Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com CHOZI LANGU! - SEHEMU YA 3. - Naomi Simulizi

CHOZI LANGU! - SEHEMU YA 3.

 Jax.


Jax alibaki ameduaa. Kichwa kilikuwa kikienda kasi. Aligongewa kengele masikioni. Kwa mara ya kwanza ndio anajua Lara alikuwa mjamzito na aliugua sana. Lara ni binti mzuri sana. Haikumsumbua hata kuwaza mara ya pili juu yake. Akajua akimuacha tu, wengine watamkimbilia. Hakuwaza mara mbili. “Wanamsingizia Tula. Kama alichukua gari, liko wapi?” Kama kawaida yake Jax akamtetea Tula. Nyumba wanayoishi haikuwa kubwa kiasi chakushindwa kuona gari hata kama imefichwa! Na mbona hajamuona na hiyo pete! Alivipataje wakati alishamkataza asimfuate Lara! Kwa nini asimwambie! Yote hayo akajiuliza Jax akiwa ameachwa peke yake hapo baa.

Gafla hofu ya kuambukizwa magonjwa ikamuingia kwa kasi. Ni kweli alilala na Tula bila maswali mengi wala kinga. Akajikuna kichwa. Muhudumu akamfuta kumuuliza kama anataka kitu kingine. “Chakula?” “Naomba kulipia vinywaji tu.” Hamu ya kula ilishamuisha. Akalipa na kuhamia kwenye gari ambako hakutaka kusumbuliwa. Hakutoa hata gari. Akabaki akifikiria palepale ndani ya gari.

Baada ya kama lisaa Tula akampigia. “Upo wapi Jax?” “Nilikuwa na dada Nelly ndio tumeachana muda sio mrefu, nataka kurudi nyumbani. Vipi?” “Nimekumiss tu. Naona muda unakwenda hurudi!” Akajilalamisha Tula kwa upendo. “Nitakuwepo hapo muda si mrefu.” “Pitia basi kuku wa Namanga.” “Nilifikiri utakuwa ulinunua tayari!” “Sikufanikiwa.” Jax akashangaa. “Tula! Uliniambia umetoka kwenda Namanga kufuata kuku!” “Nilifika hapo nikaishia kununua vitu vingine, nikasahau chakula.” Jax akanyamaza.

“Kama unaona shida, basi bwana.” “Sasa basi halafu tule nini!?” “Mbona hivyo Jax! Maswali gani hayo?” “Nimeuliza tu.” “Si ndio nimekwambia upitie kuku hapo!” Jax akaona amalize. “Nakuja.” “Unakuja vipi sasa?” “Nitaleta chakula.” Jax akakata simu.

Walikuwa na msichana wa kazi anayekuja kila siku asubuhi kusaidia kazi zile anazopewa na Tula, na kuondoka jioni, kasoro siku za jumapili tu kama kwa dada yake. Nelly hakuwa akitaka msichana wa kazi wa kulala nyumbani kwake. Hiyo ni tokea zamani anamlea huyo Jax. Jax amekua akiona nyumbani kwao anayeruhusiwa kulala ni yeye na dada yake tu mpaka alipoongezeka Tino aliyelazimishia undugu kwa nguvu. Kwa hiyo hata huyo msichana anayewasaidia kazi yeye na Tula, alimpata kutoka kwa msichana wa kazi za ndani wa Nelly. Ila hakuwa akijua kupika vizuri. Kwa hiyo Tula alikuwa akipika mwenyewe au wananunua chakula chao.

Kwa Tula.

Jax alinunua chakula na kurudi nyumbani. Tula akampokea. “Pole na kazi.” “Asante. Nimechoka sana leo. Nahisi nitawahi kulala.” “Kwema?” Tula akauliza vizuri tu. “Kwema, ni uchovu tu.” Tula akabaki akimtizama. “Vipi?” “Mbona kama kuna jambo halafu unashindwa kuniambia?” “Tula! Nimekwambia nimechoka nataka kulala, basi.” “Tokea lini tunafichana mambo!? Kwani dada Nelly amekwambia nini?” Jax akamtizama na kuelekea chumbani.

Tula akamfuata. “Mbona sikuelewi Jax!” “Labda uniulize. Maana mimi sikuelewi wewe unataka kunisikia nikikwambia nini au ulitaka nikwambie nini!? Kama ni mazungumza na Nelly, ni yakunihusu mimi na yeye. Mambo ya kifamilia.” Tula akashangaa sana. “Kwa hiyo gafla mimi nimekuwa sio familia?” “Najua unaelewa ninachokwambia, Tula. Nisichokwambia ujue hakikuhusu. Kwa kusema hivyo, kama huna swali, naomba nikaoge, nilale.” “Makubwa! Na chakula?” “Sitakula. Asante. Nimekuletea na chips. Wewe kula tu.” Jax akatoa nguo, na kuelekea kuoga.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hofu ya kuwa ameshaathirika ilimuingia sawia. Kufa mapema hakutaka. Ndio kazi ilikuwa imechanganya. Pesa inaingia kwa dola! Mafanikio ndio yananyesha kama mvua! Aje aanze kuugua! Akajifariji kuwa zipo dawa kama atakuwa ameathirika. Miezi miwili ilishakuwa imepita tokea aanzane na Tula.

“Lara!” Akamkumbuka kwa kuumia sana. Hakutegemea kama Lara angekuja kuumia kwa ajili yake. “Kweli sikufikiria!” Akawaza wakati akiendelea kuoga. Akaanza kukumbuka mabadiliko aliyokuwa nayo Lara. Kulala sana na kushindwa hata kupika. “Sikuwa hata na wazo la ujauzito!” Akajilaumu Jax huku akipitisha mikono yote miwili kichwani akiwa amesimama katikati ya bomba. Akabaki ameinama maji yakimmwagikia. “Kwa nini Lara hakuniambia?” Akalaumu mawazoni. Akataka kukasirika. Kumbukumbu zikamrudia alipokuwa hapokei simu za Lara na mwishoe kumfungia kabisa simu zake.  

Akakumbuka sura ya Lara akilia akiwa amejilaza kitandani kwake wakati akimtamkia anamuacha sababu ya Tula. “Tula aliharib..” Akasita kumtupia lawama Tula. Akanyamaza akikumbuka maneno ya dada yake akimwambia yupo kama baba yake. Alimuua mama yake. Jax akaanza kujichukia. Na yeye akajiuliza swali alilomuuliza Nelly. “Niliwezaje!? Nini kilinipata!?” Akaanza kujishangaa na kuumia zaidi kuua mtoto wake! Japokuwa hakuwa akijua, lakini kilimuuma sana. Akabaki amesimama majini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Mbona hutoki huko bafuni?” Akasikia sauti ya Tula. “We Jax?” “Ni nini leo Tula!? Mpaka bafuni?” “Hivi ujue wewe Jax mimi nakufahamu kwa kukuangalia tu? Huwezi kujificha kwangu.” Jax akafikiria. “Na hilo ndilo anguko langu.” Akawaza Jax. Akafikiria jinsi ambavyo hawezi kusema hapana kwa Tula. Alikuwa mbishi na msimamo mkali kwa kila mtu, lakini si kwa Tula. Ikifika kwa Tula ni kama hakuwa akifikiria tena.

Alitoka bafuni, akamkuta Tula amejilaza kitandani, hana nguo hata moja. “Nimechoka Tula. Naomba nilale.” “Wewe usifanye chochote, jilaze tu, niachie kazi yote mimi.” “Hapana. Sio leo.” Tula akashangaa sana. “Kuna nini Jax!? Dada Nelly mgonjwa?” Jax akajikausha na kuvaa boxer yake akapanda kitandani. Tula akaruka kama mshale. “Usiniambie kama umefukuzwa kazi!” “Unaongea nini wewe? Nani afukuzwe kazi.” Akamuona anajishika moyo.

“Afadhali. Maana nilikaribia kupata heart attack! Mjini tukiwa wote hatuna kazi! Hapatakalika.” “Nikikosa mimi si wewe utapata kazi? Hakuna chakupoteza.” “Kipo sana. Mimi siwezi kupata kazi kama yako Jax. Naomba tusiombee mabaya yakupate.” “Kwani mimi nilianzia hapa!? Si unaanzia chini unapanda taratibu!” “Na utuuzima huu!” Tula akashangaa sana. “Sisi tunakuwa watu wakuanza kila siku! Tokea chuoni mpaka leo, sisi tuwe tunaanza tu! Kwani tumelaaniwa!?” Jax akaona anyamaze. Akafunga macho kabisa.

 Old is Gold.

I

likuwa muda wa mchana Lara yupo ofisi za nyuma akifanya kazi. Kiongozi wao ambaye anakaa mbele na kina Sesi, Suzy na wengineo, akamfuata. “Unamgeni.” Lara akanyanyua uso na kubaki akimtizama. “Ni wewe Lara.” Akatoka. Lara akafikiria kidogo, na kuamua kwenda tu. Hakuamini alipomkuta Nelly pale. Akashindwa hata kumsalimia. Akabaki ameduaa. “Hujambo Lara?” Ikabidi amuanze yeye. “Shikamoo.” Lara akasalimia taratibu na wasiwasi mwingi usoni. “Marahaba. Nilikuja kukusalimia tu. Hamna jambo baya. Tunaweza kuzungumza hapo nje?” Akauliza kiungwana kama siye Nelly mkorofi. Lara akaangalia kulia na kushoto, akarudisha macho kwa Nelly. “Sitakuchukulia muda mrefu. Hata mimi nipo kazini.” “Tutoke hapo nje.” Lara akajibu na kuongoza njia.

Alisogea pembeni kabisa, ili wasisimame mlangoni. “Pole kwa matatizo.” Lara akabaki asijue ni yepi. “Namaanisha matatizo yote.” Akainama. “Unakula vizuri?” Nelly akamuuliza kwa upendo. “Nakula.” Lara akajibu huku akifuta machozi. “Kazana kula. Huo mwili umeisha kabisa!” “Najitahidi.” Akajibu Lara, asiamini kama anazungumza na Nelly. Nelly mbabe ambaye hajui kuuma maneno. Hashindwi kukwambia waziwazi kuwa hakupendi na kukufukuza kwake kwa kukuambia ondoka. ‘Sitaki kuiona sura yako’.

“Nimekuletea kitu cha kula. Twende kwenye gari yangu.” Akaongoza njia, Lara asiamini. Wakafika kwenye gari yake. “Unafikiri ni sawa nikirudi Dodoma angalau kuzungumza na wazazi?” Lara akashangaa sana. “Kwa nini dada Nelly? Itasaidia nini?” “Wazazi wako walitupokea vizuri sana. Kila wakati tulipokwenda, niliwaona jinsi walivyokuwa waungwana na wakarimu kwetu. Sitaki wote tuonekane ni wahuni tu. Tulianza kwa heshima, tunamaliza kihuni tu!” Lara akainama akifikiria.

Mwishoe akamwangalia na kumkuta akimtizama. “Sijui dada yangu! Ila sioni sababu ya wewe kupoteza tena muda wako na pesa kurudi mpaka kule tena! Sioni umuhimu.” “Japokuwa hata mimi sijui itakuaje nikifika huko, lakini acha tu niende. Angalau wasituone wote hatuna maana.” “Japokuwa hatukuzungumzia chochote, lakini nimeona mama amechukulia...” Lara akasita. Akajifuta machozi. “Pole sana.” “Naona wapo tu sawa.” “Mimi ni mtu mzima. Sidhani kama ni sawa kuacha mambo barabarani. Maadamu tulianzia nyumbani, naona nitarudi tu nyumbani.” Akamtolea mfuko wa chakula.

“Juu ni matunda, chini ni chakula.” Lara akapokea. “Asante sana.” “Kazana kula. Namaanisha weka juhudi za makusudi kwenye kula. Umenisikia Lara?” Lara akanyamaza. “Usijitese au kujiadhibu sababu ya upuuzi wa Jax. Hukuchagua litokee lililotekea. Hakuna aibu. Aibu ipo kwake. Yeye ndio anatakiwa kuona aibu na kujutia kuchukua maamuzi ya kijinga. Ni kama mwehu asiyejua ni nini anataka!” Lara akamshangaa sana Nelly.

“Yaani wewe unatakiwa kutembea mabega juu, kichwa mbele na kutizama watu usoni. Acha kulia kama uliyedhihakiwa. Umefanya kwa sehemu yako. Umethibitishia uma au jamii kuwa umekuwa mkubwa. Unaweza kutulia kama mwanamke wa kawaida na kutunza familia. Lakini umepata mwanaume mpumbavu aliyeshindwa kuingia kwenye agano. Yeye ndio mjinga. Aliyeshindwa. Acha kutembea kinyonge.” Lara akainama. “Umesikia Lara?” Lara akatingisha kichwa kukubali.

“Nitafurahi  nikija kukuona wakati mwingine, nikukute umeongezeka japo kidogo na hiyo sura imepata ujasiri.” “Nilipoteza mtoto wangu, dada. Sijui kwa nini! Japokuwa hakuwa hata ameanza kucheza huko tumboni, lakini inaniuma kupita kiasi! Nashindwa kusahau. Nashindwa kupuuzia. Najilaumu labda siku ile usiku nisingetoka hospitalini, ningemsikiliza yule nesi na yule daktari, pengine nisingempoteza mtoto wangu! Najuta na kujilaumu sana dada Nelly.” Lara akazidi kulia.

“Nalala masaa machache. Usiku nakesha nikijilaumu kwa mengi!” Nelly akaumia sana. “Pole Lara. Pole sana.” Akamshika begani. “Wala usipuuzie. Ni mtoto wako. Na hakuna njia nyingine ya kukufariji, lakini kwa ulivyo niambia, naamini ulimpenda mtoto wako, ilikulazimu tu kutoka hospitalini. Si ndio?” “Simu iliisha chaji. Nikajua Tino atanipigia kama alivyoniahidi, halafu anikose. Nilimtuma kwako angalau kukuulizia kulikoni. Nilikuwa na wakati mgumu dada! Sijawahi kupishana hata neno na mwenzangu. Sasa kuja kuachwa bila kosa! Tena kwa ajili ya mwanamke mwingine! Ilinidhoofisha sana. Sikujua kama muda wote nipo naye, kumbe alikuwa na mwanamke mwingine!” Lara akazidi kulalamika taratibu kwa Nelly na kujisahau kama ni yule Nelly wifie.

“Tula ana nguvu sana. Ana jinsi yake yakuingia kwenye kichwa cha Jax, nakumfanya ashindwe kufikiria chochote na yeyote. Anaishia kuwa mbinafsi. Na usifikiri alirudi muda mrefu! Ni kipindi baada ya sendoff yako. Hapo katikati tu. Jax alikusudia kukuoa. Kilichoendelea alipomtafuta Jax, ni wao wawili wanajua.”

“Na nimefurahi kwa kuwa mliishia pazuri na Jax. Hapakuwa na shida. Na mimi najua ulikuwa ukimuongoza Jax vizuri. Hata kama sikuwahi kukwambia, ila najua ulikuwa ukimuongoza vizuri. Ulimbadilisha, akawa kijana mzuri. Naomba katika hilo chukulia upande wa kujipongeza kuwa unauwezo mkubwa sana ndani yako. Kuwa unaweza kupenda na kuendesha familia yako vizuri. Ni vile tu uliangukia kwa kichwa maji. Lakini naamini Mungu atakupa mwanaume atakayeweza kupokea huo upendo, na kuuenzi.” Siku hiyo Lara akashangazwa sana na Nelly. Hakika hakutegemea.

Aliona upande mwingine wa Nelly ambao haukuwahi kuonekana na yeyote yule hapa duniani. “Jipe muda Lara. Utabeba watoto mpaka utafute kuwazuia.” Lara akacheka kidogo. “Wala usikate tamaa. Na hivyo unao moyo wa umama! Mungu hatakuacha. Atakulipa yote uliyopoteza na zaidi. Kaa mkao wa kusubiri.” “Nashukuru dada yangu. Nimefurahi tumeweza kuongea kidogo.” Nelly akacheka.

“Kweli watu wanabadilika! Mimi mwenyewe siamini kama ni mimi!” Lara akacheka na kumwangalia kwa aibu akimuogopa. “Unafikiri sijijui? Najijua sana, ila siwezi kujisaidia. Kuna maisha nilipitishwa nilipokuwa mdogo mpaka sasa hivi, sijui kuamini mtu. Lakini wewe nilikupenda.” Lara akashangaa sana mpaka Nelly akaona.

 “Kwani Tino hajakwambia?” “Tino nilimfukuza dada.” “Ameniambia. Lakini Lara, naomba msamehe tu. Ungemuhurumia kama ungemuona siku alipokuja kumuulizia mwenzie na kumwambia ukweli. Tino alilia. Alishindwa akwambie nini ila kumfuata Jax ofisini kwake, na kumtaka aje azungumze na wewe. Ni vile alichelewa tu. Lakini alimtoa Jax kwenye kikao na kumtaka aje azungumze na wewe. Na mpaka sasa hawazungumzi. Tino anakupenda sana, Lara. Hawezi kukuumiza hata kidogo.” Lara akainama.

“Sipo hapa kwamba amenituma! Mimi sio wakutumwa. Na wala hakuna kati yao anayejua kama nipo hapa na wewe. Kwanza hata ukiwaambia hawataamini.” Lara akacheka. Alimjua Nelly. “Naomba msamehe Tino. Alikuwa kwenye mshituko, hakujua ni jinsi gani ya kusaidia. Na ninauhakika kama angejua kuto kukupigia simu usiku ule kungeleta madhara makubwa hivyo, nina uhakika Tino asingekupigia tu simu, angekuja kabisa awe na wewe hospitalini.” Lara akainama na kujifuta machozi.

“Wote wawili wale ni wadogo zangu. Tino amejilazimishia mpaka imenibidi tu kukumkubali.” Lara akacheka huku akijifuta machozi. Nelly akatingisha kichwa. “Yaani Tino!” Wakacheka. “Lakini ujue Tino anakupenda, na asingependa kukuumiza hata kidogo. Kwanza hapendi kumuumiza yeyote. Ndio moyo wake ulivyo, hapendi kumuumiza mtu. Katika kipindi hiki, unamuhitaji sana kwenye maisha yako, usimfukuze. Anajutia sana.” Lara akanyamaza.

“Sasa mimi acha niondoke kabla sijaongea yatakayonifanya nijute baadaye.” Lara akacheka. “Asante kwa chakula, kuja na kuzungumza na mimi.” “Karibu. Jumamosi nitamlazimisha Tino anisindikize Dodoma kwa wazazi, nikaombe radhi.” Lara akainama. “Nitashukuru.” Akashangaa Nelly anambusu kichwani. Lara akamwangalia. “Nilikwambia heri niondoke kabla sijafanya mambo ya ajabu. Unaona sasa?” Wote wakacheka, Nelly akapanda kwenye gari yake, akaondoka.

Ilimfariji sana Lara. Ilikuwa faraja ya namna yake. Baada ya zaidi ya siku 60 za machungu, hofu, na kunyongea, angalau amepata faraja. Na faraja yenyewe kutoka kwa Nelly! Na busu! Lara akacheka wakati anaingia ofisini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wenzake waliridhika alipoingia akiwa anacheka. Wakamkimbilia jikoni. “Watoto wambea nyinyi!” Mdada mwIngine wa kitengo kingine aliwaambia alipowaona kina Sesi wanamkimbilia Lara jikoni. “Tuambie kila kitu.” “Ameniletea hiki chakula na kuzungumza na mimi.” Lara akawasimulia kila kitu.

Jax.

J

ax aliamka asubuhi na kukimbilia hospitalini wala si kazini. Kitu cha kwanza alitaka kuangalia afya yake. Akatolewa damu na kubaki ameinama akifikiria. Nini chakufanya kama akikutwa ameathirika ndio jambo lililokuwa likiendelea kichwani mwake. Akajilaumu kujiua akiwa mdogo. “Ni kwa nini nimeshindwa kufikiria!?” Akajiuliza Jax. Akafikiria shida zote alizopata Nelly mpaka kumfikisha hapo. Akakumbuka maneno machungu ya dada yake usiku uliopita. “Siwezi kuwa kama baba. Kama nikigundulika sija..”  Akaendelea kupanga mambo yake na kupotelea mawazoni.

Akasikia jina lake likiitwa kwa ajili yakupewa majibu yake. Akaambiwa kila kitu kipo sawa. Hana maambukizi yeyote yale ya vijidudu vya Ukimwi na hana ugonjwa wowote ule wazinaa. Hilo likamfurahisha sana Jax. Akiwa hapo hapo hospitalini akamtumia ujumbe Tino. ‘Tafadhali Tino, naomba tuonane kwa chakula cha mchana ndugu yangu. Najua tumeachana pabaya.’ Hapo hapo Tino akampigia. “Wewe ni mshenzi sana Jax. Unapoanza jambo lako unataka niwepo, ukifika mwisho huniambii. Sasa, sasahivi unataka baraka zangu kwa Tula, mwanamke aliyekwenda kujaribu maisha Norway, yakamshinda. Akaenda Uk. Amekaa Birmingham huko, wamemchezea mpaka wamechoka. Ameshindwa kufanya kazi, akawa hana hata pakuishi, analala kwa kila mwanaume mpaka watanzania wenzake huko wakamkopesha nauli kurudi nchini. Akawa anamangamanga tu hapa mtaani ndipo akapata habari kuwa unafanya kazi world benki.” Moyo wa Jax ukapasuka na kuumia sana.

Asijue mjini habari za yeyote, kokote zinaweza kupatikana. Ni yeye tu hakuwa akifahamu habari za Tula huyu aliyerudi, asijue kuvunja kwake ndoa na Lara, kukampa Tula umaarufu, watu wakaanza kuzisaka habari za huyo mwanamke aliyemudu kuvunja harusi iliyokuwa imebakiza siku chache. Walizisaka na kuzipata habari zote za Tula, kutokea siku anaondoka nchini mpaka amemuita Jax hotelini.

 “Amekuvulia tu chupi, akili yote imekuruka! Unamuacha mwanamke mzuri kwa ajili ya mal..” Tino akasita. “Wewe ni mpuuzi Jax. Achana na mimi. Umeniponza kwa mengi sana. Nimepoteza muda wangu nafanya vikao vya harusi ambayo hata wewe mwenyewe huithamini!” Tino akaendelea, Jax kimya akimjua Tino rafiki yake. “Umenifanya nimwage damu ya kiumbe kisicho na hatia kwa tamaa zako za kipuuzi tu! Lara amenifukuza, hataki kuniona kwa ajili yako wewe! Mwenzangu unafaidi mapenzi ya mwanamke wako, mimi ndio nabaki wakulaumiwa!” Tino akaendelea akijua Jax anamsikiliza.

“Washikaji wote wananiona mimi mpuuzi. Mbambaishaji. Silali vizuri kwa sababu yako, halafu wewe unalala na mwanamke wako bila shida! Acha kunibabaisha.” Tino akakata simu.  Jax akampigia tena. “Ni nini Jax?” “Naomba tukutane kwa chakula cha mchana.” “Safari hii unataka kunitumia kwa ajili ya harusi yako na Tula?” “Tino! Saa saba, pale kwenye mbuzi choma. Tafadhali.” Tino akakata. Lakini Jax alimjua. Akajua ndio amekubali. Akaondoka hapo kwenda kazini.

Jax na Tino.

Ilipofika mida ya saa saba kasoro akatoka kwenda sehemu waliyokubaliana na Tino. Alipokaa tu, akamuona na Tino naye anakuja. Tino akamwangalia kama ampige kofi. “Unamuoa lini? Ila huyo naona ugaramie mwenyewe. Sisi tuje tu kukuona unavyojifunga kitanzi shingoni.” “Kaa basi Tino!” “Unataka nini?” “Tutazungumzaje ukiwa umesimama?” Tino akakaa.

“Unasemaje?” “Naomba unisamehe.” Tino akabaki akimtizama kama haamini. “Kwa yote niliyosababisha upitie, fedheha ulizonibebea wakati wote mpaka sasa, nisamehe na ninakushukuru.” Tino akabaki amemkodolea macho.

Jax akaendelea. “Lara anaendeleaje?” “Wewe unafikiri atakuwa anaendeleaje?” “Acha nikwambie ukweli Tino. Ukweli kutoka moyoni.” Tino akajisogeza nyuma. “Wewe unajua urembo wa Lara. Unajua tabia yake. Nilipolala tu na Tula, nakushindwa kujizuia, nikarudia tena na tena bila hukumu, nikaumia sana kwa upande wa Lara. Nikajiambia kama nitamuoa yule binti, inamaana tabia yakuiba nje na Tula, itaendelea wakati yeye amekuwa mwaminifu kwangu.” Jax akaendelea.

“Nilishindwa jinsi ya kujirudi tena kwa Lara. Ningemwambia nini! Nikajua ataingia tu aibu ya muda, lakini baada ya muda mfupi tu, atakuja kupata mwanaume mwingine atakayeweza kumfanya awe na furaha.” “Katika hizo akili zako dhaifu na za kibinafsi, ulishawahi kufikiria kama yule binti alikupenda kwa dhati?” “Sio kwa kiasi hicho Tino. Kumbuka historia yangu na wanawake. Tula aliniacha kirahisi tu akahamia kwa mwanaume..” “Sio mwanaume. Kwa wanaume wengine.” Tino akamkata.

“Kwa hiyo nikajua haitakuwa shida hata kidogo kwa Lara. Tena ukizingatia uzuri alio nao, sikujua kama Lara anaweza kuumia kwa kiasi hicho.” Tino akamtizama, na kumuita muhudumu. “Sasa umenisamehe?” “Inategemea na neno linalofuata kuanzia sasa. Maana mimi nakujua Jax.” “Lara anaendeleaje?” “Hilo swali linakaribia kuniudhi Jax!”  Jax akatulia.

“Umekwenda kumuona siku za karibuni?” “Ni nini huelewi? Nimekwambia amenifukuza. Na ni wewe Jax ndiye uliyeniponza.” “Nataka kujua ukweli juu ya gari nililokuwa nimempa siku niliyomchumbia.” Tino akamtizama. “Tino?” “Wewe si unaishi na Tula?” Tino akauliza kwa hasira. “Nataka kusikia kutoka kwako kwanza kabla ya Tula.” “Kwamba sasa hivi unaniamini mimi kuliko Tula!?” “Tino! Gari nililompa Lara?” Jax alikuwa ametulia tu.

Muhudumu akaleta kinywaji cha Tino, Jax hakutaka kitu. “Ukalete na mbuzi pamoja na ndizi choma. Na mimi leo niwe kama Tula. Tule pesa ya benki ya dunia.” Tino akaongea kwa kumkashifu Jax. Lakini Jax akabaki ametulia tu. Muhudumu akaondoka.

“Gari, Tino?” “Alimpa mwanamke wako pamoja na pete ya uchumba.” “Kwa nini?” “Jax unaniudhi wewe ujue! Unaharibu zaidi!” Tino akawa kama anamtahadharisha. “Nataka kujua kama Tula alimfuata tena na kumdai au ilikuaje?” “Hebu subiri kwanza Jax. Wewe unataka nini? Itasaidia nini wakati umemtamkia wazi yule binti kuwa humtaki, unamtaka Tula. Sasa unataka nini tena?” Jax akanyamaza kwa muda. Tino akaendelea kunywa.

“Tino?” Jax akauliza tena. “Nisikilize Jax. Lara alikuwa mjamzito. Usiku ambao alinipigia mimi simu ili niende kwa Nelly nikaulize upo wapi au nini kinaendelea, alikuwa kumbe ni mgonjwa. Alinipigia simu akiwa analia. Akaniambia imebidi kusimamisha gari njiani, ameshindwa kuendesha. Ikabidi nimfuate. Nimtulize na kumuahidi nitakwenda kuzungumza na Nelly. Lakini nilimtuliza kwa uhakika kabisa kuwa asiwe na wasiwasi, wewe ni mwaminifu, huwezi kumgeuka.” Tino akaguna.

“Kumbe mshenzi wewe, umemdanganya ukiniweka mimi kwenye uongo wako, halafu usiniambie. Aliniuliza kimtego tu akitaka kujua kwa hakika kama tulikwenda wote Kisarawe, mimi nikawa sijui. Nikamwambia jumapili siku nzima nilikuwa kwa mama. Akajua umemdanganya, asiniambie. Akanyamaza tu kwa kuwa tulikuwa na wenzake na wameenda kula. Kumbe kuanzia hapo alipojua haukuwa na mimi Kisarawe, pressure ikaanza kupanda. Mimi nazungumza naye usiku ule, namtia moyo kila kitu kipo sawa, kumbe presure ipo juu sana. Tumeachana pale, mimi nikaenda kwa dada Nelly, yeye akarudi nyumbani. Anasema akajisikia hali inazidi kuwa mbaya. Akahofia mtoto, ikabidi kukimbilia hospitalini usiku wa saa 6 sijui saa 7! Wakakuta pressure juu sana. Wakamwambia lazima alale, wamuwekee dripu ili pressure ishuke.” Tino akaendelea.

“Anasema wasiwasi ukamzidia. Simu imemuishia chaji akiwa hospitalini. Akaogopa nisije nikampigia, nikamkosa. Kumbe na mimi niliposikia umejificha mjinga wewe na mwanamke wako, nilifunga simu mapema. Nikiwa nimepanga nimuache usiku ule angalau alale mimi nisiwe ndio nimempa habari mbaya, mpaka aje asikie kutoka kwako wewe mwenyewe kidume cha mbegu.” Jax kimya akisikiliza.

“Kumbe Lara anahangaika usiku huo halali mpaka kutoroka hospitalini ili kuhakikisha simu yake haizimi, ipo hewani kupata mawasiliano. Akisubiri labda mmoja wetu atamtafuta kumwambia ukweli wa kile kinachoendelea! Mimi nikaamkia ofisini kwako kukuomba uzungumze naye, kumbe na mwanamke wako naye kaamkia ofisini kwa Lara, aliyekwenda kazini pressure ipo juu, ametoroka hospitalini bila matibabu kukamilika.” Tino akaendelea.

“Mbweha wako akaanza kumpandishia Lara mbele za watu na kujigamba umemchagua yeye. Na anataka gari uliyompa wakati unamchumbia. Ile gari ni yake sasa hivi kwakuwa lengo la kupewa lile gari limekufa, yeye mwenye mme amerudi, anataka kupewa haki zake. Nasikia bosi wa Lara ndiye aliyemtoa yule mpuuzi mwenzio pale mbele ya Lara na wateja wengine, tena akivutwa nje na askari kwa kuwa alikuwa akiendelea kumtapikia Lara mbele ya wateja. Na unapajua pale jinsi panavyojaa. Lara akatolewa pale, pressure ikalipuka zaidi. Akiwa anarudishwa nyumbani kwenye kile kigari chenu kinachowatoa mate wewe na yule mwanamke wako, mimba ikatoka. Akaanza kutokwa damu kama nini sijui!”

“Kufupisha habari kwa kuwa hayakuhusu, baada ya yote, Lara aliporudi mjini, akawa amefikiria na kushindwa tena kupanda lile gari. Kwanza anasema ndipo alipofia mtoto wake. Mimba ilitoka ndani ya lile gari, na akaona alichoongea yule anayeshika akili zako, anayekufundisha kila kitu chakufanya tokea chuo, ni sahihi.” Macho ya Jax yalikuwa mekundu na mishipa yote ya kichwa ilimsimama.

“Akamtafuta mwanamke wako. Nasikia akamuomba msamaha na kumwambia yupo sahihi kwa yote aliyomwambia siku ile alipomfuata kazini kwake, ila alishindwa kujibu kwa kuwa alikuwa kwenye mshituko. Anaomba wakutane amkabidhi vitu alivyomdai. Yule mwanamke wako akaenda kukutana na Lara. Akampa gari, kadi ya gari, funguo na pete ya uchumba. Tula akaondoka na kumuacha Lara kwa amani bila matusi wala swali.” Tino akaendelea.

“Sasa najua kwa kuwa yeye ndiye anayekutawala. Anachagua nini akwambie na nini asikwambie, pengine kwa kuwa anakujua akili yako ni ndogo. Akaona hili asikwambie. Huna akili ya kulibeba na wala huna uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Ashakupima, akaona wewe ni mjinga. Akili yako ndogo. Unasubiri akwambie nini ili ufanye. Akikwambia nisubiri miaka minne mpaka nikalalwe na wanaume wengine ndio na wewe akuletee makombo, huna shida. Sasa nafikiri ameona mambo mengine yeye kama kichwa cha familia yenu ya kipuuzi, ayafanye tu bila kukushirikisha. Kwa hiyo subiri mambo ya saizi yako atakayoona yanakufaa, atakwambia.”

Chakula cha Tino kikaletwa. “Sasa mimi ninaharaka. Nikimaliza tu kula nataka nirudi kibaruani. Sasa kabla tajiri yangu na yeye hajaondoka naomba mletee bili kabisa alipe kabla mwanamke wake hajamuita. Maana akiitwa huyu na mwanamke wake, huwa akili inamruka. Anaweza akakimbia hapa bila kuaga, halafu wewe ndio ukaingia hasara. Sasa changamka ulipwe kabla mwanamke wake hajamuita. Ukimuona anaondoka, ujue mimi sikulipi. Kwa hiyo changamka.” Muhudumu akaondoka kwa haraka.

Tino akainamia chakula chake akaanza kula bila hata kumtizama Jax. Jax akabaki kimya tu. “Pesa ya benki ya dunia tamu jamani! Kweli Tula anafaidi.” Akang’ata nyama ya mbuzi, akasukumia na soda. “Aaaaah!” Tino akamkera zaidi Jax huku akiendelea kula.

“Sasa Lara anatumia usafiri gani kwenda kazini?” Jax akauliza. Tino akamtizama Jax kama ammeze. Akamuita muhudumu aliyekuwa akipita. “Naomba nifungie hiki chakula changu, nikale mbele ya safari.” Tino akasimama. “Hatujamaliza Tino!” “Kamuulize mwanamke wako hayo maswali ya kijinga. Acha kunifanya mimi mpuuzi kwa kuwa unalipia chakula ninachokula.” “Nataka kujua Tino.” “Halafu!?” Tino akamuuliza kwa kumsuta. Kimya.

“Niambie Jax. Ukishajua, utafanyaje?” “Basi tuache hilo. Naomba ukae tuzungumze.” “Changamsha mdomo maana chakula changu kikija tu, mimi naondoka. Sikuoni kama una jipya.” Tino hakukaa. “Kwa kuwa nimelipa karibu watu wote waliochangia harusi, naomba pesa iliyobaki yote umpe Lara.” “Kama kweli unamaanisha hilo, mwambie Tula anipigie yeye simu, anipe hayo maelekezo. Nakuhakikishia Jax, Tula akinipigia simu na kunipa hayo maelekezo, japokuwa Lara amenifukuza, nitafanya juu chini hiyo pesa imfikie. Lakini sio wewe. Wewe hujui ni kitu gani unaongea. Naweza nikamfikishia hizo pesa Lara, kumbe mwanamke wako hajakuruhusu. Halafu akazua jingine. Akaenda kumfuata Lara tena na kumdai.” Chakula chake kikaletwa kikiwa kimefungwa.

“Japokuwa wewe hutaki kufikiria, lakini nakushauri kabla hujajidhalilisha zaidi kwa unachotaka kufanya baada ya yote haya, ukaonekana mwehu, hujui unachokitaka, jaribu kufikiria. Na ukumbuke nafasi yako kwenye mahusiano uliyo nayo sasa hivi. Hakikisha una muomba ruhusa na ushauri mwanamke wako kwanza, akikukubalia, ndipo utoke kuja kuongea na wanaume. Acha kujidhalilisha Jax. Anzia kwa Tula, muulize akikushauri ndio utende ili kuepuka mkanganyiko.”

“Na japokuwa wewe ni mnyama usiyejali hisia za wengine hata kidogo. Mfikirie Lara. Najua kwako hujali juu ya mtoto aliyepotea, kwa kuwa alimbeba Lara sio Tula. Lakini jitahidi kuwa binadamu. Muache yule binti kabisa. Umempitisha katika wakati mgumu sana. Sidhani kama kwa sasa anashida na gari au pesa yako wewe na Tula. Ukitaka, hiyo pesa nimkabidhi Tula. Yeye ndio atajua chakufanya na hiyo pesa yenu. Kama alivyokusaidia kufanyia maamuzi ya gari yenu na ile pete.” Tino akaondoka. Jax naye akakaa pale kwa muda, akaamua kurudi kazini.

                                  ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wote wawatu, Tino, Tula na Jax, walisoma chuo kimoja. Mapenzi ya Tula na Jax, Tino anayajua ndani na nje. Wanafahamiana kwa karibu sana. Na hao wawili ni marafiki wakuongeleshana chochote, ila Tino na Tula, hawawezi kukaa sehemu moja kwa zaidi ya dakika 5, wasianze kutukanana. Hawapendani hata kwa kupishana, na sababu ni huyohuyo Jax. Wote wanamtaka Jax mahusiano. Na wote Jax ameshindwa kuachana nao tokea enzi hizo. Tino amefanyika kama ndugu na rafiki wa pekee aliyekuja kukubalika na Nelly. Tino tu. Hakuruhusu mtu mwingine yeyote afike nyumbani kwake kumuona Jax hata kwa kuazima kitabu. Na Jax alijua na kuheshimu hilo. Hakuwa akikaribisha mtu nyumbani kwao ila huyo Tino na Tula ambaye Tula alifukuzwa na Nelly vibaya sana, alipomkuta hapo kwake.

 

Jax kwa Tula.

J

ax alirudi nyumbani mapema tu, akamkuta Tula amekaa sebuleni yupo na simu yake mkononi kama anaye chati huku tv ikiendelea. Nyumba safi na amepika. Akaenda kukaa kwenye kochi la pembeni. “Pole na kazi.” “Asante. Vipi na wewe siku yako?” “Safi tu. Naona leo umewahi!” Akajibu Tula kwa kushangaa kidogo, akarudisha macho kwenye simu. Jax akatulia hakujibu, Tula macho kwenye simu. Moyo wa Jax ukashituka kuona pete aliyompa Lara, kidoleni kwa Tula.

“Naomba kuuona huo mkono wako wa kushoto.” Tula akakunja uso kwa mshangao. “Unataka nini!?” “Nimeomba kuona mkono wako.” “Kwa nini!?” “Hiyo pete umepata wapi?” “Na chupi niliyovaa pia utaniuliza nimepata wapi?!” Akajibu kwa kumuuliza akiwa na mshangao mkubwa mpaka usoni. Sio kwamba Tula amemjibu vibaya Jax, ndivyo alivyo Tula. Anaongea kile anachokifikiria kichwani na mdomo wake haukujaliwa kuchuja neno. Ila hilo halikuwa tatizo kwa Jax hata rafiki zake walipokuwa wakimlalamikia chuoni, yeye alisema hiyo ndio haiba yake. ‘Watu hatufanani’. Jax alimtetea. Sasa hapo anapotaka majibu ya kueleweka, ndipo na yeye anavuna alichopanda.

“Hiyo pete nilimvalisha Lara, imekuaje ipo kidoleni kwako?” Jax akaendelea kuhoji taratibu tu. “Unashangaa la pete tu! Mbona huulizi kwa nini mimi ndio nipo kitandani kwako na sio yeye! Acha mambo ya ajabu Jax! Umechoka nini?” Akamuuliza na kunyanyuka. “Kama unanjaa, chakula kipo mezani. Acha kupoteza amani humu ndani.” Tula akahama pale sebuleni na kumuacha Jax amekaa. Jax akabaki akifikiria. Akaamua kumfuata chumbani.

Akamkuta amejilaza kitandani macho kwenye simu. “Tula, naomba ukae tuzungumze.” “Nani amekwambia sikusikii? Wewe ongea tu.” Tula akaendelea na simu yake. “Pete ya Lara umeipata wapi?” Tula akakaa kwa hasira. “Unajua Jax, wewe unataka kunikorofisha tu! Wewe unasema ulimvalisha Lara, kwa ajili ya uchumba. Sasa unalilia nini!? Eti Jax?” Tula akauliza kwa hasira.

“Kwani Lara ni mchumba wako? Kwa nini unataka abakiwe na pete ya uchumba wakati si mchumba wako tena?” “Tula! Nakuuliza, pete ya Lara umeipata wapi?” Jax akaendelea na swali lake kama asiyetaka kupotezwa malengo. Alichokifanya Tula, akaivua ile pete na kumrushia Jax. “Hiyo hapo!” Akafyonza Tula kwa hasira. “Umenikuta nimetulia, umenianza mwenyewe! Hiyo pete hata ukimrudishia huyo Lara haiwezi hata kumuenea tena! Ataishia kuifungia tu wakati ni kitu cha thamani. Pesa yetu itapotea bure! Kimekonda kama kimbwa kilichozaa na kukosa matunzo! Labda uivae wewe kama unaona mimi nafaidi sana. Ili watu wajue na wewe umechumbiwa.” Tula akatoka. Ilimuuma Jax, mpaka akakaa chini kabisa sakafuni. Akaiona ile pete pale sakafuni. Akaiokota na kuitizama. Akabaki ameduaa akiitizama hiyo pete mkononi mwake.

Tula akarudi alikuwa ameacha simu yake kitandani. “Gari ya Lara iko wapi?” Jax akamuuliza kwa upole tu. “Kwa nini usimuulize huyo aliyekwambia ninayo?” Tula akachukua simu yake pale kitandani akataka kutoka. “Nilikununulia gari yako Tula. Kwanini uchukue na gari ya Lara?” “Nisikilize Jax. Lara mwenyewe ndiye aliyenipigia simu na kuniomba nikutane naye ili anipe gari. Nilipofika hapo ndipo akanipa na pete. Nilichofanya kwenye hiyo pete nikuongeza tu ukubwa, basi na kuivaa.”

“Kwa nini hukuniambia kama alikutafuta kabla ya kwenda kuchukua?” “Wewe Jax vipi!? Ili iweje? Nikwambie ili iweje!? Kama yeye mwenyewe ameona mimi ndio nastahili kuchukua hivyo vitu sio wewe, sasa kwa nini nikwambie?! Halafu nakushangaa sana! Kipi kinachokusononesha hapa mpaka ukae chini!? Vitu ulisema ulimpa Lara. Lara ameamua kunipa mimi, wewe unaumwa na kipi!?” Tula akamuuliza akimshangaa sana tena kwa ukali kabisa.

“Au wewe kila kitu unachopewa huko nje huwa unakuja kuniambia au mara ngapi huwa unakuja kuniomba ruhusa kabla hujapokea? Uliniambia nisimfuate tena, sikumfuata. Amenitafuta yeye mwenyewe! Ulitaka nikatae ili iweje?” Tula akaendelea kumuhoji. “Yaani mimi nipewe gari na dhahabu, halafu nikatae!? Kwa lipi? Kwa utajiri gani nilio nao!? Mimi si mjinga, wewe! Yeye karidhika na maisha, hataki gari wala dhahabu. Mimi nina dhiki mpaka kichwani. Nijikute tu na mimi nakataa! Sifanyi upuuzi huo.” Tula akatoka nakumuacha Jax hana swali la nyongeza.

Akaenda kuoga, akapanda kitandani bila hata kula. Mengi yalikuwa yakipita na kuendelea kichwani mwake. Tula alirudi pale chumbani. Akabadili nguo zake palepale mbele ya Jax akimwangalia.

“Nakwenda club.” Akamuaga Jax bila ya kumwangalia huku akivaa. “Nashauri ukitoka club uendelee tu na maisha yako.” “Unamaanisha nini!?” “Unakumbuka nilikukuta hotelini ukaniambia kama sitakukubali unarudi Norway sijui London!” Tula akashituka kidogo. Ila akajikaza. “London!?” Tula akauliza. “Ndiyo. Birmingham, London. Upo huru kurudi popote unapotaka. Hapa naomba usirudi tena Tula. Naona mimi na wewe hatutaweza kuja kuishi pamoja na maisha yakaendelea.” “Leo baada yakufanikiwa ndio unajua hilo? Miaka yote nakulisha pale chuoni hukulijua hilo?”

“Naona kwa mara ya kwanza maishani, umenifungua macho. Nitakuwa mzigo wako mpaka lini? Wewe ndio mwenye akili kati yetu. Unajua nini chakuzungumza, na kufanya. Muda na wakati sahihi. Umenisaidia sana, naona niwakati wa mimi kufikiria mwenyewe.” Jax akaendelea. “Na kwa kuwa unaakili sana, wewe sio mjinga kama mimi, naamini utafanikiwa zaidi yangu.”

“Mwanaume usiyejua kuishi na mwanamke. Kila mahusiano huyawezi. Ulianza na mimi, ukashindwa. Ukahangaika, ukampata yule mjinga mwenzio, ulikaribia kumuoa bila kufikiria. Nimekufungua macho kwa maneno machache tu, ukaamini sio mkeo, ukanitaka nikurudie. Nimekurudia, umeona nimetulia, umeanzisha tatizo, ili niondoke. Sasa hapa mimi siondoki, vimba na upasuke. Ndio ujifunze kuishi na watu. Acha kujifanya mwehu, uliyechanganyikiwa.” Tula akachukua pochi yake na funguo za gari, alikuwa amependeza haswa. Na vile alijaliwa uzuri wa umbile na sura, hakuhitaji vipodozi avutie. Na kuvaa vizuri sio tabia aliyokutana nayo ukubwani. Tula alizaliwa kwenye pesa. Anajua kuvaa kwa mavazi ya nje na ndani ya nchi. Ikifika kwenye swala la kununua nguo ya kuweka mwilini mwake, hababaishi. Hajui kujikosea.

Hapo alipo kwa muda mfupi tu aliokuwa ameamua kutoka, akajiandaa kwenda club, alishapendeza. Akatoka kwa kufunga mlango kwa nguvu sana. Jax mwenyewe akabaki kama amepigwa na butwaa. Kweli Tula alikuwa mbabe kwake. Na hakuonyesha kumuhofu hata kidogo tofauti kabisa na Lara.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment