kenny walitumia zaidi ya lisaa wakimsihi yule mama asimpelekee Zai, polisi. Alisamehe kwa masharti kuwa binti huyo asiwahi kukanyaga tena ndani ya nyumba hiyo ya kina Kenny, na ikitokea uwizi mwingine wowote, Atu na wanae watafukuzwa kabisa pale. Mpaka wanakamilisha usuluhisho huo, hakuna aliyekuwa na hamu ya kutoka tena. Naih alirudi chumbani kwake akabaki amejiinamia, hata Kenny alipokuja, alimuomba amuache tu siku hiyo, hatatoka tena. Ilikuwa aibu ya mwaka.

************************

Maisha yaliendelea kama kawaida, lakini kulionekana wazi hakuna kuaminiana tena. Kulijengeka chuki kati ya Atu na mama yake Kenny. Aliwabadilikia na kuanza kugomba hata kwa mambo ambayo zamani hakujali. Aliongeza majukumu huku akimtishia Atu kama hataweza hizo kazi basi itabidi aondoke ampishe kile chumba mfanyakazi mwingine mwenye uwezo na kazi. Atu alishaanza kuwa mdhaifu. Umri ulikwenda na pia alikuwa akipata maumivu ya tumbo yasiyoisha. Alikuwa akiingia kwenye siku zake, anapoteza damu nyingi sana. Naih ndio alikuwa msaada, kwani Zai na Mia walikuwa hawashikiki. Kwanza hawakupenda shule, pili walipenda wanaume kuliko nafsi zao.

************************

 Ijumaa hiyo aliyotakiwa kwenda na wazazi wake jijini Mwanza, aliwahi kutoka kazini akarudi nyumbani kwa Naih. Alimwambia jioni ya siku hiyo wanasafiri kwenda Mwanza, lakini atampigia kabla ya kulala, na kesho yake asubuhi atakuwepo hapo, kusherehekea siku yake ya kuzaliwa. Naih alimtizama na kuendelea na shuguli zake. “Nitawahi kurudi Nai.” “Najua huwezi kunidanganya.” Naih alijibu kwa upole huku akiendelea na shuguli zake na Kenny akimfuata nyuma. “Sasa mbona huniangalii!?” “Nina kazi, Kenny. Mama yako anataka akirudi akute zile nguo zake pale zote ziwe zimepigwa pasi. Na mama amesema usiku hakulala, tumbo linamuuma. Inabidi mimi nizipige pasi, mara baada ya kusafisha hapa.” “Si wadogo zako wakusaidie?” “Wewe siunawajua huwa hawapendi kazi? Kwanza wote hawapo. Wametoka tokea asubuhi. Halafu bado mama yako hamtaki Zai humu ndani. Kwa hiyo nimebakia mimi tu.” Naih akaendelea na shuguli zake.

“Umekasirika?” “Kwa nini nikasirike, Kenny!?” “Sijui. Labda unaona nakukimbia.” Naih akanyamaza. “Nilijua tu. Basi sitakwenda.” “Hapana Kenny. Wewe nenda tu. Ukirudi tutaongea.” “Juu ya nini?” “Umeanza Kenny! Nimekwambia ukirudi tutaongea.” “Sasa kwa nini huniambii? Unajua kabisa mimi huwa sipendi ukiwa unaniambia hivyo. Unaniacha na wasiwasi.” “Wasiwasi wa nini sasa? Lazima ujifunze kuwa na subira Kenny. Ukirudi tutapata muda wakuzungumza.” Naih alitoka pale jikoni akahamia chumba cha kufulia. Kilikuwa na mashine ya kufulia na kukaushia. Akafungua meza ya kupigia pasi.

Kenny akaingia. “Lakini sisi tupo sawa?” “Tupo sawa Kenny. Mbona unawasiwasi?” “Naona kama huna raha!” “Labda nikuchoka, halafu..” “Nini?” Alimuona Naih anatokwa na machozi. Kenny akamsogelea, akazima pasi akamvuta karibu. “Kuna nini Nai? Niambie.” “Matokeo ya kidato cha sita yametoka.” Tayari Kenny alishajua. “Pole Nai.” “Nimabaya sana. Mama amekasirika. Amesema hawezi kunisomesha tena.” “Usiwe na wasiwasi. Kesho nikirudi tutazungumza vizuri. Utosoma tu. Nitakusaidia.” “Unamaanisha nini?” “Tutatafuta chuo, nitakulipia.” “Mmh! Mimi nahisi mama yupo sahihi. Ni heri kutafuta mwanaume niolewe tu. Sina akili kama baba.” “Wewe Naih! Maneno hayo unayotoa wapi? Baba yako mwenyewe hata humfahamu!”  Kenny alishituka sana.

“Si mama ameniambia leo. Baba yangu hakuwa na akili, na mimi nimerithi kwake. Unakumbuka hata mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne pia nilifeli? Mama yako akanipeleka shule ya kulipia, akawa anamkata mama mshahara? Hiyo kitu inamuuma mama mpaka leo.” “Ngoja kwanza Nai. Kwani mama alikuwa akimkata mshahara mama yako sababu ya kukusomesha wewe?” “Ulifikiri ilikuwa bure? Mama alikuwa akikatwa kwenye mshahara wake, sasa matokeo haya ndiyo yanamuumiza mama zaidi. Anasema ni kama amechoma pesa yake bure. Sina msaada wowote maishani mwake, nammalizia pesa bure. Heri niolewe tu.”

 “Sikuwa nafahamu hilo. Usijali. Mimi nitakusomesha na sitakudai. Ila usitafute mwanaume sasa hivi.” “Nikipata mwanaume anayenipenda je?” “Subiri Nai! Unaharaka gani?” “Nimekuuliza tu!” “Wewe subiri utaenda shule. Acha mambo yakufikiria wanaume. Kesho asubuhi nikirudi tutazungumza zaidi. Lakini uniahidi hamna kukubali mwanaume yeyote.” Naih akacheka huku akijifuta machozi.

“Akija mzuri leo, naondoka naye, kesho hutanikuta hapa.” Kenny alishaanza kubadilika rangi. “Nakutania bwana Kenny. Nini?” “Nimemuona Tino jana. Wakati naingia na yeye anatoka.” Naih akaanza kucheka. “Usicheke Nai.” “Kwa hiyo unafikiri Tino ndio atanioa? Nilikwambia nilikuwa nasoma naye tu.” “Sasa jana alifuata nini hapa?” “Alimfuata Mia. Walianza mahusiano na Mia.” “Kwa hiyo sio wewe?” “Akuu! Wa nini mimi huyo Tino?” “Sijui. Ila naomba uache kuwaza mambo ya wanaume.” “Kila mwanaume ukiniona naye unakasirika, Kenny! Unaona ni afadhali Mia awe na mwanaume lakini sio mimi, wakati Mia ni mdogo wangu, tena wa mwisho!” “Bwana Nai!” “Si nimeshakuahidi sitafanya hivyo. Sasa kwa nini unawasiwasi?” Kenny akanyamaza.

Naih alianza kupiga pasi wakati Kenny amekaa juu ya mashine ya kukaushia nguo akicheza kwenye simu yake. Alijibu jumbe mbali mbali wakati Naih akiendelea na kazi. Mama yake akaingia. “Hiyo kazi ya pasi nilimpa mama yako. Huwa simuamini mtu mwingine na hizo nguo ila yeye tu.” “Mama anaumwa.” Naih akatetea. “Sasa kwa nini hajaniambia nikapeleka kwa ‘dry cleaner’ wangu? Kama anaona kazi zinamshinda aniambie nitafute msichana mwingine. Naona siku hizi kazi zake zote unafanya wewe!” “Kwa nini unalalamika mama!? Ungeangalia kwanza hizo nguo. Kama Nai hajafanya vizuri, ndio ungelalamika.” Kenny akaingilia.

 “Ninapotoa majukumu nataka yafuatwe vile ninavyotaka mimi na si vinginevyo.” “Kwani umekuta kazi hazijafanywa? Naona kila kitu kinafanywa kama unavyotaka. Sasa tatizo ni nani anafanya hizo kazi au unakuta kazi hazijafanywa?” Ukitaka kumsikia Kenny anaongea, ni pale unapomkorofisha Naih. Hapo ndipo utajua kwamba lile tabasamu lake huwa linageuka. Naih alikuwa ndio anamalizia nguo ya mwisho. Akazima pasi na kutoka pale kurudisha nguo zote chumbani kwa Mama yake Kenny. 

“Siku hizi sina raha na nyumba yangu! Unaishi na watu wezi. Unawalisha na kuwavalisha lakini bado wanakuibia! Hawana shukurani. Yaani kazi ya kuninyooshea nguo zangu pia imemshinda! Kuna faida gani sasa ya yeye kuwepo hapa?” Naih alimsikia mama Kenny akilalamika. “Mama Please! Naomba upunguze sauti. Utamuumiza Naih. Anajitahidi sana kukufanyia kile unachotaka. Naomba umuonyeshe unatambua juhudi zake.” “Yeye sio mfanyakazi wangu.” “Lakini amekwambia mama yake ni mgonjwa! Sasa ulitaka wafanyaje? Kwanza nimepanga jumatatu nimpeleke hospitalini wakajue ni nini kinamsumbua. Ameteseka kwa muda mrefu sasa hapati nafuu. Atu ni mama yangu.” “Na mimi ni nani?” “Ni mama yangu, lakini Atu ni zaidi. Atu amenilea mama. Usije kusahau hilo.” Kile kitu kilimuuma sana Mama Kenny. Aliona Kenny anamthamini mfanyakazi kuliko yeye! Naih aliweka nguo zote kitandani na kutoka kimya kimya.

Kenny akaenda chumbani kwake kufungasha vitu atakavyohitaji kwa safari hiyo ya siku moja. Alifungasha begi dogo tu, akatoka kumfuata Naih chumbani kwake. Akamkuta akilia. “Nitafanya nini Kenny? Natamani ningekuwa na uwezo nikaondoka kwenda kufanya kazi mahali pengine, nikamsaidia mama yangu. Sasa hivi mama yako anatuona ni mzigo! Ametoka sasa hivi kugombana na mama hapo. Mama anamwambia ni mgonjwa, hawezi hata kusimama, lakini yeye anamlazimisha atoke kitandani. Mama ni mgonjwa Kenny, na sina hata pesa ya kumpeleka hospitalini.”

“Usilie Nai. Chukua hizi hela.” “Sitaki.” “Kwa nini tena!? Kesho nikirudi tutampeleka hospitalini. Nisubiri, nikirudi kila kitu kitakuwa sawa.” “Unanidanganya wakati sasa hivi unahangaikia mambo yako ya kuoa.” “Naih!” “Kwani uongo?” “Unakumbuka kiapo tulichowekeana mimi na wewe? Hakuna kitakachobadilika kati yetu milele. Hakuna mtu atakayekuja katikati yetu. Nai/Kenny kwanza halafu wengine. Na ningekuwa sijamuahidi mama kwenda nao, ningebaki na wewe. Wewe unajua ninavyokupenda.” Naih hakujibu.

“Nai! Naomba tuagane vizuri. Siwezi kuondoka kama hutaki hata kuniangalia.” “Si umenikuta nalia, sasa nitakuangaliaje?” “Basi nyamaza tuagane na upokee hizi hela.” Naih akakausha machozi. “Mshahara wangu wote wa mwezi huu hapa, mama amenilipa leo asubuhi. Nilimuomba asiniwekee kwenye akaunti amwambie muhasibu anikabidhi.” “Ndio unanipa wote! Na wewe ukiishiwa?” “Nitakuomba wewe. Usiwe na wasiwasi. Kaa nazo tu. Ukiwa na matumizi yeyote, tumia. Umenisikia? Nikirudi kesho tutaongea vizuri. Nakupenda Nai.” “Na mimi nakupenda Kenny.” “Basi usilie. Kesho asubuhi nitakuwa hapa.” Akamsaidia kufuta machozi, akambusu shavuni na kutoka.  

Mwanza.

W

alitua jijini Mwanza, na kupokelewa na Nora. Kenny alitoa tabasamu lakini wazi alionekana akili zake hazikuwa pale. Nora aliwachukua mpaka nyumbani kwao, wakakuta wazazi wao wakiwasubiria nje. Ni kweli walionekana ni familia inayojielewa. “Samahani. Unaweza kunichomekea simu yangu kwenye umeme?” Kenny alimnong’oneza Nora wakati wazazi wake wakisalimiana na wenyeji wao. Nora aliipokea na kuingia ndani. Walimfuata nyuma huku vicheko vikiendelea kati ya wazazi hao.

Kama alivyokuwa ameonywa, Mzee Ole alikuwa kimya, na kutoa tabasamu kila alipoona panatakiwa kucheka, na kujibu pale alipoulizwa jambo. Wote wawili yeye na mtoto wake Kenny, walishaambiwa wasimuharibie Mama Kenny. Wakapewa onyo zito, ndipo wakaondoka jijini Dar kuelekea Mwanza. Kwa hiyo Mama Ole yeye ndiye alikuwa huru kuongea na wenyeji wake. “Tamaa zako hizo kama za fisi, huko nisikuone!” Hilo ndilo onyo la mwisho alilopewa na mkewe. Mzee Ole alicheka tu, akanyamaza. Naye Kenny aliambiwa achunge sana mdomo wake. Kwa kuwa Mzee Ole alikuwa mnywaji wa pombe kali, alishakatazwa na mkewe asithubutu kunywa kileo chochote huko ugenini. Kwa hiyo walipokaribishwa vinywaji vikali, yeye na mwanae waliomba maji ya kunywa.

Walizungumza kidogo, wakaelekezwa mezani kwa chakula. “Sijui itakuwa imeingia chaji kidogo?” Kenny akamuuliza Nora wakati wanasimama kuelekea mezani. “Ndio nimeiweka sasa hivi Kenny! Ipe muda kidogo.” “Sawa. Lakini sihitaji ijae.” Nora alinyamaza wakaelekea mezani. Kwa muonekano, Kenny alikuwa kijana anayeuzika bila kelele yeyote au bila kutoa jasho. Tayari wazazi wa Nora walishampenda. “Karibu sana Kenny. Ujisikie nyumbani.” Mama yake Nora akajaribu kutupia neno kama ishara ya kumkubali Kenny. “Asanteni sana.” Kenny akajibu wakati na yeye anaendelea kupakuwa.

“Hata kama imeingia baa hata moja, naiomba tu. Kuna simu yamuhimu sana, nataka kupiga, kisha tutairudisha kwenye umeme.” Alimgeukia tena Nora. Nora alimtizama kidogo, kisha akanyanyuka. “Wapi tena?”  Baba yake Nora akamuuliza. “Naenda kumletea Kenny simu yake. Nilimuwekea kwenye umeme.” Wote wakamgeukia Kenny. “What!? I just want to call Nai!” Ilibidi ajitetee kwa mama yake aliyekuwa amemtizama kwa jicho kali kuwa anachotaka ni kumpigia tu Naih, asijue anaharibu zaidi.

“What did I do this time!?” Kenny akauliza tena kwa kushangaa maana bado mama yake alikuwa akimtizama. “Its my phone, ma!” Kenny aliendelea kujitetea kwa mshangao kwa mama yake. Nora akarudi, akamkabidhi. “Nitarudi sasa hivi. Kuna simu ya muhimu lazima nipige kabla sijatulia.” Kenny akasimama, baada ya kama dakika kumi akarudi. “Samahanini. Nilikuwa namjulisha Nai, kuwa nimefika salama. Anawasalimia.” Ukimya mfupi ukapita.

“Kwani Naa, ni nani?” Mama yake Nora ikabidi kuuliza. “Sio Naa, ni Naih. Yenye ‘h’ mwisho. Ila wakati mwingine tunamkatisha tunamwita Nai. Ni jina la Kimasai. Alipewa na baba yake, maana yake ni kubembeleza. Na kweli Naih anapenda kubembele..” “Ni mtoto wa mfanyakazi wangu wa kazi za nyumbani.” Mama Kenny, akamkatiza mwanae. “Anaitwa Atu.” Kenny akadaikia na kuendelea. “Atu ni mama yake Naih. Alinilea mimi tokea nazaliwa. Ni kama mama yangu. Nai ni ‘mimi wangu’. Yaani unaponiona mimi ni kama umemuona Naih. Nimekuwa naye tokea amezaliwa. Ni binti wa kimasai. She is so beautiful.” Kenny alitoa tabasamu akionyesha kufurahia kutoa sifa za Naih.

 “Mimi wako! Yaani ni mkeo? Nilijua hujaoa, na wala huna mchumba!” Mama yake Nora aliuliza kwa mshangao kidogo. “No! hapana.” Kenny akakanusha. “Hujanisikia vizuri. Nimesema ni ‘mimi wangu’, sio mke wangu. Hapana. Nai si mke wangu.”  Kenny akamalizia na tabasamu lisilo hila. “Ndio nini?” “Ni nusu yangu.” Akaendelea akiongea kama jambo la kawaida tu. “Chochote unachokiona kinakosekana kwangu, ujue anacho Nai. She is total completely opposite of me. Nikiwa na Nai, ndio nakuwa nimekamilika. Ananifanya nakuwa na furaha. Ananisikiliza na ananipenda sana, kama mimi ninavyompenda. Sijawahi ona mtu mtulivu kama Nai. Mpole sana. Marafiki zangu wote wanampenda Nai.” Meza nzima ilikuwa kimya ikisikiliza sifa za Naih. Kenny hakuwa hata akila, alikuwa akiongea tu. Baba yake alibaki msikilizaji huku akila taratibu, bila kuongeza neno.

“Sasa huyo si kama mkeo?” Mama yake Nora aliongeza. “Oh noooo!!” Kenny alikataa kwa mshangao. “Nai sio mke wangu. Nitaoa, na yeye ataolewa. Lakini sitaki mwanaume yeyote amsogelee. Sijaona bado mwanaume anayemstahili Nai. Nataka atulie, asome, ajijenge. Tukipata mwanaume tutakaye ona anamfaa, ndio atamuoa Nai. Lakini sasa hivi sitaki mtu yeyote amsogelee. Sitaki mtu yeyote amguse.” Alitulia kidogotu, akaendelea. “Kesho ni birthday yake. Ndio nataka tuweke msingi wa kudumu. Nataka asomee kitu anachopenda, sio mtu amlazimishe kusomea kitu asichopenda. Tatizo la Naih anafaa katika kila kitengo.” Kenny alicheka kama anayefikiria.

“Sijui atasomea mambo gani!? Anafaa kuwa nesi, kwakuwa anaupendo sana. Anaweza kuwa mwalimu, kwa kuwa ana uvumilivu, anauwezo wakufundisha mtu akamuelewa. Anaweza kuwa mpishi kwenye mahoteli au hata akajiajiri akawa anapika kwenye masherehe, kwa kuwa ni mpishi mzuri sana. Hata Nora alisifia chakula chake. Unakumbuka chakula ulichokula siku ulipokuja nyumbani, tukadhani ni mama yake amepika? Basi ni Nai ndiye aliyekuwa amepika. Alikuja kuniambia baadaye ulipoondoka. Haya, anaweza kuwa mtu wa masoko, kwa kuwa anauwezo mkubwa sana waku..” “Jamani, kuna anayetaka kuongezewa kinywaji?” Mama yake Nora akamkatisha Kenny. Kenny alikunja uso kidogo kama ambaye hajamuelewa, bila kupata jibu huko mawazoni mwake, akainamia simu yake na kuanza kutuma ujumbe.

Mama Ole alitamani aridhi ipasuke, yeye na mwanae huyo wapotelee huko. Wazi wenyeji wao walionekana kukereka. Lakini sio Kenny. Baada ya muda kidogo, aliomba tena atoke, na kuahidi kurudi baada ya muda mfupi sana. Bila kusubiri jibu la mtu, akatoka pale mezani. Hakuwa ameweka kijiko hata kimoja mdomoni. Hakurudi tena, mpaka aliposikia wazazi wake wanaaga ndani. “Simpati Nai tena. Sijui amepatwa na tatizo gani! Nai sio mtu wakuacha kupokea simu zangu.” Kenny aliwawahi wazazi wake wakati wanasindikizwa. Kutoka ndani kuelekea kwenye gari ili warudishwe hotelini. Walimkuta hapo nje anahangaika kupiga simu ya Naih bila mafanikio.

“Unafikiri amepatwa na tatizo lolote? Eti dad?” Tayari Kenny alishaonyesha uso wa kuchanganyikiwa. “Sijui Kenny. Labda amelala.” “Namfahamu Nai. Hawezi kulala bila yakuagana. Haijawahi kutokea, na ninajua haiwezi kutokea. Labda amepatwa na tatizo.” Alipiga tena simu ya Naih, ikawa inaita tu, bila majibu.

Akapata wazo la haraka. “Wapigie simu, walinzi wa nyumbani pale getini.” Kenny akamgeukia mama yake. “Nitawapigia tutakapofika hotelini.” “Hapana. Siwezi kusubiri tena, nimeshaingiwa na wasiwasi. Wapigie sasa hivi.” Mtoto huyo ambaye hakujua kukatalia jambo tokea mtoto, alionyesha msimamo wake wa waziwazi palepale mbele ya wenyeji wao. Zaidi anapokuwa Naih, hapo ndipo utamjua Kenny ni Masai damu.

Mzee Olendekai alijua hiyo simu isipopigwa pale, ndio itakuwa mbaya zaidi. Akatoa simu yake akawapigia walinzi wa nyumbani kwake Dar. Mlinzi aliyekuwa kwenye kibanda cha walinzi getini kwa wakati huo aliwaambia Naih aliomba wakaletewe taksii, ili amkimbize mama yake hospitalini. Hawajarudi mpaka wakati huo, na hajui kinachoendelea wakati huo. Kenny alibaki kimya kwa muda, wenyeji wao wakabaki wakimtizama.

Akamsogelea Nora, akamkumbatia. “Samahani sana. Najua leo hatukupata wakati mzuri. Nakuahidi nitarudi wakati mwingine tutazungumza zaidi. Nashukuru kwa moyo wa ukarimu, nakuahidi nitarudi.” Nora aliyekuwa amepooza mpaka usoni, kidogo akafarijika. “Tutapata muda mzuri, tutazungumza. Sawa?” Kenny akaongeza akisikika kama anayebembeleza, Nora akakubali na tabasamu usoni. “Asanteni sana kwa kutukaribisha.” Kenny akawashika mkono wazazi wa Nora, akaondoka kuelekea kwenye gari. Angalau alionyesha uungwana wakati wakuondoka, nakumfanya mama yake kutoa tabasamu. Waliagana, wakaondoka. Walifika hotelini hakuna aliyekuwa akimsemesha mwenzake. Kenny aliingia chumbani kwake, huku akiendelea kujaribu simu ya Naih.

Mpaka panapapazuka ndipo Naih alipokea simu ya Kenny. “Niliiacha simu nyumbani, Kenny. Pole.” “Mama anaendeleaje?” “Yaani asubuhi hii ndio amepatiwa kitanda, na mimi ndio nimerudi nyumbani. Nilikuwa peke yangu, Kenny.” Naih akaanza kulia. “Wadogo zako wako wapi?” “Mpaka mida ile ya saa mbili nampeleka mama hospitalini, hawakuwa wamerudi nyumbani. Na nimerudi hapa pia sijawakuta.” “Usilie. Naingia kuoga, nawahi kuja huko. Usisahau simu tena, ili tuwasiliane.” “Sawa.” “Usilie sasa.” “Mama mgonjwa sana, Kenny.” “Atapona. Usiogope. Umesikia?” “Umesema unakuja saa ngapi?” “Muda sio mrefu.” “Ndio saa ngapi?” “Nitahakikisha naondoka na  ndege ya kwanza inayoondoka huku Mwanza. Wewe lala, nitakupigia nikitua tu Dar.” “Siwezi kulala. Inabidi nirudi tena hospitalini kumpelekea mama uji. Kwa hiyo ujue nakusubiria hospitalini. Usichelewe Kenny.” “Sawa na wewe unyamaze sasa. Usilie. Unanisikia?” “Bwana Kenny!” Kidogo Naih akalalamika kwa kugomba. “Basi nakuja.” Kenny alikata simu, akaingia bafuni kuoga kwa haraka, akaondoka kuwahi uwanja wa ndege bila hata kuaga wazazi wake. Swala la Naih kuwa kwenye matatizo, ndio tatizo pekee la Kenny.  


  Sehemu ya 2.

UKIPENDA BOGA, PENDA NA UA LAKE.

K

enny aliwaachia wazazi wake ujumbe mapokezi, kuwa alishaondoka kurudi Dar. Alitua uwanja wa ndege wa jijini Dar, akaelekea hospitalini moja kwa moja alipokuwepo Naih. Alimkuta amekaa nje baada ya muda wa kuona wagonjwa kuisha. “Daktari amesemaje?” “Wanapita saa nne. Ndio tutajua.” Naih akajibu kinyonge. “Umekula?” Naih akatingisha kichwa kukataa. “Twende tukale.” Walienda kukaa mahali wakala, Naih akabaki ameinama anasinzia. Kenny akajivuta karibu yake ili amuegee, akapitiwa na usingizi huku Kenny akiwa amemshikilia. Ilipofika mchana wakarudi wodini, wakaambiwa anauvumbe mkubwa tumboni, atafanyiwa vipimo, ili wafanye upasuaji utolewe.

Kenny alihangaika na Naih kwa majuma matatu mfululizo bila kuchoka. Kila siku asubuhi Kenny alikuwa akimshusha Naih hospitalini wakiwa na chupa za uji na vyakula alivyokuwa anapika Naih, ili mchana asiwe anarudi nyumbani. Kisha Kenny anaenda kazini, na kurudi tena jioni pale hospitalini kumchukua Naih kurudi naye nyumbani. Siku ambazo hakuwa na kazi nyingi kazini, alikwenda mchana hospitalini. Alimchukua Naih na kwenda kupata naye chakula cha mchana. Atamrudisha hospitalini na yeye atarudi kazini mpaka jioni akiwa anaenda kumfuata Naih ili warudi wote nyumbani.

Alikuwa naye mpaka Atu aliporuhusiwa kutoka akiwa amefanyiwa upasuaji mkubwa sana. Alitolewa ule uvimbe kwenye nyumba ya uzazi na kizazi pia. Uvimbe huo mkubwa uliokuwa umeota kwenye kizazi ndio uliokuwa ukisababisha kutokwa damu nyingi kila kipindi cha hedhi na maumivu makali. Akili na mawazo ya Naih yalikuwa kwa mama yake tu, wakasahu kuwa wanaishi pale kwa kina Kenny kama wafanyakazi. Walirudi nyumbani wakakuta Mama Ole alishaleta wasichana wengine wawili wa kazi. Atu aliruhusiwa hospitalini akiwa bado mdhaifu, alihitaji muda mwingi wakupumzika. Naih alimwambia mama yake Kenny anaweza kusaidia, lakini akamjibu kwa wakati ule haitaji tena msaada wao.

Kitendo cha Kenny kumthamini Atu kuliko yeye na kumtaja Naih kila mahali, ilikuwa ni kama kumdhalilisha yeye. Mama Ole alikusudia kuwatoa kabisa Atu na wanae kwenye maisha yao. Alisema kuwepo kwa Atu na wanae pale, nikumfanya Kenny ashindwe kuendelea na maisha yake. Anajiona ni kama anajukumu la kutimiza kwao. Wakati Mama Ole alikuwa akimsisitizia mara kwa mara kuwa wale walikuwa ni wafanyakazi tu, na yote waliyokuwa wakimfanyia yeye ni kwa kuwa alikuwa akiwalipa, Lakini yey Kenny hakuwa akimuelewa mama yake. Kitendo cha kumuacha yeye na baba yake hotelini jijini Mwanza na kuwahi kurudi Dar kuwa na Naih, kumuuguza Atu, yule mama aliapa kutosamehe.

************************

Kenny aliendelea kumtuliza Naih. “Siwezi nikaruhusu akawafukuza. Hata kama hataki mfanye kazi, wewe hakikisha mama anapata nafuu, halafu tutajua chakufanya baada ya hapo.” Kenny alimfariji Naih. Hapakuwa na chakula cha bure tena kutoka kwenye jumba hilo la kina Kenny, kwani hawakuruhusiwa kuingia mle ndani tena. Naih alikuwa akipewa pesa za matumizi na Kenny. Pesa hizohizo alizotegemea kwa chakula cha kula yeye na ndugu zake, wakati mwingine wadogo zake walikuwa wakimuibia. Waliingia chumbani kwa Naih kwa kujiiba wakati akimuhudumia mama yao chumbani kwao, wanaiba na kutoroka kwenda kwenye starehe zao. Naih na mama yake wanabakia hawana pesa mpaka Kenny awape tena.

Alipogundua kuwa Kenny anawapa pesa, Mama Ole alikasirika zaidi lakini kwa hila, akampongeza. Hakutaka kuonyesha hasira yake kwa Kenny. Akajidai yupo upande wake. Wakashangaa mama Ole ametulia. Kuna amani. Kidogo na Kenny naye akatulia. Urafiki na mama yake ukarudi.

Alipoona akili yake imetulia kabisa, ndipo akamkumbushia ahadi aliyoiweka kwa Nora, nakumtaka aende. “Naona Atu anaendelea vizuri sasa. Nafikiri na wewe ndio muda muafaka wa kwenda kumuona Nora. Tulimuacha kwenye mazingira ambayo hayakuwa mazuri.” “Ni kweli mama. Nitampigia simu, tupange twende naye mahali.” Mama Ole akafurahi sana.

Kenny arudisha Majeshi Kwa Nora.

Kenny alimpigia simu Nora, lakini Nora alimwambia weekend hiyo anatarajia kwenda Afrika kusini kikazi. “Naweza kukusindikiza?” “Nitafurahi Kenny.” Wakapanga mipango yao vizuri, kuwa Nora atafika hapo jijini siku ya ijumaa usiku, atalala hotelini, kisha siku ya jumamosi walipanga kuondoka pamoja kuelekea nchini Afrika ya kusini.

Siku ya ijumaa Kenny akiwa na Naih. “Ukiwa na shida yeyote unijulishe, Nai. Na ninakuomba upokee simu.” “Si ulisema mnasafiri kesho?!” “Lakini atafika leo usiku. Nitakwenda kumpokea, na kuwa naye hotelini mpaka kesho tutakapo safari wote. Sikumuacha vizuri tulipokuwa Mwanza. Sipendi afikiri mimi ni mtu mkatili sana. Alituandalia vizuri, lakini mambo yaliharibika pale nilipokukosa kwenye simu. Unakumbuka nilikusimulia?” Naih akanyamaza. “Naih?” “Nimekusikia Kenny!” “Kwa hiyo utapokea simu?” “Nitapokea.” “Hatutakaa sana. Jumatano tutarudi.” “Sawa.” Naih akajibu akakubali lakini akiwa kama mwenye mawazo, akili hazipo hapo. “Nakupenda Naih.” Kenny akaongeza, Naih akamtizama. “Nitakuletea zawadi.” “Nitashukuru.” Kenny akambusu shavuni akaondoka akiwahi foleni, ili kuwahi uwanja wa ndege kumpokea Nora, akamuacha mama yake akiwa na furaha zote.

************************

Alimfikisha Nora hotelini, lakini Nora mwenyewe alionekana hawezi kusubiri, anamtaka Kenny kimapenzi. Kama kawaida yake Kenny, hakumchelewesha. Usiku huo alimpa mapenzi yaliyomfanya Nora atamani Kenny atangaze ndoa haraka. Mtoto huyo chotara, aliyajua mapenzi ipasavyo. Alichezea mwili wa Nora usiku huo, nakumuacha Nora hoi kitandani, akaenda kupiga simu nje kuzungumza na Naih. Waliongea kidogo, Naih akamwambia amechoka anawahi kulala. “Nitakupigia simu asubuhi kabla hatujaondoka.” “Sawa. Uwe na usiku mwema, Kenny.” “Na wewe, Nai. Nakupenda sanaaa.” Alimsikia Naih akicheka taratibu, kisha akakata simu.

Asubuhi kabla ya kuondoka, akampigia Naih simu kumuaga. Kisha akampigia simu mama yake na kumwambia vile alivyokuwa na wakati mzuri na Nora. “Naamini tutapata muda mzuri zaidi huko tuendako. Ni kweli anaonekana ni binti mzuri.” Zilikuwa ni habari zilizomfurahisha sana mama yake. Kwani alizingojea kwa muda mrefu, ila Atu na mtoto wake Naih, ndio walikuwa wakimchelewesha Kenny. Alipohakikisha mtoto wake ametua nchini Africa ya kusini, akamfuata Atu na watoto wake, akawaambia anamazungumzo nao.

Kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho.

M

ama Ole akataka kwanza Naih amkabidhi simu yake. Naih akiwa na uso wa wasiwasi, akatoa simu akamkabidhi mama Ole. “Sasa chukua hii simu ya nyumbani, mpigie simu Kenny, mwambie unatatizo la simu, hamtaweza kuwasiliana naye mpaka atakaporudi. Mtakie mapumziko mema na mpenzi wake, kisha ukate simu.” Naih akakunja uso. “Siwezi kumdanganya Kenny!”  “Hivi unajua kama Kenny anataka kuoa?” Naih akanyamaza. “Sitaki wewe uwe sababu ya Kenny kushindwa kufurahia mapenzi ya Nora, msichana aliyetulia, mzuri wa sura na mwenye akili ya maisha. Umenielewa Nai?” Mama Ole akambadilikia.

“Nataka leo hiihii muondoke. Na msiwahi kurudi tena hapa. Na wala Naih usiwahi kumtafuta tena Kenny. Umekuwa mzigo ambao hajui atakutua lini na vipi! Kenny ni mtoto wangu wa pekee, uwepo wenu kwenye maisha yake ni tatizo. Anafikiri anajukumu kubwa la kuwasaidia. Kuweni na utu jamani! Kenny amewasaidia vyakutosha, acheni na yeye apumzike.” Naih akaanza kulia.

 “Sasa Atu kuna msaada wa mwisho naweza kukusaidia kabla ya kuondoka, ila itategemeana na wewe. Nina hundi ya pesa hii hapa.” Mama Kenny akawaonyesha hundi ya pesa nzuri tu. “Hii pesa yote nitawapa kama Atu ukiniahidi si wewe wala watoto wako, hasa Naih watakao msumbua tena Kenny maishani. Itakusaidia kuanza maisha na biashara yeyote unayotaka. Kama Naih atakataa kumpigia simu Kenny sasa hivi, ujue utaondoka na wanao, mikono mitupu.” Atu na wale watoto wake wawili mate yaliwatoka, kama fisi aliyeona nyama. Mamilioni ya pesa!

“Nipe hiyo pesa nikaanze maisha na wanangu. Naondoka sasa hivi.” Atu akajibu kwa haraka bila hata kufikiria mara mbili na kumshangaza sana Naih. “Kweli mama unamkana Kenny leo, sababu ya pesa ya huyu mama! Kumbuka Kenny anavyotuhitaji, mama. Kubali tuondoke, lakini tusiuwe undugu na Kenny.” Naih alikuwa akilia sana. “Mama tunaomba usije ukamsikiliza Nai. Unafikiri huyo Kenny akija kuoa atakukumbuka tena? Ona anavyokufungia wewe humu ndani wakati yeye analala na kila mwanamke huko nje!” Mdogo wake Naih akaingilia. “Mimi mwenyewe kashalala na mimi.” Mia akaongeza kwa kujigamba. “Hata mimi nishalala naye huyo Kenny.” Zai naye akadakia, wakacheka. Naih akazidi kuumia.

“Unamlilia nini huyo Kenny!? Kwanza hana hata mpango na wewe. Akioa anaenda kuishi na mkewe! Utajiliza hapa mpaka lini!? Kwanza hapa sio kwetu. Ulifikiri tutaishi hapa daima? Mama wewe chukua pesa, tuondoke hata usiku huu.” “Hapana jamani. Hamuwezi kuondoka bila Naih kuzungumza na Kenny na kumwambia nilichomtuma. Kenny asipompata Naih kwenye simu, kesho asubuhi atakuwa hapa.” Mama Ole aliwakatisha. “Usiwe na wasiwasi Mama Kenny. Mwanao anajua namba yangu. Namtumia ujumbe sasa hivi, nikijidai mimi ni Nai, nipe tu maneno yote unayotaka nimwambie. Na wala sitakuja kumwambia ukweli. Hata akija kunipigia tena simu, sitapokea. Wewe niongezee pesa. Ukinipa pesa yangu, mbona mimi nitarekebisha! Sasa hivi tunaondoka, na wala hatutarudi tena hapa.” Ni kweli Atu alimuhurumia sana Naih, lakini alishindwa jinsi yakumsaidia. Akaona akubaliane na watoto wake hao wadogo. “Usiwe na wasiwasi mama Kenny.” Atu alisisitiza.  Naih alinyanyuka, akaingia chumbani kwake kwenda kufungasha.

************************

Maisha yao yalishabadilika. Walishatafutwa wasichana wengine wakazi na yule mama alionyesha wazi hawataki tena pale. Kenny ndio huyo anaoa. Hawezi kuendelea kumtunza Naih akishaanza majukumu yake kama mume. Atu akajua kitakachofuata nilazima watafukuzwa pale walipokuwa wakiishi na wanae, tena mikono mitupu! Akaona ni bora aondoke mapema na hiyo pesa ya hongo ili akaanze vizuri kuliko kutoka hapo mikono mitupu, na watoto watatu watakao kuwa wakimwangalia yeye!

************************

Baada ya kukamilisha taratibu zote alizotaka Mama Ole, akawasaidia usafiri. Dereva wa pale nyumbani kwake aliwachukua na mabegi yao, wakaondoka. Naih alikuwa akilia njia nzima huku wadogo zake wakimcheka sana. “Kweli huyu tahira. Ndio maana kweli alifeli. Heri mimi nilijiachia shule mapemaa! Sasa unacholia nini!?” Mia akamuuliza, Zai akajibu yeye kwa kejeli. “Anamlilia Kenny!” Wote wakacheka. “Basi atalia sana. Maana sasa hivi Kenny anamfaidi mtoto wa Mwanzaa!” “Na si unamjua Kenny anavyoiwezea ile shuguli?” “Kama namuona yule dada anavyolia kwa raha zote!” Walicheka kwa kashfa, huku dereva akiwapeleka kwenye hoteli aliyoambiwa na bosi wake, Mama Ole.

Na kwa kuwa walifanya yote waliyokuwa wameagizwa na Mama Ole, tena wao wakamuongezea na ushauri mwingine ili Kenny asimtafute tena Naih, yule mama aliwaongezea pesa zaidi. Kwa hiyo vile vicheko vilikuwa vimejaa furaha ya utajiri wa gafla. Mia na Zai wote walilipwa pesa yao, tena wakaambiwa wanaenda kulala hotelini kwa siku mbili wakati wanatafuta chumba! Kwao lilikuwa jambo la furaha sana. Kwanza hawakuwa wakifaidi pale kama Naih. Walilala na mama yao chumba na kitanda kimoja. Hakuna hata feni, wakati Naih alilala kwenye AC! Chumba chenye bafu zuri na vitu vya thamani. Kwao hakuna walichokuwa wanapoteza. Kenny alimpa Naih kipaumbele kuliko wao. Sasa shida iwe wapi?

Kenny & Nora huko nchini Africa ya kusini.

N

ora alipata wakati mzuri sana kuho Afrika ya kusini, akiwa na Kenny. Japokuwa alikwenda kikazi, lakini alifurahia sana kuwa na Kenny. Kwanza alikuwa mjuzi wa aina yake, si kitandani tu alipokuwa akimpagawisha Nora, kila mahali alipajulia kupafanyia mapenzi. Nora alimuomba waongeze siku nyingine mbili mbele, lakini Kenny alimwambia asingeweza kuendelee kukaa kule zaidi ya alivyomuahidi Naih. “Sijamsikia kwa siku zote hizi! Ninakaribia kuchanganyikiwa.” Japokuwa aliongea kwa utani, lakini alimaanisha moyoni. “Unampenda sana Naih?” Nora akauliza. “Kwa lugha nyepesi ambayo naweza kukueleza, ukaelewa, labda nikwambie nampenda Naih kuliko nafsi yangu.” Kenny akajibu huku akicheka tena nakufikiria kidogo.

 “Nafikiri ndiye anayenifanya niwe hivi nilivyo.” “Kivipi?” Nora akauliza tena. “Hata mimi sijui. Lakini kule kujua yupo nyumbani, ananisubiri, au nikirudi nitamuona, kunanifanya nifurahie sana maisha. Ningekuwa nimewasiliana naye tokea nifike huku, au tungekuwa tukiwasiliana naye kila siku, mbona tungeweza kukaa huku hata siku kumi! Lakini nimeamka leo, najihisi kama mgonjwa. Acha nikamuone kwanza ndio tupange safari nyingine.” Nora akaanza kujisikia vibaya moyoni.

“Kwani ulishawahi kufanya naye mapenzi?” Kenny alishituka sana. “Kwa nini!?” “Jana wakati tupo bafuni, ulimtaja, Naih.” Kenny akanyamaza. Akanyanyuka na kuingia bafuni bila hata yakuongeza. Ilikuwa kwa bahati mbaya, wakati anafanya mapenzi na Nora, badala ataje jina la Nora, akaropoka jina la Naih. Alijishitukia, lakini akadhani Nora hakuelewa, kwani ilikuwa kipindi na yeye ndio anafika kileleni akigugumia raha ya mapenzi. Hakutaka kuzungumzia hilo, mpaka Nora aliposema asubuhi hiyo.

Nora alijifunika shuka vizuri, kwani walishaanza kufunuana ili wapate mchezo mwingine kabla yakwenda kupata kifungua kinywa, lakini Kenny alishindwa. Alimwambia labda ni njaa, sababu ya kufanya mapenzi kwa muda mrefu usiku uliopita. Wataendelea baadaye kabla hawajaondoka huko nchini. Ndipo mazungumzo yakaishia kwa Naih. Kenny alikaa bafuni kwa muda kidogo, akatoka akiwa ameshaoga, tofauti na alivyozoea Nora kwenda kuoga pamoja.

“Naomba nikuulize swali moja la mwisho, Kenny.” Nora akakaa. “Karibu.” “Unafikiri unaweza kuja kupenda mwanamke mwingine kama unavyompenda Naih? Au labda niulize hivi, unaweza kuja kuwa na mwanamke mwingine mbali na Naih?” Kenny akakunja uso. “Si tumekuwa na wewe kwa siku zote hizi!? Kuanzia Dar na hapa pia! Hujapata jibu lako tu? Au niulize kuna kitu gani ulitegemea kutoka kwangu na hujapata?” “Usinielewe vibaya Kenny. Mimi ni mtu mzima, na wewe sio mwanaume wa kwanza kulala naye. Nayajua mapenzi. Ufanyaji wako wa mapenzi ni mzuri sana. Nakiri ni bora sana kulinganisha na wanaume wote ambao nimeshawahi kuwa nao na mahusiano. Lakini nitofauti Kenny.” “Kivipi!?” Nora akasita kwani Kenny alishaonekana kubadilika rangi kwa hasira.

“Niambie tu. Ni nini ulichoona cha tofauti?” “Sijui nikuelezeeaje, ukaelewa! Unakuwa unafanya mapenzi na mimi kimwili, lakini unaonekana inakulazimu kuvuta hisia za mtu mwingine. Tokea tunaanza mara ya kwanza, niliona hilo. Nikajiambia labda kwa kuwa mimi ni mgeni kwako. Lakini mpaka tumefika hapa, umekuwa ukiendelea kufanya mapenzi na mimi kama upo na msichana mwingine. Sasa jana ulipomtaja Naih wakati ndio upo juu sana, kileleni, ndipo nilipojua ulikuwa ukifanya mapenzi wakati wote na mimi lakini ukiniweka sura ya Naih.” Kenny alikaa chini. Alishindwa kukanusha, wala kukubali. Alibaki ametulia kwa muda. “Inawezekana nimekosea, lakini najua wewe unajua ukweli. Lakini kama nimekuudhi unisamehe, tafadhali. Ila mimi ndivyo nilivyoona.”

UKWELI.

K

enny alianza kuzungusha kidani kilichokuwa kikining’inia shingoni mwake huku akifikiria. Alipandisha pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. “Naih nimekuwa naye tokea mtoto. Baba yake aliondoka tokea tupo watoto, mimi nikawa rafiki yake wakaribu sana. Sijui maisha mengine bila Naih.” Kenny aliongea kwa kwa sauti yenye hisia nzito. “Nilizaliwa na wazazi matajiri sana, kama unavyowaona. Lakini nilelelewa kwenye kijumba kidogo cha uwani, ambacho alikuwa akiishi Naih na mama yake. Atu au Mama Naih, alinilea mimi na Naih kama mapacha. Alijua ninakula nini, ninavaa nini, kama nimeamka mgonjwa au la. Ninafuraha au la. Atu na Naih ndio watu wapekee waliyoyajua maisha yangu kwa undani. Wazazi wangu walikuwa wakisafiri sana, na hata walipokuwepo nyumbani, hawakuwa na muda na mimi kabisa. Ndio maana nashindwa kumuelezea Naih kwa mtu akanielewa.” Kenny akatulia kidogo.

Kisha akaendelea. “Naih ni kila kitu changu. Ilikuwa nikiumwa, hawezi kulala. Hata kama mama yake atalala usiku, Nai alikuwa anakuwa macho usiku kucha akiniangalia na kunihudumia. Japokuwa alikuwa mdogo kwangu, lakini hakuwa akitaka alale, halafu usiku niamke nikiwa mgonjwa halafu yeye amelala. Nakumbuka alipokuwa akichoka anataka kulala, alikaa kitandani, wakati huo tupo chumbani kwake, halafu ananivuta kichwa changu na kuniweka kwenye vimapaja vyake vidogo, ndipo anasinzia huku amepakata kichwa changu. Nikigeuka tu, na yeye alikuwa akiamka na kuniuliza kama nipo sawa, au kama nataka aniletee maji ya kunywa.” Kenny akaendelea.

“Mimi ni muoga sana wa damu. Sitaki kuona sehemu yeyote ya mwili wangu ikitoa damu. Sasa kila nilipokuwa nikiumia, nilikuwa nikiogopa sana, na nilikuwa sitaki hata kuangalia ile sehemu. Wakati wote Nai alikuwa akiniazima macho yake. Yeye ndio alikuwa akiangalia hilo jeraha na kuniambia kama ni kubwa au la. Basi amenizoesha mpaka leo. Hata niwe na kidonda chochote kile, lazima Nai akiangalie, ndio naridhika naona kitapona.” Kenny akacheka mawazoni na kukunja uso kidogo.

“Sina jinsi nyingine yakumuelezea Nai kwenye maisha yangu mtu akanielewa, isipokuwa kuna rafiki yangu watokea watoto, Emma, huyo nafikiri anajua ninachopitia. Kwa kuwa tumekulia kwenye mazingira yanayofanana. Tukijulikana kama watoto wa mamilionea hapa mjini, kumbe wapweke sana. Mimi nilibahatisha Atu na Naih, mwenzangu amekuwa kwa shida hivyohivyo. Anampenda sana Naih, na kunisisitiza nisije nikamsahau.” Kenny akatulia.

“Nilianza kuingiwa na hofu nilivyokuwa nikiona jinsi wasichana wengine wakazi waliokuwa wakiletwa kufanya kazi pale nyumbani, hawakai muda mrefu wanaondoka, nikajua labda Atu na yeye anaweza kuja kuondoka na Naih, nikamuomba Naih tuwekeane kiapo, kuwa hata iweje, hataondoka pale na kuniacha. Tutadumu milele. Mimi ndio yeye, na yeye ndio mimi.” Kenny akacheka kidogo. “Tuliwekeana ‘amini’ na Naih.” “Amini ni nini?” Nora akauliza, Kenny akacheka tena kidogo kama anayevuta hisia huku akichezea kidani chake shingoni.

“Unajua ile yakulishana damu?” Nora alibaki ametoa macho. “Basi nilimtoboa kidogo na sindano na yeye akanifanyia hivyo hivyo, akala damu yangu na mimi yake. Tukaapiana ni mimi na yeye mpaka mwisho. Wengine wataongezeka juu ya Kenny/Naih, na si vinginevyo. Na kweli, hawajawahi kuniacha tokea wakati huo mpaka sasa wapo na mimi.” Mwili wa Nora ulikuwa ukisisimka. “Mmh!” “Nini?” “Sijawahi kuona  wala kusikia hayo. Ya kwenu ni kali! Au kwa kuwa nyinyi wote ni wamasai? Hamuoni shida kula damu!” Kenny akanyamaza kwa muda.

“Unaona hiki kidani?” Kenny akamuuliza Nora, Nora akasogelea shingoni kwa


Kenny ilipokuwepo hiyo alama kama kidani, ikining’inia kwenye cheni aliyokuwa amevaa Kenny. “Huo sio muundo wake. Ni muunganiko wa alama fulani, tulichora mimi na Naih. Hapa ni nusu ya hiyo alama. Na yeye amevaa nusu yake.

Nilimtengenezea kama hii niliovaa mimi. Tukiweka pamoja, ni alama nzuri sana. Inawakilisha neno ‘Infinity’. Yaani mpaka milele.” Ndipo kweli Nora akagundua kile kidani alichokivaa Kenny, kuwa ni nusu ya alama ya ‘Infinity’. Akabaki akimtazama Kenny kwa mshangao.

“Hakuna mtu anaelewa uthamani wa Naih kwenye maisha yangu, isipokuwa mimi mwenyewe. Sidhani hata kama Naih mwenyewe anajua. Huwa nikishachoshwa na mambo ya siku nzima, natamani nirudi nyumbani angalau nimuone tu. Nai sio mzungumzaji mzuri kama alivyo msikilizaji mzuri. Pia sio muoga au mtu wakulia hovyo kama mimi. Ana jinsi yake huwa ananituliza, hakuna anayejua kunituliza kama yeye. Hakuna sehemu naweza kutuliza mawazo yangu isipokuwa kwa Nai. Ni kweli nina lala naye, lakini si kufanya mapenzi. Nikiwa nimelala pembeni yake, kuna utulivu naupata moyoni. Najiona nipo salama, kama vile tulivyokuwa watoto. Mara nyingi sana, hasa wazazi wangu wanapokuwa hawapo nyumbani, tulikuwa tukilala kitanda kimoja na Nai. Hata shuleni walipokuwa wakinionea, au kuna tatizo, nilikuwa najua nikirudi nyumbani, nitamkuta Nai, nitamuelezea. Na kweli ilikuwa hivyo.” Kenny  akaendelea.

“Wakati wote tulikuwa tukilala taa wazi, na lazima anigeukie ili nimwambie mambo yangu. Japokuwa hakuwa akiongea sana, lakini nilijua ni msikilizaji. Ni tabia ambayo imejengeka mpaka leo. Hakuna kitu naweza kufanya bila Nai. Siwezi kumaliza au kuanza siku bila yeye. Hata mama yangu hanifahamu kama Nai.” “Kwa hiyo huwa unamwambia kila kitu!?” “Kila kitu.” “Kwa kumtaka ushauri au?” “Sijui. Lakini najikuta namwambia kila kitu. Hata kama ni maovu niliyofanya, namwambia tu.” Nora alikunja uso. “Sasa na yeye anasemaje!?” Kenny akanyamaza akijaribu kufikiria huwa Nai anasemaje, akabaki kimya.

Atu na wanae.

A

tu alitoka pale hotelini, siku inayofuata akamuacha Naih amejilaza kimya kitandani, wadogo zake walishatoka. Hakuzungumza lolote na yeyote tokea watoke kwa kina Kenny. Atu alijua Naih amemkasirikia yeye. Kwani tokea mtoto Naih alishamuomba mama yake, wasije kumuacha Kenny peke yake. “Naenda kutafuta mahali pakuishi. Usiku wa leo ndio mwisho wa sisi kuwepo hapa hotelini.” Naih hakumjibu mama yake, Atu akatoka.

Alianzia kwa ndugu waliokuwa wamemsaidia kumtoa Mbeya, kumleta hapo jijini Dar, tokea akiwa binti mdogo. Mambo hayakumwendea vizuri hata kidogo. “Leo ndio umekumbuka kama wewe Mnyakyusa? Yaani leo ndio umekumbuka kama sisi ni ndugu! Mara ngapi tumefiwa hapa, tukakutumia ujumbe na usije? Ulituona sisi tunaishi uswahilini wewe ndio mtu wa uzunguni. Leo mmefukuzwa, ndio unarudi! Sasa nisiione sura yako hapa.” Shangazi yake hakukwepesha macho wala kuuma maneno, alimfukuza Atu.

“Sitaishi hapa bure jamani. Nitalipia.” Atu alijaribu kujitetea. “Aliyekwambia tuna shida na pesa yako nani?”  “Usisahau sababu ya kumtoa hapa mama. Alilala na yule mwanaume aliyetaka kunioa wakati ule. Usimuhurumie, akarudi tena hapa akaja kuharibu tena maisha yetu.” “Kwani Atu alilala na mwanaume mmoja tu? Aliwamaliza wanaume wote hapa mtaani kabla sijamfukuza siku namfumania. Basi angekuwa muungwa, angerudi aombe msamaha! Hata kukumbuka kama nilimsaidia, mbwa huyu! Alikuwa mchafu huko Mbeya, hana mbele wala nyuma! Nikasema nimsaidie mtoto wa marehemu kaka yangu, aje mjini, labda atabahatisha. Shule akakataa, akabaki kung’ang’ania suruali za wanaume. Hebu ondoka, usituletee balaa lako.” Walimfukuza, Atu akaondoka.

Akamkumbuka rafiki yake aliyekuwa akiishi mtaa wa Tandale kwa Mfuga Mbwa. Walishafanya naye umalaya sana pale mjini. Naye alizaa watoto wawili wakiume. Kwa hiyo walijuana na Atu. Wala hakupata shida kujieleza kwa rafiki yake. “Wewe njoo shoga yangu. Hata chini tutalala tu. Kwani nini bwana? Maisha yenyewe mafupi. Au unasemaje Atu wangu wa ukweli.” Atu akaanza kucheka. “Watoto wote watatu ninao.” “Bwana eeh! Hata kumi wewe nenda kawalete. Watalala hapo chini.” “Na wanao?” “Wanachumba huko nje. Ulifikiri nalala na madume yale!? Aku! Nalipia vyumba viwili. Tena kuna mpangaji chumba cha nje anataka kuondoka. Ukija uzungumze na mwenye nyumba, akukodishe wewe.” “Nashukuru Tatu, shoga yangu.” “Yote maisha Atu. Tutabanana nao hapahapa mjini. Harudi mtu kijijini.” Walicheka wakagonga. Ndio ulikuwa usemi wao tokea wapo wasichana wadogo. “Basi tutakuja kesho.” Atu akaaga. “Nyinyi njooni muda na wakati wowote. Msiponikuta, nawaachia funguo kwa mama mwenye nyumba.” Atu alicheka baada ya kumkumbuka Tatu na vituko vyake, akatoka.

  ************************

Usiku ambao Atu alifumaniwa akiwa na shemeji yake, mwanaume aliyetaka kumuoa mtoto wa shangazi yake, alifukuzwa usiku uleule nyumbani kwa shangazi yake. Ndipo akakutana na Tatu, naye anahangaika kama yeye, baada ya kutoka kijijini na kuja kutafuta maisha jijini. Waliishi wawili hao, wakifanya umalaya jijini, bila kikomo. Hawakuwahi kugombana hata mara moja. Wakati wote Atu alisema Tatu alijaliwa moyo wa dhahabu. Alikuwa mgawaji sana. Hata kama alikuwa na kitu kidogo, haikumsumbua kumsaidia mtu yeye akakosa.

***************************

Alirudi hotelini, akamkuta Naih bado amejilaza pale kitandani, wadogo zake hawapo. Alijiweka kitandani akabaki akimtizama mwanae. Walikuwa na vitanda viwili kwenye hicho chumba cha hoteli. Kimoja alilala Naih na mama yake, kingine wadogo zake. Naih alifungua macho akamtizama mama yeke. “Nimefanikiwa mahali pakuishi kwa muda.” Naih akanyamaza. “Naih! Pale kwa kina Kenny, sio kwetu mwanangu. Hata kama ningependa kubaki pale, nisingeweza. Mwili wangu umeshakuwa dhaifu, umri umekwenda. Zile kazi nilizotakiwa kufanya, nisingeweza tena kuendelea kuzifanya.”

“Yule mama alitutunza wakati ule kwa kuwa alikuwa akinufaika na sisi. Sasa hivi tumekuwa mzigo kwake. Hawezi kuendelea kuwa na sisi. Aliyekuwa akitufanya tuishi pale ni Kenny. Na sasa hivi Kenny hatuhitaji tena. Hana anachohitaji kwangu, kwa kuwa ameshakuwa mtu mzima. Na kwako pia. Kenny anaoa, ataondoka pale kwenda kuanza maisha yake. Ulifikiri yule mama angeendelea kututunza pale mpaka lini? Hatukuwa ndugu zao, ilikuwa ni lazima tuwepo pale kama ningeendelea na kazi. Umenielewa?” Naih akatingisha kichwa kukubali.

“Tumshukuru Mungu angalau tumeondoka pale na pesa. Tutatafuta biashara, tutafanikiwa tu. Wala usiogope. Mwenzio nilishafukuzwa kwa ndugu zangu, usiku, tena mvua ilikuwa ikinyesha. Sikuwa najua naenda wapi kwenye hili jiji. Lakini mbona mpaka leo nipo? Tutaishi tu, wala usiogope. Unasikia Nai?” Naih akatingisha kichwa kukubali huku akilia.

Alikaa pale kitandani na binti yake, mpaka ilipofika jioni ndipo Zai na Mia wakaingia. Wakiwa wamejawa vicheko na kusimuliana habari nyingi za huko walipotoka. Waliingia na mifuko ya chips na kuku. Wakakaa na kuanza kula bila kumkaribisha mama yao, wala dada yao. “Mbona mnakula wenyewe?” Mama yao akauliza. “Kumbe tule na nani?” “Sisi hatujala pia.” Walitizamana na kuanza kucheka. “Si wote tulilipwa na mama yake Kenny? Sasa nyinyi pesa zenu ziko wapi?” “Amenipa hundi. Mpaka niende benki.” Mama yao akajibu.

“Hee, kwani njia ya kupata pesa ni moja tu!? Na nyinyi changamkeni. Mjini hapa!” “Eti mama anataka sisi tukahangaike kukata viuno, halafu tumlishe Nai! Na yeye si mwanamke kama sisi?” “Ndio aanze kuzungusha kiuno hicho cha kimasai. Hakuna cha Kenny, wala mjomba wake Kenny! Sasa hivi ushaingizwa kwenye uhalisia wa maisha, nikuchangamka tu.” “Asiyefanya kazi, na asile.” Wakacheka tena, nakugonga mikono yao.

************************************

Watoto hao wawili, walishamshinda Atu tokea wadogo. Viburi ndio usiseme. Wajeuri, na wakianza kuongea, huwezi kuweka neno. Mmoja aliacha shule darasa la sita, na mwingine alipomaliza tu darasa la saba, akaamua kutokuendelea. Wakabaki wakizurula mtaani. Kazi hawakutaka kufanya. Kitu walichojua kufanya, ni kuamka asubuhi, kuoga, nakujitengeneza. Wakishapendeza, wanatoka kuanzia asubuhi mpaka jioni. Japokuwa Atu alijitahidi kuwa mkali kwa wanae, alifanikiwa kwa Naih tu.

************************

“Kesho asubuhi tunatakiwa kutoka hapa.” Atu aliwakatisha vicheko. “Ushapata pa kwenda?” Mia kiziwanda wa Atu akauliza huku aking’ata paja la kuku wa kukaanga. “Nimepata, lakini ni Tandale.” “Poa tu. Si watu wanaishi? Na sisi si watu? Tutakwenda kubanana nao hukohuko. Shuguli kwa huyo binti wa kizungu. Aliyekuwa analala kwenye chumba kinachopulizwa na kipupwe. AC {Air Condtion}.” Wote wakacheka.

“Bwana Nai alikuwa anajidai, kama hajazaliwa na sisi! Basi yeye shule, akitoka shule anarudishwa na Kenny, wanaingia chumbani wanalala na Kenny kidogo, halafu wanaenda chumbani kwa Kenny, wanaendelea kuangalia movie wenyewe.” “Kwanza lugha yao ulikuwa unaisikia?” “Utasikia vipi wakati hujasoma? Wenyewe walikuwa wanaongea ingilishi.” “Bwana dada huyu atalizwa na mengi!” “Na kweli si machache! Mara aletewe nguo hizi, mara atolewe apelekwe kula nje, basi fujo! Hata kutukumbuka wadogo zake! Amwambie Kenny, angalau siku moja moja naomba tuwabebe wadogo zangu na wenyewe wapande gari la kizungu! Hakuthubutu. Yeye peke yake dada na miwani yake ya jua.” “Sasa kaula wa chuya. Kenny anaoa. Hataki ujinga mtoto wa kizungu.” “Jasho litamtoka mjini.” “Sasa kingereza hicho, utakipeleka Tandaleeeee! Ukaongee kingereza uswahilini.” Walizidi kumsema Naih huku wakimcheka sana. Atu alikuwa amenyamaza kimya akiwasikiliza wanae.

Kenny atua jijini.

K

enny na Nora walitua kwenye viwanja vya ndege vya Mwalimu Nyerere, akachukua gari yake aliyokuwa ameiacha sehemu ya kuegeshea magari kwenye viwanja hivyo vya ndege, tokea jumamosi walipoondoka, akampeleka Nora hotelini. Ilishakuwa usiku. “Hatulali wote leo?” Nora akauliza kwa utulivu, Kenny alibaki amesimama karibu na mlango. “Eti Kenny? Maana nimeona umekuwa kimya njia nzima. Au nimekuchosha?” “Hapana Nora. Nimekufurahia sana. Nashukuru kwa kunipa wakati mtulivu. Nimefurahia kila kitu.” “Basi tuagane, si unajua naondoka kesho na ndege ya asubuhi sana?” Nora akajivuta karibu na Kenny, akambusu midomo yake, lakini Kenny alitabasamu  tubila kurudisha busu. “Naomba basi nikimbie nyumbani mara moja, nitarudi tulale wote mpaka kesho wakati unaondoka. Nitakupeleka uwanja wa ndege ndipo na mimi niende kazini.” “Sawa.” Nora hakubisha.

