Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Chozi Langu! - Sehemu ya 14. - Naomi Simulizi

Chozi Langu! - Sehemu ya 14.

 Walifika hospitalini moja kwa moja Tino alimpeleka kitengo cha mifupa. Bado Lara alikuwa amebeba mkono wake akinung’unika maumivu. Wakakaa hapo wakisubiria kumuona daktari. Walikuta foleni kubwa. Tino na Lara wakapata sehemu ya kukaa, wakakaa. Watu waliokuwa wametangulia wakaendelea kuonwa na daktari, wakiitwa namba zao, Lara akiwa amejiinamia hata hakuwa na wazo na simu, ila Tino akiwa kwenye simu yake muda wote wala hawakuendelea kuzungumza.

Lara akiwa ametulia, mara akamuona Jax anawasogelea akiwa amependeza wazi akionekana ametokea ofisini. Shati jeupe kabisa, na suruali safi nyeusi iliyoiva yakitambaa. 
Amechomekea. Na kiatu safi, cheusi, kinawaka chenye ngozi nzuri sana. Wakati anamsogelea, Lara akajishangaa amesimama, Tino akageuka kule anakoshangaa Lara, mpaka kusimama. Akamuona  Jax. Yeye alimtegemea maana ndiye aliyemtaarifu kuwa yupo pale na Lara. Ilimgusa Jax, hata Tino pia, pale walipomuona Lara amesimama alipomuona. Akajua bado ipo.

Alikuwa ameshika chupa ya maji na mfuko mdogo. Akamkabidhi Tino bila hata salamu akamsogelea Lara karibu. “Pole.” “Asante.” Akamshika shingoni kule kwenye alama nyekundu na shavuni. Lara macho chini. “Wamekuangalia na huku?”  Lara akatingisha kichwa kukataa, na kujifuta machozi. “Ndio tunasubiria hapa kumuona daktari. Bado hata hatujamuona!” Tino akamjibu. “Ni mkono upi? Huu ulioshika?” Jax akaendelea kuuliza taratibu akionyesha kuumia na yeye. Lara akatingisha kichwa kukubali. “Jax ameleta dawa za maumivu ili kupunguza maumivu wakati tunasubiri.” Tino akampa dawa na maji. “Asante.” Lara akashukuru na kumeza vile vidonge viwili alivyopewa na Tino.

“Tukae.” Jax akaongeza wakati na yeye akikaa, kuashiria na yeye ndio amefika. Lara akajikuta amebakiwa na nafasi ya katikati ya Jax na Tino. Akakaa na kumgeukia Tino kama kumuuliza ni kwa nini alimuita! Tino akajidai anapiga simu akaondoka pale, akamuacha hapo na Jax. Lara alitamani kumfuata nyuma, lakini ikabidi awe mpole, atulie tu. Aibu, asijue Jax aliambiwa nini juu ya tukio lake. Akatulia.

“Upo namba ngapi?” “Tino ndio anacho kikaratasi nafikiri 55.” “Hapo nikumuona tu daktari?!” “Ndiyo.” Jax akafikiria kidogo. “Ninawazo la tofauti Lara. Hapa tutakaa sana, twende kwenye hospitali yakulipia.” “Hapana Jax. Mimi nitasubiri tu hapa.” “Kwa nini?!” Lara akabaki kimya. “Utaendelea kuwa na maumivu ukisubiri hapa mpaka muda gani? Foleni ni kubwa sana, bado hata hawajafika 20!” Kisha akamgeukia vizuri kama aliyeshangazwa na kitu ambacho hakutarajia. “Tumeanza lini kupishana mawazo!?” Jax akamuuliza kwa upendo tu. “Naepuka gharama.” “Kipi cha muhimu na haraka? Kuweka pesa benki au kupata matibabu yako?” Lara akainama mbele yake wakiwa wamekaa pale.

“Twende.” Akasimama na kumnyooshea mkono kama kumsaidia kusimama. “Acha tu, nitaweza kusimama. Asante.” Akasimama peke yake. Akampigia simu Tino, wakakutana nje. “Vipi tena?” “Naona hapa tutakesha. Acha twende kwenye hospitali ambayo watafanya mambo kwa haraka, hii siku iishe na yeye Lara akapumzike. Lasivyo tutalala hapa.” “Wazo zuri. Sasa mimi nitawafuata huko. Maana natakiwa kazini mara moja.” “Hamna shida, nitakujulisha tutakapokuwa.” Lara akashituka sana. Inamaana anaachwa na Jax! “Naomba tuzungumze Tino, kabla hujaa... Naomba tuzungumze.” Akamsukuma kwa nguvu Tino kwa mkono wake wa kushoto ambao hauna maumivu. Tino akajua anachosukumiwa ni nini. Akaanza kucheka taratibu.

“Kabla hujapaniki, sijamwambia kila kitu ila nilimwambia nipo na Lara hospitalini.” Lara akabaki akimsikiliza. “Nilimwambia umeumia mkono.” “Tino! Mbona humalizii unarudiarudia tu?” “Kwa kuwa Jax mwenyewe ananiangalia, na wewe umenisimamia hapa kwa ukali, nashindwa kuzungumza.” “Nilikuomba usimwambie mtu!” “Sijamwambia mtu yeyote ila Jax, uliyemuacha akikutafuta na kujilaumu kama mwehu. Nilimwambia nilikuona Mwanza, akanilaumu sana kushindwa kujua ni wapi unaishi au kukuomba hata namba! Nilimwambia upo na mtu wako, na ni Mr Kembo.” Lara akatoa macho.

“Kwani Jax anamfahamu Jerry?!” “Kabla hajahama pale CRDB yeye ndio alikuwa akihusika na akaunti zake. Kwa zile pesa alizokuwa akiingiza pale, mimi na Jax tukaanza kumwita ‘the god’. Kwa hiyo ndiyo,  Jax anamfahamu vizuri sana.” Lara akachoka. “Naomba usiniache naye, tafadhali Tino. Twende wote.” “Natakiwa kazini mama! Acha nikachungulie tu, nitawafuata.” “Sasa kwa nini ulimuita hapa?” Lara akalalamika akimshikilia shati kama asimuache. “Nilikwambia jinsi alivyonilaumu jinsi nilivyokuacha kule Mwanza. Nilimwambia ulikuwa na ‘the god’, pia hakuona kama nisababu yakueleweka kutokukufuatilia. Naomba utulie Lara, utibiwe tujue ni nini kinakusumbua.” “Muda unazidi kwenda.” Wote wakamgeukia Jax.

“Acha mimi niende.” Tino akakimbia kwa haraka. Akawaacha hapo. Lara alishindwa hata kumuangalia. “Twende.” Jax akaweka msisitizo. Lara akamfuata nyuma. Jax alikuwa bado na gari yake ileile. Akamfungulia mlango, Lara akapanda. Ile hali ya utulivu moyoni aliyoipata mle ndani ya gari ya Jax mara baada yakupanda kitini, hata kabla Jax hajapanda na kukaa kwenye kiti chake, Lara akajikuta anatokwa machozi. Alilia sana mpaka Jax anapanda garini, akamkuta akilia.

Akamshitua Jax. “Maumivu makali?” Akatingisha kichwa na mabega kukataa. “Nisikilize Lara. Uso wako ni mwekundi na macho mekundu na yamevimba sana, kuashiria baso upo kwenye tension. Mimi nipo hapa na wewe, naomba jaribu kutulia. Sawa?” Lara akatingisha kichwa kukubali. Jax akaondoa gari kuelekea hospitalini.

Walikaa na Jax hapo hospitalini akifanyiwa vipimo mpaka mwisho akaonekana anahitaji PoP, wakaelekea upande huo kusubiri ili afungwe. “Nimefurahi kukuona Lara.” Hilo neno likamuuma sana Lara, akainama nakuanza kulia tena. Alilia sana Lara, hata hakujua anacholia. Akajichukia kupita kiasi na kujidharau. Hao watu alitamani kuja kukutana nao wakati mambo yake yapo safi. Amependeza anayo mafanikio. Hapo alipo hajui hata baada ya hapo anakwenda kulala wapi!

 Ingekuwa mapema kidogo, angepanda basi kukimbilia nyumbani kwao, Dodoma. Yeye yupo hapo hospitalini na Jax, lakini mizigo yake ipo kwenye gari ya Tino. Ametolewa kwenye ugomvi nyumbani kwa mume wa mtu! Mtu mzima kabisa! Akiwa ameumizwa vibaya sana. Alikuwa kwenye aibu hajui hata anamtizama vipi huyo Jax aliyemkimbia tena akiwa amemuonya huko anakokimbilia hatakuwa salama.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tino alirudi hapo akiwa ameshafungwa PoP mkononi. Jax alilipia akachukua dawa za maumivu, wakaanza kutembea kuelekea sehemu waliyoegesha magari. Mapigo ya Lara yakienda mbio, hajui anafanyaje kwa wanaume hao wawili. Mmoja anayo mizigo yake kwenye gari, Jax amekuwa naye mpaka akatibiwa. Anawaaga anakwenda wapi! Lara akawa anatembea taratibu huku akiwaza chakusema na jinsi yakuachana na hao watu wawili. Wakatembea mpaka wakafika kwenye eneo yalipo magari. Wakasimama hapo kama waliopoteza dira na wao.

“Naomba nikushukuru Jax. Asante kwa matibabu. Naomba Tino mwenye mizigo yangu unipeleke nikapumzike.”  Lara akaongea taratibu akiwa hata hajui atapelekwa wapi. Ila tu alitaka kuachana na Jax kwanza. “Unakwenda wapi?” Jax akauliza taratibu tu. “Kupumzika. Najihisi kuchoka na kichwa kinaniuma pamoja na macho. Nahitaji kulala.” Lara akajieleza akikwepa swali la ni wapi anakwenda. “Lara!” Jax akamuita tena kumkumbusha swali lake. Lara akanyamaza. “Kwa chochote utakachoamua, naomba isiwe kujificha tena. Au safari hii sio kunitoroka tena. Mimi ni mtu mzima, nakuahidi kupokea na kuheshimu maamuzi yako lakini si kwakutengana.” Jax akawa muwazi kabisa.

“Umenielewa Lara?” Lara akajifuta machozi na kutingisha kichwa. “Samahani niliondoka bila kukuaga Jax. Lakini nilihitaji...” Akasita Lara. Akajifuta tena machozi. “Nilikuwa siwezi kupumua! Nilihisi nimebanwa pua! Siwezi hata kupumua! Nilihitaji kuondoka.” “Ungeniambia, ningeelewa Lara. Na ningeheshimu kuliko kuondoka tu! Kwanza ulikuwa mgonjwa. Huna damu, halafu hukuwa umenijibu chochote! Tulikubaliana nikirudi tuzungumze. Sikujua ni nini kimekupata! Sikujua kama ulikuf..” Wakamuona Jax anageukia pembeni. Anajifuta machozi. “Samahani Jax. Samahani sana.” Lara naye akajikuta akilia na yeye. Tino amebaki hajui azungumze nini.

“Naomba kujua unaelekea wapi Lara.” Jax akauliza baada yakutulia. “Nataka kujua kwa hakika. Sitakusumbua, nakuahidi nitafuata matakwa yako ila nataka kujua wapi upo.” Lara akajifuta machozi na kusafisha koo. “Kesho nitarudi nyumbani.” “Kwamba unarudi kuishi Dodoma kwa wazazi!?” Tino akauliza kwa mshangao. “Nahitaji muda wakupona. Nitulie na nijipage upya, ndipo nijue baada ya hapo nini kinafuata.” “Mimi bado hujajibu swali langu Lara. Sasa hivi unakwenda wapi?” Jax akauliza tena. “Nilitaka Tino anisindikize mpaka hotelini, nilale kwa usiku wa leo, kesho ndio nirudi nyumbani.” “Kweli Lara?!” Tino akauliza kwa mshangao sana na kuumia.

“Nitafanyaje Tino? Wewe unajua hapa mjini sina hata ndugu na...” “Sisi hapa tuliosimama mbele yako ni kina nani?” Tino akauliza. “Wewe unajua nina nyumba, na Jax ananyumba. Upo mgonjwa, kweli unataka kulala hotelini halafu urudi kwa wazazi ndio wakuuguze baada ya kula starehe mjini, unarudi kwa wazazi kuwapa wao shida!” “Usinilaumu Tino. Ningejuaje nafasi zenu?” Lara akajifuta machozi. “Nilikuacha ukiwa unatengeneza mahusiano na Suzy! Nimeondoka kwenye maisha yakina Suzy miezi mingi imepita. Siwezi tu kurudi nijifanye mambo yapo vilevile Tino! Sijui nafasi yako sasa hivi kwenye maisha.” “Na Jax je? Hata kama ndoa ilishindikana, lakini sisi tulikuwa marafiki Lara!” Tino akasisitiza.

“Ndio maana uliponiita asubuhi hata sikufikiria, nikakimbia kuja. Kwa nini na wewe unashindwa kuonyesha moyo huohuo, kwetu? Inaonekana bado hujasamehe Lara!” “Wewe nimekupa sababu Tino. Kwa nini nimeshindwa kukufikiria kuja kwako. Pia sio heshima kwa Suzy! Hata kama hamuishi pamoja, leo aje agundue nilihama pale kwetu tulipokuwa tukiishi pamoja, eti naishi na wewe! Sio sawa. Na kwa Jax.” “Ehe! Kwa Jax kuna nini?” Tino akauliza.

“Jax alinipeleka kwake Tino. Haki nilishindwa kukaa. Naomba niwe mkweli. Nilijiona naingia nyumbani kwa Tula na Jax sio kwa Jax tu.” “Lara!” Jax akashangaa sana. “Kweli Jax. Uliniacha mimi. Au ulikimbia pale tulipokuwa tukiishi wote, mimi na wewe. Ukipaona hapana hadhi kwa mpenzi wako. Ukahama naye sehemu ambayo hata sikuwa nikiijua! Ukaona mpenzi wako hastahili kuishi sehemu kama ile tuliyokuwa tukiishi mimi na wewe, ukaenda kumnunulia nyumba au kumuhamishia kwenye nyumba ya thamani ambayo ulikuwa nayo wakati tupo pamoja, tukilala tunapepewa na feni, huku joto na kelele za mtaani zikiendelea usiku kucha! Ukaona yeye hastahili shida niliyokuwa nikiipata mimi! Ukaenda kuishi naye sehemu nzuri!”

“Eti yameshindikana kati yenu, ndio eti unanipeleka mimi palapale kwenye ile nyumba uliyomthaminisha mpenzi wako, mkaishi naye kwa mapenzi yote! Leo eti mimi ambaye ulikuwa radhi kuishi na mimi kwenye joto vile, nyumba hiyohiyo ikiwepo ila hukutaka kunipeleka tokea mwanzo, ndio leo niombe hifadhi! Kweli jamani!? Hata kama mnanidharau sio kwa kiwango hicho.” “Haikuwa hivyo Lara!” Jax akajitetea akiwa ameishiwa nguvu kabisa. Hakujua kama kile ndicho anachofikiria au kinachomuumiza Lara, tena kwa upana huo!

“Lakini ndivyo inavyoonekana Jax. Hapo hata mimi namtetea Lara.” Tino akaongeza akionekana na yeye kumuelewa Lara. “Kwa vyovyote ilivyokuwa Jax, kama ungeona kuna uthamani wa mimi niliyekuwa na wewe, ukikusudia kunioa, nastahili vitu vizuri, ungenipeleka pale mapema kabla ya Tula! Hukukusudia mimi niwe pale. Ile nyumba ni ya Tula na yako, Jax. Mimi siwezi, na nimeshindwa kabisa kuwa pale. Nilihisi kubanwa punzi. Nikajiona najidhalilisha au naungana mkono na wewe kunidhalilisha. Siwezi kufanya watu waniheshimu, lakini siwezi kujipinga mimi mwenyewe.” Wote kimya. Wakabaki kama wakiwaza. Lara aliongea kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake. Akatulia kwa muda akijaribu kutulia.

“Nyumbani ni nyumbani tu. Mama alinilea nikiwa nimeachwa na kila mtu, nimeharibikiwa mimba. Nilikuwa mgonjwa wazaidi ya huu mkono. Tino ni shahidi damu zilizokuwa zikinitoka, wakisaidiana na mama kufuta njiani. Unakumbuka maneno ya mama aliyokuwa akikwambia na kukushukuru kumsaidia kunirudisha nyumbani?” Kimya.

“Kwa kifupi tu, hata jana nilizungumza na baba, akaniambia bado hajashindwa kunilea na haitakaa ikatokea ninakuwa kwake. Nitabaki kuwa kiziwanda wake daima. Hapo ndipo ninapotaka kwenda sasa hivi nikapumzike. Tafadhali Tino, nisaidie kunifikisha hotelini nilale, kesho nirudi kwetu. Nakushukuru Jax kwa kuwa na mimi leo. Asante. Safari hii nimeaga. Narudi kwetu. Sijui itakuaje baada ya kupona. Lakini safari hii naaga. Sitoroki. Tino nakushukuru, na samahani kwa ukimya wa muda wote niliokuwa nimeondoka.” Kimya. Lara akaongoza njia kuelekea kwenye gari la Tino, akawaacha marafiki hao wawili, wamesimama hapo.

Akaona gari ya Tino inawaka taa na kutoa mlio, akajua amefungua, akapanda kiti cha mbele cha abiria, akafunga na mkanda, akawaacha bado wapo nje wamesimama, pembeni kidogo kwa gari la Tino. Wakazungumza kidogo, Lara akaona Tino anafungua mlango. “Nitakupeleka hotelini, utakuwa hapo mpaka jumamosi asubuhi tutakuja kukusindikiza mpaka nyumbani.” “Hapana Tino. Jax alishaniacha na mlishakwenda kuzungumza na wazazi. Wewe na dada Nelly mlishayamaliza mahusiano yangu na Jax kwa heshima. Madeni ya ile harusi nilishayalipa yote. Nimelipa ndugu, jamaa na marafiki wote waliokuwa wamechanga na kudai wazazi wangu. Jax sio mpenzi wangu, ananirudisha vipi nyumbani? Inakuwa nikutibua wazazi wangu tu!” “Na mimi?” Tino akauliza.

“Mimi sihitaji msaada wakurudishwa nyumbani. Msaada ninaokuomba wa mwisho ni uniache hotelini, basi. Tafadhali usianze mambo mengine Tino. Mimi si mke wala mpenzi wa Jax tena.” “Na mahusiano tuliyojenga?” “Nayathamini ndio maana nilipopatwa na shida umekuwa mtu wa kwanza kukufikiria na kukukimbilia. Naomba mimi ndio nikuombe msaada. Naomba mimi ndio niseme ni nini nataka, msinipangie. Na ndio maana mara ya kwanza niliondoka bila kuaga kwa sababu nilijua kila mtu atataka nifanye vile anavyofikiria yeye.” “Samahani Lara. Ni kweli. Nitaheshimu hilo. Basi twende ukapumzike, halafu kesho asubuhi nitakuja kukusindikiza kituo cha mabasi. Ni sawa?” “Nitakujulisha usiku kama nitahitaji huo msaada, kutokana na nitakapokuwa nimelala na umbali mpaka kituo cha mabasi. Naweza pata taksii, ambayo itanifikisha kituo cha mabasi bila shida.” Tino akanyamaza na kuondoa gari.

 Wakaondoka hapo kila mtu kimya, Lara akajiegemeza vizuri. Tino akakanyaga mafuta akitafuta hoteli karibu na Ubungo. “Naomba nije kukupeleka kituo cha mabasi Lara.” Baada ya muda Tino akavunja ukimya. “Uliahidi kuheshimu maamuzi yangu, Tino.” Lara akamjibu taratibu tu. “Sawa. Basi nitasubiri unitafute.” “Nashukuru.” Wakanyamaza. Walipokuwa kwenye mataa, akamuona anatuma ujumbe mpaka taa za kijani ziliruhusu lakini Tino alikuwa akituma ujumbe. Lara akahisi anawasiliana na Jax. Akajituliza kimya.

Tino alimfikisha hotelini, akamchukulia chumba na kuanza kuhangaika yeye mwenyewe kuingiza mizigo ya Lara ndani, mpaka chumbani. “Hiyo mizigo ni mingi na ipo kwa mafungu mafungu madogo madogo Lara. Unataka nikakutafutie sanduku tujaribu kuiweka pamoja?” Lara akanyamaza. “Utasafirije na mizigo mingi hivi? Acha nikakununulie masanduku.” “Nitapanga vizuri, yote itaingia kwenye haya masanduku. Hayajajaa. Nilifungasha kwa haraka tu. Lakini nikitulia na kupanga vizuri, vitaenea tu. Nakushukuru kwa kila kitu. Asante, ila naomba uondoke, nipumzike.” Tino akabaki amekaa hapo kitandani.

“Sasa unataka nini Tino? Nenda mimi nilale, nimechoka sana.” “Basi nikalete chakula.” Lara akamwangalia na kukaa pembeni yake. “Nimechoka na kichwa kimechanganyika Tino. Nina uchungu wakupitiliza. Nahitaji utulivu tu. Tafadhali niache nilale.” “Unaahidi kuja kunitafuta tena? Maana najua kesho hutanitafuta Lara.” “Nipe muda Tino.” Tino akatulia kidogo. Lara akamwangalia. “Umependeza Lara! Umependeza sana. Tofauti na mara ya mwisho tulivyoachana baada ya tukio la Jax. Naomba usirudi kule.” Lara akawa amemuelewa.

“Nisikilize Tino. Jerry sikumpenda kama Jax. Jax nilimpenda haswa. Lakini Jerry nilimkubali ili kustarehe tu. Na ndivyo alivyonitongoza na kukubaliana starehe. Ugomvi ulionikuta nao na Jerry, ni pale alipotaka awe Jax. Nilimkatalia kabisa. Kwa kuwa nilijua Jerry ameoa na anafamilia yake. Ni mtu mzima hawezi kuja kuwa mume wangu ndio maana Jerry alikasirika. Mkewe anaumwa anakaribia kufa huko nchini kwao. Jerry anataka mimi nije kuwa mkewe! Nikamwambia hapana.” “Lakini yule jamaa anapesa Lara!” Tino akamjaribu.

“Hivi kwa hivi nilivyo Tino, unafikiria nilikosa mwanaume wakunitoa pale tulipokuwa tukiishi na Jax, na kunipa kile Jax amempa Tula?” Lara akauliza kwa pole tu. Tino Kimya maana Lara alijaliwa mvuto haswa. Jibu akawa nalo. “Niliumia kwa kuwa nilijifunga kwa Jax, nakujinyima yale ambayo watu kama Jerry walikuwa tayari kunipa. Niliumia kuona Jax ameniacha sababu ya mwanamke mwingine wakati mimi nilikuwa nawaacha wanaume wengine wathamani kuliko Jax, kwa ajili yake Jax! Nilimkubali Jerry kwa hasira tu, Tino. Nikaona nijipe kile nilichokuwa nikijipunja. Na kweli nilikipata. Haswa. Usinione nipo hapa, pesa ya Jerry nimeitumia haswa na bado ninayo. Na najua ningetaka ningeendelea kuitumia tu, lakini bado nina tumaini Tino.” “Tumaini gani?” Lara akainama.

“Lara?” “Sijakata tamaa Tino. Naamini ipo siku na mimi naweza kupata mwanaume atakayenipenda kwa dhati kama vile Jax kwa Tula. Atakayekubali kulipa kila garama kwangu, akakubali tukafunga ndoa na mimi, tukaanzisha familia. Bado nina imani Tino. Kile baba yangu alichompa mama, naamini na mimi ninaweza kupata. Sitaki watu kama kina Jerry wanipokonye hilo tumaini. Najua ipo siku itatimia tu.” “Nimefurahi kusikia hivyo. Nilijua umeamua kutupilia mbali maisha yako sababu ya kilichotokea kwako na Jax.” “Hapana Tino. Nilikuwa napumzika tu.” Tino akamwangalia vizuri.

“Sasa umemaliza kupumzika? Maana serikali ipo kwenu Dodoma. Wazito wote wapo huko. Na wewe unavutia hivyo! Nitasikitika kuja kusikia umeharibu maisha yako kwa magonjwa.” “Sitarudia tena.” “Kweli Lara?” “Mungu anisaidie. Nimejaribu, imeishia pabaya. Basi. Mungu amenitoa hapo salama, naahidi, na wewe nakuahidi, hutapata tena simu kama hizi za leo.” “Na kutokukuona kwenye mabaa Lara. Tafadhali. Wewe ni mzuri sana na mtulivu, sio msichana wakutembea na wanaume za watu! Kwanza ni dhambi.” Lara akacheka sana vile Tino alivyosema.

“Unadhani mimi simjui Mungu sababu ya kunywa pombe?” Lara akacheka zaidi. “Sikosi kanisani kila siku jumapili.” “Najua Tino.” Lara akajibu huku ameinama akifikiria. “Mbona hapo hutoi ahadi, Lara? Au unataka kwenda kuanza na Jerry mwengine?” “Hapana Tino. Nimemaliza. Sasa hivi nitatulia. Utakayekuja kunikuta naye baa, ujue nimemchunguza, nikaona atanipa ninachokitamani. Sio michezo tena.” Wakatulia kidogo.

“Nikwambie ukweli Tino?” “Niambie tu.” Tino akaonyesha utayari wakumsikiliza. “Kesho sina mpango wakuja kukupigia simu ili unipeleke kituo cha mabasi.” “Mbona najua. Hilo nilishajua.” Lara akacheka taratibu. “Yaani tokea unaniambia kule, kabla hatujafika hapa, nilijua hutanitafuta.” Lara akacheka na kunyamaza.  “Na mimi nikuulize Lara?” Lara akamwangalia. “Ulinisamehe kabisa kutoka moyoni?” “Najua unanipenda Tino, na unanijali, hutaki uniumize. Najua uliniumiza bila kukusudia. Nilikusamehe. Lakini hivi unajua sasa hivi na mimi ningekuwa nina mtoto?” Tino akanyamaza kwa kuumia.

“Tuyaache hayo Tino. Naomba unipishe, nioge, nilale.” “Wakati wowote, muda wowote, popote, ukiwa na shida, nipigie kama ulivyofanya leo. Umenifurahisha.” Lara akasimama akicheka kinyonge. Tino akaondoka na kumuacha. 

Nyumbani ni Nyumbani tu.

L

ara alitua jijini Dodoma akapokelewa na baba yake. Akashangaa alivyo. “Niliangukiwa na mlango baba. Nipo sawa kabisa. Ila mkataba wangu wa kazi uliisha, tokea majuzi, nikaona nije nipumzike huku nyumbani kabla sijarudi tena kazini.” “Pole mama. Pole sana. Sasa watakupokea tena kazini?” “Nipo kwenye kufikiria. Nirudi tena kazini au nifanye biashara mimi mwenyewe. Ndio maana nimeona nipumzike huku nyumbani bila kumaliza pesa kwenye nyumba za kupanga.” Lara akampanga baba yake mpaka akapangika “Umefikiria vizuri. Na hivyo ulivyo mgonjwa, itakusaidia kupata muda mtulivu wakupona huku ukifikiria.” Baba yake akamsaidia kuingiza mizigo kwenye gari. Wakaondoka hapo.

“Umechoka sana au unataka nikupitishe kwa mama yako kwanza?” Lara akacheka. “Nimetoka kuzungumza naye tulipofika tu hapa na basi. Ameniambia nimpitie pale, nikae naye mpaka jioni tutoke naye akanipikie chakula kizuri.” Lara anarudi kwao akiwa ameongeza heshima haswa. Alibadilisha maisha ya nyumbani kwao. Amerudi akiwa amevunjwa mkono, akiugulia maumivu ya nafsi na mwili, lakini wazazi wake wanacheka. Amebadili historia ya kwao. Kutoka kudharauliwa na kashfa aliyowaingiza baada ya Jax kuvunja ndoa, akawainua wazazi wake kibiashara, angalau wanaheshimika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Maisha yakaanza. Juma la kwanza ikawa ni kujiuguza na kupumzika tu, Lara hakutoka nje kabisa mpaka zile alama za wekundu zikapotea kabisa, ikabakia mkono tu ambao bado ulikuwa na PoP. Akaanza kutoka asubuhi na baba yake na dada yake au mama yake kama haendi kazini, anaungana nao kwenye biashara yao hiyo ya duka alilowafungulia. Anasaidia huko hata kusogeza vitu vidogo vidogo au tu kukaa nao akiwaona vile wanavyofanya kazi, kisha usiku wanarudi nyumbani. Wakaendelea hivyo kichwa cha Lara kikiendelea kuzunguka. Nini chakufanya baada ya hiyo Pop kutoka! Simu yake aliweka pembeni kabisa akitaka kutulia kwani Jerry alimpigia mara baada yakufika Dodoma. Alipoacha kupokea akamtumia ujumbe akitaka kujua kama alipatiwa matibabu na anaendeleaje! Lara hakutaka hata kumjibu. Akazima simu kabisa na kutulia. 

Kulikoungua Mpini....

S

iku moja ya jumamosi Lara akiwa na wazazi wake dukani, mida ya saa tano asubuhi hivi akaona gari inayofanana na Jax inasimama mbele ya duka lao. Moyo ukampasuka kwa mshtuko. Aliposhuka mdogo wake wa kiume, ndipo akajua ni Jax, Lara akajificha kwa kushuka kutoka kwenye kiti alichokuwa amekaa, kwa haraka mpaka wazazi wake wakashangaa. Akatambaa na kutoka pale dukani kwa haraka akitumia mlango wa nyuma. Mpaka Jax anashuka garini, Lara alishapotea. “Karibu baba.” Mama yake akamkaribisha wakati baba yake, mzee Chiwanga akimuhudumia mteja. Jax akasalimia wote na kutaka kuwashika mkono lakini mzee Chiwanga akaonekana ana kazi, hawezi kumshika mkono Jax.

“Naona biashara nzuri wazee wangu.” Jax akasifia. “Tunashukuru Mungu, mwanangu. Lara huyo ndiye ametusukuma. Ametupa wazo, mtaji na kuhakikisha biashara inaanza na kusimama.” Mama Chiwanga akaongea kwa majivuno kidogo, mumewe kimya. “Pongezeni sana.” Jax akasifia akijua ni pesa ya Jerry tu hiyo. “Kumbe upo hapa Dodoma!?” “Hapana mama. Nimeingia asubuhi hii, nimekuja kumuona Lara.” Wakaangaliana na mumewe. Mumewe akaendelea na shuguli zake.

“Lara alikuwa hapa, naona ametoka.” Ikabidi mama mtu ajibu. “Hamna shida, naweza kumsubiri tu.” Jax akasimama hapo pembeni ya duka. Lisaa likapita, na nusu. Mama yake akaamua kwenda kumtizama nyuma.

Akamkuta amelala stoo. Sehemu wanapotunza bidhaa zote wanazouza. “Lara!” Lara akakaa. “Ameondoka?” “Sasa kwa nini unamkimbia? Si umsalimie tu!” Lara akapandisha mabega, kukataa. “Sasa mimi nitaenda kumjibu nini? Unajua siwezi kusema uongo. Na amekaa pale nje ya duka anatia huruma! Jua kali, anatokwa jasho!” “Si aondoke! Wewe mwambie Lara hatarudi hapa leo. Utakuwa hujadanganya maana ni kweli sitarudi. Naondoka zangu sasa hivi.” “Lara! Si umsikilize? Ametoka Dar kwa ajili yako.” “Akuu! Kwani hii ni mara yake ya kwanza kuja kwetu kwa ajili yangu? Si alishakuja mara kadhaa mpaka akaleta na watu? Sasa hivi anakuja kufanya kipi kipya? Naomba mniache kabisa.” Lara akawa mkali kabisa. Mama Chiwanga akatoka hapo akiwaza. Ni mama aliyempenda sana Mungu. Mpole na mnyenyekevu. Hana makuu wala hajui ugomvi.

Akarudi pale dukani. “Mimi naona ungeenda tu ukapumzike baba. Jua kali kweli hapo na naona Lara hatarudi leo hapa.” “Kwani anayo simu? Nisaidie hata namba zake mama yangu. Niliyonayo haipo hewani.” Jax akauliza na kujieleza kinyenyekevu. “Lara hana simu.” Jax akatulia kidogo kama anayefikiria. “Basi nitarudi tena jioni kabla hamjafunga ili nione kama nitaweza kumuona.” Jax akaondoka, mzee Chiwanga kimya. Lara naye akaondoka kabisa pale dukani. Alichukua kabisa mkoba wake akarudi nyumbani.

Jioni kweli Jax akarudi tena pale dukani akiwa na nguo nyingine. Akaonekana alioga na kubadili kabisa. Akafika hapo na kusalimia tena. Alikuta wateja wengi mida hiyo ya jioni. Akakaa hapo akisubiria mpaka walipopungua. “Pole baba, jioni kunakuwa na wateja wengi!” “Ni jambo zuri.” Jax akatulia kidogo kama anayesita kuuliza. Na wao wakamuacha tu.

Mwishoe akauliza. “Sijui Lara amerudi?” “Hapana. Hajarudi.” Akajibiwa tu hivyo, kimya. “Basi naomba nimsubirie.” “Hatarudi tena hapa maana hata sisi tunakaribia kufunga.” Akajibu mama mtu. “Na kesho huwa mnafungua saa ngapi?” “Kesho ni jumapili baba. Tunapumzika. Biashara zote tunafunga.” Akajibiwa hivyo bila hata kukaribishwa nyumbani.

Jax akapoa. Akajua alishafedhehesha hao wazee, hata wao hawataki kumuona tena nyumbani kwao. “Naomba nije kujaribu kumuona nyumbani.” Akamuona yule mama anamwangalia mumewe. “Usiku tunakuwa na ibada.” Akajibu mzee Chiwanga akiendelea na kazi bila hata kumtizama Jax. “Oooh! Sawa. Basi naomba nije kesho kabla sijarudi Dar.” Kimya. Jax akamtizama mama Chiwanga anayefanana na binti zake kama aliyejizaa. “Kesho kanisani baba.” Akajibu kinyenyekevu. “Naweza kuja kabla au baada.” “Sawa.” Hivyo tu akajibiwa bila hata kuambiwa muda. Jax alijua hatakiwi lakini akakusudia.

“Sijui muda gani ni mzuri?” Jax akamuuliza mama Chiwanga. Yule mama akamgeukia tena mumewe. Akawa ni kama anabanwa hana jinsi. Alimjua mumewe na binti zake. Alichukia sana kwa Jax kumkatili binti yake. Hakuwahi kusahau hali aliyorudishwa nayo Lara alipokwenda kuchukuliwa na mama yake akiwa anavuja damu kama aliyekatwa sehemu na akiwa na Tino sio yeye Jax, tena na yeye akiwa na gari! Mzee Chiwanga alimuona ni kijana asiye na hekima na hajui anachotaka.

“Huwa tunakwenda kanisani asubuhi na kurudi mchana.” Yule mama akajibu akionyesha wasiwasi, mzee Chiwanga kimya. “Basi mida ya kwenye saa saba mchana nitakuja tena kujaribu kama naweza kuzungumza naye.” Kimya. “Basi muwe na jioni njema.” “Asante.” Akajibu yule mama akimtizama mumewe ambaye aliongeza shuguli hapo ndani nakushindwa hata kukaa wala kupumua mpaka Jax akaondoka. Hata alipoaga hakumtizama.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kesho yake asubuhi walikwenda kanisani wakarudi familia nzima mpaka mjukuu. Wakati Lara yupo jikoni na dada zake wakipika pamoja na kuzungumza wakicheka na mama yao, Jax akarudi. Lara aliposikia anafunguliwa mlango na Lucas, akakimbilia chumbani. “Sipo humu ndani. Mwambieni sipo na hamjui nitarudi saa ngapi.” Lara akanong’ona na kupotea kabisa pale. Jax alimkuta mzee Chiwanga pale sebuleni, akamsalimia, akaitika, kimya. Mama Chiwanga akajua huyo kijana yupo matatizoni maana alipoondoka jana yake, mzee Chiwanga alimsema vibaya sana.

“Nimekuja kumuona Lara.” “Unataka nini kijana!?” Akaanza mzee Chiwanga kwa ukali. Jax akashituka. “Ni nini unataka kwa Lara tena? Tafadhali zungumza acha kuzunguka nakutufanya sisi wote kama wendawazimu!” Mkewe akakimbilia hapo sebuleni kwa haraka. “Chiwanga! Nakuomba hapa chumbani.” Akasimama kwa hasira. “Labda kabla hamjaondoka, naomba niombe radhi wazazi wangu. Nilikosa sana na najutia kosa. Nipo hapa kwa kuwa nampenda Lara.” “Hilo umegundua lini?” Akauliza mzee Chiwanga kwa hasira.

“Sio wewe ulikuja hapa ukaomba kumuoa Lara?” “Nilikuja mzee wangu.” Jax akajibu kinyenyekevu. “Tulikunyima Lara au tulikubariki na kukukarimu? Hatukukufanya kama kijana wetu hapa?” “Mlifanya yote yaliyo sahihi mimi ndio niliharibu mzee wangu, ndio maana nimerudi baba yangu.” Jax akapiga magoti kabisa. “Kabla hujaomba msamaha, nataka uniambie ni kwa nini ulikuja mwanzoni, halafu kwa nini ukamkataa mwanangu, na kwa nini leo tena upo hapa? Huu ni usumbufu na udhalilishwaji usiomstahili yeyote yule! Ulikuja hapa, ukatudharau ndio maana ukaenda kumtenda mabaya binti yangu!” “Hapana mzee wangu. Nampenda sana Lara, nilikosa tu.” Mzee Chiwanga akarudi.

“Pengine mimi na umri huu uelewa wangu ni wakijinga sana kama unavyonifikiria.” “Hapana mzee wangu. Wewe unahekima na ndio maana nimerudi baba yangu. Ingekuwa ni mzee mwingine hakika nisingerudi, nilikosa tu.” “Ulikosaje Jackson? Ulikosea nini pengine mimi nimeshindwa kuelewa. Hebu wewe unieleweshe. Maana umenitia aibu hapa kwenye jamiii! Umefanya mke wangu adhalilishwe kupita kiasi. Hii nyumba ilikuwa ikijaa wanawake wakija kudai vitu vyao kwa mke wangu! Matusi yalitufuata kila mahali tukawa kama watu tunaotembea bila nguo! Tumemaliza madeni uliyotusababishia, hata hatujapumzika, na wewe unarudi tena! Unataka nini wewe kijana? Umetumwa na shetani wewe!? Umetumwa kutuharib..” “Chiwanga!” Mkewe akamuita kwa upole.

Akamgeukia. “Humu ndani hakuna shetani bwana! Tulia.” “Basi muulize wewe anachotaka ni nini tena baada ya yote aliyofanya! Anataka nini hapa? Maana kama ni msamaha tulishamwambia dada yako, na mwenzio Tino, sisi tumesamehe. Unarudi kutafuta nini?” “Namtaka Lara, mzee wangu. Nilikosa ndio maana nimerudi kuomba msamaha kwenu na kwa Lara. Nakiri nilikosa.” Jax bado alikuwa magotini. Nyumba nzima kimya akisikika mzee akigomba.

“Naomba nieleze ukweli mama yangu. Tafadhali.” Jax akiwa amekunja mikono akamsihi mama Chiwanga aliyeonekana angalau anahuruma. “Kaa baba, tuzungumze.” Akamwambia Jax, na yeye akaenda kukaa. “Nashukuru sana. Nianze kwa ...” “Tafadhali mwambie asiombe radhi.” Akaingilia mzee Chiwanga. “Wewe usiombe radhi. Tueleze kilichotokea Jax. Ulikuja na kuonekana kijana muungwa sana mwanzoni. Mpaka baba alikusifia sana. Ulionekana na hekima, unajua unachokitaka! Lakini ikaja kuwa tofauti kabisa mwanangu! Ilikuaje?” Mama Chiwanga akauliza kwa upendo kama mama.

“Kaa tu. Rudi kukaa tuzungumze.”  Jax akarudi kukaa. “Nilikuwa na msichana tokea nikiwa chuoni. Sisi hatukujaliwa familia mama yangu. Hatukukua kama hivi Lara alivyojaliwa na kukua akilelewa na wazazi na familia inayomzunguka. Na naomba nikuhakikishie siwadharau ila nilipokuja kupaona hapa, ikaniongezea ujasiri wa kuwa na Lara nikijua na mimi nitapata familia.” Jax akaendelea.

“Yule msichana ndio akawa kila kitu changu kwa muda mrefu sana. Kuanzia sina chochote, dada Nelly akinitunza mpaka alipokuja kuondoka nchini. Tukapotezana kwa miaka yote hiyo, akaja kunitafuta wakati ule wa harusi yetu. Sijui niliingiwa na nini wazazi wangu, nikawa ni kama nimechanganyikiwa kabisa. Na Lara ni shahidi, mimi si muhuni. Muulizeni Lara. Sina maadili hata ya utani na watoto wa kike, hajawahi hata kunishuku. Sijawahi kupishana na Lara hata mara moja jinsi nilivyokuwa nikiishi naye kwa amani.”

“Naomba niwe mkweli wazazi wangu nilifanya kosa ila nikiwa najifariji kuwa kwa uzuri wa Lara, hatapoteza muda atapata mwanaume mzuri, ataolewa na kuwa na furaha. Hata nilipokuja kumwambia kuwa naahirisha ndoa, sikujua hata kama ataona shida. Nilijua ni kama atashukuru Mungu.” “Jackson mwanangu! Uliwezaje kufikiria hivyo?” “Kipindi cha mwisho Lara alibadilika, mama. Alibadilika ikawa kama nalazimisha mambo mengi mno mpaka nikamlalamikia Tino, kumbe mwenzangu ni mjamzito! Mimi sijui, nikajua ni kama swala la ndoa anaona ni mzigo na hayupo tayari kwa ndoa. Kwa hakika sikujua kama Lara ni mjamzito na pia kama angejali mimi kumuacha. Kwa kuwa hata nilipokuwa naye mimi, Lara alikuwa akitongozwa sana tu. Sikuwa na wasiwasi.” “Sasa, sasahivi nani amekwambia anashida na wewe?” Mzee Chiwanga akauliza.

“Ulipomkataa alikufuata na kukulazimisha ndoa tena?” “Hapana mzee wangu. Mimi ndio nilimuomba msamaha na kumuomba turudiane.” “Wewe kijana ni mvurugaji na hujui ni nini unataka. Unataka kuoa wanawake wangapi? Unataka kumchukua binti yangu, ukamchanganye tu akili! Hapana. Ondoka.” “Sina mwanamke mwingine tena ila Lara. Mungu wangu ni shahidi baba.” Mpaka akamuita baba.

“Sina nimebakiwa na Lara tu. Yule msichana nimeachana naye mpaka nimempeleka polisi kuwa asije kunifuata tena.” Kidogo wakashituka. “Ninayo mashitaka yake hata kwenye gari. Sina msichana mwingine ila Lara. Na safari hii akinikubali, sitachangisha mtu, namuoa kwa pesa yangu mwenyewe. Niliporudiana tu na yule msichana wa kwanza ndipo nilipogundua kosa kubwa nililofanya. Najua mtasema namrudia Lara kwa sababu kule imeshindikana. Ndiyo ni kweli. Namrudia Lara kwa kuwa tulikuwa na maisha mazuri sana na Lara. Amani, utulivu na kuheshimiana. Lara alinipenda na kuniheshimu sana. Hata nikisema nikaanze kwengine, najua sitampata mwanamke kama Lara, ndio maana ninarudi wazazi wangu. Naombeni mnisamehe. Samahani kwa fedheha kubwa niliyowaingiza. Lakini naomba mnitizame na mimi kama Lucas tafadhali. Kama mtoto wenu tu.” Jax akapiga tena magoti. Nyumba nzima kimya, mpaka dada zake Lara walikuwa wakisikiliza huko jikoni.

“Mimi ni yatima, sina wazazi. Ningekuwa na baba, ningesema aje azungumze na wewe pengine yeye ungemuelewa zaidi au angeongea lugha inayoeleweka. Lakini sina mtetezi hapa duniani ndio maana kwa aibu yote hii bado nimerudi mimi mwenyewe kwenu. Ningekimbia au nisingerudi kabisa, lakini ni kwa vile ninavyompenda Lara. Naombeni msinitupe wazazi wangu. Nipokeeni. Hakika nimejifunza kutokana na makosa. Hamtakaa mkasikia lalamiko lolote kutoka kwa Lara. Hata siku moja. Nimejifunza, nimekoma, na sitarudia tena. Nimebakiwa na Lara tu, na Mungu wangu ni shahidi.” Mpaka Mzee Chiwanga mwenyewe akapoa.

“Mimi nimeelewa Jax. Ila nina swali. Sasa huko ulikomuacha msichana mwingine tena, hayatatokea kama haya tena, ukaamua kurudi kwake na kuomba tena msamaha kama huu?” “Nimemaliza mama. Nimemaliza mama yangu. Naomba niamini mimi sio muhuni. Na ninajua naweza nikaonekana ni kama mtu ambaye sijui ni kitu gani ninataka lakini...” “Na huo ndio wasiwasi wangu kijana. Huo ndio wasiwasi wangu mkubwa sana. Sidhani kama unajua ni kitu gani unataka.” Mzee Chiwanga akarudi kukaa kabisa.

“Muangalie mke wangu.” Jax akamwangalia. “Huyu nipo naye tuna miaka 35 sasa. Unanisikia?” “Nimesikia mzee.” “Tulikaa miaka 5, hashiki mimba, mpaka wazee wakaniambia nioe mwanamke mwingine. Achilia mbali, nimekaa mjini hapa, wanawake wanatongoza wanaume. Wanawake wadogo kabisa, wanatongoza. Zipo sababu nyingi tu za usaliti na wakati mwingine zinasikika zikiwa na maana kabisa zikitetea usaliti wa mtu kutokuwa mwaminifu. Lakini mimi nakwambia na Mungu ananisikia, sio kwamba kwa sababu mwenyewe amekaa hapa, sijawahi.” Mzee Chiwanga akasogea mbele ya kochi kama kuweka msisitizo kwa Jax.

“Sijui mwanamke mwingine mbali ya mke wangu, tokea siku namuona, nakumtongoza, mpaka nimekaa naye hapa. Wanawake wote mbali na mke wangu huyu, ni dada zangu, na mama zangu. Hiyo ndiyo heshima niliyoweka kwa mwanamke niliyemchagua tokea mwanzo. Kwani huyu anatofauti gani na wanae? Mke wangu mzuri bwana! Walihangaika kweli hapa Dodoma wakitaka kuoa mke wangu, lakini sikuwa na wasiwasi, nilijua hawawezi kumtoa kwangu.” Mama Chiwanga akacheka kidogo.

“Wanamtongoza huyu mpaka leo. Muulize. Lakini najua kwa hakika, hakuna mwanamme atamtoa kwangu huyu. Wanamuahidi magari na nyumba nzuri, lakini ametulia kwangu tokea tunatembea na miguu hata baiskeli hatuna. Ametulia, hana papara mke wangu. Tuna nyumba yenye amani, waulize binti zangu. Mpaka wanatuonea wivu! Ni kwakuwa nilijua nini nataka, Mungu akanijalia, nikapokea kwa heshima, nakutulia. Najua watakuwepo huko nje wanawake wengine wenye vigezo vingine, lakini hainihusu mimi. Sijisumbui, kwa kuwa ninaye mwenye vigezo vyangu hapa. Hata mwanamke atembee uchi, hainihusu kwakuwa ninaye wangu mimi.” Mama Chiwanga akajisikia vizuri.

“Lile duka pale ndio utajiri wa kwanza tunakuwa nao hapa ndani. Ndio kitu kikubwa na cha thamani ameshika mke wangu, lakini ukarimu wake siku ya kwanza unakuja hapa na leo ni tofauti?” “Upo vile vile mzee wangu.” “Basi ndivyo walivyo binti zangu wote. Nina ujasiri wakusema hivyo kwakuwa nalea wanangu mimi mwenyewe nikisaidiana na mke wangu. Nawajua binti zangu. Huwa namwambia na kumshukuru mke wangu kila siku, kuniletea mabinti wazuri kama yeye. Tabia zao na mioyo yao pia wapo kama mama yao. Hao binti zangu mimi najisifia kokote kule. Sina daktari humu ndani, wala mwanasheria, lakini napenda sana binti zangu. Tunakaa uswahilini hapa watu wakiishi kwa kusutana, lakini hutasikia wakifuatwa kwa ugomvi hata mara moja. Tokea wanakua mpaka leo wapo hivyohivyo. Mama yao huyu ndiye wakwanza kuja kufuatwa na maneno sababu yako Jackson! Hii nyumba ilikuwa haina kelele. Hata mimi kelele huwa zinaniisha kwa utulivu wao hawa. Wanangu na mke wangu hawana maneno kabisa. Hawajui kumkera mtu. Ndio maana uliniudhi sana ulipomtenda vibaya Lara! Hakustahili hata kidogo.” Mzee Chiwanga akaongea kwa uchungu sana.

“Huyo Lea alileta kijana hapa. Msomi tu. Nilipomuona na kumwangalia kwa kukaa naye hapahapa, nilimwambia wazi kabisa. Huwezi kumuoa binti yangu, utamsumbua sana. Muulize mama yake. Wote walishituka, lakini nilimwambia wazi kabisa. Pesa yake itamzika mwanangu, nikamwambia ni heri nibaki naye hapa, kuliko ahadi alizokuwa akitupa hapa. Na kweli, alipoondoka tu, Lea mwenyewe akanifuata nakunishukuru. Akasema nilimsoma sahihi yule kijana. Hata yeye alikuwa akisita moyoni. Nikijana aliyekuwa amefanikiwa sana, ila amejawa kiburi na majivuno. Sasa kuja kurudishiwa Lara anatokwa damu kama mbuzi aliyechinjwa machinjioni, tena anarudishwa na Tino! Wewe haupo! Nililia mimi, muulize mama yake. Nikajilaumu niliwezaje kuruhusu binti yangu kuangukia kwa kijana katili kama wewe, halafu nikashindwa kukusoma wakati ulikaa hapohapo na mimi nikikutizama!”

“Nililia nikimuuguza Lara kwa uchungu sana. Nikijutia kukukaribisha hapa na kujuta kwa nini nilishindwa kumlinda binti yangu! Leo unarudi tena, ukimtaka binti yangu, si unataka nije niletewe yupo kwenye jeneza! Nimeweka agano na Mungu, binti zangu ndio watanizika. Nimemwambia atanipa binti niwalee na kuwafikisha anakotaka niwafikishe, lakini nimekataa kazi yakuzika binti zangu. Sitazika mtoto wangu hata mmoja. Lakini wewe...” “Hapana Chiwanga. Naomba usimalizie tafadhali. Basi baba.” Akanyamaza na kuondoka kabisa pale. Mkewe akamsindikiza kwa macho ya majonzi.

Alipopotelea chumbani akarudisha macho kwa Jax. “Labda uache baba. Acha mwanangu. Hapa naona imeshindikana. Umemuumiza sana Chiwanga. Hata Lara akikupokea, mtakuwa na mahusiano gani na baba yake?” “Hata hivyo bila baba, Lara hawezi kukupokea shem. Lara ni mziwanda wa baba.” Lea akasogea hapo sebuleni na kuongeza baada ya baba yake kuondoka.

“Mimi naungana na mama, hapa hapatakufaa tena. Heri ukajaribu kuoa tu kwengine. Hata Lara mwenyewe nimezungumza naye, bado anauchungu kama haya mambo yametokea jana. Bado analilia mtoto ambaye hata hakuwa akijua jinsia! Lara hayupo tayari Jax. Kama mmeandikiwa, haitakuwa sasa.” “Daah!” Jax akainama kwa majonzi.

“Naombeni mnisamehe sana. Nisameheni jamani, nimekosa.” Kimya. Wote hawakujibu mpaka Lea mwenyewe aliyeingilia mazungumzo akashindwa kupokea huo msamaha. Akamgeukia mama yao. “Nifanyaje mama?” Jax akaomba ushauri akiwa amepiga magoti. “Mimi naona uache tu Jackson. Muda uje ujibu. Ila usiache kuwa karibu na Mungu. Huko nje shetani atakutesa mwanangu. Shetani anapenda vijana kama nyinyi mlio na maendelea hivyo, anapenda kweli. Anafanya akili zenu zinakuwa kwenye mambo yanayowayumbisha, akitumia nafasi zenu za maisha. Pesa zenu, ujana huo na maendeleo inakuwa ni kivutio chake, inakuwa ngumu kutulia na Mungu. Lakini baba, Mungu yupo. Wakati mwingine anaonekana anachelewa, lakini yupo.” Mama Chiwanga akaongea kwa unyenyekevu.

“Pata muda na Mungu, halafu vuta subira. Unaonekana wewe ni kijana mzuri sana. Unamaendeleo mazuri. Gari hiyo nzuri na watu wanaokuzunguka wanamaendeleo mazuri tu. Ninauhakika utapata mke mzuri tu huko. Au hata huyo uliyemrudia tena baada ya kumuacha Lara, rudi baba. Rudi hukohuko. Pambana na huyo mwenzio mliyeanzana naye tokea zamani kama ulivyosema. Muombee ili na yeye aje kuwa mke mzuri. Huwezi pata mtu mkamilifu Jackson. Hata mimi ninamapungufu yangu, japo Chiwanga amenipamba hapa. Lakini kuna anayoyavumilia. Utahangaika hivi ukienda na kurudi kwenye njia mbili mpaka lini?” Mama yule akaongea kwa upole tu.

“Kile kilichokutoa kwa Lara, na kukurudisha kwa mchumba wako wa zamani, kishikilie baba. Shikilia. Kama kunamapungufu huko kwa mwenzio, muombee huku na wewe ukijifunza kuishi naye. Hutapata mwanamke mkamilifu baba.” “Nimeshampata, ni Lara.” Jax akamkatisha kwa ujasiri, wote wakamwangalia. “Najua mnaweza msinielewe kwa kile nilichofanya, ila kile nimekipata kwa Lara, sijakipata kwa mtu mwingine yeyote yule na ninajua sitakipata kwa mtu mwingine ila Lara, na ndio maana nimerudi. Nimefanya kosa kubwa sana. Najua, ila nimerudi mama yangu. Nimerudi kwa Lara. Hapo ndipo nitarekebisha sio kwingineko.” Jax akasimama.

Akakaa pembezoni mwa kochi kama anayetaka kuondoka. “Nashukuru hata kufunguliwa mlango mama yangu. Najua sikustahili. Hii ni barua ya Lara na hii ni bahasha yake. Naomba mumpe tafadhali.” Jax akasimama na kumkabidhi mama yake. “Sawa. Nitamkabidhi.” “Nashukuru mama. Acha mimi niwahi safari ya kurudi Dar.” “Uwe na safari njema. Mungu akusaidie ufike salama. Nisalimie dada yako. Ni muungwana sana.” Jax akatamani kujua walichozungumza na dada yake mkorofi yule mpaka kuitwa muungwana! “Nitamsalimia mama.” Jax akatoka kimya kimya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Mmmmhhh!” Akasikika mama Chiwanga akivuta pumzi kwa nguvu. Na Lily akatoka jikoni na chakula. Akaanza kupanga kimya kimya. “Lara yuko wapi?” “Chumbani.” Lily akajibu akiendelea kupanga chakula. Kweli binti hao ni watulivu haswa. Akamfuata Lara chumbani. Akamkuta ametulia kitandani. “Ameacha hizi bahasha mbili.” “Akuu! Mimi sizitaki.” “Lara! Umeingiwa na nini?” “Wewe usipokee mama. Mimi sitaki. Jax aliniacha mimi.” Lara akaanza kulia. “Sasa hivi anataka nini? Anataka kunichanganya tu. Usimpokee vitu vyake, mama. Mimi sitaki tena. Nilitulia kwake, akamchagua mwanamke mwingine! Vimeshindikana huko ndio anarudi! Hapana mama. Mimi sitaki.” “Basi tulia usitoneshe huo mkono.” Mama yake akamtuliza akijua bado anahasira. Akatulia na kuondoka na zile bahasha mbili akijua moja ina pesa.

Kwa Nelly.

W

akati Jax yake yakimuendea kombo, yeye Nelly na Billy yao yakawa kwenye mstari. Wakawa wote wanasababu ya kukutana kila siku jioni baada ya kazi kufanya mazoezi kama maandalizi ya kupanda mlima Kilimanjaro. Walipewa aina ya mazoezi yakufanya na kocha wao akiwasimamia. Wakitoka hapo wanakwenda kupata chakula cha pamoja. Ukweli ilimbadilisha Nelly. Ikamuongezea kitu kingine chakufanya mbali na kazi. Akapata mtu mwingine wa kumfikiria mbali na Jax. Huyo Billy.

‘What is greater than God, more evil than the devil, the poor have it, the rich need it, and if you eat it, you'll die?’ Huo ujumbe ukaingia kwenye simu ya Nelly mida ya mchana kutoka kwa Billy. Kisha mwingine ukafuata. ‘Na usiigilizie, Nelly.’ Nelly akacheka baada ya huo ujumbe wa pili kuingia baada ya hicho kitendawili. Nelly alifikiria mpaka akashindwa kufanya kazi, bila kupata jibu. Akaandika kabisa kwa kiswahili. ‘Ni nini kikubwa kumzidi Mungu, kiovu kumzidi shetani mwenyewe, masikini hawana, matajiri hawahitaji, na kama usipokula hicho kitu, utakufa!’ Akili ya Nelly iliendelea kuzunguka mpaka jioni anakutana na Billy.

“Umeharibu siku yangu yote leo!” Nelly akalalamika na kumfanya Billy kucheka sana. “Hamna jibu?” “Mimi mpaka nakuhisi vibaya bwana, Billy! Kitendawili gani hicho?” Billy akazidi kucheka. “Rahisi sana. Wewe kubali kushindwa nikusaidie.” “Nipe hint hata moja.” “Huko ndiko kuigilizia. Kubali kushindwa.” “Ona unavyofurahia kushindwa kwangu leo! Mpaka nguvu ya kukimbia leo imeongezeka!” Billy akazidi kucheka akikimbia kwenye mashine.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment