Sabrina
akashindwa ajieleze lipi aache lipi. “Kwanza uko wapi?”
Jack akaendelea kuhoji taratibu akimsikia Sabrina akilia. “Nimeachwa kwenye Villa hapa Moshi. Hata sijui pakwenda
Jack! Nipo peke yangu.” “Njoo Singida. Kesho
asubuhi nenda kapande mabasi ya Singida, mimi nitakupokea kituo cha mabasi
Singida?” Sabrina alilia, akalia sana, Jack akimsikiliza. “Umenielewa?” “Naogopa
Jack, naogopa sana. Sijawahi kuogopa hivi!” Sabrina akaongea akilia kwa
kwikwi. “Kwa kuwa upo peke yako. Njoo huku tutajua
chakufanya. Hata kesho njoo. Usikae huko peke yako. Njoo, nitakupokea.” “Asante Jack. Nakushukuru.” Akakata simu na kuanza
kujifikiria. Anakwendaje kwa Jack na tumbo hilo! Na mabaya yote aliyokwisha
kumtenda mpaka hapo ana huo ujauzito!
Akaangalia
pale alipo na vinavyomzunguka, akazidi kupatwa ugumu. Abebe kipi na aache kipi!
Na wapi! Amemuona Jack na mwanamke, anakwenda kule kama nani! Sabrina akazidi
kuwaza, na kuona sio sawa kwa Jack. Starehe apate yeye, shida akale na Jack!
Jack amekuwa mwema sana kwake. Hajawahi kumchoka. Akakumbuka chuoni. Jinsi
alivyomtukana. Alivyoachwa vibaya na Emma, Jack akamuokoa. Miezi michache
iliyopita wakawa kwenye mawasiliano mazuri mpaka kufikia hatua ya kukubaliana
kuanza biashara pamoja, huku akimtamkia waziwazi anamkaribisha nyumbani kwake
na bado akitaka anaweza akawa yeye ndio mama mwenye nyumba! Tino akaingilia
kati. Akamtumia tu ujumbe wakuahirisha makubaliano yao, na kumblock kila
mahali. Leo aende akiwa na mimba ya mtu mwingine, tena Jack akiwa amebahatika
mwanamke mzuri vile! Akaona hatamtendea haki. Anastahili pumziko na mwanamke
wake mpya. Sabrina akawaangalia tena pichani na kujikuta mawazo yanamtoa pale
kwenye profile ya Jack.
Chuoni.
K |
umbukumbu
zikamrudisha alipokuwa chuoni kabla ya kutendwa na Emma. Akakumbuka kipindi
hicho Jack alipomtongoza na kumshushua vibaya mbele ya mawaziri waliokuwa
wakifanya kazi chini yake Jack aliyekuwa anababaikiwa sana hapo kwenye hicho
chuo. Kwanza alikuwa ni Jackson Msindai! Mtoto wa Msindai! Jina linavuma nchini
sababu ya mama yake na kaka yake ambao wameshika nyadhifa za juu sana
serikalini. Hata yeye uongozi wake hapo chuoni ulikuwa bora. Kijana aliyetoka
kwenye familia ya uongozi. Walimu wenyewe walikuwa wakimsifia anajua kuongoza. Halafu
hata muonekano wake ulikuwa unavutia. Jackson hakuwa mbaya! Wakati wote ni
msafi. Mtanashati. Halafu pia alisifika kwa akili nzuri za darasani. Kila mtu
alikuwa akimfahamu Jackson Msindai na
kutaka kuwa naye karibu lakini haikuwa hivyo kwa Sabrina. Alimtenda kinyume na
kila mtu na kushangaza wengi na kumuacha Jack akionekana kicheko hapo chuoni
kwa jinsi alivyomkataa bila heshima. Jack alichora vikatuni mpaka kwenye kuta
za vyooni huko chuoni akidhihakiwa sababu ya huyo Sabrina. Akachafuliwa vilivyo
kwa sababu ya huyohuyo Sabrina.
Lakini Jackson huyohuyo akiwa
amemuumiza kwa kumtia aibu chuo kizima kwa kiasi hicho yeye kama raisi
aliyeheshimiwa sana, akageuka kichekesho kwa watu sababu yake, napo baada ya kuachwa
kikatili na Emma, bado alimsaidia bila kinyongo mpaka akamaliza chuo alichokuwa
akikaribia kufukuzwa. Sabrina akabaki akimtafakari Jack asielewe moyo wake.
Sabrina akakumbuka siku aliyomfuata
wakiwa chuoni vile ambavyo hakuzungumza maneno mengi ila tu kumtaka amfuate. Kwa
fedheha aliyokuwa nayo Sabrina, alishindwa hata kusimama hapo alipokuwa
amemfuata mafichoni. Akakumbuka kushindwa kumjibu kabisa wala kusimama. Akabaki
ameangalia pembeni.
Hivi ndivyo
ilivyokuwa kati ya
Sabrina na
Jack Chuoni.
J |
ack
akamwita tena taratibu tu baada ya kushindwa tena kusimama. “Sabrina!” Sabrina akamtizama. “Naomba tuongozane.”
Sabrina akajifuta machozi, akanyanyuka bila ya kusema neno. Jack akaongoza njia
mpaka kwenye jengo ambalo ni la viongozi. Kila mtu akimshangaa Sabrina aliyepoteza
sifa pale chuoni, akiongozana na mtu kama Jack! Moja kwa moja mpaka kwenye
chumba cha Jack alipokuwa akiishi peke yake kama raisi. “Kaa ule kwanza.” “Mimi
sina njaa.” “Najua hujala, acha hasira zinazokuumiza wewe mwenyewe. Kula halafu
upumzike.” Sabrina akaangalia kitanda, akarudisha macho kwenye chakula.
Akatulia. “Nimekukaribisha chakula, ndipo ulale. Halafu tutazungumza.” “Juu ya
nini!?” Akauliza Sabrina kwa ukali kidogo huku amekunja ndita.
Jack akakaa. “Naomba ule, ulale ndipo
tuzungumze. Mimi sina vipindi vya mchana huu. Najisomea hapahapa chumbani.
Naomba ukae, acha kusimama.” Sabrina akakaa kitandani badala ya kwenye kochi
dogo hapo pembeni ya kitanda. Jack akabaki akimtizama. Kimya amejiinamia. Baada
ya kama dakika, akamuona anavua viatu, akajilaza kitandani kwake. Jack
akasimama na kumfunika. Hapohapo Sabrina akapitiwa na usingizi. Hizo kumbukumbu
nazo zikamrudia Sabrina. Akavuta pumzi kwa nguvu na kuendelea kukumbuka.
Habari zilienea kwa haraka sana kuwa
Sabrina amelala chumbani kwa Jack, raisi wa hicho chuo. Naye Sabrina kama mfu,
alilala karibu siku nzima. Alifungua macho jasho linamtoka kwa kufunikwa, Jack
anavaa nguo ametoka kuoga. Akajifunika kwa haraka mpaka kichwani. Akamsikia
Jack akicheka. “Sasa kwa nini unavaa mbele ya mgeni bwana!” Sabrina akalalamika.
“Mimi nilijua bado umelala!” Akamsikia amekaa palepale kitandani.
“Mama wewe umelala ugenini kama
kwako!” Sabrina akacheka ndani ya shuka. “Unakoroma mpaka nimeshindwa kusoma!”
“Muongo Jack, mimi huwa sikoroni.” Akabisha Sabrina. “Mbona nilijua utabisha
tu, ikabidi nikuchukue video kabisa usije sema nimekusingizia!” Sabrina
alicheka sana. “Ujue huna akili wewe Jack! Sasa kwa nini ualike mgeni halafu
uje umdhalilishe?” “Mimi huu ni ushahidi wangu mama. Wala si kukudhalilisha.”
Akamuwashia simu yake na kumuweka hiyo video. Sabrina alicheka sana, alijiona
vile alivyokuwa amelala huku akikoroma. “Bwana Jack!” “Mimi naomba uangalie
mpaka mwisho, kuna swala la mpaka ute, udenda kabisa humo ndani ya hiyo video!”
Sabrina akafuta ile video kwa haraka akamrudishia simu yake. “Sitaki. Kwanza
huyo sio mimi!” “He! Unajikana mwenyewe!” Kidogo wakacheka.
“Nilikuwa nimechoka Jack! Sana. Halafu
sikuwa napata usingizi.” “Haya, usingizi umeisha sasa tuzungumze maswala ya
shule wakati unakula.” Sabrina akakaa. Jack akampashia moto chakula, akaanza
kula. Hicho chumba cha raisi wa Chuo kwanza ungependa kuwepo humo. Mama Msindai
aliwekeza hapo kwa ajili ya kiziwanda wake, utafikiri chumba cha mfanyakazi
fulani. Kulikuwa na vitu vichache lakini vizuri vitupu. Kitanda chenyewe cha
Jack mama yake alimletea, hakutumia cha hapo chuoni. Mashuka mazuri na blangeti
safi pembeni. Kusafi kama Jackson mwenyewe. Sabrina akaanza kutulia mawazo kwa
ile mandhari pale ndani.
“Mambo yako ya shule ni mabaya Sabrina.” “Yepi
sio mabaya?” Akauliza Sabrina kwa kuumia. “Naongelea kile unachoweza
kubadilisha kwa sasa. Mengine huna uwezo wa kuyabadilisha, lakini hili unao
uwezo. Walimu wote wameshakuripoti kwa mkuu wa chuo kama huingii darasani na
haupo chuoni. Unajua sheria za chuo. Kwa kifupi umeshajifukuzisha chuo. Leo
asubuhi nimetoka kuzungumza na mkuu wa chuo nikimuomba asiwasiliane na wazazi
wako kwanza, kuwataarifu kama umejifukuzisha chuo rasmi, nione kama unaweza
kurejea.” Sabrina alishituka sana. Wazazi wake! Jack akakaa mbele yake.
“Wewe sio wa kwanza kuachwa au
kukataliwa vibaya Brina!” Vile tu kumuita Brina, kukamtuliza. “Wewe ni shahidi
yangu, mimi pia nilishakataliwa vibaya sana, tena mbele ya umati wa watu,
cafteria!” Sabrina akashindwa kuendelea kumuangalia, akainamia chakula chake.
Akakumbuka aibu aliyomtia Jack. “Unakumbuka kashfa yake! Unakumbuka jinsi
nilivyochorwa hapa chuoni? Nilipewa kila aina ya majina baada ya lile tukio.
Lakini uliniona nikiacha kuingia darasani? Kwani ilidumu muda mrefu?” Sabrina
akabaki ameinamia sahani ya chakula kwa aibu na uchungu. Hata kula akashindwa.
“Halikuwa kosa langu kukupenda, Brina.
Mimi kama mwanaume, nikajaribu bahati yangu. Ukanikataa. Katika yote, nikaishia
kujitia moyo kwa kujipongeza kuwa nilijaribu ila sikufanikiwa. Watu waliponiona
nimesimama, naendelea na shule yangu vizuri, tena vizuri sana kuliko wao. Mimi
ndio wananihitaji niwafundishe na niwaongoze, heshima yangu ikarudi. Sasa
tofauti yangu mimi na wewe ni hapo. Wewe umekubali kushindwa ndio maana mpaka
leo wewe umebaki kuwa kituko. Darasani haupo. Nasikia ripoti yako ya field
mpaka leo hujaiwakilisha wakati wenzako wote washakusanya. Ni kweli au sio
kweli?” Sabrina kimya.
“Darasani huingii, mitihani kufanyi!
Labda mimi nikuulize, ni kwa faida ya nani? Maana mmebakisha miezi michache
sana, mnaondoka hapa chuoni. Hawa watu wote hawa unawapa nafasi kwenye maisha
yako, hutaowana tena. Ushajiuliza itakuaje baada ya haya yote?” Kimya. “Sasa
mimi nimeomba uongozi wanipe muda wakuzungumza na wewe nijue kama unataka
kuendelea na chuo au unaacha!” “Nilifikiria pengine niombe kuahirisha mwaka
huu, ili nije kumaliza mwakani.” Akajibu Sabrina taratibu.
Jack akabaki amenyamaza. “Hata hivyo
nimeshachelewa Jack. Nipo nyuma kwenye kila kitu, siwezi kuwa na wenzangu tena.
Naomba uniombee kuahirisha.” “Ukikubali kushindwa leo, ujue hata ukirudi
hutamaliza Brina. Ila nakuhakikishia kabisa, ukiamua leo. Na hivi zile safari
zako za kila weekend unahamia kulala hotelini au kwenda Dar zimesitishwa,
utaweza tu.” Sabrina akamwangalia Jack na kurudisha macho kwenye chakula
ambacho hata hakuwa akila tena kwa aibu. “Inamaana alikuwa akinifuatilia
kila nilipokuwa nikitoka hapa chuoni!?” Akajiuliza Sabrina akikumbuka
utalii aliokuwa akifanya katikati ya hiyo shule yake, hapo chuoni kwa ajili ya
kumfurahisha Emma.
“Sikukejeli
Brina, ila nakwambia ukweli. Umepunguza sababu kubwa sana iliyokuwa ikikufanya
usifanye vizuri darasani. Nimekuwa nikiangalia matokeo yako yote tokea unaingia
hapa chuoni. Wakati wote wewe umekua ukipita kwa Pass.
Ni kwa kuwa akili yako haikuwa chuoni. Sasa kwa wakati huu ukiweka akili
chuoni, ukapambana mchana na usiku, ukiwa hauna kinachokufunga isipokuwa elimu
tu, nakwambia hata wale waliopo darasani sasa hivi, utawapita.” Sabrina
akakunja uso kama asiyesadiki.
“Umefikia wapi kwenye ripoti?”
“Sijafanya chochote Jack.” “Sasa leo umelala karibu siku nzima. Hujachoka,
chakula hicho hapo. Kula. Nenda kaoge, uanze kuandika.” Sabrina akabaki
akifikiria kurudi darasani na yale macho ya watu! “Brina?” “Nafikiria sehemu ya
kwenda kuandika.” “Wewe ukiwa tayari, njoo hapahapa, tena nitakutafutia mtu wa
mwaka wa tatu ambaye amemaliza yake, na nimesikia pale ofisini kwa ma lecturers,
walimu, wakimsifia ripoti yake ni nzuri. Nenda kaoge, urudi hapa. Acha
kukatakata tamaa na kukimbia.” Sabrina akamaliza kula, akatoka hapo baada ya
kushukuru.
Kila
alipopita hapo kwenye korido alijua viongozi wote wanaoishi kwenye hilo jengo,
wanamshangaa yeye na kule alikotoka, chumbani kwa raisi, Jackson Msindai.
Akajikaza akarudi chumbani kwake. Akashangaa msichana anayeishi naye hapo
chumbani ambaye alikuwa akishiriki kumkebehi kwa hali ya juu, nakumfanya
Sabrina kushindwa hata kukaa hapo chumbani na kukimbia chumba alicholipia hapo
chuoni, ni kama ametulia! Hakumsemesha. Akaenda kuoga. Akarudi kujitayarisha,
akachukua madaftari yake, na faili alilokuwa amefanyia field, akatoka tena
kurudi kwenye jengo la viongozi, gorofa ya juu kabisa ambapo kipo chumba
kikubwa cha huyo raisi wa chuo, Jackson Msindai.
Akagonga mara moja tu, akasikia sauti
ya Jack ikimkaribisha. Alibabaika alipoingia nakumkuta Jack amekaa, Phina
amemkalia kwenye mguu mmoja, Jack amepitisha mkono kiunoni. Akasita. “Samahani,
sijui kama...” “Wewe njoo. Nimekuletea mkali wangu Phina. Ushindwe wewe tu.
Atakusaidia na kukuelekeza kila kitu. Nimemuomba leo akusaidie. Sasa mtumie
vizuri. Maswali yote juu ya ripoti, atakusaidia. Tena ukimbana vizuri, hata leo
mnaweza kumaliza, kesho tukiongozana kwa mkuu wa chuo, hata ukizungumza, una
kitu mkononi. Sawa?” “Nawashukuru kwa msaada. Na asante Phina kwa kukubali
kunisaidia.” “Wala usijali. Ukituliza akili, utamaliza tu.” Mrembo Phina akamtuliza.
Akamgeukia Jack, wakapeana busu
kidogo, Sabrina akajibaraguza kama anayeangalia faili lake. Wala hakujua kama
ni wapenzi. Hakuwa hata na muda na mambo ya hapo chuoni. “Acha nikasome na
washikaji. Wananisubiri. Mkimaliza kabla sijarudi, usiondoke, unipigie.”
“Sawa.” Phina akakubali na kusimama. “Haya mrembo, kazi kwako. Kesho mimi na
wewe kwa washitaki wako. Hakikisha hatuendi mikono mitupu.” “Nitajitahidi.”
Akakubali Sabrina, kwa kuumia. Hakujua hata ni kwa nini apatwe wivu kwa
mwanaume aliyemkataa. Akakumbuka jinsi Phina alivyohangaika naye mpaka
wakamaliza hiyo ripoti na Jack kufanikisha kumrudisha chuoni baada ya kumuombea
kwa mkuu wa chuo.
Sasa Hivi.
Alipoyakumbuka
hayo yote, Sabrina akajiambia hata iweje, hatakwenda tena kwa Jack huko
Singida. “Yaani mimi nitakuwa mtu wa kukombolewa
tu na Jack! Yaani nakuwa narudi kwake nikiwa matatizoni tu! HAPANA.”
Sabrina akakataa kwa kutingisha kichwa kabisa akijifuta machozi ya majuto. “Ni heri nihangaike mpaka mwisho wangu mimi mwenyewe,
kuliko kumfanya Jack ndio kuwa mkombozi wangu kila siku, tena safari hii na
mimba juu! Hapana.” Aibu ikazidi kumsumbua. Akakubaliana na mawazo yake,
kutomfuata. Lakini kile kitendo tu cha kuzungumza naye Jack kikamfanya
ajisikie vizuri sana, angalau akaupata usingizi wa siku hiyo bila shida.
Akapata usingizi mzito wa mimba, akalala wala asijue alipo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaja kuamka saa nne asubuhi. Akakuta missed
calls 5 za Jack. Akampigia. “Nilikuwa nimelala
Jack. Mzima?” “Mzima. Sasa unakuja saa ngapi?” Jack akauliza. “Naona sitakuja Jack.” “Kwa nini tena!?” Jack akauliza
akisikika kukata tamaa. “Nimefikiria, nikaona sitakuwa
nikikutendea haki Jack. Naomba wewe uwe na amani. Endelea na maisha yako tu.
Unastahili kupumzika. Nishakupitisha kwenye mengi magumu, Jack. Inatosha. Acha
nipambane mwenyewe, pengine nitafanikiwa. Naamini nitakuwa sawa.” Kimya.
“Jack?”
Sabrina akaita na kuiangalia simu yake kama imekatika au la! Sabrina
akagundua simu haijakatika.
“Naomba uwe na amani Jack. Naamini nitakuwa sawa.” “Umepata kazi au
biashara yakufanya?” Jack akauliza. “Hapana. Nimehangaika karibia miezi miwili sasa. Kila nilipoenda
waliniambia ndio wanapunguza wafanyakazi. Ila juzi nimekutana na mtu mwingine.
Anayo baa karibu na stendi kubwa ya hapa Moshi. Ameniambia anafungua baa
nyingine maeneo ya soko la Kiboriloni, kama nitasubiri anaweza kunipa kazi.
Nimechukua namba yake ya simu, na yeye nimempa yangu. Nimemwambia nitasubiri.
Na kama atakuwa na kazi yeyote kabla ya hapo, nimeomba anikumbuke. Amekubali.
Ndio nipo kwenye kusubiri huku nikiendelea kutafuta.” Sabrina akajieleza
kwa upole.
“Unaishije sasa hapo?” Jack
akauliza kwa kujali. “Ni Villa yenye vinyumba, kama
apartment zilizo na kila kitu ndani.” Akamtajia jina la hizo Villa na kumuelekeza
zilipo. “Nina vifaa
vichache tu, hasa vya jikoni ndio vyangu. Kwa hiyo nimepewa hifadhi hapa mwezi
huu unaoanza, ukiisha ndio mwisho hapa. Nafikiria kutafuta chumba kama nitapata
hapa kazi.” “Ukikosa?” Jack akauliza tena. “Hata
sijui Jack! Nitajua mbele ya safari.” Jack akatulia kwa muda. “Lakini nakushukuru sana Jack. Asante kwa moyo wako.”
Kimya. “Naamini nitakuwa sawa tu.” Sabrina
akajaribu kumpa moyo kana kwamba sio yeye aliyekuwa akilia usiku uliopita.
Baada ya kutulia kidogo kama
akifikiria, Jack akauliza. “Unaruhusiwa wageni hapo?”
“Karibu Jack. Muda na wakati wowote ukifika getini watanipigia simu, nikiwaruhusu
wakufungulie, watakufungulia geti.” Kisha akajishitukia tena, Jack aliuliza
swali tu, yeye akaweka ukaribisho. Akaona aulize ili apate uhakika. “Kwani unataka kuja kuniona, Jack?” Sabrina akauliza
kwa unyonge. “Ndiyo. Nafikiria hivyo.” Sabrina
akaanza kulia tena. Akalia hapo, Jack kimya. Mwishoe akakata simu yeye
mwenyewe.
Old is
Gold...
I |
likuwa siku
ya ijumaa kama kwenye saa moja usiku hivi. Sabrina alikuwa amejilaza kwenye
kochi baada yakuzunguka sana mjini siku hiyo akipita kwenye mabaa na maduka
akitafuta kazi bila mafanikio. Akasikia simu ya mezani ikiita. Akaamka. Akaikimbilia,
akaambiwa ana mgeni. Moja kwa moja akajua ni Jack tu. Akawaomba wamuelekeze
alipo. Akatoka kwenda kumsubiria nje. Baada ya dakika chache tu akaona Range Rover
Sport inakuja. Akashanganzwa kidogo. Hata kwa kina Tino wenye pesa hawakuwa na
aina hiyo gari. Akaanza kubabaika akidhani si Jack pengine amejichanganya. Akajituliza
ili angaalie linapoelekea na anayeshuka. Ilivyokuwa ikimkaribia akaanza kumtambua
Jack. Ndipo akaangalia hiyo gari tena vizuri. Ilikuwa nzuri sana. Rangi nyekundu
inayokwenda damu ya mzee, ila imeiva ya kuwaka hata gizani. Akajua Jack
alinunua gari ingine sio kama ile aliyokuwa nayo chuoni. Akamuelekeza kwa
kidole ni wapi pakuegesha gari yake, Jack akaelewa, akaegesha kama
alivyoelekezwa.
Sabrina
akakimbilia mlango wa dereva, akafungua. Kwa hakika Jack alibadilika. Si
mwanafunzi tena. Jack muajiriwa. Alipendeza haswa, akaonekana mambo yake ni
mazuri na hali ya uwanafunzi imeisha. Sabrina akarudi nyuma kidogo. Jack
aliyemtegemea akutane naye si huyu. Jack akamuona amebabaika. “Hujambo mama?” Sabrina
akaanza kulia tena akiwa amesimama hapo pembeni ya mlango, Jack akimwangalia
akiwa amekaa kwenye kiti cha dereva. “Pole kwa matatizo.” “Nimefurahi kukuona Jack. Umependeza!” Akacheka. “Hata wewe umependeza.” Sabrina
akamwangalia na kuinama. “Mbona sikaribishwi! Nimechoka Brina! Nimeendesha kwa
masaa karibu saba!” “Pole Jack. Twende ukapumzike. Una mizigo mingi?” “Kibegi
kidogo tu, nitabeba.” Jack akashuka, akafungua mlango wa nyuma, akatoa kibegi
kidogo tu, Sabrina akaongoza njia. Jack akifuata nyuma, wakaingia ndani.
“Nipazuri
sana. Si itakuwa ni aghali sana?” Akauliza Jack. “Ni ghali kwa hakika. Njoo
huku chumbani. Najua ungependa kuoga.” “Nitaoga wakati wa kulala. Acha tupate
muda kidogo.” “Basi nikuwekee begi ndani.” Sabrina alimuona jinsi Jack
anavyomuangalia kwa makini. Akampokea begi, akaingiza ndani na kuelekea sehemu
ya kupikia. “Acha nikutengenezee hata chai Jack. Kunabaridi!” “Nina njaa Sabrina.
Nataka chakula kabisa, sio chai peke yake. Kama hamna chakula, twende tukale
nje.” “Nina mboga nilizounga tayari. Nipe muda mfupi nikupikie ugali.” Jack
akasogea pale jikoni, akakaa kwenye kiti cha meza ya hapo karibu na jikoni. Jiko
lenyewe ilikuwa safi na la kisasa na vimeunganishwa kwenye umeme.
“Umebadilika
Jack!” “Nimekuaje?” Jack akauliza huku akicheka. “Umezidi kupendeza. Wanakulipa
vizuri eeh!” “Siyo mbaya. Siwezi kulalamika. Halafu pia tulianza ile biashara
niliyokwambia tufanye, lakini ukaja kubadili mawazo. Ukasema hutaweza tena
kuungana nami huko Singida na wala hutafanya tena hiyo biashara. Nilipopata ule
ujumbe nikawa kama nimekata tamaa kidogo, lakini baada ya siku chache, nikaona
nianze tu.” Sabrina akajutia sana. “Vipi lakini, unaonaje?” Akajikaza na
kuuliza. “Mwanzo sio mbaya. Lipo tumaini. Japo kila biashara inakuwa na
changamoto zake, ila sio mbaya.” Sabrina akanyamaza huku akiendelea kupika na
kupasha moto chakula.
Akamuona
anatoa simu, akapiga. “Nilifika salama, japo tairi ya
nyuma iliisha upepo. Nikadhani ni pancha. Walipoiangalia, kumbe ilikuwa ni upepo
tu.” Akamsikia Jack akiongea. “Asante sana. Vipi
na wewe?” Akamsikia akiuliza. Akajua anazungumza na mpenzi wake.
Akacheka kidogo huku akisikiliza. “Mpuuzi yule, achana
naye. Anakutisha tu.” Akajibu Jack huku akicheka. Akacheka tena na
kuendelea kusikiliza. Sabrina akapotelea mawazoni huku akipika na kupasha moto
hiki na kile wakati Jack anaendelea kuzungumza. Akamuwekea chai hapo mezani.
“Asante.” Akashukuru kwa kunong’ona huku akisikiliza simu. Sabrina akaendelea
na mapishi yake.
Hata
hakujua Jack alimaliza kuzungumza na simu muda gani, lakini wakati anamuwekea
chakula mbele yake, akagundua alikuwa akimtizama muda wote. “Karibu.” Akamuwahi
ili asimwangalie zaidi. Tumbo la Sabrina bado lilikuwa halionyeshi sana
kutokana na umbile lake. Usingemgundua kwa haraka kama ni mjamzito. Akampisha
Jack anawe hapo kwenye sinki ya jikoni, akakaa pembeni yake. Jack akamwangalia
kidogo kabla hajaanza kula. “Nimefurahi umekuja kunitembelea Jack.” Jack
akacheka kidogo. Akamuona anaombea chakula na kuanza kula.
“Mbona
wewe huli sasa?” “Nilikuwa na siku ndefu. Nimerudi hapa nikiwa na njaa, nikala
viporo vyote ndipo nikalala.” “Ulikwenda wapi?” Jack akauliza na kuendelea
kula. “Nazunguka kutafuta kazi Jack. Leo niliwapitia wote walioniambia
wangenipigia, lakini sijafanikiwa. Ndio nasubiria hiyo baa ifunguliwe. Natamani
nipate kazi mapema ili nijue natafuta maeneo yapi yakuishi. Ila nimejiwekea
mwezi huo unaokuja wakati muda wa hapa ukiisha, kama sijapata kazi, niondoke
kabisa hapa Moshi, nihame mji.” Jack akamwangalia.
Kisha
akatupia swali jingine baada ya kumeza. “Unataka kuhamia mji gani kama si
hapa?” “Sijajua kwa hakika, lakini nahisi naweza kurudi Dodoma ambako
tulishaishi. Sitaki nihamie kwenye mji nikawa mgeni sana. Nahisi itanichukua
muda mrefu kujijenga.” Jack akaendelea kula.
“Unawasiliana
na nyumbani?” “Hapana Jack. Nimeona niwaache kwanza mpaka nitakapojijenga,
ndipo niwatafute. Nisiwe mtu wa kuwavunja moyo kila wakati.” Jack akaendelea
kula. “Huu ugali na mahare, na nyama ya kukaanga ni vitamu sana Brina. Naomba
ule kidogo.” Sabrina akacheka. “Ungeniona jinsi nilivyokula mchana!” “Kula tena
kidogo. Fungua mdomo nikuwekee kidogo uone ninavyofaidi.” Sabrina akacheka
sana. “Kama ni hivyo acha nioshe mkono nile kidogo.” “Hayo ndiyo maneno.”
Sabrina akaosha mkono, akajiwekea kidogo kwenye sahani akaanza kula.
“Hujabadilika sana Brina. Mwili bado mdogo! Umegoma kunenepa?” Sabrina akacheka
kidogo nakubaki akifikiria.
Akakumbuka
alitoka kwao akikimbilia kwa Sabina dada yake ili akapumzike, akaishia mikononi
kwa Lela aliyemuachia jukumu la Tino. Ulalaji ukawa wa shida kwa kuuguza. Tino
anapata nafuu ndipo huo ujauzito na kutelekezwa. Akanyanyua uso, akagundua Jack
anamtizama. Akarudisha macho kwenye chakula. “Bado sijatulia Jack. Pengine
nikija kutulia, naweza kuongezeka.” Ikabidi ajieleze tu. Jack akaendelea kula. Wakamaliza
kula, akasafisha meza, wakabaki wamekaa hapohapo mezani.
“Ulipata
kazi gani hiyo iliyokufanya ukatupilia mbali mipango yote tuliyokuwa
tumezungumza?” Jack akauliza taratibu tu. Sabrina akainama akijaribu kuzuia
machozi, mwishoe akaanza. “Unakumbuka nilikwambia nimechoka pale nyumbani
nataka kwenda kwa dada Sabina?” “Nakumbuka na hata ulipopata hiyo kazi ambayo
uliniahidi ungekuja kuniambia ni kazi gani tukikutana kabla hujagairi,
tulizungumza.” Sabrina akapoa kidogo. “Ulikuwa ukifanya kazi gani?” Jack
akauliza kwa upole tu akimtizama.
Sabrina
akamuelezea tokea akutane na Lela, mpaka akaachiwa jukumu zito la Tino. Jack
akimsikiliza tu. Jinsi alivyomuuguza kwa shida na hali aliyomkuta nayo mpaka
kuondoka kwa Lela na kuachwa wao wawili. Akanyamaza. “Nakusikiliza Brina.”
“Walifikia hatua yakuachana Jack. Hapakuwa na dalili yakuja kurudiana tena. Ile
hali ya vitisho, Tino akihofia kuja kuuwawa na Lela na mpenzi wake, akaonelea tuhamie
huku kwa matibabu wakati mwanasheria wake akiendelea na kufuatilia talaka.”
Jack akamuona midomo inaanza kumcheza kwa hofu, akajua lipo jambo hapo
linatafutiwa jinsi ya kuelezwa. Akatulia kumsikiliza.
“Tulitulia
kwa majuma kadhaa ndipo mkewe akaanza tena fujo akisema yeye bado anampenda
mumewe, ila mumewe ndiye amemtelekeza. Hapo akawa analalamika. Hata mimba
iliyosemekana anayo akawa hana tena kitu kilichomtia hofu Tino maana alijua hiyo
ndiyo ingekuwa silaha yake.” Sabrina akanyamaza baada yakumuona Jack ametulia
sana akimsikiliza.
“Ehe?”
Jack akamtaka aendelee. Sabrina akanyanyua uso kumtizama. “Ndipo sasa ikabidi
Tino arudi Dar ili kufuatilia mambo yake ya ndoa.” Akahitimisha hivyo, Jack
akajua lipo la ziada. Akatulia kidogo kisha akaona aulize tena. “Kwa hiyo
amekuacha hapa kwa makubaliano gani? Sijaelewa.” “Ndio kazi imeisha.” Jack
akakunja uso kidogo. “Mbona nahisi kama kuna kitu nyuma ya hilo jibu la sasa
hivi.” Sabrina akabaki ameinama. “Brina?” “Aliniacha hospitalini.” Akajibu
macho chini. “Ukiwa unaumwa na nini?” Kimya. “Brina!?” “Akiwa amenipeleka
kutolewa mimba.” Jack akabaki kama ameduaa. Ni kama hakuwa ametegemea hilo jibu
kabisa.
“Kwa
hiyo akaondoka akiwa ameridhia kuwa nimetoa mimba, kumbe nilimdanganya.
Nilipoingia chumba cha kutolea mimba, nikamwambia yule daktari..” Sabrina
akamuelezea tena Jack kila kitu. “Kwa hiyo hapo ulipo ni mjamzito wa mimba ya
miezi mitatu!?” “Ndiyo Jack.” Akajibu kwa aibu na unyonge, Jack akimwangalia. Akamuona
mishipa ya pembeni ya macho imesimama. Macho yakabadilika yakawa mekundu haswa.
Akabaki akimtizama. Sabrina akainama. Jack akasimama na kuondoka pale bila
yakuongeza neno akahamia sebuleni. Lakini akashindwa hata kukaa, akabaki
amesimama amegeukia tv. Sabrina akashindwa hata chakuzungumza tena. Kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hata Jack kimbilio la mwisho wakati wote kwa
Sabrina hapo amesalimu amri. Ni nini kitaendelea?
Usikose muendelezo….
0 Comments:
Post a Comment