Ikabidi Nelly akubali kushindwa tu. Kwa kuwa kweli alikosa jibu. “Ni nini jibu lake?” “Nothing.” Ilibidi mpaka Nelly asimame. “No way! Haiwezekani Billy!” Billy akazidi kucheka. “Wewe fikiria tu. Nothing is greater than God, Nothing is more evil than the devil, poor have Nothing, the rich need Nothing, and if you eat Nothing, you'll die.” “Mimi nalia.” Billy alicheka mpaka akasimama na yeye. “Hakika nalia. Hangaika yote ile, siku nzima mpaka nikashindwa kazi kumbe jibu ni rahisi hivyo!” “Tatizo unapenda kufikiria vitu vigumu sana. Wakati mwingine tunapishana na majibu yetu mlangoni wakati tunakwenda kuyatafuta nje.”
“Hakika nimeshindwa. Na hata ungenipa muda kiasi gani, sikuwa hata
karibu na hilo jibu lako. Sawa bwana.” Wakaendelea kuzungumza huku wakifanya
mazoezi mpaka walipomaliza. Walikuwa wamebakisha siku chache tu wote wachukue
likizo fupi, kuelekea Kilimanjaro. Ukweli hata Nelly alikuwa akiitizamia hiyo
safari kwa hamu sana. Kwani hakuwa amechukua likizo kwa muda mrefu! Halafu
safari yenyewe anakwenda na Billy ambaye hajui kumpunja! Akawa anahesabu masaa,
muda ufike.
B |
aada ya siku 10
wakashangaa Jax amerudi tena. Tena safari hii alifika nyumbani siku ya jumamosi
usiku wa saa tatu inaenda saa nne. Waliposikia hodi Lucas mpenda kufungua
milango aliposikia mlango unagongwa tu, akakimbilia mlangoni. “Nani?” Akauliza
Lucas kabla yakufungua. “Mimi Jackson.” Wote wakashangaa na kuangalina. Lara
akanyanyuka kwa haraka na kukimbilia chumbani kwa kunyata. Baba yake kimya.
Lucas akauliza kwa sauti ya juu ya konong’ona. “Nimfungulie au nimwambie
hatupo?” “Fungua bwana Lu, anakusikia!” Bibi yake akamuamuru kwa sauti ya chini
akijua Jax anasikia nje. Lucas
akafungua. “Lara hayupo.” “Jamani Lu! Ni nini baba!? Mgeni hata hajaingia ndani?! Mpishe bwana.”
Lucas akampisha.
Jax akaingia akijua wazi hatakiwi. “Samahanini wazazi wangu, nimekuja
usiku usiku. Nilikosa usafiri wa mapema. Ndio nimeingia mida hiihii na kuamua
kuja angalau niwaone.” “Karibu. Karibu sana.” Lily na Lea wakasimama na
kuondoka pale kumpisha mgeni. Walikuwa wamekaa wakiangalia taarifa ya habari,
ilipoisha zikaanza stori hapo wakiongea huku wakila hapohapo sebuleni. “Kuna
chakula baba. Sijui umeshakula?” Akaongea mama Chiwanga akisimama. “Nitashukuru
mama.” Jax hakujivunga. Mzee Chiwanga kimya baada yakuitika salamu tu,
akanyamaza.
“Pole na majukumu baba yangu.” Jax akaanza taratibu. “Tunashukuru
Mungu. Pole na safari na wewe.” “Asante.” Kidogo Jax akatulia kuona angalau
mazungumzo yake yamepokelewa. Akaletewa chakula. Wali, maharage na mboga za
majani. Akapokea kwa shukurani kweli. “Hapakua na nyama yeyote baba, naona
mpishi wetu ametupikia hivyohivyo! Na sisi ndio tunarudi, tumechoka,
nimeshindwa hata kupika zaidi. Nimeona tule hivyohivyo.” “Usijali mama yangu.
Hiki ni bora kabisa. Nashukuru sana.” Mara ya mwisho anaondoka hapo hata maji
hakukaribishwa. Jax akala bila hata kumuulizia Lara.
Kimya kikaendelea Jax akiendelea kula. Ni tv tu ndiyo ilisikika hapo,
wote kimya. “Lara anaendeleaje na mkono?” Akaanza Jax. “Namsikia ameanza
kumlalamikia baba yake hapa. Naona umeanza kuwashwa. Anataka kutoa, lakini baba
yake anamsihi avute siku kidogo.” “Bado. Walimwambia angalau majuma 6 ndipo
watoe na kupiga tena x-ray wajue kama umeunga.” Jax akajieleza. “Nimemletea na
dawa zake za maumivu.” “Usingesumbuka Jackson mwanangu. Hata simsikii
akilalamika maumivu. Hanywi dawa, na si unamjua alivyo na dawa?” Jax akacheka
kidogo. “Lara muoga kwelikweli wa dawa. Hatazinywa.” “Basi nitaziacha tu.”
Wakatulia akiendelea kula mpaka akamaliza, akataka kuondoa chombo alicholia.
“Usihangaike, huyohuyo Lu aliyekufungulia mlango atatoa vyombo.
Lucas akasikia. Akawa anasogea huku akicheka. “Muone! Wewe mgeni
anakuja, humfungulii mlango bwana!” Bibi yake akamwambia. “Nilitaka kujua kwanza!”
Jax akacheka kidogo. “Haya toa vyombo na hiyo stuli.” “Nikuletee na maji?”
Lucas akamuuliza Jax. “Nitashukuru.” Jax akakubali kila kitu. “Vipi biashara
lakini?” “Tunaendelea vizuri, tunamshukuru Mungu.” “Naona mna eneo zuri kweli!
Pako barabarani.” “Pazuri ila ni garama kweli. Hivi huu mkataba ukiisha,
Chiwanga anataka tuhame pale. Pesa yote inaishia kwenye pango bwana!” “Oooh!
Hiyo ni kweli.” Jax hakutaka kuongeza asije akaharibu.
Akaletewa maji. Akayanywa yote. “Najua usiku umeenda na nyinyi
mmechoka na kazi. Niliona nipite kuwasalimia tu kabla hamjalala. Nashukuru kwa
chakula wazazi wangu.” “Hivyohivyo chakulamba lamba.” “Inatosha.” Jax akatulia
akisugua mikono akionekana amejawa wasiwasi. Kimya. Hakuna hata
aliyemuongelesha tena. “Naweza kuzungumza na Lara?” Akamuona mama Chiwanga
anamuangalia mumewe ambaye alikuwa kimya muda wote, macho kwenye luninga.
Kimya. “Hata hivyo Lara mwenyewe alikuwa chumbani. Sijui atakuwa amelala!” Akaona
ajibu mama Chiwanga na kuongeza. “Lea mama mazazi, niangalizie Lara. Mwambie
Jax yupo.” Akaongea mama yao taratibu kama kawaida yake.
Baada ya muda Lea akarudisha jibu. “Lara amelala, mama.” Wote wakijua
ni uongo, Jax akawa mstaarabu. “Basi nitarudi tena kesho kumwangalia mida
ileile mkishatoka kanisani, kabla sijaondoka.” “Sawa baba. Karibu, na uwe na usiku
mwema.” Jax akasimama na kuaga kwa heshima, akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake tena walipotoka kanisani walikaa kama dakika 20 tu, Jax akarudi
tena. Safari hii alikuja na taksii yenye vyakula. Alionekana ametoka kununua
vyakula. “Usingehangaika baba.” “Sio usumbufu hata kidogo. Vyote nimepata
sehemu moja, pamoja na huu usafiri.” Wakasaidiana na dada zake Lara, wakaingiza
vyakula vyote walivyoleta, ndani. “Asante.” Wakashukuru hao kina shemeji.
“Karibu.” Jax akarudi sebuleni ambako alijua ndipo anatakiwa akae hapo,
hakumkuta mzee Chiwanga. Ikawa hivyohivyo. Lara alishakimbia kabisa hapo
nyumbani kwao. Jax anagonga mlango wa mbele, yeye akatokea mlango wa nyuma kwa
haraka. Jax akala chakula. Akasubiri bila kuchoka akijua pengine Lara atarudi,
lakini wapi.
“Inabidi niondoke tu. Lasivyo nitaachwa na ndege.” Jax aliongea macho
kwenye saa yake ya mkononi akiwa amebakiwa na mama Chiwanga tu hapo sebuleni.
Hata binti zake waliingia chumbani baada ya kula. Mzee Chiwanga ndio hata
hakutoka hata kwa chakula. “Basi uwe na safari njema.” Ndilo aliloweza
kuzungumza mama Chiwanga. “Naomba nikuachie bahasha ya Lara.” “Naomba niwe
mkweli Jax. Hizo bahasha Lara hapokei. Hata zile za mwanzoni ninazo, hakupokea.
Nashauri uache tu mwanangu. Unapoteza hizo pesa za nauli za kuja huku bure,
wakati hiyo pesa yako ungefanyia kitu cha maana. Lara hayupo tayari kwa
mazungumzo.” Mama Chiwanga akamuhurumia.
Jax akafikiria kidogo akiwa ameinama. “Mimi namuelewa kabisa Lara.
Najua ni ngumu kwa vile tulivyokuwa tukiishi mpaka kumbadilikia!” Jax akawa
kama anawaza. “Najua nimemuumiza sana Lara. Natamani hata na mimi nisiwe narudi
mama yangu niwaache mpumzike, lakini nashindwa. Kila siku ikipita, ndivyo
ninavyoona jinsi nilivyopoteza kitu cha thamani mashaini. Najuta mama, najuta
sana.” Mama Chiwanga kimya. “Natamani anipe nafasi nyingine. Hata asifanye
chochote kile. Mimi nitahangaika na kila kitu.” Jax akaendelea taratibu. Kimya,
mama Chiwanga akishindwa chakusema tena.
“Basi naomba nikuombe kitu kingine mama yangu.” “Karibu.” “Nitunzie
tu hizi barua. Naomba zitunze tu, ila umwambie nimeacha na leo. Ajue tu, halafu
uzitunze.” “Sawa Jackson mwanangu.” Safari hii ilikuwa bahasha moja tu.
Akapokea. Jax akashukuru na kuondoka.
Ya Nelly.
Mara ya Tatu.
W |
aliondoka
jijini Dar kuelekea Kilimanjaro wote wakiwa na furaha na wakitizamia kuupanda
huo mlima siku inayofuata. Walitaka kubakiza siku nyingi baada ya kupanda ili kupata
muda wakutosha kupumzika kabla ya kurudi kazini. Sasa kampuni waliyoitumia ya
utalii kupanda huko mlimani walipojua ni mwanamke na mwanaume na wanapanda
pamoja, swala la vyumba viwili wakalipuuza na kuwatafutia chumba kimoja.
Billy na Nelly wanatua uwanja wa ndege na kupelekwa hotelini,
wakajikuta na chumba kimoja. Billy akapaniki, Nelly akimwangalia. “Hakika nili
book vyumba viwili. Nafikiri tumekuja msimu ambao watalii ni wengi, wameishiwa
vyumba. Acha niulize kama tunaweza pata kingine.” Nelly kimya. Billy
akahangaika mpaka akachoka. Ikabakia chaguzi ya kuhama hoteli. Ambako huko
angepata chumba kimoja. Kwamba iwe yeye au Nelly ndio akahamie huko.
“Tafadhali usinifikirie vibaya.” “Wewe mwenyewe uliniambia kuna mambo
unaweza kuyabadili, ukiwa na maana kuwa, una control nayo na mengine hata ukiwa
na pesa, yapo nje ya uwezo wako. Naomba tulia Billy. Mimi nakuamini.” “Sitaki
uone kama nataka ku take advantaje ya hii hali.” “Hapana. Naomba tulia. Usiharibu
safari tuliyojiandaa kwa muda mrefu, ikaonekena kama mbaya wakati ni malazi ya
usiku mmoja tu! Mimi hata kwenye kochi nitalala, ilimradi kesho tuamke na
furaha tukiwa na nguvu ya kwenda mlimani.” Hilo likamtuliza Billy ambaye ni
bwana mipango. Na hata ajira yake ni mipango. Kwa hiyo alitaka kila kitu,
wakati wote kiwe kwenye utaratibu fulani, akakutana na Nelly, maisha yake
mwenyewe hayakuwa kwenye mipango. Amefika hapo kwa kupambana.
Wakapewa kadi ya chumba, wakaelekea chumbani. Kilichomshangaza Billy
ni vile Nelly jeuri alivyo. Hakutegemea. “Unataka nikusaidie nini, chakutoa
kwenye mizigo yako na kupanga hapa nje kwa muda huu mpaka tunapoondoka kesho?”
Billy akajidai akifikiria kumbe anashangaa kule kujaliwa. Hakuishi na mwanamke
kwa muda mrefu, kwa hiyo vitu vingi
alikuwa akijifanyia mwenyewe. “Sabuni za kuogea, lotion, mafuta ya nywele, nguo
za jioni hii, nguo za kulali, na vitu kama hivyo. Ili usisumbuke kuanza kuvitoa
kimoja kimoja.” Nelly akampa wazo akiwa ameshaweka mizigo yake pembeni.
“Nashukuru, Nelly. Ila naona nipo sawa. Nisikusumbue. Najua na wewe
utataka kupangilia vya kwako.” “Basi mwenzio jinsi ninavyoweka vitu vyangu,
nilimfundisha mpaka Jax. Anasema akisafiri hapati shida kabisa. Naweka mizigo
yangu kwa siku, na matumizi. Hapa nikiangalia kila mkoba wangu najua ni wasiku
gani na wakati gani. Kuna ambayo sitafungua hapa mpaka mlimani na kuna ambayo
sitagusa mpaka siku narudi.” “Haiwezekani Nelly!” “Kabisa. Mimi sipendi mtindo
eti unatafuta mswaki kwenye kila mzigo! Au eti nguo ya kulalia unaisaka mpaka
unamwaga mizigo yote! Hapana. Huwa naweka vitu vyangu kwa mpangilio na sipati
shida. Na nyumbani hivyohivyo. Kila mahali. Siwezi nikawa jikoni eti natafuta
kisu mpaka hamu yakupika iishe! Unafungua kila kabadi na droo! Hapana. Na kila mfanyakazi
anayefanya kazi kwangu sharti la kwanza ni asichanganye vitu. Ni bora aniachie
hapo, nije nipange mwenyewe kuliko nianze kukuta vijiko kwenye visu au mashati
kwenye sketi au suruali! Hapana. Kwa hiyo mimi sina shida na wala sihitaji
nafasi yote hii. Sehemu kidogo tu inanitosha.” “Umenifanya nijutie chumba
changu.” Nelly alicheka sana.
“Kweli. Mimi nikianza kutafuta soksi hapa, mpaka jasho linanitoka.
Naweza kukuta ipo moja, ingine niliacha nyumbani, naanza kununua tena.” Nelly
akazidi kucheka. “Kama hapa umenikumbusha nguo za kulalia, sidhani kama
nilibeba.” “Jamani Billy!” “Maadamu tunalala wote, bora nijisalimishe tu. Na
huo ndio ugonjwa wangu. Sasa nikiwa peke yangu sina shida, nalala tu na boxer.”
“Nipe mizigo yako nikupangie vizuri na kinachopungua, tukanunue.” “Hapo
utanisaidia.” Nelly akatoa vitu vyake vyote na kuweka kitandani. Akaanza kwa
kuweka vinavyotakiwa kuwa pamoja na kutafuta wenza. Na kweli vingine vilikuwa
kimojakimoja, kama soksi. Akamuwekea huku akiandika vitu anavyohitaji kununua
kabla ya kesho yake ndipo wakatoka kwa manunuzi.
Walishanunuliwa vitu vya kuvaa huko mlimani. Kama kawaida ya Billy,
alishalipia kila kitu. Alichofanya Nelly ni kuongeza tu. Walizunguka na taksii,
wakaishia kurudi na chakula chumbani. “Katangulie kuoga wakati naandaa chakula,
ukitoka ule.” “Nataka tule pamoja Nelly. Nipo na wewe hapa, unataka niendeleze
maisha ya upweke tena!?” “Basi utanisubiri.” Akaenda bafani na kutoka na taulo.
“Eti natamani ingekuwa tofauti nikwambie twende tukaoge wote,
tukitoka tunatoka pamoja na kula pamoja.” Nelly alibaki ameduaa kama asiyejua
aseme nini. “Basi acha tu nitangulie. Samahani, sijui naongea nini!” Akarudi
bafuni na kumuacha Nelly amesimama na mshangao.
Alitoka kuoga na Nelly akaingia bila ya kusemeshana. Ni kama ikapita
hali fulani hivi, ya tofauti. Hata wakati wa kula kukawa na hali ya ukimya. “Samahani
Nelly. Sikukusudia kukunyima raha.” “Hata kidogo. Sema sikuwa nimetegemea.” “Ni
kitu cha ajabu eeh!?” “Sidhani, ila kwangu ni kigeni kwa sababu sijawahi.”
Nelly akafikiria kidogo. “Najua kuna mambo fulani unaweza kufikiria naweza
nikawa na uelewa nayo au ukashangaa ni kama sifanyi, ni kama nilivyokwambia
Billy. Mimi sipo kama wanawake wengine. Ndio maana nilikushauri utafute
mwanamke ambaye anaweza kukufaa. Mimi najijua. Sipo sawa.” “Nahisi
nimeshachelewa. Nimekuzoea Nelly.” “Hata mimi nimeanza kukuzoea. Ila natamani
upate kitu kizuri. Mimi sina huo uwezo. Na sitaki upoteze muda kwangu.” Billy
akanyamaza.
Wakamalizia kula. Wote wakaenda kusafisha kinywa kwa ajili ya kuwahi
kulala kwa safari ya kesho. “Ungependa tulalaje?” Ni swali lililomfanya Nelly
aanze kufikiria hapo sehemu ya bafuni. Akajisafisha mdomo vizuri na kuweka
mswaki pembeni. “Lakini mimi naweza hata kulala kwenye kochi Billy. Haina
shida.” “Ni sawa tukilala wote kitandani? Sitaki ulale kwenye kochi na mimi
siwezi kulala kwenye kochi wala chini. Unafikiri kutakuwa na shida?” “Hata
kidogo. Nitafurahi.” Wakacheka na kurudi chumbani.
Walizima kila kitu na wote wakaingia kitandani. “Eti nimefurahi!”
“Nini sasa?” Nelly akamuuliza akicheka. “Tunalala wote.” “Ujue Billy wewe una
mambo ya ajabu!” “Mimi napendwa kupenda Nelly. Wala sitakudanganya na ndio
maana sitaki kuwa mnafiki wakujidai eti nitakufa peke yangu! Hapana. Kwa nini
iwe hivyo!?” “Natamani huo moyo!” “Hakika wawili ni bora kuliko peke yako. Wewe
hufurahii huu wakati tunokuwa nao?” “Nikwambie ukweli Billy?” “Nakusikiliza.”
“Sikujua kama utanibadili kwa kiasi hichi! Sikumbuki kucheka kwa kiasi hiki
maishani. Umenifanya akili zangu kuwa busy, sijifikirii sana kama zamani. Na
najiona hata uchungu unapungua.” “Hata mimi mwenyewe nakufurahia Nelly. Sana. Hapa
nilikuwa nikifikiria tunafanyaje baada ya kumalizia hizo mara nne! Nimepata sababu
ya kutizamia weekend zangu, nikijua nitakuwa na Nelly.” Wakanyamaza.
“Njoo huku karibu ulale nikiwa nimekukumbatia.” Nelly akajisogeza ila
akampa mgongo. Akamsikia pumzi zake shingoni. “Unanukia vizuri!” “Asante. Hata
wewe huwa unanukia vizuri Billy. Mpaka baada ya mazoezi huwa unanukia vizuri!”
“Mimi nina very sensitive sense of smell. Yaani kuna weza kukawa na
harufu mahali, wote msiipate, mimi nikawa wakwanza kuipata. Kwa hiyo najitahidi
sana kwenye swala la harufu. Na pia sio mzembe, nawekeza kwenye harufu nzuri.” “Ndio
maana mpaka nguo zako zinanukia!” “Nguo zangu hazifuliwi na kila sabuni Nelly,
na huwa najua. Nikishasikia inaharufu ya tofauti, sivai. Na ndio maana huwa
sivai vitu vipya mpaka vifuliwe kwanza. Si umeona nimenunua na kutafuta na
sabuni pia?” “Na kuweka msisitizo huyo mtu atakayefua hapa hotelini ni lazima
atumie hiyo sabuni pamoja na fabric softerner yake!” Billy akacheka.
“Kumbe pale mapokezi ulikuwa ukinisikiliza?” “Sana tu.” Wakacheka.
“Ndivyo nilivyo. Utanizoea tu, usinikimbie sababu ya hilo. Nateswa sana na
harufu.” “Sio sifa mbaya. Uchafu ndio kitu kibaya.” “Ila na wewe huwa unanukia
vizuri Nelly. Sijakusikia ukitoa harufu mbaya.” Nelly akacheka. “Kwa hiyo
ungenisikia ungeniambia?” Billy akacheka sana, ila hakujibu hilo.
Kwa mara ya kwanza Nelly akalala mikononi mwa mwanaume akiwa
amekumbatiwa vizuri. Hata hakugeuka ili asimsumbue Billy. Akajituliza akimsikia
alivyolala vizuri nyuma ya mgongo wake na kuhema taratibu. Ile hali
ilimfurahisha sana Nelly. Asubuhi waliamka, Billy akalala chali na kumtaka
amkumbatie kifuati. “Billy!” “Njoo acha kujishauri. Huwezi pata bahati kama
hii.” Nelly alicheka sana. “Billy wewe!” “Usifikiri nipo na wewe hapa kucheza,
Nelly. Nikikwambia nakufurahia, naomba uelewe. Ukija kumzoea huyo binti yangu
mkubwa, atakwambia. Mimi si mtu wa kila aina ya mwanamke. Hakika nakufurahia
Nelly. Tukiachana huwa nafikiria ni wakati gani tutakutana tena.”
“Sasa unafurahia huu ukorofi wangu!?” “Wewe si mkorofi. Ila
uliumizwa, ukashindwa kuachilia. Ndicho kilichokuwa kikikutesa. Nipo na wewe
hapa nikiwa sina hofu ya Billson kama Director of Strategy wa World bank
ila Billson kama mimi mwenyewe. Kwa kuwa huyo Director of Strategy wa
World Bank ulishamfukuza tokea mwanzo.” Nelly alicheka mpaka akajifunika.
“Nelly! Hakika sijakupatia mwenzio.” Nelly akazidi kucheka ndani ya
mashuka. “Hivi sasa ulishasamehe?” “Ndicho kilichonitia hamu ya kukufahamu
zaidi. Pengine ungekubali siku ile usingekuwa hapa na mimi leo, japo nakiri
ulivutia sana macho yangu. Ulivaa nadhifu mno. Umbile lako likaonekana vizuri sana.
Sasa alipoongeza Jax kwenye neno la shukurani, nikajiambia lazima nikufahamu
zaidi.” “Mimi huwa najua wanaume ni waharibifu tu, bwana!” “Sio wote.” “Sijui.
Ila wengi niliokutana nao mimi ni waharibifu ndio maana hata Jax aliniudhi
sana. Japokuwa nilimlea mwenyewe, lakini eti na yeye akaungana na wengine
kunithibitishia ukweli niliokuwa nao! Hakika iliniuma sana.”
“Sasa yeye ulimpa adhabu gani?” “Naona aliamua kujisalimisha mwenyewe
na kuniambia kwa vitendo kuwa si wanaume wote wapo hivyo. Amekosa na hatarudia
kosa. Mpaka namuhurumia! Amerudi kuishi pale makusudi na anatunza muda kama
mtoto anayebalee!” Billy akacheka sana. “Yupo nyumbani kwa wakati, na anajali
huyo! Sijawahi ona. Najua hapa atakuwa amenitumia ujumbe kutaka kujua kama
nililala na kuamka salama. Halafu nahisi, sina uhakika, nahisi anahangaika kumrudia
Lara, ila naona hajafanikiwa.” “Lara mchumba aliyemuacha?” “Mpuuzi sana Jax. Lakini
nahisi Lara amemkataa. Ameniambia rafiki yake, Tino. Inamuuma sana Jax. Ila
nimemuacha katika hili arekebishe mwenyewe. Pengine yeye atajifunza mapema
kuthamini vitu vya thamani asiwe kama baba.” Akamuona mpaka amebadilika.
“Mimi naenda kuoga.” “Acha bwana Nelly! Usiumizwe na maisha ya nyuma
kiasi chakushindwa kuishi leo.” “Mimi nipo hapa na wewe Billy. Sijashindwa
ku..” Ukanyamaza. “Unashindwa kuchukua hatua Nelly. Una kusitasita kwingi sana.
Jax si baba yako na mimi si baba yako. Kuna makosa yanatokea, lakini hayamfanyi
mtu kuwa hivyo. Mimi nina makosa yangu pengine nilichangia kuvunjika kwenye
ndoa yangu. Lakini..” “Makosa gani?” Nelly akauliza kwa haraka.
“Katika malalamishi yake makubwa niliyomsikia wakili wangu akisema ni
kutanguliza kazi kuliko familia.” “Kivipi?” “Alisema ninafanya sana kazi kuliko
kuwepo kwenye maisha yao. Kwamba hata nikiwepo nyumbani nakuwa kazini.” “Ni
kweli?” “Ndiyo. Lakini unakumbuka nilikwambia ni kwa wakati ule nikitaka
kujitengenezea jina?” “Sasa na yeye..” “Nilimwambia Nelly. Tena kwa
kurudiarudia. Mbaya zaidi garama zetu za maisha zilikuwa juu sana, ilibidi
kufanya kazi kwa bidii ili kuwafanya waishi vizuri. Na nilitaka kulipia ile
nyumba mapema nikiwa na nguvu, ndipo nikusanye sasa pesa za kustaafia. Tuje
tupumzike uzeeni! Kumbe mwenzangu yeye alikuwa akipumzika na Carlos!” “Kwani
Carlos hakuwa na majukumu mengi?” Billy akafikiria.
“Sijui nikwambie nini juu yake. Carlos ni wale watu wasiopenda makuu
tokea tupo wadogo. Alizaliwa na wazazi wenye uwezo, kama mimi, akaridhika na
utajiri wa kwao. Hata hakwenda chuo kikuu ila chuo cha miaka miwili tu. Ni mtu
ambaye anapenda maisha ya kawaida. Hana ndoto kubwa sana. Ale vizuri, alale
pazuri, basi. Sasa wanawake wazuri, wanao jielewa hawapendi wanaume kama vile
yeye asiye na mikakati, ndio akaishia kwa familia yangu, mpuuzi mkubwa yule.”
Billy akakaa vizuri, Nelly akajua hasira zinaanza kumpanda.
“Yaani wakati mimi nakuja kuoa huku Africa, nilimwambia kabisa. Akasema
yeye hadhani kama ni jambo la busara kutoa mwanamke huku. Itachukua muda mrefu kumfanya
aendane na sisi, alingane na maisha yetu ya kule. Halafu leo ndio nimekumbuka.”
Akazidi kuwaka. Nelly akajua hiyo siku imeanza vibaya tayari. “Eti akaongeza
wasiwasi wa hichi alichonifanyia yeye. Eti iweje akubali nimuoe ili tu aje
aishi nchini Uswiz tu na mali, halafu akishazoea anibadilikie iwe sio mapenzi
ya kweli! Mchezi yule yeye ndio akafanya kilekile! Akanipora mke wangu!”
“Pole Billy. Pole sana. Ila naomba utulie. Umeshapandisha hasira. Unahitaji
akili na nguvu tulivu kwa ajili ya safari yetu leo. Acha mimi nitangulie
bafuni.” Nelly akaona atoke hapo kitandani kwani Billy alishabadilisha ile hali
tulivu pale.
Na yeye Billy akajishitukia maana alimtamka Anele kama bado mkewe. Akajua
amempa uthibitisho wa hofu aliyomwambia anayo juu yake na mkewe, wakati wapo
kwenye ndege wakielekea Afrika ya kusini. Akabaki pale kitandani akijaribu
kukumbuka kwa makini kile alichoulizwa na Nelly wakiwa kwenye ndege ili akitoka
hapo bafuni atengeneze. ‘Kwa jinsi ulivyompenda Anele. Amekuzalia watoto
unaowapenda hivyo. Akakupitisha alikokupitisha mpaka ukaumia kwa kiasi hicho,
unafikiri unaweza kuja kumpenda mtu mwingine kwa kiasi hichohicho?’ Billy
alikumbuka neno kwa neno mpaka akakaa kwa hofu. Akakumbuka jinsi alivyokanusha
kwa maneno ya busara. Lakini asubuhi hiyo akajikuta akilalamikia juu ya kuporwa
mke wake na wala si mzazi mwenzie au aliyekuwa mkewe. “Oooh No!” Billy
akahamaki kwa sauti na kujua ameshaharibu.
Nelly alipotoka kuoga akamuwahi. “Naomba uelewe, kinachoniuma si
Anele, ni binti yangu. Amenipokonya na mtoto wangu pia!” Akajaribu kusawazisha.
“Hata kwa Anele inaeleweka kabisa. Alikuwa mwanamke uliyempenda ndio maana
ukamuoa. Amekuzalia binti wazuri wawili, hakuna jinsi ya kuwa sawa juu ya hilo,
na hakuna mwanamke anaweza kushindana na hilo.” Hapo ndipo Billy akajua amesharibu
kwa hakika. Nelly akaendelea kujiandaa. Akaona na yeye asiongeze neno zaidi,
akaoge tu.
Huku nyuma mtu wa kufua wa hapo hotelini akagonga kuleta nguo mpya za Bill alizotaka zifuliwe kabla hajavaa. Na kweli aliletewa zikiwa na harufu nzuri. Nelly akazipokea na kuziweka kitandani. Billy alitoka akijikausha. “Wameleta nguo zako. Ila nimewaambia kama utakuwa hujaridhika, nitawapigia waje wachukue warudie tena.” “Nafikiri itatosha. Muda wa kuja kuchukuliwa umefika. Nataka tule kabla hatujaondoka.” “Sawa.” Nelly akachukua simu yake. “Acha nizungumze na Jax kabla hatujaondoka. Naona amesahau kama mimi ni dada yake sio mtoto. Ameanza wasiwasi wa makoti, soksi nzito sijui na skafu.” Billy akacheka. “Mwambie tuna kila kitu. Utakuwa sawa.” Nelly akatoka nje kabisa kwenda kuzungumza na Jax, lakini Billy alimuona amebadilika. Siye Nelly aliyeamka asubuhi hiyo mpaka akahisi hiyo simu angeweza kuzungumza hapohapo ila anamkwepa tu.
MLIMA KILIMANJARO.
K |
ulikuwa na
utulivu wa namna yake hata walipokuwa huko mlimani wakipanda mlima. Nelly
alitulia sana. Sura yake ilitulia mno. Si ile ya ukorofi ila akawa kama mtu
aliyetingwa na mawazo. Billy alijaribu kumuongeleza mara kadhaa, na kupewa
majibu ya jumla ila matulivu tu bila jazba. Hawakutaka kuharakisha kupanda. Na
kwa kuwa pesa ilikuwepo, wao walichukua safari ndefu ya siku 8 kufika kileleni,
UHURU PEAK, kwa kutumia njia ya Lemosho, kitu kilichofanya wafikie lengo,
kufika kileleni japo ni kweli pesa ilimtoka Billy.
“Billy.” Nelly akamuita wakati
wanapumzika siku ya nne. “Nimezungumza na huyu anayetusindikiza. Nimejua hii
safari imekugarimu sana. Na najua umeshalipia. Tafadhali niruhusu kukufidia
garama zangu.” Billy akabaki akimtizama. “Mimi nina pesa Billy. Matumizi yangu
ni mimi tu, sina majukumu hata yakumnunulia mtu soksi. Acha nikufidie.”
“Unaogopa kuingia kwenye kundi la Anele?” Ikawa kama Billy amemgundua.
“Namlalamikia Anele kwa kuwa amenitenda vibaya, Nelly. Sio kwa ajili ya pesa
nilizotumia kwake. Halafu wewe hujaniomba, nimeamua mwenyewe. Wewe si nusu ya
Anele.” “Unajuaje?” “Kwa hiyo huo ndio wasiwasi wako?” “Mimi ninachotaka
kukwambia ni kuwa, ninayo pesa na sina majukumu. Hii safari nimeifurahia sana
ila ni garama! Hakuna sababu ya wewe kugaramia peke yako wakati na mimi pesa ni
nayo na inaendelea kuingia. Ni hilo tu Billy. Na sina nia ya kukuudhi au
kukuumiza.”
“Na mimi ninayo pesa. Na nimeamua kuitumia kwa namna hii. Tafadhali
naomba usijilinganishe na Anele. Nimekosea kumleta katikati yetu, tena kwa siku
kama ile ambayo tuliamka vizuri. Lakini kam anilivyokwambia, mtoto wangu ndiye anayeniuma
Nelly. Mke naweza pata mwingine, lakini kwa umri huu napata wapi mtoto
mwingine?” Hapo Nelly hakujibu. Wakatulia kidogo. Nelly akaona aage. “Acha nikalale.
Usiku mwema Billy.” “Na wewe.” Hiyo siku nayo ikaisha hivyo. Nelly akaenda
kulala kwenye hema yake na kumuacha hapo. Billy akaona amuache tu.
Siku ya nane walifika kileleni, wakapiga picha za kutosha tu na
kupewa certificate zao, kila mmoja wao akafurahia na safari ya kurudi
ikaanza. Ilichukua tena siku mbili tu kurudi hotelini. Walifika mida ya jioni
hotelini. Nelly alitangulia kuoga. Akaja Billy. Wote walikuwa wakitamani tu
kitanda. Wakaagiza chakula kiwafuate hapohapo chumbani. Wakala na kujitupa
kitandani wote kama wafu. Hakuna aliyekuwa na habari na mwenzie mpaka asubuhi
Billy alipomsikia Nelly bafuni akioga. Akabaki amejilaza tu kitandani.
Trouble in Paradise.
Tamu Yaingia Shubiri.
Nelly alitoka, akaanza kuvaa. Alipomaliza, akamuona amejitengeneza
vizuri na kutoka taratibu kama asiyetaka kumuamsha. Baada ya muda akamuona
amerudi tena hapo chumbani. Macho yakagongana na Billy pale kitandani. “Billy?”
Billy akamtizama akiwa bado amejilaza hapo kitandani. “Nashukuru kwa wakati
mzuri niliopata tukiwa wote.” “Ooohooo! Mbona kama naagwa moja kwa moja?” Nelly
akacheka taratibu na kuendelea. “Umenisaidia kunifungua akili na moyo kuwa
naweza kuwa na furaha, na maisha sio mabaya hivyo. Ila naomba safari yetu mimi
na wewe iishie hapa.” Billy akabaki tu kimya.
“Naomba mimi niondoke leo, nikamalizie likizo yangu nyumbani kwangu
na Jax. Nahisi ananihitaji sana sasa hivi. Nahofia asije kuharibikiwa na mimi
nikishindwa kumsaidia. Ni hilo tu.” “Labda niulize kwa nini umeamua kuhitimisha
kwa haraka?” “Binafsi sioni kama ni haraka. Tumekuwa na wakati mzuri zaidi ya
tulivyopanga. Na nafikiri na wewe ulimaanisha uliposema ulifurahia. Halafu Billy,
mimi sijioni kama ni mtu sahihi kwako.” “Kwa nini?” “Unakumbuka nilikwambia
nilikuwa nashindwa hata kujitizama kwenye kioo baada ya kufanya mapenzi na
mjomba?” “Nakumbuka.” “Si kwa sababu alikuwa mjomba wangu. Ni kwa sababu
alikuwa mume wa mtu. Kitendo cha kujua anaye mke nyumbani na mimi nalala naye,
kilikuwa kikinimaliza mno. Ndivyo ilivyo kwako.” “Lakini mimi si mume wa mtu,
Nelly!” Billy akashangaa sana mpaka akakaa.
“Kwenye makaratasi si mume wa
Anele. Lakini bado moyo wako umeunganishwa naye, sioni kama unayo nafasi kwa
mtu mwingine, Billy.” Nelly akaendelea. “Anele ni mwanamke inaonekana ulimpenda
sana na umeshindwa kumuacha. Bado unamlalamikia Carlos kukupokonya mke wako na
si aliyekuwa mke wako.” Billy akakunja uso.
“Inawezekana wewe hujajisikiliza, ila mimi nakusikiliza Billy. Moyo
wako hauna nafasi ya mtu mwingine, na hata kama unayo, mimi si mtu sahihi kwako.
Sitaweza. Utanimaliza kabisa. Sitaweza kuishi kwenye hiyo hali. Katikati yako
wewe na Anele! Hakika sitaweza Billy. Samahani, lakini mimi sio mtoto mdogo au
binti mdogo. Siwezi kupoteza muda zaidi. Naomba mimi niondoke, kabla
hatujaharibu chochote kilichotokea kati yetu.” Billy akachoka kabisa.
“Nimepata ndege na usafiri wa kunipeleka KIA. Naomba nikuache
upumzike na mimi nikapumzike kabla sijarudi kazini.” “Unaondoka Nelly?” “Kabisa
Billy. Naondoka. Na ninaomba tukubaliane hivyo. Naijua nguvu ya mapenzi kwa
kuiona kwa watu, hata kwa Jax. Linapokuwepo penzi mahali, halivunjwi kwa
kuandikishana kisheria. Upendo upo na nguvu ya ajabu sana.” Nelly akajiweka
sawa. “Billy, Jax alivunja uchumba uliokuwa umebakisha siku chache ifungwe ndoa!
Eti sababu ya mwanamke anayempenda kurudi kwenye maisha yake! Alimuacha binti
mzuri sana, tena akiwa mjamzito! Yule binti aliachwa na hali mbaya sana Billy. Sitaki
kuja kufika pale. Mimi sina nafasi hiyo.” Nelly aliongea taratibu tu kama
aliyekwisha kufikiria na kufikia hayo maamuzi.
“Sasa hivi Jax anajutia kuvunja uchumba na binti mzuri, akijilaumu
sana. Lakini mimi najua ni mapenzi tu. Msichana aliyemrudia kama angetulia na
hakuwa amerudi sababu ya pesa ya Jax, nina uhakika kwa asilimia 100, Jax
asingerudi tena kwa Lara. Anarudi kwa Lara kwa sababu upendo wake wa dhati kwa
yule binti wa kwanza, umeshindwa kupokelewa. Inamaana Tula angejishusha kidogo
tu na kumdanganya Jax, Jax asingerudi kwa Lara kabisa. Angesamehe pesa, muda,
mtoto na mapenzi ya Lara sababu ya mapenzi ya kweli aliyonayo kwa Tula.
Nimekataa kuwa Lara, au mama yangu, kwa yeyote yule.” “Na hiyo ndio hofu yako.”
Akamalizia Billy.
“Sijui Billy, lakini sidhani kama niliumbwa kuwa mtumwa wa mapenzi.
Hapana. Ni rahisi kuwa peke yangu na maisha yakiendelea, kuliko ile hali
niliyokuwa nikiiona kwa mama yangu na kwa Lara mara baada ya kuachwa na Jax!
Hapana Billy. Sidhani kama hata nastahili kulipa hiyo garama kwa yeyote yule.
Sitaki na sipo tayari.” Kama utani tu, Nelly akachukua mizigo yake, alikuwa
amerudi na gari ya kubebea mizigo ameacha nje ya mlango. Akapandisha mizigo
yake yote. Akarudi pale alipokuwa amerudi kujilaza Billy. Akazunguka kabisa
kwenye ule upande aliokuwa amejilaza. Akainama na kumbusu shavuni. “Nakushukuru
sana Billy. Asante. Uwe na mapumziko mema.” Nelly akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment