Tamu Inapogeuka Shubiri..
Mara
nyingi awapo nyumbani, Tino akaanza tabia ya kushinda gym. Roho ikamuuma sana
Sabrina, kuona alichokuwa akifanyiwa Lela ndicho na yeye Tino anamfanyia.
Ametafuta sehemu ya kumkwepa kama alivyomwambia alikuwa akifanya nyumbani
kwake, kuishi kwenye kinyumba cha pembeni, akikwepa karaha za Lela. “Sasa
mimi nimefanya nini mpaka awe ananikwepa!” Akajiuliza Sabrina bila jibu
asijue sumu aliyokwisha mwaga Max juu yake.
Chakushangaza,
ni kama Tino akaacha kuzungumzia maswala ya ujauzito kabisa! Akiwa anampeleka
mazoezini huko hospitalini, basi atajifanya yupo busy na simu yake ilimradi tu
kumuonyesha Sabrina yupo busy, hawezi kuzungumza kabisa, kitu kilichozidi
kumtia wasiwasi Sabrina.
Basi
akimshusha mazoezini, akiwa anafanyiwa mazoezi ya viungo na wataalamu ili
kurudisha nguvu kwenye huo mkono wake wa kulia, yeye Sabrina alibaki nje tu akisubiria
asijue hatima ya hayo maisha ni nini ila kutaka kujua kama alishika mimba au
la. Akabaki akitamani aanze siku zake/hedhi ili apate kitu chakumwambia Tino
pengine amfurahishe asijue chuki aliyo nayo Tino dhidi yake. Tino alimuhesabu kama
mtu mbaya sana aliyekaribu yake tokea mwanzo kwa hila tu ili ajinufaishe kwake.
Alibaki akijiwinda naye kwa hila zozote Sabrina anazompangia na uchawi wowote alioambiwa
anao, akitafuta jinsi ya kumtoa kwenye maisha yake. Ukimya huo uliokuwa
ukimshangaza Sabrina asijue ni Max alimwambia Tino watulie kabisa, wampe siku
chache, ili Tino ajiridhishe kwa hakika hajamuacha na mtoto ili asije kumtafuta
tena baadaye na kudai makubwa zaidi ya Lela kwa kisingizio cha huyo mtoto.
Siku ngumu na za wasiwasi kwa kila mmoja wao, zikazidi kusonga wakiwa wanaendelea na kuhudhuria kliniki ya Tino na Sabrina kutojua kinachoendelea popote hata hapo hospitalini kwani hata hapo Tino alipokuwa akiingia ndani kwa mazoezi au kuzungumza na daktari, basi alianza kumtaka amsubirie nje asiingie naye ndani. Ikawa kukaa nje akisubiri si chaguzi tena ila lazima. Huo usiri na sintofahamu ukaendelea kwa Sabrina ndipo sasa akaanzisha tabia ya kila akisikia tu simu ya Tino ikiita, yeye ndio anatoka na kuacha simu yake ikirikodi mazungumzo yote kwa siri ili kujua kinachoendelea. Akiachwa nje wakati Tino akifanyiwa mazoezi hapo hospitaini, KCMC basi ndipo alikuwa akipata muda wa kusikiliza simu yake kujua walichozungumza Tino na Max kama simu yake ilifanikiwa kuiba mazungumzo yao, ilimradi tu ajue kinachoendelea. Akafanya hivyo bila mafanikio makubwa sana. Kwani aligundua Tino ni mpokea maagizo tu. Hakuwa akimsikia akijibu sana ila mara nyingi yeye anakua msikilizaji wa kile anachoagizwa kufanya na Max au akipewa kinachoendelea huko Dar, Sabrina anaokota neno moja moja na kuunganisha yeye mwenyewe kwa kutumia akili. Ila akajua Max ndiye amemgeuka kwa hakika. Kwa umbali gani na kwa nini, bado akawa hajajua!
Kisicho
Ridhiki, Hakiliki.
S |
iku 10
tokea kugeukana kuanze na swala la Sabrina kuwa ameshika mimba kuonekana si
tatizo kwa Tino tu hata kwa Max pia, Tino akiwa anafanyiwa mazoezi, Sabrina
amekaa nje akimsubiri ikabidi Sabrina atulize mawazo na aanze kuhesabu mzunguko
wake wa hedhi. Tangia siku ya mwisho kuona siku zake mpaka siku hiyo. Akahesabu
kwa makini kwa kurudiarudia akagundua mwezi umeshapita. Hofu ikazidi. “Au
sababu ya wasiwasi nimepitisha siku!?” Akajaribu kujifariji, lakini
akakumbuka yeye sio mtu wakupitisha siku hata mara moja. Akabaki akiwaza asijue
siku hiyo ndio zimeshatimu siku za Max wakiwa wamehesabu na Tino tokea waanze
kukutana kimapenzi na Sabrina, wakapanga kumuuliza kwa hakika kujua kama
ameshika mimba au la.
Tino akatoka akamkuta amejiinamia.
“Nimeshamaliza.” Sabrina akasimama. “Vipi lakini, unaonaje?” Sabrina akajaribu
kutupia swali la kujali kwa upole. “Nafikiria kwenda nje ya nchi kwa matibabu
kama huyu therapist/mtu anayenifanyia mazoezi alivyonishauri.” Wakaongozana mpaka kwenye gari lakini Sabrina
akajua ndio anaachwa, safari haimuhusu tena. Akatulia tu.
Walipoingia
tu kwenye gari, Tino akauliza swali la moja kwa moja. “Bado hujapata tu siku
zako?” Moyo wa Sabrina ukashituka kwa hofu. Akameza mate kwa wasiwasi, Tino
akamuona na kupata jibu lake. “Nisikilize Sabrina, mimi nahitaji tumalize hili
swala la huu ujauzito, nikatibiwe. Tafadhali using’ang’anie kubakiwa na
ujauzito ambao hata wewe mwenyewe huna pakuishi!” Sabrina akaumia sana,
akamtizama Tino, asiamini. Lakini akajikaza kuendesha.
Hapo
ndipo akapata jibu lake kwa hakika kuwa anaachwa. “Tino hajakosea. Nikibaki
na hii mimba, mtoto nitamuweka wapi?” Akajiuliza Sabrina huku akijilaumu
sana. Sabrina akaanza kujiuliza na yeye. Atafanyaje! Hana hata pesa yakueleweka!
Ataishije huyo Tino atakapoondoka? Akabaki kimya. Akaendesha mpaka hapo wanapoishi.
Akaegesha gari sehemu yao. “Unapatwa ugumu gani kuamua jambo rahisi hivi
ukilinganisha na mazingira yako? Kwa nini unang’ang’ania hiyo mimba!? Una
malengo gani nayo ya baadaye ambayo labda hukuniambia?” Sabrina akamwangalia
akashindwa ajibu nini. Akachomoa funguo za gari. “Nikusaidie kubeba kitu?” Akauliza Sabrina. “Tafadhali naomba tumalize
hili swala nijue moja.” Tino akaendelea kuweka msisitizo.
Sabrina
akashuka garini na kuingia ndani, Tino akamfuata. “Sijui kama unanielewa
Sabrina!?” “Tafadhali nipe muda wakufikiria Tino. Wewe kwako umeshafikia
maamuzi ya mwisho kuwa hutaki mtoto. Mimi bado. Nahitaji muda.” “UNAHITAJI
MUDA WA NINI!?” Akauliza Tino kwa ukali sana. “Nimeshakwambia
mimi sihitaji mtoto. Nataka nikatibiwe. Mbona kama unataka kunifunga!?”
Sabrina akamtizama asiamini kama anazungumza na Tino.
“Natakiwa
Dar kesho kutwa. Sina muda wa kupoteza mimi! Nataka tufikie mwisho wa hili.
Kama ni muda, nishakupa siku 10 sasa tokea mwanzo tunazungumzia hili.” Sabrina
akajua kumbe siku hiyo ndio alipanga amuulize! Alikuwa akimuhesabia tu! Kwamba
ameshapanga siku ya kumuacha! Sabrina akamtizama nakushindwa kuamini. Tino sasa
hivi anapanga mipango yakumuhusu yeye bila kumjumuisha!
“Na
kuna sehemu kabisa naweza kukupeleka hapahapa Moshi, wanaweza kukusafisha
vizuri tu ukaendelea na maisha yako kama kawaida. Tukabaki hatudaiani.” Sabrina
akashangaa sana. “Kumbe muda huu wa siku hizi 10 nakuona kimya kumbe ndio
mipango hiyo inayoendelea kati yako na Max!?” “Tafadhali rudi kwenye pointi
Sabrina. Acha kuongea sana, utanichosha. Tafadhali tumalize hili. Na kama
utatoka hapo mgonjwa, ninaweza kuzungumza na huyu baba akatuongezea muda hapa
zaidi, ukakaa hapa mpaka upone.” “Kama muda gani?” Sabrina akauliza kwa uchungu
akijua hakuna chakuokoa tena, mipango imeshawekwa, Tino hataki kurudi nyuma.
“Wowote ule utakaotaka wewe. Ila kuwa tu muungwana, ukijua hawezi kukuweka hapa
kwa muda mrefu, hili ni eneo la biashara.” Sabrina akabaki akimtizama Tino.
“Tafadhali
naomba twende kesho, tukakamilishe hili na sitakuacha mikono mitupu. Nitakulipa
pesa yakutosha mpaka kuanza maisha yako.” Sabrina akavuta pumzi kwa nguvu. “Naondoka
kesho kutwa Sabrina. Ninayo siku ya kesho tu. Naomba usipoteze muda. Fanya
maamuzi sahihi, nimpigie simu huyo atakayekushugulikia, kesho twende.” “Sawa.”
Tino hakuamini kama amefanikisha hilo. Akajua pesa ndio imemvutia Sabrina na
kukubali. Kwa mara nyingine tena baada ya muda mrefu Sabrina akamuona Tino amerudi
kuwa mwenye furaha na kuzidi kumuumiza moyo.
“Sasa
mpigie simu huyu mwenye hizi Villa, Mzee Swai. Muombe miezi mitatu mbele. Ili
nipate pakuishi wakati nikijipanga. Halafu unipe pesa usiku huu huu nianze
kujipanga nijue nafanya nini kwenye huu mji.” “Hutaki kurudi Dar?” Tino
akauliza akimpima tu, akitaka kujua kama anarudi Dar na jinsi ya kujipanga
kumkabili huko Dar endapo anapanga kurudi. “Naomba mpigie simu mzee Swai
tafadhali.” Sabrina akaingia chumbani bila ya kumjibu swali lake. Akiwa
chumbani, akamsikia Tino akizungumza na Swai. Wakataniana tena kidogo,
akamsikia akiomba hifadhi kwa ajili yake. Akajua amekubaliwa baada ya kumsikia
Tino akishukuru.
Akamfuata
chumbani kwa furaha. “Amekubali.” Sabrina akageuka maana mlango ulifunguliwa
kwa nguvu. “Amesema usiwe na wasiwasi. Kukitokea tatizo lolote, umpigie yeye
mwenyewe simu moja kwa moja.” Akabaki akimtizama Tino alivyo na furaha
yakumuacha pale, bado Sabrina asiamini kama ni Tino yuleyule! Bila kupoteza
muda, Sabrina akachukua hiyo namba ya simu. Akaitunza kwenye simu yake. “Na
ujue nitakuachia pesa nzuri tu.” Akasisitiza Tino kama kumtaka asibadili
mawazo. Akamtajia hiyo pesa atakayompa, hata Sabrina mwenyewe hakuamini.
Akafurahia sana moyoni, lakini hakumwambia. “Nakupa hundi yako sasa hivi.” “Na
kabla hatujaenda kuua huyu mtoto, lazima tupitie benki niweke hii pesa
kwanza, nikihakikisha imeingia kwenye akaunti yangu ndipo twende tukaue.”
“Acha kusema hivyo bwana! Huyo hata sio mtoto.” Tino akakanusha huku akicheka
kama kitu kizuri. Sabrina akamtizama na kuondoka pale.
Asubuhi
Ngumu Maishani Kwa Sabrina.
A |
kiwa
chumbani akijiandaa watoke, alimsikia Tino akizungumza na mtu amkatie tiketi ya
ndege ya kuondoka hapo Moshi siku inayofuata ili kumrudisha Dar. Sabrina
akabaki akimfikiria Tino. Alikuwa na maumivu makali sana moyoni mwake, hata uso
ulionyesha lakini hapakuwa na namna. Alijua Max na Tino wote macho yako kwake,
akamilishe kumtoa huyo mtoto, asijue ni kwa nini Max ameng’ang’ania kuua mtoto
wa mwenzie wakati yeye anao watoto wawili! Ila akanyamaza tu na kumshangaa sana
Tino anawezaje kukubali ushauri wa kinyama kiasi hicho! “Labda tatizo ni
kuzaa na mtu kama mimi!” Akajidharau Sabrina kwa machungu zaidi.
Lakini
kama alivyokusudia asiachwe mikono mitupu, akahakikisha wanaanzia benki. Tino
akiwa anamsubiria kwenye gari, yeye akaingia benki. Akahakikisha yale mamilioni
ya pesa yanaingia kwenye akaunti yake, ndipo wakaelekea huko kwenye kutoa
mimba. Njiani kila mmoja akiwaza lake.
Walifika
kwenye hiyo kliniki. Tino akaomba kuzungumza na daktari aliyemtaja kwa jina
kabisa. “Anatutarajia.” Akaongeza Tino kwa muhudumu aliyemkuta hapo mapokezi,
Sabrina akamwangalia kwa masikitiko. Kwa haraka huyo daktari alipoitwa akatoka.
Wakasalimiana. “Kila kitu kipo tayari.” Daktari akaongea akifikicha mikono kama
anayesema yupo tayari kwa kazi. “Nashukuru sana.” Tino akashukuru na kumtizama
Sabrina aliyebaki akishangazwa na hayo maandalizi. Kwamba kila kitu kilikuwa
tayari ila yeye tu na hilo tumbo lake! “Unataka tuingie wote?” Tino akauliza. “Hapana.
Wewe nisubiri tu hapa.” Sabrina akakataa wakaondoka na yule daktari.
Wakaingia
kwenye hicho chumba. Akakuta hicho kitanda na vyuma vingi tu kwenye kimeza
pembeni ya hicho kitanda, vikimsubiria yeye. Hofu ikamwingia Sabrina kila
akifikiria hivyo vyuma vitaingizwa kwake ili kumuua huyo kiumbe asiye hatia!
Mwili mzima ukaaza kutetemeka kwa hofu. Wakampisha ili atoe nguo na kuvaa gauni
la hapo. Akatoa nguo akavaa kigauni cha hapo alichokuwa amekabidhiwa avae kwa
ajili ya shuguli nzima. Sabrina akabaki amejilaza hapo juu ya kitanda
alichoambiwa ajilaze baada ya kubadili nguo, akifikiria na vyuma vyote
vikimwangalia yeye. Hofu imemjaa, miguu ameifungamanisha asiamini starehe
aliyoipata yeye na Tino wakati wa kutungwa hiyo mimba, leo vyuma vinamsubiri
kumuingia yeye ili atolewe huyo mtoto!
Tino yupo nje ya chumba cha kutolea hiyo mimba
akisubiria kwa shauku kubwa shuguli nzima ikamilike, aachane na Sabrina moja
kwa moja asije akamfuata tena baadaye na arudishe ripoti nzuri kwa Max
aliyeamini yupo upande wake anamtakia mema. Max naye yupo kwenye simu wakati
wote muda huo, sikioni kwa Tino akihakisha Tino anasimamia zoezi la kuua mtoto
wake mwenyewe, linakamilika bila Sabrina kubadili mawazo na Max huyuhuyo pia
yupo sikioni kwa huyo daktari aliyemtafutia Tino kuhakikisha anakamilisha zoezi
zima la kuangamiza huyo kiumbe bila kukosea ili Tino arudi Dar wakakamilishe
kesi yake na Lela na yeye apate pesa yake. Daktari na yeye yupo tayari
kukamilisha shuguli nzima ya kuua hicho kiumbe kisicho na hatia, tumboni kwa
Sabrina ili apokee malipo yake mazuri ya uhakika.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usikose muendelezo wa Tamu inapogeuka Shubiri.
0 Comments:
Post a Comment