Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Chozi Langu! - SEHEMU YA 2. - Naomi Simulizi

Chozi Langu! - SEHEMU YA 2.

Mpaka inafika siku ya alhamisi hali ya Lara ikazidi kuwa mbaya ikambidi Sesi kumpigia mama yake Lara simu na kumuomba afike hapo mapema hata kabla ya siku ya harusi. Hata hivyo ilikuwa ndugu wa Lara wafikie hapo nyumbani kwao kutokea Dodoma wakija harusini juma linalofuata. Lakini Sesi alimwambia mama yake afike yeye peke yake kwanza. Kwakuwa Sesi alishazoeleka nyumbani kwa kina Lara kama rafiki ya karibu wa Lara, na ndio walikuwa wametoka tu huko kwa shuguli ya kitchen party, hakutumia nguvu nyingi kumshawishi mama yake Lara, kufika jijini Dar kwa haraka. 

Mama Yake Lara.

Z

ikiwa zimebaki siku 9 tu harusi ifungwe, mama yake Lara akatua jijini Dar si kwa sherehe tena kama walivyokuwa wakitizamia kufika siku ya 7 yake, yaani alhamisi ya juma linalofuata, ila ikawa matatizo. Suzy, Sesi na Tino ndio waliokwenda kumpokea. “Kwema? Mbona Lara hajaja?” “Lara anaumwa mama. Hatujui kitu chakufanya, ndio maana tumekuita labda utusaidie.” Mama yake Lara akatulia kidogo.

“Hazungumzi, hali wala kunywa.” “Tokea lini?” Akauliza mama yake. Akaona wanaangaliana. “Kuna nini Tino mwanangu?” Akaona amuulize Tino moja kwa moja, kwa kuwa Tino ndiye alikuwa mtu wa Jax wa karibu. Hata nyumbani kwa kina Lara, alijulikana ndiye anayesimamia mambo hayo ya harusi kwa karibu kama mwenyekiti wa kamati ya harusi.

“Ni vile kwa kuwa nawaheshimu wazazi wangu, na Lara amefanyika kama ndugu sasa. Lakini kama ingekuwa ni mtu mwingine, hata mimi usingenikuta hapa, kwa aibu.” Akaanza Tino. “Ni aibu na fedheha mama yangu. Sijui niseme nini!” Akasita Tino, lakini mwishowe ikabidi kumueleza huyo mama kabla hawajafika na kumkuta Lara mwenyewe.

Wakashangaa yule mama naye kimya. Hakujibu kitu wala kuongeza neno. Akajirudisha nyuma kitini, akakaa kimya mpaka walipofika. Akamshukuru Tino kwa kwenda kumchukua kituo cha mabasi, akaingia ndani. Tino naye akafuata nyuma. Hakuondoka.

Yule mama aliiingia moja kwa moja mpaka chumbani kwa Lara. Alishalala humo mara kadhaa kila alipokuwa akifika Dar. Alimkuta binti yake amejifunika shuka, anatetemeka baridi. “Sesi mama, naomba niongezee blangeti, halafu naomba chai ya rangi.” Sesi hakutoka hata nje, alijua ni wapi Lara mwenyewe anaweka vitu vyake. Akafungua kabati la Lara. Juu kabisa, akavuta blangeti. Akamsaidia kumfunika. Suzy alishaanza kutengeneza chai ya rangi. Tino akaingia. “Nisaidie nini mama?” “Tiketi mbili za kurudi Dodoma kesho.” Sesi na Tino wakaangaliana.

“Kwa hali hii, hataweza kufanya kazi si kesho wala kesho kutwa. Lazima atulie kabisa na mimi siwezi kukaa hapa Dar. Natakiwa kazini. Likizo ilikuwa nichukue jumatano ile ijayo ili alhamisi tuje huku kusubiria harusi hiyo siku ya jumamosi.” “Basi mama, mimi nitawasindikiza.” Tino akajitolea.

“Tino mwanangu, usione unawajibika. Tulia tu kazini ili tusiharibu kotekote. Lara akaja kukosa pakukimbilia atakapopona. Tulia kazini, baba. Sisi tutaondoka tu na basi.” “Usijali mama yangu. Nyinyi jiandaeni, kesho nitakuja asubuhi kwenye saa nne. Nitaanzia ofisini kwanza.” “Nashukuru baba. Mungu akukumbuke katika hili.” “Amina mama yangu. Poleni sana na samahani.” “Inatokea baba. Wala Lara si wakwanza. Atakuwa tu sawa.” Wakatulia mama yake akimsugua upande wa mgongoni taratibu.

Suzy akaingia na ile chai. Akajaribu kumfanya anywe ile chai, lakini Lara alikuwa akitetemeka kama yupo kwenye baridi kali. Mpaka midomo ilikuwa ikicheza. Alikuwa amekaa. Akajivuta ukutani akajikunja huku akitetemeka. Mama yake akasimama na kumzungushia lile blangeti, Lara akainama. Kimya. Wakamuona Tino anaondoka kimya kimya bila ya kuaga. “Mimi naona tusimpe hiyo chai mama. Ni moto sana. Na hivyo anavyotetemeka, itammwagikia.” Sesi akatoa wazo.

“Lara!” Mama yake akamuita taratibu. Lara akanyanyua kichwa kumwangalia mama yake huku akitetemeka. “Utakuwa sawa mama. Umesikia? Usiogope. Hata katika hili naamini, Mungu wetu yupo.” Wakamuona anatoa machozi huku akimwangalia mama yake. “Hata hili, litapita tu mama yangu mzazi. Umesikia Lara? Utakuja kugeuka nyuma, utashangaa ulivuka vipi. Mpe nafasi Mungu akubebe. Sawa?” Wakamuona anarudisha kichwa chini.

Yule mama alikuwa ni nesi. Mtaratibu  sana. Kama si kufanana na Lara mpaka rangi ya mwili, usingesema Lara ni binti yake. Walikuwa na haiba tofauti. Lara mtundu na mcheshi sana. Huyo mama akizungumza, utafikiri amesahau anachotaka kusema. Mtaratibu na mtulivu kama dada zake Lara. Akamwangalia mtoto wake, akaona amrudishe tu alale. Lara akarudi kujilaza. “Sasa hivi usilie tena. Tulia tu. Jitahidi kutulia.” Akamwambia mtoto wake.

“Sesi mama, nipeleke duka la madawa.” Sesi akatoka na mama yake Lara, akamsindikiza mpaka kwenye duka la madawa. Akaagiza dawa alizotaka, Sesi akimtizama tu. Ila alimuona amenunua dripu tatu. Wakarudi nyumbani. Akamuwekea mtoto wake dripu. Ile dripu ilipofika katikati wakaona ameacha kutetemeka. “Amelala. Hiyo itamsaidia.” Akanong’ona mama yake huku akimwangalia mwanae. Sesi, Suzy na Warda walikuwa kimya hapo chumbani kama wapo msibani.

Mama yake Lara akawageukia. “Na nyinyi mnaendeleje na kazi?” “Vizuri.” Wote wakajibu kwa pamoja. “Mkazane, msizembee kazini.” Akaongeza mama yake Lara akitaka kuwatoa hofu. Kidogo wakajisogeza na kukaa. “Sasa na wewe utakula nini mama? Leo hatujapika, ila tunaweza kwenda kukuletea chips.” “Wala msihangaike. Chai ya rangi itanitosha, lakini kwanza nikaoge.” “Basi tunakuandalia maji bafuni, wakati unabadili nguo.” Sesi akamtolea kitenge na taulo kutoka kabatini kwa Lara. Wakampisha hapo chumbani.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

K

esho yake asubuhi na mapema, warembo hao waliamka mapema kama kawaida yao. Wote wakaenda kumgongea Lara na mama yake kuwajulia hali na kutaka kuwaaga. “Tumelala vizuri.” Akajibu mama Chiwanga akiwakaribisha ndani. “Mimi nakwenda kuandika barua ya likizo ya Lara, na mimi kuomba ruhusa, niwasindikize. Nitarudi na Tino.” “Hapo utakuwa umemsaidia mwenzio. Nashukuru Sesi mwanangu. Na wewe Mungu akukumbuke siku utakapomuhitaji.” “Amina mama.” Wakaondoka lakini walikuwa wamemuachia chai na kitafunwa mezani.

Mida ya saa 4, Tino na Sesi wakarudi hapo nyumbani. Walikuta yule mama alishamuandaa mtoto wake, na sanduku lake. “Sisi tupo tayari.” Akaongea mama Lara wakati anawafungulia mlango Tino na Sesi. Baada ya kama dakika 20, safari ya Dodoma ikaanza Lara akiwa amemlalia mama yake, amemfunika blangeti.

Haikuwa safari yenye mazungumzo ila Lara kubadilishwa mara kwa mara njiani sababu ya hedhi kali aliyoipata. Ilibidi uanaume na aibu imuishe Tino ili kufanikisha hiyo safari kwani ni kweli Lara alikuwa akitokwa na damu nyingi sana. Kila wakati ilibidi kusimamisha gari ili Lara asafishwe na kubadili matandiko aliyokuwa anakalia na kulowa. Ilikuwa ni hali ambayo hakuna mtu angetamani kuwepo hapo. Ilikuwa ni maumivu ya namna yake kwa kila aliyekuwepo hapo na Lara.

Walifika Dodoma, Tino akaomba wao warudi Dar siku hiyohiyo. Akawaambia analazimika kuwepo kazini siku inayofuata, hakuwa na likizo. Kwa kuwa kila mtu pale nyumbani kwa Chiwanga alikuwa kwenye mshituko wakumuona bibi harusi huyo amerudishwa mgonjwa, mahututi hakuna aliyekuwa na laziada kwa Tito na Sesi, zaidi ya kuwashukuru. Wakaondoka.

Usiku huo walipofika nyumbani, hawakulala. Lara alizidiwa. Ikabidi kupelekwa tu hospitalini alikokuwa akifanya kazi mama yake Lara. Mpaka inafika asubuhi kila mfanyakazi pale hospitalini alishajua juu ya kurudishwa nyumbani kwa Lara. Maneno yakaanza kuenea.

Kwa Tino.

T

ino alimrudisha Sesi nyumbani kwao Kinondoni na kwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Nelly. “Mbona kama umetoka msibani?” Nelly akauliza wakati akimpisha mlangoni. “Kwanza nashukuru kwa kurudishiwa pesa yangu yote.” Tino akakunja uso. “Nani amekurudishia?” “Jax mwenyewe.” Tino akawa hajaelewa. Akaenda kukaa. “Naomba nilewe hapa kwako na nilale kabisa.” “Hapana Tino. Wewe unajua mimi sipendi pombe ya siku za kazi.” “Nitanywea chumbani.” “Si uende kwako!” “Nipo kwenye mshituko dada yangu! Nimeshindwa hata kupitia baa.” Nelly akaenda kukaa.

“Kutokea wapi?” “Dodoma. Kumrudisha Lara nyumbani kwao.” Nelly hakuwa anaelewa. “Mapenzi sumu dada! Bora wewe ulijiamulia kuwa peke yako. Yule binti ana hali mbaya, imebidi rafiki zake wampigie mama yake simu, aje. Wanasema ameshindwa kuongea tokea Tula amfuate ofisini kwenda kumdai gari na kumwambia Jax anamuacha yeye kwa ajili yake.” Nelly akatoa macho.

“Subiri kwanza. Anzia mwanzo. Eti Tula amefanya nini!?” Tino akamsimulia kila kitu, Nelly akabaki ametoa macho. Tino akajua hata yeye mwenye roho ngumu, imemuingia. “Yaani dada Nelly, tulisimama njiani mara kadhaa ili kubadilishwa sababu yakujichafua. Anatokwa na damu kama bomba! Ilibidi kuweka plastiki chini ili akalie. Yule mama alikuwa ametulia, mpaka akatushangaza! Hakulaumu wala kuendeleza swala la harusi. Tulisafiri akiwa amemuwekea dripu mtoto wake.” “Isijekuwa alikuwa ni mjamzito, mimba ilitoka kwa mshituko!” Nelly akafikiria kwa sauti.

Wakabaki kimya kwa muda. “Lakini ni kama Lara alihama au walisimamisha mapenzi na Jax, kwa muda.” “Kwa nini na wakati yule binti alikuwa akiishi naye!?” Akauliza Nelly. “Jax alisema Lara alimshauri waachane kwa muda mpaka siku ya harusi yao. Halafu si unajua ndio zikafika siku za shug...” Tino akasita kama aliyekumbuka kitu.

“Oooh!” Akasimama kwa mshituko kama aliyefunguliwa na yeye macho. “Nini?” Nelly akamuuliza. “Yule binti alikuwa mjamzito dada, lakini Jax hakujua. Au hata mimi sikuwa nimeelewa. Yaani hapa ndio umenifanya nifikirie.” “Kaa chini acha kunitia wasiwasi zaidi.” “Dada, yule binti alikuwa mjamzito!” “Kwa nini unafikiria hivyo?” “Miezi miwili iliyopita, akaanza uzito wa kupika mle ndani. Wote tukaanza kula nje. Nikawa namcheka Jax, namwambia amerudi kuwa seja kama mimi. Wote tunakula mtaani. Akasema Lara ameanza kubadilika. Hapiki tena. Na mara nyingi akifika pale, anaishia kulala kwenye kochi hata chumbani hafiki. Nikamuuliza kama ni mgonjwa au waligombana. Lakini dada Nelly, ushawahi kukutana na watu walioweza kuelewana?” Tino akauliza. Nelly akabaki kimya kama aliyetingwa na lake.

“Basi ni Lara na Jax. Wale watu walikutana wote hawana makuu. Kila kitu kilikuwa kikienda sawa. Sijawahi kumsikia Jax akimlalamikia Lara, isipokuwa kipindi hicho tena haikuwa kama ni tatizo kubwa. Akapunguza kwenda kwa Jax, ndio mwishoe Jax akaniambia Lara ameshauri waache mapenzi ili wafaidi kwenye fungate. Hatukulizungumzia sana hilo kwa kuwa hata Jax mwenyewe alikuwa busy kazini, na mimi ndio nilikuwa na maswala la vikao vyao vya harusi.” Tino akazidi kuvuta kumbukumbu.

“Ila nakumbuka nilijaribu kumuuliza labda kama anamshuku kama Lara anaweza kuwa na mwanaume mwingine, akasema anauhakika Lara si muhuni. Ametulia sana. Na kama hatakuwa amelala nyumbani kwake, basi atakuwa amelala kwa Jax. Akasema ni mabadiliko ya namna yake, lakini akanihakikishia sio mwanaume mwingine. Tukasema labda anachoka na maswala ya harusi.” “Yule binti alikuwa mjamzito Tino! Iwe alijua na kutaka kuja kumwambia Jax baadaye au na yeye pia hakuwa akijua. Lakini Jax ameua mtoto wake yeye mwenyewe.” Nelly akaongea akifikiria.

“Lakini dada, nimemvulia kofia Jax. Hakika Jax ni mwanaume! Au niseme, yapo mapenzi ambayo mimi sijawahi kuyapata hapa duniani.” “Kwa nini unasema hivyo?” Nelly akauliza. “Jax amemuacha Lara! Mimi bado sijaamini! Nahisi ni kama ndoto ambayo itakuja kuisha, nitaamka. Lara! Hakika siamini.” Tino bado alikuwa kwenye mshituko.

“Wewe dada hukubahatika kukaa na Lara. Lakini yule binti ni tofauti na alivyo. Mwanzoni Jax alikuwa akiogopa kumtongoza akihofia atakuja kumsumbua sana. Lakini uzalendo ukamshinda, nafikiri akazidi kuvutiwa naye, akaja kuniambia amezungumza naye, Lara amekubali kutoka naye. Yeye mwenyewe Jax hakuamini.” “Mimi mwenyewe sikuwa naamini. Nikajua atamsumbua sana. Nikamwambia kwanza ni mdogo, pili ni karembo kamjini. Akija kupata mwenye pesa zaidi yake, atamkimbia tu. Nilimuonya sana Jax amuache. Lakini kama unavyomjua Jax, alinijibu kuwa tatizo langu mimi ninamtizama yeye kama ni mtoto mdogo wa jana na hawezi kufikiria. Basi nikamuacha. Leo kuja kuona Jax ndiye anamuacha kwa ajili ya Tula! Nahisi na mimi sijayajua hayo mapenzi.” Wote wakanyamaza.

Tino amesimama, Nelly amekaa. Kimya kwa muda kila mtu akiwaza lake. Mwishoe Tino akaguna. “Namuhurumia Lara, kupita kiasi! Sidhani kama maisha yake yatakuja kuwa sawa. Alimpenda sana Jax!” “Mimi namuombea Mungu Jax mdogo wangu, awe amepatia. Lasivyo!” Dada yake akatulia kidogo. “Ila Tula naye anamaswali mengi kuliko majibu! Mmmh!” Akaona anyamaze. 

Kwa Jax.

K

weli Jax alikuwa na mpango wa kumsuprise Lara kwenye nyumba kubwa. Alipata nyumba iliyokuwa ikiuzwa kwenye mnada wa benki. Jax asiyependa makuu, sijui ramani iweje au bustani iwe mbele au nyuma, alipoona ni nyumba ya kisasa, vyumba vitatu, bei nzuri, na pesa alikuwa nayo baadhi na kazini kwao anaweza kuchukua mkopo bila shida, akafanya utaratibu wa kuimiliki, tena kimyakimya ila kwa haraka na kutaka kuja kumuonyesha Lara baada ya fungate, wahamie pamoja na kumuacha Lara aitengeneze atakavyo.

Ni kweli akili na mawazo ya Jax yalikuwa yametulia kwa Lara tu. Baada ya kutendwa na Tula, akaangukia kwa Lara. Mrembo, mtundu, maneno mengi, mchangamfu kiasi chakumfanya Jax kutulia na kufurahia penzi lake. Tula aliporudi pichani na kufanikiwa kumpora tonge Lara, hakulazia damu. Akamwambia Jax wahame pale walipokuwa wakiishi na Lara wakatafute sehemu yao wao, waanze upya. Ndipo Jax akaona kuliko kupanga tena, ni heri kuhamia kwenye nyumba aliyokuwa amenunua ambayo ilikuwa ikifanyiwa marekebisho tu madogo. Zaidi kubadilishwa rangi iliyokuwepo. Jax alitaka ipakwe rangi nyumba nzima, na matengenezo ya jikoni tu.

Tula alipogundua kuwa kuna hiyo nyumba, hakutaka kusubiri, akamwambia wahamie tu hivyohivyo, mambo mengine yaendelee wakiwa wanaishi humohumo ndani kwenye hiyo nyumba. Kama kawaida ya Tula, alijaliwa uwezo mkubwa sana wakuingia akilini na moyoni kwa Jax. Jax alikuwa hawezi kusema hapana kwa lolote, kwa Tula, tokea wapo chuoni. Wakahamia. 

Tula & Jax

T

ula na Jax walikuwa wapenzi kama kumbikumbi walipokuwa chuoni. Kuanzia mwaka wa kwanza mpaka wakamaliza. Hata Tino alikuwa akimlalamikia Jax kuwa anatumia muda mwingi na Tula kuliko mtu mwingine yeyote. Nelly yeye alimwambia asipokuwa mwangalifu, atafeli sababu ya Tula. Mapenzi popote, wakati wowote wanapopata nafasi. Tula alishawahi kwenda kulala kwa Jax wakati akiishi na dada yake. Nelly aliporudi kutoka safari na kukuta Tula amehamia nyumbani kwake, aliwafukuza usiku uleule, hakutaka hata pakuche.

Wawili hawa walivumiliana kwa mengi bila kukata tamaa. Jax na Nelly wakiwa yatima waliojikuza wenyewe, Tula akaongezeka kwenye maisha ya Jax, akawa faraja kweli. Alimjua Jax kwa kumtizama. Hakuwahi kumsaliti japo ugomvi kwao ilikuwa kitu cha kawaida kwa kuwa Tula alikuwa na tabia yakupenda kutawala mambo. Alipenda kila anachomwambia Jax, awe anafanya. Na ikitokea hafanyi hapo ndipo kulikuwa na kupishana. Au ikitokea Jax anatumia muda mwingi na kina Tino sio yeye, basi hapo kulikuwa na wivu. Alimtawala Jax kwa kila namna.

Yeye Tula alitokea kwenye familia yenye uwezo sio shida. Wakati wa uhai wa baba yake, Tula alikuwa na pesa. Kwa hiyo hata chuoni hakuwa akiishiwa, na mara kadhaa na yeye alimsaidia Jax kwenye mambo madogomadogo kama vile Nelly alivyokuwa akimsaidia Jax. Kuanzia ada mpaka malazi, ilikuwa ni Nelly. Jax hakuwa na akili nyingi za darasani kama za dada yake. Kwa hiyo alipomaliza kidato cha sita, matokeo yalipotoka amepata daraja la 2 karibu tatu, haraka bila kuchelewa, Nelly akamtafutia nafasi chuo kikuu cha Tumaini, palepale Dar. Na ndipo alipokutana na kina Tino, Tula na wengineo.

Mapenzi kati ya Tula na Jax yakaendelea mpaka wakamaliza chuo. Ikaanza kazi yakutafuta ajira. Rafiki zake karibia wote, walipata kazi, kasoro Jax. Jax akakaa nyumbani kwa muda mrefu sana. Mambo yakaanza kuwa magumu kati yao. Tula anataka ndoa, na Jax hakuwa tayari kwa ndoa kwakua hakuwa na kipato chochote chakuweza kumuweka Tula ndani. Ikawa tatizo kati yao. Jax hapati kazi, Tula anaharaka na ndoa waishi pamoja. Ugomvi na kupishana kukazidi. Tula akawa akilalamika mahusiano yao hayana baraka kama wengine. Mifano ya rafiki zake kuolewa kwa haraka yeye akiwa hana mbele wala nyuma ikaendelea kila wanapokuwa na Jax na kwa simu pia.

Na ndio kipindi hichohicho baba yake Tula kama nguzo ya familia akafariki, na yeye Tula akaanza kuhangaika maisha. Akiwa yeye ndio msaada wa kifedha kwenye mahusiano yao ya kimapenzi, na yeye akaanza kuishiwa kupitiliza. Tula aliyekuwa akiishi maisha ya kutapanya akawa hana pesa. Baba aliyekuwa akimpa pesa ameondoka, Jax hapati kazi. Tula alishazoea kuchukua chumba hotelini, anakwenda kukaa huko na Jax mpaka anaishiwa ndipo anarudi kwao kuomba zingine na Jax anarudi hosteli kwa kina Tino au nyumbani kwa dada yake baada ya kumaliza chuo. Mambo yakawabadilikia.

Huku na kule Tula mtoto huyo wa namna yake, mwenye uzuri wake, katika hangaika zake na yeye hapati kazi, akapata mwanaume wa kizungu kutokea Norway. Akamualika Tula kwenda kutembea nchini kwao. Bila kusita au kupinga na bila kumshirikisha Jax au kumuaga, akapanga safari, akaondoka nchini. Jax na rafiki zake wakaona tu picha za Tula huko Facebook na Instagram akiwa na mzungu. Mara akabadili status, ‘engage’. Picha zake na mzungu wake kama wapenzi zikaenea mitandaoni. Mawasiliano kwa Jax akakata kabisa. Ili asijiumize, Jax akafunga akaunti zote za Facebook na Istagram. Akabaki mtaani. Hana kazi wala mwanamke. Kula kulala kwa dada yake, na dada yake kimya kama hamuoni hapo ndani.

Japokuwa aliumia sana, lakini Jax alibaki kumtetea Tula kuwa yeye kama binadamu alichoka kusubiri. Akawaambia watu anajuta, angekubali kumuoa Tula vilevile alivyokuwa amekubali aolewe naye bila kazi au kipato. Mwaka ukaisha, kimya. Hamna kazi wala mawasiliano kati yake na Tula.

Baadaye Mungu akaja kumsaidia Jax, nafasi za kazi CRDB zikatangazwa. Tino akamwambia. Jax akatuma maombi na kwa kuwa Tino alifahamiana na wengi, akamuombea rafiki yake, Jax akapata kazi. Jax hanywi pombe, hana mwanamke. Alikuwa akiishi na Nelly dada yake, ameumizwa kwenye mapenzi, akili yote akaweka kazini. Mchana na usiku, akili na mawazo ya Jax yakawa kazini, na hakutaka kuharibu akikumbuka shida aliyopata mtaani muda mrefu bila ajira.

Baada ya mwaka tu, Jax akaanza kuhamishwa vitengo kwa sifa njema. Viongozi wake wakampenda kuliko cheti alichokuwa amekileta hapo kazini, ambacho kilikuwa chini kuliko kina Tino. Wenzake walifaulu vizuri, yeye alipata daraja la chini sababu ya kukimbizana na Tula bila kuchoka. Jumanne na jumatano anakuwa chuoni, alhamisi mpaka jumatatu jioni anakuwa nyumba za kulala wageni na Tula. Mitihani ya mwisho hakufanya vizuri kama wenzake. Alipofika kazini akaweka nidhamu ya hali ya juu, akarudi tena chuo kufanya shahada ya pili. Safari hii Jax alikuwa akihangaika mpaka dada yake akamuhurumia na kuona amebadilika. Kazini, chuoni. Tena chuoni akawa anafanya vizuri sana, kama anayelipa kisasi.

Nelly alisoma tokea binti mdogo tu. Nje na ndani ya nchi akijiendeleza mwenyewe mpaka ngazi ya juu kabisa, Phd, na kufanikiwa kupata kazi mapema huko TRA. Ukisikia mwadilifu na mchapa kazi, basi ni Nelly. Kazi ndio baba, mama, mume, mtoto na rafiki. Hakuwa na maisha mengine ila kazi tu. Alitoka TRA akaajiriwa na NGO moja kubwa sana hapo nchini, Nelly akawa mkurugenzi hapo. Anatengeneza pesa ya kigeni inayoingia mfukoni mwake, mpaka ikawa inakosa matumizi. Ukimtizama tu Nelly, utajua pesa ipo. Anamsimamo wa waziwazi, akikutizama tu, utajua hababaishwi na utajua anao uelewa wa mambo. Ameishi nje ya nchi akisoma, na kazi yake hapo nchini anafanya na watu wa mataifa tofautitofauti akiwakilisha Tanzania.

Kwa haiba yake, hakuwa na shida kugonga kokote, kwa mkubwa yeyote akapewa nafasi yakueleza shida yake, akashindwa kusaidiwa. Alipomuona Jax ametia akili. Amejifunza kutokana na makosa, baada ya miaka mitatu hapo benki, Jax akiwa amempita mbali Tino aliyemkuta hapo kazini, na amemaliza shahada yake ya pili, Nelly akamuunganishia huko benki ya dunia. Viongozi wake walimuandikia barua nzuri za uadilifu kazini, na mambo aliyofanya hapo kazini kuongezea benki faida, akaambatanisha na vyeti vyake vyote, yeye na dada yake wakatuma huko benki ya dunia, Jax akaitwa kwa usahili, akafanya vizuri, akapata kazi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lara na yeye alipata kazi kwenye kampuni hiyo ya simu. Akakutana na kina Sesi, Warda na Suzy ambaye alishatembea na Tino. Mchana wanapokwenda kula kwenye kibanda hicho cha chips, nyuma ya kwenye mgahawa wa Best Bite walikuwa wakikutana na wafanyakazi tofautitofauti wakiwepo na hao wa benki, kina Tino, kipindi hicho hata Jax hajahamia kufanya kazi benki ya dunia. Tino alishamshindwa Suzy. Alimwambia Jax, Suzy ni msichana mzuri lakini amemshindwa kama mpenzi. Suzy hakuwa akijua kuchuja neno analotaka kulitoa mdomoni mwake, japo si muhuni. Ataongea lolote kwa yeyote. Hana soni.

Basi mida hiyo ya mchana wafanyakazi wengi wanakutana hapo kibandani kila mmoja akitaka kula. Hapo Suzy atamchokoza yeyote amtakaye, kutoka kampuni yeyote. Haitaji kumzoea mtu. Ataongea tu. Basi yeye Jax akajitahidi kumkwepa kabisa yeye na marafiki zake wanaokuja kula hapo. Zaidi ya salamu, hatamjibu kitu zaidi ya kutoa tabasamu tu. Na hata kama watakwenda kukaa kwenye meza moja waliokaa yeye na Tino, basi Jax hatazungumza lolote. Kimya. Mpaka amalize kula.  Suzy ataongea hili na lile wakitaniana na Tino na wafanyakazi wengine. Mara watukanane na Tino hapohapo mezani. Ilimradi kila mtu atajua Suzy yupo hapo na hakuwa akijua kuongea kwa sauti ya chini. Akicheka mpaka watu wote watawageukia wao kwa kelele, lakini Jax hakutaka mazoea naye kabisa.

Tino yeye ndio akageuka mtu wa kupenda kumchokoza ili tu aanze kupayuka. Wakati mwingine Jax alikuwa akimkataza na kumwambia Tino, akianza kumchokoza, yeye ataondoka. Na Suzy akajua Jax hampendi. Ikabaki hivyo.

Mambo yalibadilika alipoanza kazi Lara, na kuungana na kina Suzy kwenda kula. Suzy mwenyewe akaanza kumnadi. “Siku hizi tunatembea na modo, watoto wakizungu, hatutaki kufuatwa.” Akaanza Suzy akitangaza hapo kibandani ambako huwa wanakuwepo wafanyakazi wengi wa kutoka maofisi tofautitofauti maeneo hayo ya Posta wakitaka kupata mlo wa mchana hapo.

Mpaka wauza chips walikuwa wakimjua Suzy. Akifika anatoa oda yake kwa kelele, na lazima apewe. “Maswala ya kuniita Suzy bonge, mkome. Sasa hivi tunakwenda mwendo wa kizungu. Hakuna kula sana.” Tino alicheka sana aliposikia hivyo. “Utaweza lakini?” Tino akiwa mbali kidogo wakiwa wao walishapata chakula, wamekaa kwenye meza yao, wafanyakazi wa benki, vijana watupu, Suzy alipomsikia, akamfuata.

“Na kwa taarifa yako, watu wanabadilika. Kuanzia sasa hivi naanza gym, kula kwa kisu na uma, tena matunda tu. Kasoro leo ndio nakula chips yai.” Tino alicheka sana, tena kwa sauti. Na wenzake wakainama huku wakicheka kwa hofu wakimuogopa Suzy, maana hakawii kumbadilikia mtu. “Tatizo lako wewe dharau.” “Sio wote waliubwa wembamba, mama. Wewe endelea tu kula chips yai.” “Sasa kwa taarifa yako nishamwambia Lara kuwa nimetembea na wewe, na hawezi kukukubali.” “Kwani mimi nimekwambia namtaka!?” Tino akauliza kwa kushangaa sana. “Nimeona sana jinsi unavyomwangaliaga.” Wakaanza kubishana kama kawaida yao, na Lara mwenyewe yupo upande mwingine na kina Sesi pamoja na Warda wakimsikiliza mwenzao anavyojibizana, wakishindwa hata kugeuka kwa aibu.

Hapo ikabidi sasa Jax na yeye kumuangalia vizuri huyo Lara, ambaye Tino alimwambia Suzy bila kusita tena kwa sauti ya juu tu kuwa wao wote wanamuangalia tu huyo Lara kama fahari ya macho tu. Kusuuza mioyo. Ndipo Jax akaanza kumtizama vizuri Lara.

Taratibu na yeye akavutiwa na Lara. Wakaanza kwa salamu. Mara kupungiana mkono wanapokuwa mbali kidogo. Tino akaona na kushangazwa. Jax alishasema hatakuja kupenda tena. Alirudia rudia kila wakati ule usemi wa ‘Love come once in a life time’. Kwamba mapenzi huja mara moja tu maishani. Alishampenda Tula, hatakuja kupenda tena. Hakutaka kujihusisha na wasichana wengine.

Lakini akaona inaanza kuwa tofauti kwa Lara. Kila kina Suzy wakifika hapo kibandani, macho hayabanduki kwa Lara. Atamfuatilia kuanzia wanafika hapo mpaka wanapata sehemu ya kukaa, anakuwa akimwangalia kwa muda mrefu tu, wakati mwingine alimuona Jax akitabasamu peke yake. Tino akajua ameshanasa. Sasa kuja kusikia anatoka naye kwa chakula cha usiku siku ya jumamosi, akajua tayari. Jax sio mkurupukaji.

Mapenzi kati yao yakaanza taratibu. Kwa mara ya kwanza Jax akasikika akisifia mwanamke mwingine mbali na Tula! Akaonekana amefika kikomo, aoe kabisa, amalize. “Hakuna nitataka zaidi, Tino. Acha nimalize kabisa.” Maneno yake kwa Tino na marafiki wengine, tena baada ya mwaka mmoja tu kuwa na Lara.

Marafiki wote wakaridhia na kujua hatimae Jax amepona mawazo ya Tula, yupo tayari kuendelea na maisha yake kwenye maswala ya mapenzi. Wakamuunga mkono katika kila hatua ya kukamilisha kuoa. Kwanza alikuwa ni Lara. Anapendeka. 

Ujanja Kupata.

J

ax akiwa ametingwa na majukumu ya kazi na vikao vya harusi ambavyo Tino alikuwa akiwaitisha akijisikia yeye, zaidi akiwa amelewa, akiwa baa. Anapojisikia yeye Tino kama mwenyekiti wa kamati ya harusi, iwe mara au baada ya tarehe ya kikao, yeye atapigia simu kila mtu kutaka wakutane kwa muda mfupi kwenye baa aliyochagua yeye ili wafanye kikao. Sasa katikati ya yote hayo wakihangaika kufanikisha mambo ya harusi yao, ndipo shilingi ikapinduka.

Jax akawa busy na Lara naye busy na mambo ya harusi yao. Mara Dodoma nyumbani kwao, mara Dar kwa maandalizi ya kitchen party ya marafiki pamoja na harusi na mambo mengine mengi ilimradi shamrashamra. Akiwa anatoka kazini mida hiyo ya jioni akapokea ujumbe kutoka kwa Tula. ‘Naomba kukuona, nipo mjini kwa siku chache. Tula.’ Moyo wa Jax ulipasuka, akashindwa hata kuwasha gari. Akabaki ametulia kwenye gari yake akiutizama ule ujumbe.

Tula akapiga hapohapo baada ya kuona Jax anesoma ujumbe wake. “Naomba unione Jax. Sitachukua muda mrefu.” Kimya. “Jax?” “Unataka nini Tula?” “Njoo kwanza ndipo nitakwambia.” “Wapi?” “Nimechukua chumba hapa hotelini.” “Naoa Tula.” Tula akatulia, hakujibu. “Umenisikia?” “Unafikiri unaweza kuja au hutaweza, sasa hivi mimi sina maana tena?” “Nitakuja, lakini sitakaa.” Akamuelekeza alipo. Jax akaondoa gari kumfuata.

Njia nzima, kumbukumbu za Tula zikaanza kumrudia. Jinsi alivyomsubiri hata baada yakumuona na huyo mwanaume wa kizungu huko Norway. Alishajiapia hata kama angerudi wakati ule, angesamehe yote, warudiane. Lakini ndipo akatokea Lara, akamtoa mawazo ya Tula mpaka hapo Tula anamtafuta, ndipo akamkumbuka tena Tula. Akaendelea kuwaza mengi akikanyaga mafuta kwenda kumuona Tula.

Akafika hapo hotelini na kwenda mpaka kwenye chumba alichoelekezwa na Tula. Ilikuwa ni saa mbili, akamkuta Tula ndio anatoka kuoga. Alimfungulia mlango na nusu taulo. Macho yakamtoka Jax. Ni Tula! “Ingia ndani. Mimi sili watu.” “Mumeo yuko wapi?” Jax akauliza wakati anaingia. Tula hakujibu, akanyamaza na kurudishia mlango.

“Mbona sioni pete hapo kidoleni?” Akauliza tena Jax, akikusudia kumkejeli Tula. “Nilishindwa kuendelea Jax.” Tula akajisikitisha huku anakaa kitandani mbele ya Jax. Jax akabaki akimtizama. “Yule mwanaume hatukukaa naye muda mrefu Jax. Nilishindwa. Hamfanani hata kidogo! Nilikataa ndoa. Aliumia, lakini ilibidi kumwambia ukweli, kuwa nampenda mtu mwingine. Nisingeweza kuolewa naye. Nilijua madhara yake, lakini sikuwa na jinsi.” Jax akabaki kimya akimsikiliza.

Alitegemea Jax amuulize madhara gani, lakini kimya. “Nilikuwa radhi anifukuze kwake kuliko kuingia kwenye ndoa ambayo sitakuwa na furaha daima, Jax. Kumbuka mapenzi yetu.” Akaanza Tula. “Yule mwanaume alikuwa hawezi mapenzi yako, Jax. Hata kidogo.” Akaanza kumsifia hapo na kumkumbusha waliyoyafanya huku na kule. Mapenzi waliyokuwa wakifanya kwa kujinafasi na kuridhishana. Shida walizopitia wakiwa pamoja.

Akampamba hapo kwa hili na lile, na kwa kuwa alimjua Jax ndani na nje alimteka fikra, alikuja kuamka hapo hotelini, asubuhi, Tula pembeni yake, uchi kama alivyozaliwa. Walifanya mapenzi ya haja usiku huo bila kupumzika. Jax aliyekuwa amekubaliana na Lara wapumzike penzi mpaka ndoa, akakatwa hamu vilivyo. Asubuhi yake nayo kabla Jax hajaenda kuoga awahi kazini, akampa penzi la funga mwaka, ndipo Jax akaondoka. Akili ya Jax ilirudishwa mbali sana. Kwenye mapenzi yake na Tula.

Jioni alikwenda kwake, akaoga na kubadili nguo, na kumfuata tena Tula pale hotelini. Walizungumza mengi sana. Jax alimsimulia maumivu aliyopitia baada yakumuacha. Tula akalia sana akiomba msamaha na kumuhakikishia kuwa amerudi nchini kwa ajili yake. Anaomba nafasi ya pili na ya mwisho. Bila kutegemea wakaanza mapenzi tena. Kesho yake ilikuwa siku ya jumamosi, Jax akawepo hapo hotelini siku nzima na Tula. Wakati wote Tula alihakikisha anamkumbusha Jax maisha yao ya zamani. Jinsi walivyopendana na watu walijua.

Kuja kufika siku ya tatu, Jax akaona atajipunja maishani kama atamuacha Tula aondoke tena. Kwani Tula alimwambia akimkataa, anaondoka na hatakuja kumuona tena maishani. Jax akaona hataweza kupitia tena kile kipindi cha upweke bila Tula. Akakumbuka siku nyingi alizoshindwa kulala sababu ya kumpoteza Tula. Akachukia kuchelewa kupata kazi na kumpitisha Tula kwenye ugumu wa maisha kiasi cha kusaliti penzi lao. Alimtetea Tula kwa kila mtu. Kuwa Tula alimvumilia, na yeye kama binadamu akachoka. Kama wangekuwa hawajapitia kwenye ugumu kwa muda mrefu, Tula asingeondoka nchini. Hakutaka mtu amseme vibaya Tula wake.

Sasa Tula amerudi. Nini chakuwazuia tena! Kama ni mapenzi, wawili hao walijua walipendana kiukweli. Tatizo ilikuwa pesa. Sasa, sasahivi pesa ipo, nini kipingamizi! Kama ni Lara, hata yeye Tula alimwambia amemuacha mchumba wake karibu kabisa na harusi kwa sababu yake yeye Jax. Hapo Tula akamwambia maneno mengi akimueleza ile garama aliyolipa kuwa naye hapo. Lakini akamwambia Jax ilimpasa kulipa garama kubwa hivyo sababu kwanza aligundua alifanya kosa kumuacha yeye Jax, na pili akamwambia amejua hakuna mapenzi ya kweli hapa duniani atakayoridhika nayo kama hayo ya Jax. Ikabaki yeye sasa Jax. Alipe garama ili wawe pamoja.

Kama kawaida ya Tula. Alipoona Jax anachukua muda mrefu akifikiria, akampanga yeye. Akampa mikakati Jax akimpanga kwa hili na lile, mpaka yeye Tula akafanikiwa kuongoza mambo yote. Wakahama pale hotelini na kuhamia kwenye nyumba aliyonunua Jax kwa ajili yake na Lara. Tena Jax ndiye aliyelipia garama za hapo hotelini tokea Tula anamuita hapo na yeye kufanya kambi.

Ni kama Jax alihamia hapo hotelini na hapakuwa na maswali kutoka kwa yeyote yule. Hata Lara mwenyewe japokuwa alikuwa mjini lakini hakugundua kama mchumba Jax amehamia hotelini, yupo na Tula. Kwani Lara alikuwa busy na mambo ya harusi, na bado kazini alihitajika kama kawaida. Na alishamwambia waache mapenzi kwa muda, na akawa hataki vishawishi. Akataniana na Jax, kuwa kwenda pale nyumbani kwa Jax, ndipo wataishia kitandani. Waachane kwa muda kumbe ndio kipindi hicho na yeye Tula akamkamata Jax.

Wakati Lara akiendelea kuvaa magauni ya shuguli na kufanyiwa sherehe mbalimbali wakingojea shuguli kubwa ya harusi, akiwa hana wasiwasi kabisa na Jax, kwani kwa asili Jax hakuwa muhuni kabisa, Lara akawa hana wasiwasi, anaendeleza sherehe kumbe mchumba kahama nyumba, yupo hotelini na mpenzi wa zamani, Tula. Lakini huku akiwasiliana kwa simu na Lara pale Lara anapomtafuta.

Kipindi cha mwanzoni wakati akiiba kotekote kabla Tula hajamzidi nguvu, mida ya mchana ambapo Lara alilazimishia kukutana, bila Tula kujua, aliweza kukutana na Lara kwa chakula cha mchana wakiwa kazini, tena kwa muda mfupi sana, Lara ndiye alikuwa akiongea yote bila kuhisi mabadiliko kwa mpenzi wake. Basi Jax atatulia akimsikiliza tu kisha anamuaga akimwambia anawahi kazini. Wanaachana na Lara akiwa ameridhika amemuona Jax, asijue mwenzie akitoka tu kazini na kulala ni kwa Tula, hotelini mpaka Tula alipomwambia lazima wahame hapo.

Umbali ambao walisharudi na Tula, hapakuwa na muujiza wa Jax kuja kurudi kwa Lara na kuwa mume tena. Akili zilijaa Tula, na Tula hakuwa akijua kuacha mwanya kwa Jax, tokea chuoni. Ndipo Tula ameibuka mshindi tena. Amempata Jax, tena kwa kuvunja ndoa yeye mwenyewe Jax na kumtangaza Tula ndio mmiliki wa nafsi yake. 

Kwa Lara.

L

ara alitibiwa mpaka akapona. Damu ilikoma, akaruhusiwa kurudi nyumbani. Kwa kuwa alikuwa kwenye likizo, basi akaamua kupumzika kwelikweli, ila kukaa ndani tu hata nje hakuwa akitoka kwa aibu. Hawezi kutembea mtaani kwa fedheha. Wengine wakaanza kumdai mama Chiwanga zawadi zao wakitaka warudishiwe, wakisema kwa sababu Lara hakuolewa na wao walishachanga na kumpa zawadi, basi wazazi hao wawe waungwana. Warudishe vitu vya watu. Ukweli Lara alipata zawadi kwenye sendoff na kitchen party aliyofanyiwa kwao na wanawake rafiki za mama yake, vikundi vya kina mama wa mtaani, kanisani, kazini kwa mama yake, marafiki waliokuwa kwenye kikundi kimoja na mama Lara, walitoa zawadi mbalimbali.

Na kwa kuwa ilikuwa ni Dodoma, na bado hajaolewa, Lara aliacha zawadi zote nyumbani kwao Dodoma. Alimwambia mama yake hana nafasi ya kuviweka huko Dar. Atakuja kuvichukua watakapopata nafasi kubwa. Alipotoka hospitalini na kusikia hiyo minong’ono alimuhurumia sana mama yake. “Samahani mama. Sikujua kama hiyo ndoa haitakuwepo. Nisingewaingiza kwenye fedheha ya kiasi hiki.” Lara alimfuata mama yake jikoni.

Majuma mawili yalishapita, hata alipotoka hospitalini yeye alikuwa mtu wa kulala tu. Hata hivyo alikuwa amedhoofu sana. Hata maji kupita kooni ilikuwa kwa shida. Ilikuwa akilazimishia kila kitu kupita mdomoni, angalau vifike tumboni asife kwa njaa. Kila kitu kilikosa ladha.

 “Lara mama yangu mzazi, hakuna anayepanga kupatwa na baya. Na wala huna sababu ya kuona haya. Hukuchagua.” Lara akakaa. “Ingekuwa kuchagua, kila mtu asingekuwa alivyo. Pengine wengine wangekuwa wameshakufa. Mungu pekee ndiye anayejua siri ya maisha. Kila mtu anapatwa na lake. Lakini tunaendelea.” Lara akanyamaza.

“Ila nilitaka upumzike, nikuombe kitu mama.” Lara akamwangalia mama yake. “Naomba turudishe vitu vya watu. Watu wanalalamika sana.” “Sawa mama.” Lara akakubali bila shida tena kwa haraka sana.

“Lakini mimi siku ya alhamisi narudi Dar, mama.” Mpaka dada zake wakageuka na kushangaa. “We Lara! Kwa kipi mno? Huoni haya?” Dada yake mkubwa akashangaa na kushindwa kujizuia. “Nikimbie wapi, nikajifiche dada Lily?” Lara akauliza swali lilowafanya wote watulie. “Maana kila anayenifahamu anajua niliachwa. Sasa niende wapi? Siwezi kukosa ndoa na kazi. Nilikutwa kazini, siwezi kuacha kazi yangu. Halafu nifanye nini?” “Mimi binafsi nakupongeza Lara. Hongera sana mama. Jax alik...” “Naomba usilitaje jina lake mama. Tafadhali.” Lara akanyanyuka na kuondoka.

Hata baba yake alimpongeza. Ingekuwa aibu zaidi kama mabinti wote wangerudi kuishi hapo nyumbani. Lily ambaye ni dada mkubwa ndiye huyo alizaa akiwa sekondari na hakujiendeleza tena. Yupo tu nyumbani. Hana kazi wala hana dalili ya kuja kuolewa. Anatunzwa hapo nyumbani kwao yeye na mtoto wake. Haya, Lea naye anayemfuata Lara ndiye huyo mwalimu. Naye anaishi hapohapo nyumbani, kila mwanaume anakasoro, hataki kuolewa. Lara kufanikiwa kuondoka hapo, ilikuwa aghueni. Leo arudi aishi hapo kama dada zake, akaona sio sawa, bora arudi tu kule kulikoungua mpini. 

Kimfaaye Mtu, Chake.

Alhamisi.

L

ara alitua jijini na kwenda alikokuwa akiishi na wenzake kimyakimya bila kumtaarifu mtu. Kina Sesi walitoka kazini mida hiyo ya jioni, wakamkuta Lara amekaa nje akiwasubiri. Wote walifurahi na kushangaa. Wengi walisema atakimbia mji kwa aibu. “Lara!” Wakamkumbatia kwa pamoja. “Mbona umerudi?” Warda akajikuta ameropoka na kuuliza na kumshangaza kila mmoja. “Naishi hapa!” Akajibu Lara huku akishangaa na yeye. “We Warda!?” Sesi na Suzy wakashangaa kwa pamoja. “Jamani! Nauliza tu. Kwanza kazini si mpaka mpaka...” Akaishiwa maneno. “Naombeni mnifungulie mlango, niingie ndani.” Lara akasimama. “Sikuwa na nia mbaya jamani!” Kweli Warda aliropoka tu, hakuwa na nia mbaya. Wakamkonyeza, wakaingia ndani.

Lara aliyekuwa ameondoka, siye huyu. Lara alirudi kama katoto kadogo. Alikwisha kama aliyetoka kwenye dhiki kali nchi yenye vita ya muda mrefu isiyo na chakula. Halafu akawa kama mfupi zaidi. Kitu kilichomfanya aonekane kama katoto na kwa kuwa alisuka yeboyebo akawa mdogo zaidi.

Siku ya ijumaa, kabla Sesi hajaondoka kwenda kazini Lara akaamka na kumfuata. “Naomba ukifika kazini, nisaidie kuingia kwenye simu ya ya ya...” Akanyamaza kwa muda na kuamua kubadili jinsi ya kuongea. “Nina shida na namba ya simu ya Tula.” Mpaka Suzy akageuka. “Tulaaa, Tula...” “Ndiyo. Nina shida naye.” Wakabaki wameduaa. “Yaani uingine kwenye simu ya Ja..” “Naomba usitaje jina lake.” Akamkatiza Warda, akarudi chumbani kwake. Wakaondoka kwenda kazini, wakamuacha Lara hapo.

Ilipofika kwenye saa nne, Sesi akamtumia Lara namba ya simu ya Tula. ‘Naomba kuwa makini kipenzi. Na usinitaje.’ ‘Usiwe na wasiwasi. Ni jambo la amani tu. Nitakwambia ukija.’ Lara akarudisha hayo majibu. Akakaa na kufikiria. Akamtumia ujumbe mwingine Sesi. ‘Nakushukuru kuwa na mimi katika kipindi chote kile kigumu. Nakushukuru Sesi. Mungu akulipe mema.’ ‘Amina.’ Sesi akafurahi sana.

Lara & Tula.

L

ara akaamua kumtumia ujumbe mfupi tu Tula. ‘Mimi ni Lara. Nashukuru kwa kuja kuwa muwazi kwangu. Samahani nilishindwa kukujibu wakati ule, kwa kuwa nilikuwa kwenye mshituko. Lakini mengi uliyozungumza ulikuwa sahihi. Kama tunaweza kuonana, ingekuwa vizuri. Nina vitu ambavyo nafikiri vipo kwangu kimakosa, ni kweli unatakiwa wewe ndiwe uwe navyo.’ Akautuma huo ujumbe. Baada ya muda mfupi Tula akapiga. “Mimi nipo tu. Naweza kukufuata popote, nina usafiri.” “Nashauri uje na taksii ili kuweza kurudi na gari yako.” Tula akatulia kwa muda. “Umenisikia?” Lara akauliza. “Nikufuate wapi?” “Tukutane Manyanya kituoni.” “Sawa. Baada kama ya lisaa nitakuwa hapo.” Akajibu Tula akisikika mwenye mshangao ila furaha. “Sawa.” Akajibu Lara na kukata simu.

Lara alitoka hapo, akasafisha kidogo lile gari ndani na nje. Akahakikisha lipo kwenye hali nzuri. Akatoka ili asije kumchelewa Tula. Alifika kituo cha Manyanya, akaegesha gari nyuma kidogo ambako daladala hazisimami. Akatoka kukaa nje. Baada ya muda akaona gari nzuri tu, Tula akashuka. Alikuwa amependeza sana. Kuanzia juu mpaka chini, alikuwa nadhifu haswa. Alinukia vizuri, pochi safi. Lara akasimama.

“Nashukuru kwa kuja. Nimeona wewe ni mtu sahihi wa kukukabidhi.” Akafungua mkoba. Akatoa kadi ya gari. “Hii hapa. Bado sijabadilisha jina. Lipo kwa jina lilelile.” Akatoa funguo. “Na hizi ni funguo za gari. Zilikuwa mbili. Zote hizi hapa.” Akapokea Tula.  Lara akavuta pumzi kwa nguvu. Akainama kwa muda. Akanyanyua uso, akaona Tula ametulia akimwangalia. Akajifuta machozi. “Na hii.” Akatoa pete ya uchumba. “Nafikiri hii ni haki yako.” Mpaka Tula akatoa macho. Ilikuwa nzuri sana. Kubwa na ilionekana ya thamani. Tula akaipokea kwa haraka.

Akabaki amekodolea macho vile vitu alivyopewa na Lara. Wakatulia kidogo. Mwishoe Lara akaondoka kwenda upande wa daladala. Akakaa hapo kituoni akisubiri daladala. Tula akapanda ile gari na kuondoka nayo. Lara alivuta pumzi kwa nguvu mara kadhaa kujaribu kutulia. Zilipita daladala kadhaa, Lara akishindwa kuondoka hapo kituoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kitu cha kwanza alichofanya Sesi aliporudi nyumbani ni kwenda chumbani kwa Lara. Alimkuta amejilaza kitandani. “Gari iko wapi!?” “Nimempa Tula.” Sesi alishangaa sana. “Una wazimu wewe Lara!?” “Ile gari nilipewa kishika uchumba Sesi. Tula hakukosea. Kwa nini nikae na kishika uchumba ambao haupo? Ni mali yake Tula.” “Umefanya haraka Lara. Hukutakiwa kurudisha. Kwa yote aliyokufanyia, bado unamrudishia! Angalau ungebakiwa nalo kama kifuta jasho chako! Mshenzi..” “Usimtukane.” Lara akamkataza.

“Na sijakurupuka Sesi. Niliwaza hivyo tokea nilipokuwa nyumbani. Nikamshirikisha na mama, akaona si wazo baya, ili kupunguza kufuatwa tena na kudaiwa tena na hilo gari.” Sesi akaumia sana. “Unakumbuka zile zawadi zote ulizokuwa ukiziangalia kule chumbani kwetu, nyumbani?” “Lara please! Usiniambie kama na zenyewe unataka kuzirudisha!” “Zimerudisha Sesi. Watu walikuwa wakiwasimanga baba na mama mpaka nikawahurumia. Wanahisi niliwatapeli kuwaletea kijana wa uongo ili wazazi wangu wajinufaishe na pesa na hivyo vitu.” “Jamani wanadhambi!” Sesi akazidi kuumia.

“Sio kosa lao. Kwetu tunahistoria ya kutokuolewa. Kwa hiyo niliposema mimi naolewa, wengi pale mtaani hawakuamini. Sasa kwa hili lililotokea, imekuwa kama uthibitisho.” “Pole Lara.” “Asante Sesi. Nakushukuru. Nashukuru kwa kunisaidi kipindi kile. Pengine isingekuwa wewe sasa hivi ningekuwa nimepoteza na kazi.” Sesi alizidi kuumia.

“Mungu atakupa mwingine.” “Mmmh! Hapana Sesi. Nahisi kweli, sio wote tumeandikiwa ndoa kipenzi.” “Acha hizo Lara.” “Hapana kwa kweli. Hiyo njia nimepita, huko sirudi tena. Kwanza naomba tubadili mazungumzo. Vipi kazini? Lipi jipya?” Wakaanza kuzungumza hili na lile. Suzy wa maneno mengi naye akaingia. Akaanza stori. Mara hili na lile, ilimradi yeye ndio asikilizwe. Warda naye akaingia akijihami. “Umeninunia?” “Kwani umefanyaje tena?” “Nahisi kila neno ninaloongea nakosea!” Wote wakacheka. Walimjua Warda. Hakuwa akipenda ugomvi wala kumuudhi mtu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jumatatu Lara alikwenda na wenzake kazini kama kawaida. Habari kuwa aliondoka akiwa mgonjwa sana, ilienea kila mahali. Wafanyakazi wengine hawakujua kama wamkaribishe kazini au waseme pole. Na yeye akaona anyamaze tu. Bosi wao akawa muungwana. Akamuhamishia kitengo cha nyuma angalau kumuweka mbali na wateja waliokuwa wanajua anaolewa. Maisha yake yakaendelea kama kawaida.

Ila kwa hakika alibadilika. Lara akarudi kuwa mkimya sana tofauti na haiba yake ya utundu. Kila mtu pale ofisini walimjua jinsi alivyo mtundu, maneno mengi ya utani kwa kila mtu. Na ndio maana kwenye harusi yake, wengi walijitoa sana, wakitaka kumuunga mkono. Lakini Lara huyu alirudi siye. Hakusikika kabisa kama ambaye hakuwepo hapo ofisini. Kimya. Hata akisikia watu wakiongea, hatachangia chochote, kimya kama ambaye hayupo hapo.

Kwenye vikao vya asubuhi kabla ya kazi, hakuwa akiuliza tena maswali yake ya kiuchozi kwa bosi wao. Kimya mpaka kikao kinaisha, anakwenda kwenye meza yake ndani, kazi inaanza. Kimya. Wote wakarudia maisha ya kupanda daladala, hakuna tena gari ya Lara. Asubuhi wakienda kazini na jioni hivyohivyo, haso ya daladala. Kila mtu alionja uchungu wa kuachwa kwa Lara kwa namna moja au nyingine. Maisha yakaendelea kimya kimya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya mwezi tokea arudi kazini, Lara aliweza kutoka kwenda kula chakula nje. Akaacha kumuagizia Sesi kumletea chakula pale ndani. Sesi alipokwenda kumuuliza amletee chakula gani siku hiyo, akamwambia waongozane. Walishangaa kidogo, lakini Suzy akafurahia kutoka na Lara pia.

Baadhi ya wafanyakazi wa CRDB ambao pia hula hapohapo, na wenyewe walichanga kwenye harusi yao kutaka kumuunga mkono Jax aliyekwisha kufanya nao kazi, na Tino rafiki wa karibu wa Jax na mwenyekiti wa kamati hiyo nao walijua kashfa ya kuachwa kwa Lara walikuwepo hapo siku hiyo wakitaka kupata mlo wa mchana.

Lara na wenzie walifika hapo, kila mtu alikuwa akimtizama Lara. Na yeye alijua, lakini akajikaza. “Nitakimbia au kujificha mpaka lini?”  Hayo alishajiuliza Lara na kukosa jibu lake. Mwishoe akajitia moyo. Hakuwa na pakukimbilia. Ajira ni ngumu kila mahali. Hawezi kuacha kazi pale. Arudi kwao! Nako hapakaliki. Heri kubaki alipo.

Wakati wamekaa wanasubiria chakula, Tino akawasogelea pale mezani. Lara akainamia simu yake kama ambaye hajamuona. Wote wakajua. Tino akasalimia, Lara akawa kama hajamuona wala kusikia kabisa. Akajiongelesha hili na lile, lakini Lara hata hakumtizama. Chakula kililetwa, Lara akainamia sahani yake. Tino akaamua kuondoka. Siku hiyo hata Suzy hakuweka utani.

Tino na Lara walitokea kuelewana sana kipindi hicho kabla ya kuachwa kwake Lara. Ule ukimya pale na kushindwa hata kumtizama usoni, Tito akaumia sana. Jioni walipotoka tu kazini, wakati ndio wanatulia. Warda anapika kama kawaida yake. Suzy, Sesi na Lara wapo sebuleni wanaangalia kipindi kwenye luninga, Tino akaingia. Safari hii akaamua kabisa kumsalimia kwa kumtaja jina Lara. “Vipi Lara?” Hata hakugeuka. Akanyamaza kimya. “Lara!” Kimya. Lara alitulia kama ambaye hakuwa akitajwa jina lake. Alikuwa amepandisha miguu kwenye kochi dogo, amejikunja, macho kwenye tv.

“Naomba usiniweke kundi moja la wasaliti, Lara! Mimi sikuwa najua. Na tangia wakati ule hata sijui alipo na wala hatujatafutana tena. Jax..” Lara akanyanyuka na kuondoka. “Hilo jina halitamkwi humu ndani wewe Tino! Mbona kama huelewi?” “Sasa mimi nimefanyaje jamani!?” Tino akashangaa akilalamika. “Alishakuonyesha tokea mchana hataki kukuona. Halafu na wewe ukaleta kichwa chako hapa!” Suzy akaanza.

“Hawataki nyinyi wala vitu vyenu. Kasharudisha pete ya uchumba na gari lenu. Achaneni na Lara.” “Subiri kwanza Suzy. Lara amemrudishia Jax gari na pete!?” “Tumekwambia usitaje hilo jina humu ndani.” Suzy akamkoromea Tino. “Sawa. Amerudisha!?” “Alimrudishia Tula ambaye alikuja ofisini kumdai.” “Mungu wangu!” Tino akashika kichwa.

“Lakini mimi nimefanya nini!?” Tino akaendelea kuhoji akilalamika. Wakasikia mlango wa Lara ukifunguliwa. Akasogea pale. “Wewe ni mbaya kuliko mwenzako Tino.” Akaanza Lara. Wote wakashituka na kugeuka vizuri. “Unakumbuka nilikupigia simu kukwambia nina hali mbaya, simpati mwenzio?” Tino kimya. “Unakumbuka ulinifuata, tukakaa wote kwenye gari?” Kimya. “Nilikwambia nina hali mbaya Tino. Nikakuomba sana, katafute ukweli ili nitoke kwenye ile hali.” Lara akaanza kutokwa na machozi.

“Tuliachana tukiwa tumekubaliana unakwenda kuzungumza na dada Nelly, kisha unitaarifu. Ulivyo mbaya wewe, ukapata ukweli na kunifungia simu zangu zisiingie kwako. Nilikaa nikikusubiri huku nikikupigia simu bila kuchoka.” Lara akaendelea kulia. “Hali yangu ilizidi kuwa mbaya, nikajua nikiendelea kubaki hapa ndani, nitapoteza mtoto wangu.” Kila mtu akashituka zaidi.

“Ikabidi niondoke, kwenda hospitalini ili wanisaidie huku nikijipa moyo pengine utanipigia simu. Nilikutwa na pressure juu sana. Wakaniambia kama sitatulia nitapoteza mtoto wangu. Nikawekewa dripu na kuambiwa nilale pale.” Lara akaendelea kulia kwa uchungu sana.

Kati ya hao marafiki anao ishi nao hapo hakuna hata mmoja kati yao aliyejua kama alikuwa ni mjamzito. “Nilishindwa kutulia hospitalini. Kwa kuwa simu iliishiwa chaji, na wewe sikupati, nikajiambia nisipopata jibu siwezi kutulia hata wangenipa matibabu ya namna gani. Huku nikitumaini utanitafuta Tino. Nilikwambia kwa machozi, usiniache vile nilivyo. Niambie chochote, nijue jinsi ya kujipanga. Niliondoka kwa haraka kutoka hospitalini, tena bila ruhusa ya daktari kurudi nyumbani kuwahi chaji nikijua wewe ndio utakuwa dawa yangu, mbali na yale matibabu ya pale hospitalini. Kwa ile imani niliyokuwa nayo kwako Tino.”

“Nilikutafuta bila mafanikio. Mpaka muda wa kwenda kazini mimi macho kwenye simu, nilikesha nikikusubiri. Nilikuwa na hali mbaya. Nikakutetea mawazoni mwangu kuwa, pengine uliishiwa chaji, utakuja kunifuata kazini.” Lara akaendelea akilia. “Ulivyo na roho ngumu wewe, ulikaa kimya, mpaka nikafuatwa na shemeji yako wa ukweli, Tula. Ukaacha nadhalilika mbele za watu, Tino! Mimi najua ukweli kwa kupitia shemeji yako, uliyejua usiku uliopita, yupo na ametulia na ...” Akasita.

“Ulisababisha kifo cha mwanangu Tino. Ule mshituko wa kusikia kutoka kwa Tula moja kwa moja, kulisababisha kifo cha mwanangu Tino. Mlimchagua Tula zaidi yangu. Nilikusihi Tino, tena kwa machozi, nikikwambia nipo kwenye hali mbaya. Nipe ukweli. Ulishindwa. Wewe na mwenzako, mlishindwa.” Lara akajifuta machozi.

“Kwa kuwa ulishindwa kuwa msaada mdogo tu kwangu. Nikiwa nimekuomba kitu kidogo tu. Ukashindwa wakati ule, sitakuhitaji tena Tino. Wewe na lile gari, mnanikumbusha kifo cha mtoto wangu. Mimba yangu ilitoka kwenye lile gari, ukiwa wewe umesababisha kwa asilimia kubwa tu.” Tino akainama. Hapo ndipo kila mtu akaelewa ni kwa nini Lara alilitoa lile gari.

“Usinitafute, sitakutafuta. Usinisemeshe, sitakusemesha. Ukiniona, uninyamazie kama usiku ule uliponinyamazia. Popote tutakapokutana, iwe kama sipo. Ulinifungia kwenye simu zako, endelea kunifungia. Ukija hapa, njoo kwa ajili ya kina Suzy.” “Hapa tusikuone Tino. Hata sisi hatutaki salamu yako.” Suzy akadakia. “Na mimi unanijua Tino, maneno na ngumi mkononi. Haya, nyanyua, ondoka.”

“Lara!” Tino akaita wakati anasimama. “Nao..” Lara hakutaka hata kumsikiliza, akaondoka. “Haya, mlango ule pale.” Suzy akaongeza. Tino akaondoka. Wote wakaenda chumbani kwa Lara aliyekuwa akilia sana. Hasira zilimfanya aongee ambayo hakutaka kuyaongea, akijua yataenea tena.

Kwa Nelly.

Tino alitoka hapo moja kwa moja kwa Nelly, alifika akiwa anaonekana alikuwa akilia kabla yakufunguliwa mlango. Alimsimulia Nelly kila kitu. Nelly akaumia sana. “Lakini sikutaka mimi ndio niwe mvunja uchumba wao, dada yangu. Nilitaka Jax mwenyewe ndio awe wakwanza kuzungumza naye. Na ndio maana kitu cha kwanza nilichofanya siku inayofuata, nikumfuata Jax ofisini na kumwambia akazungumze na Lara. Sikujua kama ndio naharibu. Sikukusudia.”

Nelly akabaki kimya kwa muda. Akamtumia ujumbe Jax. ‘Naomba kesho jioni baada ya kazi, tupate chakula cha pamoja.’ ‘Wapi?’ Akauliza Jax bila kupoteza muda. ‘Popote unapotaka. Ila naomba safari hii iwe mimi na wewe tu.’ Jax akaelewa kuwa Tula hatakiwi. Hakushangaa. Alimjua dada yake.

Nelly Kwa Jax.

J

ioni baada ya kazi, Jax akampigia simu dada yake, na kumwambia anaelekea hapo walipokubaliana kukutana. Na yeye akamwambia hatachelewa. Wakakutana. Walipoagiza tu vinywaji bila kuchelewa, Nelly akatoa picha ya baba yao na mama yao. “Unawakumbuka hawa watu?” Akamuuliza Jax. Jax akatizama vizuri. “Huyu si baba na mama!” “Ewaaa!” Akavuta ile picha. “Sasa huyu. Huyuu!” Akaweka kidole kwenye sura ya mama yake. “Mama!?” “Huyo ndiye amenifanya kuchukia ndoa, mahusiano hata na watu wengine wakawaida, na kunifanya niwe hivi kama tembo niliye jeruhiwa.” Jax akashangaa sana.

Muhudumu akaleta vinywaji, lakini Jax akabaki akimshangaa dada yake. “Najua hukumbuki maisha tuliyoishi wakati wazazi wetu wapo hai. Mimi nilikuwa mkubwa. Nakumbuka vizuri sana.” Nelly akanywa wine yake. “Nakumbuka mpaka nachukia. Kama kuna muujiza namuomba Mungu aje anitendee, nikusahau maisha yao hao. Zaidi huyu. Maana inanifanya nashindwa kuishi kwa amani.” “Mama!?” Jax akashangaa sana.

“Yeap. Huyo huyo. Muangalie baba.” Akamrudishia ile picha. Jax akawa anaangalia huku amekunja uso. “Bwana mnafanana na huyo mwanaume! Mpaka wakati mwingine nikikukuta umekaa sehemu, nahisi ni kama yeye amefufuka! Tabia, sura, mpaka sauti! Ni baba mtupu.” Jax hakujua dada yake anataka kuongea nini.

Akamaliza ile wine kwa mara moja, akamuita muhudumu tena. Jax akajua lipo jambo. Dada yake hakuwa mnywaji sana zaidi hakuwa akinywa siku za kazi ambazo kesho yake anatakiwa kazini. Alijaliwa nidhamu ya kazi ya hali ya juu. Na kazi yake kwake ilikuwa ni kila kitu. Na ndio maana alipanda cheo kwa haraka na zamani sana.

Ikaletwa wine nyingine. Akanywa nusu. Jax akimtizama. “Bwana huyo mwanaume alimfanya mama kile atakacho. Kama mpira! Alimchezea, akamnyanyasa, na kumfanya vile alivyojisikia yeye.” Nelly akanywa tena ile wine. “Kilichonikera kwa huyo mkewe, nikujifanya kama mjinga! Akikubali afanywe kile atakacho mumewe.” Nelly akamaliza ile wine yote. Hiyo ikawa glasi ya pili ya wine kwa muda mfupi sana.

“Unajua hatima ya yote? Namaanisha hatima ya ule ujinga wa mama?” Jax kimya. “Ni kutuacha sisi yatima, tukinyanyaswa, tukihangaika hovyo.” Jax kimya. “Baba alihakikisha anamuua mama kabisa.” Jax akashituka sana. Akamtizima dada yake vizuri. “Aliondoka kwa miaka kama miwili hivi. Au mmoja na miezi yakutosha kabisa. Hajui kula yetu, wala vaa yetu. Akaja kurudi baada ya muda wote huo. Na mama naye akamfungulia mlango mpaka kitandani bila kutufikiria sisi. Na wala hakubadilika. Aliendelea kumnyanyasa mama vilevile, hata alipokuwa amemuambukiza Ukimwi, hakumjali hata kidogo. Aliugua mama, peke yake. Mumewe akiendelea na maisha yake ya starehe na uhuni kama kawaida yake.” Nelly akaomba kinywaji kingine.

“Mbaya zaidi, ndugu wa upande wote, mpaka ndugu zake baba, walishamtaka mama aondoke pale. Wakimwambia wazi atakuja kuuwawa, aache watoto. Mama alibaki. Na kweli, hakuchukua muda, alikufa tukiwa peke yetu. Baba hakuwa hata na muda wakumuuguza.” Wine yake ikaletwa tena. Akainywa tena mpaka nusu. “Kesho kazini!” Jax akamkumbusha dada yake. Nelly akacheka. Akamalizia ile wine. Hiyo ilikuwa glasi ya tatu.

“Baba alikuwa mjuaji kama hivyo wewe. Hakuwa akiambilika hata na ndugu zake. Akaishia kumuua mama. Anyway, siwezi kusema kwake ilikuwa jambo baya. Kwa kuwa hakujali kifo cha mama.” Akamuita muhudumu. “Nelly!” Jax akamuita kwa kushangaa anavyoendelea kunywa. Muhudumu akaja kwa haraka. “Kule unakotoa hizi wine za vipimo, leta chupa nzima.” Nelly akaagiza. Muhudumu akaondoka, Jax akabaki ametoa macho. Ni Nelly, anakunywa pombe siku ya kazi! Jax akajiweka sawa.

“Kifo chake na yeye hakikuwa mbali. Unajua ni kwa nini?” Akamuuliza mdogo wake. “Nitakwambia kile ambacho wengi huwa hawajui. Alikosa kimbilio ambalo mwanzoni aliliona dhaifu sana. Halifai. Mama. Pale ambapo alikuwa akikimbilia baada ya kuchoshwa na yale aliyokuwa akiyatizama nje, kwa kuyathamini kuliko mwanamke aliyemuacha ndani. Alikosa kile alichokuwa anakipuuza. Yeye hakuugua sana kama mama. Kwanza hakutaka hata augue, kwa kuwa hapakuwa na wakumuuguza. Ni kama akili ilimrudia pale tulipobaki sasa, sisi watatu. Mimi nikawa sina muda na chochote isipokuwa wewe na shule.” Chupa ya wine ikaletwa. Muhudumu akataka kumimina kwenye glasi, Nelly akamuwahi. Akampokonya.

“Hii itakwenda hivihivi ikiwa kwenye chupa.” Muhudumu akacheka na kuondoka akiwa anashangaa kidogo. “Baba akaona ayafanye marefu kuwa mafupi. Bwana yule mwanaume akajinyonga usiku! Bila huruma akijua sisi bado ni wadogo, na tupo humohumo ndani, akaacha mwili wake ukining’inia chumbani kwake.” Nelly akamtizama Jax kwa muda.

Wakabaki wakitizamana. Nelly akaendelea. “Yule mwanaume alihakikisha anamuua mkewe kwanza, ndipo akajiondoa na yeye. Aliondoka vilevile mjuaji lakini aliondoka akiwa haelewani na yeyote yule hata mahawara zake.” Akatulia Nelly akimtizama mdogo wake. Jax kimya akimtizama na yeye dada yake akitaka kujua mwisho ya hayo yote, siku hiyo, yeye anahusikaje au kwa nini siku hiyo ndio aambiwe yote hayo!

“Sasa nikikuangalia wewe, naona wewe umeanza mapema sana tena kuliko hata baba. Wewe umeanza kwa kumuua mtoto wako mwenyewe. Tena bila hofu, kikatili, wala kufikiria, kama baba.” Jax akakunja uso. “Unaongea nini Nelly!?” “Nafikiri hata baba alikuwa akiwaambia hivyohivyo ndugu zake. Kwa kuwa alijiamini sana. Sauti nyingine mbali na yeye mwenyewe, hakuwa akizielewa. Kama hivyo unavyonitizama mimi kama mpuuzi fulani hivi!” “Dada Nelly, sikuoni wewe mpuuzi! Ila sikuelewi! Ni hivyo tu. Na kama nikuhusu Lara..” “Wala usimtaje huyo binti kwangu Jax. Acha kabisa.” Jax akashangaa sana. Nelly akanywa ile wine akitumia chupa yenyewe wala si glasi.

“Kwanza wewe mwenyewe hukuwa hata ukimpenda Lara! Kwa nini leo unanishutumu vibaya hivyo!?” Jax akalalamika. “Hata nilipokwambia nimemuacha, hukuongea chochote!” “Kwani uliponiambia unamuoa nilikwambia lolote?” Jax kimya. “Nakuuliza Jax. Tokea lini umefanya jambo nililokushauri juu ya maisha yako mbali na shule na ukanisikiliza?” “Sio kweli Nelly. Mimi mbona nakusikiliza sana tu!” “Nilikwambia nini juu ya Tula kabla na baada ya kumaliza chuo?” Kimya.

“Nilishauri nini juu ya Tula kabla hajakuacha na kwenda Norway na mwanaume mwingine?” Kimya. “Ulinipuuza kabisa. Tula akaondoka. Akaenda kuishi maisha yake huko. Hujui ni kwanini amerudi! Hujui aliyokwambia mpaka ukamuacha Lara ni kweli au la! Hukutaka hata kujipa muda wa kuchunguza lolote lile juu yake. Ukampokea kwa mikono miwili! Ukamuacha kikatili Lara akiwa na mtoto wako!” Jax alishituka, dada yake akamuona nakumcheka kwa kumkejeli.

“Ulivyo mjuaji wewe. Hata usiombe ushauri, au kuuliza! Ukampokea Tula kwa maneno yake ya ushawishi na kibabe kwako. Ninauhakika ukaanza naye mapenzi kavukavu.” Nelly akanywa tena. “Nina uhakika ulianza mapenzi na Tula bila hata kufikiria madhara yatakayowapata wengine, kama vile alivyokuwa akifanya baba yako. Ilimradi wewe roho yako yakibinafsi imepata ulichotaka, basi. Ukasahau madhara ya yule binti ambaye ulibakisha siku chache sana umuoe. Lara ana wazazi, marafiki, majirani, wafanyakazi wenzake wanao mzunguka. Hivi hata ulipata muda wakufikiria kwa upande wake?” Kimya.

Nelly akabaki amemtolea macho. “Si..” “Ile tu kumfikiria yeye kama mwanadamu iliyejulikana kila mahali kuwa anaolewa. Ukamuacha yule binti ameagwa mpaka nyumbani kwao! Ulinitoa mimi hapa Dar, mpaka Dodoma! Nikaacha majukumu yangu yote ukiniambia mimi na Tino, Lara ndio mkeo. Nakuuliza Jax, wakati unamvulia nguo Tula, ulikumbuka hata kama yupo Lara?” Nelly akauliza tena. Kimya.

“Na mara ya pili na ya tatu je?” Kimya. “Wakati unamkimbia. Unahama nyumba na Tula, ulikumbuka ulikuwa ukiishi na yule binti pengine ana mimba yako?” “Si..” “Offcourse hukujua.” Akadakia Nelly kwa ukali. “Huwezi kujua, kwa kuwa unajiangalia wewe mwenyewe. Peke yako. Kile unachotaka kufanya ndicho unafanya. Hufikirii yeyote hata watu wa muhimu sana kwako, kama vile baba!” Nelly akaendelea.

“Ukaua mtoto wako bila hofu! Kijasiri kabisa, ukimwambia Lara kuwa unarudi kwa mwanamke unayempenda. Uliwezaje Jax!?” Mpaka Nelly mwenyewe akashangaa. “Yaani mimi huwa watu wananisifu kwa roho ngumu, lakini sikufikii wewe Jax. Pale uliponiacha siku uliponiambia unamuacha Lara kwa ajili ya Tula, nilishindwa hata kusimama, mpaka alipokuja Tino! Kwa ile hofu iliyonikamata, nikimkumbuka baba.”

“Sikutaka kumwambia hata Tino, ila nilibaki nikimuuliza Mungu, ni kwa nini anamrudisha baba kwenye maisha yangu!? Nikamuuliza Mungu kama anatatizo la kumbukumbu! Nikamuuliza Mungu kama kweli amemsahau Nelly na Jax, au ameamua na yeye kunitelekeza! Baya gani nililotenda kiasi chakumrudisha baba kwenye maisha yangu!” Nelly akamaliza ile wine yote kwenye chupa.

“Ulijua wazi Tula alimfuata Lara kazini kwake. Akamdhihaki mbele ya watu waliomchangia kwenye harusi yenu. Niambie ukweli Jax, hivi hata ilikuuma kweli au ulimfuta Lara kwa kuwa Tino alikufuata na kukwambia? Kabla hujajibu, nikukumbushe tu pengine ulikuwa mdogo sana hukuwa unakumbuka. Baba alikuwa akifanya hivyo hivyo kwa mama, na hakuwa akijali, Jax. Kwa kushuhudia. Alikuwa akitembea mpaka na rafiki za mama. Walimdhihaki mama vile watakavyo, baba hakujali kama hivyo wewe!” Nelly akaongea kwa kuumia sana.

“Lara ametolewa hapa Dar kurudishwa kwao, anavuja damu, mgonjwa. Tino ndiye aliyemsindikiza Lara kurudi kwao! Ulipomuacha Lara pale kitandani ukimwambia umemchagua Tula badala yake, yule binti alipatwa na shock kama aliyepigwa na umeme. Hakula wala kunywa, ikabidi aitwe mama yake. Alikuwa akivuja damu, Tino anasema kama ng’ombe aliyekatwa mshipa wa shingo. Njiani kurudi Dodoma, anasema walikuwa na kazi ya kubadili plastiki alizokuwa amelalia yule binti, na dripu alizokuwa anawekewa na mama yake. Huku wewe ukiendelea kufaidi penzi la Tula. Uliwezaje Jax!? Unawezaje hata kupata usingizi katikati ya hali tete kama hiyo!? Tuseme upande wa Lara hukufahamu. Na marafiki je!? Uliowahangaisha kwenda na kurudi, mara mbili Dodoma kwa kina Lara?” Jax kimya.

“Je, marafiki waliotoa pesa zao, na muda kukuunga mkono kwa mwanamke uliyetuhakikishia wote, anafaa kuwa mama wa watoto wako?” Kimya. “Wazazi wa Lara nao?” Nelly akaendelea kuhoji. “Nakuuliza Jax, uliweza hata kuwafikiria au kwa kuwa nafsi yako ilipata unachotaka ikawa basi?” Kimya. “Jax!?” Kimya. “Utulivu huo mdogo wangu, na uwezo wa kuendelea na maisha yako kana kwamba hakuna kilichotokea, unawezaje Jax!?”

“Leo Lara anarudi mjini. Akiwa amekupoteza wewe na mtoto wenu. Anawarudishia gari na pete ya uchumba, hata hujali! Mnapokea kila kitu na unabaki kimya kama hakuna kilichotokea?” “Gari lipo kwa Lara! Nilimpelekea mpaka na kadi ya gari! Nikamruhusu abadili iwe kwa jina lake. Na nilizungumza na Tula, kumuonya asiwahi kurudi tena kwa Lara.” Nelly akamtizama kwa kumsikitikia. “Kweli dada yangu, sidanganyi. Gari ipo kwa Lara, sijachukua.” “Najiuliza. Kama hili hulifahamu! Na mnalala naye kitanda kimoja! Ni mangapi huyafahamu juu yake!?” Jax akakunja uso.

“Jax? Mangapi huyafahamu juu ya huyu Tula aliyerudi tu, akakutoa katikati ya mipango mizito kama ile, ukakimbia naye, bila kufikiria? Kama amefanikiwa kukutoa kwenye jambo zito kama hilo. Macho ya wengi ya kikutizama. Ukiwa umevunja mioyo ya wengi. Mpaka kumwaga damu ya mtoto wako mwenyewe, unafikiri atakubadili na kukutoa kwenye mangapi?” Nelly akaongea kwa kuumia sana.

“Namuomba Mungu, anisamehe kwa kile nilichokosa jamani! Hata kama ni kosa la kuzaliwa na wale wazazi, pia anisamehe. Lakini asimrudishe baba kwenye maisha yangu. Sitaweza tena Jax. Muda wote nilivumilia yoote, nikijua nakuza mtu ambaye atakuwa na mimi maishani. Kama wewe ukiwa ndiye baba, hakika Jax, sitaweza. Ni heri nitangulie ili nisije ona kile alichopitia mama, kwa mwanamke mwingine kupitia wewe Jax.” Nelly akasimama. Akachukua pochi yake, nakuondoka bila kula.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~


CONVERSATION

1 Comments:

  1. Duuuuuuuu ni hali tete sana,bora Nelly amesimama kama dada

    ReplyDelete