Akili ya Kenny ilishavurugika, hakuna ambaye angeweza kudhania. Tokea jumamosi anamuaga Naih kwenye simu, mpaka siku hiyo ya jumatano hakuwa hata amemsikia! Ni kitu ambacho hakijawahi kutokea maishani mwake. Naih alikuwa nguvu ya ajabu sana kwa Kenny. Hakuweza kuanza siku au kumaliza bila Naih. Alianza kupiga honi kabla hajafika getini, alipokaribia tu getini, geti lilifunguliwa akapita na gari lake moja kwa moja mpaka nyuma ya nyumba, ambapo ilikuwa hiyo nyumba ndogo aliyokuwa akiishi Atu na wanae.

Alishuka kwenye gari akiwa ameacha mlango wa gari wazi na wala hakuwa amezima gari hilo, akaanza kuita, “Nai! Nai!” Huku akikimbilia chumbani kwa Naih. Akakuta mlango umefungwa na funguo. Akarudi kwenye gari ili kuchukua funguo za chumbani kwa Naih, alizokuwa ameziweka pamoja na funguo za gari yake. Akarudi anakimbilia mlangoni kwa Naih bila kufikiria, akakuta kitasa kimebadilishwa. Aligonga mara kadhaa, akahamia chumbani kwa Atu, na kwenyewe kulikuwa kumefungwa, ila taa za nje zote zinawaka. Alifikiria kidogo, akaamua kwenda nyumbani kwao.

Uongo Unaofanana na Kweli Wakumuumiza Kenny.

Akawakuta wale wasichana wawili wa kazi. “Naih yuko wapi?” Kenny aliuliza bila salamu. “Shikamoo kaka.” “Naih yuko wapi?” Akauliza tena, kuonyesha anataka jibu tu. “Walipigana sana hapo kwao siku hiyo ya jumamosi usiku. Sisi tukaenda kuwaangalia.” “Namuulizia Nai, sio wale wadogo zake.” “Ndio huyo Nai alikuwa akipigana na wadogo zake.” “Walikuwa wanampiga Naih, bwana.” Binti mwingine wakazi alimkosoa mwenzake. Kenny akakunja uso kama asiyeelewa.

 “Wanampiga Nai!?” “Wanasema wamemfumania Nai na mwanaume wa Mia, anaitwa Tino. Lakini sisi huyo Tino hatukumkuta. Eti walisema Nai alijidai hamtaki Tino ni rafiki waliyekuwa wakisoma naye tu, kumbe walikuwa wakijifungia chumbani, wanamalizana. Sasa siku hiyo Nai akadhani wadogo zake hawapo, akamuingiza Tino chumbani, ndio wakawakuta wote wapo uchi, kitandani.” Kenny alijisogeza kwenye ukuta akaegamia kama asianguke.

Mlango wa jikoni ukafunguliwa, alikuwa mama yake. “Nai yuko wapi?” Kenny akamuuliza mama yake. “Mbona hunipi hata salamu za huko ulikotoka, unanianzishia maswali?” Mama yake alimsogelea ili amkumbatie na kumbusu, lakini Kenny akamsukuma kidogo. “Nai yuko wapi?” “Wameondoka. Tena niseme wametoroka baada ya kuniibia hundi yangu. Si unajua ile tabia yangu ya kusaini hundi kadhaa, tena mpaka ukanikataza, sasa imeniponza! Nai alikuja akachomoa moja ya hundi zangu bila mimi kujua, tena ametoa chumbani kwangu. Hawa mabinti walimuona akiingia chumbani kwangu. Sasa jumanne nimeenda benki, nauliza salio, nakuta hizo pesa, hazipo. Si ndio ikabidi kuanza kufuatilia? Nikakuta imetolewa siku ya jumatatu kwenye tawi la Magomeni. Nikaenda mpaka Magomeni, wakatafuta hiyo hundi, ikawa imechukuliwa kwa pesa taslimu. Ikabidi kuomba kuona uthibitisho zaidi. Nikakuta imeandikwa kwa nyuma mtoaji ni Naih Masai, na saini yake nimeonyeshwa. Sikuamini. Nikawaomba kama kuna kamera nionyeshwe. Basi, meneja akanichukua mpaka wanapohifadhi hizo video, nikamuona Naih kabisa akisaini na kukabidhiwa hiyo pesa yote. Yule meneja akaniambia kama nataka kumfungulia mashitaka, watanipa ule ushahidi. Lakini Kenny, nimeamua kusamehe. Nimemwambia yule meneja, nimesamehe, na yaishe. Nimebadilisha vitasa vya nyumba nzima, ili wasije kurudi, nakuniibia tena. Funguo zako hizi hapa. Hizo ulizo nazo hazitafaa tena.” Kenny aliomba kwenda kupumzika chumbani kwake kwa muda. Aliingia chumbani kwake, akawasha tv, akaanza kucheza game huku ameweka headphone masikioni.

Alikesha akicheza mpaka palipopambazuka bila kulala, akarudi hotelini kwa Nora. Alikuta ameshajiandaa kuondoka, alimvamia kwa ajili ya kufanya naye mapenzi. Nora aliona kuna jambo halipo sawa, kwani aliingia na kumng’ang’ania bila hata salamu, lakini hakubisha. Akaona siyo mbaya kupata penzi la Kenny kabla yakuondoka. Alivua nguo zake haraka haraka, akamrudia Kenny. Walipeana mabusu ya muda mrefu huku wakinyonyana huku na kule, lakini Kenny alishindwa kusimamimisha kabisa. Mrembo Nora alitumia ujuzi wake wote, lakini ilishindikana, mwishowe akaamua kuvaa nguo zake. “Nisubiri nikusindikize.” “Hapana. Nitachua tu taksii, asante.” Nora alitoka na mizigo yake, akamuacha Kenny hapo kitandani. Alipitiwa na usingizi hapohapo kitandani.

Huko kwa Naih!

N

aih hakuwahi kuishi kwenye mazingira kama yale tokea anazaliwa. Bafu na choo kilikuwa sehemu moja na walitumia wapangaji wote. Choo kilikuwa cha kuchuchumaa ambacho unaona kinyesi cha watu wengine. Ulikuwa ni mshtuko wa namna yake kwa Naih. Alikaa karibia siku tatu hajatumia choo. Mama yake alikuwa akimuona vile anavyohangaika, lakini hakujua jinsi yakumsaidia mwanae. Wadogo zake walikuwa hawana shida hata kidogo. Utaratibu wao ulikuwa ni uleule, kutoka asubuhi kurudi jioni.

Chumba hicho kimoja, na joto kali, walikuwa wakilala watano. Tatu alikuwa na kitanda cha kawaida tu, lakini Atu alimuomba awe analala hapo kitandani na Naih, yeye na wanae wale wawili walilala kwenye godoro, chini sakafuni, hapakuwa na kitanda kingine. Baada ya kuletewa zile pesa na Naih aliyekuwa amemtuma benki siku ya jumatatu, wakanunua godoro ndio hilo walikuwa wakitumia na wanae. Pesa iliyobaki Atu aliificha huku akifikiria kitu chakufanya, wakati anaendelea kupata nafuu, kwani ndio alikuwa na siku chache tu tokea atoke kufanyiwa upasuaji, bado wakati mwingine alikuwa akipata maumivu. Naih ndio alisaidia kazi za pale, akichukua zamu ya Tatu ya kufagia uwanja wa ndani na nje. Chooni ndio ilimlazimu Atu amsaidie Naih, hakuwa akiweza kabisa hata kuingia.

************************

Siku hiyo ya tano tokea wahamie hapo, waliamka asubuhi hawakuwakuta Zai na mdogo wake. Walikuta nguo baadhi za Naih zimetupwa chini, nyingine pamoja na begi lake havipo. Haraka sana Atu akakimbilia mkoba wake alipokuwa ameficha zile pesa zake, hakukuta hata shilingi moja, walitoroka na pesa zote, na nguo nzuri za Naih na begi lake kubwa la nguo.

************************

Mara kwa mara Kenny alikuwa akimpeleka Naih kununua nguo. Kwa hiyo Naih mara zote alikuwa akipendeza. Aliacha kuvaliana nguo na wadogo zake, kwani wao walijaliwa maumbo makubwa, hasa chini. Walichukua maumbile ya mama yao, tofauti na Naih aliyekuwa mrefu, mwembamba. Wao walikuwa wafupi, lakini wamejazia kila mahali, hasa chini.

************************

Atu alianza kulia. Alilia Atu bila kujua chakufanya tena. Uhuni, umalaya na mambo yote mabaya ni mazuri ukiwa unafanya wewe. Unajipa sababu za kufanya unayoyafanya. Unajifariji na kujitetea. Lakini isiwe kwa watoto wako wakuwazaa. Inauma kupita kiasi. Atu alilia sana. Kufumba na kufumbua wale watoto walimrudisha chini kabisa. Hakuwa nachakufanya tena na bado alikuwa dhaifu. Ataishi hapo kwa shoga yake bure mpaka lini!? Ndio swali lililokuwa likimliza. Umri Umekwenda na ameshaanza kudhoofu. Anajiuza kwa nani, ampe pesa!? Shule hana. Anafanyaje? Hata biashara aliyokuwa akifikiria kufanya mara baada yakupata nafuu, hawezi kufanya tena.

Wakati mama yake anaendelea kulia, yeye Naih alikusanya nguo zake zilizokuwa zimebakizwa, asijue hata kwa nini wamemuibia hizo nguo. Wazi alijua haziwezi kuwaenea ila walitaka kumkomoa tu. Tatu alienda kumletea mfuko wa plastiki akaweka humo nguo zake hizo chache zilizobakishwa. “Pole shoga yangu. Uzazi mgumu!” Tatu akamfariji Atu, rafiki yake. 

Uhalisia wa Maisha.

M

aisha yalikuwa magumu sana kwa Atu na Naih waliokuwa wameachwa bila pesa yeyote. Tatu alikuwa na biashara ya kuuza chakula maofisini. Anapika chakula asubuhi, anakiweka kwenye mahot pot makubwa, anapanda daladala mpaka maofisini kwenda kuuza. Alishakuwa na wateja wake ambao alikuwa akiwapelekea chakula. Naih alimuomba awe akienda naye huko kwenye biashara zake, ili nayeye awe na kitu cha kufanya, asikae tu bure na angalau ajipatie hata pesa ya kujikimu. Tatu akakubali. Walianza kuamka asubuhi na mapema, wanasaidiana kupika, kisha wanaanza safari ya kwenda posta mpya kuuza hicho chakula maofisini.

Tatu alikuwa mzungumzaji sana, na mcheshi. Wateja wao walimpenda. Aliuza chakula na mwili wake pia. Akibahatisha kupata mwanaume siku hiyo, Naih anarudi na vyombo nyumbani na kumuacha yeye akimalizana na huyo mteja wake wa mwili. Alilala na kila mwanaume aliyemtongoza, ilimradi umpe pesa tu. Atu alichelewa kupona. Bado alionekana dhaifu, kwa hiyo Naih alikuwa akienda kufanya kazi na kumuacha mama yake nyumbani.

Baada ya miezi miwili kupita, Mia alirudi nyumbani akiwa hana hata shilingi moja. Atu hakutaka hata kumuuliza. Akajiunga na biashara hiyo ya kuuza chakula. Baada ya siku 5 kuisha Zai naye akarudi, na yeye akajiunga na hiyohiyo biashara. Wakawa watu wanne kwenye biashara moja. Ilikuwa vurugu ya namna yake. Watoto hao walikuwa ni kama wamepewa ulimwengu kwa furaha ya kukutana na wanaume wasomi, tena wenye kazi za maofisini!

 Hakujua ndugu zake walifanyaje, lakini baada ya mwezi wakajikuta wamepewa kibanda, ambacho kilikuwa katikati ya maofisi mengi. Wakawa wanapika hapohapo na kupata wateja mbalimbali. Palikuwa na sehemu nzuri tu ya kukaa na kula.

Pesa ikaanza kuingia, Naih akafungua akaunti yake akawa anaweka pesa yake huko. Hakuthubutu kuacha pesa nyumbani. Wadogo zake wakaanza kutapanya pesa zao. Mavazi mazuri na kujipodoa. Walijibadili rangi, wakawa weupe kama machotara. Walilala na kila mwanaume aliye watongoza pale kwenye huo mgahawa wao. Na kwa kuwa walikuwa na maumbile ya kibantu, basi wanaume wengi waliwatongoza. Na mara nyingi walikuwa wakitoka kwenda kwenye kumbi za starehe, hasa ijumaa na jumamosi.

 Walikuwa wakimuongezea pesa Naih ili abaki aoshe vyombo, wao wawahi kurudi nyumbani wajiandae kutoka kwenda kwenye starehe zaidi siku hiyo ya ijumaa. Ilikuwa ngumu kujua kama ni ndugu. Walipendwa na wateja wao, kwa kuwa walikuwa warembo, wacheshi na chakula chao pia kilikuwa kizuri sana. Kuanzia chips, wali, ndizi, na nyama walizokuwa wakichoma, ziliwavutia wateja na kuwafanya wajaze wateja kila wakati. Sehemu ya mapishi, ilikuwa ni Naih na Tatu, mapokezi na kugawa chakula ni Zai na Mia. Atu ndiye alikaa upande wa kupokea pesa.

Vurugu zikaanza. Kupigana sababu ya kuchukuliana wanaume. Wakati mwingine walipigana wao wenyewe, Mia na Zai, hapohapo kazini. Na wakati mwingine walifuatwa na wanawake wengine waliowachukulia waume zao. Na wao hawakuwa na hofu wala aibu. Kama atafuatwa Mia, basi Zai atamtetea mdogo wake, watapigana hapo kazini hata mbele ya wateja wao, huku wakitukanana. Habari zao zikaenea kwa haraka sana pale mjini. Walikuwa wakijiita ‘watoto wa Mfuga mbwa’. Fanya fujo uone. Na kweli, wakikuamulia hao watoto wa Atu, utajuta. Wanaweza kukufuata ofisini kwako na kukufanyia fujo mpaka ukafukuzwa kazi. Usiwaanze. Ukiwaanza tu, ujue watakumaliza. Huna jinsi ya kuwatukana ukawaumiza. Kwanza kabla hujawaita wao Malaya, wao wenyewe walijitambua hivyo na kujisifia waziwazi, kana kwamba ni sifa. Naih alikuwa akiwatizama bila kuzungumza nao chochote.

************************

Miezi 6 ilishapita tokea waanze maisha hayo. Siku hiyo wakiwa wanamalizia kuuza, alifika kwa kuchelewa mfanyakazi mmoja ambaye alizoeana na Tatu kwa muda mrefu sana. Alikuwa mteja wake, na Tatu alimpendelea wakati wote. Alimuita Tatu, Mama na Tatu alimuita Mziwanda. Naih alishaanza kusafisha baadhi ya vyombo ili kumaliza siku. Wadogo zake walishaondoka kwani ilikuwa ni siku ya ijumaa, huwa wanafanya kazi nusu siku, wanasema starehe ndio zinaanza. Kwa hiyo Naih hubakiwa na majukumu mengi sana siku za ijumaa, japo huwa siku hiyo ndio analipwa zaidi kuliko wote. Tatu hakuwa akipenda kuosha vyombo, mama yake alisema hawezi kusimama wala kuinama kwa muda mrefu, kwa hiyo Naih ambaye hakuwa na kipingamizi, alifanya kazi zote walizokuwa wao hawazitaki, lakini kwa malipo zaidi. Alikuwa akilala hoi kwa kazi.

“Mama! Leo nimekuja na bosi wangu, anayeniweka mjini.” Mziwanda alikaa huku akiongea na Tatu. “Nilipata ujumbe wako, na nimekufichia chakula, kama ulivyotaka.” “Si ndio maana nakupenda  mama yangu. Turekebishie basi.” Tatu alitoa vile vyakula kule alipokuwa amevificha. Wakaungana na vijana wengine wawili waliokuwa pamoja naye. Vilianza vicheko na utani kwa vijana wale huku wakila chakula walichokuwa wamefichiwa na Tatu. “Mbona leo siwaoni warembo wetu?” Mziwanda akamuuliza Tatu. “Ijumaa leo.” “Oooh! Ndio mambo yetu yameanza?” Mziwanda akauliza na cheko kubwa. “Ndio maana yake.” Tatu akajibu huku akiwa upande wa jikoni.

 Lilikuwa ni banda kubwa la bati lililokuwa limetenganishwa mara mbili. Jikoni kulifunikwa kila upande. Kama chumba kikubwa kinachojitegemea. Chumba hicho cha jikoni na kule wanapokaa wateja wao, kulitengenishwa na dirisha kubwa lililozungushiwa bati. Kwa hiyo waliweza kuonana bila shida, kasoro Naih aliyekuwa akiosha vyombo nyuma kabisa ya hilo banda.

“Kumbe kuna warembo hapa?” Mmoja wao alimuuliza Mziwanda kwa sauti ya chini lakini wakina Tatu waliweza kusikia. “Warembo wa nguvu. Wewe tu na juhudi zako.” Mziwanda akamjibu mwenzake huku akiendelea kula. “Mbona sasa hatujawakuta!?” “Si umesikia leo ijumaa. Wanawahi kutoka.” “Itabidi utulete siku nyingine.” “Utalala na wangapi wewe!?” Mmoja wao akauliza. “Acha hizo Emma. Maisha mafupi kaka. Kufa mara moja, kuzaliwa mara moja.” Mwenyeji wao, yaani Mziwanda, akaanza kucheka.

“Lakini watoto wenyewe, jungu la bibi! Kila mtu anajichukulia tu.”  Mziwanda akawatahadharisha wenzake kwa sauti ya chini kidogo.  “Hapa panajulikana kama ‘Malaya pub’. Yaani jamaa wanasema ukiwa na njaa, hapa unashibishwa kila kitu. Wanawake wote hawa Malaya. Pesa tu ndio inaongea. Hata huyo Mama hapo, nasikia vijana wanaliaga. Jamaa wanamsifia kweli huyo mama! Anaitwa Tatu. Kule ofisini walikuwa wanabishana. Eti mtambo mzuri nani!? Kati ya hao mabinti na Mama Tatu! Unaambiwa wote walikubaliana bila kubisha Mama Tatu ndio kinara. Unaambiwa huyu mama akikuweka kitandani, utagoma kushuka!” Kiziwanda alikuwa akiongea kwa kunong’ona, lakini wote walikuwa wakiendelea kusikia.

 “Jamani mimi najitosa.” “Acha hizo, Tye.” “Kama wewe Emma unamsubiri mkeo, naomba umsubiri tu. Acha sisi tulioamua kuyavulia maji nguo, tuyaoge.” “Subiri kwanza Tye! Sasa unataka kumchukua nani? Maana wapo mabinti watatu na mama zao wawili.” “Acha nianze na huyu niliyemkuta hapa.” “Tye! Huyu mama anaweza kukuzaa wewe!” “Acha kuniwekea hukumu Emma! Acha na mimi nikaonjeshwe ya kiutuuzima. Lakini namwanzaje?” “Nimekwambia hapa ni ‘Malaya pub’, Tye. Wanawake wote hapa hawana shida. Wala usitafute maneno mengi. Pesa yako tu.” “Basi tukimaliza kula, nyinyi tangulieni ili nizungumze naye.” Emma alibaki akitingisha kichwa. “Nini kaka!? Hizi ndizo starehe zenyewe.” Tye aliweka msisitizo kuonyesha amekusudia.

Wakati wamemaliza kula, wanamlipa Atu, Tatu akamwita Naih kusafisha meza na kutoa vyombo. Naih akaenda pale mezani walipokuwa wakila kina Mziwanda na wageni wake, ndipo akamuona Emma. “Naih! Is it you!?” Naih akacheka kichovu. “Ni mimi Emma. Habari za siku?” Emma alishangaa sana. “Na wewe upo hapa!?” Naih akacheka kwa kuwa alisikia sifa zao zikitajwa na Mziwanda. “Yeap! Na mimi nipo hapa ‘Malaya pub’.” Wote wakamgeukia Mziwanda. “Mbona mnaniangalia mimi jamani!? Nimewaambia watu ndivyo wanavyopaita. Sio mimi. Mimi naheshimiana sana na mama yangu Tatu.” Mziwanda alishapaniki.

“Chukua basi  na hii mama yangu, na wewe kesho ukajidai mtaani.” Kwa kugundua kuwa alisikiwa, akatoa pesa ili amkabidhi Tatu kama hongo ya kusamehewa. Tatu akabaki akimtizama na jicho la kumsuta. “Mimi na wewe mama yangu? Tumetoka mbali sana.” Tatu akabaki akimtizama. Mziwanda akatoa tena pesa nyingine kutoka mfukoni. “Nakuongezea na hii mama yangu. Nimebakisha ya nauli tu mama yangu. Tupatane.” Mziwanda akaendelea kumbembeleza Tatu ili amsamehe kwa kashfa alizokuwa akizimwaga kwa rafiki zake. Atu alizidi kucheka huku akimtizama Tatu na Mziwanda.

“Tafadhali mama. Tusigombanishwe na maneno ya watu. Naomba yaishe.” Mziwanda akaendelea kubembeleza huku rafiki zake aliokuwa akiwasimulia wakimcheka. Akamsogezea zile pesa karibu. Tatu akazipokea zile pesa akaziweka kifuani. “Haya ondokeni. Na wewe!” Akamgeukia Tye. “Utakufa siku si zako. Haya nenda kwenu ukanywe maziwa, ulale.” “Mimi mtumzima mama, usinidharau.” Tye akajitetea. “Umeacha kuvaa diaper?” Tatu akamuuliza Tye, lakini alimfanya Atu azidi kucheka. “Mbona muda mrefu sana mama yangu. Nimekuwa kabisa.” “Jamani! Mimi kabla sijaharibu zaidi, naomba nitangulie.” Mziwanda akakimbia, Emma akamfuata huku akiwa haamini alichokiona, Tye alitoa kadi yenye namba yake ya simu, akachomoa pesa kwenye waleti. “Mimi siku za jumamosi huwa sifanyi kazi mama yangu. Nimekuwekea pesa ya taksii kabisa. Sitaki upande daladala. Nishaanza kusubiri simu yako.” Tye aliongea kwa wasiwasi. Akaweka chini zile pesa na ile kadi yenye mawasiliano yake, na yeye akawakimbilia wenzake.

 

Sehemu ya 3.

Emma & Kenny

E

mma alikuwa rafiki kipenzi wa Kenny. Wote walizaliwa na wazazi wenye uwezo sana, lakini hawakubahatika kupata malezi ya wazazi wao. Tokea chekechea mpaka chuo kikuu, walisoma darasa moja na Kenny. Aliyajua kwa undani mahusiano kati ya Kenny na Naih. Walifahamiana na Naih, kwa kuwa kila alipokuwako Kenny, ndipo alipokuwa Emma tokea watoto. Walifuatana kila mahali na hata Emma alishacheza sana chumbani kwa Naih wakati wadogo. Kwa hiyo Naih alifahamiana na Emma kwa karibu sana. Na kutokana na malezi ya wazazi wao, vijana hao wawili waliojulikana kama mapacha wa nje, mmoja aligeuka kupenda sana ngono, kama faraja yake, ambaye ni Kenny, wakati yeye Emma alichukia ngono kupita kiasi. Aliwaambia rafiki zake, anamsubiria mkewe tu, ndiye atakayemvulia nguo na si vinginevyo.

Hakuwahi kuwa na msichana hata mara moja, kuhofia kuja kuwa na ndoa kama ya wazazi wake. Emma alikuwa na kaka yake, Jay, ambaye yeye alitoroka nchini mapema sana, sababu ya wazazi wao. Aliondoka na kukata mawasiliano kabisa na wazazi wao, kasoro kwa Emma na Kenny. Naye pia alifahamiana na Naih vizuri tu. Ni kama wote walikuwa watoto wa Atu. Emma ambaye alibaki nchini na Kenny, alipomaliza tu chuo kikuu, akatumia akili za haraka kujikwamua kimaisha. Kutokana na utajiri na kujulikana kwa wazazi wake pale mjini, hakupata shida kuanzisha biashara na kumiliki nyumba ndogo tu. Jina la baba yake lilimsaidia kupata wateja. Kiwanja alichokuwa amekinunua zamani sana na kuanza kukijenga taratibu kutokana na pesa alizokuwa akipewa nyumbani tokea yupo shuleni, alipomaliza tu chuo, akakusanya pesa kwa juhudi zote. Akamalizia nyumba hiyo na kuhamia kama mchezo tu, rafiki zake wasiamini.

Wakati anakinunua kiwanja hicho mara baada yakumaliza kidato cha sita, aliwaambia marafiki zake kuwa anataka kuanza kujenga nyumba yake, waliona kama utani na mchezo fulani, wakaishia kumcheka tu Emma. Kundi hilo la watoto wa matajiri mjini hakuna hata aliyekuwa na wazo la kujenga isipokuwa Emma. Lilikuwa ni lengo alilojiwekea Emma na kaka yake. Kuondoka nyumbani kwao kwa haraka sana. Kaka yake alikimbia nchi, Emma akawa anajenga taratibu ili aje ahame nyumbani kwao.

Jay lipofanikiwa huko alikokimbilia, akamsaidia mdogo wake kumalizia hiyo nyumba, Emma akahama nyumbani kwao, akaanza maisha yakujitegemea wakati kina Kenny hawana hata habari.  Kenny mtoto wa pekee hakuwahi kuwa hata na wazo la kujenga. Kwanza hakuwahi kukua kwa wazazi wake. Kila kitu cha wazazi wake aliambiwa ni chake. Hata nyumba waliyokuwa wakiishi, mama yake alimwambia Kenny ni yake, hapakuwa na haja ya kuondoka. Hata akioa, alikaribishwa kuishi pale na mkewe, ili mama yake awe karibu na wajukuu zake.

Nyumbani kwa Emma, Kenny hakuhitaji kujieleza kuwa anakwenda huko au hakuhitaji kukaribishwa hapo. Kwanza alikuwa na funguo za nyumbani kwa Emma. Tokea Naih aondoke, ni kama Kenny alihamia huko. Akawa analala kwenye makochi, kwa kukesha kucheza game kwenye tv. Siku za jumamosi na jumapili ambazo hakuwa akifanya kazi, Kenny alizitumia kucheza game tu kuanzia asubuhi mpaka asubuhi. Siku ya jumatatu mpaka ijumaa alienda kazini, ofisini kwa mama yake kama kawaida. Atafanya kazi zote alizotakiwa kufanya siku hiyo, kisha anarudi nyumbani kwa Emma, au kwao kama mama yake akimuita. Lakini muda mwingi alitumia nyumbani kwa Emma.

************************

“Huwezi amini niliyemuona leo.” Emma aliingia na kutupa funguo za gari kwenye meza. Kenny hakujibu, akasimama na kwenda nyuma ya kabati kubadili waya, ili aanze kucheza game, na yeye ndio alikuwa ameingia. “Umekuja na chakula?” Kenny akauliza wakati yupo nyuma ya kabati la TV, kama amepuuza mazungumzo aliyoanzisha Emma wakati ameingia. “Leo si tumemuahidi Tye tunaenda kwake?” “Sijisikii kutoka. Ukirudi, unijie na chakula.” “Tena leo tulikuwa naye mchana akanikumbushia. Tulienda kumtembelea Fabian ofisini kwake. Fabian akatupeleka kula ‘Malaya pub’.” Fabian ambaye Tatu anamwita Mziwanda ni rafiki wa Emma. Hakuwa karibu sana na Kenny kama Emma.

Emma alikuwa akipeleka bidhaa za ofisini, kwenye kampuni anayofanyia kazi Fabian, ambapo alikuwa kama muhasibu. Wakawa karibu na Emma kwa sababu za kikazi na ndipo Kenny akamfahamu Fabian. Kwani kwenye baadhi ya mikutano yao ya nje, Emma alikwenda kukutana na Fabian akiwa na Kenny. Hata siku hiyo wanakutana na Fabian nakwenda kula ‘Malaya pub’, Tye alikwenda kumtembelea Emma ofisini kwake, ndipo ikabidi waongozane ofisini kwa Fabian akiwa anafuatilia mambo yake ya kikazi, wakaishia kwenda kula pamoja na Tye akiwepo.

 “Malaya pub ndio wapi!?” Kenny mpenda starehe, mtoto wa jiji akauliza kwa kushangaa. Iweje yeye asipafahamu hapo! “Wanauza chakula na ngono.” Kenny akanyamaza. Ni kama upande wa ngono alishapoteza ushabiki kabisa. Ingekuwa enzi hizo, angetaka habari kamili, pengine apachangamkie kama Tye. Alipoona amepuuza, ikabidi Emma aendelee tu. “Wakati tunakaribia kuondoka, nikakutana na Nai.” Emma alisikia kishindo kikubwa, akawahi tv yake. Kenny alijigonga kwenye tv kwa mshituko.

“Kwema?” “Daah! Nimejigonga vibaya kweli!” Kenny akatoka huku akisugua kichwa. “Daah! Umejichana kidogo.” Damu zilikuwa zikitoka kidogo kwenye kipanda uso karibu na nywele. Kenny akaelekea chooni, akatoka akiwa amejifuta damu na ametulia. Emma alishangaa kuona Kenny hauliziii habari za Naih tena. Akaona anyamaze tu.

Baada ya muda Emma alitoka kwenda kuungana na kina Tye kama walivyokuwa wamekubaliana. Akarudi usiku sana, akamkuta bado Kenny anacheza game. Alikuwa amemleta chakula. Akamuwekea hapo mezani, mbele yake, yeye akaingia kulala, akaaamka asubuhi, bado Kenny alikuwa akicheza game. Emma alijua kinachoendelea kichwani kwake.

Akaenda kuchomoa tv kwenye umeme, Kenny akamgeukia. “Naih anafanya kazi hapo. Jumatatu mpaka ijumaa, asubuhi wanauza kifungua kinywa, mchana chakula. Wanaondoka kwenye saa kumi na moja jioni baada ya usafi. Wateja wao wakubwa ni wafanyakazi wa maofisini. Hajabadilika sana, yupo vilevile ila anaonekana amechoka sana. Sasa sijui ni maisha, au ni kazi siku hiyo zilikuwa nyingi, sijui!” Emma alimaliza, akabaki akimtizama Kenny. Kenny akavua headphone zake, akaweka rimoti mezani, akajinyosha kwenye kochi, akalala bila kujibu kitu. Alipoamka mchana, akaondoka bila kuaga.

************************

Emma hakumuona wala kumsikia mpaka baada ya siku ya 5, akashangaa amemsimamia ofisini kwake. “Naomba umuajiri Nai.” Emma alinyanyua uso, akabaki akimtizama. “Mpe kazi yeyote ile, hapa ofisini kwako.” “Ofisi yenyewe ni ndogo hii Kenny! Siajiri sasa hivi. Sina hiyo bajeti ya kulipa mtu mwingine mshahara.” “Mimi nitamlipa.” Emma akakunja uso. “Unafikiri unaweza kumpa kazi au huwezi?” Kenny akauliza kwa ukali na jeuri. “Ngoja basi nifikirie kazi gani naweza kumpa! Nipe muda.” “You know what, never mind.” Kenny akawa kama amegairi. Hataki tena Emma amuajiri Naih. Atoka kwa hasira.

          Emma akamkimbilia. “Kenny, subiri. Wewe unajua naweza kufanya chochote kwa ajili yako. Subiri tuzungumze.” Kenny akasimama. “Kwa kuwa ni mzuri wa lugha, nitampa kazi ya usekretari. Ofisi haina sekretari kwa kuwa bado niliona ndogo, lakini nitamfuata na kujaribu kumwambia kama kuna nafasi ya kazi.” “Poa.” Kenny akajibu. “Sasa mshahara nitamwambia ni kiasi gani?” “Milioni..” Akamtajia huo mshahara kwa mwezi, mpaka Emma akashangaa. “Hee! Hata mhasibu wangu simlipi hivyo.” “Basi punguza laki 5 kwenye hiyo.” “Kenny!”

“Kwani hawa watu wa chini wanalipwaga kiasi gani?” “Sio watu wa chini, ni..” “Unajua nini, wewe mtajie mshahara wowote ule unaoona utamstahili, bora aje afanye kazi hapo kwako.” “Kwani unampango gani naye?” Emma akauliza.  “Sijui Emma. Bado ameniudhi sana. Tena sana. Lakini Fabian amenisimulia yale mazingira anayofanya kazi pale, hayafai. Na naomba asijue kama ninajua yupo hapa, wala nahusika na mshahara wake. Usizungumze naye chochote juu yangu.” Emma akacheka kwa kuguna. Kwanza hakuwa hata akijua kama alimtafuta Fabian.

“Nini?” Kenny akamuuliza baada yakumuona Emma anamcheka. “Acha kujiua wewe mwenyewe Kenny! Unampenda Naih. Kwa nini unacheza mchezo wa kujinyima raha?” “Ameniumiza sana moyo wangu!” “Unategemea kupona vipi, kama hutaki kumpa nafasi yakujieleza.” “Sio sasa hivi, Emma. Bado ninahasira sana.” “Haya Kenny. Mimi nakusikiliza wewe.” “Lakini naomba iwe leo.” “Si unaona wewe mwenyewe!? Nilikwambia Kenny.” “Japokuwa ameniumiza sana, lakini Naih amekuwa msaada wangu. Wewe unajua. Nataka kumsaidia tu.” “Haya Kenny. Lakini sisi tunajuana kwa kuangaliana tu. Nakufahamu Kenny. Huyu binti amekuathiri sana. Hutakuja kuwa sawa bila Naih.” “Mbona mimi nipo sawa tu!” Emma alibaki akimtizama kwa kumsuta.

          “Nini sasa?” Kenny akauliza. “Hivi unajua siku hizi maisha yako yote yamekuwa ni game tu? Hulali vizuri, hata wanawake wamekushinda!” “Mbona mimi nipo sawa tu na ninalala na wanawake kama kawaida!” “Come on Men! Unajua unazungumza na mimi, Emma!” “Najua ni wewe. Sasa?” “Sio uliniambia baada yakutoka Afrika Kusini ulikwenda mpaka Mwanza kwa Nora, ukashindwa kufanya naye mapenzi?” “Ile si ni mara moja tu?” Kenny akajitetea.

“Na siku ile alipokufuata hapa Dar?” “Na siku ile tu!” “Kenny, kuwa muwazi kwako wewe mwenyewe. Hujaweza kulala na mwanamke yeyote yule, tokea Naih aondoke.” Kenny akanyamaza kidogo. “Usimwambie kama mimi nahusika. Ila nakuomba leo ukazungumze naye.” “Nitafanya hivyo, men!” Kenny akaondoka.

************************

 Ilipofika saa kumi jioni, Emma alienda sehemu wanayouzia chakula kina Naih na wenzake. Hakumuona Naih. Akasogea pale bandani akamuona Atu amekaa, akamsalimia. Atu alimfahamu Emma tokea yeye na kaka wake ni watoto wadogo, hawajitambui. Ni kama na yeye aliwalea tu. Akamuulizia hali ya Jay, kaka yake Emma, ambaye alishaondoka nchini muda mrefu sana. Emma akamjibu anaendelea vizuri. Baada ya salamu na mazungumzo mafupi kati ya Emma na Atu, ndipo akamuulizia Naih. Zai na Mia wakageukiana na kucheka. “Makubwa! Leo na yeye anauliziwa!” Mia aliongea kwa kejeli. Naih akajitokeza baada yakusikia Emma anamuulizia.

“Karibu Emma, nilikuwa naosha vyombo huko nyuma. Karibu.” Tatu, Atu na wanae wote walibaki wakiwatizama. Emma akababaika nakushindwa kuzungumza. “Tunaweza kuzungumza pembeni?” Naih akatabasamu. “Bila shida.” Wakasogea pembeni. “Vipi?” Naih akamuuliza baada ya yakuridhika hakuna anayewasikia. “Nina ofisi yangu, natafuta sekretari. Kazi kubwa ni kupokea simu, wageni na kunisaidia mambo madogo madogo ya hapo ofisini. Nitaanza kulipa mshahara wa,” Akamtajia na kuongeza kama kumvutia zaidi. “Na marupurupu mengine.” “Okay. Basi labda uandike tangazo, nitakubandikia hapa. Si unajua hapa wanakuja watu wengi? Nina uhakika utapata tu mtu.” Emma akacheka kidogo.

“Kwa nini isiwe wewe?” “Nani!?” “Wewe Naih.” “Mmmmmmh! Mimi ni….na..” Naih akapaniki na kushindwa kuongea neno. Maisha yalishampiga akafikishwa sehemu akaamini hawezi kuja kukaa ofisini na kufanya kazi za ofisini. “Wewe utanifaa sana Naih. Unakarama ya lugha. Unaongea lugha kwa ufasaha. Kingereza chako kama umezaliwa London bwana!” Naih akacheka kwa wasiwasi sana. Usoni alishabadilika.

“Unafikiri nitaweza!? Nilifeli kidato cha sita.” “Najua, Naih.” “Unakumbuka na kidato cha nne pia nilifeli?” Emma akajaribu kucheka tena kama kumtuliza. “Ni mimi Emma, Naih. Najua kama na kidato cha 4, pia ulifeli. Lakini matokeo ya shule sio ndivyo ulivyo.” “Sijui kama nitaweza Emma! Kukaa kwenye maofisi yenu hayo! Sidhani kama nitaweza. Naomba nikutafutie mtu mwingine. Sitaki kukuharibia kazi. Hapana kwa kweli.” Emma alikuwa akisubiriwa na Kenny.

Ilikuwa lazima Naih aache kazi pale na akaanze kazi ofisini kwake. Jibu la hapana, alijua silo linalosubiriwa na Kenny, lazima aongoze nguvu ya kumbembeleza mpaka akubali. “Nina uhakika utaweza Naih. Ni mambo rahisi sana. Halafu unauelewa wa mambo mengi, hakuna aina ya watu watakao kusumbua. Na mimi mwenyewe pia nitakuwepo, tutaelekezana.” “Sina nguo. Niliibiwa nguo zote, Emma. Nitavaa nini?” Kwa hofu, Naih aliibua vipingamizi vingi tu. Emma akacheka.

“Nguo ni za kununua Naih. Kwa nini usijipe siku ya kesho ya kununua nguo, halafu ukaanza kazi siku ya jumatatu?” Naih akabaki kimya kama anayefikiria. “Nitakupa pesa.” “Pesa ya nguo ninayo. Ila nahisi nimeingiwa hofu!” Emma akatabasamu, kwani ni kweli Naih alionekana ameingiwa hofu. Kufunga na kufungua anapata kazi na mshahara mnono, tena bila kutegemea!

“Au unafurahia hii kazi?” “Hapana Emma. Nilipofeli, nilikosa tumaini, lakini Kenn..”  Akasita na kubadili alichokuwa akitaka kuzungumza. “Sifurahii, Emma. Nilijiambia hii ndio itakuwa ni njia mojawapo yakufikia ndoto zangu. Tunatengeneza pesa nzuri tu hapa. Sema tupo wengi, inabidi kugawana faida, lakini wananilipa mimi zaidi ya wote, kwa kuwa ninakuwa nafanya kazi nyingi kuliko wengine. Ila Emma, ni kazi ngumu! Nakuwa nachoka sana. Kushinda kwenye moto kwa karibia siku nzima sio kazi rahisi, unachoka! Na ikitokea unaumwa, haufiki kazini, ujue ndio hutaingiza pesa, kwa hiyo swala la kuugua hakuna.” “Ndio maana nataka uje tufanye wote kazi, Naih.” “Nikishindwa huko, ujue sitaweza kurudi tena huku, Emma.” “Kwa nini unafikiria kushindwa, Naih?” Naih akabaki kimya akifikiria.

Sura ya Kenny ilianza kumjia akionekana kukasirishwa kwa kushindwa kumbembeleza Naih. Ikabidi aongeze nguvu zaidi. “Tutakuwa pamoja. Usiogope.” “Unafikiri nitaweza?” “Kabisa. Nisingekuwa hapa kama nina wasiwasi na wewe.” Naih akavuta pumzi kwa nguvu. “Nashukuru kwa kuniamini Emma. Nitajitahidi.” “Basi chukua hii pesa itakusaidia kununua nguo kabla hujaanza kazi.” “Ninayo pesa Emma. Asante.” “Chukua tu, zitakusaidia.” Naih akacheka tena kidogo. “Ninazo pesa Emma. Utanilipa nikianza kazi.” “Naomba basi namba yako ya simu.” “Sina simu, Emma.” “Si Kenny alikupa ile Iphone, kwenye birthday yako?” “Mama yake aliichukua.” Emma akakunja uso, Naih akatabasamu. “Lakini si umeniahidi, jumatatu utakuja ofisini.” “Ndiyo, Emma. Labda kitu kibaya kitokee. Lakini nitakuja. Asante sana.” Emma akaondoka na jibu ambalo alijua litamfurahisha Kenny.

Kwa Naih.

“Umemkubali?” Mia akamuuliza mara baada ya Naih kurudi alipokuwa amewaacha pale kibandani. “Kama usipommudu, mpe namba yangu mimi.” Zai alimdaka Naih. Naih akapita moja kwa moja akarudi kule nyuma alipokuwa akiosha vyombo ili kumalizia kazi zake, bila kuwajibu kitu, wakacheka.

Usiku wakati wanalala, aliomba kuzungumza na mama yake. Mama yake akatoka naye nje. Akamsimulia mambo yote aliyozungumza na Emma. “Hela yote hiyo!?” “Hata mimi mwenyewe sikuamini mama.” “Hongera Nai mwanangu.” “Umeona pesa yako haijapotea bure?” Atu akacheka. “Ni hasira za maisha tu Nai. Sikuwa na maanisha. Wakati ule nilikuwa na maumivu ya tumbo, halafu yule mama alikuwa akinikera sana, naona nikamalizia hasira zote kwako.” Naih akatabasamu tu nakuinama kama anayefikiria.

“Bado unataka kujiendeleza na shule?” Atu akamuuliza mwanae. “Nimekuwa nikiweka pesa yangu benki, mama. Nina mpango wa kurudi shule. Lazima nitasoma tu. Pale tunapofanyia ile biashara sio mbali sana na chuo cha CBE. Nimekuwa nikiuliza kwa wanafunzi wanaosoma pale, wanasema kuna madarasa ya jioni, na ada yake sio kubwa sana. Na kwa jiinsi alivyonielekeza Emma, ofisi yake ndio ipo karibu kabisa na chuo. Nikishalipwa mshahara wa kwanza tu, nikichanganya na akiba yangu, nitaanza chuo.” “Utatumia cheti gani na kote huko ulifeli, Naih mwanangu?” Atu akamuuliza kwa upole.

 “Na mimi nilikuwa na wasiwasi huohuo. Nilipozungumza na mmoja wa hao wanachuo, nilimwambia matokeo yangu. Akasema nianzie ngazi ya chini kabisa ya ‘certificate’. Itachukua muda mrefu wa kusoma, lakini inawezekana.” “Unafikiri utaweza? Labda usomee mambo rahisi kidogo, Naih. Sitaki uje upoteze pesa yako bure. Sio kila mtu ameandikiwa kusoma.” Naih aliumia sana. Alijua mama yake amemkatia tamaa kwa kuwa alifeli kuanzia darasa la saba, kidato cha nne na sita. “Usione unajukumu la kusoma sana, Naih. Unaweza kujifunza mambo ya kuchapisha tu. Unamkono mwepesi sana. Najua hiyo utaweza na kukusaidia kuwa sekretari mzuri, mwenye uzoefu wa kuchapisha.” “Nitaangalia. Asante kwa ushauri.” Naih akatulia kidogo.

“Unawaza nini?” Naih akaanza kulia. “Siwezi kuishi hapa mama. Nimeshindwa.” Mama yake akacheka kwa kumuhurumia. “Najua, Nai. Nakuona jinsi unavyoteseka. Sasa utafanyaje?” “Nikianza tu kazi, nafikiri jambo la kwanza nikuhama. Tutahama wote?” “Siwezi Nai. Lazima niwe na hao wadogo zako. Kwanza hapa kwenyewe, Tatu ameniomba tuondoke. Ameshindwa kuvumilia. Na unamjua Tatu. Mpaka amshindwe mtu, ujue hakuna mwanadamu atakayemuweza. Hata mama mwenye nyumba alishaniomba kistarabu kama tunaweza kuondoka. Wapangaji wengine wanalalamikia hizo kelele za wadogo zako, na hivi wanavyochelewa kurudi nyumbani, na wakirudi wanaanza fujo! Wameshindwa kabisa.” Atu aliongea kwa masikitiko.

“Hivi nipo kwenye kutafuta chumba, sehemu ya kuishi nao.” “Kwa nini usiwaache wajitegemee, mama?” “Kuna hata mmoja wao unayemuona ana uwezo wakufanya jambo hapo, zaidi ya umalaya tu? Ukiwauliza kama kuna mwenye akiba, hakuna hata mmoja wao mwenye shilingi! Hawana uwezo wakulipa kodi hao! Acha tu nihangaike nao hivyohivyo.” Naih akanyamaza. “Kuna sehemu Magomeni nimeahidiwa kupata chumba, tunaweza kuhamia huko.” “Mimi naomba nisiwafuate mama. Nitabaki hapa na anti Tatu, mpaka nitakapo pata chumba changu.” Atu akacheka.

“Tatu anakupenda sana, hawezi kukataa kuishi na wewe.” “Basi naomba uzungumze naye.” “Haina shida.” “Ila mama, kesho na kesho kutwa, sitakuja kazini. Nataka nikaanze kujinunulia nguo na kutengeneza nywele.” Atu alicheka tena. “Ndio mambo ya kazi mpya?” “Sio natokea ofisini, halafu wateja wanakimbia! Angalau nifananie kidogo na hiyo ofisi.” “Mbona ile biashara itafungwa!” “Usiseme hivyo mama.” “Kweli tena Nai. Ile mikazi yote pale, unafikiri nani ataifanya? Mimi mgonjwa Nai. Inanibidi kufanya kazi sababu ya maisha tu. Lakini bado najisikia mgonjwa. Hata mimi nakusanya pesa nirudi hospitalini, sidhani kama tumbo langu lipo sawa.” “Pole mama. Lakini nashauri mtafute mtu wa 5, atakaye wasaidia.” “Nitazungumza na Tatu.” Waliongea hapo mpaka Mia na Zai wakarudi na kuwakuta wamekaa hapo nje. Walianza kufanya fujo kama kawaida yao, Naih akaingia ndani kwenda kulala.

Kwa Emma.

Baada ya kuzungumza na Naih, Emma alirudi ofisini kwake moja kwa moja. Akamkuta Kenny amesimama nje. Alijua anachosubiria. “Mbona umesimama nje? Karibu ndani?” “Umezungumza na Nai?” “Hata salamu!?” “Emma please!” Kenny akalalamika. Hakutaka kupotezewa muda. “Anaanza kazi jumatatu.” “Kwa nini jumatatu!?”  Kenny akauliza kwa kushangaa nakumshangaza Emma. “Kwani ulitaka aanze lini!?” “Kwa nini isiwe kesho?” “Kenny!?” “Nauliza tu. Kwa nini mpaka siku zote hizo?” “Leo ni jumatano, Kenny. Ameomba muda wakujiandaa.” “Anajiandaa nini!?” Emma akajaribu kufikiria.

“Tunaweza kuzungumza wakati tumekaa?” “Kwani inachukua muda gani kujibu? Kwa nini unataka kufanya maisha yangu kuwa magumu zaidi ya  hivi yalivyo?” “Samahani Kenny. Nia nikutaka tupate muda mzuri wa kuongea. Kwani leo hauji nyumbani?” “Unajua nini Emma? Basi.” Kenny akaanza kuondoka kwa hasira. “Kenny! Naih aliibiwa nguo. Hana nguo zakuweza kuvaa ofisini. Anataka atumie siku hizi mbili za kujiandaa, angalau anunue nguo.” “Ulimpa pesa?” “Amekataa. Wewe unamjua Naih.” “Mbona alimuibia mama yangu?” “Sijui Kenny. Lakini kwangu amekataa kupokea pesa niliyotaka kumpa, amesema biashara anayofanya imekuwa ikimuingizia pesa. Anahela yakumsaidia kununua hivyo vitu.” Kenny akatulia kidogo.

“Umechukua namba yake ya simu?” “Ulitaka kumpigia?” Emma akamuuliza kwa makusudi kama kumchokoza tu. “Kwa nini nimpigie mimi? Sina shida.” Akakataa kwa kujihami kabisa, Emma akimtizama. “Nilikuwa nauliza tu kwa ajili yako mwenyewe endapo hatatokea hiyo siku ya jumatatu.”  Emma akataka kumcheka, akaona asimuudhi zaidi. “Nai hana simu.” “Ati nini!? Amepeleka wapi ile simu niliyomnunulia siku ya birthday yake?” “Na mimi nimemuuliza swali hilohilo.” “Akajibu nini?”  Kenny akauliza. “Daah! Mimi sijui bwana. Lakini nafikiri unahitaji kuzungumza na yeye mwenyewe. Sitaki kuja kuonekana nahamisha maneno au nachonganisha.” “Labda amewahonga wanaume zake.” Kenny akajibu kwa hasira.

“Nini kingine?” Kenny akauliza kama kuna kingine kilijiri huko, akitaka kujua hata kama Naih alimuulizia. “Ndio hivyo tu.” “Hajasema kitu kingine chochote?” “Kama nini?” Emma akamuuliza, Kenny akatulia. Emma alimuhurumia sana, ikabidi amtulize. “Hatukuwa na muda mwingi wa maongezi, alikuwa na kazi.” “Amezungumzia kitu chochote kuhusu mimi, au hata kuniulizia?” Emma alimuona vile alivyopooza. Kama anayesubiri kusikia kitu alichokuwa akisubiri kwa muda mrefu sana. “Hatukuwa na muda mrefu, Kenny.” Kenny akaumia sana. “Sidhani hata kama ananikumbuka tena.” “Huwezi kujua Kenny.” Kenny akanyamaza, akabaki anaangalia barabarani. Alishakuwa mwekundu kama nyanya. “Kesho nitaenda kununua meza na kiti atakachotumia akianza kazi.” Emma alijaribu kumtoa kwenye mawazo, lakini Kenny hakujibu, akaondoka.

************************

Wadogo zake waliumia sana kusikia dada yao amepata kazi ya ofisini. Walianza kumnyanyasa kwa maneno, huku wakilalamika kuwa Naih anawadharau ndio maana hazungumzi nao. Mara anajitenga nao, kwa kuwa anaona wao hawajasoma. Yakawa maneno mengi kila siku usiku wanaporudi kutoka kazini na kumkuta Naih yupo nyumbani. Siku ya kwanza tu ambayo hakwenda kazini, walianza kuona utofauti. Kazi ziliwalemea, wakarudi hapo nyumbani giza lilishaingia, tena wakitukanana na kusemeana siri zao. Walipigana hapo kwenye chumba cha Tatu, mpaka watoto wa Tatu wakaja kuwatoa.

Wote walilalamikia kazi nyingi, na Mia alikuwa akitegea, akaenda kugawa mwili wake wakati wa kazi. Walitukanana, wakati Atu na Naih wapo kimya. Naih alikuwa amelala kitandani kwa Tatu, wakati Atu amejilaza kwenye godoro. Wapangaji wote walitoka vyumbani kwao na kuja kusikiliza matusi yao. Walitolewa usiku huo, Atu asijue walipolala na kesho yake siku ya ijumaa pia, hawakurudi, ikabidi Naih aende na Tatu na mama yake kuwasaidia kazi.

Siku ya jumamosi, Naih alienda saluni kuchonewa wiving’i fupi. Hapohapo saluni akapata mtu wakumtengeneza kucha. Akaoshwa na miguu. Akatengenezwa vizuri. Naih mtoto wa kimasai akapendeza haswa na nywele alizokuwa ameweka za rangi ya brown kwenye sura hiyo nyeusi. Akaenda kununua na baadhi ya nguo alizojua zitamuakilisha vizuri kazini pamoja na viatu virefu kiasi.

Siku ya jumapili, alishinda akifanya usafi na kumfulia mama yake nguo zake chafu, mpaka ilipofika jioni, wadogo zake ndio wakarudi. Wakaanza kumtania jinsi alivyopendeza. “Lazima aongeze viwango, anaenda kwa mabwana wasomi!” Walimkejeli kadiri ya uwezo wao, Naih hakuwahi kuwajibu. Aliwahi kulala ili asubuhi awahi kazini.

Jumatatu.

Maji yazidi unga.

S

iku ya jumatatu aliamka asubuhi na mapema ili awahi daladala. Lakini isivyokawaida, hakuwaona wadogo zake pale chini, wakati swala la kuwahi kuamka kwao ilikuwa ni msamiati wa kichina! Akastuka na kuruka kitandani kuangali begi lake. Hakulikuta. Safari hii hawakumbakishia hata mswaki. Walimuibia kila kitu, mpaka hilo begi jipya alilokuwa amelinunua baada ya kumuibia la kwanza alilokuwa amenunuliwa na Kenny. Walimbakiza na hizo nguo alizokuwa amelalia tu. Mpaka nguo mpya alizokuwa amenunua kwa ajili ya kuanza kazi, viatu na pesa chache alizokuwa amechukua benki kutoka kwenye akiba yake, pia waliondoka nazo.

Naih alilia kwa uchungu sana. Alilia bila kunyamaza. Atu na Tatu waliumia sana. “Lakini Atu, lazima uwasaidie hao wanao. Mwisho wao sio mzuri. Watakuja kukuua hata wewe mwenyewe.” Tatu aliongea kwa uchungu sana. Naih hakujua cha kufanya. Alibaki akilia siku nzima.

 ************************

Ilipofika mida ya saa nne, Kenny alimpigia simu Emma kutaka kujua kama Naih ameshafika kazini. “Sijamuona mpaka sasa hivi.” Kenny akatulia kwa muda mrefu sana kwenye simu. “Kenny!” “Unajua anapoishi?” “Nilichosikia watu wakiwaita ni ‘Malaya wa Kwa Mfuga Mbwa’. Basi. Sasa sijui ni mtaa, au ndio jina lao! Sikumuuliza Naih.” “Alionekana na utayari wakuanza kazi?” “Wewe unamjua Naih. Mwanzoni alisita sana, kuonyesha hofu ya kufanya kazi ofisini. Nilipozungumza naye sana, ndipo akasema atakuja leo. Sasa sijui kama alinijibu tu niondoke au alikusudia kuja.” “Naih ninayemfahamu mimi sio muongo. Labda awe amepatwa na matatizo, au amebadilika kama mama alivyotuambia. She is always true to her words.” “Basi tumpe muda. Labda atakuja.” Kenny akajikuta akimtetea Naih kuwa ni mtu wa maneno yake. Si muongo.

************************

Siku hiyo na ya jumanne ikapita bila Naih kutokea kazini. Kenny alikuwa anakaribia kuchanganyikiwa. Hakuwa akila wala kunywa. Midomo ilikuwa imemkauka. Emma alikuwa akimuacha kwake, na kumkuta alisharudi kutoka kazini. “Leo nitaenda kumuangalia pale alipokuwa akifanya kazi.” Emma alimtupia neno Kenny aliyekuwa amejilaza kwenye kochi, asubuhi hiyo ya siku ya jumatato. Kenny hakujibu akabaki kimya. “Nitakupigia simu, mara baada yakuzungumza naye.” “Okay.” Kenny akajibu kwa kifupi tu, Emma akaondoka na kumuacha mwajiriwa huyo amejilaza kwenye kochi.

Hatimaye!

E

mma alipofika ofisini, alimkuta Naih akimsubiria nje. Emma alitamani kuruka amkumbatie, lakini akajikaza kiume. “Samahani nilishindwa kuja siku ya jumatatu. Nilipatwa na matatizo.” “Hamna shida kabisa. Karibu.” Emma akafungua mlango, akamkaribisha ndani. “Ofisi yangu ni ndogo tu. Tupo mimi, kijana wa masoko na muhasibu, basi. Hiyo ndio itakuwa meza yako na kiti chako. Karibu ujisikie upo kikazi.” Naih akatoa tabasamu akishangaa asiamini kama amerudishwa kwenye kiyoyozi, upepo uliochujwa, AC. “Asante.” “Kaa hapo, unisubiri. Nitakuja sasa hivi.” Emma akatoka nje.

          Hapo hapo akampigia simu Kenny na kumtaarifu ujio wa Naih. “Mzima?” Kenny akauliza kwa upole. “Mimi namuona mzima japo alisema alipatwa na matatizo ndio maana hakutokea siku ya jumatatu kama tulivyokubaliana na jana. Sikumuuliza ni matatizo gani. Ila amependeza sana.” Akamsikia Kenny akivuta pumzi kwa nguvu, akanyamaza. “Tutaongea baadaye basi.” “Asante sana Emma. Nakushukuru.” “Anytime, men! Anytime.” Wakakata simu.

************************

Mpaka juma hilo kuisha, tayari Naih akawa amefahamu mambo mengi ya pale ofisini. Alimsaidia sana Emma, na wafanyakazi wenzake tofauti ya alivyotegemea. Ofisi ikageuka ikawa safi. Alipangilia vitu vizuri, nakuwasaidia kazi ndogo ndogo. Walianza kumpenda Naih. Utani wa hapa na pale haukuisha. Na Naih naye alijifanya msaidizi kweli kweli. Kila walipoingia ofisini, alihakikisha anawawekea chai au kahawa mezani kwao. Na saa nne hivyo hivyo. Mchana kuna mahali huwa wana wapigia simu na kuagiza chakula wanachotaka, huwaletea hapo ofisini. Basi Naih aliwaazishia utaratibu wa kuwawekea kwenye sahani na kuwatengea mezani. Waliacha kula kwenye mifuko, wakawa wanakula kistaarabu. Walikuwa hawana urafiki mle ndani, lakini Naih akawafanya wakawa wanakaa pamoja na kula, huku wakitaniana wao kwa wao. Emma alimfurahia sana Naih.

************************

Tatizo likabaki la kule anapoishi. Hakutaka kuendelea kuishi kwa Tatu tena. Kwani mama yake hakupata chumba alichotarajia, akajua wadogo zake watakaporudi, mambo yatarudi kuwa kama zamani. Ule utulivu wanaopata wakati hawapo, utaisha, na watamuibia tena. Alianza kutafuta chumba kila siku anapotoka kazini. Bei ikawa inamshinda. Aina ya chumba alichokuwa akitaka na pesa aliyokuwa nayo, havikuwa vikiendana. Alizunguka mitaa aliyodhani angeweza kuishi, akashindwa. Akajiambia ataendelea kuvumilia kuishi hapo kwa Tatu, mpaka atakapopata mshahara wa miezi miwili.

************************

Siku moja Emma alimtuma benki kufuatilia ‘bank statement’ ya mwezi uliopita. Naih akaenda. Kijana aliyemuhudumia pale benki alikuwa ni yule kijana aliyekuwa akisoma CBE, waliyekutana kwenye mgahawa aliokuwa akifanya kazi Naih, ‘Malaya Pub’. “Kumbe na wewe unafanya kazi!?” “Najiendeleza na shule, dada yangu. Nilipata kazi nikiwa nimemaliza tu kidato cha sita. Nikaamua nifanye kazi huku nasoma.” “Ni ngumu sana?”  Naih aliendelea kudadisi. “Kila kitu nikujipanga tu. Inawezekana.” Yule kijana alijibu huku akitoa tabasamu.

“Nina maswali mengiiii! Natamani tupate muda tuzungumze.” “Leo jioni sitakwenda chuoni. Mwalimu hatakuja. Naweza kukupitia ofisini baada ya kazi.” Naih akalifurahia hilo wazo. “Nitashukuru sana. Ulisema jina lako nani tena?” “Naitwa Tuse.” “Tuse kama Tusekeleghe?” Naih akamuuliza. Tuse akacheka. “Na wewe ni wanyumbani nini?” Tuse akauliza. “Mama ni mtu wa Mbeya, ila baba ni Mmasai.” “Safi sana. Kumbe ni wanyumbani! Tutaongea zaidi nikija jioni.” Naih alitoka hapo akiwa amejawa na tabasamu.

Ilipofika jioni wakati wanakaribia kufunga, wote wakiwa wamemsimamia Naih mezani kwake wakiagana, Tuse akaingia. “Nilidhani nitapotea! Kumbe ofisi yenyewe naifahamu. Pako wazi kabisa.” Naih akasimama. “Karibu Tuse. Nikweli hapapotezi. Karibu.” Wote walibaki wakiwatizama. “Huyu anaitwa Tuse. Tuse huyu anaitwa Emma, ndiye bosi wetu, huyu ni muhasibu wetu na huyu ni mtu wa masoko.” Tuse alionekana kijana mwerevu, aliwapa mkono huku akisalimiana nao. “Nisubiri kidogo, kuna kitu namalizia, tutaondoka sasa hivi.” “Hamna shida.” Tuse akajibu kiungwana. “Karibu ukae hapo. Chukua na gazeti hili usome wakati unanisubiria.” Tuse akacheka kidogo kisha akapokea gazeti na kukaa. Naih alimalizia kuandika mambo fulani, wakaagana na kutoka na Tuse.

Walitafuta mahali wakakaa. Naih akauliza maswali mengi sana juu ya shule, Tuse naye akayajibu na kumsisitiza apate muda wa kwenda chuoni akiwa na vyeti vyake vyote, ili wamshauri chakufanya. “Nashukuru kwa ushauri. Jumatatu nitaenda. Kesho nitajitahidi kufuatilia vyeti vyangu vyote kwenye shule nilizosoma, ili niwe navyo tayari.” “Utafanikiwa tu.” “Lakini ninashida sana na chumba. Halafu maeneo ninayotamani kuishi ni ghali sana.” “Ulitaka kuishi wapi?” Tuse akauliza.

“Nataka maeneo ya karibu na hapa. Angalau niwe napanda basi moja tu mpaka hapa kazini, isiwe mbali.” “Mimi naishi Makumbusho. Nilichukua kinyumba kidogo cha uwani chenye vyumba viwili, nikawa naishi na mwenzangu. Ila alihamishiwa Dodoma kikazi, sasa ameniacha pale peke yangu. Kodi kubwa na mimi nakazana kumaliza hii shule.” Naih alijiweka sawa. “Umesema ni vyumba viwili?” “Vyumba ni viwili, lakini jiko na sebule ni moja.” “Vyoo?” Naih akauliza tena. “Kila chumba kina choo chake.” Naih alitaka aende naye jioni hiyo hiyo akaone. Tuse akamkubalia.

Alipokiona chumba, akamwambia Tuse anahamia siku ileile. “Labda kesho ili leo tusafishe.” “Nasafisha sasa hivi, wakati panakauka, naenda kufuata mizigo yangu.” Tuse alikuwa akicheka sana. “Yaani dada unahamia leo!?” “Sasa hivi.” Walisaidiana kusafisha, wakaenda pamoja nyumbani kwa Tatu. Alimkuta mama yake amejilaza. “Vipi mama?” “Nimechoka tu. Mbona uso wa furaha?” “Nimepata chumba cha kupanga. Nitaenda kuishi na mtu.” “Kitanda na godoro?” “Nitajua huko mbele ya safari, mama. Acha tu niende.” Atu akacheka.

“Si utakuwa unakuja tulale wote?” Naih akamuuliza mama yake. “Nikichoka na kelele, nitakuwa nakuja kupumzisha kichwa changu huko kwako. Hata siku mbili ndio narudi huku.” Walicheka kidogo, Naih akachukua vitu vyake akatoka kumfuata Tuse aliyekuwa akimsubiria kituoni. “Mizigo iko wapi?” Naih akacheka. “Ndio hii hapa nimemaliza.” Tuse akashangaa. Naih alikuwa na kijibegi kidogo tu, tena hata hakikuwa kimejaa. “Utalala wapi? Mbona huna hata godoro?” “Wewe usijali. Hayo mambo mengine yatafuata.” Wakapanda daladala, wakarudi kwao. Tuse alimuona vile Naih anavyofurahia, lakini akabaki na maswali ya kwa nini alimtaka abaki kituoni akimsubiria na si waongozane mpaka kwake!

Naih aanza maisha yakujitegemea akiwa na Tuse.

M

aisha yakaanza. Siku ya jumamosi ambayo hakwenda kazini, aliongozana na Tuse mpaka Kariakoo kununua vifaa alivyotaka. “Kumbe una gari?” “Huwa situmii mara kwa mara. Naikodisha, ili iniingizie pesa.” “Unakodisha wapi?” “Mungu alinisaidia nikapata tenda palepale benki. Wanatumia kitengo cha mikopo. Nilipata hiyo kazi. Nikatafuta dereva. Kwa hiyo wanatumia pale benki.”  “Hongera sana.” Tuse akacheka. “Unacheka nini sasa badala useme asante?” “Haya, asante na ninamshukuru Mungu.” Tuse alizunguka na Naih, mpaka walipopata kila kitu alichohitaji. Akamsadia kufunga kitanda, na chandarua. Kwa mara ya kwanza Naih akalala kitandani kwake na nyumbani kwake.

Siku inayofuata ya jumapili, Tuse alikwenda kanisani akamuacha Naih amelala. Naih alipoamka, akaamua kupika na kumuachia chakula Tuse. Maisha ya umoja kati yao yakaanza. Tuse akaanza kula nyumbani, sio kwenye migahawa tena. Na kama Naih hatapika, basi walienda kula wote. Wakaanza kupitiana kila wakitoka kazini na kurudi wote nyumbani. Wafanyakazi wenzake Naih wakaanza kumtania Naih kuwa amepata mchumba. Naye Naih hakuwahi kukanusha, akawa anacheka tu, kitu kilichoanza kumtia wasiwasi Emma.

Tuse alikuwa kijana mcha Mungu wa kweli bila hila. Kila neno analotamka la kwanza, la pilli ni Mungu, na uweza wake. Mambo yake mengi aliyafananisha na maneno ya kwenye bibilia. Naih alikuwa akimwangalia tu. Alikuwa akianza kuomba, mpaka Naih anasimama kwenda kulala anamuacha bado anaomba. Naih alimpenda kwa kuwa alikuwa kijana aliyetulia sana, sio kama kina Kenny aliowahi kuishi nao wakipenda na kuabudu ngono. Tuse alionekana hana hata wazo la mwanamke. Naih alikuwa akimshangaa sana Tuse. Alionekana kijana wa kisasa, lakini mwenye misimamo mikali sana. Akaamua kwenda naye taratibu.

Ule utulivu aliokuwa akiupata kazini na nyumbani kwake, ulimfanya Naih kuanza kupendeza. Chuoni walipokea vyeti vyake wakamshauri aanzie ngazi ya chini kabisa, certificate kama alivyokuwa ameshauriwa na Tuse. Akakubali, akawa anasubiri mwaka huo uishe, ili ajiunge rasmi muhula mwingine utakapo anza. Kwa kuwa walilipia kodi pamoja na Tuse, aliweza kuhifadhi pesa zake benki, huku nyingine akijaribu kuishi maisha aliyokuwa akiyatamani, na kumsaidia mama yake.

************************

Alishangaa kuona anazidi kuongezewa marupurupu kila wakati kwa sababu tofautitofauti. Baada ya mwezi mmoja tu kuisha tangia aanze kazi, akapewa simu ya thamani sana. Akaambiwa ni ya ofisi. Akawa analipwa mshahara na pesa za simu. Baada ya muda kidogo, akaambiwa anaongezewa pesa ya usafiri na chakula. Naih alikuwa akishangaa, lakini akajua ndivyo wafanyakazi wote wanavyolipwa. Hakuwahi kumuulizia Kenny hata mara moja. Ni kama aliyejionya kutolitaja hilo jina kinywani mwake.

Wivu juu ya Tuse, ukaanza kumsumbua Emma, kana kwamba yeye ndio Kenny. Kila alipotaka kumpa lifti ya kumrudisha nyumbani, Naih alimwambia anamsubiria Tuse warudi naye nyumbani, au kuna mahali anapitia kabla ya kwenda nyumbani. Hakuwahi kupanda gari ya Emma. Emma alivumilia, akashindwa. Akaenda kumsimulia Kenny “Naih amebadilika sana. Hakuwa na mtindo wakuzoeana na wanaume.” Kenny akalalamika. Hasira zikamzidi.

“Ndio maana hanikumbuki tena!” Akaendelea kulalamika. “Unafikiri wanaishi pamoja?” “Sina uhakika. Ila naona pale ofisini wakimtania kama ni mchumba wake, anacheka tu. Hakanushi” Kenny akazidi kukasirika. “Itabidi nimuhamishe pale.” Emma alishituka sana. “Unampeleka wapi tena!? Namuhitaji sana Naih. Ananisaidia kazi pale!” Kenny akamshangaa Emma. “Mwanzoni nilipokwambia umuajiri, ulinijibu nini!? Mimi ndiye niliyemuajiri, na ndiye ninayemlipa mshahara. Ninaamua afanye wapi kazi. Nai ni mfanyakazi wangu mimi, sio wako. Usije kulisahau hilo hata mara moja, Emma.” “Basi Kenny. Naomba tusigombane.” Kenny alitoka usiku huo, hakulala kwa Emma. Emma alijuta kumletea maneno Kenny.

Alfajiri ya saa kumi hata Emma hakuwa ameamka, akashitukia taa ya chumbani kwake imewashwa, Kenny amemsimamia kitandani kwake. Emma alibaki akimtizama. Alionekana wazi hakulala. “Vipi?” Emma akamuuliza. “Nataka uniajiri.” Emma alivuta pumzi kwa nguvu, akakaa. “Kwa nini tena?” “Sijui, wewe niajiri tu.” “Utafanya nini pale, Kenny? Biashara yenyewe bado ndogo.” “Naweza mimi nikakulipa kwa kipindi hichi tunachofikiria kitu chakufanya.” “Mbona wewe una kazi, Kenny? Mama Ole anakutegemea!” “Acha kuzungumzia juu ya majukumu yangu! Wewe nipe kazi yeyote ofisini kwako. Nipe ofisi, nianze kazi.” Emma akabaki akifikiria huku amelemewa na usingizi. Hakuwahi kumuona Kenny mkorofi asiye ambilika kama huyu. Alijawa hasira, halali, kazi hafanyi na wasichana pia hataki tena.

“Umezungumza na Nora siku za karibuni?” Ikabidi Emma aulize tu. “Hapana. Kwa nini?!” “Kwa kuwa nafikiri unahitaji kufanya kitu Kenny. Unachanganyikiwa!” “Hata kidogo! Mimi nipo sawa kabisa. Ila ninachotaka ni kazi ofisini kwako. Naweza kununua nusu ya biashara yako tukawa tunafanya wote biashara.” “Biashara gani ile, Kenny!?” “Sisi tumefundishwa kufikiria vitu vikubwa. Kwa hiyo huu ndio wakati muafaka wakufikiria na kufanya kitu chetu.” “Sasa hivi ni saa kumi usiku. Hata hapaja pambazuka! Kwa nini tusilale tukapata muda wakufikiria asubuhi, tukiwa tumepumzika na akili nzuri. Nenda kalale Kenny.” “SITAKI KULALA. NATAKA UNIAJIRI OFISINI KWAKO. NI KIPI KIGUMU USICHOELEWA EMMA?” Kenny aligomba. Akaongea kwa sauti ya juu sana.

Emma alijua kinachoendelea kichwani mwake. “Naomba utulie, Kenny! Unajua siwezi kukukatalia jambo. Nilitaka upate muda wakufikiria.” “Nani amekwambia sijafikiria? Unafikiri mimi nilikuwa nimelala tu kama wewe? Nilikuwa nikifikiria, ndio maana nimekuja hapa.” “Unakumbuka tangia watoto tulikuwa tukimwambia Jay, tutafungua biashara yetu. Tutafanya kazi pamoja?” “Sasa kwa nini unanizungusha?” Kenny akamuuliza Emma.

“Nafikiri upo sahihi. Huu ni wakati muafaka wa kuanza kufanya kitu chetu na kuacha kutegemea wazazi.” “Naona sasa hivi umeanza kuongea vitu vinavyoeleweka.” Kenny alipanda pale kitandani na viatu vyake.

“Na ninapofika pale kazini, nataka Naih afanye kazi chini yangu mimi na si vinginevyo.” Emma hakutaka kubisha, akajua ile hali ya usingizi ndio inayomfanya kuwa mkorofi zaidi. “Umenisikia?” “Sawa.” “Nataka kuanza kazi mapema, hata leo.” “Labda leo nikakuandalie ofisi, Kenny. Nitakutafutia meza nzuri na kiti chako, kwenye ofisi ya muhasibu ambayo ipo karibu na meza ya Naih.” Hapo alimuona amekubali, akaanza kusinzia. Emma alisimama na kuzima taa, akarudi na yeye kulala. Mpaka anaamka kwenda kazini, Kenny alikuwa bado amelala.

************************************

Emma alifika kazini, akawataarifu wafanyakazi wake akiwepo Naih, kuwa ameingia ubia na mtu mwingine, kuanzia kesho yake huyo mtu ataanza kufanya pale kazi. Akamwambia muhasibu ahamishe ofisi yake kwenye ofisi ya masoko. Kuwa muhasimu na mtu wa masoko watatumia ofisi moja. Kila mtu akaelewa. Hapakuwa na maswali. Siku ikaanza.

Kenny naye  aanza kazi, ofisini kwa Emma.

S

iku inayofuata, wakiwa wote wameanza majukumu yao ya kila siku, Naih akiwa ameinamia komputa yake, akashangaa Kenny anaingia, “Nahitaji kahawa.” Alitoa maagizo hayo bila salamu, akapitiliza moja kwa moja kwenye ofisi mpya. Meza ya Naih ilikuwa wazi tu, karibu na mlango wa kuingilia hapo ofisini. Yeyote anayeingia anamuona. Naih akabaki amekunja uso, akiwa hajui kinachoendelea. Hakujua kama Kenny ndio bosi mpya, na hakujua kama hiyo kahawa ametumwa yeye. Akabaki pale kwa muda akitafakari. Kenny alitoka nakuanza kumgombesha sana Naih. Naih alibaki akimtizama.

“Sijadharau, lakini sikujua kama unazungumza na mimi!” “Kulikuwa na watu wangapi hapa wakati naingia ofisini?” Kenny aliendelea kugomba, Emma akatoka ofisini kwake kwa haraka. “Naih, naomba ukatengeneze hiyo kahawa sasa hivi.” Akiwa kwenye mshtuko, alisimama akaelekea jikoni kutengeneza hiyo kahawa. Hakujua kama aweke maziwa au aache. Hakujua kama anataka awekewe sukari au la! Ofisi nzima ilijua kama Kenny ameingia, sababu ya kugomba. Naih alitoka na ile kahawa, akagonga ofisini kwa Kenny kwa muda bila kukaribishwa. Mwishowe akaamua kuingia tu.

Alimkuta amegeukia kompyuta yake. “Ungependa niweke maziwa na sukari?” Kimya. Naih akaweka kile kikombe pembeni yake. Akaenda kuleta maziwa na sukari na kuweka pembeni yake, akatoka. Wakati anatoka tu, “Hii kahawa ni baridi sana. Siwezi kunywa jinsi ilivyo.” Naih akarudi kuchukua kile kikombe cha kahawa ili akapashe moto. “Na sina mpango wa kufungua mgahawa hapa ofisini kwangu.” Naih akaelewa kuwa anatakiwa kuondoa yale maziwa na sukari. Akabeba ile kahawa na sukari, ili avirudishe jikoni ndipo arudi kuchukua yale maziwa. Wakati anatoka na vile vitu ameshika mkononi, “Sitaki kuyaona na haya maziwa hapa.” “Nitarudi kuyafuata.” Naih akajibu, Kenny akanyamaza.

Alifikisha vile vitu jikoni, akarudi ofisini kuchukua yale maziwa, akakuta nusu yamemwagika kwenye meza na sakafuni. “Mbona ni kazi ndogo tu hii niliyokupa? Nini kilichokushinda kutengeneza kahawa tu, ukaamua kuniletea kila kitu humu ndani? Inakuwa kama unaniziria, au unafanya jeuri! Kama unaona huwezi kunifanyia kazi, uniambie mapema, nitafute mtu mwingine.” Naih hakujua yale maziwa yalimwagikaje, lakini lawama zilikuwa juu yake. “Nitakuja kusafisha hiyo meza na sakafu. Samahani.” Naih akajibu. “Kama unaona shida kunifanyia mimi kazi, uniambie mapema. Usinibabaishe.” Naih hakuwahi kumuona Kenny wa namna ile hata mara moja tokea anazaliwa. Alikuwa kama faru aliyejeruhiwa.

 “Sasa unataka kazi au hutaki?” Kenny akauliza kwa jeuri kama asiyetaka kubabaishwa. “Nataka kazi.” Naih akajibu kwa upole. “Basi fanya vile ninavyotaka mimi.” “Sawa.” Naih akajibu, akaenda kuchukua kile kikombe kilichokuwa na maziwa, akatoka. Baada ya muda alirudi kusafisha meza na sakafu. Alipomaliza, akaenda kupasha ile kahawa moto, akaenda ofisini kwa Emma. “Unafikiri niweke nini kwenye kahawa yake?” Emma alianza kumuhurumia Naih. “Nusu maziwa, nusu kahawa. Weka kijiko kidogo cha sukari. Kimoja tu, lakini usijaze. Halafu ifanye iwe ya moto sana.” “Asante.” Naih akashukuru na kutoka kwa haraka.

Alipotengeneza kahawa kama alivyoelekezwa na Emma, ndipo akaipeleka ofisini kwa Kenny. “Karibu.” Naih aliiweka chini. “Baada ya dakika kumi uje na karatasi na kalamu.” Kenny akaamuru huku akichukua kile kikombe cha kahawa. Alipoona anatoka mle ndani hajaitwa, akajua amepatia ile kahawa. Alirudi kwenye meza yake akiwa kwenye mshituko.

Emma akatoka. “Una kazi yeyote sasa hivi?” “Namalizia kuandaa kalenda yako, nikuletee uone vitu unavyotakiwa kufanya leo na kesho. Lakini unatakiwa kwenda kukutana na mteja mpya wa ile shule ya Kunduchi, saa 5 ya asubuhi hii. Sijui unakumbuka? Nilikwambia jana.” “Haina shida. Na shule ile ya Kibaha wameongeza oda?” “Nimekuta fax yao asubuhi hii, nimempa Kasimu. Naona anaandaa, atakuonyesha.” “Afadhali. Nilikuwa naingojea hiyo oda kwa hamu kweli! Sijui ni kubwa au kama kawaida yao!?” “Nimeona Kasimu amefurahia. Naona mambo sio mabaya. Na..” “Nilikwambia baada ya dakika kumi uje.” Walishangaa mlango umefunguliwa na Kenny ametoka. “Nilikuwa naongea na Emma.” “Kwa hiyo mimi sina maana?” Emma akarudi ofisini kwake, Naih akachukua kalamu na kijitabu kidogo akasimama.

Kenny akampisha mlangoni, akaingia, kisha Kenny akamfuata nyuma. Naih akasimama akiwa ameshika kalamu na karatasi tayari kwa kuandika, “Bunge, Chamwino, Chuo kikuu cha St. Johns, Soko la Chamwino… Unaandika lakini?” Kenny aliuliza kwa ukali. “Nimeandika.” Naih akajibu. “Mpaka sasa una maeneo mangapi?” “Maeneo manne.” “Tutaanza na hayohayo. Piga simu kuanza kuulizia kama hayo maeneo yana viwanja vinavyo uzwa, na ni kwa kiasi gani? Nataka kujua ukubwa wa hivyo viwanja. Nani muuzaji. Serikali au watu binafsi.” Naih alibaki amepigwa na butwaa. Hakujua habari zote hizo atazipataje. “Umenielewa?” “Ndiyo.” Kenny akageuza kiti, akaendelea na shuguli zake. Naih akasimama pale kwa sekunde kadhaa, akaamua atoke.

 

Alikwenda moja kwa moja mpaka ofisini kwa Emma. “Samahani Emma. Naomba msaada wako. Nawezaje kujua kama haya maeneo yana viwanja na bei zake?” Emma akaangalia. “Halafu wala sijui haya maeneo yenyewe yako wapi?” Emma akarudia kusoma kwa makini. “Maeneo yote haya yapo Dodoma.” “Dodoma!?” Naih akashangaa, Emma akacheka. “Nitafanyaje!?” “Yupo rafiki yetu amehamishiwa Dodoma kikazi. Alikuwa akituambia huko kuna viwanja vinauzwa kwa bei nzuri. Nitakupa namba yake, na mimi nitamuandaa kuwa utampigia, kisha umuulize hayo maswali yote.” Naih alivuta pumzi kwa nguvu kama aliyepata aghueni kubwa.

“Asante sana Emma. Utakuwa umenisaidia sana. Asante.” Emma akamwandikia namba kwenye kikaratasi, kisha akampigia simu huyo rafiki yao. Naih alitoka baada yakusikia zinaanza stori na vicheko vingi. Akarudi kukaa kwenye meza yake, baada ya muda Emma akatoka. “Unaweza kumpigia sasa hivi.” “Asante Emma.”

Naih akapiga, baada ya muda mfupi simu ikapokelewa. Akajitambulisha, na kwenda moja kwa moja kwenye maswali. Huyo mtu alimtajia maeneo mengine zaidi aliyodhani yangefaa kuwekeza, akampa bei kwa hakika, kwani na yeye alikuwa kwenye zoezi hilo la kutafuta maeneo ya kujenga. “Na mashamba huko inakuaje?” Naih akauliza. Akatajiwa maeneo yaliyokuwa na mashamba na bei zake. Akawa anaandika kila kitu. Akampa namba ya simu ya dalali aliyemwambia ni mwaminifu, atamsaidia. Naih alishukuru sana, akakata simu.

Akageukia kompyuta na kuanza kuandika kila kitu kwa mpangilio. Aliandika kwa usafi, akahakikisha hajaacha kitu hata kimoja. Chini akaweka namba za simu za dalali na rafiki yao. Akamtumia Kenny kwa barua pepe.

Ulipofika muda wa chakula cha mchana, Naih alienda kumuaga Emma, na kumwambia kuna mahali anakimbia mara moja, baada ya muda mfupi atarudi. Emma akamruhusu, Naih akatoka. Baada ya dakika 45, akarudi na kukuta Kenny anagomba. Amekuwa mwekundu kama moto. Naih akaingia taratibu akakaa mezani kwake, huku akimwangalia Emma kwa uso wa wasiwasi, kama anayeuliza kulikoni.

Kenny akamgeukia na kuanza kugomba upya. “Nilikutumia tokea asubuhi! Kila kitu niliweka pamoja nikakutumia kwa barua pepe. Sijapuuza kitu hata kimoja.” “Kwa nini unitumie kwa email, maelekezo niliyokupa kwa mdomo?” “Jana jioni Emma alitupa email address yako. Akasema tuwe tunakutumia kazi zote unazotupa kwa email, kama tunavyofanya kwake.” “Unavyoniona mimi, nafanana na Emma?” “Hapana. Samahani.” “Naih! Naih!” Emma akaingilia.

Akamgeukia Emma. “Print hiyo kazi, kisha umpelekee ofisini kwake. Kila kazi utakayokuwa ukipokea kutoka kwake, itabidi uulize jinsi ya kurudisha, ili kusitokee mchanganyiko kama leo. Alidhani hukufanya.” Naih akageukia kompyuta yake kwa haraka sana, Kenny akarudi ofisini kwake. Emma akabaki akimtizama Naih.

Alimaliza akachukua ile karatasi kutoka kwenye mashine, na kurudi ofisini kwa Kenny. “Kila kitu nimeandika hapa. Nimebahatisha na namba ya dalali, nimeweka hapa ili ukiangalia, na kupenda moja ya hayo maeneo, tumpigie. Niliuliza pia bei ya mashamba, kama ungependa kuyaangalia. Nimeweka hapohapo. Kote nilipoweka herufi SH, ujue ni mashamba. Na bei zake zipo hapohapo pembeni. Kama kuna swali la nyongeza, nitapiga tena simu ili kuwauliza.” Naih alijitahidi kutulia na kutoa maelekezo bila kuonyesha kuchanganyikiwa. Kenny aliichukua ile karatasi na kuanza kuisoma.

“Umeletewa chakula?” Naih akamuuliza. “Na nani?” Kenny na yeye akamuuliza kwa jazba. Naih akatoka, na kwenda ofisini kwa Kasimu. Wote walinyanyua uso alipoingia. “Kwema huko? Mbona kelele haziishi?” Naih akacheka taratibu. “Mliletewa chakula?” Naih akawauliza. “Chakwako kipo mezani.” “Bosi mpya hajaletewa?” “Mmmh! Hakuna hata aliyeweza kumsogelea ofisini kwake na kuuliza anataka nini?” Naih akacheka nakutoka.

Alikwenda kumpashia kile chakula Kenny, akarudi nacho ofisini kwake. “Sili wali wa mtaani.” Kenny aliongea kwa jeuri bila hata kumuangalia Naih. Naih akatoka na kile chakula, akarudisha jikoni, akatoka kwenda kununua matunda, na juisi. Akarudi kwa haraka kuyaosha na kukatakata, akaweka kwenye sahani, pamoja na juisi, akarudi ofisini kwa Kenny. “Sili matunda ya mtaani.” “Haya matunda nimetengeneza mimi mwenyewe hapo jikoni. Naomba uyale, wakati tunasubiria chips. Wameniambia wataniletea baada ya nusu saa.” Kimya. Naih akatoka na kuyaacha yale matunda pale mezani.

Baada ya dakika 45 hivi, akaletewa chips, mayai na firigisi. Akaweka kwenye sahani vizuri, akampelekea ofisini. Alipoona kimya, akajua vimepokelewa. Akatoka na sahani tupu aliyokuwa ameweka matunda. Pakatulia, mpaka jioni alipomuona anatoka ofisini kwake, akajua siku ndio imeisha. Alitoka bila kuaga mtu yeyote, kitu ambacho si cha kawaida pale ofisini kwao. Kila aliyekuwa akitoka, lazima wapitie mezani kwa Naih. Wataniane kwanza, wacheke ndipo waondoke. Naih na Emma ndio walikuwa wamwisho siku zote. Siku ya Naih ilikuwa ikiisha pale Emma anapokuwa na yeye anataka kutoka ofisini.

************************************

Asubuhi yake Naih alichelewa kuingia ofisini, akakuta anasubiriwa yeye. Kenny alikuwa kigomba, kama amerukwa na akili. “Ni leo tu nilipatwa na dharula. Lakini huwa sichelewi kazini.” “Hatuwezi kufanya kazi kwa mtindo huo. Kila mtu akileta matatizo yake hapa kazini, unafikiri tutaweza kufanya kazi? Hii ni kazi. Uniambie kama unaweza kufanya kazi au huwezi.” Kimya. “Nakuuliza wewe. Unataka hii kazi au hutaki?” Mpaka Emma akamtizama Naya, akajua siku hiyo ndipo ataacha ile kazi. “Kwanza naomba unisamehe kwa kuchelewa. Sitarudia tena. Pili ndiyo, ninaitaka hii kazi.”  Naih alijibu kwa utulivu tu, Emma hakutegemea. Kenny akaingia ofisini kwake, Emma akabaki akimtizama Naih. “Nilitakiwa kufanya nini!?” Naih akauliza kwa kunong’ona, Emma akapandisha mabega, kwamba hajui.

Kama aliyekumbuka kitu, akasimama kwa haraka sana. “Wapi tena?” Emma akauliza kwa sauti ya chini. “Kahawa.” Naih akanong’ona, Emma akacheka na kutingisha kichwa, akaingia ofisini kwake. Naih alitengeneza kahawa haraka sana kama ya jana yake, akampelekea ofisini pamoja na kitafunwa. “Ni bajia za dengu. Naamini utazipenda.” Naih akaweka chini, bila kujibiwa. “Ungependa na pilipili?” Kimya. “Nitaweka hapa pembeni pamoja na limao. Huwa ni nzuri sana.” Naih aliweka pembeni yake hapohapo mezani. “Angalia wakati unageuka. Kahawa ni ya moto sana.” Naih akasogeza mbali kidogo na mkono wake, akaondoka. Alimuacha bado anaangalia kompyuta yake, bila hata kugeukia kile chakula.

Siku hiyo Naih hakuthubutu hata kutoa mguu wake nje ya ile ofisi. Alimuagizia ndizi za kukaanga na kuku wakuchoma. Akampelekea na soda. Hakusema kitu, Naih akajua amependa. Ilipofika kama saa kumi jioni, akampelekea matunda na maji ya kunywa. Baada ya muda, akatoka tena bila kuaga. Siku ya pili ikaisha.

Siku ya tatu, Naih ndiye aliyekuwa wa kwanza pale ofisini. Emma alifika akamfungulia mlango, akaanza kusafisha ofisi ya Kenny kwanza ndipo akaendelea kusafisha kwengine. Aliposikia akisalimiana na Emma, akakimbia kutengeneza kahawa yake. Siku hiyo Naih alikuwa amemletea chapati. Aliziangalia kwa muda, kisha akageukia kompyuta yake. “Kama hutazipenda hizo chapati, naweza kwenda kukununulia bajia kama zile za jana.” Kimya. Naih akataka kutoka. “Kesho asubuhi tunakwenda Dodoma!” Naih alipatwa na mshituko, akabaki amesimama huku ameshikilia kitasa cha mlango.

“Tunaenda kufuatilia vile viwanja. Nimeongea na yule dalali, tumekubaliana kesho jioni ataweza kutuzungusha kwenye hayo maeneo. Hiyo pia ni moja ya majukumu yako.” Naih akabaki kimya. “Umenisikia?” “Ndiyo.” “Sasa unakwenda au?” Aliuliza kwa jeuri kama asiyetaka kubabaishwa. “Nitakwenda.” Naih akajibu, nakutoka.

Alikwenda moja kwa moja ofisini kwa Emma. “Unajua kama kesho kuna safari?” “Tunataka kuanza biashara ya kuuza nyumba. Tunajenga, kisha tunauza au kupangisha. Jana usiku tulizungumza na yule rafiki yetu wa Dodoma, amesema itatulipa. Ndio Kenny ameona achangamkie kabla bei ya viwanja haijawa mbaya sana. Sasa hivi hali ya uchumi ni ngumu, watu wanauza maeneo yao.” “Tunarudi lini? Maana unakumbuka uliniahidi hatutafanya kazi siku ya jumamosi? Jumamosi nina majukumu mengine, Emma.” “Nafahamu.” “Sasa umeongea na Kenny?” Emma akacheka akifikiria.

 “Nikwambie tu ukweli, sijazungumza naye. Sasa hivi hayupo kwenye nafasi ya kumsikiliza mtu yeyote. Nashauri kwa sasa fanya vile anavyotaka yeye, mpaka atakapo tulia.” Naih akanyamaza. “Nina uhakika hiyo hali itapita tu. Kenny ni mtu mzuri sana. Endelea kumvulia. Mambo mazuri yanakuja.” Naih akasimama pale kwa muda kama anaye fikiria kitu, akashindwa kukisema, akatoka.

Ilipofika mchana wakati anampelekea chakula, akamwambia anaweza kuondoka kwenda kujiandaa na safari ya kesho yake. Naih alitamani kuuliza wanategemea kukaa huko kwa siku ngapi, lakini aliona anyamaze tu. “Tutaondoka hapa saa moja kamili, asubuhi. Usinicheleweshe.” “Nitawahi.” Naih akajibu. Akatoka kwenda kumuaga Kasimu na Sifaeli, kisha akaenda ofisini kwa Emma. “Nimeruhusiwa kuondoka, ili nijiandae kwa safari ya kesho.” “Tutaonana ukirudi basi. Safari njema.” “Kwani hutakuwepo hapa, hiyo kesho?” “Anataka kuwahi kuondoka. Saa moja! Inamaana itanilazimu kuwahi kuamka kabla ya hapo, sina sababu yakufanya hivyo wakati ofisi tunafungua saa mbili na nusu. Nitakuwa nikifanya nini hapa?” Naih alibaki kimya. “Usiwe na wasiwasi, naamini mambo yataenda vizuri.” “Basi ngoja niwahi kuondoka. Sina hata begi zuri la kusafiria. Unafikiri tutakaa huko siku ngapi?” “Sijui Nai. Wewe jiandae. Mnaweza kurudi kesho kutwa ijumaa, au jumamosi. Inategemea na yeye Kenny.” Naih akatoka.

Safari ya Jiji kuu la nchi ya Tanzania.

T

use alimshusha hapo kazini saa 12:30 asubuhi. Naih akabaki hapo akisubiri. Baada ya nusu saa akaona gari ngeni kwake, SUV ya rangi ya silva, mpyaa, imesimama mbele yake. Kenny akashuka, akafungua mlango wa nyuma kabisa wa gari hilo, Naih akasogea na kibegi chake, Kenny akapokea bila hata salamu akaweka begi hilo. “Kaa kiti cha nyuma, upande wa dereva. Upande huo mwingine, kuna mtu amelala.” Naih akafungua upande alioelekezwa, akapanda bila ya kuongeza neno. Aliona msichana amekaa kiti cha mbele, pembeni ya dereva, lakini amelaza kiti chake mpaka nyuma kabisa, amejifunika mtandio. Palikuwa pananukia harufu nzuri sana. “Funga mkanda.” Kenny aliongea kwa kifupi, Naih akavuta mkanda, akajifunga, safari ikaanza. Akatoa kitenge chake, akajifunika na yeye mpaka kichwani, akajiegemeza kwenye kiti, akanyamaza kimya.

Ulipita utulivu mkubwa pale ndani, hapakuwa na sauti hata ya redio. Naih akapitiwa na usingizi. “Nataka kujisaidia.” Naih akasikia sauti ya kike ikiongea. “Nitatafuta sehemu tusimame.” Naih akamsikia Kenny akijibu. “Na njaa imeanza kuuma.” “Unaweza kuvumilia mpaka tupate sehemu ya kula, ndio utajisaidia?” Kenny akamuuliza. “Wewe twende. Nikizidiwa nitakwambia.” Naih akatulia kimya akiwa amejifunika.

Baada ya muda, akasikia wanakata kona, gari likasimama. “Naona hapa tutapata chakula kizuri.” Kenny aliongea. “Ninunulie utakachokula wewe, ngoja niwahi chooni.” Akasikia mlango unafunguliwa na kufungwa. Ukimya wa muda mfupi ukapita. “Unaweza kushuka kama unataka kujisaidia, na upate chakula.” Naih akanyamaza akiwa bado amejifunika kitenge chake. Hali ya hewa mle ndani ya gari ilikuwa baridi kwa Naih. “Nazungumza na wewe.” Naih alisikia kiti cha dereva kwa nyuma pale alipokaa, kikigongwa kidogo. “Kama ni mimi, nipo sawa tu. Asante.” Ulipita ukimya kwa muda, akasikia mlango umefunguliwa na kufungwa.

Akahisi ukimya, akajua yupo peke yake. Akatoa macho kidogo kutoka kwenye kile kitenge. Madirisha yalikuwa meusi. Mtu wa nje, hawezi kuona kwa ndani kwa urahisi. Alibaki akikodolea macho nje ya lile gari, huku akitetemeka baridi. Akapotelea mawazoni. Baada kama ya nusu saa, akamuona Kenny anarudi na yule dada. Naih akabaki ametoa macho. Alikuwa mwanamke mzuri sana. Kuanzia umbile mpaka sura alivutia kumtizama. Alivaa pensi iliyofika magotini. Alikuwa na mguu mzuri, uliojaa juu mpaka chini kwenye kiungio palipowekwa cheni ya dhahabu nzuri na nene.  Ile pensi ilimbana, na kutengeneza umbile la aina yake. Hips za duara zilijichonga sawia. Juu alivaa tisheti ndogo sana, lakini iliendana na kaumbile kajuu. Alikuwa na rangi nzuri sana, ya maji ya kunde.

Naih alibaki ametoa macho, mpaka wakakaribia garini. Haraka sana akajifunika kitenge chake, kabla hawajafungua mlango. Akasikia wamekaa, safari ikaanza. Wakaweka mziki, wakabaki wakizungumza mambo yao ya kawaida tu. Naih alijua huyo ni mwanamke wa Kenny, na yeye ndio alibahatika kukaa naye kwa muda, kwani kwa aina ya mazungumzo yao, walionekana walishakuwa sehemu nyingi pamoja. Naih alibaki kimya kabisa akisikiliza tu.

Mara Naih akaona simu yake aliyokuwa ameizima sauti, ikiwaka taa. Akaivuta karibu ili kujua ni nani anampigia, alikuwa Tuse. “Pole na safari.” “Asante.” “Mmefika wapi?” “Hata sifahamu! Nilikuwa nimelala muda wote.” “Lakini tokea mlipoondoka mpaka sasa, mtakuwa mmefika mbali.” “Hata sijui ni saa ngapi!” Naih akajibu. “Vipi na wewe?” “Ndio nataka kujiandaa na mtihani wa jioni.” “Nakuombea ufaulu.” Tuse akacheka. “Na uombe kweli, usinidanganye.” Naih akacheka. “Ni kweli nitakuombea. Lakini ule kwanza, sio ufike kwenye mtihani, ushindwe kufikiria, halafu umsingizie shetani.” Tuse alicheka sana.

“Unamtetea shetani, eeh?” “Wakati mwingine mnamsingizia bwana!” “Haya Naih. Naenda kula kisha niende kusoma. Nitakupigia kabla sijaingia kwenye mtihani.” “Haya. Shule njema. Mungu akusaidie, utakavyovisoma sasa hivi, vyote ndio ukavikute kwenye mtihani.” “Daah! AMINA kubwa.” Wote wakacheka kidogo. “Haya baadaye basi.” “Nawaombea muwe na safari nzuri.” “Asante.” Naih akakata, akajifunika tena vizuri, akajiegemeza. Muda wote alikuwa ndani ya kitenge chake akizungumza sauti ya chini ili asiwasumbue abiria wenzake. Hakuwa hata ametoa kichwa.

Mziki uliendelea kutumbuiza, wakajikuta wote wako kimya. Hakujua kama wenzake walikuwa wakizungumza wakati na yeye akizungumza au walinyamaza, lakini hakujali. Akajaribu kujiliwaza, akalala mpaka akahisi tena gari limesimama. Akasikia kiti chake kinagongwa tena. “Naongeza mafuta kwenye gari, kama unataka kujisaidia ushuke. Nikitoka hapa, sitasimama mpaka Dodoma.” Naih alimsikia Kenny akiongea. “Kama ni mimi, nipo sawa tu. Asante.” Alijibu akiwa bado ndani ya kitenge chake. Alihisi ukimya wa muda, kisha mlango ukafunguliwa na kufungwa. Akajua Kenny ameshuka, lakini si abiria mwenzake. Akaamua safari hii asijifunue abaki tu mlemle ndani ya kitenge chake.

Baada ya muda akasikia mlango unafunguliwa tena na kufungwa, safari ikaanza. Safari hii hakulala, akabaki amejifunika tu, akisikiliza mazungumzo yao. Yalikuwa yakawaida sana, na wala hapakuwa na vicheko vingi alivyovizoea kwa Kenny. Kenny alikuwa mcheshi na mpenda kucheka. Lakini Kenny huyu hakuwa hata na tabasamu. Alitulia kimya mpaka aliposikia Kenny akizungumza na mtu kwenye simu na kumwambia wameshafika Dodoma, wapo tayari kukutana naye. Baada ya makubaliano ya wapi wakutane, Kenny akakata simu.

 Wakiwa Jijini Dodoma.

Walifika mpaka hiyo sehemu waliyokubaliana na dalali. Wakasalimiana, akaanza kuwazungusha kwenye maeneo kadhaa, mpaka mwanamke wa Kenny aliposema amechoka, anahitaji kwenda kupumzika wataendelea kesho yake. Kenny aliagana na yule dalali, kwa makubaliano ya kuendelea tena kesho yake asubuhi. Naih alikuwa akiandika kila kitu alichokuwa akimsikia dalali akizungumza na Kenny. Alijitahidi kuwa makini. Kila walipofika kwenye eneo, Naih alianza kurekodi mazungumzo, kwa kutumia simu yake huku akiandika haraka sana. Kuanzia bei, ukubwa wa kiwanja, na eneo. Alijitahidi na yeye kuuliza maswali mengi ambayo hata mengine Kenny hakuwa akifikiria kuuliza. Wakaagana na dalali wakaondoka.

“Inabidi kutafuta chakula kabla ya kwenda hotelini.” Kenny akazungumza mara baada ya wote kupanda garini. “Mimi nilazima nikaoge kwanza, ndipo nitaweza kula. Nimejawa na vumbi sana. Twende kwanza tukatafute hoteli, tuoge ndipo tukale.” Yule dada alitoa mapendekezo yake, Kenny akakubali. Wakaendesha mpaka walipopata hoteli. Kenny alichukua vyumba viwili. Cha kwake na yule msichana, kingine cha Naih. Naih alipopewa funguo za chumba chake, akarudi na Kenny mpaka kwenye gari ili kuchukua mzigo wake. “Baada ya saa moja, uwe hapa mapokezi ili twende tukale.” Kenny alitoa maagizo wakati Naih anataka kuondoka. “Kama ni mimi, nipo sawa tu. Nyinyi endeleeni.” Naih hakugeuka nyuma, akaondoka kurudi ndani kutafuta chumba chake.

Alikipata chumba alichokuwa amekodishiwa na Kenny, akaingia humo ndani. Kitu cha kwanza na yeye akaingia bafuni kuoga, akatoa kompyuta ya kazini kwake, akajiweka kitandani na kuanza kuandika huku akisikiliza rekodi ya mazungumzo kati yao na dalali. Hakutaka kuharibu, ili asianze kugombeshwa tena na Kenny. Akapangilia kazi yake vizuri sana. Akaandika maswali ambayo angeuliza siku inayofuata kwa dalali, aliporidhika kuwa yapo vizuri, akaanza kufanya shuguli zake nyingine za bosi mwingine Emma.

Aliendelea kuandika, huku akipiga picha na ku ‘scan’ hizo kazi kwa kutumia simu yake, huku akimtumia Emma, Kasimu pamoja na Sifaeli mtu wa masoko. Aliendelea kusoma email za kazini. Anapokea oda, anaziandika vizuri, na kuwatumia ofisini ili waandae mzigo wa wateja wao kwa haraka, ili wasipitishe tarehe. Aliendelea kupokea hizo oda, huku akijibu wateja kuwa wamepokea oda zao, na atawajulisha mapema juma lijalo ni lini watatumiwa mzigo wao.

Akiwa katikati ya hizo shuguli, akasikia mlango ukigongwa. Akajiweka sawa, kisha akasimama kufungua. Macho yake yakagongana na Kenny. “Nimeshakuandalia ripoti nzima ya siku ya leo. Kuna mambo baadhi nitakamilisha hiyo siku ya kesho baada ya kuzungumza na yule dalali, na kukamilisha ziara yote ya kesho. Nitaweka pamoja, halafu nimezungumza na mtu wa mapokezi, amesema kuwa wanaprinti. Nikisha printi nitakukabidhi ikiwa imekamilia.” Naih alijikuta akijieleza bila kupumzika wala hakuwa ameulizwa.

“Nimekuletea chakula hiki hapa na maji. Hapo chini wanauza chakula. Jitahidi kuwahi kuamka na uende kupata kifungua kinywa kabla hatujaanza mizunguko ya kesho. Nimepatana na yule dalali tukutane saa tatu. Sitaki kuchelewa. Nikukute mapokezi.” Kenny akamkabidhi kile chakula na maji, akaondoka. “Asante.” Naih alichungulia nje ya mlango kumshukuru, lakini Kenny hata hakugeuka nyuma.

Chumba kizima kilijaa harufu ya kuku wa kuchoma. Alifungua mfuko haraka haraka, akakutana na kuku wa kuchoma na chips. Pembeni kulikuwa na kachumbari iliyokuwa na pilipili kali, kama anavyopenda. Naih alikifurahia sana kile chakula. Alikula na kutafuna mpaka mifupa. “Sijala kuku wa kuchoma muda mrefu! Tokeaa..” Naih akajaribu kuvuta kumbukumbu, akakumbuka mara ya mwisho kula kuku wa kuchoma ni alipokuwa na huyohuyo Kenny.

Naih alikuwa mpenzi sana wa nyama ya kuchoma. Kenny alikuwa akimtania kama yeye ni mmasai aliyekamilika. Wakati mwingine alimpeleka mahali walipokuwa wakitengeneza kuku wa Makange. Naih alikuwa akifurahia sana ile pilipili kali kwenye wale kuku wa Makange. Sasa kwa Kenny kumletea hicho chakula hapo, alikuwa amemfurahisha sana. Alikula kwa pupa, akabaki akibeua kama ng’ombe. Akaanza kujicheka. Aliingia kupiga mswaki, akarudi kulala. Alilala kama kitoto kichanga kwa uchovu na shibe.

Huko chumbani kwao!

“Unampango wa kuja kunitambulisha kwa Naih?” Kenny alirushiwa swali, mara alipoingia tu chumbani. Akasimama pale kama anayefikiria jinsi ya kujibu. “Mbona ni swali dogo sana, lakini kwa nini inakuwia ngumu kujibu!?” “Nimechoka na kuendesha Nora. Naomba tulale.” “Uliniambia Naih ni ukurasa uliofunga maishani. Sasa mbona leo umeshindwa kunitambulisha kwake?” “Sijaona umuhimu wake. Ananifanyia kazi. Nimfanyakazi wangu mimi. Sioni sababu ya kumwingiza kwenye maisha yangu binafsi! Hanihusu, simuhusu.”

“Kama hakuhusu, kwa nini umehangaika muda wote huo ukimtafutia kuku wa kuchoma, wakati mwenyewe amekwambia hataki kula?” “Namfahamu kuwa ni mvivu sana wakula. Chakula kwake ni kitu chamwisho sana, kufikiria. Anaweza kukaa hata siku tatu, bila kula chakula cha maana ila kunywa maji tu na kula vitu vidogo vidogo. Kwa kuwa najua anapenda nyama choma, hasa kuku, nikajua nikimpelekea aina hiyo ya chakula, ndipo atakula.” Nora alishangaa, akashindwa kuamini masikio yake.

“Hivi unajisikia kitu unachoongea lakini!?” “Ni nini tena Nora!? Mbona nilikuhakikishia kuwa huo ni ukurasa ambao nilishafunga!? Tatizo ni nini tena? Kwa nini hunipi nafasi!?” “Kwa nini sasa tumekuja naye huku kama sio unataka tu kuwa naye karibu?” “Mimi naona wewe unanitafutia tu sababu Nora. Kumbuka mimi ndiye niliyekupigia simu jana kukuomba uje tuwe wote huku Dodoma. Nikakwambia labda na wewe unaweza ukapata kiwanja kizuri, maeneo ya watu wengi, mkaweza kujenga super market huku Dodoma. Sasa kama nilitaka kuwa naye, nilikuwa na haja gani ya kukuita na wewe? Si ningesafiri naye tu tukawa peke yetu?” Nora akanyamaza. “Au umesahau kuwa mimi ndiye niliyekuomba tuje wote huku!? Hukuwa hata na taarifa kama nina safari ya huku.” Nora akanyamaza, akajifunika shuka.

Kenny akavua nguo zote akapanda kitandani na kuanza kumpapasa. “Hakuna hila yeyote ninayokufanyia leo. Nia yangu ni kuputa muda na wewe.” “Naona kama unacheza na hisia zangu, Kenny!” “Hapana Nora.” Kenny alichangamka muda uleule. Baada ya kipindi cha muda mrefu sana chakushindwa kufanya mapenzi na msichana yeyote yule, usiku huo Kenny aliweza kufanya mapenzi kwa muda mrefu na Nora aliyekuwa akionekana kufurahia kila alichofanyiwa na Kenny, lakini Kenny hakufanikiwa hata bao moja. Alihangaika usiku huo, mpaka Nora akamwambia wajaribu tena kesho yake asubuhi, amechoka sana. Nora alilala palepale bila hata kuongeza neno jingine, Kenny akabaki anawaza.

************************************

Akili zake zilimchukua moja kwa moja kwenye mazungumzo aliyokuwa akimsikia Naih akiongea kwenye simu. Likaanza kupita neno moja hadi jingine ya yale Naih aliyokuwa akizungumza huku akicheka. Alijigeuza kulia na kushoto, mpaka akapitiwa na usingizi. Aliamshwa na Nora akiwa anampapasa. Akatoa tabasamu na kumbusu. Lakini hakuwa akisikia chochote kile alichokuwa akifanyiwa na mrembo Nora. Simu kutoka kwa dalali ndio iliyomuokoa Kenny. “Samahani sana. Tumechelewa kuamka. Tupe kama nusu saa tutakuwa tumefika.” Kenny alikata simu. Akamkumbatia Nora. “Lazima uje ulipe deni baadaye Nora. Jana nimekufanikishia zaidi ya mara tatu, mimi nimeambulia patupu! Sikubali.” Nora akacheka. “Tuwahi kurudi, tu. Utachoka mwenyewe.” Walicheka kidogo, wakikumbushana hili na lile, wakaingia bafuni kuoga wote, kisha wakatoka na kujiandaa kwa haraka.

Walimkuta Naih amekaa kwenye kiti mapokezi, amejiinamia, kimya. “Twende.” Akasikia sauti ya Kenny, akanyanyua kichwa, akamuona Kenny anatoka na Nora yupo nyuma yake. “Habari za asubuhi?” Nora akasalimia. “Nzuri. Naitwa Naih.” Naih alitoa mkono wa salamu. “Naitwa Nora. Naona jana tulishindwa kusalimiana.” Nora alitoa tabasamu la utulivu. “Nimefurahi kukufahamu Nora.” “Na mimi nimefurahi kukuona.” Naih akarudisha tabasamu lisilo na hila, akaongoza njia kule alipokuwa ameelekea Kenny. Nora akawa akitembea nyuma yake.

Alibaki akimtizama Naih pengine angeona kitu cha tofauti sana na wanawake wengine, lakini hakuona kitu. Kwa kuwa alikuwa mbele yake, aliangalia juu mpaka chini, Naih alikuwa binti wa kawaida sana. Alikuwa na umbile kama mwanamke yeyote yule ambaye Mungu alimuumba kumtofautisha na mwanaume. Lakini kwa haraka, Nora hakuona uajabu wowote kwa Naih, binti anayeweza kumfanya Kenny kutokwa na machozi!

Walifika kwenye gari, Naih akaingia kiti cha nyuma, kupisha kiti cha mbele, akitambua kuwa Nora ndiye mwenye haki ya kukaa mbele. Taratibu Nora alifungua mlango na kuingia ndani. Walitoka kumuwahi dalali. Akawazungusha sehemu mbili, wakati wanaelekea sehemu ya tatu, Naih akiwa ameinamia kikaratasi chake akiandika, akamsikia Nora. “Njaa inauma, Kenny. Usiku umenizungusha wee, chakula chote kimeisha tumboni. Tusimame sehemu tule.” “Basi ngoja nimpigie simu huyu dalali tusimame sehemu tule.” Kenny alizungumza na yule dalali kwenye simu akamwelekeza sehemu yenye kifungua kinywa kizuri, wakaelekea huko.

Kenny alisimamisha gari. “Tunaenda kupata kifungua kinywa.” Alimgeukia Naih. “Sawa.” Naih akajibu na kurudisha macho yake kwenye kijitabu chake. “Sawa, unakuja au?” “Nitakula baadaye, asanteni.” Naih alijibu tena kwa kifupi, akarudisha macho kwenye kijitabu chake. Wakatoka na kumuacha. Akaona huo ndio wakati wakusoma email zake na kuwasiliana na wateja wao. Alikuta michanganyiko mingi ya oda. Akaanza kujibu na kupiga simu huku na kule akirekebisha hili na lile. Mpaka Kenny na Nora wanaingia kwenye gari, Naih ndio anamalizana na wateja wa Emma, kwenye simu. Wakafunga mikanda, Kenny akaondoa gari.

Mara simu ya Emma ikaingia kwenye simu ya Naih. “Nini kinaendelea? Mbona Ramji ananipigia simu asubuhi asubuhi?” “Pole. Lakini nimeshazungumza naye, ametulia. Ni kijana wake mwenyewe ndiye aliyekuwa amekosea kutuma oda. Sasa wamemaliza mzigo kabla ya mzigo tunaotakiwa kumtumia week ijayo. Ndio akadhani sisi ndio tulimtumia mzigo pungufu. Nimemrudishia oda niliyokuwa nimetumiwa na kijana wake. Akatulia. Sasa ili kumtuliza zaidi, nimezungumza na Sifaeli kuona kama tuna akiba yeyote, amesema tunayo, ndio nimetoka kuzungumza tena na Ramji sasa hivi kumwambia amtume kijana wake aende akachukue kwa Sifa. Naona ametulia, na ‘asante’ ametoa.” “Nakushukuru Naih. Ramji mkorofi sana. Ameniamsha asubuhi asubuhi anagomba!” “Pole.” Naih alimpa pole huku akicheka.

“Asante. Nilijua tushampoteza tena. Na anavyoniringia! Sijui kwa kuwa anajua anachukuaga mzigo mkubwa?” “Ramji mkorofi tu. Lakini anapenda bidhaa yetu. Hawezi kutuhama.” “Afadhali wewe huwa unawezana naye. Na Cosco nao vipi? Mbona wanadai mzigo leo, wakati hujatoa oda?” “Nao pia nimeshazungumza nao. Yule mama alinipigia. Lakini hawakuwa wametuma hiyo oda, alijichanganya yule mama mwenyewe. Akarudi kuangalia kama alituma, akaikuta hiyo oda ipo kwenye draft, kumbe hakuituma, anasema mitambo siku hiyo aliyotakiwa kuituma kwangu, ilikuwa chini, akasema angenitumia baadaye, akasahau.” “Sasa itakuaje?” Emma akauliza.

“Tangu week iliyopita nilijua kuna uzembe tu ulitokea huko kwao. Si unajua wao mzigo wao ni uleule kila wakati?” “Ndiyo.” Emma akajibu. “Nilishawatengenezea oda yao, nikampa Sifa. Na Sifa amesema, leo atawapelekea. Kwa hiyo na hilo usihofu bosi wangu. Limekaa vizuri.” Emma akasikika akicheka. “Sijui maisha yangu yangekuaje mjini bila wewe!” “Mmh! Kavukavu tu?” “Wewe tena! Niambie chochote utakacho.” “Nilikuwa naomba Mungu hiyo baraka initeremkie sasa hivi!” “Unataka nini?” Emma akauliza huku akicheka. “Nirushie muda wa maongezi. Si unamjua Ramji akianza kujieleza? Kaongea kihindi na kingereza, amemaliza kisalio chote! Na mimi nina mambo mengi kweli yakufanya leo, kabla sijalala. Na bado tupo na mizunguko huku ugenini, sijui wapi  napata salio.” “Yaani ni hilo tu? Na nini tena?” Naih akacheka. “Leo kweli bosi wangu umeamka vizuri! Ningekuwa na shida zangu zile ndogondogo, naona leo ungenitatulia zote. Lakini ni hayo tu.” Wote wakacheka.

“Haya Naih. Nakurekebishia sasa hivi. Usisahau zabibu.” “Sifa naye amenituma zabibu. Nitaleta. Jumatatu hakuna kula kitu kingine, muandae matumbo kwa kula zabibu na karanga.” Walicheka, wakakata simu. Naih alijisahau kama kuna watu wengine kwenye gari. Alikuwa akiongea na Emma kana kwamba wapo wenyewe kwenye ofisi ya Emma. Akagundua wenzake walikuwa kimya, na yeye akanyamaza.

************************************

Walizunguka karibu siku nzima, kila mtu alirudi hotelini akiwa amechoka. Walionyeshwa viwanja vingi na mashamba. Mpaka inafika jioni, dalali akawa ameishiwa viwanja na mashamba. Naih alishuka kwenye gari, moja kwa moja akaingia chumbani kwake kumalizia kazi ya Kenny. Aliipanga vizuri, akahakikisha hatamuacha Kenny na swali hata moja. Akatoka kwenda mapokezi kuprint ile kazi kama Kenny alivyokuwa akitaka. Kwa Emma ingekuwa rahisi, angemtumia kwa email tu, lakini hakutaka matatizo na Kenny, akaamua kufanya vile anavyotaka yeye.

Alipofika mapokezi, wakamwambia hawana wino. Mashine imeishiwa wino, hawawezi kuprinti. Wakamuelekeza mahali pakwenda kuprinti. Naih alizunguka jiji la Dodoma mpaka akajikuta amefika maeneo ya stendi kubwa ya mabasi ya kwenda mikoni. Akazunguka kidogo, akaweza kuprinti kazi ya Kenny. Akanunua na bahasha, akaweka zile karatasi vizuri.

Akakumbuka kumsikia Kenny na dalali wakizungumzia kwenda sehemu yenye nyama choma siku inayofuata, jumamosi. Naih hakutaka kuendelea kukaa Dodoma. Alijua mama yake atakuwa akimsubiri siku hiyo ya jumamosi. Akaingia standi, akakata tiketi yake, akachukua taksii. Akamuomba dereva amrudishe hotelini, na kumuomba arudi tena asubuhi ya saa 11, kuja kumchukua na kumrudisha hapo stendi. Wakakubaliana, Naih akaenda mapokezi na kuwapa ile bahasha. “Ninalipia chumba changu. Lakini huyu mwenye chumba chenye namba hii, akiamka wakati wanatoka, naomba mumkabidhi hii bahasha bila kukosa au kusahau. Nimuhimu sana.” Naih alilipia chumba chake, akaacha bahasha pale mapokezi, akarudi chumbani kwake. Ilishakuwa karibu saa tano usiku. Alioga, akalala. 

Naih aondoka Dom, amuacha Kenny na Nora

Aliamka asubuhi na mapema, akajitayarisha, nakutoka. Na kweli, akamkuta yule dereva taksii akimsubiri. Akampeleka mpaka kituo cha mabasi, Naih akapanda basi, kurudi zake Jijini Dar. Siku za jumamosi ambazo haendi kazini, Naih alikuwa akienda kwa mama yake kumsaidia kufua na kufanya usafi. Ikitokea kama kuna kitu anataka kumtuma mahali, alitumia siku hizo za jumamosi kufanya kazi kwa mama yake. Atu aligeuka akawa mdhaifu. Mara augue hiki, mara kile, akawa hawezi kujisaidia yeye mwenyewe kama zamani.

****************************

Alishamtafutia mama yake sehemu ya kuishi. Naih akawa analipia hapo kodi. Kutokana na mshahara aliokuwa akilipwa na marupurupu mengine, Naih alimudu kumlipia mama yake hicho chumba kimoja alichokuwa akiishi na wadogo zake, mtaa wa Magomeni njia ya kwenda Kigogo na yeye akaweza kujilipia chumba chake. Wadogo zake baada ya kumuibia Naih nguo zake zote na pesa, walirudi baada ya siku chache wakiwa hawana kitu chochote.

Wote wakawa wakimtegemea Naih, waliacha kufanya kazi kwa Tatu. Hakuna aliyejua wanachofanya hapo mjini, na hakuna aliyeweza kuwauliza. Na kwa kuwa Naih aliwajua wana uchu na pesa, alijitahidi hizo siku za jumamosi kununua chakula chakutosha hapo nyumbani kwa mama yake, na kumuachia mama yake pesa kidogo, tena akitaka. Vinginevyo alikwenda kufanya usafi, na kununua vitu alivyojua mama yake atahitaji, nakuwaacha bila ya kuongea na hao wadogo zake.

*****************************************

Alifika jijini mapema tu. Akaenda nyumbani kwake, akabadili nguo zake, akatoka. Akiwa njiani kuelekea kituo cha daladala akakutana na Tuse. “Wewe vipi? Mbona kimya kimya.” Naih akacheka. “Nililala, nikasahau kuchaji simu. Nimesafiri na simu imezima. Hivi nimeiacha chumbani ina chaji.” “Umeingia saa ngapi?” “Muda sio mrefu.” “Unawahi kwa mama nini?” Tuse alizidi kudadisi. “Ulijuaje? Atakuwa na wasiwasi kweli leo. Nimechelewa na sipatikaniki kwa simu! Ngoja niwahi.” “Na mimi naenda kulala kabisa. Nimechoka kweli!” “Nikirudi utanipa habari za mitihani. Ngoja mimi niwahi.” Waliagana, Naih akakimbilia kuwahi daladala.

Kwa Kenny, Huko Dom.

Kenny aliamka asubuhi akiwa amefurahia kilichompeleka Dodoma amekikamilisha, tena vizuri. Alitoka na Nora wakiwa wanacheka, alipofika mapokezi, akakabidhiwa ile bahasha. Akafungua na kukutana na barua iliyoandikwa kwa mkono. Mwandiko ulikuwa wa Naih. Naih alijua kuumba herufi. Akiandika, utapenda kusoma. Kenny alipenda sana mwandiko wake, akawa akimwambia awe anamfundisha kuumba herufi. Kwani Kenny alikuwa na mwandiko mbaya sana. Kama sio akili alizojaliwa za darasani, hakuna mwalimu angethubutu kupoteza muda kusoma kazi yake.

‘Kenny, ndani ya hiyo bahasha, kuna ripoti nzima ya tangia tumefika hapa Dodoma. Utakapo pata muda na kusoma, utakuta nimekuainishia kila kitu, ili usipate shida yakufanya maamuzi. Ila kama ningepata nafasi ya kushauri, ningeshauri ile nyumba ambayo iko karibu na chuo, ndio ingepewa kipaumbele. Inaweza kubomolewa, na kujengwa vyumba vidogo, ambavyo vingekodishwa kwa wanafunzi, na bado nje ukaweka fremu za biashara, za kukodisha. Ni biashara ambayo inauwezo wakukuingizia pesa nzuri, na ya uhakika. Uzuri ni kwamba, ikishakamilika marekebisho au ujenzi mzima, haita hitaji usimamizi mkubwa sana kwenye kuiendesha. Unaweza kuiendesha ukiwa popote pale. Nimetangulia kurudi Dar. Mambo yote yakienda sawa, nitakuwa kazini siku ya jumatatu.’

Naih!

“Ni bahasha ya nini?” Kenny alibaki amekodolea macho ile barua fupi sana. “Kenny?” Nora alimshitua. “Ni ripoti ya kazi nzima tuliyofanya hapa. Naih ameniandikia.” Nora akapokonya ile bahasha. “Haa! Anapangilia kazi vizuri, mpaka raha! Naomba na mimi nikatoe kopi. Maana nilikuwa nimesha changanyikiwa na habari za hivyo viwanja na mashamba, sijui chakufanya tena! Lakini ameainisha vizuri, hupati shida!” Nora aliendelea kuangalia. “Na hiyo barua ni ya nini? Mbona umekosa raha!” “Hapana. Nipo sawa. Ni maelezo ya hiyo kazi tu.” Nora akampokonya tena na ile barua. “Kwa nini unafanya hivyo, Nora?” “Kwani ni siri? Unataka kunificha nini!?” “Hamna siri yeyote. Lakini ungeomba tu kiustarabu.” “Kwa hiyo tatizo ni mimi kutokuwa mstaarabu au nikusoma hii barua aliyokuandikia Naih?” “Hakuna siri humo ndani. Wewe soma.” Bado walikuwa wamesimama palepale mapokezi. Wageni wengine na wahudumu wakiwashangaa wanavyobishana.

Nora akaisoma mpaka mwisho. “Kwa hiyo umekasirika kwa kuwa ameondoka!?” “Nora please!” “Ni nini sasa kilichokuudhi wakati ulikuwa kwenye furaha yote. Kazi umeandikiwa vizuri, na ushauri umepewa. Kinachokufanya unune ni nini?” “Nani amekwambia nimenuna? Kwa nini unataka kuanzisha ugomvi usio na maana?” “Usinifanye mimi mtoto mdogo, Kenny. Na usinipotezee muda wangu. Huwezi kunyanyasa hisia zangu. Naona unanichezea akili wewe!” “Naomba tuondoke hapa. Tunakusanya watu bila sababu.” Wakaondoka. 

Baada ya kurudi Jijini,

Siku ya jumatatu.

S

iku ya jumatatu Naih aliwahi kazini, akawa mtu wa kwanza. Emma alimkuta nje. Wakafungua mlango na kuendeleza stori. Ni kweli aliwaletea zabibu na karanga. Kasimu na Sifaeli wakaingia, wakaanza kula zabibu na karanga huku wakiongea na kucheka. “Bosi wako yuko wapi?” Walimtania Naih, akabaki akicheka tu. “Lakini akija tutajua tu.” Mara mlango ukafunguliwa, Kenny akaingia. Kila mtu akatawanyika kwa haraka, akabaki Emma tu pale mezani kwa Naih akicheka. Naih naye alikimbilia jikoni kutengeneza kahawa, akampelekea ofisini kwake, nakuiweka mezani kwake. “Leo nimewahi kufika. Nimepita pale mgahawani, bado hawajaanza kuuza. Nitarudi tena baadaye kukuangalizia kitafunwa.” “Sio lazima.” Naih alikuwa ameshageuka ili andoke. Hakutegemewa kujibiwa kiustarabu vile. Akasimama kidogo, kama anayetaka kusikia tena, alipoona kimya, akafungua mlango nakutoka.

Siku hiyo kazi zilienda vizuri mpaka jioni mvua ilipoanza kunyesha. Muda mwingi Kenny alikuwa ofisini kwake, akiandika. Naih alipeleka kitafunio na kahawa nyingine, mchana akapeleka chakula, jioni matunda. Mvua ilipozidi, akapeleka tena kahawa. Akaona kila kitu kimepokelewa na hakuwa akiitwa. Ofisi ilikuwa imetulia sana siku hiyo. Naih alibaki akibabaika asijue afanyeje, akaamua aende ofisini kwake. “Kuna kitu chochote unachotaka nikusaidie? Nimemaliza kazi zote, naweza kukusaidia kitu chochote.” “Sina kwa sasa.” Kenny akajibu na kurudisha macho yake kwenye kompyuta. Naih akatoka.

Kasimu na Sifaeli walienda kumuaga Emma kuwa wao wanawahi daladala kabla barabara hazijafunga kwa mvua. Emma aliwaruhusu, wakaondoka. Emma naye akatoka, akaenda mezani kwa Naih. “Unaweza tu kuondoka na wewe.” “Siwezi kutoka nikamuacha humu ndani. Heri nimsubiri tu.” Naih alimnong’oneza, Emma akacheka kwa sauti ya chini huku anaangalia ilipo ofisi ya Kenny. “Ngoja nimwangalie.” Emma akaenda ofisini kwake.

Akagonga mara moja, akaingia bila kukaribishwa. “Mvua imechachamaa kweli! Tuondoke.” Emma aliongea akiwa amesimama mlangoni. “Kuna kitu namalizia.” Kenny alijibu kwa kifupi tu. “Basi ukimaliza unipitie ofisini kwangu, tuondoke wote. Si leo tunapita wote kwa Tye?” “Sawa.” Emma alijibiwa kwa kifupi, akafunga mlango akarudi mezani kwa Naih. “Naona leo utakuwepo kuwepo sana hapa.” Alimnong’oneza Naih, wakacheka kwa sauti ya chini.

Giza lilianza kuingia nje, wakati Kenny bado yupo ofisini kwake. Baada ya masaa mawili mengine, Emma akamfuata tena Kenny ofisini kwake. “Jamaa wameanza kupiga simu, wanatuulizia.” “Na mimi nimemaliza hapa. Nisubiri tuondoke wote. Sitaki kuingiza gari yangu kwenye hii mvua. Nimekuja na ile ndogo.” “Haina shida.” “Basi nakuja sasa hivi, nipe kama dakika tano.” Emma akatoka akaenda kukaa mezani kwa Naih.

Baada ya muda mfupi Kenny akatoka. “Twende wote tukusogeze Naih.” Emma akasimama. “Asante Emma. Ila Tuse yupo hapo nje muda mrefu tu, ananisubiri.” “Ooh! Kumbe jamaa yupo nje!? Kwa nini hajaingia ndani?” “Hana neno. Alisema anataka kujilaza kwenye gari ili tukifika nyumbani ajisomee kidogo. Wapo kwenye mitihani.” Emma akakunja uso. “Kumbe mnaishi pamoja!?” Naih akachukua pochi yake, akasimama. “Ndiyo. Tunaishi pamoja.” Naih alijibu huku anatoka. “Muwe na usiku mwema. Tutaonana kesho.” “Na wewe pia.” Emma akajibu, lakini Kenny alionekana ameinamia simu yake, akituma ujumbe. Naih akatoka.

Tuse alipomuona Naih akitoka ofisini, akatoka kwenye gari na mwamvuli, akamfuata Naih, akamfunika. “Asante. Nilijua umelala!” Naih akashukuru. “Hii mvua inatisha sana. Na kelele za radi, ndio zimenifanya nishindwe hata kulala.” Emma na Kenny walikuwa wakiwasikiliza wakati wanafuata gari ya Tuse huku wakiongea. Tuse alikuwa amemshikia mwamvuli. Akamsindikiza Naih mpaka mlangoni, alipopanda na kufunga mlango ndipo na yeye akarudi upande wa dereva, akaingia kwa haraka, akafunga mwamvuli, wakaondoka.

Siku ya Jumanne.

S

iku inayofuata asubuhi akiwa njiani kuelekea kazini kama kawaida yake, aliona Mama Ole akimpigia simu. Emma akapokea. “Hey, Ms Olendekai!” Emma akasalimia. “Hey Emma!” “Vipi, upo mzima!?” Emma akauliza akitilia mashaka sauti ya mama huyo. “Nina wasiwasi sana na Kenny. Sijui yuko wapi!? Kazini aliacha kufika, na nyumbani aliondoka kwa hasira sana siku ya jumamosi. Amesema nisiwahi kumtafuta tena, na nisihesabu kama yeye ni mtoto wangu. Ameondoka na magari yake yote, japo ameacha baadhi ya nguo zake. Nina wasiwasi sana naye. Nyinyi mmewasiliana tokea jumamosi?” Emma alipatwa na kigugumizi na wasiwasi kidogo.

“Jana usiku nilikuwa naye hapa ofisini kwangu. Tuliachana jana usiku akiwa na ile gari yake ndogo. Mwanzoni tulikubaliana tuondoke na gari yangu, akihofia mvua, lakini baadaye aligairi akaamua kuondoka tu na gari yake.” “Na mvua kubwa ile ya jana!? Alikuwa anaelekea wapi?” “Sijui. Lakini ilikuwa tukutane kwa Tye, hakutokea, tukajua amegairi.” “Kwani siku hizi huwa analala wapi?” “Mara nyingi alikuwa akilala nyumbani kwangu. Lakini nashauri upate muda wa kuzungumza naye. Ameumia sana tokea ajue ukweli mzima. Usiku wa kuamkia jumapili alikuwa kwangu, hakulala. Alikuwa akizungumza na mimi kwa uchungu sana huku akinisimulia kila kitu. Kenny ameumia sana.” Mama Ole akanyamaza.

 “Mama Kenny?” Emma akaita baada ya ukimya. “Nipo.” Mama Ole aliitika, akiwa ameishiwa maneno yote. Hakujua kama na Emma alishaambiwa ukweli wote. “Nafikiri unahitaji kuzungumza naye.  Sasa hivi yupo kwenye kipindi ambacho hana kitu cha kupoteza tena. Haitamsumbua kujidhuru.” “Kwa nini unasema hivyo!?” Mama yake Kenny aliuliza kwa mshituko sana. “Mimi nakutahadharisha tu, na ninataka ujue kuwa, kwa sasa, Kenny hana chakupoteza tena.” Mama huyo alibaki kichwa kikimzunguka.

“Sasa unafikiri atakuwa wapi kama jana hakulala kwako!? Au nimpigie Nora?” “Walikuwa na Nora, Dodoma mpaka jumamosi. Hawakuachana vizuri. Sidhani kama wapo kwenye maelewano au sidhani kama Nora atataka kumsikia tena Kenny.” “Jamani Kenny! Amemfumania nini huko Dodoma? Hawezi kupata msichana kama Nora. Nilishazungumza na Nora nikamwambia baadhi ya tabia zake, tena Nora akasema labda akioa atatulia. Siamini kama ameweza kuhangaika kutafuta mwanamke mwingine tena baada ya kumpata msichana mzuri kama Nora!”  Hasira zilimpanda Emma.

 “Tatizo lenu nyinyi wazazi wetu, huwa hamjui ni nini sisi tunachotaka. Mmekazana kutupa vitu mnavyodhani ndivyo tunavitaka kwenye maisha yetu, na kusahau vitu vya msingi sana. Nani amekwambia Kenny anahitaji msichana mwenye matako makubwa na kiuno chembamba? Umeshajua aina ya wasichana aliokuwa akilala nao Kenny, na bado alikuwa akiwaacha? Ulishajiuliza ni kwa nini Kenny anahangaika kulala na kila mwanamke? Eti mama Kenny?” Emma akauliza kwa ukali kabisa.

“Kenny amelala na kila aina ya mwanamke hapa duniani na bado hajaridhika. Wewe upo kama mama yangu, na ndio maana Jay ameamua kuondoka, na kuuwa undugu na wazazi wetu kwa mambo kama haya! Mmejaa kwenye maisha yetu mkitaka nyinyi ndio muongoze, wakati hamtujui hata kidogo. Hamjui watu mnaotaka kuwaongoza wakoje na wanatabia gani!” Emma alikuwa amekasirika nakushindwa kujizuia. Alianza kwa heshima lakini kadiri mazungumzo yalivyoendelea, ndivyo hasira zilivyompanda.

“Mnataka kuvuna msipopanda! Mmeishia kutulaumu tu, wakati hamkuwahi kuwepo kwenye maisha yetu. Kama mnafikiri pesa yenu ndio ilikuwa muhimu sana, ulizeni watoto yatima, wabunge, mawaziri na maraisi. Waulizeni kama walikuzwa kama sisi, na pesa tu! Wengine wanasema walikuwa wakienda shule bila viatu, na bado wamefika walipo na ndoa zao na watoto. Mmeyaharibu maisha yetu na wala hamuonekani kujutia!” Emma akaendelea.

“Hebu tulieni na mtuangalie jinsi tulivyo kuwa jamani! Mimi, Kenny na Jay! Hatuwezi kuoa. Hatuwezi kupenda. Hakuna anayetupenda sisi kwa vile tulivyo. Wanawake wakituangalia tu, wanachoona ni pesa zenu na majina yenu mliyoyachora kwenye kila kona ya maisha yetu! Jay hataki hata mlitaje jina lake. Hataki hata ukaribu na nyinyi. Watoto wenyewe tupo watatu tu, lakini mmemkimbiza Jay. Haya, katika ulimwengu wetu ambao mmeuharibu na mnaendelea kuharibu mpaka sasa hivi tunavyozungumza, mwenzetu Kenny alipata upendo wa kweli. Mtu ambaye anaweza kumtizama yeye kama mwanaume, akampenda na kumuheshimu, kabla ya pesa yenu na jina lenu. Ukaona haitoshi, ukamuharibia kabisa.”

“Mmeyaharibu na mnaendelea kuharibu maisha yetu! Sasa hembu jiulize ni kwa nini? Kwa manufaa ya nani? Utakuja kugundua ni kwa ajili ya ubinafsi wenu tu. Wakati wote mnajiangali nyinyi, pesa zenu na hadhi zenu. Lakini sio sisi. Na kwa taarifa yako tu, hata huyo Nora unayemlazimishia kwa Kenny, hajawahi kumpenda Kenny hata kidogo. Yeye Nora anachopenda ni vile Kenny alivyo mweupe, muonekano mzuri wakichotara, kutokea kwenye familia tajiri. Basi!” Emma hakumbakiza mama yake Kenny, alikuwa akigomba kama aliyepata jukwaa lakutoa dukuduku lake. Akajua ujumbe huo utamfikia na mama yake, kwani Mama Ole na mama yake Emma na Jay walikuwa marafiki sana. Alipoona kimya cha muda mrefu upande wa pili, akakata simu.

Wakati amekata simu akakuta missed call tatu za simu asiyo ifahamu, na kaka yake Jay akaanza kumpigia. Emma akapokea. “Upo bongo nini?” “Hapana.” “Mbona nimekuta nimepigiwa simu na namba ambayo siifahamu, halafu ndio nikaona na wewe unanipigia kwa simu yako?” “Sasa kwa nini hukupokea? Huyo atakuwa ni nesi.” “Nesi?” “Kenny amepata ajali mbaya sana. Yupo hospitalini. Ameniambia alikuwa chumba cha upasuaji kwa muda mrefu sana. Nenda kamwangalie, anaongea kwa shida sana. Anaonekana bado ana maumivu.” “Haiwezekani! Mama yake alikuwa.., Kenny nilikuwa naye….” “Wewe Emma, nenda kamuangalie halafu unipigie. Nasikia hali sio nzuri. Mwangalie amelazwa kwenye chumba gani, kama mazingira ni mazuri, halafu tujue chakufanya. Yupo MOI.” “Nakwenda sasa hivi.” Watoto hao watatu walikuwa pamoja wakisaidiana kama watoto yatima, wakati walitokea kwenye majumba ya kifahari na wazazi mamilionea.                                     

Sehemu ya 4.
                                                Mwanadamu ni udongo.

M

paka inafika saa nne asubuhi, hawakuwa wamewaona mabosi wao pale ofisini. Kasimu na Sifa walifurahia ule uhuru, lakini si Naih. Aliamka kama mgonjwa, moyo wake haukuwa na amani kabisa. Alimwambia Tuse wakati wanakuja kazini, kama kawaida ya Tuse alimuombea na kumwambia asimpe shetani nafasi, hiyo ni siku njema Mungu ameiandaa kwa ajili yake. Naih alitabasamu tu, hakujua jinsi ya kumuelezea Tuse akaelewa. Alijawa na hofu, mpaka inafika saa nne asubuhi hakuwa ameweka hata kitu mdomoni.

Ndipo akaamua kumpigia simu Emma. “Naomba mtafute Kenny, tujue alipo. Moyo wangu umekosa amani tokea asubuhi nimeamka. Najua unaweza usielewe, lakini naomba mpigie tu simu ili tujue kama yupo salama.” Naih alishangaa machozi yakimtoka. Binti huyo wa kimasai ilikuwa ngumu sana kuona akitokwa na chozi. Ni kama alificha mbali sana hisia zake. Alijaliwa moyo mgumu sana. Wakati mwingine ilikuwa ni ngumu hata kujua kama amekasirika au amefurahi. Alijaliwa ukimya wa namna yake.

“Naih! Ni kweli Kenny amepatwa matatizo.” “Matatizo gani!? Yupo mzima?” Naih akauliza lakini ni kama alishajua Kenny yu matatizoni. “Amepata ajali mbaya sana. Hapa tunapozungumza, Kenny amekatwa miguu yote miwili.” Naih alikimbia chooni na kuanza kutapika. Alitapika mpaka akakaa chini, Emma akisikiliza. Tumbo lilizidi kumkata. Akaamua kuwapigia simu na kina Kasimu na Sifa, akawaeleza kwa kifupi tu, na kuwaomba wakamwangalie Naih.

 Walimkuta amekaa chini chooni anahangaika. Wakamsaidia kumtoa pale. “Pole sana Naih. Sisi hatukujua kama unafahamiana na jamaa!” “Pole sana. Ndio maana ulikuwa ukimvumilia!” “Kenny ni mtu mzuri sana. Namfahamu tokea nazaliwa.”  Naih aliongea huku akiwaza na kufuta machozi. “Emma amesema uchukue taksii uende. Mimi nitakusaidia kazi zako.” Bila kupoteza nafasi, Naih alielekea Muhimbili, kitengo cha mifupa MOI. Kenny ndio alikuwa ametoka chumba cha upasuaji asubuhi hiyo, na hali haikuwa nzuri. 

Huko Hospitalini.

Kulikuwa na ulinzi mkali sana, Naih alishindwa hata kuruhusiwa kuingia ndani. Akajikuta amekaa nje ya kitengo hicho cha MOI kama kundi jingine la watu waliokataliwa kuingia, asijue na wao walikuwa wakitaka kwenda kufanya nini mle ndani mida hiyo ya asubuhi. Kama kawaida yake, akatafuta sehemu pembeni yao akakaa akisubiri nafasi au muda wa kuona wagonjwa na yeye aingie.

Kwa muda mfupi sana habari zikasambaa kwamba Kenny amepata ajali na amekatwa miguu. Kitengo kile cha MOI kikafurika watu wakitaka kushuhudia Kenny asiye na miguu! Matajiri wote wa mjini waliomfahamu Mzee Ole, mkewe, Kenny, na familia ya kina Emma walikuwepo pale.  Wafanyabiashara wenzake baba yake Kenny, viongozi wa kisiasa wa ngazi mbalimbali nchini, waliokwisha kufanya kazi na mama yake Kenny, au kumfahamu mama huyo maarufu nchini, wakijua ana mtoto mmoja tu na yupo matatizoni, na wenyewe pia walikuwepo hapo na wake zao, na watoto wao.

Rafiki zake wote Kenny waliokuwa wakishinda naye kwenye kumbi za starehe, waliposikia tu Kenny hana miguu tena, kila mtu aliacha kazi, wakakimbilia hospitalini hapo. Haya, wanawake wote waliokwisha kulala na Kenny, kuanzia mdogo mpaka na umri ule, walioumizwa na penzi la Kenny, na kufurahishwa. Weupe kwa weusi, wembamba kwa wanene, wahindi, waafrika, wazungu, wasomi na wasiosoma, nao walimiminika hospitalini hapo kushuhudia tukio hilo.

Baada ya muda ndipo Naih alikuja kufahamu kuwa umati wote ule upo pale kwa ajili ya mtu mmoja tu, Kenny. Kila mmoja alisimulia lake. Vilikuwa vikundi mbalimbali kutokana na vile walivyomfahamu Kenny, wakisimuliana kisa hiki na kile. Wengine walisema aligombana na mama yake akaamua kwenda kujitupa baharini ili afe. Wengine walisema ametendwa na mwanamke, wengine walisema ni ajali, iliyotokana na mvua nyingi sana ya usiku uliopita. Naih akabaki amechanganyikiwa tu hajui kipi kilimpata Kenny.

“Malaya huyu, kwani alishawahi kuwa na mwanamke mmoja? Hakuna mwanamke anayeweza kumtenda Kenny. Kwanza nasikia huwa harudiagi mwanamke.” “Mbona mimi kalala na mimi mara mbili?” “Bahati yako. Mimi alinitia kwenye gari lake, hakuwahi kupokea tena simu zangu.” “Ni mshenzi huyo, mbwa nyuma. Hata mimi alinifanyia hivyohivyo! Tena mimi ilikuwa pale nje, club. Akaniambia atanitafuta tena kesho yake, sikumsikia tena, mshenzi huyo!” “Na mimi pia ilikuwa club. Jamani nilihangaika kumsaka huyu Kenny! Nikaja kumpata tena siku nyingine hapohapo club, asiniruke! Eti hanifahamu, na hajawahi kuniona. Mmeona wale washezi wenzake pale? Basi nasikia ndio watoto wa matajiri hapa mjini. Uchafu wao ndio huo. Kulala na watu, halafu wanawakimbia. Acha wanicheke siku ile, na Kenny amenyamaza kimya! Mbona niliondoka kama nimevuliwa nguo mbele zao!” Huyo dada alisikika bado anahasira na Kenny.

 “Bwana acheni Mungu ampumzishe huyu mshenzi. Aliniliza mwezi mzima. Sili wala kunywa! Nalia tu. Alinitoa bikra yangu, akanilipia taksii, akaniambia atanipigia simu jioni kujua naendeleaje, maana nilikuwa natokwa na damu nyingi sana, sikumsikia tena! Nikaja kusikia anatoka na msichana mwingine palepale darasani. Ni mshezi huyo, hujawahi kuona. Alituchanganya pale chuo cha Tumaini, wasichana tukabaki tunashikana mashati.” Huyo naye alisikika bado ana dukuduku na Kenny.

“Na siunajua ile sura yake na tabasamu? Akikuongelesha utatamani akuvue nguo hapo hapo.” “Naona Mungu angeichukua na ile sura kabisa!” Wote wakacheka. “Sasa ambakishie nini?” “Kovu. Ili asiendelee kuumiza watu. Kenny ni mshenzi sana.” “Lakini na huo ulemavu wa kudumu aliopewa pia utamtosha. Afanye atulie. Mshenzi kabisa.” “Nakwambia malipo ni hapahapa duniani. Huko mbinguni ni hukumu tu.” Naih akahama hilo kundi la hao kina dada waliokuwa wakimtukana Kenny, kwa kupokezana tena kwa jazba. Akasogea kwengine.

Akawaona hao ni watu wa karibu na Kenny. Akajua hapo atapata ukweli  wa nini kilichompata Kenny. Ili apate ukweli wote akajificha sura kwa kuwapa mgongo ili wasimtambue, ‘mimi wa Kenny’. Maana wote walimjua Naih. “Mimi ninachompendea Kenny, na umalaya wake wote, halali na mwanamke wa mtu. Ilimradi ajue tu ni wako, hapo hatapita. Hata wamlilie vipi. Hapo zipu hafungui.” Wale vijana wote wakacheka. “Bwana Kenny namsifu bwana. Yaani mkiwa club hata kwa masaa mawili tu, lakini anaweza kuyatumia, ukashangaa! Anaweza akapiga chapu chapu hata mademu wawili kwa mpigo!” “Kenny katika hilo eneo kabobea. Kasi yake ya ajabu! Kuna siku tulienda naye club, alikuja kwa kuchelewa. Yaani alifika pale kama saa tatu, mpaka saa sita tunaondoka, alishapiga vya fasta kama vinne hivi. Kila mtu alimpa pesa.” Wote wakacheka.

 “Tye unakumbuka lakini?” “Nakumbuka. Mimi mwenyewe nalala na wanawake, lakini jamaa sijawahi kuvunja rekodi yake! Sijui huwa anafanyaje aisee!? Siku ile, kila mtu alimpa pesa. Aliondoka na zaidi ya kama milioni mbili hivi! Wote tulimvulia kofia.” “Wengine tulimwaga pombe, tukampa pesa yote yeye, tukafunga starehe kwa siku ile.” Walizidi kucheka. Naih akaona na hilo kundi pia halitamfaa.

Japokuwa wote hao alishakutana nao mara kadhaa kwenye birthday za Kenny na zao wenyewe, Kenny alipokuwa akienda naye lakini alijua hata akiwauliza, wanaweza wasiwe msaada mkubwa sana kwake kwa kuwa Kenny anayempaga heshima kwa watoto hao wa matajiri hapo mjini, hakuwepo. Hata yeye Naih alijua wanampokea sababu ya heshima tu ya Kenny, lakini si watu wanao mkubali sana. Alijua hajafika kwenye viwango vyao. Hapo kwenyewe walikuwa wamesimama wakiwa wamejiundia kundi lao, wakizungumza tu wao wenyewe bila kujali yeyote pembeni yao kana kwamba hapakuwa na watu wengine. Na wazi walionekana hawana muda wa kuongea au kusikiliza mtu mwingine yeyote ila wao tu. Wakati wote watoto hao wa wenye nazo wa hapo jijini, hujitenga. Popote pale, huwa kwenye kundi lao.

Naih akaondoka hapo kimya kimya bila kuzungumza nao kitu na wenyewe wala hawakumuona. Akataka kujaribu kupenya kujaribu kuingia ndani labda angeweza kumuona Emma, lakini akakuta watu wanatolewa nje. Akasikia kunaandaliwa hapo ndani, kuna wakubwa wa nchi wanakuja. Akasikia askari mmoja akiingia kwa haraka huku akisema “Wanakuja! Wapo hapo getini wanaingia.” Akatoa amri kuwa njia ya kwenda chumba cha mtoto wa Olendekai iwe wazi na kusiwe na watu. Kabla hajakaa sawa, akaona gari ya Gavana wa pesa inaingia, mara akafuata na waziri wa pesa. Tayari kulishakuwa na ulinzi mkali pale.

Walishuka wakubwa hao. Wakasalimiana na kuzungumza kidogo.  “Nimeshituka sana! Ni Kenny bwana! Halafu katoto kenyewe kamoja kama dawa! Nilikuwa naelekea uwanja wa ndege, lakini nikamwambia dereva anipitishe kwanza hapa. Najua Rita atakuwa na wakati mgumu sana.” Yule Gavana alikuwa akizungumza na waziri wa fedha. “Sisi tulikuwa kwenye kikao, ndio tukapata taarifa.” Waziri wa fedha naye akaongeza kwa masikitiko. “Hongera bwana, naona bajeti yako wameipitisha.” Wote wakacheka. “Kwa shida kweli! Lakini nashukuru.” Wakapitiliza kuingia alipokuwa amelazwa Kenny. Naih alipoona hizo hekaheka, akaamua aondoke tu pale, asiendelee kusimama na kujichosha zaidi. Hakuwa amepata taarifa zozote zakueleweka, wala hapakuwa na matumaini yakuja kuingia mle ndani.

Akatafuta sehemu akakaa, nakubaki kusikiliza habari za Kenny. Ni kweli alikuwa akifahamu hayo yote kutoka kwa Kenny mwenyewe, na baadhi aliwaona rafiki zake waliokuwa wameangukia kwenye mikono ya Kenny, lakini hakuwahi kusikia uchungu wa wanawake waliotendwa na Kenny. Wengi walisikika wanauchungu sana. Wenye kumlaani walimlaani, wenye kucheka walimcheka na kushukuru Mungu amewalipia kisasi. Mpaka giza linaingia Naih hakuwa amemuona Emma wala Kenny. Akajikuta amebakia pale nje peke yake, asijue jinsi ya kuingia, maana ulinzi uliwekwa, kuhakikisha watu hawasogelei tena chumba cha Kenny.

Waliobahatika kumuona na kumpiga picha na kumchukua video asubuhi ile pale hospitalini kabla wazazi na ndugu hawajapata taarifa akiwa tu ndio ameletwa hospitalini na wasamaria wema waliomtoa kwenye hiyo ajali mbaya, ndio ikawa haohao, basi. Maana Kenny aliokolewa na kuletwa hapo na kuachwa kama wagonjwa wengine tu, sio kama Kenny Ole. Wakati yupo mapokezi na watu wengine wakisubiri huduma, ndipo ikajulikana ni yeye Kenny. Wachache waliomuona ndio waliosambaza habari zake na kuvuta watu maana walisema, ‘Kenny malaya sasa hana miguu tena na ameachwa tu hapo mapokezi kama wanadamu wengine’. Kwa ushahidi wa uhakika ili waaminiwe na umma, ndipo wachache hao waliomshuhudia Kenny akilia kwa maumivu, walimchukua video na kumrusha hewani wakisimulia kwa kumsanifu mbele yake Kenny mwenyewe. Wakaita watu wakashuhudie, jinsi malipo yalivyo hapahapa duniani. Ndio ikawa chanzo cha watu kumiminika hapo.

****************************

Naih akaamua kujisogeza mpaka walipo wale walinzi. “Naomba kumuona Kenny.” “Wewe ni nani?” “Au na wewe ni mwanamke wake pia? Maana kila mtu anataka kuingia!” Mwingine akauliza. Kimya. Naih akawa kama anatafuta jinsi ya kuwaaminisha wale walinzi. “Dada, wewe ni ndugu?” “Hapana. Ni rafiki.” Aliona wale walinzi wote wakimcheka bila hata kijificha sura zao. Naih akaona anajidhalilisha tu. Akaamua kuondoka maana simu ya Emma haikuwa ikipatikanika tena.

Zilipita siku tatu mfululizo, Naih anakwenda hospitalini kwa muda tofauti tofauti na kushindwa kumuona Kenny. Hakuruhusiwa hata kuwa maeneo yale. Emma alipiga simu kutoa maelekezo ya kikazi kwa haraka, akamuahidi kumpigia Naih baadaye, lakini hakupiga. Kila alipojiambia aache kuhangaika alikuwa anashindwa. Kazini hapakaliki usiku pia halali vizuri anamuhurumia Kenny.

                       Kenny huko hospitalini.

B

aada ya kutolewa chumba cha upasuaji, siku alipopata ajali, Kenny alimuomba nesi aliyekuwa akimuhudumia amtafute Emma. Alipomkosa Emma akamtajia namba za simu za Jay, yule nesi akampigia Jay, akapokea. Kenny alimwambia kwa ufupi tu kuwa yupo hospitalini amepata ajali, akakata simu na kupitiwa na usingizi. Jay akamtaarifu mdogo wake Emma. Na Emma ndiye aliyewapigia simu wazazi wao. Walifika hapo wazazi wa Kenny na wa Emma kwa haraka sana. Hata wao walikuwa kwenye mshituko usioweza kutamkika baada ya kuona Kenny mtoto wa pekee, amepoteza miguu.

Mama yake alilia karibu kuzimia. Hakuna anayetarajia au hata kudhani kupatwa na majanga makubwa hivyo! Ilibidi Mzee Ole kuzungumza na daktari aliyehusika na operesheni yake. Akaelezwa hali aliyoletwa nayo Kenny hapo hospitalini, aliambiwa hakukuwa na jinsi yakuokoa ile miguu zaidi ya kuhangaika kuokoa maisha yake. Walimwambia aliletwa pale hospitalini akiwa anakaribia kufa kwa kuvuja damu. Upasuaji wake uliwachukua karibu usiku kucha. Mzee Ole alibaki kimya asijue chakujibu au kuuliza tena.

Alipoamka akafungua macho, akamkuta Emma, na wazazi wake wamekaa pembeni ya kitanda chake. Alijisogeza mara kadhaa. “Mbona sisikii vidole vya miguu, wala nyayo zangu!?” Kenny akauliza. Usoni hakuwa ameumia sana. Kidogo tu. Wote wakanyamaza, akamuona mama yake akilia. “Ulipata ajali mbaya sana.” Baba yake akamjibu. “Nafahamu. Ninachouliza ni miguu yangu. Waliikata?” Kenny akauliza swali la moja kwa moja. “Ndiyo. Ilipondeka pondeka, haikuwa ikifaa kabisa, ikabidi waikate tu. Pole sana.” Emma ndiye aliyeweza kujibu.

Kenny alijaribu kunyoosha mkono wake wa kulia ili ajaribu kujishika lakini aligugumia maumivu. “Mkono huo nao umeumia Kenny.” Emma alimuwahi, Kenny akatulia. Akabaki kimya. “Unajisikiaje?” Mama yake alisimama nakumuuliza kwa upendo, lakini Kenny hakujibu. Wakaamua wamuache.

Siku tatu mfululizo hakuzungumza na mtu yeyote, kitu chochote. Hata madaktari waliopita kumtizama walipokuwa wakimuulizia hali yake, hakuwa akijibu. Vidonda vya miguuni kule alikokatwa, vilikuwa vikiendelea vizuri, na kwengineko pia. Marafiki zake wakaribu tu, aliokuwa akiwatambua Emma, ndio walioruhusiwa kuingia kumuona Kenny, lakini Kenny hakuzungumza neno hata moja na mara nyingi alikuwa amefunga macho. Awe amelala au yupo macho, alibaki kimya kabisa akiwa amefunga macho.

Kitu ambacho hata daktari alisema sio vizuri kwake. Anafungia hisia zake. Ni heri afungue macho aruhusu fahamu zake zione vitu tofautitofauti, mbali na tukio la mwisho la ajali yake aliyoshuhudia akipata. Daktari aliwaambia wazazi wa Kenny wajitahidi kuzungumza naye ili aweze kufungua macho na kuongea. Lakini hakuna aliyefanikiwa.

 Hakutaka kula wala kunywa kitu chochote. Hakutaka kumeza dawa zake, kitu kilichofanya arudishwe kwenye sindano, ambazo ilikuwa kama hasikii anachofanyiwa. Kenny huyu hakuwa muoga wa sindano alikuwa kama amepigwa ganzi mwili mzima, zaidi ufahamu wake.

Mshituko wa kupoteza miguu yake ulimfanya kupoteza hisia za Kenny halisi ambaye kwanza kabisa alikuwa muoga sana wa hospitali na sindano ndio hakutaka hata kuziona kwa macho. Hakuna jinsi Kenny akiwa kwenye akili na hisia zake timilifu, akakubali umtoboe kwa namna yeyote ile. Lakini baada ya hiyo ajali, nakujua kama amekatwa miguu, ilikuwa hata wamchome sindano vipi, hastuki na alitulia kimya wala hakuwa hata akijigusu au kuonyesha chochote usoni. Mama yake hakuwahi kuondoka hapo hospitalini, alibaki akimuuguza. Baba yake alikuwa akienda asubuhi na jioni. Lakini hakuwahi kuzungumza nao hata salamu.

Kisicho Ridhiki, Hakiliki!

M

ama Ole alipoona ile hali ya Kenny inazidi kuwa mbaya, akafikiria kumpigia simu Nora, ili ajaribu kuzungumza na Kenny, amliwaze. Alimpigia simu Nora zaidi ya mara tatu bila kupokelewa, kitu ambacho haikuwa kawaida yao. Akajifariji na kujiambia pengine amekuwa na shuguli nyingi sana. Asubiri mpaka atoke kazini ndipo ampigie tena. Muda wote macho yalikuwa kwenye saa akisubiri muda wa kutoka Nora kazini ufike. Maana ndio aliona atakuwa suluhisho la haraka kumtuliza mtoto wake, pengine atafunguka na kuzungumza hata na wauguzi pale hospitalini kujua kinachoendelea mwilini mwake ili atibiwe.

Alipojua muda wa kazi umeisha, akajaribu tena kumpigia. Baada ya simu kuita muda mrefu sana, ndipo Nora akapokea. “Haloo!” Alimsikia Nora amepokea. “Ni mimi mama yake Kenny.” “Ninayo namba yako.” Nora akajibu hivyo na kumfanya mama Ole kuishiwa morari. Akaamua kutoka nje ili kuzungumza naye kwa faragha wengine wasisikie. “Nilikupigia sana mchana.” “Nilikuwa na kazi! Si unajua leo ni siku ya kazi!?” Nora akajibu kwa kuuliza na kushangaa kidogo. “Ndiyo, nafahamu mwanangu. Lakini nilitaka tu kukutaarifu kuwa Kenny alipata ajali mbaya sana, yupo hospitalini.” “Nafahamu.” Nora akajibu. “Nilikuwa nakutaarifu tu.” “Sawa.” Nora akajibu na kukata simu.

Mama Ole aliumia sana, akabaki anaangalia simu yake huku machozi yakimtoka.

Mlango ulikuwa wazi, kwa hiyo mazungumzo ya nje, watu wa ndani walikuwa wakisikiliza. Alikuwepo Emma, Kaka yake Jay, ndio alikuwa amefika tu kutoko uwanja wa ndege na kupitia hapo moja kwa moja, wazazi wa Emma, na baba yake Kenny pia alikuwepo ndani. Ilikuwa kama familia tu ndio waliokuwepo hapo. Mama Ole aliingia akionekana alikuwa akilia. Akarudi kukaa, kimya bila kuongeza neno.

Baada ya ukimya wa muda mrefu pale ndani. Hakuna wakumsemesha mwenzake. Jay alikuwa akimjibu Emma tu wala hakuwa amezungumza na wazazi wake, hata hakuwa ametoa salamu kwa wale wazazi wao wanne. Akiwa ndio ametua nchini baada ya muda mrefu sana, aliingia na kukaa pale ndani kama chumba kizima yupo Emma na Kenny tu. Kenny akiwa kimya pale kitandani, Emma na kaka yake wakizungumza vitu vya msingi sana tena kwa mafumbo ili wazazi wao wasijue mambo yao. Ukimya ndio ulitawala zaidi pale.

Wakati Jay anaingia hapo wazazi wao walifurahi sana kumuona Jay, mama yake akajaribu kumsalimia, lakini Jay hakutaka hata kumtizama usoni ikawa kama hajamsikia au hata kuhisi uwepo wake. Baba yake alipomsemesha, akamjibu kwa jazba kama kutoa onyo kwa wote. “Tafadhali tusikilizane na tuheshimiane. Kila mmoja wetu hapa yupo kwa ajili ya maslahi yake binafsi. Fanyeni unafiki wenu hapa kwa kadiri ya uwezo wenu na mimi niacheni na yangu. Msinibugudhi na mimi nawaahidi sitawabugudhi. Tafadhalini sana. Msinikorofishe tusije tukaanzisha jambo baya zaidi ya hili, kwa kuwa mimi sitakuwa kama Kenny. Hakika sitanyamaza. Kwa hiyo ni bora nyinyi ndio mjifanye kama sipo hapa ili kuendelea kuwepo hapa mtimize wajibu wenu wakati mkifikiria ni wapi pakuja kutuharibia tena baada ya kukamilisha vizuri hili mlilolifanya kwa Kenny.” Jay aliongea kwa jazba, wale wazazi wote wakanywea. Kimya. 

https://cdn3.volusion.com/fjmpg.dxchy/v/vspfiles/photos/YA-56-2.jpg?1484737416

      Naih!

M

ara simu ya Emma ikaanza kuita, akapokea kwa haraka. “Naomba unisamehe Naih. Nilipitiwa. Sijui nimechanganyikiwa?” “Hamna shida.” “Ulishaondoka?” “Hapana Emma. Bado nasubiri.” “Haiwezekani Naih! Tokea asubuhi bado upo? Au uliondoka?” “Uliniambia nisubiri Emma, nisingeweza kuondoka.” “Aisee naomba nisamehe sana. Basi nakuja kukufuata sasa hivi.” Emma akakata simu. “Daah! Sijui napitiwa na nini bwana! Sijui ni ile simu ya Nora!” “Nora?” Mama Ole akauliza kwa mshangao.

“Ndiyo, Nora. Nilimpigia asubuhi, naona ndio alinichanganya akili nikasahau kila kitu. Yaani kila siku Nai anakuja mpaka hapo nje anafukuzwa. Asubuhi na usiku, anashindwa kuingia. Sasa jana usiku alinitumia ujumbe, kuniambia anaomba nimsaidie angalau aje amuone Kenny. Nikamshauri aje asubuhi sana, kabla watu hawajawa wengi. Saa 12 asubuhi alinitumia ujumbe yupo nje, nikamjibu nakuja sasa hivi. Yaani nimesahau ndio ananikumbusha sasa hivi.” “Basi utamsahau tena!” Kaka yake akadakia. “Nakwenda.” “Wewe huna haja yakutuambia, wewe ondoka tu.” Kaka yake akaongeza. Wazazi wao wakabaki kimya hawakuongeza neno.

 Kwa mara ya Kwanza Naih kufanikiwa kumuona Kenny!

Emma alikwenda mpaka alipokuwa Naih, akamkuta amekaa nje ya jengo hilo la MOI, pembeni kwenye mgahawa wao. “Pole sana. Unaonekana umechoka!” “Nashukuru umekuja kunichukua.” Naih akasimama. Alikuwa amekaa kwenye meza peke yake. Emma akaingia naye ndani kwenye jengo hilo la MOI. Wakaanza kutembea kufuata chumba alicholazwa Kenny. Wakati wanakaribia, Naih akamsimamisha Emma. “Anaendeleaje lakini?” “Sijui yupo kwenye mshituko, au nini! Hajazungumza neno lolote tokea alipojua kama amepoteza miguu.” “Masikini Kenny! Mungu atamsaidia.” Naih aliumia sana.

“Anakula?” “Nakwambia hajafungua mdomo. Hata dawa ameshindwa kumeza, wanamchoma sindano tu. Na anaishi kwa dripu. Hatujui kama anamaumivu au la! Washikaji wanakuja kumuongelesha na kumpigia stori zakumfanya acheke, lakini imeshindikana. Anakuwa amefunga macho muda wote. Hata hatujui ni saa ngapi anafungua macho!” “Mmejaribu kumpigia simu mpenzi wake?” Naih akaendelea kuuliza akionyesha kumuhurumia zaidi.

“Nani!?”  Emma akauliza, asijue mpenzi wa Kenny ni yupi tena. “Nora! Kenny anaonekana anampenda Nora. Jaribu kumpigia simu aje azungumze naye, labda atapata nafuu.” “Mmmh!” “Tafadhali Kenny. Mimi ningekuwa nina namba ya huyo msichana, ningempigia. Najua akija hapa, Kenny atachangamka tu. Ni juzi tu tulikuwa na Nora Dodoma. Niliwaacha na Kenny, tena wakiwa kwenye wakati mzuri sana. Naomba tumpigie Nora, ili Kenny awe na furaha. Atakuwa amejawa na maswali mengi tena ya hofu. Lakini akipata mtu anayempenda kwa dhati, kama Nora, atazungumza tu.” “Unafikiri na mimi sikupata hilo wazo?” Emma akamuuliza. “Sasa kwa nini hujampigia, akaja kumuona!?” Emma akacheka kwa kuguna.

“Nimepiga.” “Amesemaje?!” “Utaumia tu, Nai. Acha. Ameniharibia siku yangu yote ya leo. Nafikiri ndio maana nilikusahau.” “Amesemaje!?” “Amesema hana mpango na Kenny. Kama yeye Kenny alifikiri alikuwa akimchezea, na yeye pia alikuwa akimchezea. Anaye mchumba wake, na wanatarajia kufunga ndoa hivi karibuni. Hawezi kuhangaika na walemavu.” “Jamani yule dada! Amemfanya Kenny ampende halafu anamuacha! Wewe si unamjua Kenny huwa harudiagi wasichana? Lakini yule dada alishaenda naye mpaka Africa Kusini, wakadumu mpaka juzi walipokuwa Dodoma! Asingemfanyia hivyo Kenny. Tena hasa kipindi hiki ambacho Kenny anamuhitaji!” Naih aliongea kwa uchungu sana. Emma akabaki akifikiria wakati Naih akilalamika.

“Ila Nai, wewe hufahamu kitu cha msingi sana cha Kenny. Kuna ukweli mkubwa sana umejificha moyoni mwake. Na huo ukweli ndio unamtesa sana.” “Ni ukweli gani Emma? Kama ulivyomuona. Anahasira sana, huwezi hata kuzungumza naye. Kenny hakuwa hivi! Zamani alikuwa akiniambia kila kitu. Sasa hivi ni ngumu. Nashindwa hata kumuuliza au kumsaidia. Ndio maana unaniona nafanya kila anachotaka, ili asikasirike zaidi.” Emma akabaki akiwaza kama anayeshindwa azungumze nini zaidi.

“Emma?” Naih akamuita.  “Twende na wewe ukajaribu bahati yako. Naona wewe huwa unamuwezea. Hazungumzi wala kumwangalia mtu yeyote! Hatujui anajisikiaje! Madaktari wenyewe hawajui wamsaidiaje, wanamtibu tu kutokana na vipimo vile vya kawaida kama homa na pressure. Basi!” Wakasogea mpaka pale mlangoni, kabla Emma hajafungua mlango, Naih akasimama kama aliyesita.

“Vipi tena? Na wewe unataka kumkimbia nini?” “Siwezi kumkimbia Kenny. Hata iweje Emma. Twende tu.” Akafungua mlango, nakumpisha yeye ndio aingie. Naih alibabaika sana baada ya kukutana na wale Wazee wa jiji pale ndani. Uzuri, wote walikuwa wameinama. “Shikamooni.” “Marahaba mtoto mzuri Nai.” Jay, kaka yake Emma aliitikia kwa haraka na kumfanya Naih acheke.

“Mbona unacheka?” “Ulivyoitikia kwa haraka! Kwanza wewe ndio ulitakiwa unisalimie Jay.” “Acha masihara Nai! Wewe nimekuacha hata kuongea huwezi!” “Jay kwa kupenda ukubwa! Wakati mimi ndio nilikufundisha kufunga kamba za viatu?” Wote wakacheka. “Husahau tu!?” “Bwana Jay na kufunga viatu! Sijui alikuwa na tatizo gani!” Emma akadakia. “Basi huo ugonjwa mpaka leo ninao! Nimeamua kuacha kununua viatu vya kamba kabisaa. Navaa vyakutumbukiza tu, kama hivi.” Jay aliwaonyesha, nakuwafanya wacheke.

“Nimefurahi kukuona Naih. Unazidi kuwa mrembo!” Naih alicheka kwa aibu. “Na mimi nimefurahi kukuona Jay. Karibu mjini.” “Nishakaribia.” Naih alitulia kidogo, akageukia alipokuwa amelala Kenny. Wazazi wake walikuwa wamekaa lakini wote wametulia, kimya kabisa kama wanao ogopa kuweka neno.

https://cdn3.volusion.com/fjmpg.dxchy/v/vspfiles/photos/YA-56-2.jpg?1484737416

                                                   Kenny kwa NaiH!

N

aih akasogea taratibu mpaka pale kitandani. Kenny alikuwa amefunga macho. Naih akainama, akavuta mkono wake kutoka kwenye shuka, akashika kiganja chake. “Kenny!” Akaita taratibu huku akiminya mkono wake huo wa kushoto taratibu kwa upendo. Kenny akafungua macho. Wakabaki wakiangaliana. “Pole.” Alimuona machozi yanatoka. “Am so scared! Naogopa sana.” Kwa mara ya kwanza Kenny akaongea. Wote wakanyanyua macho. “Nafahamu. Pole.” Naih akajibu kwa upole huku bado amemshika mkono.

“Kuanzia 1 mpaka 10, ni kwa kiasi gani?” Naih akauliza taratibu. “10.” Kenny akajibu huku akitetemeka. “Na mimi?” Naih akamuuliza tena taratibu. “Sijui kama bado unataka, Naih!” Hakuna aliyekuwa akielewa, lakini walinyamaza kimya, mama yake Kenny alisikika akilia taratibu.

Naih akafungua kifungo cha juu cha shati alilokuwa amevaa, akatoa cheni nje. Ilikuwa na ile alama ya Infinity kama cheni ya Kenny. Akamuonyesha. “Unakumbuka?” Naih akamuuliza, Kenny akatingisha kichwa. “Last time I checked, Infinity didn’t have an end.” Kenny aliendelea kutokwa na machozi huku akitetemeka kwa hofu. “Sikujua kama bado unayo!” “Kwani wewe ulitupa ya kwako!?” Naih akauliza akiwa ametulia tu, bila kuonyesha wasiwasi au hali ya kupaniki.  “Hapana. Siwezi hata kuthubutu. Nilikuwa nayo mpaka muda napata ajali. Nakumbuka nilikuwa nimeishika.” Kenny akajibu huku akilia. “Okay, tutatafuta nyingine. Turudi kwenye swali langu, na mimi nachukua ngapi?” Naih aliuliza tena. “Unataka ngapi?” Akamuumiza Naih. “7” Naih akamjibu. “Yaani kwenye 10, uchukue 7!? Hiyo ni kubwa sana Nai. Hustahili!” Kenny akajibu kwa machozi huku midomo ikitetemeka kama aliyeshikwa na baridi kali.

Naih akapiga magoti pembeni yake. “Nisikilize Kenny. Unahitaji 3 tu, kwa ajili ya kuhakikisha unapata muda wakutosha wakulala, ili kufikiria na kuongea pale unaposikia una maumivu, ili wajue ni jinsi gani yakukutibu, na tatu au mwisho kufikiria unataka kula chakula gani ili upate nguvu.” “Nachukia hiyo ya mwisho Naih. Unajua sipendi hilo swali! Wakati wote wewe unajua nini napenda kula.” “Basi sawa. Basi utabakiwa na 2 tu kwenye hizo 10. Ni sawa?” “Watu wananicheka Naih, wananisanifu na kunikimbia.” “Nisikilize Kenny. Niangalie. Usifunge tena macho. Niangalie mimi.” Kenny akafungua macho akamwangalia huku akilia.

Naih akamfuta machozi vizuri. “Nisikilize Kenny, Let me worried about that. Hiyo ipo ndani ya zile 8.” “Unajua kama nimekatwa miguu? Sina miguu, Naih!” “Najua. Lakini bado ipo hii miwili Kenny. Bado tunayo miwili zaidi kwa kutumia.” Akimaanisha miguu yake. “Halafu mambo yamebadilika sio kama zamani, ipo miguu ya bandia itakayokusaidia kutembea kama zamani. Unakumbuka ile video tuliyoiona ya yule mwanajeshi wa kimarekeni alipoteza miguu vitani, amewekewa miguu ya bandia. Sasa hivi anafanya shuguli zake kama zamani, mpaka yupo kwenye mashindano ya kukimbia?” “Nilisahau.” “Unaona sasa? Ndio maana nakuomba sasa hivi ufikirie tu hivyo vitu viwili. Ili kupata miguu mingine, nilazima upone vidonda kabisaa. Ndipo wataweza kukuwekea miguu mingine. Lakini pia, kwa sasa sitaki uwe na wasiwasi juu ya hilo, kumbuka  bado tunayo miguu mingine miwili.” “Nilijua umenichukia kabisa ndio maana hukuja kuniona.” “Tokea siku ya kwanza nilipojua umepata ajali, nilikuwa nikishinda hapo nje, lakini sikuruhusiwa kuingia.” “Asante Naih.” Naih akasimama akamfuta tena machozi.

“Kenny!” Naih akamuita, akamwangalia. “Tunaweza kuanza kufanyia kazi hizo mbili?” “Nafikiri hivyo.” “Okay. Usilie sasa. I want you to focus.” Keny akajitahidi kutulia. Naih akaendelea kumfuta machozi. “Upo tayari?” Naih akamuuliza. “Nafikiri hivyo.” Kenny akajibu kwa kusita. “Haya, naomba unipe tatu tu. Lakini kila moja, iwe ya taratibu ili uweze kufikiria, ili uweze kunijibu kila ninapokuuliza maswali. Na kila swali nitakalo kuuliza, ufikirie kwanza kabla hujajibu. Sawa?” “Kama wakati ule wa baiskeli?” “Kumbe unakumbuka!?” “Siwezi kusahau. Ulikuwa wewe, Mama Naih na Babu Kaa.” “Sawa kabisa. Sasa naomba uanze. Taratibu, bila haraka.” Bado hakuna aliyekuwa akiwaelewa, lakini wenyewe walionekana kuelewana vizuri tu.

Wakamuona Kenny anaanza kuvuta pumzi kwa nguvu na kuanza kuzishusha taratibu, kisha akakunja uso. “Upande upi unauma?” Naih akauliza kwa utulivu. “Upande huu wa mbavu za kulia. Unafikiri nilivunja na mbavu?” Kenny aliuliza akiwa na wasiwasi sana. “Unaweza kurudia tena, au maumivu ni makali sana?” “Naweza kujaribu.” Kenny akajibu. “Tujaribu tena.” Kenny akarudia tena kuvuta pumzi kwa nguvu. “Naomba sasa hivi uwe makini kusikiliza mwili mzima. Ili tujue nini kinauma.” Kenny akaanza kushusha pumzi, lakini akakunja uso, na machozi yakaanza kutoka. “Pole Kenny. Basi, usifanye tena mara ya tatu. Lakini umegundua una maumivu ya wapi kwenye mwili wako?” “Kifua chote kinauma, Naih. Siwezi kuhema, maumivu makali.” Tayari alisikika amepaniki.

“Pole Kenny. Nyamaza, nikwambie kitu.” Akatingisha kichwa kukubali. Lakini alishapaniki kiasi cha kuhangaika akitapatapa kama asiyeweza kuhema tena mpaka akaanza kuwashitua wazazi wao, wote wakasimama.  “Niangalie Kenny. Unakumbuka kabla sijakuomba 3, ulikuwa ukihema vizuri?” Kenny akajaribu kuvuta kumbukumbu akiwa kwenye ile hali. “Usiogope wala usiruhusu hofu. Unaweza kuhema, lakini huwezi kuhema kwa nguvu, kwa kuwa una maumivu ya kifua. Si ndio hivyo?” Kenny akakumbuka na kutulia mara moja. “Tulia kabisa, halafu tutamwambia dokta, ili waangalie ni nini kinachosababisha maumivu. Sawa?” Kenny akakubali. Wazazi nao wakatulia na kurudi kukaa.

Kwa asili Kenny alikuwa muoga wakuumwa sana. Alikuwa hata akijikata na wembe, kwake ni tatizo. Na lazima Naih ajue kama anamatatizo, na amuhudumie yeye. Kwa hiyo Naih alimjua vizuri sana. Na alikuwa muoga wa dawa na sindano. Hakupenda hospitali hata kidogo. “Unadhani kila kitu kitakuwa sawa?” Kenny akauliza akiwa na wasiwasi sana. Uso ulikuwa mwekundu. Midomo inatetemeka “Nina uhakika kila kitu kitakuwa sawa. Usiogope Kenny.” “Sitakufa?” “Unampango wa kufa?” Naih akamuuliza. “Wewe unajua ninavyoogopa kufa.” Naih akamcheka. “Usinicheke Nai!” “Basi fanyia kazi zile mbili zako, ili tutoke hapa.” “Unamaanisha tutakuwa wote?” Kenny aliuliza kwa wasiwasi.

 “Mbona kama umesahau kila kitu!?” Naih akamuuliza. “Nakumbuka kila kitu Naih. Lakini nilidhani umeamua kunikasirikia, baada ya..” Kenny akaanza kulia. “Kenny! Kenny! Naomba usilie. Hakuna kilichobadilika. Kila kitu kipo vilevile. Ngoja nikamuite nesi aje akuangalie maumivu ya kifua.” “Mimi nitaenda kumuita nesi.” Baba yake Kenny aliyekuwa kimya wakati wote akasimama kwa haraka sana. “Wewe kaa hapo hapo, Naih.” “Sawa.” Naih akaitikia, baba yake Kenny akatoka.

Baada ya muda akarudi na nesi. Naih akataka kumpisha, lakini Kenny akamvuta mkono aliokuwa amemshika. “Nilifikiri ulisema unabaki?!”  “Nampisha nesi, ili mzungumze.” “Tafadhali usiondoke wala kusogea Nai. Naogopa sana.” “Basi sitaondoka.” Naih akasimama palepale pembeni, nesi akaanza maswali, lakini Kenny akanyamaza. “Kenny!?” Naih akaita kwa upole. “Anakuuliza. Unaweza kujibu ndiyo au hapana. Ili ajue jinsi ya kukusaidia.” “Nachukia maisha yangu, Naih. Najichukia mimi mwenyewe. Sasa hivi nachukia kila kitu. Hakuna kitu wanaweza kufanya kunisaidia tena, Naih. Hawana huo uwezo, nim...” “Kenny! Kenny! Niangalie mimi. Hilo linaangukia kwenye zile 8 zangu. Tafadhali tulia.” “Siwezi, Naih.” “Najua unaweza Kenny. Na hapa pia utapita, na tutajiandaa na changamoto nyingine. Si unajua huwa haziishi?” “Najua!” Mtoto huyo wa mama, alijibu huku akilia.

 “Basi naomba uanze kufanyia kazi mbili zako. Ni mbili tu Kenny. Uliniambia unaweza kufanya. Basi anza kwa kujibu maswali ya huyu nesi. Mambo mengine yoote, niachie mimi.” “Okay. Anataka kujua nini?” Yule nesi akarudia kwa upendo. Kisha akajaribu kutaka kumshika. “Usithubutu hata kunigusa!” Kenny aliongea kwa ukali na kumshitua yule nesi mpaka akarudi nyuma kwa kuruka. Wote waliwaangalia.

“Lazima akuguse Kenny, ili ajue maumivu yapo kwa ndani au nje.” “Wamekuwa wakicheza na mwili wangu tangia…” Akanyamaza nakuendelea kulia. “Hawajui kitu gani wanatakiwa kunifanyia. Nawachukia kabisa. Halafu nina usingizi sana, lakini siwezi kulala kwa hofu.” Kenny aliongea kwa hasira huku akilia.

“Labda tumuache alale kidogo ili apumzike. Naamini akipata usingizi mzuri, akiamka, ataweza kuzungumza vizuri. Kama mnaweza kumuongezea dawa ya usingizi, mumpe ili alale. Akiamka tutakuita ili mzungumze naye tena. Nakushukuru sana dada yangu na nakuomba usijisikie vibaya, sio kwamba anakuchukia wewe. Kenny nimuoga sana na wauguzi. Hapendi hospitali, hapendi dawa wala sindano. Akiwaona hivyo mlivyovaa nguo nyeupe! Ndio anachanganyikiwa kabisaa.” Naih alimshukuru yule nesi na kujaribu kumtuliza. Wakacheka kidogo.

“Naelewa. Lakini sasa hivi ingekuwa vizuri, kwa kuwa bado daktari yupo, na huu ndio muda mzuri kama anatakiwa kufanyiwa vipimo, hakuna watu wengi. Atafanyiwa vipimo kwa haraka.” Yule nesi akajaribu kushauri. “Hapana. Nina usingizi nataka kulala sasahivi, na sitaki mniongezee dawa nyingine. Nalala.” Kenny akadakia. “Basi naona tumuache tu, tutakujulisha akiamka.” Naih aliongeza na tabasamu kumtuliza yule nesi. “Sawa.” Yule nesi alijibu na kutoka. Baada ya muda mfupi sana, akurudi na dawa, akaweka kwenye dripu, akatoka.

 “Jaribu kulala, Kenny. Ukimka tutaendelea kuzungumza.” “Sitaki kulala hapa, nataka kuondoka. Unajua ninavyochukia hospitali, Nai.” “Basi jibu maswali yao vizuri, Kenny. Ili wakutibu tuondoke. Ukifanya hivyo, tutakaa muda mrefu sana hapa.” Kenny akanyamaza. “Lala, wakati mimi naenda nyumbani kuoga. Nitarudi…” “No way. Hata kidogo. Itakuaje usiporudi?” “Nitarudi Kenny! Naenda kuoga na kubadili hizi nguo. Nimekaa kwenye vumbi hapo nje karibia siku nzima. Nanuka.” “Mbona sisikii harufu?” “Kenny! Nitarudi. Kwani nilishawahi kukudanganya?” Naih akamuuliza.

“Uliniahidi utasubiri, lakini sasa hivi unaishi na Tuse!” Naih akajikuta anacheka tu. “It’s not funny, Naih! Wala havichekeshi!” “Yaani Kenny, jamani! Unawasiwasi na mambo mengi yasiyo hata na msingi kwa sasa. Kwa nini usitulie na kuzingatia mbili zako tu?” Tayari alishaanza kuwa mwekundu tena, Naih akajua ameanza kupandisha hasira. “Kenny! Acha kupandisha hasira bure! Umeelewa vibaya. Naishi na Tuse kama mpangaji mwenzangu, sio kama mpenzi wangu.” “Hujawahi kunidanganya Naih!” “Sasa kwa nini unafikiri sasa hivi nakudanganya? Naomba utulize mawazo, ulale tutaongea kesho.”

“Siwezi. Nataka kujua sasa hivi. Mbona anakufuata kazini, na kukusubiria? Anakushikia mwamvuli na kukufungulia mlango! Amekupigia simu tukiwa njiani, tukielekea Dodoma. Uliniacha Dodoma, ili umuwahi yeye huku Dar. Na sasa hivi unaniacha hapa ili uende kwake. Hunithamini wala kunijali kama zamani. Umekubali mama atutenganishe. Uliondoka na kuniacha pale nyumbani wakati unajua sina mtu mwi..” “Kenny! Kenny!” “Hakuna mtu ananijali mimi kama mimi Kenny! Na sasa hivi ndio nimekuwa mlemavu, ndio itakuwa mbaya zaidi.” Kenny akaendelea kulalamika huku akilia.

“We Kenny! Naomba unisikilize bwana. Naishi na Tuse ili kufidia pesa. Nachangia naye kulipa kodi ya pale tunapoishi naye, na pia namtunza mama yangu ikiwepo kumlipia kodi ya anapoishi na wakina Zai na Mia. Tuse ni kijana mpenda mambo ya dini, hana hata mpango wa kuoa leo wala kesho. Nikimuuliza, anasema anamsubiri Mungu amwambie mke wake ni nani. Ni Mnyakyusa kama Atu. Ananichukulia mimi kama dada yake kabisa, utafikiri nimezaliwa naye tumbo moja.”

“Siku ile, Tuse alikuwa na mwamvuli mmoja tu, ikabidi tutumie naye huo mwamvuli. Niliondoka Dodoma kurudi huku Dar, ili kwanza kukupa nafasi wewe na Nora. Nilitaka mpate muda mzuri, mkiwa peke yenu bila mimi kuwepo. Kumbuka kazi iliyokuwa imenipeleka kule, nilikuwa nimeimaliza. Na pili, mama ni mgonjwa. Anaishi na Mia na Zai. Hawamsaidii kwa chochote kile. Inanibidi kila siku za jumamosi, niende ili nikamsaidie kazi za pale ndani na anitume kule anapotaka, ili na mimi siku ya jumapili, nifanye usafi nyumbani kwangu.” Naih aliendelea kujieleza taratibu na kifasaha. Wote walikuwa wakimsikiliza.

“Sikurudi nyumbani kwenu sio kwa kuwa sikuwa nakujali, lakini mama alilipwa pesa na mama yako, kwa sharti ya kutokukutafuta tena wewe. Nisingeweza kukiuka makubaliano, wakati mama yangu aliipokea ile hundi! Na aliipokea mwanzoni akiwa ameahidi kufuata masharti yote aliyokuwa amepewa na mama yako. Nisingeweza kuvunja ahadi wakati Zai na Mia waliila ile pesa yote.” “Kwa hiyo Tuse sio mpenzi wako?” “We Kenny!?” “Ndiyo au Hapana? Jibu.” “Hapana.” Naih akajibu.

“Hujawahi kulala naye?” “Wewe Kenny!? Hivi unanisikiliza kweli!?” “Ndiyo au hapana?” Kenny alikuwa akitetemeka kwa hasira. Alikuwa mwekundu kama moto. “Hata wazo la kulala na yule kaka halijawahi kupita mawazoni kwangu. Kwanza ni vile humfahamu Tuse. Tuse ni wale walokole wa ukweli, sio muongo.” “Na Tino?” “Tino yupi tena!?” “Yule uliyefumaniwa naye?” Naih akakunja uso. “Unaongea nini, wewe Kenny!?” “Sio kweli.” Mama Ole akaingilia. Wakamgeukia yeye kasoro Kenny hakutaka hata kumtizama mama yake.

“Nilifundishwa na Mia huo uongo. Niseme tulimfumania Naih, ili ukasirike usimtafute tena Naih. Ndio nikawaambia wale wasichana wa kazi wakudanganye. Naih hakufumaniwa.” Yule mama alimtetea Naih, lakini Kenny ni kama hakuwa amesikia. Mama yake alipoweka tu kituo kwenye maelezo yake. Akaendelea na Naih. “Ndiyo au hapana. Na usinidanganye Naih.” “Kwani si umemsikia mama yako akisema hapa sasa hivi?!” “NAIH!?” Kenny aligomba kwa sauti. “Hapana.” Naih akajibu, Kenny akavuta pumzi kwa nguvu, nakuzishusha kwa shida, Naih akaguna na kutingisha kichwa huku akimwangalia.

“Na kwa kuwa huonekani kama una usingizi, naenda kumuita nesi na daktari.” “Hapana, mimi nina usingizi.” “Hapana Kenny. Huna usingizi hata kidogo.” “Nina usingizi.” “Huna. Ungekuwa una usingizi, usingekuwa na nguvu ya kugomba hivi na kuendesha kesi usiku huu. Wewe unakimbia vipimo. Nakujua Kenny.” Kenny akafunga macho. “Najua hujalala Kenny. Naenda kumuita dokta. Na ninakuomba safari hii ujibu maswali yote utakayoulizwa, ili tuandikiwe vipimo, ukapimwe usiku huu, ijulikane kwa nini unamaumivu.” “Sasa hivi maumivu yameisha.” Akajibu kwa ujasiri. “Okay. Nipe tena 3.” “Fine.” Kenny akaanza kuvuta tena pumzi kwa nguvu, akabaki anamwangalia Naih. “Nini sasa? Si umesema huna maumivu wewe? Endelea sasa.” Kenny akabaki akihangaika, Naih akatoka bila kuaga.

Baada ya muda akarudi na daktari na yuleyule nesi aliyetoka hapo mwanzoni.  Machozi yalikuwa yakimtoka. “Pole. Maumivu yamekuwa makali?” Naih akamuuliza Kenny, akatingisha kichwa taratibu kukubali. “Daktari yuko hapa. Naomba umwambie vile unavyojisikia. Sawa?” Kenny akatingisha kichwa kukubali. Daktari akasogea. Alimuuliza maswali machache, akajaribu kumminya taratibu sehemu mbalimbali za mwili, Kenny akawa anakunja uso, huku akigugumia hasa katika sehemu zenye maumivu. Yule daktari akamwandikia vipimo alivyoshauri afanyiwe usiku uleule.

Akachukuliwa na kwenda kufanyiwa vipimo, huku akisindikizwa na ndugu zake na Naih. Wakati yupo chumba cha vipimo, Naih akamsogelea Emma. “Unafikiri ni sawa nikikimbia nyumbani kwenda kuoga wakati yeye anafanyiwa vipimo?” “Yaani naomba hata usithubutu kusogeza huo mguu wako. Akitoka huko, halafu akakukosa hapa, itakuwa mbaya mno. Naomba usibiri Nai. Muage mwenyewe, aridhie.” Naih akabaki kimya. “Lakini pale chumbani kuna bafu. Kwa nini usioge pale?” Mama yake Kenny alijisogeza na kuuliza kwa unyenyekevu. “Nakuomba ubaki hapa hata kwa huu usiku tu, akubali matibabu. Niandikie vitu unavyotaka, baba yake akakununulie.” Naih akabaki akifikiria.

 “Naona ni usumbufu tu. Ngoja atoke nizungumze naye. Atakubali tu.” “Hapana Nai. Nakuomba usiondoke. Tafadhali sana.” Mama yake Kenny alibembeleza. “Tunaweza hata kukulipa.” Mama yake Emma na Jay alidakia. “Please hush. Nyamaza kabisa mama. Kuna mambo mengine hayalipiki! Hivi nyinyi, ni lini mtakuja kujifunza jamani!?” Emma alilalamika kwa uchungu sana. “Mimi ndio maana nakwambia Emma, hizi familia mbili hizi, hamna maisha kabisa hapa. Wao kila kitu wanaweka mbele pesa yao. Hamna utu hata kidogo! Mimi ndio maana niliamua kuondoka zangu kabisa hapa, na sitaki undugu na mtu. Wanataka kununua mpaka utu wa mtu! Ona walipomfikisha Kenny! Na bado hawaelewi tu. I can’t stand you guys!” Jay na yeye aliongea kwa hasira, akapiga teke kiti kilichokuwepo mbele yake, kikaruka mbali kabisa, akaondoka pale. Ukazuka ukimya wa aina yake.

Baada ya muda Kenny akatolewa akiwa anasukumwa kwenye kitanda cha wagonjwa. Naih akawa wa kwanza kumsogelea. “Sasa hivi unaonekana una usingizi.” Naih akamwambia akimwangalia kwa karibu. “Nasikia maumivu pia.” “Umemwambia nesi?” Naih akamuuliza kwa upendo. “Tunaenda kumpa dawa ya maumivu. Yatapungua kama sio kuisha.” Yule nesi alijibu swali la Naih. “Asanteni sana. Na poleni. Najua mida hii sio mizuri.” Naih alikuwa akiongea na yule nesi huku akitabasamu. “Hapana. Mida hii ndio yenyewe. Si umeona hatujachukua muda mrefu? Tulikuwa peke yetu kwenye vipimo.” Waliendelea kuzungumza huyo nesi na Naih mpaka wakafika kwenye chumba alichokuwa amelazwa Kenny, wakarudisha kitanda kama vilevile kilivyokuwa, wale wauguzi waliokuwa wamemsindikiza Kenny wakaondoka. Akarudi yule nesi aliyekuwa akimuhudumia Kenny, akaweka dawa kwenye ndipu yake, akaondoka.

Kenny akaanza kusinzia. “Kenny! Nitarudi asubuhi na uji. Nikuletee na kitu gani kingine?” Naih alijaribu kuaga. Kenny akamwangalia kwa huzuni. “Nikirudi kesho asubuhi, sitaondoka tena mpaka utoke hapa. Lakini leo nilazima niondoke ili nikaweke mambo sawa. Natakiwa kuonana na Tuse, nimlipe pesa ya kodi. Ili na yeye asimcheleweshewe mwenye nyumba. Halafu kuna vitu nilimnunulia mama, nimefungia chumbani, lazima kesho avipate. Ni dawa, na vitu vyake vingine. Nikishaweka mambo sawa, nitakuja tuwe wote. Sawa?” Kenny akatingisha kichwa huku machozi yakimtoka.

 “Kila kitu kitakuwa sawa, Kenny. Usiogope.” Kenny akatingisha kichwa kukubali. Naih alikuwa ameinama kwenye kitanda chake huku akizungumza naye taratibu. Akainama kwenye sikio na kumnong’oneza. “I love you for free, Kenny Olendekai!” Kisha akambusu shavuni. Kenny akabaki amefunga macho huku machozi yakimtoka. “Umesema utarudi?” “Kesho asubuhi. Nitarudi na uji. Ujiandae kula.” “Naomba urudi Naih!” “Lazima nitarudi, usiwe na wasiwasi.” “Na ukirudi, umesema hutaondoka mpaka tuondoke wote?” “Kabisa.” “Okay. Naomba usije ukasahau kama nipo hapa hospitalini nakusubiria wewe Naih.” “Siwezi.” Naih akambusu tena shavuni. “Asante.” Kenny akashukuru, Naih akamfuta machozi. “Usiku mwema.” “Na wewe Kenny.” Naih akatoka na Emma. 

Wakati wote, Ukweli huja kujitenga na uongo

Ni muda tu.

E

mma alimsindikiza Naih mpaka nyumbani kwake, akaingia ndani kuthibitisha kama kweli hawalali na Tuse kitanda kimoja. Walimkuta Tuse amelala chumbani kwake, hana habari. “Umeridhika sasa?” “Kabisa. Maana hata mimi huyu Tuse alishaanza kuniumiza kichwa. Habanduki ofisini kwetu!” Naih alicheka huku anatingisha kichwa. “Naomba uondoke, nioge, nilale. Nataka niwahi hospitalini kesho.” “Daah! Ila Nai, nakushukuru sana. Hujawahi kututupa! Wakati wote umekuwa msaada wetu.” “Lakini hebu njoo kwanza hapa, nikuulize kitu.” Emma na Naih wakakaa.

“Mbona Kenny hajashituka nilipomwambia habari za mama yake, akawa na wasiwasi na Tino tu!?” “Ndio maana nakwambia kuwa kuna jambo kubwa sana hulifahamu.” “Ni nini?!” “Atakuja kukwambia Kenny mwenyewe. Lakini siku uliyowaacha Dodoma, Kenny alikaribia kuchanganyikiwa.” Naih akakunja uso, kama asiyeelewa. Na Emma akajua.

“Lakini nilimuachia ujumbe wakumuaga pale mapokezi. Hakupata?” “Subiri kwanza nikusimulie. Alipata ujumbe, lakini haukusaidia. Sasa anasema, kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda, na hakupati kwenye simu, akawa anazidi kupaniki. Nora akakasirika sana. Nasikia wakaanza kugombana. Ugomvi ukazidi kuwa mkubwa, Nora akatoka pale chumbani, na Kenny naye hakumbembeleza, akapanda gari yake kurudi huku.” “Yaani alimuacha Nora Dodoma!?” Naih aliuliza kwa mshangao kama ambaye hajasikia sawasawa.

“Hujamjua Kenny wewe. Linapokuja swala la Naih, huwa hawezi kufikiria. Alimuacha Dodoma, yeye akaamua kuendesha muda uleule kurudi huku. Anasema alikuwa akikupigia simu njia nzima. Akaja hapa nyumbani anawaka kama moto. Nikamuuliza vipi? Akasema umemkimbia, na hupatikaniki kwa simu, umeenda kwa Tuse. Akawa analalamika kuwa hata simu ya kwanza alikununulia, kwa ajili ya mawasiliano yenu, lakini mama yake alimwambia kuwa ulimpa Tino.” “Haiwezekani Emma!” Naih akashangaa sana.

“Subiri sasa. Si mimi nami nikaharibu zaidi kwa kujaribu kumtuliza?” “Ulifanyeje na wewe?” “Si ndio nikamwambia kuwa uliniambia mama yake alikupokonya ile simu, sio kweli kama ulimpa Tino. Kenny akatoka usiku uleule kwenda nyumbani kwao, nakuanza kuitafuta ile simu chumbani kwa mama yake. Akaikuta imefichwa chumbani kwa mama yake. Akaanza kuwapiga wale wasichana wa kazi pale ndani, ili waseme ukweli. Ndio wakasema yale maneno yote waliyokuwa wamemwambia, walitumwa na mama yake, akawalipa na pesa. Ndio maana walimdanganya.” Naih alibaki kimya akisikiliza.

Emma akaendelea. “Akatoka hapo akaenda kumtafuta Babu Kaa. Maana aliambiwa na wale wasichana kuwa Babu Kaa, ndiye aliyeambiwa awatoe nyinyi pale.” “Usiniambie kuwa alikwenda kumtafuta Babu Kaa!?” “Ilikuwa shuguli hiyo siku ya jumamosi, sio mchezo. Haya, akaenda mpaka Kigogo. Bahati nzuri yule Mzee ni wa muda mrefu pale mtaani, anafahamika, tena kwa kuelezea watu jinsi alivyo, kwa kuwa Kenny hakuwa akimfahamu jina lake kamili. Jina hilo la Babu Kaa, alimpa Kenny mwenyewe tokea mtoto. Siunajua ndiye aliyekuwa dereva wake tokea mtoto? Kwa hiyo Kenny alivyokuwa akiruka ruka kwenye gari, yule babu akawa anamwambia 'kaa chini', basi Kenny ndio akaanza kumuita Babu Kaa.” Wote wakacheka.

“Ehe!” “Basi, akampata Babu Kaa, akamuuliza, swali kwa kifupi tu, ‘Wewe ndio uliwatoa kina Naih, pale nyumbani?’ Sasa unamjua Babu Kaa anavyompenda Kenny! Si ndio akamsimulia kila kitu. Kuwa uliondoka ukiwa unalia sana, lakini Mama Ole alihakikisha mnaondoka usiku uleule. Tena akamwambia wadogo zako walikuwa wakikucheka sana. Akamsimulia kila kitu. Vile walivyokuwa wakikucheka na maneno yote ya kukukashifu. Na yote yaliyokuwa yakiendelea huko njiani wakati anawapeleka hotelini. Alimsimulia bila kumficha.”

“Kenny akarudi kwao, akaita kikao wazazi wake. Akawaaga na kuwaambia kuanzia siku hiyo, ameamua kujitegemea, hataki msaada wa mtu yeyote, anaondoka kwenda kuanza maisha yake. Akachukua baadhi ya vitu vyake, vingine akavichoma moto, akaondoka kutafuta hoteli, hakurudi tena kwangu.” Naih akatoa macho. Kenny ni mtoto wa mama, mrithi wa mali yote ya Olendekai.

 Emma akaendelea. “Kwa kuwa aliondoka kwangu kwa hasira na hakurudi tena, siku inayofuata, jumapili asubuhi ikabidi nimtafute. Akanielekeza alipo, nikamfuata hotelini, akanisimulia kila kitu. Akaniambia anaumia sana, kwa kuwa aliamini uongo wa mama yake kuwa uliiba kabla hujaondoka pale kwake, ndio..” “Ngoja kwanza Emma. Yule mama alisema nilimuibia?” “Ndivyo alivyokuwa amemdanganya Kenny. Kuwa ile hundi aliyokuwa amemwandikia mama yako, eti ni wewe uliiba, ndipo ukatoroka, tena baada yakufumaniwa na Tino. Ili kuhakikisha Kenny anaamini, akaenda kuchukua video, iliyokuwa ikionyesha wewe ukiwa benki unachukua zile pesa ya ile hundi.” “Haiwezekani!” “Yule mama anaakili sana. Alitengeneza kisa chake vizuri, akijua Kenny atakuchukia, ili aendelee kuwa na Nora, kumbe ndio alikuwa akiharibu kabisa.” Naih akakuja uso.

“Sasa mimi nazuia nini?! Kwani yeye alidhani mimi ndiye ninayemfanya mwanae asioe!?” Emma akacheka kidogo kama anayefikiria. “Ndio maana nakwambia kuna jambo hulifahamu Nai.” “Sikuelewi Emma! Mimi sijawahi hata mara moja kumuingilia Kenny juu ya maisha yake na wanawake zake.” Ni kama Emma alitaka kuzungumza kitu, lakini akasita.

“Naomba huko nisiingilie, turudi kwenye stori yenyewe.” “Ehe!” “Sasa ile siku ya jumapili nilipomuacha Kenny pale hotelini, nilimuacha akiwa amejawa majuto, hasira, na chuki. Alikuwa anasema alikukasirikia na kukufanyia ubaya, akijua wewe ni mwizi na umemkimbia kwa ajili ya mwanaume mwingine, kumbe sio kweli. Akajua hutaweza kumsamehe tena. Akasema ndio maana sasa hivi upo na Tuse. Nikamtuliza kuwa Tuse sio mpenzi wako, akatulia.”

“Sasa jumatatu ulipotuambia unaishi na Tuse, akaona vile Tuse akikufanyia, alikaribia kuchanganyikiwa. Ilikuwa tutumie gari yangu, twende kwa kina Tye, palepale akasema yeye anachukua gari yake ndogo, anarudi kupumzika hotelini. Nikamwambia kwa vile alivyokasirika na ile mvua ilikuwa kubwa, barabara hazionekaniki, na kile kigari chake cha starehe kipo chini sana. Nikamwambia kuendesha usiku ule, nikutafuta matatizo. Nikamsihi nimpeleke tu hotelini, atakuja kuchukua gari yake kesho. Kama unavyomjua Kenny linapofika swala la Naih, anakuwa kama simba.”

“Lakini mimi najiuliza Emma, sipati jibu. Yeye Kenny anafikiri mimi sitakuja kuolewa, au? Maana tangia tupo watoto, Kenny hataki hata nicheze na watoto wa kiume! Alikuwa akiona mtoto wa kiume amekuja pale nyumbani kucheza na mimi, alikuwa analia mpaka anatapika! Ndio mama akasema niache kukaribisha marafiki zangu pale nyumbani, nicheze nao hukohuko shuleni. Nikaacha kabisa kuleta watu pale nyumbani kwao. Huyo Tino mwenyewe ilikuwa ugomvi kila siku. Mara atake tukasomee chumbani kwake yeye Kenny. Tena hapo na yeye anakuwepo hapohapo chumbani. Mara amfukuze ndani ya nusu saa. Au akuite wewe uje msomee palepale nyumbani, pembeni yetu. Unakumbuka lakini?” Emma alicheka tu.

“Yaani ikawa fujo mpaka Mia akaanza mahusiano na Tino, ndio akatulia. Na mimi sikuwahi hata kumkataza kuwa namahusiano na mtu yeyote yule, zaidi ya kumuomba asiwahi kulala, na wadogo zangu. Lakini hata hilo Kenny amenikiuka, Emma! Ameniumiza sana.” “Hapana Naih. Wamemsingizia. Hata hiyo pia, aliambiwa na Babu Kaa. Aliniapia kuwa hakuwahi hata kuwagusa wale watoto. Anasema walisha mfuata mpaka chumbani kwake, wakamvulia nguo kabisa, kila mmoja kwa wakati wake, tena zaidi ya mara mbili, lakini Kenny anasema aliwafukuza. Na mimi namwamini katika hilo. Hajadanganya, ila wadogo zako ndio walikudanganya ili wakuumize. Sasa majumlisho ya hayo yote, na vile alivyokuwa akikufanyia ofisini, na mimi nikaharibu zaidi, nikamwambia vile unavyomjua alikuwa akilala na kila mwanamke, akazidi kuchanganyikiwa.” Bado Emma alishindwa kumwambia ukweli wote, Naih. Aliendelea kuzungumza naye akiwa anaficha au anauzunguka ukweli wa mambo juu ya Kenny kwa Naih.

Hakutaka yeye ndio awe mzungumzaji wa Kenny. “Sasa ile jumatatu nilipomuacha pale nje ofisini, aliondoka kwa hasira, anasema alikata tamaa akajua hutakaa umsamehe, na yeye alikuwa ameshaua undugu na wazazi wake, akasema hakuona sababu ya kuishi tena. Anasema alikuwa akiendesha kwa hasira, huku haoni na mvua zikinyesha sana. Anasema akajishtukia amegonga zile chuma za daraja la Surrender, gari ikarushwa juu, ikatua ndani ya daraja.” “Mungu wangu!” Naih alishituka kwa sauti ya juu.

“Anasema alikaa ndani ya hiyo gari, maji yakizidi kujaa, mpaka akaokolewa. Alibahatika nyuma yake kulikuwa na gari ya polisi. Aliona yote yaliyokuwa yakitokea mbele yake. Ile ajali nzima yule polisi aliishuhudia, na ndiye aliyefanya juhudi ya kumuokoa. Sasa katika harakati za kumvuta, kumtoa kwenye gari huku maji ni mengi, yamechanganyika maji ya mvua na baharini. Giza, halafu kumbe miguu ilikuwa imeshikiliwa na vyuma, katika kumvuta, akaacha miguu mlemle ndani.” “Maskini Kenny!” “Ndio hivyo. Alipoteza damu nyingi sana. Siku tatu mfululizo alikuwa amewekewa damu.” Naih akabaki kama anawaza.

“Ila ujue sasa hivi Kenny anakuhitaji sana, Nai. Amemkasirikia mama yake, wala hataki kuzungumza naye. Anasema aliamua kuanza maisha yakujitegemea. Anasema hana jinsi ya kuwakwepa wazazi wake kama ataendelea kula, na kulala kwao.” “Jamani!” Naih aliendelea kusikitika.

“Ndio hivyo. Alikataa kila aina ya msaada kutoka kwa baba yake. Akawaaga na kuwaambia anakwenda kuanza yeye mwenyewe akiwa na elimu tu waliyompa. Baba yake alipotaka ampe hata pesa za mtaji, alikataa katakata. Alisema aliamua kuanza kuweka akili kwenye ile biashara ya Dodoma, akasema kama itashindikana angerudi kutafuta kazi aajiriwe popote, kuliko kurudi kuwategemea wazazi wake tena. Sasa kwa kupoteza miguu, najua yupo kwenye mshituko mkubwa sana. Inamaana mipango yake yote ataona imeharibika. Na nikwambie ukweli tu Naih, Kenny aliamua kutulia. Alitaka kubadili maisha yake kabisa kuachana na wanawake wote ili aoe. Lakini alishindwa.” “Kenny anapenda sana wanawake. Itamuwia ngumu kutulia” Naih alikuwa hajaelewa.

“Alishindwa kwa kuwa alijua hawezi kuja kupenda kama alivyopenda. Mwanamke wa mwisho aliyekuwa amelala naye ilikuwa Nora, na ndiye aliyepanga kumuoa. Lakini alishindwa. Tangia umeondoka, Kenny hajaweza kufanya mapenzi na mwanamke yeyote, nafikiri ndio maana Nora alimkasirikia sana.” Siku hiyo Naih alikuwa amepata habari nyingi sana, na alimuona Kenny asiye na miguu. Akili hazikuwa na uwezo wa kufikiria sana. Hakuwa hata ameelewa ni nini  au nani ambaye Emma anamzungumzia.

“Unajua nini Emma, mimi sijali vile Kenny alivyo. Nitakuwa naye wakati wote atakao nihitaji. Naomba nikalale. Kesho nimuwahi. Asante kwa kunirudisha nyumbani.” “Hamna neno. Tutaonana kesho, Mungu akitujalia.” Emma akaondoka na kumuacha Naih. 

https://cdn3.volusion.com/fjmpg.dxchy/v/vspfiles/photos/YA-56-2.jpg?1484737416

             Upendo Usio Hesabu Wingi Wa Dhambi.

N

aih alifika hospitalini akakuta sio kama alivyowakuta siku iliyopita, wote wakiwa ndani. Asubuhi hiyo akawakuta wote mpaka wazazi wao wapo nje tena kila mmoja wao haonekaniki yupo sawa. Naih akaingiwa na wasiwasi juu ya Kenny. “Kuna nini!?” Naih akamsogelea Emma, akionyesha wasiwasi. “Kwani wewe ulikuwa wapi Naih!? Nakupigia simu tokea asubuhi, sikupati! Nimekufuata mpaka nyumbani kwenu, nimekuta mmefunga nyumba!” Emma akalalamika. “Jamani! Mbona sasa hivi bado ni asubuhi, Emma! Halafu mbona sijapata simu yako hata moja? Ona simu hii hapa. Haina missed call hata moj..” Naih aliitoa kwenye pochi akakuta imezima.

“Sijui imejizimaje! Kwani vipi? Kuna kitu ulitaka nilete?” Naih akauliza huku akirudisha simu yake mfukoni na huku akipambana kushikilia vizuri kikapu kingine cha chakula, kibegi chake cha nguo na pochi yake. “Nipokee Emma jamani! Mbona unaniangalia kwa jicho la hasira na kunilaumu tu? Kwani kuna nini?” Emma akampokea pochi yake tu.

“Hali ya Kenny sio nzuri.” “Amezidiwa!?” Naih akauliza. “Kwani ulikuwa wapi Naih? Wewe si uliahidi utarudi asubuhi?” “Hivi wewe Emma unajua sasa hivi ni saa tatu asubuhi!? Nimetoka kufuata chakula kwa mama. Alinipigia simu asubuhi tena kabla sijaamka, akasema nikafuate vyakula vya Kenny. Wewe unajua mimi sina usafiri. Mpaka nigombanie daladala na asubuhi hii kila mtu anawahi kazini. Kwani vipi!? Mbona na wewe unaanza kuwa mkali na mlalamishi kama Kenny!?” “Naomba wewe uingie humo ndani.” “Kuna nini?” Naih aliendelea kuhoji. “Si uingie Naih!” Naih alizungusha macho kuwaangalia wazazi wao na Jay waliokuwa wamekaa kimya. Akawasalimia. “Karibu Naih.” Mama Ole aliongea kinyonge na kumfanya Naih ajiulize kulikoni!

Akaingia na kukaribishwa na dimbwi la maji, mkojo na damu sakafuni. Akabaki amesimama, ametoa macho. Kenny hakuwa na dripu, wala catheter yakutolea mkojo kibofuni. Vyote vilikuwa chini sakafuni. Naih alisimama pale kwa muda, tayari alishajua kilichokuwa kinaendelea. Alijua kule kuchelewa kwake kufika pale hospitalini, ndiko kumezua fujo zote zile za kimasai.

“Mama Nai alinipigia simu akitaka nikafuate chakula chako. Sasa kwa kuwa na mimi nilikuwa na dawa ambazo nilitaka kumpa Tuse ampelekee mama baadaye, nikaona ni bora kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Nikafuate chakula na nimuachie dawa zake na vitu alivyokuwa amenituma. Amenipa chai ya rangi, uji na supu. Amekwambia kwa sababu hujala muda mrefu, uanze kwanza kunywa chai, halafu unywe uji na hii supu. Kesho akijisikia vizuri, atakuja mwenyewe kukuletea zile ndizi ulizokuwa ukitaka akupikie kila siku, akishindwa, nitaenda kuzifuata.” “Kwani ni lazima ukafuate wewe?” Naih akaanza kucheka.

“Kumbe ulikuwa ukinisikiliza!?” “Wala havichekeshi, Nai!” “Sasa kwa nini huniangalii? Umekasirika nini sasa?” “Wewe ulikuwa wapi muda wote?” “Nimekwambia Mama Naih alinipigia simu nikafuate vyakula vyako, Kenny. Mbona hivyo lakini!?” “Mbona umenizimia simu sasa?” “Imejizima bila hata mimi mwenyewe kujua! Wewe si unajua mambo ya daladala? Kwani ulinitafuta sana?” “Usicheke bwana Nai! Unanifanyia kusudi. Hujali ninavyojisikia.” “Ungenigeukia ukaniona, ungenihurumia. Nimebeba mizigo kibao, ikiwepo begi langu. Nahamia hapa kabisa, kuishi na wewe Kenny, mtoto wa Olendekai. Ukitoka hapa na mimi ndio naondoka.” Kenny akamgeukia.

“Muone anavyocheka! Mkorofi wewe Kenny! Ukoje lakini?” “Weka basi vitu chini?” “Wapi? Wakati chumba chote kimejaa mikojo na damu?” Kenny akabaki akicheka. “Acha kufanya hivyo Kenny, bwana! Utajiongezea matatizo.” “Mimi nilijua ndio umeamua kunikimbia kabisa, baada yakuona hali yangu mbaya.” Naih akatingisha kichwa kwa masikitiko. Akabonyeza kengele kuomba nesi aje. Baada ya muda nesi alifika, wakasafisha chumba na Kenny mwenyewe akasafishwa na kubadilishwa nguo na mashuka yote. Kisha wakarudishia kila kitu kwenye mwili wake.

Naih alibaki akimtizama. “Nini sasa?” “Ujue watakufukuza hapa hospitalini? Wewe endelea kufanya fujo za kimasai. Mgonjwa gani mkorofi hivi?” “Naogopa sana Naih. Nakuwa kama nahisi nachanganyikiwa.” “Niambie ni nini kinakuchanganya?” Naih alikaa na kikombe cha chai, akaanza kumnywesha. “Mama Naih anapika vizuri! Ukinywa chai yake utaijua tu.” Kenny akasifia. “Ndio uanze kwa kunishukuru mimi niliyeenda kuifuata.” “Wewe ungekuja hapa, halafu Emma au Jay ndio wangeenda kufuata. Nakuhitaji Naih.” “Pole Kenny. Siondoki tena hapa mpaka uruhusiwe, na mimi ndio nitakwenda kwangu.” Alimuona Kenny amepooza.

“Nini tena? Hata ikiwa mwezi mzima Kenny, nitakuwa na wewe, usiwe na wasiwasi.” “Sasa itakuaje baada ya hapa?” “Kwa nini tusifanye jambo moja baada ya jingine? Naomba mambo mengine usiyafikirie sasa hivi.” “Lazima Naih. Siwezi kubadili ukweli kwamba nimeshakuwa mlemavu wa kudumu. Hata nikitoka hapa leo, maisha yangu hayatakuwa kama zamani.” Machozi yakaanza kumtoka Kenny.

“Usilie bwana!” “Unajua niliondoka nyumbani?” “Ndio ulikuwa ukijiandaa na kuoa?” “Hapana Naih! Niliamua kuanza maisha yangu, na mimi nijitegemee. Nilishawaaga baba na mama. Na kuwaambia sitaki tena wawe wananiwekea ile pesa wanayonipa kila mwezi. Iwe mwisho, naanza maisha yangu. Nilijua sababu yakunifanyia yote hayo, ikiwepo kunidanganya, kunipangia niwe na nani, niishije na ikiwepo kuwafukuza nyinyi, ni kwa kuwa kwanza pale ni nyumbani kwao,  nakula na kulala kwao bure. Kana kwamba haitoshi bado wananipa pesa kama mtoto mdogo! Nikaona ndio sababu ya kunifanyia ukatili kama huo. Bado wana amri na mimi kama mtoto mdogo. Nawategemea kwa asilimia zote, ndio maana nikaamua nianze maisha yangu, ili na mimi niwe na uhuru wakufanya mambo yangu.”

“Lakini ona yaliyonikuta! Nitarudi kuwa tegemezi. Na kama unavyojua wazazi wangu, hawana muda na mimi hata kidogo. Najua sasa hivi wanachowaza ni wapi watapata mtu wa kumuajiri ili wamtupie hili jukumu la kunilea mimi ili waendelee na maisha yao. Naanza kujiona mzigo. Naishi pale kwao kuanzia asubuhi mpaka asubuhi, tena na mtu ambaye hata hanifahamu! Najiuliza mwisho wangu ni nini, sipati jibu. Ndoto zangu zote zimefutika ndani ya siku moja!” Naih alimuhurumia sana.

Ndoto za Kenny.

“Malizia hii chai, halafu uniambie ndoto zako zote ulizokuwa nazo.” “Karibu zote unazifahamu Naih.” “Sio zote bwana! Najua ulisema lazima utakuja kuoa, na kuwa na watoto wengi sana, kitu ambacho bado unaweza kuja kufanya. Hata kama ukitaka kuoa mara baada ya kutoka hapa hospitalini, na mwakani ukawa na watoto mapacha, pia inawezekana. Unakumbuka tuliangalia ile video inayofundisha jinsi ya kupata watoto mapacha? Kwa hiyo unaweza Kenny.”

“Nani atakubali kuolewa na mlemavu, Naih?” “Hee! Wewe ukoje Kenny!? Hujaona walemavu wenye wake wazuri tu na watoto? Acha kujikatia tamaa bwana!” “Labda wale waliozaliwa walemavu. Lakini mimi!” “Wewe una nini?” “Naih! Yaani nije kumfuata mwanamke sasa hivi nikiwa mlemavu! Akiniuliza nilikuwa wapi wakati nina miguu yangu yote miwili?” “Mwelekeze kwangu, mimi nitampa majibu.” “Acha utani Naih.” “Kumbe unafikiri nakutania!? Kama wakati huo hukuwa tayari kuoa? Kwani kuna mtu anapanga kukutwa na matatizo? Yaani sasa hivi ushindwe kuoa kwa sababu umepatwa na matatizo!? Acha kabisa Kenny. Wewe nipe ndoto zako nyingine unazoona haziwezi kutimia. Hilo la kuoa sioni kama kuna kitakacho shindikana.” Kenny alimaliza ile chai, akarudi kujilaza.

Akabaki kama anayefikiria, Naih akimuweka sawa na kumfunika shuka vizuri. “Naih?” Naih akarudi kukaa. Kisha Kenny akaendelea. “Kama ikitokea nataka kumuoa mwanamke ambaye alikuwepo siku zote, halafu mimi nilikuwa nikihangaika na wanawake wengine?” “Nimekwambia niletee mimi. Kama hutaki kumleta kwangu, ukiwa tayari unataka kumchumbia, uniambie tufungue darasa. Unauliza maswali yako yote yanayokufanya ushindwe kumfuata huyo mwanamke, halafu mimi nikupe majibu yake.”

“Unavyorahisisha maisha! Utafikiri nirahisi hivyo.” “Maisha ni marahisi sana Kenny, ni wewe tu unataka kuyafanya kuwa magumu.” “Sasa mtu kama huyo unamwambiaje?” “Rahisi sana. Unamwambia katika wanawake wote uliokwisha lala nao, hivi ni elfu au ni milioni?” “Acha basi Naih!” Naih akaanza kucheka.

“Mimi namaanisha Kenny. Unamwambia, katika wanawake hao mamilioni niliokwisha sijui ni kulala nao au utamwambia kuwa nao na mahusiano, wewe unajua ulichokuwa ukifanya na hao wanawake wote, sasa unamwambia katika hao wooote, nimekuchagua wewe ndio uwe mke wangu. Hapo na mimi nitakuwepo kuongezea msisitizo. Nitamwambia tena anatakiwa ajisifu, Kenny hanaga mahusiano na mwanamke kwa muda mrefu. Kwa yeye kuchaguliwa kuja kuwa mke wa Kenny Ole, lazima akatoe sadaka kanisani. Acha utani kabisa Kenny. Wewe pona, tukaanze kutafuta mke. Mbona utaoa tu. Nipe ndoto yako nyingine ambayo unawasiwasi kuwa haitatimia tena.” Kenny alicheka na kutingisha kichwa.

“Lete ndoto nyingine.” Kenny alianza kufikiria tena. Walikuwa wawili tu hapo chumbani. “Nilipanga au tuseme nilishatoka nyumbani, na nilishawaaga wazazi kuwa naenda kujitegemea, kama nilivyokwambia. Sitaki tena msaada wao, sasa itabidi kuja kurudi kuwa tegemezi tena.” Kenny akaanza kutokwa na machozi. “Ngoja kwanza Kenny. Sasa kitakachokurudisha kuomba pesa kwenu ni nini?” “Si nimekuwa tegemezi?” “Kwani ni nini kilichokusukuma kufikiria kuanza kujitegemea?” “Nimeona umri umekwenda Naih. Nitategemea wazazi mpaka lini?” “Kwa hiyo baada ya ajali umerudi kuwa mtoto!?” “Hapana Naih!” “Sasa ni nini kimebadilika, Kenny!?” “Nafanyaje na huu ulemavu?” “Kwani wewe ulitaka kufanya nini kabla ya hapa? Nyamaza kabisa, unisimulie ukiwa umetulia.” Kenny akatulia. Naih akamfuta machozi, akanyamaza.

“Unakumbuka ile safari ya Dom?” “Nakumbuka.” “Sasa baada ya kuniandikia ule mchanganuo vizuri, na kunishauri ninunue ile nyumba nijenge vyumba vya wanafunzi, na kuweka maduka kwa mbele, ndio nilitaka kuanza kufanya hivyo. Ile siku ya jumatatu wakati nipo ofisini, nilikuwa naandika mchanganuo mzuri. Nikaongea na mwenye nyumba, tukakubaliana bei. Nikamtafuta rafiki yetu mmoja hivi, tulisoma naye na Emma, nikamuomba anitengenezee ramani nzuri ya ujenzi wa ile nyumba, akakubali, tena kwa pesa nzuri tu. Lakini ona sasa!” “Sielewi, Kenny!” “Huelewi nini Naih? Na hali hii nafanyaje hiyo biashara?” “Ndio maana nakusihi ukubali matibabu, tutoke hapa haraka, mambo yaendelee. Mimi sioni kipingamizi hata kimoja hapo. Mbona unaweza kufanya mambo yote hivyo ulivyo?” Naih aliendelea kumsisitiza.

“Najua ulisema ile biashara haihitaji usimamizi mkubwa, lakini mwanzoni nilazima kuwe na usimamizi, Naih. Kusimamia ujenzi ukamilike, na kuhakikisha inaanza na wateja wa uhakika, ndipo unaweza kuacha.” “Ulitaka kusimamia vipi? Yaani kuwepo Dodoma?” “Nilipanga kuhamia huko kwa muda. Hata lile shamba la zabibu, nilitaka nitafute pesa, niongezee na chache nilizonazo, nilinunue. Lakini vyote hivyo vitabaki kuwa ndoto.” Naih akakunja uso kama bado haoni tatizo lilipo.

“Kwanza labda niulize, unayo pesa ya kuanza hizo biashara?” Naih akamuuliza taratibu tu. “Ninazo kiasi. Nimepungukiwa kidogo tu. Nilitaka kutafuta kazi, hata kwa mwaka mmoja, halafu nifanye kazi kwa bidii, huku natunza hizo pesa, na niendelea na kile kinachowezekana sasa. Au niseme niwekeze kwengine huku nimeajiriwa. Lakini sasa hivi hata nikisema nitafute kazi, nani ataniajiri Naih?” Kenny akatoa kipingamizi kingine.

“Unakumbuka kipindi kile tunataka kutengeneza hizi cheni zenye alama yetu? Ukataka iwe ya thahabu.” “Nakumbuka Naih. Nilitaka kuweka kumbukumbu ya kudumu kwenye maisha yako. Kwa jasho langu sio baba yangu.” “Kumbe unakumbuka! Na je, unakumbuka ulivyohangaika mpaka ukapata pesa?” “Lakini wewe na Mama Naih, mlikuwa mkinisaidia. Mama Naih alikuwa akipika maandazi, sambusa na vitumbua, wewe unanisaidia kuvipanga vizuri kwenye mifuko, na kufunga kwa usafi, halafu mimi ndio nikawa naenda kuuza.” “Sawa kabisa. Unakumbuka uliuza kwa muda gani?” Kenny akacheka.

“Nilikuwa nalazimisha kila familia wanayofahamiana na mama na baba, wasinunue kitafunwa kwa mtu mwingine ila kwangu tu. Nafikiri kwa miezi miwili mfululizo, mimi ndio nilikuwa nikiwauzia familia zote kifungua kinywa.” “Sasa je?” “Lakini wakati ule wewe ulikuwepo Naih. Sasa hivi siwezi tena. Nikikosa mtu wa kuniuguza au kunisaidia? Au nikipata mkorofi?” “Sasa wakati huo mimi nitakuwa wapi?” “Sijui Naih!” “Mbona unasahau viapo tulivyoapiana Kenny? Unakumbuka nilikula damu yako na wewe ulikula yangu?” “Sasa si wakati ule? Sasa hivi nimebadilika. Haukula AMINI na mlemavu, Naih!” “Sikumbuki kama tulipeana masharti Kenny.” Naih akajiweka sawa.

Akaendelea. “Mimi bado natunza kiapo changu. Na nitasimama na wewe, wakati wote. Matatizo uliyopata, hayakuzuii kutimiza ndoto zako hata kidogo. Kenny ninayemfahamu mimi ni mpambanaji. Sijawahi kuona unataka kitu, ukashindwa kukipata. Usikubali haya matatizo yasimame mbele yako. Unauwezo mkubwa sana wakufanya mambo Kenny. Ikilazimu kuuza tena vitafunwa ili kupata pesa ya mtaji, tutafanya, na mimi nitakuwepo.” “Sasa mipango yote ni Dodoma!” Bado Kenny aliona vipingamizi.

“Tutaenda wote Kenny. Siwezi kuruhusu mtu mwingine akuhudumie wakati mimi mwenyewe nipo. Eti niwepo sehemu nimetulia, najua kabisa Kenny mgonjwa mahali, anahitaji msaada wangu! Kwanza sitaweza hata kulala. Unajua tokea unapata ajali, nilikuwa mgonjwa lakini sikujua ni nini kinanisumbua? Nikamwamsha Tuse, nikamwelezea ninavyojisikia, akaniombea, lakini sikupata nafuu mpaka kesho yake asubihi ikabidi nimpigie simu Emma kumuomba akutafute. Nikamuelezea kuna kitu nakihisi moyoni kuwa haupo salama, nikamuomba akutafute ili tujue kama upo salama. Ndio Emma akaniambia na yeye ndio amefika hospitalini, umepata ajali mbaya sana iliyokusababishia kupoteza miguu. Sikudanganyi Kenny, nilitapika kama niliyechanganyikiwa. Nilikuwa nakuja kujaribu kama nitaruhusiwa kukuona, kuanzia asubuhi nakaa hapo nje, mpaka usiku, bila kuchoka. Hapa nafanya kwa ajili yangu wala sio wewe. Mimi mwenyewe siwezi kuwa na furaha au utulivu mahali kama nikijua upo kwenye matatizo.” Kenny alilia sana.

“Naomba ukubali matibabu, turudi kazini. Hakuna kilichoharibika. Tena huu muda tutakao kuwa hapa hospitalini, tuutumie vizuri sana.” “Kufanyaje!?” Kenny akauliza huku akilia. “Kupanga mipango vizuri. Nini kinaanza na nini kisubiri. Tena kinachosubiri, kinasubiri kwa muda gani, na kwa nini kisubiri. Tatizo likiwa ni pesa, itabidi kusubiri mpaka tutoke hapa, tukazisake hizo pesa. Tena tukiwa tumeshajua jinsi ya kufanya ili kupata hiyo pesa.”

“Haya, kama tatizo ni sisi kutoweza kufanya kwa kuwa unaugua, naweza kwenda mimi mwenyewe au Emma. Lazima tuhakikishe kuwa mpaka unapona kabisa, tayari kuna biashara inayokuingizia pesa. Tena kuna biashara nyingine niliona mtu akifanya, nikajiambia ni biashara ya kuiga. Ni kama yakijinga hivi, lakini inaingiza pesa. Nitakuelezea vizuri. Ukila vizuri, na kunywa dawa ipasavyo, utapata nguvu, tutaanza kazi. Tena kwenye hikihiki chumba wanachokutibu, tutakigeuza ofisi.” Kenny akapata tumaini jipya. Alionekana mpaka usoni.

“Naomba niwekee uji.” Naih alicheka sana. “Naona bosi wangu umeamua kurudi kazini.” “Tena kwa kasi upya. Unajua nilikata tamaa kabisa?” “Pole. Utafanikiwa tu.” “Naomba useme tutafanikiwa. Ukisema nitafanikiwa, naogopa, naona kama unaniacha tena peke yangu!” “Basi tutafanikiwa sana, usijali bosi.” Naih akamuwekea uji, Kenny akaunywa wote. “Naona uzima umerudi!” “Nataka nipone Naih. Ila nimeacha vitu vyangu hotelini. Nalipia pesa nyingi. Sitaki viendelee kukaa pale, ninapoteza tu pesa!”

“Unataka nimuombe Emma avirudishe nyumbani?” “Hapana, Naih. Naona ni kama nitakuwa narudi nyuma. Unajua nilikuwa nikiishi kwa Emma?” “Sikuwa nikijua.” “Basi nilikuwa nikiishi kwake. Lakini baadaye nikajidharau sana. Nikajiona mimi sina akili. Emma na mimi tumezaliwa mwaka mmoja, tumesoma shule moja, tumekua pamoja. Alikopita Emma, ndiko nilikopita na mimi. Ona mwenzangu ana ofisi ya kueleweka na amejenga, lakini mimi nilikuwa nikihangaika tu na starehe! Nilikuja kujisikia vibaya sana. Nikazidi kujidharau pale nilipojua hata wewe unaishi kwako, halafu mimi sina hata shuka nililonunua kwa jasho langu! Niliumia sana.” Kenny aliongea kwa uchungu.

“Ile siku ya jumatatu nilichelewa kutoka ofisini, kwa sababu nilikuwa napanga pia na maisha yangu. Nilitaka na mimi nibadilishe kabisa maisha yangu.” Machozi yalianza kumtoka tena. “Nafikiria kuja kurudi nyumbani au kwa Emma, ni kama narudi nyuma.” “Nikushauri kitu?” Kenny akatingisha kichwa kukubali. “Tumtume Emma, akavichukue pale hotelini, akaviweke nyumbani kwangu. Kwa kuwa tutakuwa wote hapa hospitalini, mpaka utakaporuhusiwa haitakuwa na shida. Na utakaporuhusiwa pia sitakuacha mpaka nihakikishe unaweza kujitegemea vizuri.” Naih akafikiria kidogo.

“Unajua Mimi nilifikiria unarudi kwenu, nikataka kumuomba Mama Ole, aniruhusu nirudi pale kwa muda, nikuhudumie mimi mwenyewe mpaka upone kabisa.” “Sitaki kurudi nyumbani Naih.” “Basi haina shida. Tukiruhusiwa hata kesho, tunaweza kuishi wote kwa muda, mpaka upone. Ndio tutajua kama tunahamia Dodoma kwa muda au tunabaki hapa Dar. Kama ni hapa, nitakusaidia kutafuta kwako, ukipapenda, nitakusaidia kuhama, na kukusaidia kumuweka sawa Mama Ole mdogo. Akishakaa sawa, na tukakamilisha swala la ndoa yako, ndio nitakukabidhisha kwake rasmi. Umenielewa?” “Nimeelewa Naih. Nakushukuru sana.” Naih akacheka.

“Sasa naomba sasa hivi ulale, ili upumzike. Ukiamka, tunacheza karata.” Kenny akacheka. “Nimefurahi tutakuwa wote. Yaani sasa hivi naweza kulala. Nilikuwa silali Naih. Nikipitiwa na usingizi hata dakika mbili nashituka, nakumbuka mimi ni mlemavu! Lakini sasa hivi umenipa tumaini. Hofu imepungua.” “Safi sana. Lala basi.” Alimfunika vizuri, akampa na busu la shavuni. Akamuona amefunga macho, akataka kutoka. “Unaenda wapi tena!?” Kenny alishituka sana kama aruke pale kitandani, Naih akageuka kabla hajafungua mlango.

 “Naomba usije ukaondoka Naih. Nitachanganyikiwa nikija kuamka halafu haupo.” Naih akarudi.  “Nataka nikawaruhusu wazazi wenu na kina Emma wakalale, mimi niwapokee kukaa hapa. Unajua wamekuwa hapa tokea umepata ajali? Wamechoka sana.” Kenny akatulia. “Ni sawa?” “Hata wasiporudi tena sina shida. Ila wewe ubaki Nai. Tafadhali.” “Nitarudi Kenny. Siwezi kuondoka.” Akainama na kumbusu tena shavuni. “Asante.” Kenny akashukuru, akapitiwa na usingizi hapohapo.

************************

Naih alitoka akawasogelea wazazi wake Kenny. “Nashauri mkapumzike. Mimi nitakuwepo hapa.” “Nakushukuru sana Naih, binti yangu.” Mzee Ole alitoa shukurani yakutoka moyoni. “Na mimi nashukuru kuniruhusu kuwa hapa.” Naih naye akashukuru. Emma na Jay wakasimama na kuwasogelea. “Naomba shukurani zangu nizitoe nikiamka. Nina usingizi mpaka nakaribia kuchanganyikiwa.” “Pole Emma. Basi ukiamka nipigie nikupe maagizo.” “Si unataka vitu vya Kenny vihamishiwe kwako?” Naih akacheka. Akajua kuwa mazungumzo yao yalikuwa yakisikilizwa na watu wote pale nje.

“Ndiyo Emma. Na urudi hapa na video game zake zote. Begi lake la kompyuta, na..” Naih alitulia kidogo. “Vipi?” Jay akauliza. “Simu yake iko wapi?” Wote wakamgeukia Emma. “Nafikiri ilipotea siku ya ajali. Sikupewa kitu chochote zaidi ya mkanda wa suruali. Lakini naweza kwenda kumnunulia simu nyingine.” “Basi naomba ukiweza umuombee na line ileile.” Naih aliongeza. “Hamna shida.” “Asante bosi wangu. Au kazi imeisha sababu ya kutofika kazini.” “Mbona utalipwa tu. Yaani kuwepo wewe hapa na kumtuliza hivyo Kenny! Nahisi na mshahara utaongezeka.” Naih alicheka sana.

“Bosi wangu una jeuri wewe! Unafikiria kuniongezea mshahara?” “Kwanza wale wateja wako wakorofi, kama Pateli na wenzake utahamia nao wote hapahapa hospitalini.” Naih akacheka sana. “Wewe huwa unawawezea. Sasa endelea kupokea oda zao kisha mtumie Sifa. Sitaki kabisa shida.” “Wala usijali bosi. Wewe nenda kapumzike. Ukirudi tutaongea zaidi.” “Ulitaka turudi saa ngapi?” Mama Ole alijirudi kama sio yeye! Naih akafikiria kidogo.

“Sema tu Nai. Usisite.” Jay akaingilia, alimuona ni kama anataka kuzungumza lakini amesita. “Nilikuwa na wazo hili, sijui kama ni sawa? Kenny bado yupo kwenye hofu. Kama mtaweza kuzungumza na marafiki zenu, wamwache kwa muda kwanza atulie. Wasije hapa kumuona, na kumpa pole kila wakati, ili atulie kabisa. Akishaona mipango yake inakwenda sawa. Hakuna kilichobadilika, hata watu wakija na kumpa pole, hataichulia kwa uchungu kama sasa. Sasa hivi watu wakija na kuanza kumuhurumia, anazidi kuona yupo kwenye matatizo makubwa. Au nyinyi mnaonaje?” “Ni wazo zuri. Tutawatumia washikaji wote ujumbe, wasije huku.” Emma alikubali bila shida.

“Na tutawaachia maagizo hao walinzi wasiruhusu mgeni yeyote hapo chumbani kwenu.” Mzee Ole akaongeza. “Naona hiyo itasaidia. Lakini nyinyi mngeenda kupumzika kabisa. Mkiweza kurudi leo ni sawa. Lakini mkishindwa, hata kesho.” “Una uhakika Nai? Maana mimi nasikia kichwa kinauma, nahisi ni pressure ipo juu. Nataka ninywe dawa nilale kabisa. Naweza kupitiwa usingizi kweli nikaamka usiku sana, nikashindwa kurudi.” Mama Ole aliongeza. “Usiwe na wasiwasi kabisa mama Kenny. Mimi ndio nimefika hapa. Chochote kikitokea nitamjulisha Emma, halafu yeye atawajulisha na nyinyi. Msiwe na wasiwasi.” “Chakula chako na chake?” “Mama amesema atakuwa akipika. Akishindwa kuleta, Emma ataenda kufuata. Msiwe na wasiwasi.” Ole na mkewe wakaangaliana. “Asanteni sana Naih.” Jay akashukuru. “Wala msijali.”

Kutaka Kuvuna Kusiko Pandwa.

“Jay!” Mama yake akamuita kwa upole, Jay akamgeukia. “Utakuja nyumbani jioni?” “Unaniuliza mimi au nimekusikia vibaya!?” Jay akauliza kwa mshangao. “Ndiyo ni wewe Jay. Tutaandaa chakula cha usiku uje tule pamoja. Ni muda mrefu tokea uondoke.” Jay akamgeukia Emma, akacheka kwa kusikitika. “Leo hampo busy? Au niulize shuguli zenu na zile starehe zenu zile zilizokuwa zikiwafanya mtuache na wafanyakazi wakitutesa na kutuchapa, zimeisha? Eti?” Jay akauliza kwa hasira, akabaki akiwatizama wazazi wake.

“Au mnataka kufanya maonyesho yenu yale mbele za watu kuwadanganya sisi ni familia bora? Au niulize, ni nani leo mnayemualika nyumbani kwenu mnayetaka kutuonyesha kwao kama wanyama wa kituo cha kivutio?” Kimya. “Kama leo mlikuwa mnamgeni wenu mlitaka kutuonyeshea sisi kama moja ya vitu vyenu mnavyomiliki hapa duniani, basi mjue mmeumbuka. Hiyo biashara mimi niliiacha muda mrefu sana, na ndio maana nilihangaika nikakimbia hapa nchini. Sitaki kuwaona nyinyi wala lile jumba lenu. Linanikumbusha mateso makali sana ya makuzi yangu na Emma.”

“Mlikuwa mkituacha mle ndani tukiteswa kama paka wa porini, nyinyi hamna habari wala hamjali. Walikuwa wanatupiga watakavyo huku wakitutukana na kututendea unyama ambao hapa siwezi kuutamka sasa hivi. Unakumbuka Emma alishakwambia wewe mama?” Emma alicheka nakutingisha kichwa kwa masikitiko.

“Hawezi kukumbuka Jay. Unapoteza muda wako.” “Ngoja nimkumbushe jibu lake kama yeye amesahau. Maana mimi sijasahau mpaka leo nakumbuka mpaka ile sura yake na sauti wakati akikujibu. Tena alikuwa akikujibu bila huruma wakati wewe ulikuwa ukimlilia usiku ule ukimuomba huku umemshika gauni lake, wasituache usiku ule peke yetu. Kwanza ulimsukuma Emma mpaka akajigonga kwenye meza ya chumbani kwako, ukaendelea kujipodoa, ukatuacha huku ukitusisitiza tuache utundu ili tusichapwe. Tena uliongea mbele ya yule dada!  Ilikuwa ni kama ulitupalia makaa ya moto. Emma alipigwa usiku ule, mpaka ikabidi mimi niingilie kati, ile adhabu inipate mimi. Tukaenda kutupwa nje, mpaka mliporudi wewe na huyo mumeo, tena mlikuwa mmelewa. Mlipotukuta pale nje, wakati yule dada amelala ndani, tukawaambia tumefungiwa nje, baridi na mbu vyote vilikuwa vimetulemea. Unakumbuka wewe, ulienda kumuuliza yule dada kwa nini alituacha nje, akawaambia tulitoroka ndani, hatutaki kulala, tunamsumbua sana. Unakumbuka wewe unayejiita baba yetu?” Jay akamgeukia baba yake.

“Mkaamua msitusikilize sisi, mkamuamini yeye. Ulitoa mkanda wa suruali yako, ukaanza kutuchapa! Bwana ulitutandika mpaka nahisi pombe ilikuisha. Emma alikaa siku tatu kitandani anaumwa. Kenny na Naih ndio walikuwa wakituuguza. Mama yake Nai ndiye alikuwa akipika chakula anamtuma Kenny na Naih watuletee chakula pale ndani kwenu.  Kwa kuwa tulikuwa tukinyimwa chakula! Wakati nyinyi mlikuwepo, mnarudi nyumbani kila siku mmeshiba na mmelewa.”

“Kila siku Babu Kaa ndiye aliyekuwa akitupeleka hospitalini na Mama Naih anatupakata ili tuchomwe sindano za malaria. Tulikuwa tunaugua malaria mara kwa mara kwa kufungiwa nje kipindi cha usiku wakati wafanyakazi wenu wanalalana  ndani. Leo unasema twende wapi tena?” Jay akauliza kwa kejeli.

“Sasa naomba mnisikilize nyinyi wawili. Narudia tena. Nipo hapa kwa ajili ya Kenny tu. Kenny akipata nafuu, naondoka. Nitakuwa nyumbani kwa Emma. Endeleeni na maisha yenu ya kutafuta pesa na kufanya starehe, na mimi naendelea na maisha yangu.” Jay akaendelea taratibu tu. “Mnajua nyumba ninayoishi kule? Sio jumba kama lenu. Lakini sijawahi kufurahia maisha kama sasa hivi. Nalipa kodi yangu, nalala usingizi mnono. Siwazi fujo za nyinyi walevi, wala sifikirii kuja kuamshwa na kichapo cha mikanda kwa makosa ambayo hata siyajui. Ninalala kwa amani naamka kwa amani, nyumbani kwangu. Hakuna anayenifanyia unyama usiku.”

“Nilishawaambia, hata mkifa leo, sitaki hata shilingi yenu. Naomba msinifuate nyuma. Naweka msisitizo. Wote tupo hapa hospitalini kwa maslahi binafsi. Najua nyinyi mpo hapa kwa kujionyesha tu. Yaani mpo kama mbuga za wanyama. Hamna hata mmoja wenu hapo mwenye uchungu na sisi. Na mimi nipo hapa kwa ajili ya Kenny. Kwa hiyo tuheshimiane. Ndio maana nilipowakuta hapa, sikuwasemesha kabisa. Niliwaacha mfanye yenu lakini naona mnanifuata nyuma. Tafadhali nawaomba tena, msinibugudhi. Fanyeni yenu, na mimi niacheni nifanye yangu. Iteni waandishi wa habari muuze sura zenu na stori zenu mnazotaka zisomeke magazetini, lakini mimi msinishirikishe tena. Naamini tumeelewana. Mamilionea wa mjini! Furahieni mali zenu, achaneni na sisi, tuhangaike kivyetu.” Naih alikuwa kama amepigwa na butwaa.

“Sasa Naih, ‘Mimi wa Kenny?’” Jay alimgeukia Naih kama hakuwa ni yeye aliyekuwa akizungumza na wazazi wake kwa uchungu na hasira. Naih akacheka. “Umenikumbusha mbali! Mimi wangu!’ Nyinyi nendeni mkapumzike kabla sijabadili mawazo. Au mnataka niondoke niwapishe?” Emma akamvalicha Naih pochi yake shingoni aliyokuwa amempokea tokea anafika hapo, akaondoka bila kugeuka nyuma. Naih alibaki akicheka. “Jay! Mpe Emma funguo hizi za chumbani kwangu.” Naih alizitoa kwenye ile pochi, na kumrushia, Jay akazidaka na kuondoka, waliwaacha wazazi wao pale pale. “Tutaongea zaidi kesho, Naih. Ngoja nikapumzishe kichwa. Maana sasa hivi naogopa hata kuongea neno, nisije haribu zaidi.” Mama Ole akasimama, Naih akarudi ndani na kuwaacha wazazi hao wanne hapohapo nje.

************************

Kwa kawaida kitengo hicho cha MOI kilikuwa na vyumba vya kulaza wagonjwa vya binafsi au kulipia kwa juu zaidi na wodi wanazolazwa wagonjwa wengi kwa pamoja. Lakini hata hizo za kulipia, wanazolaza mgonjwa mmoja kwenye chumba kimoja, hawakuwa na utaratibu wa ndugu kulala hapo kumuhudumia mgonjwa wao, ila manesi ndio wanao toa huduma zote kwa mgonjwa. Sasa kutokana na ugumu au ukorofi aliokwisha wafanyia wauguzi wa sehemu hiyo, na kukataa matibabu mpaka awepo Naih, ikabidi Kenny, mtoto huyo anayekuja kuonwa na wakubwa wa nnchi, afanyiwe tofauti.

Naih alikubaliwa kuwepo hapo ili Kenny atibiwe. Kwa kawaida huwa inachukua si chini ya majuma mawili kutibiwa wagonjwa wenye tatizo kama la Kenny, waliokatwa kabisa miguu. Wengi wenye kinga bora mwilini, majuma mawili huwatosha kupona kabisa na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Lakini walitakiwa wawe wanarudi hospitalini hapo kwa ajili ya mazoezi tu.

Kenny alianza matibabu rasmi chini ya uangalizi wa Naih. Alikuwepo hapo asubuhi hadi asubuhi kumtia moyo na kufanya naye kazi. Hapakuruhusiwa wageni zaidi ya ndugu wa karibu tu. Mama Naih ndiye aliyekuwa akileta chakula, wazazi walikuwa wakija kutembea na walijiwinda kwa kila wanachoongea kwa watoto hao. Naih alishapiga simu Dodoma kuzungumza na muhusika aliyekuwa akiuza nyumba aliyokuwa akiitaka Kenny. Kwa kuwa ilikuwa nyumba ya urithi, ndugu walitaka iuzwe wagawane pesa, kila mtu aendelee na maisha yake. Wakakubaliana pesa ambayo Kenny alikuwa nayo.

************************

“Itabidi niondoke kesho asubuhi. Nikawalipe na kukamilisha mambo ya kuandikishana kisheria ndipo nirudi. Sitakawia.” “Huwezi kuniacha hapa Naih. Tafadhali. Labda twende wote.” “Sitakawia Kenny!” “Hapana. Siwezi kuwa hapa peke yangu Naih. Naogopa sana.” Kenny alishabadika. “Jamani, mimi nitakwenda. Nielekezeni ninachotakiwa kufanya, nikafanye hata kama kuna upungufu wa pesa mimi nitaongeza.” “Kweli Jay?” “Kabisa.” Jay akaendelea.

“Nipo hapa kwa ajili ya kuwasaidia. Nikiwaona wadogo zangu mnaepukana na hizi pesa za hawa wamasai, nafurahi sana. Hakuna kitu namuomba Mungu atusaidie, kuwaonyesha hawa wazazi wetu kabla hawajafa, kuwa unaweza ukatajirika na bado ukawa na roho ya kibinadamu tu. Kujali wengine, hasa watu wakaribu yako, mbali na nafsi yako.” “Basi tuondoke alfajiri na mapema ya kesho. Tunaweza kugeuza kesho kutwa, tukikamilsha kila kitu.” Emma akaongezea. Kenny alivuta pumzi kwa nguvu akajirudisha kulala vizuri.

“Asanteni sana. Basi tutawasiliana mkifika huko.” Naih akashukuru.  “Ila naona kwa awamu hii ya kwanza, pesa ipo yakutosha. Asante sana Jay.” Kenny naye akashukuru. “Pamoja sana. Hakuna kitakacholala Kenny. Kama alivyokwambia Naih, wewe hangaika utoke tu hapo, basi.” Kenny akatulia.

Wazazi hao wanne, walikuwa kimya kabisa kama waliokuwa wameonyana kunyamaza kila wanapokuwepo hapo. Walikuwa wakifika asubuhi muda wakuona wagonjwa, na kurudi jioni. Mchana walimpigia simu Naih kuulizia hali ya Kenny. Kenny hakutaka kula hata matunda waliyokuwa wakileta au juisi. Alihakikisha wanaondoka navyo, hawaachi kitu hata kimoja hapo. Alipoona hawaelewi, akiwa amekasirika wakati wazazi wake wameingia na matunda na maua, aliwataka watoke na vitu vyao wakampe mtu mwingine sio yeye. Mzee Ole hakubisha, aliondoka na vile vitu kwa haraka sana. “What part of I don’t need your help, you don’t get it?” Kenny aligomba akimuuliza mama yake ni kipi kigumu kuelewa kuwa hahitaji msaada wao tena!

************************

Kulikuwa na utaratibu wa wagonjwa wa aina ya Kenny, hospitali kuwapatia watu maalumu kwa ushauri ili kuwawezesha kuishi na hali hiyo mpya. Huyo mtu alipokuja kutaka kuzungumza na Kenny, alikataa na kumfukuza. “Utapungua wapi kama ukimsikiliza, Kenny!?” Kenny akanyamaza. “Kenny?” “Naomba nipe muda Nai. Naogopa sana.” “Ndio maana unahitaji kumsikiliza. Inawezekana unaogopa kwa kuwa umekubali habari zinazopita kichwani mwako ambazo si sahihi. Naomba tumsikilize. Mimi mwenyewe nataka kumsikiliza na kumuuliza maswali kwa ajili yangu. Ndio maana wanapopita madaktari, mwenzio nauliza maswali mengi ili tukitoka hapa nijue tutakuwa tukiishi vipi. Naomba tutumie huu muda vizuri, kwa kuuliza maswali mengi ipasavyo. Ili tukitoka hapa, tusiwe tumebakisha swali lolote.” “Si wamesema wataniruhusu hapa nikiwa nimepona kabisa?” “Sasa?” Naih akauliza akiwa hajamuelewa.

“Sasa utakuwa na shida gani tena? Si umesema nikipona utaniacha?” “Kwa nini hatuzungumzi Kenny, jamani!? Kama hicho ndicho kinachokutia hofu, si ungeniambia?” “Nikwambie nini, sasa?” “Kile kinachokusumbua mawazoni.” “Naogopa Naih. Naona ni kama nakung’ang’ania sasa hivi wakati nimekuwa mlemavu. Naona nakupa mzigo usio kuhusu.” “Kenny! Mbona unajishuku? Kwa nini usiniache mimi mwenyewe nikajisikia hivyo kuliko kunipandikizia hayo mawazo? Siwezi kukuacha mahali wakati najua wazi unanihitaji! Tutakuwa wote mpaka utakapokuwa tayari kuishi peke yako au kuondoka kwangu.” “Hata kama itachukua mwaka?” “Hata miaka miwili. Nimekuahidi nitakuwa na wewe. Na wamesema ndani ya miezi 3 hadi 6, watakupa miguu ya bandia na kuhakikisha unaweza kuitumia ipasavyo. Unaweza kukuta ndani ya muda mfupi sana, unarudia hali yako ile ya zamani. Usiogope. Naomba tuwape nafasi ya kuzungumza na sisi. Sawa?” “Sawa.” Kenny akakubali.

****************************

Baada ya majuma mawili na nusu, Kenny alikuwa amepona. Maumivu aliyokuwa akiyapata ya kifua yaliisha kabisa na vidonda vyote vikapona. Hakuwa ameweza kuangalia miguu yake tokea amepata ajali. Wakati wote Naih ndiye alikuwa akiiangalia wakati anasafishwa na wauguzi na kumpa habari inaendeleaje. Alitolewa nyuzi, akabaki amefunga macho. “Amepona kabisa. Tena vidonda vyote vimekauka vizuri tu. Leo ndio mnaruhusiwa, lakini itabidi awe anarudi kwa mazoezi. Akionekana anaendelea na mazoezi, tutampima miguu mipya, nakumfanyia mazoezi zaidi, mpaka aweze kutembea vizuri.” Nesi aliyekuwa akimuhudumia Kenny alikuwa akiwapa wazazi wa Kenny maelekezo ya mwisho kabla hawajatoka. Kenny alikuwa akitokwa na machozi, huku amefunga macho.

“Nitakufunika Kenny. Huna haraka yakuangalia sasa hivi. Bado tuna muda mrefu sana. Ukiwa tayari utaangalia. Hamna haraka. Sawa?” Naih alimuongelesha kwa upole. Kenny akatingisha kichwa. “Huna haja yakuogopa Kenny. Utarudi kutembea kama zamani. Wala hutajua kama ulipoteza miguu. Mambo siku hizi yamebadilika. Wapo wengi tu wanatembea na miguu ya bandia lakini hata nyinyi wenyewe hamuwatambui. Usikubali hata kuhisi kuwa ile ajali imebadili maisha yako. Bado una safari ndefu tu ya kufurahia ujana wako. Una uwezo wakurudia maisha yako ya zamani na ukaishi kwa furaha tu.” Mshauri aliyekuwa akipita hapo kila siku kuzungumza na Kenny, naye alikuwepo wakati nesi akimtoa nyuzi. Akasogea kitandani na kuongezea hayo maneno kwa upendo sana. Alikuwa mama mtu mzima, aliyemvumilia sana Kenny. Kwani mara nyingi alishamfukuza tena kwa ukali sana, lakini wakati wote alirudi kumtizama, bila kinyongo.  “Asante.” Kenny alishukuru, na kumfurahisha Naih.

    “Naomba na mimi nikushukuru sana, kwa kutuvumilia. Umekuwa faraja kubwa sana kwa Kenny. Hukumkatia tamaa, hata alipokufukuza. Umekuwa ukizungumza naye na kumfariji kila wakati. Angalau sasa hivi anaondoka akiwa na tumaini. Si ni kweli Kenny?” Kenny akatingisha kichwa kukubaliana na Naih.

“Sasa hii ni zawadi yetu kwako. Angalau ukapambe sebuleni kwako, kila ukiiona umkumbuke Kenny kwenye maombi.” Emma alinunua pambo zuri sana la ukutani, wakampa na kadi ya shukurani aliyokuwa ameweka saini Jay, Emma, Naih na Kenny mwenyewe. Ndani wakaweka na pesa kidogo. Jay na Emma na wao walimpa mkono wa shukurani. “Asante sana kwa kumjenga Kenny. Ni mdogo wangu huyu.” Jay aliongeza. “Asante sana, kwa kuwa na Kenny. Ni pacha wangu, lakini mwenzangu alizaliwa mzungu!” Wote wakacheka. Yule mama mshauri alipokea vile vitu, akashukuru, nakuondoka.

Sehemu ya 5

Hujafa, Hujaumbika.

Ni kweli vijana hao hawakutania. Hawakuhitaji pesa ya wazazi wao hata shilingi. Emma na Jay walilipa garama zote za hospitalini, wakaondoka kuelekea kwenye gari. “Tunaruhusiwa kuja nyumbani kuona mnapoishi?” Mama Ole aliuliza kwa huruma sana. Kenny akanyamaza. “Karibuni. Japo si pakubwa. Ni padogo sana.” Naih akajibu na tabasamu. “Hatujali Naih. Angalau na sisi tujue mnapoishi.” “Basi karibuni.” Ni kweli walitoka hapo bila hofu. Walipatiwa huduma nzuri, Kenny alifundishwa jinsi ya kuishi na ile hali. Naih naye aliuliza maswali yote, akajua ni jinsi gani yakumsaidia Kenny wakiwa nyumba. Aliona jinsi walivyokuwa wakimsaidia. Alitoka pale akiwa kama muuguzi, na utaalamu wote wakumsaidia mtu kama Kenny.

Waliongozana mpaka nyumbani kwa Naih. Walimkuta mama yake Naih alishapika, na kusafisha nyumba vizuri. Tuse naye alikuwepo. Waliwakaribisha wazee hao wenye pesa mjini kwenye kijumba hicho kidogo. Tuse alimkaribisha Kenny kwa upendo na kumwambia ajisikie yupo huru, muda na wakati wowote atakapomuhitaji, amuite tu. Ni kweli alikuwa kijana mcha Mungu. Aliwataka wageni wote watulie ili aombe. Naih alikuwa akicheka moyoni kwani alijua aina ya wageni wake. Sio mama yake wala wazazi wa kina Emma na Kenny tu ambao walikuwa na dini jina, bali hata Kenny mwenyewe na kina Jay hawakuwa wakiombea hata chakula.

Walibaki wamekodoa macho. “Anamaanisha mfunge macho na kuinama ili aombe.” Naih akawaambia, kwani walibaki wamekodoa macho hawajui wanatakiwa kufanya nini. “Aaaah!” Wote wakafunga macho, wakainama. Tuse akaanza kuaomba. Aliomba mpaka wakaanza kutafuta sehemu za kukaa. Alimuombea Kenny na wazazi wake. Akaanza kuombea roho ya upatanishi kati yao kama aliyekuwa akijua kinachoendelea kati ya watoto hao na wazazi wao. Alikemea roho ya kutokusamehe, Naih alikuwa akicheka sana moyoni, mpaka Tuse anamaliza, Naih akafungua macho na kukuta Emma, Jay na Kenny wamemkodolea macho yeye.

Alishindwa kujizuia akaanza kucheka mpaka machozi. “Usifikiri ni sifa Naih!” “Muulizeni Tuse kama mimi nilishakaa na kumsimulia habari zenu. Tuse huwa anaonyeshwa na Mungu akiwa anaomba. Si ndio hivyo Tuse?” Tuse hakuwa ameelewa. “Mimi nauliza aina hii ya uombaji ndio kila siku au ni leo tu!?” Jay akauliza na kuamsha vicheko. Naih alikuwa akicheka mpaka machozi. “Daah! Kenny akitoka hapa anafungua kanisa!” Emma aliongeza nakumfanya hata Kenny mwenyewe acheke.

“Hapana. Mbona nimeomba kidogo tu!” “Haa! Acha masihara wewe Tuse. Umeomba hapa zaidi ya dakika kumi!” Walizidi kucheka wakati Jay akishangaa. “Ndio maana Nai anamtaja taja sana Mungu siku hizi!” Emma aliongeza. “Kwa uombaji huu, lazima uwe unamtaja Mungu.” Jay naye akaongeza. Waliendelea kucheka. Mama Naih aliwakaribisha chakula, Naih akaenda kumchukulia Kenny chakula akamletea. “Kula wakati ni cha moto.” Naih akamsogeza kwenye meza ya chakula. 

Jay Atoa Mazito Na Ya Kuumiza Ya Utotoni

J

ay akaanza wakati anapakua chakula. “Mimi nina swali kwa muombaji wetu aliyekuwa akikemea roho za uchungu na kuto kusamehe.” Wazazi wao walikuwa wamekaa kwenye makochi hayo ya Tuse, ya kawaida sana tu. Kimya. “Karibu kaka.” Tuse alijibu kwa tabasamu kama kawaida yake. “Wewe niite tu Jay.” Wakacheka tena. “Karibu Jay.” “Asante. Swali langu ni hili. Unaweza ukakuta umeletwa hapa duniani na watu ambao ni kama walipewa mzigo waufikishe mahali wakiwa hawataki. Yaani wana mambo yao mengi sana yakufanya, lakini kama unavyomfahamu huyo muheshimiwa huko juu. Akikutuma anakutuma tu, hajali unajisikiaje, anakupa mzigo wake mletee huku duniani. Ndio maana wengine wanajikuta wameleta wafupi, wengine warefu, wengine vilema wengine majambazi, basi vile atakavyo huyo Muheshimwa huko juu mbinguni.” Jay akaendelea.

“Mbaya zaidi, si Mletwaji wala Mletaji anayechagua aletwe na nani au alete nini, ni vile atakavyo Muheshimiwa huko juu. Sasa ukakuta hao watu waliotumika kama njia ya kukuleta hapa duniani ni makatili kuliko hata shetani mwenyewe. Hawajakulea, walikuwa wakikutesa, wakakusababishia maisha ya kuwa unalawitiwa. Namaanisha zaidi ya mara moja, halafu huyo mtu aliyekuwa akikulawiti ni mfanyakazi wao waliyekuwa wakimpenda na kumuheshimu kuliko wewe waliyekuleta hapa duniani.”

“Akisema yeye kitu ndio anasikilizwa, na wakati mwingine anasemelea maneno ya uongo ili uchapwe, kwa ufupi, hamna pakusemelea, inabidi kunyamaza tu na kuendelea kumpa huduma kila siku usiku akitaka. Namaanisha unamuachia awe anakulawiti kila anapojisikia na mengine mengi tu.” Chumba kizima kilitulia gafla kama hapakuwa na mtu hapo ndani.

“Sasa majitu kama hayo, unayafanyaje? Maana hata ufanye nini yapo tu kwenye maisha yako na wameacha madonda ambayo hayatibiki hata kwa madaktari.” Jay alikaa chini na chakula chake. Akatulia kama anayefikiria. “Unajua wakati naondoka hapa nchini, nilihakikisha nabadili majina yangu yote. Sikutaka kutoka hapa nchini na majina yao. Nikaenda mahakamani kuapa, nikajiita jina jingine kabisa, kuhakikisha nikivuka hiyo bahari ya hindi, sivuki nao. Lakini unafikiri imesaidia?” Jay aliuliza kwa uchungu.

“Kwa nini haikusaidia?” Tuse akauliza na yeye akiwa ametulia, Jay akacheka. “Nilipofika tu huko nikaamua kurudi shule. Nikahangaika kufanya kazi ili kujisomesha kama ‘International student’. Yaani mwanafunzi asiyekuwa raia wa hapo. Sasa kwa mwanafunzi mgeni kusoma huko ugaibuni si mchezo kaka! Ada yake ni kubwa sana. Nikapambana mwaka wa kwanza. Nafanya kazi huku najilipia ada. Nilipofika mwaka wa pili, nikampata msichana mzuri sana, aliyenipenda kwa dhati. Japokuwa nilikuwa na hofu sana ya mapenzi kutokana na historia ya maisha yangu, lakini ilikuwa ngumu kukwepa ule upendo wa yule dada. Ndiye msichana wa kwanza aliyenionyesha upendo au mapenzi ya dhati hapa duniani bila ya kunijua mimi ni nani.”

“Nikimaanisha bila kujua nilizaliwa na wazazi wenye jina kubwa hapa mjini. Yaani alinipenda mimi kama Jay. Alionyesha kuwa unaweza kumpenda mtu vile alivyo, sio kwa kile atakachokupa. Turudi kwenye tatizo lilipo.” Jay akaweka kijiko cha chakula mdomoni. Akatafuna na kumeza.

“Sasa kila yule dada alipokuwa akitaka kufanya mapenzi na mimi, nilikuwa nikimkwepa, nilikuwa nikifikiria yale maumivu niliyokuwa nikisababishiwa mimi wakati nalawatiwa. Nikawa najua maumivu yaleyale ndiyo nitakayo msababishia yule dada! Nilishindwa kabisa, hata kumvua nguo. Tukaendelea na mahusiano, yeye akionyesha kuwa mvumilivu, na mimi nikaanza kumkwepa bila mafanikio. Mzigo wa ada ukawa mkubwa. Nikaanza kulemewa. Nikataka kuahirisha shule, lakini yule dada aliendelea kunitia moyo nijikaze, yeye atanisaidia baadhi ya pesa.”

“Hapo nilikuwa nimeshamwambia sina wazazi, ila ninao wadogo zangu wawili tu. Akanikubali. Hapo na yeye alikuwa mwanafunzi kama mimi, lakini yeye ni raia wa hapo nchini, kwa hiyo hata ada yake ilikuwa ndogo. Nilipomwambia sababu zakunifanya nitake kusimamisha masomo, akanishauri tuone ili na mimi niwe raia, ada yangu ipungue, nimalize shule.” Jay akacheka.

“Nikampigia simu Emma na Kenny, nikawaambia mkasa mzima wa yule binti. Wakanishauri kwa tabia zake yule binti, hakuna cha kupoteza nikumuoa tu. Kwanza atanipa uraia kitu ambacho kitanirahisishia maisha ya shule na kunifanya nipate kazi kwa haraka. Kuthibitisha baraka zao katika hilo, Kenny na Emma wakaja mpaka huko ugaibuni, kuhudhuria hiyo harusi. Tukafunga ndoa yetu mahakamani kwa kuwa sisi tulizaliwa na wanyama, hawana dini. Kwa hiyo hata yule msichana nilimwambia sisi hatuna dini. Sasa kuanza kunifikisha kanisani siku ya harusi, sipo tayari. Sisi tumelelewa kuwa haki zote zinapatikana mahakamani. Basi bwana. Unanisikiliza lakini Tuse?” Jay akauliza huku akiweka chakula mdomoni. “Nakusikiliza.” Tuse akajibu.

“Bwana Atu anajua kupika! Chakula kitamu sana. Asante Mama Naih.” Jay akamshukuru Atu na kuendelea. “Tuse!” Jay akaita. “Nipo kaka, nakusikiliza.” “Bwana shuguli ikawa baada ya harusi si unajua ndio inabidi mfanye mapenzi? Au nyinyi watu wa Mungu huwa hamfanyi? Maana sisi tulikuwa tukiishi na watu, hilo tendo ndio ilikuwa chakula au pumzi kwao. Kama kuku! Wanafanya asubuhi jua linachomoza mpaka usiku. Na kila kiumbe kilichopo mbele yao, ilimradi awe ni binadamu, basi tendo hilo litafanywa. Imetuathiri kiasi ya kwamba mdogo wangu huyu Emma, akalichukia kabisa hilo tendo, kwa kumkinahi. Mimi nilikuwa naogopa hata kuwaza kwa vile nilivyokuwa nikibakwa, na yale maumivu niliyokuwa nikiyapata wakati nabakwa.” Jay akaendelea.

“Jamaa alikuwa akiniambia nitazoea, lakini sikuwahi kuzoea bwana! Mpaka akaja kugundua naanza kunuka kwa kuoza, ndio akaogopa, akahisi atakamatwa. Ndipo akaanza kunitibu yeye mwenyewe, huku ananionya nisiseme. Na hata nikiulizwa nisimtaje. Akaniambia nikisema tu, anamuanza na mdogo wangu Emma. Niliogopa yale maumivu yasimpate dogo. Maana mimi mwenyewe niliyekuwa mkubwa kidogo, nilikuwa nikiteseka vile. Sikuwahi kuzoea. Sasa nikamfikiria mdogo wangu! Mbona nilimpigia magoti nakumsihi sana. Nikamwambia anifanye mimi chochote lakini asimguse mdogo wangu.”

“Basi kwa kuwa alijua hakuna anayetujali wala kutusikiliza, alinifanya atakavyo. Wakati mwingine unakuwa umelala anakuja kukuamsha. Ukijidai umelala humsikii, anakwambia anaenda kwa Emma. Basi hapo unaamka kama mshale. Unampa kwa haraka na ukumbuke na jana yake alikufanyia, kwa hiyo bado una maumivu makali kweli! Akipumzika jamaa ni siku moja. Na akikuanza huo usiku, utaugulia maumivu mpaka asubuhi ndio unapitiwa na usingizi. Lakini namshukuru Mungu kwa kuwa nilipo pona, hakuendelea.” Kila mtu alikuwa akitetemeka mle ndani. Ni Jay tu ndiye aliyeweza kula. Emma alisimama na kutoka nje.

“Kwa hiyo ile hofu niliyokuwa nayo na yale maumivu, tena alikuwa wakati ananiingilia, ananipaka mafuta mengi na kuniambia ning’ate taulo. Bwana usiombe hayo maumivi yake. Akimaliza hapo, taulo limelowa kwa machozi na jasho, halafu anakuruhusu urudi chumbani kwako. Hapo uombe Mungu usikutwe na hawa walevi wawili, unapita koridoni au unapandisha ngazi kurudi chumbani kwako! Tuse? Utajuta kuzaliwa. Huyo jamaa hapo.” Jay akamuonyeshea baba yake.

“Bwana, si anakukuta unachechemea koridoni, unatafuta ngazi ili urudi chumbani kwako, hapo jamaa kule kashakubaka mpaka karidhika.  Na yeye huyu anachomoa mkanda wake. Hapo amelewa, ndio na yeye anatoka kwenye starehe zake. Bwana atakutandika, mpaka unasahau jina lako. Uzuri wake ilikuwa akishakutandika hivyo, anakushika mkono mmoja. Anakuvuta kama mzoga. Anakuburuza huku anakupandisha ngazi. Anaenda kukutupa kitandani. Hapo inakuwa angalau umesaidiwa kufika chumbani. Mambo ya kuumia mbavu wakati anakuburuza kukupandisha ngazi, hayo utajua mwenyewe baadaye. Bora amekurusha kitandani, umefika.”

“Sasa unaanza kuuguza maumivu ya kila mahali. Yakupigwa na mwenye nyumba na kuingiliwa huko nyuma. Tuse! Usiombe ndugu yangu. Majumba haya makubwa yanaficha mambo! Sio utani.” “Ulikuwa ukimwambia mama?” Tuse akauliza. “Umpate wapi!? Muda wa kukaa na wewe akusikilize, anautoa wapi!?” Jay akamuuliza Tuse kwa kejeli.

“Kwanza mkewe, alikuwa anavaa kucha ndefu kuanzia jumatatu mpaka jumatatu. Kiatu chake urefu wa miguu yake. Kila siku yupo kwenye ndege kwenda nchi fulani. Na akirudi hapo anaratiba zake, huwezi kuziingilia. Ataenda kunywa na rafiki huyu, anatoka na huyu, wanaenda kwa chakula cha usiku huku na kule. Mumewe analala huku, na yeye anawake kule. Mume anarudi muda wake, na mke muda wake. Hawana muda na ‘kima’ wa mtu!” “Na wote wakirudi wanakuwa wamelewa na wanafuraha zao. Huwezi kuwaingilia.” Emma aliingia akaongezea hivyo.

“Na usifikiri hivyo anavyosema Emma ni weekend tu? Hapana. Ndio ratiba yao ya kila siku, mamilionea hawa. Ukiwaona wapo hapo nyumbani na kusisitiziwa muoge na kuvaa vizuri, mjue mnaenda kuonyeshwa mahali. Yaani mnapelekwa kuonyeshwa mahali kama moja ya bidhaa zao wanazo miliki, sio vinginevyo. Basi turudi kwenye stori yangu. Hao habari zao, usitake kuzijua, ni kichefuchefu kitupu, utatapika na kushindwa hata kula hicho chakula.” Jay  akaweka kijiko kingine mdomoni.

“Sasa kutokana na hayo yote, na jinsi yule msichana alivyokuwa mwema kwangu, hakuna jinsi ungeniambia nimuingilie yule dada, nikaona ni tendo sahihi kwa kiumbe kama yule. Sasa baada ya kufunga ndoa, si watu wanaendaga kwenye fungate? Mimi sina raha! Emma na Kenny, pamoja na ndugu zake yule binti wanafurahia, mimi nipo kama msibani. Nawaza tu. Picha ya tendo la ndoa niliyonayo ni kule nilikokuwa nikiingiliwa kikatili. Tukaaga watu tunakwenda kwenye fungate. Tumefika huko binti wa watu si anataka haki yake? Kwani niliweza?” Jay aliuliza kwa cheko.

“Nilihangaika kama mwehu! Natetemeka na jasho linanitoka kama jinga! Nilijuta kuzaliwa mrefu. Hebu niangalie hivi nilivyo, halafu mke mzuri unaye, kalala anakutaka, halafu wewe unatokwa kamasi! Utatamani uzaliwe mbilikimo uingie chini ya uvungu! Tumeenda kwa washauri, nimeshindwa kuongea kama nilikuwa na bakwa nyumbani kwetu, tena nabwakwa na mtu mwenye undugu na mwanamke aliyeshiriki kunileta hapa duniani. Tena jamaa ndiye alikuwa msimamizi wa wafanyakazi wote pale ndani. Alikuwa akilipwa na kusifiwa kama raisi wa nchi! Kwamba ameweza kumudu kazi za mle ndani. Anasimamia usimamizi wa sisi kupelekwa shule, magari yapo vizuri, wasichana wa kazi, ambao na wenyewe walikuwa wakilala naye. Pia alikuwa akisifiwa anawaongoza vizuri.” Jay akaguna.

“Uzuri wake alikuwa akijua masaa ya kufanya mambo yake. Baba mwenye nyumba akiwalala wale wasichana wa kazi usiku, yeye zamu yake ni asubuhi kabla hawajaanza kazi. Akihudumiwa vizuri na wale wafanyakazi, basi ujue usiku huo na mimi nitalala, siguswi. Sasa ole wake mwenye nyumba akabe sana usiku, yeye asipate asubuhi! Basi hamu zote zilikuwa zinaishia kwangu. Atanifanya kwa hasira zote, huku akilalamika baba mwenye nyumba analala na wanawake zake. Basi mimi nilikuwa nikisuguliwa mpaka nakoma. Yaani leo ndio kwa mara ya kwanza nimeweza kusimulia. Sikuwahi kuthubutu kusema. Sasa hebu niambie Tuse, watu kama hao, waliokuharibia maisha yako hivyo, unawafanyaje?” Watu wote walinyamaza, akasikika mama yake akilia.

Tuse alitulia kwa muda. “Eti Tuse. Au na wewe hujui?” Jay akauliza kama jambo la kawaida tu. “Tena Naih alikosa harusi yangu. Alifukuzwa. Tena kwa kusingiziwa. Bwana tulibahatika kuzungukwa na watu waajabu! Yaani mimi huwa sielewi huwa wanajisikiaje huko rohoni mwao. Au sijui hata kama wanazo hizo roho! Daah! Hebu niambie Tuse? Kama huna jibu basi mimi ngoja nimalizie chakula changu. Niondoke, nikaanze kujiandaa na safari. Ndege yangu inaondoka usiku. Maadamu Kenny anaendelea vizuri, na Naih yupo, sina hofu yakuondoka.” Jay akainamia sahani yake akaendelea kula.

Tuse alisikika akivuta pumzi kwa nguvu, kisha akaanza. “Ninaamini kutoka kwenye bibilia. Na bibilia inasema hivi, kisasi ni cha Bwana. Yaani Mungu. Halafu naamini kwa Mungu anayeumba upya, Jay. Sijaona..” “Ngoja kwanza Tuse. Unamaanisha kuniumba na nguvu za kiume mpya au? Maana huko niliko, ndiko kunasifika kwa madaktari wazuri. Wamenitibu mpaka na mimi nimechoka.” “Yale yanayoshindikana kwa wanadamu, kwa Mungu yanawezekana.” “Okay. Unataka nikuvulie suruali uanze maombi au nafanyaje?” Tuse alijua Jay anaongea kwa hasira.

“Kutokana na maelezo yako tokea mwanzo inawezekana tatizo lako linaanzia kwenye akili zako Jay. Inawezekana unanguvu za kiume, lakini umejawa woga, hasira, uchungu na umeshindwa kusamehe.” “Unaposema nimeshindwa kusamehe, unamaanisha kujisamehe mimi kwa kumtapeli mke wangu? Kukubali tuone, na kushindwa kuwa mume kwake? Au unamaanisha nini? Maana sijaona mtu anayehitaji kusamehewa hapa. Kama hufahamu, yule jamaa aliyekuwa akinibaka, sasa hivi ameoa. Ana mke na watoto. Kwa uaminifu, na ufanyaji kazi bora pale kwenye jumba la hawa watu wawili, kama shukurani yao kwake, wamemfungulia biashara. Tunavyo zungumza sasa hivi, yule jamaa maisha yake yanaendelea vizuri sana. Hana hata wazo la pili yakuwa aliishi maisha mabaya hapo zamani. Halafu hawa wawili hapo, wapo hapa kwa ajili yakutimiza wajibu kwa hawa rafiki zao.” Jay alikuwa akiwaonyeshea vidole.

“Yaani hawa, na wale ni marafiki sana. Wao huwa wanapatana sana. Wapo hapa wote wanne, si kwa kuwa wanauchungu na linalompata hata mmoja wetu hapa!? Hapana. Ni kwa kuwa wanalipiziana fadhila, ili baadaye hawa wakiishiwa pesa, hawa wengine waweze kuwakopesha. Halafu ni tukio lililojulikana kila mahali, hawanabudi kuwepo hapa. Yaani hawawezi kukwepa, au kuwaajiri watu kuwepo hapa. Kwa kuwa matajiri wenzao wote wanajua kuwa kuna ajali, sasa wakionekanika mtaani wanazurula, watasemaje? Lakini kwa mida ya usiku sio mbaya, wanaendelea na maisha yao kama kawaida. Walevi wanakwenda baa, wenye nyumba ndogo zao wanaenda kama kawaida. Ila asubuhi na mchana, magazeti si huwa yanaandika? Sasa lazima wajionyeshe kama wana uchungu vile, lakini hamna kitu. Wapo hapa kwa maslahi yao binafsi. Ingekuwa ni yale magonjwa madogo madogo ambayo watu hawajui, wangewatuma wafanyakazi wao.” Jay akaendelea.

“Sisi wote watatu, na umri huu, hatujawahi kuuguzwa na hata mmoja wao hao. Walikuwa wakituma wafanyakazi wao watupeleke hospitalini, na kuturudisha nyumbani. Hawana muda na mtu isipokuwa wao wanne. Jamaa wanapata hao, hujawahi kuona. Wamekuwa wakiishi hivyo maisha yao yote. Ndio maana hawajawahi kuishiwa. Ni matajiri wakubwa sana hapa nchini, siri yao kubwa ni umoja walionao wao wanne tu. Hata ufanyaje, hawawezi kugombana. Wanapesa hao, hata sasa hivi hapo walipokaa hapo, pesa inaingia. Nchi nzima wanaimba maisha magumu, au uchumi ukiyumba, hamna pesa Tanzania, lakini sio kwao hao. Kwao hao, ipo neema nono. Usiwaone wamekaa kwenye hayo makochi yako hapo. Wanahesabu dakika, waondoke, wakaendelee na maisha yao.”

“Ukisikia Mzee wa magari mekundi, basi ni yule pale. Wadada wanasema anahonga magari mekundu. Sijui kama unanielewa? Harufu ya manukato unayoyasikia hapa ndani, ni pafyumu ya bei inayoweza kulipa kodi ya hii nyumba yako wewe na Naih kwa mwaka. Si mwezi. Sijui kama unanielewa sawasawa Tuse!? Hakuna mwenye shida hapo. Sio ya msamaha wala ya pesa. Wakamilifu hao, kuliko Mungu. Hawajawahi kukosea na maisha yao yanaendelea vilevile kama tulivyokuwa tukiishi nao. Sasa sijui unawasamehe kwa lipi!” Jay alikuwa akiongea taratibu na kumfanya hata Tuse mwenyewe kubaki na kigugumizi.

“Mama Nai! Asante kwa chakula. Ngoja na mimi nirudi kwenye maisha yangu. Kenny, tutawasiliana mdogo wangu. Ngoja nizunguke mtaani kidogo, ndipo nikajiandae na safari.” “Asante sana kwa kuja Jay.” Kenny akashukuru. “Pamoja sana. Kiasi cha kunyanyua simu tu, utanisikia nagonga mlangoni. Kama mshale.” Jay akasimama. “Sasa Nai, ‘mimi wa Kenny’ ?” Naih akacheka kinyonge. “Sisi tutakuwepo hapa mpaka Kenny amalize mazoezi ya kwanza, ndio tutahamia Dodoma. Asante kwa kutusaidia manunuzi ya nyumba na lile shamba. Mavuno ya kwanza ya zabibu tutakuita tuje tusherehekee.” “Mnamsikia Nai, jamani? Sasa nisikute zabibu zangu.” Naih akacheka tena. “Lazima utazikuta, hata kama zimeoza.” “Hayo ndio maneno.” Jay akarudisha sahani aliyokuwa akiitumia jikoni.

“Lakini Jay!” Tuse akaita. “Nina jambo la kuzungumza.” “Unataka kuzungumza na mimi au na hawa waheshimiwa wote wakiwepo? Maana naona kama muda wa maonyesho umeisha jamani. Sioni mtangazaji hapa wala mwandishi wa habari. Nashauri mkaendelee na biashara ya kujenga nchi, ili na Kenny naye akapumzike.” Wote wakatulia.

Jay akacheka. “Au na hapa napo mnataka kuleta ubabe!? Maana hapa ni nyumbani kwa Nai. Na ninamshukuru Mungu hamjawekeza hata shilingi yenu hapa. Uzuri mlimfukuza, akahangaika mwenyewe, akapapata hapa. Hamna hata mnachodai. Maana nasikia hata ada mliyomsomeshea mlikuwa mkimkata mama yake kwenye mshahara. Kwa hiyo muda wa kuona wagonjwa umekwisha, mlango ule pale, mtupishe. Tuse anataka kuzungumza na mimi.” Jay akawatizama kwa zamu. Wakasimama, na kutoka mmoja baada ya mwingine.

Tuse alibaki kimya. “Wala usiwahurumie hao Tuse. Hapo wananishukuru kweli! Walikuwa hawajui wanatokaje hapa. Nani aanze kuaga, nani aseme nini. Tena zaidi kuona wanaondoka bila jukumu! Hapo ni muujiza. Hawana hata haja yakumtafutia Kenny mfanyakazi wakumuuguza au kumpeleka hospitalini! Wanatamani kushukuru kwa sauti lakini hawawezi. Waache wakaendelee kutafuta pesa na kufanya starehe, tutakutana nao tena mwingine akipata tukio kubwa, au mmoja wetu akifa, ndio utawaona tena lakini sio vinginevyo.” Hayo Jay anayazungumza huku wazazi hao wakitoka hapo mlangoni. Alihakikisha hata waliotangulia wanasikia. Walipotoka wote, Jay akafunga mlango nyuma yao.

Tuse hakuamini. “Umewafukuza!”“Wananipandisha tu hasira. Acha waondoke.” Jay akarudi kukaa kama hana haraka tena. “Sasa Tuse? Tunafunga kwa maombi?” Jay aliuliza huku akicheka. “Nashauri muwasemehe wazazi wenu.” “Wewe Tuse vipi? Mbona unakuwa  kama hajamuelewa Jay! Hakuna anayehitaji kusamehewa pale. Na wala usifikiri wameondoka hapa kwa majonzi! Yaani tumewapunguzia mzigo.” “Mama yenu alikuwa akilia.” Jay akacheka, Tuse asielewe.

“Msanii yule! Hujamuona akiwa analia mbele ya magazeti au kwa wageni wake. Unaweza na wewe ukalia. Pale alikuwa anafanya maonyesho. Hajawahi kumuhurumia hata mmoja wetu maishani. Muone vilevile. Hapo anaelekea kufanyiwa masaji ya kukaa kwenye hilo kochi lako dogo na kutengeneza kucha, atoke usiku kwenda kwenye starehe zake. Yaani pale kazi ya ugonjwa wa Kenny, ishaisha. Magazeti yashaandika, wamepigwa picha kuwa mtoto wa aliyekuwa naibu waziri wa fedha na Mzee Olendekai amepata ajali. Wale wengine wawili wanaojulikana kama ndio marafiki zao wakaribu, wametoa salamu zao za pole huko kwenye vyombo vya habari. Wakahurumiwa, wamemaliza. Yaani huo ukurasa washafunga, maisha yao yanaendelea kama kawaida. Wewe sema jambo jingine.” “Namaanisha nyinyi wenyewe muachilie mambo moyoni. Jay, unatakiwa kusamehe mambo ya nyuma ili uweze kuendelea na mkeo vizuri.” Tuse akajaribu kutoa ushauri.

“Haa! Kumbe nilikuwa sijakumalizia stori?” Jay akakaa sawa. “Baada ya muda na mke wangu akinivumilia na kunifanyia hili na lile, mbona nilimrudisha kwenye fungate! Tunavyozungumza hapa ni mjamzito. Ngoja nikuonyeshe picha zake.” Jay akatoa simu yake, na kuanza kuonyesha picha zake na mkewe. “Mbona mnaonekana mna furaha sana!?” Tuse aliongea kwa kushangaa.

 “Sana. Nani amekwambia nina matatizo!? Yaani hapa nasubiriwa kwa hamu na mke wangu, na mwanangu huko tumboni. Nitampa mapenzi yote mwanangu. Yale niliyoyakosa mimi, yeye yanamsubiri na zaidi. Nimepata mke mwaminifu na ananipenda sana. Sina hata shida. Nikimuweka kitandani, mpaka mwenyewe anajiita jina la utoto, kwa shuguli ninayompa kwa kujinafasi. Simchezo kaka. Sema hapa mbele zao wale, nilikuwa naua undugu kabisa. Sitaki hata mke wangu ajue kama hawa watu wapo hapa duniani na wala watoto wangu hawatakaa wakawafahamu. Ndugu wanaofahamika kule ukweni ni hawa wawili tu. Emma na Kenny, ila wanajua wazazi wangu wamekufa.” Jay aliongea bila shida.

“Sio vizuri Jay.” Tuse aliongea, nakumfanya Jay ambadilikie. “Ulishawahi kulawitiwa?” Kimya. “Eti Tuse? Ulishawahi kulawitiwa wewe mpaka ukaoza matako?” “Hapana, ila nilitaka kukushauri..” “Ngoja nikakuitie wahuni hapo nje wakubake kwanza, wakishakufungia hapo chumbani kwako kwa muda wa siiku 7 tu, wakikubaka mpaka unuke, nitarudi kukutibu. Mimi mwenyewe nitakuhudumia mpaka upone. Halafu ukipona, nitakuomba tukae chini tuzungumze, ili unishauri tena. Sawa?” Tuse akanyamaza.

Jay akatoa pesa mfukoni akaziweka mezani. “Pesa hii hapa yakuwalipa jamaa. Tena tunaweza kuanza na mmoja tu. Nitawalisha wewe na huyo jamaa. Siku saba tu. Wala si nyingi. Saba tu, jamaa anafaidi kila siku. Upo tayari?” “Basi bwana.” Tuse alishaingiwa na hofu.

Jay akasimama. “Tuse, asante sana kwa kutukaribisha nyumbani kwako na kumkubalia Kenny kuishi hapa. Hii sura utaiona sana hapa, labda Nai na Kenny wahame.” Jay alimgeukia Emma. “Nipo tayari.” “Kenny! Wewe pumzika. Naih tutawasiliana. Nitakuwa nakuja kuwapeleka hospitalini kwa mazoezi.” “Asante Emma.” Naih akasimama. Akamkumbatia Jay. “Uwe na safari njema. Nisalimie mkeo.” “Zimefika. Nitawapigia kabla sijaondoka na mara nitakapofika. Tatizo lolote lile, tafadhali nijulishe.” “Nitafanya hivyo Jay.” Jay na Emma wakaondoka. Atu alikuwa kama amemwagiwa maji.

Kenny!

 “Unataka kwenda kupumzika?” Naih akamuuliza Kenny, aliyekuwa amepotelea mawazoni. Akabaki akimtizama. “Twende. Nitakuwa na wewe hapo kitandani.” Naih alimuongelesha kwa upole. Akamsukuma mpaka chumbani, akamsaidia kumuweka kitandani, akamfunika, na yeye akapanda akajilaza pembeni yake. “Mbona huna raha tena?” Kenny akabaki akimtizama. “Kenny! Naomba uwe unazungumza na mimi tafadhali. Chochote kile.” “Najutia maisha yangu Naih. Nimechezea maisha yangu kweli! Unajua Jay na Emma, waliteseka kuliko mimi? Mimi sikuteseka sana, sema nimekuwa bila wazazi wangu kujihusisha na maisha yangu. Walijitahidi kunipa kila kitu, labda ndio maana nilibweteka.” Kenny akalalamika.

“Waangalie wenzangu. Wamejijenga. Ninavyokwambia hivi, Jay alimaliza chuo kwenye mambo yake ya kompyuta, analipwa vizuri sana. Ameoa na anakaribia kuwa na mtoto. Analipia nyumba nzuri ambayo anataka iwe yake na familia yake. Yaani anaongelea mambo ya mpaka vitukuu! Amekusudia kuanzisha ukoo wake. Haya, muangalie Emma. Mwenzangu yupo mbali kweli kimaendele. Huwezi kuwalinganisha na mimi. Tena wao ndio wangekuwa na sababu yakuwa pabaya, lakini ona walivyopambana na maisha! Mimi nilikuwa nahangaika tu. Sina mbele wala nyuma!” Kenny aliongea kwa majuto.

 “Lakini hujachelewa Kenny. Unao muda wakurekebisha kila kitu. Jay na Emma, wamekusaidia kuweka mambo sawa huko Dodoma. Emma ameahidi kukusaidia kusimamia huo ujenzi mpaka aone hiyo nyumba imekamilika. Ameanza kufuatilia ramani ya hiyo nyumba kutoka kwa huyo rafiki yenu. Ameahidi kuikamilisha mapema iwezekanavyo. Emma anasema tutaanza huo ujenzi bila kupumzika. Na Jay amesema yupo tayari kutukopesha pesa, ilimradi huo ujenzi usisimame. Baada ya muda mfupi sana utakuwa na wewe na biashara zako. Naomba ujipe muda. Na swala la kuoa na kuwa na watoto, ni jambo rahisi sana.” “Sio rahisi kama unavyofikiria Naih.”

“Ni rahisi sana Kenny. Jipe muda na fungua moyo wako, utapata mapenzi ya kweli. Tena sasa hivi ukipata mwanamke ndio utakuwa unajua umepata mwanamke anayekupenda kwa dhati. Wewe kama Kenny. Naomba usijilaumu kwa maisha ya nyuma. Tutapoteza sana muda hapo. Nahitaji akili yako ili inisaidie kuweka mipango ya baadaye. Sawa Kenny?” Kenny akatingisha kichwa kukubali.

 “Asante. Naomba tuendelee na mipango yetu kama tulivyokubaliana. Usikubali kuanza kufikiria mambo ya nyuma. Nakupenda Kenny, na nimefurahia kwa kuwa umeamua kubadili maisha yako.” “Kwa hiyo hukuwa ukifurahia?” Kenny aliuliza, lakini Naih akabaki kimya. “Sasa kwa nini hukuwa ukinikataza, wakati nilikuwa nikikwambia kila kitu?” “Kumbuka ulikuwa ukinitaarifu, Kenny. Hukuwa ukiomba ushauri. Na mimi nakufahamu wewe kama mtu mwenye akili sana. Unauwezo mkubwa sana wakufikiria. Ningeanzia wapi kukukataza? Nakupa sababu gani wakati nakuona mwenzangu unafanikiwa kuliko mimi!?”

“Darasani ulikuwa ukifanya vizuri sana kuliko mimi. Haya, wazazi wako, hasa baba yako ambaye naye anatabia kama hizo, ona alivyofanikiwa kwenye maisha! Hajamkimbia mama yako wala wewe, kama mimi baba yangu alivyotufanyia. Sikuwa na mfano au sababu nzuri ya kukosoa kile ulichokuwa ukifanya. Mimi ambaye nilikuwa sifanyi hayo mambo ndio nilikuwa na maisha ya ajabu kuliko wewe! Sasa ulitaka niseme nini?” Kenny aliumia sana, akanyamaza.

“Naomba ulale, Kenny. Nitarudi baada ya muda mfupi. Ngoja nikamsaidie mama kusafisha na kuweka vyakula kwenye friji ili kumpunguzia kazi. Bado mgongo unamuuma.” “Nakusubiri Naih. Siwezi kulala kama wewe haupo.” Naih akamuhurumia. “Bado unaogopa?” Naih akamuuliza taratibu. “Naogopa sana. Najiambia unaweza ukaondoka, halafu usirudi nikabaki peke yangu. Nitafanyaje?” “Basi nakuwashia tv, uangalie wakati mimi nasafisha. Nitarudi.” Naih akambusu shavuni, akawasha tv, akatoka.

Akamsaidia mama yake kusafisha, akampangia kwenye kapu vyombo vyake vyote alivyokuwa amekuja navyo, akampa na pesa. “Asante sana mama yangu. Nashukuru kwa kunisaidia kipindi chote hichi wakati tupo hospitalini. Najua peke yangu nisingeweza.” “Wala usijali. Naona friji imejaa. Ikipungua tu, uniambie nikuletee chakula kingine. Nataka utulize mawazo kwa Kenny ili apone kabisa. Namjua alivyo muoga huyo.” Naih akacheka, akamnong’oneza mama yake. “Hapo yupo macho ananisubiri!” “Namjua Kenny. Mbona utaoga mlango wazi!” Wote wakacheka.

“Nai! Naomba maji ya kunywa.” Walimsikia Kenny akiita tokea chumbani. “Nenda.” Mama yake akanong’ona. “Wala hana shida ya maji. Hapo amesikia tunacheka, anaona nimemsahau!” Naih akanong’ona na yeye. “Naleta Kenny. Namalizia kuagana na mama.” Naih alipaza sauti. “Acha mimi niondoke. Tutawasiliana.” Atu akaaga, na kutoka.

Naih akarudi chumbani. “Macho yamekuwa mekundu kwa usingizi! Naomba ulale.” “Njoo basi hapa kitandani.” “Nataka kuoga kwanza Kenny. Lala nitakuja kulala hapo pembeni yako.” “Basi nakusubiri.” Naih akajua kazi ndio imeanza. Ilikuwa lazima aoge kwanza, kutoa jasho. Aliingia bafuni kuoga, alitoka na kumkuta Kenny akisinzia. Akavaa kwa haraka huku Kenny akimtizima. Akapanda kitandani. “Naomba hata uniguse Naih. Labda nitalala vizuri.” Naih alimjua Kenny. Muoga, na anapenda kupendwa. Alijivuta mpaka karibu yake, akambusu shavuni, akajilaza pembeni yake, akamvuta mkono. Aliubusu na kupitisha vidole vyake katikati ya vidole vya Kenny. Kenny akapitiwa na usingizi. Lakini usiku huo ulikuwa mgumu sana kwao. Kumbukumbu za ajali zilikuwa zikimjia kila alipokuwa akilala. 

Kisasi.

W

azazi wa Jay na Emma walitoka pale kila mmoja na njia yake. Baba yake Jay, mzee Lobulu alizunguka, hata ofisini akashindwa kutuliza mawazo. Akili ilikuwa imevurugika, kila alipodhani kungemsadia kupoteza mawazo siku ile ikashindikana. Mapema sana isivyo kawaida yake akarudi nyumbani. Bila salamu kwa yoyote akapitiliza moja kwa moja mpaka chumbani. Alimkuta mkewe bado akilia chumbani kwao. Hakujua alirudi hapo mida gapi na amelia kwa muda gani! Umri nao ulishakuwa umeenda. Siku hiyo Jay akawafanya watulie na kujifikiria. Wakajigundua hata utuuzima umeshawaingia vyakutosha.

Kitendo cha kuyasikia maovu yao kutoka kwa watoto wao! Wakiyasema kwa machungu vile! Kujua ukatili waliowatendea watoto hao wawili na wao kusimulia mbele ya watu bila kificho tena wakisikika bado wamejaa hasira na uchungu! Wakajua kwa kina ukatili waliokuwa wakiwafanyia watoto wao na wao wakishiriki pia bila kujijua! Zaidi Jay! Mbaya zaidi aliyemtenda kijana wake ni ndugu yake yeye mwenyewe mama Lobulu!

Tena na wao wakiwepo ndani ya nyumba hiyohiyo, wakishindana na mumewe kufanya starehe kama waliochanganyikiwa! Na hata kama mama huyo mwenye jukumu kubwa la malezi ya wanae, alipokuwa akisafiri, hakuwa akichukua muda mrefu kurudi. Alikuwepo hapohapo jijini muda mwingi tu ila starehe za mida ya jioni na siku za weekend, pamoja na biashara zake za kutwa, ndio zilichukua ratiba yake kubwa ya maisha yake kwa muda mrefu. Kila yule mama alipojiuliza kwa nini! Amenufaika kwa lipi! Alizidi kuumia kila alipotafakari, kujiuliza na kukosa jibu. Gafla kila kitu kikakosa maana.

Siku hiyo ndio alikuwa amepoteza rasmi watoto wawili kwa mpigo. Angalau vile alivyojua Jay ameamua kuhama tu nchi. Na Emma ameamua kujishugulisha kivyake. Basi mama huyo akaendelea na maisha yake kama kawaida hata asiweze kupata muda wakutaka kujua hao watoto wanaendeleaje kibinafsi huko walipo. Wazazi hao wakaendelea na maisha yao mjini kama kawaida wasijue kama watoto wao walikuwa wakipambana kujitenga nao. Wazazi hao bila kujali, wakabakiwa na taarifa za jumla tu kila wanapoulizwa na watu wakijivuna kuwa vijana wao wameshakuwa na wameshaondoka nyumbani. Emma amejifungulia kampuni yake. Na Jay naye ameamua kuendeleza maisha nje ya nchi. Hayo yakawa majibu ya wazazi hao. Na wala haikuwasumbua kabisa mpaka siku hiyo walipoweza kujua kilichopo ndani ya mioyo ya vijana wao. Ikawa aibu na uchungu wa kupindukia. Wameweza kuongoza makampuni na watu waliowaajiri lakini wameshindwa kusaidia watoto wawili tu ambao Mungu aliowapa! Mama Jay akazidi kulia akijilaumu. Anarudije kwa Jay au Emma aliyeambiwa wakati mtoto, alimsukuma kikatili mpaka kujigonga akiwa anamlilia amsaidie usiku aliokuwa akijiandaa kwenda kwenye starehe zake?

Emma aliondoka nyumbani kwao muda mrefu tu. Hakuna kati yao hao wazazi aliyejali wala kujishugulisha na aliko na anachofanya kwa hakika. Ila wote wawili walimwambia Emma, akishindwa na maisha huko, arudi nyumbani. Hivyo tu. Hakuna aliyetaka kujua amefanya nini na kama wanaweza kusadia asishindwe! Alipata majibu mepesi na kumuacha kama mtu baki. Hilo lilimuuma sana Emma na kumwambia Jay kuwa hata kipindi hicho alichojaribu kuwaambia wazazi wake kuwa alikuwa akijenga, amemaliza na anahamia kwake, hakuna kati ya wazazi wake aliyeonyesha kushangazwa wala kutaka kujua anakohamia ila wakitegemea kushindwa kwake tu!

Siku hiyo Jay alikuwa amewaonyesha hasira yake, na kuweka wazi hataki kuwaona tena, na hata ikitokea inawalazimu wanaonana sehemu, basi wasithubutu hata kumsemesha. Aliweka wazi kabisa hataki kuhesabiwa kuwa hata mmoja wa familia akiwaambia hata na jina amebadili, yeye sio Lobulu tena.

Mzee Lobulu alimtizama mkewe kwa muda na kutafuta sehemu na kukaa hapohapo chumbani taratibu kama anayeumwa magoti. Kimya akiwaza bila hata kumsemesha mkewe aliyekuwa akilia kama yupo msibani. Nani wakulaumiwa? Jay aliwachambua kila mmoja kwa dhambi zake. Chuki na hasira zilizokuwa zimejaa kifuani kwa mzee, ilikuwa ngumu kupumua vizuri. Unyama aliotendewa Jay, tena na shemeji! Ulimuuma sana. Akajiambia, roho yake haitatulia mpaka alipize kisasi.

Kwa namna gani! Ndio swali liliendelea kichwani kwake hapo alipokuwa amekaa, akimsikia mkewe akilia kwa chungu kama anayeomboleza msiba wa hao wanae. ‘Kipimo kilekile alichompimia mwanangu ndicho nitakacho mpimia na yeye, na kumrudisha nilikomtoa. Chini mavumbini.’ Akaadhimia mzee Lobulu baada ya kukamilisha adhabu ya shemeji yake, mawazoni. Lakini akakusudia asimwambie mkewe.

Akatoka hapo mida hiyo bila kuaga kwani mkewe bado alikuwa akilia. Alikuja kurudi usiku sana mkewe akiwa amelala. Ila siku inayofuata vyombo vya habari vikatangaza kuungua moto kwa fremu kadhaa za biashara zilizokuwepo maeneo ya Sinza kumekucha. Kati ya hizo fremu, tatu zilizokuwa zikimilikiwa na huyo mdogo wa mama Jay, Tondi na mkewe. Moja ilikuwa duka la nguo, pochi na viatu vya kike na kiume, pembeni ndio ilikuwa saluni kubwa sana ya huyo wifi yake mama Jay, mke wa Tondi. Fremu nyingine walifanya duka la vinywaji. Waliuza vinywaji vikali. Tena kwa bei ya jumla. Tondi alikuwa akiwauzia bia kwa bei ya jumla, karibu baa zote zilizokuwepo maeneo ya Sinza.

Pesa ilikuwa ikiingia kama mchezo. Halafu katikati ya hizo fremu zake karibu na duka la hivyo vinywaji, alifungua sehemu ndogo tu yakuuza chakula, lakini kuliwekwa viti kwa nje tu. Watu walikuwa wakijaa hapo mchana na usiku. Zote hizo zilikuwa biashara wanazotegemea Tondi na mkewe kwa kuwaingizia pesa. Ni kweli walikuwa wamefanikiwa. Mkewe Tondi alikuwa akiendesha SUV nzuri sana. Mmama mzuri ambaye ukimuona, ungejua pesa ipo. Kwa ufupi Tondi na mkewe walikuwa wamefanikiwa sana kimaisha. Mpaka wanakamilisha zoezi la kuzima moto, hakuna kitu kilichokuwa kimesalia kwenye fremu hizo za kina Tondi na majirani zao.

Tondi na mkewe walijaliwa watoto wawili. Wakiume na wakike. Na wote aliwasomesha shule za kulipia tena pesa ya juu tu. Tondi alitoka kwa dada yake, mama Lobulu na kuanza maisha katika hali nzuri. Kama alivyosema Jay, aliagwa vizuri. Zawadi yakueleweka ya kuanza maisha huku akipongezwa kwa kazi nzuri aliyoifanya kwenye mji wa dada wake.

Kijana wa Tondi ndio alikuwa kidato cha pili, na binti yake alikuwa darasa la saba. Wakiwa katika hali ya kuchanganyikiwa, kupoteza mali yote kwa mpigo. Tondi na mkewe, jioni hiyo wakiwa nyumbani kwao Bunju. Kwenye nyumba yao ambayo bado ilikuwa mpya kabisa. Zilikuwa zimepita siku 3 tu tokea maafa hayo yawapate. Bado chanzo cha moto kilikuwa hakijafahamika. Wakaingiliwa tena na majambazi hapohapo nyumbani kwao.

Waliingia ndani vijana hao wanne walioshiba wakiwa na mlinzi waliyemtoa getini na kumfunga mikono pamoja na miguu. Walikuwa ni vijana wakubwa kwa maumbile, waliojaa utisho wa namna yake. Hawakutaka hata sura zao zionekanike. Muda wote walifunika uso na kuacha macho tu. Walikusanya watu wote wanaoishi kwenye nyumba hiyo na kuwahamishia sebuleni. Wakawafunga midomo, mikoni, miguu na kuwataka watulie, wawe watizamaji tu. Waligeuza hiyo sebule iliyokuwa sehemu ya starehe kwa familia hiyo, wakikutana kwa mazungumzo au kutizama tamthilia, kuwa chumba cha maafa.

 Ulifanywa ukatili ambao hauwezi kutamkika. Walianza kwa kumbaka kijana wao huyo wa kidato cha pili, mbele ya macho yao wote. Walimfanyia unyama huo, kwa kupokezana wakilazimisha watu wote kuangalia kwa lazima. Ambaye alikwepesha macho, walimuadhibu bila huruma na kumtisha na yeye atafanyiwa kama huyo mtoto. Ikawalazimu kutizama mwanzo mpaka mwisho.

Vijana hao wanne walipomaliza kumtenda unyama mtoto huyo ambaye hakuwa na hatia, ila kuchaguliwa kulipa dhambi ya baba yake, ndipo sasa walipo mgeuza Tondi mwenyewe. Ilikuwa mbaya na yakusikitisha mno. Tondi alifanyiwa unyama huo, mbele ya familia yake. Tena wakimtizama kwa lazima, mwanzo mpaka mwisho ndipo wakaondoka.

Kilichowashangaza, ni kuwa mkewe, binti yao na wengine wote, hawakufanyiwa huo unyama! Mkewe alidhani pengine walikuwa ni majambazi ambayo yalitaka kuwaibia pesa, lakini wakashangaa walitoka hapo bila kuchukua chochote! Waliwalawiti baba na kijana wake, na kuondoka. Ila kwa Tondi, walimlawiti kinyama kama waliokuwa wamekusudia kumuumiza na kumuweka kilema cha milele. Walimbaka kwa kurudia rudia kikatili huku wakisisitiziana kuhakikisha wanammaliza kabisa, ili asiwahi kuja kufanya mapenzi na mtu mwingine yeyote hapa duniani.

Hivyo ndivyo mzee Lobulu alivyolipiza kisasi kimyakimya bila hata kumwambia mkewe ambaye ni ndugu wa Tondi. Na familia ya Tondi, yaani Tondi na mkewe, hawakutaka habari hizo zijulikane kabisa kwa watu. Wale majambazi walipotoka tu, mama mtu akamkimbilia mwanae aliyekuwa akilia sana kwa maumivu huku akitokwa damu hapo sakafuni alipokuwa akigaragara na kumkimbiza hospitalini akisaidiwa na mumewe ambaye hakutaka hata ije ujulikane kama na yeye alibakwa. Akajikaza kiume usiku huo, ikawa wanahangaika kwa matibabu ya kijana wao tu.

Wakiwa hospitalini wakimuhangaikia kijana wao, huku nyuma msichana wa kazi aliyekuwa amebakishwa na mtoto wao wa kike, naye kwa hofu, usiku huohuo akatoroka bila hata kumuaga huyo mtoto. Na mbaya zaidi, wakati binti huyo akilia chumbani kwake, yule msichana wa kazi akapata mwanya wakuingia chumbani kwa wenye nyumba. Akajichotea dhahabu za mke wa Tondi zote alizoweza kuziona kwa haraka na pesa zote alizokuta juu ya meza, ndipo akaondoka, akawaacha kwenye matatizo yao.

Na kwa kuwa Tondi na mkewe hawakutaka hilo tukio lijulikane hata kwa majirani tu, hakuna aliyejua kilichowapata usiku ule, zaidi ya wale walioshuhudia. Mlinzi na msichana wa kazi ambaye alishatoroka. Ikabaki kuwa siri ya familia.

 Mama Ole.

Kumbukumbu hizo za ajali zilidumu kwa siku tatu mfululizo, ndipo akaweza kulala kwa masaa kadhaa bila ya kustukastuka, au kuwa na ndoto mbaya. Usiku wa usiku wa nne wakiwa wamelala, Kenny alimuamsha Nai amuwekee chupa ili ajisaidie, ujumbe ukaingia kwenye simu ya Naih. Wote wakashangazwa maana ilikuwa usiku mwingi tu wakutosha. Naih akasoma. ‘Najua sikuwahi kuwa mama mzuri kwake. Lakini nashindwa kulala vizuri Naih. Natamani kuja kumuona. Angalau katika hiki kipindi kigumu niwe naye. Hata kama sitafanya chochote, ila tu niwepo, kama kule hospitalini.’ “Nani huyo!?” Kenny akamuuliza. “Ni mama yako. Nashauri umkubalie aje akuone ili atulie. Sasa hivi ni saa saba, na huu ujumbe ametuma saa 6 usiku.” Kenny akanyamaza.

“Kenny?” “Mimi sijamkataza kuja hapa, Naih. Mbona hata hospitalini sikuwafukuza! Sikutaka kuonyesha kuwa wanaweza kuja wakati wowote wanaotaka, halafu wakaanza kujaa hapa kwako wakati walikufukuza kwao.” “Wala usijali juu ya hilo. Kwa hiyo nisawa nikimjibu ujumbe wake?” “Fanya vile utakavyo Naih. Wewe unajua mimi huwa siwezi kumkasirikia mtu kwa muda mrefu.” Naih akacheka sana huku akimwangali kwa kumsuta.

 “Kasoro wewe.” “Sasa mimi nilikufanyaje Kenny, jamani!?” “Ulinikimbia halafu nikajua unaishi na Tuse.” Naih akatingisha kichwa kwa masikitiko kisha akamuuliza. “Sasa ungenikasirikia mpaka lini?” “Wewe huoni nilikuwa sitaki kuhudumiwa na mtu mwingine ila wewe tu? Pale nilikuwa sijui jinsi ya kujirudi.” “Mbona mimi nakufahamu! Wala hukuwa ukinipa shida. Nilikuwa najua ulikuwa na hamu na mimi tu, ila ukorofi ndio ulikuwa unakuzidi.” Kenny akacheka.

‘Sasa hivi anaendelea vizuri, anaweza hata kulala. Usiwe na wasiwasi. Hali yake ikibadilika nitakujulisha.’ ‘Mbona hujalala mpaka sasa hivi? Kwema?’ Mama Ole alirudisha ujumbe kwa haraka sana. “Naona nimpigie mama yako mzungumze naye, Kenny. Mama yako ana wasiwasi sana. Na unajua ana pressure.” “Mpigie.” Naih akampigia akampa Kenny simu. “Mbona hujalala mpaka sasa hivi?” Kenny akamuuliza. “Nina wasiwasi na wewe Kenny. Najua sikuwahi kuwa mama mzu..” Yule mama akanza kulia. “Usiwe na wasiwasi mama. Mimi naendelea vizuri. Nilimka kujisaidia. Kukiwa na tatizo lolote tutakujulisha.” “Kweli utanijulisha?” Kenny akanyamaza.

“Naomba na mimi nikuuguze Kenny. Kama nilishindwa zamani, naomba unipe nafasi na mimi safari hii nikuuguze mwanangu.” “Sasa unataka kufanya nini? Naih na mama yake wanafanya kila kitu. Sihitaji msaada. Wewe pumzika tu.” “Basi niruhusu hata niwe nakuja kukuona.” Kenny akacheka kidogo. “Haya njoo, kama itakusaidia kutulia.” Mama Ole hakuamini masikio yake. Alifurahi sana. “Asante sana Kenny, mwanangu. Basi nitawaona kesho asubuhi.” “Basi ulale sasa.” Kenny akaongeza. “Sasa hivi nitalala.” Kenny akakata simu.

https://cdn3.volusion.com/fjmpg.dxchy/v/vspfiles/photos/YA-56-2.jpg?1484737416

            Kwa mara ya kwanza Naih kifuani kwa Kenny.

K

enny akabaki akiiangalia ile simu. “Umefurahi kuzungumza na mama yako?” Naih akamuuliza. “Alikuwa na wasiwasi sana. Angalau atatulia.” “Basi na wewe urudi kulala.” Kenny alibaki kimya kama anawaza kitu. “Unafikiria nini?” Naih akauliza huku akirudisha simu ili walale. Akarudi pale kitandani, akabaki akimtizama. “Nikuombe kitu?” “Niambie chochote unachotaka.” Naih akajibu kwa utulivu. “Najua haijawahi kutokea. Lakini naomba uje ulale hapa kifuani kwangu.” Naih alishituka kidogo. Hakuwahi kulala kifuani kwa Kenny, zaidi ya kulala huku wamegeukiana tangia wapo watoto.

“Ila sio lazima Naih. Najua itakuwa ngumu. Ni sawa tu, naelewa.” Kenny akajirudi tena baada ya Naih kubaki kimya kwa muda akiwa anafikiria huku ameinama. Taratibu Naih akajivuta mpaka kifuani kwa Kenny. Akapitisha mkono mmoja juu ya kifua chake kama kumkumbatia, uso ukabaki pembeni ya shingo ya Kenny huku akiangalia chini. Alimsikia Kenny akihema kwa nguvu na kushusha pumzi taratibu na yeye akamkumbatia kwa mikono miwili. “Asante.” Kenny akashukuru. Naih akanyanyua uso, akambusu shavuni, wakalala.

Usiku huo ulikuwa mzuri sana si kwa Kenny tu, mpaka kwa Naih mwenyewe. Kenny hakumuamsha tena kutaka kujisaidia, na wala Naih hakushituka kumwangalia anaendeleaje. Tuse alimka asubuhi na kwenda kazini, wao wakiwa bado wamelala, mpaka saa nne asubuhi Mama Ole alipokwenda kuwagongea. Naih akafungua macho akakuta Kenny akimwangalia. “Pole. Umeamka muda mrefu?” Naih akauliza wakati anajitoa kifuani. “Hodi ya kwanza ndio iliyonishitua. Sijawahi kulala vizuri tokea nipate ajali kama hivi.” Naih akacheka kwa aibu na kutoka kwenda kufungua mlango.

************************

“Nakushukuru kwa kuniruhusu kuja, Naih. Naomba nipe kazi yeyote.” Naih akacheka. “Sijui kama kuna kazi, Mama Ole. Naomba usiwe na wasiwasi. Ngoja nimsafishe Kenny, alikuwa amelala, halafu nimtoe hapa, mje kunywa nae chai.” “Basi ngoja mimi niiandae hiyo chai.”

 Naih na mama yake Kenny walisaidiana kumlea Kenny, bila kuchoka. Yule mama alikuwa akifika pale asubuhi, anasaidia shuguli ndogo ndogo, kama kuna nguo chafu, alizichukua kwenda kufuliwa na mashine nyumbani kwake na kuzirudisha jioni zikiwa zimekunjwa vizuri. Kama ni siku ya Kenny kwenda hospitalini kwa mazoezi, Mama Ole alikuwepo kuwachukua na kuwapeleka mazoezini. Alisubiri mpaka Kenny amalize ndipo awarudishe nyumbani.

https://cdn3.volusion.com/fjmpg.dxchy/v/vspfiles/photos/YA-56-2.jpg?1484737416                       Nguvu Ya Upendo wa kweli.

N

aih kumuona Kenny akiwa mtupu likawa swala la kawaida kabisa. Kwani ndiye aliyekuwa akimfanyia kila kitu. Tabia ya Naih yakulala kifuani kwa Kenny ikawa ni mazoea ya wote wawili. Ile hofu ya kulala kifuani kwa Kenny iliisha, akaweza kulala kifuani hapo huku akichora kifua hicho kwa kidole chake, wakiwa wanaongea na kucheka bila shida. Wakati mwingine alimwambia Kenny asikilize kwa makini ni nini anaandika kifuani kwake kwa kidole, kisha amwambie. Mchezo huo ulikuwa ukiendelea kila siku usiku ndipo wanalala.

Taratibu hisia za tofauti au mpya zikaanza kujengeka kwa Naih. Ile nakupenda ya tokea watoto, ya kila wakati ikaanza kupungua na kumfanya awe anafikiria mara mbilimbili kabla hajasema. Mabusu ya shavuni yakaanza kupata mvuto wa namna yake. Kulala kifuani ikawa sio usiku tu, hata mchana. Walitaka wajilaze kitandani ili Naih apate sababu ya kuwa kifuani kwa Kenny. Naye Kenny akawa akipitisha mikono yake yote miwili akimkumbatia Naih kila awapo kifuani kwake. Naih alikuwa akisikia furaha ya namna yake. Alikuwa akitulia kifuani kwa Kenny, kama kipaka huku Kenny akimpapasa mgongoni taratibu na kuzungumza naye taratibu.

Kukaa sebuleni ikawa mpaka Tuse awaite kwa ibada au watembelewe na wageni. Vinginevyo muda mwingi waliutumia kitandani ili wapate sababu ya Naih kuwa kifuani, na Kenny amkumbatie. Basi hapo Kenny atampapasa taratibu mgongoni huku wakizungumza hili au kimya wakingalia luninga. Siku za kazi walizipenda kwani walishinda hapo kitandani bila kuingiliwa na mtu.  Watakula hapohapo kuanzia chakula cha asubuhi mpaka jioni Tuse atakaporudi nyumbani. Tena awaite kwenda kuomba na kusoma neno. Lasivyo hawakuwa wakitaka kutoka kitandani.

Wakati Mwengine Matatizo Husogeza Watu Karibu.

U

karibu kati ya Kenny na mama yake ukarudi. Wakaanza kuwasiliana kama zamani. Ndipo wakaona na baba yake anaanza kuja kuwatembelea, na kukaa hapo. Wakati mwingine alileta filamu  mbali mbali wakati wa jioni, pamoja na nyama choma, na kukaa wote watano na Tuse akiwepo, wanakula huku wakiongea mpaka wanapoachana kwenda kulala. Kwa vile wanavyowafahamu wazazi hao, zaidi mzee Ole, Naih na Kenny walikuwa wakishangazwa sana! Mpaka wakahisi maneno ya Jay yaliwaingia na wazazi hao pia. Mzee Ole alibadilika sana na kuanza kujituma kwa Kenny wala si kutumia mfanyakazi. Yeye moja kwa moja akawa anajihusisha na Kenny mpaka akawa anamshangaza mama Kenny.

Kwanza mzee huyo wa starehe nakupenda dogodogo, aliweza kutumia muda mwingi hapo nyumbani kwa Naih akiangalia filamu na wao! Hilo likawashangaza wote. Na pia kabla yakuondoka kila wanapokuja baada ya kutoka kwenye majukumu yao, basi mzee huyo alihakikisha anamuacha Kenny msafi na amempandisha kitandani kabisa. Ilikuwa kama ni kuoga, basi atampeleka yeye mwenyewe bafuni na kumsaidia kuoga. Akishamuweka kitandani, ndipo na wao wanaondoka. Wakati mwingine walikuwa wakikaa pamoja wakicheka mpaka usiku sana ndipo wanaondoka.

Kwa hiyo muda na vimada nao ukaanza kukosekana. Mzee Ole akajikuta muda mwingi yupo na mkewe. Kama sio nyumbani kwa Naih, basi watakutana mahali na mkewe hata kama ni muda wa mchana, wakipanga jinsi ya kuhakikisha Kenny anapata miguu ya bandia ya kisasa itakayomuwezesha kukamilisha ndoto zake. Wakati mwingine walitoka nyumbani kwa Kenny na kurudi nyumbani moja kwa moja. Na mama naye akapunguza shuguli za nje na hata mahusiano ya nje aliyokuwa nayo ya kimapenzi, yakaanza kukosa maana sababu ya kuuguza na kufikiria kijana wake tu. 

Kenny ameondoka nyumbani kwenye jumba la maana anaishi kwenye chumba cha kupanga tena kwa kawaida kabisa wakipulizwa na feni! Ni vile hakuwa anaweza kubadilisha hilo. Akajilaumu ni kama wao wenyewe wamemfikisha hapo kijana wao, wapekee. Hofu ya kumpoteza Kenny kama rafiki zao walivyompoteza Jay, mtoto mzuri wa kwanza wa kiume, ikawaingia. Ila wao ilikuwa mbaya zaidi. Mtoto mmoja tu! Kila juhudi waliyoweka hapa duniani. Mali nyingi walizochuma, inamaana itakuwa bure endapo watampoteza Kenny. Taratibu mambo mengi yasiyo ya mzingi na yaliyokuwa yakiwachukulia muda mwingi, yakaanza kukosa maana.

Wakaanza kujikuta vikao vya hapa na pale wakiitana kupeana maendeleo ya kutafuta miguu hiyo, vinaongezeka. Au kuongozana kwenda kuzungumza na wataalamu wa miguu bandia. Mara chakula cha mchana wawe pamoja, ikishindikana, basi iliwalazimu usiku wawahi nyumbani ili wazungumze zaidi. Isivyo ya kawaida simu za mara kwa mara kati yao kuulizana kama amemsikia Kenny na maendeleo yake, nazo zikaongezeka. Wakaanza kujikuta wanaingia kitandani kulala muda mmoja.

“Vipi, hutoki tena?” Rita, yaani mama Ole alimuuliza mumewe. “Akili hazijatulia. Acha nipumzike tu. Kesho si ndio umesema utampigia simu yule mtaalamu mwingine wa miguu bandia?” “Naona hamna tumaini, Ole. Miguu yote aliyonitajia ni ya kawaida sana. Amesema kama tunao uwezo ni heri kumpeleka India. Itatugarimu lakini atapata miguu mizuri na ya kisasa.” “Amekutajia hospitali yenyewe?” “Ndio kesho amesema nikimpigia atakuwa na maelezo kamili. Yupo daktari mmoja kutoka huko kwenye hiyo hospitali ya India, alikuja hapa nchini kwa kipindi fulani kwenye kitengo chao, anasema upo uwezekano akatusaidia. Alitaka nimpe siku ya leo, kesho ndio nimtafute.” “Afadhali.” “Lakini nina wasiwasi kweli.” “Naelewa. Lakini jipe moyo. Kila kitu kitakaa sawa.” Ole alijaribu kumfariji mkewe.

“Hivi umeshajiuliza, jinsi tunavyohangaika kutafuta hiyo miguu, Kenny mwenyewe atakubali?” Rita akamuuliza mumewe. Mzee Ole akatulia kidogo. “Naona kama kuna mabadiliko. Hasira zimepungua. Hata nikimsaidia kuoga, hana ubishi. Tutazungumza na Naih kwanza. Tukifanikiwa kumuweka sawa Naih, najua Kenny hawezi kukataa.” Ukimya ukapita.

“Ole!” “Nipo, bado sijalala.” “Nina majuto kweli! Sijui nilikosea wapi kwenye malezi ya Kenny?” “Wote tulijisahau Rita. Tulidhani tunampa kile anachokihitaji kumbe ndio tulikuwa tukivunja mahusiano na mtoto wetu na kumjengea mahusiano na mali zetu.” “Nakumbuka nilianza vizuri kweli, sijui nikakosea wapi!?” Mama Ole alikuwa akiwaza. “Sijui kuanzia kipindi kile nahangaika kushika mimba nyingine!?” “Na ulikuwa umechanganyikiwa kweli Rita!” “Mimi nahisi ndio kipindi kile. Kule kupoteza watoto mfululizo na yule wa kike ambaye nilijenga imani ningemzaa, nikabeba miezi tisa akaja kuzaliwa, akafa hata hajanyonya, nikaishia kumpa Naih nguo zake zote, nahisi pale ndipo nilipochanganyikiwa kabisa. Nikaona nijitupie kwenye kufanya kazi nyingi zitakazonifanya hata nisifikirie kitu kingine. Na kweli ilinisaidia. Ningechanganyikiwa kama ningekuwa napata muda wa kukaa hapa nyumbani, lakini ndio imemgharimu Kenny wangu! Haamini kabisa kama namjali.” Mama Ole aliendelea kuwaza huku akilalamika taratibu.

“Unajua kipindi kile wakati bado mdogo alipokuwa akiugua, nilikuwa nikiingiwa sana na hofu. Nilikuwa nikijiambia asije akanifia. Nilijiona kama nina mkosi. Basi nikawa nikimuomba Atu awe anampeleka yeye hospitalini, akishatibiwa awe ananijulisha. Sikujua kama nasababisha madhara makubwa kwa Kenny!” Mama Ole aliendelea kufikiria huku akilalamika. “Unajua Ole?” “Nipo.” “Huyu mtoto akikataa hizi mali zote, unajua hangaika yangu yote itakuwa bure?” “Najua.” “Nimehangaika sana kufika hapa nilipo, Ole. Naumia kuja kujua jasho langu litapotea bure!” “Bado nafikiria kuna umuhimu wakumfanya Naih kuwa rafiki yako wakaribu sana, Rita. Ukimpata Naih, ujue umempata Kenny.” Mzee Ole akashauri.

“Nimejaribu, lakini naona ananisukumia kwa Kenny. Amekataa kabisa kupokea pesa zangu.” “Ulitaka kumlipa tena!?” “Hapana Ole. Nilikuwa nampa ya kununulia vitu ambavyo ataona anahitaji pale kwake. Au hata umeme, au kodi. Lakini amekataa kabisa.” Wote wakatulia wakapotelea kwenye mawazo.  

“Ila kitendo chakuanza hata kupokea chakula tunacho peleka, sio mwanzo mbaya. Tusijikatishe tamaa.” Ole aliongeza kujifariji. “Na wazo la ile nyumba?” “Juzi nilipokuwa chumbani na Kenny, nilitamani kumgusia. Lakini nikasita. Pale wanapoishi ni padogo sana. Kenny anapata shida kufikia maeneo mengi, sababu ya ile wheelchair ni kubwa, chumba au nyumba yenyewe imebana. Haiwezi kupita maeneo mengi.” “Hata mimi nililiona hilo, lakini ile furaha niliyomuona nayo Kenny, sikutaka kuvuruga.” “Basi tuache kwanza.” Ole akahitimisha hivyo, wakakubaliana na mkewe.

Hata siku hiyo waliwahi kurudi nyumbani. Walitokea nyumbani kwa Naih. Wakapata wakati mzuri na mtoto wao. Mzee Ole na mkewe walipeleka chakula kingi na vinywaji. Kuku wakuchoma mzima, chips, ndizi za kuchoma na kukaanga, kachumbari, kitimoto ya kurosti. Ilikuwa nyingi na vinywaji. Naih aliviweka mezani wakawa na kazi yakujipakulia tu na kula huku wakiangalia mpira na Kenny. Baada ya kutoka hapo, hakuna aliyekuwa na hamu ya kwenda mahali kwengine zaidi ya kurudi nyumbani.

Ile hali yakumuona mtoto wao hana miguu pekee ilikuwa ikiwanyima raha yakufanya starehe ya aina yeyote ile. Akili ziliwavurugika wazazi hao, wasijue jinsi yakumsaidia mtoto wao wa pekee, ambaye amejitenga na kila kitu chao. Japokuwa Mzee Ole alikuwa na wanawake wengi nje, hakuwahi kupata hata mtoto mmoja wakusingiziwa. Ni Kenny tu. Hata yeye alijiuliza mali zote zile anapeleka wapi! Wakabaki kitandani hapo wakiwaza kila mmoja na majuto yake. Jay aliwatukana lakini ni kama alirudisha akili zao zilizokuwa likizo. Wazee hao hawakuwa tofauti na vijana huko mtaani. Damu bado zilikuwa zikiwachemka. Jay ni kama aliwaamsha na kuwatoa usingizini.

https://cdn3.volusion.com/fjmpg.dxchy/v/vspfiles/photos/YA-56-2.jpg?1484737416

                   Naih & Kenny.                     

K

enny alijikuta macho yamehama kabisa kutoka kwenye luninga, yakatua pale mwilini mwa Naih aliyekuwa akijipaka losheni baada ya kuoga ili walale. “Njoo nikusaidie.” “Nimebakisha mgongoni tu. Nitamalizia. Asante.” Naih akajibu kwa aibu. Alishakuwa amemsaidia Kenny kuoga na kumpaka mafuta sehemu zote, hasa maeneo ya mapajani alipokuwa akiogopa kujiangalia. 

    “Njoo ulale hapa kitandani, nikumalizie mgongoni. Au huniamini?” “Hapana! Sikutaka kukusumbua.” “Hamna shida. Njoo.” Naih akapanda pale kitandani akiwa amejifunga taulo. Akalala kifudifudi. Kenny akalishusha lile taulo mpaka kiunoni, nakuanza kumpaka losheni taratibu kama kumfanyia masaji. Kuanzia mabegani mpaka chini karibu na kiuno. Taratibu huku akitumia nguvu kiasi kumchua. Mwili mzima wa Naih ulikuwa ukisisimka. Binti huyo aliyekuwa hajawahi kushikwa na mwanaume, akajikuta akiomba Kenny asimalize. Alitulia kabisa wakati Kenny akiendelea kumchua taratibu.

Akamfunika na shuka juu ya lile taulo. “Nataka kuvuta taulo. Ni mbichi, utaingiwa baridi. Ni sawa?” Kenny akauliza, Naih akatingisha kichwa kukubali. Bila kumfunua, Kenny alilivuta lile taulo, na kuliweka pembeni ya kitanda. Akabakisha sehemu ya chini tu aliyokuwa ameifunika na shuka huku Naih akiwa hajavaa nguo hata moja ndani. Kenny aliendelea taratibu bila haraka, huku akipanda mpaka shingoni na kushuka mpaka kiunoni. Mwishowe Naih alipitiwa na usingizi. Kenny alimvuta mpaka kifuani kwake, akamkumbatia vizuri, akiwa amemfunika.

Ukweli Kilichokuwa Kikiendelea Moyoni Mwa Kenny Tokea Zamani.

A

subuhi Naih alitoka usingizini na kujikuta akiwa uchi kifuani kwa Kenny. Akaingiwa na hofu na kuhisi ni ndoto tu. Akaanza kujishika mara kadhaa, akathibitisha yupo uchi. Akanyanyua uso taratibu kumuangalia Kenny kama amelala ili atoke pale kimyakimya awahi kuvaa, macho yake yakagongana na Kenny, akambusu kwenye kipanda uso kabla hajarudisha macho chini. “Ulilala salama?” Kenny akauliza, Naih akatabasamu kwa aibu. “Nilipitiwa na usingizi!” Naih alijibu taratibu akionyesha kuishiwa ujasiri. “Hakuna neno. Nakupenda Naih.” Naih akanyamaza, akarudisha uso chini. Kenny akambusu kichwani na kuendelea kumpapasa.

***************************

Tabia yakuambiana ‘nakupenda’ haikuwa ngeni kwao. Walishazoeshana hivyo tokea watoto. Lakini Kenny alihakikisha analibadili neno hilo na kuliwekea uzito wa tofauti na vile Naih alivyozoea kusikia au akiielewa. Taratibu bila haraka, lile neno akaanza kulijenga na kulipa hisia tofauti kwa Naih ambaye hakuwa akimfikiria Kenny kimapenzi. Alimkoleza kwa hili na lile, mpaka akafanikiwa kumuweka kwenye mstari mmoja.

***************************

“Natamani tuendelee kuishi hivi milele!” “Kwani ukipona utaniacha?” Naih akauliza swali ambalo hata hakutegemea. Tayari akagundua amekwenda umbali mkubwa sana na Kenny. Kenny ameshika mwili wake ukiwa hauna nguo! Hofu ya kuwa kama wanawake wengine waliochezewa na kuachwa wakimlilia Kenny, ikamwingia. Kwa mara ya kwanza alielewa kwa nini walibaki wakimlilia Kenny. ‘Ana jinsi yake yakushika!’ Na Naih naye aliwaza na kukubaliana na wale wanawake aliokuwa akiwasikia wakimlalamikia Kenny kule hospitalini. Japokuwa bado hawakuwa wamefanya mapenzi, lakini alimfikisha mahali ambapo alitamani wasirudishe yale mahusiano ya zamani.

“Binafsi naogopa hata kufikiri kuja kuachana Naih. Naogopa sana.” “Basi tusifikirie kutengana tena.” Naih akasihi. “Utakubali kuishi na mimi hivi nilivyo!?” Naih akatingisha kichwa kukubali. Kenny akabaki akimtizama kama anayetafuta uhakika wake. Naih akarudisha kichwa upande mmoja kifuani kwa Kenny akabaki akichora taratibu, akamsikia Kenny akivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.

Naih akaanza kuandika hapo kifuani, Kenny akatulia ili kujua anaandika nini, akaweza kutambua alichoandika. ‘nakupenda Kenny.’ “Asante.” Kenny akajibu kwa sauti iliyoweza kusikika akimshukuru Naih.

“Naamini naweza kuja kutembea tena, Naih.” “Sijali Kenny.” Kenny akatulia kidogo, akaendelea kumpapasa mgongoni. “Wakati nilipopata ajali walinipima na UKIMWI.” “Nafahamu Kenny.” Naih akajibu taratibu na yeye akiendelea kumchezea kifuani. “Tangia ulipoondoka nyumbani, sikufanya mapenzi tena na mtu mwingine.” Naih akanyamaza. “Nilikuwa nikisafiri na Nora, lakini sikufanikiwa kufanya mapenzi.” Naih akanyamaza kama kawaida yake kutochangia kwenye habari za Kenny na wanawake zake.

“Unakumbuka mara ya mwisho kuwasiliana na mimi tukiwa Afrika ya kusini?” “Ni Zai na Mia ndio walikutumia ule ujumbe Kenny. Sio mimi.” “Nilikuja kujua hilo baadaye sana Naih. Lakini kile kitendo cha kushindwa kukusikia kwenye simu kwa siku zote zile, ilianza kuathiri hata ufanyaji wangu wa mapenzi. Siku ya mwisho ndio nilishindwa kabisa, na mbaya zaidi, mara ya mwisho wakati nafanya mapenzi na Nora, nikawa nakutaja wewe katikati ya mapenzi.” Naih alishituka sana. Akabaki kama amepigwa ganzi, akashindwa hata kumchezea kifua chake tena. Akahisi vidole vinatetemeka.

“Kile kitendo kilimuumiza sana Nora, ndio maana alishindwa kuendelea na mimi. Sio kweli kama Nora amenikataa sababu nimekuwa mlemavu. Alikuwa yupo tayari kumuacha mpenzi wake ili nimuoe. Wakati tupo wote Dodoma, pia nilishindwa kufanya naye mapenzi. Ikawa mbaya zaidi uliponiacha tena Naih. Nilikaribia kuchanganyikiwa! Nora alikuwa akigomba kitu kilichonipandisha hasira, nikajikuta nikimwambia ukweli wote.” Naih alinyanyua uso na kumtizama Kenny kwa mshangao.

          “Ukweli gani!?” “Kuwa nampenda Naih. Na moyoni mwangu hakuna nafasi ya mwanamke mwingine yeyote yule hapa duniani isipokuwa Naih. Nikamwambia nimejitahidi kupuuza hilo kwenye moyo wangu lakini nimeshindwa. Ndio maana kila mwanamke niliyekuwa nikilala naye, ilikuwa ni lazima nimbadilishe awe kama Naih ndipo niweze kufanya naye mapenzi. Nikamwambia hata yeye mwenyewe ilinibidi nimfanye kama Naih mawazoni mwangu, ndipo niweze kufanya naye mapenzi wakati wote.” Naih akahisi anaota, atakuja kuamka usingizini. Alishindwa hata kusogea kwa mshangao na mshituko.

“Nikamwambia nimefanya hivyo kwa muda mrefu sana, mpaka nahisi inataka kuniharibu akili na kuanza kukutaja wewe katikati ya mapenzi na watu wengine! Haikuwa bahati mbaya kukutaja Naih. Ni kweli kila mwanamke niliyekuwa nikilala naye popote pale, iwe kwenye gari au kitandani, bafuni au kwenye kochi, nikimnyanyua ukutani au nimuweke sakafuni, lazima akili yangu ifanikiwe kumgeuza kuwa ni Naih ndipo niweze kufanya nao mapenzi. Hakuna mwanamke aliyekwisha kuweka historia na mimi kwenye mapenzi ila wewe Naih.” Naih akakaa kwa haraka bila kufikiria. Akagundua yupo uchi kabisa. Akavuta shuka, lakini kumbe shuka hilohilo ndilo alikuwa amejifunika nalo Kenny. Akafanikiwa kupata upande mdogo wa shuka hilo, akafunika matiti yake yaliyokuwa kifuani kwa Kenny usiku kucha.

Kenny alipoona ametulia, akaendelea. “Kila nilipokuwa nikiwagusa na kumaliza, nilikuwa na picha pamoja na hisia kama hizi ninazozipata nikiwa na wewe hapa kitandani. Kwa hiyo kile kitu kilimuuma sana Nora, akaondoka kwa hasira. Nafikiri alidhani ningemfuata, lakini nilishindwa. Asubuhi ileile nikawasha gari kurudi Dar, angalau nije kukuona. Nilimsimulia Emma habari nzima ya Dodoma. Kumbe yeye Emma alishagundua hilo. Kuwa huwa wakati wote, ninafanya mapenzi na wanawake wote hao, lakini nafsini mwangu inakuwa ni wewe Naih. Hata hivyo alishanisihi sana nikwambie, lakini mwanzoni nilijua hata nikikwambia usingenisadiki, ungejua nakudanganya kama ninavyo wadanganya wanawake wengine.” Kenny akatulia kidogo kama anayefikiria.

Kisha akaendelea. “Ulivyofukuzwa nyumbani na mama, halafu baadaye Emma akaja kuniambia amewakuta mahali mnauza vyakula. Nikamwambia nilazima akupe kazi yeyote ofisini kwake, halafu mimi nitakuwa nikikulipa. Kwanza nilikuwa napatwa na wivu kujua unakutana na watu wengi tofautitofauti kama wateja, tena wanaofanya kazi maofisini. Japokuwa ulikuwa umeniudhi sana, lakini bado moyoni sikutaka mwanaume mwingine aje akushike mwili wako kama hivi ninavyokushika mimi. Nilihakikisha Emma anakutoa pale na kukuweka ofisini kwake, nikawa nakulipa mimi mwenyewe mshahara kila mwezi.” Naih alishangaa zaidi.

 “Bado Emma alinisisitiza nikwambie tu, japo alitoa angalizo la Tuse. Aliniambia vijana wa pale walikuwa wakikutania juu ya Tuse lakini hukuwahi kukanusha. Wivu ukaanza kunitesa. Halafu nikawa nasubiri angalau Emma arudi nyumbani aniambie, ‘leo Naih amekuulizia’. Lakini hukuwahi ukiniulizia Naih!” “Nilikuwa naogoapa Kenny!” “Hata mara moja!?” “Naomba nisamehe Kenny. Lakini nilikuwa nikitamani sana kujua hali yako, lakini sikujua naanza kukuulizia vipi kwa Emma!” Naih akajaribu kujitetea. Akajirudisha kifuani taratibu.

“Basi, nikazidi kuchanganyikiwa. Kila siku nilikuwa nikisubiri salamu zako, bila mafanikio.” “Pole na samahani Kenny.” Kenny akajicheka kwa kujiguna bila kuitika hiyo pole. “Mwishowe nikaona ni heri nije pale nifanye kazi na nyinyi tu, labda roho itatulia. Sasa niliporudi kutoka Dodoma, na sikupati kwa simu, nikajua yote hayo ni sababu umempata Tuse. Nikaanza kumlalamikia Emma. Ndipo Emma akaniambia kitu kilichoibua maswali yaliyonipelekea kuutafuta ukweli. Aliniambia mama alikupokonya ile simu niliyokupa zawadi, ndio maana hukuwa na simu mpaka nilipokununulia hii simu nyingine niliyompa Emma akupe akwambie ni ya kikazi na kuanza kukuwekea pesa humo kwenye hii simu.” Naih aliambiwa na Emma ameongezewa simu na pesa kama marupurupu ya kazi, asijue anahongwa na Kenny. Alibaki amepooza hapo kifuani nakushindwa hata kuandika au kuchora kitu tena. Akatulia kimya akitafakari mshahara wake mnono na marupurupu yake aliyokuwa akipokea kazini, kumbe vyote hivyo vilikuwa vikitoka kwa Kenny!

Kenny akaendelea. “Sasa nilipokuja kujua ukweli wote wa kile mama alichowatendea, hasa wewe ndipo nikajua ndio umeangukia kwa Tuse, sitakaa nikupate tena. Emma akazidi kuharibu vile alivyokuwa akinilaumu kwa nini sikukwambia tokea zamani, nikaendelea kulala na wanawake wote wale! Nilikata tamaa Naih. Sasa nikaja kukuona tena siku ile ya jumatatu na Tuse, anakujali vile! Niliondoka pale nikiwa tayari kwa lolote litakalo nikabili.” Naih hakuwa akiamini anayoyasikia.

“Nilikuwa naogopa! Sikuwa nikijua inakuaje tena bila wewe, huku nimeshagombana na wazazi wangu! Nilikuwa nalia njia nzima huku nakanyaga mafuta kama mwehu. Sasa nafikiri sababu ya kukanyaga mafuta mengi, mvua kali, maji yalikuwa yamejaa barabarani, nikapita yale mataa ya Surrender, yakiwa mekundu. Nilipoyapita tu nikataka kugongwa na gari jingine iliyokuwa ikitokea njia ya Upanga kama unatokea Muhimbili au Kariakoo kwenda Msasani au Masaki. Nilikuwa kwenye mwendo mkali sana, nikakanyaga break kwa nguvu. Kile kigari kilirushwa juu mara mbili, kikagonga nafikiri uzio wa daraja, nikatupwa ndani ya bahari, huku gari ikiwa imeshapondeka imeshikilia miguu.”

“Akili zangu zote zilikuwa zikikuwaza wewe Naih. Nilijua utaolewa, utamzalia mtu mwingine watoto, na kunisahau muda mfupi sana mara baada ya mimi kuzikwa. Nikajiambia lazima nipone, ili nije kukwambia kuwa nakupenda sana.” Naih aliyekuwa mzito sana wa kulia, akajikuta machozi yakimtoka. Haraka sana akainamisha uso kifuani kwa Kenny. Hukuwahi hata kumfikiria Kenny kwa upande huo. Machozi yalimtoka asiamini kuwa na yeye anahusika kusababisha ajali ile.

**********************************

Hakuwahi hata kusifiwa uzuri wowote mwilini mwake na mtu mwingine yeyote isipokuwa huyo Kenny mwenyewe tokea wapo watoto, kitu ambacho alikiona cha kawaida sana. Hakurithi kitu chochote kutoka kwa mama yake. Wadogo zake walikuwa wakisifiwa uzuri wakilinganishwa na mama yao. Watu walikuwa wakisema wamerithi hiki au kile kutoka kwa mama yao. Hakuwahi kutongozwa yeye kama Naih. Mara zote walipokuwa wanne hata na mama yao, watu waliwatongoza wadogo zake, na mama yao, sio hata Naih mwenyewe.

Leo Kenny kumwambia hana nafasi ya mwanamke mwingine moyoni mwake ila yeye, ilimshangaza sana Naih. Ni Kenny jamani! Kenny aliyekuwa akilala na kila warembo! Wa mwisho aliyemshuhudia Naih ni Nora mtoto mwenye umbile la kibantu! Naih alibaki pale kifuani kwa Kenny akitafakari, asielewe.

*****************************

 “Nakupenda sana Naih. Wewe ni kila kitu changu kwenye maisha yangu. Ninaposema wewe ni ‘mimi wangu’. Namaanisha wewe ni mimi wangu kweli. Nakamilishwa na wewe Naih. Japokuwa nimelala na wanawake wengi, lakini sijui mapenzi na wanawake wengine ila wewe. Wakati mwingine nilikuwa nikitoka pale nyumbani unakuwa umenifurahisha kwa jambo dogo tu, basi nakwenda kufanya mapenzi na wewe kwa kutumia miili ya watu wengine bila kuchoka, kisha nikirudi nyumbani nataka nilale na wewe.”

“Ndio maana wakati mwingine nilipokuwa nikirudi nyumbani hata kama nakukuta umelala, ilikuwa lazima nikuamshe, uniangalie na nilale pembeni yako. Nakupenda kuliko nafsi yangu. Naogopa hata kufikiri kuwa ipo siku nitaamka tena, halafu wewe haupo hapa kifuani kwangu. Naogopa hata kuwaza! Naona ni heri nipoteze hata mikono yangu pia, ili upate sababu yakunihudumia kama hivi ili, niwe na wewe hivi. Niamke ukiwa kifuani kwangu, nilale ukiwa kifuani kwangu. Natamani mimi ndio niwe mwanaume pekee nitakayebaki kukushika mwili wako, sio mtu mwingine.” 

Taratibu akaanza kukumbuka maneno ya Emma aliyomwambia kuna siri kubwa sana ya Kenny, haifahamu. Aliona ampe muda wakuingiza mambo yote akilini na moyoni. Alimuweka vizuri kifuani kwake, akaendelea kumpapasa taratibu mpaka Naih alipotulia wakabaki wamekaa tu pale kitandani.

*******************************

Wakiwa bado wametulia hapo kitandani, simu ya Mama Ole ikaingia. Naih akasimama kwenda kuifuata simu juu ya kabati ya tv. Aliisahau usiku uliopita alipoombwa kupakwa losheti mgongoni. Bado hakuwa amevaa nguo. “Vipi? Bado mmelala?” “Ndio tunaamka. Shikamoo.” Naih akasalimia. Akarudi kutaka kujifunika pembeni ya Kenny, lakini Kenny akamvutia kifuani kwake. “Kuna jambo tunataka kuzungumza na nyinyi wote wawili. Tunaweza kuja sasa hivi?” “Bado sijamuandaa Kenny. Naomba mje kama baada ya lisaa hivi.” “Hamna shida. Kuna kitu chochote mnahamu ya kukila leo? Naweza kupita nikawanunulia, nije nacho.” “Ngoja nimuulize Kenny.” Naih akamgeukia Kenny. “Watakuja baada ya saa moja kuanzia sasa. Unataka wakuletee chakula gani?” Kwa mara ya kwanza Kenny akambusu juu ya mdomo wake, Naih akacheka taratibu.

Alipoona ameridhia, akarudi kunyonya tena midomo ya Naih. Kwa juu tu, kisha akamwachia. Nayo hiyo ni mara yake ya kwanza kupata busu la mdomoni kutoka kwa mwanaume. “Mwambie chochote kizuri.” Kenny akajibu. “Kenny amesema mletee kitu chochote kile kizuri.” Naih akajibu, “Na wewe unataka nini, Naih?” Naih akafikiria kidogo. “Bado ninacho chakula alichotuletea mama. Usihangaike juu yangu.” Kenny akampokonya ile simu na kuizima.

Akamvuta tena Naih na kuendelea kumbusu kwa muda mrefu sana huku akimpapasa taratibu. Safari hii Kenny hakuishia nje. Alitafuta ulini wa Naih mpaka akaupata na kuanza kuchezea taratibu huku mikono yake ikiendelea kumpapasa taratibu huku akimvutia kwake. Raha ile, ilikuwa ikimtoa machozi Naih. Japokuwa hakuwa akijua kitu chakufanya, na Kenny alijua jinsi Naih alivyo mgeni wa mapenzi, alibaki yeye ndio akimfanyia kila kitu. Naih aliendelea kufurahia kila kitu nakushindwa kukataa.

Alijitahidi sana kutokuvuka mipaka kitu kilichokuwa kikimshangaza Naih. “Mbona hamalizii kila kitu!?” Naih alijiuliza huku akigugumia raha ya kupapaswa na mabusu. Kenny akamsogeza pembeni. “Nataka kukuoa Naih.” “Lini?” “Siku yeyote utakapokuwa tayari.” Naih akatulia kidogo kama anayefikiria kitu. “Siwezi kufanya mapenzi na wewe mpaka uwe mke wangu.” Naih akapoa kabisa, akajua inamaana hapo Kenny hataendelea zaidi ya alichomtendea mwilini mwake. Aliamsha tamaa za hali ya juu. Mwili wake wote ulimtaka Kenny.

“Nimekuwa nikichezea wanawake wengi, lakini si wewe Naih. Nataka uwe mke wangu wa halali ndipo nitakuwa huru kufanya mapenzi na wewe.” “Lakini si nitaendelea kulala kifuani kwako?” Kenny alicheka sana. “Kumbe na wewe unafurahia!?” Naih akakubali akiwa kama anayetafakari kinachoendelea. “Na mimi siwezi kupata tena usingizi kama haupo kifuani kwangu.” “Basi tufunge ndoa.” Kenny akamvuta nakuanza kumbusu tena. Walikaa pale kitandani wamekumbatiana, Kenny akichezea mwili wa Naih huku akinyonya midomo yake taratibu bila kuchoka mpaka hodi ya wazazi wake iliposikika.

Naih aliruka kwa haraka kutoka pale kitandani akiwa uchi vilevile, asiamini kama lisaa limeshapita tokea azungumze na mama Ole. Akakimbilia bafuni. Akaoga haraka huku Ole na mkewe wakiwa wanasubiria nje. Akapiga mswaki haraka na kuvaa, ndipo akatoka bila hata kuchana nywele. Akafungua mlango na kurudi haraka chumbani bila hata kusalimia. “Usicheke bwana, Kenny! Twende ukaoge.” “Labda uniache nitulie kidogo. Hebu niangalie. Watajua kilichokuwa kikiendelea hapa.” Naih akafunga macho huku akicheka kwa sauti ya chini. Japokuwa Kenny alikuwa amevaa pensi, lakini wazi alionekana yupo kwenye matamanio makali.

“Twende ukaoge bwana!” “Ukinigusa ndio utaharibu zaidi! Heri niache nitulie kwanza. Wewe endelea kujiandaa, wakati mimi natulia. Au niletee hilo beseni dogo nianze kunawa juu.” Naih alimpigisha mswaki akamuacha akijifuta, wakati na yeye anajiweka sawa. Alikuwa amesuka rasta ndogondogo zenye mawimbi juu. Akaendelea kuziweka sawa nywele zake huku Kenny akimwangalia na kuendelea kujisafisha. “Umependeza Naih. Unazidi kuvutia.” Naih akacheka. “Asante.”

Hatua Ingie.

W

awili hao walitoka pale wakionekana kuna tofauti na wakati mwingine. “Kuna habari gani njema?” Mzee Ole akauliza baada yakuona sura za tabasamu. Wakaangaliana na kucheka kidogo. “Niwaambie?” Kenny akaumuuliza, Naih akatingisha kichwa kukubali. Gafla hofu ikamwingia. Akawatizama Ole na mkewe walivyojaa neema pale! Nyumba nzima ilinukia utajiri kwa wao kuwepo tu pale. Uhalisia ukaingia kichwani kwa Naih. Akakumbuka walivyo tofautiana hali ya kimaisha. “Mimi na Na..” “Labda usubiri kwanza, Kenny.” Naih akamuwahi kabla Kenny hajawaambia wazazi wake. “Subiri kwanza.” Naih akamsihi kwa sauti ya chini kidogo, wazazi wake Kenny wakiwangalia wasielewe kinachoendelea.

Wote walimuona vile Kenny alivyobadilika gafla, mpaka akaanza kuwa mwekundu. Macho yakawa mekundu, mishipa ya damu ikasimama pembeni ya uso. Naih akajua ameshakasirika. Wazazi wa Kenny pia wakajua hata habari njema waliyoleta haitapokelewa tena. Wasiwasi ukawaingia. “Sio kwamba nakataa, Kenny. Labda tungejipa muda.” “Wa nini!?” Kenny akauliza. “Kwa nini tusiongee baadaye, sisi wenyewe kwanza?” Kenny waliyemkuta anatoka chumbani sie huyu. Gafla ile hali ya furaha waliyoikuta mahali pale, ikabadilika pakawa na tension.

Ukweli uwepo wa Mzee Ole na mkewe ulimuogopesha sana Naih na kumkumbusha yeye ni nani na anataka kuolewa na mtoto wa mamilionea. Akaona hakufikiria vizuri. Alikubali kwa haraka bila kufikiria kwa sababu ya ile raha ya kutomaswa tomaswa pale kitandani. Uhalisia ukamkumbusha yeye na mama yake walikuwa wafanyakazi wa ndani tu nyumbani kwa kina Kenny.

“Usikasirike Kenny! Tutazungumza baadaye na utaelewa tu.” “Haina haja Naih. Mimi ninakuelewa kabisa. Sikulaumu. Najua sasa hivi ni ngumu.” “Kenny! Ungenisikiliza kwanza. Sio hivyo unavyofikiria wewe!” “Hamna neno Naih. Hata hivi unavyonisaidia inatosha.” “Kwani kuna nini?” Ilibidi Mama Ole aulize. Wote wawili wakanyamaza.

“Eti Naih? Tunaomba mtushirikishe, labda tunaweza kuwashauri.” Mama Ole akasisitiza kwa tahadhari. “Hamna neno. Yaishe tu.” Kenny akajibu. “Ni mipango tulikuwa tumepanga na Kenny. Lakini nahisi tutakuwa tunaharakisha sana, ndio maana nikaona tusubiri.” “Mimi sijaharakisha Naih. Na wala sijakurupuka.” “Naomba usikasirike Kenny!” “Hapana, nakuelewa.” “Hujaelewa Kenny!” “Nakuelewa.” “Nimeingiwa tu na hofu, lakini sio kwamba nakukataa.” “Hofu ya nini au ndio umekumbuka kuwa utaolewa na kiwete?” “Kenny!!”  Naih akashangaa sana. Lakini  angalau Ole na mkewe wakawa wamejua kinachoendelea.

“Naelewa Nai! Sikulaumu.” “Sio sababu hiyo! Nafikiria hali zetu zilivyo tofauti!” “Hali gani!?” “Mimi hivi nilivyo, sijasoma sana, halafu hata mama yangu hana elimu. Ndio maana nilikuwa nataka nikuombe baadaye kabla hatujawaambia watu, labda nirudi kwanza shule. Nimeshapeleka vyeti vyangu pale CBE, mwakani wameniambia naweza kuanza kusoma madarasa ya jioni. Nipate hata diploma, ndio tufikirie mambo mengine.” Kenny alikunja uso. “Ndio hilo tu au kuna kingine!?” Kenny akauliza kupata uhakika. “Ndio hicho nilitaka tuzungumze kwanza kabla hatujawaambia watu.” “Unauhakika?” “Nihicho tu Kenny. Na mimi nakupenda sana, sina sababu nyingine yakunizuia nisiolewe na wewe.” Naih alishusha sauti akaongea kwa upole.

Kenny alivuta pumzi kama kawaida yake na kuzishusha kama kusafisha kifua. “Jamani! Namuoa Nai.” Kenny aliongea kwa kifupi. “Nampigia simu sasa hivi Jay. Nimtaarifu kama ataweza kuja kwa haraka nataka aje, tunaenda mahakamani kufunga ndoa na Naih, na kuishi naye kama mke wangu. Wala sitasubiri tena.” Naih alitulia akiwa ameinamisha kichwa chini akisubiri kusikia kutoka kwa wazazi wa Kenny. Kimya kwa muda kama wazazi wapepigwa na butwaa.

“Hongereni sana.” Mwishowe mama Ole alijikuta akiropoka asijue ni nini chakuongeza, akanyamaza. “Kwenye harusi yenu, mtapokea zawadi?” Mzee Ole akauliza kwa tahadhari sana. Kenny akatulia kama anayefikiria. “Eti Kenny? Mtapokea zawadi kutoka kwa wageni wenu?” “Sina mpango wakualika watu kwenye harusi yangu na Naih. Watakuja kunisanifu tu, sio kufurahi pamoja na sisi.” Kenny akajibu, na kuzua ukimywa mwingine.

“Je, sisi tunakaribishwa?” Mama Ole aliuliza kwa unyonge na wasiwasi. Kenny akanyamaza. “Naomba usininyime kuhudhuria jambo la muhimu kama hili kwenye maisha yako Kenny. Inawezekana nimekosea sana kwenye kukulea, lakini wewe unajua nakupenda. Nimehangaika sana kwenye maisha yangu ili wewe uishi vizuri, Kenny.” Yule mama akaanza kulia. “Ndio maana nilijitahidi kukupa kila kitu unachokitaka bila yakuchelewa. Mara nyingi nimekuwa nikijinyima kwa ajili yako Kenny. Ukinisusia mali kwa ajili ya madhaifu yangu, utaniadhibu mpaka kifo. Jasho langu litakuwa limepotea bure. Tafadhali Kenny, usinifungie milango mwanangu. Nimehangaika sana kutafuta watoto, lakini nikaishia kwako tu. Sina tumaini wala faraja nyingine hapa duniani ila wewe mwanangu. Kila mtu anajua jinsi ninavyokupenda. Najua hata wewe unajua.”

 “Kama ungekuwa unanipenda, ungejua ni nini napenda, na kujitahidi kutunza vitu ninavyovipenda. Ulimfukuza Naih, wakati ukijua nampenda.” “Nilikosea Kenny. Nilikosa mwanangu. Naomba unisamehe. Lakini nimejifunza. Nitaheshimu maamuzi yako.” Kenny akanyamaza.

“Naih, naomba unisamehe.” Yule mama alikuwa akilia kwa kuombeleza huku akisugua mikono, na yeye akawa mwekundu kwa kulia kama mwanae. “Mimi sina tatizo na wewe Mama Ole. Nilijua lazima pale tungeondoka tu. Kwanza mama hakuwa akiweza kuendelea na kazi, halafu ugomvi na wizi wa wadogo zangu ulizidi. Hata ingekuwa mimi nahisi ningewafukuza tu. Hapakuwa na jinsi yakuendelea kutuweka pale. Na wala sio wewe tu uliyetufukuza nyumbani kwako. Mama anafukuzwa nao kila nyumba anayoenda kuishi nao na wanamwibia kila siku. Hata ile pesa uliyomlipa mama, hakuifaidi. Nilienda kuichukua benki, nikanunua godoro, nikamkabidhi  mama. Baada ya siku mbili wakatoroka na ile pesa yote."

"Kwa hiyo kwa hilo sina lawama. Nilijua pale sio kwetu, sisi niwafanyakazi tu. Ila kilichoniumiza ni pale ulipoweka sharti la kutowasiliana na Kenny. Tena hukunipa sababu yeyote ile yakueleweka wakati ulijua mahusiano yangu na Kenny. Hicho tu ndicho kiliniumiza, sio mengineyo.” “Naomba unisamehe Naih na tafadhali naomba yaishe. Nilikosea.” Hakika yule mama alihitaji msaada wa Naih ili kumpata mwanae.

“Binafsi nimesamehe na ninakushukuru kwa kuniombea pale hospitalini kuwa na Kenny. Najua haikuwa ikiruhusiwa. Yule mshauri wa Kenny alitueleza kuwa ni kitu ambacho hakiruhusiwi kabisa, lakini alisema ulihangaika mpaka mimi nikaruhusiwa kuwepo pale. Asante.” Kidogo Mama Ole akafurahia. 

“Najua na Kenny naye amesamehe. Si ndiyo Kenny?” “Naih! Kwa nini unanilazimishia kusamehe?” “Kwa sababu huna sababu yakuendelea kukasirika bwana. Yaishe tu ili kuleta amani.” Kenny akanyamaza.

“Unakumbuka mimi baba yangu alinikimbia? Hakuwahi hata kurudi kuniangalia! Na mama aliambiwa na masai wenzake alirudi, anaishi hapahapa Dar, ila alirudi na mke wake mwingine wa kimasai. Hajawahi hata kukosea njia kuja kunisalimia.” Naih alijikuta akiongea kwa uchungu. “Kupata watu wanao kuhitaji maishani ni bahati Kenny. Mpaka hivi leo tunavyozungumza, wadogo zangu hawanipendi na wala hawanitambui kama mimi ni ndugu yao. Nimebaki na mama tu. Usikubali kuwa peke yako. Sio vizuri.” Kenny akamuhurumia Naih na kujirudi.

“Pole Naih. Basi yameisha, ila sasa hivi tunaishi kwa vile ninavyotaka mimi. Sitaki mnifanyie mambo nisiyoyajua. Kila kitu lazima mniulize na nikubali ndio mfanye.” “Sawa.” Mama Ole akajibu kwa haraka sana. “Hamna shida kabisa.” Mzee Ole naye akaafiki. Wakatulia kidogo.

Wakashangaa mama Ole anaanza kucheka. “Nini?” Mumewe akauliza. “Sasa mipango ya harusi inakuaje?” “Usianze mama! Nimekwambia nataka harusi ndogo tu.” “Wewe nitajie watu wako unaowataka wahudhurie hiyo harusi, na mimi nitakupa majina..” “Hapana mama! Sitaki marafiki zako.” “Nisikilize basi Kenny. Nakupa orodha ya wageni wangu. Kama huwataki, sitawakaribisha.” “Unataka kuanza mambo mengi, maandalizi marefu halafu nishindwe kuoa haraka. Nataka kuanza kulala na Naih kama mke wangu. Siwezi kusubiri.” Kenny aliongea bila aibu, Naih akainama. Wazazi wake wakaelewa.

“Mimi nina wazo. Naomba kushauri.” Mzee Ole akaingilia. “Naruhusiwa?” “Sitaki ushauri wakusubiri. Kama ni huo, sitaki.” “Hapana Kenny, sio huo.” Kenny akatulia. “Jambo tulilokuwa tukitaka kuwambia ni kuwa, tumepata hospitali huko nchini India, ina uwezo wa kukuwekea miguu ya bandia na ya kisasa. Ndani ya majuma 3 mpaka 6, utakuwa na uwezo wa kutembea kabisa.” “Kwani miguu ya MOI ina tatizo gani? Sitaki mambo ya gharama mimi.” Kenny akakataa hapo hapo

“Hawana miguu mizuri na ya kisasa, Kenny. Tumekuwa tukifuatilia, tumepata miguu mizuri sana, itakayokufanya wala usione tofauti ya miguu yako na hiyo ya bandia. Tutagaramia garama zote. Kuanzia matibabu, malazi yenu kwa huo muda mtakao kuwa huko mpaka upone.” “Inamaana nakwenda na Naih?” “Tena safari hii unaenda naye kama mkeo.” Kenny akacheka kidogo. Wakajua ameridhika.

“Tuendelee kama ulivyosema Kenny. Twendeni mahakamani, mfunge ndoa. Mkitoka hapo muende nchini India kwa mapumziko na matibabu. Kenny akirudi hapa anakuwa na miguu yake, halafu tunawafanyia sherehe kubwa.” Hapo wakawa wamemfurahisha Kenny.

“Unaonaje Naih?”  Kenny akauliza. “Sasa hukusu shule?” “Bwana Naih! Shule ya nini tena? Kwani lazima usome? Unaigiza kila kitu mpaka mambo ambayo hayana maana! Unauwezo mkubwa sana wakusimamia mambo na kupangilia. Tukitoka huko tunarudi kazini, achana na mambo ya shule. Wenzako wanasoma ili waje kuwa kama wewe. Yaani wawe na uwezo mzuri wakufanya kazi kama wewe. Unataka kupoteza muda bure! Tuoane tuanze kuzaa watoto wengi kama tulivyokuwa tukitamani.” Naih akacheka kwa wasiwasi.

“Na ninaomba unisikilize mimi, sio kuanza kufikiria wazazi wangu watakuonaje! Hutaishi na wao, utakuwa ukiishi na mimi. Mimi sitaki urudi shule, nakutaka uwepo kwenye maisha yangu. Achana na mambo ya shule, tujenge maisha yetu.” Naih akabaki amenyamaza. “Sawa Naih? Tunajenga maisha yetu mimi na wewe. Kenny na Naih sio sisi na mama Ole au mzee Ole. Tunajipanga sisi wenyewe. Ni sawa?” Naih akatingisha kichwa kukubali. Kenny akavuta kigari chake mpaka pale alipokuwa amekaa Naih, upande wa meza ya kulia chakula. Akamvuta mkono akitaka akamkalie pale kwenye wheelchair yake. Naih akasimama na kwenda kumkalia. Kenny akamkumbatia, na kumbusu mgongoni mara kadhaa mpaka Naih alipomgeukia na kumbusu midomoni.

“Asante Naih.” Kenny akanong’ona. “Na mimi nimefurahi. Kwa hiyo lini ndio tunafunga ndoa?”  Naih naye akamuuliza kwa sauti ya chini. “Ngoja nimpigie simu Jay, nijue kama anaweza kufika sasa hivi au kwenye hiyo tafrija itakayofanyika baada ya kutoka India. Akisema hataweza kuja sasa hivi, basi nitamuomba baba akatuulizie mahakamani utaratibu unakuaje, kesho twende.” “Kweli?” Naih akashangaa sana. “Mimi nipo tayari Naih. Nakuhitaji sana.” “Hata mimi Kenny.” Naih akamnong’oneza sikioni, Kenny akacheka. “Basi naomba uniletee simu yangu nizungumze na Jay.” Naih akatoka.

“Sina haja yakwenda mahakamani. Naweza kupiga simu sasa hivi na kuweka mipango yote sawa.” Mzee Ole aliongeza. “Basi ngoja nizungumze na Jay kwanza.” Naih akarudi na simu, akampigia Jay. “Kwema?” Jay akauliza. “Kwema. Tunataka kufunga ndoa na Naih.” Wakamsikia Jay akicheka. “Umembana mtoto wa watu mpaka kakubali!” Kenny akacheka. “Utakuja sasa?” “Ngoja nizungumze na mke wangu kama atataka tuje naye na kama daktari wake atamruhusu kusafiri na ujauzito wa muda huu. Kama daktari wake akiona sio sawa kusafiri, mimi nitakata ticketi leo, kesho niondoke.” “Sawa, zungumza naye basi unijulishe sasa hivi ili niendelee na mipango. Nataka kuoa kesho lakini.” “Si unajua kwa kesho mimi sitaweza, Kenny. Labda kama utanipa siku ya kesho na kesho kutwa.” Kenny akatulia kidogo. “Kenny!” “Nafikiria.” “Kama utaona mbali, nyinyi endeleeni tu, tutakuja kuwapa pongezi wakati mwingine.” “Ngoja nizungumze na Naih. Nitakupigia tena.” Kenny alishakosa raha.

“Siku tatu sio nyingi Kenny! Najua hutafurahia kama Jay hatakuwepo. Tusubiri tu.” Naih aliongeza mara baada ya Kenny kukata simu. “Mnaweza kutumia hizo siku kujiandaa na safari. Mimi nishugulikie mambo ya hospitalini. Karatasi zote zakuombea Visa, na za kuwapelekea madaktari wa huko. Pia tunaweza kuzunguka madukani kuona kama Naih anaweza kupata gauni zuri yakuvaa siku hiyo ya kufunga ndoa yenu.” “Na mimi naweza kukupeleka ukatafute suti utakayovaa siku ya harusi yako, Kenny.” Mzee Ole aliongeza kwa mkewe. “Siwezi kwenda sehemu yeyote bila Naih. Lazima niwe na Naih.” Kenny akaweka msisitizo. “Basi tuongozane.” Mama Ole akashauri tena. Wakakubaliana, Kenny alimpigia simu Jay na Emma. Wakakubaliana baada ya siku tatu ndio harusi.

Nguvu Ya Pesa.

Baada ya chakula pale nyumbani kwa Naih, walitoka wote wanne. Njiani Mzee Ole alimpigia rafiki yake ambaye ni hakimu, wakapanga mambo yao vizuri, wakakubaliana siku ya ijumaa ndipo watafunga ndoa hiyo. “Vipi? Mbona huna raha tena?” Naih na Kenny walikuwa wamekaa kiti cha nyuma kwenye gari ya mama yake Kenny ambayo ipo chini kidogo. Naih akamvuta mkono. “Niambie.” Naih akamnong’oneza. “Nilikuwa natamani siku ya harusi yangu nikubebe! Lakini hebu nione!” Naih akacheka. “Utanibeba mpaka utachoka. Ngoja upate miguu mizuri. Mwenzio ninafuraha.” “Nakuona. Huogopi kuja kujuta?” “Hata kidogo.” Naih akajibu huku akicheka. Angalau akamtoa Kenny kwenye mawazo wakaanza kuzungumza wakicheka wao tu, hapo nyuma, mama Ole akiendesha, kimya bila kutaka kuchangia neno hata moja.

Walifika hospitalini, wakashugulikia makaratasi yote, kwa ajili ya kumpelekea daktari huko nchini India kwa matibabu zaidi. Wakaondoka kwenda madukani. Mpaka inafika jioni, wakawa wamepata nguo za kuvaa siku hiyo ya kufunga ndoa yao.

Mama Ole akawaambia waende sehemu wakapate chakula cha usiku pamoja. Kenny akakataa. Mzee Ole akaamua waende wakanunue, lakini waende kula nyumbani kwa Naih. Wakafanya hivyo na kurudi nyumbani kwa Naih. Wakati wanakula, mama Ole akaamua kuvunja ukimya.

“Baada ya kufunga ndoa siku hiyo mlitaka kufanya nini?” “Si tunarudi nyumbani?” Kenny alijibu akiwa na swali juu. “Hamtaki hata kwenda mahali tukapata chakula cha usiku pamoja?” “Umeanza mama! Unataka shuguli nyingi! Mimi sipo huru kuzunguka au watu kuniona hivi nilivyo.” “Basi. Hamna shida.” Mama Ole akatulia kidogo kisha akarudia tena kutoa pendekezo jingine. “Ungependa nije kumchukua Naih, nimpeleke saluni? Angalau akatengenezwe kidogo.” “Na mimi nitabaki na nani!?” Kenny akauliza kwa kushangaa.

“Mbona mnataka kuanza kuninyima raha jamani? Naih akiondoka nitabaki na nani? Maisha yangu yanakuaje? Hiki ni kitu kidogo tu lakini mnataka kukikuza!” “Basi Kenny. Basi baba. Nilitaka kusaidia tu.” “Unasaidia kunitenga na Naih!?” “Basi.” Tayari alishakasirika, Naih akamtizama. “Nini?” “Nafikiri na wewe unahitajika kukata hizo nywele, Kenny. Unataka nikusindikize saluni kabla ya hiyo siku ya ijumaa?” “Kwa nini tusilete kinyozi na mtu wa kumtengeneza Naih hapahapa nyumbani?” Mzee Ole akatoa wazo kabla Kenny hajajibu swali la Naih.

“Nilikuwa nikifikiria kuwachukulia chumba hotelini. Ili mkapumzike huko baada ya harusi yenu. Mnaweza kwenda huko kuanzia asubuhi, hao watu wakaja huko kuwatengeneza wote mkiwa pamoja, ndipo tukaenda mahakamani ili angalau mpate picha nzuri kwa ukumbusho hata kwa watoto wenu. Ni wazo tu, sio lazima.” Mama Ole alikuwa na furaha, hakuweza kujizuia. Alikuwa akitoa maoni yake, bila kuchoka.

“Eti Kenny, mwanangu?” Mama Ole akamuuliza akibembeleza. “Mimi sitaki kuhudumia na watu wengine. Naogopa wasinione mzigo. Naih ananijulia. Naogopa Naih akiondoka halafu nikaachwa peke yangu na mtu baki. Kama nitakuwa na Naih, sina shida ya kwenda popote.” Kidogo hilo likapita, pakatulia.

Mama Ole akaanza tena. “Sasa mtaagana na wageni wenu palepale mahakamani?” Kenny akatingisha kichwa. “Mama akitaka jambo lake! Haya sema wewe shida yako ni nini!” Mama Ole akacheka. “Nafikiria hivi.” “Nilijua tu unamipango mingi!” Kenny akamkisha. “Sio mingi Kenny. Mkishafunga ndoa, tukae mahali tule chakula pamoja. Tufurahi na kumshukuru Mungu pamoja na hao wageni wako.” “Na wako?” Kenny akauliza akijua kabisa nia ya mama yake. “Wangu hawatakuwa wengi sana. Hawawezi kuzidi 35.” “Haa! Wote hao!?” Kenny akashangaa.

“Kila siku tunakuwa tunaalikwa kwenye maharusi ya watu. Sisi hatujawahi kualika hata mara moja! Nakuomba Kenny mwanangu, uturuhusu hao watu wakaribu tu. Sitaifanya kubwa sana. Tutaifanya bustanini, tena kwenye moja ya hiyo hoteli mtakayopumzika na Naih mpaka siku mnaondoka. Mkirudi sasa ndio hapo tutafanya kubwa.” “Yaani mama bwana! Mimi sikutaka hekaheka kabisa. Unaharibu mipango yetu yote!” Kenny akalalamika. “Katoto kenyewe kamoja tu Kenny, mwanangu! Si na wewe utakuwa baba, utaona.” “Basi mama. Wewe fanya vile unavyotaka bwana. Lakini ujue huo haukuwa mpango wangu kabisa.” Mama Ole alifurahia sana.

“Twende Ole tukaanze kuandaa harusi. Kesho tutakuja kuwachukua tuwapeleke kwenye kuomba Visa, tukitoka hapo, hamtarudi tena hapa. Tunawapeleka kwenye hiyo hoteli, Naih aanze kushugulikiwa. Mpaka inafika ijumaa unakuwa umependeza. Tutaongeza gauni moja la kuvaa jioni kwenye tafrija, na..” “Mama! Mama!” Kenny akamkatisha mama yake. “Wewe nenda kapange mipango yako nyumbani kwako, halafu endelea tu. Tumekuruhusu. Naona tutaanza kuchoka kabla hata ya siku yenyewe.” “Asante mwanangu.” Akamkumbatia Kenny na kumbusu.

“Sasa Naih wewe unapenda rangi gani kwenye harusi yako.” Naih alikuwa akicheka vile mama yake Kenny alivyojawa na furaha. “Yeyote ile, sikuwa hata nimefikiria.” “Basi niachie mimi. Tena naona hamna haja ya kwenda mahakamani. Huyo mfungisha ndoa atakuja palepale bustanini. Anawafungisha ndoa, akimaliza, tunapiga picha. Wakati mnaenda kubadili nguo na kupumzika kidogo, palepale panageuzwa viti, panapangwa tayari kwa tafrija. Itakuwa ni shuguli ndogo sana. Nitajitahidi isizidi watu 50.” “Mama!” “Hao ni wageni wangu na wako Kenny.” “Mbona mimi wangu ni wachache sana. Wanaweza hata wasizidi 6. Emma, Jay na mkewe, Mama yake Naih, na wadogo zake kama watataka basi.” “Tye lazima awepo, na wale marafiki zako waliokuwa wakija kukuona hospitalini. Mama Semka, atanilaumu sana kama nikimnyima harusi yako. Halafu na..” Naih na Mzee Ole walikuwa wakicheka tu.

 Mama Ole alibadili mpango mzima, kile kitu kidogo alichotaka kukifanya Kenny, tayari kilibeba sura mpya. “Sasa kama unaalika rafiki zako hao wote, hiyo sherehe nyingine tukitoka India itakuaje?” Kenny akauliza. “Hapo ndipo nitaalika sasa na wafanyakazi wenzangu wale tuliokuwa tukifanya nao kazi wizara ya fedha, na wateja zangu. Nakuahidi hiyo nayo haitakuwa kubwa sana. Nitachukua ukumbi mdogo tu.” “Mama jamani! Mimi mambo ya ukumbini unajua huwa siyapendagi!” “Wewe usijali. Si umeniachia mimi? Wewe angalia afya yako na Naih. Kila kitu nitafanya mwenyewe.” Kenny akaamua amuache tu.

     Sehemu ya 6.

     Harusi ya Naih & Kenny

T

ayari Kenny, Jay, Emma pamoja na mkewe huyo mwenye asili ya kizungu, mjamzito, walikuwa wamewasili mbele kabisa sehemu hiyo maalumu ya kufungia ndoa yao, wakimsubiri Naih. Mama Ole alikodisha sehemu ya nyuma ya hoteli hiyo ambayo


ilikuwa ufukweni kabisa wa bahari. Kenny na Naih walikuwepo hapo hotelini kwa siku mbili. Akakodisha wapambaji wakapatengeneza sehemu hiyo iliyomtoa Kenny macho. Alitoka hapo akiwa anasukumwa na Jay ambaye yeye na mkewe ndio waliokuwa wasimamizi wa harusi hiyo, akabaki ametoa macho. “This is so beautiful, mama!” Kenny aliongea kwa kunong’ona wakati anaingizwa mahali pale na kuvutiwa vilivyo! Hakutegemea. Mama yake akacheka, akamkonyeza aende pale.

Kwa kuwa alikuwa amekaa na baba yake, wazazi wa kina Jay na rafiki zake wengine, wakasimama wakati Kenny, Emma, Jay na mke wa Jay wanawasogelea. “Asante mama. Sikuwa najua kama kitu cha muda mfupi, kinaweza kutayarishwa kwa haraka na kuwa kizuri hivi! Asante sana.” Mama yake aliinama pale kwenye wheelchair aliyokuwa amekaa, akamkumbatia na kumbusu. “Utanipaka lipustiki yako mama, bwana!” Wote wakacheka.

Jay akamsukuma kumtoa pale bila hata kuwasalimia wazazi wao wala kumtambulisha mkewe. Wakaenda kusimama mbele kabisa alipokuwa amesimama mfungishaji ndoa wao. Kenny alikuwa amekatwa nywele vizuri, na alivaa suti nzuri nyeusi. Na uzuri aliokuwa nao, ni kweli alipendeza. Jay na Emma nao walivaa suti nyeusi kama Kenny, na mke wa Jay ambaye ndio msimamizi wa Naih, alivaa gauni la kawaida tu la rangi ya pinki na ujauzito aliokuwa nao, dada huyo wakizungu akapendeza. Wakabaki wamesimama pembeni ya Kenny. Ila vile Jay alivyokuwa akizungumza naye na kutaka kujua kama yupo sawa na wakati fulani kumshika tumbo, hata wazazi wa Jay wakajua ndio mkewe ila wakashangazwa maana taarifa ya mwisho kutoka kwa Jay ni kushindwa hata kulala na mkewe. Wakatulia hapo mbele na vicheko vya hapa na pale vikiendelea.

Kinanda kilianza, ndipo Kenny akajua kuwa kuna mpiga kinanda pembeni. Akamgeukia mama yake, akatingisha kichwa. Mama Ole akacheka. Watu wakasimama, akapita mtoto aliyekuwa akimwaga maua, akafuata mtoto mwingine aliyekuwa ameshika mto mdogo tu, maalumu kwa kubebea pete. Naih akawa anaingia akiwa na mama yake. “Waw!” Kenny akasikika akishangaa, akataka kusimama, akakumbuka hana huo uwezo. “Amependeza sana. Asante mama.” Kenny alijikuta akizungumza kwa sauti. Alishindwa kujizuia. Watu wakacheka.

Juu ya mchanga huo, katikati ya viti, kulikokuwa kumeachwa barabara pana kiasi, kulitandikwa kapeti nzito ili kufanya kigari cha Kenny, wheelchair kupita kwa urahisi. Yule mtoto alimwaga maua mengi mpaka pale alipokuwepo Kenny, tayari kwa Naih kupita juu ya yale maua. Naih alikuwa amevaa shela ndefu kutokea kichwani, ikaanguka mpaka miguuni ikatambaa. Alivaa na gauni zuri, jeupe kama theluji, lilimkaa vizuri sana na kumfanya kuvutia. Na kwakuwa aliku mweusi, na ile rangi ya gauni Naih akazidi kupendeza na kuvutia kumtizama kule ndani. Lilionekana iligharimu vya kutosha mpaka kufika hapo mwilini kwa Naih. Halikuwa refu sana, lakini iliweza kufika kwenye viatu na mbele lilikuwa fupi zaidi ili kumfanya aweze kutembea kwa uhuru.

Walimtengeneza nywele vizuri, na hakupakwa vitu vingi usoni. Kwa hiyo sura yake ikabakia vilevile. Hereni zilizokuwa zimejaa kwenye sikio, zilionekana ni alumasi iliyokatwa vizuri, na iliendana na mkufu wa shingoni. Hata Kenny hakuwahi kumuona Naih wa namna ile. Wote na kina Emma walibaki wametoa macho kadiri Naih alipokuwa akiwasogelea akiwa na mama yake. “Mama umependeza, sio mchezo!” Emma alishindwa kujizuia, wote wakacheka mpaka Naih mwenyewe.

****************************************

Pesa iwapo sehemu, huwa haina mtindo wa kunyamaza. Popote ilipo huwa inapiga kelele. Kenny alitangaza kuoa, lakini ndani ya siku tatu tu, kila kitu kilikamilika. Ole na mkewe walipata nafasi yakuonyesha utajiri wao hapo. Naih alivalishwa na mama Ole, alumasi ya ukweli. Gauni yenyewe aliyokuwa amevaa, ilimgarimu sana mama huyo. Na aliibadilisha ili Naih aweze kutembelea hata akiwa anamsukuma Kenny. Nywele ya Naih ilisukwa siku iliyopita, ilikuwa ni ya gharama sana. Hata siku hiyo ya harusi walipokuja kumtengeneza hiyo nywele, haikusumbua.

Kwa weusi aliokuwa nao, na kwa kuwa hakuwahi kuweka vipodozi usoni, Mama Ole alimshauri mtu aliyekwenda hapo hotelini kumtengeneza asimuweka vipodozi vingi, lakini ile nywele iliyokuwepo kichwani, mpambaji aliitendea haki. Saluni ilihamishwa hapo hotelini, kuanzia asubuhi hiyo, Naih alikuwa akitengenezwa, wakati Kenny yupo na kina Emma.

Maua yaliyokuwa yanamwaga hapo, na yote yaliyokuwa yamepambwa hapo yalikuwa maua ya rose, tena ya asili. Sehemu hiyo ya bustani, ilipambwa kwa unadhifu sana. Wapambaji wa eneo hilo walionekana walikuwa ni wataalamu kwelikweli. Hata vitambaa vilivyokuwa vimefunika hivyo viti na meza, vilionekana ni vitambaa vyenye hadhi. Waalikwa wenyewe, waliokuwepo hapo, wote walionekana ni watu na pesa zao. Tena pesa zinazoeleweka. Kwa aina ya magari yaliyokuwa yameachwa huko nje, na askari waliokuwepo wamezagaa hotelini hapo siku hiyo, hata wahudumu walijua wateja wao wa siku ile walikuwa sio wa hali ya chini.

Habari ya kuwa Kenny Olendekai anaoa, zilienea jijini na kuamsha shauku kutaka kumuona huyo mwanamke, kwanza aliyebahatika kumtuliza Kenny, na pili kumpokea akiwa mlemavu. Kwa hiyo kukawa na ulinzi mkali sana kwenye hoteli hiyo. Kuanzia chumbani kwa Naih alikokuwa akipambwa, mpaka alipokuwepo Kenny, Emma, na Jay. Walijaa askari kanzu kila mahali wakihakikisha asiye na kadi hawezi kupenya hapo. Wachukua video na wapiga picha, walishakaguliwa kuhakikisha ndio wenyewe waliolipwa maalumu kwa kazi hiyo, sio mapaparazi wa magazeti ya udaku yaliyoendelea kusambaza habari za Kenny. Kila muhudumu wa siku ile pia walipata muda na mama Ole kuwaambia nini anataka na kutarajia kwa siku ile.

****************************************

Haikuhitaji kujua kama Naih ndio ameaga umaskini gafla. Alikuwa amependeza sana. Alimsogelea Kenny na kumshika mikono huku akicheka. “Umependeza sana Naih.” “Na wewe umependeza sana. Kama sio wewe!” Kenny akacheka. “Utundu mpaka siku ya harusi!” “Hapa ninafuraha Kenny, hamna mfano.” Naih alinong’ona na kumfanya Kenny azidi kucheka. “Nakuona, meno yote nje tu!” Wote wakacheka. “Ila umependeza sana.” “Asante. Kazi ya Mama Ole hii.” “Mama umepania!” Jay akamchokoza Naih. “Si kidogo. Hapa naona wananichelewesha mimi.” Wakacheka sana pale mbele. Marafiki hao wanne tokea watoto, wakajikuta wameshatengeneza duara lao nakuendeleza stori pale mbele za watu bila habari, mpaka wakashtuliwa. Naih alishajisahau kama yeye ni bibi harusi. Alikuwa akicheka tu kwa sauti.

Haikuhitaji kujua kama Kenny na Naih ni wapenzi wasio na unafiki. Walijuana na kupendana. Kwa kuangaliana tu, walijua kila kinachoendelea kwa mwenzake. Waliangaliana kwa upendo, hata wazo kuwa anaolewa na mlemavu, halikuwa likipita kichwani kwake. Alijikuta ametoka kwenye upendo wa zamani aliokuwa nao kwa Kenny, na kuzama kwenye mapenzi kwa Kenny aliyekuwa akimtegemea kwa asilimia zote. Hata siku hiyo alikuwa akijiuliza aliishije bila yeye, wakati wanamtengeneza. Alijua atamkuta amenuna, lakini alimkuta Kenny aliyechangamka.

Ndoa ilifungwa, Naih akashangaa anamvalisha Kenny pete ambayo hata hakuwa anajua 


aliyeitengeneza ni nani na lini! Ilibeba alama za Infinity. Na yeye akavalishwa pete mbili kwa mpigo. Ya uchumba iliyokuwa imebeba jiwe kubwa la alumasi nzuri, na ya ndoa iliyotengenezwa kwa alama zile za Infinity. Naih alibaki amekodolea macho kidole chake. “Umependa?” Kenny akamuuliza. “Sana
tu. Umetengeneza lini?” Walinong’ona. “Tunatakiwa tukiss Naih.” Kenny alibadilisha mazungumzo, wakacheka. Naih alikuwa amepiga magoti wakati wakipeana viapo hivyo, ili kumfikia Kenny. Walikuwa wakicheka kila wakiangaliana. 

Utoto uliwajaa, na sasa wanamethibitishia umma, kwa kuweka mwangani kiapo walichopeana wakiwa watoto. Akajisogeza karibu na Kenny, wakaanza kupeana mabusu. Baada ya muda kidogo, Naih akaamua kukaa kabisa mapajani kwa Kenny pale pale kwenye wheelchair na kuamsha vicheko. Waliendelea kupeana mabusu, bila kuchoka. “Mimi naona inatosha jamani!” Emma alimsukuma kwa nguvu Kenny mgongoni, “Nini bwana?” Kenny akauliza. “Inatosha Mzee! Hammalizi! Hapa ilikuwa ni kidogo tu kama ishara ya kuwa mmekuwa mwili mmoja. Kidogo tu, kwa heshima, sio mpaka wazazi waondoke!” Jay aliwafanya Kenny, Naih na Emma wacheke kwa sauti. Ulijaa utani pale mbele, walimuona mfungisha ndoa akicheka mara kwa mara. Kila kitu walikifanyia utani. Vijana hao watatu, akiwepo na Naih, waliokuwa  wamekuwa pamoja na kulelewa kwa karibu sana na mama yake Naih, walijuana vizuri sana. Hakuna aliyeweza kujibaraguza kwa mwenzie.

Ahadi Ni Deni.

Baada ya kufunga tu ndoa, wakati watu wakisalimiana Naih akainama na kumnong’oneza, Kenny. “Sasa si ndio tunaenda?” Kenny hakuwa ameelewa. “Mama ameandaa chakula cha usiku, tule pamoja na wageni wetu!” “Bwana Kenny!” Naih akamsukuma kidogo begani huku amekunja uso. “Sijaelewa!” “Si uliniambia mpaka tuone ndio, yaani vile kama vya juzi usiku.” Kenny alianza kucheka. “Twende mara moja. Tujidai unaenda kujisaidia.” Kenny alikuwa akicheka mpaka machozi.

Kila walivyokuwa wakitaka kuondoka, ndivyo watu walivyozidi kuwasogelea na kuwapa pongezi. Naih alianza kuchukia, huku akitoa tabasamu kila anapopewa mkono wa pongezi. Kila Kenny alivyokuwa akimtizama mkewe jinsi alivyo na haraka ya kuondoka pale akapewe haki yake, na watu wanavyozidi kuwasogelea na kuwaongelesha, Kenny alizidi kucheka. Wageni hawakuwa wakielewa, lakini Kenny alijua lile tabasamu la mkewe, limejaa chuki ya kucheleweshwa kwenda kupewa haki yake. Kila Naih alivyojitahidi kusogea, ndivyo watu walivyozidi kuwasogelea.

Akasogea Jay na Emma. “Nyinyi sitawavumilia kwakweli. Naomba mtupishe kuna mahali tunawahi.” Naih aliongea huku akimsukuma Emma, aliyetaka kumpa mkono Kenny, aliyekuwa akicheka mpaka machozi. “Wewe vipi Kenny? Kwani na wewe Naih mnaharaka ya kwenda wapi?” “Bwana Emma wewe vipi? Unakuwa kama mtoto mdogo!?” Jay akaanza kucheka. “Naomba mtupishe.” “Si usubiri Naih? Uchu gani huo?” “Jay! Naomba utuache.” “Kwani hawa vipi?” Bado Emma hakuwa ameelewa. “Huelewi nini sasa na wewe? Unazidi kutuchelewesha bwana. Wewe subiri, tunarudi sasa hivi.” Wakati Naih ndio anafanikiwa kuwatoa njiani Jay na Emma, wazazi wao wakawasogelea kuwapongeza.

Kenny alishindwa hata kuongea, kila akimwangalia Naih, alizidi kucheka. Jay na yeye akaungana na Kenny kumcheka Naih. “Mmefurahia nini?” Mama yake akauliza. “Wala sio kitu cha maana! Nashangaa kwa nini wanacheka! Sijui kwa nini wamegoma kukua hawa!” Naih akajibu akiwatizama Jay na Kenny. “Kweli sio kitu cha maana Naih? Basi siendi.” Naih alibaki akimwangalia Kenny. “Mnataka kwenda wapi tuwasindikize.” “Hapana Mama Kenny. Usitusindikize. Nitampeleka tu mimi mwenyewe.” “Wapi?” Naih alibaki hajui amwambie nini mama mkwe wake, Kenny akazidi kucheka akisaidiwa na Jay akaongezeka na Emma. Naih akamfinya mgongoni, Kenny akastuka sana nakuzidi kucheka.

“Ulisema nikusindikize wapi tena?” Naih akamuuliza Kenny. “Mimi sina ninapotaka kwenda tena, Naih. Nimegairi.” Kenny alijibu huku akiendelea kucheka. “Ni lazima ukajisaidie kabla tafrija haijaanza, Kenny. Lazima. Twende.” Naih akasimama nyuma ya wheelchair yake na kutaka kumsukuma. “Nafikiri ni muda mzuri na wewe ukabadili nguo kabisa kwa ajili ya tafrija. Nitamwita yule dada aliyekupamba awafuate hukohuko chumbani akutengeneze tena.” “HAPANA!” Naih alijikuta anaropoka, nakumfanya Kenny, Jay na Emma wazidi kucheka mpaka wakainama.

Naih hakutaka kuingiliwa kabisa kwa wakati ule. Alitaka Kenny akamalize safari aliyomwonjesha na kumwambia atamalizia siku akiwa mkewe. Sasa ashakuwa mkewe, hakuta kusubiria tena. “Namaanisha asante, lakini alishanifundisha jinsi ya kujirudishia hizi nywele mwenyewe. Sitaki kumsumbua. Atakuwa amechoka sana.” Naih aliendelea kujieleza mbele ya wazazi hao. “Hapana bwana Naih. Ngoja nikamwite. Yupo kazini hapa. Lazima akakutengeneza. Ataenda kupumzika kwake.”  Emma alijibu na kutaka kuondoka, Naih akamganyaga kwa nguvu na kumvuta koti. Mama Ole hakuwa ameelewa kabisa. Kenny, Emma na Jay walikuwa wakimcheka sana Naih, na Naih alionekana amekusudia kuondoka pale. “Mimi naona mngewaacha tu waende.” Mzee Ole akawa ameshaelewa. “Asante Baba Kenny.” Naih alijikuta akimshukuru mtu mmoja aliye upande wake. “Hata mimi nashauri uwaache tu waende. Watakuwa sawa.” Mama yake Emma na Jay aliongeza.

Bila kupoteza muda, Naih alimvuta Kenny na kumsukuma kwa haraka zote. “Kweli mama umekusudia! Umevuka vipingamizi vyote!” Kenny akaendelea kumtania akicheka. “Pongezi gani haziishi! Watu wazima wanakuwa kama watoto! Usiku huu ni wetu, waache fujo. Tena watulie kabisa.” “Kwani lazima iwe sasa hivi, Naih?” “Sasa hivi na baadaye pia.” “Usiku kucha!?” Kenny aliuliza huku akicheka. “Si kwa raha ile uliyonionjesha juzi usiku. Nimekaa nawaza tu sina raha! Nilipenda vile ulivyokuwa unaninyo…” Wakashtukia Zai na Mia wamewasogelea wanacheka kwa sauti za kejeli.

Wakakimbia na kusimama mbele ya wheelchair ya Kenny, kama kuwasimamisha huku wakicheka sana. Walikuwa wanacheka huku wameshika glasi za waini{wine} mkono mmoja na mwingine wakigonga. Naih akasimama akabaki akiwatizama. 

Adui Wa Mtu, Ni Wa Nyumbani kwake!

M

ia akaanza. “Wameamua kukukabidhi mzigo wao, moja kwa moja, ukahangaike naye mbele ya safari!” Mia aliongea na kumfanya Vai acheke mpaka ajimwagie wine. “Yaani Kenny, kiboko! Uzima wake kahangaika na wanawake wengine wee, mchana na usiku. Sasa hivi mlemavu ndio kaona nani mjinga, limbukeni atakayekubali kufa na mimi, akaona huyu bi dada ndiye atakayemfaa.” Vai akaongeza. “Ila Kenny ujue mnaakili sana wewe na mama yako?” Vai akauliza kwa kejeli kama anayewapongeza. “Sanaa. Yule mwanamke alimfukuza Nai kama mbwa, enzi za ujana na uzima wa mwanae. Lakini hebu waangalie leo!” “Wamenyimwa aibu hawa watu!” “Lakini hata Kenny mwenyewe, ni mwanaume. Alikuwa anaenda kwa wanawake zake wakati ule ana miguu yake yote miwili, anamuacha Nai pale kwao kama kufuli kwenye mlango! Mchafu mbwa nyuma. Sasa hivi eti ndio anajua Nai ndio mwanamke wa kuoa!!” Wakazidi kucheka kwa sauti kama mazuri.

 “Unacheza na wanawake wa mjini. Hawataki shida. Mzigo huyo, unaupeleka wapi?” “Basi kama namuona bi dada sasa hivi anavyohangaika kumgeuza. Usiku kucha ukute halali. Geuza kulia, geuza kushoto, wakati mama yake mzazi kalala usingizi kimya gorofani!” Vai na Mia walikuwa wakipokezana maneno huku wakicheka kwa sauti sana. Naih na Kenny walibaki kimya wakiwatizama. Maana waliwasimamia mbele yao.

Mama yake Kenny akawasogelea. “Mbona mnafanya fujo?” Mama Ole akawauliza kwa upole. “Muulize mwanao kama tunamfanyia fujo. Sisi tulikuwa tunakumbushia enzi zile humtaki Naih, ukamfukuza kwako kama mbwa huku ukimtafutia mwanao wanawake wakuoa.” “Ngoja kwanza Zai. Unakumbuka mama Ole, ulivyotulipa ili tuhakikishe Nai, anaondoka na hatakaa kurudi nyumbani kwako, ukasema hamfai mwanao?” Mama Ole kimya.

Mia akaendelea bila kujali. “Sasa ndio Zai alikuwa anatoa pongezi hapa, kuwa mmetumia akili sana. Maana katika ulemavu huu,” Mia akanyoosha kidole kwenye miguu ya Kenny, kisha akaendelea. “Lazima mumpate kijakazi cha kudumu. Chakumgeuza Kenny mchana na usiku. Sasa nani mwenye hadhi hiyo, kama sio Naih, mwenye shida? Basi ulivyo na akili, ukaamua kumkabidhi Zigo lote, akahangaike naye mchana na usiku.” Wote walianza kucheka upya huku wakigonga mikono.

“Bwana mimi nakusifu mama Ole. Una akili sana.” Waliendelea kucheka. “Yaani watu wakikuona sasa hivi hapa, wamaweza sema unampenda kweli Nai!” Zai akaongeza. “Sasa hapo ndipo utajiuliza mapenzi hayo ya gafla kwa Nai, mtoto maskini, aliyekimbiwa na baba yake mzazi, mlinzi wao, yameanza lini? Kama sio kuuwa ndege wawili kwa jiwe moja!” “Mfanyakazi wa mchana na wa usiku!” “Tena mjinga. Shule hana. Ndio leo wamemkabidhi rasmi Zigo, akahangaike nalo. Hamna kitu hapo. Andika maumivu Naih.” “Gorofa atalikaa, lakini na yeye cha moto atakiona.” Walizidi kucheka na kugonga, huku watu wakiwasikiliza maana walifanikiwa kuvuta masikio ya wageni wote.

Mama Ole alibakia kimya kama aliyevuliwa nguo. Kenny alikaa pale kama mgonjwa akitokwa na machozi. “Kama mmemaliza naomba mnipishe nipite jamani.” Ndilo neno Naih aliloluzungumza pekee baada ya kejeli zote zile. Zai na Mia wabaki wamesimama. Akawasogelea askari mwenye sare ya kipolisi. “Kuna shida yeyote hapa?” “Shida itoke wapi?” Zai akajibu kwa kuuliza swali kwa jeuri, wakacheka na kugeuka, wakaondoka.

Naih naye akaendelea na safari yao kama ambaye hakuwa amewasikia wadogo zake. Akamsukuma Kenny kumtoa pale watu walipokuwa wakiwatizama mpaka kwenye lifti yakuwapeleka juu chumbani kwao, akabonyeza. Baada ya sekunde chache ikafunguka Naih akamvutia Kenny ndani na Emma naye akaingia kwa haraka kabla haijajifunga. “Bwana Emma toka! Unaenda wapi sasa na wewe?” “Kweli Naih umepania! Na maneno yote yale bado unaendelea tu. Hamu hiyo hamu gani bwana! Simrudi mnywe hata soda kwanza!” “Sitaki. Bwana tuache wenyewe.” Emma alianza kucheka tena.

“Bwana toka Emma.” “Ngoja kwanza Naih.” Kenny akamgeukia. “Nini na wewe Kenny?” “Yaani na maneno yote yale, hamu haijakuisha tu! Bado unataka!?” “Bwana Kenny na wewe ndio swali gani hilo!? Kwani kuna jambo gani jipya pale ambalo hujawahi kulisikia? Ukute pale, wale watoto wamewakilisha mawazo hata ya wageni wote waliokuwepo pale.” “Kwa hiyo hujali?” Emma akauliza akimshangaa sana Naih. “Bwana Kenny mfukuze Emma, wewe atakusikiliza.” Kenny mwenyewe akabaki haamini.

Kenny akahisi pengine Naih hakuwa amesikia maneno yote vizuri, akabaki na mshangao. “We Kenny! Ni nini lakini? Mbona unakuwa mtu usiyesimamia maneno yako mwenyewe? Uliniahidi mwenyewe nisubiri mpaka tufunge ndoa. Nimevumilia sasa hivi na wewe unakuwa kikwazo! Nimekwambia mfukuze Emma atuache tuendelee na mambo yetu.” Emma alikuwa akicheka mpaka akakaa chini. “Ujue Nai wewe ni kichaa!” “Sawa. Basi naomba utupishe.” Lifti ikawafikisha mpaka kwenye gorofa ilipokuwepo chumba cha Kenny na Naih wakabaki wakibishana nje ya lifti hiyo.

“Nakuomba usitufuate nyuma Emma. Wewe shuka mwambie Mama Ole tunakuja baada ya kubadilisha nguo. Halafu endelea kuongea na wageni hukohuko chini. Usirudi huku.” “Nataka kukusaidia Nai! Acha ukorofi.” “Sitaki msaada wako, Emma. Niachie Kenny wangu. Wewe hujasikia pale nikikabidhiwa rasmi? Sitaki msaada wa mtu yeyote. Nipishe na mume wangu.” Mpaka Kenny akaanza kucheka vile Naih alivyokuwa anamaanisha, na Emma anavyomng’ang’ania. Kenny alizidi kucheka. Akasahau matusi yote ya wadogo zake Naih akabaki akimsikiliza Emma na Naih. “Leo kazi unayo Kenny. Mtoto wa kimasai amekung’ang’ania, huna pakukwepea!” “Bwana ondoka. Usitufuate.” Naih akamtoa pale Kenny, akamsukuma mpaka chumbani kwao.

*************************************

“Sasa mbona umetulia gafla?” Kenny akamuuliza huku akicheka. “Sijui natakiwa kufanya nini!” Naih alijibu nakumfanya Kenny azidi kucheka. “Sasa juhudi zote zile, kumbe hujui hata pakuanzia!” “Usinicheke Kenny, bwana! Wewe nielekeze.” Akakumbuka ni kweli Naih hajawahi kufanya mapenzi. “Unakumbuka juzi ulivyokuwa ukininyonya kila mahali? Sasa nataka iwe kama vile. Nilifurahia sana. Sikuwahi..” Kenny akamvuta mpaka pale kwenye kiti chake, akaanza kumnyonya huku akimvua nguo taratibu. Alijitahidi mpaka akafanikiwa kupanda kitandani kwa kujivuta. Alihakikisha anatumia ujuzi wote, kumfurahisha Naih usiku ule. Mpaka anamwingilia mkewe, Naih alishakuwa amefika kileleni vyakutosha, akabaki amepagawa pale kitandani, asiamini yanayoendelea mwilini mwake.

Kenny alitoa furaha ya ajabu sana ndani yake asiamini kama kuna raha kama hiyo unaweza pata. Japokuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kufanya mapenzi akiwa hana miguu, lakini Kenny alijitahidi sana kumfurahisha mkewe. Alijiona anadeni ambalo hawezi kumlipa Naih isipokuwa kuhakikisha anaweka historia nzuri kwenye maisha yeke. Kwanza ni kweli alikuwa akimfungia kama kufuli wakati yeye akienda kwa wanawake wengine. Naih hakuwahi kuwa hata na rafiki wa kiume. Alijisikia anawajibika kumtenda vyema.

Na pili alijisikia vizuri kwa hali ile ya ulemavu, bado Naih anamtaka! Tatu, ina maana ile hali yakufanya mapenzi kwa sura ya Naih, imefika mwisho. Anafanya mapenzi na Naih mwenyewe, msichana aliyekuwa akimtamani tokea zamani. Alimfanyia vituko vingi vilivyompagawisha Naih ambaye ndio alikuwa amemtoa bikra. Lakini alihakikisha mpaka anamalizana naye, Naih hayupo kwenye maumivu makali yakumfanya akose raha. Alipohakikisha ameridhika, akamvutia kifuani kwake. Akabaki amemkumbatia huku akimpapasa taratibu.

“Asante Kenny. Nimefurahi.” Naih aliongea akiwa ametulia kifuani kwa Kenny. “Asante wewe Naih.” “Kwa nini tena?” “Kunikamilisha. Sijui ningeficha wapi uso wangu bila wewe!” Naih akatulia. “Nakupenda Naih, nasikitika tumeoana nikiwa mlemavu.” “Kwani ungenifanyia nini cha tofauti?” “Jamani Nai! Hivi unanisikiliza lakini?” “Tatizo lako wewe Kenny unaruhusu watu wakuumize kirahisi. Watu walikuwa wakikusema tangia hujapata haya matatizo, na wataendelea kukusema zaidi na zaidi. Uwe una miguu au huna, watasema tu. Naomba tuongee mambo yetu yanayotuhusu sisi. Tuna maisha mazuri na marefu sana mbeleni. Tusipokuwa waangalifu, tutajikuta kila tukikutana tunazungumzia shutuma za watu.” Naih akaendelea.

“Leo ni siku yetu muhimu sana. Mwenzio ndio nimefanya mapenzi kwa mara ya kwanza, tena nikafurahia. Naomba tusiingize mambo ya watu wengine. Naomba tufurahie siku yetu. Sawa?” “Nimeelewa Naih.” “Basi tujiandae twende kwenye tafrija, tukirudi tuendelee na mipango yetu.” Naih alijua kumtuliza sana Kenny. Hapakuwa na jinsi ungebisha kuwa alikusudiwa kuwa mkewe.

Tafrija ya Kenny & Naih.

N

aih na Kenny walitoka pale kurudi kwenye tafrija, wakionekana wametulia kabisa tofauti na watu au wazazi wao walivyotegemea. Walikuwa wameoga na kubadili nguo. Bado Naih alikuwa amependeza. Nguo hizo pia zilivaliwa na cheni nzito iliyojaa kifuani kwa Naih. Aliweka masikioni hereni nzuri zilizokuwa ziking’aa na kuweza kuonekana na mtu hata aliyekuwa amekaa mwisho kabisa mida hiyo ya jioni.

Ile sehemu ilipangwa kwa mtindo wa tafrija, ikazidi kuvutia. Emma, Jay, mke wa Jaya, Kenny na Naih walikaa meza moja na kuendelea kutaniana. Watu walikula na kunywa, mpaka wakasaza, na hapakuwa na waalikwa wengi sana.

Baada ya chakula. Kenny na mkewe wakaombwa na Mama Ole, watoe neno la shukurani. Akiwa amekaa vilevile, Kenny alipokea kipaza sauti akatulia kidogo kama anayetafuta pakuanzia. Mwishowe akamuona machozi yanatoka. Naih akamvuta mkono mwingine. Akaubusu, na kubaki ameushikilia baada ya kujisogeza karibu. Akambusu tena mkono kama kumtuliza.

“Naih nimempita miaka 4. Lakini kwa mapungufu, udhaifu, kasoro zozote zile unazoziona kwangu, zinakamilishwa na yeye. Na mimi nipo kama wengi wenu hapa, kama ningepewa nafasi ya kuolewa na Kenny, si huyu tu mlemavu, hata yule aliyekuwa na miguu yote miwili, pia nisingemkubali. Mungu ameyaona mapungufu yangu, akanihurumia, akaamua kuniumbia mke atakayenikamilisha. Tangia Naih analetwa nyumbani, baada ya kuzaliwa, ipo sehemu ndani yangu imekuwa ikimuhitaji sana. Kwa wakati ule sikujua ni kwa nini, lakini sasa hivi naelewa. Nitadanganya nikisema namshukuru kwa kunilea sasa hivi, au tangia nimepata ajali. Naih amekuwa akinilea tokea anapata akili.” Kenny akaendelea.

“Nakumbuka wakati bado tupo wadogo, yeye akiwa mdogo zaidi, nilikuwa nikiumwa, hakuwa akilala. Mama yake ni shahidi. Yeye na mama yake walikuwa wakiniuguza, lakini muda wakulala ulikuwa unapofika, mama yake alikuwa akituacha mimi na Naih, yeye anaenda kulala.  Lakini Naih hakuwa akiweza kulala. Kalikuwa kadogo, kembamba zaidi ya hivi.” Watu wakacheka. “Sasa alikuwa akizidiwa na usingizi, alikuwa akinivuta kwa nguvu zake zote mpaka kwenye vimapaja vyake, ananifunika, ili nikiamka, nisijikute peke yangu na yeye aamke. Na ilikuwa kila nikigeuka, na yeye anaamka. Na maneno yake hayakuwa mengi. ‘Pole Kenny, eeh! Nikuletee maji? Unaogopa sana? Usiogope, mimi nipo na wewe.’ Basi atarudia hivyo mpaka panapambazuka, mama yake atakapokuja kwenye chumba tulichokuwa tukilala naye. Labda ataingia kutuchukua ili atuogeshe na kutupa chakula, lakini ataniacha na Naih hapohapo. Tumekuwa hivyo mpaka sasa. Sijawahi kujua maisha mengine bila Naih.”

“Wakati tupo watoto tulilishana damu. Amini. Yeye alikunywa damu yangu na mimi ya kwake. Tukaambiana ndio ishara ya kuwa pamoja milele. Mengi tulifanya katika utoto, sikujua kama leo yatatimia. Namshukuru mama yangu kwa kunilazimisha kufanya hii shuguli. Sikutaka watu waje wahudhurie ili kukwepa aibu au niseme maneno kama yale waliyokuwa wakisema wadogo zake Naih. Nikamwambia Naih tutakwenda mahakamani tu, tutafunga ndoa, Jay na Emma ndio watakuwa mashahidi zetu, basi. Kama wengi wenu mnavyomfahamu Naih, huwa hana makuu, akakubali kila kitu bila tatizo. Lakini mama aliona sio sawa kufanya mambo kimyakimya. Hatuna sababu yakujificha. Baba yangu amesimama na mimi kuhakikisha nafanikisha kupata pete za ndoto yetu. Nilitaka leo mke wangu avae kila kitu chenye alama ya Infinity, alama muhimu sana kwetu.”

“Tulivalishana hiyo alama tukiwa watoto wadogo sana, siku tulipopeana amini. Tulianza kwa kuvalishana waya wa umeme niliokuwa nimeokota tu pale nyumbani. Lakini leo nimemvalisha Naih alama hiyo ikiwa imetengenezwa na dhahabu na imebeba alumasi halisi, tena akiwa mke wangu. Nawashukuru wazazi wangu kwa tafrija hii waliyomfanyia Naih, anastahili. Sina maneno mengi ya kuongea, naona na mimi nimuige Naih, matendo yetu yatazungumza zaidi. Sitaki kuahidi chochote, wala kuongea mengi, nitakuwa kama Naih. Naacha matendo yangu yazungumze.” Kenny akaendelea.

“Natoa shukurani za pekee kwa ndugu zangu hawa wawili, Jay na pacha wangu wa nje, Emma. Hakuna watu wanao nivumilia na kunisitiri hapa mjini mbali na Naih, kama hawa wawili. Huwa nashangaa nakujiuliza ni lini watakuja kunichoka! Si mchana, wala usiku. Si nikiwa nacheka au nipo matatizoni, kila kitu kwenye maisha yao huwa kinasimama, mimi nitawekwa wa kwanza. Nawashukuru sana. Inamlazimu Jay kuwa safarini kwa masaa takribani 18 ili kunifikia mimi na Emma. Ana majukumu yake ya kikazi na  kama mnavyomuona mkewe ambaye ni mjamzito! Lakini Jay ameweza kuwepo hapa nchini na mkewe akiwa kwenye hali hiyo kwa ajili yangu mimi! Ndani ya mwezi mmoja, Jay amerudi hapa nchini mara mbili kwa ajili yangu. Inamgarimu muda, ambao ndio kitu cha thamani sana kwake, hasa kipindi hichi wanachomsubiria mtoto wao, na pesa. Lakini Jay amekubali kulipa garama hiyo kwa ajili yangu. Wakati nipo hospitalini yeye na Emma walikuwepo pembeni yangu, bila kuchoka mpaka nimetolewa. Na leo tena yupo hapa na sisi. Nakushukuru sana Jay. Asante kaka yangu.” “Pamoja sana.” Jay akajibu. Wazazi wake wakabaki kimya wakisikiliza na kuangalia huyo mkwe wa kizungu na mjamzito. Hakuwa hata amewasalimia au hata kumtambulisha kwao huyo mkewe. Na hata ilipowalazimu kuwa karibu, alijifanya kama hawaoni au hawapo pale. Na wao ni kama walijionya. Hawakuthubutu hata kumsemesha.

“Naomba nimshukuru Atu, mama mkwe wangu na mwanamke aliyenilea mimi na Naih tangia nazaliwa.” Kenny akaendelea. “Hakuna mtu ananifahamu vizuri kama Atu. Amenihangaikia kwenye kunilea, mpaka leo naona amemkabidhi hiyo kazi mtoto wake, tena kwa baraka zote bila kinyongo, huku akizifahamu tabia zangu. Atu kama nilivyozoea kumuita, nilikuwa nikilala mikononi mwake, mpaka Naih alipozaliwa.” Kenny alicheka kidogo.

“Kuna usemi wanasema ‘amempokonya ziwa’, basi mimi, Naih ndiye alinipokonya mikono ya Atu. Alimzaa Naih nikiwa na miaka 4, lakini bado alinipenda na kunilea kama mtoto wake. Wakati mwingine nilikuwa nikilala naye usiku na nikilazwa hospitalini, Atu ndiye aliyekuwa akilazwa na mimi. Mambo yalibadilika alipozaliwa Naih, ndipo ikabidi awe anatulaza pamoja ili usiku aweze kutuhudumia wote wawili kwa pamoja. Na ndivyo tulivyokuwa mimi na Naih. Tumekuwa tukilala pamoja mpaka leo. Hatujui maisha mengine mbali ya kuwa pamoja. Hata nilipokuwa nikitoka kwenye mambo yangu mabaya, nikiwa nimechukia, au nimechoka, sehemu pekee niliyokuwa nikilala vizuri ni pembeni ya Naih.”

“Asubuhi ya leo nilimuita Atu, ili kuzungumza naye na kutaka kumuhakikishia mapenzi yangu ya dhati kwa Naih, lakini alicheka, akasema yeye alikuwa akilijua hilo tokea zamani. Amejiweka upande wangu na kuniambia amefurahi ameniacha kwenye mikono ambayo hata akilala usiku hatakuwa na wasiwasi, anauhakika nipo kwenye mikono salama. Asante sana Atu.” Atu alicheka tu. Watu wakapiga makofi. Angala Kenny akapata ujasiri.

“Na pia nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitamshukuru babu Kaa. Kwa wengine ni dereva tu wa Mzee Ole, lakini kwangu mimi ni zaidi ya mfanyakazi. Tokea mtoto, alisaidiana na Atu kunilea. Wakati wote alikuwa akiniambia nitahangaika sana, lakini mke wangu yupo nyumbani, nisiwahi kuchelewa kurudi nyumbani. Alijua njia zangu mbaya na ilimlazimu wakati bado sijaanza kuendesha, yeye kunipeleka ili kwenda kufanya uovu wangu, lakini wakati wote aliniambia nina hangaika kwa kuwa nimemuacha Naih nyumbani. Babu Kaa aliniambia sitawahi kutulia mpaka nitakapokubali na kumwambia Naih ukweli kuwa yeye ni mke wangu.” Naih alishangaa sana. Kenny akacheka kidogo kama anayekumbuka kitu.

“Nilikuwa nikimbishia  babu Kaa, na kumwambia idadi ya wanawake niliokuwa nikilala nao, na yeye swali lake lilikuwa ni moja tu. Akitaka kujua ninavyojisikia kila baada ya kulala na hao wanawake. Ni kweli hapakuwa na utoshelevu na nilikuwa nikimdanganya, na kumwambia najisikia vizuri sana. Cha ajabu alikuwa akiniambia, sitakaa nitosheke, hata nilale na nani, kama hatakuwa ni Naih. Baada yakushindwa kunishawishi kutulia, alihakikisha ananifundisha jinsi ya kujikinga na maradhi. Hakuacha kuniuliza kila wakati kama nakumbuka kinga. Wakati mwingine nilikuwa nikimkasirikia, lakini kama mnavyomjua babu Kaa, hana hasira, na alihakikisha namjibu na kumuhakikishia natumia na nitaendelea kutumia kinga. Hata nikiwa namgombesha vipi! Atatulia akinisikiliza, kisha nikitulia anarudia swali lake vilevile la kusisitiza juu ya kinga.” Watu walicheka kidogo, lakini mzee Ole kushangazwa sana na huyo mfanyakazi wake wa miaka karibia 30, ambaye kwanza hakuwa hata na ukaribu naye, kumbe ndiye aliyeokoa na kulinda maisha ya kijana wake! Wazazi hao wakatulia kimya na kumuangalia sasa babu Kaa vizuri.

“Aliniambia anauhakika Naih ananisubiri, lakini inategemea na mimi. Kama nitamtaka lazima nijikinge na maradhi ili nisife mapema, na pia aliniambia nihakikishe simrudii Naih na watoto wasio wake. Alinifanya niiogope pombe, akiniambia siku nitakayoanza kunywa pombe, ndiyo siku nitampoteza Naih. Aliniambia siwezi kuwa na vilema viwili kwa wakati mmoja. Pombe itanifanya nisahau kinga na nitakufa mapema sana.” Naih hakuwa akiamini kama huyo babu alikuwa akimzunguzia kwa Kenny kwa undani hivyo! Akazidi kushangazwa moyoni akiwa kimya tu, ameinama na yeye akisikiliza. Kwani kila walipojikuta pamoja, babu Kaa alikuwa kimya tu akiendelea na shuguli zake, na Naih naye akifanya yake. Hawakuwa karibu hata kidogo na wala hawakuwa wakizungumza hata mazungumzo ya kawaida tu, mbali na salamu.  Hakujua hata kama huwa anamtaja kwa Kenny!

“Nilipopewa gari ya kwanza na baba, nikamfuata babu Kaa na kumwambia Mungu amenisaidia kuniepusha naye, sitaki tena anifuate. Hakujibu. Lakini hakuwahi kuniacha. Kama hakunipigia simu basi alinitumia ujumbe kunikumbusha kujikinga, na kurudi nyumbani kabla ya saa mbili akiniambia, nitamkuta Naih amelala. Mwanzoni niliacha kupokea simu zake kwa kuwa nilikuwa nikijua anachotaka kuniambia, badala yake nikawa nikimjibu kwa ujumbe tu, ‘nakumbuka kinga na nimeshaenda kumuona Naih kabla hajalala’. Ikajengeka tabia, ikawa mazoea. Lazima kila siku kumuona Naih kabla hajalala ndipo niendelee na starehe zangu. Ikitokea nimesafiri, basi nilazima nizungumze naye kwenye simu, kila siku bila kukosa. Na kipindi nilichoacha kuzungumza na Naih, ndipo nikaishia hapa kama hivi mnavyoniona sasa. Babu Kaa alikuwa sahihi, sina utoshelevu mbali na Naih. Leo nimejawa na furaha, najisikia nimekamilika, kwa kuwa nimempata Naih.”

“Nilimwambia baba, harusi hii haitakamilika kama babu Kaa hatakuwepo hapa leo. Na kweli, baba alihakikisha anatuletea babu Kaa. Asante sana Babu yangu kwa kunifuatilia bila kuchoka. Tena wakati mwingine nilikuwa nikimtukana kipindi kile ndio nakuwa au kupevuka, alikuwa akinikera sana kwa kunifuatilia, lakini ameokoa maisha yangu.” Watu wakapiga makofi, mpaka wakasimama. Jay na Emma wakaenda kumpa mkono, na Naih naye akaenda kumshukuru kwa kumpa mkono.

“Mwisho kabisa, niwashukuru nyinyi wote kwa kufika hapa. Najua mmeacha shuguli nyingi kuja kushuhudia mimi na Naih tukitoa kiapo chetu hadharani. Asanteni sana.” Kenny akamaliza, akarudisha kipaza sauti kwa muongoza shuguli. Wageni walisimama na kuwapa mkono wa pongezi.

Wema Hauozi.

n

dipo wazazi wake Kenny wakaomba na wao wazungumze. “Na sisi tunaomba kumpa mkono wa pongezi Naih. Alimfungulia Kenny milango kwenye chumba chake. Wanaishi mpaka hivi sasa kwenye hicho chumba. Kwenye chumba kicho cha Naih ndipo tumerudisha mahusiano au kujenga mahusiano mapya na Kenny mtoto wangu wa pekee, tena Naih akitusaidia. Naih ni mtoto mdogo sana kwetu, lakini ametufundisha kitu kikubwa sana mimi na Rita, mke wangu. Siwezi kueleza mengi, lakini Naih ameponya ndoa yetu, kwa vitendo. Ametufundisha kwa vitendo kuwa, hakuna kosa lisilosamehewa, na hakuna mwanadamu asiyestahili nafasi ya pili maishani, hasa akiwa ameharibu sana kwenye nafasi ya kwanza. Pia ametufundisha hakuna umbali mwanadamu anaoweza kwenda, akashindwa kurudi na kutengeneza kama akiamua. Ametufundisha unaweza kurudisha uhai, pale palipokufa. Tena ametufundisha kwa vitendo, bila maneno.” Watu wakapiga makofi kwa muda mrefu tu na vigelegele.

Mzee Ole akaendelea. “Nina uhakika kabisa, kama sio Naih, Kenny asingekuwa vile mnavyomuona sasa hivi. Pengine angeshakuwa amekufa. Alipopata ajali, pressure nayo ikaanza kuwa juu. Madaktari walishindwa kumtibu kwa kuwa hakuwa akiongea na mtu yeyote, kwa hiyo hawakujua ni jinsi gani ya kumsaidia. Pressure ilikuwa ikipanda kila leo, na dawa alikuwa akipewa. Siku Naih amekuja pale hospitalini na kuanza kumuhudumia Kenny, alirudisha tumaini. Anamtunza Kenny, akiwa amekataa katakata tusimlipe kitu chochote. Wakati mwingine tunamuhurumia na kutamani labda apumzike. Tulimshauri pembeni sio mbele ya Kenny, kuwa tunaweza kumtafutia nesi ili siku nyingine awe anampokea mzigo huo wakuuguza, ili yeye atoke pale ndani. Aende hata saluni au madukani, lakini Naih alikataa katakata. Anamuuguza Kenny bila kuchoka au kulalamika.”

“Wadogo zake hawakukosea, ni kweli Naih ndiye anayemgeuza Kenny kulia na kushoto, mchana na usiku. Sisi tukiwa tumelala. Wapo kama vile mnavyowaona pale. Wawili tu, na wakati wote utawakuta wanazungumza lugha yao, wanayoelewana wao wawili tu. Lakini utahisi ile hali ya amani kati yao. Tunajua hakuna malipo tunaweza kumlipa Naih, lakini kuna kitu kidogo tumemwandalia. Karibu Rita.” Ole akamkaribisha mkewe ili akabidhi hiyo zawadi.

“Kabla ya kumkabidhi, na mimi naomba nimshukuru. Asante sana Naih. Nakushukuru sana. Nashindwa hata kuongea, kwa kuwa sijui hata nianzie wapi, nahofia kuharibu. Ila nataka Naih ujue, tunamshukuru sana. Asante.” Usiku huo ukawa wakushangazwa kwa Naih. Babu Kaa, akaja tena kuongeza Mzee Ole. Shukurani hizo fupi kutoka kwa Mzee huyo, zilimgusa zaidi Naih aliyekuwa akiwajua wanandoa hao. Mzee Ole na mkewe! Tokea anapata uelewa wake, alikuwa akiona jinsi wanavyoishi kwa kupishana na kila mmoja akiwa na maisha yake. Hakujua kama alifanya kitu kikubwa sana kwa matajiri hao. Japokuwa Mama Ole hakuongea sana, lakini alionekana ameguswa zaidi na alichokifanya.

“Tulibahatika kupata mtu aliyekubali tumuhamishe pale karibu na nyumbani kwetu. Akatuuzia nyumba yake. Tumeshakamilisha taratibu, na hati hii hapa ipo kwa jina la Naih.” Naih alitoa macho akabaki amefunika mdomo aliokuwa ameufungua kwa mshituko. “Na kwa kuwa hana gari, tumemuagizia gari ambayo itakuwa rahisi kuendesha akiwa na Kenny. Ni gari maalumu kwa ajili ya hali hiyo ya Kenny, lakini ipo kwa jina la Naih. Hata kama kesho ataamua kumuacha Kenny, vyote vipo kwa jina lake. Ni vitu vyake kabisa. Yupo huru kutumia apendavyo.” Naih alimgeukia Kenny kama haelewi huku amekunja uso kutaka kujua kama anaelewa. Kenny alitoa tabasamu kuonyesha anafahamu na anabaraka zake.

Naih alibaki ameshangaa kama ameona kitu chakutisha. “Twende tukachukue funguo za nyumba, Wangu.” Emma alimpigapiga mgongoni Naih. “Siwezi! Mimi sikutaka nilipwe!” Naih alisikika akiwa na mshangao na hofu kubwa. “Wala hatutaweza kukulipa Naih. Kama Jay alivyosema, vipo vitu vingine maishani, havilipiki. Ni kweli. Hatuna uwezo wa kukulipa kwa lolote. Hivi vitu vitakusaidia kuanza maisha na mwenzio. Angalau utapata sehemu kubwa ya kumuweka Kenny. Naomba upokee tu.” Mzee Ole aliweka msisitizo.

“Na watoto wetu.” Kenny akaongeza na kufanya watu wacheke kidogo. “Au umegairi swala la watoto?” Kenny akamvuta kidogo. Naih akageuka na kutingisha kichwa kukataa akionyesha bado yupo kwenye mshangao. “Basi ndio upokee ili tupate pakuwaweka watoto wetu.” Naih akasimama huku akifuta machozi. Mama Ole akamsogelea, akamkumbatia na kumkabidhi funguo za nyumba na ile hati. “Funguo za gari tutakukabidhi mtakaporudi kutoka India, gari litakuwa limefika.” “Asanteni sana.” Naih akashukuru na kumsogelea Mzee Ole na kumpa mkono kwa heshima. “Asante sana Naih.” Mzee Ole akaongeza.

 “Mtakaa hapa hotelini mpaka siku mtakayokuwa mkiondoka kwenda nchini India kwa matibabu, ili Naih upumzike. Watakufanyia kila kitu, wewe akili yako iwe kwa Kenny tu na kupumzika.”  “Asanteni sana. Nashukuru mama Ole. Nashukuru kwa kila kitu. Sikutegemea!” Ni kweli, kufunga na kufungua, maisha ya Naih yalishabadilishwa. Wamasai hao waliweka heshima kwa Naih, gafla Naih akawa maarufu. Alitajirishwa na kupewa heshima za namna yake siku hiyo, nakuwaacha wadogo zake wamefungwa mdomo. Tafrija iliisha, Naih na Kenny wakarudi chumbani kwao kuendeleza fungate.

 

Kenny & Naih

J

apokuwa alipoteza miguu, lakini Kenny alihakikisha anaweka historia ya namna yake kwa Naih ambaye hakuwa na pakulinganisha. Kila alichofanyiwa na mumewe kwake aliona ni mambo mazuri na ya ajabu. Kila kitu kilikuwa kipya kwake. Kenny alizitumia hizo siku wakiwa wanasubiria kwenda nchini India, kulipa fadhila kwa Naih. Yale mapenzi aliyokuwa akifanya na mamia ya wanawake kwa sura ya Naih, alizidi kufaidi kwenye mwili huo wa Naih mwenyewe. Alimfundisha kufanya mapenzi vile anavyotaka yeye, kwa hiyo hapakuwa na mwanamke mzuri na alimyemfurahia Kenny kitandani kama Naih. Kwa kuwa alimfundisha afanye kile anachopenda yeye Kenny kwenye mapenzi. Na kwa kuwa Naih hakuwa na ujuzi mwingine mbali na huo, basi akawa mke sahii kwa Kenny.

Kazi yao ilikuwa ni mapenzi tu. Chakula kililetwa na wahudumu wa hoteli hiyo pale wanapotaka wao. Kwa siku 5 mfululizo, Mama Ole alihakikisha hawaingiliwi na yeyote yule. Hapakuwa na simu wala mtu aliyeenda kuwatembelea mpaka siku ya kwenda nchini India ilipofika.

Safari ya Kenny & Naih, nchini India.

Emma alikwenda kumchukua Mama Naih na kumleta hapo hotelini kwa ajili ya kupata chakula cha mchana na kina Kenny kabla hawajaondoka. Walifika hapo hotelini wakawakuta wazazi wa Emma na wazazi wa Kenny wako sehemu ya kulia chakula, wakiwasubiri. “Wako wapi hawa?” Emma akauliza wakati wanakaa. “Wamesema wanakuja.” Alijibu Mama Ole. Baada ya muda, waliwaona Kenny na Naih wakija. Naih alibadilika, mama yake alibaki akimtizama kwa kumshangaa. Alipendeza sana na usoni alionyesha anafuraha, na amepata mapumziko yakutosha.

Walikula pamoja. Vilijaa vicheko na wazazi wao na kutaniana kwingi kati ya Emma, Kenny, Naih. Jay na mkewe walishakuwa wameondoka kurudi kwao, tena Jay hakuwa ametania. Ni kweli hakumtambulisha mkewe kwa wazazi wake na wala hakuwasemesha au hata kuwaangalia tu usoni! Alihakikisha hata macho yake hayagongani na yao. Yeye na mkewe walishukia nyumbani kwa Emma, baada ya harusi, walipumzika siku mbili tu mbele na kuondoka nchini. Kwa hiyo walibakiwa na Emma tu ambaye aliwazoea Naih na Kenny na hakuwa akijiwinda maneno kwa maharusi hao wapya. Yeye akawa huru nao huku wazazi wakijiwinda kwa kila neno. Aliwafanyia utani wa hapa na pale, mpaka ilipofika muda wa kwenda uwanja wa ndege.

Naih alimvuta mama yake pembeni, akamgawia pesa. “Umebadilika!” Atu alimwambia mwanae. “Kama sio wewe Naih! Hizo ni dhahabu?” Atu aliuliza huku akinong’ona. “Ameniletea leo, mama yake Kenny.” Naih alijibu huku akicheka. “Umeuchinja Naih mwanangu!” Naih alikuwa akicheka. Alikuwa ameletewa cheni ya shingoni, mkononi na hereni zilizofanana na hizo cheni. Alibana nywele zake upande mmoja, ni kweli Naih alipendeza. Na kwa weusi ule, na urefu, alionekana kama binti wa kisomali. Kicheko kilimtawala usoni na kuzidi kuvutia.

“Nitajitahidi kukupigia mara kwa mara, mama. Jitahidi kuficha hii kadi ya benki ili kina Zai wasikuibie tena. Ndio akaunti wanayoiingiza mshahara wangu. Na wewe usimalize pesa yote.” Mama yake akacheka. “Siwezi Naih, mwanangu. Nitatumia kwa makini. Asante sana.” Kufumba na kufumbua naye Atu mambo yamemnyookea. Nani alijua kama Naih aliyekuwa akifeli darasani, anaweza kuwa msaada kwa mama yake! Mungu ananjia zake za kumbariki kila mtakaye. Leo Naih ndiye anayekula na kufaidi mali za kina Ole.

Waliondoka huku Naih akimsukuma mumewe kwa matumaini kuwa siku watakayokuwa wakirudi, Kenny atakuwa akitembea.

 

Kenny & Naih nchini India.

W

alipata wakati mzuri sana wakiwa huko nchini India. Ni kama walienda kuendeleza fungate. Kenny alihitajika muda mfupi tu hospitalini, akifundishwa jinsi ya kutembelea hiyo miguu ya bandia, muda mwingine wote aliutumia na Naih kitandani. Kwa kuwa wazazi wake walilipia pesa nyingi ili mtoto wao apate miguu hiyo ya bandia, kwanza iwe mizuri inayofanana na miguu  aliyopoteza na pia kupata mtaalamu atakayeweza kumfundisha na kumfanya atembee kwa haraka. Alianza kufundishwa jinsi ya kuitumia. Majuma matatu ya mwanzo yalienda vizuri bila shida huku mafunzo yakiendelea


na yeye kufanya mazoezi akiwa peke yake nje ya hospitali.

Na kwa kuwa shauku yake kubwa ilikuwa ni kurudi kutembea, Kenny alifanya mazoezi zaidi alivyotakiwa. Aliyekuwa akimfundisha alikuwa akimshangaa vile alivyoweza kuimudu ile miguu bila shida. Akaanza kufundishwa hata jinsi ya kukimbia nayo, kufanya nayo mazoezi, na mambo mengine mengi tu. Naih alikuwa akimsindikiza na kumsubiria wakati akifanya mazoezi hospitalini na kwenye viwanja vya mpira. 

Juma la nne, Kenny alianza kutembea bila shida. Akiwa amevaa suruali, ilikuwa ngumu kujua kama ana miguu ya bandia. Tumaini kwa Kenny lilirejea kabisa. Alijawa furaha kwani ni kama enzi zilirudi, lakini sasa hivi akiwa na mikakati mipya ya maisha.

    Baada ya majuma matatu kuisha tangia wafike nchini hapo na wakati Kenny anaendelea na mazoezi na kupata tumaini jipya, akaamua kutoka hotelini na kwenda  kuishi na Naih kwenye apartment za hapohapo Palm Green kwenye mji huohuo wa New Delhi.  

Alimwambia Naih na wazazi wake kuwa anataka kuanza kuishi maisha ya kawaida kama nyumbani sio hotelini ili  kuanza kuzoea maisha ya nyumbani na yeye akitumika kabla yakurudi nchini. Wakaweza kupata apartment ndogo tu,  iliyokuwa na kila kitu humo ndani. Hawakuhitaji kununua hata kijiko. Wakalipia kwa miezi  miwili. Maisha yakaendelea.

Kenny alikuwa akimtumikia Naih bila kuchoka. Wakati mwingine Naih alikuwa akiamka anamkuta Kenny ameshaandaa kifungua kinywa. Naih alikuwa akijitizamia na kushangaa moyoni mwake, kwani Kenny hakuwa akijua hata kufua soksi zake. Alifanyiwa kila kitu akiwa nyumbani kwao. Hata kitanda chake alikuwa akitandikiwa. Kazi yake kubwa ilikuwa nikufanya starehe huku akitapanya pesa.

Maisha yalibadilika. Mtazamo wa maisha pia ulibadilika baada ya kupewa nafasi ya pili maishani. Alijifunza vitu vingi kutoka kwa Naih, nakuiga. Wakati mwingine Naih alipokuwa akiandaa kifungua kinywa, alirudi chumbani na kukuta Kenny ametandika kitanda na kupanga chumba vizuri. Alimsaidia kusafisha kila mahali, akajifunza na kupika pia.

“Naona turudi tu nyumbani. Mgonjwa umepona!” Kenny alikuwa akicheka. “Unaonaje tembea yangu?” Kenny akauliza. “Sasa hivi hata waliokuwa wakikufahamu, wakikuona ukitembea, hawataona tofauti. Umerudia mwendo wako.” “Ni kweli Naih au unanitia moyo tu?” “Wewe unanijua huwa sikudanganyi, Kenny. Kumbuka mwanzoni mimi ndio nilikwambia unatembea vibaya, unaonekana una hofu na hiyo miguu mipya. Ukafanyia kazi hofu yako. Ona  sasa hivi unaweza hata kukimbia na kufanya mazoezi!” “Asante kwa kuniazima miguu yako Naih.” Kenny akajikuta machozi yakimtoka.

“Ulikuwa miguu yangu, na kunifikisha kule nitakapo! Umenisafisha mpaka kinyesi changu! Umenivumilia, na kuwa faraja yangu. Umenisamehe na kunipokea wakati watu wananikimbia! Umekuwa ukinipa maneno ya faraja wakati wengine walikuwa wakinikejeli. Asante.” Kenny alishangaa kumuona Naih anavua nguo. “Vipi tena!?” Kenny akauliza. “Mimi naona hiyo shukurani yako iwe kwa vitendo.” Kenny alicheka mpaka machozi ya huzuni yakageuka yafuraha.

“Hivi huwa unanisikiliza lakini.” “Mpaka uwe umenikumbatia ndio nasikia vizuri.” Kenny hakupoteza muda, hofu ya miguu ya bandia ilishamwisha, akaweza kufanya yale yote aliyokuwa akiyatamani kumfanyia Naih akiwa na miguu. “Usije kuniangusha bwana Kenny!” “Wewe si ulitaka shukurani ya matendo? Ndio utulie.” Ilikuwa furaha kati ya wanandoa hao, marafiki. Waliongeza siku nyingine mbele baada ya kuruhusiwa hospitalini, ndipo wakarudi nyumbani.

 Naih & Kenny warudi nchini Tanzania.

M

iezi mitatu ilikuwa imepita tokea waondoke nchini. Marafiki na ndugu wa karibu walikuwepo uwanjani hapo wakisubiri ndege iliyowabeba Kenny na Naih itue. Kenny aliwakatalia wazazi wake wasiende huko kuwatembelea. Alitaka na wao washuhudie kile kilichotendeka nchini India. Ni kweli ulikuwa muujiza. Kenny alitoka uwanjani akiwa anatembea, tena amevaa viatu kabisa. Usingejua kama anamiguu ya bandia. Ikawa jambo la furaha uwanjani hapo, wakakubaliana na nguvu ya pesa na tekinologia nzuri.

Walipelekwa mpaka kwenye nyumba aliyokuwa amekabidhiwa Naih siku ya harusi yao. Mama Ole alitafuta mtaalamu wa kupangilia nyumba. Basi kila kitu kilipangwa kwa ufanisi na sehemu yake. Naih na Kenny wenyewe wakavutiwa vilivyo. Palikuwa pazuri pakuvutia macho ya yoyote hata wenye majumba ya thamani vipi, ungeingia hapo ungejua ipo pesa na ujuzi mkubwa sana ulitumika hapo.

Walikula chakula cha usiku pamoja na wageni wote waliokuwa wamehudhuria uwanja wa ndege kumpokea Kenny, zaidi marafiki zake Kenny, ndipo Naih alipomwambia Kenny kuwa alikuwa mjamzito. “Kwa nini hukuniambia!?” “Sikutaka kukuingilia na mazoezi uliyokuwa ukifanya Kenny. Ulikuwa na hofu, sikutaka kukupa habari nyingine ambazo sikujua utazichukuliaje.” Kenny alifurahi sana na kutangaza palepale kuwa wanatarajia mtoto wa kwanza.

****************************************

Ukweli Kenny alibadilika. Kutoka kuwa mpenda starehe, akiendekeza ngono kwa sana, nguvu akahamishia kanisani. Akaanza kwenda kanisani kule  alikokuwa akiabudu Tuse.


Ile elimu ya kutumia vyombo waliyokuwa wakiletewa walimu nyumbani ikawekwa kwenye matumizi walipofika hapo kanisani. Yeye akawa akipiga ngoma, na Naih kinanda. Walibadilisha vyombo vya mziki kwa pesa zao. Kenny alinunua ngoma za umeme alizokuwa akipiga yeye mwenyewe. Na mkewe akamnunulia kinanda kizuri sana, alichokuwa pia akikitumia palepale kanisani. Wakawa wakristo wa kwenda kanisani na kumuabudu Mungu kwa kweli.

Maisha yao yalijaa utulivu, na kweli Mungu alimbariki Naih kizazi, akamzalia Kenny watoto watano ambao wote walikuzwa kanisani. Ndoa ya wazazi wa Kenny ilipona, na wao Mungu aliwajibu kwa kupata wajukuu hao. Mapenzi ya mama Ole yalihamia kwa wajukuu zake. Alikuwepo kulea wakati wote, kazi ya Naih ikawa kushika mimba na kuzaa huku wakifanya biashara na mumewe kwa kusaidiana kwa karibu sana.

Jay hakurudisha mahusiano na wazazi wake. Hata watoto wake aliwaambia wazazi wake walifariki yeye akiwa mtoto mdogo sana. Hakuwahi kurudi tena nyumbani kwao. Kwa hiyo kipindi alichokuwa anakuja nchini na mkewe na watoto, ndugu aliokuwa nao ni Kenny na Emma tu. Hata mkewe hakuwahi kumtambulisha kwa wazazi wake.

************MWISHO********

 

 SIMULIZI  HIZI ZINAPATIKANA PIA, WASILIANA NAMI KWA MAELEZO ZAIDI.

naomisimulizi@gmail.com


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment