Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 13. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 13.

 Sabrina alisubiri akijua ndio na yeye anaondoka. Alipomuona amesimama tu kama bado anafikiria chakufanya, anashindwa hata kumwangalia, akaona aende akamwandalie chumba cha kulala, kama ataona usiku huo ni mbali kurudi kwake Singida. Akamtolea taulo kubwa la kujifutia na dogo la kujisugulia. Akatoka. “Huko bafuni maji yanatoka kwenye shower ya baridi na ya moto. Nenda ukaoge, upumzike Jack.” Sabrina akaongea kwa upole. Jack kimya hata hakugeuka.

          “Hata mimi najichukia Jack. Sio wewe peke yako. Najichukia sana kuliko nitakavyokwambia. Week chache zilizopita mpaka nikafikiria labda nijiue, lakini nikajiambia sitakuwa na tofauti na kile alichokifanya Tino kwangu na huyu mtoto. Nikaona heri nipambane katika ugumu wangu hivihivi, nijikumbushe vile nilivyo mjinga. Kwa hiyo  kama itasaidia, jua hata mimi najichukia Jack, ni hivyo sina jinsi. Ndio maana nilishindwa kuja kwako tena, nikajiambia sio haki kuja na hali hii, pengine nikaanza kuugua au matatizo mengine ya ujauzito, wakati wewe ndio upo kwenye kuanzisha familia. Nikaona sio haki kwako.” Jack akageuka.

          “Na sababu yakuniambia niendelee na maisha yangu hutaki tena biashara, ni kwa sababu ya Tino, ukitegemea kuanza naye maisha?” Jack akauliza swali la moja kwa moja, wazi lilisikika limejaa uchungu. “Ndiyo Jack.” Sabrina hakuongopa. Alisimama mbele ya Jack kama mtoto aliyefumaniwa na baba yake mzazi. Jack akacheka kwa masikitiko. “Hivi hawa wenzangu wanaopata bahati na wewe Sabrina, huwa wanakwambiaga nini ambacho mimi nimekuwa nikishindwa kutamka kwako? Wanakupa ahadi gani zinazokuvutia na kuwakimbilia wao huku ukiniacha mimi na kunipuuza vibaya sana!?” Jack akazungumza kwa kuumia zaidi. Sabrina kimya.

          “Sikuchukii Sabrina, ila naona wivu. Nawaonea wivu wanaume wenzangu! Najiuliza wana nini hicho kikubwa walichojaliwa na Mungu mimi nikanyimwa! Ni pesa? Maana mimi najijua sio mbaya kihivyo Sabrina. Labda pengine uniambie kama labda sijafikia viwango vyako.” Akauliza taratibu tu. “Hapana Jack. Ni mimi mwenyewe nahisi nimeandikiwa kukosa tu. Wala sio wewe. Ndio maana hata mimi najichukia. Wewe sio tatizo Jack. Mwanamke yeyote angefurahia kukupata. Kumbuka hata pale chuoni jinsi walivyokuwa wakikupigania! Wewe huna tatizo, ni mimi. Naomba usijaribu hata kujifananisha na hao wapumbavu wengine!” “Sidhani kama niwapumbavu. Sidhani Sabrina. Wao wamefanikiwa kupata kitu pekee ambacho mimi nimekuwa nikikihangaikia na kukisubiri miaka! Tino amekuja kwenye maisha yako hata miezi sita haijaisha, umembebea mpaka mtoto! Huyo ni mpumbavu kweli au mwenye bahati?” Sabrina akanyamaza na kuinama mbele ya Jack akashindwa hata chakuzungumza.

          Jack akaondoka pale na kuingia chumbani. Alikuta kila kitu, hakuona haja yakuuliza. Akaingia kuoga, akatoka akiwa ameshaoga. “Tunalalaje?” Sabrina akakaa kwa haraka, alikuwa amejilaza kwenye kochi. “Lala chumbani, mimi nitalala hapa kwenye kochi.” “Na baridi hii!?” Jack akashangazwa. “Kuna mablangeti mazito mawili hapo chumbani. Nitachukua moja na mashuka.” Jack akasimama akifikiria. “Nenda kapumzike Jack. Mimi nitalala tu hapa. Ni pakubwa halafu hili kochi ni laini, najisikia vizuri nikilala hapa. Na wala leo sio mara ya kwanza kulala hapa.” “Sawa. Usiku mwema.”  Jack akarudi chumbani.

          Baada ya muda Sabrina akamfuata, akaenda kumgongea. Akamsikia akimkaribisha. Akaingia. “Nimekuja kuchukua mashuka na blangeti. Vipi wewe baridi?” “Nipo sawa tu. Unahakika pale patakuwa sawa?” “Kabisa. Wewe pumzika tu.” Akatoa mashuka na blangeti moja akasimama pale mbele ya kitanda alipojilaza Jack. “Umekuwa kimbilio langu Jack, naomba usiniache sasa hivi. Au niseme usinichukie sasa hivi. Au nikuombe usinikatie tamaa. Nina hofu ambayo haijawahi kunipata maishani. Sijui itakuwaje! Lakini kwa kuwa naona nipo hai, najua natakiwa kupambana.” Akakaa pembeni ya kitanda, Jack akimwangalia.

          “Mungu ni shahidi sijawahi kukusahau, Jack. Na huwezi amini hata Tino aliponiacha, mtu niliyejiambia ni kimbilio langu akabaki kuwa Jack. Nilipofika hatua yakutaka kujiua, nikajiambia Jack aliweza kubadili historia yangu pale chuoni, hatashindwa sasa hivi. Sihitaji chochote kutoka kwako Jack. Ninazo pesa, ila nataka tu uniambie ‘itakuwa sawa’. Nataka tu uniambie hata hili nitaweza kama vile ulivyoniambia chuo nikiwa nakaribia kufukuzwa chuo na nimefeli kila somo. Sijui uliwezaje kuweka mbali ubaya niliokufanyia, lakini ukanisaidia, nikaweza. Nipo kama hivi unavyoniona hapa na huyu mtoto atakayekuja, akiwa anahitaji kukutana na mama anayejielewa. Sasa hivi sipo hivyo. Tafadhali nisaidie kwa maneno tu. Usiache kuzungumza na mimi. Hata mimi najua nimekosa Jack. Najua sana tu. Naelewa kuwa katika hili eneo huwa nakosea sana. Najua. Lakini naomba usinikatie tamaa. Sio sasa hivi. Tafadhali Jack.” Akamsikia Jack anavuta pumzi kwa nguvu.

          “Uache kuniblock kwenye simu.” “Sitarudia tena.” “Kuanzia sasa naomba tukizungumza kitu, tukaweka mipango, unapotaka kubatilisha, niahidi utapiga simu sio kunitumia ujumbe na kuni block bila kutaka kunisikia mawazo yangu na mimi.” Jack akaongeza sharti jingine. “Nakuahidi nitafanya hivyo Jack.” “Na ninapokuwa nikipanga kitu na wewe, kama unajua wazi hutataka kukifanya, niahidi utaniambia wazi, hutakubali huku ukijua hutakifanya.” “Nitabadilika Jack. Nikikwambia ndiyo kwenye jambo, kuanzia leo nitalisimamia mpaka litimie, na nikibadili mawazo nitakutafuta tuzungumze.” Hapo Jack akaridhika, akakaa.

          “Sasa kama ulivyoona pichani, nimepata msichana. Anaakili na juhudi nzuri ya biashara. Nilikutana naye kwenye hiyo biashara ya mafuta ya alizeti. Tukakubaliana tufanye pamoja. Nikamuongezea pesa ya mtaji, amekodi sehemu ambayo tunakusanyia hizo bidhaa, anao vijana wanaomsaidia kuyaweka kwenye ujazo tofauti tofauti na kuyasambaza. Naona anafanya vizuri. Sasa je, ungependa kwenda kufanya naye?” “Unajuaje kama anayo nafasi ya kazi?” Sabrina akauliza taratibu tu.

            “Kama hatakuwa nayo nafasi ya kazi, pale Singida nafahamiana na watu wengi. Na kama nilikusikia na kukuelewa sawasawa upo tayari hata kuuza baa.” Sabrina akacheka akikubali. “Kwa hali hiyo, inamaana hutakosa kitu chakufanya Singida ukiwa pia na sehemu ya kuishi.” “Nyumba sio garama huko?” “Sio sana. Maana hata pale ninapoishi nilipanga kwa mzee mmoja hivi. Baadaye akaamua kuniuzia. Nimeikarabati hiyo nyumba imekuwa nzuri tu. Japo sio kama hapa, lakini panafaa na panatosha. Kwa maana nyingine, bado nakukaribisha. Anza hapo maisha wakati ukifikiria chakufanya.” “Kwamba tutaishi wote?” Sabrina akauliza na cheko la aghueni usoni. “Ndiyo. Utakuwa ukiishi na mimi, na kuna kijana mwingine anaishi hapo. Na yeye aliomba hifadhi au wazazi wake walimuombea ili aweze kusoma hapo Singida. Kwa hiyo tutakuwa watatu.” “Nashukuru Jack.” “Sasa upo tayari kuja lini au utanitafuta kama...” “Achana na mambo ya kale Jack! Nishasema nimebadilika. Hata kesho ukiwa tayari tunaondoka wote.” Jack akacheka, wazi alionekana hasira imepungua usoni.

          “Kwa hiyo tunaondoka wote Jack?” “Sawa. Basi iwe kesho ili nipate siku ya jumapili ya mapumziko kabla ya kazi jumatatu.” “Acha mimi nianze kufungasha wakati mgeni wangu unalala.” Sabrina akasimama kwa haraka asiamini kama amepata pakujificha. “Unataka nikusaidie?” “Wewe lala hapo wakati mimi natoa nguo huko kwenye makabati. Nitaweka hapo sebuleni. Ila...” Akawa kama amekumbuka kitu. “Nini?” “Vitu vyangu vya jikoni lazima niondoke navyo, siachi. Ngoja niende mapokezi niulizie kama wana maboksi.” Sabrina akatoka hapo kwa haraka akiwa amechangamka.

          Ilibidi tu Jack aamke na yeye amsaidie kufungasha. Sabrina alichangamkia ukaribisho kama anayeogopa Jack asibadili mawazo. “Mimi naona hii mizigo ikaingie tu ndani ya gari. Itusubirie nje.” Jack akacheka. “Kweli safari hii umeamua kuongozana na mimi!” “Nilivyo na shida na wewe Jack! Nimehangaika sana, acha nitulie. Najua nikiwa na wewe, nitatulia na kuweza kufanya jambo la kueleweka.” Jack akamwangalia, nakuanza kutoa mizigo nje bila ya kumjibu. Sabrina hakujali. Akajiambia atajua mbele ya safari.

          Ilipofika saa saba usiku ndio wakawa wamemaliza kufungasha na kupakia kila kitu garini. Sabrina akaanza kucheka. “Nini?” “Kwa furaha ya ukaribisho nimefungasha na blangeti langu la kulalia pale sebuleni. Nipe funguo nikaangalie kwenye gari nione kama nitalipata kwa urahisi.” Jack akafikiria kidogo. “Unakumbuka kuweka kwenye begi gani?” “Nakumbuka. Nipe funguo niende mwenyewe, nitalipata kirahisi kuliko wewe kwenda.” “Utavuruga bwana Sabrina! Mimi nimepangilia vizuri. Kwa nini tusilale hapo kitandani pamoja?” Sabrina akabaki amekodoa macho.

          “Nini? Au ulijiambia ni mwiko kulala na mimi kitanda kimoja hata kama sitakutaka kimapenzi?” “Kabla hujakasirika zaidi na kuharibu huu wakati mtulivu tuliopata kwa masaa machache hapa, nafikiri wazo la kulala pamoja ili tusivuruge kule ndani ya gari, ni zuri sana. Tulale Jack, kesho uamke ukiwa na nguvu dereva wangu. Twende.” Akamshika mkono wakaongozana mpaka chumbani.

          “Nahisi nikikuuliza hili swali unaweza kukasirika.” “Kwamba tunalalaje?” Jack akamuuliza, Sabrina akaanza kucheka. “Unaniringia wewe!” Jack akaongea na kupanda kitandani. “Hebu njoo usizidi kuingiwa na baridi.” Sabrina akacheka na kupanda kitandani. Akajisogeza karibu kabisa na Jack bila kujivunga. Akampa mgongo. “Unanukia vizuri Jack!” Jack akacheka taratibu. “Kweli.” “Haya, asante.” Wakatulia.

“Asante Jack.” “Nikwambie ukweli Sabrina?” Akauliza kwa upendo. “Niambie tu Jack.” Sabrina akakubali taratibu. “Nimeshakuona kwenye hali mbaya, na wala hukuhitaji nguvu nyingi sana kukutoa kwenye ile hali. Wewe mwenyewe ukachukua ushauri na ukaufanyia kazi vizuri sana mpaka ukanishangaza na mimi mwenyewe. Ukatoka kwa ushindi tu. Naamini hata katika hili hutashindwa.” Sabrina akamgeukia. “Kweli Jack?” “Kabisa Sabrina. Nini kitakushinda? Wapo mpaka watoto wadogo zaidi yako wanazaa bila waume, na wao wenyewe wanalea watoto wao! Leo vichwa viwili hivi vishindwe na mtoto mmoja tu! Haiwezekani.” Sabrina alifurahi sana kusikia na Jack atakuwepo. Akajinyanyua, akambusu shavuni. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Sabrina kumbusu Jack. Akacheka. “Asante Jack.” “Karibu.” Sabrina akatamani kama Jack angekuwa hajapata mtu, lakini akajiambia amechelewa. Akajivuta chini nakurudi kujilaza kama alivyokuwa amelala mwanzoni, Jack akamuwekea mkono juu.

          Japokuwa walikuwa wakifahamiana miaka mingi, lakini wawili hao hawakuwahi kulala pamoja kama hivyo. Sabrina akajivuta karibu zaidi. Harufu ya Jack ndiyo iliyomfanya akatulia mpaka mawazo, ikawa kama amekunywa dawa ya usingizi. Akalala hata asijue linaloendelea ulimwenguni.

Asubuhi.

“Wewe unalalaje hivyo!?” Sabrina akaanza kucheka wakati ameamka. “Umenifanya nimeshindwa hata kutoka hapa kitandani kwenda kutumia choo! Hugeuki!”  Sabrina akazidi kucheka. “Ndivyo nilivyo. Nikiwa nalala, nikiridhika na upande niliogeukia, nabaki hivyo hivyo mpaka niamke.” “Mmmh!” Jack akakimbilia chooni. Baada ya muda Sabrina akamsikia anaoga. Akaona ampishe hapo chumbani, akaenda kuandaa kifungua kinywa.

Baada ya muda Jack akatoka akiwa ameshavaa kabisa. “Umebadilika Jack! Umependeza sana.” “Sifa hizo, haziishi mama?” “Nahisi kwa kuwa sijakuona muda mrefu. Njoo hapa mezani uanze kunywa chai wakati namalizia kupika.” Jack akaenda kukaa hapo mezani. “Harusi lini?” Sabrina akatupa swali la kiuchokozi. Jack akacheka na kufikiria kidogo. “Nitakwambia. Usiwe na haraka.” Sabrina akanyamaza na kupotelea mawazoni. Akampangia kifungua kinywa, akarudi chumbani kujitayarisha na yeye.

Akatoka akiwa tayari, akamkuta Jack anazungumza na simu. Akajua lazima anazungumza na mpenzi wake. Akarudi ndani haraka kama kumpa nafasi. Akaanza kukusanya vitu vyake vyote pale chumbani. Akashitukia Jack yupo mlangoni. “Nikusaidie nini ili na wewe ukale?” “Labda kuweka kwenye gari. Namalizia kukusanya. Umeshiba?” “Sana. Nahisi umeamua kufunga friji!” Sabrina akacheka. “Ulijuaje? Maana nimejiambia sitamwaga chakula. Nilivyoona hatutamaliza asubuhi hii, nimevigandisha ili tuondoke navyo.” “Mama wewe nimekukubali kwa bajeti!” Wakaendelea kuzungumza huku wakitoa mizigo nje. Walipomaliza, na Sabrina alipomaliza kula. Akasafisha kidogo. Wakatoka. 

Sabrina Singida kwa Jack.

W

akiwa njiani stori za chuo zikaanza. Vicheko vikaendelea mpaka Sabrina akasahau matatizo yake. Akaulizia huyu na yule. Kama anawasiliana na huyu au yule. Wawili hao waliishia kuwasiliana tu, lakini mwisho wa kuonana ni siku Jack akimsindikiza Sabrina kituo cha mabasi Dodoma, kurudi nyumbani kwao baada ya kumaliza chuo. Alikaa naye kituo cha mabasi mpaka akaondoka. Hapakuwa na ahadi yeyote kwa wakati ule kwa kuwa Jack alikuwa kwenye mahusiano na msichana aliyemsaidia sana Sabrina kimasomo, Phina, akabaki akimuheshimu, asielewe Jack alizungumza naye nini juu yake mpaka akamaliza na kuwaacha kwa amani hapo chuoni bila wao wawili kugombana! Hata Phina alipomkuta Sabrina na Jack peke yao chumbani hakuonyesha chuki kitu kilichokuwa kikimshangaza sana Sabrina.

          Alipenda harufu ya Jack, akaona ajifunike tu koti lake. Akalivuta nyuma ya kiti cha dereva alipokaa Jack mwenyewe ambaye ni dereva. Jack akamuona analinusa, akalishika kidogo na kujifunika bila hata kumuomba. “Unasikia baridi?” “Hapana. Kawaida tu.” Akajibu Sabrina. “Kuna vyakula unapenda zaidi?” Hapo ndipo akamkumbusha Sabrina kama ni mjamzito. Akajishika tumbo. Akamuona amepoa. Akatulia. “Au unakula kila kitu?” Akaendeleza yale mazungumzo. “Sijui. Labda kwa kuwa nilikuwa nikiishi peke yangu! Nanunua kile ninachokuwa na hamu nacho. Lakini sijawahi kutapika hata mara moja, au kupatwa na kichefuchefu. Kinachonikumbusha ni mjamzito ni tumbo limeanza kuwa gumu kidogo hapa chini. Tena week hii naona ndio linaongezeka kwa kasi! Ila namshukuru Mungu sina tatizo lolote. Na naomba Mungu iwe hivihivi.” Sabrina akaongea kwa upole.

          Akakumbuka kitu. Akatoa simu yake kwenye pochi. Akamuona anaandika ujumbe. ‘Tino, nashukuru kwa hifadhi. Nimeondoka pale rasmi leo. Nimerudisha funguo mapokezi.’ Akautuma huo ujumbe na kuzima simu kabisa. Akatulia kidogo, akamuona anatoa kabisa ile line. Akarudishia simu bila line. Akarudisha kwenye pochi. Akamuona ametulia. Jack akaona avunje ukimya. “Ulishaanza kliniki?” “Hata sina hilo wazo Jack. Akili zilikuwa ni kwenye kutafuta kazi tu.” Jack akamwangalia na kuendelea kuendesha. Wakatulia kidogo kila mmoja akiwaza lake.

          “Naamini utakuwa sawa Brina.” “Na mimi sasa hivi naamini hivyo Jack. Naamini tutakuwa sawa.” Akanyongea na kujishika tumbo. Akamuona anacheka kwa kusikitika. “Vipi?” Jack akauliza. “Namfikiria mwanadamu.” “Wamefanya nini?” Jack akauliza. “Aaah!” Sabrina akaona hata shida kuendelea.

          “Niambie mambo yako na siasa. Au uliachana nayo?” “Hata kidogo.” “Hongera Jack.” “Asante, naona utabiri wako ni kama unadalili yakuja kutimia.” Sabrina akajiweka sawa. “Kweli Jack!?” “Kabisa. Mpaka napata tumaini pengine nitapata bahati yakuja kuwa waziri.” Akajicheka Jack. “Usicheke bwana! Sijui kwa nini mimi nina imani na wewe, Jack! Unayo hekima kubwa sana na uwezo mzuri wa kuongoza. Kila mtu pale chuoni alikuwa akikupenda na kukusifia.” “Nashukuru kwa kunitia moyo. Kwa hiyo hutashangaa ukisikia nagombea jimbo?” “Nishangae tena au ndio nitakuwa mstari wa mbele kwenye kampeni ili kuongeza nguvu!” “Nashukuru. Angalau hapo umenitia nguvu yakuendelea.” “Tafadhali usifikiri vinginevyo. Hata Tino nilikuwa nikimwambia, umezaliwa kuongoza, Jack.” Jack akamgeukia akiwa amekunja uso.

          “Ulinizungumzia kwa Tino!?”  Jack akauliza kwa mshangao kidogo. “Ndiyo. Au nilikosea?” “Hapana, ila sikutegemea!” Sabrina akanyamza kama anayefikiria kisha akaongeza. “Mpaka sasahivi historia ya maisha yangu, haikamiliki bila wewe kuwepo kwenye picha Jack. Kunakipindi nilikuwa nachoka pale nyumbani mpaka nilikuwa nahisi sitaweza kuendelea na yale maisha. Lakini kule kuzungumza na wewe, kunitia moyo bila kunichoka, kulifanya hiyo miaka niliyoishi pale nyumbani tokea nitoke chuo mpaka naondoka pale, siwezi kusema rahisi, lakini niliweza. Kwa hiyo sina jinsi nikamueleza mtu juu yangu nisikutaje wewe Jack.” Jack akajisikia vizuri. Hata hakuwa akijua kama Sabrina anathamini mahusiano ya kawaida tu waliyokuwa nayo.

          Akamuona anasinzia huku amekumbatia koti lake. “Vuta kiti nyuma, ulale kidogo.” Bila kuongeza neno, Sabrina akalaza kiti nyuma, akanusa hilo koti mara kadhaa, akamuona amelivuta mpaka puani, akalala. Hata Jack hakuwa ameelewa. Akamcheka tu mawazoni na kuendelea kuendesha. Walisimama mara moja tu Sabrina akitaka kujisaidia, Jack akaongeza mafuta kwenye gari, safari na stori vikaendelea mpaka Singida nyumbani kwa Jack. 

Nyumbani kwa Jack.

K

weli ilikuwa nyumba ya kawaida tu. Patulivu. Hapakuwa na vitu vya ajabu kama nyumbani kwa Tino na Lela. Lakini akafurahia hayo mapokezi. Mpenzi wa Jack naye alikuwepo hapo na huyo kijana aliyekuwa akiishi naye. Walimpokea vizuri sana mpaka Sabrina akajiuliza ni vipi Jack anaweza kuzungumza na wanawake zake na kuweza kuwa naye karibu. “Naitwa Pamela, lakini wengi wamenizoea kwa jina la Pam.” Akajitambulisha mpenzi wa Jack. “Mzuri kama nilivyokuona kwenye picha!” Sabrina akamsifia, wakacheka.

          “Nilikuwa na kazi, lakini nikasema nije niwapikie mara moja, msikute nyumba tupu. Kwa hiyo kama chakula kimeungua au hakijaiva, mnisamehe.” Pam akaongea akimtizama Jack na cheko. “Nashukuru kujali. Vipi lakini?” Jack akamuuliza Pam. “Safi tu.” Akajibu kiungwana. “Emma ametoka kidogo, lakini amesema hatachelewa kurudi.” Moyo wa Sabrina ukapasuka kwa mshituko baada ya kusikia jina Emma. Akamwangalia Jack. Jack akaelewa. “Karibu tukuonyeshe chumbani kwako.” Akatangulia, Sabrina akafuata nyuma akiwa ameshikilia koti la Jack kama lake! “Huyu Emma ni kijana mdogo tu. Mtulivu sana. Kwa muda huu atakuwa yupo kanisani. Ni mcha Mungu haswa.” Ikabidi Jack amtoe wasiwasi. Sabrina akanyamaza akiendelea kumfuata.

          Akamfungulia mlango, Sabrina akakuta mizigo yake yote humo ndani. “Naomba nijilaze kidogo Jack.” “Chakula!?” “Ni sawa nikija kula baadaye?” “Sawa, lakini nahisi nitatoka na Pam kidogo, ila sitachelewa kurudi.” “Hamna shida. Kama hapa mimi ndio nimefika, basi nirudishie huo mlango wewe endelea na maisha. Nikiamka nitafuata harufu ya chakula mpaka nikipate chakula chenyewe.” Jack akacheka kidogo. “Sawa.” Akafunga mlango, akatoka. Alichokifanya Sabrina nikupanda kitandani na lile koti la Jack akilinusa na kupotelea usingizini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          “Brina mama! Ni saa nne usiku. Amka ule ndipo urudi kulala.” Sabrina akafungua macho. “Nahisi kuchoka Jack! Naomba kulala tu kama ni sawa. Sijapata usingizi hivi kwa muda mrefu!” “Nikuletee chakula hapa ndani?” “Hapana. Tumbo limejaa gesi. Naomba kulala tu, kama ni sawa lakini?” “Sawa. Lakini ingia ndani ya shuka. Hilo koti pekee halitatosha.” Sabrina akajiangalia. Akagundua alijifunika koti la Jack. “Nahisi pia nahitaji kubadili nguo. Nashukuru Jack. Acha nilale, nipumzike. Pengine kesho nitaamka vizuri.” “Hamna shida. Ukiwa na shida usiku uje unigongee. Choo kipo hapo nje ya hiki chumba, ukitoka kama unarudi sebuleni. Kushoto.” “Nahisi nilikiona. Asante.”

 “Nikusaidie kutoa nguo kwenye sanduku lipi! Na hapa hakuna makabati, itabidi kuziacha nguo kwenye hayohayo masanduku yako kwa muda wakati tukijipanga tena.” “Hilo wala sijali. Maadamu sisi tumepata pakujilaza, hizo nguo zitakaa popote pale, sijali. Na wala usihangaikie makabati kwa ajili yangu.” “Lakini ni muhimu.” “Tafadhali usisumbuke kwa ajili yangu, Jack. Najua mpo kwenye kuwekeza sasa hivi. Usijinyime au ukakata mtaji eti kwa ajili ya kabati la humu ndani! Iwe kwa wakati wako. Kuwa na amani kabisa.” Jack akacheka kama aliyeridhika. Akatoka. Sabrina akarudi kulala baada ya kubadili nguo. Akavaa koti la Jack, akajifunika shuka juu na kurudi kulala baada ya kunusa tena hilo koti mpaka akapotelea usingizini. 

Jumapili, siku ya pili Singida.

S

abrina alikuja kuamka saa mbili asubuhi siku ya jumapili. Nyumba ilikuwa imetulia sana. Akajua kila mtu bado amelala. Akajivuta mwisho kabisa wa kitanda, akakaa akiwaza akiwa amejifunika koti lilelile la Jack. Akabaki hapo akiwaza mpaka akasikia mtu akitembea nje, hakujua kama ni Jack au huyo Emma. Akabaki amekaa tu. Baada ya muda akasikia sauti ya Pam kama ameingia hapo. Akajua Jack ndiye aliyemfungulia maana alisikia sauti yake pia wakizungumza. Akaona atulie. “Sitachelewa.” Akamsikia Jack akimuaga Pam, kisha akasikia kama anatembea kurudi chumbani kwake. Akajua pengine wanakwenda kanisani. Akabaki amekaa hapo kitandani. Akajiambia hatatoka mpaka waondoke. Mara akasikia mtu akisalimia. Pam akaitika. “Umependeza Emma! Ndio unakwenda kanisani?” “Ndiyo Shem. Na wewe umependeza.” “Asante.” Akawasikia wakicheka kidogo, mlango ukafunguliwa na kufungwa. Kimya. Akajua Emma ametoka.

          “Brina!” Akasikia sauti ya Jack mlangoni. “Ingia tu Jack.” Jack akaingia. “Kumbe ulishaamka! Mbona hujaja kula?” “Kwako pako patulivu! Nilijua bado mmelala. Umependeza sana Jack. Mnakwenda kanisani?” “Yeap. Tunapenda kwenda ibada ya saa nne. Ungewahi ningekwambia tuongozane.” “Wakati mwingine. Nyinyi nendeni tu.” “Kifungua kinywa kipo jikoni. Jikaze utoke hapo kitandani, ukale ndio upumzike.” “Nitaenda kuoga kwanza ndipo nile. Nyinyi nendeni tu, nitakuwa sawa.” “Sitakawia kurudi.” “Sawa.” Jack akatoka. Baada ya muda akasikia milango inafungwa, kimya.

          Ndipo akatoka sasa na kuzunguka humo ndani. Akakuta maji kwenye ndoo bafuni na jagi ya kuchemshia nje ya bafu juu ya meza. Akajichemshia maji, akaingia kuoga. Alipokuwa tayari ndipo akarudi jikoni. Akakuta kifungua kinywa mezani. Akaona anywe chai na mkate, aache chakula kilichopikwa jana yake. Akajiambia labda hicho kiporo kitakuwa chakula cha mchana. Hapakuwa na yai, wala nyama kama alivyozoea maisha akiwa na Tino. Chai inakuwa kama chakula cha mchana! Hapo ni chai ya rangi na mkate tu. Akala. Akasafisha hapo jikoni, akarudi chumbani kwake. Akaanza kupangilia nguo zake vizuri kwenye masanduku yake ili asipate shida. Akapangilia hiki na kile mpaka akawasikia Jack na Pam. Akatoka.

          “Uchovu umeisha?” Pam akamdaka kwa swali. “Najisikia vizuri. Ibada ilikuaje?” Sabrina akauliza akiwa anasogea hapo sebuleni walipokuwa wamekaa wao. “Nzuri. Vipi wewe?” Akajibu Jack na kuuliza, lakini akaonekana hana sura ya furaha, sura ya hasira kidogo. Sabrina akamwangalia vizuri. “Nimekuta maji hapo bafuni, nikajichemshia na maji ya moto kwenye jagi la umeme hapo nje ya bafu. Nikaoga. Nafikiri sijakosea?”  Akaongea huku akimtizama Jack kama kutaka kujua kama yupo sawa. “Ni sawa kabisa. Na chakula?” Akaendelea kuhoji Jack. “Nilikunywa chai na mkate niliokuta juu ya meza.” “Hukupenda chakula nilichopika mimi?”  Akauliza Pam. “Hata sikuangalia. Nimekuta vyakula vimefunikwa hapo jikoni, nikajua pengine ni mpango wa mchana.” Akajibu Sabrina taratibu tu.

          Akawatizama wote kama anayetaka kujua kama ni kwema. Akaenda kukaa mbele yao. “Vipi? Kwema?” Sabrina akauliza taratibu tu. “Kwema kabisa.” Jack akajibu na kuwasha tv kama anayetaka kufunika kombe, mwanaharamu apite. “Labda mimi niwe muwazi.” Sabrina akamgeukia Pam aliyeanza kuzungumza akitaka kuwa muwazi. “Jack anataka uajiriwe kwenye ile biashara yetu. Sasa mimi nafahamu mambo ya biashara kuliko nyinyi wote. Nimeifanya hii biashara na nyingine nyingi tu. Na siri ya mafanikio yangu ni ile mikakati niliyojiwekea tokea mwanzo na kuisimamia.” Sabrina akajivuta nyuma na kumtizama vizuri Pamela anayesema amefanikiwa.

          Akamuona kweli ni mdada anayeonekana lipo tumaini la pesa. Alikaa kimafanikio. Sabrina akatulia tuli akimsikiliza, ni kama alianza kwa jazba. “Kanuni yangu ya kwanza na ambayo huwa haibadiliki, ni siajiri ndugu au rafiki kwenye biashara zangu. Hiyo haijawahi kubadilika tokea naanza mpaka sasa. Hata ndugu zangu niliozaliwa nao tumbo moja nimekuwa nikiwatafutia kazi sehemu nyingine, sio kwangu. Hiyo ni mojawapo ya kanuni ambayo haijawahi kubadilika, na wala sipo tayari kuibadilisha.” Pam akaongea kijasiri haswa, akionyesha anajua anachozungumza sio mbambaishaji.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Haya, Sabrina tena ndio ametua jijini Singida, kabla hajabisha hodi, taarifa ya kuwa mlango umefungwa kwake na hakuna dalili yakutaka kufunguliwa, imemfuata sebuleni.

Nini kitaendelea kati yao? Maisha ya Sabrina jijini Singida atayaweza na Jack aliye kwenye mahusiano!?

Usikose muendekezo…..

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment