Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Chozi Langu! - SEHEMU YA 10. - Naomi Simulizi

Chozi Langu! - SEHEMU YA 10.

Kwa mara ya kwanza Nelly akawa amepata mtu wa kumtafakari mbali na Jax ambaye ni kweli amemlea kama mtoto wake. Billson alimshangaza na kumchanganya vyakutosha. Mwanaume anayejielewa. Msomi. Hakuonyesha kama ni mtanzania ila asili ya Africa. Kingereza chake! Nelly akajaribu kuweka ile lafudhi kwa mataifa mbalimbai mpaka akachoka. Billson alijaliwa umbile zuri japo ni mtumzima. Mkubwa kiumri kwa Nelly. Amejawa mamlaka! Nelly akacheka na kutingisha kichwa. Akatulia akisubiria aone anataka kumpeleka wapi, lakini akagundua hata hawakuwa wameambiana muda na mahali pakukutana. Na yeye Billson hakutokea tena siku na muda wa kazi mpaka Nelly akajua amegairi.

Ijumaa wakati anatoka ofisini, ameshika pochi yake na mkoba wa laptop yake na makabrasha mengine. Ametoka tu kwenye lifti, gorofa ya chini kabisa kwani ofisi ya Nelly ilikuwa gorofa ya mwisho kabisa juu, akakuta Billson akimsubiria pembeni ya lifti. Akampokea mkoba  bila kuomba. “Naweza kubeba mwenyewe!” “Najua na ndio maana sikukuomba.” Bill akatoka hapo jengoni bila ya kusubiri akiwa na mkoba wenye laptop ya Nelly na makabrasha yake, ikabidi Nelly amfuate nyuma mpaka nje ya jengo.

Wakasimama wakitizamana. “Unaendeleaje Nelly?” Mwishoe Bill akamsalimia na cheko kama anayemuweza. “Mimi mzima!” Nelly akamjibu kwa mshangao na kumuuliza. “Uliniambia tunakutana mara nne tu, tena weekend. Sasa sasahivi unafanya nini hapa!?” Billson akacheka. “Nelly! Wewe unawasiwasi gani! Unashida gani na watu kiasi ya kwamba uwepo wao unakutisha kiasi hicho!” “Naomba mkoba wangu nirudi nyumbani nikapumzike.” “Umekula mchana?” “Anayekupa habari zangu hajakwambia na hilo?” Bill akamcheka akimtizama.

“Najua hapo unaumia maana kuna linaloendelea, wewe hujui.  Hivi nilikwambia kuwa ni sawa wakati mwingine uwe unaongozwa?” “Ni wakati gani wewe huwa unaongozwa?” “Sasa hivi. Chagua sehemu yeyote twende tukapate mlo wa usiku pamoja. Popote unapopata wewe.” Nelly akashangaa sana.

“Nani amekwambia mimi nataka kwenda kula na wewe!? Nimekukubalia siku za weekend tu, tena mara nne tu. Naomba usiweke mazoea Billy!” Akataka kumpokonya mkoba wake, Billy akamkwepa. “Njaa inaniuma Nelly. Tafadhali naaomba tukale.” “Mimi sitaki kwenda popote na wewe.” “Unaogopa nini?” “Sikufahamu Billy! Sijui wewe ni nani na kwa nini upo hapa na mimi, na kwa nini umenikazania hivi! Haijawahi nitokea maishani!” “Umeshajiuliza ni kwa nini haijawahi kukutokea?” “Sina muda wakupoteza.” “Ni kwa kuwa unaogopwa Nelly. Mimi siogopi. Twende tukale.” “Wapi tena!?” “Tutumie gari yako. Tukishakula, utaniacha hapo, mimi nitatafuta usafiri wakunirudisha kwangu.” Nelly akafikiria, akamwangalia Billson. Akakuta anamcheka.

“Naomba nikwambie ukweli Billy.” “Iwe kesho. Leo nina njaa Nelly. Sitaki kusikia chochote ila chakula tu.” “Sasa mbona ni kama ulitaka jibu la swali lako, nataka kukujibu unakwepa?!” “Kwa sababu unachotaka kunijibu sio chenyewe. Hata huo ukweli unaotaka kuniambia sasa hivi, sio wa swali langu. Tafadhali nisaidie usafiri nikapate chakula.” “Kwa nini upo hapa Billy?” “Dereva amenishusha hapa.” “Unajua fika hilo sio jibu la swali langu.” Billson akacheka sana.

Nelly akaelekea sehemu anapoegesha gari yake. Billson akamfuata. “Unataka kuniacha?” “Natamani kama ningeweza.” Billy akazidi kucheka. “Ushaanza kuamini kuwa huwa sikwepeki?” Nelly hakumjibu, akataka kufungua mlango, Billy akamuwahi akitaka kumfungulia. “Hata gari yangu pia unataka kunifungulia mlango jamani!?” “Unahofia utapoteza nini kwa mimi kushika gari yako na kukufungulia mlango?” Kimya. “Eti Nelly?” Nelly akampisha kabisa hapo mlangoni. Akamfungulia mlango na kumpisha kumuashiria aingie. Akaingia bila kuzungumza, Billy akamfungia mlango na yeye akapanda. Nelly akaondoa gari akiwa ametulia.

Mwishoe akamuuliza. “Ungetamani kula nini?” Billy akafikiria bila kupata jibu. “Njaa inaniuma sana, siwezi kufikiria tena. Sijala tokea jana.” “Kwa nini!?” “Nimekuwa na majukumu mengi, nimeshindwa kuweka chakula mdomoni.” Akamuona anavuta kiti nyuma, na kujiegemeza kama anayetaka kupumzika kabisa. “Usilale sasa! Kwa hiyo utakula chakula chochote?” “Tena kikinifuata hapa ndio itakuwa vizuri kabisa.” Nelly akampigia mtu simu kumwambia anakwenda hapo. Amtayarishie chakula. Akifika atampigia ili alete chakula garini. Billson kimya.

Mara kadhaa Nelly alimwangalia kwa kujiiba, akamuona amefunga macho kabisa. “Billy?” Baada ya muda akamuita, akamuona amefungua macho. “Asante kwa nyama choma. Nilipenda.” “Karibu.” Akabaki akimwangalia, Nelly akaendelea kuendesha. Kimyakimya mpaka kwenye moja ya hoteli nzuri tu, lakini Billy akashangaa huduma zinawafuata nje. Akaanza kucheka. “Ni nini sasa?” “Usiniambie huwa unakuja sehemu nzuri kama hii, na kuishia kula garini!” Nelly akanyamaza, hakujibu. Na yeye Bill akanyamaza.

 “Nelly?” Nelly akamgeukia. “Sio watu wote ni wabaya.” “Mimi sijawahi kukutana na hao binadamu wazuri.” “Hudhani ni kwa kuwa umechagua kutowatambua?” Billy akamuuliza vizuri tu, Nelly akanyamaza. Chakula kikaletwa. Wakaulizwa vinywaji. Nelly akataka wine. “Tafadhali naomba utusubiri kidogo.” Akamuomba muhudumu awapishe kabla yeye hajaagiza kinywaji chake. Nelly akashangaa. “Naomba nikuombe kitu, Nelly.” Nelly akamwangalia.

“Moja ya sifa zako nilizosikia ni kuwa huwa hunywi pombe ya aina yeyote ile siku za kazi. Na ikitokea unakunywa, basi kuna jambo halijakaa sawa.” Hapo alimshangaza zaidi Nelly mpaka akamgeukia vizuri. “Nani anayekupa bahari zangu Billy wewe!?” “Niambie katika hilo nipo sahihi kwa asilimia ngapi?” Nelly akamtizama na kunyamaza.

“Basi inamaana ni kweli. Naomba sasa hivi usinywe kwa sababu yangu mimi. Upo sawa kabisa, naomba usiogope kiasi chakutaka kujituliza kwa wine. Sijui kama umenielewa?” Nelly akanyamaza. “Nipo hapa nikitaka utulie kabisa. Najua hujanizoea, na bado una maswali mengi juu yangu. Usiwe na wasiwasi. Haupo hapa na mume wa mtu.” Nelly akamwangalia. Billy akahakiki ndio uliokuwa wasiwasi wake. “Nisingekufuata mpaka ofisini kwako, kama nia yangu ni kukuingiza kwenye wizi wa kijinga hivyo. Humuibii mtu. Mimi si mume wa mtu wala sina majukumu ya kifamilia. Mtoto wangu wa mwisho yupo chuo kikuu na hayupo hapa. Na hata kama akiwepo hapa, sina chakujificha. Unanielewa?” “Kwa sehemu.” Nelly akajibu.

“Nashukuru kwa hiyo sehemu ndogo uliyoruhusu kuelewa. Nakuhakikishia upo salama. Usiogope.” Nelly akaanza kula chakula chake, Billy akamuita muhudumu. Wote wakaagiza juisi. Wakatulia garini wakila. Kimya. Wakala mpaka wakamaliza. “Mimi unaweza kuniacha tu hapa, nisikusumbue.” “Utarudije sasa nyumbani?” “Nitachukua usafiri hapa. Usijali kabisa. Wewe nenda ukapumzike. Nitakuona kesho.” “Sawa.” Nelly akakubali bila kutaka kumlazimisha akihofia asije kuwa na mipango yake mingine, akawa anaingilia.

“Uwe makini huko barabarani Nelly. Nitakuona kesho.” Billson akaongea kwa kujali, Nelly akamtizama na kuinama kwa muda. Billy akabaki amekaa garini. Wakatulia kwa muda. “Kesho nitakukuta wapi, na mida gani?” Nelly akafikiria kidogo kisha akawa amepata jibu. “Labda hapahapa, kwenye mida ya saa sita.” Billy akajua ameshaanza kumuweka sawa. Kwamba amekubali muda wake! Akafurahia hilo. “Basi mimi kuanzia saa sita kasoro nitakuwa hapa nikikusubiri.” Nelly akamwangalia. Akakunja uso kidogo, na kunyamaza.

“Nimefurahia huu wakati Nelly.” “Wa kula hapa garini!?” “Kabisa. Chakula kizuri, na tukapata wakati wa pamoja pia.” Nelly akakunja uso kama ambaye haelewi. Billy akacheka na kuaga. “Usiku mwema.” “Na wewe pia, Billy.” Akatoka hapo garini. Nelly akaondoka bila yakupoteza muda. Akamuacha hapo.

Jumamosi.

Mara ya Kwanza.

S

aa sita kasoro tano, Nelly akawa anaegesha gari yake hapo nje ya hoteli waliyokuwepo usiku uliopita. Wakati anashuka garini, akamuona Billy akimsogelea. Akacheka kwa vile alivyokuwa amevaa. Pensi nyeupe na shati nzuri la maua, miwani ya jua na kofia. Chini akavaa sendozi nzuri za ngozi. Na miguu yake meupe ikazidi kuvutia kwenye sendozi hizo za kiume. Moja kwa moja Nelly akajua wanaelekea maeneo ya ufukweni kwa aina ile ya mavazi aliyovaa. “Umependeza sana Nelly!” “Asante. Na wewe uko vizuri. Umependeza.” Billy akacheka. “Asante. Nikupokee mkoba?” “Hii ni pochi Billy!” “Si ndio hiyo!” “Hapana. Naomba kubeba pochi yangu.” Safari hii Nelly akaongea kike sio kwa amri. Billy akacheka.

“Sawa. Basi twende, rubani atakuwa akitusubiria!” Nelly akahisi hajasikia vizuri. “Rubani kama muendesha ndege?!” “Ndiyo.” Gari anayoendeshewa Bill bado ilikuwa ikiwaka kuashiria yupo dereva ndani. Mbele kulikuwa na dereva. Wao wakakaa nyuma. Ukweli na Nelly alipendeza. Kwa kuwa hakuwa akijua wanapokwenda, alivaa ‘casual’. Ila akajiweka vizuri kuanzia juu mpaka chini. “Tunakwe..” Nelly akakumbuka aliambiwa ni suprise. Akanyamaza. Billy akaanza kucheka. “Safi sana. Naona sasa hivi tunakwenda sawa.” Nelly akatabasamu na kutulia.

“Ulikuwa na usiku mzuri?” Nelly alishapotelea mawazoni, akamgeukia. “Usiku? Ulilala vizuri?” Akarudia swali. “Ndiyo. Na wew?” “Na mimi nililala vizuri sababu ya kushiba vizuri.” Nelly akamwangalia tena na kunyamaza. “Si unajua unaruhusiwa kuuliza?” Billy akamwambia hivyo kama aliyejua yupo na maswali mengi. “Uliniambia siruhusiwi kuuliza tena.” Nelly akajibu na kumfanya Billy azidi kucheka. Kimya mpaka uwanja wa ndege lakini upande mwingine wa ndege binafsi, tena ndogo. Nelly akazidi kushangazwa.

“Twende.” Wakatoka hapo kuelekea ndani kabisa kuliko na ndege ndogo. Nelly akashangaa anasalimiana na rubani wa helikopta moja iliyopo pembeni kabisa kama tayari kwa safari. Kisha akamwambia wapo tayari. “Billy!?” Nelly akamuita. Billy alipomgeukia akamuona kama ameingiwa hofu, asielewe ni hofu ya nini. Akamsogelea karibu. “Naomba usiogope Nelly. Na ujue tutarudi leo jioni. Usiku utakuwa kwako. Panda.” Nelly akajishauri na kuamua kwenda tu. Akamtanguliza yeye wa kwanza ndipo akafuata yeye. Rubani akawapa maelekezo. Walikuwa abiria wao tu, wawili. Nelly akabaki ameduaa kama ambaye hajui kinachoendelea na hajamuelewa kabisa huyo rubani.

Billy akamgeukia tena pale walipokaa. “Vaa hiyo headphone ili kuziba masikio na kelele, kichwa kisiume. Najua hujawahi kupanda helikopta lakini nakuhakikishia upo salama kabisa, usiogope.” Nelly akaanza kuvaa, Billy akamsaidia. Akamuweka sawa masikioni. Wote walipokuwa tayari rubani akaondoa hiyo helikopta. Ule mlio na vile walivyokuwa wamekaa wakiona nje kabisa, hofu ikamzidia Nelly. Billy akamuona.

“Nilidhani ungependa kuangalia nje!” “Hapana Billy, mimi nina acrophobia. Siwezi kuangalia sehemu ya chini kwenye umbali mrefu. Hata nikiwa juu gorofani, naogopa kuangalia chini. Siwezi. Na wakati wote kwenye ndege huwa sikai dirishani, hata iweje.” Billy akapoa kabisa. Alijua anamfanyia jambo kubwa la kifahari, lakini ikawa tofauti kabisa. Ukweli Nelly alionekana ameingiwa na hofu haswa. “Basi usiangalie nje, niangalie mimi.” Akamvuta mkono wake na kuukumbatia katikati ya viganja vyake. “Samahani. Sikujua kama ingekuwa adha. Nilitaka ufurahie.” “It’s okay.” Nelly akamjibu akiwa haangalii nje ila hapo ndani tu tena ameinamisha uso kabisa, akionekana jasiri huyo, amekamatika.

“Nelly?” Akamwangalia. “Nilikwambia kama umependeza?” “Sikujua natakiwa nivae nini! Nimevaa tu gauni.” “Upo sawa kabisa. Na hilo gauni limekukaa vizuri sana. Una umbile zuri, Nelly!” Nelly akavuta mkono wake kutoka hapo mikononi mwake. Billy akacheka. “Unaogopa nini Nelly!?” “Huku tulipo ni juu sana.” “Bado hilo sio jibu lake.” Nelly akamwangalia tu na kunyamaza. Billy akamsukuma kidogo kwa bega lake, kisha akamvuta tena mkono. “Utakuwa sawa. Usiogope.” Nelly akamwangalia tena na kunyamaza.

Wakatulia mpaka walipoambiwa wamefika, anatafuta kutua. Nelly akainama kabisa ili asione. Rubani akawashusha sehemu nzuri sana, katikati ya kisiwa, bichi nzuri. Nelly akamwangalia Billy. “Mpaka hofu imeisha! Ni wapi hapa?” Angalau hilo likamfurahisha Billy. “Unguja. Tulishawahi kufika huku na wenzangu, nikatamani kuja kurudi. Twende tuzunguke zaidi. Unaweza kutoa viatu ili utembee vizuri kwa uhuru bila shida.” Hilo likawa jema kwa Nelly kwani alivaa sendozi za juu kidogo. Akavua. Yeye Billy akabakia na sendozi zake mguuni. Akamsaidia kumbembea Nelly viatu.

Wakatembea kwa muda tu, Nelly akifurahia ile hali ya hewa pale, Billy alimpa na yeye kofia na miwani nzuri sana ya jua. Vikamfaa. Kimya kila mmoja akitembea na kuwaza lake. Bahati mbaya akakanyaga jiwe likamuumiza. Akataka kunyamazia, lakini Billy akaona. “Naomba kuona.” “Hapana, nipo sawa.” “Nimejua limekuumiza Nelly. Tafadhali naomba na mimi kuona.” “Hamna kitu! Nipo sawa.” “Nelly! Hivi unajua ni sawa na wewe kusikia maumivu na kusema unamaumivu au umeumizwa?” Nelly akanyamaza. Billy akatafuta sehemu nzuri akakaa kabisa. “Naomba ukae hapa na unipe mguu wako.” “Mimi nipo sawa Billy! Usijali.” “Najali.” Wakabaki wakitizamana kwa muda. Nelly amesimama, Billy amekaa kabisa mchangani, akimsubiria.

Nelly mtoto mgumu, aliyejilea mwenyewe akili na mawazo kwa Jax tu, hakuwa na muda wa mambo madogomadogo kama hayo. Akakunja uso na kukaa. Akatoa miwani ya jua akijishauri kama anampa mguu au la. Billy naye akabaki akisubiria tu. “Mimi sioni sababu. Nimesema nipo sawa, nipo sawa.” “Kuna ugumu gani kunipa nijionee mimi mwenyewe?” Kimya, Nelly akiwa amekunja uso.

“Eti Nelly? Unaogopa nini hicho kinachokufanya unafunga milango yako yote ya fahamu na kutaka usiwe kama wanadamu wengine wakawaida tu!? Ni nini?” “Nipo sawa, Billy!” “Kama wewe unaona sawa, kuna shida gani na mimi nikaangalia, nikajiridhisha mimi mwenyewe nikaona kama ni sawa? Hakuna mwanadamu anakuwa na maumivu, halafu anayakataa maumivu kwa kusema yupo sawa, ila kusema nitakuwa sawa, ndio sahihi!” Nelly akajifikiria na kuamua kujiweka sawa.

Akakusanya gauni lake vizuri katikati ya mapaja yake na kusogeza mguu mbele kidogo kama kumuelekezea Billy. “Ni sawa nikiuweka hapa?” Billy akauliza kiustarabu, lakini Nelly akamwangalia tu na kugeukia pembeni. Billy akaunyanyua ule mguu uliokuwa umeumia akauweka mapajani kwake. Akautoa michanga kwa kupangusa taratibu, Nelly macho pembeni. Akaangalia. “Pamechanika kidogo.” “Lakini hakuna maumivu! Mimi nipo sawa.” Akataka kuvuta mguu wake, Billy akamzuia. Akaacha na kutulia.

Billy akaanza kuuminya taratibu, Nelly akiwa amepotelea mawazoni, ila akamuona anatulia kabisa. Akaendelea kumchua kama anayemfanyia masaji, Nelly akatulia kabisa ila macho kwingine, mawazo hayapo pale. Akamvuta na mguu mwingine. Hakukataa. Akamgeukia vizuri. “Imejaa michanga!” Nelly akaongea akijihami. Billy akaendelea kumpangusa.

“Nikuulize swali Nelly?” “Juu ya hofu yangu?” “Hapana. Hilo utanijibu utakapokuwa tayari. Ila ujue ni deni. Nitataka kujua, na sitakuuliza tena. Swali ni, wakati wewe ukimlea Jax, nani alikuwa akikulea wewe?” Mwili mzima wa Nelly ukafa ganzi. “Maana jana nilimsikiliza Jax kwenye neno lake la shukurani akikutambua wewe kama mlezi pekee ambaye amemfahamu hapa duniani. Na wewe si mkubwa sana kwa Jax. Kama nimeelewa vizuri, inamaana mlikuwa yatima, si ndivyo?” Nelly akanyamaza. “Nelly?” “Baba ambaye alikuwa wa mwisho kufariki baada ya mama, aliniacha mimi nikiwa kidato cha nne, Jax anakaribia miaka mitano. Kwa hiyo sikuwa mtoto ambaye nahitaji kulelewa.”

“Binti yangu wa mwisho nilikwambia yupo chuo kikuu. Unakumbuka?” Nelly akamwangalia na kunyamaza bila kujibu. “Anaishi na mama yao. Mpaka sasa bado tunamlea!” Nelly akamuelewa anachomaanisha. “Mimi sihitaji kulelewa. Kwa hiyo kama tupo hapa kwa sababu ulimsikia Jax akiongea siku ile, ukaingiwa na huruma, ukatuhurumia, sisi hatuhitahiji kuhurumiwa. Tupo sawa kabisa.” Akavuta na miguu yake pale alipokuwa ameshikiliwa kwa upendo.

“Lakini bado hujajibu swali langu! Kwamba hata ndugu hawakuwasaidia?” “Hapana Billy! Binadamu wakipewa nafasi na Mungu hugeuka kuwa kama wanyama. Nyumba tuliyokuwa tukiishi na wazazi ilitakiwa kuwa ni mali yetu kihalali, baada ya wazazi kufariki. Ndipo mimi na Jax tulizaliwa pale, lakini garama niliyolipa ili tu kwanza kuweza kuwa na Jax kwenye nyumba moja na kumlea!” Nelly akatulia kidogo, kisha akamuona anatingisha kishwa kama anayekataa au mwenye masikitiko, kisha akaongeza. “Isee ilinigarimu sana. Nilitumika mpaka nilipokuja kufanikiwa kuipata nyumba yenyewe kihalali, nilikuwa siwezi kulala humo.”  “Kwanini?” Nelly hakutaka kujibu hilo, akaendelea. “Niliishia kuiuza na kununua ninakoishi sasa hivi, na Jax akiamua. Kujibu swali lako, hapana. Mimi mwenyewe ndiye nilibakiwa na jukumu la kumlea Jax mpaka kumfikisha pale alipo.” Nelly akatulia kidogo.

“Najua sipo sawa. Au kama ulivyosema sipo kama binadamu wengine. Lakini nilijeruhiwa mno. Nipo hapa nilipo au tumefika hapa unavyotuona mimi na Jax, kwa kujisulubisha na kujikana mno. Hata jina alilokuwa akiniita mama yangu, ilibidi kufa ili mimi na Jax tuwe hivi tulivyo. Ule uasili wangu wa kwanza kabisa, ulikufa kwa kuuwawa kilazima na mimi mwenyewe kushiriki. Ilinibidi kufanya kisheria pia nikiwa hata kinafsi nilishakufa.” Billy akawa hajaelewa kidogo.

“Hivi unavyoniona, jina langu kamili, umri wangu pia, ilibidi kubadili ili kufikia umri ambao naweza kuirithi ile nyumba na kukabidhiwa Jax. Hiyo inaweza ikasikika ni rahisi, lakini sasa hiyo safari niliyopitia mpaka ndugu kukubali, ndipo nilipofikishwa kwenye kumuogopa binadamu, Billy. Mali ilikuwa ni halali yetu, lakini ilinibidi kulipa garama mbaya sana, ili tu kutufikia mimi na mdogo wangu.” “Baba hakuacha mirathi?” Nelly akasimama kabisa na kuondoka hapo kuashiria kutotaka kuzungumzia hilo. Billy naye akasimama kumfuata. Nelly mbele, yeye nyuma wakitembea.

Ukweli hilo eneo la ufukweni hapo Unguja, lilikuwa zuri na safi kuvutia. Maji mazuri na mchanga mweupe ulioweza kuonekana mpaka nje ufukweni. Wakaendelea kutembea kwa muda. “Njaa inaniuma Nelly.” Billy akaongea akiwa nyuma yake. “Turudi ndani hotelini tuone kama tunaweza kupata chakula kizuri.” Nelly akageuka kutoka alipokuwa akielekea, na kurudi hotelini upande wa mgahawani. Ilikuwa hoteli kubwa sana ya kitalii. Na wazungu wengi walikuwa wamekaa ufukweni wakipata jua msimu huo wa baridi nchi zao za Ulaya.

Wakaingia na kukaa sehemu ya mgahawani. “Nikwambie kitu Nelly?” “Tokea lini umeanza kuniomba ruhusa ya kuzungumza?” Billy alicheka sana. “Wewe ni mtu wa namna gani Billy!?” “Ukiendelea kuwa na mimi utanifahamu tu. Lakini ninachotaka kukwambia ni..” Muhudumu akawasogelea, wakaagiza matunda, wakati wakisubiria supu.

Nelly akatulia kabisa akiangalia upande wa baharini. “Nelly?” Akamuita. Nelly akamgeukia. “Ukweli ni siwezi hata kuhisi maumivu ya ulikopitishwa maishani kwa kuwa mimi nilikulia sehemu nzuri sana. Wala sitaona aibu kusema au sitakudanganya. Nilizaliwa na wazazi waliokuwa wanauwezo na walikuwa tayari kupata watoto. Nikimaanisha walikuwa wamejiandaa na sisi. Tulisoma vizuri na malezi mazuri. Mama mzuri wa moyo aliyekuwa akitupenda sana, na baba yetu hivyohivyo. Sijui shida ya malezi kama ulikopita wewe, lakini kwa kukusikia kwa kiasi tu, japo hujawa muwazi kwangu zaidi, najua uliumizwa sana. Naomba nikupe pole. Japo najua haitasaidia, na pengine umeshapata pole nyingi sana na ya kwangu inaweza isilete maana, lakini naomba upokee na mimi pole yangu. Pole.” “Asante Billy, japo sijawahi kuzungumzia hili  na yeyote yule.” “Basi nashukuru mimi kuwa wa kwanza kujua, na pole.” Nelly akatulia.

Kisha akamwangalia, akakuta bado Billy akimtizama. “Umechoka?” “Hapana, ila sitajali kurudi nyumbani.” “Kuna kitu kizuri nimekuandalia jioni. Naomba uvumilie.” “Jioni!?”  “Unajua sasa hivi inakaribia saa kumi jioni! Ndio maana nilitaka tupate tu supu ili kuacha nafasi ya mlo mzuri wa jioni.” Nelly akabaki akifikiria.

“Kabla hujahitimisha kwa kuiona siku ya leo ni mbaya kwa kukupandisha helikopta, naomba nimalize mipango yangu yote ya leo niliyokupangia ili ujumuishe makosa yangu yote.” Nelly akajicheka alipokumbuka hali yake ndani ya ile helikopta. “Halikuwa kosa Billy. Mimi ndio natakiwa kuomba radhi nimekukatili.” “Hata kidogo. Nilifanya kwa ajili yako nikitaka kukufurahisha tu.” Nelly akakunja uso kwa mshangao mpaka cheko likaisha usoni.

“Kwamba ulikodi helikopta kwa ajili yangu mimi!?” “Oooh yeah!” Nelly akashangaa sana. “Kwa nini!?” Billy akacheka tu na kunyamaza akimwangalia vile Nelly alivyoshangaa. “Kwa nini upoteze pesa yote hiyo kwa ajili ya...” Nelly akasita na kubaki akifikiria huku amekunja uso. “Samahani sana Billy! Hakika sikujua kama ulikodi kwa ajili yangu! Natamani ungenishirikisha kwanza!” “Nilijua ungekataa. Sasa wewe ulifikiri mimi huwa nazungushwa hapa nchini na helikopta!” “Sijui Billy! Wadhifa wako na ulivyo hivyo, havipingani na aina hiyo ya usafiri. Nikajua pengine uliona ndio itakurahisishia kufika hapa kwa urahisi! Hakika sikujua kama ni kwa ajili yangu! Kwanza kwa nini unifanyie yote hayo!?” Billy alibaki akimtizama tu.

“Kwa nini Billy!? Hunifahamu, sikufahamu, ni kwa nini uende umbali wote huo na kupoteza pesa!? Na ninajua utakuwa umepoteza pesa nyingi sana!” Billy kimya akimtizama. “Tafadhali usifanye hivyo kwa ajili yangu Billy. Mimi si aina hiyo kama ya wanawake unaowafikiria wewe.” “Wa namna gani?” “Sijui Billy! Lakini tafadhali usipoteze muda wako na pesa kwa ajili yangu! Mimi sipo...” Nelly akasita. Wakanyamaza.

Matunda yakaletwa. Wakaanza kula. Walio staarabika hao walijua kutumia vifaa vya mezani vilivyo. Kimya kila mtu akila. “Billy?” Nelly akaita. Billy akamwangalia. “Nashukuru.” “Kwa nini?” “Kuweza kunifikiria. Ila tafadhali usihangaike na mimi. Mimi najijua. Nitakuvunja tu moyo. Nakuona wewe ni mtu mzuri. Mimi...” “Wewe ni mtu mbaya!?” “Sana Billy. Sana. Mimi mwenyewe huwa mpaka naogopa kujifikiria. Moyo wangu umejawa madonda ambayo hayajawahi kupona na sijui kama yatakuja kupona. Mimi mwenyewe najichukia, sina uwezo wa kumpenda mtu mwingine.” “Mbona umeweza kwa Jax?” “Jax alifanyika kama mtoto wangu, Billy! Mtoto ambaye sikuwa na pakumuacha au kumkwepa. Lakini kama ningekuwa na ndugu wakueleweka, nahisi na yeye nisingekuwa naye. Lakini imenilazimu.” Nelly akajiweka sawa.

“Nimemlea Jax na aina hii ya moyo, yeye mwenyewe amekiri kwangu kuwa imemuathiri.” “Haiwezekani!” Kidogo Billy akashituka na kuumia. “Hajakosea. Na wala hakuniambia kwa nia ya kuniumiza. Ila nataka kukwambia, nilimlea nikiwa naumizwa vibaya sana bila yeye kujua ninakopita ili yeye apate pakuishi, akue vizuri na aende shule vizuri. Kwa hiyo maisha yangu yalijaa uchungu mno. Moyo ulikuwa ukienda mbio wakati wote kwa hofu na maumivu kila wakati. Na ikanilazimu kuendelea ili tusiharibikiwe. Imemuathiri Jax, wote tumebakia sisi tu. Japo angalau yeye alijaribu, lakini pia alishindwa. Ninachotaka kukwambia Billy, mimi si mtu unayetaka kuwa naye karibu. Sio mimi. Na ninakuhakikishia kabisa, kile unachodhania nipo, au nitakuja kuwa, sipo na sina huo uwezo. Tafadhali acha kujisumbua na mimi. Na nimekwambia kwa undani ili uelewe, ili usiendelee kupoteza muda wako kwa kuwa najua unayo majukumu.” Billy akavuta pumzi kwa nguvu na kuchukua uma wake tena. Akala matunda kadhaa na kumeza.

“Ndani ya hii hoteli, kuna chumba nimekodi kwa ajili yako. Ukiingia humo, utakuta mtu wa kukufanyia masaji. Utapumzika. Kisha atakuja mtu mwenye mavazi. Atakuletea nguo za usiku tofautitofauti na viatu. Utakavyochagua kuvaa kwa chakula cha usiku leo, ujue ndio vitakua vyako moja kwa moja. Kwa hiyo chagua vitu utakavyopenda kubakiwa navyo. Kama utataka akutengeneze na nywele, ameniahidi atakuja na kijana wake. Watakufanyia kile unachopenda. Saa moja na nusu usiku, gari itakuja kutuchukua hapa, itatupeleka sehemu kwa chakula cha usiku.” Nelly akabaki amemkodolea macho kama asiyeamini alichosikia.

“Umenielewa?” “Kwa nini unafanya yote hayo Billy wewe!?” “Leo ni mara yetu ya kwanza kutoka pamoja. Tulikubaliana ziwe nne. Mara ya nne unikumbushe hili swali, nitakujibu. Lakini kwa sasa naomba tutembee kwenye makubaliano yetu.” Nelly akanyamaza kabisa.

Baada ya supu akamsindikiza mpaka nje ya chumba alichomkodishia. Hapo ni baada ya kupita mapokezi na kupata kadi ya vyumba vyao. “Nitakuwa kwenye sauna kwa muda, kisha chumbani. Saa moja na dakika 15 nitakuwa hapa nje nikikusubiri. Na nitawaambia hao dresser, baada ya masaa mawili kuanzia sasa ndipo waje, watakuwa wamemaliza kukufanyia masaji, umepumzika na upo tayari kwa kuvaa.” Nelly akatulia kidogo kama anayefikiria.

“Unanisikia?” “Nashukuru Billy. Asante.” Kama ambaye angalau alikuwa akisubiria hilo. Akacheka. “Namaanisha. Hakuna mtu ambaye amewahi kunifanyia yote haya! Nashukuru. Asante.” “Karibu. Basi acha na mimi nikakae kwenye sauna kidogo.” Japokuwa Nelly alishangaa mwanaume huyo kukaa kwenye sauna, lakini akaelewa ndio maana ana ngozi nzuri vile.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Japokuwa Nelly alikuwa na pesa, na tangia anafanikiwa moja ya agenda zake ni kuvaa vizuri. Tena sana, akitumia pesa nyingi sana kujiweka nadhifu, akinunua vitu vyake ndani na nje ya nchi, lakini siku hiyo alikutana na huduma ya tofauti! Alishangaa aina ya huduma aliyopewa siku hiyo. Hata siku hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kufanyiwa masaji. Tena alishafanyiwa ndani na nje ya nchi pia, lakini siku hiyo ikawa tofauti. Alilala hapo akihudumiwa kuanzia uso uliokuwa umepakwa vitu vya asili, akimfikiria Billy na kushindwa kumuelewa.

Akiwa kwenye masaji akalala usingizi mzito, asijue ni kwa nini kumbe aina ile ya masaji inasaidia kufanya misuli kupumzika kabisa. Na kwa aina ile ya maisha ya Nelly kufanya kazi mchana na usiku bila kupumzika, mwili ulikuwa umechoka bila yeye kuipa akili yake ruhusa ya kufikiria kuchoka. Akajikuta amepotelea usingizini katikati ya masaji na miziki mtulivu. Alikuja kuamshwa na watu wawili ambao mmoja alimwambia achague nguo, mwingine alikuwa akitayarisha meza na vitu vya kumtengeneza nywele na uso. Kumbe mtu wa masaji alishaondoka muda mrefu sana.

Matayarisho ya kwenda kwa chakula cha usiku yakaanza, Nelly asielewe wanakwenda wapi huko ambako anatakiwa kupendeza kwa kiasi hicho cha kumwaga pesa nyingi hivyo! Na hakujipunja. Alichagua vitu vya thamani tupu. Kuanzia nguo, viatu, hereni, mkufu mzuri sana na alijua ni garama. Na vyakuvaa mkononi. Akacheka moyoni. “Ameyataka mwenyewe. Acha pesa imtoke ili asirudie tena.” Akajisemea moyoni wakati ameachwa mwenyewe hapo chambani akijitizama na kusubiria muda atoke.

Chakula cha Usiku Mjini Unguja.

Mara Yao Ya Kwanza.

N

elly alitoka akiwa amejawa na furaha na ametulia. Akili safi na mwili uliopata mapumziko ya miaka kwa aina moja tu ya masaji, tena ya muda mfupi aliokuwa amepatiwa. Walimchua misuli yote mpaka anaamka, akahisi mwili si wake. Mwepesi na akili safi. “Ndio maana wengine wanavicheko kila wakati! Kwa aina hii ya masaji, lazima kila siku ujisikie vizuri.” Akajisemea Nelly akiwa anatoka chumbani kwake. Akakuta Billy akimsubiria nje ya chumba chake. Billson alipomuona na tabasamu kubwa vile, akajua masaji aliyoagiza imefanya kazi yake.

“Ulipata mapumziko mazuri?” “Mwili nausikia kama wa binti wa miaka 13!” Billy akacheka. “Nilijua utapumzika tu.” “Nilihitaji kwakweli, japo sikujua kama naweza pata aina hii ya masaji! Kwani wanafanyaje!?” Billy akacheka tena. “Nawapenda kwa sababu na mimi huwa wananisaidia sana kunipumzisha haswa kipindi ninachokuwa na uchovu wa mwili, mawazo na majanga ya maisha.” “Wewe unayecheka kila wakati unakuwa na majanga gani ya maisha?” “Unafikiri ni wewe peke yako tu ndiye ambaye wanadamu wamekutenda?” Nelly akamtizama kama asiyeamini.

“Twende, dereva atakuwa amefika. Asitusubirie muda mrefu.” Wakatoka wakitembea. “Mbona leo huniombi kunishika mkono na hivi nilivyopendeza!?” Billy alicheka sana. “Nelly!” “Mimi mwenyewe najua nimependeza. Angekuwa Jax angeniomba kunishika mkono.” “Nilikuwa najishauri Nelly! Usiku wa leo sitaki uishie pabaya. Nataka wakati mzuri. Sasa sikutaka historia ijurudie. Maana mara ya mwisho nilipokuomba, ulinikatalia mbele ya kadamnasi.” “Sikuwa nimefanyiwa aina hii ya masaji.” Billy akacheka sana.

“Usifanye mchezo na masaji ya mchina.” “Ni mjapani.” Billy akamsahihisha akicheka. “Ewaa! Umemtoa wapi huyu kijana!? Amenichoma choma na kama vijisindano, akaniwekea mawe ya moto hivi kwenye uti wa mgongo halafu...” Billy akazidi kucheka maana Nelly akawa kama anavuta kumbukumbu. “Aisee acha kabisa.” “Huwa ananisaidia sana. Ni mtaalamu. Hata ukiwa na msongo wa mawazo kiasi gani, kwake utatulia tu.” “Sasa wewe Billy una msongo gani wa mawazo? Kazi nzuri, inamaa pesa nayo ni nyingi tu. Watoto unao. Hujakua kwa hekaheka kama wengi wetu. Mzuri wa sura na umbile.” Hapo Billy akacheka mpaka akasimama.

“Kumbe mimi mzuri!” “Najua unajijua sana ndio maana unavijimaringo vyako hivi. Kwa hiyo nina maana vyote hivyo vinaweza kukupa mwanamke yeyeote unayetaka. Kwanza wakisikia tu unafanya kazi world Bank na jina la cheo chako, watakutaka tu. Sasa unamsongo gani wa mawazo?” “Maisha yana mtindo wa kumsumbua mwanadamu bila kujali  ulivyo na ulichonacho. Hakuna mwanadamu ambaye hana matatizo Nelly. Sema wengine tumeamua kupambana nayo kwa staili ingine bila hasira. Tena baada yakuona hasira na uchungu ni kujiumiza mwenyewe.” Hapo Nelly akanyamaza na wakawa wamefika kwenye lifti. Wakatulia wakisubiria.

Ilipofunguka na baadhi kushuka, wakaingia na kukuta watu wengine ndani. Nelly akatulia hapo ndani lakini Billy yeye akawaangalia aliowakuta humo ndani na kusalimia. Macho na akili zake vikatua kwa mtoto wenyewe asili ya kizungu. Akaanza kumuuliza maswali na kumtania mpaka wazazi wake na huyo mtoto wakaanza kucheka na Billy. Akaongea lugha iliyoendana na huyo mtoto akawa akijibu na kucheka sana mpaka Nelly asiyependa watu na ambaye hakuwasalimia akawageukia. Akaona vile yule mtoto anavyocheka na Billy. Akageuka vizuri.

“Unawatoto?” Akauliza mama mtu. “Binti wakubwa sasa. Wa mwisho yupo chuo. Lakini napenda sana watoto na ninamisi huo umri wa fikra zisizo na hatia. Kuongea chochote bila wazo la pili.” “Kutokudanganywa.” Akaongeza baba yake yule mtoto. “Ewaa!” Akaitika Billy kwa haraka na kufanya wote wacheke kwa pamoja. “Tunae kaka yake huyu, hapa tunapozungumzo yupo na adhabu huko chumbani. Haruhusiwi kutoka.” Akaongeza mama mtu. “Basi naamini mnaelewa ninachozungumzia.” Billy akaongeza na kufanya wacheke zaidi. Wakazungumza kidogo, lifti ikafunguka.

Kwa kuwa Billy na Nelly walikuwa karibu na mlango walitakiwa wao watoke kwanza. Billy akamgeukia yule binti. Akainama kabisa mbele ya yule mtoto na kumwambia kama anayenong’ona ila kwa sauti ya juu tu iliyoweza kusikika kwa wote. “Do your parents a favour.” “What?” Kakamuuliza Billy akicheka. Kalionekana ni kachekaji sana. “Don’t grow up so fast.” Akachekaa sana. “Okay?” Billy akamuuliza. “Okay.” Akakakubali akicheka sana. “Good! Deal.” Bill akampa na mkono kabisa kwamba wamekubaliana, asikue kwa haraka. Akaaga wazazi wake wakaondoka na Nelly ambaye alishatoka hapo ndani akisubiria nje.

“Nelinda, naomba nikushike mkono.” Nelly alishituka sana. “Umejuaje hilo jina!?” Billy akajua ameharibu maana mpaka tabasamu ilimuisha Nelly usoni. “Kwanza situmii hilo jina kabisa. Nani amekwambia!?” “Naomba usipaniki Nelly. Samahani.” Akatulia akimwangalia vile alivyobadilika na kugeukia pembeni. “Nelly?” Kimya. “Na naomba usifikirie kuondoka hapa sasa hivi. Nimekuandalia usiku mzuri sana. Nataka tukapate chakula kizuri na wakati mzuri.” Nelly akawa kama anajishauri. “Twende.” Akamshika kabisa na mkono, wakatoka pale Nelly akiwa amepoa kabisa.

Kweli walikuta gari likiwasubiria nje ya hoteli. Billy akamfungulia mlango, na yeye akafunguliwa na dereva. Wakaondoka hapo. “Samahani, sikujua kama hutumii hilo jina.” “Hilo jina liliuwawa kwa garama kubwa sana, Billy. Naogopa hata kulisikia.” “Nakuahidi sitarudia tena. Samahani.” “Nani anakwambia habari zangu Billy? Nimeshajua si Jax, kwa sababu Jax hajakua na hilo jina na nilishamkataza tokea mtoto mdogo kuwa asiwahi kuniita hivyo kwa usalama wake na wangu. Ni kama hilo jina halijui kabisa.” “Sitakwambia Nelly. Ni moja ya kiapo nilichotoa kwa huyo mtu. Naomba uelewe na ukubaliane na hilo. Mimi ni mgumu sana kuvunja viapo haswa ninapokuwa nimeahidi mimi mwenyewe nikiwa na akili zangu timamu.” Nelly akanyamaza.

“Umenichukia?” “Hapana, Billy.” Akajibu Nelly na kutulia. “Umefanya uchaguzi mzuri sana wa vazi. Umependeza sana Nelly. Sana.” “Natamani nilale hivihivi.” Billy akaanza kucheka tena. “Acha nikwambie ukweli Billy. Mimi napenda kuvaa. Tena kuvaa vizuri.” “Nimekuona.” Billy akakubaliana naye. “Lakini linapofika swala la nguo za ‘Gucci’ huwa nafikiria mara mbilimbili. Na ninaweza sema ninayo magauni yao machache sana, hayazidi magauni matatu.” Billy akazidi kucheka. “Kwamba unayakumbuka?” “Kwamba yamewekwa mahali maalumu. Nikirudi kutoka kazini, na yule msichana wa kazi akiwa ameondoka kwangu, na yenyewe yawe yamebaki pale.” Billy akazidi kucheka.

“Usicheze na ‘Gucci!’ Yanaongeza ujasiri na furaha.” “Kwa hiyo hapo unafuraha?” “Huoni mpaka nimeomba kushikwa mkono?” Billy alikuwa akimtizama Nelly asiamini kama ni yeye. Kweli alikuwa ametulia na amependeza sana. Alipambwa vizuri na kiutaalamu, hakupoteza uzuri wake wa asili.

“Nakushuru Billy. Japokuwa sijajua kwa nini unamwaga pesa zako hivi...” “Mimi simwagi pesa zangu. Najua kutumia pesa zangu vizuri, na sehemu sahihi.” Nelly akamwangalia na kuamua kuendelea. “Kama nilivyokuwa nikitaka kusema. Japokuwa sijui nia yako, acha kwa leo moyo wangu ufurahie japo kwa muda kabla sijarudi kwenye ulimwengu wangu.” “Huna haja yakurudi kwenye huo ulimwengu na kupoteza furaha yako ya leo, Nelly.  Unaweza kuishi huko ila ukaamua kuwa na furaha tu.” “Ni rahisi wewe kusema kuliko mimi kuishi.” Billy akacheka tena akionekana anafikiria kidogo.

“Tatizo lako wewe unadhani wewe ndio unamatatizo mengi hapa duniani. Watu tunamatatizo Nelly! Nikikwambia yangu unaweza ukadhania ni hadithi. Lakini ilibidi kuchagua. Watu kukutenda ni jambo moja, huna uchaguzi na huna jinsi. Ila kuendelea kujiadhibu kwa ulivyotendwa, hilo ni jambo la pili na ni uchaguzi binafsi kila mtu anatakiwa kuamua na kuishi hivyo.” Nelly akamtizama na kunyamaza bila kujibu.

Hawakuwa wakienda mbali na ni kama dereva alijua wanakoelekea. Akaona gari linaingia sehemu ambayo hapakuwa na nyumba. Akajiweka sawa kuona hicho alichoandaliwa na Billy. Akaanza kucheka vile alivyokuwa anapokelewa na taa zilizopangwa kwa mstari, tena chini mchangani kama kutengeneza njia. Akacheka na kutingisha kichwa. Billy akamuona na yeye akacheka.

“Kazi unayo Billy! Sasa yote haya kwa nini!?” “Wewe twende.” Gari lilikuwa limeegeshwa, akamfungulia mlango, akashuka. Alipokwenda upande wa pili wa gari, akasimama kwanza. “Billy wewe! Haya mambo umeyafanya saa ngapi!?” “Pesa yangu ndio inanitumikia.” Akaongea bila hata kuuma maneno. “Mwenzio haya mambo nimeona kwenye filamu tu!” “Hata mimi. Nikajiuliza hivi ni kwa nini watu wengine ndio waendelee kunufaika na pesa yangu halafu mimi mwenyewe mtafutaji hata sifaidi! Ndio nikaona tuje tufurahie pamoja. Nikawaonyesha filamu niliyokwisha ona kama hivi, nikatamani siku moja na mimi kuja kuwa sehemu kama hiyo. Walipoelewa na kuniahidi wanaweza kunitengenezea sehemu kama hii, nikawalipa wanitengenezee.” Nelly akarudisha macho kwenye hiyo sehemu. Akacheka taratibu.

“Kweli pazuri.” “Basi twende tukatumikiwe. Na mimi ni mara yangu ya kwanza kuwa kwenye madhari nzuri hivi. Nilitaka na wewe uwepo, tupumzike wote.” “Nashukuru.” Wakaanza kutembea kusogelea hiyo sehemu iliyokuwa imeandaliwa maalumu kwa ajili yao. Ni taa zilizowekwa tu hapo ndizo zilizoweka mwanga eneo hilo zima. Kukawashwa na moto maalumu wa umeme, si wa mkaa ili usizime kwa upepo. Kwa hiyo huo moto ukusaidia kuleta hali ya joto kiasi maana ilikuwa karibu na ufukweni, usiku huo tayari kulikuwa na baridi. Hakika kulivutia.

Kibanda kilichokuwa kimejengewa hapo kilipambwa vizuri sana. Halafu kulikuwa na mziki mzuri. Nelly akazidi kucheka kwa kuhamasika zaidi. “Aisee hii ni nzuri na sahihi! Kwa kutizama tu, akili inatulia!” “Nimefurahi kama umefurahia Nelly. Sikujua kama ungependa kwa kiasi hiki!” Wakaenda kukaa. Akasogea muhudumu wa kiume na kuanza kuwafungulia vinywaji hapo mezani. Na vyenyewe vilikuwa hapo na kupangwa vizuri.

Duniani Tunayo Dhiki.

Wakafunguliwa champaign. “Nataka tu toss.” Billy akaanza wakati glasi yake imeshapata kinywaji hicho cha champaign. “Kwa ajili ya nini?” Nelly akauliza baada ya muhudumu kumaliza kumuwekea na yeye kinywaji kwenye glass yake. Akawapisha kabisa pale. “Kwa ajili yetu na maisha.” Nelly akafikiria kidogo. “Mimi naona si kwa maisha. Labda kwa ajili yetu tu.” Bill akacheka na kuweka glasi yake chini.

“Nilikwambia jinsi nilivyokuwa nimezaliwa kwenye neema?” “Na wewe mwenyewe umejawa neema.” “Sikatai. Sisi ni watu wa Zimbabwe, lakini mimi na ndugu zangu ni raia au tulizaliwa na kukulia kwenye mji wa Valencia, nchini Spain. Baba na mama walipofika tu huko miaka hiyo, wote wakajiingiza kwenye kazi za medical kitu kilichotusaidia sana kimaisha.” “Inamaana kama madaktari?” “Baba ndio alikuwa daktari. Alitumwa na serikali yake kusoma. Ila kwa kuwa alifanya vizuri sana, alipomaliza, akarudi nchini Zimbabwe akatumika kwa miaka waliyokuwa wamekubaliana na nchi yake iliyompelekea huko kusoma. Akaoa na kuamua kurudi tena Spain. Anasema alipapenda sana na alikusudua kuja kuishi huko. Kufupisha habari kwa upande wao, mama naye alipofika huko akasomea mambo ya unesi. Basi wote walifanikiwa sana.” “Bado wapo?” “Mpaka leo wapo.” Nelly akashangaa sana.

“Baba anasema sisi tuna genes za kuishi miaka mingi. Lakini pia nafikiri ni jinsi ya kutunza hii miili, Nelly. Sisi tumejifunza kutunza miili yetu kutoka kwa wazazi. Wanausemi unaosema kuwa hii miili huaribika. Kwa hiyo linapofika kwenye kuitunza ni kipaumbele, ili iweze kukutumikia. Sasa hawa wazazi wangu hawa, wanandoa ya mpaka sasa hivi. Simaanishi kwamba wanandoa ya ajabu sana, ni kama wanadamu wengine tu, ila sisi watoto wao tulivutiwa au niseme mimi nilivutiwa zaidi na jinsi walivyoweza kuwa pamoja mpaka kutulea sisi. Nikimaanisha katika ugumu wote wa maisha, lakini walimudu kuwa pamoja.” Billy akanywa kinywaji kingine si ile champaign. Ni kama aliona isubiri kwanza.

Wakaletewa na supu. “Kunywa hiyo supu ikiwa ya moto kabla haijapoa.” “Nakusikiliza.” “Najua. Lakini kula wakati nikizungumza.” Nelly akachukua kijiko maalumu chakunywea supu, akaanza kunywa. “Mlizaliwa wangapi?” “Watatu. Nina kaka yangu na dada yangu. Yeye ndio wa mwisho. Mama alisema alikusudia lazima aje kuwa na mtoto wa kike. Anasema asingeacha kuzaa kama asingepata mtoto wa kike.” “Kwa nini!?” Nelly akashangaa sana.

“Anasema akiwa nesi aliona mengi. Akamuomba Mungu aje  azae mtoto wake wa kike, wakumvalisha nguo atakapokuwa mzee, sio wakwe.” Nelly akatulia kidogo. Billy akamuona amepotea kabisa pale. “Nelly?” Akamuita. Nelly alikuwa akikoroga supu yake, akamtizama. “Kwetu ilikuwa tofauti Billy. Baba hakufurahia kabisa kitendo cha mama kuzaa mtoto wa kike.” “Ambaye ni wewe?” “Yeah! Alimnyanyasa sana mama kiasi cha kumuathiri. Nafikiri pia ikaanza kumuingia na mama kuona kama alikosea na kumfanya aishi vile na mimi. Hatukuwa na mahusiano mazuri sana na mama. Sasa sijui ni kwa hilo au sababu ya mateso ya baba! Lakini ni jambo ambalo baba alihakikisha na mimi naelewa. Kwamba hakufurahia kupata mtoto wa kike. Na alisema waziwazi ni aibu kwao kwamba hana mrithi.” Billy akamuhurumia.

“Na mbaya zaidi, nafikiri mama alishindwa kupata mimba ya pili kwa haraka. Nikabakia mimi tu zaidi ya miaka kumi. Aisee tulijua na kuelewa hakuwa akipafurahia pale kwetu sababu ya kukosa mtoto wa kiume. Alikuwa anaweza akapotea hata mwaka, ndipo anarudi. Na akirudi hata msichana wa kazi kama ni mgeni, atajua shida yake ni kutojaliwa mtoto wa kiume au mkewe hana uwezo wakumpa mrithi. Alikuwa mnyanyasaji mno, kiasi cha kusikia ile hali mpaka moyoni. Alimdharau mama kwa kumpiga makofi hata mbele ya watu endapo akifanya jambo asilolipenda yeye.” Nelly akafikiria kidogo akawa kama amepata jinsi ya kumuelezea Billy akamuelewa anachozungumzia.

“Yaani anaweza kumtuma maji ya kunywa mbele za watu. Mama akimletea, anagomba labda glasi ina maji nje, hajaikausha vizuri. Atapigisha ile glasi chini kwa nguvu na kumchapa mama makofi hapohapo.” “Haiwezekani Nelly!” “Kweli Billy! Siwezi kusahau hiyo hali. Mpaka sasa huwa nakaa najiuliza, hivi mwanadamu anawezaje kumruhusu mwanadamu mwenzie amtendee hivyo!? Kwa nini mama aliruhusu hiyo hali!?” “Labda kiuchumi.” “Usifikiri baba alikuwa ni mtoaji! Hapana. Tena kwa kusikia kabisa akisema hawezi kupoteza pesa yake kulea mke wa mtu. Yaani mimi.” “Nelly!?” “Nakwambia ukweli Billy, sidanganyi. Alichokuwa akisema eti yeye hawezi kuhangaika kufanya kazi, aje alishe mtu atakayekuja kuzalishwa na mwanaume mwingine. Kwa kusema waziwazi.” Nelly akaendelea kuzungumza kwa uchungu, asikumbuke ni Billy ndiye aliyekuwa akizungumzia juu ya familia yake.

“Na ninapokwambia alikuwa akiondoka hata mwaka, jua ni mama ndiye aliyekuwa akiendesha familia japo nyumba ni yeye baba alikuwa ameijenga. Anyways, tuendelee na wewe. Vyangu vitakushangaza tu.” “Hapana. Nimefurahi kukusikia. Nimepata majibu ya maswali mengi sana juu yako.” Nelly akacheka kwa kuguna akaendelea kunywa supu yake, Billy akimtizama.

“Nakusikiliza Billy.” “Kwa aina ya ndoa ya wazazi wangu, mimi na kaka yangu tukaambiana baba alibahatika kwa kuwa alioa mtu wa nyumbani. Tukakubaliana tukaoe nyumbani. Lakini baadaye kaka yangu akapata mwanamke kulekule, mwenye asili ya kizungu, akaamua kuoa. Mimi nikakazana, nikarudi Zimbabwe nikapata mwanamke, akakubali kwa haraka sana tukaishi naye Spain. Ndoa ikafungwa ya kimila, nikapata mke, tukarudi Spain. Mungu akajalia watoto hao wawili wa kike.” Akamuona Billy anacheka kwa kusikitika.

“Nini?” “Mimi sikujua kama kuna shida kati yetu mpaka nilipokuja kujua mwenzangu anamahusiano na rafiki yangu.” Hapo Nelly akaweka kijiko chini. “Rafiki ambaye aligeuka kama ndugu ambaye tulikuwa naye pamoja ila mwenzangu hakuwa akifanya kazi nje ya nchi kama hivi mimi. Alikuwa akiishi na kufanya kazi hapohapo nchini. Mweupe wa hapo. Hivi unajua Anele aliniacha kwa ajili yake!” “Subiri kwanza Billy! Alikuachaje?!” Billy akajicheka kwa kujidharau na kutingisha kichwa kwa masikitiko, Nelly akimtizama kama asiyeamini.

“Aliniacha kirahisi kabisa bila shida akisema yeye hana furaha kwenye ndoa yetu. Alitegemea tungekuwa tukiishi wote lakini amekua na ndoa ya peke yake, mimi sipo nyumbani. Amekua akilea watoto peke yake. Haijulikani kama ameolewa au la! Watoto wanamtambua Carlos kama ndio baba yao. Kwa hiyo kule kumfumania na Carlos haikuwa bahati mbaya, ni mahusino ya muda mrefu  na anashangaa ni kwa nini nimechelewa kugundua. Akaita hiyo nayo ni ishara ya kuwa ndoa yetu ilishakufa muda mrefu bila mimi kujua. Akatafuta mwanasheria kwa ajili ya talaka. Hivi tunavyozungumza, Anele na Carlos walioana, wanaishi pamoja. Mbaya zaidi, wanaishi na binti yangu mdogo ambaye na yeye anamtambua Carlos kama baba.” “Billison!” Nelly akashangaa sana, ila Billy akacheka.

“Acha Nelly! Nilikaribia kujipiga risasi kujiua. Lakini binti yangu huyo mkubwa akanisihi sana nisije kumuacha hapa duniani kwa kujiua. Alihama mji kabisa, mpaka leo ameshindwa kuzungumza na mama yake, ila mdogo wake yupo na mama yake. Na wanaendelea vizuri tu.” “Pole sana Billy.” “Ndio maana unapomzungumzia mwanadamu, nakuelewa Nelly. Carlos alikuwa rafiki akinichekea, nisijue alikuwa akilala na mke wangu! Ameoa mwanamke niliyemuhamisha nchi na hana haya wala hajutii! Anasema Anele hakuwa na furaha na alikuwa mpweke.”

“Kwani hamkuwa mkiishi pamoja?” “Unajua hizi kazi Nelly. Na yeye nilikuwa nikimwambia. Ni kwa muda tu wakati natafuta nafasi ya kazini kama niliyonayo sasa hivi. Nilimwambia garama zetu za maisha zipo juu sana. Kuendelea kuishi vile, ni lazima na mimi nikue kimaisha. Kazini. Ili tuishi kwa furaha zaidi. Nilimwambia ni kwa muda tu, tungetulia pamoja. Akaniambia ameelewa.”

 “Kwani yeye hakuwa na kazi?” “Hapana. Ila kutumia. Hujawahi ona mwanamke mwenye matumizi na pesa kama yule na huyo mtoto wake wa mwisho. Anele ni garama haswa. Sasa aina ile ya matumizi ilikuwa nilazima nifanye kazi. Unaingiza huku, huku zinatoka. Nilikuja kugundua pia alikuwa akijenga sana kwao. Hapa ninapokwambia huko Zimbabwe ana mahoteli. Na yote hiyo ni pesa yangu.” “Sasa alitegemea upataje pesa mkiwa mnaishi naye tu nyumbani!?” “Asante.” Billy akashukuru kwa Nelly kuelewa.

“Ndio nakwambia hivi, namuelewa mwanadamu. Nilikaribia kurukwa na akili na ndio kujiua. Mbaya zaidi kaka yangu yeye ambaye alioa mwanamke wa palepale, mwenzangu ndoa yake inaendelea mpaka leo! Mimi niliyetaka ubora zaidi, nikakwama. Baba alipoona nipo vile ndipo akaniambia nitakosa na kazi ambayo imeshanigarimu ndoa na mtoto. Maana aliniacha nikiwa nakaribia kupandishwa cheo. Akaniambia nichague kujiumiza zaidi nife au nikubali matokeo na niendelee. Mama akaniambia kuchagua furaha ni rahisi japo nimeumizwa, itanisaidia. Haikuwa rahisi Nelly. Kwa kuwa binti yangu alimchagua Carlos na mama yake, ikabidi niwaachie ile nyumba nikarudi kuishi na wazazi. Ndipo binti yangu mkubwa na yeye akanifuata. Tukawa tunaishi hapo mpaka alipomaliza chuo. Akachukua kazi mji mwingine kabisa, na mimi nikachukua cheo nchini Uingereza. Nikaishi Uingereza kwa miaka zaidi ya mitano ndipo nafasi ya huku ikatokea. Nikamwambia baba narudi kuishi Afrika. Binafsi alinipongeza. Alijua ningechukia kabisa Afrika. Lakini ikawa kinyume. Ndipo nilipo.” Nelly akanyamaza akifikiria.

“Kwa hiyo Nelly, mimi ilinibidi kuchagua fungu la pili. Furaha.” Nelly akamwangalia. “Si rahisi, lakini ilinibidi kufanya juhudi za makusudi kuishi hivi unavyoniona leo. Nilipoteza nyumba ambayo nilifanya kazi kwa juhudi kwa makusudi kuilipia mpaka kumaliza. Lakini sasa hivi anaishi Anele na Carlos. Nimepoteza mtoto kwa rafiki yangu. Hutamsikia akinipigia simu kunijulia hali, labda iwe ni birthday yangu. Mara zote mimi ndio huwa namtafuta, napo hana muda mwingi na mimi kwenye simu, inakuwa kama nampotezea muda.” “Ukienda kumtembelea?” “Ndio hivyohivyo. Haonekaniki kama ni jambo analotaka. Lakini na mimi huwa najitahidi. Kila kwenye birthday yake huwa nakwenda kumuona. Hata akinipa dakika 10 pia nashukuru. Nikimuomba tutoke kwa chakula, anaweza akataka lazima mama yake na Carlos nao wawepo sababu ndio familia yake.” “Billy!” Nelly akashangaa sana.

Billson akacheka kwa masikitiko. “Acha tu.” “Unafanyaje sasa!?” “Baba aliniambia lazima nijue ninachotaka na kuhakikisha nakipata. Maadamu ni binti yangu, na ninataka muda naye, akasema hiyo ndio iwe garama yakulipa. Kuendelea kuwakubali hao wawili wawepo kwenye maisha yangu tu. Kwa hiyo huwa nikitaka kuonana naye, mara nyingine huwa nakwenda palepale nyumbani.” “Mmmh!” Nelly akachoka kabisa. Wakamaliza supu. Wakaletewa chakula. Wakaanza kula kimyakimya tu kila mmoja akiwaza lake.

Akamuona Nelly anacheka mawazoni ila tabasamu usoni. “Nini?” “Hivi kama nikuondoka hapa kisiwani usiku huu na hivi nilivyoshiba, tunaondokaje?” “Kuna chaguzi mbili. Ipo ndege ya kimataifa kutoka nje ya nchi, inapitia hapa leo usiku wa saa tano kuelekea Dar. Nimeambiwa tunaweza kupata nafasi first class. Au unaweza kurudi kulala kwenye kile chumba. Nimelipia mpaka kesho.” “Wewe umeamuaje?” “Nitaamua baada yako. Kama utaamua kulala, ujue na mimi nitalala mpaka kesho ndipo tuondoke wote. Ila kama unaamua kuondoka, pia ujue tutaondoka wote. Uamuzi ni wako.” Nelly akatulia akifikiria.

Akagundua Billy anamtizama. Akamwangalia. “Unapenda kuniangalia wewe!” “Kwa kuwa unavutia.” “Acha hizo bwana! Ila ujue nimefurahia. Kila kitu.” “Mmmh! Sidhani kama ni kila kitu. Helikopta?” Nelly alicheka sana baada ya kukumbushwa. “Aisee ile ilikuwa mbaya!” “Niliona, hata rubani aliona na kujua.” Nelly akazidi kucheka. “Sawa. Kasoro helikopta. Ila vingine vyote nimefurahia.” “Nimekuona. Leo umekuwa watofauti Nelly. Unacheka!” “Sijapata huu wakati tokea...” Akafikiria bila kupata jibu. “Aisee sijawahi kupata huu wakati Billy! Sijawahi.” “Basi nimefurahi kama umefurahia.” Wakatulia, mziki ukitumbuiza taratibu.

“Billy?” Akamuita kama aliyekuwa mawazoni. “Mimi napenda kucheza.” “Nilikuona siku ile na mdogo wako.” “Nilipokuwa masomoni nikifanya shahada yangu ya tatu, nchini Uingereza, nikajiambia nifanye kitu kigeni na chatofauti kwa kujipongeza kufikia pale nilipo. Ndio nikachukua dance classes. Madarasa yanayofundisha jinsi ya kucheza, nje ya pale chuoni.” “Hongera sana.” “Sikuishia hapo. Nilipoona nirahisi nikaongeza na ice skating.” Billy alicheka sana. “Kwa kusema hivyo, naomba tucheze wote.” “Mimi si mtaalamu wa kucheza, Nelly.” “Kwa kuwa leo nina mudi nzuri, nitakufundisha.” “Okay.” Billy akasimama na kwenda kumnyanyua pale.

Nelly akaanza kucheza mbele ya Billy, Billy akaanza kucheka. “Fuatisha sasa, acha kusimama tu.” Nelly akaongea akicheza. Walicheza wakicheka kwa muda mrefu tu. Ukaja mziki wa tarabu. “Bado unataka kucheza na mimi?” Akauliza Billy kiustarabu. “Oooh yeah! Come here Billson.” Akamuita kwa ishara ya kidole. Billy akacheka akimsogelea. Akamshika taratibu wakaanza kucheza.

“Sijui nimeanza kulewa!” Billy alicheka sana akijua ni kweli ameanza kulewa. “Huu uchangamfu si kawaida yangu!” “Mimi naona ni kupata wakati mzuri.” “Eti eeh?” “Yeah.” “Nakushukuru Billy. Na kama hutajali, naomba leo nilale hapa mpaka kesho. Hata hivyo Jax leo atakuwa kwake, sina sababu ya kurudi.” “Kwani huwa anakuwa kwako?” “Anakua kwangu na hajui kupika. Ana kazi ya kutengeneza juisi na chai tu. Kwa hiyo akiwepo nyumbani huwa na jitahidi kuwepo ili nimsaidie chakula.” “Haina shida. Tunaweza kuondoka kesho.”  Walicheza hapo kwa muda, kisha wakarudishwa hotelini.

~~~~~~~~~~~~~~~~

B

illy alimrudisha mpaka chumbani kwake na kumfungulia kabisa mlango. “Hii mara ya kwanza imeisha vizuri.” “Tutaona ya pili, tatu na nne itakavyokwenda?” Nelly akauliza. “Yeah. Nimeshaanza kuwa na hamu na ya pili.” Nelly akacheka. “Tutakwenda wapi?” “Nilikwambia sitakwambia Nelly!” “Sawa. Ila usifanye garama kwa kiasi hiki. Au niambie tuchangie.” “Wewe panga safari zako, unialike. Kama nitakua na muda nitakufikiria.” Nelly alicheka sana. “Basi kama ni hivyo na mimi nitakufikiria.” “Sio katika hizi safari tatu zilizobaki. Hizi tumeshakubaliana.” Wakakaa hapohapo mlangoni na kuendelea kufahamiana taratibu. Billy akaagiza vinywaji, wakaletewa hapohapo walipokuwa wamekaa. Nje ya mlango chumbani kwa Nelly. Kila mmoja akatamani kumuuliza mwenyeziwe swali la msingi, lakini wakaona wawe na kiasi. Wakanyamazia.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment