Mara Ya Pili.
W |
akiwa kwenye
ndege Nelly akamuona anachukua mkono wake na kuusogezea kwake. Akajiweka sawa
kutaka kujua anachotaka kufanya. Akauweka vizuri katikatika ya mkono wake
mkubwa kisha akaunyanyua na mkono wake na kufanya kama anavyopenda kufanya
wakati wote. Akawa ameegemeza kichwa chake kwenye hiyo mikono, ikabidi Nelly
amgeukie vizuri ili asiumie ubavu. Ni viti vya ‘first class’. Vikubwa na
nafasi yakutosha. Akajiegemeza kwenye kiti, Billy amejiegemeza kwenye mikono
yao akimtizama.
“Sijui itakuaje, lakini maadamu atajua
ananipenda mimi, na mimi ni wake, nina uhakika atasimama na mimi. Sijakata
tamaa Nelly. Hata kidogo, sijakata tamaa.” Nelly akamwangalia. “Mama yangu huwa
anakuwa na wasiwasi eti kwamba nitakuja kuishia peke yangu. Hata jana
nilizungumza naye na kumwambia, labda Mungu anichukue mapema, lakini sijakatia
tamaa mapenzi. Inaweza isiwe kwa haraka kama ambavyo ingetarajiwa, lakini
naamini ipo siku, Nelly. Ipo. Na mimi nitapendwa kwa dhati.” “Ni muda gani
tokea muachane?” Nelly akauliza.
“Niseme tokea aniache. Maana mimi
nikiingia agano, huwa sijui kuvunja aisee. Ilibidi kutafuta mwanasheria,
anisomee talaka yangu na ajue anachokitaka. Nikamwambia kama akiona kipo sawa,
anipe tu niweke saini, basi. Na kweli alinisaidia sana. Yeye ndiye aliyekuwa
akikutana naye pamoja na mwanasheria wake. Akampa anachokitaka, nikaweka saini.
Wakafanya utaratibu wa kunitolea vitu vyangu pale ndani ya nyumba. Nikawaomba
wakaviache kwa wazazi wangu. Nikawaachia nyumba yangu, wakaendelea na maisha yao.”
“Pole Billy.” “Kujibu swali lako nafikiri ni miaka 10 sasa tokea hayo yote
yatokee. Kama imezidi ni kidogo au pengine nakaribia 11.” Nelly akatulia
kidogo.
Akaona aulize tena. “Kwa miaka yote
hiyo, hujawahi kuwa na mahusiano tena?” “Nimekua nayo, lakini si ya uhakika. Ya
kawaida tu.” “Unamaanisha nini?” Akamuona ni kama anayefikiria kisha ni kama
akapata jinsi ya kueleza. “Niliingia kwenye yale mahusiano nikijua ni nini
anataka kwangu. Na mimi sikujali kwa kuwa sikuwa nimepona. Nilihitaji tu mtu
wakuwa naye, nisijikute peke yangu. Basi, ikaendelea hivyo mpaka nilipoona nipo
sawa, nikasitisha.” “Yeye alitaka nini?” “Billson, Director wa World bank.”
Billy akajibu bila wasiwasi. Nelly akamwangalia na kugeukia pembeni.
“Wewe ulishakuwa na mahusiano?” Nelly
akageuka. “Kuna mambo nilipitia hapo nyuma, yalinichefua mno. Nimeshindwa
kabisa kuwa na mahusiano ya kimapenzi. Kwanza si kitu nafikiria.” “Hudhani kama
unaweza kuja kupendwa?” “Sijui Billy. Nahisi ni kama sipo tayari kupita hiyo
njia! Wengi ninao waona wapo kwenye mahusiano, hawajanipa sababu ya kutamani
walichokuwa nacho. Najiona ni afadhali mimi hivi nilivyo na niliyonayo kuliko
kuongeza kitu kingine au mwanadamu mwingine kwenye maisha yangu.” Nelly
akafikiria kidogo.
“Nimekuja kumwangalia mwanadamu, aisee
ni kiumbe cha hatari kuliko simba.” “Kwa sababu sisi tuna akili na utashi,
Nelly. Sisi tumepewa uwezo mkubwa mno. Ni miungu wadogo. Sasa unafikiri kwa
sifa hizo unafikiri sisi si hatari?” “Ndio hicho kinachoniogopesha kwa
mwanadamu.” “Umeshawahi kufikiria, ukija kupatia?” “Sijui Billy. Sijaona
waliopatia. Na kama kweli wapo basi pengine wapo wachache sana.” “Mimi
nimezungukwa na mifano mizuri sana ya waliopatia, Nelly. Sana. Wazazi wangu na
ndugu zangu wanandoa nzuri sana. Mno. Mpaka nimekuja kuamini si sura au rangi
ya mwili, ila mtu tu. Mdogo wangu huyo anayenifuata, ameolewa na mwanamme
anayempenda sana. Wanawatoto wao na wametulia kwenye ndoa yao. Kaka yangu
hivyohivyo. Sasa nawezaje kusema hakuna mapenzi ya kweli?” Hapo Nelly akanyamaza.
Akaubusu mkono wake, Nelly
akamwangalia. “Sio wanadamu wote ni wabaya Nelly. Ila wengi wabaya wanatuachia
madonda ambayo shetani anayatumia vibaya. Zaidi kutuogopesha. Mimi naamini
ninao upendo mkubwa tu na uwezo wa kuushiriki na mwanamke mwingine mbali ya
Anele. Sikuumbiwa upendo mdogo kiasi cha kuishia kwake tu. Naamini Mungu wa second
chance. Nafasi ya pili. Na kama nilikosea kwa Anele, nakusudia kutengeneza
pale Mungu atakaponijalia nafasi ya pili. Nimejibu swali lako?” “Yeah. Na
nashukuru umekuwa muwazi sana na ukafafanua kwa undani.” Billy akacheka na
kutulia kwa muda.
“Tunakwenda ice skating.” Nelly
alicheka sana. “Billy!” “Nimepatia?” “Sana! Nilishakuwa na hamu nayo! Asante.”
Nelly akaendelea kucheka, mpaka Billy akafurahia. “Umejuaje kama...” Nelly
akafikiria akakumbuka alimwambia kwamba alichukua mafunzo yake baada ya
kumaliza shahada yake ya 3. “Kumbe huwa unanisikiliza na unatilia maanani!”
“Sana. Kwa kuwa huwa sina muda wa kupoteza. Kufikiria, na kuhakikisha nakumbuka
hata vitu vidogodogo visivyo na maana kwa wengine ndio asili ya mafanikio yangu.”
“Nimefurahi sana.” “Nimekuona.” “Ila sijui kama nitakumbuka! Ni muda mrefu
sana.” “Mimi ni mjuzi. Binti yangu huyo mkubwa ndio mchezo anaoupenda. Ni ice
dancer. Aisee Mungu alimjalia. Isingekuwa juhudi za shule, angafika mbali sana.
Alikuwa akishiriki kwenye mashindano yake, anamedali nyingi sana.” “Hongera
Billy.” “She is so beutiful. Ni mzuri sana. Wa kila kitu.” Nelly
akacheka.
“Ungependa nikuonyeshe?” “Tafadhali.”
Nelly akajibu akicheka. “Halafu anaakili sana. Ile ya darasani!” “Eeh!” “Anayo.
Mungu alimjalia. Na lazima kila siku anisikie na kuniona. Ananipenda sana na
anampenda sana Mungu. Mwadilifu tokea mtoto mpaka nilikuwa namwambia mama,
wakati Mungu anamuweka kwenye mikono yangu kwa mara ya kwanza amezaliwa,
alikuwa akinikabidhi tumaini jipya hapa duniani.” Akatoa simu na kutafuta picha
zake. “Hii ni ya jana akiwa kazini kwake.” Nelly akamwangalia na kushangazwa.
“Billy! Huyu ni binti yako?” “Oooh yeah. That’s my baby girl.”
Akamwangalia Billy. “Ni mzuri kama mwanamitindo!” “Nilikwambia.” Billy akaongea
kwa kujivuna.
“Sasa anafanya nini?” “Ni business
Analytical. Na nimzuri kwenye fani yake. Mzuri kwenye namba ndio maana hiyo
fani ameiwezea.” “Hongera sana Billy!” “Unaponiona napanda taksii jioni au
natumia dereva kunirudisha kupumzika baada ya kazi, basi ujue ndio muda natumia
na hao watu wawili kwenye simu. Yeye na mama. Nikiwa nimechoka, nawapigia wote
kwa wakati mmoja ili waniulize maswali yao yanayofanana, kama nipo sawa,
nimekula, kazi ilikuaje, mbona nimechoka!” Nelly akaanza kucheka. “Wote
wanakuuliza hivyohivyo?” “Hivyohivyo na kila siku.” Nelly akacheka na
kukumbuka.
Akaona aulize tu. “Sasa kama siku ile
tulikuwa wote mpaka panakaribia kupambazuka kule Unguja, si watakuwa
walikokukosa kwa simu?” “Walijua nipo na wewe.” Nelly alishituka mpaka
akapaliwa na mate. Alikohoa na kukohoa. Billy akamuita muhudumu awape maji ya
kunywa. Akampa. “Pole.” Nelly akayanywa yote na kuanza kujifuta machozi sababu
ya kukohoa. “Aisee pole. Upo sawa?” Nelly akatingisha kichwa kukubali huku
akijifuta uso.
Wakatulia. Na Billy naye akanyamaza
kama kumpa nafasi ya kutulia. Nelly akamrudishia simu yake. “Hutaki tena?” Billy
akamuuliza akimcheka. “Subiri kwanza Billy. Wewe unawaambia upo na mimi kama
mfanyakazi mwenzio?” Billy akazidi kucheka. “Acha kucheka bwana!” “Kwani wewe
unafanya kazi World Bank?” “Billy?” “Kumbe ndio paliwa yote hiyo! Acha wasiwasi
wewe.” “Sasa unawaambia upo kikazi?” “Hivyo ndivyo umemuaga Jax nini?!” Billy
akamuuliza kwa kumshangaa kidogo.
“Eti Nelly? Maana mimi sina sababu ya
kudanganya. Sina chakujificha. Tena baada ya kuwaaga hivyo na kuwaambia
tunaenda ice skating Afrika ya kusini, ona jumbe zao hizi.” Nelly akachukua
tena simu yake na kuanza kusoma ujumbe wa mama yake. ‘Treat her right.’ Mama yake
huyo. Binti yake akamwandikia, ‘Tafadhali furahia baba.
Hakikisha unafungua moyo na kufurahia kila moment na Nelly. Mungu yupo
na wewe, hajakuacha na anakuwazia mema. Nakupenda zaidi ya dunia yenyewe.
Nipigie ukitulia, uniambie iliendaje. Nakuombea.’ Mpaka Nelly akapata
vipele kama vya baridi. Akamtizama Billy.
“Hizo jumbe ni za asubuhi hii wakati
nakuja uwanja wa ndege.” “Naomba kumuona na mama yako.” “Umemuagaje Jax?” “Billy!”
“Nataka kujua.” “Mimi na yeye hatuna mahusiano kama hayo yako na mama yako au
binti yako. Sihitaji kujieleza chochote kwake. Niliamka asubuhi na mapema
kumpikia, kuhakikisha leo anacho chakula pale nyumbani. Maana yupo kwangu.
Nikampikia na kumwambia kimtoshe mpaka kesho nitakaporudi. Basi.” “Unajali,
Nelly!” “Kwa sasa hana mtu mwingine ila mimi. Ameudhi watu.” “Kwa kuahirisha
ndoa?” Nelly akashangaa sana.
“Inamaana wewe unatujua kwa kiasi
kikubwa hivyo!?” “Ukweli nawafahamu. Ehe?” Nelly akamwangalia na kuendelea.
“Kwa hiyo yupo. Na nimemuona amekusudia kunionyesha kwa vitendo kwamba
amebadilika na anajutia. Amejirudi mpaka namuhurumia tena. Hajawahi kunijali
kama anavyonijali sasa hivi. Amebadilika.
Kwa hiyo kujibu swali lako, sisi hatuna utaratibu kama huo wa kuzungumza
kila kitu.” Akaridhika na kumuonyesha mama yake.
“Anaonekana bado ananguvu! Halafu
mmefanana, nafikiri na binti yako amepata uzuri kutoka kwake. Na naongea hivyo
kwa kuwa simfahamu Anele.” Hapo Billy hakujibu. “Umebahatika Billy! Mimi sikuwa
na aina hii ya mahusiano na mama yangu.” “Katika hilo hata mimi najua. Mama
ananipenda na kunijali sana. Sisi watoto wake ndio kila kitu chake. Na yupo
hivyo kwa wote. Namshukuru Mungu.” “Nionyeshe mtoto wako mdogo.” Ni kama Billy
akasita, kisha akachukua simu.
“Sijui kama nina picha zake za hivi
karibuni. Maana nyingi anakuwa na Carlos na Anele. Kila nikizipata huwa
sizitunzi kwa muda mrefu. Zinakuwa zikiniumiza tu.” “Kwani Carlos hakuwa na mke
wala watoto?” “Hapana. Ila sasa hivi mwanangu ndio kama mtoto wake. Ila
anampenda kwa ukweli. Ni wivu tu kuona anammiliki binti yangu. Ila anampenda
sana. Na kwa kuwa na yeye anapenda kupendwa, na kule amejikuta ndio mtoto wa
pekee, anapenda sana hayo maisha.” “Huyu mkubwa huwa haendi?” “Hataki hata
kuwahisi.” “Sasa huwa anakutana vipi na mdogo wake?” “Nyumbani kwa wazazi
wangu. Wanawapenda sana bibi na babu yao. Na baba ndiye alinishauri nimuache tu
kwa Carlos. Wote wanamfahamu Carlos. Hakuwa mtu mbaya. Kwa hiyo acha nitafute
picha yake kama ninayo.” Akatafuta mpaka akapata moja akiwa na wazazi wake.
“Hii familia yenu inachanganya.
Mnafanana!” Billy akacheka. “Nafikiri mama ndiye ametupa damu yake ndio maana
tunafanana.” “Hata wazazi wenu wenyewe wanafanana.” “Tulikuwa tukimtania baba
kuwa alioa ndugu yake. Nafikiri ni hiyo rangi ya weupe na kuishi muda mrefu
pamoja.” Ilikuwa familia nzuri sana. Walionekana wamefanikiwa. Na kweli
kulionekana kuna amani. “Hiyo ni chrismass ya mwaka jana. Wote tulikutana
nyumbani kwa wazazi.” Mpaka wanatua uwanja wa ndege wa Johannesburg, Africa
Kusini, Nelly alikuwa akiwafahamu ndugu wa Billy wote, kasoro Anele na Carlos.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Tutaelekea hotelini kupumzika na
kupata chakula cha mchana. Nimepanga skating ni saa 10 ya jioni. Kisha twende
tukaangalie sinema baada ya hapo. Ni ratiba nzuri?” “Sana. Nimefurahia
skating.” Billy akacheka. Dereva aliyekuwa na jina kamili la Billson
waliyemkuta hapo uwanja wa ndege akiwasubiria, akawapeleka hotelini. Kama
kawaida ya Billy alichukua vyumba viwili.
“Ni sawa tukienda kwenye masaji wote
wawili au ungependa ufanyiwe chumbani kwako?” “Hamna shida. Twende wote tu.”
“Basi baada ya kama dakika 15, nitakugongea chumbani kwako.” “Sawa.” Vyumba
vyao havikuwa mbalimbali. Vilipakana kabisa. “Billy?” Billson akageuka kabla
hajamfungulia mlango wake. “Nilikuomba kukusaidia kulipia.” “Usijali,
nilishalipia kila kitu.” Akafungua mlango akamkaribisha na yeye akaingia.
“Naona pazuri, patakufaa kwa usiku huu.” “Nashukuru. Asante.” “Karibu. Acha
basi na mimi nikaweke vitu vyangu kisha tutoke.”
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Muda wote wa skating Nelly alikuwa
akicheka sana, tena kwa sauti ya juu mpaka Billy alijua akifurahi. Na akaja
kugundua Billy alikuwa mjuzi sana. Aliweza kucheza nyimbo mbalimbali juu ya
hiyo barafu na viatu hivyo vya ncha nyembamba chini kama soli, bila shida.
“Nifundishe Billy.” “Ni kutafuta tu balance na ondoa woga. Hivyo hivyo
unavyoskate, sasa ongeza hatua za kucheza, na jua mimi nipo kukudaka,
hutaanguka.” Wakaendelea. Na dj aliyekuwepo hapo alikuwa akiweka nyimbo
mbalimbali huku watu wakiendelea kuskate. Wakapata wakati mzuri sana. Wakatoka
hapo kuwahi sinema.
“Maisha hayatabiriki. Na wakati
mwingine ni rahisi kuchezea nafasi.” Wakawa wakizungumza baada ya hiyo sinema,
wakiwa wameshashushwa hotelini. Walikaa sehemu ya nje tu wakiendelea kuzungumza
upande wa mgahawa kwenye hiyohiyo hoteli kubwa ya kitalii. “Hilo nililiona kwa
baba yangu. Unajua baada ya manyanyaso yote hayo kwa mama, akamuua kwa gonjwa
la Ukimwi!” “Pole sana Nelly.” Ila akagundua ni kama hakushangaa. Akawa kama
aliyekuwa akifahamu.
“Sasa tulipoachwa naye sasa, akawa
hajui chakufanya na sisi. Mimi asiyenitaka, na huyo mtoto wa kiume aliyekuwa
akimpigia kelele. Akimtaka kwa hali na mali. Hakuna wakumtumikisha tena. Pesa
anayo lakini mama hayupo. Haikuchukua muda akaamua kujinyonga. Na wala yeye
hakuugua sana. Na ninauhakika kwa pesa aliyokuwa nayo, angetumia dawa na
kuendelea kula vizuri, angekuwa sawa tu. Lakini ninauhakika alifika mwisho.”
“Ikawaje baada ya hapo?” Billy akauliza.
“Ilikuwa mbaya sana Billy. Imeharibu
maisha yangu yote.” “Hapana Nelly. Usikubali huo uongo wa ibilisi. Hakuna
mwenye uwezo wa kukuharibia maisha ila wewe mwenyewe na Mungu. Na mara ya
mwisho nasoma bibilia yangu, Yesu mwenyewe alisema kwenye kitabu cha Yohana
10:10. ‘Nalikuja ili wawe na uzima, tena wawe nao
tele.’ Sijui kama unanisikiliza?” Nelly akanyamaza. “Tena hapo ni baada
ya kueleza anachokifanya shetani. Kwamba yeye ni mwizi. Anakuja ili kuua,
kuangamiza na kuharibu. Ila Yesu yeye ni mtengenezaji. Sikatai kwamba kuna
mapito tunapitia na yanaathiri maisha yetu! Najua kwa kuwa na mimi nilipitishwa
hapo. Lakini nilikataa Carlos na Anele wawe ndio wa mwisho kuandika historia ya
maisha yangu. Naitafuta furaha kwa hali na mali nikiamini na mimi siku moja
nitakuja kupumzika. Usikubali Nelly. Mapenzi ni mazuri mno. Nilijaribu nikaona
na kujua ni bora kuliko uchungu na kubaki mpweke.” Nelly akavuta pumzi kwa
nguvu, akatulia.
“Niambie ilikuwaje?” “Kama unakumbuka
nilikwambia ni kama baba alikataa kunisomesha. Kwa hiyo mama akamuomba kaka
yake mmoja ambaye anao uwezo wa kipesa awe anamsadia kunitunza na kunisomesha. Na
mimi Mungu alinisaidia uwezo wa darasani, hata mama akajua. Ndio akamsihi sana
mjomba na mkewe waniendeleze. Mjomba akakubali. Akawa akisaidia ada. Sasa
kipindi hicho kuna shule fulani hivi zipo mkoani Tanga, wilani Lushoto. Ni
shule za masista. Sasa hivi inachukua wasichana kwa ngazi ya sekondari. Lakini
wakati ule walikuwa wakichukua mpaka shule ya msingi. Sasa mimi na mtoto wa
mjomba, ni kama tunalingana, ila yeye alinizidi miaka miwili, ila tulikuwa
darasa moja kwa kuwa mimi nilivushwa darasa. Tulipokwenda kufanya mitihani ili
kuingia kwenye ile shule, kwa kulipiwa na mjomba, mimi nikachaguliwa, mtoto
wake akaachwa. Kile kitu kilimuuma sana shangazi, yaani mke wa mjomba.” Nelly
akaendelea.
“Kukawa kama na kubadilishwa mawazo.
Hawataki tena kunisomesha. Muhula wa kwanza mama akahangaika sana, akafanikiwa
kunipeleka kwenye hiyo shule kwa wakati ili nisikose nafasi kwa sababu ni shule
ambayo ilikuwa ikililiwa sana na watu. Niliweka juhudi Billy, usingenikuta sina
kitabu mkononi endapo napata nafasi. Nilikuwa nikikazana nikijua baba
ananidharau, na mama yangu anahangaika. Basi, nikawa mtu wakupata 100 tu. Ndipo
nikapata ufadhili sasa kutokana na hayo matokeo. Masista wakawa wakinilipia
kila kitu, kazi yangu kusoma tu. Likizo nyingine nilikuwa nikibaki tu pale shule.”
“Kwa nini?!” Billy akauliza kwa kushangaa.
“Mazingira ya nyumbani yalikuwa mabaya
Billy! Mabaya sana. Zaidi baba alipokuwa akiwepo. Badala ya kufurahia
mapumziko, ilikuwa ikininyong’onyeza sana. Halafu pia kama nilivyokwambia,
hatukuwa na mahusiano mazuri na mama yangu. Wakati mwingine nafikiri kwa
kunihurumia pale baba alipokuwepo, alikuwa akinipeleka kwa mjomba kumalizia
likozo yangu huko. Sasa hapo kumbuka mahusiano yangu na shangazi yalishaharibika.
Binti yake ambaye nilikuwa naye umri mmoja alishanichukia akisema nilichukua
nafasi yake. Kwa hiyo likizo hazikuwa nyakati nzuri kwangu. Ilikuwa bora kukaa
tu shuleni, labda niwe nimeishiwa sana. Ndipo ilikuwa ikinilazimu kwenda likizo
kwa mjomba ili kunisaidia ninaporudi shuleni.”
“Anyways, ile shule ya msingi ikaisha,
nikaingia tena sekondari palepale na nikawa nalipiwa tena ada, ila michango
mingine ikawa ni mama. Nikaendelea vilevile mpaka nilipokaribia kumaliza kidato
cha nne ndipo mama akafariki akiwa amemuacha Jax na msichana wa kazi tu pamoja
na baba. Mambo hayakuwa mazuri, nilipomaliza kidato cha nne, nilifaulu, mjomba
akanitafutia uhamisho ili niwe pale Dar. Kwa kuwa nilifaulu vizuri, haikuwa
shida. Nikaanza hapo. Sasa katikati ya kidato cha 5, ndipo baba akajinyonga.
Ukumbuke nilikuwa sijafikisha miaka 18. Nisingeweza kurithi chochote na wala
nisingeweza kuaminiwa kumtunza Jax.”
“Halafu hapo ukumbuke nilianza darasa
la kwanza nikiwa na miaka 5. Nilimaliza darasa la 7 nikiwa na miaka 11. Kidato
cha nne nilimaliza hata mika 15 sijafikisha. Baba anajinyonga ndio nilikuwa
nakaribia 17. Kukawa kama kuna dalili za kuchukuliwa na mmoja wa kaka zake baba
ambaye na yeye akili yake ilikuwa kama baba tu.” “Ikoje?” Billy akauliza.
“Kuwa mtoto wa kike si wakusomesha. Na
hapo akawa alishasema nimesoma vyakutosha, nitafutiwe mume niolewe. Halafu Jax
atunzwe na mkewe, wanachukua nyumba yetu. Na yeye alikuwa mmoja wa watu
waliochangia kumnyanyasa sana mama yangu. Nikafikiria kwa haraka, ikabidi
kumfuata mjomba. Yuleyule aliyekuwa akinisaidia maswala ya shule, nikamuomba
anitetee kwamba nipo umri sawa na binti yake.” “Yasinta?” Hapo ndipo alipojua
ni wapi anapata habari zake.
“Ulimfahamia wapi Yasinta!?” Billy akacheka.
“Nimalizie kwanza hiyo habari.” Nelly akakunja uso na kuendelea. “Mjomba
akakubali ila akaniambia nilazima nianze kuonekana na kuishi kama niliyekua,
sio mambo ya kitoto. Nikakubali kwa haraka bila kuelewa anachomaanisha. Siku
moja akaja nyumbani akaniambia lazima tuzungumze. Bado tulikuwa na msichana wa
kazi ambaye alikuwa akinisaidia sana maswala ya Jax.” Nelly akacheka kwa kusikitika.
“Tukahamia kuzungumza kwenye chumba
kilichokuwa cha wazazi na mimi nilikuwa naogopa sana kuingia humo kwa kuwa
ndipo alipojinyongea baba. Basi, mjomba akaanza kunipa mikakati aliyofikiria
tufanye ili kufanikiwa. Maana wakati huo ni kama yeye aliachwa awe anatusimamia
mpaka mahakama itakapoamua.” “Kwani baba hakuacha mirathi kwa yeyote?” “Hapana
Billy. Yule mtu alikuwa mbinafsi wa kupitiliza. Hawezi kumfikiria mtu ila yeye
tu. Akaacha fujo tupu kila mtu anataka kujimilikisha anachokitaka. Ila kwa kuwa
mjomba angalau alikuwa karibu na sisi tokea mwanzo, wakasema aendelee kutusaidia
mpaka mahakama itakapo amua.”
“Basi, akasema nilazima kutengeneza hati ya kuzaliwa mpya yenye jina
jingine sio Nelinda. Na iwe na tarehe ya tofauti lakini inayoendana na kidato
nilichopo.” Billy akakunja uso. “Usiniulize Billy, maana hata sijui. Ila
akaniambia nikifanya hivyo, nitaonekana nina miaka 18 tayari na wakili
atanitetea kuwa nimefikisha umri wa kumlea mdogo wangu, na kupewa mali zote za
baba bila shida ila chini ya usimamizi wake. Nikakubali kwa haraka sana. Ila
sasa akasema lazima kuwa na akili za kiutuuzima, niachane na utoto. Akarudia
tena, ila safari hii mkono kwenye matiti yangu. Mimi nikakwepa. Akaniambia kama
nihivyo, inamaana sina akili za kiutuuzima, siwezi nikaaminiwa. Napoteza kila
kitu.” Nelly akacheka.
“Nilivua nguo mimi mwenyewe Billy.” “Nelly!” “Wala sikubakwa. Kwa
hiari yangu, nikamruhusu. Ila akaniambia kwa wakati ule hapakuwa na mazingira
mazuri, lazima kutafuta nafasi. Alimfukuza kazi yule msichana wa kazi aliyekuwa
akitusaidia sana, akimwambia atakuja kumtafuta tena baadaye, mambo yakitulia.
Kwamba lazima tuonyeshe mimi ni mkubwa naweza kumtunza mdogo wangu. Akamuanzisha
Jax shule. Akamuweka shule anayokwenda asubuhi na kurudi jioni. Mchana najikuta
nipo nyumbani nikiwa nimetoka shule, basi nikageuka kuwa mke wake mdogo.”
“Nelly!” “Ooh yeah. Nilijua njia zote za kujikinga na ujauzito. Nilijua jinsi
ya kumtumikia bila shida wala kushurutishwa. Mwenyewe, nikimbembeleza
anisaidie.”
“Nikageuka kuwa kama baba yangu. Mbaya zaidi, niliyafanya hayo nikijua
fika mjomba anaye mke wake nyumbani ila nikabaki nikimtumikia kama mke wake
wakati nilikuwa ni mdogo kuliko binti yake. Tena bila huruma wala aibu.
Akatutafutia mwanasheria. Tukafanikiwa kumuua Nelinda bila shida. Nikandikishwa
Nelly. Na akanionya nisiwahi kujiita hivyo tena. Sikufanikiwa kumaliza kidato
cha sita.” “Kwa nini tena?!” Billy akauliza kwa kuumia.
“Daah! Acha Billy. Aliniambia lazima kufuta historia yote ya nyuma.
Niliposhinda ile kesi, nikapata mali zote, nikamwambia sitaweza kuendelea
kuishi kwenye ile nyumba aliyojinyonga baba, ukweli nilikuwa nikiogopa sana.
Basi, akanisaidia kununua nyumba ninayoishi sasa hivi na Jax. Zilikuwa nyumba
za msajili wa majumba, na yeye alikuwa mkurugenzi huko. Ukweli alikuwa na uwezo
mkubwa sana kifedha. Basi, ndipo akanisaidia kutafuta nyumba nzuri tukapata kwa
bei nzuri. Kwa jina langu. Pesa iliyobakia ndipo nikaanza chuo sasa nikitumia
matokeo yangu ya kidato cha 4.”
“Ikabakia jinsi ya kumkwepa. Maana alikuwa akinisumbua Billy, huwezi
kumkwepa. Alikuwa akinitumia zaidi ya mkewe. Nikajiambia sitaweza kuwa naye na
kumtunza Jax. Na mbaya zaidi kile kitendo kikawa kimeniathiri sana. Sikuwa
mwenye furaha kabisa. Yale mahusiano yalinifanya kuwa na uchungu wa kupitiliza.
Nilijawa na hasira ya kupitiliza. Kila nilipokuwa nikilala naye, nashindwa hata
kupata usingizi. Nikawa mtu niliyejawa hasira sababu ya kutolala na hukumu.”
“Nikajilinganisha na wanawake wote waliokuwa na mahusino na baba
yangu wakijua mama yupo. Nilikuwa siwezi hata kujitizama kwenye kioo. Siku moja
alikuja pale nyumbani akitaka alale, nikashindwa. Alisema ameaga nyumbani kwake
kuwa amesafiri, nisiwe na wasiwasi. Nikaenda kuchukua kisu jikoni. Nikamfuata
chumbani. Nikamueleza jinsi anavyoniumiza nafsi yangu na akili. Nikamueleza
vile ninavyojitizama baada ya kumalizana na yeye, nikamwambia furaha yangu ni
kumuua yeye kwa kuwa sina chakupoteza tena. Nikamwambia siku atakaporudi tena pale,
awe ameamua kuniua mimi au awe amekubali kifo. Aliondoka, hakurudi tena. Ila
aliniacha nimeathirika vibaya sana. Ndio nikabakiwa na Jax mpaka hivi
tunavyozungumza.” “Aisee pole sana Nelly.”
“Ndio maana jina la Nelinda situmii. Lilikufa kwa garama kubwa sana. Hapa
ninamiliki miaka karibu miwili ambayo sijawahi ishi hapa duniani. Na jina
ambalo mama yangu hakunipa ila mjomba.” “Yasinta ndiye aliyenipa habari zenu
kwa ufupi tu. Ilibidi kumtafuta ili kuweza kukufahamu. Maana nilijua
nisingeweza kumuuliza Jax. Kwanza si sawa kwa wadhifa nilio nao pale kazini.
Katika kupeleleza hata kwenye faili la Jax, liliandikwa alichokuwa amezungumza
siku ile ya tafrija. Ukawa upo wewe tu kwenye maisha yake. Nikasema
haiwezekani. Ndipo nikaambiwa na mmoja wa wafanyakazi wenzake Jax aliyekuwa
kwenye kamati ya harusi ya Jax, kuwa alisikia rafiki wa karibu sana wa Jax
akimuuliza kama atawashirikisha ndugu zenu wengine. Jax akasema huo utakuwa ni
uwamuzi wako wewe. Katika kupeleleza zaidi ndipo nikamjua huyo mjomba wenu na
binti yake ambaye na yeye anafanya kazi benki. Haikunigarimu sana kumtoa ukweli
Yasinta.” Nelly akashangaa sana.
“Kwani ulimlipa!?” “Tuache hilo. Ila nikakufahamu kupitia yeye.”
“Yule yupo kama mama yake! Wanapenda sana pesa. Alishakuja kuniomba pesa
akinikumbusha jinsi nilivyosaidiwa nyumbani kwao.” “Kweli?!” “Wewe usicheze na
Yasinta. Kwanza mlevi. Halafu anapenda pesa kama benki. Nilimpa na kumuonya asiwahi
kurudi pale kunitafuta mimi na wala asiwahi kumfuata Jax. Nilimwambia
nikimsikia amemsogelea Jax, nitampasua kichwa.” Billy alicheka sana. “Kumbe
alisema kweli, hakudanganya!” “Mpuuzi sana. Ila mbona unazo habari zangu mpaka
za sasahivi!?” “Hizo nyingine ni za watu wa karibu yako na sitakutajia maana
mbali na kuwalipa, niliwaahidi sitawataja kwako. Naomba tuliheshimu hilo.”
Nelly akamtizama na kunyamaza.
“Sasa umeridhika kunifahamu kwa asilimia ngapi?” Nelly akauliza na
kumfanya Billy kufikiria. “Mmmh! Labda 90.” “Sasa hizo 10 zimebakia wapi? Maana
nimekwambia mpaka hofu yangu!” “Hapana. Hapo umepachanganya sana. Nimebakia
kubuni tu. Mpaka nahisi umekuwa makini kutonijibu hilo.” Nelly akanyamaza
akifikiria, kisha akamwangalia.
“Nikwambie ukweli ambao utakusaidia hata usipoteze muda wako?”
“Sitaki.” Billy akajibu kwa haraka. “Sasa unakataa nini wakati hata sijasema?”
“Kwa kuwa nimeshajua unachotaka kuniambia.” Nelly akakunja uso. “Si unataka
kuniambia wewe si kama wanawake wengine. Moyo wako uliumizwa sana. Haupo tayari
kwa hili au lile! Maneno yanayofanana na hayo. Sivyo?” Billy akamuuliza. “Na
usinidanganye Nelly.” “Ni kama hivyo ila..” “Hapana.” Billy akasimama kabisa.
“Sasa unakwenda wapi?” “Kupumzika. Twende ukapumzike. Naona kwa leo inatosha.
Tumekuwa na wakati mzuri naomba tukapumzike.” Nelly akasimama. Wakaanza kurudi
chumbani.
“Nakushukuru kwa wakati mzuri. Nimefurahia sana.” “Hata mimi
nimefurahia. Zaidi kuona wewe umefurahi.” Nelly akamtizama na kuendelea
kutembea. “Nikuulize swali Nelly?” “Mmmhhh.” Billy akamtizama. “Ulishawahi
kupenda?” “Ukweli hapana Billy. Sikuruhusu fikra zangu zifikirie hayo maisha
kabisa. Kwanza nilijiambia sistahili. Nimekua mwizi. Kuna wakati mpaka nilikuwa
nikitamani pengine ningebakwa ili kujisamehe, lakini sikuwahi kubakwa Billy!”
“Ni kama ulibakwa Nelly, ila hapakuwa na kutumia nguvu. Ulikuwa ukifanyia
kinyume na matakwa yako. Wewe hukuwa mwizi. Ulifanya kile uwezavyo kwa wakati
ule ili wewe na Jax muwe hapo mlipo. Tafadhali tafuta jinsi ya kujisamehe.
Itakusaidia sana.” Nelly akanyamaza. Wakaongozana mpaka juu kabisa vilipo
vyumba vyao. Vilikuwa vikitizamana.
“Kesho tunaondoka saa ngapi?” “Mchana. Lakini nilitaka tupate chakula
cha pamoja kabla yakuondoka.” “Basi unijulishe angalau nusu saa kabla.”
Wakasimama hapo nje ya milango yao wakizungumza tu. Mwishoe wakakaa kabisa chini
kama walivyofanya walipokuwa kisiwani. Lakini siku hiyo Billy alipanga angalau
apate busu la shavuni. Ila historia ya Nelly aliyotoka kumsimulia muda mfupi
uliopita, ikamrudisha nyuma kabisa. Akaona awe muungwana zaidi, asiwe kama
mjomba wake. Wakatulia hapo mlangoni, watu wakipita na kuwashangaa.
“Mara ya tatu inabidi kukwambia ninapopanga twende.” Nelly akacheka
na kumwangalia. “Kwa kuwa kunahitajika maandalizi.” Nelly akakunja uso.
“Unanipeleka sayari ya ngapi?” “Hutafika kwenye sayari ila mlima Kilimanjaro.”
Nelly akatoa macho. Billy akacheka. “Usiogope. Mimi hii itakuwa safari yangu ya
tatu. Ya kwanza tulipanda na baba, pamoja na kaka yangu. Carlos pia alikuwepo.
Zamani sana. Nafikiri tulipomaliza tu chuo mimi na Carlos, tukaja na mzee. Mara
ya pili, nilikuja na watu wa kazini. Na mara ya tatu ndio nataka twende wote.
Utafurahia.” “Mimi sidhani bwana. Sasa kwa nini kupanda milimani, Billy!?” Billy
akazidi kucheka.
“Usiogope, ni kitu kizuri sana. Nakuandalia mtu atakayekuandaa, mpaka
siku yenyewe tunakwenda, itakuwia rahisi.” “Labda hivyo. Mwenzio hata mazoezi
huwa sifanyi.” “Sasa kwa nini unamwili mzuri hivyo?!” “Mimi naona tulinyimwa tu
miili mikubwa. Si unamuona hata Jax? Anakula sana, lakini hutamkuta na mwili
mkubwa hata mara moja. Na yeye pia si mtu wa mazoezi. Basi na wazazi wetu
walikuwa hivyohivyo. Sikumbuki kumuona mama amenenepa hata alipokuwa mjamzito
wa Jax, alikuwa kama mimi tu.” Wakaendelea kuzungumza.
Lakini Nelly akakubaliana bila ubishi na hilo la kupanda mlima
Kilimanjaro, kitu kilichomfurahisha Billy kuona angalau wanakubaliana kwenye
mambo fulani fulani japo habari alizosikia juu ya Nelly ni mkorofi, mkali kama
simba. Na akamuonyesha hivyo tokea wanakutana. Akijua fika wadhifa wake, lakini
akadiriki kumkatalia maombi yake bila kufikiria mara mbili.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment