Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com CHOZI LANGU! - SEHEMU YA 5. - Naomi Simulizi

CHOZI LANGU! - SEHEMU YA 5.

 “Naona unamalizia chakula chako.” Jax akaendelea. “Ndiyo.” Akajibu Lara. “Pole na majukumu.” Jax akaendelea. “Asante na wewe.” Lara akajibu. Kimya kikazuka. Akainamia sahani yake ili amalizie chakula. “Nimesikia kingereza chako.” Lara akacheka. “Kumbe ulikuwa hapa tokea mwanzo!?” “Nilikuwa nimekaa pale nasoma gazeti.” Lara akacheka sana. “Lara wewe ni mtundu sana!” “Sasa kwani sehemu kama hii huwa wanazungumza kiswahili?” Jax akacheka huku akimwangalia.

“Mimi nimeshangaa kingereza kinatoka tu!” “Nimekusikia. Nikasema huyu mwingereza ametokea wapi hapa katikati ya jiji. Kumbe Lara!” Wakacheka tena. “Kumbe unakuja kula huku!?” Lara akauliza. “Sio kila siku.” Akajibu Jax. Wakacheka kidogo wakatulia. Akamuona Lara ameinama kama anayetaka kupotelea mawazoni, akamuwahi. “Wana chakula kizuri.” Jax akamrudisha pale. “Lakini garama! Nikila hapa week moja tu, mshahara wangu wote wa mwezi utaishia hapa.” Wakacheka na kutulia tena kidogo.

Lara akainama na kuendelea kupanga chakula hapo kwenye sahani akitumia uma wake bila kuweka mdomoni. “Lara!” Akamuita, Lara akamwangalia. “Unaendeleaje?” Lara akamwangalia na kukunja uso. “Nataka kujua unaendeleaje? Afya yako kwa ujumla.” “Vizuri.”  Akajibu Lara taratibu. “Unakula vizuri?” Lara akainama. “Eti Lara?” Akamwita tena. “Unakula vizuri? Namaanisha milo yote. Kuanzia asubuhi mpaka jioni na kuhakikisha unakula vitu vya kuongeza damu?” Lara akamshangaa kidogo na kunyamaza kama anayefikiria.

“Walikupa dawa za kuongeza damu?” Lara akajua kama alishajua kama alikuwa mjamzito, mimba ikatoka. Akabaki ameinama. “Kwa nini hukuniambia kama ulikuwa mjamzito?” Kimya. “Eti Lara?” “Inasaidia nini sasa hivi Jax? Mtoto nilibeba mimi sio Tula. Mahusiano yalikufa na mtoto alikufa. Si ushukuru Mungu huna sababu ya kuangalia nyuma! Huna sababu ya kukufunga kwa yeyote, isipokuwa kwenye mapenzi ya kweli.” Lara aliongea taratibu tu.

“Japokuwa iliniuma sana, lakini naona ni kama Mungu aliruhusu kwa sababu, Jax. Hebu fikiria huyo mtoto angezaliwa, nabaki naye mimi tu. Halafu anakuja kujua historia yangu yakuachwa nikiwa nina mimba yake. Tena naachwa kwa kuwa baba yake hakuwa akinipenda, anampenda mtu mwingine! Hudhani kama na yeye angeumia sana?” Lara akamuuliza taratibu bila sauti ya juu akiheshimu watu wengine waliokaa pembeni yao.

“Huyo mtoto angekuwa kwenye mazingira gani? Angeishi hapa duniani akijiona mimi na yeye wote hatufai.” “Lakini nilitakiwa kujua Lara. Ilikuwa haki yangu kujua kama yupo mtoto wangu.” Lara akafikiria kidogo. “Mwenzio nimejifunza kitu, Jax. Sio mambo yote yapo na majibu. Kuna mambo mengine yalitakiwa yawe na majibu mazuri tu, lakini hayana. Mengine yalitakiwa kuleta maana, lakini hayaleti maana. Nikujifunza kuishi vile ilivyo.” Jax akabaki kimya.

Lara akaendela kula chakula chake na juisi yake, Jax akiwa ametulia mbele yake. “Lara?” Lara akamwangalia. “Kuna kitu nataka kukwambia. Na ninaomba uamini namaanisha.” Lara akabiki akimwangalia wakati anamalizia juisi yake.

“Unanisikiliza?” “Naomba usirudie kuniambia unampenda Tula kuliko mimi. Hilo ulihakikisha nalielewa kwa vitendo. Tafadhali usirudie tena. Nilielewa na ndio maana nilikaa mbali kabisa na wewe Jax. Kwa kuwa nakuheshimu na ninajua hujakurupuka. Hilo nimeelewa. Huhitaji kurudia.” Lara akaendelea kuweka sawa chakula chake kwenye sahani.

“Naomba unisikilize tu.” “Hivi unajua Jax na mimi nina hisia kama zako na watu wengine? Kama zako zakupenda zilivyo juu, basi ndivyo ujue zangu za kuumizwa zipo juu. Usiendelee kufurahia kuumia kwangu, Jax. Au wewe hudhani kama inatosha? Ni nini kibaya nilichokutendea kiasi..” “Lara! Naomba unisikilize. Sina nia yakutaka kuendelea kukuumiza.” Lara akatulia.

 “Samahani kwa yote. Zaidi naomba uamini kuwa najuta kwa kusababisha kupotea kwa mtoto wetu.” Lara akaweka uma chini. “Hivi unajua unaongea na Lara hapa na si Tula?” Lara akamuuliza taratibu tu. “Nafahamu.” “Basi naomba nikufariji kwa hili. Hukusababisha kupotea kwa mtoto. Ila Mungu alikusaidia kukupunguzia matatizo. Na kwa kuwa ni Mungu, atakupa mtoto mwingine kupitia Tula, kama mtataka. Kwa yule niliyekuwa nimembeba mimi basi jua ni wa bahati mbaya kama watu walivyozoea kuita mimba zinazoharibika kama kwangu na mwanangu. Kwa kuwa pia aliingia kwa bahati mbaya.” Lara akasimama.

“Naomba tunapokuja kukutana wakati mwingine, tuache mambo ya nyuma, yabakie nyuma, Jax. Mwenzio ninapotoka hapa, sina faraja yeyote ile. Inanichukua muda kujituliza na kuweza hata kwenda kazini. Tafadhali kuwa na ubinadamu hata kidogo kwangu. Na mimi naomba unifikirie hata  kidogo, Jax.” Lara akaondoka nakumuacha Jax pale mezani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jax alimuharibia kabisa siku yake. Badala yakurudi kazini akiwa amefurahia chakula chake, akarudi akiwa amepoa kabisa. Kila mtu akamshangaa, lakini akakataa kuwaambia kulikoni. Baada ya nusu saa, bila hofu Jax akamfuata pale kazini. Kila mtu akabaki amemkodolea macho. Ni bwana harusi aliyeahirisha harusi, tena wakiwa wameshachanga.

Jax akamsogelea kiongozi wao wa pale mbele. Walifahamiana vizuri tu. “Habari ya saa hizi?” “Nzuri tu, karibu Jax.” “Asante. Samahani, sijui Lara yupo?” Akawa kama anaangaza pale. “Siku hizi Lara anafanya kazi huko nyuma ya ofisi.” “Naweza kumuona?” “Subiri kidogo nimwite.” Akanyanyua simu na kumpigia.

Baada ya muda Lara akatoka. Akashangaa kumuona Jax pale. Jax akamsogelea. “Naomba tuzungumze kidogo hapo nje.” Lara akatangulia nje bila ya kumjibu. Jax akafuata. Lara alikwenda kusimama pembeni kabisa ya jengo. Jax akamsogelea.

“Sikutaka kukuharibia siku yako. Ndio maana nilikuomba unisikilize.” Lara akatulia tu. Akakumbuka yeye ndiye aliyemaliza mazungumzo yote. “Naomba nikwambie kile nilichotaka kukwambia.” Lara akamwangalia. “Nataka ujue tu, kuwa nimeumia tumepoteza mtoto wetu. Namaanisha wangu mimi na wewe. Najua wewe sio Tula, ni Lara. Msichana uliyenipenda kwa dhati ila mimi ndio sikujua jinsi ya kuthamini mapenzi ya kweli na ya dhati. Kwa hiyo najua nazungumza na wewe Lara.” Lara akainama. Akajisikia kama machozi yanataka kutoka.

“Imeniuma na najutia kuliko mtu yeyote yule atakavyoamini. Sikukusudia kuleta maafa makubwa hivyo kwako na kwa mtoto wetu.” “Ulitegemea nini kitokee, Jax!?” “Nilijua ingekuwa tukio la kushangaza kwa muda, lakini ungekuwa sawa, Lara. Ungepata mwanaume kwa haraka, akakupenda na kukuthamini. Usingeumia wala kujali kama nikiendelea na maisha yangu.” Lara akamwangalia kwa kumshangaa, akaona amuache tu. Haina maana tena.

“Naomba nirudi kazini.” “Sijamaliza.” Jax akamuwahi. “Ni nini tena!?” Lara akauliza kama aliyechoka tayari. “Pole kwa kuugua sana baada ya kupoteza mtoto na nasikitika nilishindwa kuwepo kukuuguza.” Mpaka Lara akakunja uso. “Ni nini unafanya Jax!? Ni nini unataka kwangu zaidi? Au wewe unanichukuliaje? Kwa nini unanifanya mimi kama mdoli wa kunifanya kile utakacho? Kama sina akili yakufikiria! Kweli Jax? Umeishi na mimi zaidi ya mwaka. Kwa upendo na kukuheshimu. Kweli hiki ndicho kipimo unachofikiria akili zangu zipo? Kwamba siwezi hata kufikiria!?” “Ndio maana nipo hapa Lara. Ungekuwa mtu mwingine, nisingerudi.” “Kwamba uthamani wangu upo chini kiasi cha kushindwa kufikiria?” “Sio hivyo Lara! Najua unaakili sana na wala si mjinga. Ila nilitaka ujue kile ninachofikiria. Sijawahi kukuficha.” Jax aliongea kwa tahadhari kama asiyetaka kuharibu.

“Kipindi unaniambia hunipendi mimi unampenda Tula, n..” “Sijawahi kukwambia sikupendi Lara.” Lara akakunja uso. “Jax!” “Sijawahi kukwambia sikupendi.” “Naomba nimalize kuongea kabla hujanichanganya zaidi.” “Nakusikiliza Lara. Lakini sijawahi kukwambia sikupendi.” Hapo Jax akakanusha.

“Vyovyote ulivyoniambia, lakini siku unanitamkia unampenda Tula, huwezi kuwa na mimi, ndio na mimi nilikuwa nimepoteza mtoto. Sasa, sasa hivi unaongea nini na uliniambia nini?” Lara akamuuliza taratibu tu.

“Sio kweli kama ulishindwa kuwepo kuniuguza kama mimi nilivyokuwepo kwenye maisha yako nikikuuguza vipindi ulivyokuwa mgonjwa. Ulikuwepo, lakini ulimchagua Tula, badala yangu na mtoto. Ulikuwepo, lakini ulikuwa na Tula! Tena kwa kuniambia mwenyewe! Sasa, sasahivi unaongea nini!? Kwa nini unataka kunichanganya tu na kuniharibu zaidi?” “Sio nia yangu. Nia yangu ni kuomba msamaha kwa yote, Lara.” “Yapi, Jax!? Nashindwa kuelewa! Ni kama umechagua kuniumiza tu!” “Hata kidogo.” Lara akakunja uso kama asiyemuelewa na ameshamvuruga.

“Naomba uniamini Lara, najutia.” “Hapo ndio sikuelewi Jax! Au haya yote yanaletwa na wewe kujua nilipoteza mtoto au ni nini? Maana hata mtoto mwenyewe hukujua kama yupo! Umesikia tu kuwa mimba ilitoka. Unajuaje kama ilikuwa yako? Maana sijawahi kumwambia yeyote yule kuwa nina mimba yako!” “Najua alikuwa wangu. Najua ulitulia Lara. Najua hukuwa na mwanaume mwingine ulipokuwa na mimi. Najua kwa asilimia 100 kuwa alikuwa wangu.” “Basi kama unajua hivyo, amini utapata mwengine kwa mwanamke unayempenda Jax. Tafadhali naomba niache.”

“Sawa. Lakini nilitaka tu ujue hilo. Najua nimeharibu. Sasa hivi sina haki yakurudi kinyume nyume tena. Ila niliona nisibaki nalo moyoni. Sitaki kukuficha. Nataka ujue ukweli. Hata kama haita leta maana kwa yeyote. Hata kama sitaeleweka kwa yeyote. Ila nilitaka WEWE ujue kuwa, NAJUTIA YOTE, SAMAHANI NA POLE. Hilo ndilo nilitaka ulisikie kutoka kwangu. Hata kama ukisikia nimekufa leo, nataka uwe umesikia kutoka kwangu.” Lara akashituka sana.

“Unaumwa?”  Akamuuliza kwa kujali kama kawaida ya Lara kwa Jax. “Hapana siumwi. Lakini vifo vinatokea Lara. Naweza nikatoka hapa, nikafa ndani ya gari yangu tu. Bila kuumwa au hata kugongwa na gari.” “Hapana Jax. Wewe bado mdogo sana. Huwezi kufa sasa hivi.” “Huwezi jua Lara.” “Hapana. Usiseme hivyo. Huwezi kufa. Bado unamaisha marefu na mazuri tu mbeleni. Mungu atakulinda. Hutakufa bali utaishi.” Lara akawa kama yeye ndio ameingiwa tena na hofu.

“Lakini nilitaka unisikie mimi mwenyewe Lara. Sitaki nije nijute, niseme ningejua ningekwambia.” “Japokuwa sijaelewa, lakini nimesikia Jax. Naomba uwe na amani tu. Kuna mambo mengine yanatokea, yanakuwa magumu kweli, lakini Mungu anayaruhusu kwa sababu.” Lara akaanza kutoa faraja.

“Kuna mstari wa bibilia baba anapenda kunikumbusha tokea nipatwe na matatizo. Hata jana usiku alinipigia akanikumbusha. Unataka nikwambie na wewe?” Lara akamuuliza kwa upendo tu. Jax akatabasamu kidogo. Alijua wazazi wa Lara ni wacha Mungu. “Unasemaje?” “Unatoka kwenye kitabu cha Warumi 8:28 nitakwambia kwa kingereza kwa kuwa nimetoka kula kwenye mgahawa wakizungu, bado naona ulimi unataka kuongea kingereza tu.” Jax akacheka sana.

“Lara!” Jax akawa anamwangalia. Kwa asili Lara alikuwa mtundu na maneno mengi ya utundu kama Suzy kasoro matusi. Pale kazini kwao wao wawili wakikosekana, kila mtu atataka kujua kulikoni. “Usifanye mchezo na chakula ya kisu na uma!” Jax akaendelea kucheka. “Haya niambie.” “ ‘And we know, ALL things works together for good to those who love God...’.” Inaendelea hapo. Lakini katika yote, kumbuka kila kitu kinatokea kwa sababu. Hata katika lililonipata mimi..” “Na mimi Lara?” Lara akakunja uso.

“Haya na wewe kupata mpenzi wako. Mimi kupoteza ndoa na mtoto, hata katika hilo kuna kusudi tu.” “Mimi nilifikiri umenipoteza mimi, kumbe ndoa!” Jax akalalamika. “Jax, huwezi kupoteza kitu ambacho hujawahi kuwa nacho wala hujawahi kukimiliki! Ulinithibitishia wazi kuwa, hukuwahi kuwa wangu japo tulikuwa pamoja. Hata tungekuwa na ndoa, bado usingekuwa wangu. Kwa hiyo na hilo nalo nashukuru Mungu. Ni bora hata ulivyonikimbia na kuhama nyumba kwa siri bila kujua, kuliko ningeishi na wewe. Tukazaa, kumbe mwenzangu mawazo na moyo wako viko kwa mtu mwingine! Isingekuwa sawa kwako wala kwangu. Ni bora ulifanya maamuzi magumu.” Lara akataka kuondoka, akarudi.

“Lakini Jax, kwa jinsi tulivyoishi mimi na wewe, nafikiri nilistahili kuambiwa mapema. Tena kutoka kwako wewe mwenyewe, si kutoka kwa mpenzi wako. Kule nikunivunjia heshima ambako sidhani kama nilistahili, Jax. Tuliishi vizuri sana. Tulikuwa marafiki wakucheka usiku kucha, hata mambo ya kijinga, yalitufanya tucheke. Hatukuwahi kugombana. Tulielewana sana. Tena katika kila jambo! Sikuwahi kukuvunjia heshima ndani wala hadharani! Nilistahili kusikia kutoka kwako Jax. Tena mapema. Sio kunidanganya kuwa ulishinda Kisarawe ukitafuta mashamba, kumbe ulishinda jumapili nzima kitandani na mpenzi wako!” Jax kimya.

“Nafikiri sikustahili Jax. Ulinilipa tofauti kabisa na mahusiano yetu. Ulinifanya nivae magauni ya sherehe, huku ukijua wazi hutanioa! Usingeacha mimi niadhirike hadharani kwa kiasi hicho Jax. Au kuniacha stedi ya basi nikikusubiri, wakati upo hapa hapa Dar, kitandani na mpenzi wako! Hebu fikiria Jax. Ingekuchukua dakika ngapi kuja kunitoa pale kituo cha mabasi, na kuturudisha kwangu na wewe kurudi kitandani kwa mpenzi wako? Ingekugarimu nini Jax? Hasa ukijua unanifanyia mimi! Hata kama hapakuwa na mapenzi, lakini tulikuwa marafiki wazuri tu. Wakati mwingine tulikuwa tukiwa na Tino mahali, tunapata muda mrefu tu wakucheka na kufurahi. Sijui Jax, mimi nafikiri sikustahili.”

“Kweli hukustahili Lara. Ndio maana nipo hapa kukuomba msamaha.” “Sawa Jax. Kila la kheri. Mungu akujalie mara dufu. Yale uliyopoteza, yale uliyokosa kutoka kwangu, yale unayostahili na usiyoyastahili pia, Mungu pia akustahilishe na akupe.” Lara akarudi ndani ofisini akiwa ametulia sio kama mwanzoni aliporudi.

Wakati anaingia kila mtu alimwangalia. Ndio ilikuwa sehemu ya mbele ya ofisi yao. Ilikuwa wazi tu, sehemu ambayo wafanyakazi wanaohusika na kuzungumza au kuhudumia wateja ndipo walikaa hapo. Kila mmoja alikuwa na meza yake na kiti mbele kwa ajili ya kukalia wateja wakiwahudumia. Na meza ya Lara ilikuwa hapohapo mbele, ila alihamishiwa ofisi ya nyuma. Akapitiliza ndani back office.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hapohapo Suzy akamtumia ujumbe Tino. ‘Jax alikuwepo hapa muda si mrefu, alikuja kuzungumza na Lara.’ Tino akampigia simu Lara. Lara akapokea. “Suzy ameshakwambia kuwa Jax alikuja?” Tino akacheka. “Upo okay?” “Mimi mzima tu.” “Nilitaka kusikia hivyo.” Lara akacheka. “Asante kujali Tino.” “Basi tutokeni leo, tuunge msafara wa wafanyakazi wa benki wote kwenye beach Party. Suzy amesema hamna shida, nikuulize wewe.” “Sasa nyinyi si wafanyakazi wa benki, sisi si watatushangaa?” “Mtakuwa na mimi. Halafu ipo wazi kwa ndugu, jamaa ya wafanyakazi.” Lara akanyamaza.

“Ni jioni. Najua wazee wataondoka, tutabaki vijana. Tule mziki mpaka asubuhi. Ukichoka nakurudisha nyumbani.” Lara akacheka kidogo. “Umekaa ndani sana. Tutoke kidogo ucheke.” “Sawa. Si utakuja kutuchukua au unataka tukutane huko huko?” “Nitawafuata. Nyinyi muwe tayari kwenye saa mbili. Tufike wazee wakiwa washaondoka. Hasa bosi wangu.” Wakacheka kidogo wakakata.

Baada ya kama dakika 5 akasikia Suzy anakuja huku akipiga kelele. Akajua tayari Tino amemfikishia ujumbe. “Party! Ehehe Party! Oooh Party!” Akawa anacheza na kuimba mbele ya Lara. Lara akaishia kucheka tu.

Juu ya Jax na Tula.

K

wenye mida ya saa moja na nusu usiku Tino akawa amefika. “Lara yuko wapi?” “Naona bado yupo chumbani kwake anajiandaa.” Tino akaenda kugonga chumbani kwa Lara. “Ingia Tino.” Akamkaribisha. “Nikwambie kitu?” “Usianze kama mwenzio Jax. Ni nini mnachoongea kinachoanza na kutaka kuweka msisitizo hivyo?” Tino akacheka. “Sijamsikia huyo mtu wala kumuona kwa muda mrefu. Mzima?” “Anaonekana mzima kama mfanyakazi wa benki ya dunia. Ananukia neema tupu.” Tino akafurahi kuona Lara ameanza kuchangamka hata akimzungumzia Jax, sio kwa hasira.

“Nataka kukwambia juu ya Jax na Tula.” Lara akageuka. Maana alikuwa amesimama mbele ya kioo anajitengeneza usoni. “Nikupe tu historia yao.” “Sidhani kama ni lazima Tino. Haitabadilisha chochote. Tuache tu.” “Hapana. Kuna kitu natamani ukifahamu juu ya hao watu wawili. Nisikilize tu.” Lara akafikiria, akaenda kukaa kitandani na kumwangalia.

“Jax na Nelly ni yatima. Walio na ndugu lakini walisuswa.” Tino akaanza hivyo. “Jax amelelewa na dada yake tokea mdogo. Sijui ndipo wote wawili walipo athirika, au la! Lakini kama unavyomuona Nelly. Yeye Nelly athari yake ipo bayana. Haamini mtu. Hataki ndugu wala rafiki. Hataki watu wanufaike naye sasa hivi, wakati alihangaika yeye mwenyewe kufika pale. Haamini watu na pia hataki watu wamsogelee halafu waje kumbadilikia kama walivyowafanyia tokea watoto. Hapo napo ni parefu tu, anayo yake mengi.” Akaendelea.  

“Kwa upande wa Jax, mapenzi anayoyajua ni ya dada yake tu. Ndio yupo vile. Haamini kama kuna kitu cha kudumu. Haswa mahusiano. Mahusiano aliyonayo ni yale ya kijeshi kutoka kwa dada yake. Na habari aliyokuzwa nayo ni kutoamini mwanadamu kwa asilimia zote. Kuwa, mwanadamu ni mdanganyifu na anaweza kukubadilikia vibaya sana. Mbaya zaidi kwake Jax, msichana wa kwanza na wa pekee kuwa naye ni Tula. Akaja kuwa kilekile Jax alichokuzwa akiaminishwa na dada yake. Halafu sasa, haiba ya Tula haina tofauti sana na Nelly ila yeye yupo upande wa pili. Ni control freak. Sijui kama unanielewa?” Lara akanyamaza.

“Hata tulipokuwa na Jax chuoni, washikaji walikuwa wakigombana na Jax sababu ya Tula. Alitaka kumtawala hata muda wake, awe na nani na afanye nini. Akawa anafika umbali hampi nafasi Jax hata na mimi! Akiwakuta mko naye, anaweza kuanza ugomvi makusudi tu, ilimradi tu amtoe pale Jax.” “Sasa na Jax alikuwa akisemaje?” Tino akafikiria.

“Mimi sijui yule msichana alikuwa akimwambia nini Jax wanapokuwa naye, aisee! Jax alikuwa hawezi kusema hapana kwa Tula. Ni kama aliyekuwa na nguvu ya ajabu sana kwa Jax, ambayo kati yetu wote hata dada yake hakuwa akielewa! Hata amkute katikati ya kujisomea, anaweza kumtoa hapo, Jax akapotea. Na hapo labda mnakuta mna mtihani kesho yake! Mtakuja kukutana naye chumba cha mtihani.” Lara akakunja uso.

“Mimi nilivyoona hivyo ilinibidi kwenda kuzungumza na dada Nelly, ndipo akazungumza naye. Haikusaidia sana, lakini ndipo akaishia Jax kupata daraja alilopata wakati kwenye kundi letu wote tulifaulu sana. Nikikwambia tulifaulu, tulifaulu wote tena vizuri. Ndio maana hata tulipomaliza chuo, japokuwa wote tulipata kazi, na Nelly anakazi nzuri sana, na anafahamiana na wengi, alisema waziwazi hatamsaidia Jax kupata kazi. Kuonyesha amekua, ni kuwajibika na makosa yake aliyoyaruhusu chuoni mpaka kumpelekea kupata daraja alilopata, na ahangaike yeye mwenyewe mpaka afanikiwe. Alisema atamlisha na kumpa malazi tu, mengine ahangaike mwenyewe. Na kweli Nelly hakutania. Jax alisota mtaani na dada yake akimtizama tu. Maana sisi wote kwenye kundi letu ni kama tulipata ajira siku ya mahafali yetu, au kama tuliwahiwa na hii benki sababu ya kufaulu vizuri. Kwa hiyo hatukuhangaika kazi kabisa.”

“Sasa kipindi hicho Jax ndipo alipomjua Tula vizuri.” “Kipindi gani?” Lara akauliza. “Matokeo yalipotoka na yupo mtaani hapati kazi halafu wenzake wote tuna kazi! Aisee Tula alimnyanyasa. Ndio kidogo Jax ni kama akapata akili. Na hakuishia hapo, alimkimbia kabisa na kwenda Norway na mzungu. Jax akajua na kuumia sana. Akajua hakuwa akimpenda ila tu kumtawala.” Tino akafikiria kidogo. Kisha akaona aseme tu.

“Nimesikia kutoka kwa mtu ambaye anauhakika. Nasikia Tula hakuolewa na huyo mzungu japo alivalishwa pete ya uchumba. Maisha yakamshinda huko, akakimbilia London. Huko nako wakamchezea kupita kiasi. Akawa hapati kazi, kwa kuwa UK bila karatasi au vibali vya kazi vya kueleweka nasikia hapakaliki. Ndio nasikia akahangaika, akabahatika kupata nauli yakurudi nyumbani. Sasa Pius anasema siku moja akakutana naye. Si unamkumbuka Pius, yule jamaa wa auditing? Rafiki yetu na Jax lakini yeye alimaliza CBE, unamkumbuka?” “Namkumbuka Pius.” Lara akajibu.

“Pius anasema alipokutana na Tula, akamuulizia Jax. Ndio Pius akamwambia Jax siku hizi mambo yake safi sana. Akampa habari za Jax. Na akamwambia Jax siku hizi anahonga magari. Anaoa mwarabu wa jiji kuu la Tanzania. Pius akatusimulia akamrusha sana roho Tula, kwa kuwa sisi wote tulikuwa tunamjua jinsi alivyokuwa anampelekesha Jax, halafu alivyoharibikiwa, akamkimbia. Ndio washikaji wanahisi Tula kama kawaida yake atakuwa alimtafuta Jax, akampanga tena. Hatujui aliongea nini, lakini nataka ujue Tula anayo nguvu kubwa sana kwa Jax. Sio kwa uzuri au ubora wake tu, ila mdomo wake. Na ikifika kwenye swala la Tula, Jax anakuwa kama hajielewi. Sasa sijui kwa kuwa alilelewa na mwanamke! Kuwa amejifunza kumtii mwanamke tu au la! Hana mfano wa mwanaume aliyejifunza kwake kujua wanaume wanatakiwa wawe vipi, sielewi!” Lara akaguna akifikiria.

“Sijui Tino! Mimi amenitafuta na kuniambia mambo matatu aliyohakikisha nayasikia. Alinifuata mpaka kazini tuliposhindwa kumalizana naye pale mgahawani.” “Mambo gani?” Tino akauliza. “Ameniambia anajuta, anaomba msamaha na amenipa pole yakupoteza mtoto wetu.” “Wewe ulimwambia maswala ya mtoto!?” “Hapana Tino. Leo ndio nimemuona Jax tokea aje hapa aniambie ananiacha sababu ya Tula! Sikumsikia tena wala kumuona kwa bahati mbaya. Sijui ameambiwa na nani!” Wakanyamaza wakifikiria.

Tino akapata wazo. “Itakuwa dada Nelly. Maana mimi ndiye niliyemwambia dada Nelly. Atakuwa amezungumza naye. Halafu pengine Jax amepata muda wa kufikiria.” Tino hakutaka kumwambia Lara kama alishakutana na Jax na kuzungumzia juu yake. Hakutaka maswali ya nini walizungumza juu yake. Akaona anyamazie hilo. Kwanza hawakuachana vizuri na Jax. Akaona ayaache tu. “Lakini Tino, naamini na mimi nastahili mwanaume atakayenipenda kama vile yeye anavyompenda Tula. Nimeridhika na kuja kwake na kuomba msamaha na kukiri kosa. Inatosha. Naomba twende tukafurahie maisha.” Tino akacheka.

“Lakini ujue nimefurahi kuona umefunguka Lara. Ulibadilika ukawa mnyonge sana.” “Kukataliwa kubaya Tino! Sikia kwa watu, wewe yasikupate. Tena kwa kutamkiwa! Heri uhisi, halafu mgombane muachane. Lakini si kwa kuambiwa yupo mtu mwingine, eti bora zaidi yako! Inauma mno. Hata kama nitacheka sasa hivi, haiondoi ukweli.” “Naelewa. Twende zetu tusirudi nyuma. Tumekubali kwenda kufurahia. Tukafurahie.” Suzy akaingia.

“Umemuona mke wa Tino? Kibonge wangu mwenyewe?” “Uringe?” Suzy akamshushua. “Huwezi kuwa na mke kama mimi.” Lara akacheka. “Mimi nakupenda kama ulivyo Suzy wangu. Sitaki upungue wala nini. Hivyo hivyo ulivyo mimi nakupenda tu.” “Usijidai  wewe ndio unachakunivumilia, mimi sina. Unakunywa pombe mimi sinywi na sijawahi kulalamika.” “Umeona jinsi tunavyopendana?” Lara akazidi kucheka.

 “Uje uniache nyumbani ukalewe baa?” “Halafu nikose hizo kelele zako?” Wote wakacheka. “Achana na mimi Tino. Kwanza siku hizi siongei sana.” “Nitamisi hiyo sauti yako!” Sesi akaingia. “Ni nini humu ndani?” “Tino anamtongoza Suzy.” Lara akajibu. “Anataka warudiane?” “Hatukuwahi kuachana wenyewe. Tulipeana tu mapumziko.” Akajibu Tino. Suzy akabetua midomo. “Humtaki tena?” “Wa nini mimi Tino? Sina haja. Naombeni twendeni.” “Wanasemaga hivyo hivyo lakini unakuja kushangaa kesho vigelegele. Tino na Suzy kanisani! Tunaapiana wenyewe mpaka kifo. Wawili tu.” Lara na Sesi wakaendelea kucheka, Suzy akatoka. Wakamfuata nyuma. Wakaondoka.

Njia nzima Tino alikuwa akimpamba Suzy. “Ungekuwa unanuka pombe, ningesema umelewa.” Suzy akaongeza. Kwanza alitaka kukaa naye mbele. “Tatizo lako Suzy unapenda tupoteze muda mama watoto wangu. Tuje tuzae watoto matahira, uzeeni.” Lara na Sesi walikuwa wamekaa vitu vya nyuma, wakicheka. “Utakuwa na nani uzeeni?” Suzy akamuuliza. “Unafikiri nikikuoa nitakuacha!? Wewe mpaka kifo.” Wakaendelea kutaniana mpaka walipofika eneo la tukio. Tino akawaambia wapitilize moja kwa moja nje, ndio wapo vijana upande wa baharini.

Upepo wa Ufukweni, Hapaharibiki Kitu.

N

a kweli upande wa bahari kulishakuwa giza, lakini mziki uliendelea. Kulikuwa na watu wengi. Wafanyakazi wa mabenki mbalimbali hapo jijini na ndugu, jamaa pamoja na marafiki. Fujo. Watu wanakunywa na kula bure kwa idhini ya mabenki waliodhamini hilo tukio la kuwaweka wafanyakazi wao pamoja kama kubadilishana mawazo na kufurahia tu.

Wakatafuta sehemu wakakaa. Tino akaenda kuwatafutia vinywaji, akaja navyo. “Sasa twende mama watoto wangu nikakutambulishe vizuri kwa bosi wangu mpya. Siku ile alikuona ulipokuja kunitukana tu. Hamkupata muda wa kusalimiana.” Mpaka Suzy mwenyewe akacheka. Wao wawili wakaondoka. “Hawa watu, huwa wanawezana wao wawili tu!” Sesi akaongeza na kucheka. Wakabaki hapo Sesi na Lara.

Walikaa hapo kwa muda, Suzy na Tino hawarudi. Sesi naye akaona watu anao fahamiana nao. Akanyanyuka kwenda kucheza mziki. Lara akakataa kwenda kucheza akabaki amekaa pale peke yake. Kila mtu alikuwa akinywa na kucheza, kasoro Lara alikuwa amekaa peke yake. Ametulia tu anaangalia watu wanavyofurahia. Lara huyu sio Lara mtoto anayependa kujirusha tena. Enzi zake angekuwa katikati ya umati akicheka na kugonga na kila mtu kwa furaha akisikika akishangilia. Lakini mapenzi yalimtenda vibaya! Akadhalilika. Akapunguzwa, hata kwenye mizani alijua hataonyesha uzito. Ujasiri uliondolewa kabisa. Akabaki aibu tupu! Alinywea hata alipokuwa peke yake alihisi watu wanamwangalia na kumnyooshea vidole. Akabaki kimya pale akiwaza yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akiwa mawazoni hata asijue alipo akasikia mtu amemfunika koti mgongoni. Akageuka. “Jax!” Akashituka sana. “Nimekuona unatetemeka baridi.” Lara akacheka kidogo akijiangalia lile koti mabegani kwake. “Nahisi siku hizi nina ugonjwa wakusikia baridi! Nalala na mablangeti na joto hili!” Jax akakaa. “Ni upungufu wa madini ya chuma.” Lara akakunja uso. “Huna damu yakutosha Lara. Ndio maana nilikuuliza kama walikupa dawa zakuongeza damu.” Lara akanyamaza na kugeukia pembeni, akatulia kama ambaye hakutaka kujibu asione umuhimu wake.

“Lara? Ni muhimu kujua.” “Sikupewa dawa Jax. Ila nilipokuwa nyumbani mama alikuwa akinikazania mboga za majani na ile juisi ya losera. Sikuwa na wasiwasi, nilijua nimerudisha damu vizuri.” Lara akamjibu. “Basi inaonekana bado hujarudisha damu yakutosha.” “Na mama naye anawasiwasi huohuo. Hata juzi kina Tino na dada Nelly walipoenda, akawafungashia mboga za majani nyingi! Mpaka nikamuonea huruma Tino.” Jax akashituka kidogo.

“Dada Nelly na Tino walikwenda Dodoma!?” Lara akashangaa kidogo. “Kwani dada Nelly hakukwambia kama alirudi kwa wazazi kuzungumza nao baada ya wewe kunikataa au kuamua kuvunja uchumba na kuahirisha ndoa!?” Jax akanyamaza. “Mimi sikuwatuma Jax. Naomba usinifikirie vibaya. Ni dada Nelly mwenyewe alinifuata ofisini akazungumza na mimi. Alitaka kujua ninaendeleaje. Akaleta chakula na matunda.” Jax akamwangalia kwa mshangao zaidi.

“Hata mimi alinishangaza hivyohivyo. Sikutegemea kama angeweza kuja kuzungumza na mimi na kuniletea chakula na matunda. Na huwezi amini Jax, ameniwekea oda ya chakula na matunda pale uliponikuta kwenye ule mgahawa, siku ile nikizungumza kingereza.” Jax akacheka. “Wewe unafikiri kwenye aina ile ya migahawa ningefikaje kama sio dada Nelly!” Wakacheka. “Basi mwenzio, naletewa juisi na matunda kila siku. Jumatatu mpaka ijumaa. Na siku nyingine za weekend naletewa vyakula nyumbani.” Jax akawa anacheka tu.

“Napendwa mwenzio!” Lara akamringishia. “Nakuona.” “Na ujue napendwa na dada Nelly!”  Wote wakacheka kwa pamoja. Nelly huwa hajui kupenda mtu. “Lakini bado unaonekana hujarudisha damu, Lara. Hiyo hali ya baridi kila wakati ni upungufu wa madini ya chuma.” “Nitakwenda kupima jumatatu. Na nitamuomba daktari aniandikie dawa nzuri.” “Naomba nikusindikize.” Lara akakunja uso na kumgeukia vizuri akimshangaa.

“Namaanisha Lara.” Jax akamsihi kwa kubembeleza. “Unataka kufanya nini Jax!?” “Kukusindikiza hospitalini.” “Unajua simaanishi hivyo, Jax!” “Unakumbuka ulinikumbusha tulikuwa marafiki?” Lara akamtizama na kuamua kunyamaza tu. “Siwezi kushindwa kila kitu, Lara!” “Kwa hiyo unataka kusema kuwa urafiki hutashindwa?” “Hata kama ni mjinga wa kiasi gani, na urafiki pia unishinde! Hapana bwana!” Lara akamtizama na kujiingiza vizuri ndani ya koti bila ya kumjibu kitu tena.

“Unataka kula nini?”  Akamgeukia na kumwangalia Jax vizuri. “Nikwambie kitu Jax?” “Kitu unachotaka kula?” “Hapana. Kitu kingine.” “Tule kwanza.” “Hapana Jax. Naomba na wewe unisikilize.” Lara akaweka msisitizo. “Naomba uwe na amani. Binafsi nimeshasamehe ndoa na yule mtoto. Naomba usijisikie hukumu au kama unawajibika kwangu kwa lolote. Sikudai kwa lolote, moyo wangu una amani na kila kitu. Nahitaji tu muda na matibabu sahihi kama hizo dawa za hayo madini ya chuma. Naamini nitakuwa tu sawa. Tafadhali acha kujisumbua na mimi. Hunisaidii. Unaniumiza na kunifanya nishindwe kuendelea. Sijui kama unanielewa?” Kimya.

“Wewe kwangu hukuwa rafiki tu, Jax. Ulikuwa mpenzi! Na sikudanganyi wala sioni haya kusema. Nilikupenda na kufunga macho na akili zangu nikawa kwako tu. Swala la kunikataa, tena nikiwa nimebeba mtoto wako na nikiwa nimeshajiona nakuwa mkeo, tunaishi pamoja, sio kitu naweza kusahau na kupotea moyoni mwangu kwa haraka.” Lara akajifuta machozi.

“Nahitaji tu muda Jax. Naamini nitakuwa sawa. Kumbuka mwenzio nimepoteza mtoto na wewe, Jax. Sio kitu kidogo. Siwezi eti nikageuka tu kuwa rafiki, tukaendelea kuanzia hapo na kusahau kila kitu au kujifanya kila kitu kipo sawa! Lara unayemfahamu wa zamani, siye huyu Jax. Moyo wangu  umejeruhika kupita hivi ninavyoonekana nje.” Lara akajifuta tena machozi.

“Nahitaji tu muda. Naamini nitakuwa sawa. Ila naomba muda mbali na hivi.” Akajionyeshea kidole yeye mwenyewe na Jax. “Chochote unachotaka kukianzisha sasahivi, sipo tayari. Misaada ya muda kwangu, kwa sasa haitanisaidia. Unipeleke hospitalini, halafu ndio inakuaje?” “Tutajua kuanzia hapo.” Lara akakunja uso huku machozi yakimtoka.  “Jax please! Usicheze na hisia zangu kwa kuwa unajua nakupenda.” “Na hilo ndilo linanipa ujasiri wa kurudi kwako Lara. Najua unanipenda kwa dhati. Najua kwangu ulitaka tu mapenzi. Najua unanipenda.” Lara akamwangalia kwa muda, akaamua kunyamaza. Wakatulia kwa muda.

“Naenda kukuletea mchemsho wa kuku wa kienyeji na mboga mboga. Au unataka wa samaki?”  “Samaki tafadhali. Nimekula kuku mfululizo. Asante.” Akambusu kichwani mara mbili. Lara akajikunja na kuinama.

Baada ya kama dakika 20 akarudi na muhudumu na chakula. “Asante.” Jax akamshukuru na kumpa pesa kidogo. Muhudumu akaondoka, akampa Lara supu, yeye akachukua kuku wa kuchoma. “Ukitaka kuonja kuku, chukua hapa.” Lara akaangalia chakula chake. “Naona hiki kitanitosha. Asante.” Akashukuru na kuendelea kula.

“Tino na Suzy wamenikimbia! Walikuwa hapa.” “Tino yuko kule karibu na maji, anapiga tu kelele. Naona ameshaanza kulewa.” Jax akaongeza. “Leo amesema hanywi. Anataka kumthibitishia Suzy kuwa yeye ni mwanaume wa kuoa.” Jax akacheka na kubaki akifikiria. “Anaonekana anampenda Suzy! Pengine wao watafanikiwa kuoana.” Lara akaongeza akiwa ameinamia sahani yake. Jax kimya.

“Unajua kesho pia tunaweza kwenda hospitalin?” Mwishoe akavunja ukimya kwa kubadili mazungumzo. “Jumamosi!?” “Yeah. Naweza kuja kukuchukua mchana au hata jioni.” Lara akakunja uso, akamwangalia kwa muda akaendelea kula.

Sesi akarudi akiwa amechangamka huku akimuita Lara kwa shangwe. Akapoa gafla mara alipomuona Jax pembeni ya Lara. Lara akamwangalia na kuendelea kula. Sesi akamwangalia Lara na lile koti la Jax, kisha akamgeukia Jax. Wakaangaliana na Jax kwa muda bila salamu, kisha akaenda kukaa pembeni ya Lara upande mwingine. “Kula.” “Acha nikamtafute Tino na Suzy, tukale. Njaa inauma.” “Si ndio nakwambia ule hapa?” “Chakula chenyewe kidogo hicho Lara. Kinakutosha wewe tu. Kula urudishe mwili. Nitarudi baadaye kukuangalia.” Sesi akaondoka na kuwaacha wamekaa pale wao wawili wengine wakiendelea kusherehekea.

Wakamaliza kula, Lara akawa amechoka. “Tino aliniahidi nikichoka, atanirudisha.” “Umeshachoka?” “Naona kwangu inatosha. Nataka nikalale. Baridi inanitesa tu. Acha nimtafute.” “Naweza kukurudisha Lara.” Lara akamwangalia, nakusimama. “Najua una majukumu yako mengi tu Jax. Naomba na mimi nisiongezeke kwenye hiyo orodha. Asante kwa chakula na koti. Usiku mwema.” “Sina majukumu yeyote yale Lara. Sasa hivi ni saa tano usiku, nipo hapa na wewe. Jua sina majukumu mengine.” Lara akabaki amesimama anafikiria.

“Lara?” Lara akamwangalia. “Naomba nikurudishe mimi nyumbani.” Jax akasimama na kumsogelea karibu kabisa. “Hamna sababu Jax. Tino atanirudisha.” “Tino yupo na Suzy, na wanafurahia na wenzao. Yeye ndio ana majukumu kwa sasa. Mimi sina. Sasa kwa nini hutaki mimi nikurudishe?” Lara akakunja uso huku ameinama.

“Eti Lara?” “Uliniacha nikiwa nakuhitaji Jax. Ukaniambia hunipendi. Kwa nini sasa hivi unataka...” Lara akajifuta machozi. “Sijawahi kukwambia sikupendi Lara. Na sasa hivi nipo na wewe hapa. Sina pakwenda.” “Unamaanisha nini!?” “Naomba nipe nafasi na muda ili kila kitu kijijibu.” Lara akabaki akimwangalia kama hamuamini.

“Please Lara.” “Sikuelewi Jax!” Jax akamsogelewa na kumshika mkono. “Naomba nisiongee chochote. Ulisema unahitaji muda, basi nakupa muda. Ila usinifukuze. Mimi ndiye niliyeharibu. Naomba nafasi ya kurekebisha kwa namna Mungu atakayonijalia.” “Iweje uje unigeuke tena, Jax?” “Naomba tutoke hapa. Tukazungumze sehemu ambayo hamna kelele.” Lara akakubali. Akaenda kumuaga Tino.

“Naondoka na Jax.” Tino akahisi hajasikia vizuri. Akamvuta pembeni. “Unaondoka?” “Naondoka na Jax ananirudisha nyumbani.” Tino akamtizama kwa muda. Lara akainama. “Kuwa mwangalifu Lara!” Lara akatingisha kichwa kukubali akionyesha hana ujasiri. Akaondoka.

Alipomsogelea tu Jax, akashangaa Tino anampita na kusimama katikati yake na Jax. “Unataka kufanya nini Jax?” Tino akamuuliza kwa hasira. “Kwa nini unataka kumchezea Lara wakati sisi wote tunajua hapatakuwa na muendelezo wowote ule ila kutaka kurudia yale yale?” Jax akatulia akimwangalia.

“Huondoki na Lara hapa.” Lara akainama nyuma ya Tino. “Usitufanye sisi wote wajinga. Na sitakubali umuumize tena Lara. Ondoka na umuache. Usirudi tena kwa Lara. Toka Jax.” “Simchezei Lara, Tino. Najua umekasirika lakini...” “Hapana Jax. Ninakujua jinsi unavyokuwa, linapofika swala la Tula, na akili yako. Huwezi kujisaidia. Ondoka. Mwache Lara.” Tino alishaanza kuvuta watu kwa sauti ya juu aliyokuwa akiongea kwa hasira.

“Ondoka Jax. Ondoka. Sitakuruhusu uondoke na Lara, hata iweje. Lara anabaki hapa, mpaka mimi nimrudishe. Toka Jax. Nenda kwa mwanamke wako.” Jax akajikaza, watu walishatulia kutaka kusikiliza. “Acha fujo Tino.” “Mimi sifanyi fujo yeyote hapa. Ila ninachokwambia hutaondoka na Lara hapa. Unataka kumfanya kama mdoli! Hapana Jax. Sitakuruhusu. Wewe umemchagua Tula, nenda kwa mwanamke wako. Acha kuchezea hisia za Lara.” Tino akazidi kuwa mkali. Jax kimya akimwangalia yeye na Lara.

Tino akashangaa sana. “Una nini Jax lakini!? Hebu muangalie Lara mwenyewe alivyo! Hata bado hajapona, na wewe unataka kurudi tena kumuumiza! Unataka kuona nini kinatokea kwa huyu binti? Kwa nini humuhurumii?”  “Mimi ndiye niliyemsababisha awe hivyo. Mimi ndiye nimesababisha maradhi ya Lara, nimemuomba nafasi ya kutengeneza nilipo haribu.” “Ili iweje? Eti Jax!?” Tino akamuuliza.

“Wewe si uliniona nilipokimbia na kujificha? Wewe mwenyewe ulinitafuta na kunifuata. Ukaniambia mimi ni mjinga, fala na siwezi kufikiria. Tula ameshika akili zangu, sijiwezi. Sasa nimejirudi, nataka kusimama sasa hivi na nichukue hatua mimi kama Jax, kwa nini unanizuia!?” “Akirudi tena Tula?” Tino akauliza. “Aliyekwambia Tula hayupo ni nani!? Tula yupo mjini. Na sasa hivi nipo hapa na Lara.” “Mimi nakuona upo hapa na Lara. Je, Tula anajua kama upo hapa na Lara?” “Sihitaji kumjulisha Tula kila ninachofanya Tino! Nina uhuru wangu mimi mwenyewe.” Jax akajibu.

“Hilo umeligundua lini? Au unaongea sasa hivi kwa kuwa Tula hayupo hapa?” “Hata angekuwepo hapa bado ningeongea hivihivi. Hanidai kitu. Na kama makosa kufanya, nilifanya mimi mwenyewe kwa akili zangu. Tula hausiki. Mimi ndiye niliyekosa.” Jax akaendelea. “Kutenda kosa si kosa, bali kurudia kosa Tino.” “Jax usiniudhi wewe!” “Sasa kwa nini hutaki kunipa nafasi nyingine Tino!? Ni lini mimi nilishamkosea Lara?” Kimya.

“Muulize Lara. Hatukuwahi hata kupishana neno. Kwa mara ya kwanza nilikosea. Nilianguka. Nimegundua kosa, ndio najirudi. Na wewe nilikuita, nilikuomba msamaha. Kwa nini unashindwa kunisamehe Tino?” “Kwa kuwa tunaijua historia yako na Tula. Upo leo umesimama hapa, kwa kuwa Tula hayupo. Akikupigia simu tu, utaondoka hapa kama unakimbizwa! Ondoka Jax.” Mpaka kina Suzy na Sesi nao wakasogea.

“Basi kama wewe huondoki mimi naondoka na Lara.” Tino akageuka na kumshika mkono Lara. “Twende Lara.” Wakaanza kuondoka. Jax akamfuata. “Nisikilize Tino.” “Usinigusee Jax. Niachie.” “Sawa. Simama basi.” “Unataka nini wewe?” “Unisikilize.” “Huna jipya Jax. Mimi nakujua.” Jax akasimama mbele yao.

“Tula yupo mjini. Nilishaachana naye zaidi ya mwezi sasa. Akili na mawazo yangu yapo kwa Lara tu tokea siku ile nilipokuita tuzungumze ukaniacha pale. Nilitoka pale nikawa na Lara tu.” Lara akakunja uso. “Kivipi?” “Siwezi kueleza mengi. Lakini naomba mnipe nafasi.” Jax akajiweka sawa. “Tino, punguza hasira. Lara, nakuomba nipe tu muda. Naomba matendo yangu yaongee.” Tino akatulia kidogo.

“Tula yuko wapi?” “Mimi sijui na wala hainihusu Tino.” “Sasa haikuhusu vipi? Akirudi?” “Anarudi wapi?” “Si kwako? Kwani wakati wote huwa anarudi wapi!?” “Nishamalizana na Tula. Naomba ukubali na uamini. Nimemalizana naye na yeye anajua.” Wakatulia. Wote. Suzy, Sesi, Lara na Jax wakabaki wakimwangalia yeye Tino.

“Hakuna baya nakwenda kufanya na Lara. Namrudisha tu nyumbani. Akilala, mimi naondoka zangu. Kesho narudi kumchukua na kumpeleka hospitalini kuangalia afya yake. Zaidi damu.” “Na wewe upime ukimwi. Tula alikuwa ana wanaume zaidi ya 110 huko Uingereza!” Jax akacheka na kutingisha kichwa. “Sitanii Jax!” “Mbona nilishapima tokea mara ya kwanza uliponiambia?” “Majibu yakawaje?” “Sijaathirika Tino!” “Na kesho ukapime tena mbele ya Lara.” “Sawa mzee.” Akamwangalia Lara.

Wakamuona ameinama tu kama anayefikiria. “Twende Lara.” Lara akamwangalia Tino na Jax. “Twende nikurudishe nyumbani.”  Akamgeukia tena Tino. “Utakuja?” Akamuuliza Tino kwa upole. “Baadaye kidogo. Wewe nenda kapumzike.” “Haya. Usiku mwema.” Akaondoka na Jax, watu wakiwaangalia.

Lara Ataka Ukweli zaidi Kwa Jax.

K

wenye gari wakawa kimya. Lara ametulia, macho nje ya dirisha akionekana mawazo yapo mbali na pale. “Unajisikiaje?” Lara akamgeukia. “Baridi?” “Hapana. Nipo tu sawa. Nikuulize kitu Jax?” “Niulize tu.” Lara akamgeukia.  “Ni nini kilitokea kati yako na Tula?” Lara akauliza tu taratibu. “Maana mimi uliniambia unampenda. Ikawaje mmeachana tena! Maana hii ni mara nyingine tena mnaachana. Na kwa maneno yako mwenyewe, uliniambia unampenda. Japokuwa alikusaliti kwa kuwa na mwanaume au wanaume wengine, bado alipokurudia, uliweza kuniacha mimi karibu na harusi, ukamrudia yeye! Hicho ni kiwango kikubwa sana cha upendo, Jax!” Lara akaendelea taratibu tu.

“Sasa, safari hii ni nini kimetokea kwenu nyinyi wapenzi wenye upendo mkubwa kiasi hicho!” Lara akaendelea. “Na kabla hujanijibu, naomba nikukumbushe Jax, unazungumza na mimi. Mwanamke uliyenikimbia kwenye nyumba tuliyokuwa tukiishi ili uwe naye. Sasa safari hii ni kipi kinaweza kuwatenganisha nyinyi wapenzi wa muda mrefu kiasi hicho?” Lara akauliza akiwa ametulia tu, akionyesha kutaka majibu ya uhakika sio kuendeleza mchezo ambao hata yeye hakujua ni mchezo gani safari hii Jax anataka kucheza naye.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ 

J

ax akafikiria kwa haraka, kisha akatoa wazo. “Naomba nikujibu tukiwa tumetulia. Ni sawa?” “Sawa.” Lara akakubali. Walifika nyumbani kwa kina Lara. “Utaingia ndani?” “Ukinikaribisha nitashukuru.” “Karibu.” Wakashuka garini. Lara akafungua mlango wa kuingia ndani. “Natamani nioge kabisa, nitoe michanga ya baharini ndipo niingie ndani ya blangeti.” “Nitakusubiri.” Jax akakaa kwenye makochi, Lara akaelekea chumbani kwake. Baada yakuoga na kuvaa, akamwita Jax chumbani kwake. Akapanda kitandani na kujifunika. Jax akaenda kukaa pembeni yake. 

Lara Apata Upande wa Jax na Tula.

Jax aeleza Kilichotokea Mpaka Kuvunja ndoa.

J

ax akamfunika tena vizuri akiwa amekaa hapohapo kitandani “Umechoka sana au unaweza kunisikiliza juu yangu na Tula?” “Naweza kukusikiliza.” Akamfunika tena vizuri kama anayerekebisha. Akavuta lile blangeti mpaka juu kabisa. Akaliweka vizuri mpaka akaridhika kuwa amemfunika Lara vizuri. Ndipo akaanza. “Tula tulianzana naye tukiwa chuoni. Ni mwanamke aliyekuwa kwenye maisha yangu kwa karibu sana. Naweza kusema kuliko hata Tino unayefikiria damu yake ikitolewa itakuwa na jina langu.” Wakacheka kidogo. Maana ndio usemi wa Lara kwa Tino na Jax.

“Tula alikuwa kama mke kwangu. Akanijua na kunielewa udhaifu wangu wote. Nilikuwa siwezi kujificha kwa Tula. Aliishi na kuongoza mahusiano yetu vile alivyotaka yeye, kwa kuwa ni kama nilimpa uhuru wote. Hapakuwahi kuwa na jibu la hapana kutoka kwangu kwa Tula.” Jax akaendelea.

“Japokuwa kina Tino walishanilalamikia sana juu yake, lakini sikujali kwa kuwa sikuona madhara yake kwangu na kwa yeyote yule. Nikahesabu ni kama mtu anayenihitaji sana, kitu kilichonifariji mimi kama mtu ambaye sikuwa na ndugu ila dada Nelly tu. Ile hali yake yakunitaka kupita kiasi, tena nikiwa sina kitu! Naomba nikwambie ukweli Lara, niliifurahia sana na kunipumbaza kabisa.” Lara akabaki akimwangalia.

“Najua unaweza usinielewe, lakini sisi ni yatima Lara. Na ndugu walitususa. Nikabakiwa na dada Nelly tu. Tena yeye peke yake na ndugu tulikuwa nao wala si mbali. Wako karibu tu na wanauwezo mzuri tu. Sasa kuja kupata msichana kama Tula, mzuri wa kutamaniwa na wanaume wengi, halafu akaning’ang’ania vile, kwangu nilihesabu na kutafasiri ni bahati ambayo haijawahi kutokea na sikuwahi kufikiri inaweza kuja kujirudia maishani. Na mimi nikabakia kwake tu, nikihakikisha simuudhi kwa lolote ili nisije mpoteza maishani. Nikabaki nikimsikiliza yeye kwa kila kitu.”

 “Aliponiacha na kwenda kwa mwanaume mwingine, au wengine. Nafikiri nilikwambia kuwa aliniumiza sana. Unakumbuka?” Lara akatingisha kichwa kukubali. “Aliniacha na hofu ya hali ya juu nikiona ni kama nimetelekezwa peke yangu, sijui tena chakufanya. Nikapatwa na ile hali kama mtoto anayemlilia mama yake asiondoke na kumuacha peke yake mahali, na bado huyo mama akamuacha kikatili. Mimi ndivyo nilivyojisikia kwa Tula. Narudia tena. Unaweza usielewe hiyo hali maana haieleweki na nimeshindwa hata kujieleza kwa wengine, najitahidi kwako, kwa kuwa najua nawajibika kwako.” Jax akaendelea.

“Sasa nakumbuka siku moja mara baada ya kutoka kwenye sendoff yako Dodoma. Nafikiri juma lilelile, akanipigia simu na kuniomba tukutane kwenye hoteli aliyofikia kutoka Norway. Hata sikuwa nikijua kama alikuwa Uingereza. Nilichokosea, hata sikumwambia Tino au wewe, nikaenda.” Jax akatulia kidogo. Tula akamuona mpaka macho yamebadilika rangi.

“Nakwambia ukweli. Naomba niwe muwazi kwako Lara. Tula hakutumia nguvu nyingi kunishawishi. Nilikuja kuamka asubuhi pembeni ya Tula. Nikajiuliza, niliwezaje kulala na mtu ambaye hata sikuwa nimemuona muda wote huo! Haikuishia hapo. Ni kama ulimwengu mzima ukawa umesimama. Ni mimi na Tula tu.” “Wakati huo hata ulinikumbuka Jax!?” Lara akauliza kwa upole.

“Ile shauku niliyokuwa nayo wakati ule, nilijiambia hakuna jinsi nikalinganisha ule upendo ninaojisikia kwa Tula.” Jax akaendelea bila yakujibu jibu la moja kwa moja. “Akanikumbusha na kunirudisha kule tulipokuwa naye zamani! Ugumu wa maisha tuliopitia. Na sijui ni kwa vile alivyoniambia alishindwa kuolewa sababu yangu! Sijui. Lakini nikampokea kwa upendo mkubwa sana huku nikimuhurumia. Aliniambia aliteseka sana baada ya kumwambia huyo mwanaume wake kuwa ananipenda mimi.” “Sijaelewa Jax.” Lara akataka maelezo zaidi.

“Yaani Tula aliniambia alitaka kuolewa na huyo mzungu, akamvalisha kabisa mpaka pete ya uchumba, akatambulishwa mpaka kwa familia ya huyo mwanaume wa kizungu, lakini akagundua mapenzi yake yako kwangu. Kwa hiyo akamwambia huyo mwanaume kuwa ananipenda mimi, huyo mwanaume akakasirika sana. Akaanza kumtesa. Akaniambia ni kama akamfungia, ndio hapo ameweza kutoroka na kurudi Tanzania kunitafuta.” “Ni kweli?” Lara akauliza.

“Aliniambia kila kitu alichojua nataka kusikia na kitakachonifanya nishindwe kufikiria kabisa na nimuhurumie. Basi, akaanza kuweka mipango. Yaani mambo yakawa yanakwenda kwa haraka. Ikaanza sasa aibu ya kuja kukutizama baada ya uchafu wote ule. Nikamweleza jinsi ulivyo kwangu na vile ulivyo mwaminifu. Nikamwambia najisikia vibaya nashindwa hata kurudi kwako. Akanifariji sana na akaniambia utaelewa tu. Kwa jinsi ulivyo mzuri, utapata mwanaume atakayekupenda. Hilo nalo likapitishwa kichwani kwangu kwa haraka. Nikasema unaweza kuumia lakini baada ya muda mfupi, utapata mwanaume mwingine, maisha yataendelea.” “Uliwezaje kufikiria hivyo Jax!?” Lara akashangaa sana, lakini Jax hakujibu akaendelea.

“Tukaendelea kukutana hotelini. Baadaye akataka tuhame pale. Nikamwambia sithubutu kuhamia naye pale nilipoishi na wewe. Ile ni kama nyumba yangu mimi na wewe. Nikamwambia itakuwa mbaya sana.” Jax akatulia kidogo.

Kisha akaendelea. “Kuna kitu nilikuwa sijakwambia Lara. Nilitaka iwe kama suprise.” “Nini?” “Nilinunua nyumba. Nikasema iwe suprise. Kwamba wakati tunatoka honeymoon, badala turudi pale Sinza, nikupeleke pale. Kama kukufurahisha tu. Ni nyumba niliipata kwenye mnada. Nzuri tu na bei ilikuwa nzuri. Hata Tino sikumwambia kwa kuwa nilijua, akijua tu yeye, atakuja kukwambia.” Asijue anazidi kumuumiza Lara ambaye alishajua inamaana ndiko walikohamia na Tula! Lara akaumia sana kuona yeye alijibana naye kwenye sehemu ndogo, tena yakupanga, halafu Tula akaja kwa muda mfupi tu, na kuhamia kwenye nyumba kubwa! Lara akazidi kuumia hata kule kuanza kumuelewa kukaanza kupotea.

“Basi, Tula akaweka pressure. Lazima tutafute sehemu yakuishi pamoja. Huku akinikumbusha jinsi tulivyo hangaika sehemu yakuishi baada ya kumaliza chuo, maana dada Nelly alishatufukuza nyumbani kwake na kumuonya Tula asiwahi kurudi pale. Basi Tula akanilalamikia sana akinikumbusha tulikotoka na shida tuliyopata kwenye maisha akiwa na mimi akinivumilia kwenye vijumba vya kupanga tena uswahilini! Kama jinga vile, hilo nalo likaniingia, nikahamia naye kwenye ile nyumba.” Lara akapoa, akawa kama amejibiwa kuwa na Tula naye alitoka naye mbali sana, tena pengine mbali zaidi yake yeye. Kuwa Tula anayo haki yote yakulia kivulini na Jax. Lara akapoa kabisa.

“Maisha yakaanza hapo. Yakatokea yote yakutokea kati yetu. Mimi na wewe. Sikuwa na jinsi ya kujirudi kwa yeyote tena Lara. Nilishafika mbali. Kama kawaida yake au kama vile nilivyomzoeza zamani nilivyokwambia mpaka wakina Tino walinionya au kulalamika. Tula akawa tena kama yeye ndio mwenye ile nyumba pale. Anajua kufanywe nini kuanzia asubuhi mpaka usiku. Hapo nikawa sijui kama mwenzangu ulikuwa mjamzito na wala kama mimba ilitoka!” Lara akamuona mpaka uso umebadilika tena.

“Alikuja kunitapikia dada Nelly, sijawahi kumuona akiwa amekasirika vile! Katika maneno yake machungu, ndipo nikajua kama ulipoteza mtoto! Gari na pete ulishampa Tula!” “Kwani hukujua!?” Jax akajicheka kwa uchungu. “Mahusiano yangu na Tula! Wewe utashangaa tu. Anyways, nikachanganyikiwa sasa. Kwamba Lara aliugua! Lara hana usafiri! Nikapata hukumu kwamba ni kama nimekuadhibu zaidi ya nilivyotarajia! Nilijua ungeumia tu, ikawa basi, na ungeendelea na maisha yako. Lakini sio kuugua kwa kiasi hicho! Dada Nelly aliondoka tulipokuwa tumekutana, kama aliyeniomba nisimtafute tena.”

“Ikabidi kujikaza sasa na kumtafuta Tino. Naye akanitukana kwa kadiri ya uwezo wake, lakini akanipa ukweli wote. Nikarudi nyumbani kwa Tula. Naye akaniambia maneno machafu na ya kashifa ambayo hayakuwa mageni, lakini ikawa kama amenifungua macho na amethibitisha alichoongea Tino miaka yote. Kwa mara ya kwanza kila kitu kikafunguka mpaka akili zangu anazoita Tino za kijinga.” Lara akabaki kimya akimsikiliza.

“Usiku uleule nikamuomba aondoke, nikamwambia ndio mwisho wetu na nikamwambia nimejua amenidanganya.” “Kama angekuwa hajakudanganya je?” Lara akauliza tena. “Nahisi nilifika mwisho Lara. Yaani kwa mara ya kwanza nikafunguka macho nakuona yale hayakuwa mahusiano ya watu wawili. Na hayakuwa sawa kwangu wala kwake. Tula hajui kunisikiliza Lara. Hivi au vile tulivyokuwa tukiishi mimi na wewe na kupanga mambo yetu kwa pamoja na kuelewana, usingetukuta hivyo na Tula.” “Sasa mlikuwa mnafanyaje!?” Lara akashangaa, maana alimjua Jax anaakili nzuri ya maendeleo na mipango mizuri tu, na hakuwa mbishi kabisa.

“Yeye atoe maagizo, mimi nikubaliane naye. Na nisikosoe hata kwa kuongeza wazo. Sijui kwa wengine, ila ndivyo ilivyokuwa kwangu. Kwa hiyo nikajua sitakaa nikamsaidia, na mimi sitakaa nikaweza kufanya hatua yeyote ninayofikiria ni njema.” Akajicheka tena yeye mwenyewe. “Hata yeye mwenyewe aliniambia sina akili ya kufikiria.” “Jax!!” Lara akashangaa sana.

“Kwani alikosea? Alikuwa sahihi Lara. Navunja ndoa iliyokuwa imebaki siku chache tu, kwa maneno yake! Bila hata kuthibitisha! Hata mimi nilikubaliana naye na kujidharau sana.” Lara akabaki akifikiria. Ni kama akapotea kabisa pale kimawazo na Jax akamuona hasikilizi tena. Akavuta tena blangeti kama anayemfunika tena kumbe nikutaka kumrudisha pale. “Asante.” Akashukuru akionekana amerudisha mawazo pale.

Jax akaona aendelee. “Basi, nikamwambia aondoke pale. Kwa jeuri kabisa, akakataa.” “Jax!” Lara akashangaa tena. “Tena hapo anavaa ili aende club. Yaani ananiacha mimi ndani kwa kunitaarifu tu, wala si kuniomba ruhusa. Sikumsemesha. Nikawa kama nimeshindwa kwa kuwa amenikatalia kuondoka. Nililala pale kitandani kama lisaa au masaa mawili hivi, ikawa kama kengele masikioni. Niliruka kama swala. Nikamkusanyia vitu vyake vyoooote. Nikamtupia nje.” “Jax! Akija kurudi!?” “Nani amekwambia hakurudi? Humjui Tula wewe! Yaani alishajiaminisha mimi ni mali yake kabisa.”

“Ulifanyaje?” “Ilibidi kusimama kiume haswa ili kumuhakikishia, mimi ni mwanaume, nimeamua, na sitabadilisha mawazo hata iweje. Na nilihakikisha tunapata muda wakutulia kama hivi, ili asifikiri namkimbia na kunifuata nyuma.” Lara akabaki akimtizama. “Alifanya fujo nyingi tu aliporudi nyumbani na kukuta mizigo yake ipo nje. Mlinzi akampeleka polisi. Nikaenda kumtoa kesho yake.” “Jax!” “Kabisa. Tula ni mbabe na mkorofi sana.” Jax akafikiria.

“Halafu hatukuwa tumeanzia tu hapo. Unajua tangia tunarudiana hapa baada ya kuvunja harusi yangu, nikaanza kuona tofauti. Unajua jinsi tulivyoishi mimi na wewe kwa utulivu! Halafu tukaja kuishi naye, haikuhitaji matusi ya Tino kuniambia nimejiingiza kwenye shida! Ile hali ya utulivu ikaisha. Jambo moja, hadi jingine. Hali yakupokonywa uhuru wangu ikaanza kuwa dhahiri kabisa. Hakuna amani, hakuna heshima” Jax akatulia kidogo kama anayetafuta jinsi ya kuweka sawa neno linalofuata, asiharibu.

“Tula anapika. Ni mpishi mzuri sana. Anaweza...” Jax akasita. Akawa kama anayefikiria tena, ila akaona abadili anachotaka kusema. “Lakini hakuna utulivu. Sijui yupo na...”  Akafikiria tena. Akawa kama amekosa jinsi ya kumuelezea. “Anyways. Nafikiri heri mimi na wewe tungekuwa tumeachana kwa ugomvi au labda heri tungekuwa na matatizo, lakini nikawa ni kama nimetoka kwenye kivuli, nikafuata moto! Kila kitu kikakosa maana. Lakini nikasema nivumilie tu, nione mwisho wake halafu nikawa ni kama najiadhibu. Nikajiambia yote yanayonipata ninastahili. Nikatulia.”

“Sasa kuja kusikia wewe ni mgonjwa, na mimi ndiye nilisababisha kupotea kwa mtoto! Halafu bado hakuna nidhamu! Sio mke wangu wala hatuna mtoto anayetufunga pamoja mimi na Tula! Nikajiuliza garama yote hiyo ninayolipa ni kwa ajili ya nini na nani! Nini kinanifunga! Nikajiuliza nitaishi vile mpaka lini! Kwa nini! Hayo yote yakaibuka kwa wingi na kasi kichwani mwangu nakujigundua ni kweli sina sababu!”

“Sasa kilichoniuma zaidi ni pale nilipokuja kukuona wewe mwenyewe?” “Wapi tena!?” Lara akauliza kwani hakukumbuka kumuona Jax ila siku hiyo mchana. “Nilikuja nikaegesha gari karibu na ofisini kwenu ili kukuona.” Lara akashangaa sana. “Nilikuona unatoka na kina Sesi mnakwenda kula. Nilikaribia kulia.” Lara akakwepesha macho. “Ulikuwa umekwisha zaidi ya hivyo. Ulitoka ukawa kama unaota jua. Nikaanza ku google palepale. Kwa nini kuwe na joto halafu unatetemeka baridi!” Lara akacheka taratibu. “Na kweli baridi inanisumbua!” Lara akaongeza.

“Basi na mimi nikashangaa hivyohivyo. Ndio nikajua ni upungufu wa damu. Nikaanza kufikiria vitu vya kuongeza damu. Matunda na jui..” “Subiri kwanza Jax, kwa hiyo wewe ndio umeniwekea bili ya matunda na juisi!?” Jax hakujibu. Ikawa kama ambaye hakutaka Lara ajue. Lara akakaa kwa mshituko. Ni kama akawa amepata jibu. “Oooh my Jax! Basi mimi muda wote najua ni dada Nelly, kwa kuwa yeye ndiye aliyenifuata ofisini kwetu na kunisisitiza nile kwa kuwa nimekonda sana! Akaleta chakula na matunda. Sasa jioni yake nilipojiwa na muhudumu wa ule mgahawa, na yeye akasema hajui ni nani muhusika, sisi wote tukasema ni dada Nelly na anafanya makusudi kutojitambulisha kama ni yeye muweka bili ili asifuatwe nyuma. Nikaendelea kula bila shida!”

“Sijamtafuta dada Nelly kwa muda mrefu kidogo. Mara ya mwisho alikuwa na hasira na mimi kama nilivyokwambia. Sijawahi kumuona akiwa hivyo! Alinionyesha kwa maneno na vitendo kuwa nimemkera mpaka mwisho. Nikaona nimuache kwanza mpaka nitengeneze. Au mimi mwenyewe nielewe ni nini kinaendelea kwenye maisha yangu, ndipo nimtafute.” Lara akabaki ameinama akifikiria.

“Nikikuomba tena msamaha, unafikiri itasaidia hata kidogo?” Lara akamwangalia, na kuinama. Akajivuta mwisho kabisa ya kitanda, Jax akasimama na kumzungushia blangeti. “Asante.” Akatulia. “Eti Lara?” Jax akauliza tena. “Ili iweje Jax?” “Tujipe muda tuone kitakachotokea. Please Lara.” “Hivi unajua tumeishi pamoja kwa zaidi ya mwaka? Tena kama mke na mume mpaka ulipoamua kuwa mimi sikufai! Sasa, sasahivi ni kipi cha tofauti unataka tufanye tena?” Jax akanyamaza.

“Nimeingiza aibu na fedheha kubwa nyumbani kwetu, Jax! Watu wananyanyasa wazazi wangu wanasema ni matapeli. Walitangaza kuwa naolewa ili kujinufaisha! Watu wawachangie!” Jax akaumia zaidi. “Hapa ninapokwambia zile zawadi zote nilizokuwa nimepewa, watu walidai. Mama akawa na kazi ya kuwarudishia mmoja hadi mwingine. Kwa zile ambazo walishatumia pale nyumbani, maana niliacha vitu vyote nyumbani, imebidi kumsaidia mama kununua na kulipa. Mshahara wangu wa mwezi uliopita, karibu wote nimewatumia nyumbani uwasaidie kwa kuwa baba na mama wanakusanya pesa za kulipa michango ya sendoff ambayo ilishafanyika na watu wakala na kunywa. Lakini leo hii wanadai wazazi wangu!” Lara akaendelea taratibu na kwa uchungu sana.

“Hali ilikuwa mbaya mno, sina jinsi nikakueleza ukaelewa. Baba alishukuru vile dada Nelly alivyokwenda na kuwaachia pesa. Angalau anasema ameweza kumaliza kwa wale waliokuwa wakimsumbua na kutuchafua. Kwa kifupi tu Jax, ni mimi, mimi Lara, tuliyeishi wote muda wote huo nikikupenda, kukuheshimu na kukujali kwa moyo wangu wote. Na bado hukunichagua mimi! Uliamua kuniacha, tena nikiwa nimeshavaa magauni ya sherehe! Nikitangaza naolewa. Niambie Jax, leo tunajipa muda wa nini tena?” Lara aliongea taratibu akiuliza kwa uchungu akiwa ni kweli haelewi Jax anataka wafanye nini tena.

“Mimi ndiye niliyeharibu Lara. Nipe nafasi ya kurekebisha. Sihitaji chochote kutoka kwako. Ila tu niahidi hutabadilika. Nakutaka Lara wangu ubakie vilevile. Ila mimi ndio nibadilike, niwe mwanaume ambaye ulimstahili.” Jax akajisogeza karibu. “Niangalie Lara. Niangalie tu.” Lara akamwangalia. “Najua sasa hivi ni mapema sana. Huwezi kuniamini na bado unamaumivu. Usiharakishe kwa chochote, usibadili mawazo juu yetu. Niachie mimi nirekebishe pale nilipoharibu. Tulia tu mpaka utakapoona nimefanikiwa kutengeneza, ndipo wewe mwenyewe uniambie kama upo tayari kwa ndoa.” Lara akakunja uso.

“Usinijibu kitu sasa hivi wala naomba usinikatalie, tafadhali. Tumeshafanyiwa kila kitu, ilibaki tu ndoa kanisani. Tuachie hapo. Nipe mimi muda. Niangalie. Nichunguze mpaka utakapoona nipo tayari kuoa. Kisha niambie. Na safari hii hatutachangisha watu. Tutafanya harusi kulingana na uwezo wetu. Hata kama watu watakuwa 10, basi tutafunga ndoa. Ni sawa?” Lara akainama.

“Lara? Nimekosa mama. Nakubali kuwa nimeharibu haswa. Nisamehe mpenzi wangu. Sasa hivi hakuna mtu mwingine kati yetu, ni mimi na wewe tu. Makosa yangu yatatokana na mimi sio mwanamke mwingine. Na ninajua  na wewe ni shahidi yangu, tokea tuanzane mimi na wewe, sijawahi kutoka nje ya mahusiano isipokuwa kwa Tula, na nakuahidi haitakaa ikatokea tena.” Jax akaendelea kujisogeza. “Nakuahidi kutulia. Nimejifunza kwa kumwaga damu ya mwanangu mwenyewe! Hakika sitarudia Lara. Nakuapia na Mungu wangu atanisaidia.” Kimya.

“Nijibu basi Lara! Au wewe hutaki nitengeneza nilipoharibu?” “Sijui tena Jax! Hakika sijui. Nipo kama niliyevurugwa haswa.” “Basi naomba tujipe muda. Nisubiri huku ukikumbuka nimekosa sana na nimekuomba msamaha. Niangalie matendo. Ukijiridhisha, niambie tufunge ndoa, tukaishi kama zamani. Tupate ule usiku wakucheka.” Lara akazidi kuumia akiwa anakosa tumaini. “Lakini hayo yote hayakutusaidia kuwa pamoja Jax! Hatukuwa na mengi lakini tulikuwa na amani kubwa sana. Sikuwahi kulala na hasira, nililala..” “Na Jax.” Jax akamalizia maana ndio ulikuwa usemi wao wakijisifia kwa watu wao wa karibu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jax alikuwa na usemi aliopenda kuusema na kujisifia kwa watu mpaka watu waliomfahamu Jax wakaanza kuutumia huo usemi. “Siku hizi hata nikiwa na njaa, sijala usiku, silali na njaa, nalala na mpenzi wangu Lara.” Au alikuwa akisema. “Maisha yanaweza yakanipiga nje. Kila kitu kikanipa sababu ya kukasirika. Lakini siku hizi usiku ninaporudi kwa Lara wangu, anahakikisha anamuondoa hasira kitandani kwetu, tunabakia kulala sisi tu wawili.” Wakati wote Jax alikuwa akisema ameacha kuleta wageni kitandani kwake tokea amkaribishe Lara kwenye maisha yake. Mgeni njaa, hasira, kutokuwa na usingizi, wote wameondolewa na Lara kitandani. Wamebakia wao tu wawili. Na kweli ndivyo ilivyokuwa kwa wawili hao mpaka kushangaza watu!

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wote wakawa kama wamepotelea mawazoni tena. Kama wanaojiuliza walifikaje hapo walipo! Lara ndio alikuwa haamini kama hayo yameweza kuwatokea wao! Vile walivyokuwa mpaka watu kuwatamania mpaka kufika kuwa gumzo! Ingetokea kwa wapenzi wengine pengine ingeleta maana. Lakini sio Lara na Jax. Wote wakabaki kimya mpaka Jax alipovunja ukimya. “Kesho nitakuja kukuchukua twende hospitalini. Ukaangaliwe damu na mimi nipimwe UKIMWI, mbele yako.” Lara akacheka kidogo. Akamkumbuka Tino.

“Nitamtafuta tena Tino nizungumze naye, japo najua nishamkera kupita kiasi. Lakini nitamtafuta tu. Tino amenivumilia kwa muda mrefu sana. Tokea chuoni! Anahaki yakuchoka.” Lara hakujibu. “Basi nitakuona kesho. Usiku mwema.” “Na wewe Jax.” Jax akaondoka.

Jumamosi.

Jumamosi asubuhi akiwa anakwenda kazini, Jax akampigia simu Lara. “Uliamka salama?” “Bado nipo kitandani.” “Samahani nimekuamsha.” “Hamna neno. Mbona asubuhi asubuhi?” “Nakwenda kazini. Nitatoka kwenye saa sita.” “Oooh! Kazi njema.” “Asante. Nije kukupitia twende tukale ndio twende hospitalini?” Lara akabaki kimya. “Lara?” Bado moyo wa Lara ulisita. “Naona labda ukitoka kazini ukapumzike tu Jax. Jana tumechelewa kulala, asubuhi hii upo barabarani kwenda kazini. Usijali. Mimi nitakwenda tu mwenyewe hospitalini. Nitakujulisha majibu yatakavyokuwa baada ya vipimo.” “Natamani muda na wewe Lara?” Hapo akagusa moyo wa Lara, akajisikia vizuri.

“Au unaona shida kuonekana na mimi tena hadharani?” “Hapana Jax. Sina chakuficha tena. Kila mtu ameshasikia habari zangu. Wanaonijua na wasio nijua. Sina chakuficha tena, ila nilikuwa nakuhurumia. Nilifikiri ungependa usingizi wa mchana!”  Akajirudi na kuwa muugwana tu. “Usijali. Nitawahi kulala usiku.” “Sawa. Nitakuwa nikikusubiri basi.” Wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika mida ya saa 7 mchana, Jax akawa ameshafika nyumbani kwa kina Lara. Aliona kabisa hakuna aliyemchangamkia. Hata Suzy maneno mengi alifungua tu mlango, alipomuona ni yeye, akaondoka akiwa amemuacha palepale mlangoni. Jax akaingia mpaka sebuleni. Aliwakuta wote kasoro Lara. Akasalimia, lakini hakuna aliyeitika. Wote macho kwenye luninga. Kimya. “Lara yupo?” Kimya. Akaona isiwe tabu, akatoka pale bila kuwaaga.

Alipotoka nje akampigia simu Lara. “Nipo hapa nje ya nyumba yenu.” “Nipo chumbani, nitatoka baada ya muda mfupi sana.” “Basi nakusubiria hapa nje kwenye gari.” Jax akarudi kwenye gari yake akakaa. Baada ya muda Lara akatoka. Alivaa kawaida tu lakini alipendeza na bado alionekana mnyonge usoni. “Pole na kazi.” Akaanza Lara wakati anapanda garini. “Asante. Umeshindaje?” “Vizuri tu.” Jax akaondoa gari.

“Unataka kwenda kula wapi?” “Popote pale. Sina uchaguzi.” “Huna hamu na kitu maalumu?” Lara akafikiria. “Hapana sina chaguzi. Tunaweza kwenda kula pale unapopenda kula ugali wa muhogo.” Lara akatoa wazo, wakacheka. Kisha kimya. Mpaka sehemu ya chakula.

Wote waliagiza soda kwanza, ndipo akaja mtu wa jikoni wakaagiza chakula. Kweli Jax akataka ugali wa muhogo, mboga za majani na samaki wa nazi. Jax hakupenda pombe kabisa, si kama Nelly au Tino. Lara akata ndizi mchuzi. Muhudumu akaandika na kuondoka. Kulikuwa na watu wengi tu pale siku hiyo ya jumamosi mchana. Lara akajituliza kitini akawa anaangalia pembeni lakini Jax alijua hayupo pale.

“Tunakuwa na hospitali maalumu kwa ajili ya wafanyakazi wa benki na familia zao kutibiwa. Tunalipiwa matibabu. Tunakuwa na kadi kabisa. Kwa hiyo nilikuwa nikifikiria, twende kwenye moja ya hizo hospitali, mimi nitakulipia wewe.” “Hivi siwezi tu nikaenda kununua dawa za kuongeza damu na kuanza kutumia bila kuhangaika kwenda kupima?” Lara alipomaliza tu swali, Tula akaja.

ATAFUTAYE HACHOKI!

“Mambo!”  Akamsalimia Lara na kuvuta kiti palepale kwenye meza yao, akakaa pembeni yao. Jax alikuwa amekaa mbele ya Lara. Lara akamwangalia Tula na Jax. Akanyamaza. “Kuna kitu nataka kukuonyesha Jax. Sina ugomvi na wala sikutaka kukukorofisha.” “Mpaka sasa hivi, umenikorofisha Tula. Na nilikuonya.” “Nimefanya nini hapa? Nimekuja hapa mezani kwenu, nimemsalimia Lara kwa heshima, na kukaa. Nimekosea wapi?” Lara kimya.

“Hiki unachokifanya hapa, wewe unaona ni sawa?” Jax akauliza taratibu akionekana kubadilika kabisa na ameshapandwa na hasira. “Hupokei simu zangu na umenizuia nisiingie nyumbani kwetu.” Jax akabaki akimwangalia. “Lakini sitaki kesi Jax. Nimekufuata hapa ili kuzungumza tu.” Jax kimya akimwangalia. Lara akashangaa hajibu. Ila akatoa simu yake akaangalia na kubonyeza kidogo, na kuiweka mezani.

Tula naye akafungua mkoba wake akatoa karatasi na kama kijikaratasi kidogo tu akaweka mezani. “Hiki ni kipimo. Ukiweka kwenye mkojo, kikionyesha mistari miwili, ni mjamzito, kikionyesha mstari mmoja sio mjamzito.” Moyo wa Lara ukalipuka ndani kwa ndani. “Sasa mimi nilipima. Ikatokea mistari miwili. Nikawa sijaamini. Nikaamua kwenda hospitalini. Wakanipima, nikakutwa mjamzito. Ndio maana nilikuwa nikikupigia tokea week iliyopita ili kukwambia ni mjamzito.”

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usikose muendelezo kujua kitakachojiri. Jax anaomba nafasi ya pili kwa Lara aliyeharibikiwa na mimba, huku Tula naye amerudi na habari za ujauzito, nini kitaendelea...

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment