Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Makosa! - Sehemu ya 1. - Naomi Simulizi

Makosa! - Sehemu ya 1.

Sabrina alijaliwa na Mungu kitu cha pekee ambacho hata yeye mwenyewe hakuwa akijua. Japokuwa alidharaulika hata na watu wa nyumbani kwao, lakini hakuna alipopita na kushika, asibadilishe kwa namna ya ajabu. Mbaya kwake kila alipowafanikishia, hakuwahi kuthaminiwa yeye kama yeye mleta hayo mafanikio kwa sababu ya nafasi ndogo aliyokuwa akipewa, tena wakati wote waliziona nafasi hizo wampazo hazina thamani machoni pawatu. Lakini kumbe kila ashikacho yeye, huleta mafanikio makubwa sana. Yeye asijue na wanaomzunguka wasijue kuwa mikono yake na juhudi zake kwenye mambo hata madogo, Mungu huweka mkono wake hapo kufanikisha.

    Kwa wakati huo ilipomlazimu kuwepo nyumbani, baada ya shule yake ya daraja la diploma akiwa amesomea mambo ya stoo kuisha, tena fani hiyo kuimaliza kwa shida sana huko chuoni hata nyumbani kwao wasijue mazito na magumu yaliyokuwa yakimsibu mtoto wao akiwepo chuoni, napo ikashindikana kupata ajira baada ya kuhitimu. Hilo nalo likawa jambo lililomuongezea fedheha nyumbani kwao. Wakaendelea kumsema vibaya na kudharauliwa vibaya sana kuliko wadogo zake waliorudisha matokeo mazuri nyumbani kutoka shuleni kuliko yeye aliyekuwa akifeli kila anakopita.

Sabrina akawepo nyumbani akisaidia kazi za nyumbani zaidi ufugaji wa ng’ombe na kubadilisha biashara hiyo ya wazazi wake, na kufanyika kama kitega uchumi kikubwa cha familia. Wakati wazazi wakifurahia mafanikio hayo na kumtusi Sabrina akionekana ameshindwa maisha, wakidhani ni mbinu zao mpya zimeleta mafanikio kwenye ufugaji kumbe mkono wa Mungu ulikuwepo juu ya Sabrina kama vile Yakobo kwa Labani. {Kwenye bibilia kitabu cha Mwanzo kuanzia Mlango wa 29.} Ukweli kulikuwa na utofauti. Mafanikio makubwa sana kwenye ufugaji. Ng’ombe wachache waliokuwa nao tena mbegu mbaya, wakaanza kuzaliana na kuongeza maziwa kwa wingi.

Sabrina akawajulia hao ng’ombe kwa kuwaangalia tu. Wakirudishwa kutoka machungani kama hawajashiba basi alijua nini chakufanya ilimradi washibe. Kama kuwaongezea majani na maji. Usafi wa banda lao nao akaweka juhudi akisaidiana na kijana anayehudumia ng’ombe kuhakikisha ni pasafi na ng’ombe wenyewe kuoshwa kwa maji yenye dawa yenye vipimo maalumu ili kuua kupe na wasipatwe magonjwa. Hayo yote aliyokuwa akiyafanya hayakuwa yakionekana yamaana, wakihesabu nafasi yake ni ya chini sana. Kufuga ng’ombe! Wazazi na ndugu wakabaki kuona kushindwa kwake kwa shule na kushindwa hata kuolewa, amebakia tu nyumbani na kazi hiyo ambayo kwao ilikuwa yakudharauliwa. Yote hayo yakawaziba macho kuona au kutambua juhudi zake kwa kile awafanyiacho hapo nyumbani, wakabaki wakimuita ‘fungu la kukosa’. Mtoto aliyeshindwa kusomea kitu cha kueleweka na kupata kazi ya ofisini, na hata mwanaume wa kumuoa, kumtoa hapo nyumbani.

Manyanyaso zaidi maneno machungu aliyokuwa akipewa na kusikia zaidi kutoka kwa mama yake akiwa analalamika hata kwenye simu juu yake, yalikuwa yakimuingia mpaka moyoni! Wakati wote alikumbushwa jinsi alivyoshindwa kimaisha, huku akilinganishwa na ndugu wa familia waliomudu elimu hapo nyumbani kwao, ilikuwa ikimuumiza sana asijue yataisha lini. Yeye akabaki mtoto wakusemwa vibaya na kila sifa za mafanikio ya hapo nyumbani kwao wakajipa wao utukufu na kumsahau yeye aliyekuwa akijituma kupindukia. Japokuwa alikuwa ni dada mwenye wadogo wawili chini yake, haikuwasumbua wazazi kumsema vibaya au hata kumchapa wanapoona anastahili adhabu hiyo hata mbele ya wadogo zake.

Hakuna aliyejali hisia zake popote, na hata wadogo zake wakaweza kumfanyia dhihaka tu kwa jinsi alivyokuwa akichukuliwa hapo nyumbani kwao. Aliyafanya yote akiwa amechoka nafsi na roho, akiamini ipo siku Mungu atamkumbuka na yeye japo hapakuwa na tumaini. Hakuacha kujituma, tena wakati mwingine alifanya zaidi hata ya alivyotakiwa, ilimradi tu kujipendekeza kwa wazazi wake, pengine wamuone na kumtambua lakini ikawa bure tu. Kuanzia asubuhi mpaka usiku akisaidia wafanyakazi wa ndani na nje. Zaidi huko kwa ng’ombe ambako wazazi wake walimtaka awepo huko asubuhi na mapema na jioni wakati mfanyakazi anakamua ili kuhakikisha haibi maziwa na ndiko hukohuko alitumia ujuzi wake aliojifunza akiwa hapohapo nyumbani kutunza hao ng’ombe walioongezea kipato familia.

Kuitwa na baba yake na kutumwa kama mtoto mdogo huku akidharauliwa kuliko hata wadogo zake wa mwisho kikawa kitu cha kawaida. Na mara nyingine alikuwa akiitwa awatumikie hao wadogo zake mapacha ambao walikuwa wakija nyumbani kwa likizo wakitokea shule ya bwani ambako ni kweli walikuwa wakifanya vizuri sana darasani, usingeweza kuwalinganisha na huyo Sabrina dada yao alipokuwa shuleni. Akayafanya yote kwa muda mrefu tu tokea amalize chuo, akajisikia kutaka kupumzika kidogo ndipo arudi kuendelea na maisha hayo ya nyumbani, kwani ni kweli hakuna lililokuwa likionekana likiendelea kwenye maisha yake. Shule aliyosomea kwa ngazi ya diploma ikaishia kichekesho tu hata kwa familia. “Hivi kwa karine hii ya utandawazi, nani anasomea mambo ya stoo jamani!” Wakamkejeli. Na kweli akalithibitisha hilo kwa kutopata kazi ya kuajiriwa. Hakuna aliyemwajiri hata kwa kuuza duka. Akabaki akionekana ni mzigo uliododa.

          Familia hiyo ya watoto watano. Wakike ni wawili tu. Sabina na Sabrina. Sabina ndiye aliyekuwa dada yao mkubwa. Dada wa familia. Alibeba sifa nyingi akamfunika kabisa Sabrina. Ukizungumzia mfano wa kuigwa, alikuwa Sabina. Tabia yakujali nyumbani, ni Sabina. Ajira nzuri ambayo mama yake alikuwa akijivunia hata kwa marafiki, alikuwa Sabina. Kaka yake ambaye anamfuata Sabina, alikuwa na kazi ya kawaida tu. Hakusoma kama Sabina mpaka PhD, lakini aliyamudu maisha yake. Kijana mdogo tu lakini akawa na maisha yake yakujitosheleza, nyumbani kwake hana shida kiuchumi. Wadogo zao ambao ni mapacha wanao mfuata Sabrina, bado walikuwa shule ya sekondari.

          Alipochoka na maisha ya nyumbani akajua sehemu pekee atakayokubaliwa kwenda kusalimia hata kupumzika kwa siku chache ni kwa Sabina dada yake. Akamtumia ujumbe. ‘Niombee nije kukusaidia kazi hapo kwako angalau nipumue hata kwa siku chache dada yangu. Wewe ukizungumza nao watakubali.’ Akaona dada yake anampigia huku akicheka. “Usicheke bwana!” “Washakutibua tena nini?” “Nataka tu kupumzika, nije kidogo hapo mjini, nioshe macho.” Sabrina akabembeleza. “Nitampigia baba nizungumze naye. Unataka kuja lini?” “Ijumaa.” “Usijali.” Kwa ahadi hiyo, Sabrina akaanza kujiandaa kwa safari ya jijini. Alijua baba yake huwa hawezi kumkatalia chochote Sabina.

          Na kweli, usiku wakati ameshamaliza shuguli zake zote, Sabrina akasikia anaitwa akiwa chumbani kwake. “Jiandae kesho kutwa utaenda kwa dada yako. Naona anashida.” “Na huwezi jua ukifika huko unaweza kupata hata kijikazi na wewe maisha yaanze.” Mama yake akaongeza. Sabrina akashangaa moyoni. Yaani mpaka hapo maisha hayajaanza! Lakini kwa kuwa walishamwita ‘fungu la kukosa’. Akaona anyamaze, bora aondoke hapo.

 Usilolijua....

S

iku hiyo ya ijumaa, Sabrina alifanya shuguli zake zote ndipo akaruhusiwa kuondoka mida hiyo ya saa nane. Kutoka Chalinze nyumbani kwao mpaka Dar haikuchukua muda mrefu sana. Alimkuta Sabrina akimsubiria kituoni. Akaanza kucheka. “Ulivyochoka!” “Nimepewa kazi zote ndipo nikaruhusiwa. Tena ni kama mama alitaka kubadili mawazo, baba akakazania ili nije kukusaidia.” Sabina akazidi kucheka huku akiondoa gari hapo kituoni. “Sasa mimi hata sijapika. Na nyumba yenyewe chafu, sina muda.” “Wewe twende. Ni heri kukusafishia nyumba yako, halafu napumzika, kuliko kule kwa wazazi wako. Wanatuma kuanzia asubuhi mpaka usiku! Na kugomba juu huku wakinitusi sina akili! Wewe twende tu.” Sabina akazidi kucheka kama mazuri vile. “Twende tukanunue chakula, ndio twende kwangu.” “Popote wewe twende tu.” Ndugu hao stori za nyumbani zikaendelea na vicheko.

          Kesho yake dada yake hakuwa akienda kazini. Wakasaidiana usafi hapo ndani mpaka nyumba ikabadilika. “Afadhali ulikuja.” Akashukuru dada yake wakiwa wapo sebuleni. Kila mtu kwenye kochi lake wanapumzika. Simu ya Sabina ikaingia. “Nipo getini kwako.” “Unawazimu wewe Lela! Kwa nini hujanipigia?” “Naomba ufungue geti bwana Sabina! Ni nini bwana? Tangia lini mimi na wewe tunaombana ruhusa ya kutembeleana!” Akamtuma Sabrina kwenda kumfungulia geti.

          “Nimekuja kupumzika.” Sabrina akashangaa wanacheka. “Leo naona tutaanza mapema!” ‘Wala hujakosea. Tena nimemwambia leo jioni tunakwenda kwenu kuna shuguli. Nakusindikiza, nitarudi jumapili usiku.” Sabina akazidi kucheka. “Unamuacha na nani?” “Si yule kijana anakuja na kuondoka! Yeye hawezi kubana haja zake. Basi usiku akijisaidia anasubiri asubuhi yule kijana akija anamsafisha!” “Lela wewe! Unamuacha usiku kucha?” “He! Kwani imekuwa adhabu! Yaani anataka maisha yetu wote yakwame!” Akalalamika Lela mrembo haswa, shoga ya dada yake, Sabrina haelewi ni nani anayezungumziwa.

          “Mimi nina wazo.” Akawahi Sabina. “Kama wazo lakunisaidia mimi, sawa. Lakini si kunididimiza.” “Wazo zuri tu.” “Wazo gani?” Akauliza Lela. “Nisikilize. Ili usiingie dhambi, na usije laumiwa. Wewe sasa hivi unayo pesa. Mtafutie mtu wakumsaidia ili wewe uwe huru kuendelea na maisha yako, na yeye ajifie salama, usilaumiwe.” “Yaani pesa hiyohiyo ndogo nayo nigawane na mtu! Hilo wazo lako silo Sabina. Wala silitaki.” “Lakini alikuwa mumeo!” “Kwani mimi nimekataa? Sijakataa. Lakini siwezi kukwama maisha kwa ajili yake Sabina! Hilo nimekataa. Nikiamka mapema, nambadilisha asubuhi kabla ya kwenda kazini na kumlisha. Nikichelewa namwachia kijana akija ambadilishe. Halafu yeye kama binadamu wengine jamani, kwani mtu anajisaidia mara ngapi!? Tuwe wawazi na wakweli jamani! Na mimi nafanya kwa nafasi yangu. Hata ndugu zake wenyewe wamechoka, walianza kwa kupeana zamu, naona wameacha baada yakujua hatapona tena. Wameniach..” “Wewe Lela, mimi nimekupa tu wazo, sio nakulaumu.” Sabina akamkatisha.

          “Hapana, naona ni kama naonekana sifanyi wakati na mimi kama binadamu nahitaji kupumzika na maisha yaendelee. Tena ukute yeye angeoa kabisa kama mimi ningekuwa kitandani kama hivyo yeye. Lakini...” “Wewe Lela, usituharibie siku bwana. Mbona unapaniki vitu vidogo vidogo! Wewe niambie leo tunakwenda kupumzika wapi, basi. Acha kujiliza kwangu.” Kidogo Lela akatulia, vicheko vikaanza.

          Siku ya jumatatu ilikuwa sikukuu, hakuna kazi Sabina na Lela wakapanga watoke jijini, wakapumzike Kigamboni na wanaume zao. Walikuwa na kundi kubwa tu, vijana wenye pesa yakuwatosha, wapenda starehe. “We Lela! Siku mbili? Heri umuombe Sabrina akakuangalizie, Lela shoga yangu. Akifa huku nyuma wewe haupo? Utawaambiaje walimwengu.” Hapo Lela akakubali. “Nitakulipa Sabrina mdogo wangu. Naomba kanikalie na nyumba yangu. Huna haja yakufanya chochote. Wewe nitakuachia namba yangu. Lolote litakalotokea nijulishe. Yupo kijana wakusafisha kila kitu. Mpaka mzoga wangu.” “Wewe Lela, mwachie maagizo mazuri bwana.” “Si nishamwambia!?” Lela akashangaa kisichoeleweka mpaka hapo ni nini!

          “Mimi nakuacha Lela, lakini usije kunililia siku moja.” “Mimi sijaona wakuniliza hapa duniani. Maneno nishazoea. Anaeona simjali Tino, amchukue yeye. Nawapa bure!” Sabina akacheka kidogo na kunyamaza. “Sasa Sabrina mdogo wangu? Wewe kazi yako kutuma tu. Mpe kazi yule kijana, atafanya. Usipompa, ujue atalala nyuma, barazani. Nitakupa na pesa ya matumizi mpaka nirudi.” Sabrina akabaki anamshangaa, hajui hata ni kazi gani, nani na nini wanazungumzia mpaka hapo.

          Ila akawa kama ameshajua kuna Tino, ndiye mume wa Lela na ni kama ni mgonjwa. Swali likawa ni kwa nini yeye ndio akamwangalie wakati mkewe anakwenda kupumzika na mwanaume mwingine! Hilo ndilo likaleta sintofahamu kwa Sabrina. Akabaki hajui azungumze nini. “Usikatae mdogo wangu. Tena kwangu kuzuri kuliko hapa.” Sabina akacheka sana. “Unavyojiuza!” “Niombee na wewe!” “Sabrina hana shida. Wewe mpe pesa kidogo, ajikimu.” “Siku ngapi?” Ikabidi Sabrina aulize. “Jumatatu usiku nitakuwepo kwangu.” Wakacheka machoga hao wawili, Sabrina asielewe kinachowachekesha ni nini na kuna swala la mgonjwa!

Kuliko Ungua Mpini, Kukabaki Shoka!

W

alitoka Madale alipojenga Sabina mpaka Kunduchi nyumbani kwa Lela. Kweli palikuwa pazuri. Nje pasafi. Vitofali kutokea getini mpaka mlangoni. Hapo Lela alikuwa amevaa kigauni tu kifupi na sendozi ila alipendeza akavutia. “Hapa nilikuwa nimetoka kutengeneza kucha za mikono na miguu ili nitoke. Nashukuru kunikubalia mdogo wangu na mimi nipumzike.” Wakashuka garini na kumkaribisha ndani. Napo wakapokelewa na vigae safi vya sakafuni mpaka ndani. Kweli palikuwa pazuri sana. Akamtembeza humo ndani.

          “Wewe utalala chumba hiki hapa. Halafu hicho hapo mwisho ndicho yupo huyo aliyekuwa mume wangu. Yupo tu hapo, hana analofanya. Kila kitu ni hapohapo. Alipatwa na shindikizo la damu baada ya mikasa yake mingi, tena yakujitakia! Maana nilimuonya, hakunisikiliza. Anakijitabia fulani chakijinga hivi. Tokea zamani. Anaamini amini sana watu. Sasa wanaume wanzake walimtenda. Akasingiziwa yeye wizi. Wakamfunga kama mwaka hivi, akaja kutoka. Tena hapo nilipoteza pesa yangu kweli! Akatoka na mapressure ndio akaishia kupata shindikizo la damu. Hana awezalo. Ni kama mzogo tu.” “Sasa si anakusikia!” Sabrina akanong’ona.

          “He! Kwani naongopa?” Lela akaongea kwa sauti ya kishari kama aliyekusudia asikie. “Kwanza sidhani hata kama anaelewa. Ninachoona anafanya nikutoa mimacho tu na mate. Sitaki hata kukwambia mengineyo. Njoo kwanza umuone.” Kile chumba kilipofunguliwa tu, Lela mwenyewe akatoka ameziba pua. “Basi ndio kazi yake hiyo. Kujinyea na kujikojolea kila wakati! Nahisi hata kijana amemchoka.” Akaufunga ule mlango kwa nguvu mpaka Sabrina akashituka. “Wewe huko achana nako. Njoo nikuonyeshe tv.” Akaongea mengi akamuacha amekaa sebuleni yeye akasema anakwenda kujitayarisha aondoke.

          Baada ya lisaa, alitoka Lela watofauti. Alikuwa amependeza haswa. “Umependeza dada!” “Asante mdogo wangu. Hela nishakupa na simu ya hapa inayo pesa. Mtu akipiga au akija japo sidhani, mwambie ndio nimetoka nimekwenda Chalize msibani.” “Sawa.” Baada ya nusu saa, Sabrina akajikuta amebaki pale peke yake, Lela alishaondoka haraka hata hakumuona akimuaga huyo mume mtu mgonjwa.

           Akaendelea kuangalia tv, lakini mawazo yakawa kwenye kile chumba kilichokuwa kikinuka. Akasubiri labda huyo kijana atafika hapo, kimya. Moyo ukazidi kumuuma na kujisuta. Anawezaje kukaa hapo akiangalia tv na kuna kiumbe kinanuka ndani! Kila alipojaribu kupuuza na kuacha kama alivyoshauriwa na mama mwenye nyuma wa hapo, Lela, akashindwa. Baada ya lisaa bila huyo kijana aliyesikia huwa huwa anakuja, kutotokea, Sabrina akaamua kwenda. Akagonga na kufungua. “Naomba kuwasha taa.” Kimya. Kulikuwa giza haswa. Akawasha. Akaingiwa na hofu baada ya kukiona hicho kiumbe hapo kitandani. Alijawa nywele mwili mzima mpaka usoni ndevu ndefu kuzunguka uso zikamfunika nakushindwa kuelewa anaonaje! Na kweli kulinuka.

          “Naitwa Sabrina. Najua unaye mtu wako wakukusafisha, lakini kwa kuwa hayupo naomba nitoe hizo nguo.” Kimya. Sabrina akakumbuka aliambiwa ni kama mzoga. “Sijui ananielewa!?” Akajiuliza Sabrina. Akafikiria kwa haraka, akamsogea akiwa anaogopa. Akamuona yupo macho. “Naitwa Sabrina. Kama unanisikia na kunielewa, naomba ufunge macho mara moja.” Akamsogelea mpaka machoni. Akafunga macho. “Kumbe unasikia na kunielewa!?” Akafunga macho mara moja. “Afadhali. Basi naomba nikubadili. Usikae na uchafu muda mrefu. Kama umekubali, naomba funga macho mara moja. Kama haupo tayari, funga mara mbili.” Sabrina akaendelea. Akamuona amefunga mara moja na machozi. “Basi, usilie. Nitakubadilisha. Akija huyo kijana wenu, nitamwambia nilipofikia.” Akamuona anafunga macho.

          Sabrina akaanza kutafuta wipes. Akakuta mfuko mtupu. “Mmmh! Zimeisha. Sasa sijui kama kuna nguo safi!” Sabrina akaendelea kujiongelesha huku akizunguka hapo chumbani. Akafungua kabati la ukutani. Akakuta nguo za kiume zimepangwa vizuri sana. Safi. Na mataulo makubwa kwa madogo. “Mimi naamini hivi vitu ni vyako. Natumia. Dada akija, nitamwambia kama nilitumia.” Akaendelea kujiongelesha yeye mwenyewe Sabrina. “Kwanza nabadili mashuka yote. Hiki chumba kinanuka sana.” Akatoa mashuka masafi, mataulo makubwa na madogo. Suruali nyepesi na tisheti nyeupe. Akaweka pembeni na kuelekea bafuni. Napo palikuwa pasafu na pakavu kama ambako hapajatumiwa kwa muda mrefu.

          Akakuta vitu vingi asijue ipi dawa, ipi sabuni ipi lotion. Akajiambia atachukua tu beseni na maji akamfute. Akatengeneza maji ya povu la sabuni. “Inanukia vizuri!” Akaipenda. Akatoka hapo na maji ya vuguvugu. “Nyumba yenu nzuri sana na safi!” Sabrina akamsifia. “Niliambiwa unaitwa Tino. Ni kweli?” Akafunga macho mara moja. “Sawa Tino, naomba nikuoshe. Natoa shuka.” Akakubali kwa kufunga macho.

          Ile Sabrina anatoa lile shuka, akarudi nyuma. Ilikuwa kama kitu kimekufa hapo. “Mungu wangu! Umeoga mara ya mwisho lini!?” Akauliza Sabrina, kimya. “Mimi nakuogesha. Kama dada atachukia, basi. Unanuka vibaya sana. Lakini ngoja nitoe kinyesi na mkojo.” Machozi yalimtoka Sabrina vile alivyovikuta hapo. Kinyesi kibichi na kikavu kimeganda. Tino alikuwa na manywele na vinyweleo vingiii vilivyosababisha kushikilia kinyesi. Sabrina alimsafisha mpaka mgongo ukauma. Alijawa na madonda sehemu za siri na nyuma kwenye makalio. Alimuona yupo kwenye maumivu. “Pole, lakini nakuomba uvumilie Tino. Unakinyesi kilichoganda, lazima kukusafisha.” Baada ya lisaa ndipo akafanikiwa kumsafisha na kubadili yale matandiko akimgeuza kulia na kushoto mpaka akafanikiwa kubadili matandiko na Tino akiwa hapohapo kitandani ila kutumia akili akimsogeza huku akitandika upande upande. 

          “Najua una maamivu lakini angalau unatizamika Tino. Nitakupa dawa ya maumivu. Umekula?” Akamuona anatoa machozi na kufunga macho mara mbili kukataa. “Okay. Utapenda uji?” Akafunga macho mara moja. “Basi nitaenda kukupikia nitakuletea. Lakini naomba nisikuzimie taa. Usikae gizani. Ni sawa?” Akakubali. Akamfuta machozi na mate. “Sasa ili tisheti isiloe na mate, naweka hiki kitaulo.” Akamuegeshea mito miwili nyuma yake, akamuweka na kitaulo kuzunguka shingo. Kwenye sehemu za siri akampaka mafuta mengi sana. Alipata na diaper akamvalisha. Akapulizia chumba air freshner aliyoikuta hapo. Chumba kikanukia. “Naomba niwashe hii tv ili usikae peke yako halafu kimya muda mrefu. Ni sawa?” Akakubali. “Natamani ningejua huwa unapenda kuangalia nini nikuwekee. Ila kwa sasa nakuwekea chochote. Utanisamehe.” Akaweka na kutoka hapo na nguo chafu.

          Alichofanya ni kwenda kuzifungia kwenye chumba alichoambiwa ni chakufulia. Nyumba hiyo ilikuwa safi kwa hakika na ilipangiliwa. Akaelekea jikoni. Uzuri Lela alimuonyesha kila kitu na vyakula maana alimwambia hatarudi hapo mpaka siku ya jumatatu usiku. Akamwambia kitakachopungua akanunue. Basi, Sabrina akawasha jiko la gesi, akapika uji mzuri sana akaweka na maziwa na sukari ya kiasi tu. Akaupoozesha na kuuweka kwenye bakuli kubwa. Akarudi chumbani.

          Alimkuta amesinzia. “Tino!” Akamuita taratibu kama asimshitue. “Kula, unywe dawa za maumivu ndio ulale.” Akabaki akimwangalia na ndevu nyingi usoni. Nyusi nazo nyingii. Akajua kwa asili ni mtu mwenye nywele nyingi. “Nimeona mikono yako dhaifu Tino. Nitakulisha. Ni sawa?” Akafunga macho mara moja. Akamfuta mate yaliyokuwa yamedondokea kwenye ndevu. Akamuweka vizuri, akampa kijiko cha kwanza. “Upo sawa?” Akafunga mara moja. “Moto sana?” Akafunga mara mbili kuashiria ‘hapana’. Sabrina akacheka. “Tutaelewana hivyo hivyo. Nashukuru unanijibu.” Akamlisha tena. Akamuona anakula tu bila shida.

          “Nikwambie kitu Tino?” Akamuona anamwangalia. “Unanywele nyingi sana zinazofanya inakuwa ngumu kusafishwa. Ungependa zipunguzwe? Namaanisha kote.” Akafunga macho mara moja. “Basi akija kijana wako leo, nitamwambia. Nikiona hajaja mpaka kesho, mimi nitakukata na kukunyoa vinyweleo kote ili kuvipa nafasi vidonda vipone. Ngozi yako imekuwa dhaifu mno.” Sabrina, msichana aliyezoea kusafisha ng’ombe, akijua kumtunza ng’ombe kwa kumwangalia mpaka kwatu kama inatatizo na kujua nini kipakwe, hapo napo akawa amefikishwa. Alishahudumia ng’ombe wa kwao wakiwa wagonjwa na madonda, mpaka wakapona. Hata hayo madonda hapo hayakumtisha.

          “Na wala usiogope. Hayo madonda yatapona tu kwa haraka. Nitamfundisha ujanja huyo kijana wako jinsi ya kuyahudumia ili yapone kwa haraka. Halafu kingine Tino, tukiwa wote tumia chupa. Niliiona pale chooni. Nitakuwa nakuuliza kila baada ya lisaa au masaa mawili ili ukojolee kwenye chupa, usiwe unatumia diaper ukakutanisha hayo madonda na mkojo. Ila kinyesi ndio sijui.” Sabrina akaanza kuwaza huku akiongea mwenyewe, Tino anamtizama na kumeza.

          “Nitajua tu chakufanya. Usijali.” Akaongea Sabrina huku akimalizia kumpa lile bakuli la uji. “Huwa unakula vyakula vigumu?” Akakubali. “Lakini sitakupikia kitu kigumu sana. Nakupa dawa, nitakuacha upumzike, halafu baadaye nitakuja kukuchungulia. Unataka nikujaribishe labda utajisaidia?” Tino akakubali. Akampa dawa za maumivu. Alikuta madawa mengi hapo. Hakujua anatakiwa anywe saa ngapi na ni za nini! Akaona ajiachie. Ila alipopata za maumivu, akaona ampe. Akanywa ndipo akaenda kumchukulia chupa maalumu ya kukojolea wanaume. Akamtoa nguo, akamuweka. Akasubiri kidogo, akamuona anatoa mkojo. Sabrina akafurahi sana. “Umeona mambo hayo. Na baadaye tena tutajaribu. Ila haja kubwa ndio sijajua chakufanya. Wewe ukijisikia, jisaidie tu, nitakubadilisha diaper mpaka nitakapojua chakufanya.” Akamsafisha tena kidogo. Akamfunika. “Unataka tena maji ya kunywa?” Akakubali, akampa tena. Ndipo akamuacha akiwa ameridhika.

          Sabrina alitengeneza supu nzuri, akatupia tambi humo ndani. Ikawa nzuri na tamu. Akasubiri kama masaa mawili mengine akaenda kumchungulia. Alipoingia akamuona anamwangalia. “Umeshindwa kulala kabisa?” Kimya. “Unamaumivu makali?” Akakubali. “Pole Tino. Lakini tokea nilipokupa zile dawa sasa hivi ilitakiwa maumivu yawe yamepungua! Halafu ni kama ulikuwa na joto wakati nakusafisha. Nafikiri unahoma. Itakuwa ni hivyo vidonda. Na hapa kuna dawa nyingi, sijui ipi ni ipi! Acha nimpigie simu mke wako anipe maelekezo.” Sabrina akatoka kwa haraka akarudi na simu mkononi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

           Akasimama karibu na zile dawa, akampigia simu Lela kwa kutumia simu ya hapo ndani. “Namuona anahoma na anamadonda mabichi. Zipo dawa nyingi, sijui nimpe ipi?” “Huyo anazo dawa kibao. Mpaka madawa ya kukausha hayo madonda. Isingekuwa kunya hovyo na kujikojolea, sasa hivi angekuwa amepona. Naona huyo kijana pia amecho.” Sabrina akatoa kwenye spika. Alijua Tino anasikia. “Maana imekua ni kazi ya kumfuta yeye tu mav..” “Da Lela! Da Lela!” Sabrina akamkatisha. “Naomba nitajie hayo majina ya dawa, mimi nitampa. Hata kama zipo za kumsafishia.” “Yaani hapo kuna kila aina ya madawa, ushindwe tu mwenyewe. Maana...” “Na kweli nimeona. Kuna kila kitu.” Lela akamtajia kila kitu baada yakumpigia kwa video. Sabrina akawa anaandika kila anachoelekezwa. Akaingia na bafuni. Akawa anamtajia kipi chakutumia na kwa wakati gani.

          Sabrina akashangaa jinsi alivyo na vitu vingi vyakutumia lakini havitumiki! “Sasa wewe naona nikirudi tutaongea zaidi. Unaonekana una moyo wa kusaidia. Tutampanga Sabina vizuri, ukae hapo mpaka apone hayo madonda. Asije akafa nayo, wakati wakuosha maiti yake wakayakuta na kuanza kulaumu bure!” Sabrina akaumia sana. Tino ni kweli anatisha kwa muonekano, lakini hakutakiwa maneno makali hivyo! Alikumbuka jinsi baba yake anavyohangaika kwa ng’ombe tu! Mchana na usiku, akitumia pesa kwa kuita madaktari wa ng’ombe mpaka apone! Leo wanamfanyia hivyo mwanadamu! Sabrina akaumia sana. Alimuhurumia Tino, lakini akakumbuka jinsi mwanaume anavyo weza geuka kuwa mnyama hatari kuliko simba. Walishamtenda yeye, akajiambia labda na yeye Tino alimtenda Lela, ndio analipwa. Akakusudia kufanya yake, aondoke. Akapata kila kitu kutoka kwa Lela, huku akimshangaa ni kwa vipi huyo Tino ameweza kukaa kwenye hicho chumba muda wote huo! Mwishoe Sabrina akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Unaonekana ulikuwa na infection kali, Tino. Naomba tuanze dawa. Naamini utapona. Tujitahidi usafi. Kinyesi kisiingie kwenye njia ya mkojo tena, na kwenye vidonda. Utapona tu. Sawa?” Akamuona amenyamaza. “Naomba usikate tamaa. Niangalie Tino.” Sabrina akaenda. “Uponyaji mkubwa na wa kwanza, unatoka kwako wewe mwenyewe. Inawezekana umeugua sana, umeshindwa kupata msaada ambao unajua unastahili, lakini Tino, anza kuamini utapona na kutoka hapo. Wewe mwenyewe amua kutoka hapo. Kwa sababu kama ni kifo, Mungu angeshakuchukua. Kuwepo hapo mpaka leo ni kwamba siku yako bado. Sasa jinsi ya kubaki hapa duniani ni wewe mwenyewe utakavyoamua. Utajikuta unalala hapo kitandani siku zikizidi kwenda, ukiwa gizani na kujionea huruma au kuwa na hasira wakati watu wengine wakikufanya kile watakacho!”

          Akapiga magoti  kabisa mbele yake ili amuangalie vizuri usoni, kisha akamshika mkono. Akashangaa jinsi kucha zilivyo ndefu. Akatulia kidogo na kumwangalia tena. “Sijui umekuwa hapo kitandani kwa muda gani Tino. Lakini nataka tu kukwambia upo hapo kwa sababu, na narudia tena Mungu hayupo tayari kukuchukua maana wapo wengi tu, dakika iliyopita, wewe ukiwa hapo, wamekufa kwa sababu tofauti tofauti tena wakiwa chini ya uangalizi mzuri sana tena wa thamani na wapendwa wao wakimlilia Mungu wawaponye, lakini wamekufa na hata sasa hivi hapa tunapo zungumza, wapo wanao kata roho. Lakini jiangalie wewe. Unafikiri Mungu amekusahau au kifo kinakuogopa?” Tino kimya akimtizama tu na mate yakimtoka.

          “Ni kwa kuwa Mungu hayupo tayari na wewe. Sasa kwa kuwa bado upo hapa duniani, nakuomba na kukushauri, chagua kupambana. Mimi leo nipo na wewe hapa. Usifikirie kesho nikiwa sipo. Pokea nitakachokupa sasa hivi. Kitumie vizuri. Akija mwengine kesho, hata akiwa mbaya kwako, kile kidogo atakachokupa, pokea. Halafu jitahidi unapokuwa mwenyewe, zungumza kidogo. Najua upo dhaifu, lakini pambana Tino. Umenielewa?” Sabrina akamuuliza. Akafunga macho mara moja huku akilia.

          “Naomba niminye huu mkono mara moja kama unavyofanya macho.”  Akamuona anaangalia mkono wake huku akijitahidi. Akamsikia akigugumia kwa mbali kama anayejitahidi. Akashindwa. “Nimekusikia kwa mbali. Tujipe siku ya leo, kesho, halafu jumatatu tutajaribu tena. Ule vizuri, utumie dawa kwa siku hizi tatu mfululizo, halafu tutaona.” Akamuanzishia dawa alizokuwa amepewa hospitalini muda mrefu, akamuangalia kama hajajisaidia, akamfunika mpaka miguuni. Akahakikisha hana baridi. Akamuacha alale kidogo.

          “Chumba chako kizuri na kikubwa Tino, naweza kukaa hapa, au unataka nikakae sebuleni?” Sabrina akauliza, akakumbuka hawezi kuzungumza. Ikabidi arekebishe swali ili kupata jibu la ndio au hapana kwa rahisi. “Nikae?” Akakubali. “Basi nitakaa hapo kwenye kochi. Kuniita uniite kwa kufunga macho mara tatu. Sawa?” Akakubali. “Baada ya lisaa, nakupa chakula tena.” Akakubali. Sabrina akakaa hapohapo chumbani. Akatafuta kitu anachopenda yeye kuangalia, akawa anaangalia tv hapo kwenye kochi. Chumba kilikuwa kikubwa na kizuri sana. Makochi mazuri na tv kubwa sana kama sebuleni kwa mtu! “Nyumbani kwenu ni pazuri Tino! Kila kitu chenu kizuri! Halafu kumepangiliwa mpaka chooni!” Hizo sifa zilikuwa zikimtoka Sabrina bila kuchoka. Tino akabaki akimwangalia tu. Sabrina akacheka kidogo. “Sikuongeleshi tena. Lala.” Akanyamaza. Akamuona amefunga macho.

          Kila wakati Sabrina alisimama kwenda kumwangalia. Baada ya lisaa, akaenda kumshika, akagundua anatokwa jasho, akajua homa inashuka. Lela alimwelekeza dawa kali yakumshusha homa. Akampunguzia shuka, akamfuta kidogo, lakini hata hakufungua macho. Akaamua kumpa lisaa jingine. Akajiambia pengine amekuwa na hayo maumivu kwa muda mrefu sana, ndio anapumzika. Akamuacha.

          Baada ya masaa matatu, akajiambia labda dawa zinamlevya. Hakuonekana ni kama mtu aliyekuwa akilishwa vizuri. Akaenda kumtengenezea chakula. Akaleta kwenye bakuli tena. Akamkuta amefungua macho. Akafunga na kufungua mara tatu. Akajua anamwita. Akacheka. “Unaona tunaelewana? Haya, niambie unataka nini? Unataka kujisaidia?” Akafunga macho mara moja. Sabrina akafurahi hilo. “Haja kubwa?” Akakubali. “Sasa bado sijapata jinsi yakukusaidia kwa haja kubwa. Nakugeuza upande. Ujisaidie kwenye kwenye kwenye....” Akabaki akifikiria. Akakimbilia chooni.

          Akatafuta kama mfuko. Akapata na gazeti. Akatoka na ile chupa ya kukojolea kwa haraka. Akamwekea kila kitu. “Jisaidie, kila kitu kipo sawa.” Alimuweka ubavu. Baada ya muda akajisaidia haja zote. Sabrina akafurahi sana. Akagundua anavyo vitu vya kumsafishia pia. Gloves na cream ya kupakwa kwenye makalio na inasaidia pia kupunguza maumivu. Akamfuta vizuri na kumpaka. “Safi sana Tino. Si unaona mambo hayo?” Akamuona anamtizama kwa kutulia. Akamvalisha tena na kumrudisha kuwa kama amekaa. Akaanza kumlisha. Alikula vizuri hiyo supu aliyokuwa amemtayarishia, mpaka akamridhisha Sabrina mpikji. “Umependa?” Akakubali. Sabrina akacheka. Akamaliza yote. Akamfuta vizuri. “Kaa kidogo ili usitapike.” Akakubali. Akawa kama anaangalia tv. Lakini Sabrina akagundua anamwangalia sana.

            Akampa na maji ya kunywa. Akaonekana ameridhika. Sabrina akarudi kukaa palepale kwenye kochi. Kimya. Wote wanaangalia tv. Akamuona anaanza kusinzia. Akamrudisha kulala. Alilala mpaka usiku wa saa mbili. Akampa tena uji, akarudi kulala tena. Baada ya kumsaidia haja ndogo akamsafisha vizuri. Kila wakati alihakikisha hawi na mnyevu mwilini. Japokuwa hawakuwa akiongea lakini kila wakati alimpa neno la faraja. “Utapona tu Tino. Jipe muda.” Na hapo tena wakati akimfunika, akatupia faraja. Akabaki akimwangalia. Baada ya muda mfupi sana akamuona anarudi kulala.

          Sabrina hakujua kama ni hofu au mshituko au ni kuingiwa na huruma, lakini alishindwa kulala kabisa. Akaanza kujifunza kutumia mashine za kufulia. Hakuwahi kuona mashine za kufulia kabla. Siku hiyo ikabidi ajifunze. Nguo alizomkuta nazo Tino na mashuka aliyoyatoa kitandani mwake, vilikuwa vikinuka sana na huyo kijana aliyeambiwa na Lela huwa anakuja kumsadia Tino na kufua, hakutokea mpaka usiku huo. Ikabidi tu kufua yeye mwenyewe.

          Aliyafanya yote lakini bado hakuwa na usingizi. Akaanza kutafuta jinsi ya kumsaidia mgonjwa kama Tino. Madonda yake, kwa nini anashindwa kuongea, jinsi yakumnyoa nywele, mara ngapi anatakiwa kula na kunywa akiwa vile mgonjwa na yupo kwenye matibabu, vitu gani ampikie na kumlisha ili apate nguvu kwa haraka. Mpaka panapambazuka, bado hakuwa amelala. 

Jumapili.

S

abrina akaanza kwa kupika uji ndipo akaenda kumwangalia chumbani kwake, akakuta bado amelala. Akamshika kichwa kuangalia kama anahoma. Akafungua macho. “Unamaumivu?” Tino akakubali. “Nimekupikia uji. Nataka kukuosha ndipo nikupe uji halafu unywe dawa. Utaweza kusubiri?” Akakataa. “Basi nakupa uji kidogo ndipo nikupe dawa halafu nikuoshe. Ni sawa?” Akakataa. “Huwezi kunywa dawa bila kula, Tino! Utaumwa zaidi. Haitakusaidia. Madawa yako ni makali sana. Nitakulisha haraka haraka. Naomba usikatae. Halafu nitakupa sababu nzuri.” Tino akakubali.

          Wakati anamlisha akaanza kumsimulia mambo aliyosoma mtandaoni juu yake na vitu vyakufanya ili aweze kupona. “Natukifuatisha hivyo, baada ya muda mfupi sana utajisikia vizuri.” Akamuona amenyamaza tu akimtizama. “Naomba uamini pamoja na mimi, Tino. Usikate tamaa. Na usifikiri nitakukimbia kwa haraka, mpaka nikuone unanafuu ndipo nitaondoka. Da Lela alisema atataka nikae hapa kwa muda, sasa sijui ni kwa muda gani, lakini kwa muda mfupi tutakao kuwa wote, naomba ushirikiano wako ili hata nikiondolewa hapa, uweze hata kujisaidia kwa vitu vidogo vidogo. Usirudi kuwa tegemezi tena. Sawa?” Akakubali kwa kufunga macho mara moja.

          Alikunywa huo uji vizuri bila shida. “Hapo umenitia moyo.” Akamfuta mdomo. Akampa dawa. “Lala kidogo, na mimi nilale kidogo, ukiamka tutafanya usafi wako.” Wakakubaliana. Sabrina hakuweza hata kufika chumbani kwake. Akaishia kulala hapohapo kwenye kochi chumbani kwa Tino. Alilala kama mfu.

          “Tino!” Baada ya masaa manne mbeleni akatoka usingizini akiita jina lake kwa mshituko. Akamkuta Tino akimwangalia. “Samahani nimekushitua. Sijui nilikuwa nikiota! Nimepitiwa na usingizi. Unajisikiaje?” Akaenda kumshika. Akakuta hana homa. Akafurahia hilo kwamba matibabu anayompa yanamsaidia. Akaanza kumuhudumia. Usafi. Kuanzia utosi mpaka unyayo. Tino alikuwa akitoa ngozi zilizokuwa zikidondoka mwili mzima. Kichwa ndio zaidi. Haukuwa mba tu, ila magamba na mba. Kila alipoosha, aliona bado kichwa kina magamba. Akaamua kumlaza mapajani na kuanza kumkwangua taratibu ili kuyatoa yote. Akamuona anasisinzia. “Unasikia raha?” Akakubali. Sabrina akamcheka. “Unapenda raha wewe!” Akaendelea kumkwangua ngozi ya kichwa kutoa  huo uchafu. Ukweli alionekana ni kama walisahau kumuosha hicho kichwa kwa muda mrefu. Alikuwa amepauka vibaya sana na hata kichwa kilikuwa kikinuka. Alimuosha tena na tena mpaka Sabrina mwenyewe akaridhika. Ndipo akampaka mafuta sasa.

          “Unangozi nzuri Tino! Kesho nitakunyoa ndevu na nywele nitapunguza. Utakuwa msafi na miwasho itapungua.” Akamkata na kucha za mikono na kuzitengeneza kwa muonekano mzuri. “Ona zilivyopendeza! Na una vidole vizuri.” Sabrina akaendelea kumsifia wakati anamkata vinyweleo vya vidole vya mkono. Akamminyaminya mkono mzima vizuri kuanzia mabegani alipomnyoa vinyweleo vyote mpaka vidoleni. Akamuona anasinzia, akaona asiongee ili alale.

          Siku hiyo nayo aliendelea kutumia dawa, huku akimlisha milo yote vizuri na kumfanyiwa usafi wa kina. Taratibu. Kila alipokuwa akimuona anasinzia akiwa anamtoa magamba ya kichwani au kumminya miguu, alikuwa akimuacha kumuongelesha ili alale. Akagundua anafurahia akimshika. Anatulia sana na kulala. Kwenye mida ya saa nane mchana akiwa anamchua mikono kama kumsaidia kuipa nguvu Tino akiwa amaeshapitiwa na usingizi, Sabrina amekaa chini sakafuni pembeni ya kitanda na yeye akapitiwa na usingizi akiwa amemshika Tino mkono. Alilala mpaka ute ukamtoka.

Akasikia kwa mbali kama anaminywa mkono taratibu. Akashituka. “Tino!” Akajifuta ute. “Pole, nimepitiwa na usingizi. Sikujua kama mkono huu wa kushoto unanguvu kidogo! Au ni glukozi niliyokuwa nikikulambisha imekusaidia?” Akakubali. Sabrina akacheka kufurahia. “Tujaribu na upande wa kulia.” Kulia hakuwa na nguvu. akagundua aliathirika zaidi upande wa kulia kuliko kushoto, njaa ndiyo ilimfanya ajisikie dhaifu. Akagundua alimuamsha ajisaidie. Sabrina akampa vifaa, na kweli akajisaidia, hakutaka kukojolea diaper. 

Jumapili hiyo ikawa yake na Tino tu. Sabrina akashangaa sana. Inamaana huyo Tino ndio angefungiwa hapo mpaka siku hiyo akiwa na kile kinyesi au ni kwa sababu yupo hapo labda Lela alimwambia kijana asifike! Sabrina akawaza huku akiendelea kumuhudumia Tino. “Tino!” Akamwita wakati anampa dawa. Akamwangalia. “Najua sasa hivi unajisikia dhaifu sababu ya madawa ninayokupa. Ukirudisha nguvu, utajitahidi kuongea?” Akamuona amenyamaza. “Hata kama ni vibaya kabisa. Maneno hayaeleweki. Mate yanamwagika. Upo na mimi, huna chakuonea aibu. Toa tu sauti. Nitajifunza kukuelewa. Ukiona shida mbele ya watu, basi usizungumze. Ila tukiwa wawili, jaribu.” Akamuona analia.

Akaenda kumfuta machozi na mate. “Jaribu tu Tino. Nakuahidi sitakuomba kitu ambacho najua huwezi. Na hakuna jinsi ya kurudisha uwezo wa kuzungumza, kama hutaanza kuzungumza. Au mdomo haufunguki kabisa?” Akakataa. “Unaona sasa, kama mdomo unafunguka, basi ni wakati wakutoa sauti. Sio lazima sasa, ukipona kabisa. Ongeza sauti, au matumizi ya kichwa kukubali na kukataa. Utaona tofauti. Sawa?”  Akakubali. “Basi na leo nitalala hapahapa ili kuhakikisha ukitaka kujisaidia, nakuwepo. Ni sawa?”  Akakubali. “Bado koo lipo kavu?”  Akakubali. “Basi nakupa tena maji usiwe na wasiwasi na kukojoa. Kwa kuwa hata mimi nataka ukojoe ili kusafisha ndani. Mkojo wako ni mchafu Tino, na unanuka sana. Maji pekee ndiyo yatasaidia. Kwa hiyo ni heri unywe mengi, nitakusaidia chupa ya kujisaidia.” Tino akakubali.

          Akamuhudumia vizuri kisha akakaa chini ya kitanda, kulikuwa na kapeti zuri sana limewekwa hapo chini ya kitanda. Akaweka movie nzuri wakawa wanaangalia. Akamuona anasinzia baada ya kumlisha viazi vyakuponda na nyama ya kusaga. Ni kweli kwa Lela kulikuwa na vyakula vyakutosha. Sabrina alikuwa na kazi yakuchagua tu, nakupika. Jumapili nayo ikaisha wakiwa wao wawili tu. Hapakuwa hata na hodi ya mpotea njia! Sabrina akashangaa sana na kushindwa kuelewa. 

Jumatatu!

U

siku waliamka kama mara mbili tu, Tino akijisaidia haja ndogo. Sabrina akimgeuza ili asiendelee kulala upande mmoja akaendelea kutonesha madonda. Alisoma lazima kumgeuza kila baada ya masaa mawili. Lakini usiku alikuwa akipitiwa na usingizi. Akiamka kumsaidia kukojoa, ndipo alipokuwa akimgeuza. Alipoamka alfajiri saa 11 kumsaidia haja ndogo, akaona akapike uji kabisa. Akampikia uji wa dona, akaweka maziwa akapigia yai. Wakati unapoa, akamsafisha mdomo. Akamuomba akae kabisa. Akamvuta mpaka akaweza kumkalisha kwa kumuegemeza ukutani na kumpangia mito. Kilichomfurahisha Sabrina, Tino alikuwa mlaji. Hakusumbua. Alimlisha, akala vizuri. Akampa dawa zote. Ya maumivu na antibiotic.

“Endelea kukaa kama nusu saa tena, ndipo urudi kulala tena. Ukiamka unaoga.” Akamuona anajitahidi kunyoosha mkono, Sabrina akajua anataka kumshika. Akasogea. “Unataka maji?” Akakataa. Akaendelea kunyoosha mkono. Sabrina akamshika. Akamuona ametulia. Sabrina akacheka. “Unataka kusema asante?” Akakubali. “Sasa si useme ‘asante tu’!”  Akabaki akimtizama. Sabrina akacheka. “Haya, karibu.”  Akamuachia. Sabrina akatoka akiwa ameshamwashia tv.

Akarudi jikoni kusafisha huku na yeye akinywa uleule uji. Alipohakikisha jiko safi, maana alishagundua Lela ni msafi sana. Hakutaka kuacha chochote kichafu. Kisha akaenda kuoga kwa haraka, akabadili nguo, akawa msafi. Akarudi chumbani kwa Tino. Akamuita karibu. “Unataka kujisaidia?” Akakubali. “Namba 1?” Akakubali. “Unataka tujaribu na namba 2?” Akakubali kwa haraka. Sabrina akacheka. Akamuweka vizuri hapo kitandani. Akamuwekea chupa ya haja ndogo na gazeti nyuma ili kinyesi kiangukie hapo. Akajisaidia, Sabrina akaona amuogeshe tu ili akilala alale moja kwa moja. Kwa haraka sana akamsafisha hapohapo kitandani. Hakuwa amemkata bado nywele. “Nahofia da Lela! Sijui huwa unakata staili gani! Maadamu nimekutoa manywele ya mwilini, akija nitamuuliza juu ya kichwani na ndevu.” Akamuona ametulia tu.

Akamuweka kichwa mapajani baada ya kumsafisha chini na kumpaka mafuta na dawa zakukausha madonda. Akaanza kukwangua tena mba. “Leo hamna ngozi chafu nyingi.” Sabrina akaendelea kuongea wakati akimkwangua kichwani taratibu, Tino anasinzia. “Ukiamka tunaosha kichwa na kuweka mafuta.” Akamchungulia machoni, akamtiza. Akacheka. “Ukishikwa tu kichwani unalala Tino! Kichwa kinakuwa kinawasha sana?” Akakubali. Sabrina akacheka nakuendelea kumkwangua taratibu.

Siku hiyo nayo wakashinda hapo peke yao. Kimya. Patulivu. Hapakuwa hata na simu kutoka kwa Sabina dada yake, wala Lela mke wa huyo mgonjwa. Akabaki akimlea Tino. Jioni akamuona Tino ameamka akiwa na nguvu. Hata macho yalionekana yana uhai. Meupe, maangavu. Akampa tena uji, na maji, wakabaki wamekaa tu hapo.

Sabrina akachukua mafuta ya maji aliyaona bafuni. Akapanda kitandani. “Nyayo zako kavu sana Tino. Nilipaka mafuta asubuhi, acha nikuongeze. Halafu nitakufanyia masaji ya miguu. Mwenzio mtaalamu.” Tino akamwangalia, akamuona kama anatabasamu. Akakaa kitandani, akamvua soksi alizokuwa akimvalisha kumpa joto. Akaanza. “Basi hii masaji alikuwa akiipenda sana boyfriend wangu. Hata kama alikuwa amekasirika, unamuona anatulia. Inafanya miguu inatulia, na akili.” Sabrina akamwangalia huku akiminya miguu yake, akamuona anatabasamu. “Usizoee lakini!” Akamtahadharisha huku akiendelea kuminya na kucheka. Tino alitulia kabisa.

“Unahisi chochote huku miguuni?” Akakubali. “Miguu yote!?” Akamuona anakubali na kukataa. Sabrina akafikiria kwa haraka. “Upande upi zaidi?” Akauonyeshea wa kushoto. “Oooh! Ndio unahisia zaidi?” Akakubali. “Nimeelewa. Basi nikujitahidi ili kote urudishe nguvu Tino. Si bado upo na ndoto nyingi unataka kuona unazitimiza kabla hujaondoka hapa duniani?” Akamuona amenyamaza. 

Sabrina na historia yake.

S

abrina akajua amekata tamaa. “Acha kukata tamaa bwana Tino. Acha mimi nikwambie na mimi ya kwangu yaliyokuwa yamenikuta nikiwa chuoni.” Akaanza Sabrina akiwa anamminya miguu. “Huyu boyfriend niliyekwambia nilikuwa naye, tulifika ngazi ya karibu kunichumbia. Lakini kabla sijaitwa mchumba, akaniachia jina la fungu la kukosa. Akiwa ameniabisha vibaya sana. Si nyumbani, si chuoni.” Akaendelea Sabrina. “Tulikuwa tukipendana sana. Lakini yeye alikuwa mkubwa kidogo kwangu. Nilikutana naye nilipomaliza tu kidato cha sita. Alikuwa akifanya kazi kwenye kampuni ya simu. Nilikuwa na hela Tino, sikuwa na shida ndogo ndogo. Akawa ananitunza na kunijali kweli.” Sabrina akaendelea. “Nilipofeli kidato cha sita. Matokeo yangu hayakuwa mazuri, nikaamua kutorudia mitihani, nikaamua kutumia cheti cha kidato cha nne, ili kuomba chuo Dodoma kusomea mambo ya stoo kwa ngazi ya Diploma. Nikazungumza naye, akaniambia hamna shida, atakuwa na mimi na akasema ataendelea kunisaidia maswala ya fedha, kwa kuwa ada alikuwa anilipie baba.” Tino alionekana anamsikiliza.

“Mipango ilipokamilika, nikaanza chuo. Kila weekend ilikuwa lazima Emma awepo Dodoma. Akiwa ameshindwa, basi mimi nakuja huku kwake Dar. Nakaa mpaka jumatatu ndipo narudi Dodoma. Chumba nilichokuwa nimechukua Dodoma palepale chuoni, kilikuwa gumzo jinsi kilivyokuwa kimejazwa thamani na Emma. Tukawa tunatumia na dada mmoja yeye alikuwa akisoma ngazi ya juu zaidi, Advance. Tukazoeana sana na yule msichana anaitwa Kasandra. Umri hatukutofautiana sana. Lakini mwenzangu alimaliza sekondari, akafaulu vizuri na kuunganisha chuo. Alikuwa mwaka wa pili wakati mimi nipo mwaka wa kwanza. Yeye bado mwaka amalize na mimi hivyo hivyo.” Sabrina akaguna.

“Kila mtu alikuwa akijua mtu wangu mimi sio kijana wa mchezo, kwamba pesa ilikuwepo. Walimjua Emma kwa jinsi alivyokuwa akinitunza. Kuanzia mimi mwenyewe mpaka chumba changu. Nilikuwa na redio hiyo, yule niliyekuwa nikiishi naye alikuwa akiiwasha, jengo zima mtasikia. Flatscreen ya nguvu! Tena smart tv. Nilikuwa na simu nzuri sana. Iphone ya wakati huo ilikuwa imetoka, vyote hivyo Emma alikuwa akininunulia. Ulikuwa huwezi kunikuta nazungumza na vijana wa pale chuoni. Kwanza wataniambia nini! Pesa ninayo yakuchezea, hata muda wa makundi yakujisomea sina. Ijumaa ikifika, safari ya Dar au nahamia hotelini na Emma mpaka aondoke. Watu wakawa wananisema, lakini mimi ndio naona raha naona kama wananipandisha cheo. Nikawa nimejawa na kiburi, ninauhakika wa ndoa!” Sabrina akaendelea.

“Na usifikiri uhakika huo wa ndoa naupata kwa fikra, Emma alikuwa tayari kujitokeza mpaka nyumbani. Sema sisi kwetu baba na mama wote wakali sana. Zaidi kwangu mimi sio kwa Sabina. Sasa nikamwambia Emma, akienda kujitokeza kabla sijamaliza hiyo Diploma, Mzee atamfukuza kwa kuwa nilifeli kidato cha sita. Anisubirie mpaka nitakapomaliza hiyo shule, ndipo tuone kama kunakuendelea na shule, basi niwe nishakuwa mkewe.”

“Kwetu sisi ni kazi. Hakuna kucheza, ni kazi. Kutoka ni kwa ruhusa maalumu. Huwezi kuaga hovyo hovyo, kwanza unakwenda wapi! Sabina wakati huo ndio anamalizia PhD yake nje ya nchi. Hakuna pakwenda, labda kijijini kwa bibi. Basi ninapokuwa nyumbani ikawa ni shida sana kukutana na Emma, mazungumzo ni kwa simu, simu yenyewe naficha. Simu niliyokuwa nayo, sikuwa na maelezo nayo. Hata anayenisomesha, yaani baba mwenyewe hakuwa na aina ile ya simu! Mimi nitasema nimetoa wapi! Nikawa naficha, nikiiwasha ni mbali na nyumbani nikimpigia Emma. Emma akaanza kulalamika. Akawa akiniambia niwe natoroka ili kukutana naye na kumpigia. Nikajaribu kumuelezea mazingira ya nyumbani, mwanzoni ni kama akawa ameelewa na kunipa moyo kuwa ni kwa muda tu, nivumilie.”

“Nikaanza field maeneo ya kulekule karibu na Chalinze. Baba alinitafutia, akakataa nisiende Dar, akasema hana anayemwamini kunitunza huko mjini, lazima nifanye field sehemu karibu na nyumbani. Hilo nalo likamchosha zaidi Emma, ambaye tulipanga nikaishi naye kipindi hicho cha field. Basi, likizo yenyewe ndefu. Ukiwa mwaka wa pili au wa mwisho wanaugawanya ule mwaka wa masomo kwa field na darasani. Hiyo ni kwa chuo chetu enzi hizo. Kwa hiyo ukumbuke nilikuwa na likizo na uchanganye na field, muda ukawa mrefu.”

“He! Si nikashangaa hakuna tena simu wala kulalamikiwa kumisiwa na Emma! Akawa mtu muelewa, kwanza akawa kama hana haja ya mimi niende. Nikamuuliza ni kwa nini tena! Akasema hataki mwanzoni tu eti aharibu ukweni, tuwe wavumilivu. Nikawa tu nacheka, nafurahia amani. Ikaja simu zikawa hazipokelewi kwa wakati, na wakati mwingine unampigia ni kama unamsumbua! Nikamuuliza kulikoni? Akawa mkali kweli kweli. Nikajua tayari mipango ishaharibika. Nikajikaza kwa kila namna, nikijiambia labda ni vile hajaniona muda mrefu, nijiibe niende.” Sabrina akacheka.

“Nikatoka kazini siku hiyo ya ijumaa asubuhi kabisa nikiwaambia narudi nyumbani sijisikii vizuri. Nikapanda basi mpaka Dar. Alikuwa akiishi maeneo ya Ubungo maziwa, alipangisha nyumba kubwa tu. Na mimi nilikuwa na funguo. Kufika, nakutana na Kasandra! Yule msichana niliyekuwa nikiishi naye kule chuoni. Bwana dada ni mzuri huyo! Asikwambie mtu Tino. Mzuri haswa. Nikamuuliza Kasandra, unafanya nini hapa na umepafahamu vipi? Akaniambia alipata field Dar, akamuomba Emma aishi kwake. Nikamuuliza kwa nini basi asiniambie mimi! Akaniambia labda sijamuelewa, yeye anaishi kwa Emma wala si kwetu mbele ya Chalinze. Nikahisi kama miguu inakufa ganzi. Maana alivyonijibu, ni kwa jeuri haswa. Na mtu mwenye mahusiano na mtu utamjua tu. Ile heshima ya mwanzoni akitumia vitu vyangu ilimwisha, ikawa dharau.”

“Basi, mimi nikamwambia nimekuja kuonana na Emma. Akaniambia Emma ndio ametoka muda sio mrefu, wamechelewa kuamka siku hiyo. Emma alisomea mambo ya Eletronics. Kwa hiyo ni fundi mitambo wakutegemewa huko kazini. Amepewa usafiri na nyumba analipiwa. Hawezi kuwa ameingia kazini saa nne, nikajua anataka kunifikishia ujumbe kuwa amelala naye. Sikupaniki, nikamwambia basi nitamsubiria, akaniambia sio pale. Kama namtaka Emma nimfuate kazini kwake au nimuachie yeye ujumbe. Niliumia Tino, nikabaki nimeduaa. Hakutaka kupoteza muda, akampigia simu palepale Emma. Akamwambia, “Sabrina yupo hapa, anasema anashida na wewe.” Nikaona napewa simu. Nikapokea. Emma alishindwa hata kunisalimia, akaniuliza nafanya nini pale na kwa nini nimekwenda bila taarifa! Nilishindwa hata kujibu. Akaniambia kwa kifupi tu, yeye ameamua kuendelea na maisha yake, na Hawa ndio mtu wake. Anaomba niache funguo zake za nyumba na vitu vyake vingine atafuata, kama nina  simu yake nimuachie hapo. Akakata simu. Hawa akaniambia nimkabidhi yeye. Nikampa, nikaondoka.”

“Kufika nyumbani tena, baba akawa amepita kazini, amenikosa. Nikakuta nasubiriwa nyumbani kwa hamu sana. Bwana nilitandikwa Tino, kama mwizi! Nikakaa jumamosi na jumapili najiuguza kipigo cha baba, jumatatu tena kazini. Nimerudi kazini na majeraha yakuchapwa na ya moyoni, nikawa kama nipo kwenye bumbuwazi. Sikumsikia Emma mpaka chuo kinafunguliwa.” Sabrina akacheka kwa masikitiko.

“Nimefika tu chuoni nikawa nimepangiwa chumba na msichana mwingine wa certificate. Yeye mgeni pale chuoni. Alishafika tokea chuo kinafunguliwa. Sasa ndio sisi mwaka wa mwisho wa diploma na advance ndio tunarudi sasa muhula wa pili, kumalizia. Nikaenda kuchukua vitu vyangu nilivyokuwa nimeacha stoo wakati tunaondoka chuoni, na kuvipeleka chumbani. Jioni yake nashangaa Kasandra na marafiki zake wananijia. Kasandra akaniambia anataka vitu vyake, ameambiwa na Emma achukue. Nikamkatalia. Nikamwambia vile vitu nilipewa mimi, siwezi kumpa. Huwezi amini Tino, kesho yake Emma alifika Dodoma, akisindikizwa na walewale wasichana, akaja kuchukua kila kitu pale chumbani kwangu. Aibu, maana walikuwa wakinicheka na kunizomea kabisa. Na kwa kuwa nilikuwa nikiishi na Kasandra, alijua kila kitu nilichokuwa nacho. Yule msichana alinisafisha, nikaachwa na nguo, nazo pia nafikiri aliamua kuacha kwa kuwa zisingemuenea. Kasandra anaumbile la upana chini zaidi. Yupo nane fulani hivi. Bwana ni mweupe, kama hivyo unavyomuona mkeo, Da Lela. Rangi yake moja. Juu mpaka chini. Huo mguu! Utampenda akivaa gauni fupi.”

“Watu wakawa wananicheka pale chuoni. Wanasema ni haki ya Emma kuniacha mtu kama mimi na kwenda kwa mwanamke kama Kasandra. Wengine wakasema kuna wanaume hata wakiiba nje ni haki yao. Huwezi kulaumu. Zikawa ni kejeli, Tino! Sina pakupitia. Chuo kizima kikajua aibu yangu yakupokonywa vitu. Marafiki sina, sina wakuzungumza naye na yule msichana pale mgeni akawa kama ametiwa sumu! Nilitamani kukimbia chuo, lakini sina pakwenda. Namwambia nini baba!”

“Si unaona hivi sina mwili, lakini pia nilikonda Tino. Hapakuwa na chakula kinachoweza kuingia mdomoni kikaweza kumezeka. Na pesa yenyewe nikawa sina sasa. Pale ndipo nilipojua baba alikuwa akinipa pesa ndogo. Nilipomaliza kulipa ada na michango mingine ya chuo, nikabaki kama sina pesa. Si unaona hii rangi yangu ilivyo, sasa niwe nimepauka, halafu nimejawa wasiwasi, huwezi kunitizama mara mbili. Darasani sielewi, kwanza hata mwalimu akisimama mbele ya darasa, simuoni kwa msongo wa mawazo. Nguo zenyewe zikaanza kupwaya sasa. Kule zilipokuwa zikinikaa vizuri, nikawa kama kijiti.”

“Nikafika hatua hata siwezi kujitokeza mbele ya watu! Darasani sitaki kuingia. Chumbani sipataki maana yule binti niliyekuwa nimepangiwa naye akawa analeta wenzake wanaanza kucheka mambo yao, lakini nikawa nahisi wananicheka mimi. Basi, nikapata sehemu ya kwenda kukaa huko peke yangu. Nikiamka asubuhi, naoga, nakimbilia huko. Nikafanya hivyo kwa muda tu. Zikavuma habari nimekimbia chuo, maana darasani sionekani. Kufupisha habari nilikuja kuokolewa na mwana chuo ambaye nilimkataa vibaya sana mbele ya mawaziri wake, maana yeye alikuwa raisi wa hapo chuoni. Sijawahi kuelewa ni kwa nini alifanya hivyo, lakini Jack ndiye aliyebadili historia yangu na kunifanya nimalize kile chuo, nikiwa mimi nilimtenda vibaya.” Sabrina akaendelea.

          “Huwa Mungu akitaka kufanya jambo lake, au akitaka kukamilisha jambo lake, haihitaji watu wengi ili kumfanikishia mambo yake. Huyu Jack ninayekwambia, alisimama na mimi mpaka nikaweza kutoka pale chuoni kwa heshima. Nikiwa nataka kufukuzwa chuo maana ni kama nilishajifukuzish kwa kutoingi darasani bila udhuru, mitihani sikuwa nikifanya. Lakini yeye kama raisi wa chuo, aliniombea kwa mkuu wa chuo nisifukuzwe. Akanisaidia kunitafutia mtu, akanifundisha mengi niliyokosa kipindi najificha, nikatengeneza ripoti ya field niliyokuwa nikitakiwa kuiwakilisha na muda ulishapita kuiwakilisha. Nilipokamilisha ndipo yeye kama raisi, akanipeleka sasa kwa mkuu wa chuo. Nikiwa sasa na hiyo ripoti ambayo ilikuwa ni lazima kuwa nayo ili kukubalika kama mwanafunzi wa darasa hilo na ahadi yakutokosa tena darasa hata moja, na kufaulu.”

“Jack akahakikisha kila ninakokwama ananitafutia msaada. Baada ya mwezi, nikarudi kwenye chati. Nikaanza kufaulu vizuri. Heshima ikaongezeka kwa kuwa nilikuwa na raisi wa chuo. Watu wakawa wananiogopa sasa, wanajua wakinisema, au wakinifanya kibaya, Jack atajua, na Jack alikuwa karibu sana na kila Lecturer au mwalimu pale chuoni zaidi Mkuu wa chuo.” 

“Kufupisha stori wakati tunakaribia kumaliza. Tumebaki pale chuoni mwaka wa mwisho wa diploma na advance. Yaani sisi na kina Kasandra, si Kasandra akasikia Emma anataka kuoa. Tena hapo aliambiwa na rafiki yake wa karibu sana wa Emma. Akamwambia Emma alirudi kuomba msamaha kwangu, mimi nikamkatalia. Akajiambia kama hatanioa mimi basi yeyote, lakini alishajiambia yeye Kasandra hawezi kuwa mkewe. Akamwambia Emma alinifuata kwa mara ya mwisho na kuniambia hanidanganyi, anakwenda kulipa mahari, kama ni hasira tu nimwambie, yeye atasubiri mpaka hasira ziishe. Lakini akamwambia mimi nilimwambia aoe tu, sipo tayari kuolewa na yeye tena. Sitaweza kuja kuwa na yeye maishani mwangu. Kasandra alikuja kwangu akilia. Akaniuliza kama ni kweli Emma alikuja kuniomba msamaha akitaka turudiane na kama kweli anaoa. Nilimwambia kwa heshima kabisa, naomba akazungumze na Emma mwenyewe.”

          “Basi, sijui alimuuliza Emma, Emma akakubali au kama alipeleleza akapata ukweli! Lakini nikaacha kumuona Emma pale chuoni akija kumtembelea Kasandra. Sijui rafiki zake wakajua, yeye mwenzangu hakupokonywa vitu, lakini mawasiliano yakakatwa kabisa. Akabaki kama amechanganyikiwa. Mwezi mmoja ili tumalize chuo, Kasandra akanywa sumu.” Akamuona Tino ameshituka. “Lakini hakufa. Walimuwahisha hospitalini, lakini akafukuzwa chuo kwa hilo kosa. Sijamuona tena, maana kwao ilikuwa Arusha. Kwa ufupi mimi nikamaliza shule yangu vizuri tu. Nikiwa nimefaulu vizuri, lakini sijawahi kupata kazi.”

“Ninachotaka kukwambia Tino, mimi nilimaliza shule yangu sababu ya mtu mmoja tu ambaye hakunikatia tamaa. Alihitajika mtu mmoja tu kubadili historia yangu ya aibu, na kunirudishia heshima pale chuoni. Binafsi nilikuwa nimekata tamaa kabisa, lakini nafikiri kwa kuwa Jack alipita pale nilikokuwa napitia, ndio maana aliweza kunisaidia. Mimi sijawahi kuugua kama wewe. Ila nina historia mbaya mbaya za maisha mpaka naitwa fungu la kukosa. Sipati kazi, na hakuna wakunisomesha. Mambo mengi nakufanyia hapa, ni ujuzi niliopata kutoka kwenye ufugaji niliojifunza nyumbani. Kama mambo niliyokufanyia hapa mengi, nimetumia tu akili nikikumbuka vile tunavyowafanyia ng’ombe labda waliokuwa wamekula sumu, wakaanguka kabisa wakiwa katika hali ya kufa, tukawafanyia mengi niliyokufanyia wewe, wakaweza kusimama baada ya muda mfupi sana wa matibabu, nakuweza kutoa maziwa.” Hapo Tino akaelewa ni kwa nini amejisikia nguvu mwilini mwake kwa haraka.

“Au ng’ombe wenye madonda. Unakuta labda mtu anayekwenda kuwachunga amewasahau. Wakaingia kwenye mashamba ya watu. Wanarudi nyumbani wamekatwa mapanga vibaya sana. Wapo waliokuwa wakiishia kufa, lakini wapo tuliokuwa tukiwahudumia mpaka wanapona. Nimeshugulika na madonda yako kama vile kwa wale ng’ombe tu. Sina ujuzi mkubwa wala akili kubwa sana, lakini nishaona viumbe vilivyokuwa kwenye hali ya kufa, vikarudisha uhai. Au mimea iliyoingiwa na wadudu wabaya, lakini ikawekewa dawa, mpaka ikarudi kuwa kijani kibichi kabisa.”

          “Sasa kwa wewe kuwepo hapo mpaka leo, nakuhakikishia Tino, Mungu hayupo tayari na wewe. Wewe ndio unao uwezo wakubadili hatima yako katika muda uliobakiwa nao hapa duniani. Ukikubali, utakufa ukidharaulika hivyo hivyo watu wakikuhesabu mfu wakati upo hai, na unauelewa wako. Mimi sijui wewe ulikuwa nani kabla ya hapa! Lakini kwa jinsi ninavyopaona hapa, uzuri wa da Lela, hawezi kuwa alikubali kuolewa na mtu mchovu au kukutunza mpaka sasa kama wewe hukuwa mtu fulani wa maana. Usikubali kufa ukiwa unadharaulika. Kufa ukiwa vilevile juu au na zaidi. Tena safari hii ukijua nini chakufanya, nani wa kumkwepa.”

“Emma aliporudi kwangu akitaka turudiane, nilijiambia ni kweli ninashida, lakini Emma si mwanaume nitakaye muhitaji maishani. Hana roho ya ubinadamu. Amerudi kwangu baada yakukumbana na uhalisia wa ubinadamu, akakumbuka wema niliokuwa nikimfanyia, uvumilivu kipindi cha matatizo yake, heshima kwake na pesa yake, akagundua Kasandra hayupo hata nusu yangu japo alikuwa mwanamke mzuri sana wakuvutia macho. Kasandra ni wale wasichana walevi wapenda club na kujirusha. Hajui maisha yakuwekwa ndani. Sasa nikajua kwa kuwa Emma ameshindwa huko kwa Kasandra ndio amerudi kwangu, akitaka kunitumia, aniweke ndani, apate sifa ya kuwa ana mke mwema, huku hanipendi! Nilikataa Tino. Nikajiambia bora nirudi kwetu mbele ya Chalinze, kuliko kuletwa mjini niwe nalia usiku kucha. Sikumtafuta tena, wala sikutaka habari zake.”

“Nimebaki nikitumika kwetu huku nikimuomba Mungu anisaidie jinsi ya kujikwamua. Ni kweli nilisomea kitu ambacho sipati kazi. Na wazazi wangu ni kama wameshachoka na mimi. Nipo hapa kwa ajili ya mapumziko ya muda mfupi, nirudie yaleyale maisha yangu. Lakini Tino, nina imani sana na Mungu. Sijui ni huku kubakia sina kimbilio! Najijua sina uzuri wakutisha. Sina akili sana kama Sabina, lakini namlilia Mungu aniinue. Sijui msaada wangu utatoka wapi, lakini kila inapoitwa leo, naishi kwa uaminifu sana ili Mungu anione. Nakufanyia wewe hivi, sikufahamu kabisa, na sijui kwa nini tumekutana hapa, lakini najiambia labda pengine Mungu ananipima! Nikizembea halafu akaniona sifai je? Kwa hiyo nikijua wewe ni mtoto wa Mungu, na Mungu anakusudi na wewe, ile mimi kuwepo hapa, nakuombea Tino, sana tu. Namkumbusha Mungu aliyekuumba akurejeshee kile ulichopoteza, lakini pia najiombea na mimi, nisije nikakutenda vibaya kwa kuwa huna uwezo. Sijui kama unanielewa?” Akamuona Tino analia.

“Nikwambie ukweli Tino, kule ninakowasaidia wazazi wangu, hapana hata shukurani ila kukosolewa tu. Mchana na usiku, lakini pia namuomba Mungu anitie nguvu nisifanye kwa ulegevu. Bila kuamshwa, saa 11 alfajiri nakuwa nimetoka kitandani na ujue hapo kurudi kwenye hicho kitanda ni mpaka usiku. Hakuna atakayeniambia asante, ila utasikia sifa zangu zikisemwa vibaya pale kaka au Sabina wakipiga simu. Utasikia wakiambiwa, “Yupo tu hapa! Hana la maana analolifanya.” Kama binadamu inaniuma sana, natamani watu waone ninachofanya, lakini pia namkumbusha Mungu anikumbuke. Kwa jinsi gani, hakika sijui Tino. Msaada wangu unatoka wapi! Hakika sioni Tino. Lakini namjua Mungu huwa ana mtindo wa kufanya yale magumu sana. Naomba badili fikira zako. Mimi kila ninapokushika, kila kiungo chako, nakitamkia uzima.” Tino akashangaa sana.

“Ndio maana nakuomba uungane nami. Amini tu na mimi. Najua haileti maana. Hata pengine unaponitizama mimi sina zile sifa za wasichana wengi kama kina Lela, lakini nina imani kubwa sana Tino. Naamini mambo makubwa sana kwenye maisha yangu kuwa siku moja yatakuja kutokea. Siku moja nitakuja kukwambia ni nini ninachoamini kitanitokea kabla sijafa. Na ukijua, pengine unaweza kunishangaa sana, lakini pengine ikusaidie Tino. Nawaza mambo makubwa ambayo pengine wanastahili kuyawaza wasichana warembo tu. Lakini na mimi najiona nastahili mengi mno, ambayo naamini ipo siku nitapata tu. Unaweza usinielewe kwa kuwa unaniona nipo hapa na wewe, hakuna hata aliyenitafuta hata kunijulia hali, lakini sikati tamaa Tino. Najua ipo siku na mimi nitakuwa mtu muhimu sehemu fulani na kwa mtu fulani. Hivi hivi nilivyo na mikono yangu migumu wala sina vingi vyakueleza vizuri. Sasa sembuse wewe Tino! Unaugulia kwenye AC! Nyumba imejawa wadawa! Vyakula vya kila aina! Wheelchair hiyo hapo inakusubiria wewe ikupeleke utakapo! Mungu amenileta sasa hivi nikutumikie wewe Tino, niambie unasababu gani yakutoona mwisho wa ushindi?” Akamfuta machozi.

“Wewe upo kwenye nafasi ya matumaini zaidi yangu mimi ninayetembea kwa imani tu. Wewe umezungukwa na neema! Na pengine umesoma sana. Ombea mifupa yako irudishe nguvu. Mwambie Mungu akuguse tena utembee, ufanye mambo makubwa na ya ajabu. Geuza kilio chako kiwe kwa Mungu wala si mwanadamu ambaye hawezi kukusaidia. Nakuhakikishia Tino, hapo hutakaa kwa muda mrefu. Utagundua mimi ni mtu wa mwisho kabisa unayemuhitaji maishani, ila Mungu. Ipo amani ipitayo amani zote. Faraja zote, Mungu atakupa. Mgeuzie Mungu uso uone jinsi anavyokupenda na kukujali. Na ninakuhakikishia Tino, Mungu wako yupo ila wewe ndiye humuoni. Mimi kuwepo hapa, kama ungenijua hata nusu tu, ungejua ni Mungu alinileta kwako nikusaidie.”

“Mimi sistahili kuingia kwenye majumba kama haya Tino! Sifahamiani na watu kama mkeo. Mimi ni mtu wa chini sana. Hata ungekuwa mzima unatembea barabarani, usingeweza kukutana na mtu kama mimi au hata tungepishana, nina uhakika usingegeuka hata kwa bahati mbaya kunitizama. Lakini ona. Leo nimeletwa na Mungu mpaka kwako. Tena nikiwa nimemuomba dada Sabina aniombee kwa wazazi waniruhusu niende kwake nikapumzike kidogo, nikusanye nguvu za mwili na roho ndipo nirudi kwetu. Lakini Mungu akaona hapana, lazima nije kukutumikia kwanza ndipo nirudi kule aliponiweka kwa sasa. Nakuomba mtazame huyu Mungu anayekupenda Tino. Bado anakuhitaji. Kwa hali niliyokukuta nayo, ilikuwa mbaya. Lakini jiangalie sasa hivi! Madonda yapo kama yameanza kutibiwa muda mrefu kumbe juzi tu! Yamekauka. Maumivu uliyonayo sasa, si kama niliyokukuta nayo! Kama huamini kama huyo ni Mungu, naomba upone nikupeleke kwenye yale mahospitali yenu yakulipia.”

“Utakutana na watu wenye uangalizi mzuri kukuzidi wewe, lakini hawaponi kwa haraka kama wewe! Mimi mpaka nashangaa Tino! Kila dawa ninayotumia kwako, inafanya kazi kwa haraka. Tafadhali usikate tamaa. Pambana, utoke kwenye hiyo hali. Samahani nimeongea sana, lakini nilitamani usikie.” Akamuona anakazama kumshika. Akasogea na kumpa mkono. Akaminya kwa nguvu. Sabrina akacheka. “Ule upumzike sasa. Siongei tena.” Amauona anacheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku hiyo nayo Tino alilala karibu siku nzima. Ndio ilikuwa siku ya mwisho ya kutumia hizo dawa kali za antibiotic. Sabrina hakujua kama Lela akirudi ndipo atamtaka aondoke au la. Alimlisha chakula cha usiku. Akamuosha tena na kumbadilisha nguo ndipo akamuweka alale. “Nitaenda kumsubiria da Lela pale sebuleni. Alisema atarudi leo. Sasa sijui atataka nifanye nini, ila nitakuwa nikija kukuangalia.” Tino akafunga macho mara mbili kuonyesha kukataa.

Sabrina akamuhurumia. Akarudi kupiga magoti pale alipolala, pembeni ya kitanda. “Tino! Sina amri ya kubaki hapa. Ningependa kubaki na wewe mpaka upone, lakini unajua sina huo uwezo. Namsikiliza da Lela. Akitaka niondoke, siwe...” Akaona anamshika kwa nguvu. Sabrina akainama kama anayefikiria, akamuona anamvuta zaidi. Wakabaki wakiangaliana machozi yakimtoka Tino. “Nitafanyaje Tino?” Akaendelea kumvuta. Sabrina akafikiria, akapata wazo. “Basi labda akija, akitaka niondoke nimuombe kazi ya kukuhudumia.” Hapo akamuona anakubali mara kadhaa. Kwa macho na vidole. “Basi nitambembeleza. Angalau tukae wote kidogo. Usilie basi.” Akamfuta machozi kwa mkono mmoja, maana mwingine alibaki amemshika. Akaona akae pale atulie. Alipopitiwa na usingizi, akatoka kwa kunyata.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sabrina akabaki pale sebuleni akiwafikiria wana ndoa hao. Mpaka mida hiyo Lela hakuwa hata amepiga simu kumuulizia mumewe! Hali aliyomkuta nayo huyo Tino! Malalamishi aliyomsikia akilalamika Lela kwa Sabina! Ikaibua maswali mengi kwa Sabrina. Hakutaka kumlaumu yeyote kwa kuwa hakuwa akiwajua, ila alishangaa hata kama Lela analipiza kisasi, akahisi amepitiliza. Inamaana bila yeye kuwepo hapo, kijana hakutokea, Lela ndio huyo hayupo, inamaana huyo Tino angebakia gizani, akiwa na njaa na uchafu mwingi vile! Sabrina akajishangalia ya uzunguni, akabaki akimsubiria Lela, mama mwenye nyumba wake.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment