“Nilikwambia sina shida ya kukosea na wewe.” “Billy!” “Sasa bora lipi Nelly? Tujaribu, tushindwe au tusijaribu kabisa?” “Mimi sijui Billy.” Jax na Lara wakabaki wameshangaa. “Mimi naona ni bora tukubali yote kwa asilimia zote. Maswali mengine yote, yaje yajijibu baadaye. Kama hili la mtoto, hatuna majibu yote, lakini kila siku inajijibu yenyewe. Kama leo umejua hakuna kunywa wine, mpaka azaliwe. Umeacha. Leo itapita, tutakabiliana na kesho tena. Hatuwezi kupanga kila kitu leo wakati hatujui kesho itakuaje. Ninachotaka kukwambia ni kuwa, usifungue milango kwa hofu ya leo, tukashindwa kufurahia leo.” Nelly akatulia.
“Magoti yanauma!” Nelly akaanza
kumcheka. “Nelly!” “Anza tena.” Nelly akamwambia huku akicheka sana. “Kweli
Nelly?!” “Juu ya nini?” Nelly akajifanya kama hakumbuki tena. “Unanicheka!?”
“Wewe anza upya. Hata sikumbuki kinachokufanya upige magoti hapa ni nini!” Jax akacheka
taratibu na kuinama vile dada yake alivyokuwa akimfanyia dhihaka Billy. “Kweli
Nelly?” Nelly akazidi kucheka mpaka akainama.
“Sawa Nelly.” “Usichoke Billy.” “Wewe
kwako sitachoka.” “Ona ulivyo mtu mzuri. Haya anza, nakusikiliza.” Billy
akaanza kucheka na yeye. Wote wakaanza kucheka. “Si ukubali tu nikuvalishe?” “Nikubali
nini?” Nelly akamuuliza. “Sawa Nelly. Acha mimi nianze.” Akajiweka sawa. Mpaka
akatengeneza na shati. “Mpigeni picha ili akili yake ikirudi, kiburi kikianza tena,
tuje tumuonyeshe huu wakati.” Nelly akafanya Jax na Lara wacheke tena. Jax na yeye
akatoa simu yake.
“Nelly, will you marry me?” “Yes,
Billy.” Akataka kunyanyuka ambusu. “Nivalishe kwanza Billy, acha kuruka hatua!
Wewe vipi bwana!?” “Acha kwanza nifurahie.” “Hapana Billy bwana! Ujue
nitabadili mawazo mimi?” Billy alicheka sana. “Nelly anajua kuniringia!” “Wewe
nivalishe pete kwanza.” Akamvalisha ndipo wakaanza mabusu hapo. Nusura Jax
aondoke. “Umefurahi?” “Sana. Acha nimwambie binti yangu na mama. Wapo macho
wanasubiria kujua kama umekubali.” Wote wakashituka. “Billy?” “Sasa wewe
unafikiri ni siri?” Nelly akaanza kujitengeneza.
Billy na yeye akaanza kumcheka. “Acha
bwana Billy!” Billy akachukua simu yake, akapiga videocall,
chakushangaza akakuta mpaka baba yake anasubiria. “Amesemaje?”
Wote wakauliza kwa pamoja, Billy akaanza kucheka. Akamvuta mkono Nelly
akaweka kwenye simu. Wakamsikia binti yake akishangilia. “She said, ‘Yes’.” “Hongera sana Billy.” Baba yake
akampongeza. “Asante baba. Lakini usingekesha
ukisubiria! Ningekupigia kesho kukutaaribu.” “Nilipomuona Britney amekuja hapa
kwa bibi yake na kumuomba wakae naye asubiri ajue kitakachoendelea huko,
nikaona niungane nao kusubiri.” “Pole. Lakini nilimwambia Britney asiwe na wasiwasi
kila kitu kitakwenda sawa!” Kidogo kama Billy akawa akilalamika kukuta
mpaka baba yake alikuwa akisubiria hilo. “Usijali.
Tumekuwa na wakati mzuri.” “Basi acha Nelly na mdogo wake wawasalimie.” Billy
akamkabidhi Nelly simu.
Kwa mara ya kwanza Nelly akazungumza
na wazazi wa Billy pamoja na binti yake mkubwa. “Ni
mzuri zaidi kuliko kwenye picha.” Nelly akamsifia na kumfanya acheke. “Usiwe kama dad!” “Ni kweli. Na nimefurahai kuzungumza na
wewe, Britney.” “Nikuulize kitu?” Britney akataka kuweka msisitizo
kwenye swali lake akimtaka Nelly kuzingatia. “Niulize
chochote tu, karibu.” Nelly akajibu. “Unampenda
kwa dhati baba yangu?” Nelly alishituka, akamtizama Billy. Billy akabaki
akimwangalia.
“Nataka
kujua.” Akamsikia Britney akiongeza upande wa pili. Mpaka wazazi wa
Billy walikuwa kimya. Jax akabaki akimtizama dada yake. Nelly akatulia kama
anayetafakari akijua wanamsubiria. Akacheka kidogo, akamtizama Billy na
kurudisha macho kwenye simu. Akakuta huyo mtoto ametulia, akisubiria.
“Labda nikwambie
vile ilivyo, pengine utaelewa kwa urahisi.” Akaanza Nelly. “Billy ni sehemu ya maisha ambayo ilikosekana kwa muda wote,
na sikuwa nikijua kama kuna kitu nakikosa au nakihitaji mpaka alipokuja yeye.”
Nelly akatulia kidogo kisha akaendelea. “Ameongeza
maana nyingine ya maisha ambayo sikuwahi kujua kama naiweza kuishi au hata kama
nastahili kuipata. Na..” Wakamuona amesita kidogo ila akaendelea. “Naweza nisiwe na lugha nzuri yakueleza, lakini ni mtu ambaye
naomba Mungu nisije kuishi hapa duniani bila yeye.” Akamuona yule binti
akijifuta machozi.
“Waw! Jamani dada Nelly!” Akasikika
Lara. “Yeah! Nampenda Billy.” Akamwangalia Lara kuweka msisitizo mpaka
akatingisha na kichwa. Akarudisha macho kwenye simu. “Kwa
hiyo kujibu swali lako Britney, ni ndiyo. Nampenda baba yako. Sana.”
“Mimi nilijua tu, lakini ukawa unanibishia.” Billy akaongeza na kufanya wote
wacheka. “Thanks sweetheart.” Akamsikia mama
yake akisema upande wa pili. Kisha akasogea kwenye simu. “Namaanisha kutoka ndani ya moyo wangu, Nelly. Asante.” Akaongeza
huyo mama na kuendelea. “Billy amekuwa akiniambia, na
nikatamani kukusikia, lakini sikuwa jasiri kukuuliza kama Britney. Kwanza
niliona ni mgeni kwetu, sikutaka kuweka wasiwasi. Lakini nimefurahi kukusikia. He
is my baby.” “Sasa hapo mama unaharibu. Nilimwambia Nelly mimi ni kaka
mkubwa, mwenye mdogo wangu!” “Dad hakui hapa nyumbani.” Akaongeza mwanae.
“Haya kwaherini. Naona mnaniharibia sasa.” Wakazidi
kucheka.
“Love you
dad.” “Love you too sweetheart. Ukalale sasa.” “Haya enjoy.” “Billson?” Akasikia
baba yake akiita. “Yes, dad.” Akaitika kwa
heshima zote. “Hujatutambulisha mdogo wake.” “Ni kweli.
Huyu hapa. Ndiye tunayefanya naye kazi.” Akamkabidhi simu Jax.
“Wasalimie.” Jax alikuwa ameingiwa na hofu, akapokea akitetemeka. Akawasalimia
wote kisha akamtambulisha na Lara. “Mungu akipenda
nitamuoa hivi karibuni. Mnakaribishwa.” Akaongeza Jax. “Kweli?” Britney akadakia kwa kuhamasika. “Eti Nelly?” Billy naye akauliza kutaka uhakika wa huo
ukaribisho. “Kabisa. Tutapanga vizuri na Billy kisha
atawajulisha. Lakini tungependa kuwaona. Karibuni sana.” Wakamsikia
Britney anashangilia. Wakacheka.
“Lakini
nafikiri mtaanza safari ya huku kwanza. Kama Billy atakuwa hajabadilika,
alisema anataka kuoa kwa haraka.” Nelly akakunja uso. “Sijazungumza na Nelly, baba! Yale yalikuwa mawazo yangu tu.”
Billy akajihami. “Oooh! Basi nimeharakisha.” Wakacheka
lakini Nelly akabaki akimwangalia Billy. “Usiogope. Tutazungumza.” Wakaagana.
Nelly akabaki akimwangalia. “Unakumbuka
nilikuwa nikikudai kutoka mara ya nne?” “Billy!” “Tulikubaliana Nelly. Najua
tumetoka zaidi ya mara nne, lakini naomba kumbuka zangu za makubaliano yetu
zilikuwa nne. Tumeshatoka mara tatu. Unguja, Afrika ya Kusini na Kilimanjaro. Ya
nne ndio niliwaambia tutakwenda nyumbani, na kama utakuwa umekubali basi
ndio tutafunga ndoa. Hii safari ya safari hii sio suprise. Nilipanga kukwambia
na tuandae safari.” “Lini sasa?” “Mapema. Hatuna sababu ya kusubiri. Tunakwenda
kufanya yote kwa pamoja, kisha tukitoka fungate ndio tuna...” “Hivi wewe Billy
ujue unamipango mingi ambayo mimi siijui!” Billy akaanza kucheka kama kawaida
yake.
“Sasa hapo unachocheka ni nini?!”
“Kwamba na hili liliendelea kupangwa bila wewe kujua. Hivi nilikwambia ni sawa
kuwa sio kila kitu uwe unapanga wewe wakati mwingine ni sawa..” “Acha Billy.
Hii natakiwa kujua bwana. Sasa wewe ulifikiri nasafiri vipi bila kupanga likizo
yangu!?” “Ningekwambia Nelly. Baba ndiye ameharakisha. Acha wasiwasi. Na utulie
usianze kukasirika. Ni jambo zuri.” Nelly akamtizama na kunyamaza.
“Hongera.” Lara akapenyeza pongezi
zake kwa hofu. Nelly akacheka na kuitizama ile pete. “Umeipenda?” Billy
akauliza. “Ni nzuri, asante Billy.” “Karibu na nimefurahi kwa kuwa umeipenda.”
“Na Lara, asante kwa pongezi. Ila nawashukuru sana.” Lara akawa hajaelewa.
“Nyinyi mmenifanya kuamini kama kuna kupendana. Na Jax naye alinifanya...”
“Badili lugha, Nelly!” Billy akamlalamikia. “Sio lazima kila kitu kusikia.”
“Acha Nelly.” “Hujapitwa bwana. Nilikuwa nikimwambia Lara na Jax kuwa wao
wamekua sababu ya kukukubali. Wameweka mfano mzuri wa mapenzi, katika shida
zote walizopitia, bado wamethibitishia kila mtu kwamba, kitu walichonacho ni
cha thamani kutunza kiasi chakuweka hisia zao pembeni na kurudiana kwa ajili ya
hicho kitu.”
“Ndipo Jax aliponionya juu yako,
niache kuwa mkorofi, sio kila mtu ni mbaya, ndipo na mimi nikajiambia nijipe
nafasi, pengine naweza kukipata hicho Jax alichokiona au kukipata kwa Lara. Kwa
hiyo nawashukuru kwa kuweka mfano mzuri. Japo nyinyi ni wadogo kwangu lakini
mmenifundisha kitu.” Simu ya Billy
ikaanza kuita. Wakamuona ameiangalia na kucheka. “Mama bado hajalala huko!” Akaongea
Billy huku akicheka na kupokea.
“Hongera sana.
Mama amenimbia.” “Nilimwambia alale.” Akamjibu kaka yake. “Alikuwa na wasiwasi mpaka nikaenda kukaa naye leo jioni
kidogo kumtoa mawazo kwako. Hongera sana.” “Nashukuru Mungu. Naamini safari hii
na mimi nitapumzika.” Wakamsikia Billy akicheka sana baada ya
kusikiliza. Mara akaangalia tena simu. “Beila naye
anapiga. Mama atakuwa anakazi ya kutangaza tu! Acha nimuunge.” Billy
akamwambia Brandon, kaka yake. Akaishia na kumuongeza mume wa Beila pia. Vikajaa
vicheko kwa ndugu hao wakimpongeza Billy. Nelly akashangazwa sana kugundua
kumbe upande wa pili huko wote walikuwa wakisubiria kuvalishwa kwake pete!
Akabaki ametulia, akapotelea mawazoni.
Akasikia Billy akisema yupo hapa
mwenyewe. Akamkabidhi simu. Nelly akajikaza na kuipokea. Wakamsalimia na kumpa
pongezi. Nelly akamtambulisha na Jax, Jax naye akamtambulisha Lara, ndipo
wakarudisha simu kwa Billy. Wakazungumza ndugu hao na kuwaaga.
“Nyinyi kwenu mnaonekana ni watu wa familia!” Nelly akaongeza. “Ni mama huyo. Mama ndiye anapenda kufanya jambo la mmoja ni kama la kila mmoja kwenye familia. Mume wa Beila alikuwa akishangaa, mpaka sasa hivi namuona yeye ndio amekuwa kama mama!” “Nimemsikia. Anaongea kuliko hata kaka yako!” Nelly akaongeza. “Sasa akitoka hapo, ujue yeye anaenda tena kumpigia simu mama na kumwambia kila kitu.” “Tena?” “Nakwambia yeye ndio yupo karibu na mama kuliko hata Beila mwenyewe. Lazima kila siku wazungumze na mama. Na huwa hawana agenda mpaka tumeshawazoea. Wanaweza kupigiana simu juu ya jambo hilo, wote mkachoka, lakini wao ndio likawapa sababu yakuwa kwenye simu hata zaidi ya dakika kumi wakilizungumzia hilo jambo tu.” Wakazungumza mengi wakifahamiana zaidi na kula na kunywa ndipo wakaagana.
Safari ya Ukweni.
N |
elly
na mdogo wake pamoja na Lara waliondoka nchini na mwenyeji wao Billy kuelekea
nchini Uswiz, wakiwa wanasubiriwa na familia nzima. Lara alifurahia sana hiyo safari.
Hakuwa akiamini kama na yeye yupo safarini. Tena anapokwenda kulihisika ni pa wenye
heri! Alijawa furaha akasahau hata mambo ya harusi yake ila harusi ya wifie.
Maana ilikuwa ndio wanakwenda kufunga ndoa kabisa, yaani wakirudi wanakuwa
walishafunga ndoa.
Yakawa mapokezi mazuri mno.
Watoto wa Billy, Britney na Briana, wote walikuwepo. Ila ni kweli hata Nelly
alihisi huyo mdogo, Briana ni kama amelazimishwa kuwepo hapo. Alimuonyesha
dharau za waziwazi Nelly. Na hata alipompa mkono, hakutaka kushika mkono wa
Nelly. Billy aliona, ikamuuma sana, ila binti yake mkubwa akaingilia kati kwa
haraka kwa kuushika yeye mkono wa Nelly. Muda mwingi alikuwa kwenye simu. Hata
alipoongeleshwa, alijibu macho kwenye simu yake.
Walikuta vyumba viwili vimeandaliwa kwa ajili yao, hapohapo nyumbani
kwa kina Billy. Yaani kwa wazazi wake. Walionekana watu wazima lakini
waliostaafu wakiwa na pesa. Weusi hao waliishi kwenye mtaa wa kitajiri sana. Nyumba
kubwa nzuri na ya thamani. Akajua ndiko alikotolea maringo yake huko. Alitokea
kwenye familia yenye uwezo.
Mama yake aliandaa chakula cha watu wote jioni hiyo, kama kuwakaribisha
wa kina Nelly kwenye familia. Walikuwa ndugu tu. Nelly akapata nafasi yakuwaona
wote na watoto wao. Bado Briana, mtoto wa Billy akawa akifanya vituko vya
kukera kila mtu, na wenyewe wakawa kama wanamuogopa. Akijibu vibaya,
wananyamaza tu, hakuna anayeweza kumuongelesha. Ila Nelly akamuona Billy
amebadilika.
Wakati wanaandaa chakula na kuweka mezani, akamsogelea Nelly huko
jikoni kwani Nelly alivutiwa jikoni na Beila mdogo wake Billy anayemfuata,
mtoto wa kike wa pekee hapo kwenye hiyo familia. Dada mtu mzima tu, mkubwa hata
kwa Nelly. Beila alipotoka tu hapo na mama yake kufuatilia kitu upande mwingine
wa nyumba ndipo huyo binti mdogo wa Billy, Briana akamsogelea. “Kwa nini
unataka kuolewa na baba yetu?” Kabla Nelly hajajibu, akaendelea. “Maana wengine
wanampendea pesa. Wengine wanataka tu kuitwa jina lake. Sasa wewe unataka nini
kwake?” Alikuwa binti mzuri sana kwa kumtizama. Nadhifu lakini alijawa kiburi
na dharau mpaka akikutizama unaweza ukajishuku. Sasa akakutana na Nelly, dakika
kadhaa mbele. Kwanza hakupenda jinsi alivyomuuliza. Alibaki akimtizama,
akifikiria jibu la kumpa huyo mtoto ili asiharibu hapo ukweni, maana alishamkera
Nelly mpaka mwisho.
“Nelly!” Billy akaingia hapo bila kutarajia. “Huna haja ya kujibu
hilo. Twende.” Billy akanyoosha mkono. Nelly akasimama akataka kutoka, lakini walipofika
mlangoni akamwachia Billy mkono na kurudi karibu na yule binti, kwa karibu
kabisa, wengine wote waliokuwepo pale jikoni wakawa wamepigwa na butwaa.
“Mbali na pesa. Jina na mengine mengi yaliyokuwepo kwa baba yako.
Ukitulia. Ukampa nafasi, ukimtenga na mengine mengi hata mapungufu yake,
utagundua katikati ya yote hayo na hata uliyoyataja, ndani yake yupo mwanadamu
anayestahili kupendwa yeye kama Billy. Wakati mwingine jaribisha na wewe,
utagundua yeye ni zaidi ya pesa, cheo na jina lake.” Jeuri Nelly akampaka kama
sekunde 10 hivi kuhakikisha hana swali la nyongeza, akimwangalia machoni kisha
akaondoka hapo kumfuata Billy pale alipokuwa akimsubiria kwenye mlango wa kutokea
pale jikoni. Ukweli Billy alifurahi sana. Waliacha pale jikoni wote wamesimama
kwa mshangao wakimtizama yule mtoto wa Billy.
“Mnashangaa nini sasa?” Akawauliza kwa hasira, bibi yake akaingia.
“Kila kitu kipo sawa hapa?” “Wewe unafikiria nini?” Akamjibu hivyo bibi yake na
kutoka. Ikaanza minong’ono huko jikoni. Chakula kikaandaliwa na kuwekwa mezani.
Watu wote wakaitwa hapo mezani. Huyo binti akaja hapo mezani wa mwisho na simu
yake mkononi. “Diva ameingia.” Junior, kijana wa Beila, dada yake Billy
akarushia neno. “Nani unamuita Diva?” Wakaanza kubishana wao wawili mbele ya wazazi
wao. Junior na Briana.
“Kwanza mimi wangeniambia wewe utakuwepo, nisingekuja.” Akaongea
Briana. Billy akaweka uma na kisu chini kwa nguvu. “Huna lazima ya kuwepo hapa
Briana.” Kila mtu akashituka mpaka Briana mwenyewe aliyezoea kubembelezwa na
baba yake. “Umenisikia na kunielewa?” Billy akauliza kwa ukali mpaka wote
wakatulia. “Huna sababu na hulazimishwi kuwepo hapa. Hii ni familia moja,
tumekutana kujenga si kubomoa. Kama wewe unajisikia shida kuwepo katikati ya
hata mmoja wetu hapa, dereva atakurudisha kwa mama yako.” Mpaka Britney
akashangaa.
“Yote haya ni sababu ya kumuuliza swali dogo tu huyo Nelly?” “Hivi
karibuni ‘huyo Nelly’ anakuwa mke wangu na yeye atakuwa mama wa mtoto wangu.”
Wote wakashituka. “Sitaruhusu yeyote kati yenu amvunjie heshima. Ukiona umeshindwa
kumuheshimu, ondoka.” Pakazuka ukimya, Briana akasimama kwa hasira na kuvuta
pochi yake. “Na Briana.” Baba yake akamuita kabla hajaondoka. Akageuka machozi
yakimtoka. “Huna sababu yakuja hata kwenye harusi yangu. Na ninakuahidi
sitakusumbua tena.” Hiyo ilikuwa habari kubwa sana kusikika kwa kila mtu.
Briana mwenyewe alionekana kuingiwa hofu. Akasimama pale kwa muda.
Akamtizama babu yake kama anayetaka amtetee lakini ikawa kinyume. “Dereva
atakuwa tayari utakapokuwa tayari kurudishwa kwa mama yako.” Watu wote kimya,
Lara akabaki kuangalia waafrika hao uzunguni. Wote walionekana wamestaarabika
sana. Watoto wengi waliokuwepo hapo kasoro ya hao binti za Billy, walichanganya
damu ya kizungu. Na vile wazazi wao walivyokuwa weupe, walibeba rangi nyeupe
zaidi. Lara na Jax kimya wakisikiliza na kuangalia ya uzunguni.
Briana akasimama kwa muda, chakushangaza wakamuona amerudi kukaa.
Pakazuka ukimya kwa muda, kila mtu akarudi kula. “Billy?” Baba yao akaita,
Billy akaitika. “Umesema Nelly ni mjamzito?” “Ndiyo. Amemaliza mwezi wa nne.”
Kila mtu akashangaa. Hapo ndipo Briana akanyanyuka na kuondoka kabisa. Hakuna
aliyetegemea Billy kupata mtoto tena. Nelly akabaki ameinama.
“Hongereni.” Akadakia mama yao. “Nelly, hongera sana.” Akaongeza
akimwangalia Nelly. “Asante.” Ndipo sasa wengine wakaongeza pongezi na utani.
“Mbona wewe Britney hushangai?” “Dad alishaniambia.” Nelly akashangaa na
kumtizama Billy. Billy akaanza kucheka. Akatamani amwambie kitu, lakini kila
mtu alikuwa akiwaangalia. “Wewe sema tu.” Billy akamkejeli akicheka sana. “Mimi
sina usemi Billy.” Akamjibu kama anayemwambia tutaonana baadaye.
Wakamaliza kula wakizungumza na kucheka, hakuna hata aliyekumbuka
swala a Briana. Lakini Nelly alikuwa amechoka sababu ya safari, akataka awahi
kwenda kupumzika. Wakatoka hapo wote wanne. Lara na Jax na wenyewe wakawa
wameshatosheka kwa siku hiyo. Wakaamua kwenda chumbani kwao wakatete ya
uzunguni.
Maandalizi ya Harusi.
Mama, dada na shemeji yake Billy, huyo mwanamke wa kizungu aliyeolewa
na kaka yake Billy wakataka kumsindikiza Nelly kutafuta gauni la harusi. Ikamgusa
sana Nelly. Wote walikuwa ni watu na majukumu yao tena mazito. Lakini wakaahirisha
na kuamua kumsindikiza yeye! Hilo likamfurahisha na kumgusa sana Nelly. Lara
naye akaomba kuongozana nao. Wakiwa kwenye hilo duka la nguo za harusi, Nelly
akitafuta gauni lake, Lara naye akaona gauni alilopenda sana. Nelly akamuona
kila wakati analishika. Anazunguka, lakini anarudi palepale kwenye lile gauni. Analiangalia.
Anajiweka nyuma yake. Akiangalia bei, anaondoka. Nelly akamuona amefanya hivyo
kwa muda mrefu tu, akirudiarudia.
“Kama umelipenda, si unajua unaweza kwenda kujaribu kwa kulivaa
kabisa sio hivyo unavyosimama nyuma yake?” “Naona kama tamaa! Nimevutiwa na
haya manyoya ya tausi walivyoyapanga vizuri kwenye gauni zima! Sijawahi ona
kitu kizuri hivi, kilichotengenezwa kwa ustadi wa hali ya juu! Nimelitamani japo
bado ninalo lile la mwanzoni.” “Wewe nenda kajaribu, ulinganishe. Nakuona
umeshindwa kutoka hapo.” “Kweli nimependa. Ila bei!” “Huyo Jax anamajukumu gani
ya kushindwa kununua gauni la harusi? Kama atashindwa kununua gauni lako, basi
aache kazi!” Wakaendelea kuzungumza wawili hao kwa lugha ya kiswahili, na
wenyeji wao wakiwa sehemu ya kusubiria.
Lara akachukua lile gauni na kwenda kujaribu. Akatoka kwenda chumba
cha pili alichokuwepi Nelly. “Asipolinunua hilo gauni Jax, mimi nitakununulia.
Umependeza sana, Lara. Sana.” “Ila ni garama!” “Wewe mtoto mbona unapenda kujiliza
shida? Si nimekwambia nitakununulia mimi?” Lara akacheka kwa wasiwasi. “Asante
wifi yangu.” “Naona umefurahi mpaka umeweza kuniita wifi!” Lara akacheka kwa
furaha. Hakuamini kama hilo gauni ndio limekua lake. Nelly akarudi ndani
kujimalizia kuvaa.
“Eti mimi naona umependeza na lile gauni la pili!” “Hata mimi naona
hivyo, ila hawa wakwe wanataka kuanza kunichanganya. Sasa acha nitoke hapa hii ndio
itakuwa mara ya mwisho kabla sijawabadilikia.” Lara akaanza kucheka, alimjua
Nelly. “Kwanza hata hili sivai. Nimechoka mimi.” “Jikaze umalizie ukawaonyeshe
mara ya mwisho. Unaweza kupendeza zaidi.” “Na wewe usiwe mtu wakuyumbishwa!”
Akamjibu na kuendelea kuvaa maana alitaka kuvua.
Mpaka wanarudi nyumbani, Lara naye akawa amenunua kila kitu kipya cha
harusi, Nelly ndiye aliyekuwa akimnunulia bila hata kujali pesa. Na Nelly naye
akapata nguo nzuri sana, na ya hali ya juu.
Harusi ya Billy na Nelly.
S |
iku
ya harusi akiwa kwenye chumba alichokuwa akikitumia kwa kulala yeye na Billy watu
wakimpamba tayari kwa harusi, hata Lara alikuwepo pamoja na hao watu wanao watengeneza
hapo kwenye hicho chumba. Billy alitaka
kaka yake ndiye amsimamie, akamwambia na yeye Nelly yupo huru kumuomba yeyote
yule amtakaye amsimamie. Nelly asiye na marafiki na hakuwa na mpango na yeyote,
akamuomba mkewe huyo kaka yake Billy na yeye amsimamie. Dada wa kizungu
akakubali bila shida. Tena alifurahi na kusema yeye anaichukulia kama ni jambo
la heshima kwake.
Billy akataka harusi yao ifungwe
nyumbani kwao tu. Kwa nje kwenye ua. Kwani msimu huo wa ‘Spring’ nchi hiyo maua
yalishakuwa yamechanua vizuri sana hapo nje kwao. Nelly hakuwa na shida wala
ndoto za harusi sijui ufungwe kanisani, avae shela kama Lara! Akakubali bila
shida. Nalo hilo likamuongezea sifa kwa Billy kwamba ni mwanamke asiye na
makuu, kumbe hakuwa hata na mipango mingine aseme abishe. Msimamizi wake yeye
akasema wao waanze kutengenezwa hapo, angefika mwishoni kabisa kwa kuwa yeye
hakutaka kutengenezwa sana zaidi ya uso tu.
Siku hiyo nyumba hiyo ilijaa hekaheka
tokea siku iliyopita, wajukuu wote walishafika hapo tokea asubuhi wakapata
kifungua kinywa wote na wazazi wao, pamoja na bibi na babu yao wenye nyuma, kasoro
tu Briana hakuonekana. Hawakushangaa. Watu wa chakula, mapambo, keki, picha
kila mmoja akileta lake tayari kwa harusi jioni hiyo, wakaongeza hekaheka ndani
ya hiyo nyumba. Beila alikuwepo hapo chumbani kwa wifi yake akipambwa,
kuangalia mambo yanavyokwenda na mama yao. Wachangamfu yeye na mama yake. Wakaongea
hapo wakicheka, wao wakatoka kuangalia mambo ya chakula na keki. Billy, kaka
yake na baba yao walikuwa nje wakiangalia mambo yanavyoenda upande wa tafrija
watakapofungia ndoa, wakatafuta sehemu wakakaa kabisa wakiongea na kucheka.
“Hii familia kwa kucheka jamani! Hawachoki!”
Lara akamsikia wifie akishangaa kwa sauti ya chini kidogo akiwa anatengenezwa
nywele. Walimuanza kichwa. Lara akacheka, Nelly akamwangalia kupitia kioo. “Unamsikia
Billy lakini huko chini? Yaani sauti yake inasikika mpaka huku juu, kama kaka
yake!” “Halafu wanafanana wote. Baba, mama na watoto wao pia!” “Mpaka hao
waliochanganya na damu ya kizungu, wote wanafanana! Nilimwambia hilo Billy.”
Wakaendelea kuteta kiswahili, wapambaji wao wakiendelea wasielewe ni nini
wanaongelea. Lara alishamuona wakati mwingine Nelly akicheka akiwa anamsikia
Billy akicheka kwa sauti. Alikuwa akimwangalia Nelly asiamini kama ni yeye.
Katikati ya yote hayo mlango
ukafunguliwa kwa nguvu mpaka wakashituka. Briana na mama yake wakaingia. Nelly
alimtambua kwa kumfananisha na wanae. Na kwa jinsi walivyoingia kwa shari,
Nelly akajiweka sawa. “Naombeni nyinyi mtoke, ninataka kuzungumza na huyo.”
Nelly akapandisha nyusi zote juu, na kujiweka sawa akimtizama kupitia kioo
wakiwa wamsimama nyuma yake. Maana alionyeshea kidole wengine wote watoke,
abakie Nelly tu. Wakatoka. Nelly kimya akiwatizama.
Wanasema Mswahili
Atakunyima Chakula Lakini Si Neno.
“Nimetafuta habari zako huko Tanzania,
nimejua wewe ni tapeli. Umemdanganya Billy kama ni mjamzito ili akuoe.” Anele
akaanza. “Umembambikizia mimba isiyo yake ili akuoe.” “Hilo unalizungumza kwa kuwa alikunyima
wewe mtoto wa tatu ndio unafikiri hawezi kwa mwanamke anayempenda?” Nelly
akamuuliza taratibu tu na kugeuka akizungusha kiti alichokuwa amekalia. Hilo
likamuuma sana Anele lakini akajikaza. “Nakujua wewe ni tapeli. Na sitakuruhusu
umtapeli Billy. Kwanza hata ufanye nini ni baba wa watoto wangu daima. Siwezi kukubali
umdanganye. Uchukue urithi wa watoto wangu.” Nelly akamshangaa sana pale moyo wake
ulipo. Kwenye mali za Billy tu!
“Umeingia kwenye hii familia kuitapeli.
Unataka kunitoa mimi ili ubakie wewe kwenye picha, unufaike! Sasa habari zako
ninazo, na nitawaambia wote.” “Tutakutangaza, wote wakujue. Ulimkuta mama, na
huwezi kumtoa.” Akadakia Briana. Mmoja wa anayewatengeneza hao wasimamizi wa
harusi na biharusi alipotolewa hapo chumbani na Anele akaenda kwa haraka kumtafuta
Beila anayefahamiana naye na ndiye anayewalipa kwa hiyo kazi.
Lara naye wala hakusubiri nje ya
mlango, moja kwa moja akarudi chumbani kwao alipokuwepo Jax, aliyekuwa akifanya
kazi kupitia kompyuta, kana kwamba ni siku ya kazi. Baadhi ya wafanyakazi
wenzake Billy walishafika nchini hapo siku iliyopita, wakiwa hotelini na wake
zao wakisubiria muda ufike, waje hapo nyumbani kwao kwa harusi. Jax hakuwa na mtu
mwingine wa kualika. Ingekua kipindi yupo kwenye mahusiano na Tino angemualika,
lakini hawakuwa kwenye maelewano. Hata hakumshirikisha kama Nelly anaolewa. Na
ofisini kwa Nelly viongozi wenzake wawili ndio walifika hapo nchini kuhudhuria
harusi. Na walishawasiliana na Nelly kumtaarifu walishafika hotelini na wake
zao wanasubiria tu muda wasogee hapo nyumbani.
Yule mpambaji alikimbia mpaka upande
aliokuwepo Beila na mama yake wakiangalia jinsi wanavyopanga upande wa chakula
na keki. Walipomuona akija vile. Wote wakaingiwa na wasiwasi. Mpaka kina Billy
upande mwingine walipokuwa wamekaa na baba yao, pamoja na Brandon wakashangaa. “Kuna
nini!?” Beila akamuuliza. Alikuwa ni mwanamke mweusi wa hukohuko, anayejua
kutengeneza nywele za wanawake weusi na alishawafanyia hiyo kazi mara nyingi
tu, anaifahamu hiyo familia vizuri tu. “Anele ametutoa sisi chumbani yupo na
yule binti yake mdogo, amesema anataka kuzungumza na Nelly. Sidhani kama ni
kitu kiz..” “Subiri kwanza. Umesema Anele?” Billy akasikia na kusogea.
“Yupo kwenye kile chumba yeye na Briana. Wana...”
Billy akatoka hapo kwa haraka bila kusubiria amalizie na Beila naye akafuata
kwa haraka. Kaka yake na baba yake wakaangaliana na kufuata. Mama mtu naye akaunga
msafara.
“Nashauri usogee kwenye kile chumba
cha dada yako.” Jax akatoa macho kwenye kompyuta na kumwangalia Lara akiwa
amekunja uso. “Nahisi Briana na mama yake wamemfuata kishari. Maana wametuambia
sisi tutoke wanajambo wanataka kuzungumza naye. Sasa wewe unamjua Nelly,
atawabadilikia hapa uzunguni, mpaka washangae.” Jax akaruka na kutoka hapo,
mbio. Alimjua dada yake. Akaona akaokoe jahazi kabla hawajazijua rangi zote za
dada yake.
Baada ya muda mfupi wakajikuta humo
ndani ya hicho chumba mpaka watoto wao nao wakaingia hapo wakiwa wameitana wote.
Chumba kikawa kimejaa. “Ni nini kinaendelea?” Billy akauliza akimwangalia Anele.
Kimya. Anele hakutegemea uvamizi wa namna ile. Akawa yupo kwenye mshituko
kidogo. Kimya. “Nataka kujua unachotaka kuzungumza na Nelly kiasi cha kujiiba
kuingia humu ndani?” “Mami hajajiiba kuingia humu ndani. Tumeingilia...” “Wakati
mwingine ninapozungumza na mama yako, ukaingilia, utajuta Briana. Wewe huna
adabu na heshima.” “Hajui ni wakati gani wa kunyamaza wala kuongea!” Akadakia dada
yake aliyekua na yeye kwenye moja ya chumba anachotumia kila akiwa hapo kwa
bibi yake, hata usiku huo alifikia na kulala hapohapo, alikuwepo mida hiyo akijitengeneza
mwenyewe kwani na yeye alikuwa msimamizi wa harusi hiyo ya baba yake. Mmoja wa
bradesmaids. Lakini aliposikia kelele ndugu zake wakiitana kwenye hicho chumba,
na yeye akaacha kila kitu na kwenda.
“Kila wakati anataka yeye tu ndio awe
anasikilizw!.” “Sio kweli na wewe Britney. Unafiki tu. Unamwacha mama yetu..” “Sina
muda wa kujibishana na wewe Briana. Dad akizungumza, nyamaza kwanza.” “Narudia
tena swali langu Anele. Ni nini hicho ulichokitaka kukizungumza?” Wote kimya,
macho kwa Anele kama aliyefumaniwa kwenye kitanda cha wakwe.
“Waambie mami, kile ulichochunguza juu
ya huyu mwanamke.” Briana akamwambia kwa sauti ya chini kama kumtia moyo. “Usiogope.
Sema mami.” “Usimuite Nelly, huyu mwanamke. Anaitwa Nelly. Ukishindwa kumtamka,
acha kuzungumza chochote kinachotakiwa kumtambua yeye kama Nelly.” Isivyo
kawaida ya kumuona Billy akizungumza hivyo kwa watoto wake, zaidi huyo Briana,
safari hii akasikika akiongea kwa ukali. Wote kimya wamejaa kwenye hicho
chumba.
“Mami?” Briana akaita akisikika kumtia
moyo mama yake aongee tu. “Nilitaka tuzungumze tukiwa tumetulia.” “Sisi wote
tumetulia hapa. Wewe uongea.” Billy akasisitiza. “Labda ningezungumza na Billy
kwanza.” “Katika hili sitakuruhusu. Kwa sababu ulinifuata hapa. Ukatoa watu
wote humu ndani, ukionyesha huwezi kusuburi mpaka uzungumze na mimi, tena sasa
hivi. Ukawa ukinimbia ni uchunguzi ambao umefanya juu yangu, utakuja kuwaambia
wote. Sasa nafikiri hawa ndio watu ambao ungetaka kuwaambia juu yangu kabla
hatujafunga ndoa na Billy. Wote muhimu kwa Billy, na Billy mwenyewe wapo hapa. Tafadhali
zungumza Anele. Mimi huwa sichelewi popote, sitaanza leo kwenye siku yangu
muhimu.” Nelly akaongea kwa jazba kidogo.
“Ni uchunguzi gani ulifanya juu ya
Nelly? Na ulifanya wewe kama nani!?” Akauliza kaka mkubwa. “Asante Brandon! Maana
na mimi ni swali lililokuwa likiendelea ndani ya kichwa changu! Wewe kama
nani?!” Beila naye akadakia na kuuliza. “Ni mama yetu! Mnawezaje kuuliza
hivyo!?” “Mama yenu nyinyi, ndiyo. Lakini anahusika vipi na maisha ya Billy!?
Billy anaruhusiwa kufanya maamuzi za maisha yake vile atakavyo!” “Mami anataka
mtu asichezee mali za dad, kwa kuwa ni urithi wetu!” Briana akatetea na kuzidi
kumuanika mama yake, asijue inasikika vibaya sana.
Billy akaumia sana. “Yaani wewe mpaka leo
bado unalinda mali zangu tu!?” Billy akamuuliza kwa kushangaa sana. “Subiri kwanza
Billy. Wewe wakati unaolewa na Billy, nani alikuchunguza?” “Si kwakuwa mimi ni
mkewe na nina watoto wawili kwa Billy! Ninawajibika na maisha ya Billy kwa
sababu ni baba wa watoto wangu! Acheni kuzungumza kama ambao hamuelewi mambo!” Anele
akaongea kwa ukali.
“Wewe ulivyoachana na Billy si uliomba
mahakama mgawane mali sawasawa na Billy, mpaka nyumba iliyokuwa ya kwake Billson,
uliichukua wewe ukidai kwa kwa unabaki na Briana?” “Nyumba ilikuwa yetu. Si Billy
peke yake.” Akarekebisha Anele. “Vyovyote vile unavyotaka kujiaminisha. Billy
alikubali kukupa kila kitu ulichotaka kwa kwa sababu ya Briana aliyetaka kubaki
na nyinyi akidhani ni mapenzi, asijue ni maneno yako ya sumu unayomuingiza juu
ya baba yake, ili abaki na wewe, uendelee kutumia hata kidogo ulichombakiza
nacho Billy!” Brandon akaongea kwa kuumia mpaka akashangaza wote. Hawakuwahi kuzungumzia
hilo.
“Unadanganya mbele ya watoto wangu,
Brandon. Na sitakuruhusu.” “Kila mwenye akili ya kufikiria, anajua unamtumia
Briana, kuendelea kutumia pesa ya Billy. Wewe na Carlos mnaishi maisha yasiyo
na kutafuta pesa kwa bidii kwa kuwa mnajua Billy yupo na anaendelea kuwatunza nyinyi
wote watatu.” “Unamsingizia mami!” “Sweetheart, nani huwa anakutuma kuomba pesa
kwa baba yako?” Baba yake mkubwa akamuuliza kwa utulivu tu. “Ni mami kwa kuwa yeye
ndiye anayehusika na bajeti nzima, kuanzia ada ya shule mpaka..” “Wewe unajua
ada yako ya shule ni kiasi gani?” Shangazi yake akapenyeza swali kwa haraka. “Acheni
kumuhoji mwanangu ili kumchanganya!” Anele akaongea kwa hasira.
“Hilo ni swali rahisi sana, ambalo yeye kama
msomaji anatakiwa kujua.” Dada yake akachangia. “Sio swali gumu. Jibu Briana.”
Britney akaweka msisitizo. “Hayakuhusu.” “Hasomi huyo. Ameacha chuo.” Mtoto wa kiume
wa Beila nyuma akasikika. Wote wakamgeukia. “Muongo. Anadanganya.” Briana
akadakia kwa haraka. “Rafiki yake waliyekua wakichukua naye madarasa ya ijumaa,
asubuhi ameniambia Briana mwenyewe amemwambia ameacha chuo, sababu ilikuwa
asubuhi sana. Yeye sio mtu wa kudamka. ‘She is not a morning person’. Abishe
nimpigie simu sasahivi rafiki yake, athibitishe. Mwenzie anaendelea.” “Au
aingie kwenye Student Portal yake amuonyeshe dad matokeo yake ya muhula
huu.” Britney akatoa wazo rahisi na uhakika.
“Toa simu yako unionyeshe.” Billy
akamgeukia Briana. “Lakini nimemwambia mama nitarudi muhula ujao.” Briana
akajitetea akisikika amekamatika. “Na ada anayonidai mama yako pamoja na garama
za chuo!?” Billy akauliza akimtizama Anele. “Unamsingizia mami sababu ya kutaka
kuoa! Mami hadai ada tena, kwa sababu anajua siendi chuo, alinikubalia nirudi nitakapokuwa
sawa.” Billy akabaki akimwangalia Anele. “Si umemsikia mwenyewe anarudi chuo
mwakani? Sasa si bado pesa itahitajika?” Anele akamuuliza Billy kwa kumshangaa.
“Mnachezea pesa ya Billy nyinyi watatu
nyinyi!” Brandon akaongea kwa kusikitika sana. “Wala Carlos haishi na sisi siku
hizi. Carlos alishaondoka. Mnamsingizia mami mkidhani anataka kutumia pesa na
Carlos.” Briana akaendelea kumtetea mama yake asijue ndio anatoa siri za kwao. “Sikukwambia
mimi mama kuwa Carlos hayawezi mahusiano na ndio maana hata mimi sikumtaka
anioe?” Beila akadakia kwa haraka. “Nilisema mimi. Mwacheni tu huyo Anele aende
kwa Carlos. Mimi namjua Carlos kwa kukua naye, wala si kusimuliwa.” Beila
akaongeza.
“Carlos alipotaka kunioa mimi, akaja
mpaka hapa kwa mama akimuomba anibembeleze anioe wakati ule nipo intern,
kabla hata sijamaliza shule yangu ya udaktari, nilimwambia mama. Carlos ni muoga
wa majukumu hawezi kuwa mume wa mwanamke yeyote yule zaidi mimi.” “Ni mtu mzuri
na alikuwa akinipenda sana.” Akaongeza Briana akinitetea. Beila akamtizama na
kuendelea. “Wakati ule alionekana anawaweza na kuwapenda watoto wa Billy, kwa
kuwa Billy mwenyewe alikuwepo kwenye picha akifanya yote, yeye kuwepo kuwakilisha
kwenye matukio ambayo mwenzie ndiye halali kwa kuyagaramia. Bithday zao hawa,
yeye ndio alikuwa mstari wa mbele kuwakilisha, kwa kuwa Billy mwenyewe alikuwepo
kugaramia kwenye mahoteli ya garama mama yao aliyokuwa akiyachagua.” “Sio mimi
ni watoto wenyewe ndio waliokuwa wakitaka birthday zao zifanyiwe huko. Acheni
kunisingizia.” “Wewe ni mama wa namna gani unayesema ‘ndiyo’ kwa kila kitu mtoto
anachotaka? Unafaida gani ya kuwa mama kama unashindwa kuongoza wanao kwenye
njia sahihi? Acha kuzungumza kijinga hapa.” Akauliza mama Brandon kwa hasira.
Kimya, Beila akaendelea. “Haya,
hospitalini yeye Carlos akawa mstari wa mbele kuonyesha anajali watoto wa Billy
kuliko baba yao, wakati Billy ndiye aliyekuwa halali akifanya kazi mchana na
usiku ili kufanya watoto wake wawe wanauwezo wa kuonwa na madaktari wazuri hapa
nchini. Haya tena, nyumbani kwa mwenzie ndio ikawa kituo, kutwa yupo pale
akijionyesha yeye bora kuliko Billy mwenyewe aliyekuwa akihangaika kuhakikisha familia
yake ina nyumba nzuri. Umeme usikatwe pale ndani, maji yapo kila wakati na chakula kizuri kisikosekane
kwa familia yake. Wakawa na kazi ya kupika na
kupakua tu mle ndani wakilishwa na Billy kama makinda ya ndege.” “Carlos
anapenda watoto wangu na alikuwa akitujali sana kuliko Billy alivyo..”
“Huo ndio uongo uliokuwa ukimuaminisha
Briana ambaye alikuwa mtoto asiyejua maana ya maisha. Mlitegemea maishi mazuri na
ya hali ya juu kivipi, na Billy naye aishi kama vile Carlos ambaye hakuwa hata
na kazi ya maana?” “Carlos alikuwa na kazi na alikuwepo nyumbani pia.” “Unaongea
nini wewe Anele? Yuko wapi sasa hivi huyo Carlos? Yuko wapi?” “Halafu wakiitwa
wanaume wenye kazi unafikiri Carlos naye atakwenda?” “Anakwenda sana. Kazi si
kazi?” “Anele, tunamfahamu sisi Carlos kama mtoto aliyekulia humu ndani. Tunamfahamu
zaidi yako. Beila anapokwambia Carlos hapendi majukumu, anamaanisha ni mvivu.
Mvivu watokea shuleni akisoma na Billy. Wewe ulipomtoa Billy kwenye picha,
hukujua ndio unavunja mahusino yako ya wizi na Carlos. Ungemtaka Carlos, ni
kuendelea kumuacha Billy kwenye picha ili aendelee kuwatunza nyinyi wote. Ona kinachokutokea.
Mtoto ambaye mmeaminisha mahakama mnampenda na kumjali mpaka akawachagua
nyinyi, amewashinda! Mkaendelea kumtumia mjinufaishe naye, yeye mwenyewe
hanufaiki na wewe hujali Anele!”
“Mimi sijinufaishi na Briana.” “Mbona
sasa unaendelea kudai ada ambazo hasomi?” “Briana mwenyewe aliacha shule. Ningefanyaje
baba yake hayupo?” “Mbona ukitaka pesa yangu unahakikisha napokea simu zako
hata kama nipo kwenye kikao unanitoa? Kweli Briana anaacha chuo, unashindwa
kuniambia, unadai tu pesa?” “Au hata kwa nini asiniambie mimi ambaye nipo hapa,
sina ninalofanya, nikapata muda na Briana nikazungumza naye?” Babu yake
akadakia.
“Mimi simtumii Briana.” Anele
akajitetea. “Sasa ukishalala, usingizi ukikuisha, huwa unafanya nini wewe
Briana?” Dada yake akamuuliza. “Shopping.” Akadakia Junior, mtoto wa Beila,
mgomvi wa Briana. Wote wakageuka. “Anajulikana kwa kutapanya huyo. Angalieni Istagram
yake. Ana watu wanamfuatilia kwa mavazi tu.” “Linafiki wewe, Junior. Una...” “Niwafungulie
niwaonyeshe picha zako za majuzi ulipoenda kujirusha beach. Ukawa unaonyesha
watu huko Insta hoteli ya kifahari uliyofikia na picha za nguo ulizonunua?”
Junior akamuuliza Briana. “Kwa nini hukusema?” Mama yake akamlaumu mwanae. “Tumeambiana
wote sisi mpaka watoto wa mjomba, tumuache mpaka aharibikiwe kabisa. Briana
mjeuri mama. Anatudharau sisi wote. Hata bibi tuliambiana tusimwambie ili
asimuonye mpaka apatwe na janga. Na hana muda mrefu huyu mama, janga litampata
maana anavutia macho ya wengi mpaka wahalifu wataanza kumfuatilia. Watu huko
Istagram wanajua mpaka chumba anacholala huyo Briana.” Ilimuuma sana Billy. Britney
akalia sana, mwishoe akatoka hapo.
“Hamkufanya vizuri.” Brandon
akawageukia wote. “Dad, wewe huyajui matusi ya Briana.” “Anatukejeli pia. Anatuita
sisi wote wapuuzi. Hatuna akili kama yeye na dada yake Britney. Eti wao wamejaliwa
akili za darasani, sio kama Junior anavyofeli darasani, inabidi afanye summer
class kila mwaka ili kulingana na wajinga wenzie huko shuleni kwao. Ndio
tukaambiana tumuache, tuone mwisho wake.” Mtoto mwingine wa Beila wa kiume akadakia
akimtetea kaka yake. Watoto wengine wote wakaanza kusema madhambi ya Briana.
“Naomba turudi nyuma kidogo.” Bibi yao
akawakatisha maana walikuwa wakimchangia kumsema Briana, mpaka akaanza kulia. “Anele
ulikuja kuzungumza na Nelly. Ukisema umemfanyia uchunguzi unataka kuja
kutushirikisha. Tafadhali maliza, ili tufikie hitimisho.” Watu wote kimya
wakamgeukia Anele. “Tafadhali zungumza, nataka nimfuate Britney nimtulize. Umeharibu
maisha ya watoto wangu kwa sababu ya tamaa ya pesa ambayo sikuwahi kukunyima,
Anele!” “Mimi siku...” “Tafadhali zungumza kilichokuleta, acha kutupotezea
muda.” Billy akamkazania.
“Ni
uchunguzi aliofanya juu yake. Amegundua Nelly amekudanganya wewe kuwa ni
mjamzito wako ili umuoe. Kwamba...” Briana akawa kama na yeye amevurugikiwa hakumbuki tena. Akamgeukia
mama yake. “Ulisema ni mjamzito wa mtu mwingine
aliyemlipa ampe mimba au alikuwa kwenye mahusiano mengine, dad hajui, au
ulisema hana mimba anadanganya tu?” Briana akiwa anamsaidia mama yake
kujieleza, akawa na yeye hana taarifa za kutosha. “Bado sijakamilisha uchunguzi
vizuri.” Anele akajibu. Briana akakunja uso kama na yeye amempoteza.
Billy akatingisha kichwa kwa
masikitiko. “Kweli Anele, unashindwa kumfanya mtoto wangu atulie shuleni,
unamwingiza kwenye maisha yako ambayo umeyachanganya wewe mwenyewe hujui ni
nini unataka!?” Billy akaongea kwa kuumia sana. “Unatumia uharibufu wako hata
kwa mtoto uliyezaa mwenyewe!?” “Mimi sijamuharibia Briana maisha. Kama ni shule
atasoma tu.” “Angesoma kwa ada ipi wakati umekuwa ukitumia pesa yake?” “Pesa
yote naitunza ili akija kurudi shule asipate shida. Kuna leo na kesho jamani.
Ya kesho hatuyajui. Iweje atake kurudi shule tushindwe uwezo?” Anele akaendelea
kujitetea.
“Bila sisi kuona, muonyeshe Briana mwenyewe hiyo
pesa unayomtunzia.” Akadakia Beila. “Toa simu muonyeshe akaunti ambayo unaweka
hiyo pesa.” “Hana hela. Mimi najua. Hata hoteli alizofungua huko nyumbani, ni
kama amefilisika tu. Watu wanyumbani wamemwambia baba yenu.” “Sio kweli.” Akambishia
mama mkwe. “Basi fanya hicho alichokwambia Beila, sasa hivi. Muonyeshe Briana
ada uliyokuwa ukichukua kwa baba yake.” Kimya wote wakampa muda.
“Kama hilo limeshindikana, tuambie huo
uchunguzi uliofanya juu ya Nelly. Hata kama haujakamilika, wewe utuambie tu.
Binafsi nataka kujua.” Akasisitiza mama mkwe. Kidogo Nelly akaanza kuingiwa
hofu. “Mpaka nipate uhakika wa jambo la mwisho ili niwape habari kamili.” “Wewe
vipi Anele? Mbona ulimfuata sasa Nelly?” Beila akamshangaa sana. “Kumtaarifu.” “Haya,
mtaarifu sasa.” Billy naye akaongeza. “Alikuwa na mahusiano mengine mbali na
Billy. Kwa hiyo hata mimba kama anayo, si ya Billy kwa hakika.” Akaanza Anele.
“Na nimeambiwa na mtu wa karibu yake
kabisa. Anasema alishakuonya wewe Billy juu yake huyu, lakini hukumsikiliza. Anasema
alikuwa akinitafuta mimi tokea asikie Billy anataka kumuoa huku. Akajua wanakimbia
kule Tanzania ili isijulikane.” Anele akaongea. Alipoona kimya akaongeza
ujasiri.
“Aliniomba nisimtaje jina, lakini kwa
kuwa hamniamini, namtaja. Alinitafuta yeye mwenyewe kwa njia ya Facebook. Akani
inbox. Anasema alianzia kwa Briana Instagram. Alipojua jina langu kamili
ndipo akanitafuta mpaka akanipata Facebook kwa kuwa sikuwa na akaunti Ista. Niliifunga.
Kufupisha habari ni ndugu yake kabisa. Walilelewa nyumba moja. Anaitwa Yasinta.”
Nelly alishituka nusura aanguke.
“Ingekuwa ni jumbe ningewaonyesha. Ila
aliomba nimpigie kabisa ili aniambie ubaya wake huyu. Na kingine ambacho
amekiri wazi japo amesema hana ushahidi wakutosha, ndio nilikuwa nikisubiria
hilo ili nipate habari kamili, ni kama alisema huyu Nelly alishakuwa na
mahusiano na baba yao, ambaye ni mjomba wake kabisa, kaka ya mama yake Nelly pamoja
mdogo wake wakiume, anaitwa Jackson, lakini Nelly alimpa jina la Jax.” Anele
akaendelea.
“Anasema Nelly alimtumia baba yao,
yaani mjomba wake, kimapenzi mpaka akawapa nyumba na maisha mazuri. Alipofanikiwa
kimaisha, akamuacha baba yao vibaya sana. Anasema huyo mzee mpaka alipata stroke
kwa mshituko wa kuachwa na Nelly. Na mpaka leo yupo amepalalazi upande mmpoja. Sababu
ni huyu Nelly.” Anele akawakilisha hoja. Chumba kizima kilikuwa kimetulia kimya
kikimsikiliza. Jax akarudisha macho kwa dada yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hakuna Yanayokaa Gizani
Daima. Huwa Ya Gizani Yanamtindo Yakuja Kujiweka Bayana Mwangani. Ni Muda Tu,
Ila Yote Huishia Mwangani.
Hakuna Siri Ya Milele. Kuwa makini na nini unafanya sirini.
0 Comments:
Post a Comment