Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com CHOZI LANGU! - SEHEMU YA 1. - Naomi Simulizi

CHOZI LANGU! - SEHEMU YA 1.

 Lara alifika kituo cha mabasi makubwa yatokayo mikoani akiwa na rafiki  zake  waliokuwa wamemsindikiza kwenye kitchen party  yake aliyokuwa amefanyiwa na  shoga za mama yake nyumbani kwao, Dodoma, akitegemea kumkuta mchumba wake Jax akiwasubiria kituoni hapo ili kuwarudisha  nyumbani kwao. Lara aliwasiliana naye mara ya mwisho kwa ujumbe walipokuwa wanapita Chalinze kumtaarifu walipo ili kama anashuguli zake basi ajue wanakaribia kufika. Aliona ujumbe umefika, ukasomwa, lakini hapakuwa na jibu. Alimjua mpenzi wake yupo na majukumu mengi, kwenye ajira hiyo mpya aliyokuwa amepata mwaka mmoja uliopita, kutoka benki ya CRDB mpaka world Banki, lakini si kwa kiasi chakushindwa kujibu hata neno, ‘OK’! Wasiwasi ukamwingia Lara.

Basi lilipofika Kibaha, akampigia. Ikaita mara mbili tu, ikakatwa. Walipofika Kibamba akampigia tena, ikaita mpaka mwisho, safari hii haikupokelewa kabisa wala haikukatwa. Lara akashangaa. Akaamua kumtumia ujumbe. ‘Vipi babe, kwema? Nakaribia kufika.’ Safari hii hata ujumbe haukuonekana kufika. Wasiwasi ukazidi kumtesa Lara. Si kawaida ya Jax!

Walifika Ubungo na marafiki zake watatu, na wote walikuwa wakifanya   kazi sehemu moja, kwenye kampuni ya simu. Alishawaambia tokea jana yake kuwa Jax atakuwepo standi ya mabasi akiwasubiria kama alivyoahidi Jax mwenyewe. Marafiki zake walikuwa wamejawa cheko wakikumbushiana taarabu na jinsi msasambuaji alivyokuwa akicheza jana yake kwenye kitchen party ya Lara. Walikuwa wakicheka mpaka machozi, wasijue wasiwasi wa bibi harusi waliye naye hapo.

Wote walishuka kwenye basi, Lara akijiaminisha atamkuta tu Jax nje ya basi akiwasubiria, lakini hakuwepo. “Si ulisema Jax atakuwepo hapa akitusubiria?!” Sesi akauliza. “Amebanwa kazini. Tuchukueni taksii tu.”  Wakaangaliana marafiki hao bila wazo la pili, wakakubali kupanda taksii.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lara na warembo hao watatu walijikuta wametoka chuo, wapo jijini wakifanya kazi kwenye kampuni hiyo ya simu. Wakaamua kuchukua sehemu, waishi pamoja wakichangia garama. Maisha yakaendelea kwenye hiyo nyumba yao ndogo tu bila shida wala matatizo. Warembo hao wanne wakiishi pamoja na kufanya kazi sehemu moja. Wote hawakuwa wameolewa ila sasa Lara ndiye aliyekuwa hata na mahusiano ya uhakika na kutamaniwa na wengi, ndiye huyo alikuwa amebakiza siku chache sana kufunga ndoa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lara hakumsikia Jax mpaka  usiku. Simu yake iliita, akaamka kama mshale. Alijua ni Jax tu. “Vipi Jax!?”  “Aisee pole sana.  Asubuhi nilidamkia Kisarawe. Jamaa alikubali kutuuzia lile shamba. Tumetoka hapa na Tino, kufika kule kumbe nilikuwa nimesahau simu nyumbani. Sikuwa na wasiwasi kwa kuwa nilijua tutawahi! Si mchezo!” Lara akabaki kimya akimsikiliza tu.

“Kuna gari ilianguka katikati ya barabara, halafu mvua ilikuwa ikinyesha Kisarawe, kama mafuriko!” Akaendelea kutoa sababu, lakini zilikuwa na maswali nyuma yake. Lara akajiuliza hili na lile wakati akimsikiliza. “Kwa nini asitumie simu ya Tino kuwasiliana na mimi!?”  Akajiuliza Lara. Lakini hakutaka kutibua mambo.  Akaona anyamazie, yaishe.  Zilikuwa zimebaki siku 13 tu wafunge ndoa. Hakutaka lolote liharibike. Akaona afunike kombe, mwanaharamu apite.

“Pole.” Akaongea Lara kwa sauti ya chini kidogo ya mashaka, lakini ya aliyekubali yaishe tu. “Asante. Yaani ndio nimeingia muda sio mrefu. Nipo hoi!” “Basi nikuache upumzike. Tutazungumza kesho.” “Nitakupigia kesho nikiwa nimepumzika vizuri ili unipe habari za kitchen Party.” “Nilifikiri ulisema kesho tutakuwa wote kwa chakula cha mchana!” Lara akashangaa kidogo.

“Kichwa kimechanganyikiwa kwa kuchoka. Basi tutapanga vizuri kesho asubuhi tukiamshwa salama. Usiku mwema.” “Nakupenda Jax. Naomba usisahau hilo.” Lara aliongea kwa kumaanisha. Jax akatulia kidogo. “Jax!” “Asante Lara.” Akajibu tu hivyo, na kukata simu.

 Jumatatu

Baada ya Kitchen Party.

W

ote wanne walikuwa wakitumia gari ya Lara, aliyokuwa amenunuliwa na Jax miezi 7 iliyopita kama kishika uchumba, alipomchumbia nyumbani kwao, Dodoma. Ilikuwa kama Suprise, hata Lara hakuwa akijua. Alijua atavikwa tu pete na kulipiwa mahari, lakini Jax alimvisha pete na kumkabidhi hilo gari mbele ya umati. Sasa hilo gari likawa msaada mkubwa sana si kwa Lara tu, hata hao wenzake aliokuwa akiishi nao hapo. Kwa mizunguko yao mjini, zaidi kuwahi kazini. Walichofanya ni kuchangishana pesa ya kuongeza mafuta ya gari hiyo tu.

Asubuhi hiyo ya jumatatu baada ya weekend nzuri huko jiji kuu la Tanzania, wakatoka na gari ya Lara kama kawaida yao, wakafika kazini kila mmoja akaanza kazi huku wakisimulia wafanyakazi wengine mambo ya kitchen Party. Ukajaa utani kwa Lara, wakimwambia yupo tayari kwa ndoa, kwani amefundwa vilivyo. Lara akicheka tu, moyoni akiwa hana amani moyoni.

Mpaka inafika mchana, muda wake wa kwenda kula, Jax hakuwa amepiga simu wala kutuma ujumbe. Lara akamtumia ujumbe.  ‘Vipi, bado nikusubiri kwenda kula  pamoja.’ ‘Nimebanwa hapa  kazini! Vikao haviishi! Nenda tu, nitakutafuta  baadaye.’ Lara akatazama yale majibu,  akabaki ameduaa kwa muda.

Akatoka na marafiki zake kwenda kula. Walipokuwa wakisubiria chakula, wakasikia, “Shemejiiiiii!” Lara akajua ni yeye, akageuka huku akicheka. “Bwana shemeji unazidi kuwiva!” Tino akamsifia Lara, akacheka. “Mzima lakini?”  “Mzima Tino. Jana nilijua mtakuja kutupokea kumbe....” “Jana bi Mkubwa  alikuwa anadeka! Alitaka nimpeleke kanisani, kisha nikae naye. Jana nimetajiwa mpaka majina ya wake za mababu na babu zetu!” Wengine walicheka na kuendelea kutaniana na Tino, lakini si Lara.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tino ni rafiki kipenzi wa  Jax. Tokea chuoni, mpaka  ajira yao ya kwanza kwenye benki ya CRDB. Ndipo mwaka mmoja uliopita, Jax akabahatika kazi kwenye benki ya dunia. Lakini hakuna linaloendelea kwa Jax, Tino asijue. Hivyo hivyo kwa kwa Tino. Wawili hao walitokana kuelewana  tokea chuo mpaka wakati huo. Tino alikuwa mmoja wa  marafiki  walio msindikiza Jax kwenye sendoff aliyofanyiwa Lara nyumbani kwao Dodoma. Kwa hakika waliweka heshima kwenye jamii inayowazunguka familia hiyo ya kawaida sana ya kina Lara. 

Jax na rafiki zake wakiwemo wafanyakazi wenzake waliokuwa wakifanya kazi pamoja CRDB na alipo sasa hapo kwenye benki ya dunia, pamoja na Nelly dada na mzazi pekee wa Jax, walifika jijini Dodoma na magari ya kifahari. Kabla ya tafrija hiyo usiku, walialikwa nyumbani kwa kina Lara kwa chakula cha mchana. Walifunga mtaa kwa magari mazuri. Tafrija yenyewe ilikuwa  simulizi!

Nyumbani kwa mzee Chiwanga, walizaliwa mabinti watatu tu. Lara akiwa mtoto wa mwisho na dada wawili waliofanana kama mapacha na mama yao. Lily ambaye yeye ndio alikuwa dada mkubwa, aliishia kidato cha tano, alipopata ujauzito. Shule yake ikaishia hapohapo lakini akaletea familia hiyo mtoto wa kiume, Lucas, ambaye naye alilelewa hapo kama kiziwanda wa familia wala si mjukuu. Mama yao alimpenda huyo mtoto, ungedhani ni wake aliyemzaa na si mjukuu. Binti mwingine alikuwa Lea, ambaye ni wakatikati kuzaliwa, yeye alikuwa mwalimu wa shule ya msingi hapohapo jijini Dodoma. Na yeye hakuolewa na wala hakuwa na mchumba. Na wote walikuwa wakiishi nyumbani kwa wazazi wao.

Japokuwa wazazi wao hawakuwa na uwezo mkubwa, lakini waliwapenda hao binti kiasi cha kutengeneza mazingira ya watoto wao kujisikia salama zaidi hapo nyumbani kwao. Mfano wa ndoa waliokuwa nao ni ndoa ya wazazi wao na wote walitamani kuja kuwa na ndoa kama ya wazazi wao. Kila mmoja wao alikuwa akitafuta kupendwa kama vile walivyoona mama yao akipendwa hapo na baba yao. Wakabaki kusubiri mume mwema kama baba yao.

Lara ndiye aliyekuwa binti wa kwanza kwenye familia hiyo kuleta mchumba, kulipiwa mahari na kufanyiwa sherehe ya kuagwa kwenye familia hiyo. Ilikuwa furaha na faraja kubwa sana kwenye familia yao. “Hatimaye na sisi tunachangiwa kwenye harusi ya mtoto wetu!” Akafurahia mama Chiwanga. Hata dada zake walimpongeza mdogo wao na kusimama naye katika maandalizi ya harusi yake. Walikuwa ni mabinti walioshikana haswa na walipendana kwelikweli. Mafanikio ya mmoja wao ni ya wote. Dada zake Lara walikuwa watulivu sana kama mama yao, si kama Lara aliyekuwa mtundu na maneno mengi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Ni nini kinaendelea kwa Jax!?” Ni swali alilobaki nalo Lara siku nzima akiwa kazini. Mambo yao yalikuwa yakienda vizuri tu. Hapakuwa na ugomvi wala kupishana neno.  “Kwa nini anidanganye? Nini kinaendelea?”  Akajiuliza Lara. “Mungu nisaidie tafadhali. Nakusihi Baba yangu wa mbinguni, lolote lisitokee.” Wasiwasi ulizidi kumpata Lara, mpaka akaamua kumuomba Mungu. Ilikuwa jioni wanatoka kazini kurudi nyumbani kwao. Hakuwa amemsikia Jax mpaka muda huo.

Ilikuwa imebakia kitchen Party ya hapo jijini ili wafunge ndoa. Wafanyakazi wenzake ndio walikuwa wamemuandalia jumamosi hiyo kabla ya harusi yao, ambayo ilikuwa jumamosi inayofuata. Alipanga mambo yake vizuri. Alihakikisha hachukui likizo mpaka baada ya kufunga ndoa, ndipo waende kwenye fungate na Jax. Kwa hiyo hata tafrija za nyumbani kwao, alijitahidi ziwe siku ambazo hafanyi kazi. Weekend, ili jumatatu awepo kazini. Akafanikiwa zote. Hapo alikuwa amebakiza hizo tafrija mbili tu ya kitchen Party ya hapo ofisini kwao na mashoga wa jijini Dar walioshindwa kuhudhuria Dodoma, nyumbani kwao, halafu ndipo harusi sasa.

Watu walishachanga. Zawadi za pamoja kama za ofisini kwao zilikuwa zimeshanunuliwa. Sare ya kuvaa siku hiyo wengine zilikuwa kwa fundi zikimaliziwa kushonwa na wangine walishachukua nguo zao wakisubiria tu siku yenyewe. Ofisini shamra shamra, marafiki zake pia shamra shamra kwa ajili ya Lara aliyekuwa akitarajia kuolewa na Jax, kijana aliyetamaniwa hata na mashoga zake. Hata kama angekuwa na sura mbaya, Jax anafanya kazi kwenye benki ya dunia! Kishika uchumba ni gari! Nani asingetamania bahati hiyo! Lara akawa gumzo kwa wanaomjua, hata marafiki walisimulia marafiki zao wengine na familia.

Tokea mpenzi wake ahamie ajira katika benki hiyo ya dunia, hata Lara alibadilika vaa yake, simu anazotumia, viatu na nguo. Ulikuwa ukimuona Lara, utajua anatunzwa vizuri. Kwa asili Jax hakuwa mchoyo na walikuwa wakielewana sana na Lara. Swala la kupika na kupakua nyumbani kwa Jax, lilikuwa la kawaida sana kwa Lara. Mara nyingi siku za ijumaa mpaka jumapili usiku au jumatatu, Lara alikuwa nyumbani kwa Jax. Walitumia weekend nyingi pamoja, labda Jax awe amesafiri.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walifika nyumbani kwao, Lara akiwa mwingi wa mawazo. Aliingia kuoga nakuamua kwenda nyumbani kwa Jax ili angalau kujionea na kuzungumza naye. Akatoka hapo kwao Kinondoni akiwa amependeza tu, akitumia gari yake bila hata kuaga shoga zake. Kila mmoja alikuwa chumbani kwake akifanya lake. Jax alikuwa akiishi kwenye nyumba yakupanga maeneo ya Sinza Mori, alichukua kama upande mmoja wa hiyo nyumba. Palikuwa padogo tu wala si pakubwa. 

Shilingi Yapinduka Pabaya!

L

ara alifika mpaka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na Jax. Akaacha gari yake nje ya geti, akaingia ndani kwa haraka baada yakusalimia watu aliowakuta nje ya duka walilokuwa wakipenda kununua vinywaji nje ya nyumba hiyo kwa mbele ambako mwenye nyumba aliweka fremu aliyotumia kama duka. Alifika ndani, hakukuta gari ya Jax na kulikuwa kumefungwa. Akampigia. Simu haikupokelewa. Akajaribu tena, safari hii haikuwa tena hewani. Akakunja uso. Ilishakuwa saa mbili na nusu usiku. Jax alitakiwa awepo nyumbani!

Lara akaingiwa na wasiwasi. “Isije kuwa ameanguka humo ndani!” Akashika tena kitasa cha geti dogo lililopo nje ya mlango. Akatingisha mara kadhaa, wazi lilionekana limefungwa na funguo. Akachungulia ndani, akakuta patupu kabisa, hakuna hata kochi! Akashituka sana.

Akatoka kwa haraka mpaka nje kwa mwenye duka. Walishazoena na Lara ambaye ni kama na yeye alikuwa akiishi hapo. “Niambie mtoto mzuri.” Mama mwenye nyumba hiyo akiendelea kuhudumia wateja wa dukani hapo, akamuwahi Lara kwa uchangamfu mara alipomuona tu amesogelea hapo. “Umemuona Jax leo?” Lara akauliza. “Mmmh! Labda kama alipita tena asubuhi nikiwa nimetoka. Ila tokea amalizie kuhama hapa jumamosi, sijamuona amerudi. Kwani alisema angerudi tena?” Lara akabaki kama amepigwa na butwaa.

“Mjaribishe kumpigia simu. Lakini sidhani kama atarudi tena hapa, labda kusalimia. Maana nilimuona baba mchana wa leo tu akiwa na mpangaji mwingine, tena amemuongezea na bei. Halafu alikuwa akisifia kuwa mmeiacha nyumba yetu vizuri, hana matengenezo yeyote labda kama mpangaji mpya atataka kupakiwa rangi ingine. Nafikiri atampangisha tu.” Huyo mama akamalizia hivyo, huku akihudumia wateja wake kwa uchangamfu kama kawaida yake.

Lara akaondoka bila hata kuaga wala kujibu. Akapanda ndani ya gari yake, akaondoka pale. Akahisi anaweza kuchanganyikiwa. Akasimamisha gari yake pembeni ya barabara kabisa, akampigia simu Tino. “Niambie mtoto wa jiji kuu! Shemeji yangu mimi.” “Ni nini kinaendelea Tino?” Akauliza Lara. “Mbali na habari ya mjini, hakuna jingine. Mpaka tukuweke ndani, ndio masikio yatasikia mengine.” Tino akajibu kwa utani.

“Jax yupo wapi?” Akauliza tena Lara. “Leo sijamsikia Jax. Lakini jumatatu zake si unazijua?” “Wewe unajua kama amehama Sinza Mori?” Tino kimya kwa muda. Akaitizama simu yake. “We Tino?” “Kwani wewe si ni Lara, na tunamzungumzia Jax, au nishalewa tayari?” “Ni nini kinaendelea Tino?” “Juu ya nini tena!?” Tino na yeye akawa kama haelewi tena.

“Jax yuko wapi, na amehamia wapi?” “Jax yupo kwake!” “Kwake wapi?” “Si Sinza Mori!”  Tino akajibu kwa uhakika. “Jax amehama pale.” “Jax! Lini!? Unauhakika?” Tino akasikika kama amepatwa na sintofahamu zaidi. “Nimetoka pale sasa hivi. Mama mwenye nyuma ameniambia amehama tokea jumamosi, hivi wanatarajia mpangaji mwingine. Wewe ulikuwa unajua kama anahama?” Lara akauliza.

 “Yaani wewe ndio unaniambia sasa hivi! Ila ninachojua, aliniambia miezi kama minne iliyopita kuwa mkataba wake unakaribia kuisha karibu na harusi yenu. Alikuwa akifikiria labda muhame pale baada ya mkataba kuisha, ili mkifunga ndoa, mkaishi kwenye nyumba kubwa zaidi. Pale alipaona ni padogo. Hatukulizungumzia hilo tena.” Kimya.

“Lara?” Tino akaangalia simu yake na kumuita. “Ni nini kinaendelea Tino? Tafadhali usinifiche. Nina hali mbaya sana.” “Naomba usipaniki Lara. Inawezekana mambo ya suprise. Anataka akusuprise nyumba mpya mara baada ya fungate kama alivyofanya kwenye gari aliyokupa. Si unakumbuka hata mimi hakuwa ameniambia juu ya hiyo gari, wote tukashangazwa siku ya kulipiwa mahari yako na kuvalishwa pete ya uchumba!” Akajaribu kumtuliza.

“Unafikiri hivyo Tino?” “Kabisa. Sioni sababu nyingine. Jamaa ameamua kukuoa Lara. Na ninamjua Jax. Hana mambo ya wanawake tuseme amebadili mawazo kwa ajili ya mwanamke mwingine! Wewe ni shahidi. Halafu kama nilivyokuwa nimekwambia. Jax alishatoa pesa yake yote aliyokuwa ameahidi kwenye kamati tokea mwanzo kabisa, mpaka jamaa wakashangaa. Mwenyewe Jax akasema amekusudia kukuoa. Sina mwanamke ninayemjua hata kumuhisi yupo karibu kimapenzi na Jax. Na wewe unajua, kama angekuwepo mimi ningekuwa wakwanza kujua. Na Lara, wewe ni wangu. Unajua nisingekuficha.” Lara akavuta pumzi kwa nguvu.

“Nina wasiwasi, nimeshindwa kula.” “Kwa nini? Nakuhakikishia kila kitu kipo sawa.” “Sijui Tino. Unajua tokea ijumaa sijazungumza na Jax! Tulipanga aje anipokee na wenzangu siku ya jumapili, lakini hakuja.” Lara akaanza kulia.

“Usilie bwana.” “Nina hisia mbaya Tino. Nahisi kuna kinachoendelea. Nimeshindwa hata kuendesha gari. Nimeegesha hapa barabarani.” Akamuelekeza alipo. “Nahisi miguu imekufa ganzi. Nimechanganyikiwa Tino, shemeji yangu.” “Mimi nahisi unapatwa na wasiwasi wa bure! Tulia bwana. Nakuja. Sipo mbali na hapo.” Wakakata simu.

Lara akaanza kumpigia simu Jax bila mafanikio. Baada ya kama dakika 15 hivi, Tino naye akafika hapo. “Nahisi simu yake ina matatizo. Simpati.” “Hata mimi Tino. Na kinachonitia wasiwasi amenidanganya.” Tino akakunja uso na kupanda kwenye gari ya Lara.

“Amekudanganya nini?” “Kwanza alianza kukata simu zangu, baada ya kuacha kupokea. Nikajaribu bila kuchoka, jumapili usiku akanipigia akaniambia mlikuwa naye Kisarawe kununua yale mashamba ya wakati ule tulikwenda, tukashindwana na wanakijiji.” Tino akakunja uso na kunyamaza.

“Na aliongea uongo wa muda mrefu tu, akisema mvua iliwakuta huko njiani na mkakuta gari imepata ajali katikati ya barabara ikasababisha foleni. Yaani usiku ule ndio alisema ndio mnarudi nyumbani. Amechoka, atanitafuta leo. Sijamsikia tena. Na ndio nikaambiwa amehama.” Tino akafikiria kidogo.

“Sababu kubwa ambayo naweza kuwanayo ya bila kukudanganya na vile ninavyomjua Jackson, ni kuwa, anataka kukufurahisha tu. Suprise.” “Ndio mpaka anidanganye!? Jax sio muongo Tino. Nahisi kunalinaloendelea. Tafadhali nisaidie kujua ukweli kabla sijaingia aibu hapa mjini. Nitajificha wapi kama akinigeuka?” “Jeuri hiyo hana. Kwanza anaanzia wapi kupata mwanamke kama wewe! Sio kwamba nakupamba, ila Jax anakupenda na anasema wazi wewe ndiye mwanamke wakuweka ndani. Hawezi kubadilika.” Lara akabaki kimya.

“Basi ili kukuhakikishia kuwa hakuna jambo, acha niende kwa dada yake usiku huuhuu. Yeye atakuwa anajua ukweli.” “Labda safari hii dada yake amefanikiwa kumwingia kichwani akaona kweli mimi simfai mdogo wake, ameamua kuniacha!” “Ngoja nikuhakikishie Lara. Nelly hamuamini yeyote na mdogo wake. Hata mimi alishakuwa na wasiwasi akihofia nitampoteza Jax kwa pombe. Tokea tupo shule alikuwa hanipendi. Tumekuja kuzoeana na dada yake au hata kupokea salamu yangu tulipokuwa chuoni tena mwaka wa pili tukienda wa tatu. Mimi nilikuwa nikienda nyumbani kwake kumfuta Jax, hakuwa hata akiningalia mara mbili. Na ikitokea yeye ananifungulia mlango, ananiacha mlangoni bila hata kuniambia karibu.” “Kweli Tino?” Lara akataka uhakika.

 “Kwani Jax hajakwambia? Alishamwambia hataki kumuona na mimi. Ni vile tu tulitokea kuelewana sana na Jax, na Jax mwenyewe alikuwa mtu mwenye msimamo. Akaniambia nisijali. Nia ya Nelly ni nzuri. Hataki aharibikiwe. Nikaendelea kwenda nyumbani kwake hivyohivyo mpaka sasa hivi tumegeuka mabesti. Acha niende nikazungumze naye.” Tino akataka kushuka.“Tino!” Akaita Lara kwa upole.

Tino akajirudisha kitini vizuri na kumwangalia Lara. “Ikitokea unakuta jambo baya huko juu ya hatima yangu mimi na Jax, utakuwa muungwana uniambie kuliko kunikimbia kama Jax?” Tino akababaika kidogo. “Naomba uchukue nafasi yangu Tino. Nifikirie ndugu yangu. Usiniache hivi. Ninalo mpaka gauni la harusi na la kitchen party ya hapa Dar! Jumamosi hii ndiyo siku ofisini wananifanyia party kama kunipongeza. Watu wameshachanga, nita..” “Acha bwana Lara. Acha woga. Nakuhakikishia kila kitu kipo sawa. Na nitakupigia simu kabla ya kwenda kulala. Naomba tulia. Sawa?” “Sawa.” Lara akakubali kwa shingo upande wakaagana kwa makubaliano ya Tino kwenda kumuona dada yake Jax, nyumbani kwake Masaki. 

Usiku wa giza nene.

I

lishakuwa mida ya saa nne wakati Tino anamsalimia mlinzi anayelinda nyumba ya dada yake Jax. Tino akaenda mpaka mlangoni kubonyeza kengele. Bila kuchelewa mlango ukafunguliwa. “Naomba na wewe usiniharibie usiku wangu zaidi.” “Shikamoo!” “Marahaba.” Nelly akaacha mlango wazi na kurudi sebuleni. Tino akamfuata nyuma.

“Kwema?” Tino akamuuliza. “Uniambie wewe!” Tino akamwangalia vizuri kama anayetaka ukweli usoni kwake. “Unashangaa nini?” “Jax yuko wapi?” “Kwani hapa kwake na wewe? Acha kunichanganya.” “Labda nikuulize, mara ya mwisho kuwasiliana na Jax ilikuwa lini?” “Ametoa kichwa chake hapa muda si mrefu. Kama nusu saa tu. Aliponiacha hapa nimekaa, hata sijaweza kunyanyuka.” Tino akatulia kidogo. Nelly akimtizama.

“Mimi simpati kwa simu.” “Ameniambia.” Akajibu dada yake. “Ni nini kinaendelea dada Nelly?” “Mimi nipo kama nimepigwa na butwaa. Naona umsubiri mwenyewe, amesema atakuja kukutafuta akiwa tayari kuzungumza na wewe.” Tino akakunja uso.

“Tangia lini mimi na Jax tumeanza huo utaratibu wa kuwasiliana kwa utayari!?” “Tokea alipoamua kumuacha kile kitoto Lara, na kurudiana na Tula.” “Tul, Tull, Tu!” Tino akakwama. Akatulia kidogo, akajirudisha nyuma. Nelly akabaki akimtizama. “Samahani dada Nelly. Tula huyu ndiye yule aliye aliye...” “Ni Tula huyo huyo unayemjua wewe. Aliyekuwa akimfanya Jax kama mwehu. Akaondoka hapa na mzungu, akakimbilia Norway, sasa amerudi. Amemuomba Jax msamaha, Jax anasema ameamua asamehe. Ndio huyo.” “Kweli Jax anarudi kwa Tula!” Tino akashangaa akisikika kuumia sana.

 “Mimi najua humpendi Lara, dada Nelly, lakini...” “Subiri kwanza Tino. Kabla hujanikorofisha, nataka unielewe wazi kabisa. Sipo upande wa Tula wala Lara. Na sio kwamba sitaki Lara aolewe na Jax. Kumbuka nimetoa mamilioni ya pesa kwenye hiyo harusi. Mimi sio mjinga.” Nelly akawa mkali kama kawaida yake.

“Nilikuwa na wasiwasi na Lara kwa kuwa alikuja baada ya Tula. Lara anaonekana mjanja mjanja. Kama kamapepe hivi!” “Lara si mapepe, dada Nelly!” “Basi niseme hajakomaa akili. Sikutaka habari za Tula zije zijirudie kwa Jax. Ndio maana ilibidi kuwa makini sana kwa kila msichana aliyekuwa akijisogeza kwa Jax, ili nijue nani mkweli nani tapeli.” Nelly akaendelea.

“Baadaye sasa ndio nikaweza kukosoma Ka-Lara. Nikagundua kumbe nikatoto kazuri tu. Hata nikaona mabadiliko kwa Jax mwenyewe. Amekuwa mtu ambaye anaongea mipango ya kiutu uzima. Akahama hapa na kutafuta kwake. Na mengine mengi mazuri. Moyoni. Narudia tena, moyoni, nikajiambia inamaana amepata msichana mwenye akili tofauti na Tula. Akaanza kuishi tofauti na alivyokuwa akiishi alipokuwepo Tula kwenye maisha yake. Hasira kila wakati na kuishiwa hovyo.” Nelly akaendelea.

“Japokuwa sikuwahi kuwa karibu na Lara, lakini nikajua yeye ndiye anayemuongoza Jax vizuri. Maana Jax alianza kuniletea hata zawadi, kitu ambacho sikuwahi kumuona akifanya tokea mtoto. Na zawadi alizokuwa akileta, hazifananii kabisa na Jax. Kwa hiyo nikajua wazi zinatoka kwa Lara. Aidha kwa kutumia pesa zake mwenyewe Lara, au anamuomba Jax pesa na kwenda kuninunulia. Sijui. Ila nikajua kabisa, kunakouzwa hizo zawadi ninazoletewa kwangu, Jax hawezi kufika na sisi wote tunamfahamu Jax. Hana akili ya kumfikiria mtu, japo si mchoyo. Akili yake haiwezi kumtuma kumnunulia mtu zawadi, japo ukimuomba pesa, atakupa na hata kama hana, atahangaika mpaka aipate, akupe. Kwa hiyo nikaridhika kuwa Lara anamuongoza vizuri.”

“Aliposema anataka kumuoa, sikumuuliza swali. Mliponipa bajeti ya harusi, sikuuliza swali zaidi ya kukutafuta na kukupa mchango wangu. Au umesahau?” “Sijasahau. Sasa kwa nini umetoa baraka zako na kwa Tula!?” Tino akaongea kwa kulaumu kidogo. “Nani amekwambia nimetoa baraka zangu kwa Tula!?” Akauliza kwa kushangaa. “Tokea lini umemuona Jax ananisikiliza mimi linapofika swala la kuamua kwake?” Akaendelea kumuhoji.

“Wewe mwenyewe nishahidi. Nilimkataza asiwe na wewe. Si mara moja! Zaidi ya miaka miwili. Alikuacha urafiki?” Kimya. Nelly akaendelea. “Haya, nilimkataza juu ya Lara. Mbele yako. Alimuacha!?” Kimya. “Nakuuliza wewe Tino.” “Wote tunajua majibu yake.” “Kama unayajua majibu, ni kipi sasa kinachokufanya ufikiri nahusika au naweza kumbadilisha sasa hivi? Najiangalizia na kunyamaza kimya.”

“Alikuja hapa. Alinieleza nikiwa nimekaa hapa, akaondoka na kuniacha hapahapa bila kumjibu, wala kumuuliza lolote. Aliyaongea yote, alipoona kimya, akaaga na kuondoka. Sasa kwa kuwa mimi namjua, najua atakuwa ameshafikia maamuzi na amefikiria nini chakufanya, sikutaka kujichosha.”

“Sasa itakuaje?” “Juu ya nini?” “Unaulizaje swali kama hilo dada Nelly!?” “Sijakuelewa.” “Juu ya Lara!” “Ndio ndoa kwa Jax ajue imekufa hivyo.” “Dada Nelly!?” “Kumbe? Kwani yeye atakuwa wakwanza? Ndoa zinavunjika ije kuwa uchumba! Yeye si wa kwanza na wala hatakuwa wa mwisho.” Nelly aliongea bila kumumunya maneno kama kawaida yake. “Daah!” Tino akainama akimfikiria Lara.

“Tino, naomba mimi nikalale. Kama unalala hapa, niambie nikafunge mlango tulale. Kama unaondoka naomba iwe sasa hivi, ondoka nifunge mlango nikalale. Wengine ajira zetu ndio waume zetu. Binadamu wana mengi. Hayatabiriki. Sasa usiniharibie kwangu kwa ajili ya Jax.” “Na michango ya watu?” “Afadhali umenikumbusha. Sasa, kabla hujaanza kurudishia watu wengine pesa zao, tafadhali, kesho kabla sijaanza kikao cha kwanza ofisini, uwe umenirudishia pesa yangu. Mapemaa kabla sijakutafuta nikaanza kikao na wewe. Unanisikia Tino?” “Nishalipia ukumbi na...” “Hayo hayanihusu. Narudia tena. Kesho, kabla sijakutafuta, hakikisha nimepata pesa yangu yote kama nilivyochanga.” Nelly akasimama na kusogelea mlango.

“Naomba uondoke.” Tino akasimama. “Na ninakushauri wale wakorofi wote waliochanga, wawe wa kwanza kulipwa, kabla wewe na mwenzio hamjaniharibia jina langu hapa mjini. Unanisikia Tino?” Tino akabaki kimya.  “Tino?” Nelly akaita kwa ukali.

“Katika hili sitanii. Sihami huu mji mimi kwa ajili yako na Jax!” “Sasa mimi nahusikaje!?” “Pesa yote unayo wewe. Lipa watu pesa zao, tumalize kwa amani. Sitaki watu waje waseme niliishiwa, ndio maana nikatoa kisingizio cha mdogo wangu kuoa ili wanichangie pesa. Wote unaowajua wananihusu mimi moja kwa moja, na walichanga kwa heshima yangu, walipe baada yangu. Haya, kaanze kuandika hundi za watu na neno la shukurani uwatumie.” Tino akabaki kama ameshangaa.

“Toka bwana Tino, nini? Unachoshangaa hapa nini?” “Siamini!” “Basi toka kafikirie nyumbani kwako au hapo chumbani. Usinicheleweshe kulala mimi.” “Naomba simu yako nimtumie ujumbe Jax. Maana amefungia simu yangu.” Nelly akarudi sebuleni kuchukua simu yake, akarudi alipokuwa amesimama Tino.

“Na ufanye haraka Tino.” Akamkabidhi. Tino akamuandikia ujumbe Jax. ‘Tafadhali maliza mambo kiume. Acha kujificha kama fala! Zaidi kwa Lara. Yupo na hali mbaya sana. Malizana na binti wa watu, maisha yake yaendelee. Acha kuwa mkatili kwa kiasi hicho! Na nipe muongozo juu ya pesa za watu, maana nyingine nilishalipia mambo ya harusi.’ Akautuma ule ujumbe.

 Tino akatoka na kwenda kukaa kwenye gari yake, akiwaza kama ampigie simu Lara, au amuache. Alikaa pale akiwa kama amepigwa ganzi. Nelly alishafunga mlango wake nakwenda kulala. Mlinzi alishamfungulia geti akidhani anatoka, lakini akabaki ndani ya gari kwa zadi ya nusu saa mpaka mlinzi akafunga tena geti, Tino bado akabaki ndani ya gari yake. “Tula!” Bado Tino hakuwa akiamini.

Maji Yazidi Unga.

L

ara alisubiri simu ya Tino mpaka akapitiwa na usingizi. Alishituka saa 6 usiku Akamtumia ujumbe. ‘Tino, bado nakusubiri shemeji yangu. Hata kama nikosa nimemtendea Jax, tafadhali niambie kama nimebakisha pakurekebisha au la. Usiniache na hii hali. Tafadhali Tino.’ Kilichomtia wasiwasi Lara hata kushindwa kurudi kulala, ni ule ujumbe kutofika kabisa.

“Haiwezekani kama hata Tino amenifungia simu zangu!”  Lara alishindwa kurudi kulala. Pressure ikazidi kupanda, akahisi hali mbaya, akaona akimbilie hospitalini kunusuru kilichobaki. Aliyempima pressure mwenye alishangaa hata aliwezaje kufika hapo. Akamuita dakitari kwa haraka. Na yeye alipompima akashauri atulie kwenye chumba cha hapohapo karibu na mapokezi, kupewa huduma ya kwanza. Wakati daktari akihangaika kushusha hiyo pressure, yeye Lara macho kwenye simu.

Ilipofika saa 9 usiku huo wa giza nene, simu yake nayo ikawa inaishiwa chaji. Akaomba chaji kwa kila muuguzi bila mafanikio. Hakuna aliyekuwa na chaji ya aina hiyo ya simu yake. Uzalendo ukamshinda. Akatoroka hospitalini kurudi nyumbani ili apate chaji ya simu yake ili endapo Tino anampigia simu, asimkose. Alikesha tumbo likimuuma, bado pressure ilikuwa juu ila macho kwenye simu mpaka asubuhi wenzake walipomgongea. Wakajiandaa, nakutoka kuelekea kazini. Aliomba mtu mwingine aendeshe, aliwaambia hajisikii vizuri. 

Ukweli Mchungu.

L

ara na wenzake walifika kazini kila mmoja akaenda kwenye meza yake wakisubiria wateja waingie mara baada ya kikao cha asubuhi cha wafanyakazi kuisha. Ilipofika mida ya saa nne, mbele ya meza ya Lara alikaa mrembo kama anayetaka kupewa huduma na Lara. “Karibu. Nikusaidie nini?” Lara alianza taratibu tu akionyesha uungwana kwa mteja. “Naitwa Tula.” “Karibu Tula. Nikusaidie nini?” Lara akauliza tena. “Nilikuwa napita tu, nikaona niingie humu ndani tuzungumze.” Akaanza Tula bila jazba wala sauti ya kishari. Lara akakunja uso kidogo.

“Kari-bu. Japo huu ni muda wa kazi. Tunahudumia wateja!” “Sitakuchukulia muda mrefu. Nilitaka tu kujitambulisha kwako. Mimi ni Tula wa Jackson au Jax. Najua unanifahamu.” Lara akahisi kuishiwa nguvu, lakini akajikaza. “Hapana, sikufahamu.” Tula akakunja mikono kifuani na kumtizama kama kumsuta. “Acha kunidanganya. Jax amenieleza kila kitu. Ameniambia alikwambia kama hatanioa mimi, basi yeyote na ndio maana alikuchumbia wewe, kwa kuwa mimi sikuwepo. Sasa nimerudi mwenyewe ndio maana unaona kimya.” Lara akabaki kimya.

“Wala usiumie. Kila mtu anatujua mimi na Jax. Dada yake ambaye ni kama mama yake ananifahamu na ananipenda sana. Na ndio maana alishindwa kukupokea wewe, kwa kuwa alijua mapenzi ya kweli ya Jax kwangu.” Tula akaanza kuvuta masikio ya watu.

“Kina Tino, Praygod, Chazi, wote wananifahamu mimi na Jax. Wapenzi wa tokea chuoni. Kwa hiyo hakuna geni wala jipya. Niliondoka nchini, sasa hivi nimerudi. Jax aliponiona tu, akaniambia kama nitamkubali, nimrudie, ataahirisha ndoa yenu.” Mwili mzima wa Lara ulikuwa umekufa ganzi. Kila mtu alibaki akiwasikiliza wao.

“Nilimwambia tujipe muda, tuangalie kama bado zile hisia za zamani zipo au la. Na ndio maana alikuomba umpishe pale kwake. Ni kwa ajili ya kutaka muda na mimi.” Hilo lilikuwa uongo. Lara akakunja uso.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ni yeye mwenyewe Lara ndiye aliyemuomba Jax kama wanaweza kuacha angalau kwa mwezi bila mapenzi ili kujiandaa na fungate. Akaacha kwenda kulala kabisa nyumbani kwa Jax. Na ndio ukawa huo mwezi wa hekaheka kwa tafrija zake yeye Lara. Sendoff na Kitchen party nyumbani kwao Dodoma.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Ni kama majuma matatu sasa tokea turudiane na Jax.” Akaendelea Tula. Bila ugomvi wala jazba lakini maneno mengi yakumuumiza sana Lara. “Tumeamua kuendeleza penzi letu. Hata yeye anaona haitakuwa sawa kwako. Akuoe wakati moyo wake upo kwangu! Hata mimi naona itakuwa si...” “Lara!” Alikuwa kiongozi wao. “Kuna tatizo lolote?” Akauliza huku akimtizama Tula na Lara. “Hamna tatizo. Nilikuja kuzungumza na Lara.” “Kuhusu maswala ya kazi?” “Mimi ni mpenzi wake...” “Kama si maswala ya kikazi, hapa sio sehemu yake. Umenielewa binti?” Yule baba ambaye ni kiongozi wao pale kazini akamkata na kumtolea macho.

“Kama huna shida yeyote ile ya kikazi, tafadhali mpishe Lara afanye kazi. Mtazungumza nyumbani.” “Naondoka lakini nilikuwa naomba funguo za gari alilokuwa amekupa Jax akijua mtaoana.” “Kamwambie Jax kama yeye ni mwanaume aliyekamilika, aje alipokonye hilo gari yeye mwenyewe. Haya simama binti kabla sijakuitia walinzi.” Tula akasimama.

“Lakini hilo gari bado ni la Jax, kwa kuwa hata kadi za gari zipo bado kwa jina la Jax. Anataka ni..” “Kwa nini wewe hushangai kama kweli anakupenda na kukuhitaji kama hivyo, kwa nini wewe upo hapa na si yeye?” “Jax yupo kazini. Ana mambo mengi. Tumetoka kula naye chakula cha mchana, ndio ameniambia mimi nije nichukue..” Akamuona yule bosi wa wakina Lara anamkonyeza mtu nyuma yake. Tula akageuka. Walikuwa askari.

“Mimi sijafanya fujo wala kumtukana mtu. Muulizeni Lara. Nimeongea kiustarabu kabisa. Ninachotaka ni funguo za gari yetu.” “Naombeni mumtoe nje, au mumpeleke kituoni. Anawezekana akawa ni tapeli.” “Mimi sio tapeli na..” Wale askari wakamvutia nje. “Jax atakuja kuchukua gari yake yeye mwenyewe. Ndio mtajua kama sidanganyi.” Tula akaongea kwa sauti ya kupayuka wakati anatolewa nje.

“Lara! Nakuomba ofisini kwangu.” Yule kiongozi wao akamuita kiustarabu kama kumtoa pale mbele ya wateja maana ni kama Lara alibaki pale ameduwaa. Mmoja wa anayeishi naye, mfanyakazi mwenzake aliyekuwa amekaa meza ya pembeni ya Lara, Sesi, akasimama na kumshika mkono. Akamnyanyua pale kwa nguvu na kumuingiza ndani upande wa ofisi za viongozi zilipo.

Wakaamua arudishwe nyumbani kwani Lara aligeuka kuwa bubu gafla. Hakuna neno lililotoka tena. Kila mtu akashangaa. Lara cha utundu, muongeaji. Hakosi jibu! Gafla kawa bubu! Bosi wao akashauri arudishwe tu nyumbani.

Sesi ndiye aliyemrudisha kwa gari yake ambayo ndiyo hiyo anadaiwa na Tula, mpenzi wa Jax. Alishuka akiwa amelowa damu. Mpaka kiti alichokuwa amekalia, kilikuwa kimelowa damu. Sesi akamsaidia kusafisha gari wakati yeye ameenda kuoga. 

Kwa Tino!

Suzy, mmoja wa wasichana wanaoishi na Lara, aliyekuwa naye kazini wakati Tula akiongea na Lara, alitoka hapo kama mbogo. Tena bila kuaga. Alitoka hapo kama apae. Moja kwa moja mpaka ofisini kwa kina Tino, mbele ya meza ya Tino bila hodi. “Nyinyi ni wanaume wa wapi ambao mnashindwa kufanya kazi za kiume, mnatuma mahawara zenu?”  Akaanza hivyo Suzy. “Washenzi nyinyi. Wapuuzi. Wajinga. Malimbukeni mnaohonga halafu mkiishiwa mnatuma mahawara zenu kuja kudai! Mmeishiwa kiasi hicho!? Mnafanya kazi kwenye mabenki. Mnakazi ya kuja kutubembeleza tukope hapa kwenu, kumbe nyinyi wenyewe hamna pesa!” Suzy akaendelea Tino akimsikiliza asielewe ni nini kinaendelea.

Akaona ujumbe wake haufiki vizuri. Akaongeza na yeye sauti huku anaangalia kila mahali zaidi ofisi ya bosi wake Tino ambaye na yeye ni meneja mikopo. “Badala yakutuma wafanyakazi wenu kutafuta wateja wakukopa hapa, anzeni kukopesha wafanyakazi wenu kwanza. Mkimaliza wafanyakazi wa hapa, nashauri muhamie kule World benki. Mkamkopeshe mwanamke mmoja anaitwa Jax, ili akaendelee kuhonga wanawake wenzake huko mtaani.” Suzy akafyonza na kuondoka.

“Suzy! Suzy!”  Suzy akawa anaondoka tena kwa mwendo kasi. “Simama basi!” “Achana na mimi. Wanaume suruali tu nyinyi. Mnajiliza njaa mpaka kwa mahawara zetu! Wapuuzi nyinyi.” Tino akakimbia mpaka mbele yake, akamsimamia, kumzuia.

“Unaongea nini!? Mbona jazba, matusi!? Haya safari hii nimefanya nini tena?” Suzy alishakuwa na mahusiano ya muda mfupi na Tino, wakashindwana tabia. “Kamuulize hawara yako Jax.” “Jax amefanya nini tena!?” Suzy akamuelezea kila kitu tokea Tula anaingia pale. Na kwa kuwa alikuwa ni Suzy, akaongeza na yake ili kunogesha lawama.

“Mkitembea hivi na hayo mashati yenu meupe na tai, mnaonekana wa maana! Kumbe shida tupu! Mwanaume anahonga halafu anadai! Mmezaliwa na wanaume nyinyi, wala si wanawake.” Suzy akaanza tena huku Tino amebaki ameduaa mbele yake. Mwishoe akamuona Tino anaondoka bila kujibu.

Kwa Jax.

M

oja kwa moja mpaka ofisini kwa Jax. Lakini akaambiwa yupo kwenye kikao. “Mwambieni ni dharula lazima atoke aje tuonane.” Akasisitiza Tino. Alipotoka tu Jax, Tino akaanza. “Najua wewe ni mkatili Jax, lakini si kwa kiasi chakumuharibia Lara kazi!” Jax akatulia. “Unawezaje kumtuma mwanamke wako akadai gari kwa Lara, tena ofisini kwake!? Kazini!? Na unajua kazi ya Lara ni kukaa pale mbele akihudumia wateja!? Lara!? Binti ambaye ulitakiwa kumuoa juma lijalo!?” Tino alijawa hasira mpaka midomo ilikuwa ikimcheza.

“Unaongea nini T..” “Don’t. Usitaje jina langu. Wewe ni mshenzi Jax, lakini sidhani kama umekosa utu kwa kiasi hicho! Mwisho wa yote ulitaka iwe nini? Ulitaka siku ya harusi Lara ndio atokee kanisani, halafu wewe ndio usitokee kama mtoto wa kike!?” “Najua unaweza usielewe Tino lakini...” “Kwa mara ya mwisho kutunza heshima yako hapa mjini. Jikaze kiume, maliza mambo kiume. Acha kumtumia Lara hawara yako ndio akazungumze naye, kisha na kumdai vitu ulivyompa kwa heshima mbele ya wazazi wake!” “Tino?” Jax akataka kuongea Tino akaendelea. “Na kingine ambacho wewe hufahamu kwa kuwa hukujaliwa kuwa na wazazi kama wengi wetu, inawezekana hukupata mtu wa kukufundisha. Watoto wakiume wanafikiria kwa kichwa sio...” Tino akatamani kumtukana ila akanyamaza.

“Maliza kiume Jax. Hata kama unatudharau kwa kuwa sasa hivi umepata. Kumbuka watu walijitoa ulipowaitisha kuwa unataka kuoa. Kwa pesa zetu za madafu, tulikuchangia. Acha dharau kwa kuwa sasa hivi umefanikiwa, ndio unatuona sisi ni wapumbavu. Tunaendelea kuchangishana katika kidogo tulichonacho, kumbe mwenzetu unaoa watoto wa uzunguni! Acha dharau Jax. Achana na watu kwa heshima.” Tino akaondoka. 

Kwa Lara.

Baada ya kuoga, alipanda kitandani. Akatamani usingizi umchukue umtoe hapa ulimwenguni kwa muda, lakini hata hakusinzia. Sesi aliingia chumbani kwake. “Unataka nikuletee nini?” Lara akabaki kimya. “Maji?” Sesi akaendelea kuuliza kiiungwana. Kimya. “Basi mimi nitakuwa hapo sebuleni. Ukitaka kitu chochote, uniite.” Kimya. Sesi akamuwashia tv ya hapo chumbani kwake, akatoka. 

Jax kwa Lara.

Alibaki hapo kitandani ametulia, kimya. Baada ya masaa kadhaa kupita akishindwa kulala, akasikia mlango umefunguliwa baada ya kugonga mara mbili tu. Alikuwa Jax. Akaenda kukaa pembeni ya kitanda. Akamwangalia, Lara alibaki kimya. Akamuona machozi yanamtoka tu. “Kwanza naomba nikuombe msamaha Lara. Sikumtuma Tula aje akudai gari.” Kimya. Lara hakujibu kitu.

“Nakuhusu Tula. Nakumbuka nilikwambia habari zake mwanzoni kabisa. Sasa..” Akasita. Lara akabaki akimsikiliza huku machozi yakiendelea kumtoka kwa hofu kubwa iliyokuwa imemwingia. Kuwa hisia zake zilikuwa sahihi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          Anaishije tena bila kofia ya kuwa mchumba wa Jax aliyemjengea heshima kila anakojulikana! Maisha ya Lara yalibadilika. Si kipesa tu, ila ile heshima Jax aliyomuwekea! Mbaya zaidi, hawa wapenzi hawakuwa na matatizo. Lara alikiri kuwa Jax ni mtu rahisi sana kuishi naye. Alimpenda Jax karibu ya kuchanganyikiwa. Walielewana kwa kila kitu. Leo anamuacha kwa ajili ya mwanamke mwengine!

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Samahani sana Lara. Umekuwa mwema sana kwangu. Sitaki nikuumize maishani. Nisingeweza kuwa na utulivu huku nikijua Tula yupo mahali na ananihitaji. Sikutaka kuja kukuumiza. Nina uhakika kwa uzuri ulio nao, tabia njema, wema na ukarimu wako, utapata mwanaume atakayekupenda na kukuenzi mpaka kifo.” “Natamani ungekuwa wewe Jax!” Lara alidhani anaongea kwa sauti kumbe ni mawazoni. Mbele ya Jax alibaki kimya, machozi yakichirizika kama mvua.

“Na kuhusu gari, nilikupa wewe na litabaki kuwa lako.” Kimya. “Lara?” Kimya. “Samahani sana. Sikukusudia kukuumiza. Isingekuwa Tula, ingekuwa ni wewe. Unajua nisingewahi kuja kukusaliti. Nakuthamini ndio maana sikutaka kuja kukuumiza.” Kimya. “Kadi ya gari hii hapa. Gari ni yako na hakuna mtu atakuja kukupokonya. Na samahani sana.” Jax akanyanyuka na kuondoka. Lara alishindwa hata kusogea pale kitandani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilikuwa fedheha, na aibu ya miaka. Si kwa Lara peke yake, hata wazazi wake pia. Lara ndio angekuwa binti wa kwanza kuolewa nyumbani kwao. Jax alianza kwa heshima sana. Na ni kweli aliweka heshima. Hapakuwa na shaka kuwa Lara alibahatika. Jax hakuwa mlevi, sio muhuni, kazi nzuri, kijana wa kawaida wa kiafrika. Hakuwa na maumbile ya ajabu sana, au sura kama malaika, ila mwanaume wa kiafrika aliyefanikiwa kwenye upande wa ajira. Mwadilifu, asiye na makuu. Wakafanikiwa kutulia wao wawili. Akamuhakikishia penzi Lara. Akatulia. Leo amemuachia aibu na fedheha kwenye jamii! Heri ingekuwa mwanaume mwingine mwenye tabia za ajabu tokea zamani ila si Jax.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sesi alisikia kila kitu alichozungumza Jax alipomfuata Lara chumbani kwake. Akashindwa kuvumilia, akawapigia simu wenzie wanaoishi nao hapo, na waliokwenda pamoja mpaka Dodoma kwa kitchen party wakiwa hukohuko ofisini, wala hakusubiri warudi hapo nyumbani. Akawaambia yote aliyosema Jax kwa Lara akimuacha kwa ajili ya Tula. Kwamba Tula hakuongopa, kweli ni mwanamke wa Jax. Wenzake wakawaambia wengine na wengine wakawaambia wengine hata wasiokuwa wakiwajua maharusi hao wakasikia hilo tukio siku hiyohiyo.

Hata kabla siku haijaisha habari zikawa zimeshaenea kuwa hakuna tena harusi. Lara ameachwa, na mpenzi wa Jax alimfuata ofisini. Na Jax mwenyewe akamfuata Lara kumthibitishia kuwa anamuacha kwa ajili ya mwanamke mwingine. Ikawa gumzo. Ikawa kashfa juu ya maneno. Wakuongeza wakaongeza ya kwao na kusambaza maneno zaidi na zaidi. Likawa tukio la kusemwa midomoni mwa watu bila kikomo. Jumbe za pole kwa Lara zikawa zikimiminika.

Lara alishindwa kutoka hata kitandani! Sesi huyohuyo aliyejulikana rafiki wa karibu wa Lara, na ndiye msambaza maneno ndiye ikabidi sasa aanze kumsaidia tena Lara kwa kila kitu kwani Lara alibadilika akawa mgonjwa, tena bubu. 

Kutokea anafuatwa na Tula ofisini mpaka siku ya alhamisi bado Lara alikuwa hazungumzi chochote, hali wala kunywa zaidi ya kwenda kuoga na kujihifadhi kwani alikuwa akitokwa na damu nyingi sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usikose kujua na kufuatilia machozi ya uchungu na ya aibu yanayotoka kimyakimya bila maneno kwa Lara.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment