Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Makosa! - SEHEMU YA 4. - Naomi Simulizi

Makosa! - SEHEMU YA 4.

Kitu kikawa kimemshika kooni. Akashangaa analia. Akakaa chini kabisa hapo jikoni. Akalia kwa uchungu, akasahau kama anamgonjwa sebuleni tena anamsikiliza. Akalia hapo kama dakika kumi. Kisha akajiona mjinga. Akabaki amekaa hapohapo chini. Akajicheka. Ila akafurahi ameweza kujitetea kwa Lela na Emma. Akacheka tena kidogo. Akasimama kuanza kupika.

Alipika uji wa mchele na nyama ya kuku. Akachemsha kila kitu humo humo ndani. Kitunguu, kitunguu swaumu, karoti, hoho. Akachemsha mpaka vikaiva akiwa hapohapo jikoni. Vilipoiva, wakati anasubiri vipoe asage ndipo ampe Tino ili iwe rahisi kumeza, akaenda kumuangalia. Tino akampokea kwa macho alipotoka tu jikoni. Akakumbuka Tino huyo sio wa asubuhi aliyejawa mandevu. Sabrina akacheka. “Nusu nikuulize kama umemuona Tino!” Tino akacheka. “Umependeza sana Tino. Sikujua kama huo ndio muonekano wako. Sasa ukazane kula, urudishe nguvu.” “Ni-tajitahidi.” Sabrina akacheka.

“Njaa imekuzidia?” “Kido-go.” “Pole. Nasubiri kipoe, nikusagie kidogo ndio nikupe.” Akamuona anamwita. Akasogea. Akamwambia anaomba amtafutie begi jeusi dogo chumbani. Aliunganisha hayo maneno mpaka Sabrina akaelewa. “Nitalijuaje Tino?” Akamwambia akifungua ndani atakuta vifaa vya mazoezi, zaidi mipira, mmoja utakuwa mdogo kabisa. Akamuelekeza chini ya sinki bafuni kwake. Sabrina akatoka hapo na furaha, akijua Tino ameamua kupona kweli.

Hiyo nyumba ilipangiliwa vilivyo. Usingepata shida kupata kitu. Na kweli, alipofungua chini ya kabati chini ya sinki, akakuta hilo begi dogo jeusi. Akampelekea na kufungua mbele yake. “Unataka nikutolee nini?” Akamuomba mpira mdogo kabisa kama kitenesi. Sabrina akaanza kupekua ndani ya begi, akakuta mipira miwili ipo chini kabisa. Kijani na njano. Akatoa yote. Mgumu kidogo akapokea mkono wa kushoto. Laini akamuomba amuwekee mkono wa kulia. Sabrina akafanya hivyo. Akamuona anakazana kukunja ngumi, Sabrina akimwangalia. Alipofanikiwa mikono yote miwili, akamuona anaanza kuminya taratibu.

“Ndio mazoezi hayo?” Akatingisha kichwa kukubali. “Umenifurahisha sana Tino. Hongera.” Akacheka huku akikazana kuminya ile mipira. Alikuwa akitetemeka kama anayefanya kazi ngumu. “Ukimaliza kula, ukapumzika, nitakusaidia ya miguu.” “Sa-wa.” Akarudi jikoni, akamuacha hapo sebuleni akiendelea kufanya mazoezi ya mikono. Akasaga chakula, akakifanya kizoto kidogo, akatoka nacho. Akamkuta amekuwa mwekundu.

“Pumzika kidogo. Kula kwanza ndipo tuendelee.” Akamuona ametupa mipira yote kwa hasira. Sabrina akaweka chakula chini, akaenda kuikota, Tino amegeukia pembeni. Akajua amekasirika. Akaenda kukaa mbele yake kule alipogeukia. “Naomba niangalie mimi Tino.” Macho pia yalishakuwa mekundu. Akamvuta mikono yote miwili. Akawa ameishika. Akamgeukia. “Naomba jipe muda. Leo ndio umeanza. Hata ufahamu wako umeshasahau ni nini unatakiwa kufanya. Mimi nipo na wewe. Nitakusaidia, mpaka utaweza. Siwezi nikaondoka, nikakuacha huwezi kujisaidia kwa chochote. Sawa?” Kimya.

Akaokota mpira wa njano akamuwekea mkono wa kulia ambapo hauna nguvu. akamshikisha, na kumfungisha ngumi. Akaanza kumsaidia kuminya ule mpira. Taratibu tu. “Unaumia?” Akakataa. “Akaendelea huku akihesabu kwa sauti mpaka 9, kisha akamwacha, akaminya mwenyewe lakini haikuwa kwa nguvu kama vile Sabrina alipomuwekea mkono juu. “Si umeona? Tutafanya wote kwa muda mpaka mishipa, mifupa na misuli ielewe na kukumbuka kinachotakiwa kufanya. Na kwa kuwa umeamua, nakuhakikishia ndani ya mwezi mmoja, utaona tofauti kubwa sana.” Akamuona ameanza kutulia.

Akamuokotea na wa kijani, akamuwekea mkono wa kushoto. “Usiwe na haraka na matokeo. Taratibu tu huku ukila. Kwanza kule tu kukaa kwenye viganja bila kuanguka hiyo mipira, huoni kama ni jambo zuri?” Akamtizama. “Usikasirike bwana! Lazima kuwa na subira. Halafu nikwambie kitu?” “Ni-ni?” “Nilikununulia mafuta yakupunguza miwasho ya kichwa, na kuondoa mba. Ila yanaharufu mbaya.” “As-ante.” “Karibu. Halafu ukishiba, nataka nirudi kwenye duka la madawa. Kuna kitu nimeona online. Unakiweka chini ya miguu yako wakati umekaa. Ukisimama, wakati nataka kukuweka kwenye kiti, nakuzungusha tu kwa urahisi, kwakuwa kunakuwa kama kinakisahani kwa ndani kinachozunguka. Nitakwenda duka la madawa la pale Mwenge na Masaki nione kama wanavyo. Sitachelewa kurudi.” “Na m-imi.” Sabrina akacheka.

“Unataka twende wote?” Akakubali. “Hujachoka?” Akakataa. “Sawa. Nilitaka tupitie tulipotoka saluni, sema nilikuwa nimekasirika. Emma alinikera! Sijui yukoje Emma jamani! Kama amechanganyikiwa!” “Pole.” “Yatapita tu Tino. Ukipona tu wewe, na nikawa ninauhakika umeweza kujitegemea mwenyewe, nataka nikaanze kutafuta kujijenga mwenyewe niache kuwa tegemezi.  Nimeamua sitarudi tena nyumbani.” Tino akamtizama kwa huruma.

“Najua kufuga kuku na ng’ombe. Kwa nini nisianze kufuga kuku wangu mwenyewe nikauza? Naamini sitashindwa. Eti Tino?” Tino akamkubalia. “Sihangaiki tena kutafuta kazi, napoteza muda. Mambo niliyosomea ni kweli ajira zake ni za shida. Na kama hufahamiani na watu, ndio kabisa. Nimepoteza muda mwingi nikitaka kuhakikishia watu kuwa nimesoma kitu kitakachonilipa, lakini...” Akanyamaza akapotelea mawazoni huku akimlisha.

“Unakipenda hiki chakula?” “Zuri.” “Sikupika kingi, sikujua kama utapenda. Niambie unahamu yakula nini?”  Akawa anafikiria. “Niambie chochote kile, hata kama hakipo hapa, nitakwenda kununua nipike.” Akafikiria, akawa kama hajapata jibu. “Kwa kuwa sasa hivi unakula, ni vigumu kuchagua chakula.” Wakacheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jioni Sabrina na Tino wakiwa sebuleni mlinzi akawagongea kuwa kuna mgeni ametumwa kwa Sabrina, achukue nguo zote alizopewa na Lela. Sabrina akatoka. “Habari kaka yangu?” “Nzuri tu. Naitwa Jose, nimetumwa na Lela. Huwa namuuzia nguo zake. Kila akitaka kubadilisha nguo, mimi ndiye huwa namuuzia za zamani.” “Sawa. Naenda kukuletea, lakini nikuombe kitu, mwambia anipigie na mimi ili niwe na uhakika. Kuwe na makabidhiano mazuri.” “Kweli kabisa.” Sabrina akarudi ndani, akasikia simu yake ikiita.

Akarudi kupokea akijua ni Lela tu. “Sabrina mdogo wangu! Bado umenikasirikia?” “Hapana sijakasirika bwana. Ila kuna kijana amekuja, anaitwa Jose, amesema umemtuma zile nguo.” “Ndiye ambaye ananiuzia kwa kina dada wanaojua nguo nzuri. Huwa ananiletea pesa nzuri kweli!” “Sawa. Na hizi ambazo bado zipo kwenye hangers, nimpe kama zilivyo au nizitoe nimkabidhi tu?” “Huyo mzoefu. Anavifaa vyote vyakutunzia nguo. Wewe mpe tu. Atakaa hapo nje kidogo akizipanga kwa uthamani, ataondoka zake. Usiwe na wasiwasi.” “Sawa.” “Nashukuru mdogo wangu.” “Usijali. Na zile chupi?” Sabrina akauliza. “Kweli hutaki hata moja?” “Hapana. Asante.” “Basi mpe tu vyote. Ataniletea huku, kesho nitakwenda kubadili.” “Sawa.” Sabrina akakata simu.

Akamtolea nguo zote alizokuwa amepewa. “Na huu ni mfuko wa kumpa yeye mwenyewe. Usiuze vilivyopo kwenye huu mfuko. Amesema umfikishie.” “Hamna shida.” Akapokea. Akapanga vitu palepale nje. Akaingiza pikipiki yake ndani. Akapanga vizuri. “Vitu vyote hivyo unauza?” “Vingi nimeshapata wateja. Mida hii ya jioni nakwenda kuwapelekea majumbani kwao au bar. Ila vipo vitu vya urembo kama unataka.” “Hapana kaka yangu. Asante.” “Bado hujalipwa mshahara nini? Nakopesha pia?” Sabrina akacheka. Akajua na yeye ameambiwa kuwa yeye ni mfanyakazi wake. “Hapana kaka yangu. Nashukuru. Wakati mwingine.” Jose akachukua vitu vyake akaondoka.

Akarudi ndani Tino akimtizama. Akaenda kukaa kochi jingine kabisa. Macho kwenye tv. Akapoa kabisa. Akamsikia Tino anasafisha koo. Akamgeukia. “Nikuletee maji?” Akamwita na kumuonyesha akae pale pembeni yake. “Hutaki maji tena?” Akakataa akimuonyeshea aende akakae naye. Ikabidi anyanyuke na kuhamia kukaa hapo alipokuwa amekaa Tino. Akaona anamshika. Sabrina akacheka kidogo, akamvuta mkono vizuri, akamshika. Wakatulia wakiwa wameshikana mikono.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

S

abrina na Tino ukaribu wao ukaongezeka. Sabrina akawa analala chumbani kwa Tino. Tino akakazana mazoezi. Hata akiangalia tv, atamuomba Sabrina amsaidie hiki au kile, ilimradi tu afanye mazoezi. Juma hilo likaisha bila kumsikia Lela kabisa. Walishatoka kwenda kununua vifaa vyakumsaidia Sabrina kumuhamisha kutoka sehemu moja kwenda ingine kwa urahisi.

Juma jingine la pili nalo likaisha bila kumsikia Lela. Tino akaweza kushika kijiko vizuri kwa mkono wa kushoto na kujaribu kujilisha. Sabrina akiwa pembeni akimwangalia bila kumwingilia. Hata alipochukua muda mrefu kula, alimtia moyo. “Utazoea tu.” Wakaendelea wawili hao kutiana moyo peke yao bila hata hodi ya bahati mbaya ya mpotea njia. Sabrina akawa akikazana na vyakula vinavyotia nguvu mwili. Anahakikisha anakula kila mlo tena mzuri. Tino akaendelea kuongeza nguvu hata mwili kuongezeka. Akaacha kuogea kitandani. Sabrina akawa akimpeleka bafuni. Anamkalisha kwenye sinki kubwa yakuogea. Anamsaidia kumsugua sehemu ambazo Tino mwenyewe hafikii ila anazoweza kufikia anajisugua na kujisafisha vizuri tu.

Akaacha kujisaidia kwenye chupa na magazetini. Sabrina akawa anampeleka chooni. Akishamfikisha, anamuacha amekaa kwenye choo, anatoka kumpa faraga akimaliza anarudi kumsafisha vizuri. Akaachana na kuvaa diaper. Tino akawa mtu wakuvaa nguo za ndani za kiume. Anajifuta midomo mwenyewe. Taratibu nguvu za mdomo zikamrudia. Akaanza kuweza kutafuna vizuri na kuzuia mate.

Juma la tatu kuisha tokea Lela awaache hapo rasimi, Tino akawa anaweza kujivuta na kupanda kigari chake. Akiona Sabrina amechelewa popote, basi alishitukia amemfuata. Hakutaka kukaa mahali bila Sabrina. “Naona wewe umepona! Mbona sijachelewa bwana!” Basi watakaa naye kama ni jikoni au chumbani kwa Sabrina kama amekwenda kuoga. Anatoka bafuni, anashitukia Tino yupo chumbani ameingia anamsubiria. Watakaa hapo chumbani wakiongea hili na lile. Hakuna aliyemtaja Lela. Lakini Sabrina akashangaa kama ndio kusahau au la! Hakupiga simu kuuliza la kheri wala la shari! Hata ile miahadi ya kumtafutia Tino nafasi ya kumuona daktari ili Sabrina ampeleke, ikawa kimya! Hata ujumbe wa mwendelezo wake ikawa hakuna! Haya, pesa yao ya matumizi pia hakuwa akituma! Sabrina akashangaa kuwa anafikiri wao wataishije pale ndani bila pesa ya matumizi! Akaonelea ampe muda zaidi.

Maisha yakaendelea Sabrina akitumia mshahara aliolipwa na Lela kwa matumizi ya hapo nyumbani, kwake na Tino. “Natamani kwenda kusuka Tino. Nywele zimeshakuwa mbaya. Natisha!” Tino akamwangalia kichwani. “Twende wote.” Sabrina akacheka sana. “Da Lela ataniua warembo wa pale Mwenge wakikuiba. Halafu huwa inachukua muda mrefu sana. Utachoka.” “Kwa hiyo unataka kuniacha hapa peke yangu muda wote huo!?” Hapo Sabrina akapoa, akakumbuka hali ya Tino bado kuna mambo alikuwa akimtegemea yeye. “Samahani Tino, nimekusahau. Nitafumua, nizioshe tu. Ukiweza kutumia choo peke yako, ndipo nitakwenda kusuka.” Tino akamwangalia na kunyamaza.

“Unataka nikurudishe kwa kinyozi?” “Utapata wapi pesa?” Tino akamuuliza. “Ninazo.” Tino akamwangalia. “Utaanza kutisha tena. Nitamwambia Da Lela awapigie simu wale watu wa ile saluni uliyokuwa ukienda zamani.” “Mwache kwanza.” Sabrina akatulia kidogo kama akitafakari. “Kuna chumba kipo kwa nyuma ya hii nyumba. Kina mashine zangu za mazoezi. Naomba uangalie funguo sehemu tunayoning’iniza funguo. Ipo moja tu kwenye kidani cha nembo ya ramani ya Tanzania.” Sabrina akajua hataki kumsikia mkewe. Hakuongeza neno. Akaenda kuangalia funguo, na kweli akaikuta pale.

“Ni hii Tino?” “Asante.” Akamuona anageuza kigari chake anarudi ndani. Sabrina akamfuata nyuma. “Unataka twende ukafanye mazoezi sasa hivi?” “Kama hujachoka tafadhali.” Akamsaidia kumvalisha nguo na viatu vya mazoezi, akatoka naye hapo. Akamzungusha nyuma ya hiyo nyumba, wakafika kwenye hicho chumba. Sabrina akafungua, wakaingia. “Waooo!” Sabrina akashangaa. “Pazuri!” Palizungushiwa vioo chumba kizima. Kulikuwa na mashine mbili za kukimbia na iliyobeba vyuma mbalimbali vya mazoezi. Vyuma vyenyewe vilikuwa vimepangiliwa vizuri.

“Tino wewe ndio ulikuwa ukitumia huku?” “Kila siku ilikuwa lazima nije hapa. Kuna utulivu wa namna yake. Na kulikuwa na tv kubwa sana hapa, nchi 72, pamoja na redio yenye spika 4 kubwa. Nafikiri vimechukuliwa.” Sabrina akaendelea kushangaa. Kulikuwa na makochi mazuri sana. “Nataka kujaribu kusimama hapo kwenye mashine nione kama naweza kutembea kwa muda gani.” Wasiwasi ukamwingia Sabrina. Tino akajua. “Nitaanza kwa spidi ndogo sana. Naomba usimame pembeni yangu ili nisianguke.” “Hapo sawa. Niliingiwa na hofu! Sitaki uanguke tena na kuumia.” Akajitahidi mpaka akasimama. Akaweza kuegemea upande wa kushoto, akamwambia Sabrina awashe mashine. Kwa wasiwasi Sabrina akawasha akiwa amesimama pembeni yake upande ule usio na nguvu sana. Akaanza kutembea hapo. Kila Sabrina alipomshauri apumzike, alikataa. Alitembea mpaka jasho likawa linamtoka kama mvua. Yeye mwenyewe anatetemeka, lakini bado alitembea.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku tatu mfululizo Sabrina alikuwa akimleta hapo asubuhi na jioni. Anatembea, halafu anaanza kunyanyua vyuma vile vilivyounganishwa kwenye mashine sio vile 

vyakujitegemea. Taratibu kwa uzito mdogo mdogo, Sabrina akimsimamia ili asijiumize. Alifanya hivyo akaweka mazoea, mpaka Sabrina ndiye aliyekuwa akichoka. Analala kwenye kochi wakati mwenzie akifanya mazoezi. Atalala hapo mpaka aamshwe kwenye saa nne usiku warudi ndani wakalale. Au mchana anakwenda kupika, anamuacha hapo akifanya mazoezi. 

“Mimi naona kama unazidisha Tino!” “Nahitaji Sabrina. Naomba nitie moyo.” “Samahani. Sina nia ya kukuvunja moyo, ila sitaki ujiumize. Vipi lakini?” “Si unaona sasa hivi naanza kupata hata nguvu upande huu wa kulia! Natembea kwa kushika sehemu, kitu ambacho kingechukua muda mrefu bila mazoezi.” “Naomba tukapumzike Tino. Itoshe kwa leo. Umeshinda humu ndani siku nzima!” Tino akanyamaza. “Tino?” “Sawa. Lakini kesho nataka unisindikize mjini.” “Sawa. Naomba basi nikupokee hivi vyuma, twende tukale.” Akamkabidhi, wakatoka akitembea. Amemshikilia ule upande wa kulia, taratibu wanarudi ndani.

“Unanuka Tino!” Tino akacheka. “Nitaanza kuoga kwanza.” “Hapana. Glasi ya shake niliyokutengenezea kwanza.” Tino akamwangalia nakunyamza kama anayewaza. Wakaingia mpaka sebuleni. “Hapana Tino. Usikae bwana! Unatokwa jasho na unanuka. Kesho utapachukia hapo. Twende bafuni, nakuletea hukohuko.” Tino aliendelea kucheka tu, wakielekea bafuni chumbani kwa Tino. Akamuacha amekaa kwenye kiti cha plastiki bafuni kabisa, akarudi jikoni. Alirudi Tino anaoga mwenyewe. “Namalizia. Nitatoka muda si mrefu.” Sabrina akashangaa.

Tino alitoka mwenyewe akitembea kwa kushika ukuta, akakaa mbele ya kioo kwenye kiti maalumu cha hapo bafuni. Sabrina akakaa kwenye sinki kubwa ya pembeni, sinki ya kuogea, akabaki akiwaza, Tino anajipaka lotion mwilini. Tino alimuona ameinama kwa kupitia kioo cha ukutani. Sabrina akajua kazi yake inaanza kuisha. Umuhimu wake kwa Tino unaanza kupungua. Nini chakufanya baada ya hapo? Wapi pakwenda baada ya kibarua chake hapo kuisha. “Lakini si nyumbani!” Akawaza Sabrina huku amejiinamia.

Tino alimaliza juisi yote. Akageuka. “Upo?” Tino akamuuliza. Sabrina akanyanyua kichwa na kumtizama, akakuta akimwangalia na amemaliza hata shake aliyokuwa amemtengenezea, yeye hakuwa na habari. “Wakati unavaa, nakwenda kuandaa chakula. Najua hutanihitaji hapa.” Akasimama na kutoka bila kusubiri nyongeza kutoka kwa Tino. Tino akabaki kama hajaelewa. Yeye akaelekea jikoni kuandaa chakula. Alishapika. Akakiweka mezani, akarudi jikoni akabaki akiwaza huko. Tino kwa kutumia fimbo akaweza kufika jikoni. “Njaa inauma!” “Chakula kipo mezani tayari. Twende tukale.” Siku hiyo usiku wakala kimyakimya mpaka wakamaliza, Tino kimya na yeye akimwangalia. Akasafisha pale walipokula na jikoni.

“Nakwenda kuoga Tino. Nashauri na wewe ukajilaze upumzike. Lasivyo utashindwa kuamka kesho.” “Naona ni wazo zuri. Naomba na dawa za maumivu.” Sabrina akampa na glasi ya maji. Tino huyu alihitaji kulishwa tu vizuri na kutiwa moyo. Uhai wake haukuwa mbali kama Lela alivyodhania. Ujio wa Sabrina ulirejesha tumaini kubwa sana kwa Tino, na kuinua shauku ya kurudi kusimama tena. Akamsindikiza mpaka chumbani kwake. Akamsaidia kuweka kitanda tayari wakati anasafisha meno, alipokiweka sawa, akatoka hapo chumbani kwa Tino, akijua baada yakutoka hapo atalala.

Sabrina alizima taa zote, akaenda kuoga, akaenda kujitupa kitandani kwake. Ilishakuwa ngumu kumshika Tino huyu. Anaanzia wapi kulala miguuni kwake tena! Hata kumchezea miguu ikawa kwa woga na aibu sio kama zamani. Tino huyu ni mzuri haswa, sio yule mchovu, mzoga kama alivyokuwa akimwita Lela. Hamfuti tena kinyesi. Alishaweza kujifuta mwenyewe. Muda mwingi aliacha kumuona akiwa mtupu, hata kumuona mtupu akaanza kuona aibu tena. 

Tino kwa Sabrina.

A

lijilaza pale kitandani macho kwenye simu. Akasikia mlango unagongwa. Akakaa. Tino akaingia. “Hauji kulala?” Sabrina akababaika. Tino alikuwa msafi. Amevaa suruali nyeusi ya kulalia na singlendi nyeupe. Ananukia kutokea mlangoni. Akachechemea na fimbo yake mpaka kitandani akakaa. “Nilijua utakuwa umeshalala, sikutaka niingie nikuamshe.” Tino akamtizama. Sabrina akainama. “Lakini nilipanga baada ya masaa mawili nije kukuangalia ndipo nilale.” Tino akabaki kimya kwa muda.

“Vipi? Unajisikiaje?” “Umebadilika Sabrina. Sio kama ulivyokuwa mwanzoni. Nammiss Sabrina wa mwanzoni kabisa.” Sabrina akacheka kwa woga, akainama. “Nini kimebadilika? Tunakuwa mbali mbali!” “Hamna kitu. Labda kwa kuwa sasa hivi vitu vingi unajifanyia mwenyewe ndio maana labda unaona tupo mbali mbali. Zamani ulikuwa ukinihitaji kwa kila kitu.” Sabrina aliongea taratibu akizungusha simu yake mkononi.

“Nakuhitaji Sabrina. Bado nakuhitaji.” “Bado nipo Tino. Sitaondoka mpaka muda alioniambia da Lela uishe.” “Lela siye anayekuhitaji. Mimi ndiye ninayekuhitaji. Yeye anaweza hata kuja kesho na kukwambia uondoke, utafanyaje?” Sabrina akanyamaza akifikiria. “Sabrina?” “Nitakuuliza wewe nifanyaje Tino. Ni kama sasa hivi tunamtegemea yeye kwa kila kitu.” “Kwa hiyo akikwambia uondoke, utaniacha?” Sabrina akanyamaza.

“Bado nakuhitaji Sabrina.” Ikamgusa Sabrina akamwangalia. “Nipo hapa ni kwa sababu yako. Umenitoa kwenye hali mbaya kwa chakula, maneno ya faraja na kuniombea. Bado nakuhitaji. Kuna wakati kama binadamu naingiwa hofu, nashindwa kujua itakuaje, lakini nikikumbuka wewe upo, inanitia nguvu.” Akaendelea Tino, taratibu tu. “Naelewa kwa nini Emma, amebaki akihesabu siku tokea utoke kwenye maisha yake. Maana ndiyo yanayonipata na mimi.” “Lakini mimi nipo hapa na wewe Tino!” Akamsogelea na kumshika mkono. “Nipo Tino.” “Lakini sio kama zamani Sabrina. Unaanza kuniaga siku hadi siku mpaka unanifanya nichukie kupona!” “Hapana Tino. Sitaondoka mpaka tukubaliane mimi na wewe.” “Sasa kwa nini umebadilika?” “Nahisi ni mawazo tu.” “Unawaza nini?” Sabrina akafikiria akimchezea mikono yake, simu alishaweka pembeni.

Akamgeuza viganja, akawa anapitisha mikono yake juu chini, juu chini akifikiria. “Nini unawaza Sabrina?” “Sijawahi kujitegemea Tino.” Akajifuta machozi. “Kwa muda wote nimekuwa hapa na wewe, huwezi amini sijapokea simu hata mara moja kutoka kwa wazazi wangu wakinitafuta hata kujua ninaendeleaje!” “Wewe umejaribu kuwapigia?” “Nilitamani kupata hata robo wanachompa Sabina, Tino. Siku mbili haziishi bila baba na mama kujua Sabina anaendeleaje. Mimi ndiye niliyekuwa nikitumwa kwenda kununua vocha/ bando ili apigiwe Sabina. Wakati mwingine nilikuwa nafuata mbali kwenda kununua, na ilikuwa lazima wapate ili tu kuzungumza na Sabina.” Tino akamfuta machozi.

“Nilikuwa nikifanya kazi bila kulalamika pale nyumbani, lakini bado waliniona ni mtoto niliyewaangusha. Mama alishaniambia mimi nimeandikiwa shida tu. Fungu la kukosa na sijuagi kufanya maamuzi sahihi, ndio maana nilisoma vitu vya ajabu. Sasa nilipokuja kuachwa na Emma, ndio ikawa shida zaidi. Maana ili angalau wanione wa maana, nilipompata Emma, nikamtambulisha kwa Sabina nikijua angalau atamwambia mama kwa namna yake sitaingia matatizoni, kuwa kwa nini nina mwanaume, halafu ingeniongezea heshima. Na kweli mama alipojua japo mahusiano yangu na Emma hayakuwa rasmi lakini angalau nikaheshimika. Sasa aliponiacha, mama akasema alijua tu nisingeweza kuwa na mtu kama Emma. Sina akili wa uwezo wa kutunza vitu vizuri.” “Pole sana Sabrina.” Tino akamuhurumia.

“Lakini Tino, nimeamua kubadi maisha.” “Utafanyaje? Ndio unapanga kunikimbia?” Sabrina akacheka taratibu huku bado wameshikana mikono. “Nimekuahidi sitaondoka mpaka tukubaliane.” “Unataka kwenda wapi?” “Jana na leo nimekuwa nikizungumza na Jack.” Tino akatoa macho. “Jack yule aliyekuwa raisi wa chuo ulichosoma Dodoma?” “Kumbe ulikuwa ukinisikiliza tokea mwanzo!” “Vizuri sana. Huoni nilianza kuhangaika ili nipone! Nilikuwa nakula si kwa sababu nilikuwa ninahamu ya chakula, nilikuwa nakula kama dawa, sababu yako.” Sabrina akacheka.

“Unataka kurudiana na Jack?” “Hapana. Kusema kurudiana si sahihi kwa kuwa kama unakumbuka nilikwambia nilimkataa, tena vibaya sana. Nilimaliza chuo yeye akiwa na msichana wake. Hakuja kunitongoza tena japo alinisaidia sana. Swala la mapenzi lilishapotea katikati yetu. Ila Jack ni wale watu wanaopenda kusaidia sana. Hajui kumkatia mtu tamaa, kama nilivyokusimulia vile jinsi alivyosimama na mimi mpaka nikamaliza shule.” “Nakumbuka.” “Basi kwa sasa yupo Singida. Ni muhasibu wa wilaya ya Singida mjini. Nilikuwa nikimcheka kuwa amekimbia jiji, lakini anasema huko alipo kunamsaidia kimaisha. Amenipa dili za biashara. Anasema naweza kufanya naye biashara. Atatoa mtaji. Tukusanye mafuta ya alizeti ambayo yapo kwa wingi huko na bei nzuri. Tuyaweke kwenye chupa za ujazo tofauti tofauti pamoja na ulezi, kisha tusambaze hapa nchini. Anauhakika tutafanikiwa tu.” Tino akanyamaza.

“Lakini hata leo nimemwambia nina jukumu nimepewa kwa muda wa miezi mitatu, ndipo naweza kuanza, ila kama mambo yakibadilika kabla au baada ya huo muda, kwa kuwa tunaendelea kuwasiliana, nitamjulisha. Kwa hiyo sitaondoka mpaka tuone upo sawa peke yako. Unaponiona nakuwa kimya, nakuwa na mengi yanaendelea Tino. Lakini wewe huusiki. Na huwa nakupa nafasi yakufanya mambo yako peke yako kwa uhuru. Najua ukikwama utaniambia. Si ndio?” Tino akabaki akifikiria.

“Naomba usiwaze mbali Tino. Siwezi kukuacha nikijua bado unanihitaji.” “Nakuhitaji Sabrina. Bado nakuhitaji. Najua nakuwa kama nakuchelewesha, lakini ukiondoka sasa hivi utanirudisha nyuma kabisa.” Sabrina akajisikia vizuri kuhitajiwa na mtu kama Tino! Japo hakuwa na hela hapo alipo, alikuwa akitumia pesa aliyolipwa na Lela hata kumtunza huyo Tino, lakini alimfurahia Tino. “Nipo na wewe Tino.” “Basi iwe hivyo na vitendo. Naomba usibadilike. Tuzungumze kama zamani. Bado nahitaji masaji ya miguu.” Sabrina akacheka na kujificha uso.

“Kumbe ulikuwa ukipenda!” Sabrina akauliza kwa aibu. “Nahisi kama ndio imenisaidia kwa asilimia kubwa kufanya damu isafiri miguuni nakuanza kupata nguvu. Unakumbuka vile ulivyokuwa ukinifanyia kuanzia juu mpaka chini kwenye nyayo?” Sabrina akatingisha kichwa kukubali. “Nahisi imenisaidia sana. Bado sijarudi kuwa na nguvu kabisa. Usiishie njiani. Nguvu ileile uliyoanza nayo ndio uendelee hivyo hivyo.” “Nilijua hunihitaji tena kama zamani.” “Umesahau tu Sabrina. Wewe ndio umeniambia niungane na wewe. Nafanya hivi ili kukutia moyo na wewe. Nafanya haya yote kwa ajili yako, ukiacha na mimi utanivunja moyo.” “Nimefurahi kusikia hivyo Tino, na asante kuniambia. Nitajitahidi.” Wakatulia hapo.

“Twende ukalale. Umekuwa na siku ndefu.” Sabrina akaongea kwa kubembeleza. “Unajua nilipokuwa peke yangu nikawa nikilala kwa shida. Ukaja ukanizoesha kunibembeleza mpaka nalala.” Sabrina akacheka sana kwa aibu. “Nilikuwa nakufanyia masaji bwana!” “Na kunichezea nywele pia.” Sabrina akajificha uso. “Kumbe ulikuwa ukinichora tu! Unajidai huwezi hata kuzungumza!” Tino akacheka sana. “Nilitaka kukusoma na wewe kujua moyo wako.” “Basi umechukua muda mrefu sana kunisoma. Mpaka nikakuomba uongee!” Tino akacheka.

“Twende.” Sabrina akaruka pale kitandani kwa furaha, akamsaidia kusimama. Wakatoka huku amezungusha mkono kiunoni upande wa kulia. “Kwa hiyo Jack amerudi kwenye picha?” Tino akarusha swali na tabasamu usoni akimtizama wakiwa wanatembea. “Hata sijui Tino. Ila ninachojua Jack ni mwema sana. Tumekuwa tukiwasiliana tokea zamani. Sema mimi ndio nimekuwa mzito wa mawasiliano. Lakini yeye ni mwepesi. Muda na wakati wowote ukimtumia ujumbe tu, anajibu au kupiga.” Tino akamwangalia tena, akanyamaza.

Akapanda kitandani akajilaza Sabrina akapakata miguu yake, akaanza kumfanyia masaji taratibu lakini safari hii hakulala. Akabaki akimwangalia. “Unataka kesho twende wapi?” Sabrina akauliza, Tino akacheka kwa kuguna kidogo. “Nataka kufanya kitu ambacho nilitamani kukifanya muda mrefu sana lakini nilikuwa sina uwezo.” “Sababu ya kuugua muda mrefu?” Akadodosa Sabrina taratibu. “Nafikiri sababu ya ujinga kama anavyosema Lela.” Sabrina akatamani kuuliza zaidi, lakini kwa ujibuji ule, akaona anyamaze. Tino alijibu kwa uchungu. Sabrina akaendelea kumpapasa miguu. “Unataka nikupitishe kwa kinyozi kabla?” “Huna hela wewe. Nimekuona manunuzi uliyokuwa ukifanya hapa.” “Sitakosa pesa ya kulipia kinyozi Tino. Ndevu zinaanza kuwa ndefu na nywele zimeshakuwa. Kama unakwenda kukutana na watu wa maana, angalau uende ukiwa upo msafi.” “Ni kweli.” Akakubali.

“Unataka nimtaarifu Da Lela?” “Achana na ‘Da Lela’.” Sabrina akacheka jinsi alivyomugilizia kumwita ‘da Lela’ na si dada Lela. “Atakasirika akijua kama nimekutoa hapa bila yeye kujua.” “Na kweli ujiandae. Maana najua kesho atakuwa hapa.” “Amekwambia?” “Kwa nitakachofanya kesho, lazima mwanamme wake huko atamfukuza, atarudi hapa kunitukana.” Sabrina akashtuka kidogo. Hakujua kama Tino anajua kama Lela ana mwanaume. Akaona anyamaze asije akaanzisha jambo jingine.

Akajivuta pembeni, kulekule chini ya miguu, akajilaza. “Hapo haumii?” “Hapana. Nipo tu sawa. Kuna kitu unataka kabla sijapotelea usingizini?” “Hapana. Wewe lala tu.” Akampapasa vinyweleo vya miguu taratibu. “Nywele zimeota Tino. Utataka nikuonyoe?” Akamsikia anacheka. “Mimi mtoto wa kiume Sabrina. Acha kunitengeneza ngozi kama mtoto wa kike.” Sabrina alicheka sana. “Kumbe ulikuwa hutaki!? Mbona hukuniambia?” “Kwa wakati ule nilikuwa sina uchaguzi. Ilikuwa lazima kutoa vinyweleo vyote ili kutibu ngozi. Sasa nikaona umetoa kote!” Sabrina akazidi kucheka mpaka akakaa.

“Tino wewe mbaya mbana. Ulitulia kimya!” “Nikawa nikikusikiliza tu unavyonisifia. Mara ninangozi ya kitoto. Mara nina nywele nzuri! Sasa nikajiuliza, mnyoaji huyu mbona hatoi za kifuani! Ukazizunguka wee, ukapunguza tu na kuzichonga vizuri ila zenyewe ukaziacha! Nikajiambia umezipenda.” Sabrina alicheka mpaka  akajifunika uso na mto. “Tino!” “Wewe kuwa mkweli tu.” Tino akamsuta. “Si kwa kuwa kifuani hukuwa na mapele au madonda!” “Kwani mgongoni nilikuwa na mapele?” Sabrina akazidi kucheka. “Sasa ukilala nakunyoa kifuani.” “Huwezi. Ulivyozitengeneza vizuri hivyo! Najua huthubutu. Kwanza nakuonaga jinsi unavyotuliaga ukifika kusafisha hapo. Mpaka najiambia sijui kama tutamaliza tena.” “Bwana Tino unanisingizia mimi.” “Sawa! Pengine ni vile hujijui.” “Najijua sana. Na kesho nazinyoa zote.” “Labda mgongoni kwa kuwa huko ndiko nilikuwa nikienda wananifanyia waxing.” Sabrina akakaa vizuri.

“Kwa hiyo huwa ulikuwa ukitoa za mgongoni tu?” “Itabidi nikutafutie picha zangu za zamani ili unifahamu vizuri.” Sabrina akacheka taratibu kama anayemfikiria. “Kwa hiyo hapo bado hujafikia zamani?” Tino akacheka tu na kunyamaza. Sabrina akarudi kujilaza hapo miguuni. Akajifunika vizuri, akaamua alale. Aliamka mara kadhaa kumtizama, akamkuta yupo sawa. Wakalala hapo mpaka asubuhi.

Sabrina aliamka akashangaa Tino amelala pembeni yake. “Tino!” “Ilibidi nigeuke, nilihofia kukupiga mateke nikiwa usingizini.” Sabrina akacheka taratibu Tino akimwangalia. “Ulilala vizuri sasa?” “Sana!” Akajibu Tino, Sabrina akacheka na kumruka hapo kitandani akashuka. Yeye akaelekea jikoni, Tino mazoezini. Akaandaa kifungua kinywa bado Tino hakuwa amerudi. Akaamua kwenda kujiandaa na hiyo safari ambayo alitamani kumuaga Lela lakini Tino alimkatalia. Akaanza kuwaza juu ya muonekano wake. Sabrina hakuwa na rangi nyeupe wala mweusi. Maji ya kunde tu. Na sababu ya kazi nyingi, na mawazo, hakujua kama kwa asili ndio alinyimwa mwili kabisa au pengine angepata nafasi nzuri mwili ungeongezeka. Maisha yake yote alikuwa mwembamba. Na wakati wote alikuwa na kazi ngumu au majukumu yakumfanya afikiri zaidi ya kawaida. Hata mikono yake ilikuwa ni migumu ya shuruba kama mikono ya mwanaume mwenye shuguli nyingi za mikono. Rasta za mabutu makubwa alizokuwa amesukwa mtaani kwao, zilishafumuka, hazikuonekana safi hata kidogo. Akajitizama mara kadhaa kwenye kioo. Hakujua chakufanya na hizo nywele.

Akaoga na kuvaa moja ya gauni alilokuwa amenunua siku alipompeleka Tino kwa kinyozi. Ilikuwa gauni refu mpaka chini. Na mara nyingi alipenda kufunika miguu, hakupenda miguu yake. Alisema haina umbo. Imenyooka juu mpaka chini. Wakati mtoto walikuwa wakimtania miguu kama fito. Kama hakuvaa suruali, basi gauni refu kabisa. Nguo chache sana ndizo zilikuwa fupi, tena fupi haswa ili kuonyesha angalau unene kidogo wa mapaja. Tena alipokuwa na Emma, lakini si maeneo ya nyumbani kwao.

Akajipenda vile lile gauni lilivyomkaa. Akacheka. Akaweka hereni. Mtihani bado ukawa nywele kichwani mwake. Akahangaika hapo kwenye kioo, mwishoe akaamua vuta zote juu na kuzisuka butu moja kisha akazungushia kitambaa chembamba cheupe, kuzunguka kichwa. Gafla akajipenda. Akaonekana msafi sana kichwani. Kule zilipofumuka, kukazibwa na kitambaa. Juu kibanio kisafi. Na zile hereni, angalau akajipenda.

Katika hekaheka zote hizo kumbe na Tino alishakwenda kuoga. Wakati yupo jikoni akimalizia kuweka mambo sawa, Tino naye akatoka akamfuata jikoni. “Umependeza Tino!” “Hata wewe umependeza. Lakini nimebadili mawazo.” “Hatuendi tena?” “Hapana. Ila nafikiri umeshahangaika vyakutosha. Hiki ninachoenda kukifanya leo, kitaibua kichaa cha Lela. Na ninauhakika hutataka kumuona akiwa kama tembo aliyejeruhiwa. Utajuta kunifahamu.” Sabrina akabaki kama haelewi.

Lakini akaona aulize tu. “Kwa hiyo unataka nichukue mizigo yangu niondoke moja kwa moja?” “Ndiyo. Lakini si uliniambia ulipanga kama ukitoka hapa, utaondoka kwenda kujitegemea bila kuwataarifu nyumbani kwanza?” “Ndivyo nilivyokuwa nimepanga.” Sabrina akajibu akiwa ameishiwa nguvu. “Basi naomba ibakie hivyohivyo kwa sasa.” Sabrina akawa hajaelewa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tino anaanza kurudia enzi na kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, anataka kutoka. Anakwenda wapi? Kipi anapanga kumfanyia mkewe? Usikose muendelezo kujua kitakachojiri kati ya Tino&Lela na Sabrina & Tino. 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment