Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Chozi Langu! - SEHEMU YA 7. - Naomi Simulizi

Chozi Langu! - SEHEMU YA 7.

 Disco Imeingia Mmasai Wa Lubega.

H

awakujua Nelly, dada yake Jax alipotokea, wakashangaa anaegesha gari kwa fujo pembeni ya gari ya Jax. Akashuka. Jax mwenyewe akaonekana ameshituka. Akamwangalia Tino. Tino akarudi nyuma kabisa. “Kuna nini?” Akauliza Nelly. Tula akatoa mikono pale dirishani kwa haraka. “Tula..” Jax akataka kujibu lakini dada yake akamwangalia kwa ukali. “Ninapozungumza na wewe, usikae ndani ya gari ukinichungulia nje wakati mimi napigwa na jua nje.”  Kwa haraka Tula akampisha Jax mlangoni, akashuka. Lakini gari aliliacha likiwa linawaka. Lara akabaki ndani akitetemeka.

“Nilikuja ku..” “Sijakuruhusu uzungumze na mimi. Nyamaza.” Akamkata Tula, akamwangalia Jax. Jax akajua ndio anaulizwa yeye. “Nilitoka ofisini, nikaenda kumchukua Lara ili nimpeleke hospitalini akaangaliwe afya yake. Lara bado anasikia baridi hata kwenye jua.” “Hana damu.” Dada yake akaongeza. “Ndilo hilo nilihisi. Tukakazana na matunda na juisi ya kuongeza damu, sasa hivi ni kama miezi miwili, bado hali yake ipo vilevile.” Nelly akamwangalia Lara ndani ya gari, Lara akainama.

“Sasa hakuwa amekula.” Jax akaendelea. “Nikasema nimlete hapa ale kwanza kabla ya kwenda hospitalini. Hata hatujaanza kula, Tula akanifuata hapa kuwa ni mjamzito mimba ni yangu.” “Anajuaje kama mimba ni yako!?” Akauliza Nelly kwa kushangaa. “Mimba ni...” “Sijakuuliza wewe. Nazungumza na Jax. Nyamaza kabisa.” Wakamsikia Tino anacheka. “Mimi sijui dada yangu! Ila nilimwambia sikatai majukumu kwa mtoto wangu. Mtoto akizaliwa na akawa ni wangu, nitamtunza mtoto wangu. Akauliza kwa sasa hivi yeye ataishi wapi?” “Kwani mliishia wapi? Si mlikimbia mkaenda kuishi pamoja?” Tino akakohoa. Na Nelly alimuuliza kwa kumkejeli tu. Hakuna linaloendelea kwa huyo mdogo wake asijue. Zaidi aliporudi Tula.

“Alishaondoka nyumbani kwangu. Siishi na Tula. Lakini napo hapo nilimwambia anayo magari yangu mawili. Moja alilochukua kwa Lara, na jingine nilimnunulia wakati naishi naye. Ndio nikamwambia atafute kazi, na wakati anatafuta kazi, ayafanyie hayo magari biashara mpaka atakapojifungua na kuthibitika mtoto ni wangu.” Akataka kubisha lakini akasita, akakumbuka aliambiwa anyamaze. “Muulize Lara kama sijamuhakikishia kuwa nitatunza mtoto kama ni wangu?” “Lakini..” “Nitakubamiza Tula, mpaka nikuvunje taya! Acha kutufanya sisi wote hapa watoto wadogo. Nimekwambia nyamaza. Huna adabu wewe! Hujafundishwa kwenu jinsi ya kusikiliza watu wakiongea?” Nelly akambadilikia, mpaka Jax akarudi nyuma.

Akamtizama Jax. Jax akajua ndio anatakiwa kuendelea. Hakupoteza muda, akaendelea. “Akaanza fujo pale ndani, mpaka Tino akaja. Tukazungumza na nikamwambia Tino, na wewe nakwambia dada Nelly. Nimemalizana na Tula. Kama mtoto kweli ni wangu, nitamlea mwanangu bila shida. Lakini sitarudi kuwa na mahusiano na Tula. Hata leo mkisema nirudiane na Tula sababu ya hili, kweli mnataka  watoto wangu wazaliwe waone jinsi ninavyodhalilishwa kila siku? Nitakuwa baba wa namna gani mimi? Hapajawahi kuwa na mahusiano kati yangu na Tula. Ila yeye Tula akitaka nifanye anachotaka yeye! Hata yeye amekiri kwangu.” Jax akaendelea.

“Matusi anayonitukana Tula, hata kama ninastahili, nimeishi na Lara karibia miaka miwili, mbona yeye hajawahi kunitukana hata mara moja?” “Hilo umelikumbuka lini?” Dada yake akamuuliza kwa kumsuta huku akimwangalia machoni. Tino akacheka kiumbea taratibu huku anajificha. “Si ndio nimegundua kosa dada yangu! Nipo kwenye kurekebisha. Hata Lara nimemuomba anipe muda nirekebishe.” “Muda wa kurekebisha wakati hawara yako anamkera? Anafikiria saa ngapi huyo Lara wakati unamletea mahawara zako karibu? Nilikwambia nini Jax?” Dada yake akawa mkali.

“Nakwambia ukweli dada yangu. Mimi sijamleta Tula karibu na Lara. Lara ni shahidi yangu. Tula amenifuata mwenyewe. Na Tula huyu hapa, muulize kama sikumpiga marufuku asiwahi kumfuata tena Lara. Muulize.” “Sina muda wakijinga mimi.” Akafyonza Nelly na kuendelea. “Alimfuata Lara ofisini akimdai gari, ukaendelea kumchekea huku ukimbembeleza! Amepewa tena gari na pete bila kukwambia, ukajua, bado unamchekea! Unafikiri ni kipi kitakachomfanya aelewe sasa hivi kama unamaanisha?” Dada yake akamuuliza kwa ukali.

“Lakini nilimfukuza.”  Jax akajitetea kama mtoto mdogo mbele ya dada yake. “Ulimfukuza au ulimtolea nguo nje akiwa ameondoka?” Jax akashangaa kidogo. “Unafikiri mimi sijui?”  Akamuuliza kwa ukali. “Wewe mwanaume mzima, upo nyumbani kwako, unamfukuza hawara. Hawara anakwambia hatoki, ulivyo mjinga wewe, unasubiri aondoke, ndio unamtolea mizigo nje na kuwaomba walinzi wakusaidie kumzuia kuingia ndani! Anapelekwa polisi, unaenda kumtoa! Kama huo sio upumbavu na ujinga wa kupindukia wa kupigwa makofi ni nini?” Nelly akamuuliza kwa ukali.

“Halafu eti leo upo na mwanamke wako, yeye anakuzuia kuondoka, na wewe ulivyo dhaifu unaita askari wakusaidie kumtoa! Una nini Jax!? Upumbavu huo umerithi wapi wewe? Unarudi kwa Lara, ili iweje wakati hata wewe mwenyewe hujielewi?” “Najielewa?” Jax akajitetea. “Mbona umeshindwa kumtoa hapa Tula?” Kimya. “Anakudharau kwa sababu anakujia upo dhaifu! Once and for all, simama kama mwanaume. Muonyeshe wewe ni mwanaume unayejielewa uone kama atakufanyia michezo ya kipuuzi. Ameshakusoma na kukujua wewe ni dhaifu sana.” Nelly akaendelea.

“Hujui hali yake Lara kwa kuwa hukuwepo kushuhudia madhara uliyoyasababisha baada yakupotea. Tino alimuona. Kwa kifupi tu. Ulimdhalilisha vibaya sana mpaka kuugua. Ya pili ya mtoto wenu. Nafikiri hilo unalijua na ndio maana yupo na hiyo hali mpaka sasa. Ya tatu ndiyo hii inatokea hapa mbele yetu. Na mimi nashuhudia! Unaacha hawara, mpumbavu kama huyu, anaongea na mwanamke wako ambaye ni mdhaifu, kwa kumsababishia wewe mwenyewe, na wewe umetulia tu ndani ya gari! Inatofauti gani na mama?” Jax akanyamaza ila mpaka macho yalikuwa mekundu. Kimya, akainama.

“Umelaaniwa na nani wewe mtoto?” Kimya. Jax akabaki ameinama. “We Jax?” Akamuita kwa ukali kila mtu akashituka. Jax akamwangalia dada yake. “Mwanaume gani unashindwa kulinda watu wa nyumbani kwako wewe! Ulishindwa kwa maamuzi ya kufunga zipu ya suruali tu. Ona yanayokupata! Unafuatwa na mimba mpaka baa! Umelogwa wewe! Una hamu gani usizoweza kuzizuia?” “Mimi sio muhuni dada.”  Jax akajitetea. “Kama sio hukumu ya kumsaliti Lara baada ya kulala na Tula, na kushindwa kurudi kwake, ukajificha mpaka mwenzio Tino kukufuata na kukulazimisha ni lazima ukaonane na Lara uyamalize kiume, ni nini?” Kimya.

“Kama wewe mwanaume kweli, mbona ulishindwa kumfukuza Tula nyumbani kwako, ukasubiri mpaka aondoke ndio mtupie nguo nje? Kama kweli wewe mwanaume kweli, mbona amekushinda hapa kumtoa?” “Naomba unisikilize dada Nelly. Tula ni mzushi na muongo. Muulize Tino. Niliogopa nisije nikafanya chochote hapa, akanisingizia jambo kubwa na baya zaidi hata kufungwa jela.” Jax akajitetea.

“Nakuhakikishia dada yangu, simu ambayo ungeipata sasa hivi baada ya mimi kumtoa Tula hapa, ingekuwa unifuate jela, wala sio hapa. Tena akiwa amenisingizia jambo zito sana. Mimi namjua Tula kwa kuishi naye.” Jax akaendelea. “Nimeamua kuishi maisha ninayoyataka mimi bila yeye kunifanya mtumwa zaidi. Sikubali mitego yake tena. Ndio maana kwa amani kabisa, nataka kuachana naye. Mimi sio mjinga, ila nafanya ili kujinusuru mimi mwenyewe. Nisipokuwa mwangalifu, Tula anaweza akanifunga dada.” Nelly akamgeukia Tula.

“Gari ya Lara liko wapi?” Nelly akamuuliza. “Lara hakunipa gari mimi.” “Haaa!” Kila mtu akashangaa. “Mnashangaa nini? Lara anadanganya, hajanipa gari. Labda amehonga wanaume zake. Kama ningekuwa na gari yake si hata Jax angeiona!” “Tula!” Jax akashangaa sana mpaka Lara ndani ya gari akahisi hajamsikia vizuri.

“Subiri kwanza Jax.”  Nelly akataka atulie. Akamgeukia tena Tula. “Gari aliyokupa Jax iko wapi?” “Gari aliyonipa Jax?” Na yeye akamuuliza swali lile lile, Nelly akabaki akimwangalia. “Lipo.” Akajibu. “Lakini ni langu. Nina haki nalo maana niliishi na Jax kama mkewe. Na Jax ananipenda, anachohitaji ni kukumbushwa tu.” “Nakupa dakika tatu, mkumbushe.” Akaanza kubabaika.

“Sasa hivi hawezi akiwa kwenye hali hiyo. Na hasa Tino akiwepo.” Kila mtu akashangaa. “Subirini kwanza.” Nelly akawatuliza. “Tino yuko pale nyuma. Hajaongea chochote. Na hataongea chochote. Wewe ongea na Jax hapa. Na ninamaana yangu, maana leo nataka kuweka kikomo. Huu mchezo mnaotaka kumchezea Lara, nyinyi wawili, sitauruhusu.” “Kabisa dada Nelly.” Akaitikia Tino.

“Maana nyinyi wawili haya ni maisha yenu yatokea enzi na enzi. Mmeona havinogi tena, mnataka kuongeza mtu mwingine katikati yenu wa kumvuruga akili. Sasa leo nataka kuweka kikomo. Ni aidha mnaondoka nyinyi wenyewe wawili, mkaendelee kutoana roho, na mumuache Lara kabisa. Kwanza Lara mrembo sana, hata mimi naweza kumtafutia mwanaume anayejielewa akamuoa aachane na ujinga huu!”  Akamnyooshea kidole mdogo wake. “Lara ni wangu mimi. Na mimi nimeamua kutulia na Lara. Mimi nimeharibu, na nitatengeneza mimi mwenyewe. Na nimeapa. Iwe na Lara au mwanamke mwingine, mimi nitaanzisha familia, na wewe Tula hutakuwepo. Hakuna atakachozungumza sasa hivi, kikanibadilisha msimamo.” “Unauhakika?” “Ndio dada.” Akajibu kwa kujiamini.

“Hata itokee hapa ni chumbani na kitanda kipo pembeni yenu na yeye yupo uchi?” Mpaka Tino akacheka kwa sauti. “Mimi sio mdhaifu wa ngono.” Akajibu Jax akijitetea. “Nakuuliza Jax, usinichezee akili.” “Ndiyo dada. Hata kama tupo peke yetu, sehemu ya faragha, sitabadili mawazo. Nina uhakika na ninachokujibu dada yangu. Kwa sababu hata baada ya kumtoa polisi, nilihakikisha namtoa kwa chakula cha usiku. Mimi na yeye tu ili tupate muda mtulivu, peke yetu bila muingiliano. Nikazungumza naye Tula, kuhakikisha ananielewa na yeye anapata muda wa kuzungumza na mimi. Akaongea na kuuliza maswali yote ndipo nikaachana naye rasmi. Hana jipya atakalozungumza sasa hivi.” “Mtoto je?”  Akauliza Tula.

“Sasa ni hivi Tula. Nazungumza na wewe, na nikitoka hapa, mimi na Jax tunaenda polisi kuandikisha hili. Usimfuate Jax popote pale.” “Mtoto..” “Nimekuonya na sitarudia kukuonya Tula. Usiniingilie ninapozungumza.” Tula akanyamaza. “Dada, barua ya polisi ya kuonywa asinifuate ninayo na yeye nimempa nakala yake, anayo na hata polisi walimwambia. Wala hakuna haja yakurudi tena polisi labda sasa nikamshitaki tu.” “Sasa kama huwa akiongea Jax huwa humsikii unamona ni kama yupo tu uchi mbele yako, nisikilize mimi maana hutabahatika kupata kikao kingine kama hiki na mimi.” Tino akacheka tena kishabiki.

“Usimfuate tena Jax. Nakupa onyo Tula. Siku ingine kuiona sura yangu ukiwa umekiuka hiki ninachokwambia, nitakapokuwa nimekufuata kukuangalia itakuwa jela kuhakikisha hutoki huko.” Tula kimya. “Unanisikia?” Nelly akauliza kwa ukali. “Nimesikia lakini...” “Sina muda wa kukusikiliza Tula. Nitaishia kukuchapa makofi na kukupeleka polisi sasa hivi. Salama yako hapa, kwa kukiuka onyo la polisi kwa kukaa  mbali na Jax, ni kunyamaza na kunisikiliza. Unanielewa? Au unataka nikakueleweshe polisi baada ya kukucharaza hapahapa sasa hivi? Tena nitakuchapa kama mwizi, sina utani na wewe. Unajibu swali nitakalokuruhusu kujibu bila nyongeza. Umenielewa?” “Ndiyo.” Tula akapoa haswa na hofu.

“Sasa ni hivi, kesho kutwa. Siku ya jumatatu. Saa nne na nusu, tukutane hospitali ya Muhimbili. Tupime. Mimi nikiwepo sio Jax. Mimi na wewe. Ukikutwa ni mjamzito, tukajua ni mimba ya miezi mingapi. Bila maswali, nitalipia kliniki yako. Tena private. Mimi nitalipa mpaka siku ya kujifungua kwako.” Nelly akaendelea. “Nitakuja mimi, si Jax. Tutachukua DNA ya huyo mtoto sio sasa hivi akiwa tumboni, akiwa amezaliwa, atapimwa. Akiwa ni wa Jax, tutakwenda Ustawi wa jamii, watusaidie kwa haki kabisa, jinsi ya kumtunza mtoto wetu. Na jinsi Jax atakavyopata muda na mtoto wake. Sijui umenielewa?” Kimya.

“Narudia tena Tula. Kwa kuwa sitavumilia huu upuuzi. Jax ameshatamka hapa, hakutaki tena, anataka kuendelea na maisha yake. Na mimi sitakuruhusu uje uharibu maisha ya Jax kwa sababu zako mwenyewe. Sasa je, umenielewa?” “Sasa kwa nini Jax mwenyewe asilee mimba yake?” “Haa!” Tino akashangaa sana.

“Subiri kwanza Tino. Wewe Tula, ulitaka Jax aleeje hiyo mimba? Tuambie vile unavyotaka wewe.” “Kuna kuugua usiku. Nani ataniuguza?” Wakaanza kucheka ila si Lara wala Nelly. “Najua shida yako ni kutaka kurudi pale kwangu Tula. Nimekuhakikishia hutawahi kuja kurudi pale. Sahau. Nenda kanishitaki popote, usinibabaishe.” Jax akawa amekasirika. “Wewe hutaki majukumu Jax. Unakimbia majukumu. Ulikimbia mimba ya Lara, sasa hivi unakimbia yangu.” “Sema chochote unachotaka wewe kusema. Lakini hutarudi pale. Na kuhusu mimi na Lara, haikuhusu tena. Lara ni wangu, wewe tuache.” Akamgeukia dada yake.

“Mimi nashukuru kwa hilo. Na nina kuhakikishia dada yangu, sitatupa damu yangu. Kama mtoto ni wangu, mimi nitalea bila shida. Ila naomba nimuwahishe Lara hospitalini. Mimi Tula ninamjua. Hatutamaliza hapa. Nimemshauri kama hajaridhika, akashitaki Ustawi wa jamii. Basi. Na swala la kukaa mbali na mimi alishaambiwa polisi. Wala si geni na yeye. Na ameambiwa akirudia tena, nikamshitaki, ni kesi.” Kila mtu akamgeukia Tula.

“Naombeni niondoke jamani.” Jax akaweka msisitizo kwa dada yake. “Nataka kukusikia Tula. Unakubali tulichokushauri au unataka kwenda Ustawi wa jamii?” “Kama Jax hataki kulea mimba yake, ni heri nikatafute msaada mbele ya vyombo vya sheria.” “Sawa kabisa. Na mimi nakushukuru kwa kunipunguzia kazi. Ila nakupa onyo, kaa mbali na Jax. Kama amekwambia hakutaki na umepewa restrain order, nashauri kuwa makini kuifuata. Mimi sijui kucheza na wapumbavu. Nitakuweka ndani, ukazalie jela. Usinitanie.” Kimya.

Nelly akarudi kwenye gari yake, na Jax naye akarudi kwenye gari yake alipokuwa amekaa Lara. Akaondoka kabla ya dada yake, maana dada yake alibaki ametulia ndani ya gari yake kuhakikisha Jax na Lara wanaondoka bila Tula kufanya tena fujo yeyote tena. Lara akavuta pumzi kwa nguvu na kujirudisha nyuma na kunyamaza.


Jax & Lara Hospitalini.

Walifika hospitalini kila mtu kimya. Ilikuwa hospitali nzuri na yenye vifaa vya kisasa. “Unajua ni kwa nini nilichagua hapa?”  Akamuuliza Lara, Lara akamgeukia wakati wanaingia. “Wanavifaa ambavyo hata kama ulipata maambukizi jana, leo wataona.” Lara akamwangalia na kunyamaza. “Lakini nilishapima Lara. Nataka tu kurudia nikiwa na wewe.” Akarudia tena Jax. “Sawa.” Lara akajibu taratibu. Akafikiria kidogo. “Tula anaonekana anakupenda sana Jax. Nimemuangalia jinsi anavyokugombania! Hana hofu mbele ya yeyote kuonyesha wewe ni wake na anakuhitaji! Unawezaje kuachia upendo mkubwa kiasi hicho!? Tena kutoka kwa msichana mzuri vile!?” Lara akauliza taratibu tu akishangaa.

“Humjui Tula, Lara. Tula hanipendi. Ananihitaji kwenye maisha yake. Yaani mtu wa kumfanikishia mipango yake. Hujawahi kutuona maisha ninayoishi na Tula, Lara. Tino mwenyewe alikuwa ananiambia ni aibu kuwa na sisi wawili.” “Kwa nini sasa uliendelea kuwa naye!? Au kwa nini ulimrudia, Jax!?” Lara akauliza akiwa haelewi wala haamni. “Lara, naomba uniamini nipo hapa na wewe nikiwa najua ni kitu gani nafanya na kutaka. Nimegundua najipunja kwa kuwa nilishaishi na wewe na Tula pia. Nitatafuta furaha ya maisha kwa garama yeyote ile. Naomba tu Mungu uwe wewe.” Lara akamtizama akiwa kama bado hajaelewa.

Wakaingia kupimwa wote. Jax hakuwa na ugonjwa wowote, ila damu ya Lara ilikuwa bado ipo chini. Dokta akawaandikia dawa, wakaenda kuchukua upande wa dawa. Wakarudi kwenye gari.

“Twende tukanunue chakula twende tukale kwenye gari, sehemu iliyotulia.” Lara akakubali. Wakafanya hivyo, kisha wakaenda kuegesha gari maeneo ya Gymkhana. Wakabaki ndani ya gari wakawa wanakula. “Kesho nitasafiri kwa majuma mawili. Kama nilivyokwambia. Nakwenda Uswiz.” Lara akanyamaza. Jax akamwangalia. “Lara?”  “Abee!” Akaitika akiwa hata hamwangalii. “Ni safari ya kikazi na nafikiri itakusaidia kufikiria kama unanihitaji au la!” Lara akamwangalia na kunyamaza.

“Lara?” “Nakusikiliza unavyozungumza kirahisi Jax! Hivi unajua ulichonifanyia?” “Najua Lara, na ndio maana nimeomba nafasi ya kurekebisha mimi mwenyewe kwa kuwa najua ni wapi nimeharibu. Sina jinsi nyingine Lara, labda unishauri wewe.” Kimya. “Na hata ukinikataa pia sitakulaumu. Naelewa nimekuwa mtu ambaye sio wakuaminika. Hilo nalijua. Ila ninachojua, kama utakubali kusimama na mimi, nakuhakikishia utaona mabadiliko.” Lara akabaki kimya tu.

“Sihitaji ufanye chochote kile, ila niahidi hutabadilika. Namtaka Lara wangu yule yule.” Hata hapo Lara akakosa jibu. Akanyamaza na kuendelea kula. “Mimi ndio nitafanya kila kitu.” Lara akamwangalia tena. “Au umeshanipatia jibu langu? Niondoke nikiwa najijua kabisa. Kama nimekosa bara na pwani!” “Nani bara na nani ni pwani?” Lara akauliza, Jax akanyamaza. Wakaendelea kula.

“Nikuulize swali Lara?” “Langu hujanijibu.” “Kuwa nani bara na nani pwani?” Akauliza Jax. “Ndiyo.” “Ni mama na mtoto, Lara. Naomba mawazo yasiende mbali. Mimi nipo hapa na wewe. Na nimekusudia hivyo.” Lara akanyamaza. “Eti Lara? Unafikiri kwa jinsi nilivyokuumiza, utakuja kusamehe na tukarudi kuja kuwa pamoja, au yatakuwa yale maisha ya kukumbushana mpaka mwisho?” “Sijui Jax. Sikuwahi kuishi na wewe baadaye ila nina kumbukumbu ya jinsi tulivyoishi kabla ya yote haya.” Lara akafikiria kidogo na kumeza mate.

Sikumbuki kama tulikuwa na shida kati yetu. Hivyo ndivyo ninavyokumbuka. Hata nikikaa peke yangu nikitafuta wapi pengine nilikosea, sipati jibu! Wapi pengine nilitakiwa kurekebisha! Nini nilitakiwa kufanya tofauti! Pengine nakuwa mbinafsi, lakini sioni Jax!” “Kwa kuwa hakuna. Hakuna ulipokosea Lara. Nakutetea kabisa hakuna uliponisababisha nikafanya niliyoyafanya. Na ingekuwa ipo sababu uliyonitenda, kwa hakika nisingerudi kwako tena. Hii aibu yangu ningetafuta kuanza kwengine lakini si kurudi kwako nikijua si kwamba narudi tu kwako bali na kwa wengine wote wanaojua nilikosa vibaya sana. Ni kama kujidhalilisha zaidi! Lakini kwa vile ulivyo, maisha tuliyoishi zamani, ndio maana narudi nikijua kwako nitakuwa salama kama hakutakuwa na mabadiliko.” Jax akajieleza vizuri tu. Lara akanyamaza.

 “Kwa hiyo?” Jax akauliza. “Hata sijui Jax! Sina jibu sasa hivi, lakini ninachojua kwa hakika mimi sikuwa kama wewe. Yale maneno uliyonifuata na kuniambia juu ya upendo wako kwa Tula, mimi nisingeweza kukwambia Jax. Hata iweje. Kwa kuwa mwenzio nakupenda Jax. Nakwambia ukweli na Mungu wangu ni shahidi, nilipokuwa na wewe nilikuwa nimemaliza. Sikuwa hata nikiangalia nje wala sikuwa na nyuma pakuangalia. Mawazo yangu yalikuwa kwako tu.” Jax akavuta pumzi kwa nguvu.

“Narudia tena kukuomba msamaha Lara. Naomba nipe nafasi nyingine, naamini safari hii mambo yatakuwa mazuri zaidi kwa kuwa nimejifunza na nitakuwa nimetulia kama wewe. Nitajifunga kwako tu na sitayumbishwa tena. Na nikirudi naaamini tutapata muda mrefu mzuri wa pamoja. Nimejifunza Lara. Nakuahidi sitarudia kosa.” Lara na hapo akashindwa chakuongea. Jax akamuona amefikiria kidogo na kurudi kula. Akaona bado haamini au bado yupo na maumivu. Akaona amuache. Wakatulia mpaka wote wakamaliza kula.

“Utanisindikiza uwanja wa ndege kesho?” Lara akamwangalia kama kumkumbusha kitu, Jax akabaki akimwangalia akisubiria jibu. “Sina usafiri Jax.” “Nitakufuata na hili halafu twende mpaka uwanja wa ndege, kisha utarudi nalo na kuja kunichukua siku narudi.” “Na hii gari yako, Jax!?” “Oooh yeah. Kwani si gari au lina nini?” “Naona kubwa halafu la thamani sana!” “Sijaelewa!” “Pale uswahilini tunapoishi, litavuta wezi bure! Mimi sina ulinzi wa hivyo. Si unakumbuka ile gari ya mwanzoni nilikuwa nikiicha CCM?” “Sasa kwa nini na hii usiache CCM?” “Naogopa Jax. Naomba nikusindikize lakini si kwa hili gari.” Jax akafikiria.

“Basi unisindikize halafu ukaliache nyumbani.” “Nyumbani kwako!?” “Ndiyo.” Lara akashangaa kidogo. “Sipafahamu Jax!” “Unataka kupafahamu?” Lara akainama kama anayefikiria. “Tunaweza kwenda wote, ukapafahamu. Ili kesho usipate shida.” Lara akasita. “Hapapotezi. Pako wazi kabisa. Na ninaamini utapapenda. Twende.” “Sijui Jax. Naona kama sio sawa tena!” “Kwa nini?” “Nia yako ilikuwa sio kunipeleka hapo mpaka niwe mke wako.” “Ni lini unakuwa mke wangu?”  Akauliza Jax. “Sijui Jax!” “Hapana Lara. Sasa hivi wewe ndio una majibu ya haya mahusiano. Nimekwambia nakusubiri wewe. Ni lini, ni inategemea na wewe na utayari wako.” Lara akainama.

“Lara?” “Sitaki twende huko halafu...” Lara akasita kwa muda. “Lara, kuna tatizo gani?” “Bado hujaweka sawa mambo yako na Tula, Jax! Tusianze kitu ambacho hatuna uhakika na mwisho wake.” “Wewe ulikuwepo leo pale. Mpaka dada Nelly akaingilia. Kwa vile ulivyoona na kusikia, kutakuwa na mwisho wa Tula kwangu?” Lara akanyamaza.

“Nakuhakikishia Lara, kama unamsubiria Tula, hakuna matokeo mazuri yatakayotokea kati yetu kwenye kusubiri kwako. Mimi nipo na wewe. Naomba mawazo yako yawe kwangu mimi. Achana kabisa na Tula. Utajichelewesha sana. Sijui kama unanielewa?” Lara akamwangalia. “Naomba fanya kile moyo wako unajisikia na wala usijiwekee mipaka, ukijua mimi nipo na wewe. Unanisikia?” Sio kwamba Lara hakuwa akisikia, lakini tayari ameshachanganyikiwa.

Ni kweli hakuna mwisho wake Jax na Tula, zaidi kama kweli amebeba mtoto wake. Lara akashindwa kujua ndio itakuaje! Tula anayo nguvu kubwa sana kwa Jax. Aliweza kumbadilisha mawazo wakiwa wanakaribia harusi iliyokuwa imegarimu sana na Jax akijua pesa iliyokuwa imeshakusanywa hapo kwa ajili ya harusi yao! Pesa za nguo zao tu wao mpaka wasimamizi wa harusi! Ilikuwa mamilioni ya mapesa. Achilia mipango iliyokuwa imepangwa na watu na akili zao! Wenye nyadhifa kubwa mpaka Nelly dada yake! Tula alifanikiwa kumuingia vizuri Jax mpaka yote akayatupa mbali! Sasa aongezeke mtoto! Lara akaishiwa tumaini kabisa. Akavuta pumzi kwa nguvu na kujirudisha nyuma kwenye kiti akaegemea kitini na kuangalia nje.

“Naomba niangalie na kunisikiliza Lara. Najua na wewe Tula amefanikiwa kwako. Kwa sekunde chache tu ulizomruhusu kuingiza maneno yake kwako najua amekuchanganya vilivyo. Usimruhusu. Nakuhakikishia nimemalizana na Tula, nipo hapa na wewe. Na mimi nakuhitaji sana Lara. Nilikuwa na hamu na wewe kuanzia siku ya kwanza nahamia kwenye ile nyumba.”  Lara akawa bado haamini. “Kweli Jax!?” “Kwani huwa inachukua muda kugombana na Tula? Siku yenyewe tunahamia pale tuligombana, nikaishia kulala kwenye makochi.” Lara akamwangalia kama haelewi.

“Lakini anaonekana anakupenda sana!” “Ananihitaji sana. Naujua upendo sasa hivi sababu niliishi na wewe na nikaheshimiwa. Najua nilichokuwa nakikosa. Mimi najua, wewe unaweza usielewe. Naomba usinizirie ile nyumba.” Lara akatamani ingekuwa wakati ule sio sasa moyo ukiwa umekinahiwa vilivyo. Ni kweli angefurahia nyumba nzuri. Hakuzaliwa kwenye jumba kubwa au hata mazingira ya kifahari.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lara alizaliwa kwenye nyumba ndogo tu wakibanana ndugu wote na bado ndugu wa familia wakija kutembea mjini walifikia kwao. Wakaishi na huyo Jax sehemu ilikuwa ndogo tu. Joto la Sinza hata feni ikipepea ni joto tu. Nyumba zimebanana, hakuna nafasi. Anapoishi na rafiki zake ni uswahilini tu. Kelele nje ya dirisha la chumbani kwa Lara, zilikuwa zikipotea pale anapofanikiwa kulala. Hata Jax alijua moja ya kitu angemfurahisha Lara ni hiyo nyumba. Kuhamia sehemu yenye nafasi. Lakini hata yeye alimuona hata hamu imemuisha kabisa. Akapoa. Swala la nyumba ikawa sio kitu chakufurahia tena. Jax akaumia maana na hilo nalo amepoteza. Heshima ya kumpa Lara nyumba sio tena kitu anachohitaji tena Lara. Imeshakosa maana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lara akabaki kimya akiwaza kama anayejishauri. “Hiyo nyumba ipo sehemu nzuri sana. Niliinunua makusudi nikijua ni sehemu kwa mara ya kwanza kwenye maisha yetu tutapata utulivu. Hakuna kelele. Na ndani kuna ua kubwa tu sio vile tulivyokuwa tukizima redio yetu ili kusikiliza ya jirani!” Kidogo Lara akacheka. “Mwenzio najua mpaka tarabu zilizotoka juzi, kwa kusikiliza usiku kabla sijalala na asubuhi nikiamka, kutoka kwa jirani.” Wakacheka. Jax hakukosea. Hiyo nyumba ingekuwa pumziko kubwa kwa Lara.

“Twende tu ukapaone. Najua inaweza ikakosa maana, lakini twende tu angalau na wewe uone.” Lara akaona hilo si wazo baya. Wakaondoka. Njiani kimya. Mara kadhaa Jax alijaribu kumtizama Lara, akamuona amepotea kabisa pale ni kama ni sanamu tu amekaa nayo. Alikuwa amepandisha miguu hapo kwenye kiti cha gari na kuegemeza kichwa chake akiangalia nje tu. Mara kadhaa alimsikia akivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.

Walifika mpaka nyumbani kwa Jax. Getini akamsalimia mlinzi na kumtambulisha Lara. Kwamba atakuwa akiingia na kutoka na lile gari, wakimuona, wamfungulie. Mlinzi akaelewa, wakaenda kuegesha ndani, Lara akiwa kimya tu akisikiliza. Hata salamu hakutoa. Lara akapaangalia akiwa ndani ya gari na kushindwa kushuka kwa haraka. Nje ilionekana nyumba ndogo tu, na haikuwa ya ajabu sana. Ila ni kweli ilikuwa maeneo matulivu.

“Karibu Lara.” “Asante.” Lara akajua ndio anaambiwa ashuke garini. Taratibu akajifungua mkanda wa gari na kuvaa viatu vyake, akashuka. Akaangaza macho. “Pazuri!” “Nimefurahi kama umepapenda. Unataka kuzunguka nyuma ndio ukaangalie ndani?” Akatulia kidogo akiendelea kuangalia. Jax akamuona ni kama anajilazimisha tu, lakini sio kitu anachofurahia. “Twende tukaangalie na nyuma, upaone.” Jax akatangulia, Lara akamfuata. Akamzungusha nyuma ya ile nyumba. “Aliyekuwa akiishi hapa mwanzoni anaonekana alikuwa akipenda maua! Alikuwa na vyungu vizuri!” “Sina muda wa maua. Kwanza sina hata wazo la maua. Labda uje kuanza wewe.” Jax akamwangalia, lakini Lara hakujibu. Wakazunguka kidogo Lara akifuata nyuma nyuma.

“Twende ndani.” Jax akaongoza tena njia. Wakaingilia jikoni, mlango wa nyuma tu. “Kusafi!” “Yupo mtu anasafisha. Twende ukaone na kwengine.” Akamtembeza hapo ndani. Hapakuwa pakubwa sana ila panatoshea. “Nilipoambiwa tu panauzwa, na ofisini walikuwa wakitoa mikopo ya nyumba, nikapachangamkia. Pakuanzia hapa sio pabaya.” “Ni kweli. Huwezi kupalinganisha na pale tulipokuwa tukiishi Sinza. Hongera Jax.” “Asante. Unataka kupaona na chumbani.” Lara akacheka akionekana wazi anasita. “Nitapaona wakati mwingine. Acha nikusubirie hapa sebuleni.” Jax akamtizama kwa uchu, Lara akacheka na kurudi sebuleni. Jax akaingia ndani upande wa vyumba.

Baada ya muda akamfuata pale sebuleni bila shati ila nguo ya juu ya ndani. “Nikuulize swali?” “Jax kwa maswali!” “Ni latokea wakati ule ila hukujibu.” Lara akajaribu kufikiria. “Ni juu ya mtoto?” Jax akacheka. “Ulijuaje?” “Nakujua  Jax. Kila swali unataka liwe na majibu wakati nilikwambia kuna mambo mengine hayana majibu!” Akaenda kukaa pembeni yake.

“Mbona umekalia mikono? Baridi imekuzidia?” “Umewasha baridi kali sana.” Nyumba hiyo ilikuwa na A/C sio kama walivyokuwa wakipepewa na feni. “Njoo ni kukumbatie hapa.” Akamvuta bila kusubiri jibu. Lara akapandisha miguu kwenye kochi akajikunja vizuri mwilini kwa Jax. “Umekuwa katoto! Kazama kula.” Akambusu. “Nakula. Si umeona nilivyokula pale kwenye gari? Na ile ni mara ya pili.” Akampapasa juu ya mwili. Akambusu tena.

“Kwa nini hukuniambia kama ni mjamzito?” Lara akataka kukaa, Jax akamvuta karibu kama kumzuia kutoka pale mikononi mwake. Akacheka. “Nataka kukuelezea vizuri.” “Nakusikiliza. Wewe ongea tu hapahapa.” Lara akatulia kidogo kama anayefikiria. Mikono ya Jax ikaendelea kupita mwilini mwake, Lara akisikilizia asijue kama ni kitu anahitaji kwa wakati ule au ilishapitwa na wakati! Kwa hakika kila kitu kati yake na Jax ni kama kilipoteza maana. Lara akatulia kidogo, akashindwa.

“Naomba nikae tu hapa pembeni yako Jax. Acha, usinikumbatie.” Lara akajitoa kwa nguvu na kujiweka pembeni. Kabla Jax hajaongea kitu akiwa na mshangao usoni, Lara akaendelea. “Kujibu swali lako maana najua hutaacha kuuliza. Ni niliogopa.” Lara akaanza. Jax akakunja uso. “Kwa nini!?” “Unakumbuka siku ile tulipokuwa na Tino, akauliza tunampango wa kuwa na watoto wangapi na lini, ukajibu kwa haraka kuwa sio kwa wakati huu. Unakumbuka?” Jax akatulia kabisa. “Ulisema kwa wakati huu unataka kujijenga kwenye kazi yako kama Nelly dada yako alivyofanya. Ukasema huna haraka na watoto. Ndio nikaanza kujichunguza. Maana nilikuwa nimejisahau mambo ya kuhesabu siku za hatari. Ni kama mipango ya harusi ilipochanganya, nikajisahau kabisa kwenye swala la kuangalia mzunguko wangu wa mwezi ili kuzuia mimba. Sasa baada ya kusema vile ndipo nikawa kama umenistua. Kuja kuhesabu nikagundua ni miezi miwili ilishapita bila kuona siku zangu.” Lara akaendelea.

“Nikagundua ndio maana nilikuwa nikilala sana na harufu nyingi zilishaanza kunisumbua. Nikaogopa kukwambia ili usije badili mawazo ukaona nakuletea matatizo. Nikajiambia ninyamaze mpaka tukishaoana ndipo nikwambie. Ndio pressure nayo ikaanza kusumbua. Nikaenda kuzungumza na daktari wa kawaida tu, sio daktari wa mambo ya wakina mama. Akaniambia nipunguze shuguli, nipate muda mwingi wa kupumzika.” Lara akatulia.

“Nilikaa kama siku 13 nikiwa najisikia vizuri, na kweli nilikuwa nikijitahidi kupumzika ili kuhakikisha pressure inatulia. Kila nikipata nafasi, nilikuwa nalala. Ndio maana ulikuwa ukiniona nalala sana. Ili kufanya akili na mawazo vitulie kabisa. Siku nilipogundua umenidanganya hukuwa Kisarawe, niliingiwa na hofu sana. Kwa sababu ukweli Jax, ulikuwa ukinijali sana tokea zamani. Nikashangaa umeweza kutonipokea nikiwa natoka safari ambayo hatukuonana zaidi ya siku nne! Mbaya zaidi hatukuwa tumefanya mapenzi kwa zaidi ya kama siku 20! Nikajua kwa vile ulivyo wewe, kupenda kuwa na mimi ukinishika kama hivi, lakini ukamudu bila kulalamika! Nikajua kwa hakika utakuwa umeshapata mtu mwingine.” Lara akaendelea.

“Hofu ikaniingia. Nikajua utaniacha. Kumbe pressure nayo inazidi kupanda. Na kweli. Usiku niliomtuma Tino kwa dada Nelly, ilipanda nikashindwa hata kuendesha. Nikasimamisha gari njiani. Tino akaja kukaa na mimi. Akanifariji sana. Angalau nikaweza kuendesha mpaka pale nyumbani tunakoishi.” Lara akatulia kama anayetafuta jinsi ya kuendelea. Jax kimya akisikiliza.

 “Nilirudi pale tunapoishi na wenzangu nikajaribu kutulia, huku nikijiambia lazima nitulie ili mtoto asitoke. Lakini nilishindwa Jax. Nahisi labda Tino angeniambia pengine ningetulia hospitalini, nikaweza kutibiwa. Maana hata hospitalini nilishindwa kutulia.” Lara akaanza kutokwa na machozi.

Jax akashanga. “Kumbe ulikwenda mpaka hospitalini!?” “Nilikuwa na hali mbaya sana. Nilijawa na hofu Jax, siwezi kukwambia. Moyo ulikuwa ukienda mbio sijawahi pitia hiyo hali. Sasa kwa kuwa nilikusudia kuwa na huyo mtoto, nikasema nikimbilie hospitalini ili wanisaidie. Lakini haikusaidia. Nilikwenda tena peke yangu usiku, wenzangu wakiwa wamelala. Na kwenyewe nikashindwa kukaa nikarudi nyumbani eti kwa kugundua simu haikuwa na chaji, ilikuwa inazima. Nikahofia Tino atanikosa. Nikiwa nimeambiwa nilale pale kwa kuwa pressure ilikuwa juu sana, nikaondoka ili nikachaji simu, Tino asinikose.” Lara akajifuta machozi na kuendelea.

“Basi ndio mpaka asubuhi nikawa sijamsikia Tino wala wewe, ila Tula aliponifuata ofisini. Nilipatwa na mshituko ambao sikutegemea. Tula alionekana ananifahamu vizuri tu. Na hakuonyesha kama anaongopa. Halafu sio kwamba alikuwa akizungumza na mimi kwa jazba! Hapana. Taratibu tu, kwa kituo kama aliyekuwa amekusudia kunifikishia ujumbe wote aliopanga, mimi na watu wote waliokuwepo pale tusikie. Taratibu ila kwa sauti iliyoweza kusikika na wote pale mpaka wateja. Akanitajia na majina ya marafiki zenu wote. Hapo ndipo nilishituka sana maana ni kama alinithibitishia kila kitu. Na ninahisi ndipo pressure ililipolipuka zaidi.”

“Sesi alikuja kunitoa pale kwenye kiti, nilikuwa siwezi hata kujisogeza. Ile nimepanda tu kwenye gari akiwa ananirudisha nyumbani, nikasikia tumbo linakoroga, hap hapo damu zikaanza kumwagika kama bomba. Nikajua mtoto ameshatoka.” Lara akatulia kidogo.

“Ukaja sasa na wewe kunithibitishia aliyozungumza Tula, na kuniambia unampenda Tula. Umemchagua yeye.” “Sikusema hivyo.” Jax akajaribu kukanusha. “Sijui Jax, ila matendo yako yalizungumza hivyo na maneno ya namna hiyo.” Jax akanyamaza. “Pale ulipokuwa ukiniambia vile, muda ule, nilikuwa natamani nife palepale nipotee. Ni kama ulimwengu mzima ulikuwa umewekwa kichwani kwangu! Nilikuwa nimelemewa! Najiuliza maswali ambayo hayana majibu.” Lara akajifuta machozi yaliyokuwa yakiendelea kumtoka. Akajifuta na kutulia ili kuweza kuzungumza.

“Unajua swali kubwa lililonisumbua ni nini?” Lara akauliza baada ya kutulia. Jax kimya. “Jax?” “Wapi ulikosea?” “Hilo, lakini kubwa ni nini alichonacho Tula ambacho mimi Mungu alininyima! Siri yake kubwa ni nini kiasi cha kukufanya kuwa tayari kutupa kila kitu tulichokuwa nacho kwa miaka karibu miwili, na kumfuta yeye! Nilijiuliza na kupatwa na wivu wa ajabu. Ila nilimuheshimu sana. Nikajiambia ni wa thamani sana. Hata nilipokuwa nikizungumza naye, nilimuheshimu mno yule msichana. Kwangu hakuwa mshari. Jinsi alivyojibeba, unadhifu wake, uzuri, na ujasiri wake! Nikajiambia amebeba kitu cha thamani sana ndani yake kiasi cha wewe kuniacha, Jax!” Lara akaendelea taratibu kama anayejaribu kuvuta kumbukumbu.

“Unajua angalau kama tungekuwa ni watu wakugombana au hata kupishana! Lakini tulikuwa tukiishi kwa utulivu ambao hata sasa sijui ilikuwaje! Ulilokuwa ukiniambia au nililokuwa nikikwambia tukawa tunakubaliana kirahisi sana kama tuliokuwa tukisomana mawazo! Sijui kama unakumbuka mpaka wakati mwingine tulikuwa tukicheka jinsi tunavyowaza mawazo yanayofanana!” Jax alikuwa amebadilika sura, anashindwa hata kuongea. Lara akaendelea. “Halafu ile hali ya kunisifia kwa watu kuwa mimi ni mke wakuoa, gafla unaniambia umemchagua Tula, unaniacha! Nilivurugukiwa mno Jax.” Lara akafikiria tena kidogo.

“Naweza kusema nilishituka kuliko kuumia. Kwa sababu sikuwahi hata kukuhisi na mwanamke! Unajua kama ingekuwa ni tabia yako, ingekuwa rahisi. Sasa kutoka katika yale maisha tuliyokuwa nayo, mpaka kuja kuniacha gafla! Tena unanitamkia waziwazi ni kwa sababu ya mwanamke mwingine! Nilishituka sana. Anyways, nafikiri nimeongea mambo mengi lakini nafikiri utakuwa umepata jibu lako.” “Nimeelewa Lara. Na naomba nisamehe. Kwa hakika nilikukosea sana. Ila juu ya mtoto, ningefurahi kama ungeniambia. Nisingechukia na kuona kama ni tatizo. Kwanza mimi nilikuwa nikikuhofia wewe Lara. Hivyo ulivyo, halafu kuja kubeba mtoto! Nilikuona kama haupo tayari au sio jambo unalitaka kwa wakati ule. Kwa hiyo nilimjibu vile Tino kuhofia asije kukuogopesha ukaona unawajibika kuja kuanza kunibebea watoto ukaharibu kaumbile kako! Nikahofia usije ukadhani kama nina mpango wakuja kukuuzeesha bure!” Lara akacheka kidogo.

“Kweli! Hata hapa kukusikia katika yote yale na bado ulikuwa na mpango wa kumtunza huyo mtoto, siamini!” “Ukweli sikuwa nimepanga. Lakini sijui nilipatwa na nini! Japokuwa nilikuwa nikikuhofia wewe, lakini ni jambo nililolifurahia mno. Nikawa namfikiria yule mtoto jinsi atakavyokuwa au atakavyofanana na wewe au jinsi atakavyochanganya sura zetu! Nikafurahia sana. Nikajiambia ni kitu chakutunza tu kwa garama yeyote ile.” Wakanyamaza kila mtu akiwaza lake.

Baada ya muda akaona aage tu. “Acha mimi niende Jax. Nitakuja kukutembelea wakati mwingine.” “Kwa hiyo kesho utaweza kunipeleka uwanja wa ndege?” “Nitakupeleka. Ila nikipata usafiri kabla, naweza kuja kukufuata hapa. Ili usihangaike kuja mpaka kule!” “Basi tutawasiliana.” Lara akasimama. “Mbona unaharaka?” Lara akacheka na kuinama kama anayefikiria. “Hatutaonana kwa week mbili Lara!” “Nilijua utataka muda wa kujiandaa na safari, Jax.” “Hutaki kunisaidia?” Lara akacheka akionyesha kutokuwa radhi na hilo kabisa.

 “Nilikuomba usibadilike Lara. Ulikuwa ukinijali sana, kiasi nilikuwa nakumiss mno! Nilikuwa nikikaa hapa nafikiria kama ndio wewe ungekuwa ukiishi hapa na mimi, pasingekuwa na zile siku nilizokuwa nikilala na njaa au hasira, tena wakati mwingine hapahapa kwenye makochi wakati kitanda kizuri kipo ndani! Vyakula vizuri vinakuwepo hapahapa ndani na pesa zipo! Ni wewe ulikuwa ukikosekana Lara. Nimekiri nilikosa, naomba usibadilike na kunipuuza.” “Unajua siwezi kukupuuza Jax, ila naomba nipe muda tafadhali. Sipo kwenye hali nzuri hata kidogo. Natamani kama ningekuwa kama hivyo wewe ambavyo umeweza. Unafanya inaonekana rahisi sana, kama kuzima na kuwasha taa!” Lara akaongea taratibu huku akiwa amesimama.

“Sio rahisi Lara! Si rahisi hata kidogo, lakini nimeamua. Nimepoteza mengi mno mpaka heshima ambayo nilitarajia ningekuwa nayo sasa hivi sababu ya kazi nzuri niliyonayo. Lakini maamuzi yangu mabovu yananigarimu mno. Furaha ya mabadiliko yangu ya kiuchumi yalileta maana tu tulipokuwa wote.” “Nipe muda Jax. Tafadhali. Nahitaji muda. Pengine nikipona na kurudia hali yangu nitaweza kufikiria sawasawa. Lakini sasa hivi nina mengi yanayoendelea! Mengi mno.” “Ni nini?” Lara akafikiria kidogo.

“Kama ni pesa nitakusaidia Lara.” “Natamani kama ingekuwa ni pesa tu Jax!” “Sasa ni nini?” Lara akafikiria tena kidogo. “Nafikiri hata kuweza kulijibu hilo pia nahitaji muda. Nifikirie, ili niweze kujipanga tena kwa upya. Kwa sasa sina jibu hata kwangu mimi mwenyewe. Nasikia mvurugano, fujo na kelele tu kutoka ndani yangu mimi mwenyewe. Wakati mwingine natamani hata hizo kelele ziwe nazisikia kutoka nje, lakini zaidi zipo ndani yangu mwenyewe! Acha niweze kutulia kwanza. Nirudishe hali yangu ya zamani. Japo tu hata kujiamini tena. Sasa hivi najidharau mno! Nina majuto ambayo si kwa maneno hata kutoka kwako yatakayosaidia. Nafikiri ni mimi mwenyewe. Mbaya zaidi nimejawa hofu yakupita kiasi. Moyo, nafsi, akili na mwili wangu vyote vinakataa kurudi kwenye mahusiano. Sipo tayari kabisa.” Hapo Lara akafunga mjadala mzima.

Lakini Jax akajikaza na kuuliza. “Ni kwangu tu, au?” Jax akauliza. “Kwa yeyote yule sipo tayari Jax. Nimefilisika ndani yangu, sina kitu chakumpa yeyote yule. Nimechanganyikiwa kupita kiasi. Kila kitu kimepoteza maana hata sijui tena kupenda mtu kukoje! Kujali ndio inakuwa vipi! Mahusiano ndio kabisa! Hata sijui tena unapokuwa kwenye mahusiano ndio inakuaje, au inatakiwa iweje! Nahitaji muda. Mpaka lini, ndio wasiwasi wangu. Sijui. Nafikiri muda ndio utajibu.” Jax akaishiwa nguvu kabisa.

“Naomba mimi niondoke Jax. Nakuona upo na moyo wa kuendelea mbele ambao mimi huko sipo kabisa. Sitaki kukurudisha nyuma.” “Kwa hiyo unaniambia nini Lara?” Jax akauliza. “Kile unachokisikia nakuongea, nashauri kifanyie kazi. Hata mimi sijui Jax. Pengine baada ya leo na kesho kama alivyosema dada Nelly, labda. Mbali na wewe na Tula, nikapata nafasi yakutafakari kilichonitokea, tulipo na kitakachoendelea. Nikijua nikirudi kwako hutakuwa tu wewe Jax niliyedhani tupo wote ila yupo Tula, na ataongezeka mtoto wenu. Kwamba inabidi nifikirie kama nilidhania Tula anayo nguvu kwako, basi inaongezeka nguvu ya mtoto wenu pia. Sasa je, nipo tayari kuwa na mtoto wako uliyezaa na Tula, nikiwa nimepoteza wangu!” Jax akawa kama anafunguliwa mawazo na Lara. Akabaki anamsikiliza akionekana amefunguka zaidi.

“Kwa hiyo kabla sijajibu chochote kile, nafikiri nahitajika kufikiria. Inawezekana wewe ndio utahitajika kunipa nafasi mimi ili unisome kama nimebakia Lara unayemfahamu na ambaye unataka kumuoa au Lara uliyekuwa ukimfahamu alikufa na mtoto wake!” Jax akashituka moyoni. Lara akajifuta machozi. “Yote hayo ni yakuyafikiria Jax. Hata mimi sipo salama sana. Unaweza ukawa unamuacha mwanamke unayempenda na yeye anakupenda au kukuhitaji, ukarudi kwangu ukakuta mambo mengi sana yamekufa. Ukidhani hofu ya kukumbushwa yaliyotokea kati yetu ndio itakukabili kwangu, kumbe ukaja kukutana na Lara ambaye amejeruhiwa vibaya sana. Kila kitu kikakosa maana. Ikawa unakosa tena bara na pwani ya Tula. Tula na mtoto wenu.” Jax akawa kama amemwagiwa maji. Taratibu Lara alirudia maneno yake yeye mwenyewe. Jax akainama.

Lara akachukua pochi yake na kutaka kutoka. “Naomba nikusindikize Lara. Utapata shida ya usafiri.” “Nitashukuru.” Jax akaingia ndani kuvaa shati. Akatoka akiwa anajirekebisha. Wakatoka hapo ndani kimyakimya mpaka kwenye gari. Wakaondoka hapo. Njiani pia hapakuwa na mazungumzo tena. Lara aliongea moyo wake na kumuacha Jax na yeye akifikiria.

Walifika anakoishi Lara na wenzake, wakabakia ndani ya gari. “Naomba nisiingie Lara. Naona kila mtu hapo ndani hana hamu yakuiona sura yangu.” “Sawa. Usiku mwema.” Lara naye hata hakubembeleza tena, Jax akajua kweli amembadilikia. “Kama bado ungependa nikusindikize kesho, unijulishe tu.” Jax akabaki akimuangalia. Lara akainama kidogo.

“Unafikiri ukiamua kuja kuwa kwenye mahusiano tena, mimi nitafanikiwa hata kufikiriwa au ndio nisahau kabisa?” “Sijui Jax. Ila nashauri usinisubiri mimi. Kama ulivyosema, umekusudia kuendelea. Na unaonekana huna shida na utakayeendelea naye. Ulisema unaendelea tu, iwe na mimi au mwingine. Nashauri uendelee tu Jax. Mimi sijui nitakuwa tayari lini. Sitaki kukuchelewesha. Usiku mwema.” Lara akashuka na kuondoka bila kugeuka nyuma. Jax alibaki ameduaa akikumbuka maneno aliyozungumza alipokuwa na hasira za Tula, kwa Lara aliyejeruhiwa moyo.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usiku wakati analala, ujumbe ukaingia. ‘Inaweza ikakuchukua kipigo kama nilichopigwa mimi huko nje yetu ili kuja kugundua tulichokuwa nacho mimi na wewe hakipatikaniki kwa urahisi. Ni cha pekee mno Lara. Niamini nikikwambia hivyo na ndio maana nipo tayari kurudi na kurekebisha. Sitaki upitishwe nilikopitishwa mimi. Unaweza usifanikiwe kutoka salama. Tafadhali fikiria kwa upya. Naamini nikirudi kutoka safari tutapata muda zaidi. Ubaki salama.’ ‘Asante na wewe safari njema.’ Lara alijibu hivyo tu kirahisi na kuweka simu pembeni. Jax alipoona hayo majibu, hakuamini. Lara hakujali hata Jax anafikaje uwanja wa ndege! Jax akaanza kuhisi ameshampoteza Lara, lakini akajiambia pengine anahitaji tu muda. Atakuja kupona na kumpata Lara wake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kiburi cha kiume kikaanza kuisha. Mafanikio yake ni kama yakapoteza maana kabisa. Lara amekataa hata hilo gari ambalo Tula alikuwa akiliabudu! Alitaka kumuachia atumie mpaka atakaporudi, lakini Lara akakataa bila hata kuonyesha atapungukiwa na kitu. Amempeleka kwenye nyumba aliyodhani ingemuhadaa lakini Lara hakuonyesha hata kama kuna utofauti! Jax alilala na mawazo, lakini Lara akameza dawa zake za usingizi, akalala bila kujali zaidi.

Lara!

A

subuhi yake, Lara hata hakujisumbua kumtafuta tena Jax hata kujua kama aliondoka salama au la. Siku hiyo ikapita kimyakimya. Siku ya jumatatu akatoka mapema tu kuwahi kazini kabla hata ya foleni. Akawa wa kwanza kutoka hapo na kuacha wenzie. Alipofika tu ofisini bosi wao akamuita hata kabla ya kikao. Hata hivyo watu hawakuwa wamefika wengi. Lara akamsalimia. “Kuna jambo nimefikiria nikasema nikushirikishe pengine utapenda. Sijamwambia yeyote. Hili ni wazo langu moja kwa moja kwako.” Lara akajiweka sawa. “Kwa haya yaliyotokea hapa. Unafikiri kama ungepata sehemu nyingine yakuhama kikazi, kampuni nyingine ya simu, unafikiri ungependa?” “Sana. Angalau nikafiche huu uso kidogo.” Lara akakubali kwa haraka bila kufikiria.

“Sikwambii ukimbie!” “Wote tunajua sikimbii bosi wangu. Ni nimekimbiwa ndio nakwenda kupumzika. Na kabla sijajua ni wapi unafikiria kunihamishia, naomba nikushukuru kunisaidia. Sio kwa hili tu. Tokea mwanzo. Najua ningefukuzwa kazi kama si wewe. Nakushukuru.” “Karibu. Sasa kuna nafasi nimeiona imetokea Zanzibar. Nimesoma kwenye gazeti. Kampuni ingine lakini.” Akamtajia. “Sasa afisa mwajiri wao nafahamiana naye sana. Nilimpigia jumamosi, akasema ni kweli wanatafuta mtu, wapo kwenye usahili. Ni kama hiki unachokifanya hapa, lakini kwa kuwa unajuhudi na uzoefu, utakuwa ukiwasimamia wenzio. Naweza kukuandikia barua ya kukupendekeza, kisha tuone.” Lara hakuamini.

“Unaweza usiwaambie watu kama nitaondoka?” “Lara! Hutaki kuaga?” “Nina maana yangu. Nataka nikaanze upya bosi wangu. Hata kama nitakuja kukutana na wanao nifahamu, basi angalau niwe nimeshapona ndani. Wanao nizunguka wote wananikumbusha machungu yangu. Labda nikiwa mbali angalau itanisaidia.” “Wakikuulizia?” “Kwa kuwa nakujua huwezi kudanganya, naomba na mimi nikuapishe kuwa hutasema.” “Hapo sawa. Na mimi nitawaambia nilikuahidi sitasema, basi itabakia hivyo.” Bosi wao alikuwa mwenye maadili sana. Wakasaidiana na Lara kuandika barua ya maombi asubuhi hiyohiyo watu wakiwa hawajafika hapo. Lara akamtumia na CV yake, bosi wake akamtumia huyo rafiki yake afisa mwajiri wa hiyo kampuni. Lara akatoka wakati wanazungumza kwenye simu.

Mwanzo Mwingine.

Baada ya siku tatu Lara akaitwa kwenye usaili. Na mshahara pia aliotajiwa ulikuwa wa juu kidogo na ule. Aliambiwa atalipwa na pesa ya usafiri na marupurupu mengi tu. Na kwa kuwa walihitaji mtu kwa haraka, Lara akatakiwa baada ya siku tano awasili kazini. Hakufikiria mara mbili wala hakumwambia yeyote yule. Akaandika barua yakuacha kazi. Akamkabidhi bosi wake. Maandalizi ya kuacha jiji la Dar yakaanza kimyakimya bila hata kuwaambia kina Sesi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku ya ijumaa karibu wote pale walitoka kwenda kwenye starehe, lakini Lara hakutaka kuongozana nao. Walielewa tu bado yupo kwenye majonzi. Kumbe alibakia usiku kufungasha. Tino alitoka na Suzy akitaka muda naye, na wengine walitoka kivyao. Lara akabaki peke yake kwenye hiyo nyumba na kupata uhuru wote. Alikusanya kila kitu chake na kuwaachia ujumbe pale. Aliwashukuru sana kwa kusimama na yeye kipindi chote. Ushirikiano waliomuonyesha. Na kuwaambia amepata nafasi ya kwenda kuanza upya maisha sehemu nyingine. Akaahidi mambo yakikaa sawa, atawatafuta. Aliandika huo ujumbe kwenye kikaratasi wala si simu. Akafunga vizuri na kuweka juu ya kitanda chake. Akaita usafiri, akapandisha mizigo yake yote. Lara akaondoka hapo. Usiku huo akatafuta nyumba ya kulala wageni. Akalala hapo huku akijipanga na angalau kujawa furaha ya kuanza upya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ukweli Jax aliomba msamaha, lakini kila kitu kilishapoteza maana. Lara hakujua hata wakirudiana wanaanzia wapi. Nini atafanya na huyo Jax aliyemtamkia wazi hatamuoa, amemchagua Tula. Lara akajiangalia vile alivyo na kujifananisha na Tula, akajua hataweza hiyo vurugu kwenye maisha yake yote. Akajua kurudiana na Jax, ni kama kuanzisha mahusiano yenye hekaheka tupu! Zaidi akiumia kuona Tula yeye ndiye atafanikiwa kumzalia Jax mtoto, halafu wake amekufa! Lara akajiona hayupo tayari. Ana mengi yakufanya na kufikiria, kuliko hekaheka ya Jax na Tula. Mbaya zaidi, hakuona kama kutakuwa na mwisho.

Halafu akajiambia, inamaana kama Tula asingeharibu, Jax asingemrudia yeye. Hilo likazidi kumtesa sana Lara. Akajiambia inamaana Jax amemrudia kwa kuwa kule imeshindikana! Anataka kwenda kumtumia tu. Kwa kuwa amekosa heshima kwa Tula, basi anarudi kwake si mapenzi! Lara akahesabu yote hayo. Alijua ipo heshima kuolewa na mtu kama Jax. Mwenye pesa na muonekano ambao unapokelewa na jicho lolote lile, lakini akajiambia garama ni kubwa. “Nimeshalipa garama kwa kifo cha mtoto wangu. Mwishoe nitafuata mimi mwenyewe.” Lara akawaza na kuamua kujiweka pembeni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alifika Zanzibar na kukutana na wenyeji wazuri sana. Watu wazima ambao hawana mambo ya kitoto. Halafu akajikuta wapo wachache sana hapo ofisini. Kijana alikuwa mmoja tu na yeye alitokea bara, lakini Iringa. Hakuwa hata ameanzisha familia. Wengine wote walikuwa wenyeji wa hapohapo Zanzibar. Huyo kijana akamsaidia kumuonyesha mazingira. Akapata pakuishi, akatoka hotelini baada ya siku chache tu. Hakutumia pesa nyingi. Hakuna anayemfahamu, ikabidi kuanza kujichangamsha tu kwani kuanza kazi na huzuni, nikuibua maswali ambayo itabidi aeleze alichokikimbia Dar. Hata wazazi wake hakuwaambia kama alihamia Zanzibar. Ila aliwaambia alicha pale kazi.

Huku Nyuma jijini.

Huku nyuma alipokuwa ameondoka, wenzie walirudi kutoka kwenye starehe, wakijua Lara amelala ndani. Hawakutaka hata kumuamsha. Siku inayofuata ya jumamosi, wakashangaa hatoki chumbani, wakahisi siku hiyo na yenyewe aliwahi kazini kwani jumamosi hiyo ilikuwa zamu yao kwenda kazini. Na tokea ampe Tula gari, wote walirudi kupanda daladala. Ila Lara yeye alikuwa akitoka alfajiri zaidi kuepuka adha ya usafiri. Lakini walipofika kazini hakuwepo. Wasiwasi ukawaingia wakajilaumu kuondoka bila kumtizama chumbani kwake. Wote walijua Lara anapitia kipindi kigumu, wakahofia asijekuwa aliamua kujidhuru, lakini wakakumbuka Jax ni kama anajirudi. Wakajua amekusudia tu kulala.

Bila kujua kinachoendelea, wakamtetea kwa bosi wao kuwa Lara ni mngonjwa, wamemuacha amelala. Wakadanganya. Bosi wao hakusema kitu. Simu yake haikuwa ikipatikanika. Kwa kuwa ilikuwa ni nusu siku ya kazi, walipotoka tu moja kwa moja mpaka nyumbani kwao, chumbani kwa Lara. Ndipo wakakutana na huo ujumbe. Walitaka wasiamini, lakini wakagundua hakuacha chochote kilicho chake. Walihuzunika sana. Wakampigia simu Tino kutaka kujua kama yeye aliagwa na kama anajua wapi alipo Lara. Wakagundua hata Tino hajui, ndio na yeye wanampa habari za kusikitisha.

Kwa Jax.

K

idume huyo mwenye mafanikio ya kiuchumi, kazi nzuri na wanawake wazuri wawili akiwachanganya akili wasijue nani ndio zaidi maana kila mmoja alitesa na Jax kwa wakati wake ndipo kugonganisha sasa magari, wakidai wote walipewa mimba na huyohuyo Jax, alirudi nchini kutokea nchini Uswiz, baada ya siku 15 zakuondoka bila hata kusindikizwa na yeyote yule. Akachukua tu taksii hapo uwanja wa ndege na kurudi kwake.

Nyumba ikawa kubwa zaidi. Na pweke. Akajiambia siku 15 zitakuwa zimetosha kwa Lara kutulia kabisa na kutoa majibu ya kueleweka kwake. Jax akajipima ubora wake, akagundua amejaa kwenye mizani. Hakuna mwanamke angepata nafasi ya kuwa naye akaikataa. Akakumbuka Tula anavyomlilia mpaka baa mbele za watu! Nini chakumfanya Lara aliyemuhakikishia kutulia naye asimkubali tena! Mafanikio si ya ahadi. Jax amefanikiwa kiuchumi na anakokwenda ni bora zaidi kuliko hata hapo alipo. Hapo alipo tu alikuwa ametokea nje ya nchi, bado ananukia harufu ya Ulaya. Akajisifia kwa hili na lile, akajiaminisha kwa yote.

Akajaribu kumtumia ujumbe Lara kumtaarifu amerudi nchini. Haukuonyesha kama huo ujumbe umefika. Akakumbuka pia alipokuwa kule alijaribu kumpigia mara mbili hakumpata. Akafikiria, na kuamua kwenda kumuona. Ilikuwa siku ya jumapili. Akagonga akasikia akiambiwa subiri. Hakufurahia Suzy alipomfungulia. Alitamani angekuwa mtu mwingine sio yeye.

“Tukusaidie nini?” Akauliza Suzy kwa jeuri. “Hata salamu Suzy!?” “Salamu yangu itakusaidia nini wewe, matawi ya juu?” Suzy akaanza. “Unaongea na kulala na waliofika nchi za nje na wenye migongo mikubwa. Mimi nyuma sijajaliwa kama mwanamke wako. Sina...” “Suzy, nipo hapa kwa amani tu. Sitaki kukuudhi.” Jax akamtuliza. “Basi umechelewa, maana sitaki hata kuiona hiyo sura yako. Na huna sababu yakurudi tena hapa maana wote humu ndani hawataki kukuona.” “Naomba basi niitie Lara.” “Lara haishi hapa. Haya potea.” Suzy akataka kufunga mlango, Jax akauwahi.

“Nitakuitia mwizi Jax wewe! Jifanye wewe ndio mwanaume hapa mjini.” “Sitaki ugomvi Suzy, namuomba Lara.” “Unatatizo lakusikia? Nimekwambia Lara haishi hapa.” “Amehama?” Jax akauliza. “Kama hujui, inamaana hayakuhusu.” Suzy akafunga mlango kwa nguvu na kumuacha Jax hapohapo mlangoni. “Na nakupa dakika 5, upotee mlangoni kwetu, lasivyo nakuitia mwizi. Na siku nyingine ukirudi pia nakuitia mwizi. Hatutaki kuiona sura yako hapa.” Akamsikia Suzy akizungumza ndani. Jax akaondoka maana alimjua Suzy, huwa hajui kutania. 

Kwa Tino.

Akarudi kwenye gari na kujaribu tena simu ya Lara. Haikuwa hewani. Akampigia Tino. “Mzee wa benki ya dunia!”  Akaanza Tino. “Vipi Tino?” “Nipo kwa bi Mkubwa. Umesharudi mjini?” “Nipo mjini ndio nimerudi. Namtafuta Lara.” Kidogo Tino akashangaa. “Hata wewe hujui alipo!?” “Sijawasiliana naye tokea usiku mmoja sijaondoka. Kuanzia hapo akawa hapokei simu halafu baada ya siku kadhaa nikawa simpati kabisa. Nimemfuata hapa alipokuwa akiishi na kina Suzy, Suzy ameniambia haishi hapo tena. Unajua alipohamia?” Jax akauliza ila safari hii akisikika hali ya uwanaume imeanza kupungua.

“Daah! Basi naona ameamua kweli. Lara hajulikani alipo. Na kazi pia aliacha. Mimi nilikwenda kumchukua Suzy siku hiyo usiku, nikamuacha chumbani kwake hakuniambia chochote. Kesho yake wenzie ndipo wakagundua ameondoka na ameacha ujumbe kuwa ameamua kwenda kuanza upya, akiweka mambo sawa, atawatafuta.” Jax alihisi jasho jembemba likimtoka wakati gari ilikuwa ikitoa hewa safi iliyochunjwa.

“Amesema ni wapi amehamia?” “Nimekwambia hakuna anayejua Jax! Nilichosikia ameacha tu kazi na kuondoka.” Jax akawa ni kama haamini. “Lara hawezi kuacha tu kazi. Anahitaji sana ile kazi. Umejaribu kumuuliza bosi wake?” “Mimi nimeheshimu maamuzi yake. Binafsi nimeona anastahili kupata mapumziko mbali na sisi wote, zaidi wewe na Tula.” “Kwa nini una...” “Subiri kwanza Jax.” Tino akamkatisha.

“Nisikilize tu Jax. Najua wewe una akili nzuri tu. Ulifikiria kwa fujo yote ile siku ile pale baa. Kati yako na Tula, tena Tula akisema ana mimba yako, ulifikiri Lara angebaki?” Tino akamuuliza. Eti Jax!? Maana nilimwambia hata dada Nelly. Kwanza amefurahia sana kuondoka kwa Lara. Nakwambia hujawahi kumuona dada Nelly akiwa na furaha vile! Kafurahi mno. Na kwa taarifa yako tu, amesema sasa hivi hajali tena na wala nisimtafute hata nikikuona unafungwa jela na Tula. Amesema wazi siku ile alikuja pale sababu ya Lara tu. Kwa heshima ya wazazi wake. Lakini amesema sasa hivi hataki kusikia tena habari zako na Tula. Ameniambia nikwambie ukijisikia kwenda kwake iwe ni salamu tu. Hata ukifungwa jela na Tula, nisimwambie wala kumtafuta. Labda ukiwa umekufa ili akakuzike karibu na kaburi la baba yenu.” Jax akaumia sana.

“Sasa mimi nimefanya nini tena!?” “Samahani nilisahau. Amesema hataki kukusikia wewe, Tula na huyo mtoto wenu pia usiwahi kumpeleka nyumbani kwake. Amesema wewe endelea kuzaa tu na Tula mpaka mayai yakuishie. Lakini asione sura zenu nyumbani kwake.” “Kwani..” “Sijamaliza.” Tino mshabiki akaendelea kutoa ujumbe. “Amesema dada Nelly siku ukiwa naye, halafu ukataja jina la Tula, anakutoa meno ya mbele. Na ukijichanganya ukaenda wewe na Tula nyumbani kwake, anawakata miguu. Amesema nihakikishe unapata huu ujumbe kwa kuwa na yeye amemuwekea restrain oder Tula.” Kimya.

“Umesikia vizuri Jax?” “Nashukuru kwa ujumbe. Kwaheri.” “Sasa hakuna zawadi za ulaya hata kidogo!?” Tino alijua wazi Jax amekasirika ila kutaka kumkera tu. “Nilimletea Lara tu.” “Ulifikiri atasamehe kila kitu kwa zawadi za Ulaya?” Tino akauliza akicheka kwa kejeli. “Naomba nikuage Tino.” “Sawa kaka. Msamilie Tula wakuchorwa. Lakini mwenzangu utafia pazuri! Tula huwezi kumlinganisha na Lara hata kidogo! Tula yupo kama umemchonga mwenyewe!” “Unatafuta kuniudhi tu Tino!” “Mimi nakusifia kaka! Uchaguzi wako mzuri. Tula si mchezo. Huwezi kumlinganisha na Lara ambaye sasa hivi ni kimbaumbau. Halafu amewapisha na kuwapa uhuru wote. Mshindwe wenyewe, hakuna tena hukumu. Si kwa Lara au kwa dada Nelly. Wote wamewapa baraka zote. Sasa hivi nenda kamfaidi Tula wako tu, mlee watoto wenu.” Alipoona Jax ametulia, akaona amkere zaidi. “Kalee kaka. Nenda kalee watoto wa wanaume wenzako huku ukipoozwa na penzi. Na wewe unakuwa unagawiwa kidogo kama pongezi ya kulea watoto wa mabwana zake Tula. Unashika pembe, wenzio wanakamua tu.” “Tino!” Tino akacheka na kukata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment