Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com CHOZI LANGU! - SEHEMU YA 4. - Naomi Simulizi

CHOZI LANGU! - SEHEMU YA 4.

 Maamuzi mengine Magumu ya Jax,

Safari hii kwa Tula.

J

ax akakaa pale akifikiria. Lisaa likapita akifikiria. Likapita na la pili. Akaamua kufanya maamuzi mengine magumu. Akatoka pale kitandani kwa haraka kama swala. Akavuta shuka iliyokuwa imetandikwa na Tula pale kitandani. Safi. Akailaza sakafuni. Akaanza kutoa vitu vya Tula mezani, anavitupa sakafuni, juu ya ile shuka. Chupa za pafyum zilikuwa zikivunjika kila zikigonga sakafuni, lakini hakujali. Akakusanya kila kitu juu ya meza akatupia hapo kwenye shuka. Akaingia kwenye madroo na kabatini. Akamtolea vitu vyake vyote. Kila mahali mpaka mswaki wake. Alichanganya humo ndani mpaka taulo alilokuwa ametoka kuogea. Akatupia hapo. Akafunga vizuri. Akavuta mpaka getini.

Jax alipata nyumba mpakani mwa Kawe na Mbezi beach. Haikuwa nyumba kubwa sana, lakini nzuri na ya kisasa. Akatoa nje kabisa ya geti. Mlinzi akamsogelea. “Unataka nikatupe?” “Hapana. Ni mizigo ya Tula. Akirudi kutoka matembezini, hakikisha anachukua mizigo yake. Mwambie hakuna kitu chake chochote kilichobakia ndani. Kwa hiyo asiingie. Umenielewa?” Yule mlinzi akabaki ametoa macho. “Akiingia hapa ndani, ujue umeruhusu mtu hatari ndani ya nyumba yangu. Na umpigie simu bosi wako, umwambie  kwa miezi miwili mfululizo, nataka ulinzi wa mchana na usiku. Umenielewa?” “Ndiyo.” “Kwa maana nyingine, hilo geti lisikae bila mlinzi, na Tula ni mtu wa kwanza anayetakiwa kukaa mbali na hii nyumba.” Jax akarudi ndani.

Akakumbuka Tula ana mabegi stoo. Akaenda kuyachukua na vitu vyake vyote na kwenda kuvitupa nje. Juu ya lile furushi lake kubwa la vitu. “Usihangaike kumjibu chochote. Mpe ujumbe wake, basi. Akibisha, mwambie unamuitia mwizi au unampeleka polisi kama mwizi mwingine tu.” Akamalizia hayo maagizo kwa mlinzi, akarudi ndani. Kwa mara ya kwanza akajisikia amepata nafuu kifuani.

Kwa Lara.

K

esho yake mchana muda ambao alijua kina Lara huwa wanakwenda kula, Jax akaendesha mpaka karibu ya ofisi yao. Akaegesha gari ili kujaribu bahati yake kama atamuona Lara. Lile neno aliloombiwa na Tula kuwa Lara amekonda kama mbwa aliyezaa na kukosa matunzo, lilimuuma sana Jax. Baada ya muda akamuona Lara ametoka peke yake akaenda kusimama nje kabisa, sehemu yenye jua kama aliyekuwa akisikia baridi. Akasimama kwa muda mfupi akamuona Sesi ametoka na sweta, akaja Suzy akionekana anaongea zaidi anapowasogelea. Sesi na Warda aliyekuwa anakuja nyuma yao wakaanza kucheka kile anachoongea Suzy. Akajua ni kawaida ya Suzy, porojo zake. Lara alikuwa akivaa lile sweta aliloletewa na Sesi.

Wakamsubiri amalize kuvaa wakaongozana. Akajua wanakwenda kwenye kibanda cha chips. Lara nyuma amekunja mikono ndani ya sweta kama anayesikia baridi kali, kimya! Wenzake wanacheka mbele. Jax akabaki ameduaa. Kweli Lara alirudi kuwa kama mtoto wa darasa la tatu. Kwa asili hakuwa mnene. Lakini aliisha sana. “Sasa kwa nini asikie baridi na joto lote hili!” Jax akaendelea kumuangalia akipita kwa mbali kidogo. Alijua kwa hakika hawatamuona. Walimpita na kupotea kabisa. Jax akabaki ameduaa.

Mwishoe akatoa simu yake na kuanza ku Google kwa lugha zote mbili. Kingereza na kiswahili. ‘Kwa nini mtu asikie baridi kwenye joto?’ Majibu yakaanza kuja mengi. Akaanza kuyasoma huku akimtafakari Lara vile alivyomuona. “Alionekana mnyonge, lakini si mgonjwa.” Akajaribu kuvuta kumbukumbu zaidi akimlinganisha na yale majibu.

 Akajiambia sababu itakuwa ni upungufu wa madini ya chuma. Hana damu yakutosha mwilini. Akakubaliana na hiyo sababu. Akakumbuka aliambiwa Lara alitokwa na damu nyingi sana kipindi mimba ilipotoka. “Sasa sijui kama walimuongezea damu! Na kwa kiasi gani!” Kwa mara ya kwanza Jax akaanza kumuhurumia Lara zaidi. Hali yakujali ikamjaa, akaanza kufikiria nini chakufanya ili kumsaidia. Akakaa pale kwenye gari akifikiria. Muda ukizidi kwenda.

Mwishowe wazo likamjia. Akaenda kwenye mgahawa uliokuwa karibu na ofisini kwa kina Lara. Hakuwa ameegesha mbali na hapo. Ni kama alizunguka tu mbele yake. Huwa wanauza vyakula vizuri sana, ila bei ilikuwa juu. Mtu wa mshahara wa kawaida, asingeweza kumudu kula kila mara hapo. Hata yeye mwenyewe Jax hakuwa akila hapo kipindi anafanya kazi CRDB japo baada yakumpata Lara, walishakwenda hapo mara kadhaa. Zaidi mwanzoni ili kumtoa katikati ya Suzy na Sesi. Wapate muda wa chakula cha mchana wakiwa wawili tu.

Jax akaingia hapo na kuomba kuonana na muhasibu wa hapo. Akaingizwa ofisini kwake. “Nataka kuweka bili ya matunda yakuongeza damu na juisi. Kuanzia jumatatu mpaka ijumaa. Lakini nitataka huduma ya delivery.” Yule muhasibu akajua hiyo ni pesa nzuri. “Ulitaka vipelekwe wapi?” Akamuuliza Jax. “Pale kwenye kampuni ya simu. Afikishiwe Lara.” Yule muhasibu akakumbuka. Akamtizama vizuri Jax. “Yule binti aliyekuwa aolewe, lakini mwanamme aka..” Akatulia. Kama aliyejiambia isije kuwa anaongea na huyo bwana harusi mwenyewe. Akatulia. Jax akabaki ametulia mbele ya kiti chake huyo muhasibu ambaye ni kama meneja wa huo mgahawa pia.

“Ulitaka apelekewe muda gani?” Akabadili mazungumzo kwa haraka na kuanza kuandika ili Jax asibadili mawazo. “Kwa leo iwe kwenye saa 9 mchana. Lakini huyo atakayempelekea, amuulize ni muda gani anataka awe anapelekewa.” Yule muhasibu akaandika kidogo. “Naomba kujua itagarimu kiasi gani.” Akataka kumuita muhudumu wa jikoni. “Hapana. Hii nataka iwe kati yangu mimi na wewe. Mtu yeyote asijue hayo matunda na juisi vinatoka wapi. Sijui unanielewa?” “Kabisa.” Akajibu kwa haraka.

“Hapana. Nataka uelewe vizuri. Si Lara, wala wafanyakazi wengine wanatakiwa wajue hili. Yapo matunda niliyoona yanaongeza damu kwa haraka. Nataka hayo ndio awe anatengenezewa juisi kwa siku atakazokuwepo kazini na matunda. Apelekewe na akiuliza yanatoka wapi, mpelekaji aseme hajui. Kwa kuwa ni kweli awe hajui yanakotoka zaidi ya jikoni kwenu. Sijui unanielewa?” Akatulia kidogo.

“Namaanisha nikitoka hapa, iwe ni makubaliano kati yangu mimi na wewe tu. Basi. Unafikiri utaweza?” “Nitaweza na nitahakikisha kila siku anapata matunda yake na juisi.” “Asante. Basi naomba kujua garama.” Yule muhasibu akapiga simu, akazungumza na muhusika. Akapiga mahesabu, akampa Jax. Jax akalipia kwa siku tano. “Tutaona itakavyokwenda. Kama hakuna litakaloharibika, tutaendelea.” Walipowekana sawa, Jax akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika saa 9 mchana, Lara akiwa anafanya kazi akapokea simu kuwa anaitwa mbele, kuna mgeni wake. Lara akatoka na mshangao. Akakutana na kijana aliyevaa sare za ile hoteli. “Haya ni matunda yako, na hii ni juisi yako pia. Nimetumwa nikuletee. Ila nataka kujua, kesho unataka nikuletee saa ngapi?” Bado Lara hakuwa hata ameelewa. “Hivi vitu vinatoka wapi?” “Pale mgahawani kwetu.” Akamtajia jina. “Nafahamu hilo ila nataka kujua nani amekutuma ulete?” “Sifahamu. Ila natakiwa kujua muda unaotaka uwe unaletewa kila siku.” “Mimi siwezi kupokea vitu ambavyo...” “Wooo! Wooo!” Suzy akaruka kama mshale na kumuacha mteja aliyekuwa akimuhudumia.

Akamsogelea yule muhudumu. “Naomba nikupokee.” Akavivuta kutoka mkononi kwa yule muhudumu. “Sasa, uwe unaleta kila siku saa nne asubuhi.” Suzy akamwambia yule muhudumu. “Suzy!” Lara akashangaa sana. “Acha habari zako za zamani.” Akamjibu Lara na kumgeukia yule muhudumu. “Na kesho ulete saa nne asubuhi. Haya, kazi njema.” Suzy akamuaga yule muhudumu. Watu wakacheka.

“Haya mwali, twende ukale. Unakataa nini wewe!?” Akamvutia Lara jikoni. “Mwili huo unahitaji chakula. Umekonda Lara, hutizamiki.” “Matusi hayo Suzy.” “Nakwambia ukweli. Kula.” “Sasa nani amemtuma?” “Inahusu!? Wewe kula. Atajijua mwenyewe huyo secret admirer.” Lara akacheka na kufungua ule mfuko.

Matunda yalipangwa vizuri. Akafungua na juisi. “Hii juisi mbona nyekundu hivi! Nitaweza kweli!” “Kunywa kama dawa. Huwezi kujua, inaweza kukusaidia Lara. Ulipoteza damu nyingi sana.” Aliposema tu hivyo akapata wazo. “Nini?” “Nimejua mleta matunda.” Sesi alikuwa akimuhudumia mteja wakati yale matunda na juisi vikiletwa. Alipomaliza tu, na yeye akakimbilia jikoni.

“Niambie mwali. Nani secret admirer wetu?” “Wewe akili zako kama Suzy. Hakuna secret admirer, ni dada Nelly huyu.” “Kweli.” Wote wakakumbuka alimletea chakula na matunda. Lara akakumbuka alimwambia alipoteza mtoto, akajua ndio anataka aongeze damu. Lara akacheka na kuanza kula. Alifurahi sana kuona amemjali zaidi.

“Njooni tule.” “Mmh! Japokuwa natamani, lakini hapana Lara. Unahitaji kula. Umekonda sana.” Akakataa Sesi. “Hata kuonja tu Sesi na wewe?” Akauliza Suzy. “Kidogo tu Suzy na uondoke hapa, umuache mwenzio ale.” Suzy akacheka na kuchukua uma. Akala kidogo, wakamuacha Lara peke yake. Akatamani kumshukuru Nelly, lakini hakuwa na namba yake. Akabaki kujiuliza ni jinsi gani atamshukuru. Asijue. “Tino!” Wazo likamjia. Akakumbuka hazungumzi na Tino. Akaamua kunyamaza na kuendelea kula. 

Wema Hauozi.

N

elly alikusudia kurudi kwa wazazi wa Lara kuonana nao. Bado hakujua ni nini atawaambia. Ila aliazimia kwenda kuonana nao. Walikuwa wakarimu sana kwao kipindi walichoenda kutoa mahari na kwenye sendoff ya Lara. Nyumbani kwao ilikuwa uswahilini haswa na ni padogo, kwa hiyo wageni wote wa Jax na huyo dada yake walishukia hotelini, lakini mama yake Lara alihakikisha anawapelekea chakula kizuri na kila wanapokwenda kwao pia aliwatayarishia vilivyo, ilimradi tu kuonyesha upendo wao kwao.

Ijumaa akampigi simu Tino. “Nina tiketi yako ya ndege ya kwenda Dodoma, nyumbani kwa kina Lara. Tunaondoka mimi na wewe tu. Kesho asubuhi, tunarudi jioni.” Nelly akamaliza. “Hata hujanijulia hali dada yangu! Kama nipo hospitali?” “Nitakuja kukufuata hukohuko tuondoke. Usinipotezee muda mimi. Nakutumia picha ya tiketi uone muda halisi. Usinicheleweshe.” “Au nije nilale kabisa nyumbani kwako ili iwe rahisi?” “Kwa nini hupendi kwako wewe Tino?” Tino akaanza kucheka.

“Kumbuka nakusindikiza Dodoma.” Nelly akacheka. “Na sio uchelewe kuja. Ukikuta nimefunga mlango, usigonge kengele. Uondoke.” “Sasa si nakuja na njaa kabisa?” Nelly akamkatia simu. Tino akaanza kucheka mwenyewe. “Nelly!” Akatingisha kichwa huku akimfikiria. Lakini akafurahia wazo la kurudi kwa kina Lara. Angalau kutengeneza au kuachana kwa amani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tino alipokuwa nyumbani kwa Nelly, akampigia simu mama yake Lara na kumuomba kama wanaweza kwenda kuwaona siku inayofuata. Mama yake Lara aliwakaribisha lakini akiwa na wasiwasi sana. Akajua wanakwenda kudaiwa tu mahari yao. Hapo hapo akampigia simu Lara. “Naona wakwe zako wanakuja kudai mahari yao.” “Kwa nini udhani hivyo?” Lara akamuuliza mama yake. “Wanakuja kesho. Tino, yule kijana aliyeturudisha huku wakati mgonjwa amenipigia, amesema anakuja na dada yake Jax, ambaye ndio kama mama na baba yake.” Lara akatulia akimsikiliza mama yake anavyomuelekeza kwa wasiwasi kana kwamba hamfahamu Tino na Nelly.

Mama yake akajieleza mengi kwa hofu mpaka akamuingizia hofu hiyo Lara. Akawahurumia wazazi wake. “Lakini vile vitu kama vitenge, blangeti, vipo. Ni pesa tu. Tulitumia zote. Mambo ya...” “Usijali mama. Wakihitaji mahari yao, waambie tutawalipa kidogo kidogo. Dada Nelly anapesa sana. Sidhani kama atajali. Usiingiwe hofu.” Lara akajaribu kumtuliza mama yake. Huo usiku haukuwa mzuri kwa Lara. Historia ikajirudia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Asubuhi siku ya jumamosi alibaki amelala tu kitandani akiwaza. “Haiwezekani dada Nelly akawadai wazazi wangu. Anaonekana alinihurumia na ni kama alisema anataka aende akamalize mambo kwa amani.” Akajifariji Lara. “Lakini watu wanabadilika!” Akamkumbuka Jax alivyombadilikia. Akawa mpole akisubiria kusikia kutoka kwa wazazi wake kujua kitakachojiri.

Japokuwa wazazi wa Lara walikuwa na wasiwasi wa kudaiwa, lakini walijitahidi kuwa wema. Waliandaa chakula cha mchana kizuri na mapema ili wakwe zao wakija, wawakarimu. Hawakuwa na gari la kusema watakwenda kuwapokea uwanja wa ndege, wakabaki tu hapo nyumbani wakiwasubiria. Ilipofika saa tano na nusu, Nelly na Tino wakawa mlangoni wakigonga. Wakakaribishwa kwa ukarimu mpaka Nelly akajisikia vibaya, wasijue ule ukarimu umejawa na hofu ya kudaiwa pia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika kwenye saa 6 mchana, mtu akagonga wanapoishi Lara na wenzake. Warda akafungua. “Nimetumwa kwa Lara.”  Wote wakatoka. “Nina mizigo yako hapa. Nimeambiwa ukipokea, ukasaini hapa, ndio nitalipwa.” “Na nani?” Lara akauliza, akitegemea safari hii pengine atamjua kwa hakika huyo anayemuagizia vitu.  “Mwenye duka.” Lara akashangaa. “Wakati wewe unashangaa, acha mimi nichangamkie mlo. Tumuwezeshe Warda huko jikoni.” Suzy akaanza kuingiza ndani mifuko hiyo ya chakula na mafuta yakupikia. Ikabidi tu Lara aweke saini na kumshukuru huyo dereva, akafunga mlango na kukimbilia hiyo mifuko. Alikuta mayai trei mbili, mafuta ya kupikia, sukari, blueband, maziwa fresh na mtindi, pamoja na kuku wabichi wawili. Lara akawaangalia wenzake.

“Vinatoka wapi jamani!?” Lara akauliza tena. “Si ulisema kwa dada Nelly!” Sesi akajibu huku akiendelea kuangalia. “Dada Nelly yupo safarini!” “Si yule aliyeleta alisema ametumwa na mwenye duka. Pengine alitoa maagizo kabla hajasafiri.” “Labda.” Akajibu Lara huku akifikiria. “Mimi naomba wakati mnawaza, tumpe huyo kuku Warda, aanze kufanya vitu vyake.” Suzy akatoa wazo. “Ila Lara apate kwanza supu jamani! Nahisi hawa kuku wameletwa wakienyeji makusudi ili Lara apate supu. Tusijisahau. Nafikiri lengo la mletaji, ni kwa ajili ya Lara arudishe huo mwili.” “Sesi naye!” “Vyakula vipo Suzy, tuwe waungwana.” “Mimi nafikiri tutengeneze tu mchemsho, tule wote.” Lara akatoa wazo lililomfurahisha sana Suzy akampa mpaka busu.

“Hufai wewe! Si umesema unataka kupungua?” “Sio kwa kutokula kuku, Sesi bwana! Kwanza kuku hawanenepeshi.” Wakabishana hapo wakifurahia kuku lakini Lara tumbo joto, akifikiria wazazi wake na ugeni walio nao huko kwao.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika saa nane, Lara akaona simu ya mama yake. Akakimbilia chumbani kwake. “Wamesema nini? Wamewadai?” Lara akauliza kwa wasiwasi. “Mwenzangu imekuwa kinyume! Dada yake mkarimu huyo!” “Dada Nelly!?” Lara hakuamini. “Sana. Ametuomba radhi na pesa ametoa.” Lara hakuamini. Zikaanza stori kati yake na mama yake. Kidogo akafarijika. Akaweza hata kwenda kunywa supu iliyotengenezwa na Warda. Akaamini Nelly ndiye mtumaji. Akafarijika na angalau akaona imemrudishia sifa kwa wanao mzunguka. Alijua hata kule kuletewa matunda ofisini, angalau alijua maneno yataenea na kuona hata kama mchumba alimkataa, basi mkwe anamjali. Akafurahia hilo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika mida ya saa mbili, wakasikia hodi tena. Suzy akaruka. “Weza kuta mzigo mwingine.” Mpaka Lara akacheka. Akaenda kufungua. Wakamsikia akisema, “Akhaaa! Kumbe wewe!” Akafunga mlango bila kumruhusu mgeni kuingia ndani. “Nani!?” Wote wakamuuliza. “Hakuna mtu. Upepo tu.” Wakasikia hodi tena. Safari hii Lara akasimama yeye ili akafungue kwa kuwa Warda alikuwa akimsuka Sesi. “Wala usijisumbue. Utakasirika tu.” Suzy akamuonya.

Lara akafungua. “Kabla hujanifungia nje..” Lara akaondoka pale mlangoni kurudi sebuleni walipokuwa wamekaa wakiangalia tv. Tino akafuata nyuma. “Nilikwambia mimi. Usifungue mlango. Ona ulichoingiza humu ndani!” “Acha hizo Suzy! Mimi nimetumwa na mama yake Lara.” Lara akamwangalia. “Kweli tena nimetumwa.” Akaweka msisitizo kwa Lara. “Umetumwa nini kama sio uongo wako, wa kutafuta gia ya kuingilia hapa?” Suzy akaendelea kumkaba Tino. Lara akabaki akimtizama. Tino akameza mate.

Akaanza. “Kwanza alitaka kujua unaendeleaje!” “Toka Tino. Huna jipya. Lara anaongea na mama yake kila wakati. Anajua anavyoendelea. Toka.” Suzy akamfukuza. “Subiri kwanza. Mbona haraka?” Tino akajaribu kumtuliza Suzy. “Haya, sema.” Lara alibaki akimwangalia tu. “Amenituma, nimsalimie sanaaaaa.” Mpaka Warda na Sesi wakacheka. “Toka Tino.” “Lara kipenzi changu, mama anakusalimia sana. Amenituma.” “Ungetuma ujumbe sio kuleta bichwa lako hapa.” “Si unyamaze Suzy! Hayakuhusu.” “Lara shoga yangu. Ukimuumiza yeye ujue umeniumiza na mimi.” Lara alikuwa kimya tu.

“Nimekuletea na korosho, Lara.” Tino akaendelea akibembeleza. “Nashukuru Tino.” Akajibu Lara taratibu tu. Tino alifurahi mpaka akaruka. Akaenda kukaa pembeni yake. “Lione lilivyofurahi. Ungelifukuza hilo.” “Suzy kwa wivu! Asione wenzake tunapendwa!” Akauvuta mkono wa Lara na kuubusu. Lara akacheka. “Bwana nimekumiss! Usinifukuze, wangu! Ujue mimi siwezi kukuumiza.” “Uliniumiza Tino. Sikutegemea kama na wewe unaweza kunifanyia hivyo!” “Ni vile nakupenda Lara. Sikutaka mimi ndio nikupe habari za kukuumiza.” Lara akanyamaza.

“Pole wangu.” “Nimepoa. Asante kwa kurudi kwa wazazi.” “Wazo la dada Nelly! Mimi mwenyewe kanishangaza! Nilikuwa siamini kama ni yeye au Mungu ameshusha mwingine.” Angalau wakaanza kucheka. Tino akampa habari za Dodoma alikotoka kwa wazazi wake, angalau Lara akafarijika na aibu ya kuachwa ikaanza kupungua.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Zawadi za hapa na pale kwa Lara hazikukoma. Zaidi vyakula. Matunda na juisi vikaendelea kila siku. Jumatatu mpaka ijumaa. Na kama jumamosi hii aliletewa vyakula vingi, basi jumamosi inayofuata kuna kuwa kimya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Angalau kicheko kidogo kikarudi kwa Lara, Tino naye akajisogeza karibu zaidi. Upendo, kujali kwa hapa na pale. “Dada Nelly amekuwa akiniletea vyakula, Tino. Natamani kumshukuru lakini sina namba yake.” Lara alimwambia Tino jioni hiyo wakati wametoka kazini, Tino anawarudisha nyumbani. Huwapa lifti pale anapoweza. “Naomba niwe mkweli kwako Lara.” Lara akamtizama. “Dada Nelly hapendi mtu asiyempa yeye mwenyewe namba yake, ampigie. Si unamjua alivyo mkorofi?” Lara akatulia.

“Na katika watu wagumu kuwaelewa hapa duniani, ni Nelly. Haileweki muda gani anaweza akawa ametulia au amecharuka. Nelly niliyemuona Dodoma, sijawahi kumuona tangia namfahamu. Na sitashangaa kuwa anaweza asinitafute tena mpaka hata baada ya miezi.” Lara akatabasamu.

“Ukimfuta nyumbani?” “Anaweza akufungulie mlango au asikufungulie, akuongeleshe nje ya mlango.” Mpaka kina Sesi wakacheka. “Au akakwambia acha matatizo yako kwa mlinzi getini, atamwambia asubuhi wakati akienda kazini.” “Na bado tu unaenda!?” Akauliza Suzy kwa mshangao. “Sana tu. Tena wakati mwingine naenda na kulala kabisa.” “Sasa si anakuwa amekufukuza?” “Kufukuzwa na dada Nelly ni jambo la kawaida. Kuitwa au kufunguliwa mlango ndio kitu cha ajabu. Nishamzoea nafikiri na ndio maana ananipenda. Sijali akinifukuza. Naweza nisiondoke, nikaendelea kuongea naye hapohapo. Yeye yupo sebuleni kwake, mimi nipo nje.” Wakashangaa lakini sio Lara. Lara alimjua huyo dada, yeye alikuwa akicheka tu.

“Siku akiamua, ananipigia simu nikanywe naye. Mtakunywa mpaka mchoke, kisha analipia yeye. Jax anasemaga akiwa anakunywa hivyo anakuwa na kitu kina mkera.” “Hajaolewa?” “Hataki hata kusikia. Wala hataki mtoto.” Tino akajibu na kuongeza. “Kwanza sijui kama ana moyo wa umama yule!” “Lakini alimlea mdogo wake mpaka amemfikisha vile! Kwa hiyo anaweza ila labda hataki ameamua kuweka akili zake kazini tu.” Akaongeza Lara kinyonge. “Na kweli. Naona amewekeza kazini. Na upande wa kazi, amefanikiwa sana. Ila ninachojaribu kukushauri Lara, mwache tu.” Lara akamwangalia.

“Kama angetaka shukurani, angekufuata au angetaka ujue. Kufanya hivyo ni kukufikishia ujumbe kuwa hataki kufuatwa. Dada Nelly hawezi mahusiano hata ya urafiki wa kike. Hawezi hata simu za salamu. Jax mwenyewe akimpigia kumsalimia anamuuliza anashida gani?” Wakacheka na kuanza kusimuliana vituko vya Nelly, lakini Lara akaelewa kuwa ndio ameambiwa amuache.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mambo ya Lara yakaendelea kutulia. Ile aibu na maneno ya kuachwa vibaya yakaanza kubadilika. Habari iliyokuwa imebaki kuwa Lara amepata secret admirer, anamtunza na kumjali. Suzy maneno mengi akasaidia kusuta watu kwa kusambaza hiki na kile. Kutoka kurudi kutembea na daladala, Tino akaanza kuwarudisha jioni anapoweza au kama hajatingwa na kazi zake. Basi atawachukua wote wanne na kuwarudisha kwao ndipo apitie baa kunywa. Asubuhi kina Lara walimwambia huwa wanawahi sana kuamka, wanapata daladala ya mpaka Posta kiurahisi.

Maisha ya Lara yakaendelea. Akaanza hata kutulia. Kila alipokuwa akimkumbuka Jax, aliweza kujituliza kwa hili na lile akijiambia Jax hakukusudiwa kuwa wake. Alimtamkia wazi amemchagua Tula, mpenzi wake wa zamani. Hilo bado lilikuwa likimuuma sana Lara. Kwamba muda wote huo wa karibu kumaliza miaka miwili, alikuwa naye lakini mawazo yapo kwa Tula! Ilikuwa ikimuuma sana.

Kwa sababu ni kweli kwa upande wake Lara, yeye alitulia kabisa. Tokea ampate Jax, akili ilitulia kabisa. Hakuwa akihitaji chochote kutoka kwa yeyote. Alimkuta Jax anakazi CRDB bank, alikuwa na pesa ya kawaida ya kumuhonga japo kidogo. Na kwa kuwa Lara mwenyewe alikuwa na kazi, na hakutoka kwenye familia yenye shida sana ila matatizo tu ya kawaida, basi, akatosheka na vile alivyo Jax.

Mambo yakazidi kuwa mazuri pale Jax alipohamia kwenye benki ya dunia. Neema ikaongezeka. Maisha yao yakawa mazuri hata muonekano wa nje wa Lara, ulionekana mambo ni mazuri. Japokuwa Jax hakuwa mwanaume wa ajabu sana kwa uzuri. Kijana wa kibantu tu, lakini Lara binti mzuri wa mjini, akaridhishwa na maadili yake. Si mlevi wala macho juu. Mtulivu. Ukimuomba chochote ndani ya uwezo wake, anasaidia. Anakula chochote atakachopikiwa na Lara. Hajui kukosoa, si mkali, Lara akampenda sana Jax.

Alishakuwa na mwanaume mwingine kabla ya Jax, lakini ujana ulikuwa mwingi. Hakuwa ametulia. Maisha yake ni starehe tu na Lara, akijionyeshea ufahari kwa kummiliki Lara. Akiwa na Lara atajisifia kujishindia mrembo wa kutoka jiji kuu. Kina Lara walikuwa wanatoa kwenye kabila la Warangi, hukohuko Dodoma, wilaya ya Kondoa.

Alikuwa binti mzuri sana kwa kumwangalia. Hakuwa mrefu wala mfupi. Ila katika udogo wake wa maumbile, ungependa kumuangalia vile alivyogawanyika vizuri. Mcheshi, na maneno mengi kama Suzy sema yeye hakujua kutukana na alikuwa na mipaka. Alijua aongee nini na kwa nani. Si mropokaji hovyo mbele ya asiowajua. Kidogo alijaliwa soni ya kike.

Nywele nzuri, laini halafu kama za mama yao. Lakini wao wote watatu nywele zao zikawa nyingi kutokana na baba yao sio kama mama you zilikuwa chache. Alizijulia hizo nywele na umbile lake! Lara alijipenda sana tofauti na dada zake. Alipenda vitu vizuri tokea mtoto. Mama yake alikuwa akimsimulia wakati mtoto kama akimvalisha kitu kibaya, asichopenda yeye, alikuwa akilia sana na hataki kutoka chumbani. Basi Lara akakua akipenda vitu vizuri tofauti na dada zake. Aliijua mitumba ya kila mahali, na huko ndiko alikokuwa akipata mavazi yake. Ukimuuona sehemu, unaweza sema ni toto la milionea, linaishi uzunguni, kumbe kiziwanda wa mama Chiwanga, anaishi uswahilini tu.

Kujipenda ndio kipaumbele kwake na kupenda kujirusha. Weekend ilikuwa lazima waende club. Zaidi siku za jumamosi ambazo huenda kazini nusu siku na mara nyingine hawakuwa wakienda kabisa, wanapeana zamu kufanya kazi siku hiyo ya jumamosi. Basi watatumia siku hiyo kujitengeneza, ikifika jioni wanakwesha club mpaka karibu kunapambazuka jumapili, ndipo wanarudi nyumbani kulala. Kasoro Warda mtoto wa swala tano. Walikuwa wakimuacha nyumbani. Ila Lara, usingejua kama anatokea kwenye nyumba ya baba na mama washika dini, walokole wanaoishi kwa hofu ya Mungu, na yeye kukuzwa hivyohivyo.

Lara alipoanzana na Jax, akaacha kwenda club. Siku hizo za weekend akawa akienda kulala nyumbani kwa Jax aliyeonekana ametulia na anaakili za kiutuuzima kuliko mpenzi wake wa wakati huo. Alipoona Jax anamuelekeo, akaamua aachane naye kabisa, atulie kwa Jax tu aliyeonekana anaweza kuja kumuoa lakini akaishia kumuacha na gauni la harusi mkononi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mwezi huo nao ukaisha. Mambo yakiendelea hivyo hivyo. Mwezi wa pili nao, zawadi za hapa na pale, bila ujumbe wala kukutana na mletaji ambaye alidhania ni Nelly. Akawa anapokea na kula bila shida. Akidhani labda siku hiyo ndio mwisho, kesho yake ataletewa tena. Tena mambo yakazidi kuongezeka. Akiwa kazini akaanza kuletewa chocolate, wakati mwingine Icecream, ilimradi tu. Ila kwake aliendelea kufurahia. Faraja ikaongezeka.

Kabla ya mwezi huo wa pili kuisha tangia aanze kuletewa hivyo vitu, yule muhudumu wa mgahawa aliyekuwa akileta matunda akamuuliza anataka mchana amletee chakula gani? Akampa na Menu ya hotelini kwao. Lara akashangaa sana. “Na chakula!?” “Nimetumwa niulize uletewe chakula gani kwa leo. Sijui kama na kesho, ila leo.” Suzy akaruka na kuivuta ile menu. Akaanza kuisoma yeye huku akimuuliza yule muhudumu maana ya yale majina ya vile vyakula, huku yule muhudumu akieleza. Suzy akachagua. “Sasa sio upunje. Ulete kingi.” Suzy akaweka msisitizo. “Wewe si upo kwenye diet wewe? Unataka kupungua kweli wewe?” Bosi wao akamuuliza. “Naanza kesho bosi wangu.” Akajibu Suzy usemi wake wa kila siku na kesho yake haikuwahi kufika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ikaenda hivyo juma la kwanza na la pili. Chakula mara mbili kwa juma ila matunda na juisi mara tano kwa juma. Chakula kikawa kinaletwa siku ya jumatatu na alhamisi. Walipomletea matunda siku hiyo ya alhamisi asubuhi wakati muhudumu anataka kujua amletee chakula gani mchana, Lara aliomba asiletewe. Akasema angependa kwenda kula palepale. Ilipofika mchana alitoka peke yake, kwa kuwa Suzy, Warda na Sesi hawakwenda naye sababu ya bei. Wao wakaelekea kibandani, Lara mgahawani.

Lara Mgahawani!

L

ara alifika hapo akamuulizia muhudumu ambaye huwa anamletea chakula. Akaenda kuitiwa. “Mzima Lara?” “Nimekuja kula au ...” Lara akapunguza sauti. Kulionekana na watu wa maana pale ndani. Na kila mmoja yupo na shuguli zake. Wengine kama mazungumzo ya muhimu, wengine wakila huku wakisoma magazeti. Lara akababaika. “Bosi tena! Wewe tafuta nafasi ukae, nitakuhudumia.” Lara akacheka kidogo kwa kuridhika. Akaanza kutembea kwa kunyata akitafuta sehemu ya kukaa.

Akiwa anaangalia meza ya mbele akagongo kiti kilichokuwa kimepangwa kwenye meza iliyokuwa imekalia na watu wawili. Watu wazima tu, walionekana wapo kwenye mazungumzo yao ya maana. Wakamwangalia kwa kushituka kidogo “Sorry!” Akanong’ona Lara huku ameshituka na uso wa kubabaika. “Hamna shida.” Wakamjibu. Akaenda kukaa meza ya mbele yao lakini akavuta kiti badala ya kukinyanyua, kikatoa mlio mwingine uliosumbua wateja wengine. Akawageukia tena. “Sorry!  Wengine wakatoa tu tabasamu la kiungwana, na wengine wakageuka kuendelea na mazungumzo yao.

Akaanza kugongagonga meza na vidole akitumia kucha zake ndefu kama anayejituliza kwa wasiwasi kuwepo sehemu kama ile, wakamgeukia mpaka wa pembeni yake na mbele kama anayesumbua. “Sorry!” Akanong’ona tena. “Am trying to calm myself down.” Akaendelea kuongea taratibu na lugha ya uzaliwa ikawa imepotea kabisa. “Na nikiwa nawasiwasi naongea kingereza kama mlevi!” Lara akaendelea kuongea kwa sauti ya kunong’ona akiwaangalia. Wote wakacheka na kugeuka kuendelea kula.

Akaanza kuvuta pumzi kwa nguvu, yule muhudumu aliyekuwa akimletea chakula akaja na juisi yake. “Uwiii! Heri umekuja. Na nafikiri uwe unaniletea tu kulekule. Hapa sijawahi kuja peke yangu. Panaogopesha!” Yule muhudumu akaanza kucheka. “Kweli tena, mpaka nimeanza kuzungumza kingereza!” Yule muhudumu akaendelea kucheka. “Utazoea tu. Ila unatakiwa uwe unakuja mara kwa mara sasa. Na ukija uwe unaangalia unakopita, usigonge meza na viti vya wateja wengine.” “Na wewe kumbe umeona!?” Wakaanza kucheka taratibu.

“Hapa pametulia sana. Wengi wanakuja kwa mazungumzo maalumu na watu wenye pesa zao.” “Kwa hiyo watajua mimi mgeni, eeh?” Akacheka. “Njoo mara kwa mara, hofu itaisha na utaendelea kuongea kingereza tu.” Lara akacheka sana. Akamtania kidogo, akaagiza chakula, yule muhudumu akaondoka.

Akaanza kuangaza macho pale. Akajikuta ni yeye peke yake ndio mshangaaji. Kila mtu ana lake. Waliokuwa wamekaa peke yao walikuwa kama hawajainamia simu zao, basi wanasoma magazeti. Akavuta pumzi kwa nguvu, akatoa simu yake na yeye angalau aperuzi, aonekane wa maana.

Jax kwa Lara.

C

hakula kikaletwa akaanza kula taratibu, mawazo yakamtoa pale akaanza kufikiria hili na lile. Akatulia na kupotelea mawazoni. Mara akamuona Jax amevuta kiti mbele yake, akakaa. Akashituka sana karibu aangushe uma. “Jax!” “Mzima Lara?” Lara akabaki akimwangalia. Wakatulia kwa muda Lara akishangaa. “Unaendeleaje?” Jax akauliza tena. Lara kimya. “Lara?” “Sikutegemea...” Akakumbuka anaongea na Jax, mfanyakazi wa benki ya dunia. Kuwepo pale sio kitu cha ajabu. Akatulia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hatimaye wawili hao wamekutana tena. Jax akiwa amemuacha Lara kikatili sana tena akiwa mjamzito, wakiwa wameishi vizuri bila tatizo, sasa hivi amerudi mezani kwa Lara. Baada ya mazungomzo yake ya mwisho kwa Lara akiwa kitandani hajiwezi amepoteza mtoto na mshituko wa kuachwa vibaya, hatimaye wamekutana tena. Sasa, sasahivi Jax ana kipi tena chakuzungumza?

Usikose muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment