Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Chozi Langu! - SEHEMU YA 19. - Naomi Simulizi

Chozi Langu! - SEHEMU YA 19.

 Kwa ile hali ya mshituko na kuchanganyikiwa aliyokuwa nayo, japokuwa alikuwa amechoka na njaa, lakini Nelly alishindwa kula, akaishia kuoga na kupanda kitandani. Na usingizi nao ikawa shida kupatikana. Akabaki akiwaza hapo kitandani jinsi maisha yake yatakavyobadilika. Huyo mtoto atakavyobadili maisha yake. Nelly akabaki akigeuka pale kitandani masaa yakizidi kwenda na utabiri wa Billy ukatimia. Hapakuwa na jibu la swali lake hata moja, akazidi kujitia hofu.

Mida ya saa 6 usiku akasikia mlinzi akigonga dirishani. “Unamgeni.” Nelly akajua ni Billy tu. “Amekwambia yeye ni nani?” “Bilzons.” Nelly akajua ni Billson ila ameshindwa kulitamka. “Kamwambie nimelala.” Yule mlinzi akaondoka. Baada ya muda akarudi. “Anaongea lugha ya kigeni, ila amekaa pale getini anasubiri.” Nelly akajua amekataa kuondoka. “Mfungulie.” Nelly akatoka. Akamkuta ameshafika mlangoni, akimsubiria. “Ni nini Billy!?” “Nimeshindwa kulala.” “Sasa kwa nini uko hapa kama umeshindwa kulala?” “Fungua milango yote. Niingie.” “Wewe ni msumbufu Billy.” Nelly akawa anafungua huku akilalamika. Akaingia na kukaa kwenye kochi. Nelly akafunga milango na kupitiliza chumbani kwake. Billy akamfuata.

Bila kukaribishwa akapanda kitandani. “Acha kulala na nguo uliozokalia huko kwenye magari ambayo hata sijui kama ni masafi!” “Halafu hapa kwako kuna joto Nelly, siwezi kulala.” “Billy wewe ni msumbufu bwana! Wewe unafikiri kila nyumba inakuaga na A.c?” “Basi twende tukalale kwangu.” “Kesho ni kazini, na wewe upo hapa na unasumbua!” Baada ya ubishani wa muda mrefu, wakatoka hapo na kwenda nyumbani kwa Billy ambako kweli kuna mazingira mazuri.

“Unawaza nini Billy na mimi nimekupa tiketi ya bure ya kujitoa kwenye hili janga?” “Usiite janga. Huyo ni kiumbe asiyekuwa na hatia yeyote. Ni sisi tu tunatakiwa kujipanga, basi. Ila nimefurahi tupo wote.” Nelly akatulia. “Na mimi nilishindwa kulala.” “Hatuwezi kutengana sasahivi wakati wakati wa starehe tulikuwa wote! Hapana. Naomba tusikimbiane.” Nelly akatulia, na Billy akanyamaza. “Billy?” Nelly akaita. “Nipo.” “Nimefurahi umenifuata.” “Lala vizuri nikukumbatie, tujaribu kulala.” Nelly akajipanga vizuri akimpa mgongo. Billy alipomuwekea tu mkono, Nelly akapotelea usingizini mpaka alamu ilipomuamsha kurudi kwake.

Siku Inayofuata.

Ijumaa.

M

ida ya saa nne asubuhi Billy akampigia Nelly. “Upo sawa?” “Usingizi tu. Jana tulilala muda mbaya.” “Pole. Ila naomba utulie Nelly. Tafadhali ili pressure isipande.” “Nimetulia. Najitahidi kutoa mawazo huko nafikiria kazi zaidi.” Wakatulia kidogo. “Kwa kuwa jana hatukuweza kuzungumza na daktari, nimeomba kesho asubuhi mida ya saa 4, atuone. Atakuwa ni yuleyule ila hospitali ingine.” Nelly akashangaa amempatia wapi huyo daktari! Akajua ndio kazi aliyokuwa nayo asubuhi hiyo, kumsaka mpaka akampata. Akakubali tu. “Sawa.” “Mchana uletewe chakula gani?” Nelly akamuhurumia Billy. Akaona amemuingiza kwenye jukumu ambalo hakutarajia.

“Usihangaike Billy. Mimi nipo sawa. Na nikisikia njaa nitamtuma sekretari wangu.” “Hujanijibu swali langu.” Nelly akakumbuka tabia ya Billy. “Acha nifikirie, nitakujulisha.” Wakaagana. Nelly akabaki akifiria. Akakumbuka majukumu yanayomkabili kwa wakati huo, akakumbuka bado ni dada, anajukumu la Jax. Akaamua kuanza kutengeneza kamati ya harusi ya mdogo wake. Kwa kichwa kilivyozoea mipango, ndani ya lisaa akawa ameshapata wanakamati wote na kuwapigia simu akiomba kuwakabidhi majukumu kwa vile alivyowapangia. Na kwakuwa alishachangia wengi hapo mjini na kuhudhuria shuguli za watu, kila mmoja akakubali. Akagawa majukumu, hilo likakaa sawa.

‘Bado nasubiri jibu.’ Ujumbe wa Billy ukaingia. ‘Nina mambo mengi, sitakula sasa hivi labda chakula cha usiku.’ ‘Basi matunda yanaletwa.’ ‘Asante.’ Akarudisha hayo majibu na kubaki akiiangalia simu yake. Billy alimuonyesha kumjali kwa hali ya juu. Kwamba na ubusy wa siku hiyo na majukumu mazito aliyonayo bado anambembelezea chakula! Nelly akajirudisha nyuma kitini, akaegemea na kujishika tumbo akitafakari.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jioni akiwa amepotelea mawazoni akasikia mlango unafunguliwa baada ya kugongwa tu mara moja, Billy akaingia. “Twende tukale.” Nelly akavuta pumzi kwa nguvu na kuanza kukusanya vitu vyake, Billy akimtizama. “Nyumbani kwako kuna joto, Nelly. Siwezi kulala feni ikinipuliza. Kwanza huwa sipendi feni kwenye maisha yangu yote. Popote pale nilipo sitaki feni.” Nelly akajua anachomaanisha. “Na mimi siwezi kuendelea kulala kwako, Billy. Inanipunguzia muda wa kupumzika. Inanilazimu kuwahi kuamka asubuhi na mapema kuwahi kurudi kwangu ili kujiandaa kuja kazini.” “Tatizo lak

o linatatulika kwa usiku huu, ila langu haliwezekani. Twende ukachukue nguo zako za kuvaa kesho, kisha twende kwangu. Nimeagiza chakula kipelekwe kwangu.” Nelly akaona hata asibishe tena kwa kuwa ni kama kujichosha tu. Billy akishaamua kufanya jambo, lazima liwe vile anavyotaka yeye. Akajua hata akimbishia tena, atamsumbua usiku huo kama usiku uliopita.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya yote, wakaelekea nyumbani kwa Billy. Wakati wapo kitandani, Nelly amemlalia katikati ya kifua akimchora kuzunguka kitovu chake kwa kidole huku Billy ametulia tu ameegemea mto, akamuita. “Nelly?” Nelly akaitika akisikika yupo mawazoni. “Nikikuomba nikuoe, utakubali?” Nelly alishituka mpaka kidole kikawa kama kimeganda na kushindwa kutembea. Alitulia kimya bila hata ya kujibu. Pakazuka ukimywa mpaka Billy akazima taa ya pembeni ya kitanda, wakalala bila ya Nelly kutoa jibu na Billy hakumuuliza tena.

Jumamosi.

A

subuhi ya siku hiyo ya jumamosi Nelly ambaye huwa anafanya kazi kama kawaida, ila nusu siku, Billy huwa hafanyi kazi isipokuwa msimu huo inamlazimu kuwepo kazini siku za jumamosi tena mpaka saa 10 jioni. Wote waliamka na kuanza kujiandaa kwenda kazini. Nelly akamaliza wa kwanza na kuwahi kuondoka kabla ya dereva wa Billy hajafika kumchukua kumpeleka na yeye ofisini kwake. Nelly aliondoka akiwa hajamjibu juu ya swala la ndoa. Alipofika tu ofisini, ujumbe ukaingia. ‘Tafadhali usisahau swala la kliniki. Nitakuja kukuchukua.’ ‘Sawa.’ Nelly akajibu na kubaki akifikiria juu ya swala la ndoa.

Mapema tu Billy akawa ameshawasili ofisini kwa Nelly, wakatoka bila kuchelewa. Walipoingia tu garini, Nelly akaanza. “Hivi hivyo unavyozurula, kazi zako nani anakufanyia?” Billy akamgeukia. “Umeniita mimi mzurulaji?” “Acha kuhangaika na kufanya maamuzi ya ajabu sababu ya huu ujauzito, Billy!” Billy akawa amemuelewa, akatulia kumsikiliza. “Mimi nipo sawa kabisa. Nilimlea Jax peke yangu, sitashindwa kumlea huyu mtoto endapo atafanikiwa kuzaliwa.” “Kama unafikiri nataka kukuoa sababu ya huyo mtoto, basi umekosea sana. Huyo mtoto sio sababu ya mimi kutaka...” “Sasa ni nini? Maana tulikukuwa tukiendelea vizuri kabisa, hata maswala ya ndoa hayakuwepo!” Nelly akawa akigomba.

“Naomba tulia na ukumbuke nina watoto wawili tayari. Sikuwa nikitafuta watoto ila mtu wakuwa naye maishani.” Nelly akatulia. “Unanielewa Nelly?” Kimya. “Unakumbuka nilikwambia nakupenda?” Kimya. “Hukumbuki au umeamua kuninyamazia?” “Ninachotaka ni usijichanganye, Billy. Sisi ni watu wazima. Hatuna haja yakufanya...” “Hivi tokea lini umekua ukijua moyo wangu wewe Nelly?” Billy naye akaanza kugomba, dereva kimya akiwapeleka hospitalini.

“Yaani wewe unayajua mawazo yangu na moyo wangu pia!?” “Acha kugomba Billy!” “Na wewe acha kuzungumzia moyo wangu na mawazo yangu kwa kuwa sivyo. Nisikilize kile ninachokwambia mimi. Acha kuzungumza kile ulichozoea kukisikia mtaani. Mimi sina shida na watoto.” “Kwa hiyo...” “Tafadhali nisikilize Nelly. Nisikilize kile ninachokwambia mimi na sicho unachodhania.” Nelly akatulia.

“Mtoto uliyebeba si janga wala wa bahati mbaya.” “Sasa mbona umebadilika?” “Nilikwambia nahitaji muda kwa kuwa mtoto hakuwa kwenye mipango yangu kabisa. Ila wewe. Mtoto si habari mbaya au janga kwangu. Na tafadhali usimuite hivyo.” Nelly akatulia. “Nahitaji muda wa kujipanga na kujua ni jinsi gani mimi nitakuwa kwenye maisha yake bila kumuathiri yeye. Sijui kama unanielewa?” Kimya.

“Huyo mtoto hana hatia na hana atakapokwenda ila sisi ndio tunatakiwa kujipanga. Mambo yatabadilika ili yeye akute mazingira mazuri, asije akakuta sisi ni kama wapuuzi wengine tu. Kama tunaweza kuongoza watu na akili zao na mambo yakaenda, basi kwa kiwango hichohicho na kuzidi, inatakiwa kufanya kwakwe kwa kuwa yeye anatokana na sisi na atakuwa na sisi kwa maisha yetu yote. Kwa hiyo nikutakiwa kujipanga.” “Sasa umeshajipanga?” “Sio kitu cha siku moja, Nelly! Na naomba utulie.” Nelly akajirudisha nyuma na kutulia.

Akamwangalia, akakuta akimwangalia. “Nini?” “Ukitulia hivyo unakuwa mtoto mzuri!” Nelly akacheka. “Nimeanza maandalizi ya harusi ya Jax.” “Yanaendaje? Na unataka msaada gani?” “Naona nimepata uungwaji mkono mpaka wengine wananipigia simu kuuliza majukumu. Jinsi ya kusaidia. Sikutegemea!” “Kwa sababu aliahirisha mara ya kwanza?” “Ndiyo Billy! Mimi nilijua watu watasusia, lakini imekuwa tofauti! Wanauliza wapi wapeleke michango. Imebidi kuwaambia michango wasubiri kwanza. Sikuwa nimejiandaa na michango. Sina mtu wa kukusanya.” “Aliyekusanya mwanzo?” Billy akauliza.

Nelly akafikiria kidogo kama ambaye na yeye hailewi. “Sijui imekuaje! Lakini amekata mawasiliano  kabisa na mimi! Alikuwa rafiki wa karibu sana na Jax, lakini naona amebadilika! Sijui Billy.” Nelly akatulia kidogo akifikiria. “Ila mimi huwa simshangai mwanadamu. Nimezoea kubadilika kwao vibaya, kuliko kubadilika kuwa wema kwangu.” “Sio wote Nelly. Tafadhali naomba hilo ulibadili kichwani mwako.” “Labda wewe, Billy. Pengine wewe utabadili historia. Kuona nimekosea, na bado kuwa na mimi!” Nelly akaongea kwa kupooza kidogo. Billy akatulia na kumfanya Nelly aamini ndivyo hata Billy anavyomuona. Amefanya uzembe. Akatulia kabisa na kugeukia dirishani.

“Nelly?” Akamuita na kumshika mkono. Nelly akamgeukia. “Wote tulijisahau. Mimi nipo makini sana, sijui kwako ilikuaje. Nimeizoea kondomu hata kwa aliyekuwa mke wangu ndio ilikuwa kama njia ya uzazi wa mpango. Mwanamke niliyekuwa naye baada ya kuachana na Anele, sikuwahi kulala naye bila kondomu. Hata mara moja. Na yeye alikuwa akishangaa sana. Na alitegemea ningemzoea, baada ya muda nikamuamini na kuacha kutumia naye kinga. Lakini hata yeye nilimwambia ni zaidi ya uaminifu kwake. Sikuwahi kulala naye bila kinga na haikuwa kwa bahati mbaya, nilikusudia.” Billy akaendelea.

“Kilichotokea kwako si kosa lako moja kwa moja. Mimi huwa sisaidiwi kufanya mipango yangu ya maisha. Huwa ninawaza na kupanga nikifikiria madhara na faida. Ila kwako nilishindwa na ninashindwa kujizuia. Ndio maana nimeamini wewe nakupenda Nelly. Inapofika swala lako, akili yangu inashindwa kufikiria ila najikuta natenda tu, ilimradi niwe na wewe. Kwa hiyo naomba usichukue hili kuwa ni kosa lako moja kwa moja. Na mimi nawajibika kwa asilia zote. Kwa kuwa sikukusudia kuwa na mtoto tena. Kweli sitaki mtoto. Lakini kwa kuwa amekuja. Na ni wangu, ndio inanibidi kujipanga. Kama muda huu ningekuwa ofisini, nikifanya kazi, lakini siwezi kuepuka jukumu la kuhakikisha yeye yupo salama, na wewe upo salama.” Nelly akajifuta machozi kwa kuumia.

“Mimi ndio natakiwa kubadili maisha yangu ili kuweza kuwa naye, maana sasa hivi siwezi kukwepa tena. Ameshakuja na ni wangu. Lazima kuwajibika, kubadili maisha yangu yote kwa jumla, ndio maana nakwambia si kazi ya siku moja. Si mabadiliko ya siku moja. Ni mabadiliko yatakayogarimu pia maswala yangu ya kikazi.” “Unamanisha nini?” Nelly akauliza.

“Kwa mfano, kwa sasa siwezi kuchukua cheo chochote kitakachonitoa mbali na nyinyi.” Hapo Nelly alishituka mpaka machozi yakakata. “Hapana Billy. Mimi si Anele na wala si aina ya mwanamke nitakayetaka kulelewa kama mtoto mdogo. Popote utakapotakiwa kwenda, tafadhali wewe nenda, ilimradi tu tuwe na mawasiliano. Sijui kama unanielewa?” Billy akamtizama. “Kama unatakiwa cheo sehemu, na nikitu kizuri, nenda. Nenda kabisa. Tuwasiliane na kutembeleana. Mimi sitakuwa na neno nikijua upo mahali na bado unamtaka mtoto. Sitakutenga na mtoto na sitakuwa na shida na wewe. Nataka ufanikiwe zaidi kwenye ajira yako.” Billy akavuta pumzi kwa nguvu na kujirudisha nyuma, akatulia. Nelly akahisi kuna dili la kikazi alishalipata mahali. Akamuhurumia ila akamuacha afikirie.

Walifika hospitalini. Kila kitu kwa Nelly na mtoto kilikuwa sawa. Nelly alishafikisha miezi mitatu bila kujijua ila kufurahia mapenzi ya Billy. Kuhama kitanda kimoja hadi kingine, bila kujiuliza mbona hapati hedhi. Alitulia akiwaza pale kitandani akifanyiwa ultrasound wakati anayewahudumia akijaribu kutafuta mapigo ya mtoto. Billy alisogea karibu na screen pale mapigo ya moyo yalipoanza kusikika kwa nguvu. Nelly akamuona anacheka. “Yanasikika kwa nguvu!” Akaongea kwa hamasa, macho kwenye screen. “Anaonekana atakuwa mkubwa na mrefu.” “Kweli eeh!” “Kabisa. Kwa umri wake, amepita vipimo vyake.” Billy akacheka. “Si utatutolea picha zake?” “Ndiyo.” Billy akamtizama Nelly pale alipokuwa amelala, ametulia tu.

Akamshika. “Umesikia?” “Hapa ndio uhalisia wa mambo unazidi kuingia akilini na moyoni.” “Weka pembini hofu, halafu sikiliza hayo mapigo ya moyo.” “Ulivyofurahi!” “Muwekee tena.” “Nimesikia Billy!” “Hapana. Umesikiliza ukiwa na mawazo. Sikiliza hayo mapigo ya moyo ya kiumbe kisicho na hatia, ndani yako, wewe Nelly. Mzima wa afya njema, anatumia tumbo lako kuumbwa mpaka akamilike. Mungu amuone yupo tayari ndipo amtoe na kutukabidhi sisi kama wetu!” Nelly akacheka na kumshangaa Billy alivyobadilika gafla. “Acha mchezo Nelly!” “Sawa Billy. Mimi naomba tuhitimishe hili zoezi kwa leo, nirudi kazini.” “Mara ya mwisho Nelly!” “Billy!” “Nakuahidi safari hii nikisikia mapigo yake narikodi, ili nikasikilize mwenyewe.” Nelly akamwangalia kama asiyeamini.

Akajirudisha kulala vizuri maana alishatoka hapo kitandani na jelly yake aliyokuwa amepakwa. Hakutaka kufutwa na huyo aliyekuwa akiwaonyesha mtoto wao, akamwambia atajifuta mwenyewe. Akampaka tena na kuanza kutafuta mapigo ya moyo, Billy akichukua video. Yalipoanza kusikika, akamuona anacheka tena. “Tulia hapohapo kwa angalau dakika moja tu, niyapate hayo mapigo ya moyo.” Nelly akatulia mpaka Billy akaridhika.

“Si unajua siku nyingine sitakuja na wewe huku?” Nelly akamuuliza wakitoka hapo. Billy akacheka sana. “Ubaya wangu uko wapi?” “Wewe utanifukuzisha kazi. Au kufanya watu wadhanie ujauzito nilio nao ndio unanifanya nishindwe kazi.” “Acha kuishi kwa kutaka kuthibitishia watu, kile unachodhania wanatakiwa kujua. Nelly wa sasa hivi siye Nelly wa miezi minne iliyopita.” “Acha kuniambia hivyo, Billy bwana!”

“Nakwambia ukweli Nelly. Kadiri utakavyopoteza muda hapo, ujue ndivyo unavyojichelewesha mwenyewe na utaharibu. Utaharibu kila kitu. Ukikubali kuwa yale mapigo ya moyo tuliyosikia pale, yapo ndani yako. Na yataendelea kuwepo kwako mpaka Mungu aseme inatosha. Ukakubaliana na hilo. Ukabadili jinsi unavyofikiri na kutenda. Kwanza itakurahisishia na kukufanya pengine ukawa bora zaidi.” “Kivipi?” “Utajua jinsi ya  kumtunza mtoto. Utakuwa makini. Kisha utajifunza kufanya majukumu yako, na yeye akiendelea kukua vizuri. Kwa kuwa wewe sio mwanamke wa kwanza mwenye majukumu mazito, kushika mimba. Wapo na wanafanya vizuri tu, tena wakijivunia mimba zao. Hujafanya jambo la kwanza tena la ajabu hapa duniani. Acha kujiumiza kichwa.” Nelly akatulia.

Wakati anashushwa garini, wakamuona Jax naye ni kama anaingia hapo. Billy hakuwa hata na mpango wakushuka, na yeye akashuka. “Sasa unaenda wapi Billy na wewe ulisema unawahi kazini?” Billy akaanza kucheka. “Nimemuona Jax, nataka kumsalimia.” “Si ukamsalimie huko kazini kwenu!” “Hivi unajua ofisi yangu na anakofanya kazi mdogo wako ni pande mbili tofauti na  ni mpaka uwe na sababu ya ku..” Jax akawasogelea.

Akawasalimia. “Nimekuletea hii chupa ya kutunzia ice cubes.” Nelly akaipokea. “Na humo ndani ni barafu za nyumbani kwako. Nilinunua, nikaisafisha, na kwenda kwako kufuata barafu za kwenye friji yako, ulikosema unapenda ladha na harufu ya friji yako.” “Asante.” Nelly akafungua hapohapo na kuweka mdomoni. “Upo mzima lakini?” “Mzima tu. Tulitoka kuangalia mtoto.” Akamgeukia Billy aliyekuwa amesimama hapo, Nelly na mdogo wake wakizungumza kwa lugha ya kiswahili. “Muonyeshe mapigo ya mtoto.” Billy akafurahi sana. “Si nilikwambia tutahitaji?” “Muonyeshe bwana ili awahi kurudi kazini.” Billy akatoa simu yake akionekana amehamasika. Jax akacheka tu akiwafikiria watu wazima hao.

“Umekula?” Jax akamuuliza. “Sijala. Tulikuwa tukiwahi kurudi kazini. Tumechukua muda mrefu huko hospitalini sababu ya maswali yake huyu.” Nelly akamteta. “Anataka kurudia mambo! Mfano hiyo video, tumeonyeshwa mara mbilimbili. Huko kwa daktari kwenyewe mpaka nikaanza kusinzia! Anamaswali mpaka amemaliza muda wote huko.” Jax akacheka tu, na Billy naye akawa ameipata hiyo video, akamuonyesha Jax. “Kwanza ni mkubwa zaidi ya umri wake, halafu....” Billy akaanza kurudia maelezo waliyopewa huko hospitalini.

“Mimi naona huko World Bank hamna kazi zakufanya. Mwenzenu nina majukumu, naingia ofisini.” Nelly akaanza kuondoka. Billy akamvuta mkono, Jax akabaki akiangalia ile video kwenye simu ya Billy, bosi wake huku akiwatizama kwa kujiiba. “Niache bwana Billy mimi niende kazini. Hayo unayoyaongea kwa Jax nayajua, halafu hayamuhusu. Acha ku..” “Yananihusu Nelly.” Wote wakamgeukia Jax. “Yananihusu kwa kuwa huyu mtoto si wako peke yako. Ni wetu. Mungu ametupa mtu mwingine Nelly. Huoni ni jambo la ajabu! Miaka yote tumekua ni sisi tu! Sasa hivi ameongezeka mtu wetu ambaye tutakuwa naye mpaka kifo!” Nelly akatulia kabisa mpaka akajihisi machozi kumtoka, yale maneno yakawaingia wote wawili.

“Mimi nimefurahi Nelly. Nimefurahi sana. Na kwa kuwa nakujua wewe, naamini tutakuwa sawa tu.” “Asante Jax. Nilikuwa kama nimechanganyikiwa! Lakini kwa jinsi ulivyoiweka, angalau nimepata moyo.” “Isiwe angalau. Labda kama umekutwa na ugonjwa.” “Sina tatizo lolote hata pressure imeshuka. Ipo sawa.” “Basi tulia. Hili si tatizo, ila baraka.” Jax akawa faraja kwa dada yake. “Naenda kukuletea chakula na matunda.” “Nimeshamuagizia, ataletewa.” Akajibu Billy.

 “Nakushukuru kwa video. Ila naomba na mimi nijitumie kama hutajali.” “Bila shaka.” Wote wakacheka. Wakati anajitumia Billy akaanza tena.  “Nawakaribisha wewe na Lara kwa...” Nusura simu zimuanguke mikononi mwa Jax, mbele ya dada yake na bosi wake mara aliposikia jina la Lara linatoka kinywani kwa Billy na wanakaribishwa! “Acha kumtisha bwana!” Akamsikia Nelly akilalamika. “Nelly! Nataka kuwakaribisha kwa chakula cha jioni kesho, siku ya jumapili! Nimemtisha nini?!” “Acha kucheka Billy. Ungeniambia mimi na mimi ndio nimwambie.” Nelly akawa kama analalamika. “Kwani wewe ungetumia maneno gani? Si hayahaya? Lazima Jax ajifunze kuwa na mimi kwa..” “Hapana Billy. Anahitaji muda.” “Mimi nipo sawa Nelly. Nahisi nilishika simu vibaya.” Akamrudishia Billy simu yake na kuondoka bila kuaga.

“Sasa unafikiri kesho watakuja au?” Billy akauliza cheko limemjaa baada yakuona Jax amewakimbia. “Mimi sijawahi ona mtu wa namna yako Billy! Ukoje lakini!?” “Hivi unajua Jax ni mtu mzima? Mtu na familia yake?” “Naomba umuache.” “Nasikia ndio tatizo lako hilo Nelly, hutaki mtu kwa Jax ila wewe tu.” “Sasa kama umeshaambiwa hivyo kwa nini hueshimu hilo? Mwache. Na ukitaka kitu kwake niambie mimi.” “Hapana Nelly. Nafikiri ni wakati muafaka wa wewe na yeye kukaa chini mzungumze juu yangu. Na umwambie na mimi sasa hivi nipo. Aache kunikwepa na kupaniki kila akiniona na wewe. Sitakwenda popote. Na wewe umeshalijua hilo. Sikwepeki.” Akaondoka na kumuacha Nelly hapo, amesimama. “Jumapili tunachakula cha jioni pamoja. Umkumbushe.” Akamsikia Billy akiongea huku akielekea garini. Nelly na yeye akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Jioni akiwa amejiinamia, amepotelea mawazoni mlango ukafunguliwa kisha ukagongwa. Nelly akahisi tu ni Billy, akageuka. “Hivi unajua huwa wanagonga wakiwa nje ya mlango sio ndani?” “Nani aliweka huo utaratibu?” Billy akauliza akikaa. “Wala sitapoteza muda wangu kukujibu.” Billy akaanza kucheka. “Taratibu zinawekwa na watu na mimi ni mtu, kwa hiyo nimeweka utaratibu wangu.” “Kugonga ukiwa ndani?” “Yeap.” Billy akakubali akimwangalia. “Ingekuwa mtu mwingine ningemuuliza habari za kazi. Ila wewe!” Billy alicheka sana.

“Mimi si stahili?” “Kwa nini hukai ofisini kwako, ukatulia Billy?” Billy akazidi kucheka tena kwa sauti ya juu. “Acha kelele bwana!” “Twende tukapumzike. Tuanze weekend yetu fupi.” “Wewe nenda, mimi nipo busy.” “Nimekukuta umekaa tu ukiwaza matatizo yako, wala hufanyi kazi.” “Basi hiyo ndio kazi.” “Basi twende ukafanyie hiyo kazi kwangu.” Akasimama na kwenda kuchukua pochi yake. “Subiri kwanza Billy!” “Twende sasahivi, mimi nimechoka.” “Kwa nini unakua kama mtoto mdogo linapofika swala la kwenda nyumbani!?” “Nelly!” Nelly akajikusanya na kunyanyuka, wakatoka hapo.

“Umekula?” “Sijala Nelly! Si umeiona siku ya leo ilivyokuwa ya hekeheka?” “Unataka nikakupikie?” “Hapana kwakweli. Ila nakushukuru kwa huo moyo. Nishaagiza chakula, kinatusubiri nyumbani.” Nelly akashukuru Mungu nafsini mwake, hata yeye hakuwa akijisikia kwenda kuanza kupika. Wakatoka hapo kwenda kwake kuchukua nguo zake baadhi na vitu alivyojua angehitaji, wakatoka tena hapo kuelekea nyumbani kwa Billy. Na bado hakuwa amemjibu swali lake kama angekubali kuolewa na yeye. Billy alikuwa akikumbuka, ila akaamua kumuacha tu akijua hata yeye anakumbuka ila hakuwa tayari kujibu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usiku wakiwa wamejilaza kitandani, Nelly alikuwa ametulia sana. Wapenzi hao hawakuwa wamekutana kimwili tokea wapate taarifa ya huo ujauzito. Ni kama hamu ilikata gafla. Kutoka kwenye mapenzi ya kila siku tena zaidi ya mara moja na kupitiliza siku! Tena wakiwa wamelala kitanda kimoja! Ikawa sio kawaida yao. Alimuona Nelly vile alivyokuwa mwingi wa mawazo tokea wanatoka kazini, njiani aliendesha akiwa kimya kabisa, na yeye hakutaka kumsemesha. Akamuacha tu. Na wakati wakila akawa hivyohivyo.

Hapo kitandani akawa napo amejilaza ubavu ametulia kimya kabisa, ila Billy alijua hajalala. Alipomaliza kuangalia luninga, akazima na kujisogeza mpaka kwenye mto wake, akamchungulia. “Nelly, unataka tuzungumzie kile ulichokuwa ukikiwaza pale ofisini?” “Hapana.” “Sawa.” Billy akaliheshimu hilo, ila akajivuta karibu na kulala nyuma yake kama anayemwambia yeye yupo. Wakatulia.

Baada ya muda wakati Billy ameshaanza kuchukuliwa na usingizi, akamsikia. “Billy?” Billy akatulia akijaribu kufikiria kama ni ndoto au la. “Iweje mkeo atake mrudiane?” Akamsikia akiuliza hilo swali. “Unaota Nelly!?” Billy akamuuliza. Hakujibu, na yeye Billy akapotelea usingizini asijue mwenzie alishindwa kulala.

Billy alipojigeuza mida ya saa nane usiku, akajikuta peke yake kitandani. Akaangalia saa ya mezani, ikaonyesha ni saa nane usiku. “Nelly ameondoka!” Alishituka, akaruka hapo kitandani na kuanza kuita akielekea chooni. Akatoka huku akiita. “Acha kelele Billy! Ujue ni usiku sana sasa hivi!” Akamfuata sebuleni aliposikia sauti yake. “Sasa kwa nini umeniacha kitandani? Mimi nilijua umeniacha!” “Zima taa bwana! Usiwashe.” “Kwa nini unakaa hapo gizani?” “Sipo gizani! Naangalia huo mwanga wa nje.” Nelly alikuwa amekaa kwenye kochi moja ambalo linaweza kunyayua miguu juu. Billy aliliweka dirishani kabisa, likiangalia upande nje. Hapo ndipo Nelly alikaa. Mbalamwezi  nje zikimulika ndani.

“Umenishitua Nelly!” “Kwa nini unashituka? Mimi siwezi kuondoka bila kukuaga Billy! Tafadhali tulia na rudi kulala.” Akazima taa ya hapo sebuleni na kumsogelea. “Kwa nini umetoka kitandani?” “Sikutaka kukusumbua. Nilikosa usingizi, nikabaki nikigeuka tu. Nikajua nikiendelea hivyo, nitakuamsha na wewe.” “Ni bora hivyo kuliko kuamka na kujikuta peke yangu. Hapa ndio usingizi umeisha kabisa.” Nelly akamtizama  na kurudisha macho nje. Wakatulia.

Na yeye akavuta stuli ya pembeni akakaa pambeni yake. “Nisikilize Nelly.” Nelly akamgeukia. “Jana wakati unaniuliza lile swali mpaka nikahisi nimeota!” “Kwa nini sasa?” “Nelly! Wewe unajua sina mke, halafu unaniuliza itakuaje endapo mke wangu akitaka turudiane!” “Unajua ninachomaanisha Billy.” “Hakika sijaelewa! Labda kama unamaanisha Anele ambaye nilishawahi kumuoa. Lakini pia, Anele si mke wangu! Na nilikwambia ameolewa na...” “Najua. Lakini endapo akitaka mrudiane?” “Kivipi tena Nelly!? Hivi unajua hatujaachana naye jana  au juzi?” “Watu wanajirudi Billy. Na wewe unaonekana uliumia sana kuachana na mkeo. Na ni kama bado unampenda.”

“Nisikilize Nelly. Nikikwambia kama sikuwa nikimpenda Anele, nitakudanganya. Nilimpenda na ndio maana nilimuoa na kuzaa naye. Kuumia sababu ya kuachana, niliumia sana. Wala sitakudanganya. Kweli niliumia Nelly. Narudia tena, Anelle alikuwa mke wangu, mama wa watoto wangu. Aliniacha sababu ya rafiki yangu! Hakika niliumia au naumia mpaka leo. Ila sasa, na wenyewe wanaishi na mimi kunithibitishia kuwa hawajakosea. Wao walikusudiwa kuwa pamoja.” “Billy!” Nelly akashangaa.

“Kweli Nelly. Kwa maneno na vitendo wanathibitishia kila mtu wao walikusudiwa kuwa pamoja, mimi nilikuwa ni kosa walilorekebisha. Na ninauhakika Anele angekuwa na uwezo kama huo wako, angezaa na Carlos ila sema hana huo uwezo ila najua angezaa makusudi pia ili kunikomoa.” “Kwa nini!?” Nelly akauliza.

“Kwa nini ya kwanza, angenikomoa kwa sababu alitaka tuongeze mtoto wa tatu, mimi nilimkatalia katakata. Kabla hujauliza kwa nini ya tatu, maana najua ya kwanza ilibeba mbili. Sikutaka kuzaa mtoto wa tatu kwa sababu kama nilizokupa wewe. Sikuwa na muda wa kulea, Nelly. Kazi ilikuwa imenibana, na yeye akawa analalamika sipo nyumbani, namuachia jukumu la kulea. Sasa nikamuuliza, kama analalamikia watoto wawili tu, tukiongeza wa tatu atafanyaje? Akaniapia atajitahidi, lakini nilimkatalia nikijua nia yake anatafuta mtoto wa kiume. Yeye anayo imani ya kutaka mtoto wa kiume awe mrithi au sijui! Lakini mimi nilisharidhika na binti zangu, nikasema hao wawili wananitosha. Maana mimi mwenyewe ni mtoto wa kiume, lakini mpaka sasa sijarithi chochote kutoka kwa wazazi wangu. Hilo nalo likaleta mjadala mrefu na shida. Ila nikasimamia hapohapo kuwa sitaongeza mtoto.” Billy akaendelea na kuzidi kumuumiza Nelly kuona amefanya makosa.

“Na kwa nini ya pili kwenye swali la kwanza, kwamba angezaa na Carlos kama angeweza ila ameshindwa, ni kwa kuwa Anele ni mtu mzima. Nilimuoa akiwa amenizidi miaka mitatu.” Nelly akashangaa mpaka Billy akamuona. “Hilo sikujali kwa kuwa kwa muonekano hakuonekana ni mtu mzima. Tena mimi nilionekana ninaumbile kubwa kwake. Nilichojali na kukubali kumuoa ni kwa kile alichonihakikishia kuwa ananipenda na yupo tayari kuhama nchini kwao na kwenda kuishi na mimi. Hilo nikalifurahia sana, maana nilijua kwa umri wake, alishajijenga kwao. Kukubali kuacha kila kitu na kuambatana na mimi, hilo likanivutia zaidi. Sikujali umri.”

“Sasa kwa bahati mbaya pia, aliwahi sana kuingia menopause. Nafikiri hata kabla hajaingia miaka 50, alishakoma hedhi. Kwa hiyo hana uwezo wa kuzaa tena. Kwa kujibu swali lako. Mimi Billson, sina mke. Ila nilikuwa na mke. Na hata kama akirudi sasa hivi, akaomba msamaha japo najua anaamini hajanikosea, nitamsamehe kwa kunidanganya alinipenda ila kumbe alikuwa akinitumia kumtoa kwenye maisha aliyokuwa ameniaminisha alikuwa akiishi kwao ya kifahari na amefanikiwa, akayaacha kwa ajili yangu, kumbe alikuja kwangu kujinufaisha tu. Nitamsamehe, ila si kurudi kwenye maisha yangu kama mpenzi.”

“Najua kupendwa na kutapeliwa kimapenzi, maana nimejifunza kwa garama kubwa sana. Ukiniona napaniki kwamba umenikimbia kitandani kwangu, ni kwa sababu nakutaka wewe Nelly ndio niwe naamka pembeni yako. Ungekuwa mwanamke mwingine sio wewe, hakika sasa hivi usingekuwa umekaa hapa, Nelly.” “Billy!” “Hakika nakuhakikishia. Kwani wewe unafikiri wewe ndio mwanamke wa kwanza kuwa naye baada ya Anele?” Nelly akanyamaza.

“Wewe ni mwanamke wa kwanza kujiruhusu kufanya kosa, baada ya Anele.” “Unamaanisha nini?” “Hata kwa Anele nilikuwa nikiwa mwangalifu kwenye swala la watoto. Ninapokwambia sikuwa na mpango wa mtoto mwingine, hilo linajulikana na kila anayenifahamu. Anele alinipeleka kunishitaki mpaka kwa mchungaji ambaye alitufungisha ndoa na ambapo ndipo wazazi wangu wanaabudu huko. Nilizungumza na yule mchungaji kwa ufasaha mpaka akakosa cha kuniambia juu ya swala la mtoto! Sikuwa nataka mtoto Nelly, na nilikuwa makini mno. Nilihakikisha kwenye hilo hakuna makosa, ndio maana unaniona nipo kama nimepigwa na butwaa! Swala la ujauzito unaonihusu mimi, ni habari niliyojua sitakuja kuisikia mpaka kifo changu. Ndio maana nimekuomba unipe muda.”

“Sasa kwa nini unataka tena kunioa kama nimekusababishia yote hayo?” “Kwanza tofautisha mambo mawili hapa. Kuna wewe kama Nelly. Wewe nakutaka kwenye maisha yangu. Kwa jumla yako yote. Nakutaka wewe Nelly.” “Kwa nini sasa wakati...” “Kwanza najua unanipenda sana zaidi ya vile ulivyoniambia eti ulijua unanipenda siku uliyoondoka hapa, baada ya kukataa kunitambulisha kwa Jax.” “Billy wewe! Ujue uache kujiaminisha hivyo!” Billy alicheka sana.

“Nakujua Nelly, nakujua kwa asilimia 95. Kama sio kunipenda, najua usingekuwa hapa sasa hivi. Bisha.” “Naomba niache Billy, endelea na jambo la pili.” Billy akazidi kucheka. “Kwa kuwa unajua nimepatia.” “Sema jambo la pili, Billy, acha kucheka kwa sauti! Watu wamelala.” “Pili, acha kujipa credit. Wewe hujafanya kosa kwa kubeba mtoto wangu.” “Billy?” “Wewe hujanijua Nelly. Natamani uwe na Anele siku anayojua umebeba mtoto wangu. Nahisi atajinyonga. Aisee linapofika swala la mtoto huwa sihitaji ushauri nasaha. Na sikosei Nelly. Najua. Yaani hata Anele alishindwa kunitega, na nilipogundua kuwa anajaribu kunitega, nilimuonya, mpaka akaelewa na ndipo aliponipeleka kwa mchungaji.”

“Kwako nilijiruhusu kukosea, Nelly.” “Kwa nini sasa Billy!? Mimi sitaki mtoto. Si kitu nataka Billy. Nina maisha yangu ambayo nilishayazoea na kuyamudu vizuri sana. Hakika mtoto ni jambo la mwisho na sikuwahi hufikiria mimi kubeba tumbo lenye mtoto ndani.” Nelly akajikuta akilia.

“Natamani kama  mimi ndio ningepata hiyo bahati ya wewe kutokukosea Billy. Sitaki mtoto na kutoa mimba siwezi. Natamani hata niamke asubuhi nikute nilikuwa nikiota.” “Nisikilize Nelly. Hii imeshatokea. Tafadhali maliza mshituko, uanze kujipanga. Lasivyo itatuondolea wakati wote mzuri tunaokuwa nao mimi na wewe. Niangalie na uache kulia.” Nelly akajifuta machozi.

“Unajua leo ni siku ya ngapi hujapata muda na mimi?” Nelly akatingisha kichwa kukubali. “Nakumisi Nelly.” “Mimi nilijua ndio umeingiwa hofu, hutaki tena.” “Hata kidogo. Wewe nakuhitaji usiku wakati nalala na asubuhi kabla sijaenda kazini.” “Acha kufanyia utani kila kitu Billy, bwana!” “Mimi nakwambia kweli. Siku yangu inakuwa nzuri ninapokwenda kazini nikiwa nimeamka na wewe, halafu nikapata penzi zuri! Hapo nakuwa safi hata naweza kufikiria vizuri. Tafadhali hili lisitupotezee tulichonacho, Nelly.” Nelly akatulia akifikiria.

Akakuta Billy ametulia akimwangalia. “Kwa hiyo tutafanyaje na huyu mtoto?” “Cha kwanza ambacho nataka ujue ni kwamba hiyo hofu yako uliyonayo wewe, mimi ninayo tena yakupitiliza.” “Ipi? Maana mimi nina mengi.” “Hiyo ya kuharibu kwa huyo mtoto. Na ndio sababu sikutaka mtoto mwingine. Wewe unahisi kuharibu tu kwa huyo mtoto. Kwamba hatakuwa kile kinachotarajiwa. Ni kwa kuhisi, mimi mwenzio ni kwa uhalisia. Nimepoteza mtoto wangu kipenzi kwa aliyekuwa rafiki yangu. Tena mtoto akimtambua yeye ni baba anayempenda zaidi yangu mimi.” “Pole Billy.”

“Naogopa historia isije kujirudia kwa huyu. Kile anachotegemea niwe, nisiwe, akaja kulaumu ukubwani. Nimeingiwa sijui niseme ni hofu au  ni nini! Sitaki tena kurudia kosa na sikuwahi kutamani nafasi ya pili kujaribu ili kuona kama naweza kupatia. Nilijiambia kama ni kosa, acha nibakie kuwa mkosaji tu, basi. Paishie hivyo ila si kwa mtoto. Kwa hiyo kama unadhani wewe una hofu, basi jua mimi zaidi. Lakini ninajiambia kuwa imeshatokea. Kila siku itajijibu yenyewe. Nitafanya kwa kadiri ya uwezo wangu kwa mtoto wangu, mengine nitamuachia Mungu.”

“Hujanichukia hata kidogo, kuona nimechangia kwa kiasi fulani?” “Ukweli ni hapana. Ila sikutegemea kwa mtu kama wewe, kama unaweza kushika mimba kirahisi na nafikiri ndio maana nilijiachia. Nilijua ni kitu unachojilinda nacho sana.” “Sikuwa hata na wazo Billy! Sikuwahi kuwa na mahusiano kama hivi.” “Ndicho nimekuja kukumbuka jana. Kwamba usingekuwa ukitumia kinga kwa sababu hukuwahi kuwa na mahusiano na mwanaume. Naomba tupite hapo Nelly. Tuendelee. Au wewe hupendi kuwa na mimi?” “Napenda Billy. Na mimi najua wewe unanipenda. Hakika nisingekuwa hapa kama si wewe. Eti niwepo Dar, nisilale kitandani kwangu! Hakika sikuwahi hata kuwaza kama ni kitu naweza fanya maishani!” Billy akacheka sana.

“Kweli Billy.” “Na mimi najua. Na ninakushukuru sana. Twende tukapumzike. Haswa wewe. Nataka utulie kabisa Nelly. Jiambie utakuwa sawa. Mtoto ataongeza shuguli, lakini yeye ndio kipaumbele maana ndiye anayeongeza maana ya maisha kuliko kazi.” “Billy! Hivi unajua kazi kwangu ndio kila kitu?” “Ni kwa kuwa mimi na mtoto hatukuwepo. Nakwambia inamaana yake tofauti, Nelly. Mimi nimeona hayo maisha, najua ninachozungumzia. Kazi haiwezi na haitakuja kulinganishwa na familia, zaidi mtoto wa damu. Huwa inafika kipindi kila kitu kinakosa maana, isipokuwa familia. Jipe muda, utakuja kuniambia. Utakuwa ukiacha kazi, unakimbilia mtoto nyumbani.” “Kweli Billy?” “Acha Nelly. Mtoto ni mzuri kuliko pesa. Unafikiri ni kwa nini nilitaka kujiua?” Nelly kimya akimwangalia.

“Familia yangu ilikuwa sehemu nakwenda kupumzika baada ya yote. Nakuwa kwenye ndege kurudi kwa watoto wangu, nikitizamia kuwepo pale. Muda nitakaotumia na binti zangu. Kicheko tutakachocheka. Kuwasikia wakiniambia habari zao hata zile za kitoto kabisa! Au kuwepo kazini, kuwapigia nakuwasikia sauti zao tu, ilikuwa ikinipa nguvu na furaha ya ajabu, sina jinsi nikakueleza ukaelewa hilo. Halafu eti gafla familia ikaja kusambaratika, nikapoteza mtoto mmoja! Na usifikiri yule mkubwa alibaki sawa! ilimuathiri sana. Ila ninachokwambia, mtoto wako, huwezi kumlinganisha na kazi. Jipe muda uone.” Akamsikia akivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha.

“Umeridhika sasa?” “Kukusikia hivyo nimeridhika Billy. Nilijua nimekuvunja moyo kama baba yangu.” Nelly akaanza kulia kwa uchungu. “Kwa baba hakuwahi kunipenda kwa kosa la kuzaliwa mtoto wa kike. Hata nilipojitahidi kujipendekeza na kumfurahisha, ni kama hakuwa akiniona kabisa. Sasa nilipokupata wewe, nikajiambia nimepata mtu anayenipenda, gafla nikashika mimba! Na mimi nikija kuzaa mtoto wa kike?” Hapo ndipo akajua kwa hakika wasiwasi wa Nelly. Mengine alijua ni ziada tu. Hofu ni kuja kuzaa mtoto wa kike kama mama yake.

“Nisikilize Nelly. Mimi nina watoto wa kike wawili. Sijawahi kuona uhitaji wala upungufu wa binti zangu. Sijui baba yako alichokuwa akikitafuta kwa watoto wa kiume, hapo siwezi kuzungumza kwa upande wake. Ila kwetu sisi mtoto ni mtoto kwa kuwa mzee wetu sisi hakuwa akitafuta mtu wa kumrithisha. Alishasema tokea zamani, urithi ni elimu atakayokulipia ukitaka kusoma. Ndio maana sisi wote tulisomeshwa na mzee mpaka kila mmoja wetu aliporidhika na kusoma. Sidaiwi deni lolote la shule, mzee wetu na mama wanalipia ada zote mpaka vyuoni. Tena wao ndio waliokuwa wakikopa ada zetu za shule badala yetu. Huo ndio urithi mzee anasema alishatupa. Na alikuwa akisema tusishangae akifa yeye na mama hata nyumba yake ikachukuliwa sababu ya madeni aliyokopa kwa ajili ya shule zetu.”

“Wote sisi watatu tumeiga huo utaratibu. Tunafanya hivyohivyo kwa watoto wetu. Sasa basi. Dada yangu yeye alijaliwa watoto wa kiume, mimi na kaka yangu tulizaa wakike, hakika hatujaona tofauti ya aina ya watoto. Tena nafikiri ni bora sisi wenye mabinti, watoto wetu hawajasumbua sana.”

“Nelly, nikikwambia nina binti wazuri. Ni wazuri wa kila kitu. Si watoto wakusumbuka hata kidogo. Walijifunza maisha wakiwa wadogo. Walipenda shule si wakusuma. Hawajasumbua mambo ya wanaume. Watulivu. Ndio maana Anele alipokuwa akilalamika anahangaika nao, sikuwa nikielewa! Maana kama mama au mzazi, kuna majukumu tu ya kawaida ya uzazi kwa mtoto, huwezi kulalamikia. Kinachoniuma ni kule kuniadhibu mimi, kuchukua binti yangu na kumrithisha kwa Carlos! Halafu wakaja kumgeuza moyo, imekuwa akiniona mimi ni kama mtu wa kumtatulia matatizo yake tu, lakini si baba ninayempenda na kumjali kama Carlos anavyomuaminisha. Inaniuma Nelly, huwa nikikumbuka hilo, siwezi kulala mpaka nakunywa dawa ya usingi. Na ni binti wala si  mtoto wa kiume!”

“Ninachotaka kukwambia. Tokea mwanzo, sijawahi kutafuta mimi mtoto wa kiume au wa kike. Na hiyo tumepata kwa wazazi wetu. Tunapokea kile Mungu anachoona tunauwezo wa kukilea. Nimeishi na Anele sijaona upungufu wake kwa kunizalia mtoto wa kike, na sikumuacha mpaka aliponiacha yeye. Ninachojaribu kukwambia ni, upo hapa na mimi usiku huu nikiwa sijalala najieleza hivi kwako,..” Nelly akaanza kucheka.

“Hakika tena! Yaani mimi mpaka najishangaa kwako Nelly! Au nimezeeka!?” “Bwana malizia.” “Ungekuwa mtu mwingine, yaani sasa hivi ungeshakuwa umeondoka humu ndani muda mrefu sana unipishe nilale.” “Billy!” “Hakika tena. Kwanza kitendo cha kushika mimba, mimi ndio ningekuomba unipishe nifikirie. Eti kwako nataka kufikiria na wewe ukiwepo! Hakika si Billy huyu.” Nelly akazidi kucheka.

“Nakupenda Nelly. Na ninakuahidi tutakuwa sawa tu.” “Kweli Billy?” “Kwa jinsi nilivyokujua wewe, labda ubadilike.” “Siwezi.” “Basi huyo mtoto hatatushinda. Nimekusoma wewe si mlalamishi. Najua hata huyo mtoto akizaliwa na kujikuta na wewe muda mrefu, atakuwa salama tu.” “Na hata kama ukitakiwa kwenda kufanya kazi kwengine, tafadhali uwe na amani. Nenda ukijua mtoto wako atakuwa salama kabisa.” “Hilo nimeshakuwa na uhakika nalo, japo ndio nakwambia, sitaki itokee hivyo ndio maana umeniona nipo kimya nikifikiria. Ipo garama yakulipa Nelly. Sitaki kurudia kosa kwa kisingizio cha kazi.” “Haitakuwa kisingizio, ila sababu ya kazi. Mimi najua umuhimu wa kazi, na bahati ya milango ya cheo inapofunguka. Sitaki usichukue nafasi yeyote ile eti sababu ya huyu mtoto! Hapana Billy. Ikitokea kuna nafasi, popote, tafadhali nenda. Sisi tutakuwa tukija kukutembelea kama utaruhusu, na wewe uwe unakuja kututembelea.” Billy akatulia kidogo akifikiria.

“Turudi ukapumzike Billy, na mimi nijipumzishe kidogo kesho nina mambo ya kufanya ofisini kabla juma halijaanza. Nimekua na juma gumu kwa mawazo ya mshituko nimeshindwa kufanya kazi vizuri. Kesho lazima nienda kazini japo kwa masaa machache.” “Si upumzike kesho ni jumapili!?” “Acha niende japo kwa masaa machache tu. Huwa napenda kujipanga kabla sijaanza juma. Kwa hiyo nakwenda kufunga juma, na kujipanga kwa juma lijalo. Hayo ndio maisha yangu Billy. Sina maisha mengine ila kazi.” “Na ndio maana unafanya vizuri. Hata mtoto akija, utakuwa sawa tu Nelly. Usiogope.” “Nashukuru.” Wote wakatulia kila mmoja akiwaza lake.

“Twende.” Billy akasimama na kumnyooshea mkono. Nelly akasimama na kujikuta mikononi kwa Billy. Mabusu yakaanza hapohapo wamesimama. Nelly akahisi mikono ya Billy ndani kabisa ya nguo yake yakulalia. Akafurahia na kujisogeza zaidi huku mabusu yakiendelea. Alipomtoa nguo yote na kuhamia kwenye matiti, kochi likapata matumizi. Billy akakaa, na kumpakata, mdomo kifuani Nelly akimchezea nywele taratibu akisikilizia midomo yake kwenye chuchu zake. Alipenda jinsi anavyochezea chuchu zake. Uzalendo ukamshinda, akajinyanyua kidogo, Billy akajua anataka amwingilie. Akamkamata vizuri, mapenzi ya haja yakaanza. Taratibu kwa hisia zote wawili hao wakiwa wamehakikishia mapenzi, wakaridhishana, wakajilaza chini kwenye kapeti.

Billy akagundua Nelly amesinzia. Akaenda kuleta mito na vitu vya kujifunika, akamnyanyua kichwa, akamuweka vizuri, akamfunika na kulala pembeni yake akiwa amemkumbatia. “Asante.” Akamsikia akishukuru na ndio akapotelea usingizini kabisa.

Jumapili.

          Isivyokawaida yake siku hiyo  aliamka saa sita mchana. Akajikuta amelala chini peke yake. Akaanza kukunja yale mashuka na blangeti. Akagundua Billy anaongea chumbani. Akajua anazungumza na watu wa kwao. Akaweka vitu pembeni ya kochi, akamtumia ujumbe. ‘Naondoka.’ Wakati anafungua mlango atoke, akamsikia Billy. “Nelly! Nelly! Nelly!” Akajua amepata ujumbe ndio anaita kwa kupaniki. ‘Billy anakua kama mtoto anayenyonya!’ Akawaza akiwa amesimama akimsikiliza anavyoita.

          Akatoka kama anayekimbia. “Kwa nini huniitiki?” “Unapiga kelele, hata ningeitika usingesikia. Ndio maana nimeona nitulie tu.” Billy akaanza kucheka kama kawaida yake. “Sikutaka kukusumbua, nimesikia ukizungumza na simu. Na mimi nimechelewa kuamka, nina mambo mengi leo.” “Ulilala vizuri?” “Nashukuru nimelala na mwili nao umetulia.” “Akili?” “Pia. Akili ilikuwa imechoka na nimejawa hofu. Nashukuru kwa muda wako wa jana. Ile kuzungumza na mimi imenisaidia kujua moyo wako na kunituliza.” “Nakupenda Nelly.” “Najua. Sasa hivi nimejua. Na mimi nakupenda Billy.” Wakacheka. “Basi nitakuona baadaye. Acha mimi nianze siku. Lazima niende kazini na saluni.” Wakaweka mipango ya jioni. “Tafadhali usisahau kuzungumza na Jax.” “Watakuja, usiwe na wasiwasi.” Nelly akajibu na kutoka.

Nelly, Jax, Billy na Lara.

L

ara hakujikosea. Na yeye alijitengeneza akapendeza kutokana na aina ya hoteli waliyoalikwa kwa chakula cha usiku. Jax alikuwa na wasiwasi mpaka akamuogopesha na Lara. Wakawa wamependeza ila kama watoto wa shule ya msingi waliokosa, sasa wameitwa ofisi ya mwalimu mkuu. Njiani kimya wakielekea huko kukutana na Billy pamoja na Nelly.

          Waliwakuta nje wakiwasubiria. Lara akasalimia kwa goti, Billy akaanza kucheka kama kawaida yake. “Acha bwana Billy!” “Sasa mimi nimefanyaje?! Mbona nafanya kama ulivyoniagiza.” “Sasa kwa nini unacheka?” “Nimefurahi! Nalo hilo ni kosa?” Wakabaki wanazungumza wao wawili, Lara na Jax wametulia. “Acha bwana! Unazidi kuwatia wasiwasi. Wewe si umesema usiku wa leo unataka uwe mtulivu?” “Ila sasa umeona wageni wetu wenyewe?” “Wewe ndio unawatia wasiwasi.” “Basi Nelly. Haya Jax habari?” “Nzuri.” “Na Lara, hujambo?” “Sijambo. Shikamoo.” Lara akasalimia tena. Billy akazidi kucheka, hana mbavu.

          “Twendeni. Achaneni na Billy. Huwa anakuwa kama anaakili za kitoto!” Nelly alizungumza kiswahili. “Ni kama nimekuelewa Nelly! Umenisema kwa watoto.” Nelly akamtizama na kuanza kuingia ndani. “Twendeni.” Billy akamkimbilia. “Nelly?” Akamuita lakini Nelly akaendelea kutembea. Lara akamvuta Jax shati karibu alichomoe. Akasimama. “Kumbe hazungumzi kiswahili?!” “Kwani sijakwambia?” “Bwana Jax!” “Lakini anajua maneno machache.” “Jax wewe! Yaani usiku huu mzima mimi nitakuwa na kazi ya kuzungumza kingereza tu! Si kichwa kitaniuma!” Jax akaanza kucheka. “Ungeniambia bwana!” “Nilisahau. Sikujua kama litakuwa tatizo kwako. Kwanza si ulisema ukiingiwa na wasiwasi unaongea kingereza tupu?” “Si kwa muda mrefu bwana! Ni maneno machache na wewe!” Jax akazidi kucheka akimtizama Lara jinsi alivyopaniki.

          “We Jax?” Akamsikia Nelly akimuita. Jax akageuka na kuondoka kwa haraka, Lara akaanza kumfuata. Wakaongozana mpaka ndani kabisa sehemu ya kula chakula. Palikuwa pazuri na palionekana pa hadhi ya juu sana. Lara hakuwahi kufika hapo japo anapafahamu. Billy alimvutia kiti Nelly ndipo akakaa. Lara alijivutia kiti mwenyewe na kukaa.

          Muhudumu akafika hapo. Nelly akaagiza wine. “Oooh, No!” Billy akakataa mpaka muhudumu akashituka na wote wakashangaa. “Hapana. Hawezi kunywa wine.” “Ni nini Billy!?” “Na mtoto wangu? Huwezi kunywa kinywaji chochote kile chenye kileo ukiwa mjamzito Nelly. Inamadhara kwa mtoto. Naomba ujikaze, mpaka ujifungue na umalize kunyonyesha.” “Billy wewe!” “Kwani hukuwa ukijua!?” Nelly na yeye akashangaa sana. “Hakika Nelly. Tutakwenda hata kwa daktari akueleze kitaalamu. Lakini naomba kwa sasa epuka kabisa kileo chochote. Pole, lakini ndivyo ilivyo.” “Mimi sikujua. Basi naomba juisi ya chungwa.” Nelly akawa amepoa.

          “Pole. Ndio umama huo.” Nelly akamtizama na kunyamaza. Na yeye akaagiza kinywaji. Na wengine pia wakaagiza. Mtu wa chakula akaja na kuwaachia Menu. Wakatulia kila mmoja akisoma menu. “Umeshajua ni kitu gani utataka kula?” “Bado sijapata chakunivutia.” Nelly akabaki akiangalia ile menu. “Wewe umeshajua nini chakula?” Nelly akamuuliza kwa kujali wakati Lara na Jax nao wakiendelea kutafuta chakula kwenye menu.

          “Sielewi Jax!” Lara akanong’ona. Nelly akasikia, kabla Jax hajajibu yeye akamjibu. “Usiogope. Muulize huyo muhudumu kila chakula ambacho hukifahamu lakini unafikiri kinakuvutia. Atakuelekeza mpaka jinsi wanavyopika. Ndio kazi yao hao.” Nelly akamuita kwa karibu yule muhudumu. “Naomba msikilize na umuelekeze.” Kidogo Lara akatulia. Akaanza kuuliza maswali akawa anaelekezwa. “Umepata?” Billy akamuuliza. “Nahisi nitakula grill steak, lakini iwe well done. Ila nitaomba wasiunguze.” “Utakula na nini?” “Ndio nafikiria. Labda bake sweet potato.” Nelly hakutaka mengi. Akaagiza hiyo nyama choma ya ng’ombe na kiazi kitamu cha kuokwa. “Tena sweetpatotoes ni nzuri kwa afya yako na mtoto. Naona umefanya uchaguzi mzuri.” “Ujue utanichosha sana ukianza kunichunga sasa hivi na kila ninachokula kwa mtoto ambaye hata hana mikono!”

          “Nelly! Mtoto yupo. Na sasa hivi akiwa anatengenezwa, tafadhali zingatia lishe yako kwa ajili yake pia. Yupo. Na tulimuona. Usidhara kwa sababu hajakamilika ndio usimzingatie!” “Basi utanichosha mapema sana.” “Usifikirie hivyo. Ni kubadili tu mlo. Kwa mfano hivyo ulivyoagiza sasa hivi si umependa?” “Ndiyo.” “Basi ndio hivyohivyo, ila tu kuhakikisha huli tena makapi. Kila unachokula hakikisha kinamanufaa kwako na mtoto pia. Utakuwa sawa Nelly. Na ukizingatia hivyo, utabeba huyo mtoto wewe mwenyewe ukijisikia vizuri, sio mchovu. Lasivyo utajikuta mtoto anachukua kila kitu anachohitaji mwilini mwako, halafu wewe ndio unabakiwa na mapungufu.” “Hapa kazi itakuwepo, hapa!” Nelly akaongea kwa sauti ya chini kwa lugha ya kiswahili na kurudisha macho kwenye menu.

          “Basi niongeze matunda, na mboga za majani.” Billy akacheka kwa furaha. “Muone alivyofurahi! Unapenda kusikilizwa wewe!” “Sitaki uchoke. Nataka usianze kuwa mgonjwa sababu ya kutokula vizuri, ukamsingizia mtoto.” “Sasa na wewe unakula nini?” Wakaendelea kuulizana wao wenyewe. Ila Jax akajua anamjali dada yake. Akafurahi.

          “Umependa nini?” Jax na yeye akamuuliza Lara. “Naona niagize prons na mashed potato.” “Nzuri.” “Na wewe?” Lara akamuuliza. “Nitakula grill steak, medium rare.” Lara akamtolea macho, Jax akacheka akijua hajaelewa. Akataka kumuelezea, akaona Billy na dada yake wanawatizama. “Utaona wakileta.” Billy naye akataka kama Jax, lakini yeye akataka na ndizi za kuchoma.

          “Unawatoto wa ngapi, Billy?” Jax akauliza swali la moja kwa moja mpaka akamshangaza Nelly. “Asante kuuliza. Nilijaliwa mabinti wawili. Acha nikuonyeshe picha zao.” Billy akatoa simu yake kwa furaha zote. Akamuonyesha yule mkubwa. Jax alishangaa, akarudisha macho kwa Billy kisha kwenye simu tena, akamuonyesha na Lara. “Ni mtoto wake.” “Waw!” Lara akashangaa kwa sauti. “Kumbe unabinti mkubwa hivi halafu mzuri sana. Ni mwana mitindo?” Nelly akacheka. Billy akamuuliza amesema nini. Nelly akamuelezea. Billy akaanza kucheka. “Sema tena kwa kiswahili.” Akamtaka Lara arudie. “Nimeuliza kama..” “Hapo utampoteza. Wewe rudia tu hilo la mwanamtindo. Basi.” “Ehe! Hilohilo neno ndio nataka kusikia.” Billy akadakia. “Sema tena Nelly.” Akataka Nelly arudie. “Wewe mwache Lara mwenyewe akuulize.” Lara akarudia kwa kifupi. Billy naye akalirudia, wakamrekebisha mpaka akaelewa.

          “Sio mwanamitindo. Ila tu anajipenda na anapenda nguo nzuri. Kwa kifupi anajijulia. Anaakili sana. Ni mtoto..” Billy akaanza kumsifia huyo binti yake mkubwa wakimsikiliza. “Hapo hatamaliza.” Nelly akamsengenya kwa sauti ya chini kwa kiswahili. “Waonyeshe na mdogo wake sasa.” Nelly akamkumbusha. Hapo Billy akaweka uzito. Akawazungusha kwa maneno mengi akaishia kusema atawaonyesha siku ingine. Akajua kuna alichomuudhi siku hiyo, hataki kuwaona yeye na mama yake.

          “Mama yao yuko wapi?” Jax akauliza tena. Nelly akamtizama Jax kwa kumshangaa. “Nataka kumfahamu!” Jax akamjibu dada yake. “Na mimi napenda tufahamiane.” Billy akajibu yeye na kuwapa historia yake ya ndoa kwa ufupi, mpaka  Jax akaonekana kuelewa na kuridhika. “Pole sana Billy.” “Ndio maana nataka kumuoa Nelly.” Nelly akakunja uso, Lara na Jax wakashangaa.

          Wakamuona anatoa kimkoba mfukoni, akavuta kiti nyuma, akapiga goti. Lara alivyoona tu vile akatoa simu yake. Ila Jax yeye akabaki amepigwa na butwaa na kushangaa sana. Billy akatoa ile pete kwenye kimkoba. Akamuuliza tena. “Will you marry me, Nelly?” Akamuuliza tena kwa kumaanisha, sio tena kwa mzaha kama kawaida yake akitaka kujua kama atakubali amuoe. “Kubali tufunge ndoa. Tuishi kwa utulivu. Tupeane kile wengine wameshindwa kutupa, na kingine cha muhimu, tulee mtoto wetu.” “Kwa nini unataka tuweke mazingira ya kuja kushindwa badaye Billy? Kwa nini unataka kuja kujiumiza tena? Haya maisha hapa Tanzania si yako. Siku moja utakuja kuondoka, na mimi sina mpango wakuacha kazi yangu. Unataka kurudia tena kosa lilelile la mwanzo?” Nelly akamuuliza na yeye hayo maswali kwa kumaanisha kabisa, mwenzie akiwa amepiga magoti. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment