Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Makosa! - SEHEMU YA 5. - Naomi Simulizi

Makosa! - SEHEMU YA 5.

                        Tino afanya mapinduzi.

“Sijaelewa Tino!” “Najua sehemu ambayo tutapanga, ili uwepo hapo kwa muda wakati nikiweka mambo ya hapa sawa.” “Lakini sina hela Tino. Alizonipa da Lela ndio nimekuwa nikizutumia hapa.” “Najua. Usiwe na wasiwasi.” Kwa sehemu Sabrina hakuwa ameelewa bado. Ni kama hofu ya ‘kesho yake’ ikamfanya azidi kutoelewa. Ikabidi awe mkweli ili kupata ufafanuzi zaidi. “Bado sijakuelewa Tino! Kwa hiyo ndio itakuwa mwisho wa kukuona?” Akauliza Sabrina kwa wasiwasi. Tino akamsogelea karibu. “Nilipokwambia nakuhitaji, nilimaanisha.” “Itakuaje sasa!?” “Kwa majuma kadhaa, nitataka tukakae sehemu ambayo nitakuwa na uhakika Lela hatatusumbua. Huku nikiongeza mazoezi na kumuona daktari. Na wataalamu wa viungo wanishauri vizuri. Nikipona na kurudisha nguvu kabisa, ndipo nitarudi tena hapa kuweka mambo sawa.” “Kwa hiyo inakuaje juu yangu? Mimi nabakia hapa au nakuwa na wewe?” Sabrina akauliza kutaka uhakika.

“Si umesema mpaka tukubaliane?” Sabrina akatingisha kichwa kukubali. “Basi bado tutakuwa wote. Mambo mengi nakutegemea wewe.” Sabrina akajisikia vizuri. “Sasa naomba msaada wakubeba begi. Nimeliandaa lipo tayari. Weka kwenye gari kabisa, pamoja na kila kitu chako. Usichukue kitu chochote kile alichokupa Lela au ulichokikuta huko chumbani. Sitaki aje akulaumu.” “Bado atanilaumu tu Tino. Ataona nimemgeuka.” “Nikuombe kitu kingine kigumu?” Sabrina akakubali. “Kwa kuwa umekuwa ukiwasiliana na Jack, mwambie hutakuwa hewani kwa muda. Kisha zima simu kabisa ili usichanganywe na simu za Sabina, na pengine Lela mwenyewe. Sitashangaa kama atakwenda kukutafuta hata kwa wazazi.” “Tino!” “Kweli tena. Linapokuja swala la pesa, huwa Lela hana undugu wala aibu. Sasa nataka nikafunge mianya yote ya pesa zangu alizokuwa akimtunzia mwanamme wake hapa mjini. Kisha nitamtafuta sasa tuje tuwekane sawa. Nitampigia kumtaarifu kuwa mimi nimekutoa pale nyumbani.” “Basi naomba na mimi nimtumie huo ujumbe kuwa umenitoa hapa nyumbani, nimekwenda kuanza maisha yangu. Hivyo hivyo kwa Sabina, ndipo nizime simu.” “Sawa.” Wakakubaliana.

Tino akachukua hati zote za nyumba na magari. Akaweka kwenye gari wakati Sabrina anakusanya vitu vya muhimu ambavyo alijua angevihitaji kwenye kuanza na Tino. Akaweka kwenye gari. Wakati wanahangaika kukusanya vitu, kwa mara ingine tena baada ya muda mrefu sana Tino akawa ameweka simu yake kwenye umeme ili arudi kuwa hewani. Sabrina alikuwa amejawa furaha, asijue kwa nini. Wakapata kifungua kinywa pamoja, Tino akajisaidia tena, wakatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakaanzia saluni. Safari hii Tino alishuka kutoka kwenye gari akitumia magongo, lakini la upande mmoja tu. Akachechemea mpaka ndani. Wale vijana wakashangaa. “Naona sista umekazana mpaka ametembea!” Wakacheka. “Vipi, staili ni ileile?” Wakamuuliza Tino wakati wanamfunika ili asichafuke. “Tafadhali.” Akajibu Tino na tabasamu. Sabrina akakaa. Walimtengeneza Tino vizuri! Na kwakuwa aliongezeka mwili na uhai ulisharudi usoni, akapendeza sana. “Umependeza!” Sabrina akanong’ona. Tino akacheka wakiwa wanaangaliana kwa kupitia kioo. “Asante.” Na yeye akashukuru kwa kunong’ona akimwangalia kwa kupitia kioo. 

Akasubiria hapo mpaka akamalizwa na kusafishwa kabisa. Akatoka Tino wakuvutia zaidi. “Sasa twende kwanza benki, niangalie hali ilivyo huko.” Wakaamua kwenda kwenye tawi la benki lililopo Mlimani City ambako ni karibu na hapo walipokuwa. Tino aliingia moja kwa moja ofisini kwa meneja akiwa na Sabrina, akaomba salio za akaunti zake zote. Akaandikiwa kila moja. Sabrina akashangaa amebadilika rangi, anatetemeka. “Haiwezekani!” Akasikika Tino. “Unauhakika hujakosea namba hata moja?” Akamuuliza tena yule meneja. Akaanza akaunti ya kwanza, akamgeuzia laptop. Sabrina akaona 0.00. Ya pili nayo ilikuwa ya mshahara, ikaonekana kila mshahara ulipokuwa ukiingia, unatolewa kama ulivyo. Ya tatu ambayo ilikuwa yake na Lela, ndiyo ilikuwa na pesa ambazo wakamuona Tino anafuta machozi. Ni akaunti ambayo ndipo ilipoingia pesa aliyolipwa baada ya kushinda kesi. Yalikuwa mamilion ya pesa, Lela alishatumia kama nusu yake.

Akainama kwa muda mbele ya yule meneja na Sabrina. “Tino!” Sabrina akaita kwa upole. Akamwangalia na macho mekundu haswa kisha akamtizama yule meneja wa tawi hilo la benki. “Nafunga akaunti zote, nataka kufungua mpya. Inawezekana au nihamishe pesa yangu sehemu nyingine?” Akawa amekasirika, Sabrina akamshika mkono. Akatulia. Yule meneja kwa haraka akamsaidia kufungua akaunti ingine kwa jina lake tu. Akahamisha pesa yote hapo. Akafunga akaunti zote akabakisha moja tu ile aliyokuwepo pamoja na Lela lakini hakumbakishia pesa hata shilingi moja. Akachukua pesa kiasi. Alipomaliza hapo, wakatoka.

Akamuelekeza ofisini kwao. Ilikuwa Kinondoni karibu na Ubalozi wa Ufaransa. Sabrina akatoa gari hapo Mlimani City kuelekea huko. Tino alikuwa amekasirika, akashindwa kuficha hisia zake. Akamuona anapiga simu ya kwanza. Akamsikia anasalimia kwa heshima, akajua ni mtu mzima. “Naomba huduma yenu tena.” “Mkeo alitufukuza Tino. Kwanza alitangaza unakaribia kufa, umepoteza ufahamu kabisa, yeye hana uwezo wa kutulipa.” “Naelewa Mzee wangu. Lakini alishahama pale. Na mimi nasafiri kwa muda, naomba ulinzi wa mchana na usiku. Kusiruhusiwe mtu yeyote kuingia hapo mpaka nitakaporudi.” Sabrina akashangaa sana. Akamuomba baada ya lisaa, wakutane nyumbani kwake na mlinzi atakayeanza. Sabrina kimya.

Akampeleka mpaka ofisini kwake, kimya. “Tunaweza kwenda wote.” “Kama si lazima, naomba nikusubiri hapa Tino. Naepuka maneno.” Sabrina akaongea kwa kujihami. Tino akafikiria kidogo, akakubaliana naye, akashuka. Sabrina akabaki akifikiria hapo kwenye gari. Baada ya kama dakika 13 hivi akamuona anatoka. “Umefanikiwa?” Akauliza taratibu wakati anamsaidia kumfunga mkanda. “Nimemaliza. Kwanza hawakuamini nilipoingia pale. Ilikuwa ni kama wameona mzimu. Muhasimu ikabidi aongee tu. Akaniambia waliambiwa na Lela hata madaktari wamesema sitapona tena, eti nimepewa muda mfupi wa kuishi.” Sabrina akashangaa sana. “Tino!” “Najua ni kwa nini amewaambia hivyo pale ofisini. Kwa kuwa ili kila mwezi nilipwe mshahara, masharti ilikuwa nilazima wahakikishe na mimi natibiwa ili nipone, nirudi kazini nisiendelee kuwaingiza hasara bila kuwaingizia faida. Maana hakuna anayetaka kuendelea kumlipa mtu ambaye hafanyi kazi. Mpaka lini! Sasa ndio alikuwa akiwadanganya ili kuwafariji mwisho unakaribia, akijua wazi nitakufa, alipwe sasa pesa nyingi ya mwisho.” Sabrina akaumia sana.

“Sasa na mimi nikajaza fomu zakumtoa kwenye matibabu wanayomlipia hapa kazini, na kuhamisha mshahara wangu kuwaambia uingie kwenye hii akaunti mpya. Namuhurumia sana Lela.” Akaongea akisikika na hasira. Sabrina akavuta pumzi kwa nguvu. “Tunakwenda wapi?” “Tunarudi nyumbani kwanza.” Sabrina akatoa gari hapo Kinondoni kurudi Kunduchi. Akamuona anapiga simu ingine tena. “Ni wewe mwenyewe bosi wangu au!?” Sabrina akamsikia mtu wa upande wa pili akihamaki. “Ni mimi mwenyewe Chalii! Habari?” “Habari ya mji ni umekuwa mlemavu wa mwili na akili. Nilisikia huna hata uwezo wakuzungumza bosi wangu!” Tino akatingisha kichwa kwa kuumia sana. “Sio habari za uongo sana. Mungu amenirejesha. Lakini ninashida na huduma yako. Unakumbuka aina ya vitasa ulivyoniwekea mlango wa mbele na nyuma?” Sabrina akabaki akisikiliza, akajua Tino ameamua.

“Ninavyo ila bei imepanda sana. Si unajua uimara wa vile vitasa?” “Ndio maana navihitaji vilevile. Unaweza kuja baada ya lisaa ili unibadilishie kabla sijasafiri? Naondoka leo.” Wakazungumza kidogo, wakakubaliana wakutane nyumbani kwake. Sabrina akaendelea kukanyaga mafuta kurudi Kunduchi.

Ukweli kwa Kilichompata Tino.

S

abrina akamgeukia kumuona anahali gani ili amuulize swali lililokuwa kichwani mwake. “Nikuulize kitu Tino?” Tino akamgeukia. “Kwa nini ofisini kwenu wanaendelea kukulipa kama walishakulipa fidia?” “Nina hasira nao wale, acha waendelee kunitunza tu. Wamenisababishia matatizo ambayo leo ndio nilikuwa nikiwaambia. Nakwenda kufanya matibabu ya mwisho. Nikishindwa kupona, wataendelea kunilisha mimi na vizazi vyangu vyote.” Akamuona hasira inazidi kupanda.

“Huu mkono ambao hauna nguvu, ndio mkono unao niweka mjini.” Sabrina akawa hajaelewa. “Kwa kuwa ni wa kulia?” “Kwa kuwa ndio niliokuwa nikiutumia kufanya kazi. Mimi ni mchoraji. Nikipaji nilichokuwa nacho tokea mdogo. Nilikuwa nikichora kitu au mtu, utafikiri umepigwa picha. Ile kampuni ipo pale mpaka sasa wanamamilioni ya pesa ni kwa sababu yangu. Niliwaingizia sana pesa na bado mpaka sasa wanajiingizia pesa kwa kutumia ramani zangu. Niliingia nao mkataba. Walipoona wanauza sana ramani zangu mimi, tena kwa mapesa mengi sana kuliko vijana wengine tuliokuwa nao kitengo kimoja, na mkataba niliokuwa nimeingia nao wao ulikuwa tumekubaliana kila wakiuza, mbali na mshahara wanipe asilimia fulani ya hayo mauzo. Sasa wawili wa wale vijana tuliokuwa nao kitengo kimoja na mmoja wa mmiliki wa ile kampuni wakanigeuka. Wakati huo Lela alikuwa anataka niondoke pale, nifungue kampuni yangu kwa kuwa alisema kazi zangu zinauzwa sana. Sina sababu yakumfanyia kazi mtu.” Akaendelea.

“Sasa mimi nilikuwa najua aina ya mkataba nilioingia na ile kampuni. Ulikuwa hauvunjiki mpaka kwa miaka hiyo tuliyokuwa tumekubaliana. Lela haelewi anataka nitafute mwanasheria anisaidie kuvunja mkataba. Mimi sio mtu wa tamaa ya pesa. Nikamwambia napenda pesa ila naheshimu makubaliano niliyofanya na kampuni. Nitasubiri mpaka muda uishe. Sasa kama nilivyokwambia, mmoja wa wamiliki wa ile kampuni akaungana na wale vijana, wakaiba moja ya ramani ya jengo moja tulilokuwa tumekubaliana kuwauzia watu wa Nairobi. Mimi nikaitengeneza vizuri. Kumbe wakati mimi nahangaika ikamilike, wao wanatafuta mteja mwingine.” “Tino!”  Sabrina akashangaa.

“Sasa walivyo wajinga, wakauza kwa mtu ambaye na yeye akarudi kumuuzia yuleyule mteja wa kwanza. Wakapata pesa nyingi sana, wakagawana. Kampuni inampelekea mteja ramani, mteja anasema haitaji tena, amepata ingine kama ileile ila kwa pesa nzuri. Kuona, ni kama ile. Ikaanza kesi. Mteja akasema ameuziwa. Alipokamatwa aliyemuuzia, akasema na yeye ameuziwa na mfanyakazi wa pale, anaitwa Costatino. Moja kwa moja wakaja kunikamata huku nchini na kunifunga bila kutaka kunisikiliza. Si ndio nikatafuta mwanasheria?” “Ndiye huyo da Lela alikutafutia?” Tino akamwangalia kwa kushangaa.

“Lela anitafutie mwanasheria wakunitoa jela wakati aliniambia nimejitakia mwenyewe! Hakutaka hata kujihusisha mwanzoni mpaka aliposikia nimeshinda kesi, nalipwa fidia. Hapo ndipo akajirudi. Lakini nilishaanza kuugua. Sababu ya mshituko nilipokuwa jela, pressure ikaanza kunisumbua wakati sikuwa na hayo matatizo. Hata nilipotolewa kwa dhamana na kesi ikawa ikiendelea, nilikuwa nimepokonywa mpaka ile nyumba.” “Tino!” “Acha Sabrina. Pale ndipo nilipojua rangi zote za Lela. Alininyanyasa yule binadamu! Mpaka nikaanguka na stroke. Kesi inaisha, nashinda kesi, sina hata raha na ile pesa. Alichofanya baada ya kurudishiwa kila kitu ni kunifungia kwenye kile chumba, basi. Na nikwambie tu ukweli Sabrina, sikupata stroke mbaya sana. Inaitwa partial stroke. Kama angenihudumia kama ulivyofanya wewe tokea zamani, nisingefikia ile hali uliyonikuta nayo.” “Pole Tino.”

“Hali ilizidi kuwa mbaya kwa kukosa lishe nzuri, wala si stroke na ndio maana  ulipoanza kunihudumia wewe sikuchukua muda mrefu sana kusimama. Sasa ndipo mwanasheria wangu akaniambia kwa kuwa wao ndio wamesababisha kupoteza nguvu za huu mkono, tena Lela alikuwepo siku nazungumza na yule mwanasheria. Akasema naweza kuendelea kudai ule mkataba wa zamani wa kazi. Na hata ukiisha, uongezwe ili nibakie kuwa mfanyakazi wao waendelee kunilipa hata kama sitaweza kuwafanyia kazi kama zamani. Ndipo nikamuomba sasa anisaidie kisheria.” “Sio Lela?” Tino akacheka akitingisha kichwa.

“Wewe kwa sehemu umeishi na Lela ulishamjua. Kila jambo anakimbilia kulisema yeye nje kwa watu ili watu wamuone yeye ndio amefanya, asifiwe. Lakini mwanasheria wangu ndiye aliyenifuata pale nyumbani akaniambia. Tukaweka hayo madai. Wakanilipa na mshahara wangu wote tokea nipo jela na kuendelea kunilipa na wakaamuriwa na mahakama, wahakikishe napona. Yaani wagaramie matibabu yangu yote. Yule mmoja wa mmiliki aliyehusika, alifukuzwa kwenye ile kampuni bila kulipwa kitu pamoja na wale vijana wakafukuzwa kazi bila fidia ili wasifungwe.”

“Ila Sabrina, Lela amekula pesa yangu vibaya sana. Na ninajua ni kwa kuwa alijua malipo ya mwisho baada ya kifo changu yanakuja hivi karibuni ndio maana alitapanya hivyo.” Sabrina akabaki akisikiliza huku akiendesha. “Na ninajua hata huyo mwanaume wake anampenda sababu ya pesa yangu tu. Lela sio mwanamke wa kuweka ndani kama yule mwanamke uliyenisimulia Emma alimkimbilia badala yako.” “Kasandra?” “Yeah! Kasandra.” Tino akakubali.

Walifika nyumbani, Tino akamuomba Sabrina amasaidie kuongeza baadhi ya vitu alivyojua angevihitaji zaidi, akamuongeza na nguo. “Kwani tunakwenda wapi Tino?” “Moshi. Nataka niwe mbali na huu mji kwanza mpaka nipone kabisa. Nitatibiwa katika hospitali ya KCMC mpaka nipone ndipo nijipange kwa upya.” Sabrina akalifurahia hilo. Hata yeye alikuwa tayari kuwa mbali na watu wa nyumbani kwao.

Mwenye kampuni ya ulinzi alifika muda mfupi baada ya fundi vitasa. Alishaanza kung’oa vilivyokuwepo na kuweka vipya. Tino akarudisha mkataba wa zamani waliokuwa nao na hiyo kampuni ya ulinzi akitaka ilinde hapo masaa 24. Akalipia na kumwambia yule Mzee awaambie walinzi wake kuwa, wasimfungulie yeyote yule hilo geti. Wakakubaliana akaondoka wakati Sabrina akiendelea kupakia vitu garini. Akahamia vya jikoni alivyojua angehitaji kwenye makao mapya. Mashine za kusagia vyakula na juisi. Na vyombo baadhi. Akawa amemaliza. Akatoka kumsubiria Tino.

Maisha mapya ya Tino & Sabrina.

Hotelini.

M

paka wanamaliza kila kitu hapo nyumbani kwa Tino, ilishafika saa 10 jioni. Tino akamwambia wakatafute hoteli walale, waanze safari asubuhi na mapema. “Pumzika leo dereva wangu. Kesho tuanze safari ya Kilimanjaro. Nakutegemea wewe kulifikisha hilo gari huko.” Sabrina akacheka huku akifikiria. “Usiogope. Ukichoka, tunalala hotelini, kesho yake tunaendelea na safari.” “Nitakufikisha salama. Usiwe na wasiwasi.” “Wewe tena! Mbona mimi nitakuwa nalala tu.” Wakacheka na kuendelea kutafuta hoteli yakulala usiku huo.

Sabrina akashangaa hoteli aliyochagua Tino. “Sasa hapa si itakuwa mahela mengi sana!” “Yeah! Nataka upumzike vizuri baada ya kuuguza kwa muda mrefu.” Sabrina akacheka taratibu kwa kuridhika. Wakapata chumba, wakaingia humo. Ilikuwa siku iliyojaa hekaheka, wote walikuwa wamechoka. “Nimebeba chupa ya uji Tino. Kunywa kwanza halafu nitaangalia wanachakula gani kitakachokufaa. Au unahamu ya kula nini?” “Acha ninywe kwanza uji. Naona kama nishazoea uji! Siku haiendi bila uji.” Sabrina akamuwekea kwenye bakuli. “Kwani ulibeba na vyombo!?” Sabrina akacheka tu. “Nimekukubali.” Akamsaidia kumpa, mpaka wakamaliza.

“Nataka kuzungumza na Sabina.” “Si kumtumia ujumbe tena?” Sabrina akakaa. “Lela ni muongeaji Tino na ndio kitu amekuwa akikifanya hata kwenye mahusiano yenu. Kila mtu kwenye kitu chochote kinachomuhusu yeye au wewe anahakikisha yeye ndiye anakuwa msemaji wa kwanza ili atengeneze stori zake vile anavyopenda. Mimi nina familia Tino. Ipo siku nitarudi nyumbani. Sitajali watakachokiamini, lakini nakuomba Tino, katika hili mimi ndio niwe wakwanza kusema.” “Sawa.” Tino akakubali.

Kwa Sabina.

A

katoa simu yake akampigia Sabina dada yake, Tino kimya ametulia. “Za siku wewe mtoto!? Umepotelea baharini?” “Nipo dada yangu. Hata kupiga kunijulia hali!?” “Nilitingwa bwana. Vipi lakini?” Akamjibu mdogo wake kirahisi tu na kuongeza swali jingine bila kujua jinsi Sabrina anavyoumia ambavyo hawamjali. “Ile kazi pale iliisha. Lela aliondoka, akaniachia mgonjwa. Tokea aondoke mpaka naondoka pale leo, hajarudi wala kupiga simu kutujulia hali wakati aliniacha pale kwa makubaliano atatafuta daktari niwe nampeleka Tino.” “Subiri kwanza we Sabrina! Huo ni muda gani?” Ikabidi Sabina aulize. “Kama mwezi sasa na majuma mawili hivi.” “Haiwezekani!” “Kweli tena.” “Ujue Lela amechanganyikiwa yule msichana!” Sabina akashangaa sana.

“Na amenidanganya juzi nilipoenda kumwangalia hospitalini.” “Anaumwa?”  Akauliza Sabrina. “Tena hakutaka hata nijue kama yupo hospitalini. Mdomo wake umemponza yeye mwenyewe. Nasikia kashika mimba. Ndiyo inayomsumbua. Hana anachoweza kula. Tena nafikiri ndio sababu ameshindwa kuja hapo kwa Tino. Sasa mmoja wa shoga zake akanipigia kimbea kuniambia Lela mjamzito, ila hataki watu wajue kama anamimba, mpaka mumewe afe, wakishazika ndipo atakapojitokeza.” “Da Sabina wewe! Yaani anasubiria kifo cha mwenzake!” Sabrina akashangaa sana.

“Kweli tena. Sasa sijui wanapanga kumuua huyo Tino yeye na mwanaume wake au la! Mimi sijui. Lakini ndio habari niliyosikia kwa shoga yake wakaribu sana. Sasa mimi nikasema niende nikajionee mwenyewe. Siku hiyo nilipopigiwa nakupewa hizo habari, nilipotoka kazini tu nikasema niende nikamwangalie makusudi huko hospitalini alipolazwa kabla hajatoka ili ajue najua. Maana kila nikizungumza naye namuuliza mbona simuoni baa siku hizi, ananipa maneno mengi. Baada ya muda, nikawa simpati tena! Ndio sasa ikabidi nimfuate. Eti nimemkuta wodi ya kina mama wajawazito pale Agakhani, ananiambia anaumwa malaria! Wakati shoga yake alishaniambia mimba imekuja na maradhi, kutwa yupo hospitalini na huyo bwana ake.” Sabrina akatulia kidogo.

“Sasa nikamwambia, wewe upo hapa, mgonjwa wako umemuachia mdogo wangu, halafu mimi huniambii kama unaumwa umelazwa, nitajuaje juu ya mdogo wangu huko ulipomuachia mgonjwa! Akaanza kujitetea hapo mbele ya mwanaume wake, kuwa simu ilipata matatizo lakini angeniambia. Hata hivyo amekuacha vizuri sana nisiwe na wasiwasi. Kutokurudi nyumbani ni kutotaka kukupa wewe mzigo wa watu wawili kwa kuwa wewe unajituma sana, ungeishia kuwahudumia watu wote wawili ndio maana ameona yeye augulie hospitalini na akitoka ataenda kukaa kidogo kwa mwanaume wake mpaka apone kabisa, usilemewe. Ila nisiwe na wasiwasi kabisa, amekuachia gari na pesa ya kutosha. Akasema tena hapo ilikuwa amtume Rama, huyo mwanaume wake akurushie pesa nyingine.” “Mmmh!” Sabrina akachoka kabisa.

“Ninachoweza kukwambia dada yangu, si kweli. Lela ni muongeaji sana asiyeweza vitendo. Alinipa huo mshahara.” Sabrina akamtajia dada yake kiasi cha pesa alicholipwa na kuishia kufanya mshahara wote matumizi ya hapo ndani. “Haiwezekani Sabrina. Pesa ya kitoto kiasi hicho!?” “Mungu wangu ni shahidi, tena alisema mlikubaliana naye.” “Mimi nikubaliane malipo yako kwani mimi ndiye ninayefanya kazi! Yeye mjinga nini?” “Mimi mwenyewe nilishangaa, lakini kwa sababu nilimkuta mgonjwa na hali mbaya sana, nikikwambia mbaya, niamini ilikuwa mbaya dada. Na hakuwa na matunzo kabisa. Nikaona nisiweke pesa kwenye uhai wa mtu.” “Sasa hilo ndilo kosa lako. Kwa nini ulikubali kuendelea naye bila pesa yakueleweka! Lela ni mshenzi kupitiliza. Ukimchekea yule, atakufanya mjinga. Na usimuone vile, anamahela ya Tino kibao. Anayachezea yeye na mwanaume wake bila huruma! Halafu leo anakupunja! Atanitambua. Na huwa ananijua mimi huwa sitaniani na vima. Hawezi kunichezea akili mimi, nitamtia adabu mshenzi mkubwa yeye!” Sabina akasikia ameshakasirika.

“Mimi nilifanya kwa sehemu yangu dada yangu kwa kadiri Mungu alivyonijalia.” “Ndio maana wanakuonaga mjinga na wewe! Mpaka wadogo zako wanajua kupata pesa palepale nyumbani kwa baba na mama wanaojulikana ni mabahili, halafu wewe umeshia kukaukwa mdomo! Acha kuwa mjinga wewe Sabrina. Simamia haki yako!” Sabrina akacheka kidogo bila nyongeza katika hilo. Akaona aendelee na yake.

“Sasa nilichokupigia simu dada yangu nikutaka kukutaarifu kuwa nimepata kazi kwengine. Nikitulia na mambo yakienda vizuri nitawatafuta. Sitaki sasa hivi kuongea mengi, ikaja kushindikana huko mbeleni, wazazi wakaendelea kuniita fungu la kukosa. Acha nikapambane na dunia. Nitajijua huko huko.” “Mmh! Kwa hiyo hutaki kuniambia unapokwenda?” “Acha nisimame dada yangu. Nimekuwa mtu wakusema kila kitu ndio maana naona nikishindwa, nakuwa kicheko cha familia.” “Sawa, lakini nakuhakikishia Lela atanitambua. Anajidai anakupa mahela na vitu, tena kwa kutangaza kila mahali kuwa amebadilisha maisha ya mdogo wangu, kumbe muongo!” Bado Sabina alisikika na hasira na Lela, wala si mdogo wake kwenda wasipopajua.

“Mimi sijui amesema nini, lakini sijachukua chochote kutoka kwake dada. Nilimuona ni mtu wa maneno maneno hata zawadi alizokuwa ameninunulia za chupi, lotion na sabuni yake nikamrudishia.” “Kweli!?” “Kweli dada. Na Mungu ni shahidi. Alimtuma kijana mmoja huwa anamuuzia nguo, akaja kuchukua kila kitu chake.” “Atanikoma Lela. Katangaza kila mahali kuwa amekupa vitu kibao!” “Hasemi kweli.” Akakataa Sabrina.

“Mimi naomba nikuage dada yangu, na utanifikishia salamu kwa baba na mama.” “Wewe Sabrina! Huwapigii?” “Unajua tutakapoishia na wazazi wako dada yangu. Wataniharibia mipango yote kwa vitisho, kunikatisha tamaa kwa kuniambia sina nitakapofanikiwa kwa chochote nitakachofanya na kutaka nirudi nyumbani nikawafugie ng’ombe na kuku wao bila shukurani,  halafu matusi yaendelee wakinitolea mimi mifano mibaya mpaka kwa wale watoto wao wadogo wa kiume. Hata hivyo sidhani hata kama watajali nilipo, au hata kuhisi kuna mtu amepungua kwenye maisha yao. Hakuna anayenitafuta kwenye ile familia. Mpaka mimi ndio niwatafute.” Kwa mara ya kwanza Sabina kikamuingia moyoni na kujisikia vibaya. Hata yeye tangia atoke nyumbani kwake ni Sabrina amekuwa akimpigia kumjulia hali na kumuuliza hili na lile juu ya Lela na Tino, lakini si yeye kumtafuta mdogo wake kujua anaendeleaje.

“Acha nikahangaike na mimi na maisha yangu, nitawatafuta kikieleweka.” “Mmmh! Haya mwaya. Kila la kheri. Kuwa tu mwangalifu huko.” “Nashukuru dada yangu.” Sabrina akakata haraka. Na kumblock kila mahali ili asije kumpigia tena akampata au hata wazazi wake. Nao akawablock wote, familia nzima.

Kwa Lela.

“Sasa nishamalizana na familia yangu yoote kwa kupitia Sabina. Acha nimtumie ujumbe da Lela. Nasikia ni mgonjwa, hapatikaniki kwa simu. Mimi namtumia ujumbe hivyo hivyo atapata ujumbe wake atakapofungua simu.” Tino kimya ametulia. Sabrina akamwangalia. Akamuona amebadilika rangi tena. Mwekundu. Akajua amesikia kila kitu, ndio amekasirika. Akaona amalize kwanza na Lela, aliyemtangaza vibaya. ‘Da Lela. Naona muda mrefu sana umepita tokea tuwasiliane au tokea uniachie mgonjwa pale nyumbani. Najua ulinilipa pesa ya miezi mitatu ili nifanye kazi kwa muda huo, lakini hukuacha pesa yeyote ile ya matumizi ila ahadi tu yakuja kuwasiliana mbayo hujatimiza. Ilikuwa ikinilazimu kutumia uleule mshahara ulionilipa, kununua umeme ulipoisha, vyakula na matumizi mengine ya pale ndani. Kwa hiyo ile pesa yote iliisha na naona na kazi pia iliisha. Kuanzia leo nimetakiwa kuondoka pale. Mambo mengine nashauri uzungumze na Tino mwenyewe. Ila ndio nataka kukutaarifu kuwa nimeondoka. Na Tino ni shahidi, sikuchukua chochote zaidi ya vitu vyangu nilivyokuja navyo. Nakutakia maisha mema. Asante.’ Akamaliza kuandika. “Naomba nikusomee kabla sijatuma.” Kabla Tino hajajibu, akaanza kumsomea. Tino alipokubali, akautuma na kumblock na yeye kila mahali. Hakutaka awasiliane naye tena.

Aluta kontinua.

A

lipomaliza Sabrina na yeye Tino akatoa simu yake. Akamuona na yeye anapiga. Kimya akisubiria ajue na yeye anampigia nani. “Ni wewe Tino au Lela anatumia simu yako?!” “Ni mimi kaka.” “Daah! Nimeona simu yako ikiingia nikataka kutupa simu.” “Kwa nini kaka?” Tino akauliza akijua wazi ni nini kinachoendelea kwenye jamii juu yake. “Nilikuwa na Lela kama mwezi mmoja uliopita akiulizia juu ya malipo yako ya mwisho kwenye ile kampuni!” “Unamaanisha nini!?” Akauliza Tino akitetemeka kwa hasira. “Madai baada ya kifo chako. Alitaka kujua yeye kama atakayeachwa mjane kwa kifo walichosababisha wao kama kampuni, atalipwa fidia kiasi gani! Na kama tunaweza kuwadai zaidi.” Tino akazidi kuumia.

“Sasa alichofanya kibaya zaidi, kabla hatujamalizana mimi na yeye, maana mimi nilimwambia ile kampuni mpaka sasa wamekuwa wavumilivu na waungwana sana. Wanaendelea kumlipa mshahara wako japo hawaoni maendeleo yako ya hospitalini. Tusiwatibue kwa madai mengine. Akaondoka hapa kwa hasira, akaenda kumfuata muhasibu wa pale kwenye ile kampuni, anamuulizia malipo ya mwisho baada ya kifo chako! Yule muhasibu akanipigia akilalamika akisema tunadai vipi pesa ya mwisho wakati hatujapeleka hata kopi ya hati ya kifo chako!” “Yule muhasibu amenisimulia yote hayo.” Tino akaongeza. Sabrina akashangaa sana.

“Ndio maana nimeshituka sana kukusikia. Maana Tino niliyemsikia mimi mara ya mwisho ni wa kufuatilia hati ya kifo siye Tino anayeweza kuzungumza mkasikilizana!” “Naelewa kaka, najua anatafuta kifo changu ili apate pesa zaidi. Ameniacha pale ndani bila pesa wala kujali kwa lolote huu ni mwezi sasa na majuma kadhaa. Na kabla ya hayo alikuwa akiniacha, ananifungia ndani chumbani, gizani, bila chakula wala mtu wakunisaidia hata maji, makusudi tu na mengine mengi.” “Ndio maana alikuwa akikataza tusije kukuona nini? Maana hata ndugu zako walinilalamikia kuwa anawazuia kufika pale!” Mwanasheria, ambaye alijulikana kwa jina moja tu, Max, mashuhuri hapo jijini kwa kushinda kesi ngumu, akaongeza. “Asingekubali mnione kwenye ile hali aliyokuwa akiniacha nayo, kaka. Ilikuwa mbaya, yeye mwenyewe alikuwa hataki kuniona jinsi nilivyotisha na kunuka.” Tino akazungumza kwa kuumia sana.

“Atakuwa yuko wapi sasa? Au kwa mwanaume niliyesikia anaishi naye?” “Ndio nilichokupigia ili unisaidie, kaka. Hapa nazungumza kwa kuwa Mungu alinitumia malaika wake kunitoa kwenye ile hali. Bila yeye, pengine kweli sasa hivi mngekuwa mlishanizika, na yeye Lela anasubiria malipo kama mjane wakati kiukweli Lela alishaanza maisha yake.” “Nakuelewa kabisa Tino, lakini kisheria bado ni mke wako. Na kama unavyomjua mkeo ana….” “Tafadhali muite Lela tu.” Akamkatisha Tino kwa hasira.

“Sawa, Lela.” Max akarekebisha. “Lela amejaa kwa kila anayekufahamu wewe akijionyesha anakujali na kukushugulikia kwa hali ya juu. Ameniambia hata mimi kuwa ameajiri msichana wa kukuhudumia japo upo kwenye hali mbaya sana, lakini hajakukatia tamaa, amekutafutia mfanyakazi maalumu kwa ajili yako.” Sabrina akashangaa sana. “Muongo kabisa. Anamuacha msichana pale huku akimwambia asinihudumie kwa lolote, na wala asiingie kwenye chumba changu. Ni kama Mungu tu alimgusa akiwa amemkataza, akaingia. Alinikuta nimeoza kaka. Sifai kwa madonda, nina kinyesi, mikojo, halafu amenizimia taa, na kufunga madirisha nikawa naishi gizani! Eti anasema nini?” Tino akaongea kwa hasira.

“Sasa Tino mdogo wangu, hayo ni maneno yake dhidi yako. Hakuna uthibitisho. Ila alichokuzidi mwenzio anaongea sana Lela. Iwe uongo au ukweli, amejaa kila mahali.” “Je kwa hilo lakunitelekeza na kutokuwa nyumbani zaidi ya mwezi?”  Akauliza Tino. “Labda nikuulize Tino, unataka nini sasa hivi?” Ikabidi Max,  mwanasheria wake wa tokea mwanzo kuuliza. “Kwa yote hayo niliyokwambia bado unaniuliza tu? Au unataka kunisikia nikiongea nini? Au unataka kusikia nini kimetokea kwenye maisha yangu ndipo ujue naishi na mtu hatarishi kwenye maisha yangu? Hivi unajua ile pesa yote niliyolipwa ameitumia zaidi ya nusu?” “Haiwezekani Tino! Pesa yote ile!?”   Max akashangaa sana.

“Acha kaka, hapo bado pesa yangu ya akiba iliyokuwa kwenye akaunti zangu nyingine. Nimekuta hakuna kitu kaka, halafu anashindwa hata kuninunulia chakula mimi mwenyewe! Hata kuajiri mtu wakunitumikia ameshindwa kumlipa! Hata kama kwake nilikuwa nikinyaa, hata kumlipa mtu anihudumie! Pesa zote za dawa na vitu vyangu vya hospitalini alivyonunua mwanzoni kabisa kwa kushauriwa na daktari, yule muhasibu anasema alikwenda pale kudai kwa vitisho!” “Aliniambia yule muhasibu.” “Halafu usifikiri hata vilitumika kaka! Alinunua vifaa vyote vya kisasa alivyoshauriwa na daktari ili kunisaidia kujisaidia mimi na msaidizi atakayekuwepo, lakini kaka, havikuwahi kutumika. Tena kwa makusudi tu, wakati yule daktari alimwambia nikitumia vile vifaa, kwa muda mfupi sana kwa kuwa sikuwa na stroke mbaya, ningeweza kujitegemea. Akamsisitiza, nahitaji mazoezi na kula vizuri, nitapona.” Akaendelea kulalamika Tino kwa sauti yake yakuumia.

“Kwa makusudi kabisa, akaanza kufanya kila kitu kinyume na alivyoshauriwa na daktari. Makusudi kabisa kunifanya niwe dhaifu. Akajidai mwanzoni amechukua likizo kuniuguza.” “Nakumbuka. Alitangaza kwa kila mtu. Na kuomba nihakikishe ndugu zako hawafiki pale ili wakuache upumzike, na wasikutapeli tena.” “Basi ile ilikuwa njia yake yakunitenga na kila mtu ili atimize kusudi lake. Alinifungia kaka, karibu siku 4, mchana na usiku nipo peke yangu gizani.” “Haiwezekani Tino!” “Mbona hiyo ilikuwa mwanzo tu kuhakikisha sina tena nguvu! Ndipo sasa nikaishiwa nguvu kabisa hata kukaa ikawa shida. Si kwa stroke, ila njaa. Na ndipo mateso yalipoanza. Kila alipomleta mtu wakunisaidia ili kuonyesha hayupo mtaani akizurura tu bila kunipa mimi msaada, alihakikisha anampotosha huyo mtu makusudi. Kumuwekea chuki dhidi yangu. Akionyesha ana moyo wa kukaa, anaanza kumnyima malipo makusudi. Basi mfanyakazi anaondoka, naachwa peke yangu hapo. Huyu binti aliyekuja kuniokoa, alinikuta nimejawa na kinyesi na mkojo, ngozi ina madonda matupu. Natetemeka kwa hofu, baridi iliyokuwa ikinipiga bila kufunikwa nikiwa mnyevu mpaka nakauka, na maumivu. Alichokuwa akifanya Lela, kama ambaye alikuwa hataki nikate roho, ni kunipa maji tu kila akija, kama aliyekuwa akimwagilizia ua alilolifungia mahali. Ananikuta nanuka, ananiacha hivyo hivyo na matusi juu!” Tino aliongea kwa uchungu sana.

“Pole sana Tino. Pole.” Max akamuhurumia sana. “Na kwambia kaka, ni Mungu tu. Alikusudia Mungu mwenyewe kuniokoa kwenye ile mikono maana wote mliacha hata kuja kuniona! Nilibaki sina mkombozi.” “Unamjua Lela, Tino mdogo wangu. Alihakikisha kwa vitisho hakuna anayepita.” “Hata kutaka kunisikia kwa simu! Hata kupita jamani! Zaidi wewe ambaye ulikuwa ukimsaidia madai! Angalau ungemwamuru kuwa nilazima unione ndipo uendelee na madai, kaka! Lakini ni kama na wewe ulinitelekeza. Ukaishia kupokea malipo yako, ukaachana na mimi!” Sabrina akajua Tino hatambakisha mtu. Alikuwa mwekundu, anatetemeka kwa hasira.

“Samahani sana Tino. Nahisi nikutingwa na maneno mengi ya Lela.” “Sikutegemea kaka! Kila mtu alinisusa wakati nilikuwa kwenye maisha ya watu nikisaidia kwa hali na mali! Nikapata shida mimi, hata wale waliojua ukweli juu ya ndoa yangu waliniacha kwenye mikono ya Lela, mwanamke waliyejua wazi alinigeuka hata kabla sijapata matatizo. Hata wale waliojua anatumia pesa yake yote kumtunza mwanaume wake, huku akitapanya yangu, waliniacha kwenye vitisho vya maneno matupu ya Lela! Mtu baki kabisa, ndiye aliyeniokoa! Asiyenijua wala hanitambui ndiye aliyehangaika na mimi mpaka leo nazungumza na wewe hapa!”

“Lela alimleta nyumbani kama kumlindia nyumba wakati akihamia kuishi kwa mwanaume wake, kusudi tu alimuacha ili mtu akipita pale nyumbani, akute mtu asilaumiwe kuwa ameniacha nyumbani peke yangu, halafu anamuacha hapo nyumbani huku akimuonya kabisa hata chumbani kwangu asiingie, aniache tu. Halafu akaishia kutangaza kwa kila mtu ameajiri tena mfanyakazi mwingine na amemlipa mshahara wa miezi mitatu,..” “Hata mimi aliniambia baada ya kutaka kujua unaendeleaje na kwa wakati huo upo chini ya uangalizi wa nani anapokuwa kazini.” Max akajaribu kujitetea.

“Basi kama alivyokuwa akifanya kwa wengine aliokuwa akiwaleta wanihudumie, ili waondoke na kuniacha peke yangu na yeye kupata nafasi yakuendeleza kuniangamiza, huku huko nje akitangaza na kunisema vibaya kwa watu kuwa ninamatatizo ndio maana wafanyakazi wa kunihudumia hawakai, nakwambia akaanza kumpandia chuki huyu binti dhidi yangu. Alipomuona huyu binti anahangaika mchana na usiku bila kuchoka, akaendelea kumsisitiza asihangaike na mimi, hata asiingie chumbani kwangu yeye atanihudumia. Kwa kumsikia mwenyewe akimkataza. Wakati alikuwa akiondoka hapo nyumbani hata siku nne, na akirudi haji hata kuniangalia chumbani kwangu. Alipomuona huyu binti hamsikilizi, amekazana kunisaidia, ndipo akatutelekeza sasa na hiyo pesa aliyokuwa akiwatangazia amemlipa mshahara wa miezi mitatu. Bila chakula wala pesa ya matumizi. Ndipo hapo sasa nasema ni yeye Mungu mwenyewe alikusudia kuniokoa maana aliona binadamu wote ambao wananizunguka wamenisusa na kunichoka. Akaniletea na kuniacha kwenye mikono iliyokuwa na ubinadamu na upendo.” Sabrina akajisikia vizuri.

“Ilimbidi yule binti atumie pesa yote ndogo aliyokuwa amelipwa na Lela, kuendesha maisha ya pale huku akijitahidi kuninunulia virutubisho ambavyo najua vilimgarimu. Aliondoka Lela akimdanganya huku akijichanganya na mimi nikimsikia, mara amuage anasafiri kikazi, mara aseme anataka akupumzike kwa kuniuguza muda mrefu. Mara atakuwa hapahapa mjini, mara nje ya mji, lakini yule binti akamuomba atafute appointment ya daktari, tena alimwambia kwa kumsikia, yeye mwenyewe angenipeleka, Lela akasema atafanya hivyo. Sijamsikia akimtafuta huyu binti, ila alimpa masharti kuwa asinitoe kwenda popote kuhudumia kwa lolote hata kukatwa nywele, mpaka amwambie yeye, yeye ndio awaambie watu huko atakapotaka kunipeleka ili watu wajue yeye ndiye aliyetoa wazo, wajue yeye ndio ananihudumia.” “Haiwezekani Tino! Alimwambia kabisa?” Max akashangaa. 

“Kabisa kaka. Sasa huyu binti alipoona nimepata nafuu yakuweza kukaa mwenyewe, na alinikuta ngozi ya kichwa kimejaa ukoko, kama ambayo haijahudumiwa miaka na Lela hapatikaniki, akanipeleka kwa kinyozi wakati alimkataza. Akamwambia asinipeleke kwa kinyozi ni aibu.” “Kwa nani sasa?” “Labda yeye, mimi sijui! Lakini alisema naweza nikajisaidia huko, ikawa aibu. Kwa hiyo nisipelekwe, yeye huwa analipa watu wakunipunguza nywele palepale nyumbani. Sasa huyu binti, hapana, acha nimtaje jina, anaitwa Sabrina. Sabrina alipoona siku zinazidi kwenda, na hakuna simu wala hodi pale kwangu ndipo akanipeleka yeye mwenyewe saluni anayojua yeye. Tulipotoka sasa ndipo akamtumia ujumbe Lela kumtaarifu kuwa alinitoa pale lakini alinirudisha salama. Hivi unajua Lela kwa mara ya kwanza tokea aondoke na ya mwisho alipiga simu akimlaumu huyu binti huku akishangaa!” “Analaumu nini na alikuwa akishangaa nini?” Akauliza.

“Alidhani Sabrina alinipeleka kwenye ile saluni wanayotufahamu mimi na yeye, bila yeye kujulikana ndiye ameamuru nipelekwe. Kwamba sifa atapata Sabrina, yeye ataonekana amenitelekeza. Si kwa kuwa watu wanamuona mtaani! Na nilisikia saluni ileile niliyokuwa nikinyoa mimi na wakinifanyia waxing ndipo alipomuhamishia mwanaume wake.” “Haiwezekani Tino!” Max akahisi kama ni hadithi tu na si kweli.

“Nakwambia kaka. Aliniambia yule kaka anayeninyoa pale nilipoenda mara ya mwisho wakati nilipoanza kuumwa, na yule msichana aliyekuwa akinifanyia waxing akathibitisha makusudi ili kumuharibia Lela, kwa kuwa ni wagomvi, walishapigana pale. Akimkataza asiwe ananihudumia.” “Lela!” Max akamtaja kwa masikitiko. Sabrina akishangaa na yeye, asiamini ujasiri wa Lela.

“Na ndio maana hakutaka mimi nirudi pale, japo nasikia alimtafutia mwanaume wake kinyozi mwingine. Yule aliyekuwa akinihudumia mimi alimkatalia akamwambia tayari anao wateja wengi, hapokei wateja wengine.” “Lakini pale wanabei!” “Sana, lakini alikuwa na shida gani wakati pesa yangu anayo!” “Na kweli. Sasa ukute na hofu ilimuingia aliposikia umeweza kutoka ndani wakati huku nje alikuwa anakutangaza upo mahututi, haja zote hapohapo mpaka wafanyakazi wanakimbia nyumba.” Max akajikuta anaongeza. Asijue anavyozidi kumuumiza Tino. Kama kweli aliyajua hayo yote, alishindwa vipi kupita na kumsalimia tu!

“Kumbe na wewe uliyasikia hayo!?” Tino akauliza kwa kuumia sana. “Ni hivyo alikuwa akikataza wat…” “Hapana kaka. Naomba achana na hicho kisingizio. Unazidi kuniumiza tu. Kumbe mlijua nina hali mbaya kwa kiasi hicho! Hata kuja kuniona jamani!? Angalau kujua kama nina matibabu au la!” Max akanyamaza.

“Anyways ndio nilikuwa nikisema hakutaka nitolewe tena ndani. Zaidi kwa watu wanao nifahamu na aliowafikishia taarifa zangu. Anawaambiaje walimwengu tena? Tena naonekana na kuhudumiwa na mtu baki tu. Halafu mdogo kuliko yeye! Sabrina amewezaje, yeye ameshindwaje? Sasa ili kufunika aibu yake, na watu wajue kweli nakaribia kufa, nahisi anazo njama zakutaka kuniangamiza kaka. Japokuwa sijamsikia tena tokea siku ile alipolalamika na kumlaumu Sabrina kwa simu, lakini uhakika wa kifo changu aliompa yule muhasibu wa kampuni yetu ili amwambie ni kiasi gani atapata baada ya kifo changu ndio unanitia wasiwasi na kunifanya niondoke pale kwa muda.”

“Asingepata nguvu ya kutangaza kifo changu wakati Sabrina alimuhakikishia ninaendelea vizuri, na wala sijajisaidia saluni. Inamaana amejua naendelea vizuri. Lakini tujiulize tu mimi na wewe, ujasiri wa kuendelea kutangaza kifo changu anautoa wapi kama si kuna hila nyuma yake!” “Hawezi kuona unapona kabisa Tino. Kuwa kwako kitandani kunawasaidia kupata pesa kila mwezi. Na wanajua wazi, kifo chako kitawanufaisha zaidi. Watapata Bingo kubwa ya mwisho ambayo alijua ni pesa kubwa zaidi.” Akaongeza Max akisikika anafikiria zaidi.

“Ndio maana nimeona niondoke kabisa pale. Nikajifiche mbali kabisa. Huku ukinisaidia jinsi ya kuachana naye moja kwa moja. Na hata tukiachana, asiniache nalala nje. Yaani akaniacha mavumbini kabisa! Yaani mahakama iamuru tugawane kidogo alichoniacha nacho!” “Lakini kama nimekusikia vizuri Tino, ni kama sasa hivi umeishiwa kabisa. Huna chakupoteza mkiachana, si ndivyo?” Ni kama Max akataka uhakika. “Bado nina zile pesa na nyumba yangu. Najihisi nastahili ile pesa yote jamani! Ameshatumia nyingi mno. Halafu ile nyumba nilijenga mwenyewe kwa msaada wa marehemu baba yangu. Ndio urithi na ukumbusho pekee kutoka kwa marehemu baba yangu. Alinisaidia hata kusimamia ujenzi wakati mimi nikienda shule. Lela aliikuta tu. Kweli anufaike nayo tu!”  Akaongea kwa kuumia na kulalamika.

“Katika hilo huna jinsi Tino. Mtatakiwa mgawane tu. Lela amekuwa na sauti kubwa kukupita wewe. Yeye ndio anaonekana amehangaika na wewe tokea upo mgonjwa hujiwezi. Watu watasema sasa hivi umepona ndio unamgeuka! Yote uliyonieleza mimi, ni mageni kabisa kwangu. Lela anapita mtaani akitangaza halali mchana na usiku akikuhudumia wewe. Pesa yote inaisha kwa kukuhudumia wewe. Wewe mzito wa kuzungumza Tino, nani atajua hayo yote uliyoniambia mimi na kukuamini wakati ulifungiwa ukiwa una hali mbaya, unatoka ukiwa na hali nzuri!  Sabrina umemfahamu kupitia yeye mwenyewe Lela, kwa kumleta nyumbani akuhudumie. Sijui kama unanielewa pointi yangu?” Tino akaumia sana, akabaki ameinama.

“Kwa kuwa mimi nawafahamu nyinyi wote wawili, tena tokea zamani. Nakuamini, na ninajua uwezo wa Lela. Lakini nakwambia huu ukweli mgumu kukufungua ufahamu wako si kama Max, ila mwanasheria. Nataka uelewe utakavyosikika mbele ya watu na sheria! Kwa hakika najuta sana Tino. Natamani hata hapo katikati ningelazimishia kuja kukuona ili niweze kumshinda kwa hoja.” “Hatuwezi kuanzia kwa kunitelekeza mimi na msichana aliyemwajiri? Yaani huku kutokuwepo nyumbani muda wote huo, hatuwezi kuanzia hapo?” Tino akauliza kwa machozi akiwa anaona tayari hoja za msingi atakazomshinda nazo Lela.

“Ukiwa tayari tunaweza kujaribu. Hakuna kinachoshindikana. Na kama Sabrina, aliyekukuta kwenye hiyo hali akikubali kuwa shahidi yako….” “No way! Siwezi kumuingiza Sabrina kwenye ugomvi wangu na Lela. Ni heri nipoteze kila kitu lakini si kumuanzishia vita huyu binti na Lela. Lela na mwanaume wake watamsumbua sana. Itakuwa ni kama namlipa Sabrina ubaya kwa wema alionitendea! Hapana. Tafuta njia ingine.”  Hapo Tino akakataa kwa ukali kabisa na kwa msisitizo, akiona ni bora kushindwa kuliko Sabrina! Mbaya zaidi, msamiati au neno kushindwa halijawahi kukubalika kwa Max, tokea aanze hiyo kazi iliyomjengea heshima mjini. Leo Tino anataka huduma yake na kuweka mazingira ya kushindwa! Max akaona awachukulie taratibu kwani hata hivyo Tino alishakuwa na hasira naye. Akaona amrudishe kwake kwa hatua.

“Basi niachie nianze kulifikiria hilo au kulifanyia kazi. Nitatafuta njia zote zitakazo saidia kesi.” “Na mimi nimemdhibiti kwenye pesa yangu yote. Hata matibabu. Sasa nataka uwe shahidi na uwe upande wangu. Sijui utamjulisha, lakini ujue kuwa nimedhibi mianya yote ya pesa. Nimemtoa kwenye matibabu kazini na nimebadili ulinzi ili asiweze kuingia tena nyumbani kwangu.” “Sasa hapo lazima kutumia akili, Tino. Cha kwanza, nitamuandikia barua kuwa umemripoti kuwa aliondoka nyumbani kwa muda wa mwezi mzima na majuma kadhaa akakutelekeza na binti ambaye alimuajiri, bila matunzo. Sasa umeamua kwenda kutibiwa na kwa kuwa alishaondoka kwenda kuanza maisha yake na mwanaume wake, moja, umebadilisha ulinzi wa nyumba kwa ajili ya usalama wa nyumba yako.” Akili ya Max ikaanza kazi kwa haraka.

“Pili, kwa kuwa hukuwa na pesa na pesa yote amekuwa akiitumia yeye na yeye pia anayo kazi, umeelekeza pesa yote katika kujitibu wewe mwenyewe. Tatu, kwa kuwa bado hujapona kabisa na kama nakumbuka, mkataba wako na kazini kwako ni kama unakaribia kuisha, ila mahakama iliamuru wakulipe mpaka upone. Sasa nitamjulisha Lela, kwa kuwa alishaondoka nyumbani na kuanza maisha yake, wewe huwajibiki tena kwenye matibabu yake, na ili kampuni isilemewe na watu wawili, ielekeze nguvu zote kwako, umemtoa.” Tino alitamani kulia kwa furaha.

“Nakushukuru sana.” “Bila shaka. Nitahangaika angalau kulipia vile tulivyokutelekeza.” Tino akajua amepata ujumbe wake wa vile walivyomtelekeza, hapo hakumjibu akamuacha ahangaike na dhamira yake. “Nitaandaa huo wakala, nitaufanyia utaratibu wote kisheria, kisha niufikishe mahakamani na yeye nimpe. Tena kesho tu ili asituwahi.” “Hapo utakuwa umenisaidia sana. Na umwambie chochote anachotaka kuzungumza na mimi, azungumze kupitia wewe. Namuwekea restrain oder asinitafute kwa simu au kuniona, kwa kuwa amekuwa akitangaza kifo changu wakati mimi mwenyewe nipo hai. Kunitafuta ni kutaka kutimiza adhima yake.” “Sasa hapo utakuwa umefanya jambo la msingi sana. Ufanikishe hilo kwa haraka kwa kwenda mapema polisi kumshitaki na kuomba hiyo restrain order, kisha uniletee hiyo kopi na mimi.” Max akachangamkia hilo wazo. Tino akawa ameongeza nguvu kwenye kazi ya mwanasheria wake.

“Nitafanya hivyo kesho. Nitamripoti sehemu zote alizopita akidai madai yangu baada ya kifo changu wakati amenitelekeza gizani. Halafu nikuletee kopi, umfikishie.” “Hapo sawa kabisa.” Max akaafiki. Sabrina akaingiwa hofu akiwa anamsikiliza Tino na mwanasheria wake wakiongea na kupanga mipango mizito dhidi ya ndoa hiyo aliyosikia Lela aliipigania mpaka akaolewa yeye. Akakumbuka stori alizopewa na Sabina juu ya mwanzo wa Lela na Tino. “Lela anahistoria ya kutokubali kushindwa. Hii vita ni kali na mimi nipo katikati yao!” Hofu ikamwingia Sabrina.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ni nini kitaendelea kwa wanandoa hawa walioizoea sheria kuwatatulia kila jambo? Lela anaijua sheria na Tino naye hivyohivyo. Usikose muendelezo. Mambo ndio yanaanza.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment