Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Chozi Langu! - SEHEMU YA 9. - Naomi Simulizi

Chozi Langu! - SEHEMU YA 9.

Jijini Kubanana.

L

ara aliyerudi Dar, siye aliyeondoka. Alirudi akiwa amejawa tumaini la maisha, akiwa na Jerry anayejielewa. Moja ya biashara za Jerry ni kununua nyumba mbovu, anabomoa na kuzijenga kisasa, kisha anauza. Mpaka mahoteli. Alikuwa akimiliki kampuni ya ujenzi. Na kama haitoshi, pia alikuwa na kampuni ya ujenzi wa barabara. Akishinda tenda za ujenzi, anajenga. Walifikia hotelini tena. “Kwani unaishi wapi?” “Naishi kwingi! Kila mahali. Kama leo nipo hapa na wewe na sina mpango wakuondoka hapa. Nahisi nimenogewa.” Lara akampiga kidogo. Jerry akacheka. “Ila tuna nyumba Masaki. Huko ndiko walizaliwa hao watoto wetu. Hatupauzi ni kumbukumbu yao. Wakirudi nchini wanafikia hapo.” “Naomba kuwaona.” Jerry akamtizama kama anayesita.

Lara akamshangaa. “Hutaki niwaone wanao?!” Akamuona anatoa simu yake nyingine ambayo haitumii sana. Akafungua na kumuonyesha. Lara akashangaa. “Kwani...” “Subiri nikuonyeshe mama yao, ili ujibu hilo swali ulilotaka kuniuliza na kupunguza adha ya baadaye utakapo pata hamu yakumuona mke wangu.” Lara akacheka. “Unajuaje swali langu?” “Subiri umuone mama yao ndio uniambie kama sio jibu lake.” Akachukua simu, akafanya mambo mawili matatu akamuonyesha. Lara akabaki ameduaa. Hakujua aseme nini. “Kumbe wewe si mnafiki!” Akachukua simu yake. “Hapana sikujua kama mkeo ni mzungu!” Lara akajitetea. “Kwamba ni mzungu, mnene sana na mtumzima kuliko mimi?” “Sijasema hivyo Jerry!” “Uso wako umesema yote. Wala usijali, hata mimi najua.” Lara akaishiwa maneno akabaki na butwaa. Pakatulia kidogo, Jerry akiangalia simu yake.

“Ila umefanana sana na watoto wako!” Jerry akacheka na kumtizama. “Kasoro tu rangi! Sasa walivyo wazuri hivyo, hukupatwa hamu ya mtoto wa kike pengine....” “Angefanana na mama yake.” “Acha kumalizia sentensi zangu, unakosea. Mimi nilitaka kusema kama kaka zake. Maana umetoa vijana wazuri sana. Mimi ningepatwa tamaa na wakike.” “Linapofika swala la watoto huwa sina utani Lara. Sitaki kuwa na watoto wanao mangamanga mtaani wakati mimi nipo! Hilo halina nafasi ya mjadala.” “Nimekuelewa Jerry. Ila una watoto wazuri sana. Kwa kifupi unafamilia nzuri.” “Asante.” “Nikuulize swali?” Jerry akacheka kidogo.

“Unataka kujua nilimpata wapi mke wangu?” “Kwani wewe unasoma mawazo ya watu!?” Jerry akacheka. “Moja ya biashara yangu nyingine ni kuuza mageti ya kisasa, kufunga kamera za usalama kwenye nyumba au maofisi. Barbara, alikuwa akifanya kazi kama mkurugenzi au muwakilishi kwenye moja ya kampuni aliyokuwa amefungua raisi wa zamani wa Marekani hapa nchini. Raisi Clinton. Mimi nikapata tenda ya kufunga kamera hapo. Ilikuwa zamani sana na akashangaa kwa miaka hiyo hapa nchini nilipata wapi hilo wazo maana hapakuwa na watu wengi sana tunaofanya biashara hiyo kwa miaka hiyo. Akavutiwa, katika maongezi nikamtajia aina nyingine za biashara ninazofanya akazidi kuvutiwa nami. Na ndiyo, ni mkubwa kwangu, hata hao watoto tulipata kwa shida sana. Kwa uangalizi mkubwa tukifuata ushauri wa daktari mpaka akafanikiwa. Lakini ni mtu mzuri sana. Napenda moyo wake. Na asilimia 60 ya biashara nilizonazo sasa, amewekeza yeye kwa kuniamini tu. Kwamba alinipa pesa, ndio nikawa na uwezo mkubwa wakufanya.” “Kwa hiyo mnafanya naye biashara?” Lara akauliza.

“Sio zote. Ila za madini na cocoa ndio tunafanya naye. Nakusanya Cocoa hapa Africa, tunaingiza Marekani pamoja na madini zaidi ya Tanzanite. Napeleka huko.” Lara akajua ni kweli Jerry anayo pesa. “Mtu kama mimi, ungenishauri nifanye bishara gani?” “Unapenda biashara?” “Umenifanya nianze kufikiria kujiajiri.” “Ni kitu kizuri. Wewe unapenda nini? Ukijua unachokipenda au kitu unachokifikiria mara kwa mara, unaweza kukifanyia uchunguzi na kuanzisha biashara.” “Nikwambie kitu nilichofikiria Jerry?” “Niambie.” “Unishauri lakini.” Akatulia akimsikiliza.

“Nifungue sehemu ambayo nitakuwa nikiuza bando.” Jerry akabaki akimtizama. “Ndio hivyo.” “Wewe Lara!” “Ni mbaya?” “Naomba panua akili bwana. Sasa ndio utakuwa milionea lini!? Fikiria vitu vikubwa ambavyo hata wewe mwenyewe ukiviongea, unaogopa! Mimi mwenzio sikutokea kwenye familia kama zenu za mjini. Nilikuja mjini kutafuta pesa. Na kwa sababu ya umasikini, nilishindwa kuanzisha familia nilijiambia mpaka nifanikiwe. Kwa hiyo sikuwahi kufikiria kuuza bando. Biashara yakupata faida ndogo! Hapana. Ilinilazimu kufikiria makubwa, nipambane mpaka nitoke, ili nije kutulia hivi. Huna haraka, lakini fikiria kitu kikubwa zaidi. Au fikiria hata kufungua ofisi kama ile uliyokuwa ukifanya kazi. Lakini si kwa kampuni moja.” Lara akakaa sawa.

“Fungua ya kwako ukiwa umeingia ubia na makampuni yote ya simu hapa nchini. Uza simu, bando, kompyuta, games za watoto za kisasa. Kwamba mteja akiingia kwenye sehemu yako, anapewa huduma zote kwa mitandao yote hapa nchini. Kutuma na kupokea pesa hapa nchini na nje ya nchi. Na mambo kama hayo.” Lara akatoa macho. “Jerry wewe! Napata wapi hiyo pesa?!” “Kiasi gani?” Jerry akamuuliza. Lara akaanza kubabaika. Mwishoe akajibu. “Sijui.” “Sasa kama hujui ni kiasi gani, unajuaje kama huna?” Lara akapoa. “Hapo nakutengenezea akili ya biashara Lara. Mfanyabiashara hawazi mtaji. Anawaza aina ya biashara. Naweza nikakwambia mimi nina biashara ninazofanya mpaka sasa na hazijawahi kufa sababu ya kufikiria tu. Ukiniambia niliweza vipi kuanza kupeleka biashara Marekani, kwa upande nilipata wapi pesa, naweza nisiwe na jibu. Ila ilikuaje, hapo ndio ilikuwa changamoto. Sijui kama unanielewa?” Lara akajiweka sawa.

“Mtaji haikuwahi kuwa tatizo kwenye biashara yangu yeyote. Ila wazo la biashara na jinsi ya kuifanya ndio ilikuwa tatizo na ndio vitu vilivyokuwa vikiniweka macho. Mtaji ilikuwa baadaye. Ondoa hofu, waza. Fikiria. Jua ni nini unataka, halafu fanyia kazi hatua kwa hatua.” Lara akafurahia kuwa na Jerry mtu mzima. Akajua atamuongoza vizuri. “Asante Jerry.” Akambusu kwa muda. Jerry akajua amemgusa. Lara hakumalizia hapo akaendeleza. “Naona nitaongeza juhudi ya kutoa ushauri. Haya malipo sikuyategemea.” “Bwana nyamaza mimi nikushukuru.” Jerry alicheka sana. Lara akaendelea bila kujali vile anavyomcheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya siku kadhaa za mapenzi matulivu, Lara akiwa ametulia akitumikia ajira yake ya mapenzi tu, akimfurahisha Jerry vilivyo, akamtafutia sehemu ya kuishi. Akamfuata hotelini alipokuwa amemuacha. Alikuwa akitoka, anakwenda kwenye mizunguko na kurudi hapo hotelini. Usiku hakuwa akiondoka, wanalala naye. Na mchana sio kwamba alikuwa akiondoka siku nzima, kwa baadhi ya msaa, anarudi. “Uliacha maisha yako na vitu vyako ambavyo sijaviona kule Zanzibar, ili uambatane na mimi. Hilo nakushukuru.” Lara akacheka tu akimsikiliza. “Nimekupatia sehemu yako yakuishi.” Lara akatulia akimwangalia. “Lara?” “Sijaelewa. Kwamba sehemu natakiwa niwe nalipia au?” “Lara wewe muoga sana wa maisha bwana! Utaishije hapa duniani!?” Lara akacheka tu kwa wasiwasi.

“Ni sehemu itakayokuwa yako. Twende.” Lara akajitengeneza vizuri, akatoka. “Nipo tayari.” Jerry akambusu na kumshika mkono. “Na ujue sina shida kama ukitaka kutoka. Usijifungie ndani kwa hofu, ukinihofia mimi. Wewe kuwa mwaminifu na jipangie mambo yako. Chamsingi ni uwe na kiasi kwenye mambo yako.” Lara akamwangalia maana ni kweli alitamani kutoka kwenda saluni lakini alimuogopa asije kumuona mzurulaji.

Alimpeleka mpaka Kinondoni karibu sana na ubalozi wa Ufaransa hata unaweza kutembea. Sio mbali lakini ni nyumba ilikuwa katikati ya nyumba nyingine. Kumetulia sana. Ilikuwa na geti nzuri, na ndani ilikuwa ya kawaida tu. Pasafi kumepangiliwa. “Hapa ilikuwa ni nyumba ya serikali kama hizo tulizoona huko nje. Niliinunua, nikaivunja na kuijenga upya. Sio kubwa, lakini ina kila kitu ndani. Mpaka maji hutahangaika. Kuna kisima. Tutakuwa tukiishi hapa tukiwa hapa mjini.” Lara akamwangalia na kurudisha macho nje. Geti lilishamaliza kujifunga lenyewe bila hata mlinzi kuligusa. Akashuka na kwenda kumfungulia mlango kama kawaida yake. “Twende.” Akakumbuka na kwa Jax ilikuwa hivyohivyo akionyeshwa nyumba yake na kumuahidi itakuwa kwao japo alishaishi na Tula. Mawazo yakamrudisha Lara mbali na kupoa kidogo akijiuliza hayo ni maisha ya mpaka lini! Jerry hawezi kuwa mume wa baba watoto. “Haya ni maisha ya kuazima. Mpaka lini!” Akawaza Lara.

Akashuka, Jerry akafunga mlango na kumshika mkono. “Upo kimya sana Lara! Natamani kujua unachofikiria. Lakini pia sitaki lile jibu lako kuwa ni moja ya mambo ambayo hutaki kuzungumzia. Ni nini?” Lara hakujibu, ila akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Akamzungusha ndani, Lara akawa anashangaa. “Huu ni muundo wa wapi! Sijawahi ona!” Hilo ilibidi kuliongea. “Ndio aina zangu za nyumba ninazotengeneza. Nikikuuzia nyumba mimi, hata kama ni ndogo, hutalalamika hata nikikupa bei kubwa. Barbara amenifundisha au tulikuwa tukifanya naye hii biashara mpaka alipoondoka nikawa nimeelewa. Nikapata uelewa kinachotakiwa ni nini na nini cha muhimu ndani ya nyumba, chumba, jiko au choo.” “Pazuri sana. Nimependa.” Akamuona Jerry eti anapumua mpaka anajishika kifua.

“Acha utundu bwana!” “Ulinitisha je! Maana hukuongea chochote! Sasa sikujua kama umependa au la. Na hakuna kuanza. Ni tunaendelea. Binafsi nachukia kuanza kila siku. Hapa kuna kila kitu.” Lara akasimama na kufikiria. “Nikuulize swali?” Lara akauliza. “Kabla hata sijakukaribisha! Ushafanya mapenzi jikoni wewe?” Jerry akamuuliza, Lara alicheka sana na kujificha uso. Jerry hakumtania, akambeba na kumpeleka jikoni akamuweka juu ya kaunta ya jikoni. “Uchafu bwana Jerry!” “Acha hizo Lara. Hutaki kitu kipya na kigeni?” “Nataka.” “Sasa? Wewe fungua mawazo na akili ufurahie.” Hakuamini walipofanya mapenzi hapo jikoni juu ya kaunta za jikoni. Lara alicheka sana.

“Sasa cheko hilo ungepata wapi?” Lara akazidi kucheka. “Haya niulize swali.” “Inamaana utakuwa ukiishi hapa na mimi kila siku au kuna siku utakuwa ukienda huko nyumbani kwako, Masaki?” Jerry akakaa vizuri na kumsogeza na Lara. “Nakuona huna mtu mwingine ila mimi. Labda kama sijakusoma vizuri. Si ndivyo?” Lara akakubali. “Ungekuwa una mtu wako labda nisingefikiria hivi. Lakini nimekuona huna mtu ni mimi, ndio maana nikaona tuishi hapa. Lakini si kwa nia ya kutaka kukubana. Na sikulazimishi. Kama ukitaka ukaishi peke yako tuwe tunakutana  tu, sawa, lakini mimi sioni sababu.” “Na kule Masaki?” “Kwanza huwa sikai sana. Ni nyumba kubwa na ninakuwa peke yangu! Inanikera. Kwa wakati fulani nafurahia kuwa peke yangu, hakuna kelele au watu. Napata muda wakufikiria, lakini wakati mwingine napatwa upweke. Kwa hiyo basi, akija Barbara na watoto, nitakuwa nao kule. Lakini wakati mwingine, nikiwa Dar, nafikiri tuishi hapa. Unasemaje?” Akataka kumsikia Lara.

“Ndugu zako wako wapi?” Jerry akacheka sana. “Ushakutana na mawifi nini, wakakuchemsha mpaka ukakimbia?” Lara akacheka na kumkumbuka Nelly. Lakini Nelly hakuwa hata akifika kwao. Akanyamaza baada ya kukumbushwa Jax. Jerry akamuona ametulia hata hakumbuki swali. Akambusu begani, akacheka. “Lara kwa kusafiri! Sasa hapo ulikwenda wapi?” “Nipo Jerry.” “Lakini si unajua kutokuongelea jambo haisaidii kuliondoa ila kulifunika kwa muda na wakati wote utajikuta unarudi kulichungulia tu?” Lara akasimama na kuanza kuvaa. Jerry akasimama na kuanza kumsaidia.

“Baba alikuwa na ndoa ya wanawake wengi.” “Wangapi?” Lara akauliza. “Waliokuwa wakijifahamu na kuishi pamoja walikuwa wanne. Mama yangu alikuwa watatu. Alinizaa mimi na mdogo wangu wakiume. Nikiwa na miaka 15 akaanza kufariki mdogo wangu, baada ya mwaka mmoja baadaye akafariki mama. Tupo wengi kwa baba na baba siye ambaye alikuwa na jukumu lakutunza watoto. Ni mama mwenye watoto ndio anahangaika na watoto wake. Baba alikuwa mlevi sana. Sasa ile kuondokewa na mama, na nikawa nimebakia peke yangu tu kwa mama, ni kama nikakosa nguvu. Wakaanza kuhamishia kaka zangu pale kwenye nyumba niliyokuwa nimeachwa na mama yangu. Uonevu ukaendelea nikawa sina mtetezi. Baba hayupo kama mzazi, na mama ndio amefariki.” Jerry akaendelea.

“Gafla nikaanza kuonekana kama mimi ni tatizo pale. Sikukaa sana hata chumba nilichokuwa nikiishi wakanipokonya! Na ukumbuke hapo ni nyumba aliyokuwa amejenga mama yangu akisaidiwa na kina mjomba, lakini kwenye mji wa mzee. Kwa kifupi ilikuwa ni nyumba ya mama yangu ambayo aliniachia mimi, wakanipokonya.” “Jerry!” Lara akashangaa sana.

“Wanasemaje wakati ni kwenu?” “Kwangu, aliniachia mama yangu. Lakini wao wanasema ni kwao wakati hata mama zao wanajua kuwa ukiolewa pale ni wewe mwenyewe unajijengea nyumba kama wao walivyofanya. Lakini wakaacha watoto wao wanipokonye. Nilipoona uonevu unazidi, nikaenda upande wa kina mama. Kwa kina wajomba. Na wao wakawa wananiambia natakiwa kusimama kiume, nirudi nikachukue mji wa mama. Nilipoona na wenyewe wananilazimisha na kuniona kama nipo dhaifu kwa kuachia ile nyumba wakati kaka zangu walikuwa wakinipiga kabisa, kwa kunionea tu, nikaamua kuondoka kabisa pale kijijini. Kukatisha stori ndefu, nilikuja kurudi nikiwa nimeshafanikiwa. Nikaenda kujengea kaburi la mama yangu na mdogo wangu. Nikarudi tena wakati mwingine kupeleka wanangu na mke wangu kuona kaburi la mama na mdogo wangu, basi. Sikurudi tena mpaka leo.” “Baba yenu?” Lara akauliza.

“Alikuja kufariki baadaye. Kwa hiyo huna wifi wala shemeji atakayekusumbua kutoka kwangu. Hapa ni wewe na mimi tu. Wala Barbara hapajui hapa kusema atakuja kukusumbua siku moja. Hapana. Kwanza ni mtu mzima kama ulivyomuona. Akili zake zimejaa wale watoto na biashara tu. Hana muda wakufuatilia vitu vidogo vidogo kama hivi. Tumejijenga sana kule. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi.” Lara akaridhika. Baada ya kujisafi wakatoka hapo.

“Nikuombe kitu Lara?” “Nini?” Lara akauliza kwa utulivu tu wakiwa ndani ya gari wakirudi hotelini. “Biashara zinakuwa na mambo mengi. Ukianza biashara sasa hivi, zitakuhitaji akili na zitakuchukulia muda mwingi sana.” Lara akawa ameshajua nini anataka kumuomba. “Mke wangu yupo busy mno. Na mimi nipo busy. Na wewe utaanza kuwa busy. Wote tutakuwa tukitafuta pesa, hakuna mwenye muda na mwenzie. Naomba angalau wewe usianze sasa hivi.” “Nikae tu Jerry! Siwezi. Kwetu wananitegemea sana.” “Nakuahidi hutahitaji kitu na inaweza isiwe kwa muda mrefu. Ndio nimekupata tu Lara! Ukianza tu mambo ya biashara, ujue huu muda tulionao unaweza ukaisha kabisa. Najua ni kitu gani naongelea. Ni maisha tuliyoishi na Barbara, nikaja kuwa na Paulina. Yeye alikuwa ameajiriwa.” “Huyo mke wa mtu?” Lile swali likamfanya Jerry acheke sana.

“Bwana ulivyouliza vibaya! Na mimi mume wa mtu, Lara!” Lara akamwangalia kwa kumsuta. “Ninachotaka kusema, napo ikawa kama haieleweki. Kukutana kwa shida, havina uhuru kama hivi. Labda mpaka adanganye anasafiri kikazi, ndio angalau. Ikawa haieleweki, vurugu tupu! Amefungwa na majukumu ya kila namna. Nakutaka wewe Lara. Angalau na mimi nipumzike kidogo. Tafadhali. Na sikulazimishi. Unaweza kukataa na bado nitakuwa na wewe tu, lakini naomba ufikirie. Hii furaha yote itaisha. Hutaweza kuwa na mimi safarini. Utajifungia kwenye kitu kimoja, hiyo biashara. Ninachoomba tujipe muda wa pamoja. Mimi nitakutunza.” Lara akanyamaza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lara akaanza maisha mengine tena ya unyumba kama mke. Ila safari hii na Jerry mume wa mtu na baba wa vijana karibia umri wake, si Jax. Ila safari hii akijua yeye ni msaidizi wa Barbara, na Jerry hataki mtoto mtu wa kustarehe naye tu. Ukweli kulikuwa na mapenzi. Kujaliwa kwa hali ya juu. Lara akawa waviwango. Ukweli Jaerry alikuwa akimpa pesa nyingi hata nyumbani kwao maisha yalibadilika wakajua Lara anayo pesa. Na ndio watu pekee alikuwa akiwasiliana nao. Akisikia tu wanashida au wanalalamika, Lara alituma pesa na sio pesa kidogo. Pesa yakutosha.

Akawafungulia duka la jumla nyumbani kwao, angalau baba yake akapata ajira yakueleweka akisaidiwa na dada yao mkubwa Lily ambaye hakuwa na ajira ila kuwepo tu akisaidia nyumbani, pamoja na mama yao akiwa haendi kazini. Kwa muda wa miezi mitatu tu, Lara akawa amefanya makubwa sana nyumbani kwao. Kazi yake ni kumfurahisha Jerry, akisafiri naye kokote ndani ya nchi. Alipo Jerry basi ujue ndipo alipo na Lara. Vaa yake, kula yake ikabadilishwa. Ungemuona Lara, ungejua anatunza huo mwili wake. Safi, nadhifu, ajira ni mapenzi kwa Jerry. Maisha yakaendelea.

Kwa Jax.

H

uku kwa Jax yeye maisha yakawa nyumbani na kazini. Nelly akaelewa anataka kumuhakikishia ametulia, na amebadilika. Juhudi za kumjali zikaongezeka. Akili na mawazo ya Jax ikawa kwa dada yake akimuonyesha kumtambua kwa hali na mali. Zawadi na mambo mengine mengi ambayo Nelly alijua Jax hawezi kuwa akimfanyia mtu kwa vile alivyomuona na akili za kibinafsi kama baba yake. Na yeye Jax akakusudia kumuhakikishia yeye si baba yake.

          “Kazini nimeweza kutambulika kama mfanyakazi bora. Sipo peke yangu. Ila ijumaa jioni kuna tafrija ya kupewa tunzo.” “Naangalia taarifa ya habari, na unanipoteza.” Nelly akajibu na kurudisha macho kwenye luninga. “Naomba unisindikize.” “Wanawake zako wote wamekukimbia?” “Itaanza saa kumi na mbili jioni. Tafadhali naomba pendeza dada yangu. Na Gavana atakuwepo.” Akamsikia akicheka bila kugeuka. Akajua amekubali. Jax akaondoka kuelekea chumbani kwake. Akafikiria na kurudi. “Na kwakuwa mimi ndio nakutoa, naomba mwambie dereva wako mimi ndio nitakuendesha.” “Mbona masharti mengi!” “Na naomba nilipie nguo na saluni.” Jax akaongeza na kuondoka.

Ijumaa.

          Ilipofika mida ya kutoka, Jax akatoka chumbani kwake akabaki sebuleni akimsubiria dada yake. Ukweli Jax alipendeza. Alivaa suti nyeusi nzuri sana. Na vile alivyo nyooka mwili, suti ikaonekana nzuri zaidi mwilini mwake. Akatoka Nelly sasa. Jax akashangaa mpaka akasimama. “Sasa unashangaa nini? Si ulisema nipendeze?” “Si kujua kama ni kwa kiwango hicho!” “Sasa usinicheleweshe. Mimi huwa siingii sehemu kwa kuchelewa.” “Naomba basi nikufungulie mlango, Nelly dada yangu! Mbona hivyo?” “Nakuona unashangaa, shangaa tu!” Jax akacheka na kukimbilia mlangoni, akamfungulia mlango. “Umependeza dada yangu, mpaka nimefurahi!” “Kwa hiyo siku nyingine huwa natisha?” “Unapendeza sana tu, lakini sijawahi kukuona na nguo ya usiku ya namna hiyo! Imekukaa vizuri sana!” Akatoa gari hapo nyumbani kwa dada yake.

          Nelly akafungua pochi yake ndogo. “Zawadi yako hii.” Jax akashangaa sana. “Wewe leo vipi!? Mbona unashangaa shangaa!” Jax akacheka na kupokea kwa mkono mmoja akiwa anaendesha. “Ni nini?” “Utasababisha ajali wewe! Utafungua tukifika. Acha haraka.” Jax akacheka na kutulia. Kisha akacheka tena na kutingisha kichwa, Nelly akamuona. “Wewe sema.” “Hakika umependeza!” “Ujue uache mambo ya ajabu Jax, wewe!” “Natamani tukitoka hapo, nikupeleke tena sehemu ingine ya starehe.” “Sina muda huo. Kesho mimi naenda kazini.” Jax akacheka kwa sauti. Alimjua dada yake mgumu kupendwa.

          Walipofika kwenye hiyo hoteli ambayo wanafanyia hiyo tafrija, Jax akamuwahi kabla yakushuka. “Naomba nikushike mkono dada yangu. Upembendeza sana.” “Wewe leo unababaika!  Ni nini lakini Jax!?” “Ni utaratibu tu dada yangu. Na wewe uingie hapo ukumbini kwa heshima.” “Sasa sio uniangushe. Gauni lenyewe refu, na kiatu changu kama unavyokiona.” “Nitakutendea haki.” Akaenda kumfungulia mlango, akampa kiwiko, Nelly akapitisha mkono ndani ya kiwiko cha mdogo wake, na kushikilia pochi yake kwa mbele. Kweli yatima hao walipendeza sana. Ungewaona, ungedhani wanatokea kwenye familia ya matajiri fulani hivi.

          Wakati wanaingia mlangoni, Jax akakutana na kiongozi wake wa kitengo akiwa pamoja na viongozi wake wakubwa sana. Nelly akamuona mdogo wake amebabaika. Kama kawaida yake Nelly akaweka sura yake ya kisomi. Nelly na yeye kichwa kina shule ya kueleweka, na yeye anao wadhifa kazini kwake. Ashazoea kukutana na watu wenye nyadhifa kama yeye. Akaongeza ujasiri na kuweka mabega sawa akitembea. Jax akataka kusalimia na kupita lakini mmoja wao akawataka salamu ndefu, ikabidi Jax atulie.

“Sikujua kama ulikuja kuoa tena, Jackson!” “Oooh noo!” Jax akahamaki kwa sauti. “Huyu ni dada yangu, kama mama kwangu.” Hilo likamfurahisha Nelly, ila ikabidi wamgeukie vizuri Nelly. Nelly ni dada mkubwa ila tumbo halikuwahi kubeba mtoto hata mmoja na analinda huo mwili ubaki kama msichana. Hapo kiuno kilikuwa kimeingia ndani, tumbo kama mgongo. Umbile sio mwembamba wala mnene, ila nguo aliyokuwa amevaa, ilimtengeneza umbile vizuri sana. Na jinsi alivyokuwa amefunga hizo nywele, usingeweza amini Jax akisema ni mama. Wakamtizama wote kwa makini.

 “Hawa ni viongozi wangu.” Jax akaendelea na utambulisho. Lugha iliyokuwa ikizungumzwa hapo ni kingereza tupu, kama upo London. “Huyu ni country director wa Tanzania, Malawi, Zambia and Zimbabwe. Anaitwa Ms Wick.” Nelly akampa mkono kisomi na kumsalimia. Alikuwa mwanadada wa kizungu kutokea Australia. “Na huyu ni Director of strategy upande wa mashariki na kusini mwa Africa. Anaitwa Billson.” Nelly akampa mkono. Alikuwa mweusi. “Umependeza sana.” Akaongea kwa lugha ya kiswahili, ila akamjua si mtanzania kwa lafudhi yake. Wakacheka kwa pamoja ila Jax akamwangalia dada yake vizuri na kwa kujivunia.

Ms Wick akataka kujua Billson ameongea nini, ikabidi bosi wa Jax, ampe tafasiri. Na yeye akakubaliana naye. Bosi wa Jax na Nelly walikuwa wakifahamiana, kwani walishaonana kabla ya hapo kwa hiyo kwao ikawa ni kusalimiana tu.

Baada ya hiyo salamu iliyochukua muda kidogo hapo mlangoni Nelly na Jax wakaaga na kuondoka hapo kuelekea ukumbini, kabla hawajaingia ukumbini wakashangaa Billson amewakimbilia tena. Nelly akakunja uso wakati wanageuka. Maana aliita jina la Jackson, ambaye alikuwa amemshika dada yake mkono vizuri tu wakitembea. “Naweza kumshika mkono dada yako na kumsindikiza kwenye kiti?” Akamuuliza Jax kiungwana, lakini Nelly akawahi. “Hapana.” Wote wakashangaa mpaka Jax akamgeukia dada yake kwa hofu.

“Kwa nini!?” Jax akamuuliza dada yake kwa sauti ya chini kidogo kama Billson, kiongozi wake asisikie. “Sitaki!  Heee! Kwani lazima?” Akamjibu Jax akimshangaa na swali juu. “Nelly please!” “Acha kunipotezea mudi na wewe! Twende.” Jax alitamani aridhi ipasuke aingie ndani na huyo dada yake. Ni kiongozi wake mkubwa sana. Nelly akamvuta mkono kwa nguvu ili waendelee kwenda. Akageka kwa Billson akamkuta akitabasamu tu. “Samahani sana.” Akanong’ona Jax kwa wasiwasi, dada yake akimvutia ndani.

“Nelly!!” “Nini?” “Tafadhali dada yangu!” “Kama ungeniambia unakuja kuniuza huku kwa mabosi zako ili upandishwe cheo, mimi nisingekuja. Unanisikia Jax?” Hapohapo akambadilikia mdogo wake. “Sijaja hapa kwa ajili ya mtu mwingine yeyote ila wewe tu. Kama nia yako ni...” “Basi twende dada yangu. Umependeza sana, naomba usianze kugomba sasa hivi. Twende. Ila naomba weka lugha laini kidogo. Hawa watu ni wastaarabu sana.” “Nipo nao hao kila siku. Najua tabia zao. Usinifundishe kuishi na wanaume malaya hapa mjini.” “Basi dada yangu. Twende.” Wakaingia ndani.

Ukweli kulipangiliwa vizuri na kiutalamu. Kila mfanyakazi na jina la mgeni wake vilikuwa vimewekwa juu ya meza. Unakaa kwenye kiti ambacho meza ina jina lako. Jax akatafuta meza yao, mpaka jina la dada yake lilikuwepo juu ya meza pembeni ya jina la Jax. Akamuonyeshea ishara, akamfuata, akamvutia kiti kiustarabu, akakaa ndipo Jax naye akakaa pembeni yake. Wakatulia Jax akifikiria kilichotokea kati ya dada yake na kiongozi wao.

Tafrija ikaanza. Wakanywa na kula ndipo muda wa kutangazwa wafanyakazi bora ukaanza. Ilipofika wakati wa Jax, akaenda kupokea tuzo na katika kutoa neno fupi, Jackson akamtambua dada yake. Akamshukuru sana pale kwenye umati mpaka Nelly akashangaa. Akatambua mchango wake mpaka pale alipofikia. Akamtambua yeye kama mzazi wa pekee aliyekuwa akihangaika naye tokea wazazi wao wanawaacha, ambapo pia alikiri hakuwa akiwakumbuka vizuri ila Nelly aliyekuwa akihangaika naye katika uzima na maradhi mpaka hapo alipo.

Nelly alikuwa ameinama tu akisikiliza. Hakujua kama mdogo wake anamtambua kwa kiasi hicho. Mara kadhaa Jax alijifuta machozi akieleza hakuna mafanikio yeyote kwenye  maisha yake bila Nelly. Kwamba kuna mengi ilimbidi Nelly kusamehe, au yasubiri maishani ili kumfikisha yeye vile alivyo. Mpaka Jax anamaliza, ukumbi mzima ulisimama kwa heshima kumpigia Nelly makofi. Nelly alicheka tu na yeye akasimama na kumpa mkono mdogo wake aliporudi pale mezani. Tafrija ziliendelea baada ya wenzie Jax pia kupokea tuzo zao na kupata nafasi ya kutoa shukurani kama Jax.

Kikafika kipindi cha mwisho wa tafrija, ikawa ni kucheza. Jax akamuomba dada yake akacheze naye, wakaenda. Nelly alipenda sana kucheza na alijua. Linapofika swala la kucheza huwa hajipunji. Wakati wanacheza, Billson akasogea tena. Safari hii akamtizama Jax. “Naomba kucheza na dada yako.” “Hivi wewe shida yako nini!?” Nelly akamuuliza Billson. “Wewe unachoogopa ni nini?” “Mimi siogopi. Ila sitaki.” “Wote tunajua hiyo si sababu. Unachoogopa ni nini?” Billson akamuuliza tena akisikika ametulia tu, Jax akitamani kama ageuke upepo. Wawili hao walikuwa wakibishana katikati ya ukumbi, wengine wakicheza na kucheka. Nelly na Billson wakibishana, Jax ameduaa katikati yao.

“Unaogopa nini Nelly?” “Sitaki kucheza na wewe. Naomba utupishe tuendelee kucheza na Jax.” “Nelly! Haina shida!” Jax akamsihi dada yake. “Najua haina shida na ndio maana sitaki. Unanilazimisha nini na wewe?” Kwa mdogo wake walizungumza kiswahili ila kwa Billson kwa lugha ya kingereza. Billson akacheka. Nelly akaondoka pale na kuwaacha Jax na Billson wamesimama. “Samahani sana.” Jax akaomba tena msamaha kwa Billson na kumkimbilia dada yake.

Alipofika tu mezani hakukaa, akachukua pochi yake na kutoka. Jax akamkimbilia. “Nimechoka, nirudishe nyumbani.” Nelly akaongea akimsikia mdogo wake akitembea kwa haraka nyuma yake. Jax hakujibu. Wakaongozana mpaka karibu ya gari. Nelly mbele na kiatu chake cha juu akitembea kama amevaa kandambili. Kwa mwendo wa haraka ila kwa madaha haswa akipiga hatua kwa kupishanisha miguu kwa mahesabu asianguke “Unanifungulia mlango au?” “Nakuja dada yangu.” Jax akakimbilia mlango, akamfungulia na kupanda. Wakaondoka hapo.

Jax kwa dada yake.

“Nashukuru kwa kuja.” “Karibu.” Nelly akajibu kwa kifupi, macho nje ya gari. Wakanyamaza mpaka walipokaribia na nyumbani kwake Nelly. “Umenikuza nikiamini siwezi kuja kupendwa, au wanadamu ni watu hatari sana.” Jax akaanza. “Hiyo imani nilijaribu kuikwepa kwa kutotamka kama wewe. Kumbe imani hiyo ya kumuogopa mwanadamu na kutoamini kama naweza pendwa mimi kama Jax, ilishaniathiri kiasi ya kwamba nikawa nikiishi hivyo kwa kujihami bila kujua mpaka imenigarimu Lara na mtoto wangu.” Nelly akamwangalia.

“Sio wanadamu wote ni wabaya dada! Na sio watu wote wanafiki. Huko duniani wapo watu wenye upendo wa dhati kwa watu wengine. Sema sisi hatukubahatika wakati ule. Tukazungukwa na watu  wakatili watupu, tukaishia kuwa watu tusiojua kupokea upendo wa kweli.” “Wewe umeharibu mwenyewe, acha kunijumuisha.” Nelly akajibu kwa jeuri kidogo.

Jax akamtizama na kuendelea. “Ninachotaka kusema ni kuwa, sio wanaume wote wako kama baba. Na sio binadamu wote wapo kama ndugu zetu, Nelly. Nimejifunza kwa machozi na kwa kumwaga damu ya mwanangu. Wewe umenisaidia kujitizama na nikakusudia kufanya kwa makusudi kuwa mtu mwema hata kama si tabia niliyoumbiwa. Na mimi nakushauri fungua moyo wako.” “Sina muda wa kipuuzi mimi.” Jax akanyamaza ila akajua amemsikia.

Jumatatu.

N

elly akiwa ofisini kwake katikati ya siku, mchana kabisa, hata sekretari zake wawili walitoka kwa chakula cha mchana, yeye akabaki ofisini akifanya kazi kama kawaida yake. Mlevi wa kazi. Mlango ukagongwa mara moja, Nelly akainua macho kumtizama mgongaji, kabla hajamkaribisha, Billson akaingia. Nelly hakuamini. “Hivi wewe shida yako nini na kwa nini unakuja bila miahadi?” Nelly akawa mkali. “Mkurugenzi wako ameniambia nitakukuta hapa, kwa kuwa huwa ni mara chache sana unaenda kula.” “Mimi ni mkurugenzi hapa.” “Basi mkurugenzi mwenzio.” Billson akajibu akijikaribisha na kwenda kukaa mbele yake.

“Kwa hiyo kumbe ni kweli?” Nelly akabaki akimwangalia. Billson akacheka akimtizama. “Kweli nini?” Ikabidi amuulize. “Kwamba wewe ni mlevi wa kazi?” “Unanipotezea muda. Huwa sioni watu bila kuangalia muda wangu.” “Na hilo nimeambiwa.” “Kama unalijua hilo, ni kwa nini upo hapa!?” “Wewe unaogopa nini?” “Nani amekwambia mimi naogopa!? Nina mambo mengi, sina muda wakuchezea.” “Wote tunajua kazi imekuwa kimbilio tu na kigezo cha kujificha, lakini sio kweli. Nini unaogopa Nelly?! Niambie na ninakuahidi sitakusumbua tena.” “Kwa hiyo kumbe unajua kama unanisumbua?” “Jibu kwanza swali langu kabla sijajibu lako?” “Huna swali la msingi, ila unadhania tu.” Nelly akarudisha macho kwenye kompyuta yake, Billson akabaki akimwangalia.

Billson mwenyewe alikuwa amevaa kiofisi. Msafi haswa. Kwa haraharaka tu ukiangalia suti aliyokuwa amevaa, utajua anajielewa. Akakunja na nne kabisa kisha akaegemeza kicha kwenye mkono alioweka mezani kwa Nelly, akabaki akimwangalia kama anayemwambia ndio amefika.

Nelly akamgeukia. “Shida yako ni nini wewe!? Naomba utoke kabla sijakuitia askari akutoe.” “Cha kwanza ambacho nataka uelewe Nelly, mimi sikuogopi hata kidogo. Najua umeweka ukali iwe kama kinga yako inayokusaidia kukwepa watu, na umefanikiwa kwa asilimia 100. Lakini mimi sikuogopi au huniogopeshi.” Mpaka Nelly akanywea. Akabaki akimtizama. Billson akaendelea. “Hilo moja. Pili, mimi si mtu utakayefanikiwa kunikwepa kwa haraka. Ni afadhali unipe muda wako, usinipuuze, halafu mimi ndio nikuage. Lakini si kwa wewe kunifukuza.” “Sasa unataka nini?! Mimi nina majukumu mengi Billy! Sina watu wakunifanyia kazi kama wewe unavyoagiza tu.” “Na hilo nalo nimeambia. Kuwa kazi zako zote unafanya mwenyewe, huamini watu, na ndio maana huna muda na wewe mwenyewe.” Nelly akashangaa sana.

“Nani anakupa habari zangu za uongo!?” “Una sekretari wawili, lakini mara nyingi unaishia kuchapisha barua zako mwenyewe. Huo ni uongo?” “Sasa kama wanakosea na sitaki waniharibie!” Billson akamtizama kwa kumsuta. “Ni hilo tu umepatia. Mengine ni uongo. Naomba uondoke unanipotezea muda.” “Nakufahamu kwa asilimia 70, Nelly.” “Hongera. Naomba ondoka.” “Weekend nzima nilikuwa na kazi ya kukufahamu wewe tu. Kwa hiyo nimeishia na swali moja ambalo nilazima unijibu ndipo utaweza kumalizana na mimi vizuri.” Nelly akabaki akimtizama kwa mshangao mpaka usoni akaonyesha.

“Unaogopa nini Nelly?” “Mbona nimeshakujibu zaidi ya mara nyingi! Unataka kusikia nini?” “Ukweli.” “Halafu ili iweje!?” “Nitakwambia baaada ya hapo.” “Billson, nina kikao baada ya lisaa limoja kuanzia sasa. Tafadhali naomba usiendelee kunipotezea muda wangu.” “Naheshimu hilo.” Billson akasimama.

“Ili nisikufuate ofisini, kwa sababu ujue nilazima nipate jibu langu. Naomba tukutane nje ya ofisi.” “Sitaki.” Billson akarudi kukaa. “Ni kwa nini unafanya mambo ya kitoto na wewe ni mtumzima na majukumu mazito, Billy!?” “Nipe weekend 4 tu, nakuhakikishia sitakusumbua tena.” Nelly akashangaa sana. “Weekend nne za nini?!” “Tukutane nje ya ofisi. Kwa chakula. Sio lazima unijibu siku ya kwanza tunapotoka. Ila ndani ya hizo mara nne, ni lazima niwe nimepata jibu.” “Hata unipeleke wapi, jibu langu litakuwa hilohilo.” “Sawa. Kwa hiyo tunaanza weekend hii?” “Sitaki.” “Unaogopa nini wewe?” Nelly akafunga macho.

Nelly ni mkorofi, lakini hakuwahi kukutana na mtu kama Billson. Kwanza anajua huwa watu wanamuogopa sana. Hakuwahi kupata mtu akamkaidi kama hivyo Billson. “Kama ulichoniambia ni kweli juu ya kikao chako, umebakisha muda mfupi sana.” “Sasa ni kwa nini huondoki?!” “Nasubiria muda na wapi nakuja kukuchukua.” “Kwa nini unalazimishia mambo, Billson?” “Nisingefika hapa na kuwa hivi nilivyo bila kulazimishia mambo. Okoa muda wako. Muda na wapi?” Billson akaonekana hana haraka kabisa.

“Nani amekwambia sina usafiri?” “Najua unao, na una dereva ambaye huwa unamtumia unapotaka kufanya shuguli zako garini. Kama ukiwa na simu za alfajiri ukiwa barabarani ndipo huwa unamtumia. Na ninajua pia kuwa wakati mwingine huwa dereva wako anakufuata nyumbani, lakini unakataa kupanda gari ya ofisi, unajiendesha mwenyewe.” Nelly akachoka kabisa. Billson akamuona na kumcheka.

“Umeamini sasa kuwa nakufahamu kwa asilimia 70?” Nelly akabaki kimya. “Safari ni yangu. Mimi ndiye niliyekualika, na mimi ndio nitahusika na usafiri wako. Katika hilo hakuna mjadala Nelly. Imebaki muda na mahali.” Nelly akabaki akimwangalia, Billson akabaki na yeye akimwangalia, kisha akatazama saa yake kumuashiria anapoteza muda wake mwenyewe.

“Tunakwenda wapi?” Ikabidi Nelly aulize. “Ni suprise.” Bill akajibu akimtizama. Nelly akashangaa sana. “Sasa natakiwa kuvaa nini!?” “Sijali vile utakavyokuwa. Nipe muda na mahali, Nelly.” “Kwa  nini uni suprise!?” “Sasa hivi huruhusiwi tena kuuliza maswali.” “Kwa nini!?” “Unarudi palepale kwenye swali langu ambalo hutaki kujibu. Unaogopa nini?” “Nataka kujua tu!” “Hapana. Si kujua tu. Unataka kujua ili wewe ndio uongoze mambo. Sio kila wakati unatakiwa kuongoza mambo, Nelly! Ni sawa kabisa na wakati mwingine sio vibaya na wewe uwe unaongozwa.” “Nani amekwambia nataka ku..” “Nimekwambia huruhusiwi tena maswali, Nelly. Naomba muda na mahali nitakapokuja kukuchukua.” “Hakika sijawahi kukutana na mtu wa aina yako! Ni nini?” “Huruhusiwi maswali.” Nelly akatulia kama anayetafakari, Billy kimya akimtizama.

Mwishoe akanyanyua uso na kumtizama, akakuta bado akimwangalia. “Jumamosi huwa nakuja kazini mpaka saa 8 mchana.” “Naomba angalau iwe saa sita Nelly. Tafaddhali. Saa nane mchana hatuwezi kupata muda wakutosha.” Billson akaongea kwa kubembeleza tena. Nelly akashangaa sana. “Muda wa kutosha kufanya nini!?” “Wewe jiandae kupumzika, kula vizuri na wakati mzuri utakaokufanaya utulize mawazo na kuweza kunijibu swali langu.” Nelly akabaki akimwangalia. Akavuta kalamu pale mezani na kijitabu cha Nelly kilichoonekana anaandikia mambo yake muhimu.

“Najua kwa asilimia 99.9999, hutaitumia hii namba kwa sasa. Ila najua ipo siku utaihitaji.” Akaiandika namba yake ya simu na kusimama.  “Kama aliyenipa habari zako hajakosea, basi nyama choma ya mbuzi ambayo haijakaushwa sana, medium rare, italetwa muda si mrefu. Ule kabla ya kwenda kwenye kikao.” Billson akatoka na kumuacha Nelly na mshangao. Ni kweli Nelly alipenda mbuzi choma, ila asiwe amekaushwa kabisa. Abakie kama na rangi ya pinki kidogo. Akashangaa ni nani amempa Billson habari zake! Alijua kwa hakika Jax hawezi kuwa amezungumza naye kwa kuwa ni mkubwa sana kwake kwa wadhifa kazini na umri pia, asingethubutu kuweka mambo ya dada yake kazini. Nelly akabaki ameduaa hata kusahau alichokuwa akifanya kabla ya Billson kuingia hapo.

Na kweli baada ya muda akaletewa nyama ya mbuzi ya kuchoma, ndizi na pilipili nyingi kama anavyopenda pamoja na matango yaliyowekwa limao! Vimefungwa na kupangwa vizuri kiutaalamu kama vilivyotolewa kwenye migahawa ya walionazo. Nelly akashangaa sana na kubaki amekodolea macho kile chakula. Kwanza hata hakuwa na mpango wa kula mida hiyo ya mchana. Ukweli alikuwa na majukumu mengi siku hiyo. Na kwa Nelly, kazi kwake huwa hazisubiri. Kazi kwanza, tena kwa ustadi wa hali ya juu, kisha mengine baadaye.

Mwishoe akaanza kula kwa uchu. “Sasa ndio atanifuata wapi!” Nelly akajiuliza akila kile chakula kwa kukifurahia sana maana hata hakuwa amempa muda na sehemu ya kukutana ili waanze hiyo safari ya kwanza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Nini kitakachoendelea? Usikose muendelezo....


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment