Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Chozi Langu! - SEHEMU YA 11. - Naomi Simulizi

Chozi Langu! - SEHEMU YA 11.

 Kwa Lara.

K

adiri siku zilivyozidi kwenda, Lara akazidi kuvutia. Si kwa nje tu, Lara alikua zaidi ya kile Jerry alitegemea. Lara akawa kama aliyepata anachokitaka, akatulia kabisa. Hana makuu, mridhikaji, si mlalamishi kabisa, si mgomvi, hana hekaheka, haulizi chochote kinachoendelea kwa Jerry. Akawa kama aliyeelewa nafasi yake, akajifunza kuipokea, akatulia ndani kimya. Mzuri kwenye kila eneo, wivu ukaanza kwa Jerry mwenyewe. Kanuni alizoziweka yeye mwenyewe zikaanza kumsumbua na kuanza kumshinda. Akaanza kumchunga mtu aliye ndani. Wasiwasi kwa Lara anayemuacha ndani.

          “Nani huyo?” Lara akashangaa sana na kumgeukia kwa mshangao kama yameanza lini! “Ni siri?” “Hapana!” Lara akajibu kwa mshangao maana haikuwa kawaida yao kuuliza. Walikuwa wapo hotelini Mwanza. Alimsindikiza Jerry. Akaondoka asubuhi kwenda kwenye shugli zake, akarudi hapo hotelini baada ya kama masaa 5 hivi. Ndio maswali hayo yakaanza kwa Lara aliyemkuta hapo amekaa tu na simu mkononi akichati.

          “Mbona ni swali rahisi tu lakini unashindwa kujibu!?” “Ni Lucas.” Lara akamjibu. “Lucas ndio nani?” “Mtoto wa dada yangu!” Jerry akamtizama. “Ni nini Jerry!?” Lara akamshangaa. “Si nimeuliza tu!” “Ila umeuliza kwa wasiwasi! Kila kitu kipo sawa?” Lara akaweka simu na kumsogelea pale. “Kila kitu kipo sawa, nilitaka tu kujua.”

“Bado sijapata mwanaume mwingine Jerry! Ni wewe tu. Naomba usiwe na wasiwasi.” “Kwa hiyo upo kwenye kutafuta?” Lara akamwangalia vizuri na kumshangaa. Makubaliano ya tangia mwanzo sio kuchungana. Ni kutaarifiana tu, na kuwa makini! “Ni nini kinaendelea Jerry? Kuna makubaliano mapya kati yetu ambayo umesahau kuniambia? Maana umeahidi kuwa muwazi kwangu! Ni nini kinaendelea ambacho sijui au nakosea?!” “Ninachotaka ni kujua tu kinachoendelea, basi. Sitaki kupitwa au kushangazwa baadaye, kuja kujua kuna lililokuwa likiendelea mimi sijui.” “Usiwe na wasiwasi. Hutapitwa na chochote. Kama kuna mahusiano mengine nitayaanzisha mbali na haya, uliniambia mwanzoni kabisa, nikwambie tuzungumze. Nafikiri ndivyo hivyo?” Lara akauliza vizuri tu, akashangaa Jerry anaondoka kuingia bafuni.

Akamuacha kidogo na kumfuata. Akamkuta amesimama mbele ya kioo. “Naomba nigeukie Jerry.” Akatulia kidogo na kugeuka. “Naomba unikumbatie.” Lara akajisogeza. Jerry akamkumbatia. Akajituliza hapo mikononi. Akamsikia anavuta pumzi kwa nguvu, Lara akatulia kabisa hapo mikononi. Akaanza kumuhisi anatulia na kumkumbatia vizuri. Akajitoa hapo na kumshika mkono akamtoa hapo bafuni wakarudi kwenye kochi.

“Tumezaliwa watatu nyumbani kwetu.” Lara akaanza kujieleza. Ilikuwa mara yake ya kwanza kuzungumzia mambo yake. “Wakike watatu na dada yangu anamtoto wa kiume anaitwa Lucas. Anasoma darasa la sita. Mama amemlea kana kwamba ni mdogo wetu wala si mtoto wa dada. Na huwa napatana naye sana. Akiwa na uhitaji wowote ule, hata shule, huwa ananitafuta mimi. Ndiye tulikuwa tukichati naye hapa uliponikuta.” Lara akaendelea taratibu.

“Samahani kama uliingia na kuhisi nimekupuuza. Nilikuwa namalizia kumtumia ujumbe ili niweke simu pembeni tuwe na muda wa pamoja.” Lara akaongea kwa upendo. “Na hakuna kinachoendelea. Nakuruhusu uwe unaangalia simu yangu. Nitakupa hata namba ya siri. Sina ninachokuficha Jerry. Sina ninachotafuta. Na sina mpango wakuanzisha mahusiano mengine sasa hivi. Nimetulia kabisa. Ni wewe tu kwa sasa. Kitakachonitoa kwako na kutafuta mtu mwingine ni nitakapokuwa tayari kuanzisha familia ambayo haupo tayari kunipa. Hicho tu, lakini si vinginevyo. Ninaridhika na wewe. Napenda unavyonijali. Hunifichi kokote, upo na mimi. Sina sababu yakutafuta mwanaume mwingine kwa sasa.” “Mpaka lini?” Jerry akauliza akisikika ametulia.

“Sijui Jerry. Lakini si kwa haraka. Nimetoka kutendwa vibaya sana na mwanaume ambaye tulibakiza siku chache tu, tuone. Sina hamu yakurudi huko kwa sasa. Hiki tulichonacho, kwangu, kwa wakati huu ndicho nahitaji.” “Pole. Lakini natamani ungeniambia zaidi.” “Hapana Jerry. Lakini ujue sina mpango kwa kuwa sina hamu. Nipo na wewe kwa asilimia 100. Naomba uniamini kwa kuwa pia mimi sio muhuni. Ikitokea nipo na mtu mmoja, huwa najifunga kwake tu. Na hata nikipata mwanaume mwingine ambaye tutakubaliana kuanzisha familia, sitakuwa na wewe. Huwa siwezi.” Hilo likamuuma sana Jerry. Akamuona amepoa kabisa.

“Naomba niangalie Jerry.” Akamgusa taratibu. “Naomba uwe na uhakika. Unaponiona nipo hapa na wewe, jua upo peke yako. Huwa siwezi kuchanganya.” “Nitajuaje kama ndio upo kwenye kuanza kutafuta mtu wakuanza naye maisha?” “Nitakwambia Jerry. Nitakwambia kuwa nataka kuanzisha familia. Uliniambia nikwambie ili tuzungumze. Naahidi muda utakapofika, wala hutahitaji kuhisi. Mimi mwenyewe nitakwambia na nitakuaga rasmi.” Jerry akavuta pumzi kwa nguvu na kupoa.

“Niambie unachofikiria Jerry. Uliniahidi utakuwa muwazi.” “Nahisi nimeanza kukupenda Lara. Lengo la kwanza linaanza kupotea.” Lara akakunja uso. “Mwanzoni nilitaka tu mtu wa kumtumia kwa haja zangu. Lakini kwako napata kitu ambacho sijawahi kupewa na mtu yeyote yule hapa duniani. Pengine kwa kutofungua milango mwenyewe, lakini sijawahi kuishi na mtu akanifanyia kama hivyo wewe. Nilishakuwa na wanawake kabla yakuoa. Lakini sio kuishi nao hivi. Na tamaduni zetu na mke wangu ni tofauti. Mengi unayonifanyia wewe, hajui hata kama anatakiwa kunifanyia. Sio kwa kuwa hanipendi, lakini haipo kwake. Halafu ni mtu mzima kwangu.” Jerry akaongea kwa upole.

“Ninachotaka kukwambia, napata zaidi ya nilichotegemea mwanzoni. Naanza kuingiwa na ugumu wa kukuchangia na mtu.” Lara akashangaa mpaka akatoa macho. “Jerry! Lakini hivyo haikuwa...” “Najua Lara. Nakumbuka nilichokwambia. Sijasahau. Tuache tu.” Jerry akasimama na kurudi upande wa chumba, akamuacha Lara ametoa macho. Hakuwa tayari kwa wakati huo, lakini alihitaji kuwa na watoto na mume wake. Jerry alionekana hataki kabisa kuanzisha familia na yeye, lakini anataka kumiliki! Lara akabaki akimfikiria hapo kwenye kochi akajiambia hatamuahidi chochote kwa kuwa hataishia kuwa nyumba ndogo daima.

Alishajua hapo kwa Jerry anapumzika tu baada ya yaliyomsibu. Maisha lazima yaendelee baadaye, tena kwengine. Alichokuwa akikifanya ni kujijenga. Kujenga kwao na kujiwekea kila pesa anayopewa na Jerry huko benki bila kusahau kujikumbusha kuwa hapo ni mpitaji tu. Leo Jerry anataka kuanzisha jambo jingine! Lara akaadhimia asimpe nafasi. Yeye ameshakuwa na familia, hawezi kumzuia yeye kuja kuwa nayo. “Hakika sitampa hiyo nafasi yakunibana.” Akaadhimia moyoni huyo Lara ambaye alishampa mwanaume moyo wake, akamtenda bila huruma. Alishang’atwa na nyoka, akajifunza mwanadamu hatakiwi kupewa moyo ila Mungu tu. 

~~~~~~~~~~~~~~~~

Akaagiza chakula ambacho alijua Jerry angependa. Akasubiria mpaka kilipoletwa hapo chumbani kwao na muhudumu, ndipo alipomfuata chumbani akamkuta amejilaza. “Nimekuagizia chakula unachopenda. Twende tukale.” Akamwangalia Lara. Akacheka na kwenda kumkalia. “Kwa nini unatafuta kujinyima raha kwa kitu cha baadaye wakati wewe mwenyewe uliniambia tufurahie leo?” Akabaki akimwangalia. “Nishike basi kidogo Jerry! Ni nini? Mambo hayakwenda vizuri huko?” “Kila kitu kipo sawa, nafikiria tu. Unajua tangia nimpoteze mama yangu, sijapata mtu wakunijali hivyo mpaka wewe!” Lara akamwangalia akiwa ametulia tu juu yake.

“Nilihangaika mpaka nikakata tamaa!” “Ya nini?” “Yakuja kupata upendo na kujaliwa kama vile alivyokuwa akinifanyia mama yangu! Niangalie kwa umri wangu huu, nakwambia mpaka naishi na wewe ndio napata kitu nilichokuwa nikikitafuta na kukikatia tamaa! Leo nakipata kwako wewe ambaye najua utakuja kuniacha! Unafikiri nitajisikiaje?” “Kwa hiyo unataka tuanze kukosa amani kati yetu kwa kitu ambacho hata sijui kitatokea lini!?” Jerry akatulia.

“Niangalie Jerry. Niangalie nipo hapa na wewe. Akili, mawazo na mwili wangu vyote vipo na wewe hapa na popote utakaponihitaji.” “Nakuhitaji uwe wangu daima.” “Wewe unajua haiwezekani Jerry. Nataka siku moja kuja kupata kile unachompa Barbara. Heshima ya mke na watoto. Familia kwa ujumla. Na mimi naamini siku moja nitakuja kuwa navyo. Nilikukubali kwa haraka kwa sababu pia ulionekana muwazo na una msimamo na unachotaka. Mwanzoni ilinisumbua, lakini nikaelewa napita tu kwako.” “Au mimi ndio napita tu.” “Jerry! Ni nini kinakuingia? Naomba usikiruhusu. Twende tukale. Jioni tutaenda kula nje, tutakuwa na wakati mzuri. Twende.” Akamtoa pale kitandani wakaenda kula.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika mida ya saa 11 jioni, Lara akaanza kujiandaa ili waende kula. Kuna mahali walikuwa wakichoma nyama vizuri hapo jijini, walipenda kila wanapokuwa hapo Mwanza, angalau kwenda mara moja kula. Alipendeza Lara, ungependa kumuangalia. Jerry naye alivaa jinsi ya blue na t-shert nyeupe tu wakatoka wakiwa wamependeza. Wakati wanaingia kwenye hiyo baa, sehemu ya nje tu wakapata sehemu ya kukaa. Jerry akamvutia kiti, akakaa. “Asante.” “Karibu.” Akavuta kiti pembeni yake, wala si mbele, pembeni. Na yeye akakaa. 

Milima Haikutani Lakini Binadamu Hukutana.

Kabla hawajaagiza vinywaji Lara akashangaa Tino anamsimamia mbele yake. Alishituka mpaka Jerry akamuona. “Lara!” Lara akabaki kimya. “Kumbe ulikimbilia huku Mwanza!” Tino akaendelea kumuongelesha lakini Lara akabaki kimya hata Jerry akabaki akiwaangalia. “Samahani mkubwa, sijakusalimia Mr Kembo. Heshima yako.” “Na wewe niii!” Jerry akataka kumfahamu. “Pengine utakuwa hunifahamu. Naitwa Tino. Nafanya kazi kwenye tawi la CRDB ambako huwa unapenda kutumia kufanywa Swift. Na mimi nilishapata bahati ya kukuhudumia.” “Oooh!”  Jerry akaitika hivyo tu na kumgeukia Lara kama kumuuliza kinachoendelea.

Tino na yeye akarudisha macho kwa Lara. Walivyokaa pale walionyesha wazi kuna mahusiano. “Angalau ungeniaga Lara! Sio kuondoka kimyakimya. Au bado ulikuwa na hasira na mimi? Na haukuwa kweli umenisamehe kama ulivyoniambia?” “Nilihitaji kupumua Tino. Wala wewe hausiki. Habari za siku?” Tino akabaki akimwangalia. “Huyu anaitwa Jerry ni...” “Namfahamu.” Tino akajibu na kuondoka.

Jerry akageuza kiti vizuri kumuangalia Lara. “Anaitwa Tino kama alivyojitambulisha.” Hilo ndilo Lara aliloweza kuongea na kunyamaza. Jerry akakunja mikono yote kifuani kama anayemshangaa. Lara akainama. Jerry alimpa kama dakika moja. Alipoona kimya, na Lara amebaki ameinama. Jerry akasimama, Lara akamuona anaondoka. Akamfuata.

“Jerr! Jerry!” Lara akawa anamuita huku akimfuata nyuma. Jerry akasimama na kumtizama, walishafika sehemu ya kuegesha magari. “Hatuli tena?” Lara akauliza taratibu. “Unanitania Lara!?” “Hapana. Kwa nini?” Lara akauliza akiwa hana hata ujasiri. “Unanijua mimi ni nani?” Lara kimya. “Unajua wadhifa wangu?” Kimya. “Nakutoa kwa chakula sehemu unayopenda wewe! Isiyoendana na hadhi yangu. Lakini nipo hapa kwa ajili yako. Mwanaume anakufuata mbele yangu akionyesha anakufahamu vizuri tu na mnaonekana hamjamalizana!” Jerry akawa mkali. Lara kimya akimtizama. “Halafu unataka kuniambia nini!?” “Kwamba sasa hivi umekasirika. Na kwa kuwa upo hapa kwa ajili yangu, si pa hadhi yako, naona kweli tuondoke.” Lara akampita na kuita taksii.

Taksii ikafika na kusimama karibu yao. Jerry akabaki akimuangalia asiamini. Akahisi kudharauliwa sana na Lara. Bila kutegemea Lara akafanya kosa ambalo Jerry alikusudia kiumbe mwanadamu asiwahi kuja kumfanyia tena maishani. Alishajiaminisha amefanikiwa kuweka kikomo cha kudharauliwa. Alikuwa akihangaika kwa kadiri ya uwezo wake akitafuta heshima aliyopoteza tokea mtoto. Jerry alishaathiriwa na maneno ya familia akionekana dhaifu. Akatoka kwao na kukimbilia mjini kutafuta heshima kwa njia ya pesa. Na kweli akafanikiwa sana. Jerry alikuwa akifika sehemu, inajulikana ‘Mr Kembo’ yupo hilo eneo. Leo Lara ni kama akamrudisha kihisia kule alikopitishwa! Yeye ni wa kudharauliwa tu, hastahili kuambiwa chochote, hana hadhi hiyo! Akabaki amesimama lakini hisia zimebadilika kabisa.

“Twende Jerry.” “Sio na mimi.” Lara akashituka sana. “Unamaanisha nini?!” “Wewe unanifahamu kwa asilimia kubwa sana. Kwa nini hutaki mimi nikufahamu? Ni nini unaficha au unaona sina akili ya uelewa? Mimi ni dhaifu sana, sina uwezo wa kujua mambo na kuweza kuyabeba kama wengine?” Lara asijue hayo yanazungumzwa kutoka kwenye hisia zilizoathirika sana, ila kufunikwa na pesa tu. “Hapana Jerry! Hakuna ninachoficha ila sikutaka kujikumbusha machungu.” “Yepi?” “Nilishakwambia Jerry. Nilikwambia pengine ni kwa kuwa unahasira, unashindwa kukumbuka.” “Juu ya nini ambacho umeshindwa hata kunitambulisha kwa mwanaume wako!” “Unaongea kwa sauti ya juu Jerry, unavuta watu bila sababu! Naomba tukazungumze.” Jerry akabaki amesimama.

“Umeingiwa na nini wewe?!” “Nimekwambia nakupenda Lara. Unanipuuza na unanidharau. Ni kama..” “Naomba tulia twende tukazungumze Jerry! Unataka kuanza fujo zisizo na maana. Hukuwa hivyo! Ni nini kinakubadilisha wakati mimi nipo na wewe?” “Kimwili tu, lakini vingine vyote havipo na mimi.” “Sasa kwa hiki unachokifanya hapa kitasaidia kweli? Naomba twende.” Jerry akakumbuka anajiharibia zaidi sifa yake hapo kwenye huo mji na wanao mfahamu. Kuonekana analilia mapenzi ya mwanamke, akajiambia ataonekana dhaifu zaidi. Akapanda kwenye taksii ili kuondoka hapo. Akamwambia dereva taksii aliyekuwa akiwasubiria muda wote wakizungumza, awarudishe hotelini. Kimya mpaka hotelini.

Lara alishuka bila kusubiri kufunguliwa mlango wa gari, akaondoka. Jerry akalipia na kumfuata nyuma. Walikutana wote wagonjwa ambao hawajapona, ila kufunika athari zao tu. Haikuhitaji nguvu nyingi sana kuwaona wao kama wao bila unadhifu wao wa nje. Ndani walikuwa wameathirika vibaya sana. Wakaingia chumbani, Lara akaanza kufungasha. Hataki kubabaishwa tena. Alishababaishwa na Jax, huyu Jerry hawezi kumruhusu. Lara kwa hasira zote akajimbia hatarudia kutendwa, asijue ujumbe anaopokea Jerry asiyejua mapito yake ni kumdharau.

“Unakwenda wapi sasa?” “Nilikimbia mambo ya kitoto, nikajua nitapumzika kwako, naona unaanza vituko visivyoeleweka. Hukunikuta barabarani mimi.” Lara akaendelea kufungasha. “Subiri kwanza Lara. Mbona unakasirika wakati mimi ndio nilitakiwa kukasirika!?” “Unakasirishwa na nini wakati nipo na wewe? Lini umenihisi hata nina mwanaume mwingine tokea tunaanzana? Na pia uliniambia ni ruksa ila nikwambie. Unaniona nimetulia, umepata mwanamke huko, unashindwa kuniambia, unanitafutia sababu. Hutaninyanyasa Jerry.” Lara akaondoka chumbani kuelekea bafuni.

“Umenisingizia Lara. Na nahisi unatafuta tu sababu ili uondoke. Uniache.” Lara akasimama na kukunja uso. “Mimi sio malaya. Sijatafuta mwanamke mwingine.” Lara akaondoka kurudi chumbani bila kumjibu na yeye akimfuata nyuma. “Lara?” “Mimi sio mkeo Jerry. Hilo uliliweka wazi tokea mwanzoni na ukasema swala la watoto halina hata nafasi ya mjadala. Nikakwambia nimeelewa. Na ukaniambia nikipata mtu wangu nikwambie. Nazungumza na nani, nasalimiana na nani, sio jambo la kutufanya tugombane. Hichi unachokifanya sasa hivi ni kunitafutia sababu tu. Umeona sijui ugomvi, hata ukifanya jambo baya sina ninalosema, umekosa sababu ya kunitoa kwenye maisha yako, ndio unaanza sababu! Sasa acha nikusaidie kwa sababu sitaishi na wewe kwa ugomvi. Itakuwa hamna sababu ya wewe kuwepo kwenye maisha yangu kama hata pumziko sipati!” Lara akaendelea kulalamika.

“Tokea tunaanzana mimi na wewe, ni lini nilikutamkia kuwa nakupenda?” Lara akasimama kama anayefikiria hilo. Hata hakuwa amezingatia hilo kwani kwa asili ya wanaume wengi aliokutana nao Lara, neno la ‘nakupenda’ wanalitamka hata ukiwa umekutana nao siku hiyohiyo hata hakufahamu, atakwambia tu ‘nakupenda’. Kumbe kwa mtu kama Jerry aliyeishi kwenye tamaduni tofauti, ukisema kwa mwanamke ‘nakupenda’ si kukurupuka tu. Unamaanisha kumpenda haswa kimapenzi kwa kuwa unamfahamu, umejua yeye ni nani, ndipo kupenda kunapofuata. Kwamba kweli unampenda yeye. Si neno la kutamka tu kutokana na hisia zilizojawa tamaa tu. Lara mpita njia kwenye maisha ya Jerry, hata hakuwa amezingatia hilo na kulitilia maanani, ashalizoea hilo neno kutoka hata kwa vijana wa vijiweni tu. Kwa tamaduni ya alikoishi Lara, neno ‘nakupenda’ halina uzito kama aliotegemea Jerry, huyo Lara apate na kusikia.

“Kwa kufikiria hivyo ni kwamba sijawahi kukwambia. Leo nimekutamkia nakupenda, si kwa sababu nimekurupuka Lara. Kwa sababu ni kweli nimeanza kusikia upendo wa kweli kwako. Na mwanzoni haikuwa hivyo. Nilikueleza makuzi yangu. Jinsi nilivyozaliwa na kukuzwa na mama tu wakati baba alikuwepo. Nilijiapia sitafanya hivyo maishani. Kuzaa watoto na kuwatelekeza kwa wanawake tu, hovyo hovyo. Kwako nilikuwa muwazi. Na sikutaka kutoa ahadi ya uongo halafu tukishindwana nije kukuacha wewe, ambaye utakuwa tayari na watoto wangu!” Jax akaendelea kujieleza.

“Ndio maana unaona sasa hivi nahangaika na wanangu mchana na usiku ili tu wasione pengo langu. Sitaki kuwaacha kama wasio na baba, lakini pia sitaki kukupoteza na wewe. Nipo kwenye wakati mgumu ndio maana unaona nakuwa mkali. Sio sababu eti nimepata mwanamke mwingine! Nitakuwa mwendawazimu, eti baada ya kuishi na wewe muda wote huo, nisikwambie nakupenda, sasa hivi nikiwa nimepata mwanamke mwingine eti ndio nikutamkie nakupenda!” Lara akaweka kila kitu chini na kwenda kuanza kumbusu.

Alimbusu Jerry mpaka akatulia. Akambusu tena na tena huku akimbembeleza, wakajilaza kitandani. “Nipo na wewe Jerry na wala sina ninapokwenda.” “Si ni kwa sasa tu! Ukiamua kuanzisha familia yako je?” “Ulisema tutazungumza hiyo siku. Siku haijaja, nipo hapa, kwa nini unakosa amani? Hata mimi nimejua umebadilika. Jinsi ulivyokuwa unanichukulia mwanzoni, ni tofauti na sasa. Nimeona upendo umeongezeka hata kuzungumza na mimi umebadilika. Hivyo ndio vitu nilikuwa nahitaji Jerry. Nilitaka mtu kama wewe ndio maana hata nikaanza kuona uzito wakufikiria nje. Ndio maana unaniona nipo na wewe kila wakati na ukiwa mbali nakutaka urudi ili tu niwe na wewe. Unanijali Jerry, unanijali sana. Naomba usibadilike na kunirudisha niliko toka.” “Wapi?” Bado Jerry akataka kujua.

“Wewe unataka kuharibu Jerry. Naomba mimi na wewe tuendelee pale tulipoanzia, tulipokutana Zanzibar. Ya nyuma hayakuhusu na mimi hayanihusu tena. Nina uhakika unayemtaka ni Lara huyu sie huyo unayejaribu kumchimbua. Naomba utulie, tafadhali.” “Ni nini hicho kikubwa unachokificha ambacho hutaki kukisema!?” Lara alikuwa amemkalia miguuni, akatoka na kuondoka. Jerry akasimama kwa haraka.

“Kwa nini unaondoka kwa dharau bila yakunijibu wakati mimi nilisimama na kujieleza kwako mpaka ukaelewa?” “Sio dharau Jerry, ila tokea mwanzoni nilikwambia sipo tayari kuzungumzia hilo.” “Kwa nini? Maana nia yangu mimi ninzuri tu, nikutaka kukufahamu zaidi.” “Mbona mimi kuna mambo mengine huniambii na siulizi?” Jerry akatulia. “Ni kwa kuwa najua kwenye maisha yako ninamipaka na hilo uliliweka wazi kuwa mimi sio mkeo. Unaposema nakufahamu sana, unadanganya Jerry. Na nakuona unatumia hiyo sababu tu ili kutaka kunitawala.” Hapo Lara akaweka msisitizo.

“Wewe chagua na kuamua. Unataka kuishi na Lara huyu au la.” “Unaninyanyasa Lara!” “Nakwambia ukweli kwa sababu kama unataka maisha yangu ya nyuma, nitakutaka na wewe mambo ambayo najua hutakuwa tayari kuyajibu. Halafu tujiulize ili iweje!” Jerry akatulia kidogo, Lara akaondoka hapo alipokuwa amesimama, na kurudi sebuleni. Baada ya muda Jerry akamfuata.

“Hakika sijawahi pata mtu ananipuuza kama wewe Lara! Kweli naongea na wewe, unaondoka?” “Sikupuuzi wala kukudharau Jerry. Ila naona unataka kuanzisha jambo ambalo halikuwepo kwetu na ulishalikataa.” “Kama kweli si dharau, endapo nikikujibu maswali yote utakayoniuliza leo, na wewe utajifungua kwangu?” Lara akabaki akimwangalia. “Nijibu Lara, usiniangalie kama kituko.” “Ili iweje? Unataka nini Jerry?!” “Mwanzo mpya.” “Upi?” Lara akaendelea kumuuliza akijua wazi hana uwezo na hataki kumuoa wala kumpa watoto.

“Wangu mimi na wewe.” “Jerry, usinifanye mimi mtoto mdogo. Hapatakaa pawe na mimi na wewe hata siku moja. Kwa kuwa ni kweli mimi si mkeo uli...” “Nilisema mwenyewe, nakumbuka.” “Sasa!?” Lara akamshangaa. “Mimi sio kama wewe. Mimi nataka kuja kuwa na familia yenye watoto. Na Mungu akinijalia nitakuwa nao zaidi ya wawili, lakini si zaidi ya watano.” “Lara!” Jerry akashangaa sana.

“Mimi sijui ulizaliwa na kukulia wapi Jerry! Lakini mimi ninamtizamo wa familia wa tofauti kabisa. Nimetoka kwenye familia ya kawaida sana, lakini tulilelewa vizuri tu. Mfano wa ndoa nilio nao ni kutoka kwa wazazi wangu. Mama yangu alizaa watoto watatu, sijamsikia akijuta kutuzaa, ila akijutia kutozaa zaidi. Hana majuto na mtoto hata mmoja aliyeleta hapa duniani, na baba hivyohivyo. Usemi wa baba ni kuwa, watoto ni urithi kutoka kwa Mungu na zawadi kutoka kwake Mungu mwenyewe. Tena anasema ametoa kwenye bibilia kitabu cha zaburi 127 na mstari wa 3. Tena mwenyewe akiendelea kuusema kwa kichwa mpaka mstari wa 5, utamuonea wivu! Anaongea kwa kujivuna mno, akijivunia binti zake na mjukuu wake. Hana majuto hata kidogo ila shukurani kwa Mungu. Wewe tumekutana miezi saba tu iliyopita, unafikiri nawezaje kufikiri kama wewe na si baba yangu? Eti sasa hivi niogope kuwa na watoto kwa sababu yakushindwa kuwalea!” “Sio kwamba naogopa.” Jerry akapoa.

“Mimi napenda watoto, na nitakuja kuwa nao tu. Hilo ujue Jerry. Sina kipingamizi cha kutokuwa na watoto. Sisubiri kuwa milionea ndio niwe na watoto.” “Sasa unasubiri nini?” Lara akamtizama na kunyamaza. “Nataka kujua nina muda gani na wewe Lara?” “Mbona unaonekana unawasiwasi na mimi ambaye nimetulia, wakati kwanza, ulishakuwa na mahusiano na mke wa mtu! Pili, wewe una mke wako Jerry!? Ni nini unataka kuanzisha sasa hivi?” “Si nimekwambia kama nakupenda!” “Kwa hiyo kama unanipenda ndio unataka nifanyeje Jerry!? Mbona mimi nimetambua mapenzi yako na nimekudhihirishia hata kwa vitendo ndio maana unaniona nimetulia! Unataka nifanyaje?” Lara akauliza taratibu tu. Jerry akaondoka. Wala Lara hakumfuata.

“Asinitanie kabisa! Anataka kuniweka nyumba ndogo nizeeke bila mume wangu mwenyewe wala watoto wakati yeye anafamilia yake! Aache utani na mimi!” Lara akawaza na kuwasha tv kabisa na kujiweka sawa hapo upande wa sebuleni, Jerry chumbani akidhani Lara atamfuata tena, asijue Lara alishatendwa, anamadonda ambayo hajayatibu ila kuyafunika tu. Haitaji nguvu kubwa kuyatonesha. “Nishabembeleza sana wanaume, malipo yao ni  ushenzi mtupu.” Lara akaendelea kubadilisha tv akiwa ameshatibuka moyoni.

Moyo Wa Mtu Msitu

“Kwa hiyo nilazima uwe na watoto wanne?” Lara akageuka nakushangaa Jerry amerudi na swali. “Maana kama nimekuelewa vizuri, ni kwamba unataka watoto wanne, au wasizidi watano.” “Kwa nini umeamua kuondoa amani kati yetu Jerry?” “Mimi nauliza tu kutaka kujua.” “Ili iweje?” Lara akamuuliza tena taratibu tu. “Nijipange.” Lara akakunja uso. “Unataka kujipangaje?” “Kwa nini unapenda wewe ujibiwe halafu hupendi kunijibu?” “Nisikilize Jerry. Mimi sio wewe ambaye ndio unakuwa mwenye kauli kwenye familia. Litakapofika swala la idadi ya watoto kwenye familia, nitatoa nafasi na mume wangu achangie. Ikitokea anataka watano sawa. Akitaka wawili, ndipo nitakapomuomba angalau wazidi wawe watatu. Hiyo itakuwa kati yangu na mume wangu. Sasa wewe unaulizia nini!?” “Kama mimi ndio nataka kukupa hao watoto je?” Lara akageuka vizuri.

“Kwamba unataka kunipa watoto kama unavyonipa pesa, nikatumie nitakavyo?” “Unataka nini Lara? Mbona unanichanganya?” “Wewe ndio umekusudia kujichanganya Jerry. Wala si mimi na nakuona umekusudia. Kipo kitu unataka kitokee, ambacho sidhani kama unauwezo nacho Jerry. Mimi nina misingi yangu ya maisha. Na tokea nimekutana na wewe umenipa ya kwako bila kutaka kunisikiliza. Nikaheshimu na kukubali kwa kuwa uliniahidi mapuziko na furaha. Nikiangalia hapa, sioni mapumziko wala furaha. Naona kudhalilishwa na ukiukwaji wa...” “Nimekudhalilisha mimi!?” “Umesahau kugomba ulikokufanya masaa machache pale baa na kuvuta watu?” Jerry kimya.

Lara akaongeza sauti kwenye tv. “Usinidharau Lara! Nataka tuzungumze.” “Nimekuona umenyamaza Jerry, nikajua umemaliza.” Lara akazima kabisa tv. “Kaa basi.” “Nikiamua kuzaa na wewe, utatulia?” Akauliza akiwa amesimama. “Chakwanza rekebisha usemi wako. Mimi nimetulia kabisa. Pili, mimi sihitaji watoto kama maembe. Tatu, sasa hivi sipo tayari kuwa na watoto, ndio maana hata yale makubaliano ya mimi naweza kutafuta mtu wangu kisha nikujulishe, unaona sijayafanya, kwa kuwa sipo tayari.” “Mpaka lini?” “Nitakujulisha.” “Come on Lara! Lazima utakuwa na hata wazo! Sitaki unishitukize.” Jerry akamshangaza sana Lara.

“Ulipokwenda kwa mkeo miezi miwili iliyopita, ulizungumza na mimi tukapanga au hata kuniambia mwezi kabla ya hiyo safari kama unampango wa kwenda kwa mkeo?” Lara akauliza taratibu tu. Kimya. “Uliniona hata nimelalamika?” Kimya. “Uliondoka na kuniacha karibia siku 15. Hiyo ni nusu mwezi. Ulinisikia nikilalamika au kukutaka urudi kama unapokuwa hapa nchini?” Kimya. “Hukudhani kuwa ile safari yako ya kuniambia unakwenda kwa mkeo ilikuwa ni kunishitukiza mimi mtu ninae ishi na wewe nyumba moja kama mkeo? Unakumbuka hata kuniambia unarudi lini?” “Kwa sababu nilikuwa nikienda kwa matatizo.” “Hayo unayasema leo!” “Sasa kwa nini hukuniuliza, kama ulitaka kujua?” Lara akakunja uso na kushangaa sana.

“Kutokuniambia wewe, binafsi nilielewa ni kwa kuwa hayanihusu. Uliweka wazi mwanzoni kabisa. Unanitumia kwa starehe na mimi nitanufaika. Si mkeo na wala sitakuwa mkeo. Leo naanzia wapi kukuuliza maswali kama mkeo wakati unakwenda kupata starehe hiyohiyo kwa mkeo?” “Lara!” “Wewe ni muwazi na umenifundisha kuwa muwazi. Nakwambia ukweli. Na ndio maana nakushangaa unapoanza kunichimbua kama vile kuna jambo la ziada unataka kutoka kwangu na ambalo tulikubaliana, mimi nimekiuka! Nisivyo na haki kwako kwa mambo fulanifulani, ndivyo hivyohivyo kwangu. Kile ninachoona kinaumuhimu kwako kujua, usiwe na wasiwasi, nitakujulisha bila hata maswali.” Jerry akakaa kwenye kochi akiwa amechoka kabisa.

“Lara wewe ni mkorofi.” Lara akamtizama na kunyamaza. “Sikujua kama upo hivyo!” Akaendelea kulalamika. “Mimi najitoa vyote hivyo kwako na bado hunithamini nakuona nastahili majibu ya maswali ninayokuuliza!?” Lara akacheka kwa kuuumia kidogo. “Kujitoa kwako kukubwa, unamaanisha kunipa pesa nyingi?” Lara akamuuliza akiwa amemgeukia kwenye kochi alilokwenda kukaa. “Eti Jerry? Umeshahesabu pesa ulizonipa, ukaona zinatosha kuninunua, sasa natakiwa niwe kama unavyotaka?” “Hakuna mwanaume atakayekutunza kama mimi Lara. Hata kama mtazaa watoto, lakini hatakuwa na uwezo kama wangu. Ulitakiwa uniheshimu sana. Huko nje naliliwa na wasichana wengi tu, tena wazuri sana. Lakini nimetulia kwako na bado unanidharau! Unafikiri huko nje ndio watakupa kila kitu! Mimi nahangaika kuzisaka pesa kwa udi na uvumba, wewe unatumia utakavyo na bado huthamini hilo!” Lara alibaki kimya akimtizama na kumsikiliza kwa mshangao.

Jerry akaendelea kuongea akilalamika jinsi anavyomtunza na bado Lara anashindwa kumthamini! Lara akajishangaa machozi yakimtoka huku akimtizama Jerry aliyekuwa akiendelea kuhesabu kwa kumsimanga. Ikawa kama Jerry amembadilikia gafla. Sivyo walivyoagana asubuhi wakati anatoka hapo hotelini. Asijue hata yeye hakuhitaji nguvu nyingi sana kutonesha madonda ya Jerry, na kuweka udhaifu wake bayana. Jerry akaongea mengi Lara kimya kabisa bila yakujibu ila kushangaa nakushindwa hata kujifuta machozi. Akajihisi kunyanyasika haswa. Akaongea mwishoe akanyamaza. Aliponyamaza tu, Lara akanyanyuka kuelekea chumbani bila yakujibu asijue ndio anamuumiza zaidi Jerry. Kuwa amempuuza hata alichokuwa akizungumza amekipuuza. Asijue na yeye alivyomuumiza Lara, kuona historia yake kwa wanaume inajirudia. Kutulia kwao, akijituma kwa upendo, lakini kumlipa vibaya.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Ndio kwa mara ya kwanza Jerry anamuona Lara asiye na shukurani, na Lara anamuona Jerry wa namna hiyo! Mpaka akashangaa moyo wa mwanadamu ulivyo msiti! Ni kama aliyeipindua shilingi kwa haraka na kirahisi sana. Kutoka kwenye mapenzi mpaka kwenye kumuhesabia! Kwa mara ya kwanza tokea atoroke jijini Dar, akamkumbuka Jax. Akamkumbuka si kwa kingine, ule wakati aliokuwa nao alipokuwa naye kabla Tula hajarudi pichani. Kweli hakuwa tajiri, lakini hakuna usiku waliolala wakiwa wamepeana maneno ya kuudhiana au yakuumizana kwa kiasi kile. Mpaka wao wenyewe walikuwa wakishangaa jinsi walivyokuwa wakiwaza vitu vinafanana. Hakuwahi kuhisi utofauti alipokuwa naye, ila uthamani aliokuwa ameweka Jax kwake. Hakuwahi hata kuhisi manyanyaso kutoka kwa Jax kwa chochote alichompa, ila kufurahia kuwa na uwezo wa kuweza kumpa mpenzi wake.

Jax hakuwahi kusaidia familia ya Lara kama Jerry. Kwa muda mfupi sana aliokuwa na Jerry, hata watu waliona utofauti nyumbani kwao. Lara aliwafungulia biashara wazazi wake, hata dada yake mkubwa akawa akifanya kazi kwenye duka la jumla la wazazi wao. Aliitumia pesa ya Jerry vilivyo, hakuwahi kufikiria kama atambadilikia kwani ni kama hakuonyesha kujali. Usiku huo ameongea mengi sana akimuhesabia Lara mpaka akashangaa. Alibadili tu nguo na kupanda kitandani kulala. Walikuwa wakiondoka kesho yake.

Kwa Nelly.

N

elly jeuri si huyu aliyerudi jijini baada ya mapumziko ya kisiwani. Alikuwa amepoa kama aliyeona kitu ambacho amekosa maelezo yake ya kutosha. Alibaki akimtafakari Billson bila kumtafuta. Mara kadhaa aliangalia namba yake akitamani kumpigia na kushindwa. Tofauti na alivyozoea, siku zikawa haziendi kabisa ili weekend ifike apate alichomwandalia maana alishamuaminia kwa mambo makubwa, mazito na mazuri. Ikawa mchana, ikawa usiku, siku ya kwanza, ya pili, ya tatu na nne, kimya. Alhamisi jioni akashindwa kutoka kwa haraka hapo kazini. Akajichelewesha hapo ofisini ili kumpa Billy muda kuona kama atamfuata, lakini mpaka inafika saa mbili usiku, hakupata hata ujumbe kutoka kwa Bill. “Kwanza sidhani hata kama anayo namba yangu!” Akajisuta na kuamua kuondoka tu hapo ofisini. Kwanza akajidharau. “Tangia lini mimi nimekuwa mtu wa kusubiria kiumbe kingine!?” Akawaza kwa kajilaumu Nelly, asijue na yeye ni mwanadamu kama wanadamu wengine, anahitaji mtu.

          Ulikuwa usiku mgumu akimuwaza Billy. Akahisi labda amempuuza. Pengine amekumbuka jinsi alivyotendwa na mkewe ndio ameamua kuachana naye moja kwa moja. Nelly akawaza mengi na kujilaumu ni kwa nini hata alikubali kwenda naye hiyo mara ya kwanza. Akahisi ni kama alijidhalilisha tu. Akalala kinyonge, akijihisi kukataliwa.

~~~~~~~~~~~~~~~~

          Akiwa ofisini kwake siku ya ijumaa jioni ametulia na kushindwa hata kufanya kazi mpaka akajishangaa mwenyewe. Alivua kabisa viatu vyake na kubaki amekaa tu nyuma ya Kompyuta yake, mezani kwake. Hata sekretari wake walikuwa wameshaondoka kazini. Jengo zima limetulia kabisa ni kama alibakia peke yake. Akahisi mlango ukigongwa taratibu, akageuka, Billson akaingia.

          Kuna hali ikamuingia Nelly akashindwa kujielewa. Akajikuta anainama na kugeukia pembeni. “Huwa watu wanakosea namba, Nelly! Hata kupiga kwa kunidanganya tu?” “Mimi sitakudanganya Billy.”  Billy akakaa kwenye kochi kubwa la mbele ya meza yake, akiwa amejisuta ila kuridhishwa na hilo jibu. Nelly akamwangalia, akamkuta ametulia akimtizama. “Umekua na siku nzuri?” “Kwa nini hata hukutuma ujumbe kama kweli unataka kujua?” “Sijui Billy.” Nelly akajibu, wakatulia. Ila jinsi alivyomjibu tangia anaingia hapo, Billy akahisi amekutana na Nelly wa tofauti.

           Akamuona amenyanyuka na kwenda kukaa pembeni yake pale kwenye kochi. Akatulia kimya vilevile bila viatu. Wakabaki wametulia tu. Tokea waachane siku ya jumapili walipotoka kisiwani, ndio wanakutana na kuzungumza. Walikaa kimya zaidi ya dakika 10. Hakuna aliyemuongelesha mwenzie kama wasiojua ni nini waongee au kohofia kuongea na kuharibu.

          Mwishoe Billy akamsukuma kwa bega lake. Nelly akamwangalia. “Kesho tunaondoka asubuhi ya saa nne. Namaanisha ndege ndio inaondoka mida hiyo.” Nelly akabaki akimwangalia. “Tutarudi jumapili. Unataka nikufuate wapi?” “Nitamwambia dereva aje anichukue nyumbani anilete uwanja wa ndege. Ni sawa?” Billy akafikiria kidogo, akaafiki. “Sawa. Uje na hati ya kusafiria.” “Sawa.” Hakuuliza hata wanapokwenda. Ila alifurahia sana kuwa pale na Billy.

          Billy akasimama. “Nikuache ukapumzike.” “Kama huna haraka, naomba tukae tena kidogo.” Billy akarudi kukaa pembeni yake. Wakatulia. Kimya kwa muda. “Umekula?” Nelly akauliza kwa kujali. “Bado. Wewe?” “Sijala. Nikikwambia nilikuwa nikikusubiria wewe hapa ofisini. Utaamini?” Billy akamwangalia vizuri. “Ulijuaje kama nitakuja?” “Sijui Billy. Lakini nilijua ungekuja tu.” “Kwa nini unashindwa kuchukua hatua ingine, Nelly?” Nelly akacheka kwa kusita. “Na mimi nilikuwa nikisubiria simu yako tokea jumapili tulipoachana. Nikatarajia angalau ujumbe wakujua kama ulifika nyumbani salama na kutaka angalau kujua kama nilifika salama!” Nelly akabaki kimya kwa muda.

          “Twende tukale.” “Leo Jax hayupo nyumbani?” “Atakuwa sawa tu. Hata hivyo niliamka alfajiri sana. Usingizi ukaisha, nikaamua kupika. Anacho chakula cha jioni. Twende.” Nelly akaenda kuvaa viatu vyake na kuchukua mkoba wake. Wakatoka. “Hivi unajua bado sijaweza kuendesha kwenye huu mji?” Nelly akamcheka lakini alimuelewa. “Usijali. Mimi nitakuendesha. Wewe mruhusu dereva wako tu.” Wakashuka mpaka sehemu ya kuegesha magari, Billy akazungumza na dereva wake nakuhamishia mikoba yake kwenye gari la Nelly, wakaondoka.

          Walikwenda kwenye hoteli nzuri na kukaa ndani sehemu ya mwisho kabisa. wakaagiza vinywaji na chakula na kubaki wakiangaliana. “Nikuulize kitu Nelly?” “Nakusikiliza.” “Unafikiri utakuja kunipigia simu hata siku moja?” Nelly akatoa simu yake, akashangaa anabonyeza namba kwa kichwa, akampigia. Billy akaitizama simu yake na kumtizama Nelly. Ikaita mpaka ikakata. Nelly akamuandikia ujumbe. ‘You go at red but stop at green. What am I?’ Billy akasoma na kucheka, akafikiria kidogo na kujibu ujumbe. ‘Watermelon.’ Akamrudishia huo ujumbe, Nelly akacheka na kurudisha simu yake kwenye pochi baada ya Billy kupatia kitendawili chake. Alichomuuliza, ‘Unasimama kwenye kijani na kupita kwenye nyekundu. Mimi ni nani?’ Ndipo Billy akajibu kuwa ni, ‘Tikitimaji’. Akimaanisha huliwa sehemu yenye nyekundu na kuachwa sehemu ya kijani.

          Pakawa na utulivu jioni hiyo wa namna yake. Hapakuwa na maongezi mengi ila kila mmoja akaonyesha kufurahia uwepo wa mwenzie. Wakala mpaka akamaliza. “Tukawahi kupumzika kwa ajili ya safari ya kesho. Ila ujue huko tuendapo utahitaji hiyo miguu.” Nelly akacheka. “Na nini kingine?” “Vingine vyote utakutana navyo hukohuko. Lala vizuri, pumzika, ukijua utapata wakati mzuri.” Billy akataka kulipia, Nelly akakataa. “Mimi ndio nimekualika kwa chakula cha usiku, Billy. Acha mimi ndio nilipie.” Billy akacheka na kutingisha kichwa. “Kwani wewe unajisikiaje ninapolipia mimi?” “Wewe ndiye unayeshindwa kuwapokea ofa, Billy. Umekula, umeshiba, that’s my treat.” “Sawa Nelly.” Akalipia ndipo wakatoka.

          Billy akaangalia muda. “Kuliko kuanza kusindikizana na ratiba inayotusubiria mbeleni, acha mimi nikodi gari, inipeleke nikapumzike na wewe uende kwako.” Bila kubisha, Nelly akaliheshimu hilo. Akamsindikiza mpaka garini, alipoondoka ndipo na yeye akakodi taksii na kumrudisha kwake.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Safari hii Nelly anapelekwa wapi? Itakuaje kwa Lara na Jerry? Usikose muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment