Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Makosa! - SEHEMU YA 2. - Naomi Simulizi

Makosa! - SEHEMU YA 2.

Saa nne usiku akasikia geti likifunguliwa, akajua Lela ndio anarudi. Akatoka kwenda kumpokea. “Nilijua ushakimbia!” “Nipo dada. Karibu.” Akampokea. “Kumbe wewe mtoto mzuri hivyo! Itabidi nimuombe Sabina aniachie kwa muda.” Sabrina akacheka. “Au ushachoka unataka kuondoka?” “Hamna shida. Ila yule kijana hajaja da Lela!” Wakawa wanaingia ndani. “Basi kazi ndio hiyo. Wafanyakazi hawakai mdogo wangu. Hakuna mtu anapenda kuchezea kinyesi cha mtumzima! Sasa ukimwambia hivyo Tino, anajidai kazidiwa. Matokeo yake ndio kukimbiwa na wafanyakazi wote. Na mimi nilishamwambia kabisa Tino, maisha yangu hayawezi kusimama kwa yeye kushindwa kuzuia haja zake, kutaka watoto wa wenzake eti ndio wachezee uchafu wake!” Sabrina akatamani kumtuliza, alijua Tino atasikia.

“Lakini naona anaendelea vizuri.” “Atajijua na balaa alilojitafutia mwenyewe. Hapa nimechoka, nataka kitanda tu!” Akavua viatu. “Starehe pia zinachosha!” Akalalamika Lela. “Sasa mimi asubuhi huwa nawahi foleni kuwahi kazini. Nakuomba ubaki mdogo wangu unisaidie. Mimi mwenyewe nitampanga Sabina, ili akubali ubaki hapa kwa muda ukinisaidia. Ukiwepo hapa napata hata sababu yakuonekana mtaani. Nawaambia watu Tino anaye mtu wakumsaidia nyumbani.” Akaendelea kudai uhuru wake akimbembeleza Sabrina. “Usikatae mdogo wangu. Nitakulipa. Au unasemaje?” “Wala usijali. Nipo mapumzikoni. Kwanza kwako hamna hata kazi. Napata muda wa kutosha kupumzika.” “Afadhali. Tino huyo niachie mwenyewe. Usihangaike naye.” Akamtolea pesa, akampa. “Mimi nakwenda kuoga, nilale. Nipo hoi!” Akaingia chumbani kwake bila hata kupita kumuona mumewe.

Sabrina akashangaa sana. Akasubiri patulie, akaenda chumbani kwa Tino akiwa na wasiwasi. Akamkuta ameamka. “Da Lela amekuja lakini amechoka, ameenda kulala.” Akamuona amebaki kimya akimtizama tu. Akasogea. “Amesema ataenda kuzungumza na Sabina, ili nikae hapa kidogo.” Akafunga macho mara moja. “Unataka kula?” Akakubali. Sabrina akacheka. Akamletea tena uji, akamuweka vizuri. “Umemaliza dawa Tino. Ukiendelea kula hivi, utapata nguvu mapema.” Akaendelea kula bila shida mpaka akamaliza. Tukae tena nusu saa ndipo ulale. Akamuwashia tv sauti ya chini ili asimuamshe Lela.

Wasiwasi ukamwingia Sabrina, wapi pakulala. “Tino!” Sabrina akamuita kwa sauti ya chini kama kunong’ona na kumsogelea pale alipokaa. “Itakuaje kuhusu kulala?” Sabrina akanong’ona zaidi. Tino akabaki akimtizama kama hajaelewa. “Naogopa kulala hapa kama jana! Labda niende kulala kule kwenye chumba alichonikaribisha dada, nitaweka alam, kila baada ya masaa mawili niwe...”  Akakataa kabisa tena kwa kuguna kabisa. “Tino!” Sabrina akashangaa kwa woga. “Naogopa.” Akakataa. Akamshika mkono kwa nguvu. “Hatakasirika akinikuta nimelala hapa?” Akakataa kama kumwambia hapana. Sabrina akashangaa. “Tusije kuharibu Tino, nikafukuzwa kabisa!” Akatingisha kichwa kumwambia hapana. “Unauhakika?” Akamuuliza tena kama kutaka uhakika. Tino akamuhakikishia huku akimvuta mkono kwa nguvu. “Sawa. Basi nakwenda kuoga, nitarudi.” Ikabidi Sabrina amkubalie.

Wakati ananyanyuka, Tino akamvuta tena. “Nitarudi Tino. Nakuahidi nitarudi. Sitakuacha.” Akamuona amevuta pumzi kwa nguvu, akamwachia. Sabrina akamuhurumia, asijue mwishowe ni nini. “Bora aweze kujitegemea mwenyewe. Pengine anaogopa!” Akajisemea Sabrina, asielewe maisha ya Tino pale ndani. Lela alimuacha tangia ijumaa, akimwambia asihangaike naye! Anarudi jumatatu usiku anamwambia kijana hajatokea, bado anamwambia aachane naye, anaingia chumbani bila hata kujali maendeleo yake! “Hata chakula jamani!” Sabrina akashangaa sana huko chumbani akiwa anaoga. Akafurahia pesa aliyompa. Aliiweka tu juu ya meza ya pembeni ya kitanda. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya kuoga akatoka tena kurudi chumbani kwa Tino. Akamkuta ametoa macho kama anayesubiri kwa wasiwasi. “Mbona hujalala Tino!?” Akabaki akimwangalia. Akajua alikuwa akimsubiria. “Nilikwambia nitarudi Tino. Au unataka kujisaidia?” Akakataa na kunyoosha ule mkono wake wa kushoto. Sabrina akapiga magoti na kuupokea. Akamshika kwa nguvu akiuminya minya. “Utapona Tino na utakuwa na nguvu kama zamani. Ujitahidi kula. Sawa?” Akakubali. “Basi ulale, mimi nipo hapa, ukipitiwa na usingizi nitahamia kwenye kochi.” Akakubali. Akampa maji na kumfunika vizuri. “Miguu bado inapata baridi?” Akakubali. Akakaa kitandani. Akachukua mafuta akaanza kumkanda taratibu. Aliikuta hiyo miguu ipo na magamba kama nyoka. Kwa kuipaka mafuta na kuisugua mara kwa mara, ikaanza kuanguka ngozi nakubakia na nafuu kubwa. Akamuona anaanza kusinzia. Akaendelea kumsugua mpaka akajua amelala kabisa, akamvalisha soksi nzito, akamfunika tena, akahamia kwenye kochi akabaki akiwaza. 

Sabrina Apata Kwa ufupi ila kwa undani juu ya

Wanandoa Hao. 

A

kaona ampigie simu Sabina. “Hujalala?”  Sabrina akashangaa alivyopokea simu kwa haraka. “Ndio nataka kurudi kulala tena, nilirudi nilikuwa hoi. Mchana nikapitiwa na usingizi hapahapa kwenye kochi. Nimeamka muda si mrefu, ndio nataka kuhamia kitandani. Vipi? Lela amerudi?” “Alirudi kama lisaa limepita sasa.” “Lela kwa starehe! Mimi nilimuacha tokea asubuhi. Mumewe hajambo?” Sabina akauliza. “Anaendelea vizuri ila kijana anayemuhudumia tokea ijumaa hajaja, da Sabina! Ndio ameniomba nibaki nimsaidie.” “Muongo Lela. Huyo kijana alishaacha muda mrefu tu.  Nafikiri kama sio jumanne iliyopita, nibahati. Nilikuja kugundua jana kwenye mazungumzo yake.  Huyo Tino anaachwa hapo hivyohivyo.” “Nimeiona hali yake! Nilimkuta vibaya sana.” Sabrina akaongea kwa sauti ya chini kwa kulalamika.

“Huyo Tino huwa hanipendi kabisa mimi. Anajua eti mimi ndio namuuza mkewe kwa wanaume. Tulikuwa hata hatuongeleshani. Alikuwa akinikuta hapo kwake, ananisalimia tu na kupita ndani. Hatoki mpaka asikie nimeondoka. Tena hapo baada ya kujibishana naye sana. Nilimwambia Lela si mtoto mdogo, anayoyafanya ni kwa kupenda kwake. Na yeye mwenyewe Lela ndio anapenda kuongozana na mimi, wakati mwenzie sina majukumu ya ndoa! Lela hajui kukaa nyumbani huyo. Yeye na starehe, starehe na yeye kama mimi nisie na majukumu ya familia. Sasa huyo Tino ndio akawa anafikiri eti mimi namuuza mkewe kwa mabwana.” Sabrina akatulia tuli ili kumuelewa sasa Tino. Akaamua kutoka kabisa pale na kwenda kujifungia chumbani kwake ili asimuamshe Tino.

“Kwani, huyu Tino na mkewe walikuwa na matatizo kabla hajaugua?” Sabrina akaanza kudodosa. “Sasa ngoja nikwambie habari ya Tino na Lela. Lela mpenda starehe tokea zamani, kila mtu anamjua nashangaa ni kwa nini Tino ananilaumu mimi. Akamuona Lela na huo urembo wake, akachanganywa harakaharaka. Lela naye alivyomuona Tino mzuri hivyo na anayo pesa, na jumba hilo si akamkubali kwa haraka, akafungia macho mapungufu mengine yaliyokuwa yakimkera kwa Tino, mpaka dini akatoa muhanga dini yake na kanisani akawa anaenda huyo Lela. Alikuwa akimfanya  Tino kama Mungu wake.” “Da Sabina!?”  Akashangaa Sabrina.

“Kweli tena. Hivyo huyo Lela unavyomuona hivyo hata kwao hawamtaki kumuona sababu yakubadili dini, japo ndoa walifunga mahakamani. Ila sababu ya pesa ya Tino, Lela alikuwa anakwenda sana kanisani. Nikisema sana, namaanisha kila jumapili alikuwa pembeni ya Tino kanisani kama yeye ndio mkristo. Yote hayo ni sababu ya pesa ya Tino.” “Kwani huyo Tino alikuwa na pesa?” Ikabidi Sabrina aulize tu. “Umeona hilo jumba lake hapo?” “Lake na mkewe au?” “Aringe Lela mtoto wa uswahilini huyo! Vyote hivyo Lela kavikuta. Na unafikiri ni kwa nini huyo Lela yupo hapo na Tino mpaka leo? Au unafikiri mahela anayochezea Lela anayapata wapi?” “Si anakazi nzuri!” Akajibu Sabrina.

“Kazi nzuri gani itakayomlipa pesa yakuendesha gari kama hilo na kutapanya pesa kiasi hicho na kupata yakumuhonga huyo mwanaume wake! Kwa mshahara upi watakao mlipa huyo Lela aliyesomea usekretari tu tena vichochoroni wala si kwenye chuo chamaana kama wenzie? Hata diploma hana huyo.” Sabrina akashangaa sana. “Hana shule yeyote huyo kichwani. Hana ajira yakumlipa pesa nzuri. Kama amekwambia hivyo, basi kakudanganya. Hana lolote. Hapo anamvumilia Tino kwa kuwa pesa ya Tino bado inaingia kila mwezi kama mshahara. Aliposingiziwa wizi, akafungwa, ikajakugundulika kuwa alisingiziwa, ikabidi kulipwa fidia, mamilioni ya pesa.”

“Yaani alifungwa kwa kusingiziwa. Alipotoka tu jela na kushinda hiyo kesi ndipo akashitaki hiyo kampuni. Akashinda kesi na kulipwa hayo mamilioni ya pesa na hatujui ikaweje, akataka kurudi tena kazini. Watu wakamuonya asirudi maana ile kampuni itakuja kumsingizia kitu, yeye Tino akasema anachukua pesa na anarudi kazini maana alishawekeza sana kwenye hiyo kampuni, na yeye anaubia hapo, hawezi kuachia hivihivi. Akasaini kila kitu chakurudi kazini, hapo alishaanza kuwa dhaifu sababu yakukaa jela. Alikuwa mtu mkubwa sana hapo kazini na pesa yake ya mshahara kubwa na matibabu yote yakawa ya hiyo kampuni. Ugomvi ukaanza na Lela. Lela anataka kutapanya, halafu akawa alishaanza mahusiano wakati mwenzie yupo jela. Kanogewa nje, ndani hawezi kutulia tena. Ugomvi wa hapa na pale, ndipo akaanguka na pressure. Akapata shindikizo la damu. Akalazwa.” Sabina akaendelea.

“Mwanasheria wake akatengeneza kesi ingine kuwa hawawezi kumfuta kazi kwa kuwa ugonjwa walimsababishia wao. Lazima waendelee kumtibu na kumlipa mshahara kama yupo kazini. Kesi ikanguruma wee, Tino akashinda tena. Hapo Tino anaugua, lakini mshahara wake unaingia kila mwisho wa mwezi, na ukumbuke pia mara ya kwanza alishashinda mamilioni ya pesa, basi ndio asili ya utajiri wa Lela na utapanyaji wake. Kwa hiyo huyo kulala kwake hapo ndani ndio neema ya Lela. Anakula mshahara wake na wa Tino. Na mshahara wa Tino si mdogo. Akiumwa huyo Tino, matibabu yote analipiwa na kazini kwake. Kwa hiyo ukimuona Lela hapo kama kachanganyikiwa, ni kwa kuwa anamtaka huyo Tino, huku hamtaki. Uhai wa Tino, unampa pesa na kumnyima uhuru wa kuishi na huyo mwanaume wake.” “Kwani mwanaume wake hana kazi?” Ikabidi Sabrina kuuliza. 

“Mpuuzi mmoja tu wa huko mtaani. Sijui yupo kwenye kampuni gani! Sijui ana kijikazi gani! Lakini huwezi kumfananisha na Tino hata kidogo. Ni kijana tu, lakini Lela anampenda kufa. Anasema mzuri sana kitandani.” “Da Sabina wewe!” “Mungu tena. Kwani si tulikuwa wote siku zote hizo huko Kigamboni? Watu tulikuwa tunatoka kunywa, wao wamejifungia ndani chumbani kwao. Anasemaga hawezi kuishi bila kushikwa na huyo kijana. Kamnunulia gari, na nyumba pia anamlipia kodi. Pesa ni ya huyohuyo Tino.” “Dada wewe! Sasa ndugu zake Tino wako wapi mbona hawaji?” Sabrina akaendelea kudodosa akizidi kushangazwa.

“Sasa nayo hiyo habari ingine.” “Nini tena?” “Si unamuona huyo Tino yupo kama shombe?” “Namuona ana manywele mengiii!” “Basi, baba yake alioaga mwanamke kama wakisomali hivi au mwarabu, sijui mzungu, watajijua wenyewe. Ndio akatoka huyo Tino. Wakati mdogo sana, mama yake akafariki ndio baba yake akaoa tena. Inavyosemekena baba yake huyo Tino alikuwa na pesa nyingi sana, yule mama wa kambo akawa anamkandamiza Tino makusudi ili asije kuwa mrithi. Mke ana nguvu yake bwana. Yule mama akazaa mtoto wa kwanza na wa pili wote wakike. Sasa jinsi yakumtoa Tino kwenye familia inasemekana ikawa shuguli.” Sabina akaendelea.

“Huyo Tino ukimwangalia kwa haraka ana kama kaujinga fulani hivi. Kama mzubavu hivi! Mzito wa maneno, na sauti pia haitoki. Sema alijaliwa sana akili na anakipaji kikubwa sana cha uchoraji ndio hicho kinamuingizia pesa mpaka hapo akiwa mahututi. Nasikia majengo mengi sana makubwa hapa nchini, yeye ndio mtengeneza ramani zake. Anauza ramani na michoro ndani na nje ya nchi, ndio mmoja wa waanzilishi wa hiyo kampuni waliyomfunga. Sasa turudi kwa yule mama yake wa kambo akafikiria wee, akaona jinsi ya kutoa kwenye familia ili abakiwe na wanae tu hao wa kike, ni amsingizie kubaka dada yake.” “Da Sabina!” Sabrina akashituka sana.

 “Kweli tena. Lakini kila aliyesikia hivyo nasikia alimpingia Tino, wakimtetea. Lakini hapo nizamani sijui ndio alikuwa anaanza chuo au sijui. Ndio yule mama nasikia akataka kumpeleka polisi, baba yake akamuombea msamaha, yule mama akamwambia kama ndio hivyo Tino aondoke pale ndani na asije kurudi tena hapo nyumbani. Akirudi tu anampeleka polisi.” “Jamani!” Sabrina akazidi kuumia.

“Ndio sasa chanzo cha mafanikio hayo ya Tino kikaanzia hapo. Kwa siri nasikia huyo baba yake akamjengea mwanae hilo jumba, nakumpa mapesa. Tino akakazana na shule huku anaishi hapo, na baba yake alikuwa akimpa pesa, yule mama hajui. Akajitenga nao kabisa. Wakawa hawajui Tino alipo, kumbe mwenzao maisha yanaendelea huko Kunduchi huku akisoma. Yule mama akaja kupata watoto wakiume wengine wawili. Yule baba alipofariki, wakabadili mirathi, nasikia wakasema mali zote yule baba amewaachia watoto wa mke mdogo, na yule mama akiwepo. Unaambiwa Tino hawakumpa hata shilingi. Lakini Tino hakujali. Alivyozika tu, nasikia akaachana nao.”

“Sasa kipindi yupo jela, Lela akijua hiyo habari kuwa walimzulumu Tino, pesa imepungua, si Lela akaenda kule kwa mama yake wa kambo Tino kumtisha! Akamwambia ametafuta mwanasheria, kufufua kesi ya madai ya Tino.” “Da Sabina!” Akaazidi kushangaa sana Sabrina. “Kwenye pesa, Lela hana undugu wala urafiki. Na amejaliwa hana hofu wala aibu. Haogopi mtu huyo.” Sabrina akashangaa sana.

“Basi. Akawatisha hapo wee, wakakubali kulipa garama za mwanasheria na kuwa akimpa pesa kila mwisho wa mwezi mpaka kesi ya Tino itakapoisha. Ndio akatulia na wale ndugu wakamtafuta mwanasheria mzuri sana kwa sharti kuwa kesi ikiisha, waachane kwa amani. Na kweli kesi ikaisha kwa Tino kushinda mapesa hayo anayochezea Lela. Alipougua tena, ukumbuke ndugu sasa, zaidi wale wadogo zake wa kiume, walikuwepo kwenye picha. Wakawa wanamsaidia kaka yao. Hiyo pesa ilipotoka tu, Lela akawageuka wale ndugu. Akawaambia kwa uwazi kabisa, hawaamini. Walishamtapeli Tino mara ya kwanza, na kujitenga naye. Sasa hivi wanajirudi sababu ya pesa.” “Da Sabina!”

“Usicheze na Lela. Akawaambia kama wanakuja pale, iwe kufua mavi ya ndugu yao lakini hawapati kitu.” “Jamani!”  Sabrina akaumia sana. “Sasa hapo hebu niambie. Tino mwenyewe akawa wakugeuza kulia na kushoto. Anajisaidia mchana na usiku, huku unatukanwa! Ndugu wakaanza kupungua mmoja, baada ya mwingine mpaka akabaki naye tu. Kila siku ana kazi yakubadili wafanyakazi. Huyo Tino akipata wakumuhudumia siku tatu, anafufuka. Akiondoka, ujue ndio basi. Yale maneno ya Lela aliyotuambia hapa siku ile eti anamlisha asubuhi kabla hajaenda kazini, ni uongo mkamilifu. Lela hana huo muda. Tena wakati mwingine anaweza akatoka ijumaa hapo akienda kazini, anakwenda kwa huyo mwanaume wake harudi hapo mpaka jumatatu usiku.” “Da Sabina wewe!” Akaumia sana Sabrina.

“Kama ungekaa hapo mbona utamuona. Yupo hapo ili tu kuendelea kujulikana kama ni mke wa Tino, apokee pesa yake, basi. Lakini si kumsaidia.” “Nimeingiwa huruma!” “Hata mimi namuhurumia Tino, lakini alishanikera sana. Badala agombane na mkewe, ananitafuta mimi uchawi! Kwanza tulikuwa hata hatuongeleshani naye huyo.” “Natamani kumsaidia kidogo mpaka apone kabisa!” “We Sabrina! Unataka kuchezea mavi ya mtu mzima huyo!” “Sasa si bora nimsaidie Tino huku nalipwa, kuliko kufuga ng’ombe za wazazi wako, dada yangu halafu hata pesa ya mafuta yakupaka nikiomba natukanwa!” Sabina akacheka.

“Eti Sabina dada yangu? Hapa Lela karudi, kanilipa kidogo. Si uongo. Kesho nakwenda kujinunulia vitu vyangu kidogo, angalau na mimi nionekane mtu. Hata pesa ya pedi nilikuwa sina, nikarudi kutumia vitambaa kama wabibi wa zamani!” “Kama huoni shida, sawa. Maana wenzio wanashindwa nasikia na hicho kinyesi na hayo madonda.” “Kwanza madonda yenyewe nimehangaika nayo naona yananafuu kubwa. Yamepungua harufu.” “Mtoto umekazana!” Sabrina akacheka.

“Sasa nawaagaje wale wazazi wako?” Akauliza Sabrina akimtega dada yake yeye ndio atoe wazo, akijua akikubali yeye ndio wazazi wake wamekubali. “Wewe niachie mimi. Nitawaambia nimekutafutia kazi, wakuache kwa muda.” Sabrina akafurahi sana. “Kweli Sabina?” “Wewe kuhusu baba na mama wala usihangaike nao tena. Mimi nitawapigia kesho asubuhi wakati nakwenda kazini. Wewe kaakaa hapo, ukichoka rudi. Tutajipanga upya.” “Mungu akubariki dada yangu. Angalau kwa mara ya kwanza na mimi nitajulikana natengeneza pesa.” Sabina akacheka. “Kweli. Niache kuomba pesa za pedi.” “Na nitamwambia Lela asikupunje. Sio akazane kuhonga pesa ya mwenzie, huku inashindwa kumsaidia Tino mwenyewe.” “Sawa dada yangu. Nakushukuru sanaaaaa!” “Wewe kweli wa ajabu! Unafurahia kuchezea kinyesi!” Sabina akamshangaa sana mdogo wake. “Wewe lala, kesho wapange baba na mama. Baadaye mpange na Lela, basi mengine niachie mimi.” “Sawa.” Sabina akakubali bila shida. “Ila Lela muache kwanza, akuonyeshe yeye ndio mwenye shida, halafu ndio uwe kama unampa wazo la mimi kumsadia. Maana alisema atakutafuta akuombe nibaki kidogo.” Sabrina akatoa yeye hilo wazo. “Sawa sawa.” Wakaagana, Sabrina akakata.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwa mara ya kwanza angalau Sabrina akajua anamuhudumia mtu wa namna gani na anaishi na wanandoa wa namna gani. Akamuhurumia sana Tino. Akamfikiria. Akaangalia pale alipo na thamani inayomzunguka! Akawaza Sabrina akimuhurumia mmiliki ambaye anafanywa kama mtumwa asiye na hadhi! “Anawezaje Lela!” Akawaza Sabrina, lakini akaona anyamaze na kufanya kilichompeleka pale. Akarudi chumbani kwa Tino.

Akamkuta hajalala. Akashangaa. Akamsogelea pale kitandani. “Tino! Mbona hujalala?” Akabaki akimwangalia kwa huruma. “Nimekuamsha nilipokuwa nikizungumza na simu?” Akakubali. “Samahani sana. Ndio maana nilitoka ili nisikusumbue. Pole.” Akataka kumshika, Sabrina akapiga magoti pembeni ya kitanda, akamvuta mkono na kumshika vizuri. “Sasa hivi sitazungumza tena. Rudi kulala.” Akakubali. Akaanza kusinzia, Sabrina amemshika mkono. Alipomuachia tu akafungua macho.  “Kazi ipo!” Akajisemea Sabrina moyoni. Akakaa miguuni. Akaanza kumshika shika miguu. Anaiminyaminya taratibu. Akamuona anasinzia tena. “Sasa sijui ndio nalala hapahapa!” Akajiuliza Sabrina huku akimwangalia anavyosinzia. “Watakuwa wamemtesa sana mpaka amekuwa kama na hofu vile!”  Akaendelea kuwaza.

Akaanza kusinzia palepale, akajilaza vizuri miguuni, akalala asijue yuko wapi mpaka simu ilipoita alarm ya kujisaidia kwa Tino. Akatoka hapo kitandani akiwa na usingizi, akaenda kuchukua chupa asijue Tino anamtizama. “Naomba tujaribu kujisaidia Tino, ili usiingie mikojo.” Akakubali. Akamuwekea chupa. Na kweli akajisaidia. Akamfuta vizuri. “Nakugeuzia ukutani, ili usilalie huo upande zaidi. Ni sawa?” Akakubali. “Kabla sijakugeuza, unataka kula?” Akakataa. “Maji ya kunywa?” Akakubali. Akakaa karibu yake, akampa maji. Akashangaa ameyavuta mengi karibu amalize chupa. “Ulikuwa na kiu sana?” Akakataa. “Nimefurahi kama unajilazimisha. Maji yatakusaidia.” Hapo akakubali mpaka kwa kichwa. Sabrina akacheka. Nakumgeuza upande mwingine na kumuwekea mto kwa nyuma. Akampapasa begani kidogo kama kumbembeleza. Akamfunika na kurudi kulala miguuni. Wakalala mpaka asubuhi.

Jumanne!

S

abrina aliamka saa 11 na nusu kwenda kupika uji. Wakati yupo jikoni akasikia mlango wa chumbani kwa Lela ukifunguliwa. “Unapika nini? Kunanukia vizuri!” “Ni uji tu dada yangu. Unataka na wewe?” “Akuuu! Uji ndio nimekuzwa nao. Sitaki hata kuusikia.” Sabrina akacheka. “Unawezaje kunywa uji wewe Sabrina wakati kuna vyakula kibao!” “Uji wa mgonjwa huo dada yangu!” Akajibu Sabrina. “Acha utani Sabrina!” “Kwa nini?” “Yaani wewe unaamka mida hii kupika uji wa Tino!” “Namuona kama anaupenda. Na nikipika sasa hivi, nampa tena na saa 10 jioni.” “Basi ndio ujue hataacha kujinyea hovyo. Wewe mpe chakula chepesi kila wakati kama hujamkimbia kama wenzako. Hana ustaarabu huyo. Mpe mikate, angalau kumziba choo. Na akila mkate asubuhi anakaa bila njaa kwa muda mrefu tu.” Sabrina akaumia sana. Akajua na Tino atakuwa anasikia huko chumbani.

“Wewe usijali dada yangu. Vipi lakini na wewe, ndio unajiandaa kwenda kazini?” “Tena nina safari ya kikazi. Nilitaka tu uhakika mdogo wangu. Ile kauli ya jana si bado haijabadilika? Au ushachoshwa na huo mzoga wangu?” “Usimuite mzoga da Lela bwana! Unataka kusafiri lini?” “Yaani wewe ukinihakikishia upo. Na Sabina akakubali, nikija jioni nachukua tu mizigo yangu, naondoka na ndege ya usiku.” “Mpaka lini?” Sabrina akauliza akijua wazi anamdanganya. “Sasa hapo inategemea na wewe mdogo wangu. Maana huyo unayesema si mzoga, amenifunga kweli! Nashindwa kufanya mambo yangu ya muhimu. Misiba inatokea nyumbani, nashindwa hata kuhudhuria, sababu yake.” Lela akalalamika wee, akimuumiza tu Sabrina jinsi anavyomsema vibaya mumewe mbele yake.

 “Mimi nitakuwepo dada.” Ikabidi Sabrina amkatishe. “Kweli! Maana nisije ondoka, na wewe ukaondoka. Halafu wakaja watu hapa wakamkuta peke yake wakadhani huwa namfungia tu simjali. Wakati mimi nahangaika naye mchana na usiku huyo. Si umeona madawa yake huko chumbani kwake? Diaper, baby wipes, gloves pia nanunua ili watu wasione shida kumsafisha, lakini pia wanachoka!” “Mimi nitakuwepo dada yangu. Wewe usiwe na wasiwasi.” “Hapa natamani kukubeba!” Akafurahi sana Lela.

“Na nitakulipa mdogo wangu. Wala usione kazi yako itakuwa bure. Au unateseka bure. Na ungekuwa unajua kuendesha, ningekuachia funguo za lile gari ndogo nimefungia.” “Mbona mimi najua! Sema tu leseni imeisha muda wake.” “Sasa usijali. Mimi nafahamiana na mtu, leoleo utapata leseni. Nitakupigia simu mchana, uje mjini. Tushugulikie. Mbona wewe utanifaa!” “Sawa.” Akamuona amefurahi sana. Akamshukuru kwa maneno mengi mpaka Sabrina akaivisha, akaweka na uji kwenye chupa ya chai, mwingine kwenye bakuli bado alikuwa akizungumza yake.

Alipoona hamalizi kujitetea na kulalamika akaona yeye ndio ahitimishe. “Basi tutaongea baadaye.” Sabrina akamuaga ili asimcheleweshe kwenye shuguli zake huko chumbani kwa Tino. “Sawa. Tena chakula cha mchana wala usipike. Nakupeleka sehemu nzuri, ukale vizuri kama shukurani yangu kwako.” Sabrina akaona shida kwenda kula mahotelini na kumuacha Tino hapo nyumbani peke yake. Akaona akatae tu. “Da Lela, tafadhali usijali. Mimi nipo sawa kabisa. Kwanza kama ulivyosema, unakila kitu cha mumeo.” “Tino.” Akakanusha kwa kumrekebisha. “Samahani, Tino. Hamna hata kazi kubwa ninayofanya.  Wewe jiambie umepata nafasi yakufanya mambo yako. Nitakuja mjini mara moja tushugulikie leseni ili pakitokea tatizo, niweze kumpeleka Tino hospitalini.” “Hapo utakuwa umenisaidia kufunga mdomo wambea wote mjini. Tena ukitaka nitakupa kadi yake ya kliniki uwe unampeleka, hata huko hospitalini wawe wanamuona waache umbea.”

“Hamna shida dada yangu.” “Basi nikirudi jioni nitakupa maelekezo yake yote ya hospitaini. Ila ukiona unalemewa, wewe acha, mengine nitafanya mwenyewe.” “Sawa.” Sabrina akakubali akijua wazi hana afanyalo kwa mumewe. “Basi acha mimi niwahi foleni. Nikajiandae haraka, nitoke.” “Sawa dada, safari njema.” Sabrina akachukua trei yake ya chakula alichokuwa amemwandalia Tino, akaelekea chumbani.

Na kweli Tino alikuwa hajalala. “Uji bado ni wa moto. Mpaka nimalize kukuosha, utafaa kunywa.” Tino akakubali. Akamsaidia kujisaidia, kisha akamtengenezea beseni la maji yenye povu ya sabuni, jingine maji ya kusuuzia yenye delto kiasi kwa sehemu yenye madonda na beseni jingine maji ya vuguvugu. Akachukua na mataulo. Akaanza kumfuta kwa upendo. Kuanzia usoni mpaka kwenye nyayo huku akimfunika kwa taulo kubwa kavu ili asimuache wazi. Tino akimwangalia tu. Alishamtoa nywele za mwili mzima, akabaki kama mtoto. Ilikuwa ni kazi aliyoifanya kwa haraka ili kumsafisha vizuri na kuyapa madonda uwezo wakupona.

Hata uogeshwaji wake ukawa rahisi kweli. Tino akabaki akimwangalia vile alivyomwangalifu kwake na akijitahidi asiingiwe baridi asijue adha aliyopitia hapo. Hapakuwa na kujaliwa kwa kiasi hicho. Kila mfanyakazi aliyeletwa hapo na Lela, Lela mwenyewe aliwaingizia sumu juu yake. Kwa hiyo hata jinsi walivyokuwa wakimuhudumia ikawa kama mnyama tu asiye na thamani. Hawakujali anajisikia vipi, wala wanamuacha na hali gani. Chakula ndio walifanya kama walivyoelekezwa na Lela, mkewe. Kumpa mikate ili kumziba haja. Akaishia kumezeshwa mikate na chai tu. Tena mfanyakazi akijisikia. Leo Sabrina anamlisha kila baada ya masaa matatu! Eti anamgeuza kila baada ya masaa mawili ili asiumize upande mmoja! Anamwambia anataka akojoe sana kutoa sumu mwilini! Wakati alikuwa akisimangiwa kujisaidia! Tino akajiambia Mungu amemkumbuka kumletea Sabrina. Lakini atakaa kwa muda gani? Huo ndio ukawa wasiwasi wa Tino. Je, atachoka kama alivyokuwa akishauriwa na Lela? Akabaki akimtizama kwa huruma ili tu amuhurumie.

Alishakuwa ameandaa nguo zake. Akamkausha kwa haraka huku akimpaka sehemu nyingine mafuta, kwengine lotion na kwengine dawa. Yeye mwenyewe Sabrina akawa ameugawa huo mwili, Tino ametulia tu. Akamvalisha kwa haraka. “Pole kwa baridi.” Tino akakataa. Akimaanisha yupo tu sawa. Sabrina akacheka huku akimfunika shuka na blangeti, apate joto wakati anapasafisha pale na kutoa nguo chafu.

Alipoweka pale sawa, akamuweka vizuri ili ampe uji sasa. “Nitakupigia baadaye Sabr...” Lela akafungua mlango, akasita. “Hiki chumba mpaka kimebadilika harufu! Kilikuwa hakiingiliki! Mavi matupu!” Kimya. “Ujiandae kama kwenye saa nne hivi uje mjini, nikupeleke kwenye kutafuta leseni.” Tino akamtizama Sabrina. Sabrina akajua ameshaingiwa hofu ya kuachwa. Alitaka amwandae kwanza kwa mazungumzo ndipo amuage lakini Lela akawa ameharibu mipango yake. Tino akabaki akimtizama. “Nauli nakuwekea pale kwenye meza ya sebuleni. Ita usafiri. Usihangaike na daladala. Halafu upige picha za passport size kabisa, uje nazo.” “Nashukuru dada yangu. Basi nitafanya hivyo.” Lela akatoka, Tino akabaki akimtizama Sabrina.

“Da Lela atasafiri. Anataka kuniachia gari ndogo. Sasa leseni yangu ilishaisha. Emma ndiye aliyenifundisha kuendesha na akanitafutia leseni. Sasa tokea aniache, sikurudi tena kuendesha gari wala kutafuta leseni. Ndio ameshauri niende mjini akanisaidie kutengeneza mpya, ili ikitokea kuna tatizo niweze kukupeleka hospitalini. Au hata niwe nikikutoa angalau ubadili mazingira. Au unasemaje?” Sabrina akamuuliza kwa upendo. Akamuona amepoa, amenyamaza.

“Sitakawia kurudi Tino. Nitajitahidi kufanya harakaharaka ili nirudi tuwe wote, usiwe peke yako.” Kimya. “Tino?” Kimya. Hakukubali wala kukataa. “Sitachelewa Tino. Nakuahidi nitarudi.” Kimya macho yake ameangalia miguu. Sabrina akaona amlishe tu. “Huu uji umeshapoa, unafaa kunywewa. Naomba ule.” Akamuona ametulia zaidi ya kawaida yake. “Tino! Huu uji ukiwa baridi, utakuumiza tumbo!” Akamuona ni kama aliyekata tamaa kabisa hataki tena hata kula. Akaweka ule uji kwenye stuli, akakaa pale kitandani akamvuta mkono.

          “Natamani uzungumze na mimi Tino ili nijue unawaza nini!” Tino akabaki akimwangalia tu. “Kama una wasiwasi wakujisaidia halafu ukajichafua, nakuhakikishia sitaondoka mpaka umejisaidia haja zote. Umesikia?” Kimya. “Nijibu Tino, tafadhali. Au hutaki niende?” Akabaki vilevile kimya akimwangalia kwa huruma. “Unadhani sitarudi au nitachelewa?” Kimya. “Basi sitakwenda. Nitamwambia da Lela, kwa kuwa sasa hivi si haraka, basi tufanye wakati mwingine. Sawa?” Akamminya mkono kwa nguvu kidogo, hiyo ndio ilikuwa shukurani yake, Sabrina alishamgundua.

Sabrina akacheka nakumuhurumia. “Basi kwa sasa nitamwambia da Lela nisiwe natoka mpaka upate nguvu kabisa. Ikitokea dharula, tutamuamini Mungu, tutatoka tu na gari, huku tukiamini hatutakamatwa njiani. Sawa?” Hapo Tino akakubali. Sabrina akacheka. “Naona umeridhika sasa.” Akakubali. “Basi nakwenda kupasha uji moto ili uje ule.” Akatoka. “Sijui kama kuna kuondoka tena hapa!” Akajiuliza Sabrina huku akiandaa kwa upya kifungua kinywa hicho.

Tino alishasoma moyo wa Sabrina, akajiambia yeye ndio wakumganda mpaka amsaidie atoke hapo kitandani. Akajua Sabrina akitoka hapo, akaungana tu na Lela, atambadilisha moyo kama wengine. Akajua siku hiyo Lela akifanikiwa kumtoa Sabrina hapo nyumbani tu atampitisha kwenye starehe, na kumjaza maneno ya kumchukia yeye Tino. Alimjua Sabina, akaogopa wakifanikiwa kumfikisha kwenye starehe zao, atamsahau yeye. Hofu yakurudia yale maisha ya upweke, njaa, kuzimiwa taa na kuwa gizani wakati wote akilalia kinyesi, mikojo, baridi ikimpiga akishindwa hata kuvuta shuka akitetemeka kwa maumivu makali na njaa, ikamjaa. Akakusudia kumbana Sabrina, pengine atafanikiwa kumvuta kwake.

Akarudi na chakula tena. Safari hii akafanikiwa kumlisha. “Ukipata nguvu, nitakuwa nikikutoa hata hapo nje, angalau uwe unakaa sebuleni unaangalia tv ya sebuleni. Halafu ukijitahidi, nitakuwa jioni au asubuhi kabla jua halijawa kali, nakutoa nje upigwe na jua kidogo. Utapenda?” Akamuona anatabasamu. “Hizo ndefu na nywele zinakuziba wala sikuoni! Ungekubali niende kutafuta leseni, ningekuwa na uwezo wa kukuendesha nakukupeleka mpaka saluni ukakatwe nywele.” Tino akamwangalia. Sabrina akacheka. “Nimeshaelewa kuwa hutaki niende. Siendi. Tunabaki wote.” Akaendelea kumlisha huku akifikiria chakumwambia Lela.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sabrina alishakusudia kumsaidia Tino katika kila hali, na akajua mkewe yupo kinyume na Tino. Akahofia kumwambia eti ameshindwa kwenda kutengeneza leseni sababu hataki kumuacha Tino peke yake! Akajua hataeleweka. Yeye mke mtu mwenyewe anaweza kumfungia mumewe hata siku tatu na asijali, yeye amekutana naye hata week hajamaliza ndio ajionyeshe anajali sana! Sabrina akasita kusema ukweli. Lakini atamwambia nini na Lela ameshamwachia nauli yakumfikisha mjini! Sabrina akaendelea kuwaza, asijue Tino anamtizama tu.

Tino aliyemkuta siku chache zilizopita siye huyu. Amerudisha nguvu kwa vitu anavyomlisha na kumnywesha. Kwa heshima anayompa tu, na kumjali anachotaka, hata nuru ilianza usoni kwa Tino. Leo amerudisha mamlaka yakumwambia mtu asiende sehemu na kutii! Hali ya uanaume ilishaanza kurudi ndani yake. Akajisikia vizuri sana. Amebakishwa kwenye hilo jumba na Sabrina anayemjali na kumuhudumia vile! Akajisikia umaana wa kumiliki ile sehemu ambayo uzuri wake na fahari yake vilishapoteza maana kwa muda mrefu sana. Alidharauliwa na wote wanaowekwa mjini na pesa yake. Kuanzia Lela na wafanyakazi wote wanao fika hapo na kufundishwa kumdharau yeye.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alikuwa amepotelea mawazoni wakati amekaa tu hapo kitandani. Alishamlisha, akamsafisha mdomo. Akaenda jikoni na kuacha jiko safi. Akarudi kukaa palepale kitandani akisubiria nusu saa iishe amlaze. Akahisi Tino anamkanyaga. Akamshika ule mguu kwa upendo nakumwangalia. “Umechoka, unataka nikulaze?” Akakataa kwa kichwa. Akamwita kwa kufunga macho mara tatu. Sabrina akaelewa. Akamsogelea. Tino akamshika mkono huku amekunja uso kidogo.

Sabrina akaelewa ndio anamuuliza kulikoni. “Usiwe na wasiwasi Tino. Kila kitu kitakuwa sawa.” Akamminya mkono zaidi. Akajua anataka amwambie tu. Sabrina akacheka kidogo na kuinama kama anayefikiria, Tino akimwangalia. “Nafikiria jinsi yakumwambia da Lela! Nahofia anaweza asinielewe, wakati tulikubaliana vizuri kuwa tukutane mjini, na pesa ameniachia!” Akamuona Tino amepoa. “Ila na mimi nahisi sikufikiria vizuri Tino. Bado huna nguvu yakuachwa peke yako.” Akamminya tena mkono kama kumtuliza. “Ndio nafikiria njia nzuri yakumwambia da Lela bila kumuudhi.” Wakatulia.

Alipoangalia saa, akaona inatosha kukaa. “Ulale, nitakuamsha baada ya masaa mawili unywe maziwa yenye asali na yai. Naona vinakupa nguvu. Hata sasa hivi ukiniminya mkono au ukinikanyaga nakusikia.” Akakubali. Akamlaza vizuri, akarudi kukaa miguuni kwake. Tino huyu sasa hivi analala kwa kubembelezwa! Hakuwa amemvalisha bado soksi. Akachukua tena mafuta ya mzaituni, akaanza kumkanda kuanzia magotini mpaka kwenye uwayo. Taratibu huku akifanya kama kuamsha mishipa ya damu. Akaendelea kuminya misuli yake taratibu na kuvuta vidole vya miguu kimya kimya. Kimoja baada ya kingine. Miguu hiyo ilisharudisha uhai kwa muonekano. Ngozi zote zilishatoka. Alishamtoa vinyweleo na kumkata kucha. Ungedhani ni mguu wa mtoto wa kike vile ulivyosafishwa vizuri.

Taratibu kwa upendo akaendelea. Mguu wa kulia na kushoto. Hivyo hivyo. Alipomuona anaanza kusinzia, akapunguza nguvu ya kumchua. Ikawa kama anambembeleza kwa kumpapasa, mpaka akamuona amelala kabisa. Akabaki anampapasa huku ameipakata hiyo miguu. Na yeye akapotelea mawazoni, kidogo akasinzia akiwa amejiegemeza ukutani.

Walilala wawili hao, mpaka muuguzaji akasahau kama aliahidi maziwa baada ya masaa mawili. Akajilaza kabisa ubavu ubavu vilevile alivyokuwa amepakata miguu ya Tino. Akajiweka vizuri, akapotelea kabisa usingizini kule miguuni. Tino aliamka baada ya kama masaa mawili na nusu akagundua amelala hana habari. Akaona amuache apumzike. Sabrina alikuwa hana mchana wala usiku wa kumuhudumia huyo Tino. Kila wakati alitoa huduma kwake, akijituma bila kuchoka, tena kwa unyenyekevu wote! Ikawa kinyume na matarajio yake, akiwa amekuja mjini kupumzika baada ya shuruba za kwao akihudumia ng’ombe sasa imekua Tino.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment