Kwa Lara.
L |
ara na Jerry waliondoka
jijini Mwanza, Lara akiwa hajui kitakacho endelea wakifika jijini Dar. Hakuwa
na pakwenda ila tu kwa Jerry. Kama kawaida ya Jerry alikuwa busy na simu yake
mpaka wanaingia ndani ya ndege, Lara kimya akiwaza huku mapigo ya moyo yakienda
mbio asijue kama ndio mwisho wa hizo starehe au la. Kwenye ndege nako kukawa
kimya, Jerry akisoma magazeti mpaka wanafika Dar. Alichojiamulia Lara moyoni,
safari hii hataondoka tena mpaka afukuzwe. Na akijirudi, ajinufaishe kwa
haraka, kwa kuchukua pesa nyingi ndipo aondoke. Akapoa.
Walifika wanakoishi wawili hao, Jerry akamwambia anakwenda nyumbani
kwake Masaki, atarudi baadaye. “Sawa.” Lara akakubali bila swali. “Au unataka
nikwambie nakwenda kufanya nini?” “Huna sababu yakufanya hivyo, lakini ukiona
ni sawa, nipo kukusikiliza.” Jerry akamtizama na kutingisha kichwa kama
anayesikitika, akaondoka hata hakukaa. Alichofanya Lara ni kuingia chumbani
kwao kwa haraka na kuanza kukusanya nguo zake za maana tupu, alizojua ni za
gharama sana. Viatu na dhahabu zake zote. Akaweka kwenye masanduku, akafunga
vizuri, akachukua moja ya gari ya Jerry aliyomwambia ni yake, lakini akajua
atakuja kumbadilikia siku moja kama alivyoanza kumuhesabia walipokuwa Mwanza.
Akakimbilia kituo cha mabasi makubwa yaendayo mikoani.
Bado ilikuwa mapema tu maana walirudi na ndege ya asubuhi. Mpaka
wanafika nyumbani ilikuwa saa 7 mchana. Lara alitaka kuwahi basi la mwisho
linalokwenda Dodoma. Alishampigia simu baba yake kuwa atatuma masanduku mawili
na boksi ambalo anaomba visifunguliwe mpaka afike mwenyewe nyumbani. Lara
aliendesha kwa haraka. Akafanikiwa, akasafirisha vile vitu vyote alivyojua ni
vya maana sana kwake ambavyo hataki kupoteza hata kama ikitokea kama
alivyoachwa na Jax, basi hatapoteza vitu vyake vya thamani. Alishang’atwa na
nyoka, jani likitikisika tu, anajua ni nyoka.
Shilingi Yapinduka Tena.
Akapitia sokoni kununua vyakula na matunda, ndipo akarudi anakoishi
na Jerry. Nje alikuta gari ya Jerry. Akajua amerudi. Akatoa mizigo aliyorudi
nayo kutoka sokoni na mkoba wake pembeni. Akapitiliza jikoni, hakuwa amemkuta
Jerry sebuleni. Wakati yupo jikoni anashusha vitu, akashitukia Jerry yupo nyuma
yake. Akampiga kibao cha mgongoni, Lara alishituka akaachia mfuko na kuinama
kwa mshangao.
“Umeanza umalaya! Natoka tu kidogo na wewe unatoroka, halafu unarudi
na upuuzi huu, kama kisingizio! Mlinzi ameniambia umetoka mara tu na mimi
nilipotoka.” Lara alikuwa kwenye mshituko, asitegemee kama mikono ileile
iliyokuwa iking’ang’ania kiuno chake na hips zake, ndio imeishia kumpiga! Jerry
akamsogelea akiwa amejawa hasira, Lara akapiga magoti na kuficha uso. Hapakuwa
na pakukimbilia kwani ni kama alimbana kwenye kona. Lara alishindwa hata kulia kwani
alikuwa kwenye mshituko mkali sana.
“Unatumia mali zangu kujinufaisha! Nikikuuliza unaleta jeuri! Hapa ni
kwangu, unatakiwa kuwa na heshima.” Hakumpiga tena ila Lara akashitukia
ananyanyuliwa na kwenda kutupwa nje. “Kama umeshindwa kuishi kwa unyenyekevu,
unaleta kiburi kujidai wewe ni mjuaji, nenda kaonje maisha ya wenzio
wanavyoishi huko nje.” Hapo anamfukuza bila hata pochi yake. Akarudi ndani na
kufunga mlango.
Lara akarudi kugonga, akamfungulia. “Naomba nijihifadhi mpaka kesho.
Tafadhali Jerry. Sasa hivi ni jioni tayari. Sina pakwenda.” “Kumbe unajua
kuomba! Nilijua wewe nikiburi, hujui kujishusha.” “Samahani kama nilikuudhi.”
“Sasa hivi ndio unajirudi baada yakugundua huna maisha bila mimi! Nimehangaika
sana kufika hapa nilipo! Eti wewe unakuja tu, nakutaka kunitawala! Unajua
nilifikaje hapa?” Jerry akazidi kugomba. Na hawakuwa na eneo kubwa. Inamaana
hata mlinzi alikuwa akisikiliza anavyotukanwa.
Hapo Jerry alikuwa akimtukana huku Lara na yeye akijitukana vile
alivyoweza kuacha kazi na kukimbia na Jerry kwa ahadi ya maisha mazuri. Akawa
anawaza pakwenda jioni hiyo akifukuzwa bila pochi yake wala simu. Wapi
pakwenda! Akaanzie wapi! Lara akabaki ametulia hapo akiwaza huku Jerry
akiendelea kugomba. Hata hivyo alishamchukia Jerry kutoka moyoni, alisimama
hapo akiomba Mungu amguse amfungulie tu, aingie ndani.
“Mali zote hizi ni zangu. Ulitakiwa kunyenyekea sio kuleta kiburi.”
“Samahani Jerry. Samahani sana kwa kuudhi. Mimi ninaondoka, lakini nilitaka
kukuomba msamaha kabla sijaondoka. Natambua upendo wako na vile ulivyojitoa
kwangu. Nasikitika tunaachana, lakini sitaki tuachane ukiwa kwenye hali hiyo.
Umenipa maisha mazuri sana Jerry. Ni kweli hakuna mtu anaweza kunitunza kama
wewe. Naomba tuagane tu vizuri. Tafadhali Jerry.” Jerry akapoa.
Ilikuwa kama amepandwa na wazimu wa gafla, akapoa. “Kwa hiyo upo
sawa?” Lara akamuuliza taratibu tu akijikomba. Kimya. “Kwani ulinisubiria sana?
Nilikwenda kutuma mzigo nyumbani labda ndio maana umeniona nimechelewa.
Samahani.” Lara alikuwa akibembelezea malazi ya siku hiyo na vifaa vyake vilivyobaki
hapo ndani. Jerry akampisha mlangoni. Lara akaingia. “Naomba nioge kwanza,
nimechafuka, halafu nije nipike.” Lara akaongea kwa tahadhari. Jerry hakujibu
lakini alikuwa amepoa kabisa.
Akakimbilia jikoni, akachukua pochi yake na kwenda nayo chumbani.
Akaoga harakaharaka akatoka wakati anataka kwenda jikoni, Jerry
akamuwahi. “Subiri kwanza Lara. Sasa hivi lazima uishi hapa kwa masharti yangu.
Huwezi kunipelekesha. Sasa je, upo tayari kujibu kila swali langu?” “Hapana.”
Bila kufikiria Lara akajibu na kumshangaza sana Jerry! “Naahidi kukujibu ukweli
kwa yanayotuhusu Jerry, sitaki kuwa muongo kwako. Mengine siwezi kuzungumza na
wewe.” “Kwa hiyo unataka kuzungumza na nani!?” Akauliza kwa ukali mpaka uso
ukabadilika.
“Tafadhali usinipige tena Jerry. Nimekuwa muwazi kwako, usinipige.
Tuzungumze, ikishindikana basi, nipo tayari kuondoka. Uniache kama
ulivyonikuta. Kwa amani kabisa.” “Una nini wewe Lara!? Ni nini unaficha kikubwa
hicho chakukubali kupoteza kila kitu?” “Siwezi kupoteza kitu ambacho sikuwahi
kuwa nacho Jerry!” Lara alijibu bila woga na kumshangaza sana Jerry.
“Hiki ulichonifanyia muda mfupi tu uliopita, ni kwa hivi unavyonifahamu.
Ningekwambia undani wangu kidogo tu, ungezidi kunidharau na kunidhalilisha.
Wewe ni mbinafsi Jerry. Umeruhusu maisha yako ya nyuma na watu walivyokutenda
vibaya, wageuze moyo wako. Unaweka mali mbele kuliko utu.” Lara akajishangaa
anaongea bila hofu.
“Unawezaje kusema hivyo na vile nilivyokuthamini!?” “Hii ya leo, hiki
unachofanya na maneno yaliyokutoka, yamekufungua moyo wako na kukuanika undani
wako. Vile ulivyo kwa halisi. Hujui kupenda Jerry, unajua kutawala. Unapoona
unapoteza nguvu yako kwa mtu, ndipo udhaifu wako unapojidhihirisha. Huwezi
kuishi na mtu mtulivu kwa kuwa hujui amani inakuaje. Hufahamu kupendwa, halafu
pia unaogopa kupendwa na kuthaminiwa. Ukiona kuna dalili ya kupendwa tu, wewe
kama Jerry, wala si vitu vinavyokuzunguka, au mali zako, ukigundua ni mapenzi
halisi, unatafuta sababu ya kukimbia ili kuepuka yaliyokupata utotoni pale mama
yako alipokuacha. Unaogopa yasijirudie.” “Usimwingize mama yangu Lara!
Tafadhali sana.” “Sawa Jerry. Mimi ni mbaya. Acha nikuache na maisha yako.” “Utanikumbuka
Lara!” Lara akamtizama na kutabasamu.
“Unanidharau!?” “Hapana. Wewe ndio utanikumbuka Jerry. Na
utakaponikumbuka, nasikitika hata pesa na mali zako ulizokuwa ukijisifia nazo
tokea jana, hazitakupa ninachokupa.” Lara akaongea kwa kijiamini mpaka akamshangaza
zaidi Jerry.
“Naomba nikuombe kitu kimoja cha mwisho Jerry.” Jerry akabaki
akimtizama. “Nakwenda kukusanya vitu vyangu niondoke, naomba usinipige kama
ulivyonifanyia pale jikoni. Nimekubali kuondoka, usinipige tena. Na kama uwepo
wangu hapa unakupandisha hasira, unaweza kunisaidia kukusanya vitu vyangu na
kuniwekea pale kwa mlinzi nikaja kufuata hata kesho. Usinipige tafadhali. Kosa
nililofanya ni kukupenda sana na kuwa mwaminifu kwako, sidhani kama ninahitaji
adhabu kwa hilo.” Lara akarudi chumbani kuanza kufungasha kwa haraka akiwa na
furaha yakuruhusiwa kuchukua vitu vyake japo lengo halikutimia na aliogopa
kuendelea kuishi hapo asije akatoka maiti. Akakazana kukusanya.
“Mke wangu anaumwa sana.” Lara akageuka. Jerry alikuwa amesimama
mlangoni. Akashindwa hata asijue ajibu nini. “Alikuwa na kansa, imerudi tena.
Jana nilipotoka pale hotelini, watoto walinipigia simu kunijulisha. Na kumbe
safari hii amechelewa kuigundua. Amekuja kurudi hospitalini ikiwa imesambaa
vibaya sana.” Jerry akaendelea. “Alikuwa ndio kila...” Jerry akasita. “Pole
sana Jerry. Pole. Lakini anaweza kupona.” “Hapana. Safari hii ni mbaya. Maisha
yangu yanabadilika Lara. Nampoteza mke wangu na wewe kwa pamoja! Ndio maana
nachanganyikiwa.” “Pole sana, Jerry. Pole.” Hilo ndilo Lara aliweza kusema,
hakutaka kujiingiza hata kidogo kwenye matatizo ya kifamilia ya mtumzima huyo.
Akabaki amesimama akimtizama.
“Maisha yangu yananibadilikia! Wakati nalala juzi, sikujua kama
nitapitia hii hali. Nimempoteza mama yangu, sasa hivi wewe, kisha mke wangu!
Napaniki.” “Pole sana Jerry.” Lara hakutaka hata kumpa wazo la kumuomba abaki.
Akaendelea kukusanya vitu vyake vyote, Jerry akimwangalia. “Natamani kama
ningeweza kukupa kila kitu Lara.” Lara akasimama tena. “Hata mimi Jerry.
Natamani kama ningeweza kukupa kila kitu nikakuridhisha. Au hata kuweza
kukutuliza nikawa kimbilio kipindi kama
hiki. Lakini inaonekana mimi sio msaada Jerry. Nakuongezea matatizo.”
“Sio kweli Lara.” “Ni kweli. Au basi niseme nakuwa ndio mtu wakunimalizia
hasira. Sio sawa kwangu. Nimepita hapo kwenye magumu Jerry! Hapo ulipo wewe,
mimi nimepita nikiwa peke yangu, lakini nilipita kimya kimya, sikuwa na
wakumuumiza ila nikabeba mpaka ukanikuta Zanzibar.”
Lara akajieleza. “Mimi sijui ugomvi Jerry. Hiki ulichonifanyia leo ni
kipya, hakijawahi kunitokea tokea nazaliwa. Na si kwa bahati mbaya. Hata
shuleni sikuwahi kuchapwa. Hata walimu walipokuwa wakitaka kuadhibu watu wote,
mimi nilitolewa pembeni. Sijisifii, ila ni kwa vile nilivyo. Sijui ugomvi, wala
kelele za kumkera mtu. Najua ni wakati gani wakuzungumza na wakati gani
wakunyamaza. Ndio asili yangu. Wakorofi huwa wananikimbilia. Wewe umeweza
kupata sababu ya kunipiga na kunitupa nje! Hakika mimi sio msaada kwako sasa
hivi. Acha nikupe nafasi tulivu ili uweze kufikiria na kusaidia familia yako.”
Lara akaendelea kukusanya.
“Kwa hiyo unashindwa kunisamehe japo nimekuomba msamaha!?” Jerry
akaanza. “Yote niliyokutendea, unashindwa kunisamehe wakati nimejieleza mpaka
nimekupa ya undani! Bado huoni sababu yakuwa na mimi japo kwa kipindi hiki tu!”
Lara akanyamaza akajua anatafuta kumpiga tena. Akataka kujutia misaada
aliyochukua ya Jerry, lakini akakumbuka furaha aliyoweka kwa wazazi wake.
Moyoni akapata faraja, akatulia na kuamua hata iweje hapo hatabakia tena, lazima
aondoke.
“Unaondoka lini?” Lara akajaribu kuuliza ili kumtoa kwenye mawazo kwa
kile alichokuwa anataka kukifanya. Kujipandisha hasira. “Naweka mambo sawa,
ndipo niondoke.” “Unataka nikusaidie nini kwenye kujiandaa?” Hapo akamfanya
atulie kabisa. “Sasa hivi nimechanganyikiwa, hata sijui.” “Sanduku la safari
ndio hilihili ulilokwenda nalo mara ya mwisho?” Lara akaendelea kuuliza.
“Nitatumia hilohilo, unataka kunisaidia kuandaa?” “Kama ni sawa.” Lara akamtoa
kwenye ile hali wakaanza kuandaa safari angalau Jerry akawa amepoa lakini Lara
akawa hataki hata kumuona tena.
“Kesho unataka nikusaidie nini kurahisisha maandalizi yako.” “Natakiwa kwenda benki kufuatilia na kupanga mambo yangu ya biashara angalau kuweka sawa kabla sijaondoka.” Wakazungumza hapo Lara akamtuliza, wakaweka mipango nini anahitaji Lara amsaidie. Huo usiku ukaisha kwa shida, kwa uzito mno.
Asubuhi
ya Machozi Mengine ya Aibu Kwa Lara.
A |
subuhi Jerry
alimka kisirani, hata Lara alimuona. Akabaki kujiwinda. Kwani alimuona akisoma
jumbe bado wakiwa kitandani. Akamuona akijibu, akaona aondoke. “Acha nikaandae
kifungua kinywa.” Lara akajiwahi kutoka kitandani. “Umekuaje Lara!? Unaniachaje
hivihivi! Jana sikupata kitu sababu uliwahi kulala. Wakati narudi kuzungumza na
simu nikakukuta umeshalala! Sikulalamika wala kukuamsha, nikaamua kukuacha.
Asubuhi hii nayo unakimbilia jikoni, unaniacha peke yangu! Unamaanisha nini?
Kuwa umeshanichoka?” Lara akabaki ameduaa, maana usiku ni kweli alitoka nje
kabisa kwenda kuzungumza na simu. Na yakawa mazungumzo ya muda mrefu, akaamua
kwenda kulala. Hata hivyo hakujisikia kwa penzi baada ya kumtenda unyama.
“Unaona ni kama nakubebesha majukumu yasiyokuhusu? Yaani unakuwa ni
mtu wa starehe tu, mwenzio nikiwa na shida unashindwa hata kuwa na mimi?!”
“Nimekuona upo kwenye simu Jerry. Halafu mimi na wewe mapenzi siku zote
hayajawahi kuwa wajibu. Tunakuwa tunaanza tukiwa kwenye hali nzuri. Ukiwa
umetulia na mimi nimetulia.” “Kwa hiyo sasa hivi kosa ni langu?” Lara
akanyamaza. “Huna tofauti na wengine Lara! Upo na mimi sababu ya pesa tu,
lakini si mimi kama mimi. Nimekwambia pale ninapopitia. Unashindwa vipi hata
kuniulizia maendeleo ya mgonjwa! Unalalaje hata hujui ripoti ya huko? Jana
ulijua kabisa kwamba nazungumza na watoto pamoja na mama yao ambaye ni mgonjwa,
umelala kabisa na kuniacha usiku nakesha kwa mawazo! Unafurahia kitanda ambacho
nimenunua kwa jasho langu halafu mimi mwenyewe mlipa garama hunitaki!” Lara akabadilika
sura akawa mwekundu asijue ni hofu au hasira.
“Wewe ni jeuri. Na ninajua chakufanya na huo ujeuri wako.” Alipotaka
kutoka tu kitandani Lara akakwapua simu yake na kukimbilia choo cha hapohapo chumbani
nakujifungia kwa hofu akijua anataka kumpiga tena. “Fungua Lara.” Lara akaanza
kutetemeka huku akiwaza jinsi ya kujitetea. Wanapoishi ni patulivu, hajui
jirani hata mmoja ambaye angempigia kwa haraka kuja kumsaidia maana Jerry
alikuwa akigonga kwa hasira na kunguruma kama simba.
Mjini hapo hana tena shoga. Alihama jiji bila taarifa, alirudi bila
taarifa. Akili ikaendelea kufikiria kwa haraka jinsi ya kujiokoa wakati Jerry
akiendelea kutoa vitisho nje ya mlango, akimtaka afungue. Hakujua wazo lilipotoka,
kwa haraka akajikuta akimpigia simu Tino. Japokuwa alikuwa na namba mpya,
lakini namba za watu wake wote wazamani hakufuta kwenye simu yake.
Baada ya Raha, karaha.
S |
imu ikaita.
Tino hakupokea. Akatuma ujumbe. ‘Mimi Lara. Naomba
msaada wako.’ Akautuma. Akaona simu inaingia. Tino. Akaanza moja kwa
moja kumuelekeza anakoishi na Jerry. “Mbona kuna
kelele? Upo sawa wewe!?” “Umeelewa, nilivyokuelekeza?” Lara akauliza
swali kwa sauti ya juu akisikika anaanza kulia. “Nimeelewa,
mbona unanitisha? Unataka nini sasa?” “Njoo sasa hivi unitoe Tino. Usimwambie
mtu, iwe siri yako. Tafadhali. Haraka, Jerry ataniua.” “Fungua mlango
Lara. Nitauvunja huu mlango!” Jerry akasikika akiunguruma kama simba.
Lara akakata simu huku akilia na Tino akionekana ameshapaniki kwenye
simu. “Kwa nini unataka kunimalizia mimi hasira
zako, Jerry? Nimefanya nini?” “Nimekwambia fungua mlango.” Lara
akaendelea kulia. “Nitavunja huu mlango na nitakuumiza vibaya Lara! Fungua.”
Lara akawa analia kwa uchungu. Akiwaza ni nini kibaya amewatendea hawa wanaume
kiasi chakumuadhibu vibaya hivyo kila anapokuwa nao! Lara akaendelea kulia kwa
kuadhibiwa na Jerry kwa kupokea starehe alizoahidiwa tokea mwanzo!
Akakumbuka na ndio sababu ya kukubali hayo mahusiano na mwanaume mwenye
majukumu ya familia yake, tena
aliyemuonyesha tokea mwanzo kuwa familia yake kwanza, yeye yupo pale
kumridhisha tu. Amemnunua kwa kumtumikia kimapenzi. Bila yakujua au kwa
kushindwa kufikiria sababu ya hofi, Lara amesahau uthamani wake ni pale Jerry
anapokuwa na furaha. Ili awepo kwenye maisha ya Jerry, ni Jerry aendelee kuwa
na furaha na sivinginevyo.
Hapakuwa na kudanganyana kati yao ila kutofikiria tokea mwanzo,
madhara ya makubaliano yao, kwa pande zote. Sasa wote wamekutana na
uhalisia. Pengo la Jerry maishaini haliwezi kuzibwa na mwanadamu yeyote yule,
ni mpaka kumpa Mungu nafasi amsaidie tokea chini kabisa, kukarabati pale wanadamu
waliharibu moyoni mwake. Na ndipo angepata utoshelevu wa kweli na wala si
kuhangaika kwa kutafuta wanawake kwa kuwahadaa kwa mapesa mengi akidhani
watakuwa kile anachodhania.
Na kwa Lara hivyohivyo, kutoka kuumizwa na mwanadamu mmoja, haraka
sana kabla hajapona, kuelewa na kujua jinsi gani ataishi tena na ile hali ya
usaliti, akakimbilia kwa mwanadamu mwingine akidhani atatulia au itakuwa
tofauti.
‘Kufanya kilekile, au vilevile wote wawili wakitegemea matokeao ya
tofauti.’ Ndio asubuhi hiyo wameishia hapo. Lara analia upande wa pili
akimlaumu Jerry kwa usaliti wa ahadi zake mwenyewe, na Jerry naye anakaribia
kuvunja mlango akiahidi kumuumiza vibaya sana huyo Lara aliyekuwa akimfaidi kwa
muda wote huo. Akimridhisha atakavyo bila kikomo wala kulalamika akidhani Lara
ndio angetakiwa awe na uwezo wa kuwa kile alichotaraji au anachokosa nafsini
mwake. Anataka kumuadhibu kwa kushindwa kwake.
Tino siye mtu aliyetaka hata ajue kama anamatatizo. Alitamani
aje akutane naye akiwa mambo safi, lakini akajikuta hamna tena namna. Hana
kimbilio jingine ila Tino ambaye ni mwepesi kutenda. Muda na wakati wowote
unapomuhitaji Tino, huwa hana sababu nyingi sana za kukataa ila kutenda. Akaishia
kwake akijua wazi akijua Tino, ni kama watu wote watajua tena. Ila hakuwa na
jinsi. Hakuwa na ndugu hapo jijini pengine wangemfichia hiyo siri ya kukutwa
anadhalilishwa na Jerry. Tino akabakia ndio mtu pekee wa kumpa msaada kwa
haraka, kwa wakati ule.
Akaendelea kumsikia Jerry akigonga mlango kwa nguvu. Akamtisha kwa
maneno mengi lakini hakufungua akiendelea kuomba Mungu Tino aliyemuacha Mwanza,
awepo Dar ili afike hapo kwa haraka, kama amepaelewa. Mara akasikia kama Jerry
anatumia kitu kizito kugonga mlango, Lara akazidi kulia kwa sauti akijua Jerry
atafanikiwa tu. Aliendelea kama kwa dakika 20 akimsikia anazidi kupandwa na
hasira, alisukuma mlango kwa nguvu ukafunguka na kumgonga vibaya sana Lara
mkononi. Alilia Lara. Akalia kwa hofu kubwa sana kwani Jerry aliyeingia hapo
hakuwahi kumuona kabla.
Alimvuta mpaka nje, Lara akiwa na nguo za kulalia tu akamtupia
kitandani kama paka. Mlinzi akawa anagonga kwa nguvu sana. Jerry akatoka kwa
hasira. “Salama huko? Imebidi kupiga simu kituoni kuomba msaada. Nimesikia
kelele.” “Wewe ulitakiwa kulinda watu wabaya wasiingie ndani. Sio kuwa mbea wa
mambo ya ndani. Umeona mtu ameingia ndani mpaka kuomba msaada kituoni?” Jerry
alikuwa akilindwa na kampuni kubwa ya ulinzi ambayo makao yake makuu yalikuwa hapo
karibu tu, Kinondoni. Si mbali na hapo.
“Ni katika kutaka kusaidia tu.” Yule mlinzi akajitetea. Wakati
wanazungumza gari ya kampuni hiyo ya ulinzi na walinzi wengine wanne waliovaa
sare za ulinzi wakaingia na risasi. Kwa kuwa geti liliachwa wazi na mlinzi
akitarajia wenzie waje kumsaidia. Wakasogea pale mlangoni alipokuwa amesimama
mwenzao na Jerry, mwenye nyumba. Lara alikuwa akilia sana, amefungiwa chumbani
akilia, aliposikia sauti ya wale walinzi nje akaongeza kilio na kuomba msaada. ‘Naomba mniokoe’. Akaongeza kuwa Jerry anataka
kumuua. Wakashituka sana.
“Haya ni mambo ya unyumba, hayawahusu. Nyinyi mnalinda nje sio
ndani.” “Naelewa mkuu. Lakini hatuwezi kuondoka tukiwa tunasikia mtu akilia
kwamba maisha yake yapo hatarini! Chochote kitakachotokea kwake na sisi kuwepo
hapa tukasikia na tusitoe msaada, sisi na wewe wote tutakuwa na hatia.” Hapo
wakapandisha hasira za Jerry. Akaanza ubishi na ukali.
Baada ya muda polisi na Tino wakaingia wakiuliza kama pale yupo mtu
anaitwa Lara. “Hii ni nyumba yangu. Hayupo mtu anayeitwa Lara humu.” Jerry akawakatalia.
Tino akampigia simu Lara wakiwa wamesimama palepale kwani Tino aliwahakikishia
kuwa lazima Lara atakuwepo humo ndani, kwani aliwaona wakiwa pamoja jiji Mwanza.
Simu iliita na kweli Lara akaisikia ikiita chooni akakimbilia kwenda kuikota. “Jerry ataniua Tino. Kama upo mjini tafadhali niokoe.”
“Uko wapi? Mimi nimefika hapa na polisi kwenye ile
nyumba uliyonielekeza. Nimemkuta Je...” “Basi
nipo chumbani amenifungia. Naomba usiondoke hapa bila mimi Tino. Amenivunja
mkono tayari, nipo na maumivu. Nisaidie. Usije ondoka bila mimi. Ata...”
Tino akashituka sana. “Lara yupo ndani ya hii nyumba, jamani. Nimeongea naye
kwenye simu. Amemfungia chumbani na ameshamvunja mkono.” Tino akawaambia askari
polisi aliofika nao hapo.
“Muongo.” Jerry akakanusha. “Kwa hiyo unakubali kuwa yupo ndani?”
Askari mmoja akawa amemkamata uongo. “Kwani kuwepo ndani kunamfanya hapa kuwa
kwake?” “Ninachotaka ni kuzungumza naye tu. Nikimsikia yupo sawa na anataka
kubaki, hayupo hatarini, basi nitaondoka. Au sisi tutaondoka. Lasivyo hatuwezi
kuondoka tukipuuza ombi la mtu anayelilia msaada! Itakuwa sisi tunashirikiana
na wewe kwa chochote kitakachomtokea baada ya hapa!” “Ndivyo na sisi
tulivyomwambia hivyo hivyo.” Kiongozi wa walinzi wa ile nyumba akaunga mkono
hoja.
Jerry akiwa amewaka hasira akaanza kuwatukana. Wao hawajosoma na
hawana uwezo wakufikiria. Wanaongea kama wajinga tu kwa kuwa hawana pesa.
Akawatukana hapo akikataa wasiingie ndani, Tino akimshangaa Jerry. Alionekana
ni mtu aliyefanikiwa sana. Akiwa anapeleka pesa nyingi sana pale benki! “Kumbe
wewe ni hovyo hivyo!” Tino akajikuta akitamka waziwazi. “Nilikuona ukiwa
unakuja pale benki nikawa nakutamania maendeleo yako mpaka kuanza kutafuta siri
ya mafanikio...” “Hata ufanye nini, huwezi kunifikia.” Jerry akajibu kwa
kiburi. “Na mimi sitaki tena. Sitamani hata kuwa kama wewe. Hovyo tu! Huna hata
hekima! Pesa yako hapo inakusaidia nini sasa?” Tino akamuongelesha kwa ukali.
“Na ngoja nipigie simu magazeti ya udaku waje hapa wapate habari ya
kesho.” Tino akamtisha. “Unang’ang’ania mtoto mdogo wakumzaa mwenyewe wewe baba
mzee hivyo! Acha kinuke magazetini kesho.” Tino akatoa tena simu yake. Kabla
hajabonyeza, Jerry akataka kumkimbilia kule alipokuwa, hapo ndipo wakamkamata
na kumuweka chini, akawa amelala chini kabisa.
Kwanza alishawaudhi kwa kuwatukana. Wakamshikilia pale chini kwa
nguvu, Tino akakimbilia ndani. “Lara!” Akamuita akifuata sauti alipokuwa
akilia. “Amenifungia. Kama funguo haipo hapo
mlangoni, basi anayo mfukoni.” “Haipo hapa. Usilie sasa. Nilikuja na
polisi, wamemshikilia.” Lara akashituka sana. “Tino!
Nilikwambia usimwambie mtu!” Lara akalalamika tena akiwa ndani.
“Ulifikiria ningefanyaje Lara? Wewe umenipigia simu ukilia, halafu nikasikia
kelele nyuma! Sikujua hatari iliyokuwa ikikukabili! Nisingeweza kuja tu
mwenyewe.” Lara akanyamaza huko ndani. “Usiwe na wasiwasi. Sijawaambia watu.
Niliomba tu ruhusa kwa bosi nikamwambia ninadharula kwa kuwa tulikuwa kwenye
kikao, natoa ripoti ya kanda ya ziwa, nikakimbilia polisi hapo Surrender,
nikaja nao na gari yangu.” “Nashukuru Tino. Ila
naomba usiniache hapa.” “Acha ni..” “Yuko ndani kweli?” Polisi mmoja
akaingia.
“Yupo huko chumbani amemfungia. Funguo atakuwa nazo mfukoni.”
Wakatoka tena, Jerry akiwa chini ya ulinzi. Tayari walishamfunga pingu.
“Tunaomba funguo ya chumba kile ulichomfungia Lara.” Akaanza Tino. “Lara ni
mpenzi wangu, na nimekuwa nikiishi naye hapa ndani. Ulizeni hawa walinzi
wanaokuja kulinda hii nyumba kila siku. Kilichotokea kati yetu ni mambo ya
unyumba tu, tutayamaliza wenyewe.” “Hayo ayakubali na Lara pia. Msikubali
kusikiliza upande mmoja. Lara analia ndani, amemvunja mkono, anahitajika huduma
za hospitalini. Na hivi mnavyochelewa kufungua, hatujui tunahatarisha vipi
maisha yake.” Tino akaongeza. Askari mmoja akaanza kuingiza mikono mifukoni kwa
Jerry kikatili bila kusubiri, Jerry akiwa bado na pingu.
“Mnaingilia mambo ya kiunyumba.” Akalalamika Jerry akiwa amekalishwa
chini. “Lara ni mkeo?” Askari mwingine akauliza. “Haikuhusu.” Jerry akajibu kwa
jeuri. Wakapata funguo wakaenda kumfungulia Lara akiwa ameshabadili zile nguo
za kulalia zilizokuwa zimemuacha uchi. Tino akamsogelea. “Amekupiga?” Lara
akaendelea kulia. “Kuna nini?” “Naomba usiniache
hapa. Jerry ataniua kwa hasira.” “Unamaanisha nini?” “Nilishakusanya vitu vyangu. Nataka kuondoka kabisa Tino.”
Tino akatulia kidogo.
Lara akasogea kumuonyesha mizigo yake. Kumbe wakati akilia alikuwa
akiendelea kukusanya vitu vyake. “Nisaidie Tino!”
Tino akasogelea ile mizigo. Akabeba yote kwa pamoja mikono yote. “Nihivi tu?” “Ni nguo tu na viatu ndio vyangu humu ndani. Na
nimemaliza.” “Haya twende.” Wakati wanatoka chumbani na polisi mwingine
akaingia akampokea Tino, ndipo wakatoka kabisa nje barazani.
Jerry akataka kusimama wakamzuia. “Huwezi kuniacha kipindi nina
matatizo Lara!” “Umeniumiza Jerry. Sijui umepatwa
na nini lakini umeniumiza na isingekuwa kuingiliwa, sasa hivi ungekuwa umeniua.
Sitakuwepo hapa kuendelea kuteseka, halafu na mimi unisababishie matatizo!
Hapana Jerry. Mimi sio mkeo, sina sababu ya kukuvumilia.” “Kwa hiyo
ulitaka starehe tu?” “Ndivyo ulivyoniahidi, starehe
imeisha, naondoka. Umeniumiza naenda kutibiwa.” “Huwezi kuondoka. Kwanza
hivyo vyote ni vitu vyangu.” “Tino naomba nisaidie
kufungua aangalie hapahapa mbele ya polisi ajue nimeondoka na vitu vyangu tu
sijaiba hata kijiko. Wewe ni mnyanyasaji Jerry.” “Ningekuwa mnyanyasaji
ungechezea mamilioni yangu ya pesa?” “Si kwa kuwa
na wewe ulikuwa ukichezea mwili wangu! Wewe vipi? Bakia na pesa yako uone kama
utapata wakati mzuri kama niliokuwa nikikupa mimi.” Tino akaanza
kufungua mizigo ya Lara huku akiwasikiliza wapenzi hao wanavyojibishana.
Vitu vya thamani tupu. “Hizo zipo set nzima, nilikununulia mimi.”
Tino akashika. “Hizi?” Tino akamuuliza. “Ndiyo.” Wakashangaa Tino anacheka.
“Sasa Mkuu, unataka uanze kujipaka na kujipulizia pafyumu za kike!? Maana hivi
vyote vya kike!” “Kama yeye ameshindwa wapo wanawake wenzie wanalilia hiyo
nafasi anayoichezea.” Jerry akaongea kwa kiburi. “Kwa hiyo unataka kuja kuwapa
wanawake zako makombo ya Lara!? Umeishiwa kiasi chakupokonya mafuta!?” Wale
polisi wakacheka. “Ni jasho langu. Kwa hiyo ni haki yangu.” “Aisee wewe ni wa
ajabu! Haya, mbali na haya mafuta na hivi vitu vya kike, na hizi chupi za Lara
pia unataka?” Tino akamuuliza kwa kejeli.
“Hata ukinikejeli ni vyangu.” “Umeishi na Lara kwa muda gani hapa?”
Kimya. “Eti Lara?” Yule polisi akamgeukia Lara. “Miezi 7 sasa.” Lara akajibu
kwa aibu. “Sasa huyu si kama mkeo kabisa! Kisheria anatakiwa adai haki zote
kama mkeo, mtakapoachana.” Yule polisi akawa mkali. “Tino, funga hiyo mizigo,
twende kituoni. Huu ni udhalilishaji wa hali ya juu. Rudisha hata hayo mafuta
ndani, tukaandikishe kesi, tuone sheria inataka kumgawia nini Lara baada ya
kuachana.” “Mimi sitaki kumuacha.” “Kwa kipigo ulichompiga, umemvunja mkono na
kumchubua mpaka usoni! Hataki kuishi na wewe, anaondoka kisheria. Wewe si ni
mkorofi na unamatusi? Sasa twende ukatukane jela. Umepiga mwanamke.”
Wakamuingiza kwenye gari ile ya kampuni ya ulinzi pamoja na askari polisi
mmoja, Tino akachukua mizigo ya Lara na polisi mwingine, wakaelekea kituoni
wakitumia gari ya Tino.
“Mimi sitaki kesi Tino.” Njiani Lara akaongea taratibu. Wote
wakamgeukia pale alipokuwa amekaa kiti cha nyuma. “Huyu jamaa anaonekana ana
pesa sana, usiondoke na maumivu tu. Wakimbana vizuri pale kituonia, utaondoka
na pesa hata ya matibabu, ukaenda kuanza maisha kwengine ukiwa umetulia.
Usiende kulala njaa.” Yule polisi akamshawishi. “Na anapesa kweli! Mimi
namfahamu kwa kuijua pesa yake.” Tino akaongeza. “Hapana. Jerry alikuwa mtu
mzuri sana kwangu. Sana. Kuanzia Juzi sijui amepatwa na nini! Hakuwahi kuwa
hivyo. Sitaki kumtia matatizoni.” “Na alivyokupiga vyote hivyo!” Polisi
akamuuliza. “Hajanipiga. Leo hakunipiga ila kuvunja mlango ndio ukaniumiza.”
Gafla Lara ndio akawa mtetezi wa Jerry tena.
“Unamtetea nini mshenzi tu yule! Ametutukana sana. Lazima
aadabishwe.” Lara akanyamaza akimfikiria Jerry. Anatakiwa na familia yake.
Mkewe mgonjwa. Akamuhurumia. Wakafika kituo cha polisi, wakamshusha Jerry kama
mtuhumiwa, wakaenda mapokezi. Wakataka kuandikisha kesi. “Mimi sitaki
kuandikisha kesi.” Lara akashangaza wote. Aliongea kwa upole akiwa ameshikilia
mkono wake. Usoni akionekana ameumizwa. Jerry akashangaa. “Ninachotaka ni
kuondoka na kumuacha kwa amani. Sitaki kesi.” Lara akaweka msisitizo. Mkuu wa
kituo hapo akatoka kumbe anafahamiana vizuri sana na Jerry.
“Unafanya nini hapa, wewe!?” Akamuuliza akionekana kufahamiana kwa karibu.
“Waulize vijana wako! Wamenivamia nyumbani kwangu na kunitia pingu.” Jerry
akataka kuwageuka. “Hapana Jerry. Ukifanya hivyo kwa hakika nitakufungulia mashitaka.”
“Ni nini kinaendelea?” Yule mkuu wa kituo akauliza. “Jerry alitaka kunidhuru ndio
mimi nikapiga simu kuomba msaada.” Lara akawahi yeye hujibu. “Nani alikwambia
nilitaka kukudhuru wewe Lara!?” “Huu mkono na uso mpaka shingoni, ni wewe
umeniumiza Jerry. Acha kubisha na kutaka kufanya watu wote wajinga hapa.
Ukitaka kufanya ubishi nafungua shitaka.” Lara akamjia juu, mkuu wa kituo
akaomba wakazungumze ndani ofisini kwake.
“Pesa ni kila kitu jamani!” Akasikika Tino akilalamika kwa sauti ya
chini wakati Lara, Jerry na mkuu wa kituo wakiingia ofisini. “Ilikuaje?” Akauliza mkuu wa kituo wakati wanakaa. “Ni
mambo ya kifamilia.” Akawahi Jerry. “Na kama nilivyowaambia wale askari, ni
mambo ambayo tunaweza kuyamaliza sisi wawili.” Yule askari akaonekana kama
hajaelewa. “Labda nianzie kwenye swali la mwanzoni kabisa nililotakiwa kuuliza.
Huyu binti ni nani?” Lara kimya.
“Mpenzi wangu na tulikuwa tukiishi pamoja. Ikatokea kutokuelewana,
mwenzangu akapiga simu kuomba msaada, nashangaa navamiwa!” “Husemi ukweli
Jerry. Unamdanganya.” Lara akaeleza tokea wapo Mwanza mpaka siku hiyo.
Alivyompiga jana yake, yule polisi mwenyewe akabaki ametoa macho.
“Nilimueleza ni kwa sababu ya matatizo yakifamilia.” “Jeremiah!” Lara
akawasikia wanabadilisha lugha. Wanaongea kilugha kwa muda mrefu tu lakini alionekana kumsemesha kitu kwa kuweka
msisitizo na ukali kidogo. Ila kuna sehemu Lara akasikia akimwambia, ‘hasira
zinaweza kukusababisha ukaua’. Akaendelea kwa kilugha tena. Akasikia, ‘haitajalisha
sababu, ila utaishia jela na pesa yako ije iliwe na watu baki’. Alizungumza
naye kwa muda mrefu wakimuacha Lara ametulia anasikiliza bila kuelewa.
“Tafadhali naomba myamalize Jerry. Yamalizeni hapahapa. Mwache
aondoke kwa amani kabisa. Kama mnakuja kuanza, mje muanze wakati mwingine. Huyu
anao ushahidi wa kukutwa na hawa polisi amefungiwa na umemuumiza. Unataka haya
mambo yaende mbali? Unataka aje adai haki za kama mke?” Akauliza kwa ukali
kidogo.
“Mimi sitaki kesi. Nataka niondoke kwa amani na aahidi asinitafute
kuja kunidhuru tena. Hilo tu.” “Kwa hiyo unaniacha Lara?” “Wewe ndio unaniacha
Jerry. Tulikuwa na amani, ukaamua kuvuruga. Tukiwa Mwanza nilikuhakikishia mimi
sina mwanaume na wala sina mpango wa kuondoka, lakini umeendeleza fujo na
manyanyaso ukinihesabia vitu ulivyonipa! Hata kama sasa hivi tunasema tunarudiana,
naishije tena na wewe kwa mabaya yote hayo uliyonifanyia na vile
ulivyoninyanyasa!?” “Ni hasira tu Lara.” “Hasira za
nini kwangu mtu ambaye nimetulia tu sijakufanya chochote?!” Lara akaanza
kulia tena.
“Nasikia maumivu makali. Naombeni niende hospitalini. Naona
mmekutana ndugu, mnaongea mambo yenu sasa hivi mnanisahau mimi.” “Jerry!” Yule mkuu wa kituo akamuita
kama kumkumbusha kitu. “Kama unamkumbusha ili aniombe msamaha, usijisumbue.
Mimi namjua Jerry. Hawezi kuniomba msamaha na wala mimi sihitaji msamaha wake.
Nimesamehe na sitaki afunguliwe kesi. Ana mambo ya kifamilia yanamsubiri.
Kumfungia kokote ni kuadhibu familia yake. Mwacheni tu ila naomba mwambie
asinifuatilie tena, wala asinitafute hata kwa ujumbe. Tukiachana hapa, ndio iwe
basi.” “Kweli Lara una roho ngumu!” Wala Lara hakumwangalia tena. Akabakiza
macho kwa yule mkuu wa kituo. Baada ya mazungumzo marefu hapo, ikabidi wamalize
na kuwaruhusu maana Lara alizidi kulia maumivu, Jerry akimng’ang’ania mpaka
ikabidi yule mkuu wa kituo awe mkali sana kwa Jerry.
Tino alisimama wakati Lara anatoka akijifuta machozi. “Acha basi
nikupeleke mimi hospitalini. Naomba Lara. Ili tuachane kwa amani.” Jerry
akatoka na hilo ombi akiwa hana pingu. “Asante,
lakini hapana Jerry. Inatosha. Twende Tino.” “Lara! Ni hospitali tu! Sita..”
“Hapana Jerry. Tumezungumza. Naomba fanya kama nilivyokwambia, ondoka. Mwache
huyo binti kwa sasa.” “Nataka kusaidia tu.” Jerry akaendelea kung’ang’ania wale
polisi pale wakimshangaa.
“Twende Tino.” Lara hakutaka hata kumjibu. Wakamuona anatoa walet yake. Lara akajua
ameambiwa awalipe wale polisi waliofika nyumbani kwake na kumchukua. Lara
hakusubiri. Akatoka, Tino akamfuata baada yakuwashukuru wale polisi walioongozana
naye mpaka nyumbani kwa Jerry na kumsaidia kumtoa Lara. Kwa kuwa alijua Jerry
atawalipa, aliwanong’oneza kitu wale polisi, wakacheka na kutoka akiwaambia
ulaji mkubwa unakuja. Akimaanisha kutoka kwa Jerry.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment