Jumanne.
Usiku wa jumanne wakiwa nyumbani, Lara na Lea wametoka, Jax akarudi
tena. “Mimi naona uhamie tu huku, baba.” Wote wakacheka jinsi mama Chiwanga
alivyozungumza kwa upole lakini akimaanisha. “Nimekuja kumfuata Lara.” “Huyu
Lara si alisema anaondoka ijumaa sababu miahadi yake ni jumamosi si alhamsi
tena!” “Hata yeye hajui kama ninakuja. Nilifikiria tu leo asubuhi nikaona ni
msuprise.” “Haya, baba. Karibu. Ila ametoka na Lea.”
“Acha nimpigie ili
niwafuate huko walipo.” Bila kusubiri akatoa simu, mzee Chiwanga na mkewe wakaangaliana.
Lara alipopokea tu, Jax akatoka hapo mbio bila ya kuaga kama anayewahi kuokoa
kitu. “Huyu kijana atachanganyikiwa jamani!” Mama Chiwanga akaongea kwa
kumuhurumia Jax.
Jumatano.
“Jax hatakwenda kuniweka unyumba tena mpaka tutoke kanisani.” Lara
akaongea bila wasiwasi akimtizama mama yake, mpaka Jax akapoa. “Nishaamua
kubadilika mama yangu. Natulia kabisa. Na ahadi yangu ipo palepale. Natulia
kabisa. Ukinisikia tena, ujue ni mke wa huyo mtu. Wala usiwe nawasiwasi.
Nakumbuka shida na maombi yako yote juu yangu. Sitajiingiza tena matatizoni. Nimejifunza
kwa machozi. Nakuahidi nakwenda kutulia kabisa. Na sitaanzisha safari ingine na
mwengine mpaka nihitimishe na Jax rasmi.” Hapo Jax akaridhika.
“Natoka hapa kwenda kuendelea na maisha, nikiwa na Mungu wangu.
Nimetubu, tumeomba pamoja mama yangu, ujue nimekusudia kubadilika. Endelea tu
kuniombea mama yangu.” “Hapo sawa. Maana nimehofia msije mkatoka hapa, mkaanza
tena maisha mliyoishi zamani.” “Hapana mama yangu. Huko sirudi tena. Naendelea
tu na naomba Mungu atusaidie. Ikishindikana na Jax, basi anipe mwingi..”
“Naomba acha kusema hivyo, Lara! Nimekuomba mara nyingi tu!” “Basi, Jax. Ila
huo ndio msimamo wangu.” “Nimekusikia, Lara na mimi nitaheshimu hilo.” Wakapoa
kabisa, zaidi Jax mpaka wote wakamgundua ndio ilikuwa nia yake akijua anamtoa
hapo Lara kwenda kuishi naye.
“Na wewe Jax, mpe Yesu maisha, baba. Sio dini. Mruhusu akulinde. Wala
usitake mengi. Yeye akiwa mlinzi atakusaidia kwenye huo ujana wako. Atatawala
maisha yako na utashangaa uhuru utakao kuwa nao ndani ya Kristo. Atakupigania
na kukulinda.” Mama Chiwanga akaendelea. “Amani iliyopo ndani yake, inapita
yote. Haifananishwi na kiwango cha pesa kilichopo benki, wala elimu iliyopo
kichwani mwa mtu. Upo utulivu, Jax mwanangu, na utoshelevu wa aina yake. Ni
baba wa yatima. Anayofaraja ya ajabu na atakusaidia kwenye kila hatua kwenye
maisha yako. Tafadhali mruhusu, mfungulie mlango aingie kwenye maisha yako.”
Lara kimya akimsikiliza mama yake akizungumza na Jax.
“Mtakuwa na ndoa nzuri yenye utulivu. Hata mambo yakiwawia magumu,
mnakuwa na kimbilio.” “Nimekusikia mama yangu.” “Mimi nitakuombea, halafu usiache
kwenda kanisani. Nendeni tu, huko ndiko utakutana na Mungu na utajifunza maisha
ambayo Mungu anataka wewe uishi na yanayompendeza yeye.” Mama Chiwanga
akamuongoza sala ya toba. Jax akakubali kumpa Yesu maisha akiwa hata hafahamu
vizuri ni nini anatakiwa kufanya, akawatamkia baraka, wawili hao wakaondoka
kurudi Dar.
Safari Mpya ya Jax&Lara.
Njiani kulikuwa na hali ya utulivu kati yao lakini kama wageni kwa
kila mmoja wao. Hawajui wazungumze nini kati yao. Kila mmoja akijiwinda kwa
neno wakati ni wapenzi waliokuwa hawamalizi mazungumzo na vicheko. Wakajikuta
wamekuwa wageni kwa kila mmoja wao. Simu ya Nelly ikaingia. “Mpitie nyumbani kwa chakula.” Angalau hilo likamfurahisha
zaidi Jax. Kwa mara ya kwanza Nelly anampokea mwanamke wake nyumbani kwake na
kumkarimu! Hilo likamfurahisha sana Jax, na likaleta maana kubwa sana asijue
dada yake ameamka na hali mbaya, akiwa hajui chakufanya, akaishia kupika.
Hakuwa amemtafuta Billy hata kwa ujumbe wa kumjulia hali na wala Billy naye
hakumtafuta. Alikusudia kumuacha kabisa kitu kilichomuuma Nelly. Alijua pengine
Billy angemtafuta, lakini ikawa kimya kabisa.
“Dada Nelly ametukaribisha nyumbani kwa chakula cha usiku.” Lara
hakuamini. “Kweli Jax?!” “Hata mimi nimemshangaa. Ila amebadilika! Sio Nelly
nimekua nikimuona siku zote.” “Amekuaje tena?” Lara akaingiwa na hofu kidogo.
“Hapana. Amekua wa tofauti kwa upande mzuri. Nashindwa kumuelezea, lakini sasa
hivi angalau anaweza kukaa na kueleza siku yake iliendaje huko kazini. Akataka
kunisikia ninavyoendelea. Yaani ameongeza kujali kwa namna ya tofauti! Anazungumza
na mimi heart to heart. Sijui umenielewa?” Lara mwenyewe alicheka jinsi Jax
alivyokosa maneno sahihi kwa dada yake.
“Wewe unafikiri ni kwa nini yupo hivyo?” “Wakati gani sasa? Maana
Nelly huyu si yule wa zamani. Hakika amebadilika.” “Namaanisha yule wa zamani.”
“Mimi nahisi, narudia tena nahisi maana sipo karibu naye sana kujua
kinachoendelea na kilichoendelea tulipoachwa.” Hapo Jax akatulia. “Nini?”
“Unajua sikuwahi kumuuliza maisha yalikuaje, au alifanyaje fanyaje kufanya
tuishi! Maana niliachwa na wazazi hata sikuwa na miaka 5, na Nelly alikuwa
mdogo tu. Na simkumbuki mwanadamu mwingine kwenye maisha yanu ila yeye!” Jax
akawa kama ameingiwa na kitu kichwani na kumfanya afikirie zaidi.
“Kuanzia hospitalini mpaka shuleni, ilikuwa ni Nelly tu. Na nakumbuka
alikuwa akinisisitiza nitulie shuleni ili asiwe anaitwa, ili na yeye aweze
kufanya vitu vingine. Kwa hiyo tumekua tukiwa sisi tu. Sijui alikuwa
akifanyaje, nahisi kwenye hicho kipindi ndipo alipokutana na magumu au ndivyo
alivyoumbwa, sijui! Lakini nimeanza kujichukia kushindwa hata kupata naye muda
kumuuliza ilikuaje kunifikisha hapa! Japo pia kwa Nelly yule, nahisi
nisingepata hilo jibu. Alikuwa amefunga sana moyo.” Jax akaendelea kuzungumza
lakini kama anayemfikiria dada yake, Lara akabaki kimya akisikiliza kama
asiyetaka kumuingilia.
“Halafu pia siwezi kumlinganisha kitabia na hata mmoja wa wazazi wetu
kwa kuwa kweli siwakumbuki kabisa zaidi ya kwenye picha chache sana alizonazo
yeye mwenyewe Nelly. Sasa sijui! Ila najua japokuwa ni mkorofi sana, anaweza
kufanya chochote kwa ajili yangu. Hilo ninalijua na japokuwa huwa namuudhi
sana, hawezi kunitupa.” “Kwa hiyo ni kama mtoto wake?” “Kabisa. Nimerudi kuishi
naye wala hajaniuliza mpaka leo. Ananipikia na kuhakikisha msichana wake
anaingia chumbani kwangu kusafisha, kufua na anamuwekea mashati yangu kwenye
nguo zake anazopeleka dry clener.” “Jax!” Lara akashangaa.
“Kweli tena. Hapa nilipo nimerudi kulelewa kama mtoto. Nguo zangu
zinafuliwa wala sipati shida. Anahakikisha nakula na chumba changu
kinasafishwa.” “Ndio maana umehamia moja kwa moja!” Jax akacheka sana. “Ila
acha tu nikwambie ukweli. Nilikuwa na
hali mbaya, Lara! Sikuwa na jinsi ila kurudi tu kwa Nelly. Na nafikiri na yeye
alijua nimeharibu kiasi cha kwamba hata marafiki wamenikimbia, akawa kimbilio
langu na kunisaidia pale anapoweza. Na kweli imenisaidia.” “Kwani siku hizi
hampo na Tino?” Jax akacheka na kunyamaza.
“Nini?” “Hapana. Hatupo tena pamoja.” Vile alivyomjibu akajua kuna
ambalo anamficha. Akaona aendelee kumdodosa. “Mbona aliniambia alikwambia
aliniona Mwanza!?” Jax hakujibu akaendelea kuendesha. “Mimi nilijua mpo kwenye
mahusiano kama zamani!” “Hapana. Tino alinichukia sana. Siku hizi ukiona
ananipigia simu, ujue ni kutaka kuniumiza tu.” Lara akakunja uso akionekana
hajaelewa. “Yaani akiwa na taarifa anayojua kama itaniumiza, basi ndipo
atanipigia. Anasema hataki hata kuonekana na mimi ili wote tusije onekana ni
wahuni. Akasema wasichana wanawakataa wakidhani wote tuna tabia zinazofanana.” Hilo
likamuumiza Lara.
“Na nafikiri ni kwa ajili ya Suzy pia. Amekusudia kumuoa Suzy, na
Suzy hanitaki kabisa. Alinifukuza pale mlipokuwa mkiishi na aliniambia nikija
kurudi pale ataniitia mwizi.” “Jax!” “Kweli. Sasa nafikiri ndio maana Tino
ananikwepa. Halafu pia nafikiri aliumia kuona dada Nelly amerudi kusimama na
mimi japo alimwambia hataki kuniona tena na hatajali hata kama Tula atanifunga
jela. Sasa dada Nelly akafanya kinyume kabisa na kunipokea. Tino ameacha hata
kufika pale nyumbani kwa dada Nelly na nilimsikia dada Nelly akisema ni kama
kuna siku alimpigia, hakupokea na hajamrudishia simu yake tena.” “Jax wewe!”
“Ndio hivyo.” Lara akazidi kushangazwa.
“Sasa yeye Tino alitegemea dada Nelly akuchukie moja kwa moja!?”
“Hata hivyo amenivumilia sana.” “Nani?” “Tino. Amenivumilia sana ndio maana na
mimi nimeona nimuache tu. Tokea chuo, amekua na mimi katikati ya fujo zangu na
Tula. Ashatukanwa sana na Tula kwa ajili yangu. Ndio maana hata alipokuwa akinipigia
simu akiniambia mambo ya kuniumiza, nilikuwa nikimuacha tu. Ila aliponipigia
kuniumiza juu yako akisema amekutana na wewe umependeza na upo na the god,
pale ndipo nilipomlaumu sana kushindwa hata kuchukua namba zako za simu. Ila
tuyaache hayo. Kwa Tino ninavuna nilichopanda, na nimemuacha kama kumpa
mapumziko tu. Nitakuja kumtafuta nitakapoweka mambo yangu sawa. Sitaki
niendelee kumchanganya na mambo yangu.” Hapo Lara akanyamaza akifikiria.
Walipokuwa wanakaribia Dar, akaona awe muungwana. “Najua haisaidii
Jax, lakini samahani juu ya Jerry. Sikujua kama ni mtu mliyekuwa mkimfahamu.
Alikuja kwenye maisha yangu na ahadi ya mapumziko tu bila kutaka mambo ya
undani, nikaona atanifaa kwa kipindi kile nahitaji kupumzisha akili.” “Sasa
akili zimeshatulia?” “Upo wewe Jax. Umerudi kwenye maisha yangu, naamini kila
kitu kitakuwa sawa.” Hilo likamfurahisha Jax. “Naamini tutakuwa sawa Lara.
Tutabakia sisi tu, na pengine Mungu ataturejeshea ule wakati tuliokua nao
zamani.” “Nimekusikia siku hizi unamtajataja Mungu!” Jax akacheka. “Siku hizi,
siku za jumapili kama tupo nchini, mimi na Nelly tunajitahidi kwenda kanisani
kama wakristo.” Lara akacheka. “Kwa kweli mmebadilika!” Angalau wakaendelea
kucheka mpaka wanafika nyumbani kwa Nelly.
Lara kwa Nelly.
W |
alikuta
Nelly amepika, meza imejaa. Amechoka mpaka uso unaonekana. Jax na Lara
wakamsalimia. “Vipi?” Ikabidi Jax kumuuliza. Alikuwa amepoa sana. “Nipo tu
sawa, ila nimechoka! Nilikuwa napika tokea alfajiri.” “Nilikwmbia nakuja tu na
Lara, si ndivyo?” “Nyinyi kuleni kitakachobaki tutaweka kwenye friji.”
Akasimama. “Lara karibu sana nyumbani. Acha mimi nikaoge, ndio nije
tuzungumze.” Lara na Jax wakamsindikiza kwa macho, Lara akamgeukia Jax. Jax
akapandisha mabega juu kama na yeye hajui. Akanyanyuka kumuwekea Lara kinywaji.
“Nashauri tumsubiri tule naye.” Lara akatoa ushauri. Jax akaona sio wazo baya.
Baada ya muda akatoka akionekana ameoga. “Mbona hamjala?” “Tumeona
tukusubiri.” Wakahamia mezani. “Mimi ni muwazi Lara, na sijajaliwa lugha ya
kulainisha maneno.” Akaanza Nelly akijipakulia chakula. Lara akaanza kuingiwa
hofu. “Swali.” Akaendelea Nelly. “Huyu Jax amekuumiza sana. Amekutenda vibaya,
lakini sasa hivi nakuona upo naye, kwa makubaliano gani?” Akamuuliza na
kumtizama. “Nataka kukusikia wewe maana yeye nimeshamsikia. Na ameniahidi ya
kwake. Amenionyesha kwa vitendo amejutia alilofanya. Sasa je, upo naye kwa
makubaliano gani?” Mwili mzima wa Lara ukaanza kutetemeka kwa hofu. Nelly ni
mkali na hapendi ujinga.
“Nampenda Jax.” “Kwa upendo uleule wa tokea mwanzo? Maana acha
nikwambie ukweli Lara. Tula sikumpenda kwa vile alivyokuwa akiishi na Jax. Sasa
wewe nilianza kuvutiwa na wewe kwa sababu Tino aliniambia wewe ni tofauti
kabisa na Tula. Sasa kwa hili alilokutenda Jax, unafikiri utaweza kuishi naye
kama zamani?” “Naamini hivyo dada yangu. Naamini hivyo. Ni kweli nimemsamehe
Jax ndio maana leo unaniona nipo naye. Na nipo naye kwa kuwa na mimi nilipenda
tulivyoishi naye mwanzoni. Na mimi nayatamani yale maisha yetu ya mwanzoni
kabla hajarudiana na Tula.” “Nilishaachana na Tula.” Hapo Jax akaingilia.
“Najua Jax. Ila ninachotaka kusema, sina shida yakupata mwanaume wa
kunioa, ila mtu ambaye nitaishi naye kama Jax. Ambaye ni Jax mwenyewe. Jax sio
mjeuri wala mbishi. Hajui kugomba na ni mtu mzuri. Najua atanipa ndoa nzuri
kama ya wazazi wangu.” Nelly akacheka. “Kweli dada. Mimi napenda ndoa kama ya
wazazi wangu. Wanakitu cha tofauti mbali na mali. Wanacheka mpaka unawasikia
chumbani kwao wakicheka na wapo wawili tu! Huwa sisi tunaambiana na kuwashangaa
ni nini wanachocheka miaka yote huwa hawamalizi! Na wanakumbushana stori za miaka
na miaka hawamalizi! Watu wanaoweza kukaa sehemu kwa muda mrefu na hawachokani!
Sisi huwa tunawashangaa, lakini ni kama tulivyoishi na Jax, japo Jax huwezi
kumlinganisha na baba yangu, ila ni kama tulivyoishi, tuliwakaribia.” Hapo Jax
akakunja uso.
“Kwamba mimi nimepungua kwa baba yako!?” Jax akauliza. “Namaanisha
yeye baba yupo na mama akiwa amemaliza. Na mwenyewe baba anasema hivyo ni tokea
mwanzoni.” Ndugu hao wakapoa. “Baba anasema alivyoamua kuwa na mama, hakuna
alichokuwa amebakisha. Kwa wazazi wake ambao walitaka amuache mama kwa kuwa
alichelewa kumzalia watoto na kuja kumzalia watoto wakike watupu, na akamaliza
hata kwenye vishawishi vya nje. Usemi wa baba ni kama alivyokwambia Jax.
Hasumbuliwi na vishawishi vya nje kwa sababu yeye aliamua kujifunga kwa mama tu.
Ndivyo walivyo tokea sisi ni wadogo mpaka leo. Na mimi natamani hiyo dada
yangu.” “Lakini mimi nimejirudi Lara!” “Si ndio maana nipo hapa, Jax!”
“Sasa mbona unasema ni kama sipo kama baba yako?” “Na wewe Jax tumia
akili acha kutaka sifa ambazo ulishaharibu. Lara hamjui Jax aliyejirudi. Mpe
muda aone kama kweli hutarudia kosa. Wewe vipi?” Nelly akawa mkali kidogo.
“Ndio mmerudiana kwa kosa la kumwingiza mwanamke mwingine katikati yenu,
umejirudi tu! Halafu eti unataka uanze kupewa sifa! Wewe vipi bwana? Ishi hata
miaka 10 mbeleni. Pata vishawishi na sisi tukuone umeweza kuvishinda ndipo
usifiwe.” Jax akanyamaza.
“Sitamnyanyasa Jax, dada. Mimi si mnyanyasaji na sipendi ugomvi
kabisa. Ni bora nikishindwa niondoke kuliko kuishi maisha ambayo hata mimi
hayanipi furaha. Siwezi na sijui ugomvi.” “Kwa hiyo unataka ndoa au unataka
kusubiri kwanza umchunguze?” Nelly akaongeza swali jingine na kuendelea. “Maana
mimi nimezungumza na Jax. Sitaki upuuzi. Asinitie shuguli ya kumuandalia
harusi, halafu aje anifanyie kama alichomfanyia Tino. Tino ametuchukia kabisa,
hataki hata kutusikia mimi na huyu shoga yake, sababu ya aibu aliyomtia hapa
mjini. Na ndio maana leo upo hapa, ili tuzungumze, tuwekane sawa.” Jax
akamshangaa dada yake.
“Nelly!” Jax akajikuta akishangaa kwa sauti. “Kabisa Jax. Sina muda
wa kupoteza, na sitaki mambo ya kubabaisha. Nilitaka afike nyumbani rasmi na
kutaka kupata naye muda kama huu nizungumze naye. Narudia tena, sitaki
vijimambo mimi. Jina langu na wadhifa wangu ndio nilichonacho hapa mjini. Sasa
sitaki drama. Sio niandae harusi, halafu mje muanze habari za ajabu.
Narudi kwako Lara, unataka ndoa? Na upo tayari kwa lini?” “Labda...” “Usiniingilie
Jax. Nilishazungumza na wewe. Ukanijibu maswali yangu yote mpaka nikaridhika.
Sasa hivi nataka kumsikia Lara. Usiingilie.” Nelly akamgeukia Lara.
“Mimi nataka ndoa na Jax hata kesho.” “Wewe mtoto!” “Nampenda Jax,
dada, wala sina sababu ya kusubiri. Mimi sijui unaishi na Jax wa namna gani, ila
mimi niliishi na Jax ambaye nilibaki nikimkumbuka mpaka kumuonea wivu Tula.”
Lara akaanza kulia. “Nilikuwa nalia natamani Jax
anichague mimi. Na hata nilipohisi ataniacha, pia nilikuwa radhi kumtunza mtoto
wake mimi mwenyewe nikijua atakuwa mtoto mzuri kama Jax.” Hapo akamgusa
sana Nelly na Jax mwenyewe.
Akajifuta machozi. “Na nimemuona jinsi
alivyokuwa akirudi kunitafuta pale nyumbani, naamini Jax hajabadilika. Na
ananihitaji mimi, ndio maana nipo hapa na Jax. Kama alivyosema Jax, naamini
Mungu ataturejeshea maisha yetu ya zamani.” “Yalikuaje?” “Dada Nelly!?”
Jax akashangaa sana. Wote wakacheka.
“Wewe unawasiwasi gani, mimi nazungumza na Lara?” “Sasa Lara si
ashakujibu! Unataka kumrudisha nyuma bwana!” “Wewe achana na mimi. Nijibu mwaya
Lara.” Lara akacheka kwa wasiwasi.
“Tulikuwa hatuna mengi. Halafu tunaishi uswahilini tu. Joto. Chumba kimoja
halafu kumebana! Lakini dada, ungetamani kuwepo kwetu.” “Hata Tino alikuwa akisema.
Lakini akawa anasema eti hana jinsi ya kueleza.” “Hata mimi sina jinsi nzuri
dada yangu, ila kulikuwa na utulivu. Jax hana makuu.” “Mimi nahisi ni wewe tu.
Huyu Jax sijui kama...” Jax akacheka na kutingisha kichwa. “Mimi ni mtu mzuri
sana, dada yangu.” “Mmmhh!” Nelly akaguna na kusimama kufuata barafu kwenye
friza.
Jax akashangaa anatafuna barafu na si chakula. Akashangaa kidogo ila
akaona amuache tu. “Sasa mimi nimeambiwa unataka harusi ya kanisani na uvae
tena shela.” “Kabisa dada yangu.” Nelly akacheka na kutingisha kichwa. “Huoni
aibu?” “Dada Nelly!” Jax akashituka sana. “Hata kidogo dada. Naolewa na Jax!
Nilimkubali tokea mwanzo na ndiye huyohuyo ananioa! Sina sababu yakujificha
dada. Wakati mwingine natamani angekuwa si yeye Jax, awe mwanaume mwingine
tuliyeishi naye kwa fujo. Lakini Jax alikuwa ananipenda. Ananitangaza mpaka kwa
marafiki zake! Hanifichi! Anataka watu wajue mimi ni wake! Napata wapi mwanaume
kama huyo dada?” Hapo Nelly akapoa. Akakumbuka alivyomkatalia Billy asifahamiane
na Jax. Akatulia kabisa wakamuona amepotea kabisa pale.
Jax akamkonyeza Lara. Akajua anatakiwa kuaga, kwani ni sauti ya
barafu tu alizokuwa akitafuna Nelly ndiyo iliyokuwa ikiendelea kusikika hapo.
“Nashukuru kwa chakula dada yangu.” Nelly akamwangalia. “Hivi na wewe
utaendelea kuniita dada mpaka lini?” Lara akacheka. “Mimi ni dada yake Jax tu.”
“Haya dada, nimesikia.” Wote wakacheka. “Ni wifi.” Lara akarekebisha. “Haya.
Mimi nitaanza maandalizi ya harusi. Naamini tutafanikiwa.” “Nashukuru dada
yangu.” “Na mimi nashukuru kwa kila kitu
dada...wifi yangu.” Wakacheka. “Na asante kunikaribisha nyumbani. Nimefurahi na
asante kwa chakula.” “Nimepika kingi nikiwa na mawazo. Unachotaka kuchukua,
mwambie Jax akufungashie uende nacho.” Akasimama na kutoka hapo kama kuwapisha
wawili hao.
“Wala sijivungi. Ndio dada Nelly anapika vizuri hivi!” “Amekwambia
uache kumuita dada.” Wakacheka. “Wewe nifungashie chakutosha, nikale huko
niendapo.” Jax akamsaidia na kutoka. “Unarudi au unalala kwako?” “Narudi dada
yangu. Nampeleka tu na kurudi.” “Ikitokea unabadili mawazo huko, naomba
unijulishe, usiniache nikeshe nikikusubiri.” Jax akacheka akitingisha kichwa.
Akatoka na Lara.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jax na Lara wakatoka hapo. “Nakushukuru kwa kunizungumza vizuri kwa
dada yangu.” “Ndivyo ulivyo Jax. Wewe si mgumu kuishi pamoja.” “Nafikiri
tuliendana tu Lara. Haikuwahi kuwa hivyo kwa Tulla. Kila wakati alikuwa na kitu
cha kunilalamikia. Ndio maana na mimi nilikuwa nikikukumbuka.” Wakatulia mpaka
nyumbani kwa Jax. Jax akamtambulisha tena getini kuwa yeye ndiye atakuwa
akiishi hapo. Kisha akamsaidia kubeba mizigo, wakaingia ndani. Lara akacheka.
“Naona umebadilisha hapa ndani.” “Nimeweka tu tailizi/marumaru nyeusi
na kubadili rangi. Umependa?” “Sana. Aina hii ya marumaru ni nzuri.” “Na garama
pia. Ila nimeona itapendezesha nyumba zaidi. Karibu.” Akamuona anamuingizia
vifaa vyake chumba kingine. Lara akafuata nyuma. “Kile chumba kingine bado kina
vitu vyangu. Zaidi nguo. Huwa nakifunga kabisa mpaka niwe nakuja kubadili nguo.
Au ungependa kutumia kile ambacho kina bafu ndani? Maana hivi vingine
nivyakuchangia choo. Masta ni kimoja tu.” “Popote Jax. Mimi sitachagua. Ilimradi
umenipa hifadhi, nashukuru.” “Nikwambie ukweli Lara?” Lara akaweka vitu chini
na kumwangalia.
Alimjua Jax ndio jinsi ya zungumza yake. Anataka mtu amsikilize kwa
kumwangalia. “Sikutaka kabisa urudi kuishi kwa kina Suzy. Ndio maana ilinibidi
kuharakisha uje uishi hapa. Wale wasichana wamenivunjia sana heshima.” Lara
akanyamaza. “Najua nilikosa, lakini sikupenda walivyonibadilikia.
Walinibadilikia kwa kunidharau sana. Zaidi Suzy! Sikutaka kuja kurudi tena pale
hata kwa kuja kukuona wewe.” Lara ndio akaelewa kuwa hataki kuja kuwaona hata
pale. “Nimeelewa Jax.” “Ni kwa muda tu. Acha sisi tukae kwanza sawa. Mambo yetu
yaeleweke ndipo hata tukirudi kwao, iwe tumeleta maana kwenye jamii. Najua kwa
hakika Tino atakuwa amewashirikisha mambo yako pia na Jerry.” Hapo Lara akakosa
nguvu kabisa.
“Ndio maana naona tutulie mpaka tujipange sisi wenyewe kwanza, ndipo
tuwatafute.” “Nimeelewa Jax.” “Ila watu wa nyumbani wanakaribishwa muda na
wakati wowote ule. Nilimsikia Lea akikwambia usimsahau.” “Lea anataka na yeye kuja
kujaribu maisha huku Dar. Sasa nilimwambia pengine mpaka nipate mahali pakuishi,
pakueleweka ndio nitamuita.” “Basi uwe huru.” “Kweli Jax!?” “Kabisa. Hapa ni
kwetu. Kuwa kuru.” Lara akamsogelea kumpa busu la shukurani, ikawa kosa.
Yakaanza mabusu kwa wawili hao. Lara akanogewa. Alikuwa na hamu na
huyo Jax wakisubiria fungate. Jax naye akaona asimkumbushe swala la kusubiri.
Yakaendelea mabusu ya haja kwa wawili hao waking’ang’aniana. Yalipotaka kuanza
tu mapenzi, Lara akagutuka. “Hapana Jax.” “Lara!” “Kweli Jax. Naomba na safari
hii uwe mvumilivu kwa hakika. Sio utoke hapa uende ukatafute kwengine.
Ukishindwa safari hii basi.” “Nimesubiria kwa muda mrefu Lara! Nihurumie mpenzi
wangu. Nakutamani wewe. Nimekaa muda mrefu sana bila ya...” “Sasa wewe utakuwa
ukifanyaje nikiwa najifungua?” “Mimi si mdhaifu wa ngono kiasi hicho Lara, na
wewe unanijua. Ilimradi nipate mara moja tu, basi natulia. Na nakuahidi sio
kwamba na...” “Bwana ondoka Jax! Unanifanya nianze na mimi kukutamani wakati
tulikubaliana mpaka mbele ya mama kuwa tutasubiri.” “Wewe ndio ulikubali,
lakini mimi sikusema kitu. Nilikubali maombi. Na ninakuahidi hakutakuwa na
mwingine badala yako.” “Toka Jax.” Lara akamsukumia nje kabisa, Jax akicheka.
Usiku huo wakafanikiwa. Jax akaondoka.
Alhamisi.
N |
elly
akajifikiria, akaona aende tu hospitalini. Akadamkia ofisini. Akafanya vikao
vyake vyote mida ya asubuhi, kwenye mida ya saa tano, akatoka hapo kuelekea
hospitalini. Alikaa huko mpaka mida ya saa saba. Akaona simu ya Billy ikiingia.
Alishituka karibu atupe simu. Ikaita mpaka ikakata. Ikaita tena, Nelly hakujua
amwambie nini. Ikakata akiitizama. ‘Tafadhali pokea
simu yangu.’ Ujumbe ukaingia na simu ikaanza kuita tena. Safari hii
akapokea. “Uko wapi?” Nelly akatulia. “Nelly?” Kimya akimsikiliza Billy. “Umetoka ofisini tokea asubuhi na hakuna anayejua ulipo. Si
kawaida yako. Uko wapi?” “Hospitalini.” Nelly akajibu. Pakazuka ukimya
kidogo.
“Wapi?” “Nakaribia kumuona daktari. Namba yangu imekaribia.
Bado watu wanne tu mbele yangu. Nikitoka hapa narudi ofisini.” “Sio jibu la
swali langu.” Nelly akatulia
akifikiria. “Nelly?” “Nafikiria.” “Ulipo!?” “Kama uje
au la.” “Kwa nini?!” “Nitakuja kukwambia. Ila kwa sasa naomba muda Billy. Kuna
jambo nataka likikaa sawa ndipo nikutafute.” “Sawa. Lakini nataka kujua ulipo.”
“Si nimekwambia naomba muda!?” “Na mimi si nimesema sawa? Kwani tokea lini
ninachokitaka mimi ndicho unachokitaka wewe?” “Ni kwa nini unakuwa mtu wa
kung’ang’ania maamuzi yako hata kama...” “Unapotezea muda Nelly. Uko wapi?”
Nelly akamuelekeza.
Billy anafika hapo na namba ya Nelly ikawa ndio imefika anaingia
kumuona daktari. Na yeye akaingia bila kuomba ruhusa. Nelly akawa anamkabidhi
dakitari baadhi ya makabrasha aliyokuwa nayo baada ya vipimo vya awali kwa
manesi. Kabla yule daktari hajashika yale makabrasha vizuri, Billy akampokonya
makabrasha yote na kuwashangaza Nelly na yule daktari. Akaanza kusoma.
“Nelly anaumwa nini?” Billy akawa anauliza huku akisoma. “Pressure
ipo juu, ndio maana daktari aliyemuona mwanzoni amemshauri aanza kliniki mapema
ili kuhakikisha yeye na mtoto wapo salama.” Yule daktari alimjibu kwa lugha ya
kingereza kama anavyoongea Billy. “What!?” Billy alishituka na kumwangalia
Nelly kwa mshangao.
“Naomba mkabidhi daktari hilo faili na umuache amalizie, tutoke hapa.
Nataka kurudi kazini.” “Kwamba ni mjamzito, halafu huniambii!?” “Kwani wewe
ulipanga kuzaa na mimi? Mimba ipo kwangu, wewe unashituka nini?” “Umenikosea
sana Nelly.” Nelly akashangaa sana. “Wewe vipi Billy?” “Kwa upande wa Jax sina
amri nako. Ila linapofika swala la mtoto wangu, mimi nina jukumu la kujua.”
“Sasa ningejuaje kama unataka?!” “Uliniambia, nikakataa?” Daktari akabaki
akiwaangalia watu wazima hao.
“Eti Nelly?” “Acha kugomba hapa kama baba aliyekuwa amekaa kwenye
ndoa mika 50 hajapata mtoto wakati wewe ni baba mwenye watoto wakubwa kabisa.”
“Nelly?” “Ni nini Billy wewe? Hivi unajua na mimi ndio nimejua leo kama ni
mjamzito? Hivi unajua hofu niliyoipata baada ya kujua mimi mtumzima ni
mjamzito?” Hapo Billy akatulia kidogo. “Niliingiwa hofu nusu kuzimia ofisini
kwa daktari baada yakusikia hali ninayojisikia ni ujamzito! Hata sikujua
mtumzima kama mimi naweza kushika mimba! Nipo hapa sasa hivi baada yakupewa
mapumziko mafupi sababu ya mshituko. Tafadhali acha kuniongezea hofu Billy.”
“Samahani.” Hapo Billy akasikika ametulia ila na mshituko.
“Kwanza inakuaje mtumzima kama mimi nashika mimba jamani?” Akamgeukia
daktari akilalamika. “Maadamu hujakoma hedhi, unaweza kushika mimba.” “Huyo
mtoto atazaliwa salama kweli? Maana nilisikia ukiwa mtumzima ukishika mimba
unaweza zaa mtoto tahira. Au hata kufa. Kufa mimi mwenyewe au..” “Naomba utulie
Nelly?” Billy akamtuliza. “Hivi unajua umri wangu wewe Billy?” Nelly akamuuliza
Billy kwa ukali. “Unajua majukumu niliyonayo mimi? Sina muda na kubeba mimba.
Halafu sina moyo wakulea mtoto.” Isivyo kawaida yake, Nelly akaanza kulia hapo.
Homoni za mimba zikamsaidia kulia bila shida. Akalia hapo akijieleza hili na
lile jinsi asivyotaka yeye mtoto, mwishoe wakatoka bila hata daktari kuzungumza
chochote, ila wao wenyewe kubishana hapo na Nelly kulia na kuamua kutoka kabisa
hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba niache mimi nirudi kazini. Usinifuate Billy. Nataka nirudi
kazini.” “Ulisikia kitu chochote kama pressure ipo juu?” “Kwa hiyo?” “Naomba
ukapumzike kama daktari alivyokuandikia mapumziko.” “Haijawahi kutokea nalala
siku ya kazi. Na hii mimba haitanifanya hivyo.” “Labda mimi niulize, unapingana
na nani sasa hapa? Uhalisia?” “Nyinyi ndio mnataka kuonyesha mwanamke hawezi
kuzaa na kufanya majukumu mengine. Mimba si ugonjwa wala haimfanyi mwanamke
akashindwa kufanya majukumu yake.” Billy akaanza kucheka.
Nelly akaanza kulia. “Maisha yangu
yameshabadilika. Ndio nimetoka tu kumwambia Jax juu yako, leo narudi tena na
mimba! Hakika si..” “Kabla hujaweka mipango migumu. Acha mimi
nikupongeze kwa hatua ngumu ya kunitambulisha kwa Jax.” “Acha kunikejeli Billy!” Nelly akazidi kulia. “Hakika homoni
leo naona zipo juu sana. Nashauri ukapate mapumziko Nelly. Unahali mbaya!” “Tafadhali usiendelee kucheka Billy.”
“Nakuhakikishia utakuwa sawa Nelly.” “Unajuaje?
Nimemuharibia Jax maisha, unafikiri nitawazaje kuwa mama kwa huyu mtoto?”
“Hapo nimeelewa wasiwasi wako. Sasa twende ukatulie halafu nikwambie kitu.”
“Sitaki. Wewe niambie sasa hivi.” “Wewe unamoyo wa umama, Nelly.” “Kweli Billy?” “Kabisa. Huoni jinsi unavyomlinda
Jax kwa kila baya?” “Kwa hiyo?” “Huo ndio
moyo wa kimama. Umemfikisha Jax pale alipo! Hudhani umefanya jambo zuri?” “Kwa hiyo nisitoe hii mimba?” “Kama ni mtoto wangu
tafadhali usimuue. Kama ni mimba ya mwingine, nashauri pata naye muda
wakuzungumzia hilo, napo sishauri uue kiumbe kisicho na hatia.” Nelly
akanyamaza.
“Twende ukapumzike nyumbani.” “Nikirudi nyumbani ndio pressure
itapanda. Acha nirudi ofisini ndio nitaamini sina cha kupoteza.” “Hivi unajua
kinachokutokea Nelly?” “Maisha yangu kubadilika?” “Hapana. Yaani sasa hivi hapa
tunavyozungumza, ndani ya tumbo lako, kuna maisha ya mtu mwingine yanaendelea.”
Nelly akatulia akitafakari. “Yaani ni hivi Nelly, hapo ulipo, ndani yako kuna
maisha zaidi yako wewe. Kipo kiumbe kimefichwa na Mungu, anakitengeneza. Kwamba
ni hivi, Mungu ameangalia kwa wanawake wote, akakuchagua wewe akiona unafaa kwa
kiumbe hicho kukua kwako na wala si mwanamke mwingine. Na Mungu huwa hakosei.”
“Unauhakika?” “Kwa asilimia 100. Mungu huwa hakosei Nelly. Kinachoendelea kwako
sasa hivi ni mpango wa Mungu kwa asilimia 100. Tulia, mwachie Mungu.” Nelly
akatulia.
“Kama kurudi ofisini ndio kutakufanya ujisikie vizuri, basi turudi
ofisini.” “Acha nirudi ofisini tu. Ndio nimejua leo, acha nipokee taratibu hizi
taarifa Billy. Sijui maisha mengine bila kazi. Kwenda kulala sasa hivi nyumbani
na jua kali hivi, presure ndio itapanda zaidi.” “Sawa.” Wakatoka hapo kurudi
kazini, Nelly akiendesha mwenyewe Billy amekaa pembeni. “Nimekumiss Nelly, ndio
maana nilikupigia.” Nelly akamwangalia. “Mimi nakupenda.” “Najua Billy, lakini
na mimi sikujua kama nakupenda mpaka nilipoondoka kwako. Kipindi hiki sijui cha
siku 4 mbali na wewe, ndipo nilipojua nakupenda Billy.” Nelly akaendelea.
“Mchumba wa Jax amerudi. Nilipata naye muda yule binti, ndipo
nikajisuta.” “Kwa nini?” Billy akauliza. “Aisee upo upendo Billy, na
nimejifunza kwa wale watoto! Nilishindwa kulala. Ikabidi kumuamsha Jax jana
usiku nikamwambia nakupenda.” Billy akacheka. “Jax alihisi naota. Lakini
nikamwambia tumekuwa tukitoka, na nikamwambia alikuwa sahihi. Uko upendo huko
nje, ila hatukuwa tumebahatika. Nikamwambia nahisi safari hii nimebahatika.
Mimi na wewe tumegombana kwa mimi kutokua tayari kukutambulisha kwake. Jax
hakuamini kama upo tayari ujulikane kwa watu.” “Na si kwa watu tu, mama yangu
anakufahamu Nelly. Binti yangu mkubwa pia anakufahamu. Nakupenda Nelly, na
sitaki kukuficha.” Nelly akamwangalia na kurudisha macho barabarani.
“Unajua nimemwambia mama inawezekana wewe ndiye niliyekuwa
nimeandikiwa na Mungu tokea mwanzo?” Nelly akashangaa sana na kumgeukia.
“Nakupenda Nelly. Na Mungu anajua nakupenda. Tunakuwa na furaha tukiwa wote.
Tunakuwa na wakati mzuri. Unanifanya akili zinatulia, siwi kama mtu
unayetegemea niwe kwenye kiwango kikubwa. Umeridhika na mimi kama Billy
mwenyewe humtaki Billy mwenye hela au cheo. Nakupenda Nelly.” “Tutafanyaje na
huyu mtoto Billy? Hakika mimi sipo tayari na vitoto vichanga. Nahofia
kuharibu.” Billy akatulia akifikiria. Akanyamaza kabisa kama na yeye ndio
anapata nafasi ya kutafakari juu ya hilo.
“Unataka tuwe wote ofisini?” Billy akavunja ukimya wakati wakikaribia
ofisini. “Hapana Billy! Mimi nakwenda kufanya kazi.” “Naruhusiwa kukutembelea
nyumbani?” Nelly akanyamaza, hakujibu hilo. Akamuona anatoa simu na kutoa
maagizo afuatwe ofisini kwa Nelly. Akajua anazungumza na dereva wake. Akamuacha
tu na kuendelea kuendesha mpaka ofisini kwake. Wakaachana hapohapo.
Jioni mida ya saa kumi na nusu akamtumia ujumbe Billy. ‘Nakukaribisha nyumbani. Itakuwa vizuri uje hapa, tuondoke
wote.’ ‘Nashukuru.’ Billy akarudisha huo ujumbe akiwa amefurahi sana. Akajua
Nelly amepata muda wakufikiria na kuamua.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Saa kumi na mbili kasoro Billy akawa amewasili ofisini kwa Nelly.
“Unajisikiaje?” “Kwenda nyumbani. Nifikie friji, nipate barafu, nitafune.”
Billy akacheka sana. “Hakika nimekamatika mimi!” “Lakini Nelly, niambie
umebakiza nini kwenye maisha?” “Sijui Billy. Ila nafikiri pia sijiamini kama
naweza kuwa mama, ila hii kazi. Kuhudumia kiumbe ni ngumu Billy, bora kazi.”
“Kwa sababu unauzoefu wa kazi wa muda mrefu ila si kubeba mimba, kuzaa na
kulea. Naamini utakuwa tu sawa. Jipe muda.” Wakatulia kama wote wamepatwa na
kibumbuazi.
“Twende ukapumzike.” Billy akasimama kabisa. “Lakini Billy, naomba
usijisikie kama una jukumu na huyu mtoto. Najua ni kitu ambacho hukupanga. Hata
mimi pia sikupanga. Kwanza sikujua kama kwa umri wetu tunaweza pata mtoto.
Nimekaa hapa nikiwaza, nikamkumbuka Lara jinsi alivyolilia mtoto wake. Hata
jana alimzungumzia kwa upendo. Nimejisuta. Nikajiambia kama mtoto kama yule
alikuwa tayari kulea mwanae kwa upendo vile, tena akiwa hana uwezo kama wangu,
nashindwaje mimi!” Billy akatulia.
“Unanisikiliza Billy?” Akawa kama amemtoa mawazoni. “Billy?” “Nipo
Nelly.” “Najua upo. Na ninaelewa ni jukumu kubwa. Tafadhali usione unawajibika
kwa namna yeyote ile.” “Nahitaji na mimi muda, Nelly. Swala la mtoto mwingine halikuwahi kupita akilini mwangu. Hizi ni habari mpya
kabisa, ila siyo mbaya. Ila nahitaji tu muda.” Nelly akanyanyua mizigo yake.
“Twende.” Wakatoka hapo, wote kimya mpaka nyumbani kwa Nelly.
Nyumbani Kwa Nelly na Jax.
Akamuona Billy anacheka. “Sasa unacheka nini?” “Hivi unajua kwamba
Jax ni baba mkubwa na anakaribia kuoa?” Akamuelewa. “Ila hana mfano wa kuiga au
mtu wa kumwangalia ila mimi. Hana nyumbani, isipokuwa hapa. Sijui kama
unanielewa Billy?” “Nakuelewa na ndio maana nashangaa jinsi unavyojitilia
mashaka kwenye swala la umama. Unaweza Nelly na utakuwa mama mzuri tu.”
Wakatulia garini nje ya nyumba, mwishoe Nelly akaona washuke.
“Tuingie nikutafutie chakula kabla hujakwenda kulala. Karibu.”
Wakashuka garini, kwa mara ya kwanza Billy akakaribishwa hapo wakati yeye Nelly
alikuwa akilala kwake. Akaenda kukaa sebuleni. “Nina wazo la tofauti. Badala ya
kupika, naomba tuagize chakula, ili wewe upumzike leo.” Nelly akabaki
akifikiria. “Dereva atakileta hapa muda na wakati tutakaomwambia. Niambie
unahamu ya kula nini.” Nelly alikuwa
akijisikia kuchoka, akamshukuru Mungu wake. Akavua viatu na kwenda kujinyoosha
kwenye kochi. Billy akahamia hapo kwenye kochi, akamnyanyua miguu na kuanza
kumchua. Nelly akajiweka sawa na kutulia.
Wakati wapo kwenye ile hali, Jax akaingia. Alikaribia kukimbia,
akabaki amedua. Ni Nelly na bosi wa mabosi zake, amepakata miguu ya dada yake
akiichua! Kimya kikapita kwa muda, akapitiliza hapo bila salamu mpaka jikoni.
“Ulifanikiwa kwenda hospitalini?” Akamuuliza dada yake akiwa jikoni. “Ndiyo.”
Nelly akajibu. “Wamekwambia nini?” Jax akauliza kwa sauti ya juu tu. Kimya.
“Nelly?” “Ni ujauzito.” Nelly akajibu, wakasikia glasi imeanguka huko
jikoni. Kimya. Nelly akajua ameshituka sana. Billy akamuona Nelly anafunga
macho kwa masikitiko.
Baada ya muda Jax akatoka jikoni na kurudi pale sebuleni kwa dada
yake. “Utakuwa mama mzuri Nelly. Hongera.” Mpaka Nelly akaanza kulia. “Aisee naogopa sana. Iweje nimuharibie kama wewe?”
“Kwani wewe ukiangalia unaona maisha yangu yameharibika?” Jax akamuuliza vizuri
tu. “Nina kazi nzuri na mchumba mzuri tu, na nimekuahidi natulia. Sasa ni nini
unaona kimepungua? Utakuwa sawa kabisa, usiogope, na mimi nipo kukusaidia.” “Kweli?” “Kabisa. Huyo mtoto amebahatika kukupata
wewe kama mama. Anauhakika wa kuwa mtu mzuri kwenye jamii na anauhakika wa mtu
wa kusimama naye hata kama wengine watamchukia.” Nelly akacheka akijifuta
machozi. “Halafu pia amebahatika kupata mjomba mzuri sana. Na Lara atakuwepo.
Sema tunaweza kumuharibu kwa kumdekeza.” Angalau wakacheka. Nelly alishashusha
miguu vile ilivyokuwa imepakatwa na Billy.
“Mimi nakwenda kulala kwangu. Nimekuja kuchukua vitu baadhi,
naondoka.” Jax akawa muungwana, na kuamua kumpisha dada yake. Aliona haitakuwa
sawa kwao kama ataendelea kuwepo pale. “Hutakula kwanza?” “Lara amepika.
Nitakuwa sawa, asante.” Akataka kuondoka, Nelly akamuita. “Huyu ni Billy, na
Billy huyu ni Jax, mdogo wangu.” Wote wakacheka. Jax karudi na kumpa mkono.
“Karibu nyumbani.” “Asante.” Jax akarudi jikoni akaenda kumletea dada yake
barafu. Nelly akapokea kwa furaha sana. “Yaani nilikuwa nikiziwaza hizi barafu
siku nzima!” Akaanza kutafuna. Jax akacheka na kutoka hapo. Akaanza kukusanya
mizigo yake tena. Ila Nelly alijua wazi hakuwa na mpango wa kuondoka hapo,
akamuacha tu. Akapakia kwenye gari mpaka akamaliza. Akarudi. “Mimi sijui
kupika. Niagizeni chakula chochote nikanunue. Nelly, najua anachopenda.”
“Tumeshaagiza Jax. Asante.” Jax akaaga na kuondoka hapo akiwapa nafasi.
Kwa Lara.
Lara akashangaa Jax waliyeagana wakikubaliana watapigiana simu wakati
wa kulala, anaingia na mizigo yake. “Kwema?” Ikabidi amuelezee Lara. “Mimi
naona umefanya jambo la busara Jax. Mpe nafasi na yeye aishi kidogo.”
Wakatulia. “Acha kuniangalia hivyo bwana Jax!” Jax akacheka sana. “Mimi mbona
sijakuangalia tofauti!” “Hapana Jax.” Lara akanyanyuka kabisa hapo sebuleni na
kukimbilia jikoni, Jax akicheka.
“Nenda ukaoge uje kula, au ule ndio ukaoge, ulale.” “Acha nioge
kwanza.” Jax akaingia chumbani kwake kwenda kuoga, lakini akatoka na taulo tu.
“Jax jamani!” “Mimi nimefanyaje Lara?” “Kavae nguo bwana!” Jax akazidi kucheka.
“Mimi nipo sawa kabisa Lara, sina shida na hili taulo.” “Unanitamanisha
makusudi, bwana!” Lara akalalamika. “Wewe jikaze mpaka siku ya harusi. Usiwe na
wasiwasi.” Lara akaacha kumuangalia. Akaendelea kupanga chakula huku
hamuangalii. “Nikusaidie?” “Sitaki Jax, na naomba usinisogelee.” “Kwani wewe
unaogopa nini?” “Usije bwana Jax!” Jax akamsogelea na karibu kabisa na kumshika
kiunoni.
Lara akamgeukia vizuri. “Nikwambie ukweli Jax?” “Nakusikiliza.” “Ni
kweli nakutamani. Sana tu. Tena nilikuwa nikiwa na Jerry, namkumbuka Jax wangu.”
Jax akatulia akimsikiliza. “Ila kuna kitu hapa, nakitengeneza kwa shida
sana.” Lara akajionyeshea moyoni. “Na si moyoni tu. Nafsini mwangu, akilini au
mimi kwa ujumla wangu.” Akamuona Jax anakunja ndita kidogo kama ambaye ameanza
kumpoteza. “Natengeneza kitu ambacho nataka kije kuwa msaada hata kwenye ndoa
yangu na watoto wangu. Najijengea tabia ya kujiwekea mambo na mimi mwenyewe
kuyasimamia mpaka yatimie. Hata katika ugumu vipi, basi nisijipinge. Nataka kuwa
na tabia kama mama yangu, Jax. Mama ambaye anasifiwa na msimamo wa mambo. Anayeweza
kusimama na mwenzie hata katika magumu.” Lara akajisogeza pembeni.
“Baba akikwambia anajivunia mama, amini Jax. Unamuona vile mama yetu
ni mzuri mpaka leo, na nyumba anayoishi au maisha aliyokuwa akiishi na baba
kabla sijawafungulia lile duka. Maisha ya chini kabisa. Baba akikwambia wanaume
matajiri kwenye ule mji wanamsumbua mkewe, ni kweli. Wanamsumbua mpaka leo
wakimpa vishawishi mbalimbali, lakini mpaka sisi tunashangaa Jax! Mama hashawishiki
hata kwa zawadi ya gari, Jax! Na ametulia na mumewe hana hata wazo la pili. Sasa
ile sio tabia ya kuweza kuiishi kwa kwenda tu kanisani au kuombewa. Ni tabia
inatakiwa kujengwa. Kujenga stamina. Kwamba kweli kuna kitu kizuri
kabisa. Unahitaji. Na pengine hakina madhara kibinadamu.” Lara akaendelea.
“Kwa mfano kama hivi sisi ni wachumba mpaka wazazi wanajua. Tunatamaniana
kabisa, na tunaweza kufanya chochote kile tunachotaka sasa hivi. Lakini si sawa
Jax. Si sawa na wala hatuna hadhi ya kuishi maisha ya ndoa iliyotushinda
kuifikia tena si kwa ugumu, ila kwa kuchagua kutofikia lengo! Sisi wenyewe
tulishindwa kujikaza na kufikia ndoa. Eti leo watu wote wakijua tulishindwa
kusimamia mipango yetu sisi wenyewe, halafu eti huku nyuma ya pazia, tunaishi
ndoa ambayo tuliikataa! Si sawa mbele ya macho ya wazazi wangu, na Mungu zaidi.”
Jax akapoa mpaka mzee akashuka kabisa.
“Samahani Jax. Nataka kuwa mke mzuri kwako au yeyote atakayefanikiwa
kusimama na mimi kanisani na kupeana viapo.” “Ni mimi Lara.” “Nashukuru Jax. Basi
ujue nataka kujijengea tabia ambayo hata kama kesho wewe unatatizo, hujiwezi
kwa uzima au hata mali, basi niwe mtu wa kusimama na wewe. Na sitaki
nijifunze wakati huo wa tatizo, ila nijijengee hiyo tabia kuanzia sasa.”
Lara akaendelea taratibu tu kama ambaye hajakurupuka, asijue huyo binti
alishakalishwa chini na mama yake, akazungumza naye sana tena kwa kituo. Baada
ya kugundua hata mkono huo si ajali, alivunjwa na mwanaume. Hakumwambia kama anajua
anadanganya. Ila mama Chiwanga akafunga na kumuombea binti yake, mpaka akapata
hekima ya kuzungumza naye kwa kituo mpaka vikamuingia Lara moyoni.
“Nimekuwa mtu wa kutoka kitanda kimoja hadi kingine na wanaume ambao
wote hawajawahi kunioa. Nimebakiwa na idadi zao tu! Wao wametumia mwili wangu,
ndoa wamewapa wanawake wengine, mimi nimebaki na idadi zao pamoja na majina yao
tu.” Lara akaendelea. “Naomba nivumilie Jax. Acha nijifunze kuwa na msimamo
kwenye mambo yangu mwenyewe kwa kuwa mwenzio sitakudanganya wala sitaona aibu kama
wanawake wengine. Mimi nataka ndoa ya kanisani. Na hilo nalijua toka mtoto, halijawahi
kubadilika moyoni mwangu. Najua kwa hakika nini nataka. Sasa kwa nini huwa
najipinga mwenyewe? Ni kwa kuwa sina huo uwezo. Ndio sasahivi nataka kujifunza
kama mama yangu. Katika shida na tamaa zote na uwezo wakuweza kukipata hicho
kitu, lakini kama si sahihi, basi niweze kujiambia mwenyewe hapana au subiri.”
Jax akajirudisha nyuma kabisa.
“Na si tabia ya kujengwa kwa siku moja kama mama anavyosema. Mama anasema
kuna tabia zinajengwa kama vile mwanamazoezi anavyokwenda gym. Ile misuli haitengenezeki
kwa siku moja. Anasema kuna siku huwa wanachoka na kukata tamaa. Ila kama lengo
ni misuli, unakuta lazima warudi, waendelee na mazoezi mpaka misuli itokee. Na
mimi nataka hiyo Jax. Nataka na nimekusudia kuweza.” Jax kimya. “Naomba na wewe
ujiulize Jax, kama nikivunja hili kwa kukutamani sasa hivi, nitaendelea kuvunja
mangapi kwa wengine.” “Basi nimeelewa, Lara. Tusubiri wote.” Jax akarudi
chumbani kuvaa.
Akatoka na kumkuta Lara akimsubiria mezani. Akamuona amepoa hata
usoni hamwangalii kwa ujasiri. Lara akamuhurumia. “Nikwambie Jax?” Akamwangalia.
“Nyumbani kwa wazazi wangu wanafanya ibada kila siku usiku palepale nyumbani
kabla ya kulala. Tunaweza kuanza na sisi.” “Sawa.” Jax akakubali. “Lakini
itabidi wewe uniongoze Lara. Mimi ni mkristo jina tu.” Lara akacheka, angalau
wakabadili agenda. Wakaanza kuweka mikakati kwenye hiyo nyumba yao.
Kwa Nelly.
Ukweli Billy alikuwa kwenye mshituko kama ambaye hajui chakusema na
hawezi kukimbia. Ikawa kama amepigwa tu na butwaa. “Naomba nikwambie kitu
Billy.” Billy akatoa macho kwenye luninga, Nelly akijua wazi hakuwa akielewa lililokuwa
likiendelea kwani aliweka kwa lugha ya
kiswahili ambocho Billy huweza kuokota maneno machache sana na kutumia akili
kuyaunganisha ili kuelewa.
“Hili ni jukumu langu kwa asilimia 100 kwa kuwa ni mimi mwenyewe ndiye
niliyeruhusu hili litokee. Kwanza sikuwa nikijua kama watu wa umri wetu
tunaweza kushika mimba.” “Usijichanganye na mimi. Wewe bado ni mdogo Nelly.”
“Kwa nini wewe unafikiria mtoto atakuwa ni wako Billy!?” “Ni wa nani?” “Siwezi
kukwambia.” “Kwa nini?” “Kwa sababu sina uhakika.” Billy akamtizama kwa
kumsuta.
“Huyu mtoto si wako Billy.” “Uliniahidi wewe hutanidanganya, Nelly.” Akawa
kama amembana. Nelly akababaika lakini akapata jibu. “Mimba zinaweza kushikwa
kwa njia nyingi sana. Hata kwa kukaa chooni. Unaweza kukalia mbegu za kiume,
ukashika mimba kama ni siku zako za kushika mimba. Kwa hiyo anaweza kuwa mtoto
wa yeyote yule.” “Unakumbuka lakini ulivyosema wewe hutakuja kunidanganya?”
“Ninachotaka kukusaidia Billy ni kuwa, usijihisi unahusika na huyu mtoto.
Usijihisi nimekuingiza kwenye jukumu zito ambalo hukuwa umepanga kuja kufanya
tena maishani. Mimi nawajibika kwa hili kwa asilimia 100, nitawajibika.
Tafadhali naomba uondoke.” Nelly akambadilikia.
“Unazungumza nini wewe?” “Biashara au mchezo wowote uliokuwa
ukiendelea katikati yetu, nausitisha kuanzia sasa. Sitaki tena na ninaomba
uondoke.” Billy akabaki akimtizama. “Tafadhali ondoka Billy. Nataka nikaoge,
nilale.” “Chakula...” “Sina shida na chakula. Nina viporo kibao kwenye friji.
Nikisikia njaa nitakula. Tafadhali ondoka nipate muda wa kutulia. Nijipange
kwanza kichwani kwangu, nilale ili kesho niende kazini.” Nelly akasimama na
kumfungulia mlango. “Tafadhali usinifukuze Nelly.” “Nakufukuza. Ondoka Billy.
Mambo yamebadilika, najhitaji nafsi na akili zangu. Nahitaji muda tafadhali.
Naomba nipishe. Nipo kwenye mshituko, kichwa kimevurugika. Nikiendelea hivi,
naweza kujikuta leo naenda kulala ofisini. Nikafanye kitu nilicho na uzoefu
nacho kuliko hofu niliyonayo sasa hivi.” “Niambie hofu yako.”
“Kubeba mimba. Inamaana nitabadilika kila kitu. Kuanzia kula yangu,
vaa na maisha kwa ujumla. Kuzaa. Ni maumivu ambayo sikuwahi kufikiria wala
kutamani kuja kuwa nayo. Kingine kuja kushika katoto kachanga! Sijui hata kama
nina uwezo huo wa kumtuliza mtoto mkononi, akajihisi anapendwa na yupo salama.
Sijui ratiba zangu zitaingiliwa kwa kiasi gani na jukumu zima. Nikisema jukumu
zima, namaanisha kuanzia ujauzito mpaka kujifungua na kulea. Nina mengi
ambayo natakiwa kuyatafakari na kujipanga.” “Nakuhakikishia hayo yote
hayatakupa majibu sasa hivi ila kujipandisha pressure.” “Hata hilo ulilosema nahitaji
muda kukaa chini na kulikubali. Kuwa nimeshakuwa mjamzito, nini chakufanya na
majibu mengine sitaweza kuyapata sasa hivi. Kwa hiyo nahitaji nafasi mbali na
kila mtu ila mimi tu. Tafadhali kwa mara ya kwanza naomba heshimu hilo.
Nimeshakuitia usafiri, yupo nje. Tafadhali ondoka.” Billy akasimama na kutoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tamu Yageuka Shubiri. Nini
kitaendelea kwa WOTE?
Usikose muendelezo....
0 Comments:
Post a Comment