Chumba kizima kilitulia wakati Anele akieleza ya Nelly kwa ujasiri. “Na sidanganyi kwamba nataka kumuharibia Billson! Ni ukweli, hata mkitaka naweza kumpigia simu huyo Yasinta. Amebakisha kitu kimoja tu, athibitishe. Lakini vingine vyote anauhakika kwa asilimia 100.” Anele akaweka msisitizo. “Acha nikusaidie Anele. Maana najua unapoteza pesa yako kwa Yasinta.” Billy akaanza alipoona amemaliza na wazazi wake pamoja na ndugu wakihisi anarudia kosa kwenye ndoa. “Wewe ni kosa nililojifunza kwa machungu sana. Umenigarimu mimi na watoto wangu. Mpaka leo watoto wangu wanalipa garama.” “Sasa mimi hapa nimefanya nini!? Kwa nini unanigeukia mimi na sio huyo mwanamke unayefikiri ni mwema unataka kumuoa?” Akauliza Anele akishangaa sana.
“Ninachotaka kukwambia Anele, kwa sababu unachofanya hapa hakikuhusu.
Hii ni kuniingilia mimi na Nelly, na sitakuruhusu.” Hapo kidogo hata Jax
akapumua. Maana alishamuhurumia dada yake kuona kama amewekwa kati, anasomewa
shitaka. “Jamani, nilifanya kosa kwa Anele, kumuoa bila kumfahamu. Lakini
nimejifunza wazazi wangu. Mama anajua. Nimekuwa nikimshirikisha hatua moja hadi
nyingine juu ya Nelly, japo sikumpa taarifa zisizomuhusu juu ya Nelly. Nelly
ninayemuoa leo namfahamu kwa asilimia 95, zilizobaki ni chake sana kwa sababu
simfahamu Nelly ajae. Nelly atakayekuwa na mimba ya miezi 9, au Nelly
atakayekuwa mama na mke. Ambazo hizo asilimia 5 zilizobaki, zinanipa ujasiri wa
kumuoa Nelly kwa asilimia 95 ninazomfahamu. Nelly anampenda Billy kama
Billson.” Billy akaendelea.
“Huyu Yasinta anayemzungumzia hapa, na mimi namfahamu kwa kuwa mimi
ndiye niliyemtafuta nikitaka kumfahamu Nelly kwa karibu sana. Nilikubali
kumlipa kama alivyonidai yeye mwenyewe ili kunipa habari za Nelly. Hichi anachowaambia
Anele sasa hivi, mimi niliambiwa na Yasinta, na kutaka kunipeleka mpaka kwa
mama yake mwenyewe ili kuthibitisha.” Mpaka Nelly akakunja uso. Jax akashangaa
sana aina ya ndugu zake na kumuelewa Nelly ni kwa nini anajaribu kuwa nao
mbali.
“Nilimlipa Yasinta na kumwambia alichoniambia kinatosha kabisa, sina
sababu ya kwenda kwa mama yake kwa uthibitisho. Tukaachana. Alipokuja kusikia
namuoa Nelly, na sijui aliambiwa na nani, Yasinta alinitafuta sana. Akaomba
miahadi ya mpaka kwa sekretari wangu, akaambiwa kalenda yangu imejaa, mpaka
nitoke likizo, pengine anaweza kupata nafasi. Sikuambiwa, ila nilimkuta
akinisubiria getini. Nikamwambia dereva asimamishe gari na kumruhusu aingie.
Narudia tena, aliyarudia yote na kunionya nisimuoe Nelly.” “Kwa nini
hukuniambia Billy!?” “Ili iweje Nelly?” Billy akamuuliza, Nelly akatulia.
“Nikampa jibu ambalo pengine na wewe Anele litakusaidia na uache
kunifuatilia mimi na Nelly. Ubaya wooote uliosikia juu ya Nelly, nimepata
uthibitisho kutoka kwa Nelly mwenyewe akinithibitishia kwa kadiri ya
tulivyokuwa tukiishi naye na mengine kunishirikisha yeye mwenyewe bila
kumlazimisha. Namfahamu Nelly na ninampenda, na ndio sababu ya kunifanya
nikubali au nimuombe akubali nimuoe. Wewe sijawahi kukupigia goti nikikuomba
nikuoe. Lakini kwa Nelly, nikiwa namfahamu kwa asilimia zote hizo, nilifanya.
Na hata nikipewa nafasi nyingine tena, kwa Nelly nitafanya. Na jibu la hapana
kutoka kwake si chaguzi na yeye ananijua. Ameshanifukuza zaidi ya nitakavyosema
na Jax mdogo wake huyu ni shahidi. Nafikiri hakuamini aliposikia tupo pamoja na
dada yake. Nelly hakuwa akinihitaji japo alijua wadhifa wangu. Nelly alinikataa
akiwa ametambulishwa mimi ni nani. Ila wewe Anele ulinikubali kwa haraka kwa
kuwa ulitambulishwa mimi ni nani.” Kimya.
“Niliweke hili wazi pengine litawasaidia nyinyi wote. Na nafikiri
Nelly alimwambia hata mama na Britney. Sijui kama mlimuelewa?” “Labda urudie
Billy. Taarifa nyingi zinapita sasa hivi.” “Usichanganyikiwe mama yangu. Nelly
niliyekutambulisha kwako na ukaniahidi kuniombea ukinipa baraka zako, ndiye
Nelly huyuhuyu anayemzungumzia Anele na ndiye ninayemuoa.” Mpaka hapo Billy
hakuwa amekanusha jambo hata moja.
“Naliweka hili sawa kwa wote. Nelly alikuwa na maisha yake, wala
hakuwa na mpango wa mwanaume wala mtoto. Hichi anachozungumzia Anele kuwa mimba
ndio imekuwa sababu ya Nelly kuninasa au sijui ni ujauzito wa mwingine ameshika
kwa ajili yangu, jamani si kweli. Huu ujauzito ndio unaomnyima Nelly
usingizi. Nelly hataki mtoto wala hakuwa akitaka mume. Mimi ndio nilimlazimisha
sana mahusiano. Kwa kutumia kila nguvu mpaka kumuona yupo hapa ni mimi kumtaka
wala si yeye kunirubuni. Kuahirisha harusi sasa hivi kwake ni jambo la furaha
kuliko kuendelea na hii harusi, maana haikuwa kwenye mipango yake ya maisha.
Nina uhakika kwa asilimia 100, sasa hivi tukisema harusi hamna, atabeba mizigo
yake na kurudi kwenye maisha yake bila shida na asione amepungukiwa.”
“Sio kweli Billy.” Hapo Nelly akakanusha. “Wewe nakupenda. Nitasema ‘ndiyo’
kwako tena na tena, popote kule. Wewe nakuhitaji na wala sitaogopa kusema. Kama
nilishafanya kosa nyuma, sio wewe. Na hata mtoto japokuwa sikuwa nikitaka
kabisa, lakini naanza kujifunza na kumfurahia kadiri ninapomsikia akicheza.
Hofu ya pengine nitashindwa kuwa mama mzuri inaanza kupungua. Kwa hiyo hapa
nilipo, na wewe Billy, sijutii na sina mpango wa kukimbia kwa haraka.” Billy
alifurahi sana.
Akamsogelea na kupata busu hapohapo, tena la muda tu akivuta midomo
ya Nelly kwa utulivu tu. “Nashauri msubiri baada ya harusi.” Angalau Brandon
akafanya watu wacheke lakini Billy akaendelea kidogo na kumuachia maana Anele
alitaka kutoka. “Subiri kwanza Anele. Sijamalizana na wewe.” Akabaki amemshika
Nelly mkono. “Nakushukuru Nelly. Asante.” “Nakupenda Billy.” Nelly akanong’ona.
Wakati Billy anataka tu kuinama kwa busu jingine Brandon akamuwahi. “Nope.
That’s enough man! Mtachelewesha ratiba.” Wakacheka sana. “Fine. It was
just a peck though!” “No, man! I saw that. It was NOT just a peck.
Ulikuwa ukiiendea midomo kabisa.” “Hata mimi nimeona.” Beila akaongeza nakufanya
wazidi kucheka. “Fine.” Billy akamuachia Nelly.
“Anele, kwa kuwa hapa si nyumbani kwangu, sina uwezo wa kukufukuza.
Ila hukaribishwi kwenye harusi yangu. Eneo ambalo nitafanyia mimi harusi leo, huruhusiwi
kusogea hapo. Huruhusiwi kufika jikoni ambako kuna vyakula na vinywaji vya
harusi. Japokuwa sina amri juu ya hii nyumba, lakini nimeruhusiwa na wazazi kufunga
ndoa hapa. Hivyo basi, kama utabaki hapa, nitataka uwe eneo la wazi ambalo kila
mtu atakuwa akikuona. Nashauri iwe sebuleni. Ikitokea unaonekana eneo jingine
lolote zaidi huku vyumbani ambako wageni wangu mimi wapo, zaidi Nelly,
utakamatwa na kupelekwa polisi.” “Kwa nini!?” Anele akashangaa sana.
“Moja, nakuhofia kuwa karibu na Nelly pamoja na mtoto wangu
aliyetumboni. Uchu wako wa mali zangu unaniogopesha sana, naona unaweza kufanya
chochote ili kujinufaisha na pesa yangu. Chochote kitakachompata Nelly, hata
food poison, wewe utakuwa mtuhumiwa wa kwanza.” “Naondoka.” “Hata ukiondoka. Omba
Mungu chochote kibaya kisitokee leo. Maana umeingia kwenye hii nyumba kwa siri
na kutokezea chumbani alipo Nelly. Sijui ulijuaje alipo! Sijui umepita wapi na
umeshika nini, maana baadhi ya vyakula na vinywaji vilishaanza kuletwa tokea
asubuhi.” “Sio sawa kwangu, Billy. Unaniadhibi bila sababu!” “Ilikuwa sawa
kwako kumuanika Nelly hapa mbele za watu? Si kwamba ulitaka kumuharibia tu? Na
je, nitajuaje kama umeridhika na kukubali kumuacha au kutuacha moja kwa moja
kwamba hutatumia njia yeyote ile kuhakikisha unatimiza azma yako?” “Mami...”
“Nyamaza Briana, na wewe sijamalizana na wewe.” Akamkatiza Briana.
“Umenielewa Anele?” “Mimi naondoka jamani. Na japokuwa nilipitia
jikoni, lakini nilikuwa na Briana, hatukushika kitu.” “Briana.” Billy
akamgeukia Briana. “Na hili nataka Anele ulisikie, ili mkitoka hapa mjue ni
jinsi gani mtaendelea kuishi. Sitakulazimisha uishi kama Britney.” “Unampendelea Britney. Wakati wote unampendelea Britney,
mimi hunipendi, dad.” Briana akaanza kulia. “Wala sijawahi kuonyesha
upendeleo kati yenu ila wewe umekuwa ukinitenda ubaya Briana. Kila nilipotaka
mahusiano na wewe, umekuwa ukinipa sababu zote za wewe kutotaka kuwa na mimi
ila Carlos na mama yako. Ni lini wewe umeshawahi kunyanyua simu ya salamu
kunisalimia tu, kama si kuniomba hela?” Kimya.
“Kila siku Britney kabla hajatoka kitandani kwake lazima atume ujumbe
wa kunijulia hali kama amechelewa, lasivyo atapiga simu kunisalimia. Hata kwa
sekunde 30 tu, lakini atanisalimia. Na lazima atanipigia simu jioni kujua
nimeshindaje! Hataki pesa yangu kwa kuwa anasema pesa anayolipwa inamtosha.
Muulize babu au bibi yako kama sijawatuma kumchunguza Britney ili tujue uhitaji
wake ili niweze kumsaidia!” “Ni kweli.” Bibi yake akajibu. “Na wala hatujawahi
kujua uhitaji wake. Anaishi maisha ya kawaida sana ambayo nafikiri ndio sababu
anaweza kumudu garama zake.” Babu yake akaongeza. “Anko, Britney is a good
people.” Junior akafanya wacheke jinsi alivyozungumza. Lakini wote
wakamtetea kuwa yeye hana shida na anaupendo.
“Kisheria, siwajibiki kukutunza Briana. Ila nilifanya kama wazazi
wetu walivyotufanyia sisi. Tafadhali amka Briana, angalia maisha jinsi yalivyo.
Sijui mama yako huwa anakwambia nini, ila sisi kwetu hatuna kurithishana mali
ila kusaidiana elimu, basi. Wote sisi tuliozaliwa na hawa wazazi,
hatutamrithisha mtu kitu ila elimu.” “Mimi najua maana ni wimbo naimbiwa na
mama kila siku.” Junior muongeaji kuliko wote akadakia tena.
“Ndivyo ilivyo sweetheart. Sina mali ya kukurithisha kwa sababu mimi
si kama mama yako mwenye mahoteli huko Zimbambwe. Sina cha kukupa. Na kwa kuwa
hutaki shule, usithubutu kunipigia simu na kuniomba pesa. Mkataba wangu mimi na
wewe umekwisha.” “Si amesema atarudi shule!” Mama yake akaingilia. “Akiwa
tayari kusoma, ndipo sasa wewe ambaye unaakiba yake, kutoka kwenye pesa
mlizokuwa mkinidai, nikijua nimeshamaliza ada yake, utatumia hiyo akiba
kumalizia ada yake. Umenielewa Anele na Briana?” Palizuka ukimya hapo, Briana
hakuamini. Kwamba akafanye kazi!
“Unauhitaji wa pesa, fanya kama Britney. Wewe si wa tofauti. Tena kwa
sababu umepunguza jukumu la shule, inamaana unaouwezo wakutengeneza pesa kwa
kadiri utakavyo. Kama utataka lakini. Sikulazimishi kufanya kazi, ni pale
utakapoona kuna uhitaji.” “Sio sawa Billy!” Anele akashangaza wote.
Billy akamgeukia Briana. “Mama yako alikwambia kama anahoteli zaidi
ya moja huko Zimbambwe?” “Aliuz...” “Hayawahusu
Briana. Huna haja yakuwaambia, baby.” “Kweli hayatuhusu. Ila kama hakukwambia,
wakati ananipa talaka ili muanze maisha na Carlos, alitaka tugawane hata
kichache alichokuwa amenibakiza nacho. Tukagawana mpaka salio langu benki.
Alipoona sijakataa, akadai mahakama iniamrishe nimuachie ile nyumba kwa sababu
yako wewe. Napo sikubisha. Na baba huyu nishahidi. Alisema Anele anabaki na
wewe, si sawa kwako kuanza kuhamia sehemu ingine kimaisha, itakusumbua zaidi.
Kwahiyo hata ile nusu aliyonibakisha nayo, nayo pia alikuja kudai. Ninachotaka
kukwambia ni hivi, mimi sina uwezo kama alionao mama yako. Mama yako anamiliki
nyumba zaidi ya moja. Mimi sina nyumba hata
moja. Huko Tanzania naishi kwenye nyumba niliyopewa na ofisi, niitumie
wakati nikiwafanyia kazi zao. Nikishindwa kufanya kazi zao, inamaana na mimi
nitakuwa sina pakuishi. Sijui kama unanielewa?” Briana kimya akilia.
“Narudia tena, sijui mama yako amekuwa akikwambia nini juu yangu,
lakini mimi si tajiri kama pengine unavyodhania. Unaponipigia simu kunidai
pesa, sina sehemu ingine ninayopata pesa isipokuwa ni kama hivi Britney
anavyokwenda kazini kila siku, wanamlipa. Ndivyo hivyohivyo na mimi. Ila
tofauti yangu mimi na Britney ni mimi inanilazimu kutoa kwenye mshahara wangu,
kukupa na wewe nikidhani upo shuleni, nikitaka kukusaidia usome tu. Sasa kwa
kuwa umeshakuwa mkubwa, unaelewa maisha ni nini, na wewe tafuta pesa za
kujikimu. Ukitaka kurudi shule, rudi ila jua utakapokuwa na uhitaji, simu
hazitakuwa kwangu tena kudai pesa ila wewe mwenyewe kufanya kazi kwa bidii na
kukabiliana na maisha yako, au mama yako mwenye uwezo.” “Au Carlos.” Akaongeza Beila.
“Kwani Carlos ni baba yake? Acha kuzungumza kama mtoto mdogo, Beila!”
Anele akawa mkali. “Hayo umeyagundua lini? Yaani sasa hivi, gafla Carlos sio
baba yake!?” Beila akamuuliza kwa kumshangaa sana. “Siye huyu Briana aliyesema
pale mahakamani kuwa Carlos ni baba bora kuliko Billy? Na si ametoka kusema
hapa kuwa Carlos anampenda sana. Sasa atashindwa vipi kumsaidia akiwa na
shida?” Beila akauliza. “Wakati akisema hivyo pale mahakamani, Briana alikuwa
mdogo, auntie. Na ni mama ndiye aliyetufundisha wote tuseme hivyo. Briana
hakuwa akijua jema na baya, ila kufanya kile mama alichokuwa akimwambia.”
Britney akamtetea mdogo wake. Kumbe alirudi akawa amesimama mlangoni kabisa.
“Sio kweli.” “Unabisha nini
mama jamani!? Hukutukataza tusiseme ukweli kama tunavyojua na kuona jinsi tulivyokuwa
tukishi? Wewe unafikiri ni kwa nini mimi nilikataa kuzungumza mahakamani?” “Kwa
sababu ni jeuri.” Mama yake akajibu. “Hapana, ni kwa sababu ulitukataza
tusizungumze tunachofikiria ila kile ulichotaka wewe kisikike siku ile, ndio
maana mimi nilikataa. Na babu alipokuja kututembelea, ndio maana nilimlilia
asiniache pale nyumbani kwa sababu wewe ulishaanza kuwa mkali kwangu. Na
kuonyesha hasira.” “Wewe sasahivi utazungumza chochote sababu umesifiwa.” Mama
yake akaongeza.
“Hata Briana si mtu mbaya. Naombeni tumpe nafasi. Dad, nakuahidi
Briana atabadilika kuanzia leo. Mimi nitapata naye muda. Akikubali nitamchukua
akakae na mimi kwa muda wakati akijipanga. Atatafuta kazi na kurudi shule.” “Mimi sitaweza kusoma na kufanya kazi.” “Hakika
utaweza Briana. Labda mama yako akusaidie.” Billy akaweka msisitizo. “Utapata
nafasi nyingine, lakini ambayo nilazima uilipie wewe mwenyewe garama, na
sivinginevyo. Kama watoto wengine wanafanya, basi na wewe utafanya tu.
Ukishindwa, chukua mikopo, utakuja kulipa ukimaliza chuo. Watu wengi sana
wanafanya, wewe hutakuwa wa kwanza wala wa mwisho. Nashauri mtumie dada yako
vizuri, atakusaidia maishani.” Billy akahitimisha kwa upande huo.
“Jamani, naomba tuhitimishe, mtupishe wote hapa ndani, ratiba
inaendelea kama kawaida.” “Njoo Briana.” Dada yake akamfuata na kumshika mkono.
“Dad, anaruhusiwa kubaki?” Britney akamuulizia mdogo wake. “Kama atataka.
Sitamlazimisha kwa lolote.” “Mimi naomba abaki, dad. Nakuahidi atatulia. Si
ndiyo Briana?” Akakubali akilia. “Basi twende kule chumbani kwangu.” Akatoka na
mdogo wake na kumuacha mama yao hapo. Wengine wakaanza kutoka pia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jax akamsogelea dada yake. “Upo sawa?” “Kidogo. Nahisi nimeshituka
sana.” “Nisikilize Nelly. Lara alipoteza mtoto kwa sababu kama hiyo. Tula
alimfuata na kumvamia kama hivi. Pressure ikapanda, tukaishia kupoteza mtoto.
Tafadhali tulia. Nimemsikia Billy yupo upande wako. Na hapa hutakaa kwa muda
mrefu, umesema baada ya harusi tu unaondoka. Si ndiyo?” “Ndiyo.” “Basi Lara
atakuwepo hapa, mpe maelekezo nini unataka kianze kufungashwa na mengineyo ili
kukusaidia kuokoa muda. Najua hutaki kuchelewa popote. Tulia. Kila kitu
kitakuwa sawa.” “Nashukuru Jax na naomba..” “Huhitaji kujieleza kwangu Nelly.
Ulifanya kile ulichoweza kutufikisha hapa. Ila ukitaka kulizungumzia hilo, iwe
baada ya kutoka fungate, umetulia. Sio sasa hivi. Na wala usione unawajibika
kujieleza kwangu. Tafadhali tulia kabisa.” Hapo Jax akamfanya Nelly atulie.
Walibakia wao wanne tu hapo chumbani. Lara, Billy, Jax na Nelly mwenyewe. Jax
akampa maji.
“Naombeni na nyinyi mtupishe. Nahitaji muda na Nelly.” Billy
akawafukuza Jax na Lara. “Nelly atakuwa sawa, Jax. Naomba uamini na wewe
uondoke hapa unipishe.” “Sitaki kosa lililotokea kwa Lara, lijirudie kwa Nelly.”
“Nakuahidi yeye na mtoto watakuwa sawa. Wewe ondoka.” “Nipo sawa Jax. Nahitaji
tu kutulia ila kweli nahisi pressure imepanda. Sijisikii vizuri.” “Acha
nichukue BP machine ya mama nikuangalie.” Billy akatoka, Jax na Lara wakabaki.
“Nielekeze nini chakufungasha.” “Hutaweza Lara. Huwa napangilia vitu
vyangu kwa namna yake. Najua Jax anaelewa. Hapa kila kitu kipo kwenye
masanduku. Vilivyo nje ni kwa kuwa bado navihitaji. Na kabla sijatoka hapa,
ndio nitakuita ili uchukue baadhi ya mizigo yangu nitakayotaka mrudi nayo
Tanzania. Mingine yote inaendelea na safari. Kwa hiyo nipo sawa. Acha aje
anipime. Nikiona ipo juu, wala sitataka kuendelea na kupambwa. Nitalala kabisa
ili nitulie.” Billy akarudi na machine yakupimia pressure pamoja na dada yake
ambaye ni daktari.
Wakampima na kukuta sio mbaya ila juu kidogo. Billy akaangalia muda.
“Unaweza kupata masaa mawili ya kulala. Naomba umwambie huyo anayetengeneza
watu aje achukue vitu vyake aendelee na watu wengine, Nelly alale kabisa.”
“Sasa na yeye kupambwa?!” “Naona Billy yupo sahihi Beila. Nahitaji kutulia
kabisa. Sijisikii vizuri.” “Nahitaji afya yake na mtoto kuliko urembo wake.
Hata akiwa hivi tukifunga ndoa, mimi sina tatizo.” “Nafikiri mpo sahihi. Uzima
ni muhimu.” Beila akatoka. Lara akamvuta mkono Jax kama anayemzuia asitoke kwa haraka.
Nelly na Billy wakashangaa kidogo. “Mimi na Jax huwa tunaomba.” Lara
akaanza akitetemeka. “Naomba tuombee hii siku nzima. Sitachukua muda mrefu.”
Hata Jax hakutegemea. Akageuka vizuri akimtizama Lara. “Naomba tuombee amani,
utulivu na furaha katika siku ya leo mpaka tutakapoondoka hapa.” Lara
akaendelea akimwangalia Nelly kwa hofu. “Anasema nini?” Billy akamuuliza Nelly
kwa kuwa Lara alizungumza kwa lugha ya kiswahili. “Anataka tuombee siku ya leo.
Tuombee amani, utulivu na furaha.” Billy akacheka kama kawaida yake na
kuongeza. “Wazo zuri sana, ila aombe kwa kingereza.” Lara alishituka nusura
akimbie chumba.
“Hapana Billy! Utamnyima uhuru wa kuomba.” “Sasa mimi nitaelewaje!?” “Kwani
anazungumza na wewe, Bill au unataka uchokozi tu hapa? Si anazungumza na Mungu!
Wewe nishakwambia atakachozungumza na Mungu, utulie na uache kucheka. Unazidi kumtia
hofu.” Eti Billy akajifunika uso na mto kwa haraka. “Yaani Billy wewe! Hakika sijakupatia
mwenzio!” “Wewe umesema nitamtia hofu, nitamfanya ashindwe kuzungumza na Mungu.
Na mimi nataka amani, utulivu na nini tena?” “Furaha.” Nelly akamjibu. “Yeap. Sasa
kwa nini nisipunguze vikwazo.” Nelly akamtizama na kumwangalia Lara. “Achana
naye huyu. Wewe omba. Kweli tunamuhitaji Mungu.” Nelly akamruhusu.
Mtoto wa mama Chiwanga akaanzisha sala kwa kiswahili huko uzunguni. Akamuombea
mtoto wa Nelly tumboni. Akamuombea Nelly mwenyewe afya yake amani na uwezo wa
kumbeba mtoto wake bila matatizo ya mwili. Akakemea magonjwa yote kwenye mwili
wake. Akaombea harusi yao na kumbariki Jax. Ndipo akamaliza.” Nelly akaanza
kucheka.
“Kwanza asante kwa kuniombea Lara. Nashukuru. Ila nina swali.” “Niambie
na mimi, Nelly.” Billy akadakia. “Lara ameomba vizuri sana. Na wewe amekuombea.”
“Oooh! Asante.” “Ila nina swali juu ya maombi yake kwa Jax. Huwa unambariki
hivi kila siku?” Lara akacheka kwa aibu. “Huwa ananiombea hivyo mara kwa mara.”
“Ndio maana siku hizi kichwa chako kimetulia!” Jax akacheka kwa masikitiko. “Kwani
uongo?” “Mimi kichwa changu kilikuwa kimetulia tokea zamani.” “Mmmh!” Nelly
akaguna kwa kutomsadiki mdogo wake. “Twende Lara, tumuache apumzike.” Jax na
Lara wakatoka, wakamuacha Billy na Nelly.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Njoo ulale hapa nikukumbatie.” “Usiondoke nikipitiwa na usingizi,
mpaka niamke.” “Japokuwa najua hakuna atakayeingia tena hapa, lakini
sitaondoka. Usiwe na wasiwasi.” Nelly akajilaza. Na kweli akapotelea usingizini
kwa haraka tu.
Akiwa usingizini akasikia “Nelly! Nelly!” Sauti ya Billy ikimuita
taratibu kama asiyetaka kumuamsha kwa kumshitua. Lakini alikuwa amechoka, mwili
hautaki tena kufanya chochote, sio kama asubuhi walivyoamshana kwa hamasa wakiambiana
hiyo ni siku yao. Wakapeana mabusu mazito hapo kitandani wakitizamia penzi la
fungate ndipo wakakiacha kitanda. Lakini mchana huo Nelly amelala hapo, moyo
hautaki tena kama mwili wake. Akabaki amejilaza tu bila kuitika japo Billy alijua
amemsikia.
Akamsikia tena Billy, “The More You Take
The More You Leave Behind. Who Am I?” Nelly akajua anampa hicho
kitendawili makusudi ili afikirie mpaka usingizi uishe. Na kwa kuwa Billy
alimjua kwanza ni ‘light sleeper’. Kwamba huamka kirahisi sana. Hata
yeye huwa hawezi kutoka kitandani kabla ya Nelly kama anataka Nelly apumzike. Hata
kwa kwenda chooni wakati wa usiku au kujigeuza mara nyingi hapo kitandani, huwa
Nelly anaamka. Kwa hiyo hata hapo alijua amemsikia, hana haja ya kurudia. Pili
alimjua Nelly hapendi kushindwa. Akajua lazima hapo alipotulia, anafikiria. Akamuacha.
Alipomuona anatabasamu, hajafungua macho, akaanza kucheka. “Wewe sema
kama umeshindwa.” “Si kirahisi hivyo.” “Sawa Nelly.” Nelly akamgeukia. “Nina
jibu, lakini sina uhakika.” “Na unapata nafasi moja tu ya kukosea. Kwa hiyo
kuwa mwangalifu.” Nelly akatulia kidogo kisha akamwangalia tena. “Gari.” Akajibu.
“Mmmh! unakaribia ila sio jibu.” “Billy wewe! Mimi nahisi wewe mwenyewe hujui
hicho kitendawili.” Billy akacheka sana. “Yaani mleta kitendawili hajui jibu?” “Hushindwi
kutunga tu jamo ili kunisumbua.” “Sawa Nelly. Ila mimi nakwambia hilo sio jibu
lake.” “Basi katika hilo jibu lako ongeza na hili langu. Maana linaleta maana. Yaani,
jinsi gari inavyotembea, inachukua umbali zaidi, na kuacha umbali nyuma.” “Wewe
tunga cha kwako na uweke hilo ndio jibu lake. Acha kulazimishia majibu kwenye riddle
yangu.” Akamuona ametulia. Akajua anafikiria tena. Hakubali kushindwa. Billy
akacheka sana na kutoka hapo kitandani.
“Usikimbie sasa!” “Nakwenda kutumia choo, nitarudi kuja kusherehekea
kukuweza.” “Si kirahisi hivyo Billy. Ukirudi nitakuwa na jibu. Ila ujue nafasi
ya kujaribu zinakuwa mara nne.” “No way!” Billy akakataa kabisa. “Mimi
ndio nimekupa kitendawili na mashariti ya kujibu.” “Sijakataa. Mimi mara mbili,
na mtoto mara mbili.” Billy alicheka mpaka akarudi kukaa. “Nelly!” “Kumbe! Wewe
unavyosema nile, kunywa na kuishi nikijua sasa hivi tupo wawili kwenye huu
mwili, unategemea nini? Ndio ujue tupo wawili kwenye kila kitu. Ila kwa jinsi
ya akili ya huyu mtoto na mimi mama yake tulivyo, usiogope, dad. Hatutatumia nafasi
zote tatu zilizobaki. Tutakuwa tumeshapata jibu.” Billy akacheka sana. Ila kwa
furaha kuona kwa mara ya kwanza Nelly anazungumzia ujauzito wake akitambua
mtoto aliyebeba na kumuunganisha na yeye. Akajua ni kweli ameanza kukubaliana
na matokeo.
“Sawa Nelly. Ila siamini kama umeshaanza ku play pregnacy card!
Hayo ni matumizi mabaya ya huo ujauzito.” “Ndio ukweli wenyewe. Wewe tupishe
tufikirie.” Billy akatingisha kichwa kwa masikitiko akicheka na kuelekea maliwatoni.
Akiwa chooni akamsikia Nelly akimuita kwa kuhamasika sana. Akajua amepata jibu la
hakika na hataki kusubiri. “Nitajikojolea Nelly!” “Nimepata jibu. Ni footsteps. Hapo huwezi kubisha.” Akamsikia akicheka
sana huko chooni. Akajua amepatia.
“Yes!” Nelly akajipongeza. Billy akatoka akicheka. “Kweli mwanangu
anakusaidia sana.” Nelly alicheka mpaka machozi. “Sio akili yangu mwenyewe?” “Wewe
ulishashindwa. Hiyo ni akili ya mwanangu. Hongera sweetheart. Akambusu Nelly
tumboni. Utakua na akili kumzidi mami wako?” “Nahisi ni kukuzidi wewe dad.
Maana amepata nafasi ya kwanza na kuitendea haki.” Billy akazidi kucheka. “Mimi
sina shida ya kupitwa na mtoto, Nelly!” “Mimi
nina shida.” Billy akazidi kucheka akimjua Nelly, kweli hapendi kushindwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakasikia mlango ukigongwa taratibu. “Ni mimi, dad.” Sauti ya Britney.
“Unapenda kucheka kwa sauti wewe! Nyumba nzima wameshajua tumeamka!” Billy
akakimbilia mlangoni. “Hey baby girl.” Akamfungulia kwa furaha. Nelly alijua
jinsi Billy anavyompenda huyo mtoto, kuliko nafsi yake. “Umependeza sana,
sweetheart.” Akamsikia Billy akimsifia. “Asante dad. Naweza kuongea na Nelly?” Billy
akarudisha kichwa ndani kumtizama Nelly pale kitandani. Nelly akatingisha kichwa
kukubali akimjua huyo mtoto jinsi alivyo mwema. “Ingia.” Billy akampisha
mangoni.
“Vipi Britney?” Akamsogelea pale kitandani. “Kwanza umependeza sana.”
Britney akacheka lakini akionekana ana
jambo anataka lazima kuzungumza. “Asante. Wanamalizia kutengeneza wengine ili
waje kwako.” “Hamna shida. Vipi?” Akatulia kidogo, baba yake akiwa nyuma yake. Wote
wakampa muda wa kujipanga na kuzungumza. Akamuona baba yake anambusu kichwani
kwa nyuma taratibu kama asiyetaka kuvuruga nywele. Britney akacheka taratibu na
kugeuka. “Thanks dad.” Billy akamkumbatia. “Si unajua unaweza kuongea na Nelly
chochote?” Akajua anamtuliza na kumtia moyo aongee.
Akabaki amesimama na baba yake, amemkumbatia kwa upendo. Wakamuona anacheka.
“Ni nini?” “Kwanza nataka kumuombea msamaha Briana. Kabla dad hajasema
chochote, acha nimalizie.” “Mimi sitaingilia. Wewe umesema unataka kuzungumza
na Nelly. Ila nitataka kujua huo msamaha unatoka kwake au ni wazo lako?” “Labda
nimwambie Nelly ukweli pengine italeta maana.” Akaendelea Britney. “Wakati mama
akidai talaka, Briana alikuwa mdogo na hatukutaka au alifichwa mambo mengi ili
isimuathiri. Hakuwa akijua kinachoendelea kabisa. Hata mimi sio kwamba
niliambiwa. Ila nilikuwepo nyumbani, nilijua kinachoendelea, dad akiwepo na wakati
hayupo. Kuna mambo hata kabla mami hajaomba talaka alikuwa akituambia mimi na
Briana, juu ya dad, lakini kwangu hayakuwa yakileta maana kwa vile nilivyokuwa
nikimuona dad anavyokuwa kwetu na hata kwa mama mwenyewe, pale dad anapokuwepo
nyumbani.” Britney akaendelea.
“Kwa haraka sana mimi nikajua kama kuna ukuzwaji wa mambo. Alichokuwa
akikizungumza mama kwetu ni kama kukuza au kuweka tatizo ambalo kwanza
halikuwepo na dad mwenyewe alionekana ni kama hajui kabisa kama hilo tatizo
lipo. Kwa jinsi dad alivyokuwa akiishi pale nyumbani anaporudi. Kwa hiyo kwa
upande wangu nikawa napata muda wakumwambia Briana kile ninachojua kitamsaidia.
Kuwa dad anatupenda sana, ila inamlazimu kufanya kazi ili sisi tuishi vizuri. Kwa
kifupi tu ili kumfanya asihisi tupo kwenye mazingira mabaya. Na ukweli hakuwa
akielewa sana kwa kuwa hata mama alipokuwa akitaka kuanzisha ugomvi, dad
alikuwa akitaka wakazungumzie nje kabisa wala si chumbani au pale ndani ambako
sisi tupo. Kwa hiyo mara nyingi maneno yaliyokuwa yakiendelea kati yao, yaani
kati ya dad na mom, dad aliyaweka kwa kificho ili kupunguza wasiwasi kwetu pale
nyumbani.” Britney akaendelea taratibu tu.
“Ninachotaka kukwambia, ni kuwa, mimi nilikuwa nikijua mambo mengi
kuliko hata Briana na dad, kwa kuwa nilikuwa mkubwa, niliweza kujua
kinachoendelea tukikuzwa katikati ya hawa wote watatu. Dad, mami na Carlos. Lakini
si Briana. Na tabia ya Briana kutaka vitu vizuri na kuhakikisha anavipata ni
tabia iliyopo ndani yake ila tu hajapata uongozi mzuri ya jinsi ya kujipatia
yeye mwenyewe. Nimetoka kuzungumza naye hapo chumbani nikijaribu kumuelewesha
na kumpa uhalisia wa mambo zaidi maisha kwa jumla. Anaonekana ameanza kuelewa,
ila anahitaji muda. Hajui maisha mengine bila mama. Hawezi kuishi kwengine ila
na mama. Mama anamjulia sana Briana. Na ni marafiki wale ambao wanasindikizana
kila mahali. Ila ameanza kuelewa. Anaomba msamaha kwa kuwaingilia. Hakuwa hata
akijua kama mama ndiye aliyeomba talaka. Yeye alijua dad aliamua kututelekeza
ndio Carlos akawepo kumsaidia mami.” Billy akaumia sana.
“Alikuwa akijua dad alichagua maisha yake zaidi yetu sisi. Na sio
kosa lake. Alifichwa na kila mtu, akabaki kusikiliza upande mmoja tu. Tafadhali
naomba msamehe. Sio mtoto mbaya. Na usibadili mawazo juu ya baba hata juu yetu.”
“Nimekuelewa Britney. Na asante.” Nelly akajibu hivyo tu kwa jumla. “Utamsamehe
Briana?” Akamuuliza Nelly kwa upendo kama alivyo, akiwa amejua ametoa jibu la
jumla sana.
“Acha nikwambie ukweli Britney. Hapa si kwenye kusamehe au
kutokusamehe, kwa sababu wote tunajua ni zaidi ya hichi alichokifanya hapa na
mama yenu, au kushindwa hata kunishika mkono kwa salamu, au kuniuliza maswali mabaya
mbele ya watu, akionyesha kunidharau na kutaka kunidhalilisha. Sidhani yeye
kama Briana anashida na mimi kama Nelly, ila mwanamke yeyote anayejaribu kuonekana
kuchukua nafasi ya mama yenu kwa baba yenu. Hata kama nikisema sitamsamehe au
ninamsamehe yeye, ukweli haitajalisha kwetu sisi wawili. Nikimaanisha mimi na
yeye kama mtoto wa Billson.” Nelly akaendelea.
“Kama ulivyosema. Anahitaji muda. Basi apewe muda na mimi nina mambo
mengi, hamtanisikia hata kuwabugudhi. Pale mnapohitaji msaada wangu, mnijulishe
kwa njia yeyote ile, hata kupitia baba yenu nitafanya kwa kadiri ya
nitakavyoweza. Lakini ninachotaka kukuhakishia Britney, nampenda baba yenu, na sitaki
kumtumia kifedha. Mimi sina shida na hela ya baba yenu hata kidogo. Yaani hata
akiniacha leo na huyu mtoto, kifedha nakuhakikishia tutakuwa sawa kabisa wala
hatutahisi kupungukiwa ila kumkosa Billy kama Billson mwenyewe. Hilo tu.”
“Nampenda Billy na ninamuhitaji. Hapa nilipofika, hakuna mtu atafanya
nisiwe naye, hata kama ni mara moja kwa mwezi ndio nitakuwa nikimuona, mimi
sitajali, ilimradi najua nipo naye. Nishafikiria, nishahesabu garama zakulipa
na faida, nikaishia kuona mizani inalemea kwenye faida za kuwa na baba yenu. Anachohangaikia
kwenye maisha ni kama mimi tu. Hatuna tofauti. Najua maana ya kufanya kazi kwa
bidii, kujituma zaidi ya unavyotakiwa na kulipwa, na uthamani pamoja na nidhamu
ya pale milango inapofunguka mahali. Kwa kuwa na mimi nimekua si kama nyinyi
Britney. Mimi nimejikuza kwa shida sana huku nikimkuza huyu mdogo wangu. Nimepambana
sana kufika hapa nilipo nikisubiria milango migumu ifunguke ili niweze kuingia.
Najua maisha kwa kuyaishi. Na namjua binadamu kwa kuishi nao.”
“Pressure ilipanda si kwa maneno aliyoyasema mama yako na Briana. Hata
kidogo. Mimi namfahamu mwanadamu. Najua anaweza kugeuka mbaya kuliko simba
mwenye njaa. Ila nafikiri nilishitushwa na kule kuvamiwa kwao, nikiwa tayari na
tension ya maandalizi, na mambo mengine mengi. Billy ananijua. Napenda vitu vizuri
ndio maana nafanya kila kitu changu mwenyewe na kwa bidii. Na ninapenda kwenda
na muda. Siwezi kuchelewa popote pale. Ndivyo nilivyo. Kwa hiyo sio mzuri sana
kufanyiwa mambo na baba yako ndio yupo kwenye kunisaidia. Siwezi kufanyiwa mambo
na zaidi nikiwa sijui kinachoendelea. Nataka kusimamia kila kitu mpaka kuona
mwisho wake. Sasa kitendo cha kukaa hapa ndani, jambo letu muhimu likiendelea
huko nje, halafu sijui kinachoendelea, ila kuambiwa tu tulia, usiwe na
wasiwasi, tayari sikuwa sawa. Nipo stress out.” Billy akacheka.
“Billy ananijua. Anyway, kingine huu ujauzito umekuja na
pressure.” “Pole Nelly.” “Asante. Sio mbaya sana, ila huu mwili huwa unatafuta
sababu yeyote ile ili kuipandisha. Ninachotaka kusema kwako ni, acha muda ujibu
kila kitu. Tusiwe na haraka ya kesho kabla hatujaishi leo. Leo naolewa na
Billson. Na wewe ni mmoja wa wasimamizi wangu, hilo nimeliheshimu sana,
Britney. Asante kunipokea na kuniamini bila kunifahamu.” Britney akacheka
taratibu. “Karibu Nelly. Nataka dad awe na furaha kama hivi ninavyomsikia
anacheka sasa hivi! Mpaka bibi alikuwa anasema Billy wake wa zamani amerudi. Dad
alibadilika, Nelly!” “I am standing right here!” Nelly na Britney
wakacheka vile Billy alivyosema wasimtete, anasikia.
“Huyo nimekutana naye akicheka hivyohivyo.” “Anapenda kucheka kama
babu na baba mkubwa. Lakini hakuwa akitoa kicheko cha kutoka rohoni cha kweli.”
“Britney!” Baba yake akajidai kushangazwa kwa kuumia sana akishika moyo. “Kweli
dad! Ila nakupenda.” Wakazidi kucheka hapo. “Baba yako ananijua. Nikikusudia kufanya
kitu, huwa nafanya kwa juhudi zangu zote. Leo naolewa na Billy, hakuna
kitakachonibadii mawazo labda Billy mwenyewe akatae. Ila si kwa maneno ya
yeyote yule au vitisho. Hata pressure ipande vipi, leo nitaolewa na bili hata
wodini, nitaita atakayefungisha ndoa, hili limalizike leo, wala si kesho, Mungu
akipenda. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi kabisa. siwezi kubadilika kwa baba yako. Sisi
wawili tupo sawa kabisa.” “Asante Nelly. Ni sawa nikiku hug?” Akaomba
kumkumbatia kwa upendo. Nelly akacheka. “Karibu.” Akaenda kumkumbatia pale
kitandani.
“Ila na wewe ni mzuri Nelly. Hata babu amekusifia.” Nelly akacheka. “Asante
Britney.” “Acha niwaite watu wa kukutengeza wakuweke sawa kabla ya harusi. Shangazi
ameondoka na kuniachia maagiza ya usisumbuliwe kabisa. Unywe maji mengi na
lazima utengenezwe vizuri.” “Nitamshukuru Beila baadaye. Lakini kwa sasa nipo
sawa.” “Basi nakupisha kwa muda. Baada ya dakika 20 wapiga picha na wachukua video,
pamoja na wasimamizi wote wa kike tutakuja kupiga picha za kitandani tukiwa na
robs zetu, ndipo tukavae, tuje tupige tukiwa na nguo rasmi. Kila kitu kipo
vizuri. Hakuna kitakachoharibika. Tumejipanga vizuri.” “Bora umuhakikishie wewe.”
Billy akaongeza, wakacheka, Britney akatoka.
“Acha nikupime pressure kabla sijawaruhusu waingie wakutengeneze.” “Sitamani
mtu anishike tena Billy. Sijui kwa nini! Natamani hata kubaki hivihivi tu.”
“Jikaze utengenezwe. Huu ni ukumbusho wako wa muda mrefu. Utakuja kujichukia
kama hutatoka kama ulivyotamani. Tuna siku nyingi tu za mapumziko, utapumzika
tukiwa sisi wawili tu bila mtu mwingine. Jikaze.” Baada ya yote, Nelly
akafanikiwa kutengenezwa na picha kupigwa hapo chumbani akiwa na wasimamizi
wake kisha kubakiwa na msimamizi wake, ambaye ni mke wa Brandon, akamsaidia
kuvaa.
Nelly&Billy
|
“Unachukua muda wangu wote na Nelly, bwana! Unazungumza nini humalizi?
Wewe mlete hapa mbele, niachie mwenyewe.” “Sawa Billson.” Jax akamshika dada
yake na kuanza kutembea kuelekea mbele alipokuwa amesimama Billy, kaka yake na
wasimamizi wengine pamoja na mchungaji.
Harusi ya Billy na Nelly ikafungwa palepale nyumbani kwao ila nyuma
tu kwenye ua. Palitengenezwa vizuri sana. Ukweli Billy alionekana amefurahia sana.
Billy alitaka wimbo wa ‘Your my african qeen’
uwe unarudiwa rudiwa kila wakati na baadaye wakafungua mziki kwa kucheza wimbo wa
taratibu wa George Benson wa ‘Nothing’s Gonna Change My
Love For You’. Aliimba Billy huku akicheza na Nelly, mpaka watu
wakaelewa safari hii amepata mwanamke anayempenda. Aliimba akiwa amewekewa
kipaza sauti kile chakushikiza kwenye tai aliyokuwa amevaa, sauti yake ilisikika
vizuri sana kupitia kipaza sauti hicho kidogo tu, akimwambia Nelly, ‘hakuna kitakachobadilisha mapenzi yake kwake’. Akaendelea
kumuimbia huku amemshikilia vizuri wakicheza.
Walipomaliza wakamuona anamnong’oneza kitu Nelly, akatingisha kichwa
kukubali, akambusu na kutoka kwenye dance floor, sehemu waliyokuwa wakichezea
akaenda kumnong’oneza kitu Jax. Jax akasimama na kwenda kucheza na dada yake, yeye
Billy akaenda kumuomba binti yake wacheze naye. Britney alifurahi sana. Akasimama
na kumbusu baba yake, akaenda naye karibu na Nelly. Kama waliojua, wimbo
ukabadilishwa kwa haraka, ukawekwa wa Whitney Huston wa ‘I will always Love you’. Alilia sana Britney kila maneno
yalipokuwa yakirudiwa na baba yake, kuwa hata akiondoka, akimaanisha akibadili
maisha yake kuwa na Nelly, lakini wakati wote atabaki akimpenda. Britney
akachukulia kama anamwambia upendo wake kwake utabakia vilevile hakuna kitakachobadilika
daima. Akamlalia baba yake begani wakiendelea kucheza. Briana akabaki ameinama
sehemu aliyoachwa na dada yake. Billy alicheza na binti yake huyo mpaka
akamaliza.
Akamrudisha na kumvutia kiti akakaa. Kisha akamsogelea binti yake
mdogo pale alipokuwa amekaa pembeni ya dada yake, akamuomba wakacheze. “Nilijua umenichukia, dad!” “Never sweetheart. Hata
iweje, sitakuchukia.” Akamnyoshea mkono, Briana akapokea mkono wa baba yake akijifuta
machozi. Akasimama na kurudi pale katikati sehemu ya kuchezea. Wakarudia tena
wimbo uleule kama aliomuimbia dada yake. Ila Billy akaanza kwa binti yake. “Unaweza
kusahau kila kitu juu yangu Briana. Lakini nataka ujue hili, wakati wote
utabakia kuwa my little princess. Nakupenda sana, sweetheart. Na sijawahi
kubadilika kwako na hakuna atakayechukua nafasi yako kwenye moyo wangu. Ila
nataka usichelewe kwenye maisha. Ishi maisha ya uhalisia. Na nataka uanze kuishi
mimi nikiwepo. Nakuahidi kukushika mkono, endapo utanipa nafasi, au ukinichagua
nitembee na wewe.” Briana akalia sana. Na yeye akamuimbia wimbo uleule kama
dada yake. ‘I will always Love you’. Akamuimbia mpaka
ukaisha. Ulipobadilika tu na kurudiwa wimbo wa, ‘Your
my african qeen’. Jax akaenda kumchukua Lara. Wakarudi naye kucheza pale
mbele. Billy akapenda jinsi wanavyoucheza huo wimbo, akaanza kufuatisha. Walicheza
usiku huo wakicheka mpaka Nelly akasahau swala la ujauzito wake na Anele. Baada
ya harusi kuisha wawili hao walitoka hapo kuelekea fungate.
Lara&Jax.
K |
esho
yake Jax na Lara wakapelekwa uwanja wa ndege kurudi nchini Tanzania. Jax
alitakiwa kazini. Ikawa kama mchezo tu, dada yake ambaye hakuwa hata na mipango
mingi juu ya ndoa, ndio akaolewa kwa haraka bila kikao cha harusi wala mipango
ya muda mrefu, na baraka ya mtoto juu. Wakiwa kwenye ndege Jax akaanza. “Nakupenda Lara. Na nakusubiria kwa
hamu kwenye siku yetu na sisi.” Lara akacheka. “Na safari hii nasema wazi
kabisa, nataka watoto.” “Wangapi?” Lara akauliza akicheka. “Nguvu yako tu.” Lara
akafurahi sana. “Hata watano!?” “Ukiwa na uwezo huo, mimi sina shida.” “Jax! Huogopi
garama za maisha?” “Nikikwambia hivyo nitakuwa nakudanganya Lara. Wewe unajua
historia yetu mimi na Nelly. Hapakuwa na mipango mingi tuliyowekewa na wazazi
wetu kwenye maisha, lakini si unaona tulipo? Wewe mwenyewe umekuwa ukinifundisha
juu ya mipango ya Mungu kwa mwanadamu. Wala si mipango ya mwanadamu kwa mwanadamu
mwingine. Japo mimi kama baba sitazembea na kufanya kosa kama baba yangu. Nakusudia
kufanya vizuri zaidi. Lakini sitaogopa.” Hilo likamfurahisha sana Lara.
“Mwenzio napenda watoto, Jax.” “Hilo nimekuja kugundua kwako. Sikuwa nikijua
kabla.” Akamuona Lara ametulia kabisa, anataka kupotea pale kimawazo. Akajua kumbukumbu
zinataka kumrudisha vile alivyopoteza mtoto. “Mungu atatujalia wengine Lara. Tafadhali
jipe moyo.” “Naamini hivyo Jax. Sijui kwa nini yule mtoto ananiuma sana! Huwa
nakaa nahesabu, najiambia pengine nisingefanya hili au lile, leo angekuwa
amefikia hiki au kile! Umri huu au kile! Ilimradi tu. Ila tuache hilo.
Nimefurahi kama huna shida na kuwa na watoto wengi.” Jax akatulia kidogo.
“Nikuulize swali?” Lara akamgeukia. “Huwa ukikumbuka hivyo unanichukia?”
“Hapana Jax! Hata kidogo! Kwa nini unafikiria hivyo?!” “Sijui!” “Hapana. Unajua
mama aliniambia Mungu huwa akipanga jambo lake hakuna mwanadamu anaweza
kusimama na kuzuia. Akaniambia wapo wanawake huwa wanapigwa na waume zao kila
siku na bado wanauwezo wa kubeba mimba na kuzaa. Kama Mungu angeona wakati ule
nina uwezo wakumlea yule mtoto, angeacha niwe naye. Nahesabu ni kama Mungu
alimchukua kiumbe chake, aliona sipo tayari naye au hapakuwa na mazingira
mazuri yakumlea. Simaanishi kifedha, ila pengine hata mimi. Sijui Jax. Kuna mambo
mengine hayana majibu. Lakini kwa hakika sikuchukii. Au unafikiri ni kwa kuwa
hatufanyi mapenzi?” “Eti nakuhisi umebadilika Lara. Siye Lara ninayekufahamu. Siye
Lara unayetaka nikuweke mikononi.” “Ni kwa sababu ya kukataa usinikumbatie jana
usiku?” “Sijui Lara.” Jax akajibu kama ambaye anakata tamaa.
“Jax, amini nakupenda na
kukutamani sana mpenzi wangu. Jana nilikuwa nimezidiwa, nikajua ukinishika tu
pale kitandani, naweza kuamka asubuhi na majuto na kujichukia sana. Nilitamani sio
unishike tu. Nilikuwa natamani unifanyie kila kitu ndio maana nilikuwa
nakukwepa. Nahisi nipo mwenye siku za kushika mimba ndio maana nimepandisha
joto na hamu ilinizidia. Ila sio kwa sababu nakuchukia Jax. Nisingekuwa na wewe
kama najilazimisha. Sina sababu Jax. Na sitafanya hivyo.” “Kufanyaje?” “Eti kujilazimisha
kuwa na wewe! Hapana Jax! Sina sababu yakufanya hivyo. Kwa nini kwanza? Nakupenda
Jax na ndio maana nipo na wewe na nakusubiria kwa hamu.” Jax akaridhika.
“Nelly ameniambia mambo yanaenda vizuri. Naamini tutafanya kila kitu
kwa wakati. Na nimebania siku zangu za likizo ili nizichukue zote kama zilivyo
tukapate muda mrefu wa pamoja baada ya harusi yetu. Tutakuwa na wakati mzuri
sana.” “Mimi mwenyewe nasubiria kwa hamu. Nakupenda Jax. Huna makuu. Rahisi kuishi
na wewe. Namimi nakuwa kama Nelly. Nakutaka wewe, sibadiliki hata iweje.” Wakacheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nelly alirudi nchini akiwa amepata mapumziko ya kutosha. Mke wa
Billy, kazi na ujauzito ambao unao mume.
Akawa ametulia, akili kwenye harusi ya mdogo wake. Ndani ya miezi mitatu
akawa amekamilisha harusi ya Jax. Lara akawa amejawa furaha, ndoto zake
zimetimia. Gauni alilokuwa kiota tokea mtoto, akawa amelipata tena la hadhi
zaidi ya alivyotaraji. Jax ni wake na Nelly anampenda, yupo upande wake.
Alikuwa akimuhangaikia na mimba ya miezi saba lakini akawepo mstari wa mbele
kuhakikisha jambo haliharibiki.
Siku mbili kabla ya harusi yake akiwa ofisini akashitukia shemeji
yake amemsimamia. “Siku ya harusi yangu sikumbuki kama ulinipa zawadi.” Jax
akakunja uso akimwangalia Billy. “Nimekuja kukwambia kuwa hujachelewa.” Jax akabaki
akimwangalia na uso wa sikuelewi, na Billy naye akabaki amesimama kama
anayesubiria. “Unataka zawadi gani!?” Ikabidi Jax amuulize. “Umeuliza swali
zuri sana. Sasa, nataka kujua jinsia ya mtoto wangu.” Jax akakunja uso. “Hapo
ndipo wewe unakuja. Fanya juu chini umlazimishe Nelly, akaangalie jinsia ya
mtoto.” Jax alishangaa mpaka akarudisha kiti nyuma na kubaki akimtizama Billy.
“Naanzia wapi!? Hivi unajua mimi na Nelly hatuzungumzii mambo kama
hayo?” “Na hivi unajua ni wewe peke yako hapa duniani ambaye Nelly hawezi
kusema ‘hapana’ kwako hata kama umemuudhi?” “Billy!” “Hakika nahitaji
msaada wako Jax, na nilazima unisaidie. Nelly amekataa kabisa, na mimi mama
ananiulizia kila wakati. Mpaka muda mfupi uliopita amenipigia kutaka kujua
jinsia ya mtoto!” “Sasa ni kwa nini humwambii Nelly mwenyewe?” “Nelly amekataa.
Na amesema niwaambie nyumbani kwetu wote wasubiri mpaka ajifungue.” “Sasa kwa
nini huheshimu hilo?” Jax akamuuliza. Akamuona anauma meno huku akisema.
“Shhhhhhh, nope!” Akakataa.
“Billy!?” “Siwezi kusubiri mpaka siku anazaliwa eti ndio nakwenda kukutana
na mtoto nisiyemjua! Hapana! Nataka kuandaa jina kabisa. Yaani siku ile
anazaliwa, nakwenda kukutana na mtoto ninayemfahamu. Hapo sasa ndipo unapokuja
wewe kusaidia.” “Sidhani kama nitaweza kuwasaidia, Billy.” “Usijali.
Nimeshaanza kukutengenezea mazingira mazuri. Kliniki ya kesho, nitamwambia
uende naye wewe. Atashangaa kwa sababu kesho ni siku ya kuangalia mtoto,
anategemea ning’ang’anie kwenda naye, lakini mimi nitajidai nipo busy, ili wewe
uende naye. Mkiwa njiani na kule sasa ndipo umwambie unataka kujua jinsia ya
mtoto.” “Nelly anaakili sana, atagundua ni wewe umenituma!” “Sio kwako. Kwako
huwa hafikiriii.” Jax akabaki akimtizama.
“Tafadhali Jax.” “Siwezi kumdanganya Nelly. Wewe nipe siku ya leo,
nitazungumza naye.” Billy akavuta punzi kwa nguvu, kwa furaha. “Do you Jax. Do
you man.” Akamwambia hivyo akimpigapiga mgongoni, kisha akaondoka kwa furaha
akimwambia afanye vile awezavyo yeye.
Hapohapo Jax akampigia simu Nelly. “Naweza
kukuona mida ya jioni?” “Nakuja hapo ofisini kwenu kumsuprise Billy. Amekuwa akinisumbua
anataka kujua jinsia ya mtoto.” “Umeshajua?” “Nimejua. Nilienda leo sehemu
kumuangalizia, ili amwambie mama yake, waache kunikera. Kwa hiyo nakuja
hukohuko, nitakupitia na wewe.” “Huna haja ya kuja. Nilitaka kuzungumza na wewe
juu ya hilo.” “Usiniambie na wewe alikufuata kwa ajili ya hilo!?” Jax
akacheka na kumjibu. “Inaonekana kwao inamaana kubwa
sana.” “Hana lolote huyo Billy. Ni mpenda kujua tu mambo. Acha nikazungumze
naye.” “Ni mtoto gani?” Jax akauliza. “Acha
kwanza nikamwambie yeye wa kwanza, yeye mwenyewe ndio akwambie. Akijua wewe
umejua kabla yake anaweza kuumia.” Wakacheka na kuagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kitendo cha Billy kujua Nelly amebeba mtoto wake wa kiume, ikawa
shida. Kila mtu alijua mtumzima huyo anatarajia mtoto. “Wewe si ulisema hujali
jinsia wewe?” “Hata angekuwa wakike pia ningefurahia tu.” Nelly akamtizama kwa
kumsuta, lakini kwa hakika wote walifurahia huyo mtoto, wakaongeza kitu kingine wanachokitizamia kwa hamu, wakijua ni jukumu si la kutumia tu akili na pesa, ila wao wenyewe kama wazazi. Na Billy alionekana
kuwa na furaha na Nelly, zaidi ya walivyotarajia. Akawa akilala akiwa na
uhakika wa kuamka pembeni ya Nelly wake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jax alihamia kuishi nyumbani kwa Nelly
kwa muda wakisubiria harusi, kwani Nelly ni kama alihamia anakoishi Billy, Lea
naye alishakuwepo jijini tokea Lara na Jax wanarudi nchini kutoka Uswiz. Akawa
akiishi hapo na mdogo wake. Kwa hiyo hata ndugu wa Lara walitua jijini mapema
tu tena wakiwa na furaha wakiwa na tumaini safari hii harusi ipo tena wakiwa na
uhakika na sehemu ya kufikia. Nyumbani kwa Jax na Lara. Japokuwa Lara
alimwambia Jax angeenda mwenyewe kuwapokea ndugu zake kituo cha mabasi, lakini
na yeye Jax akataka kuwepo. Wakaongozana kwenda kuwapokea na kuwapeleka
nyumbani kwao.
Baada ya chakula cha usiku cha pamoja, Nelly
na Billy nao wakiwepo kuwakaribisha, mama Chiwanga akaona atoe neno la
shukurani. “Nelly mama, Mungu akubariki kwa kusimama na wanangu. Kumpa kazi Lea
na kusaidia Lara kwenye kila hatua ya harusi yake. Na wewe Mungu akuinulie wakusimama
na wanao.” “Ni mmoja tu mama yangu. Hii shuguli sirudii tena.” Nelly akawahi
kwa haraka nakufanya wacheke.
“Kamoja kama dawa, mama!?” “Kabisa
baba yangu. Huyuhuyu. Sitaongeza. Na umri wenyewe umekwenda. Sitaki Jax aje
alemewe kusomesha baadaye.” “Basi mimi nakuombea umri mrefu. Usomeshe mwenyewe,
ulee mpaka uje umkabidhi kwa mkewe kama hivi unavyohangaika kwa Jax na wanangu,
basi na wewe Mungu akutendee.” “Amina mama yangu. Hilo nashukuru.” “Kabisa
mama. Huyu Lea alishachoka hiyo kazi aliyokuwa akifanya huko Dodoma. Akabakia
kwenda tu kazini ilimradi siku ziende. Kwa hiyo kama anavyosema mama yao,
asante kwa kumtafutia Lea kazi.” “Ni amempa kazi ofisini kwake, baba.” Lara
akamrekebisha. “Kumbe! Basi Mungu wangu akubariki.” “Amina baba, lakini nimempa
masharti magumu huyo, na hana jinsi. Nimemwambia nilazima ayatimize yote lasivyo
namfukuza kazi.” Jax akajua Lea ataonja joto vilivyo, Nelly hana utani.
“Ameniambia. Nakuahidi atarudi tu
shule. Atasoma.” “Lara alishanisindikiza chuoni. Nimeshachukua fomu na kulipia,
nitakuwa nikisoma masomo ya jioni, na nimeshaanza kufanyia kazi kuzungumza
kwangu. Namfanya Lara ndio mtu wangu wa kunisikiliza nikitoa ripoti yangu
ofisini kila siku. Na Jax naye pia ananisaidia kwenye swala la kuzungumza na
jinsi ya kusimama na kuangalia watu.” “Na lugha Lea.” Nelly akaweka msisitizo.
“Anafanya na anajitahidi kwakweli. Ripoti zote anazokuwa akiandika, anaandika
kwa lugha ya kingereza. Namsaidia kurekebisha jioni nikipitia hapa kuwaona,
ndipo anajaribisha kuizungumza kama yupo mbele yako. Naona na hofu imeanza
kupungua.” “Hapo sawa. Ilimradi kila muhula uwe unanipa matokeo yake ya chuo,
nijue bado yupo chuoni. Aweze kujieleza vizuri, basi ajue ajira anayo. Lasivyo
ajira itaota mbawa. Mimi siwezi kuwa karibu ya watu wasiojituma, wazazi wangu.
Naona kama wananichelewesha.” “Lara alishatumbia.” Jax akacheka akitingisha
kichwa. “Sasa unasikitishwa na nini na wewe Jax. Si bora niwaambie ukweli tu,
na Lea aelewe. Sifanyi michezo ya kizembe. Lazima ajifunze kukimbia na timu
yangu.” wao wakaondoka mpaka Jax, wakamuacha Lara na ndugu zake. Vilikuwa
vimejaa vicheko hapo.
“Ameniambia. Nakuahidi atarudi tu
shule. Atasoma.” “Lara alishanisindikiza chuoni. Nimeshachukua fomu na kulipia,
nitakuwa nikisoma masomo ya jioni, na nimeshaanza kufanyia kazi kuzungumza
kwangu. Namfanya Lara ndio mtu wangu wa kunisikiliza nikitoa ripoti yangu ofisini
kila siku. Na Jax naye pia ananisaidia kwenye swala la kuzungumza na jinsi ya
kusimama na kuangalia watu.” “Na lugha Lea.” Nelly akaweka msisitizo. “Anafanya
na anajitahidi kwakweli. Ripoti zote anazokuwa akiandika, anaandika kwa lugha
ya kingereza. Namsaidia kurekebisha jioni nikipitia hapa kuwaona, ndipo anajaribisha
kuizungumza kama yupo mbele yako. Naona na hofu imeanza kupungua.” “Hapo sawa. Ilimradi
kila muhula uwe unanipa matokeo yake ya chuo, nijue bado yupo chuoni. Aweze kujieleza
vizuri, basi ajue ajira anayo. Lasivyo ajira itaota mbawa. Mimi siwezi kuwa
karibu ya watu wasiojituma, wazazi wangu. Naona kama wananichelewesha.” “Lara
alishatumbia.” Jax akacheka akitingisha kichwa.
“Sasa unasikitishwa na nini na wewe
Jax? Si bora niwaambie ukweli tu, na Lea aelewe. Sifanyi michezo ya kizembe. Lazima
ajifunze kukimbia na timu yangu.” “Nitajihidi au najitahidi kwa kadiri ya uwezo
wangu.” “Na wewe mwenyewe usiwe kipimo chako. Maana unaweza kudhani umefikia mwisho
kwa kuangalia uwezo wako tu. Angalia kwa walioweza ndio ujiulize kwa nini wewe
ushindwe! Kwa hiyo upambane, bila kujihurumia na kuubembeleza huo mwili. Weka malengo
na ujiambie lazima yatimie. Kushindwa sio chaguo.” “Nimeelewa bosi wangu. Utapata
matokeo mazuri.” “Hilo ndilo nilitaka kulisikia sio uniambie kwa kadiri ya
uwezo wako.” Nelly akawa anataka kusimama, Jax akamuwahi kumshika mkono,
akamsaidia kusimama. “Nakushukuru.” “Karibu. Ukapumzike sasa.” “Ndicho ninachoenda
kufanya. Maadamu nishalisha haya matumbo matatu, hapa ni kitandani tu.” Akimaanisha
tumbo la Billy, lake na mwanae. “Lea na Lara, tunashukuru kwa chakula kizuri.” “Karibu.
Nimefurahi mmekuja kusalimia wazazi na kuungana nasi kwa chakula cha usiku.” Wakaondoka
mpaka Jax, wakamuacha Lara na ndugu zake.
~~~~~~~~~MWISHO~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment