“Naomba utulie tafadhali. Nahisi ni hali tu ya mwili. Labda
nakaribia siku zangu. Lakini si sababu ya Tino.”
Sabrina akatoka kabisa nje ya chumba na kufunga mlango ili asimuumize Tino.
Akasogea pembeni kidogo, akapunguza sauti. “Naomba mipango
yako isisimame sababu ya hiyo leseni. Mimi nitakuwa sawa kabisa kubaki na Tino.
Kukiwa na dharula nitaita taxi au nitampeleka mimi mwenyewe hospitalini kwa
kutumia hili hili gari nikiamini hakuna trafiki atakaye nisimamisha njiani.”
“Kweli Sabrina mdogo wangu!?” Akamsikia
ametulia.
“Kabisa dada yangu. Kuwa na amani kabisa na mipango yako. Nipe
ratiba nzima ya kliniki yake au sijui kumuona daktari! Mimi nitampeleka,
nitawaambia ni mfanyakazi wenu, umenituma wewe. Usiwe na wasiwasi kabisa.”
Hapo akawa amemfurahisha na kumtuliza Lela. “Kama hivyo,
hapo sawa. Maana nilishajua amenikwamisha tena huyo! Maana tokea aanze kuugua
huyo, mambo yangu yamekwama kabisa!” “Usijali. Ulishazungumza na Sabina?” “Huyo
naye ananiringia! Ameniambia nimpigie baadaye akitoka kwenye kikao tuzungumze
vizuri. Hataki nikufanye mtumwa.” Sabrina akacheka kidogo kama kumtuliza.
“Usicheke Sabrina! Mimi namjua Sabina. Mkorofi kweli dada yako!
Naomba nisaidie kumwambia sikufanyi mtumwa.” “Hata hivyo hunifanyi mtumwa bwana.
Kila kitu nafanya hapa ni kwa kupenda kwangu. Kwani mara ngapi umeniambia nisijishugulishe
na mambo ya Tino, lakini si nimefanya mwenyewe!” “Si hata leo asubuhi
nimekwambia mdogo wangu, eeh?” “Ndiyo.” Sabrina
akakubali akicheka. “Basi naomba na hilo umwambie
Sabina dada yako, na uhakikishe anaelewa. Mimi namjua Sabina. Anaweza kuja
kukutoa hapo hata sasa hivi!” “Usijali. Wewe uwe na amani. Endelea na mipango
yako.” “Hata leo si naweza kusafiri au unasemaje?” Akamtega kwa swali.
Sabrina
alishagundua uwepo wake pale unamkera tu Tino. Akajiambia akiwaacha pale hata
kwa siku nyingine tatu, Tino atatulia kabisa. Na alijua wazi hasafiri ila
anakwenda kwa mwanaume wake. Sabrina hakujali. Alichotaka ni uzima wa Tino. “Au unaona shida?” Akauliza tena Lela kwa kubembeleza. “Nisikilize da Lela. Mimi nipo sawa kabisa. Na uzuri huwa
unapokea simu zangu. Kukitokea lolote, akija yeyote, kabla sijazungumza naye na
kumfungulia mlango, wewe utakuwa wa kwanza kujua. Sitampeleka Tino popote
ambako najua kutazua maswali bila wewe kujua dada yangu.” “Wewe unanifaa sana
Sabrina. Na ndio maana nilitaka nikutoe leo, ukale chochote utakacho! Sema
mwenyewe umekuwa mzito!” Lela akawa amefikishwa.
“Sasa wewe hicho chakula ulichotaka nikakilie hotelini, niletee
hapahapa. Wala usijali.” “Hilo tu, wala usitie shaka. Nakuletea kuku mzima
wakushoma na chips. Soda zipo hapo ndani. Kunywa tani yako. Unataka nini
kingine?” Sabrina akacheka sana. “Ninavyopendwa mimi!” “Sana! Wewe mkombozi wangu mbona! Hata
mahitaji yako binafsi niambie mimi nitaenda kukununulia nikuletee hapo hapo.”
“Hamna shida dada yangu. Nakushukuru.” “Basi nitaleta na zawadi nzuri, ili ujue
nakushukuru.” Sabrina akacheka tena.
“Usisahau kuzungumza na Sabina tafadhali. Mwambie sikunyanyasi na nitakulipa
tu vizuri. Angalau na mimi nikapumzike mdogo wangu. Nimekaa kwenye hali ya
kuuguza muda mrefu sana. Mwili na akili vinachoka! Acha na mimi nikatulizwe
kidogo.”
Akajisahau na kuanza kufunguka. Sabrina akaona amuwahi. Maana Lela ni
muongeaji wa ulalamishi. Akianza, hamalizi na yeye alishajua muda wa kunywa
maziwa Tino umeshapita, na Tino yupo
ndani anamsubiri. “Usijali dada yangu. Mimi nipo.”
Sabrina akakubali kwa haraka, wakaagana. Hakujua ni mangapi ameyasikia Tino,
maana alijisahau akaendelea kuzungumza kama kawaida.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alielekea
jikoni, akamtengenezea maziwa kwenye kikombe kikubwa. Akaweka na kiini cha yai
bichi pamoja na asali. Akakoroga vizuri, akaweka na Milo, akampelekea chumbani.
Akampokea kwa macho. “Ujisaidie kwanza ndipo unywe maziwa.” Akaweka maziwa na
kwenda kuchukua vifaa vyakujisaidia pamoja na kumsafishia. Akampanga vizuri.
“Naomba ujaribu na haja kubwa kabisa. Tokea jana hujajisaidia! Naomba usibane
tafadhali, itakusaidia kufungua tumbo.” Sabrina akaongea kwa kujali. “Nakupisha
ili upate nafasi. Nipo tu hapo chooni, sitakwenda mbali. Pengine ukiwa na mimi
unashindwa kujisaidia.” Akakubali. “Na ujue wazi hutajichafua. Nimetegesha
vizuri, mkojo utaenda kwenye chupa, na kinyesi kwenye gazeti, hutachafuka wala
kuchafua shuka. Nimekuwekea na taulo chini. Hutachafuka kabisa. Kwahiyo jiruhusu
kujisaidia.” Akakubali akionyesha uso wa shukurani. Sabrina akampisha.
Alipopata
harufu ya kinyesi, akajua amefanikiwa. Akasubiri tena kidogo akaingia chumbani
akicheka. “Afadhali. Sasa hapo utapata njaa.” Akaongea Sabrina kuonekana
ameridhika na alichofanya Tino, wakati wengine walimsimanga. Akaenda kuanza kutoa
chupa ya mkojo. “Wakati nasafisha chupa, jitahidi kuendelea kujisaidia.
Nitarudi baada ya muda mfupi tu.” Akarudi tena bafuni. Akasafisha shupa na
kuiweka delto ili isitoe harufu, ndipo akarudi kutoa kinyesi. “Umemaliza au
unahitaji muda zaidi?” Akagundua amemuuliza maswali mawili kwa wakati mmoja
akacheka mwenyewe Sabrina. “Haya, ngoja nianze tena. Umemaliza?” Tino
akakubali. Akatoa kinyesi na kumsafisha vizuri tu. Akampaka tena dawa huku
akimsugua.
“Madonda
yamekauka Tino. Bado una maumivu makali?” Akakataa. “Afadhali. Nitaendelea kukupa
dawa ya maumivu asubuhi na usiku wakati unalala ili usiwe na maumivu kabisa.”
Akaendelea kumsugua sehemu ya nyuma vizuri, na mbele napo akampaka cream hiyo
yenye dawa, akarudisha diaper. “Unywe sasa maziwa, yasipoe zaidi.” Akamkalisha
na kumpa kwa kikombe tayaribu. Akamaliza yote. Hilo likamfurahisha Sabrina.
“Nakwenda kupika Tino. Uangalie tv ukiwa umekaa angalau hata kwa lisaa limoja
au mawili. Usilale sana. Ni sawa?” Akakubali. “Nitarudi kuwa nikikuangalia kama
utahitaji kitu. Sitakuacha kwa muda mrefu, na nikimaliza tu kupika, nitarudi
tukae wote.” Akakubali.
Siku
hiyo wakashinda wawili hao kwa amani. Sabrina akihakikisha Tino anakula na
kushiba. Hamuachi mchafu wala mnyevu nyevu. Kitaulo alichokuwa akimuwekea
shingoni ili akitoa ute asilowe nacho alikuwa akikibadili mara kwa mara na
kuhakikisha hanuki mate wala haloweshi t-shirt aliyokuwa amemvalisha.
“Nitamuuliza da Lela ni wapi huwa ulikuwa unakwenda kukata nywele ili nije
kukupeleka. Sitaki kukunyoa mimi nikakuharibu, ukajichukia.” Akamuona
ametabasamu. Wakati wote alipokuwa amekaa, kama ni hapo kitandani basi alitaka
aminye miguu. Alimuona anatulia. Hata aliposinzia, hakutaka kumlaza.
Alimpunguzia muda wa kulala kwa kuwa madonda yalipona, akajua hataumia kukaa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mapema
tu kama majira ya saa 10:30 jioni, Lela akarudi. Sabrina akamsikia akizungumza
na simu sebuleni. Akasubiri amalize ndio atoke. Lela alijaliwa sauti. Kila
alichozungumza huko sebuleni, walisikia hapo chumbani. Sabrina akatulia kama
hasikii. Aliweka mipango yake kwenye simu huku akicheka sana. Wote walijua
amejawa furaha.
“Sabrina
mdogo wangu!” Wakamsikia akiita. Sabrina
akatoka kwa haraka. “Mungu wangu mkubwa, nimembembeleza Sabina, naona
amekubali. Amesema atazungumza na wazazi, awaambie kabisa umepata kazi ya miezi
mitatu. Ila Sabina nyie!” Akacheka Lela huku anatingisha kichwa. “Amesemaje?”
Sabrina akauliza huku akicheka kidogo. “Amesema nikulipe pesa yote ya miezi
mitatu ndio tuendelee na kazi ili kichaa changu kikipanda, nikikunyanyasa tu,
anakuja kukuchukua.” Sabrina akacheka kidogo.
“Nitamwambia
huninyanyasi.” “Bora asikie kutoka kwako mwenyewe. Lakini hilo nimemwambia
halina shida. Tena nina nguo nataka kugawa. Nataka kubadilisha mavazi jamani!
Miaka nenda miaka rudi nguo hizo hizo! Sasa nataka wewe ndio uwe wa kwanza
kuchagua. Chukua zote unazotaka, zitakazobaki ndio nawapa wengine.” Sabrina
hakuamini.
“Chakula
chako kipo jikoni. Kama huna njaa, njoo uchague kwanza nguo wakati mimi
najiandaa na safari.” “Mbona njaa imeisha! Twende tu.” Wakacheka hapo koridoni.
“Ngoja nimwangalie Tino mara moja, halafu nakufuata dada yangu hukohuko chumbani
kwako.” Sabrina akarudi chumbani kwa Tino, Lela akaelekea chumbani kwake.
“Dada
anataka kunipa nguo. Naenda kuchagua, halafu nitarudi baada ya kumalizana naye.
Anaonekana anataka kusafiri leo. Sasa nataka wakati nachagua nguo, niulize na
maswali yooote ili tukibaki tusipate shida. Sitakaa huko sana. Unataka maji ya
kunywa kabla sijaondoka?” Akamuona amenyamaza kama anafikiria kitu. “Tino?”
Sabrina akamsogelea karibu. “Unafikiria nini? Au hutaki tubaki peke yetu?” Akakataa
kwa haraka sana. “Sasa ni nini? Au hutaki nikachukue nguo?” Akamuona amekunja
uso kidogo, akageuza kiganja kama anayesema hajui.
Sabrina
akakaa pale kitandani. “Nikwambie ukweli Tino?” Tino akakubali. “Ninashida sana
ya nguo. Manunuzi makubwa ya nguo na ya mwisho alinifanyia Emma kipindi nipo
naye. Na hiyo ni miaka mitatu iliyopita. Nguo ninazovaa hapa wewe unaziona.
Nyingi napata kwa Sabina. Huwa anazileta nyumbani, nachagua. Tokea namaliza
chuo, sijawahi kuajiriwa. Hapa naona kama mwenzio Mungu amenijibu. Acha nikaangalie
pengine nitapata vivazi vizuri hata siku tukitoka na wewe kwenda hospitalini au
saluni, popote pale nisikutie aibu. Sitakawia.” Tino akakubali. Akamnywesha
maji. “Unataka nikuache umekaa?” Akakubali. Sabrina akamuweka sawa, akatoka
akiwa amejawa furaha.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
S |
abrina akagonga
mlangoni kwa Lela. “Da Lela niingie?” “Ingia. Nguo zote nimezirusha kitandani.
Kazi kwako. Kuna watu wanapenda sana nguo zangu wao huwa nawauzia. Nikiwa
nabadilisha kama hivi, basi nawauzia. Watu wangu wakaribu huwa ndio nawapa bure.”
“Mbona nakushukuru dada yangu! Tena ni mpyaa! Mbona nimelala masikini nimeamka
tajiri!” Akafurahia Sabrina huku akiendelea kuchagua. “Sijui tamaa! Mbona kama
zote nimezipenda!” Lela akacheka. “Wewe tu na nguvu yako. Ulivyonifaa hivyo!
Hapa nishatangazia wambea wote kuwa nimeajiri mtu msomi na wa maana wakumlea
huyo Tino. Wakome kunifuata nyuma.” Sabrina akajua wanamsema hao wanaomuona
kwenye starehe.
Sabrina
akaendelea kuchagua. “Na hili gauni dada yangu?!” “Kabisa. Hilo nishaonekana
nalo zaidi ya mara tatu! Silitaki tena.” “Acha mimi nichukue. Nitakwenda kubana
kwa kufundi.” “Sasa kwa kuwa unaonekana wewe umependa zote, fanya hivi. Chukua
zote hamishia chumbani kwako. Zitakazo kukera au usizozipenda, zifunge kwenye
mfuko, tupia stoo. Nikirudi safari nitajua chakufanya.” “Kweli!?” Hakuamini
Sabrina. “Kabisa. Na mfuko ule pale nimekununulia zawadi yako. Naomba tufanye
kama ulivyosema. Akiugua huyo, kabla hujampeleka hospitalini, niambie ili mimi
ndio niwe nimetoa habari kwa watu. Akija mgeni kama ulivyosema, kabla
hujamfungulia mlango, nipigie simu. Niambie alivyo, nitakwambia kama umfungulie
au la. Usikubali maswali juu yangu na Tino. Waambie wanipigie mimi mwenyewe.
Sitaki umbea.” “Wala usijali dada. Naamini hakuna litakalo haribika. Kwani
unarudi lini?” “Usijali. Tutakuwa tukiwasiliana. Ukinihitaji tu, kama mshale
nitarudi. Ila ujue pakiwa na amani hapa, na mimi nitakuwa na amani huko.
Angalau na mimi nitulie mdogo wangu. Nimekuwa mimi mtu wa shida tu!” “Basi
usijali. Tutakuwa tukiwasiliana.” Akakubali Sabrina bila shida.
Akahamisha
vitu vyote alivyopewa chumbani kwake. Akafungua sasa hiyo zawadi kwenye mfuko.
Akakuta amemnunulia chupi nzuri sana. “7!” Sabrina akahamaki na kubaki ametoa
macho. Akaangalia moja hadi nyingine. Akakuta lotion nzuri, shower gel inayofanana
na hiyo lotion na body spray yake. “Yaani set nzima!” Akanusa. Akakuta
inaharufu nzuri, akaipenda. Sabrina akaanza kucheka mwenyewe. Nguo zenyewe
alizokuwa amepewa na Lela akisema amezichoka, ni kama zilikuwa mpya tu.
Akaziweka kwenye moja ya kabati la ukutani hapohapo chumbani, akatoka kwa
haraka kurudi kwa Tino.
“Mwenzio
nimepata nguo nzuri kweli! Ameninunulia na set ya lotion, sabuni ya kuogea na
body spray pamoja na nguo za ndani. Nzuri kweli! Nimefurahi.” Tino akamshika
mkono, lakini bila tabasamu usoni. Akarudisha macho kwenye luninga. Sabrina
akafikiria ni nini anachofikiria Tino. “Nakwenda kukuletea uji. Ni sawa?” Akakataa.
Akamwangalia usoni. Akamuona kama mtu aliyetingwa na mawazo. “Naomba
usinikatalie Tino! Unahitaji kula kwa ajili yako mwenyewe. Au hukupenda ule uji
asubuhi!?” Akakataa. “Sasa kama
ulipenda, kwa nini ukatae kunywa wakati kila siku nakupa uji asubuhi na saa
kumi?” Akabaki akimwangalia. “Hutaki kupona?” Akanyamaza. “Tino?” Kimya.
“Umekasirika?” Akamtizama na kuangalia pembeni.
“Naomba
hasira zikufanye upambane upone, Tino. Isiwe vinginevyo, tafadhali. Kasirikia
hiyo hali. Ichukie na ujiambie utakula chakula kwa kujilazimisha kama dawa,
utaanza mazoezi kuanzia kesho. Kwa nguvu zote, mpaka urudie afya yako. Mimi
nakwenda kuleta uji. Kama utanikatalia, basi.” Sabrina akatoka. Akaenda kuandaa
uji. Akaweka kwenye bakuli, akarudi nao chumbani.
Wakati
anamlisha, mlango ukafunguliwa. “Basi hivyo unavyomfanyia huyo, hatakaa
akapona. Anapenda kutumikiwa kweli huyo! Hapo kukuona huna unalofanya ila yeye tu,
ndio raha yake!” Akaongea Lela akiwa amesimama mlangoni. Sabrina kimya akiendelea
kumlisha. Akamfuta mdomoni. Akahisi pengine ndio maana Tino alikataa kula Lela
akiwepo, akijua atamsema. “Na kama utaendelea kumlisha vitu vya maji maji, ujue
utachezea kinyesi wewe, mpaka ukome.” “Naomba usiongee hivyo da Lela. Tafadhali
sana. Zaidi kwangu. Nimechagua mimi mwenyewe. Si Tino wala wewe mlioniomba.
Tafadhali usiwe na wasiwasi juu ya lolote.” “Sitaki uchoke mapema!” Akajirudi
Lela.
“Hapana
dada yangu. Naomba usiwe na wasiwasi. Tumekubaliana kwa miezi mitatu, ujue
nitasimamia makubaliano yetu. Sitawakimbia hata iweje. Naomba uwe na amani.”
“Basi kama ni hivyo sawa. Sitaki nije nionekane nimekuachia wewe shuruba yote.”
“Hapana. Na huna haja yakumwambia hata Sabina jinsi ninavyoishi hapa. Mwache
ajue tu kuwa mimi nipo hapa na Tino. Ni nini nafanya, haimuhusu.” Lela
hakuamini.
“Kwa
hiyo hata akikupigia wewe simu akikuuliza kama ndiwe unayemfuta mavi Tino
hutamwambia?” “Da Lela! Nawezaje kutangaza hivyo? Kwanza haimuhusu, na Sabina
hana muda huo na mimi. Ni mpaka mimi nimpigie. Na mimi si mlalamishi. Naomba
wewe usiwe na wasiwasi. Huna hata haja yakujitetea kwa Sabina kwa chochote.
Kwanza hata akijua, nimekuruhusu umwambie ukweli. Kuwa nimependa mwenyewe.
Hujanilazimisha.” “Hapo umenituliza. Kuwa ya hapa hayamuhusu mtu.” Akajirudi
Lela kwa unyenyekevu kama sio yeye.
“Kabisa.
Niliyoyakuta hapa, nitayaacha hapahapa. Hutanisikia nikisema chochote kwa
yeyote. Labda wewe mwenyewe.” “Hapo sawa. Angalau tuwe ukurasa mmoja. Nibakie
mimi tu ndio msemaji wa hii familia. Maana watu ni wambea kweli! Wivu tu.” “Usijali
dada. Mimi sitakuwa msambaza maneno hata kwa Sabina. Wewe niachie maagizo ya
nini unataka kifanywe.” “Ukiona nyumba ni chafu, inatakiwa kusafishwa, niambie
mimi. Kuna mama huwa anakuja kunisafishia na binti zake. Usihangaike kabisa.
Kufua naona unafua mwenyewe. Ukiona umechoka, niambie. Yupo kijana huwa
namwita, anakuja kufua na kupiga pasi.” “Labda za kwako tu dada, ili
nisikuharibie kama zina maelezo maalumu. Ila sitashindwa kufua kwa mashine na
kuzinyoosha mwenyewe.” Lela akacheka.
“Mbona
Mungu amenikumbuka mwaka huu! Nakushukuru. Haya, hospitalini huyo labda nipige
tena tufufue kliniki zake. Tena utakuwa umenisaidia. Ili maendeleo yake yatumwe
huko ofisini kwake, waendelee kutulipa. Maana mimi niliwaambia sitaweza kuwa
nakimbizana na mambo ya hospitalini, kumuuguza yeye na kazini kwangu. Tena
niliwaambia nikifukuzwa na mimi nawashitaki na wao. Ndio wakapoa.” “Wewe
utaniambia ni siku gani na muda wa kumpeleka huko hospitalini.” “Wewe unapenda
siku gani?” “Sijali dada yangu. Wewe tu.” Lela akazidi kufurahishwa na huo utayari wa Sabrina.
“Naona
wewe hutaniumiza kichwa! Basi nitampigia simu daktari wake, nitakujulisha ni
lini umpeleke. Tena kama utampeleka mwenyewe, nitawaambia wakulipe ya usafiri.
Maana walitakiwa kumtuma mtu aje amchukue huyo. Mimi niliwaambia siwezi. Yupo
kama mlemavu. Libaba lote hilo unaliingizaje kwenye gari! Ndio wakawa wanalipia
gari la hospitali, linakuja kumchukua na kumrudisha.” “Hamna tatizo. Wewe panga
kila kitu, kisha unijulishe.” Akamuona anaandika kitu kwenye simu yake.
“Kabla
sijasahau dada yangu.” Lela akatoa macho kwenye simu na kumuangalia. “Hivi huwa
ulikuwa ukimpeleka saluni gani? Naona kabla sijamrudisha hospitalini,
akapunguze nywele.” “Walikuwa wakimkata haohao vijana waliokuwa wanakuja
kumsafisha mavi. Wanamkata, nawalipa.” “Sasa kwa kuwa mimi siwezi, naomba
nimpeleke saluni.” “Akijinyea huko saluni utafanyaje naye huyo? Si aibu tupu?
Wewe mkate tu vyovyote au mkate kipara kabisa wote tupumzike.” “Wewe niachie
hilo mimi. Wala usijali. Nielekeze saluni aliyokuwa akienda, na wanayowezea kupunguza
aina hizi za nywele zake na wanaojua mitindo yake. Ili nikienda naye
hospitalini, wakusifie dada yangu. Kuwa unamtunza vizuri.” Hapo akagusa moyo wa
Lela.
“Naona
wewe ndio kiumbe pekee unayenitakia mema. Nashukuru mdogo wangu. Maana
wakiniona tu mtaani, utasikia Tino umemuacha wapi? Wanataka nimbebe mgongoni!
Umbea tu na unafiki kuingilia mambo ya watu. Sasa safari hii nimewafunga mdomo.
Kabla hawajaanza umbea wao, nawaambia nimemtafutia Tino mtu mzuri wa kumtunza,
ili akija kufa wasije nisingizia kuwa simtunzi, ajifie mwenyewe.” Akamuelekeza
ilipo saluni huku Sabrina akitamani kumfunga mdomo. Akamuhurumia Tino, akajua
ndio maneno anayoyasikia kutoka kwa mkewe kila akifungua mdomo wake. Lela hakuwa
na jema hata moja linalomtoka mdomoni juu ya mumewe!
“Na
pia ili usikae sana pale saluni tukaingia wote aibu akianza haja zake huyo, siku
ukitaka kumpeleka, niambie ili niwapigie simu kabisa ili wasikuweke. Wote pale
washikaji zangu. Walishanizoea kipindi hicho cha uhai wake huyo. Nilikuwa nikienda
naye pale, nakaa mpaka wammalize nikiwepo mwenyewe. Sikutaka wale wasichana wa
pale wanaojidai kuosha wanaume za watu, waanze mambo ya ajabu. Wanizunguke,
waanze kuchezea pesa yetu. Maana wanawake wa mjini nawajua mimi. Utaishia wewe
kuitwa mke, wenzio wanashika waleti ya mumeo! Sitaki ujinga.” “Basi
nitakwambia. Ila itakuwa siku moja kabla ya kwenda hospitalini, na naomba
isichukue muda mrefu. Kichwa kinamuwasha Tino.” “Muongo huyo! Wala
usimsikilize. Walikuwa wakimuosha kichwa kila wakati na..” “Na naomba unisaidie
picha yake ya zamani. Angalau nijue mitindo yake ya zamani. Wakimkosea, nijue.”
Akamkatisha kwa haraka.
“Sijui
hata sura yake ipo wapi hapa ulimwenguni! Maana nahisi ana miaka mingi hajapiga
picha. Kabla hajaanza matatizo yake yakujitafutia mwenyewe mpaka akafungwa na
baada, sidhani hata kama alipiga tena picha. Na usimuone hivyo huyo, mbishi
kuliko shetani. Hashauriki huyo, ndio maana amejifikisha hapo. Ni kwa kujitakia
mwenyewe!” “Inamaana hamna hata albamu zenu za zamani! Picha za harusi au zozote
tu?” “Tino wa wakati ule hatakaa akarudi hapo. Hata umpeleke saluni za
mbinguni! Kwisha habari yake. Wewe mpeleke wakampunguze tu nywele, hamna
watakachokifanya kwenye hicho kichwa na sura wakamtoa Tino yule.” “Sawa.
Nitafanya hivyo. Mambo mengine nitakupigia. Nisikucheleweshe.” Sabrina akaona
aondoke tu pale.
“Bahasha yako hii hapa.” Akaweka juu ya meza. “Asante.” “Mimi ndio nikushukuru. Na naomba usisahau kumwambia Sabina kuwa nimekulipa pesa, na nikakupa nguo nzuri sana, kisha nimekupa zawadi nzuri sana nilizokununulia kwa pesa yangu mbali ya malipo ili ajue nakujali.” Sabrina akashangaa na kuumia moyoni. Kumbe tena anatangazwa! Akapoa kidogo kama aliyeshikwa na ganzi ya gafla. “Lakini usijali. Nitampigia wakati nipo njiani, nitamwambia kila kitu. Akikupigia kukuuliza, naomba mthibitishie.” “Sawa.” Akajibu kwa kuishiwa nguvu.” “Funguo za gari zipo zimening’inia pale kama unaingia hapa ndani. Pesa za matumizi ya hapa ndani ni kama hutahitaji kabisa. Maana nimenunua kila kitu ninachojua kitahitajika hapa, kwa hiyo hutahitaji pesa kwa mambo ya hapa ndani. Gari limejaa mafuta. Na umeme huwa nanunua wa mwezi mzima. Hamtakuwa gizani. Maana ukikatika, jenereta linajiwasha lenyewe. Ila pesa zako zote nimeweka hapo juu. Tutawasiliana endapo utakwama popote. Kwanza nitakuwa nikikupigia.” “Sawa dada. Nashukuru.” Lela akatoka.
Maisha ya
Tino na Sabrina peke yao.
T |
ino akawa
amemuona. Akamshika mkono. Sabrina akacheka kidogo huku ameinama. “Uji utakuwa
umepoa. Acha nikaupashe, uje umalize.” Sabrina akatoka bila kumtizama.
Alishaumia moyoni. Akajua kumbe Lela anafanya ili ajulikane kwa watu sio kwa
moyo wa shukurani kama alivyomwambia! Inamaana kila mtu atajua amechukua nguo
zake! Akakereka sana rohoni asijue ni nini cha kumkera hivyo! Asijue alishaanza
kukerwa na Lela tokea aanze kumsikia akimsema vibaya Tino aliyekuwa mgonjwa.
Alikusudia asiingilie mambo yao, kwa kuwa hakuwa akijua uhalisia wa ndoa yao
japo Sabina alishamwambia kwa sehemu, lakini akakuta moyo umelemea kwa Tino
mgonjwa. Lela akaanza kumkera. Akachukia kuwepo tena pale, akaona historia ya
kama nyumbani kwao inajirudia. Hakuna anayethamini anachokifanya kwa juhudi ila
kumtumia vibaya. Akatamani iwe vinginevyo hata kuwepo sehemu ingine isiwe hapo
au nyumbani kwao, ila kwa ajili ya Tino, akaamua ajitulize hukohuko jikoni,
arudi akiwa ametulia. Akanywa maji ya baridi, akatulia.
Aliposikia
mlinzi anafungua geti kisha na kufungwa, akajua ndio Lela ameondoka. Akapumua
kwa nguvu. Akarudi chumbani kwa Tino. Akapokelewa na macho ya Tino. “Malizia
uji, baadaye nitakupa chakula. Au unaanza kusinzia?” Tino akakataa. “Utapona
Tino. Na naomba usiache kujisaidia kwa hofu. Ukiweza kujua kama unataka
kujisaidia, niambie. Haja ikitoka bila kujua pia naomba usijisikie vibaya.
Nitakusafisha. Sawa?” Tino akabaki mpole. “Na kabla hatujaenda saluni
nitahakikisha unajisaidia kwanza, halafu nitahakikisha unavaa diaper ili
usijichafue mbele ya watu. Na nitakuwepo pale. Nikisikia tu harufu kama haja
itatoka, nitakurudisha kwenye gari, nitakusafisha. Nakuhakikishia hutaingia
aibu. Usiogope. Sawa?” Kimya akiwa amepoa.
“Lazima
kukubali kutoka hapa. Huwezi kujifungia daima Tino. Sio sawa kwa afya yako na
akili yako. Mimi sijui ulikuwa nani zamani. Ulikuwa na hadhi gani! Lakini Tino,
yapo mambo hatuchagui kwenye maisha, yanakuja tu. Sasa jinsi ya kukabiliana
nayo ndio kipimo cha ubinadamu. Kama wewe ni jasiri au la. Muangukaji na hukai
chini au unayekubali kushindwa. Hata kama umesikia kwa muda mrefu sana kama
hutapona, naomba amini kwa upya. Usijifiche, na wala huna chakuona aibu. Hujui
utakuwa msaada kwa wangapi watakaokuona ulianguka, unapambana na utarudi
kusimama. Na mimi nipo na wewe, sitaacha uaibike nje. Nitakusitiri, hutatembea
na uchafu. Sawa?” Akakubali na kutaka amshike mkono.
Sabrina
akafurahi, akamshika mkono na kuubusu ule mkono wa Tino. “Utakuwa sawa tu Tino.
Jipe muda.” Akakubali. Akamalizia kumnyesha uji wote. Akamfuta vizuri, akarudi
kukaa pembeni yake. Safari hii bila hofu. Akakaa karibu kabisa na alipokuwa
amekaa Tino hapohapo kitandani. Wakatulia wakiangalia tv. Baada ya muda akamhisi
anataka kushika. Akamwangaia, akumuonyesha kwa macho anamwita. Sabrina
akafikiria kwa haraka. “Unataka ujisaidie?”Akakataa. “Maji ya kunywa?” Akakataa.
“Akafikiria tena. “Nikulaze?” Akakubali. “Ila nakupongeza. Umekaa muda mrefu!” Akamuona
anatabasamu.
“Kesho
tunaenda kukaa sebuleni. Sawa?” Akazungumza naye huku akimuweka sawa.
Akakubali. Akampanga hapo kitandani vizuri. “Upo sawa?” Akakubali. “Unataka
kitu chochote?” Akakubali. “Maji ya kunywa?” Akakubali kwa haraka, Sabrina
akacheka na kutoka. Akakutana na chakula alicholetewa na Lela. Akatamani kuzira
kula, lakini akajiambia ni pesa ya Tino, acha na yeye aile.
Usiku
huo baada ya wote kula, akaenda kuoga chumbani kwake. Akakutana na zile nguo za
Lela. Akafikiria. Akajiambia hapana. Akazikusanya zote. Akajiambia hata kama ni
masikini, hajatembea uchi. Akazifunga sehemu moja. Akaenda kuziweka stoo kama
alivyoambiwa, akarudi kuoga. Akajifunga kanga yake, na kuvaa tisheti yake aliyochagua
yakulalia usiku. Akatoka na mto wake bila shida wala wasiwasi akijua atakwenda
kulala chumbani kwa Tino. Akachukua na shuka, akarudi kwa Tino. Akaingia na
kuweka ile mito na mashuka kwenye kochi, kisha akamsogelea Tino. Alishamuosha
na kumpaka dawa tayari kwa kulala. Kama kawaida yake aliacha kumvalisha soksi
miguuni kama kitu cha mwisho chakumbembelezea.
Akapanda
kitandani Tino akimwangalia. “Upo sawa?” Akamuuliza kwa upole wakati anapanga
miguu yake mapajani kwake. Tino akakubali. “Nikuulize kitu Tino?” Akakubali.
“Hujisikii hamu ya kunywa juisi baridii? Maana nimekuwa nikikupa maji tu.
Nimeona kwenye friji kuna juisi nzuri mpaka za nyanya na zimeandikwa ni za
asili. Ungependa kunywa? Usiogope mkojo, nitakupa chupa ya kujisaidia kabla
kujalala na nitakusafisha tena mdomo. Hutalala na meno machafu.” Akakubali.
Sabrina akatoa ile miguu mapajani
kwake na kutoka. Akarudi jikoni kwenye friji. Akaanza kusoma zile juisi.
Zilionekana za gharama na zote ziliandikwa zinaongeza Vitamin C na nguvu. Akachukua
juisi ya stafeli. Alishaambiwa huwa inavirutubisho vyakuponyesha magonjwa mengi
tu. Akamuwekea kwenye glasi pamoja na mrija, akarudi nayo chumbani. “Lini
utaanza kuzungumza na mimi Tino?” Akauliza taratibu wakati akimnyeshwa hiyo
juisi. Tino akamtizama tu. “Umependa juisi?”
Akakubali kwa kutingisha kichwa taratibu. “Naomba uanze kujaribu
kuzungumza Tino. Nitajua ni hatua ya kwanza, uliyokubali kuchukua kufikia
uponyaji.” Akakubali. Sabrina akafurahi sana. “Asante Tino.” Akampa hiyo juisi
mpaka akamaliza.
Baada
yakumsafisha kinywa, na kujisaidia, akarudi kukaa miguuni. Akaanza kumchua
taratibu, Tino akimwangalia kwa utulivu. Macho yakagongana. “Unafikiria nini?”
Sabrina akamuuliza huku akiendelea kumchua taratibu. Akatingisha kichwa
taratibu kukataa. Sabrina akacheka na kuendelea kuminya miguu yake, akivuta
vidole. “Umeanza kuhisi hata kidogo upande wa kulia?” Akakubali. “Kweli!?” Sabrina
akashangaa. Akakubali. “Tuendelee kuomba Tino. Mungu atakuponya tu.” Akakubali.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walikaa
hapo kwenye hilo jumba wao wawili tu. Amani na kubembelezana kama Sabrina
hakuwa amemsikia Lela. Siku ya kwanza na ya pili hakumtoa chumbani. Ila
akaendelea vilevile kumfanya akae kwa muda mrefu zaidi. Siku ya tatu baada ya
kuamka usingizi wa pili wa asubuhi. Kama kwenye saa nne hivi, Sabrina
akamsogelea pale alipokuwa amelala. “Leo nataka utoke hapo kitandani Tino.
Tujaribu tu, naamini tutaweza kufika sebuleni. Nitakuweka kwenye kigari chako.”
Akafikiria kidogo, akakubali. “Itakuchangamsha akili.” Akamsogezea kile kigari.
Kazi ikawa kumsaidia kutoka hapo kitandani kuhamia kwenye hicho kigari. Upande
wa kulia haukuwa na nguvu sana.
Sabrina
akajaribu mara ya kwanza, ya pili na ya tatu akashindwa kumuhamishia kwenye
kigari. Akamrudisha kitandani, akabaki akifikiria. Tino akamkatalia. “Lazima ipo
njia wanatumia kwa watu kama wewe Tino. Wewe sio wa kwanza. Naomba nipe muda
wakufikiria.” Tino akabaki akimtizama. Akachukua simu yake akaanza kutafuta
google na kuangalia video Youtube jinsi
yakumuhamisha mtu kama yeye. Akagundua kuna vifaa maalumu. Ila wengi wanatumia
misuli ya mapaja sio kiuno ili wasiumie na pia kuwa na nguvu nyingi.
Akaweka
kiti upande utakao kuwa rahisi kumuweka. “Nikumbatie kwa kuweka mikono juu ya
shingo yangu. Nitakuwa upande wa kulia ambao hauna nguvu nyingi, na wewe
nisaidie kwa kadiri utakavyoweza. Tukifanikiwa kusimama, tutageuka pamoja, pole
pole mpaka kwenye kigari chako. Umenielewa?” Tino akakubali. “Usiogope,
sitakuangusha. Taratibu tu mpaka tutaweza.” Akakubali. Akamvuta mpaka mwisho
kabisa ya kitanda. Madonda yote yalikuwa yamekauka. Ila ndevu zilikuwa ndefu
sana kuzunguka uso mzima hata sura yake ilikuwa ngumu kumtambua ni mwenye uso
wa namna gani! Kwa ufupi alikuwa akitisha.
Akamuweka mikono shingoni, akahesabu mpaka tatu, akamvuta juu akiwa amemshika kiuno. Wakasimama. “Upo sawa?” Akanyanyua uso akimtizama. Akamuhisi anatetemeka sana. “Pole Tino. Naomba usiogope. Sitakuangusha. Tugeuke taratibu, utaweza tu. Umefanya vizuri sana.” Wakafanikiwa kugeuka, akiweka nguvu nyingi kwenye ule upande dhaifu. Wakafikia kigari. Akamkalisha taratibu, hata Sabrina mwenyewe hakuamini kama wameweza. Akaanza kucheka. “Nipe tano Tino. Umefanya kazi nzuri sana.” Wakagonga mikono. Akamtoa hapo chumbani.
Sabrina
afanikiwa kumtoa Tino Kitandani.
“Nakuzungusha
nyumba nzima, uone, ndipo ukae sebuleni. Sijui mara ya mwisho ni lini
ulipotoka!” Tino kimya akiangaza macho. Akamtembeza nyumba nzima, akamrudisha sebuleni.
“Umefurahi?” Akamuona anataka kumshika. Akajua amefurahi. Akafanya vilevile kumuhamishia
kwenye kochi. Ikawa rahisi tu. Akampangia mito. Kwa mara ya kwanza baada ya
muda mrefu, hatimaye Tino akafanikiwa kurudi kukaa sebuleni tena wima.
“Ukichoka nitakulaza hapohapo. Tunarudi chumbani usikuuu! Utaweza?” Akamuuliza
huku akicheka. Akashangaa Tino amekubali. Akajua amefurahia.
Walishinda
hapo sebuleni siku nzima. Mara nyingi Sabrina alikaa chini ya miguu akimfanyia
masaji ya misuli ya miguu. Akajisaidia hapohapo sebuleni. Akamsafisha. Alimlisha
hapohapo, ilipofika usiku akamrudisha chumbani. Safari hii akaenda naye mpaka
bafuni. Akamsafisha kinywa akiwa amekaa kwenye kigari chake ameegemea sinki.
Akamuosha juu na kumvalisha nguo ya juu ya kulalia akiwa palepale bafuni
amekaa. Ndipo wakahamia kitandani. Akamalizia kumsafisha chini na kumvalisha
akiwa amemlaza kitandani, alipomaliza akamfunika. Hakuchukua muda mrefu,
akalala kabisa. Sabrina akajua alichoka kukaa, ni kitu hakufanya muda mrefu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kesho
yake akafanya hivyo hivyo kumtoa kitandani. Ila kwa kuwa alikuwa ameshajifunza
jinsi ya kumtoa kitandani, safari hii hakupata shida. Wakahamia sebuleni. Mpaka
siku hiyo na muda huo Lela hakuwa amemtafuta hata kwa kuwajulia hali! Na yeye
akaona amwache tu, asije akalalamika anamsumbua. Jumapili nayo akamtoa mpaka
nje. Akamuona wazi amefunguka mpaka usoni. Akamuacha kwenye kigari chake, yeye
akakaa pembeni, chini kwenye ukoka. Tino akawa akiangaza macho.
“Ukichoka
niambie nikurudishe ndani.” Akakubali, akaendelea kuangalia. “Unataka
nikuzungushe mpaka nyuma ya nyumba?” Akakubali kwa haraka akitingisha kichwa.
Sabrina akamtembeza kuzunguka nyumba nzima akimsukuma kwenye kigari chake.
{Wheelchair}. Hiyo nyumba ilikuwa imezungushiwa ukuta mkubwa sana, huwezi kuona
nje. Na walikuwa wao tu wawili na mlinzi kwenye kibanda cha getini.
Pasafi
na ukuta wenyewe mzuri. Umejengwa na kuweka marembo mazuri. Maua mengi na
vyungu vya maua vyakuvutia vikitangaza utajiri wa wanandoa hao. Ukweli Lela
alijua kutunza nyumba yake. Msafi ndani na nje. Sabrina mwenyewe akazidi
kuvutiwa. “Mnanyumba nzuri sana Tino. Na da Lela anajua kupatunza!” Tino kimya.
Akamuacha nje kama lisaa, akaamua kumrudisha ndani baada ya kumnywesha maziwa
na kukaa tena kidogo. “Umefurahia?” Akamshika mkono, ishara yake yakushukuru.
“Karibu.” Sabrina akajibu akicheka.
Akamrudisha
tena kwenye kochi. Akamuwekea mito ili asiumie. Akakaa pembeni yake. “Naomba
niongeleshe kitu chochote Tino.” Akamuona anatabasamu. Akafikiria kidogo, “Asi-an-te.”
Sabrina akashangaa sana. “Tino wewe! Kumbe unazungumza! Sasa kwa nini hutumii
maneno?” Akacheka tu. “Tino?” Akamwangalia na kucheka tena kidogo. Wazi siku
hiyo alionekana amejawa furaha. Hata aina hiyo ya uchekaji, Sabrina hakuwa
amemuona. Alicheka angalau meno yalionekana. “Unatabia mbaya Tino!” Wakazidi
kucheka. Akamfuta mate yaliyokuwa yakidondoka, gafla akapoa. Akajua pengine
ndio sababu.
Akamvuta
mkono. “Naomba usijali juu ya haya mate yanayodondoka Tino. Naamini baada ya
muda utakuwa sawa.” Akamtizama na kunyamaza. “Niambie sawa.” “Saa-waa.” Sabrina
akacheka. Hiyo siku nayo wakamalizia hapo sebuleni. Hapakuwa hata na hodi siku
hiyo ambayo karibu watu wote hawaendi kazini. Mchana wakati amekaa kwenye kiti,
Sabrina alimkwangua tena mba taratibu huko kichwani mpaka akalala hapohapo.
Akamfunika vizuri na kumuacha amelala huku amekaa.
Alilala
mpaka usingizi ukamuisha mwenyewe bila ya kuamshwa. Sabrina alipomuona
amefungua macho akamsogelea. “Nimefikiria Tino.” “Nii-nii?” Sabrina akashangaa
ameongea bila kuombwa. Akaendelea. “Kwa kuwa da Lela hajapiga simu. Naona
twende tu saluni kesho. Nywele na ndevu vimeanza kutisha. Nyusi ndio zimefunika
macho kabisa, huonekaniki! Si umejiona pale bafuni?” Akakubali. “Na kama hutaki
kurudi kwa wale waliokuwa wakikufahamu ukiwa mzima, tunaweza kwenda kwengine.
Ukachagua staili yako unayotaka wakunyoe, ukipata nguvu, tutarudi kule
walipokuzoea.” Akakubali kwa haraka.
Sabrina na
Tino saluni.
K |
wa kuwa
alishajua njia zakumtoa kitandani kwa urahisi, hakupata shida kumuweka garini. Alilisogeza
hilo gari aliyoachiwa aitumie mpaka karibu kabisa na mlango. Alihakikisha
amemlisha vizuri, na kushiba. Amejisaidia. Akamvalisha nguo safi, soksi na
viatu, raba, na vyote vilikuwa vya Nike. Nzuri sana. Sabrina mwenyewe akapenda.
Alionekana ni mtu aliyejijali sana. Sabrina akajifungulia geti mida hiyo ya saa tano asubuhi siku ya
jumatatu, akatoa gari nje, akiwa amemfunga
mkanda hapo kitini, ametulia tuli akijiangalizia anayoyafanya Sabrina.
Akaegesha gari nje, akarudi kufunga tena geti, ndipo akarudi garini.
“Nimesahau
kumpigia simu da Lela kumtaarifu kama tunatoka!” Tino kimya. Akaondoka hapo
taratibu akiwa amevaa nguo zake zilezile za kawaida tu alizokuja nazo na
sendozi. Akampeleka kwenye saluni aliyokuwa akiifahamu, aliyokuwa akiipenda
sana Emma, mpenzi wake wa kwanza, maeneo ya Sinza. Alijua hapo watamnyoa Tino
vizuri. “Tino, ni sawa wakati wakikushugulikia na mimi niende madukani, pale
pale karibu na saluni? Angalau nijinunulie nguo mbili hivi nipate za kutokea na
viatu? Sitakuacha muda mrefu.” Tino akakubali.
Akaendesha
mpaka hapo saluni. Sasa kwa kuwa pale saluni palikuwa na ngazi, Sabrina
akamuacha ndani ya gari, yeye akaingia ndani. Akazungumza na vijana aliowakuta
pale, wote walikuwa wageni kwake lakini mmoja wao akakubali kutoka naye kwenda
kumsaidia kumleta Tino ndani. Sabrina akashukuru sana. Tino akamuona Sabrina
anatoka na kijana. Akafungua mlango. “Tino! Huyo anaitwa Dula, amekubali
kukunyoa na kutusaidia kuingia ndani.” “Asa-nte.” Tino akamshukuru Dula. “Hamna
shida Mkuu.” “Lakini naomba tuwe makini.” Sabrina akatoa angalizo. Mara akatoka
kijana mwingine. “Acha tukusaidie sista.” Sabrina akashukuru sana. Hata
hawakutaka kutumia kigari. Wakambeba kwa kumnyanyua chini ya makwapa, kila
mmoja upande wake, wakamwingiza ndani mpaka kwenye kiti cha saluni.
“Naomba
niwaachie namba yangu. Akinihitaji tu, mnipigie. Nitakuwa hapa karibu,
madukani. Sitakawia.” Wakampa karatasi, akaandika. “Sitakawia Tino. Nitarudi.
Lakini kwanza naomba mitindo yenu achague anachotaka. Wakamgeuza kwenye kiti,
wakamuonyesha picha za ukutani. “Lakini kwa hizo nywele na hizo ndevu, huu
mtindo utakufaa broo!” Kinyozi akamchagulia. Tino akamgeukia Sabrina kabla ya
kukubali, Sabrina alipocheka baada ya kuangalia vizuri na yeye, ndipo na yeye
Tino akaukubali. Ulikuwa mtindo mzuri. Alipoona pako sawa hapo saluni,
akaondoka kwenda madukani.
Akaanza
kuzunguka madukani akiwa amejawa furaha zote. Sabrina huyu alikuwa amelipwa
mshahara wa miezi mitatu. Hamu yake ni kubadili nguo. Angalau hata tatu tu. Baada
kama ya dakika 20 hivi akawa anarudi pale saluni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
W |
akati
anakaribia mlango wa saluni, akakutana na Emma amebeba mtoto wa kiume. “Sabrina!”
“Ni mimi Emma. Habari za siku?” Sabrina akauliza huku akimtizama yeye na mtoto aliyebeba,
akajua wazi ni wake. “Naona hujabadilika kabisa Sabrina! Vipi!?” “Safi tu. Hongera
naona ulijaliwa na kijana mkubwa tu.” Sabrina akaongea kwa utani. “Wewe si
uliniringia ukijua nakutania, sijui! Ikabidi nioe. Na Mungu akanijalia mtoto.
Nikajua sasa hivi utakuwa umeolewa, kumbe upo vilevile na nguo zilezile
nilizokununuliaga mimi! Ona hasira na moyo wakutosamehe ulipokuacha? Umebaki
palepale na kukosa bahati nzuri ya ndoa.” Sabrina akamshangaa sana Emma.
“Una
nini wewe Emma!? Nani amekwambia najuta kutoolewa na wewe!?” “Kama hujuti basi
unalo tatizo, na nikilema hicho Sabrina. Hivi unakumbuka huu ni mwaka wa ngapi
tokea nikuache?” Sabrina akabaki na mshangao ametoa macho, akijua wazi ndani wanasikia.
Maana walikuwa nje ya mlango. “Kama umesahau jua huu ni mwaka wa tatu na miezi mitano
na siku 12, tokea ukubali hasira zikutawale, ukakataa ndoa. Pengine kama Mungu
angekujalia kizazi na ningekuoa mimi sasa hivi huyu mtoto angekuwa wako. Na hizo
nguo ungekuwa umebadili. Umebakia na vitu vilevile nilivyokununulia ila
ukachoka zaidi, na nywele ukarudia ile mitindo yako ya zamanii! Mwanamke gani
bado kwenye karine hii unasuka mitindo hiyo?” Sabrina akabaki ameduaa kama
amefumaniwa.
“Shauri
yako! Miaka nenda, miaka rudi utabakia umepauka hivyohivyo! Ulichezea bahati
sana wewe!” Emma na mwanae wakaingia ndani. Baada ya sekunde kadhaa kama akili
ikamrudia Sabrina, na yeye akaingia ndani. Akakuta Emma akisalimiana na wale
vinyozi, Tino anasafishwa. Akamsogelea pale kwenye sinki. Wazi alikuwa
amebadilika usoni. “Vipi, yupo sawa?” Akamuuliza anayemuosha. “Tumemaliza.
Ninauhakika utamsahau.” Sabrina akacheka kwa kujilazimisha, Tino akafungua
macho. “Nimerudi Tino. Nakaa pale kwenye makochi.” Akakubali.
Mwili
mzima wa Sabrina ulikuwa ukitetemeka kwa hasira. “Niambie mtoto mzuri, ajira
wapi?” Emma akamuuliza kwa kejeli huku akicheka. Sabrina akamwangalia na kuamua
asimjibu. “Nilijua tu hukupata ajira! Si nilikwambia wewe masomo unayosomea na
dunia inapokwenda! Ninauhakika unanikumbuka sana wewe Sabrina.” “Sidhani kama nimekufikia
wewe, Emma. Wewe unahesabu siku tokea nikukatae!” “Ni kwa kuwa tu nina
kumbukumbu nzuri.” Akapinga, Sabrina akamtizama kwa kumsuta.
“Wengine
tulijaliwa kumbukumbu nzuri na za haraka.” “Niambie ni muda gani tokea umuoe
mama wa huyu mtoto? Nitajie kama ulivyonitajia mimi muda kamili tokea nikatae usinioe.”
Akababaika kidogo. “Lakini hayakuhusu.” Akajikaza na kujibu kibabe. “Unajua
nini Emma, ningekuwa sikufahamu wewe, ungefanikiwa kuniharibia siku yangu.
Lakini kwa kuwa nakufahamu vizuri, ninauhakika huko ulikokimbilia anakukimbiza
mchakamchaka ndio maana bado unanikumbuka mpaka mavazi yangu. Na pia ndio maana
upo hapa siku na muda wa kazi kumleta mtoto mdogo hivyo anyolewe nywele, na si
mama yake.” “Majukumu ni kugawana!” Akajitetea Emma.
“Si
wewe Emma. Na nilikwambia utanikumbuka tu. Ila nikwambie kweli Emma, hata kama
unaniona nipo dhaifu namna gani. Sijafanikiwa kama hivyo wewe, ila Mungu
amenipa amani na utajiri zaidi yako Emma. Sizunguki kutafuta nani nilimsaidia
nani namdai. Sina umasikini huo.” “Kwa kuwa huna ambaye umemsaidia.”
“Usingebaki ukinikumbuka Emma. Au usingerudi kunibembeleza unioe na kunitumia
marafiki zako wakuombee msamaha.” “Walijipendekeza wenyewe kwa kuwa walitaka
nikuoe wewe.” “Sawa Emma. Ila nakuhurumia na ninaomba Mungu afanikishe nafsi
yako na roho kama hivyo unavyojionyesha umefanikiwa.” “Sijionyeshi, ni kweli
nimefanikiwa.” Sabrina akanyamaza, hakujibu tena.
Emma
akaendelea kuzungumza kwa jazba akimsema vibaya Sabrina, watu wote pale ndani
wakawa kimya. Akabaki akiongea peke yake. Mmoja akaongeza sauti ya redio. Emma
akakasirika sana. “Hiyo ni dharau kubwa sana. Unajua nafahamiana na Dula mwenye
hii saluni? Nimeanza kunyoa hapa zaidi ya miaka 7. Tokea nyinyi wote hamjaanza
kufanya kazi hapa. Muulizeni Sabrina.” Sabrina akanyanyua uso na kumtizama kwa
mshangao. “Sista naona sisi tupo tayari.” Akabaki na mshangao alipomtizama
Tino. Tino huyu hakuwahi hata kumdhania kama ndivyo alivyo. Alibadilika na
walimtengeneza ndevu zake vizuri sana. Ukatengenezwa mustachi mzuri uliotoa
manywele yaliyokuwa yamefunika midomo yake, basi hiyo midomo ikawa kama ya
mtoto wa kike maana ilionekana ya rangi ya pinki kama aliyepaka rangi ya
midomo! Ikamfanya avutie zaidi. Mpaka macho mazuri ya rangi ya ugoro safi
iliyozungushiwa nyeupe nzuri yakaonekana baada ya kupunguzwa mpaka nyusi
zilizokuwa na zenyewe nyingi sana. Sabrina hakuamini.
“Umependeza Tino! Kama sio wewe!” Akamuona ametabasamu. “Asanteni sana.
Nashukuru kwa kila kitu.” Emma akawa amepoa kidogo akiangalia kinachoendelea.
Akatoa pesa, akawalipa na ya shukurani. “Msaada tafadhali ili tuondoke.”
Sabrina akaongea huku akitoa tabasamu la heshima. “Bila shaka sista.”
“Asanteni.” Akamsogelea Tino. “Upo tayari?” Akakubali. “Umependeza sana Tino!”
Bado Sabrina hakuwa akiamini kama ni Tino. Alitokea wa tofauti kabisa.
Akakumbuka maneno ya dada yake kuwa moja ya kitu alichovutiwa nacho lela kwa
Tino ni uzuri. Hapo akaamini.
Vijana
wawili akiwepo aliyemnyoa Tino ambaye na yeye ni Dula kama mmiliki wa hapo,
wakaenda kumnyanyua Tino pale kitini kumpeleka garini.” Emma akacheka kidogo.
“Nimeelewa sasa.” Sabrina akamtizama. “Kumbe mwenzangu upo kazini hapo!”
Sabrina wala hakujibu. Akatoka kuwafuta. Akafungua gari, na kukimbilia mlango.
Wakamwingiza ndani. “Jamani kaka zangu nawashukuruni sana. Na Mungu awabariki.”
“Bila shaka dada. Wewe ukitaka apunguzwe tena, mlete tu. Usiache mpaka zikawa
kubwa tena.” “Sitajisahau tena. Nitamrudisha baada ya muda mfupi tu.” Sabrina
akaaga, wakaondoka.
“Asa-ntee!”
Tino akavunja ukimya baada ya kumuona Sabrina anaendesha, mawazo yapo mbali
kabisa na pale. Akageuka, akampa tabasamu wazi alijua hayupo pale. “Umekuwa
msafi Tino! Umependeza sana! Tukiendelea kusafisha kichwa kikiwa hivyo mba wote
utaisha kwa haraka, miwasho itaondoka.” Alipomaliza tu hivyo, akaendelea
kuendesha bila ya nyongeza. Hakuzungumza tena mpaka wanafika nyumbani akafanya
kama alivyotoka. Kujifungulia geti na kuingiza gari, kisha kurudi tena kufunga
geti. Hiyo nyumba ilikuwa na ulinzi masaa 24, kutoka kwenye kampuni ya ulinzi
ambayo Tino alikuwa akilipia na silaha. Kwahiyo hiyo nyumba ilikuwa na askari
wenye silaha wakati wote. Lakini Lela aliwafukuza na kuwaambia hawana
wanachokifanya, wanakula tu pesa yao. Akatafuta mlinzi wake wa kawaida, wale wa
kulinda na mshale wakisaidiwa na filimbi. Anakuja kulinda hapo usiku asubuhi
anaondoka.
Akamtoa
Tino pale kitini peke yake akihangaika naye bila msaada. Akamuweka kwenye
kigari chake. “Kuna joto sana Tino, labda nikutoe jioni. Sasa hivi ukapumzike
ndani.” Tino akakubali. Akamsukuma mpaka ndani. “Unataka ujaribu kujisaidia?” Akakubali
kwa haraka. Sabrina akakimbilia chooni, akaleta vifaa vyote. “Unataka namba
mbili pia?” Akakataa. “Hutaki tujaribu?” “Si sa-asa.” Sabrina akacheka kidogo.
Akamuwekea chupa, akajisaidia haja ndogo. “Diaper kavu kabisa! Tuongeze kunywa
maji Tino.” Akakubali. Akamuhudumia vizuri kwa haraka, akampanga kwenye kochi.
Akampa maji.
“Acha
nimjulishe da Lela. Nilimuahidi kuwa nikimwambia kila kitu. Sijui huu ni wakati
mzuri wa kumpigia! Au nitume ujumbe?” Sabrina akawa anajiuliza taratibu wakati
akimlisha matunda Tino. Tino kimya. “Naona nitume ujumbe.” Akakubaliana na wazo
lake. ‘Da Lela, nimefanikiwa kumpeleka Tino saluni. Tulikwenda
salama na ndio tumerudi salama.’ Akatuma huo ujumbe. Hapo hapo Lela
akapiga. “Sasa mbona hukuniambia ili niwajulishe wale vinyozi
mimi mwenyewe!?” Lela akalaumu kidogo kama aliyenyimwa sifa. “Sikwenda kule dada, kwa kuwa sikutaka kukusumbua. Niliona
kimya. Nikampeleka kwengine. Samahani kama nilikosea.” “Hamna neno. Nilijua
ulimpeleka kule kwa siku zote! Sikutaka uende bila mimi kujulikana ndiye
niliyekutuma. Watu wanamaneno mdogo wangu. Wanaweza kusema nimemtelekeza Tino,
wakati mimi ndio nakulipa wewe.” Hilo likamuua zaidi Sabrina, akapoa.
“Si unajua binadamu lakini?” Akauliza
Lela, Sabrina kimya. “Wanaweza kunisahau mimi
ninayekuweka hapo na kukupa gari, wakasema nimemtelekeza Tino. Lakini nikianza
mimi mwenyewe, nawaambia kabisa, namtuma mfanyakazi wangu, kumleta Tino. Sijui
kama umeelewa?” “Nimeelewa dada. Siku nyingine sitafanya kitu mpaka wewe
mwenyewe utangulie kupiga simu huko ninakotakiwa kumpeleka, ili wajue wewe ndio
umenituma.” “Nashukuru mdogo wangu. Vipi nguo lakini? Maana nimejisifia kweli
kwa Sabina.” “Samahani pia nilishindwa kukwambia. Naona mambo yalikuwa mengi.
Sikupata inayonienea. Zote nimerudisha kule stoo!” Mpaka Tino
akashangaa. Maana aliiona furaha usoni kwa Sabrina siku alipopewa hizo nguo.
Gafla zote hazitaki tena!
“We Sabrina! Katika nguo zote zile yaani hujapata hata moja!
Unakumbuka ile yenye madoa mekundu na nyeupe ulivyokuwa umeipenda!”
Lela akauliza kama kwa kushangaa. “Wewe ni mpana zaidi chini
dada yangu. Mimi kwangu hazikai vizuri. Zinaonekana wazi si zangu! Naona
uendelee tu na ule mpango wako wa kuuza na kugawia rafiki zako. Nimezikunja na
kuzining’iniza vizuri tu pale stoo.” “Mmh! Sasa hapo ndipo Sabina atakaponiona
muongo! Na zile chupi nilizokupa zawadi?” “Nimekuja kuzifungua, ni zile chupi
zakuingia katikati huku nyuma kwenye makalio. Mimi huwa sivai chupi za aina
hiyo.” “Sasa si ndio za kisichana! Na kamwili kako hako kembamba si ndio
zinakaa vizuri? Acha ushamba bwana Sabrina mdogo wangu.” “Naona kweli ni
ushamba dada, huwa siziwezi. Zinanishinda kabisa. Nakosa raha ninakuwa na kazi
ya kuzivuta kila wakati.” “Mmmh!” Lela akaishiwa nguvu.
“Ila da Lela, bado zipo na lebo zake, sijatoa, unaweza kuziuza
kabisa. Ukarudisha pesa yako.” “Au nikabadilishe nikuchukulie nyingine? Au nije
nikuchukue ukachague upendazo?” Akasahau kuwa aliaga
amesafiri. “Tafadhali usihangaike na mimi dada yangu.
Namaanisha kabisa. Wewe kabadilishe, ujichukulie kitu unachopenda. Kwanza mimi
ninazo chupi zakutosha, sihitaji nyingine.” “Mwanamke huwa hatimizi nguo za
ndani mdogo wangu!” “Hapana. Mimi sihitaji. Naomba ukiweka appointment ya Tino
hospitalini unijulishe.” Sabrina akabadili kabisa mazungumzo.
“Kesho itakuwa sawa?” “Naomba iwe kesho kutwa. Leo nimemuhangaisha
huko saluni, angalau apumzike kidogo, nimpeleke kesho kutwa kama kutakuwa na
nafasi, ila ikilazimu kesho, basi.” “Usimuedekeze huyo. Tino si mgonjwa wa
hivyo. Anapenda kufanya wenzake watumwa tu.” Sabrina
akasimama kuondoka pale karibu na Tino alipokuwa akimlisha matunda. Akamfuta
mdomo. “Basi utanipigia ukipata hiyo nafasi ya daktari.” Ikabidi Sabrina aage. Alisha
kerwa na Lela pamoja na Emma, alitamani angekuwa peke yake alie uchungu uishe.
“Sasa Sabina nitamwambia nini tena?” “Naomba unisikilize vizuri da
Lela. Nilishakwambia, labda hukunilewa. Na ninajua tabia zinatofautiana. Mimi
sio mtu wakufanya kitu, au kumsaidia mtu, nikamtangaza. Sina tabia hiyo.” “Sio
kwamba mimi ndio...” “Samahani naomba nimalizie.”
Tino akajua Lela amepata kiboko yake, na akaanza kumuelewa Sabrina. Alikuwa
akisikiliza tu wakati Sabrina yupo jikoni.
“Ninapoamua kufanya jambo langu, nakua nimeamua kutoka moyoni, na
sifanyi kwa ajili ya mtu.” Sabrina akaendelea
akiwa na hasira. “Nitafanya kwa moyo wote nikijua Mungu
ananitizama. Sijali ninayemfanyia atanishukuru au la. Na nikijua nimempendeza
Mungu wangu, wengine sijali. Sijui kama umenielewa sasa hivi?” Kimya. “Nipo hapa si kwa sababu ya yako kwakuwa unanilipa au Sabina.
Ni kwa kuwa mimi nimependa. Halafu mimi si mtoto mdogo ambaye nataka ruhusa ya
kila kitu. Ndio maana uliniona nilinyamaza uliponiambia nimpigie simu Sabina
eti nimwambie umenipa nguo! Sifanyi hivyo mimi. Kama wewe umetangaza ili upate
sifa, utajua wewe mwenyewe jinsi ya kurekebisha. Ila jua vitu vyako vipo stoo.”
“Naomba usikasirike Sabrina.” Lela akabembeleza.
“Sijakasirika ila nakwambia ukweli dada yangu. Mimi nilikwambia
tokea mwanzo. Sitatoa mambo ya humu ndani kwako nikamwambia hata Sabina. Hivyo
ndivyo nilivyo. Nitafanya nitakachoweza si kwa kuwa unanilipa pesa uliyopanga
wewe bila kuniuliza mimi, ni kwa kuwa nimechagua kuwepo hapa.” “Kwani pesa
niliyokupa ni ndogo?” Akauliza kwa kutulia. “Hilo ni swali ulilotakiwa kuniuliza kabla ya kuamua kunilipa.
Nilikuja hapa, nikafanya ninayofanya sio kwa sababu uliniahidi pesa. Naomba
hilo usije lisahau. Mpaka sasa nipo hapa si kwa sababu ya pesa, ni kwa kuwa
nimechagua. Usisahau hilo tafadhali.” “Basi mdogo wangu. Naomba usikasirike.
Kuanzia sasa hivi kabla sijafanya kitu, nitakuuliza.” “Nashukuru. Naomba
nikutakie siku njema.” Sabrina akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment