Maamuzi Magumu…
B |
aada ya
muda yule daktari akarudi kwenye chumba alichokuwa ameachwa Sabrina. Akamtia
moyo katika maamuzi yake ili kumfanya atulie na asibadili mawazo kama
alivyoagizwa na Max. Maana umbali wa pesa iliyononeshwa na waleti yake huyo
daktari ni huyo mtoto tumboni kwa Sabrina. Sabrina akatulia akimwangalia na kumsikiliza
jinsi anavyomshawishi mpaka akakinahiwa rohoni. “Nimebadili mawazo.” Sabrina
akamkatisha na kukaa. “Max amekuahidi Tino atakulipa pesa nzuri ili umuue huyu
mtoto.” Sabrina alikwenda moja kwa moja akiitambua hila ya Max kwa yule daktari,
kama akimwambia najua nani yupo nyuma ya huo mdomo wako. Yule daktari
akababaika sana Sabrina akimwangalia tu jinsi anavyoongea hili na lile akiokota
hekima za hapa na pale akijitetea mpaka Sabrina akajua anaweza akamtoa kwenye
malengo yake na yeye.
Akamuwahi
kwa kumuweka na yeye sawa. “Mimi naelewa upo kazini na unatengeneza pesa kwa
kuua hawa watoto.” “Ukiiweka hivyo unakosea.” Akakanusha huyo daktari, Sabrinaakimtizama kwa kumsuta. “Sasa fanya hivi, tukae humu ndani kwa muda wakutosha
tu. Kisha wewe utoke hapa, ukamwambie Tino kuwa wakati ukinishugulikia nimepoteza
damu nyingi sana, inabidi unilaze uniangalie kwa siku mbili. Yeye anaondoka na
hana mpango wa kuja kukutana na mimi tena. Basi. Wewe utakuwa umepata pesa
yako, mimi naendelea na masha yangu. Hutaniona tena na wala Tino hataniona
tena.” Yule daktari akasita.
“Hii
nafanya kwa ajili yako tu. Kukusaidia kupata pesa uliyoahidiwa. Mimi naweza
kutoka hapo kwenye huo mlango, na nikamwambia nimeamua kutoua mwanangu, na
asinifanye chochote ila wewe ndio
utakosa pesa. Sasa unataka pesa ya bure au la!” Sabrina akamuuliza kijasiri.
“Lakini utataka nikulaze hapa kwa siku mbili?” “Anarudi Dar kesho asubuhi. Nikishauliza
pale tunapoishi nikiambiwa kama ameshaondoka na mimi naondoka hapa. Sina haja
ya kuendelea kulala hapa siku mbili.” “Sawa. Ila usije nitaja?” “Na wewe
hivyohivyo. Jibu lako ni ulifanikiwa kuua huyu mtoto.” “Tafadhali usitumie
lugha hiyo.” Sabrina akamwangalia tena kwa kumsuta, yule daktari akanyamaza.
Akatafuta na yeye sehemu, akakaa hapo ndani kwa muda. Nje wakijua kazi
inaendelea huko ndani, kumbe wote wamekaa tu hapo ndani.
Baada
ya muda huyo daktari akaangalia saa yake ya mkononi. “Sasa itabidi hata
kukuwekea maji, ili akitaka kukuona angalau aamini.” “Hata ukitaka kunichoma
sindano ya usingizi pia sawa. Ili akija ajue nimechoka sana, siwezi hata
kuzungumza.” Hilo akalikubali kwa haraka. Akamuwekea dripu vizuri, akamuwekea
na dawa ya usingizi, Sabrina akaanza kusinzia. Akamtoa hapo na kwenda kumuweka
kwenye chumba cha kupumzikia wagonjwa. Hapakuwa na watu wengine. “Huwa hatulazi
watu hapa.” Sabrina akamshukuru na kupotelea usingizini.
Kwa
mbali akamsikia yule daktari akizungumza hapo na Tino. Akimdanganya kwa mengi
huku akitumia maneno mazito ya kidaktari mpaka Tino akaamini. “Pole Sabrina.
Lakini umefanya uamuzi mzuri na sahihi. Kesho nitakuja kukuaga wakati
naondoka.” Sabrina akatingisha kichwa kukubali huku amefunga macho. Sababu ya
mawazo na wasiwasi, Sabrina hakuwa amelala usingizi mzuri vile. Alilala bila
hata kugeuka. Asubuhi sana akamshwa na haja ndogo. Alikwenda kujisaidia huku
akipepesuka kwa madawa ya usingizi akiwa peke yake hata Tino hakujitolea kulala
naye kinafiki tu, ili amuuguze japo kwa usiku huo mmoja tu angalau akumbuke
fadhila! Akamuacha Sabrina peke yake hospitalini akijua mgonjwa na amepoteza
damu nyingi. Alipofika tu chooni, kitu cha kwanza akajiangalia vizuri akiwa na
wasiwasi pengine yule daktari alimtoa mimba akiwa amelala, akagundua alikuwa
muaminifu bado hakuwa akitokwa damu yeyote. Akatoka hapo chooni.
Palikuwa
kimya kuashiria hapakuwa na mtu hapo ndani. Akarudi kulala mpaka kama kwenye
saa moja hivi akasikia mlango ukifunguliwa, alikuwa yule daktari. “Dripu
niliitoa usiku ili usisumbuke ukitaka kwenda chooni. Lakini itabidi
niirudishie. Anaonekana atapita hapa kwenye saa mbili kasoro akiwa njiani
kuelekea uwanja wa ndege.” “Nakushukuru sana. Asante.” Akamrudishia tena ile
dripu, akapotelea usingizini tena.
Mpaka
alipoamshwa na Tino. “Vipi?” “Uchovu tu. Ndio unaondoka?” “Hapa nawahi KIA.
Nimekuitishia kifungua kinywa. Daktari amesema anaweza kukuruhusu mchana.”
“Nashukuru.” Sabrina akafunga macho. “Acha mimi niwahi. Nitamtuma mtu aje
achukue gari.” Sabrina akashituka mpaka akafungua macho. Akakumbuka na gari sio
yake. “Lini?” “Nafikiria labda weekend hii.” “Sawa.” Ikabidi awe mpole. Tino
akasimama hapo kwa muda, akaondoka asiamini kama anafanikiwa kuondoka Moshi
bila huyo Sabrina aliyekuwa akisakwa na Lela kwa udi na uvumba huko Dar, awe
shahidi yake, Sabrina asijue maana amewafungia watu wote simu. Hapatikaniki.
Max
alihakikisha anamwambia Tino, asijerudi Dar au hata kuja kuonekanika tena na
Sabrina kwa kuwa ndio ushahidi pekee uliobaki kwa Lela. Lela akifanikiwa
kumpata tu Sabrina tu, yeye ndio atakuwa shahidi wake kuwa Lela hakumtelekeza
Tino, alimuacha kwenye mikono ya mfanyakazi aliyemtafuta mwenyewe ambaye ni
Sabrina. Max akamwambia Tino, hatari kubwa ni pale Lela atakapo kutana na
Sabrina aliye mjamzito. Akamwambia kwa hakika watamuacha barabarani asiwe hata
na pakuishi. Tino anaondoka Kilimanjoro bila Sabrina, akipongezwa na Max
vilivyo.
Mwisho
wa Sabrina na Tino.
A |
kashangaa
kitu kimemkaba kooni anashindwa hata kuhema. Alilia Sabrina. Alilia kwa kwikwi
na uchungu mkali sana moyoni. Akakumbuka jinsi alivyohangaika na Tino!
Alipokuwa akimpangusa mavi na kumtibu madonda yaliyokuwa yamesuswa na watu wote
waliokuwa wakimfahamu Tino mpaka huyo Max mwenyewe! Madonda mabaya yakutisha yaliyokuwa
yamejaa matakoni kwake mpaka kufika mgongoni na katikati ya mapaja yakiwa na
kinyesi chake! Akakumbuka jinsi alivyomuuguza kwa shida, akisimangwa na Lela
mwenyewe. Akakumbuka kashfa za Emma alipomkuta na huyo Tino, lakini akajikaza
akimtibu kwa upendo! Lakini leo Tino anamuacha yeye hospitalini! Sabrina
akazidi kulia asiamini kama ule ndio ulikuwa mwisho mbaya vile na Tino.
Alishakuwa
na wasiwasi na hitimisho lao. Alijua wao hawaendani kabisa, lakini hakujua kama
wangeachana vibaya vile. Akakumbuka maneno ya faraja aliyofarijiwa na Tino kuwa
wataweza kuishi tu pamoja. Asiwe na wasiwasi juu ya tofauti ya umri na utajiri.
Lakini leo Tino anamuacha yeye hospitalini akiwa mgonjwa! Sabrina akajiambia
kweli mwanadamu si Mungu. Hubadilika. “Lakini
asingekuwa Tino!” Akazidi
kuumia na kulia mpaka akapitiwa tena na usingizi.
Sabrina
Aachwa Tena. Safari hii na ujauzito.
Mchana
alimshwa na yule daktari, akamruhusu. Alitoka hapo kwenye hiyo dispensary
asiamini anarudi kwenye ile Villa akiwa peke yake. Tino hayupo! Lakini hapakuwa
na jinsi, ilibidi aondoke pale na maisha yakaendelee. Alipofika ndani alikuta Tino
alichukua nguo zake zote. Hakubakisha hata chupi moja. Sabrina akaanza kulia
tena huku amejishika tumbo. Aliitumia siku hiyo na mbili mbeleni kulia tu na
kushindwa kufikiria. Alipoanza kusikia kichwa kinagonga kama kuna mtu anapiga
ngoma huko ndani, akajiambia asijilize tena, Tino ndio ameondoka, hatarudi
tena. Hana mama wala dada wa kuzungumza naye kinachoendelea kwenye maisha yake
kwa wakati huo. Akajua anatakiwa kupambana peke yake. Akajituliza.
Ilipofika
ijumaa, Tino akampigia simu. Baada ya salamu ya kawaida akamwambia kuna kijana
amemtuma huko Moshi kuchukua gari yake. “Sawa.”
Bila shida Sabrina akakubali. “Kwaheri.” Tino
akaaga bila nyongeza ya kumjulia hali. Hakuuliza hata maendeleo yake tokea
amuache hospitalini daktari alipomwambia anamlaza kwa kupoteza damu nyingi!
Sabrina akaanza kulia tena, lakini akakumbuka anajihitaji yeye na akili yake
ili kuweza kuendelea na maisha. Akanyamaza kwa haraka akijifuta machozi. “Kulia haitanisaidia kwa lolote.” Akakumbuka
gari ya watu inakuja kuchukuliwa. Akatoka hapo na kwenda kwenye gari kuangalia
kama aliacha kitu chake chochote humo. Akachukua kila kitu na kuisafisha hiyo
gari.
Kesho
yake asubuhi na mapema gari ikaja kuchukuliwa. Sabrina akilisindikiza kwa
macho. Akajishika tumbo asiamini kama ameachwa rasmi na mtoto. Hapakuwa hata na
dalili ya tumbo kuwa na mtoto. Kamwili kake kembamba kaliachwa vilevile. Baridi
ikamrudisha ndani. Upweke ukamwingia mpaka kwenye mifupa. Kweli akatamani kama
angekuwa nyumbani. Gafla akamisi mpaka yale mazingira ya nyumbani kwao. Japokuwa
alikuwa akisimangwa, lakini kulikuwa na watu wakuzungumza naye. Kijana wa
kushugulikia ng’ombe aliyekuwa akifanya naye kazi, na dada wa kazi pia walikuwa
wakipatana sana. Wakiwa jikoni vicheko vilikuwa haviishi kati yao, wakipeana
stori za mtaani na gengeni wanapokwenda wakitumwa. Basi hayo ndio yakawa maeneo
yao hao wawili yakujidai. Wakajikuta wakipatana hata usiku wakilala stori huwa
zilikuwa zikiendelea na vicheko. Lakini siku hiyo Sabrina akajikuta kwenye
hicho chumba kizuri sana, Moshi, ndani ya Villa ya kitalii, akipishana na
wazungu tupu kuashiria ndio wageni wa hapo na ndio wanaoweza kupamudu hapo
kimalipo. Inamaana alikuwa kwenye mazingira mazuri sana kuliko nyumbani kwao,
pesa ipo benki sio kama zamani, lakini yuko peke yake na mtoto anayekuwa
tumboni, baba yake ameondoka akiridhia amemuua!
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
M |
wezi wa kwanza
ukaisha akiwa peke yake hata Tino asimsikie. Na wembamba wake mimba ya miezi
miwili kitumbo chake kidogo kikaanza kuwa kigumu kwa chini. Taratibu akili
ikaanza kuamini kuwa kuna mtoto humo ndani. Akili inatakiwa izidi kufikiri zaidi
kabla mtoto hajaja duniani. Wapi atamuweka! Ni kweli kwa wakati huo alikuwa
akiishi bure, kasoro chakula ndio alikuwa akigaramia. Huo ukawa mwezi mmoja
tokea kuondoka kwa Tino. Akajiambia amebakisha miezi miwili kuondoka hapo.
Akaanza kuzunguka hapo mjini kwenye madaladala. Pesa anayo yakufanyia biashara,
swali likawa biashara gani atafanya na huo ujauzito! Akapiga mahesabu. Muda wa
hiyo biashara kuanza, makosa atakayofanya hapo katikati mpaka aifahamu hiyo biashara
na kupunguza makosa na kuanza kupata faida, akajua kwa wakati huo muda haupo rafiki.
Anaweza anza, biashara ikiwa ipo sehemu inayomuhitaji zaidi yeye ili iianze
kumlipa sasa, ndipo kikawa kipindi cha yeye kujifungua. Akaona ni bora atafute kazi yeyote
yakujishikiza mpaka ajifungue na mtoto akue kidogo ndipo aanza biashara.
Ikaanza
kazi ya kutafuta kazi. Kukawa na ahadi tu. Mwezi wa pili wa kuisha hapo nao
ukaisha bila kitu chakumuingizia kipato ila kutumia akiba aliyokuwa nayo. Na upweke
nao ukazidi. Akamkumbuka Jack. Akalia sana akimkumbuka Jack akijutia nafasi
aliyompa akimkaribisha kwake, ila yeye kuamua kumkatalia yeye Jack, ili abakie
na Tino. Akaumia sana na kumkumbuka Mungu aliyemtoa nyumbani kwao. Sabrina
akalia sana kwa majuto.
Akakumbuka
maombi aliyokuwa amemuomba Mungu. Akifunga kwa uwaminifu bila kula japo alikuwa
akifanya kazi ngumu, lakini alikusudia kuutafuta uso wa Mungu ili kumsihi
amkumbuke pale alipokua. Alimsihi Mungu alainishe mioyo ya wazazi wake
wamruhusu kwenda mjini kuwa huko ndiko akakutane na mlango wake wakutokea
kimaisha. Mungu akafanya. Ndio ameishia hapo! Akajutia sana akiamini mlango wa
kwa Tino haukuwa sahihi, alijipitisha tu huko bila Mungu. Mlango sahihi Mungu
aliokuwa amemuandalia kumtoa kimaisha ilikuwa ni kwenda kwa Jack kufanya naye
biashara. Akajuta sana lakini asiwe na jinsi ya kubadilisha hilo.
Zoezi
la toba nalo likaanza akitubu kwa Mungu aliyempa nafasi na kuichezea. Ikawa
hali ya kujilaumu kwa hili na kujifariji kwa lile akijiambia ni Mungu ndiye
aliyemtuma kwa Tino ili amtoe kiumbe chake mautini. Basi akikumbuka hilo na
kukubaliana nalo kwa wakati huo, zoezi la kufunga akimdai Mungu, Yeye ndio
amlipe linaaza. Atafunga akilia bila kula na ujauzito wake akiwa mwaminifu
kwenye maamuzi yake hayo mbele za Mungu akitaka yeye aliyemtuma kwa Tino, akawa
muaminifu akimuhudumia Tino mchana na usiku bila kumfanyia ubaya wowote mpaka
akapona, basi yeye Mungu aliyemfanikisha kwa kiwango kile kwa Tino, basi amlipe.
Basi hapo atadai haki zake mbele za Mungu akisimamia milango yake atakayochagua
kutoka kwenye bibilia bila kuchoka. Akifanikiwa siku moja na ya pili kumdai
Mungu akiwa amefunga, mawazo nayo ya hukumu yanamrudisha nyuma. “Lakini Mungu hakunituma kukimbilia kwenye kitandani cha
ndoa cha Tino!” Basi hapo napo Sabrina ataanza tena zoezi la kutubu tena
kwa uzinzi. Atafunga akiomba toba mchana na usiku akijitakasa bila kula wala
kunywa, ilimradi tu ikawa hali ngumu na mvurugano kwa Sabrina.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
S |
iku moja
akiwa amezidiwa na upweke asijue hata kama Mungu anamsikia tena na amemsamehe
maana mambo yake yalizidi kwenda sivyo, kazi hapati na wala hapakuwa na dalili,
akaamua kuingia Whatsapp
ili kumfungulia Jack.{Unblock} Ili tu kumuona sura yake ajitulize nafsi. Lakini
alipofungua akakutana na picha ya msichana mrembo sana. Ilikuwa usiku. Akalia
Sabrina, akajutia sana kuchezea bahati. Jack ameweka mwanamke kwenye profile
yake! Inamaana safari hii, kwa mara ya kwanza amepata wa ukweli, ameamua kuweka
hadharani! Sabrina akaumia sana. “Nilifikiria
nini mimi!?” Akajiuliza bila jibu huku akijilaumu kwa kukimbilia
kitandani na Tino ili kumfurahisha mume wa mtu.
Napo
alipochoka kulia, akarudi tena kwenye profile ya Whatsapp ya Jack
kumuangalia mrembo aliyefanikiwa kuipamba profile yake. Dada alionekana ni wa
viwango haswa. Alionekana ni dada anayejielewa, msafi na amejitengeneza,
amevutia. Akaona asiwe mchoyo wa pongezi. Akachukua ile picha, akamtumia tena
Jack mwenyewe na ujumbe mfupi. ‘Hongera sana Jack.
Naona umepata kitu chema.’ Akautuma huo ujumbe. Baada ya muda akamuona
yupo online. Akaona amesoma baada ya kuona tiki mbili za bluu. ‘Leo umenikumbuka mrembo?’ Jack akarudisha huo ujumbe.
‘Sijawahi kukusahau Jack. Ni maisha tu. Mzima lakini?’
Sabrina akafurahia kujibiwa na Jack, na
yeye akarudisha majibu kwa haraka. ‘Mimi mzima mama.
Hofu kwako!’ ‘Nimefurahi kusikia hivyo Jack. Nakuombea ufanikiwe.’
Akarudisha huo ujumbe.
‘Mbona unaninyima kujua hali yako? Unaendeleaje? Kazi iliisha?’ Baada
ya kusoma huo ujumbe wa Jack, Sabrina akajikuta
akilia. Akalia sana kwa uchungu asijue amjibu nini Jack. Akaona atoke kabisa Whatsapp.
Akabaki ameshikilia simu akilia. Alijawa hofu na mimba hiyo ya miezi mitatu,
akaamini alichoambiwa na Tino. Na Tino hakutania. Alimuonyesha kwa vitendo hana
muda naye. Tokea achukue gari yake, hakumsikia tena. “Ila kwa hakika sitarudi nyumbani na hii mimba!” Sabrina
akalipitisha hilo wazo kwa machozi ya hofu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mimba inamiezi mitatu, amebakisha mwezi wa kuishi
bure hapo kwenye Villa. Kazi imekua ngumu kupata. Kwa Jack nako kumeshakuwa na Mrembo
mwingine.
Ni nini Kitaendelea kwa Sabrina?
Usikose muendelezo….
0 Comments:
Post a Comment