Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Chozi Langu! - SEHEMU YA 17. - Naomi Simulizi

Chozi Langu! - SEHEMU YA 17.

 

Hilo juma likaanza kuwa zito kwa Lara. Hajui awashe simu au la. Hakujua kama Jax ndio amekata tamaa au la. Akaumia kana kwamba sio yeye aliyekuwa akimkimbia! Akaona thamani yake imeisha kwa muda mfupi tu! Akaumia sana Lara. Kumuulizia pale ndani, hawezi. Kumuuliza Lucas ambaye waligeuka kuwa marafiki, akashindwa kwa aibu. Anajirudije?

    Juma hilo ambalo alitakiwa kutolewa PoP, baba yake ndiye aliyempeleka hospitalini, akatolewa. Akaonekana amepona kabisa hata mfupa umeunga vizuri, lakini alitoka hapo hana furaha. Baba yake hakutaka hata kumuongelea Jax tena, maana alisema mwenyewe hamtaki. “Unataka turudi wote dukani au unataka ukapumzike?” “Nishapata mkono wangu, inabidi nichangamke baba. Mapumziko yameisha, inabidi nirudi kazini. Twende wote dukani nikafanye kazi kidogo.” Hilo juma nalo likaisha bila Jax kutokea.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~.

S

iku ya ijumaa wakati wanakaribia kwenda kulala, wakiwa tu hapo sebuleni, wakasikia mtu anagonga. Mzee Chiwango akaenda kufungua. Jax alikuwa hapo mlangoni na mizigo yake yote. “Samahani mzee wangu. Naona usiku sana, lakini sikuwa na jinsi. Naomba hifadhi.” “Ingia ndani. Tukupokee na mizigo.” Lucas akaruka. “Nilijua umesahau mechi ya kesho!” “Ukoje Lu bwana!? Mpokee mwenzio mizigo!” “Sio mizito mama. Asante.” Wakacheka.

“Sasa hapa ni padogo baba, utalala wapi? Lu mwenyewe analala kwenye hilo kochi hapo. Labda ule halafu Chiwanga akusaidie kutafuta chumba kwenye nyumba za kulala wageni.” “Kwani kochi hilo hapo nani analala?” Wakacheka. “Hamna mtu mwanangu. Lakini unataka kulala hapa sebuleni?” “Kama hamtajali.” Wakaangaliana hapo kwa wasiwasi.

“Gari nimeacha pale CCM wamenihakikishia ni salama.” “Hata letu tunaacha hukohuko. Pako salama kabisa. Ila tunawasiwasi na ulalaji wako!” “Au Lily ahamie chumbani kwetu na Lara halafu....” “Naombeni msiwe na wasiwasi kabisa. Mimi nitakuwa sawa. Na safari hii naona nitakaa kidogo. Nimechukua likizo fupi.” Kwa kifupi Jax alitangaza kuwa amefika pale. “Sawa. Karibu sana, wewe jisikie upo nyumbani.” “Yess!” Lucas akashangilia. “Muone huyu naye! Badala umfikirie mgeni!” “Jax hana neno. Amesema yeye hata kwenye kochi atalala. Kesho mechi kubwa Jax. Kila mtu alikuwa anakuulizia.” Lucas akawa amechangamka kwelikweli.

“Jioni yote hii walipotoka mpirani, wenzie walikuwa hapo nje wakikusubiria wewe, Jax.” Mama Chiwanga akaongeza. Jax akacheka. “Nilichelewa kutoka Dar. Ila niliwaahidi mazoezi ya jioni hii ya leo kabla ya mashindano ya kesho, na mimi ningekuwepo nao, nafikiri ndio maana walinisubiria.” “Basi mama aliwafukuza hapa ndani. Eti alisema wananuka!” Lucas akasemelea wote wakacheka. “Nyumba yenyewe ndogo hii, nawenyewe eti wametoka mpirani tu na kuja hapa, wanakuulizia! Lea aliwaambia haupo na hatujui kama utakuja leo, eti na wenyewe wakajipanga hapa sebuleni, wakikusubiria! Nyumba nzima ilijaa harufu yao ya jasho. Nikawafukuza mimi. Hivi ungewahi kidogo tu, ungewakuta hapo nje, wakikusubiria.” Akaongeza Lily, mama Lucas, dada mkubwa wa familia.

Akapokelewa mizigo yake. “Karibu ukae.” Akaenda pale sebuleni kukaa. “Lara anaendeleaje?” “Anaendelea vizuri kabisa na wamemtoa POP. Alikuwa hapa, hivi ametangulia tu kulala. Ila nimzima kabisa.” Akatulia kidogo wakamuona ameinama. “Bado kuna chakula. Tukuwekee ule kabla ya kulala?” Mama Chiwanga akavunja ukimya. “Nitashukuru mama yangu, sijala tokea asubuhi. Lakini kabla sijala, naomba niwaombe kitu.” Wote wakamgeukia.

“Karibu.” “Najua mmeniambia Lara amelala, naomba niingie nimwangalie tu.” Mama Chiwanga akamtizama mumewe. “Tafadhali wazazi wangu. Naomba tu nimuone. Lara ni mtu ambaye alikuwa akinifanya akili inatulia. Kuumia kwa Lara ni zaidi ya mimi kuvunja ndoa. Hamuwezi amini jinsi tulivyoishi na Lara. Hatukuwahi kupishana hata kwa neno! Mpaka sisi wenyewe tulikuwa tukishangaa. Kila nilichoongea, au alichoongea yeye, kiliendana na kile nilichokuwa nikikifikiria wakati ule. Mabadiliko yote niliyokuwa naonekana nayo, si kwa sababu nilipata kazi kwenye benki ya dunia, hata kidogo.” “Kumbe unafanya kazi benki ya dunia!” “Luuuu!” Mama yake akamuita, akimshangaa. “Si nimeuliza tu!” Jax akacheka.

“Kile ulichosema baba juu ya nilichomfanyia Lara, ni kweli mzazi wangu, hakustahili. Hata kidogo. Mimi nawajua binadamu, najua kuna wanao stahili, lakini Lara hakustahili. Si hasira tu, yupo kwenye mshituko.” Mama yake akatulia tu. “Na ninajua hautaisha kwa haraka, ndio maana hata mimi naheshimu hilo kumpa nafasi. Ila naomba kumuona. Nimuone tu, pengine akili yangu itatulia. Hii likizo nimechukua, kwa kuwa nahisi akili inavurugika. Hata kazini nimeanza kuharibu. Akili hazijatulia!” Jax akaendelea wakimsikiliza.

“Kiongozi wangu aligundua hilo, akanipa safari iliyokuwa aende mtu mwingine. Siku 10. Lakini nimerudi na kumwambia nafikiri nichukue tu likizo. Ndio maana nipo hapa wazazi wangu. Hapahapa alipo Lara. Sijali nitalala wapi, nyinyi mnifanye kama Lucas tu. Nipeni kazi, nitumeni, ilimradi niwe tu hapa. Msijali wala kuwa na wasiwasi kama yupo mgeni. Kile mnachokula, ndicho nitakula. Kama mnakwenda kazini, nyinyi msiwe na wasiwasi. Nifundisheni hata kufunga milango yenu, ilimradi tu niwe hapa. Lasivyo nitachanganyikiwa, niharibikiwe kabisa.” Wakamsikia mzee Chiwanga anavuta pumzi kwa nguvu.

“Ukifungua mlango huo, chumba cha upande wako wa kulia, ndiko anakolala Lara.” Jax hakuamini. Akasimama na kumshika mkono mzee Chiwanga. “Asante mzee Wangu. Asante sana.” Akatamani kama amkumbatie, akasita. Wote wakacheka. “Asante mama yangu kunivumilia. Asanteni sana.” “Karibu Jax.” Akaelekea alipoelekezwa. Wakamuona kabla hajafungua mlango anavuta pumzi kwa nguvu mara tatu kama anayesafisha kifua. Akajipangusa mikono kwenye suruali mara kadhaa, akavuta tena pumzi na kuingia ndani. Mzee Chiwanga akatingisha kichwa na kuinama. Kimya wote. 

Jax kwa Lara.

J

aax akaingia moja kwa moja, akamkuta kweli Lara amelala ndani ya chandarua. Akajisikia furaha kumuona pale alivyolala. Akamtizama, akaona asiishie kwenye kuona tu. Akavua viatu na kuingia ndani ya chandarua kabisa, akajilaza pembeni yake. Lara alikuwa amelala kabisa. Akauvuta mkono wake na kuunusa kiganja kwa nguvu zote. Akajifunika nao usoni. Akatulia. Lara akataka kugeuka akiwa usingizini, Jax akamuita. “Lara!” Akafungua macho, akabaki akimwangalia kama aliye usingizini haamini kama ni ndoto au la. Kisha akarudi kufunga macho. Jax akajua amedhani anaota. Lakini akamuona anatokwa na machozi. Akageuka vizuri na kuanza kumfuta, lakini Lara akajifunika mpaka usoni na kuendelea kulia. Alilia sana.

“Nilikosa Lara. Naomba nisamehe mpenzi wangu. Nisamehe mama. Nimejifunza kutokana na kosa langu. Nisamehe.” Jax akaendelea taratibu. Jax huyu si Jax yule aliyemwambia Lara kwamba amekusudia kuanza upya. Bila Tula ila anaanza. Iwe na Lara au la, anaanza. Jax huyu alikuwa amejishusha, anamtaka tu Lara. “Nisamehe Lara. Nisamehe mama watoto wangu.” Lara akashangaa kusikia mama watoto tena! Akageukia pembeni akijaribu kutulia.

Jax akajivuta juu kabisa akajiegemeza kichwa kwenye mkono wake. “Nachanganyikiwa Lara. Nachanganyikiwa bila wewe. Nisamehe mpenzi wangu. Wakati ule nakwambia naanza na yeyote yule, sikujua kama itakuwa ngumu hivi. Narudi mpenzi wangu, naomba nipokee. Wala tusianze upya, tuendelee vilevile. Sihitaji kitu kipya kutoka kwako, vilevile ulivyokuwa.” Lara akamgeukia. Jax akafurahi. Akawa amelala lakini amejikunja. Jax akajishusha chini kidogo kumfikia usoni.

Akamsaidia kujifuta machozi. “Nilijua hutarudi tena!” Lara akaanza taratibu. “Nilipata safari ya kikazi.” “Hongera.” Lara alijua lazima atakuwa ametengeneza pesa nzuri. “Nashukuru Mungu. Kwani ulinisubiria?” Lara akanyamaza, hakujibu. “Naona wamekutoa Pop. Vipi maumivu?” “Hamna maumivu. Umerudia hali yake ya kawaida. Namshukuru Mungu.” Jax akaendelea kuushika kuanzia begani mpaka chini. “Haujabadilika hata kidogo! Au wewe unauonaje?” “Naona haujabadilika, na mimi nilijua labda ukija kutoka, utakuwa mwembamba! Lakini upo tu sawa.”  Jax akaubusu.

“Nimekumisi Lara, nakaribia kuchanganyikiwa!” Lara akatulia. “Nakupenda Lara. Nakupenda sana na ninakuhitaji mpenzi wangu.” “Lakini sivyo ulivyoniambia Jax! Sivyo ulivyoniambia siku unavunja mahusiano na mimi rasmi. Ulisema unampenda Tula.” “Hapana, sikusema hivyo Lara. Ninakumbuka nilichokwambia kwa kuwa nilikifikiria na kukifanyia mazoezi zaidi ya nitakavyokwambia. Hapakuwa na neno la kumpenda Tula. Naomba ukumbuke mpenzi.” Lara akanyamaza akiwa amekunja uso.

“Sikukutamkia kama nampenda Tula, ila nilikutaarifu kuwa Tula amerudi, na nisingeweza kuendelea na mahusiano nikijua Tula yuko mahali ananihitaji. Unakumbuka hayo maneno?” Lara kimya. Akashitukia machozi yanamtoka tena. “Na nikakwambia pia haitakuwa sawa kwako. Itakuwa sikutendei haki. Eti niko na wewe, mawazo yako kwa Tula! Nilikwambia isingekuwa haki kwako. Unakumbuka mama?” Kimya. “Sikusema nampenda Tula kuliko wewe, nilikuwa nikijisikia kama nina deni kwa Tula. Nilikwambia jinsi nilivyohangaika na Tula.” Jax akataka akumbuke. Lakini Lara kimya.

“Tula alikuja akinikumbusha kule tulikotoka, nikajisikia nina deni kwake. Ikabidi kufanya maamuzi magumu nisijue najiingiza kwenye kitanzi. Tula hakurudi kwa mapenzi ila kuniangamiza tu au kunitumia. Nilikuwa naye huku akiwa na mahusiano mengine nje. Nilikwambia ile hali niliyoisikia mara tu ya kuhama naye kwenye ile nyumba. Nilijua nimepungukiwa. Lakini sikuwa na jinsi tena yakujirudi kwako nikijua nishaharibu sana.” “Mlijaliwa mtoto gani?” Lara akauliza taratibu tu.

“Dada Nelly alikuja kuniambia alikuwa muongo, hakuwa mjamzito.” “Jax! Ile fujo yote alifanya siku ile pale baa, unataka kuniambia alikuwa akiongopa!” “Wewe acha Lara. Tula! Namshukuru dada Nelly mpaka leo. Unakumbuka alimuonya asinisogelee lasivyo atamfunga?” “Nakumbuka.” “Sasa huwa anamuogopa sana dada Nelly, anajua huwa hajui kutishia mtu, na hajui kumpa mtu nafasi ya pili. Sasa anasema baadaye, baada ya kutulia na kufikiria vizuri akaingiwa na wasiwasi. Kwa nini akatae kuongozana naye hospitalini! Ikabidi aende Ustawi wa jamii yeye mwenyewe.” “Jax!” Lara akashangaa sana.

“Dada Nelly hajui kupuuzia jambo linalonihusu mimi au yeye mwenyewe. Japokuwa nilikuwa nimemkera mpaka mwisho, lakini alishindwa kupuuzia. Alikwenda Ustawi wa jamii, akawasimulia kila kitu, na akawa ameshajua mahusiano yake na mwanaume mwingine. Akashitaki yote akitaka lazima Tula akapimwe mimba kwanza, kisha baadaye DNA. Si ndio Tula akaitwa na kupewa sasa kama amri. Akataka kukataa, lakini akalazimishwa akipewa madhara ya kukataa. Ndipo wakaenda hospitalini wakisindikizwa na mtu wa Ustawi wa jamii. Kupimwa, hana hata mimba na alikutwa kwenye siku zake.” Lara akashangaa sana.

“Basi, ndio dada Nelly akamshitaki tena na kumuwekea msisitizo asiwahi kurudi kwake wala kwangu. Nilikuja kukutana naye sehemu, hata hakunisalimia. Na mimi sikumsemesha. Basi.” Lara akanyamaza.

“Sasa mama, hapa ni ukweni. Na niliomba ruhusa nikuone tu. Najua mnalala na Lea, pengine na yeye anataka kulala. Tutaongea kesho.” “Utarudi?” “Nikikwambia nimefika, ujue nimefika. Nalala hapo kwenye makochi.” Lara hakuamini. “Hapa kwetu!?” “Hapahapa. Tutaonana kesho. Wewe pumzika. Tutaongea zaidi. Nina likizo fupi, nitakuwepo hapa. Na kesho tuna mechi.” Lara akacheka. “Lucas anavyoiimba! Wenzie walikuwepo hapa ndani wakikusubiri mpaka mama yake akawafukuza. Lakini alijua hutarudi tena. Alijua hutakuwepo.” “Basi nipo.” Akambusu shavuni, akanogewa akasogea midomoni, akaona Lara hakatai.

 Jax akatulia hapo midomoni akiinyonya hiyo midomo kwa muda mrefu kama anayekata kiu. Lara naye alimng’ang’ania. Jax akajua na yeye alikuwa na hamu naye. Wakapeana mabusu, mpaka Jax akaona awe mstaarabu hapo ugenini. Akamwachia. “Nitafukuzwa ukweni. Acha nitoke, niwe na kiasi. Ila ujue hali mbaya Lara. Mbaya mno.” Lara akacheka taratibu. Jax akambusu tena na kutoka kitandani kama mtoto anayeogopa kufumaniwa. Akavaa viatu, Lara naye akatoka kitandani.

“Umeshakula?” “Nilishindwa. Nilisema mpaka nikuone kwanza. Lakini naona nitakula tu kesho. Sitaki niwasumbue sasa hivi.” “Basi twende, nikuandalie mwenyewe.” Lara akabadili nguo hapo harakaharaka Jax akimsubiria, wakatoka. Kila mtu akamuona vile Lara alivyofurahi, wakajua wameyamaliza.

Jax akarudi sebuleni, Lara akaelekea jikoni. Lily akamfuata. Wakasikia wakicheka. “Daah, nawashukuru sana wazazi wangu. Asanteni. Angalau moyo umetulia. Nahisi leo hata nikilala sakafuni, usingizi utanijia.” Wakacheka. “Acha nitoke nikampigie simu dada, nimwambie nimempata Lara. Najua hataamini.” Jax akasimama na kutoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jax alipoondoka tu jijini, na dada yake akahamia anakoishi Billy. Wote walishanogewa kama watoto wadogo, hawawezi kuachiana. “Upo sawa?” Nelly akapokea kwa haraka akiwa kitandani na Billy. “Nimemuona Lara, dada yangu.” Akamsikia Nelly akicheka. Nelly huyu siye yule mchungu, angalau kulishaanza na mahusiano ya tofauti kwa ndugu hao. Yakuzungumza na kucheka. “Daah! Siamini!” “Anaendeleaje?” “Vizuri. Na amenisamehe.” “Ukome na usirudie tena.” “Aisee siwezi. Nimekoma.” “Nipe nimsalimie.” Jax akafurahia hilo sana.

Akarudi ndani kwa haraka. “Lara?” “Nipo jikoni, Jax.” “Dada Nelly anataka kukusalimia.” Lara akatoka kwa haraka. “Naogopa Jax!” Akanong’ona wazazi wao wakisikiliza. “Usiwe na wasiwasi.” Akapokea simu kutoka kwa Jax. “Shikamoo dada.” “Marahaba Lara. Habari za siku?” “Nzuri. Nipo kwa wazazi huku, nakula na kulala tu.” Wakamsikia akicheka. “Itabidi mtafute nyumba huko, naona na Jax atahamia hukohuko. Jiji la Dar limemshinda.” Lara akacheka akimwangalia Jax. “Nimefurahi kukusikia Lara. Naamini nitakuona hivi karibuni.” “Naamini hivyo.” Wakaagana na kumrudishia simu Jax. Jax akamuaga dada yake. Wakacheka kidogo na kurudisha simu mfukoni.

Nelly na Mpenzi Billy.

“Lini unanitambulisha kwa Jax?” Lilikuwa swali lililomshitua Nelly. Akaweka simu pembeni na kutoka kabisa kitandani. Akaelekea bafuni kuoga na kutoka. Billy akamuona anavaa. “Si unajua hujanijibu?” “Nakwenda kulala kwangu.” “Nisubiri basi na mimi nioge, tutoke wote.” Nelly akashangaa sana. “Unakwenda wapi?” “Si umesema kwako!” “Mimi ndio nakwenda kulala kwangu.” “Kwa kuwa sivyo tulivyokubaliana, basi ujue unakokwenda kulala leo, ujue na mimi nitakuwepo.” Nelly akachoka kabisa na kurudi kukaa kitandani.

“Sitachukua muda mrefu.” Billy akasimama kabisa kuelekea bafuni. “Naomba uache mambo ya kitoto Billy. Unakwenda wapi sasa?” Billy alijua wazi Nelly hawezi kumruhusu akalale nyumbani kwake sababu ya Jax. Na hapo anakimbia swali tu, maana walikuwa na wakati mzuri sana kabla ya simu ya Jax. Billy akasimama akimtizama. “Wewe ulitaka kutambulishwa kwa Jax kama nani?” Billy akarudi kukaa. “Utakavyotaka wewe.” Billy akajibu na kutulia.

“Basi ipo siku nitakutambulisha.” “Yeah, hilo linasikika jibu zuri sana lakini mimi na wewe tunajua hiyo siku inaweza isifike Nelly.” “Sasa wewe shida yako ni mimi au Jax?” “Sijui kama unakumbuka miaka yangu?” Nelly akawa ameshamuelewa. “Yeah, sifanyi mapenzi ya wizi. Yaani na umri huu, mimi, baba na majukumu yangu, eti niishi kwa kujificha! Hapana Nelly. Naomba kujua. Hii tabia yakujificha kama watoto wadogo, sitaki.” “Nani anajificha sasa?” “Wewe.” Billy akajibu.

“Hivi unakumbuka kuwa mimi ndio ndugu wa pekee wa Jax na mtu anayenitizama kwa karibu?” “Kwamba unaogopa ukikosea au jambo likiharibika utakuwa unaweka mfano mbaya?” “Nashukuru kwa kulielewa hilo. Basi tutaonana kesho.” Nelly akasimama ili aendelee kuvaa. “Kama unaharaka basi nitaenda kuogea kwako.” Billy naye akarudi kutafuta nguo. “Hivi ni nini Billy, jamani?” “Ukishasema ndio kwenye mipango yetu, hutanibadilikia katikati Nelly. Huwezi kunikatisha starehe zangu usiku huu wa leo kwa hofu zako za kuhofia kuthubutu.” Nelly akarudi kukaa.

“Naomba tuamue moja Nelly. Tunaenda au tunabaki hapa na ujibu swali langu sio kukimbiakimbia.” “Tunabaki hapa. Ila sipo tayari kwa Jax kufahamu chochote kinachoendelea kati yetu. Na naomba muache Jax kabisa kwenye hili.” “Yeah, about that!” Akaanza Billy. “Haiwezekani labda kama unataka kuahirisha kila kitu kati yetu. Mimi sifanyi mambo ya uwizi. Sina sababu.” “Basi tuahirishe.” Bila hata kufikiria mara ya pili, Nelly akaamua kuachana na Billy.

Billy aliumia sana. “Kweli Nelly?” “Mimi sipo tayari Billy, na wewe unataka lazima umfahamu Jax!” “Kweli unaniacha mimi kwa hofu ya kutotaka Jax kujua kama umeamua kuchukua hatua ya imani kwangu!? Unavunja mahusiano na mimi sababu ya kutotaka Jax atufahamu?” “Kama mimi nisipomlinda Jax, ni nani atamlinda?” “Unamlinda na nini?!” Billy akamuuliza na kuendelea. “Maana Jax mwenyewe anaendelea na maisha yake kama kawaida! Humlindi Jax, unajilinda mwenyewe. Na kama mpaka sasa umeshindwa kuniamini, ni lini utakuwa tayari?” “Sijui.” Nelly akajibu akiwa ameshakasirika.

“Unajua nini Nelly, upo huru kuondoka. Sitakuzuia tena.” Bila yakujali, Nelly akamalizia kuvaa na kuchukua vitu vyake vyote pale kwa Billy akaweka kwenye gari yake na kuondoka kama utani tu, tena Billy akiwa bafuni. Walipanga weekend hiyo wakae tu hapo kwa Billy. Watoke siku ya jumamosi kwa sinema na chakula cha usiku kisha kurudi tena kupumzika hapo, lakini Nelly ameondoka! Ikamuumiza sana Billy, ila akaona amueache tu.

Kwa Chiwanga.

Ilibidi dada mkubwa, Lily, ampishe Jax na mwanae chumbani chake, akalale chumbani kwa Lea ambako analala na Lara. Lakini Lara na Jax walibaki sebuleni, Jax akila. Lara alijua anajiwinda sana maneno. Akawa mchache sana wa maneno. Lara naye alibaki tu kimya. “Nimefurahi kukuona Lara.” Ndio neno alilokuwa akirudia rudia kila wakati. “Kesho una ratiba gani?” Akauliza baada ya kula. “Wewe pumzika Jax. Mimi bado sijajiingiza kwenye ratiba za hapa kwa kuwa nilikuwa nikijipanga. Siwezi kuendelea kuishi hapa. Lazima niondoke nikaendeleze maisha.” “Wapi?” “Nina uhakika kwamba si hapa. Nafikiria kurudi Dar.” Hapo Jax akanyamaza.

“Nimekuwekea maji, nenda kaoge, ukapumzike.” “Hujanijibu juu ya kesho.” “Naweza kubaki hapa ili ukiamka unikute. Kwa hiyo kesho nitakuwepo nyumbani ili Lea akasaidie dukani. Siku za jumamosi kunakuwa busy sana pale dukani. Baba anatumia kila msaada tutakao wapa yeye na Lily.” “Sawa. Basi nikiamka tutazungumza.” Lara akamuacha anakwenda kuoga akiwa ameshamuonyesha mpaka chumba atakacholala.

Jumamosi.

Asubuhi Lara ndiye aliyekuwa wa kwanza hapo kwao kuamka. Kila mtu anaamka, akawa ameshaandaa kifungua kinywa cha kila mtu, wakajua tu ni kwa sababu ya Jax. Wakala na kukimbilia kufungua duka. Wakamuacha hapo yeye, Jax na Lucas ambaye baadaye wenzake wakafika hapo kumchukua Lucas na Jax kwenda mazoezini. Lara akawa akicheka tu.

Ilibidi jioni yake wamuache mzee Chiwanga peke yake huko dukani kwenda kushuhudia hiyo mechi ya Lucas ambayo alimuingiza na Jax. Akatia hekaheka kama ni mpira wa kimataifa kumbe wa vijana tu wadogo wa mtaani. Wakacheza mida hiyo ya jioni, japokuwa hawakushinda, lakini pia hawakufungwa. Ikawa kelele kwa Lucas akifurahia huo mpira, mama yake akamwangalia na kuamua kurudi tu kazini pamoja na wengineo, Lara akawa alishapika mpaka chakula cha jioni, akabaki na Jax hapo uwanjani, Lucas akaondoka na wenzie wakishangilia.

Jax&Lara Tena.

“Ukaoge. Maana unatokwa jasho!” Jax akacheka na kumsogelea karibu.” “Nina swali ambalo naogopa kukuuliza Lara.” “Swali gani?” “Kama umenisamehe kabisa.” Lara akainama kama anayefikiria. “Najua nimekuumiza sana. Lakini natamani kujua kama umenisamehe au unampango wa kuja kunisamehe.” “Nimesamehe Jax.” “Kweli Lara?” “Kabisa. Yameisha. Huwa wakati mwingine natamani kama kungekuwa na matatizo katikati yetu ili nikuchukie moja kwa moja.” “Naomba tusirudi nyuma. Tuendelee. Nina swali la pili.” Jax akakaa haraka.

“Ukirudi Dar, unampango wa kuishi wapi?” “Hilo ndilo linanifanya nifikirie, sehemu yakuishi. Ila kama nini chakufanya ni kama nimepata wazo, nikuchukua tu hatua.” “Nini?” “Biashara. Sitaki tena kuajiriwa. Nataka nijaribu biashara. Ninayo pesa na wazo.” Jax akafikiria. “Naishi na dada Nelly.” “Unamaanisha nini?” “Nilirudi nyumbani. Nilimuudhi sana. Nikajua neno samahani halitatosha mpaka kumuonyesha kwa vitendo kuwa nimeamua kubadilika. Sasa na wewe uliposema ile nyumba huitaki, nikaona niifanyie biashara.” Lara akamtizama na kunyamaza.

“Ila najua hatutakosa sehemu ya wewe yakuishi.” Lara hakumjibu. “Unajua ile nyumba ndogo ya pale nje kwa dada Nelly alishamaliza?” “Kwamba nikaishi kwenu?!” “Basi kama ni wazo baya, Lara. Naomba safari hii nikusikilize tu wewe.” “Mimi bado nafikiria. Nikipata jibu ndio nitachukua hatua.” “Kwani harusi yetu ni lini?” Lara akakunja uso akimshangaa na akajua amefanya kuchomekea tu.

“Nilikwambia nakusikiliza wewe Lara. Mimi nipo tayari kukuoa wewe. Utakapokuwa tayari tu, tunamalizia tulipoachia. Ndoa. Na sitafanya kitu kikubwa. Kidogo tu.” “Mimi ndoto zangu ni kuolewa sherehe kubwa, kanisani na nivae shela. Sitaki vitu kama najificha!” “Basi mama. Samahani. Tutafanya kubwa. Na nini tena unataka?” “Sasa unaniuliza wakati hata pakuishi hatuna!? Au unataka tena mimi unirudishe kwenye vile vyumba vya uswahilini?!” “Hata kidogo mpenzi wangu. Kwanza hatuna sababu yakufanya hivyo wakati pesa ipo. Ukiniruhusu, hata kesho asubuhi naondoka hapa kwenda kuanza kufuatilia maswala ya nyumba. Mji mkubwa ule, hatuwezi kukosa kwetu. Au unasemaje?” “Mimi sijui Jax!” Lara akasimama.

“Naomba safari hii wewe ujue Lara. Kile unachotaka ndio tutafanya. Na nimekuhakikishia mimi ni wako. Au bado unawasiwasi?” “Ndiyo.” “Basi naomba usiwe na wasiwasi. Wewe niambie kile unachotaka.” “Harusi kubwa, na nivae shela kubwa. Pakuishi mimi sijali ilimradi tuwe wote Jax. Na safari hii usinikimbie.” “Basi hivyo umepata. Mimi kesho narudi Dar, naanza maandalizi mapya ya harusi huku nikitafuta nyumba.” “Itachukua muda gani?” Lara akauliza.

“Niambie wewe unataka tufunge ndoa lini?” Lara akabaki kimya akifikiria huku wote wamesimama. “Nafikiri kitakachokwamisha labda ukumbi na...” Akafikiria. “Ila safari hii nataka dada Nelly ndio anisaidie. Tino nilishamfedhehesha sana.” “Na dada Nelly?” “Hana jinsi. Mimi ni jukumu lake hata afanye nini. Hawezi kunikwepa. Ila kwa Tino si sawa. Acha na yeye nimualike tu. Nipe tarehe.” “Wewe utakapokamilisha mambo yako, uniambie.” “Asante Lara. Basi kesho nitaondoka mapema asubuhi, nikaanze na dada Nelly. Safari hii sitakuangusha. Nakuahidi Lara. Nitafanya vizuri. Kama ingekuwa si kuharibu tokea mwanzo, ningekwambia wewe ukaishi kwenye ile nyumba wakati mimi naishi kwa dada Nelly mpaka tukifunga ndoa, ndipo nihamie pale.” Lara akajua ndio anamuomba hivyo ila anahofia.

Akafikiria jinsi lile eneo lilivyo zuri. Akajiambia asimzirie Tula ambaye aliondolewa pale akipalilia. Halafu akajitizama alipo, akajiona mjinga kuziria nyumba. Akatulia akifikiria na Jax naye akatulia kidogo. “Ila lile eneo ni zuri sana Lara. Pale watoto wetu watakua kwa furaha. Kumetulia halafu upande ule wa nyuma tunaweza hata kujenga kanyumba kazuri. Namuonea wivu atakaye pakodisha pale!” Lara akacheka kidogo akifikiria.

“Usizire mpenzi wangu. Wakati nikinunua ile nyumba, nilikuwa nikikufikiria wewe. Halafu acha nikwambie ukweli. Mkopo wake bado nakatwa pamoja na magari niliyokopa. Sasa nikianza kutafuta...” “Sawa Jax.” “Kweli Lara?” “Ni sawa.” “Daah! Afadhali sana. Utarahisisha mwanzo wetu na mambo ya harusi. Hatutajimaliza kabisa. Basi acha nikaweke mambo sawa. Ili ufikie hapo. Niliifanya Air B&B. Kama haijapokea wageni sasahivi, naenda kuweka kikomo, uje ukaanze kuishi hapo mpenzi wangu. Ukapaandae kwa ajili yetu.” Lara akacheka akisikika safari hii ametulia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jioni wakati wanakula na mzee Chiwanga yupo na mkewe, Jax akaanza. “Wazazi wangu, mimi naondoka kesho.” “Tena!?” “Kwa baraka za Lara. Nakwenda kuandaa harusi yetu, tunamalizia safari yetu.” Pakazuka ukimya wa gafla. “Najua hapa alishaagwa, bado ndoa tu. Ndio nakwenda kuiandaa. Naomba nyinyi msifanye lolote, nikikamilisha kila kitu, nitarudi kuwapa tarehe.” Kimya.

“Na nakwenda kumuandalia mahali pazuri pakuishi. Kuna nyumba niliinunua, nikaifanya yabiashara, mimi nikarudi kuishi kwa dada. Sasa nitaenda kuiandaa ili Mungu akipenda ndani ya juma moja, Lara ahamie hapo wakati mimi nikiweka sawa mambo yetu ya harusi. Tukiona, mimi ndio nitamfuata Lara.” Kimya. “Naomba muwe na imani wazazi wangu. Safari hii siharibu tena. Nimejifunza kutokana na makosa, sitarudia tena. Lara ni mwanamke wangu, ndiye atakuwa mama wa watoto wangu mimi Jackson. Hilo sitabadilika na Lara amekubali. Tafadhalini naomba mumtie moyo ili kumuondolea hofu.” Akataka kupiga tena magoti, mzee Chiwanga akamzua.

“Hapana Jax. Inatosha. Nyinyi endeleeni tu. Tunawaombea safari hii mfanikiwe.” Jax akasimama na kwenda kumpa mkono. “Nashukuru baba yangu. Asante sana.” Lara alikuwa kimya tu akifikiria. “Nakuahidi tutakuwa sawa Lara. Naomba usiogope.” Jax akaongea hapo mbele ya wote, Lara akamtizama. “Natamani niondoke usiku huu ili nikaanze maandalizi.” “Hapana Jax. Naomba utulie tu. Kama ni jambo la Mungu, atalisimamia tu na litakamilika. Wewe nenda kapumzike.” “Nashukuru mama yangu. Endelea kuniombea. Safari hii sitaharibu.” Akampa na yeye mkono. Pakatulia kimya. Jax akajua wote wameingiwa hofu, ni vitendo tu ndivyo vitawathibitishia hilo. Pakatulia kabisa mpaka kila mtu akaaga kwenda kulala bila ya kuongeza neno tena.

Jumapili.

Lara aliamka tena asubuhi na mapema kuandaa kifungua kinywa. Wakati yupo jikoni Jax akamfuata. “Vipi?” “Nataka niwahi kuondoka. Ili leo nimpate dada Nelly akiwa ametulia sio siku ya kazi. Ili tupate muda wa mazungumzo. Mipango ianze.” Lara akasimama. “Mimi naomba nikwambie kitu Jax. Najua nilikwambia, ila nataka nikukumbushe.” Jax akatulia akisikiliza kwa makini.

 “Nilikusudia maisha yangu yasiwe hapa Dodoma. Mpaka sasa chaguo ni Dar. Niliondoka kwa muda ili kutuliza mawazo. Na nilikuja hapa nyumbani kwa mapumziko nikijipanga. Nipo tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha yangu kiuchumi nikiwa najua nini nataka. Biashara. Nina wazo, mtaji na jana usiku tulipoachana pale, nimepata mahali pakuishi.” “Wapi!?” Jax akashituka kidogo. “Nilirudisha mawasiliano na kina Suzy na Sesi. Japokuwa chumba changu walipangisha, lakini jana usiku wakati nalala, Sesi alinipigia simu kunijulia hali na kutaka kujua ninampango wa kurudi lini Dar. Nikamwambia nasubiria sehemu ya kuishi, ndio amenikaribisha kwenye chumba chake. Amesema hatakuwa na shida ya kunihifadhi wakati nikijipanga upya.”

“Kwa nini usinisubiri, Lara?” “Hapana Jax. Wewe ni binadamu kama binadamu wengine tu. Hilo umelithibitisha kwa vitendo. Haitakuwa sawa kwako na kwangu pia kuweka tumaini langu lote kwako. Hapana Jax. Maisha yangu hayatasubiri tena. Wewe endelea na mipango yako kama kawaida na mimi acha niendelee tu. Ikitokea inakuja kukutana huko baadaye, sawa. Ikishindikana tena, isiwe sababu yakukimbiana.” “Lara! Mbona kama umenikatia tamaa kabisa!” “Sitakudanganya Jax, kweli nimekukatia tamaa. Na haikuwa sawa tokea mwanzo kukuamini kwa kiasi hicho. Wewe ni binadamu.” Lara akaendelea.

“Naomba tuagane kwa amani kabisa.” “Unamaanisha nini?” “Hakuna kitakachobadilika. Endelea na kile kilichopo akilini mwako na moyoni. Nakuahidi sitabadilisha namba ya simu. Kwa sababu yeyote ile, pengine kuongeza tu, lakini hii itakuwa hewani. Utakapotaka kuwasiliana na mimi, kuwa huru muda na wakati wowote ule tuwasiliane. Ila naomba nikuombe kitu Jax.” Hapo Jax alikuwa amebadilika kabisa.

Lara wa safari hii sio mgonjwa na anamipango yake. Afya nzuri, amependeza na si mnyonge tena. Swala la ndoa sio kipaumbele kinachomnyima raha tena au kutizamia kwa haraka, ila maisha kuendelea. Mwanaume wa mwisho ambaye Jax ameshuhudia amekuwa nae, ni Jerry. Mwanaume mwenye pesa. Lara ametulia mbele yake hayumbishwi tena.

“Jax?” “Nakusikiliza Lara.” “Naamini tumeshakua watu wazima sasa. Tafadhali tuwasiliane. Tuwasiliane tu. Hata kukitokea kuna kubadilika kwa mipango ni..” “Nimekwambia sitabadilika Lara. Tafadhali niamini.” “Wewe si Mungu Jax. Mambo huwa yanatokea.” Jax akainama kama aliyechoka kabisa. “Kama nilivyokuwa nikikuomba, tafadhali tuwasiliane. Kuwe kunakutobadilika mawazo au la, tuwasiliane.” “Na wewe utawasiliana na mimi?” “Ukiniruhusu, bila shida.” Jax akamwangalia, Lara akarudi kukaa kuendelea kupika chapati za kifungua kinywa.

“Kwani unataka kuondoka huku lini?” Jax akamuuliza tena. “Kuna mtu nimepewa mawasiliano naye. Nimemtumia ujumbe kumuomba nikutane naye tuzungumze.” “Mnazungumza nini Lara!?” “Ni maswala ya biashara!” Jax akabaki akimtizama. “Sasa ameniambia hana uhakika kama ananafasi alhamisi au ijumaa. Ila amesema mida ya jioni ndio anakuwa na nafasi. Nimemwambia kwa kuwa sina usafiri, kama anaweza basi anipe muda wa mchana. Amekubali. Sasa kwa kujibu swali lako, nafikiria jumatano jioni niwepo Dar nisubirie jibu lake hukohuko.”

“Naomba umwambie huyo mtu huo mchana tutakuwa wote.” Lara alicheka mpaka akapaliwa. “Umeanza lini wivu, wewe Jax!?” “Mimi naondoka, ila mwambie hiyo siku na mimi nitakuwepo.” “Sasa na wewe unataka kufanya biashara wakati umeajiriwa!?” “Naomba chapati, Lara. Nile njiani.” “Angekuandalia chai harakaharaka uondoke umekula kabisa.” Wakamsikia mama Chiwanga huko sebuleni, wakajua walishaamka na walikuwa wakisikilizwa.

“Acha niwahi tu mama yangu. Namuwahi dada Nelly ili nizungumze naye kabla hili juma halijaanza.” Jax akatoka na kumkuta mama Chiwanga na mumewe. “Mimi naondoka ila naomba wazazi wangu, msipokee mahari ingine tena ya Lara.” Lara alicheka mpaka akatoka jikoni. “Ni kwa nini umekuwa na wasiwasi hivyo wewe Jax?” “Mimi nazungumza na wazazi Lara. Maana sasa hivi umekuja na mipango inayo niogopesha! Mimi nishalipa mahari, naenda kuandaa harusi. Na ni kwa vile Lara hataki harusi ndogo.” “Unataka kubwa mama?” Baba yake akamuuliza. “Ndio baba! Kwa nini mimi ndio niolewe kwa kifocho? Ndio ndoto zangu baba na wewe unajua. Nataka kuvaa shela kubwa, na nimwagiwe maua.” Kila mtu akaanza kucheka mpaka wa vyumbani.

“Hujakata tamaa wewe Lara?” Lily dada mkubwa akamuuliza. “Hapana dada yangu. Lazima. Vikishindikana, naendelea kwa mwingine mpaka nipate wakusimama na mimi kanisani.” “Na Lara anapenda harusi tokea mtoto!” Lea naye akajitokeza na kuchangia. “Basi hakuna kutafuta tena. Ushapata. Na nimekwambia naenda kukuandalia harusi. Naomba utulie.” “Sawa Jax. Lakini ukichelewa utakuta mwana si wako!” Lara akajibu kwa ujasiri kabisa na kushanganza wote na kurudi jikoni. Pakazuka ukimya. “Nakufungia chapata Jax. Usiondoke.” Lara akasikika huko jikoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jax aliondoka jiji kuu la Tanzania akiwa amerushwa roho na Lara vilivyo. Wasiwasi ulimjaa. Lara huyu anayo na pesa! Jax akazidi kuingiwa hofu. Simu alizokuwa akipigiwa Lara, mpaka mwenyewe akachoka. Kila baada ya muda mfupi alimpigia kumwambia alipofika. “Naona leo na mimi nipo safarini na Jax!” Lara akalalamika. Wote wakacheka. “Nahisi ameingiwa hofu.” “Basi mimi ndio nakoma. Haya ametuma tena ujumbe!” “Basi atapata ajali. Anaandika huku anaendesha!” “Hapana mama yangu. Ananitaarifu amesimama kuongeza mafuta.” Wote wakazidi kucheka. “Acha nikampigie pengine atatulia.” Lara akatoka hapo sebuleni na kurudi chumbani ili azungumze naye.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment