“Mimi
nipo sawa, mpaka baadaye kidogo. Naona kama bado mapema.” Akajibu Jack. “Na
Pam?” “Angekuwepo Emma ningemtuma dukani akalete kinywaji. Nina kiu!” “Kwani ni
mbali? Mimi nimelala sana. Nataka kutembea kidogo.” Jack akashituka kidogo,
akamgeukia Sabrina na kumtizama kwa mshangao kidogo. “Ningefurahi kutoka. Kama
mna kitu kingine mnahitaji mniagizie tu huko dukani.” Pam akamwangalia Jack,
Jack akabaki kimya. “Unakunywa soda gani?” Akamuuliza Pam. “Nataka bia
baridiii.” Sabrina akacheka. “Aina gani na ngapi?” Akamtajia. “Na wewe Jack?”
“Sprite tafadhali.” “Sawa. Hakuna kitu kingine mnahitaji huko dukani?” Wakaangaliana.
“Naona ni hivyo tu.” “Basi nitarudi baada ya muda mfupi.” “Mbona huchukui pesa
sasa?” “Msijali. Hiyo itakuwa ofa yangu.” Sabrina akarudi chumbani, akachukua
pesa na kutoka baada ya kuelekezwa wapi pakwenda.
Alitoka hapo nia pia ilikuwa nikusoma
mazingira. Hapakuwa mbali. Akakuta duka kama alivyoelekezwa. Akanunua hivyo
vinywaji alivyoagizwa, akarudi navyo kwa haraka. Akawapangia mezani. “Mmesema
bado hamna njaa?” Akauliza Sabrina. “Mimi ningekula kidogo.” Pam akataka
chakula. “Na wewe Jack?” Sabrina akauliza. “Mimi naona wakati moyo huo
wakutuhudumia ukiwa bado upo, basi kipashe moto tu chote, ukiweke mezani.”
Sabrina akacheka na kuanza kuondoka pale. “Naona hilo wazo lako lina akili.
Ngoja nikipashe, niwawekee chote mezani.” Akarudi jikoni.
Akakuta chakula kilichomtoa hata hamu
ya kula. Wali mweupe, kama mbichi! Mchuzi mwingi wa nyama ya ng’ombe,
ulishaganda mafuta, lakini aliweza kuona maganda ya nyanya. Akabaki amekodoa
macho. Akatamani arekebishe, akajiambia asije kumuudhi Pam. Akawapashia moto
hivyohivyo kwa kutumia microwave, akawawekea mezani na kwenda kuwakaribisha.
“Wewe huli?” Jack akauliza. “Nataka kutoka nitembee kidogo, nisome mazingira ya
hapa.” “Usije potea tu?” Pam akatoa angalizo, Sabrina akacheka na kutoka hapo
ndani. Angalau Jack akaonekana ni kama ametulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
J |
ack
alikuwa akiishi mjini. Sabrina akaanza kutembea huku na kule akiangalia hili na
lile. Akapita kwenye baa kadhaa, akiulizia kazi. Mmiliki mmoja akamwambia
anatafuta muhudumu wa usiku. Sabrina akafurahi sana. “Naweza kuanza lini?”
“Hata kesho.” Hilo akalifurahia sana. Akatoka hapo akiwa na furaha zote. Akarudi
nyumbani giza likiwa limeshaingia asijue kama alizunguka siku nzima. Jack
akaenda kumfungulia mlango. “Naomba usiwe unafanya hivyo Sabrina. Umenitia
wasiwasi.” “Kwani nimechelewa sana!?” Sabrina akauliza taratibu tu. “Umeondoka
mchana, unarudi sasa hivi na sikupati kwa simu!” Akamshika mkono.
“Acha wasiwasi Jack! Mkubwa hapotei.
Njoo nikupe habari za nilikotoka.” Akamvutia kwenye makochi, wakakaa. “Nini?”
“Mwenzio nimetoka hapa nikaanza kuzunguka kwenye mabaa. Nimepata kazi kwenye
Pub ya Macha. Ameniambia naweza kuanza kazi hata kesho. Lakini ananafasi ya jioni.”
“Hapana.” Sabrina akatoa macho kwa mshituko, akahisi hajamsikia Jack vizuri.
“Napafahamu pale Pub, Sabrina. Na ndiko wanawake wanapokwenda kujiuza. Na yule
mzee anapenda wasichana kama wewe ili kuvutia wateja.” “Mimi sio msichana Jack,
nakaribia...” “Hapana Sabrina. Hapana. Naomba utulie tutafute kazi sehemu
nyingine.” “Jack! Mimi ni mtu mzima, siwezi kufika pale nikajiuza!” “Hapana
Sabrina. Huu mji ni mdogo sana. Hivi karibuni utajulikana unaishi hapa na mimi
ninayefahamiana na watu wengi. Watu watanishangaa kwa nini ukafanye kazi za
usiku za kuuza bia, wakati ninaweza kukuunganishia kwengine?” “Muda haupo
rafiki kwangu Jack! Nahitaji kufanya kazi.” Sabrina akaongea taratibu. “Una haraka
gani Brina?” Jack akauliza kwa ukali kidogo.
“Kweli unataka nikujibu hilo Jack!?”
“Wewe niambie una haraka gani! Ndio umefika tu hapa jana, leo unaona
unachelewa!” “Mimi sianzi maisha Jack. Naendeleza. Ninavyozidi kuchelewa,
ndivyo nitashindwa kuajiriwa. Hakuna mtu anaajiri mama mjamzito. Watajua sio
mtu wa kudumu. Nitakosa kazi na mwishoe nitashindwa hata kujikimu mimi na huyu
mtoto.” “Baa! Hapana Sabrina. Naomba katika hilo ulielewe tu. Tutatafuta sehemu
nyingine.” Sabrina akajirudisha nyuma kwenye kochi, akanyamaza.
“Umenielewa lakini?” “Labda unisaidie
kuniambia ni wapi na wapi nisihangaike tena kuomba kazi.” “Kwa nini usitulie ukajifikiria
wewe na mtoto?” Sabrina akakunja uso. “Mimi sio mgonjwa Jack! Ni mzima kabisa. Kwa
nini nisiingize pesa kwa kipindi hiki? Nitakuwa sawa, tafadhali usiwe na
wasiwasi juu yangu.” Jack akanyamaza. “Niangalie Jack.” Jack akamwangalia.
“Najua unanifahamu. Mimi sijui maisha yakukaa tu. Maisha yangu yote nikufanya
kazi.” “Itakuaje uzidishe kazi, chochote kitokee kwa mtoto?” Ilimgusa sana
Sabrina, mpaka akabaki ameduaa. “Mimba changa huwa zinatoka Sabrina!” “Kama kuna
tatizo. Lakini mimi sina tatizo lolote, na nitakuwa muangalifu Jack. Asante kwa
kujali.” Wakanyamaza kwa muda kila mmoja akiwaza lake. Akamuona amesimama.
Akaelekea chumbani kwake.
Baada ya muda akatoka akiwa ametoa
nguo zile za kanisani, amevaa nguo za kawaida tu. “Unataka kuangalia nini
kwenye tv?” Sabrina akafikiria. “Kwani wewe unalala saa ngapi?” “Najitahidi
angalau saa 4 niwe nimeshalala ili saa 12 asubuhi niwe nimeamka vizuri.” “Na
Emma?” “Atakuwa ameshakwenda kulala. Shule yake ipo mbali kidogo, kwa hiyo huwa
anawahi kulala na kuamka.” “Njoo ukae hapa.” Jack akaenda kukaa pembeni yake.
“Huwa unapenda kula nini na hupendi
nini?” Jack akabaki akimwangalia. Sabrina akacheka. “Kesho nitakuwepo hapa siku
nzima, nataka niwapikie, mkija mkute chakula.” “Aaah! Emma namuona anakula kila
kitu, nafikiri kama mimi tu. Hakuna mchaguzi hapa ndani. Chochote. Lakini sio
ujichoshe kwa makazi ya humu ndani. Naomba tulia Sabrina.” “Jack ni muoga
jamani! Hebu niangalie jinsi nilivyo. Sina ugonjwa wowote ule!” “Ndio sitaki
uanze kuugua ukiwa na mimi. Wewe mwenyewe umesema siku hizi mbili tatu tumbo
limeanza kukua kwa haraka. Inamaana mtoto naye anakua. Umehangaika huyo mtoto
asitoke, sasa utulie mpaka mwisho.” Sabrina akacheka.
“Usicheke. Mimi namaanisha.” “Nakuona
Jack. Naona mwenzangu upo makini kuliko hata mimi! Lakini naomba nikutoe
wasiwasi. Hakuna kitu nitafanya chakumdhuru mtoto. Nitaongeza umakini, lakini
lazima kutafuta kazi Jack. Ninajukumu la mtoto ambalo siwezi kulikwepa.
Kunakutakiwa chakula, malazi, hospitali, kabla na baada yakujifungua. Yote hiyo
ni pesa. Ukizungumzia kliniki, ni pesa pia. Kula vizuri pia ni pesa. Jioni hii
nimetoka kununua matunda hapo sokoni, ni garama kweli! Lazima nifanye kazi ili
hata kuendelea kumtunza mtoto.” “Naelewa. Naomba nipe muda. Usinikatie tamaa
kwa sababu nimeshindwa hii mara moja tu.” Sabrina akamsogelea na kumshika
mkono.
“Tafadhali usione umeshindwa Jack. Nafikiri
Pam yupo sahihi. Ndugu na marafiki wanaweza kukurudisha nyuma. Pengine ingekuwa
ngumu kwake kuniwekea mimi msisitizo kwa kuwa anajua unanihusu. Ndio maana na
mimi nimejaribu kutafuta kwengine. Wote tujaribu tu mpaka tufanikiwe. Sawa?” “Kama
unachukulia hivyo utanifanya nisitafute kwa kupaniki.” “Tafadhali usipaniki.
Mimi mwenyewe najua kupata kazi ni shida. Nimezunguka sana pale Moshi bila
mafanikio. Kwa mara ya kwanza leo ndio nimepata hapa kwenye huu mji wako.”
“Achana na Macha. Tutapata kwingine.” “Sawa.” Sabrina akamuachia mkono.
Wakatulia hapo kwenye kochi wakiangalia tv mpaka Sabrina alipoaga anakwenda
kuoga alale.
“Mbona huli wewe?” “Nilikula mishikaki na kachumbari kwenye moja ya hizo baa nilipokwenda kutafuta kazi. Hapa nimeshiba. Nitakula tu matunda kabla yakulala. Wewe nenda kapumzike.” Jack akazima tv na kwenda kulala. Sabrina akaanzia jikoni. Akakuta vyombo vichafu. Akasafisha, akala matunda yake hapohapo jikoni., ndipo akaenda kuoga na kulala akiwa amevaa koti la Jack.
Jumatatu.
S |
abrina
hakupendelea kitafunio alichokula asubuhi ya jumapili. Alikiona dhaifu sana. Hata
kwao tu kwenyewe walikuwa wakifuga kuku wa kienyeji kwa hiyo swala la mayai ya
kukaanga au kuchemsha asubuhi halikuwa jambo la kushangaza. Sasa siku iliyopita
alipopita sokoni alinunua baadhi ya vitu, akarudi navyo pale. Aliamka asubuhi,
akatengeneza chai na kuchemsha tambi za sukari, akakaanga mayai kwa Jack na
Emma. Lakini akawa amemchelewa Emma, aliondoka akiwa ndio anamka. Kwenye saa moja
kamili Jack akatoka chumbani akiwa ameshavaa. “Ndio unaondoka?” Sabrina
akamuwahi. “Nilikwambia leo nakwenda kazini, mama.” “Nimetengeneza kifungua
kinywa.” Jack akacheka. “Wenzio asubuhi humu ndani hakupikwi. Kila mtu anawahi
kazini.” “Sasa mimi nimepika Jack. Huwezi kuondoka hapa bila kula.” Jack
akakaa.
“Chakula gani hicho chakulazimishiwa
Sabrina!?” “Hata kama hutapenda lazima ule. Mimi nimedamka vyote hivyo!” “Kwani
mimi nimekataa kula? Sema hapakuwa na mpikaji asubuhi. Emma naye mapishi yake
sijayaelewa vizuri. Huwa namuwekea mazingira yakutopika.” Sabrina akacheka
sana. “Kwani anapikaje?” “Natamani nikwambie umuombe apike, lakini tutalala
njaa. Tena anajuhudi kweli akiwa hapo jikoni. Unaweza sema utalamba sufuria,
lakini akikuwekea kwenye sahani, hata kupitisha vijiko vitatu huko mdomoni ni
shida. Nyama inakuwa kama iliungwa, halafu ikaoshwa na maji mengi ikarudishwa
tena kwenye mchuzi.” Sabrina akazidi kucheka.
“Halafu hivyo vyombo atakavyotumia
huko jikoni, utashindwa kwa kupita. Jiko linakuwa chafu utafikiri amepika
chakula chakuuza mgahawani!” Sabrina akazidi kucheka. “Kwa hiyo nani anapika?”
“Mwenyewe. Yeye huwa namuomba anifulie na kupiga pasi. Chakula ndio huwa napika
au nanunua. Tukipata mfadhili kama hivyo Pam, anakuja kutuchemshia hapa na
yeye, anatuachia tunaendelea kula.” Sabrina akazidi kucheka. Akakumbuka mchuzi
na wali aliopika Pam. “Kwa maneno hayo, lazima nije kuonja mapishi yako.” “Wala
usiwe na wasiwasi. Sio mtaalamu sana, lakini nahisi kuna niliowapita.” Sabrina
akazidi kucheka.
“Haya, kula uende kazini.” Jack
akaanza kula. “Kwa mwendo huu, kunawili lazima.” Sabrina akazidi kucheka. “Una nguo
za kufua na kupiga pasi nikusaidie?” “Wewe pumzika Sabrina, Emma atafua.” “Nataka
kufua nguo zangu nilizokuwa nazo safarini na ile niliyozunguka nayo jana,
naweza kukufulia na zako.” “Nitashukuru. Sasa ukiingia tu hapo chumbani kwangu,
nyuma ya mlango nimeweka kwenye tenga la nguo chafu, aliliweka hapo mama
Msindai. Hilo ndio linakuwa la nguo chafu. Usiangalie chumba wala kitanda.”
“Kuchafu sana?” “Huwa nafanya usafi siku za jumamosi, mama Msindai
akiniongelesha kwenye simu mpaka nimalize. Sasa jumamosi hii ndio kama
ulivyoiona. Ila nitasafisha nikirudi.” Sabrina akamuacha kumuongelesha ili ale
huku akimfikiria Jack na mama yake. Huyo mama ukimsikia na huyo mwanae utafikiri
mama asiye na majukumu. Amejaa kwenye maisha ya Jack tokea Jack yupo chuoni
habari za ujio wa huyo mama aliyekuwa waziri wa afya akija kumtembelea mwanae
huyo alikuwa akizisikia mara kwa mara. Sasahivi yupo naye na huko Singida japo
yeye anaishi Dar.
Akawa anakula huku anaangalia simu
yake. Akapitia hiyo simu, akamuona amerudisha mfukoni, akarudisha mawazo kwenye
chakula. Akala mpaka akamaliza. “Nashukuru kujali Brina. Angalau leo nakwenda
kazini nimeshiba na nimekula kitu kizuri.” “Karibu, na uwe na siku njema. Kwa
hiyo ni mpaka jioni?” “Saa kumi na nusu nakuwa nimesharudi. Labda nimpitie Pam
pale kwenye biashara.” “Sawa.” Wakazungumza kidogo, Jack akaondoka.
Sabrina akasafisha hapo jikoni, na kuingia chumbani kwa Jack. Hapakuwa pachafu sana ila kwa jinsi alivyopaona mle ndani na vitu vyake, akajua ni kazi ya mama Msindai tena. Kulikuwa na vitu vizurivizuri, vingine vidogovidogo ungeweza kupuuza. Ila jinsi vilivyopangiliwa humo ndani vikaleta maana na kuvutia, ndipo akajua muwekaji na mpangiliaji lazima awe na jicho la kike. “Nani kama si mama Msindai anayeweza kuweka vitu vya namna hii, tena kwa mpangilio huu?” Akajiuliza Sabrina huku akimsaidia kusafisha na kutandika kitanda. Aina yenyewe ya mashuka yenyewe ni kotoni ile ya maana kama aliyomuona nayo Jack chuoni. Akapangilia viatu na nguo vizuri na kwa usafi, akapiga na deki kabisa, akachukua nguo chafu. Vile amezibeba tu, harufu ya zile nguo chafu za Jack ikamvutia. Akaingia nazo chumbani kwake. Nguo hizo chafu za Jack, Sabrina akaanza kuzinusa mpaka anafunga macho kwa furaha yake. Akaona avae moja wapo kabisa, akajiweka kitandani huku akiendelea kunusa zile nguo mpaka akapitiwa na usingizi hapohapo kitandani. Akaja kushituka kutoka usingizini ni saa nne asubuhi. Akakimbilia nje kufua. Alikuta kuna matanki makubwa ya maji, yamejengewa vizuri, na maji safi. Akafua nguo zake na za Jack, akaanika.
Sabrina
aanza kuwa Kero kwa Pam.
W |
akati
anaingia ndani, Pam naye akawa anaingia getini. “Karibu.” Sabrina akamkaribisha
kwa furaha zote, asiwe na habari kuwa bado amevaa shati la Jack. Akashangaa Pam
anamwangalia kwa kutomuelewa. “Karibu ndani.” “Naona umeshakuwa mwenyeji!” “Nitafanyaje
wakati wenye nyumba wangu wameniacha peke yangu! Inabidi kuchangamka tu. Nilikuwa
nafua huku napika ndani. Tuingie ndani.” Sabrina akaweka msisitizo, yeye
akaingia. “Nisije unguza.” Moja kwa moja akaelekea jikoni.
Sabrina akaongeza maji kwenye nyama,
akatoka. Akamkuta Pam ni kama amezubaa pale sebuleni. “Vipi! Kwema? Mbona hata
haukai?” “Nilikuwa napita tu.” Akajibu Pam kama aliyekuwa na jambo akagairi.
“Nashukuru kupita kuja kuniona. Ila kuna tambi za asubuhi. Nikuwekee kidogo
upate chai?” Sabrina akauliza, hana habari. “Kidogo tu, usiondoke bila kula.”
“Mimi sina njaa.” Pam akajibu tu hivyo na kuondoka. Sabrina akakunja uso kama ambaye
na yeye hamuelewi mpenzi wa Jack. Alipokosa jibu, akafunga mlango nakuendelea
na shuguli zake.
Pam Kwa
Jack.
B |
ila kujua,
kumbe Pam alimpiga picha wakati wamesimama sebuleni, akamtumia Jack na ujumbe. ‘Mbona sielewi!!’ Jack akaangalia ile picha na ujumbe,
hakufanya haraka kujibu. Akabaki akifikiria. Mara simu ya Pam ikaingia, Jack
akapokea. “Mbona hujanijibu sasa!?” Pam akauliza
kwa hasira. “Juu ya ile picha? Au juu yakubadili mawazo
kumpa kazi Sabrina?” Jack akauliza taratibu tu. “Yote.
Maana nimekutumia ujumbe kuwa nafikiri kuna kazi Sabrina anaweza kufanya pale
kwenye biashara. Hukujibu. Nikaamua kwenda mimi mwenyewe kuzungumza naye, ndio
nimemkuta amejaa kwenye nyumba kama mama mwenye nyumba na amevaa gauni zuri tu,
na juu akavaa shati lako lile ulilovaa jana kanisani! Ndio nikakuuliza,
sielewi.” “Sikujua kama ni swali.” Pam akashangaa jinsi Jack alivyo
jibu.
“Wewe Jack! Inamaana
unaona sawa kwa Sabrina kuvaa nguo zako!? Maana nimeshindwa hata kumuuliza.
Anaonekana kama yeye hana cha ajabu alichofanya! Ni kama ni jambo la kawaida tu
kwake! Labda mimi ndio sielewi!” “Kwa kufikiria kwa haraka mimi nahisi wakati
anafua ile asubuhi, alipatwa baridi, akavaa hilo shati, akasahau kutoa. Vipi lakini
wewe?” Jack akaona abadili mazungumzo. “Mmmh!
Nahisi kama sielewi tena!” “Juu ya nini tena? Bado tupo kwenye shati au juu ya
siku yako?” “Mimi naona kama wewe unaona ni sawa tu!” “Ndio maana nauliza juu
ya nini? Tunazungumza juu ya mambo zaidi ya mawili kwa wakati mmoja. Ndio maana
na mimi sijui unataka kunisikia nikisema nini!” “Basi bwana. Pengine mimi ndio
nakuza. Lakini sidhani kama ni kitu cha kawaida.” Jack akanyamaza.
Akaona amekatiwa simu.
Jack akampigia tena. “Naona simu ilikatika bila kumaliza mazungumzo. Mzima
lakini?” “Kama ungetaka kujua juu ya hali yangu si ungenipigia?” “Si ndio tunazungumza
hapa, Pam! Vipi asubuhi hii ya leo, kwema?” “Nikuulize wewe! Maana nakwambia
juu ya wasiwasi wangu kwa Sabrina, ni kama huonekani kushangaa.” “Ndio nauliza
juu ya kazi au shati! Ni nini Pam?” “Mimi sijapenda kumuona anavaa nguo zako.
Jumapili alitoka na koti lako. Leo shati! Wote nyinyi mnaonekana kwenu ni jambo
la kawaida, lakini si kwangu Jack. Si sawa kwa yeyote yule.” “Mimi naona unakuwa
na wasiwasi bure. Sasa uliamua nini juu ya kazi?” “Nilishindwa hata kuzungumza
naye kwa mshituko.” Pam akaongea kwa kulalamika.
“Niliondoka
bila hata kukaa!” “Yote hiyo ni sababu ya shati tu ndio amekosa kazi au kuna
jingine?” “Nimeona hili tuliweke sawa kwanza kabla hatujaendelea.” “Sawa.” Jack
akajibu kirahisi tu bila kuonyesha kujali. “Lakini wewe
ni mzima? Uliamka salama?” “Niliamka salama, naona siku ndio inataka kuwa
mbaya.” “Usiruhusu iwe mbaya. Maadamu umeamka mzima, hilo ndilo la msingi na ni
zawadi tosha kutoka kwa Mungu.” Pam akashangaa sana. Akaamua kumuaga tu.
Jack akamtakia siku njema, akakata.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa Sabrina akaendelea na shuguli
zake asiwe na habari. Wakati anataka kukaa ili kuanza kupika rasmi, ndipo
akagundua amevaa shati la Jack. Bila wazo la pili, akaenda kulifua, akalianika
na kuendelea na kupika. Nyumba haikuwa chafu. Aliisafisha tu kidogo, ndipo akapika
chakula huku akiumua maandazi ya kifungua kinywa. Aliyatia hiliki, nyumba nzima
ilikuwa ikinukia. Maana hata maji ya wali aliyachemshia na hiliki, lakini wali
aliukaanga na kitunguu maji tu ndipo akaweka hayo maji ya hiliki.
Maandazi
yalipoumuka, akaanza kuyachoma huku akisafisha pale jikoni. Akayafanya yote
hayo. Inakuja kufika saa nane mchana mtoto wa pwani akawa amemaliza kufanya
vitu vyake huko jikoni, nakuacha nyumba ikinukia tu. Chakula cha usiku na maandazi
kwa ajili ya kifungua kinywa vikawa tayari. Akarudi kwenye nguo alizofua. Za
kwake hakuwa akipiga pasi. Akazikunja tu na kuziweka kwenye masanduku yake.
Nguo chache za Jack akakunja na alizoona zinahitaji kupigwa pasi, basi
akazinyoosha vizuri akitumia pasi. Akaenda kuzilaza vizuri kitandani ili mwenyewe
aje aweke kabatini kwake. Inafika saa kumi jioni, Sabrina yupo hoi. Akaamua
alale kidogo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Saa 10:30 jioni Jack anaingia ndani,
anakutana na harufu nzuri ya chakula. Akapitiliza jikoni moja kwa moja. Akakuta
chakula na maandazi. Akacheka na kuchukua andazi moja. Akaelekea chumbani kwake,
alipoingia akastaajabu. Chumba kisafi, na pamepangwa vizuri mpaka kitanda
kimetandikwa mashuka masafi. Akatulia kidogo akizungusha macho. Hata yeye
aliposema huwa anafanya usafi hapo ndani siku za jumamosi, si kwa kiwango hicho!
Akaona nguo zile chafu zimefuliwa zote na kupigwa pasi, na kuwekwa kitandani nyingine
zikiwa zimekunjwa. Akajua kwa aina ile ya usafi, lazima Sabrina atakuwa
amelala.
Akaenda chumbani kwake. Akagonga mara
mbili tatu, kimya. “Brina! Brina!” Akaita taratibu. Kimya. Akapatwa na
wasiwasi. Akaona aingie. Sabrina alikuwa amelala hapo kitandani, sio amevaa
lile koti lake, ila amelikumbatia lipo usoni kama aliyekuwa akilinusa mpaka
kupitiwa na huo usingizi. Jack akacheka taratibu. “Hakika Jack upo
matatizoni!” Akajiambia huku akimtizama Sabrina asiamini kama Sabrina yupo
nyumbani kwake yeye! Akabaki ametulia akimtizama. Moyo wake ukajawa furaha, asiamini
hatimaye amefanikiwa kufika kwake. Alishamsubiri huyo Sabrina kwa miaka mingi
sana. Akafurahia kutendwa na Tino, ikawa bahati yake yeye.
Akamuona jinsi alivyokumbatia lile
koti lake. Akakumbuka jinsi walivyolala pamoja Moshi. Akacheka. “Anajua
kulala vizuri huyu!” Akabaki amesimama akila andazi lake huku akimtizama.
Akaamua akae palepale kitandani. Hakikuwa hata kitanda kikubwa. Sabrina akashituka.
“Baba mwenye nyumba, umerudi?” “Nimerudi mama. Umeshindaje?” Sabrina akakaa. “Pole na kazi.” “Asante. Vipi
wewe?” “Nimekuwa na siku nzuri tu, nimelala kujipumzisha.” “Sasa kwa mwendo
huu, naona nikuajiri tu humuhumu ndani. Naona hii ofisi itakufaa.” Sabrina
akaanza kucheka. Akaanza sasa kulivaa lile koti la Jack.
“Unataka kuniajiri?” Akauliza huku akiliweka
sawa hilo koti mwilini mwake. Akamuona analinusa tena hilo koti kidogo,
akamuona jinsi alivyotulia usoni kama amefurahia harufu aliyokutana nayo, kisha
akaendelea kuliweka sawa mwilini mwake. Akagundua ni jambo analolifanya bila
kufikiria, hana hata habari na anachokifanya. “Sasa kama ndio alifanya
hivihivi mbele ya Pam, basi ndio maana Pam alichangayikiwa!” Akajiambia
Jack, na kucheka. Sabrina akamwangalia. “Wewe unafurahia maandazi ya chai
asubuhi bwana, Jack! Kula wali. Mbona unataka kuniharibia bajeti?” “Nimeonja tu
mama! Nikienda kuongeza moja, basi ndio la mwisho. Nakua nimekula sasa mawili.”
“Sidhani kama yatafika kesho!” “Yatafika wala usitie shaka. Nikiongeza la nne
la kwenda kulalia, basi.” “Umefika saa ngapi la nne, wakati tupo la pili!?” Wakaanza kucheka. Stori zikaanza.
Sabrina akimuulizia kazi anazofanya
kazini kwake. Anaonaje hiyo kazi. Akataka kujua kwa nini alichagua Singida.
“Kwanza nilipangiwa. Wenzangu tuliokuwa tumepangiwa nao na Wizara ya fedha,
wengi wakaamua kuacha kabisa kazi baada yakushindwa kupata uhamisho. Maana
sheria ilikuwa lazima uje angalau uripoti eneo la kazi, ufanye kazi kidogo ndipo
uombe uhamisho. Wakaona hawataweza, wakaacha. Unamkumbuka Ibra?” “Yule
aliyekuwa waziri wako wa fedha chuoni?” “Kumbe bado unamkumbuka!” “Mlivyokuwa mkifuatana
kama kumbikumbi vile! Kila mtu alikuwa akiwajua ni marafiki.” Jack akacheka.
“Alikuwa hapa kama majuma matatu
yaliyopita. Akichoka tu na kelele za jiji, anakuja huku kupumzika.” “Kumbe!
Sikujua!” “Tulipangiwa naye kazi. Ila yeye alipangiwa Mpiji. Bwana
alikasirika!” Wakaanza kucheka. “Kwa hiyo hakwenda?” “Wewe si unamjua Ibra
anavyojipenda? Mtoto wa mama yule. Hakutaka hata kwenda kuripoti.” “Anafanya
nini sasa hivi?” “Biashara tu, Ibra utamuweza? Lakini inaonekana sio mbaya.
Halii njaa.” “Hivi alikuja kumuoa yule msichana wake wa chuoni?” “Stela?”
“Ewaa, Stela.” “Walikorofishana mwishoni kabisa. Hawakurudiana tena. Yupo
amechumbia msichana mwingine, lakini naona anamlalamikia kila wakati. Sasa
sijui ataoa!” Sabrina akanyamaza.
“Nashukuru kwa kunisafishia chumba na
kunifulia. Maana nimeingia pale, nikahisi nimepotea chumba! Mwenzio huwa sina
hata muda wakupanga vile mpaka siku mama Msindai aje kunitembelea, ndio
anapapanga vile. Mimi ni bora kusafi, basi.” Sabrina akacheka akiwa amepata
jibu lake. Kazi ya mama Msindai. “Asante.” “Karibu.” Mara wakasikia mlango wa sebuleni
unafunguliwa. Wakajua ni Emma. “Ametoka shule huyo!” “Si atakuwa anachoka
sana?” “Ndio maisha, atafanyaje?” Mara wakasikia mlango wa hapo chumbani
unagongwa. Sabrina akamtizama Jack, akamuona amekunja uso. Akageukia mlangoni.
“Nani, Emma!?” Akauliza Jack kwa mshangao. Mara mlango
ukafunguliwa bila jibu. Alikuwa Pam. Jack akaonekana kushangaa. “Karibu Pam.
Tunakumbushia enzi.” Sabrina akaongea na cheko, lakini Pam akaonekana kama
anamshangao. “Vipi, kwema?” Jack akauliza akiwa amekaa palepale kitandani
ambako Sabrina alikuwa amejivuta mpaka ukutani amekunja miguu na kuvaa lile
koti la Jack. Wote wakabaki wakimwangalia yeye baada yakubaki kimya.
“Pam, upo mzima?” Jack akarudia tena. “Nimeshangaa
hujaja kule kwenye biashara?” Akaongea kwa kulalamika, Jack akakunja uso.
“Kwani tulikuwa na miahadi kule?” Akauliza Jack kiustaraabu tu. “Kwani siku
zote unaponipitia unakuwa na miahadi? Mbona sikuelewi wewe Jack!?” “Pam, mgeni
siku ya kwanza. Nimerudi nyumbani moja kwa moja ili kuangalia huyo mgeni
tuliyemuacha siku nzima anaendeleje.” “Mgeni huyo naona mpaka na nguo
mnavaliana!” Jack akashituka moyoni, akajua Pam anataka kutibua hali ya hewa.
“Maana sasa hivi joto, lakini amevaa
koti lako!” Sabrina akajiangalia. “Mimi nahisi sio maswala ya baridi. Kuna
kijiharufu nakipata kwenye hili koti, inanifanya nitake kulivaa kila wakati!
Linanifanya kama natulia fulani hivi! Imetulia.” Wote wakashangazwa vile
alivyojibu. Sabrina aliongea bila hata hofu. “Ndio maana basi nikakukuta umevaa
shati la Jack!” Sabrina akaanza kucheka. “Nimekuja kujishitukia nipo jikoni,
nataka kuanza kupika. Nikasema hapa ndio kuja kukutwa nimevaa nguo ya baba
mwenye nyumba. Nilifua zote, nikasahau shati nililokuwa nimevaa.” Akatulia
kidogo kama anayejaribu kufikiria.
“Mimi nahisi ni lotion anayopaka Jack
ndio inayonifanya nipende kunusa nguo zake, si bure! Imetulia kweli! Lakini
usiwe na wasiwasi baba mwenye nyumba wangu. Shati nililifua vizuri, na nikalipiga
pasi kabisa, nimekurudishia. Na hili koti harufu ikiisha tu, nalifua,
nakurudishia koti lako. Usikonde.” Jack akatamani kucheka kwa sauti, lakini
akajua Pam atakasirika.
“Najua wote mmekuwa na siku ndefu
sababu ya kazi, njooni mezani mle.” Sabrina akatoa lile koti na kulipanga
vizuri hapo kitandani. “Pam kipenzi, njoo uonje maandazi niliyopika. Mazuri
sana. Nakutengenezea na kikombe cha chai kabisa. Au unasemaje?” Mpaka Pam
akaishiwa nguvu. Akamtizama Jack, Sabrina akacheka. “Haya nawapisha wapenzi
nyinyi, lakini mje kula.” Sabrina akatoka na kuwaacha hapo chumbani.
“Wewe
Jack!” Pam akanong’ona kwa mshangao, Jack akaanza kucheka. “Si umemsikia
mwenyewe?” “Naona na hasira zote zimeisha!” Wakaanza kucheka taratibu. “Ndio
nini sasa!?” Akauliza Pam. “Au ndio hiyo mimba yake?” “Mimi sijawahi kuishi
naye kama hivi, ila tumekuwa karibu kwa miaka mingi. Naomba tumpe muda tuone.
Unaweza na wewe kujipatia rafiki mzuri!” Pam akawa kama ameshaanza kulainika.
Akatulia. “Nilishaanza kuingiwa na wasiwasi. Nikajiambia anataka kunipindua!”
Jack akasimama na kumkumbatia Pam, akataka kupata busu. Kufika mdomoni akapata
harufu ya pombe. Akarudi nyuma.
“Umeshaanza kunywa mapema hii Pam!?
Jumatatu hii!?” “Nimepata mbili tu na wewe Jack, acha wasiwasi. Tena nilimtuma
mtu akaniletea palepale kazini. Sijakwenda baa.” Jack akamwangalia akaamua
kunyamaza. “Wewe vipi Jack!? Ni bia mbili tu nimekunywa, pia unakasirika? Mimi
ndio starehe yangu.” Jack akaamua anyamaze na kutoka hapo chumbani. “Kwa hiyo
ndio umesusa hata kunibusu hutaki sababu ya bia mbili tu tena nilizonunua kwa
pesa yangu mwenyewe!?” Sabrina akawasikia kwa kuwa walitoka nje ya chumba.
“Ningekuwa nimehongwa je?” Hakumsikia Jack kujibu, akawasikia wanaelekea
chumbani kwa Jack.
Baada ya muda akasikia wanatoka, Pam
anacheka kilevi kidogo. “Wewe hukuwa na nia. Umenitafutia tu sababu ya
kunikasirikia, uninyime. Lakini si hizi bia mbili! Eti Jack?” Akawasikia
wanakuja upande ule, Jack kimya. Bahati nzuri Emma naye akawa anaingia.
“Pananukia vizuri humu ndani! Huyo atakuwa mgeni tu.” “Nilikwambia mgeni
anaitwa Sabrina.” Akamsikia Jack akimjibu. Emma akacheka. “Shikamooni.”
Wakaitikia. “Habari za shule?” “Shule ni shule tu kaka yangu. Vipi Shem langu
la nguvu? Naona ushakolea mapemaa, kabla giza halijaingia.” “Bia mbili tu na
wewe Emma! Acha umbea.” “Hata mimi nakubaliana na wewe, Shem. Mbili tu!”
Wakaanza kucheka Emma na Pam.
“Acha mimi nielekee jikoni. Njaa inauma kweli!”
“Hujala mchana?” Jack akamuuliza. “Wala asubuhi kaka. Hapa nina njaa, hata
kujisomea sitaweza.” Emma akaingia jikoni. “Mungu wa ajabu jamani! Mgeni njoo,
wenyeji tupone. Hii nyumba haijawahi kupikwa maandazi! Kitafunwa chetu, mkate.
Si umeona jumapili?” Sabrina akaanza kucheka. “Na hakuna vyombo vyakuosha! Wewe
usiondoke humu ndani.” Jack akamsikia. “Vya usiku wewe ndio unaosha Emma.
Usimfanye Sabrina kijakazi wako.” “Sawa kaka. Harufu ya chai unaipata lakini
huko?” Sabrina akazidi kucheka.
“Na huyo umpe yale mashariti ya ulaji
wa maandazi. Hana kikomo huyo.” Jack akaongeza. “Kuna masharti ya ulaji tena!?”
“Kwenye maandazi tu. Ni ya kifungua kinywa.” “Jamani huo mtihani! Mimi naomba
kutoa ushauri.” “Usimsikilize huyo. Usimuone mwembamba hivyo, anakula bila mchezo.
Ukiendelea kumchekea hapo, asubuhi wote tutakuwa hatuna kitafunywa.” “Mbona
hunipi nafasi kaka?” “Haya sema.” “Kwa kuwa ni mapishi ya mara ya kwanza humu
ndani, basi tuyasherehekee haya leo. Kesho kupikwe mengine, ya kila asubuhi.”
Wote wakacheka kasoro Jack. “Si nilikwambia mimi?” “Lakini wazo sio baya kaka!
Najua hata wewe unatamani.” “Mimi nimekuwa mstaarabu, nimekula moja tu.” “Acha basi
na mimi nipate moja lakuonja, mengine nitapewa kwa huruma za Sabrina.”
Wakaendelea kuzungumza na kucheka, mpaka Jack na Pam wakahamia hapo mezani.
Wakala, Pam akaaga. “Asante Sabrina.
Chakula kitamu kweli!” “Karibu.” “Unaondoka Shem?” “Naona leo upepo unavuma
visivyo.” Akaongea akimtizama Jack, Jack wala hakumwangalia. “Eti Jack?” Jack
akamtizama bila kuongea neno. Emma akaanza kucheka. “Si umeona mwenyewe?” Akamuuliza
Emma. Jack kimya akaendelea kunywa chai. “Mimi naona kweli ukapumzike Shem
wangu. Ukitoka hapa, gari yako isisimame sehemu. Moja kwa moja nyumbani. Zibakie
zilezile bia mbili tu.” Pam akazidi kucheka. “Hata deni langu nisiende kudai
baa?” “Kwani leo ulipoenda hawakukulipa?” “Wameniweka hapo, ndio ikabidi
niagize hizo mbili tu.” Jack akamtizama. Maana alimdanganya kuwa hakwenda kunywea
baa. Alimtuma mtu. “Ndio nataka nipitie hapo tena, nione kama watanilipa.” Emma
akazidi kucheka. “Sasa mimi naona kwa leo, acha tu. Pita tena kesho.” “Eti eeh?”
Akauliza tena Pam huku akisimama. Akateuka kwa sauti mpaka Jack akamtizama.
“Sabrina huyo! Ametulisha kupita kiasi.” Pam akavuta kiti nyuma.
Alikuwa dada mrefu. Mwenye mwili
uliojaa. Si mwembamba hata. Mnene aliyejazia vizuri. Umbile zuri. Mweupeee! Mpaka
ngozi ya kichwa ilikuwa nyeupe haswa. Ukweli kwa kumwangalia, alivutia haswa. “Nashauri
uwe mwangalifu huko barabarani.” “Sijalewa Jack na wewe, acha wasiwasi! Au
unirudishe nyumbani?” “Unakumbuka leo ni jumatatu, Pam?” “Jack naye kwa
maadili! Hivi Sabrina anajua kama unataka kuwa mbunge wetu?” Akauliza Pam na
kuendelea. “Mimi nishamwambia ni biashara haramu ya kufilisiana. Siasa ni
mchezo mchafu, wenzie mpaka wanajiua! Wanawekeza mipesa yote kwenye kampeni, wakati
mshindi alishajulikana tokea mwanzo. Unapoteza pesa, halafu kushinda pia
hushindi!” Sabrina akajua hapo hawataelewana na Jack.
Akakumbuka jinsi alivyomuuliza akiwa
Moshi juu ya yeye na siasa. Akakumbuka jinsi alivyofurahia jibu lake. Akajua
mpenzi wake ndiye anayemkatisha tamaa. “Si umefika kwenye huu mji Sabrina? Sasa
utapata habari zake. Yupo kijana mmoja, wala si mtu mzima. Kijana wa makamu tu,
kwa miaka yote yeye ndio mbunge hapa. Hili jimbo la chama pinzani. Hakuna jinsi
chama tawala wakawatoa. Wamejaribu miaka na miaka, chama tawala wameshindwa.
Sasa eti huyu Jack ndio anakuja na sera za chama tawala hapa! Nani atamsikiliza
kama sio kujidhalilisha tu? Yeye baa haendi. Mwenzie akija hapa, anaanzia baa.
Anatunywesha usiku kucha. Sasa huyo hutampa kura kweli?” Sabrina kimya.
“Jamani mimi nina mtihani kesho. Mkishamaliza kula, nitakuja kuosha vyombo. Acha nikajisomee.” Emma akaaga kwa haraka pale tu alipopata upenyo. “Wewe soma tu Emma. Mimi nimetoka kulala. Nitaosha hivi vyombo nakusafisha hapa.” “Udumu Sabrina. Kesho nitakuletea zawadi.” “Na ulete kweli sio umdanganye.” “Kaka bwana! Ungenyamaza pengine Sabrina angekataa.” Wakacheka. “Kumbe ulikuwa ukinidanganya?” “Sio kudanganya, kujaribisha tu!” Wakacheka kidogo, Pam alipoona hakuna uungwaji mkono wa hoja yake, akaondoka bila hata kuaga tena.
Nyumba Huanzwa
Kwa Msingi Imara.
S |
abrina
akasafisha pale, akamuona Jack amebaki palepale mezani na kikombe chake cha
chai. Akajua maneno ya Pam yamemuingia. Akamkumbuka Lela na Tino. Alipomaliza usafi
akaenda kukaa pembeni yake Jack. Akamvuta kumgeuzia kwake, akamshika mikono
yote miwili. “Niangalie nikukumbushe kitu.” Jack akakunja uso. “Tulianza chuo
mwaka mmoja. Ila mimi nikakuacha chuoni. Unakumbuka shida kubwa waliyokuwa nayo
wanafunzi waliokuwa wakitegemea mikopo?” “Nakumbuka.” Jack akajibu.
“Yule waziri wa fedha tuliyemkuta
chuoni alikuwa akiwasumbua kwa makusudi tu kuwapa pesa zao. Wasichana wengine
walikuwa wakilalamika, hawapi pesa zao mpaka alale nao. Unakumbuka?” Jack
akabaki ametulia. “Unakumbuka nani alifanya yale mapinduzi?” Jack akacheka
kidogo. “Uliandika historia ya ajabu sana pale chuoni, Jack. Ukiwa mgeni kabisa
ukabadili mambo. Ukaingia kwenye uongozi uliokuwa ukisifika kwa ubabe pale.
Kuanzia raisi aliyekuwepo wakati ule madarakani, mpaka mawaziri wake, wewe
mwaka wa kwanza, ukaleta mapinduzi ya ajabu sana, kila mtu akawa akikusifia na
kuimba sifa zak...” “Kasoro wewe, Brina!” Jack akamkatisha. Sabrina akacheka.
“Acha kunitoa kwenye pointi ya maana. Na
achana na Sabrina, mimi mwenyewe simuelewi. Kwanza nimemchukia.” Jack akacheka.
“Turudi kwenye kampeni za pale chuoni. Yule raisi alishakuwa na mtu wake au mtu
wao, ambaye walitaka yeye ndio aje kuwa raisi. Unakumbuka?” “Nakumbuka na ule
ugumu wa kampeni pale.” “Sawa sawa. Sababu ya rusha. Lakini unakumbuka jinsi
ulivyofanya kampeni zako kilaini bila kuhonga, na ukashinda kwa kishindo mpaka
mkuu wa chuo akaja kukupongeza mbele ya chuo, akasema hajawahi kuona raisi
aliyeshinda kwa kura nyingi kwa kiasi hicho pale chuoni, wewe umeweka historia?
Unakumbuka lakini?” “Nilijua hukuwa hata ukisikiliza Sabrina! Muda wote ulikuwa
umeinamia simu yako!” Sabrina akashangaa sana.
“Jack! Kwenye ukumbi ule! Ulinionaje
mimi siku ile, wakati nilikuwa nimekaa karibu na mwisho kabisa, tena kule juu
kabisa!?” “Ilikuwa lazima kabla sijakaribishwa kuzungumza na wanafunzi,
nikutafute nijue kama upo kwenye huo mkutano, Sabrina. Sijui ni kwa nini,
lakini nilikuwa nikitamani hata kukuona ukisikiliza! Lakini hata makofi ulikuwa
hupigi! Kama niliyekuwa nikiongea pumba tu, wakati wengine walikuwa
wakinishangilia na kunisifia kweli!” Sabrina akashangaa sana.
“Sio kwa kukudharau Jack! Nilikuona
unauungwaji mkono mkubwa sana, sikujua hata kama unajua kama nipo! Nahisi hata
kukujibu vibaya siku ile pale kantini, ni kwa kuwa nilipaniki. Sikukutegemea.
Na nikwambie ukweli, siku ile ilikuwa mbaya sana. Natamani ingekuwa wakati
mwingine. Emma alikuwa amenikorofisha usiku uliopita. Sikulala. Na kesho yake nikashindwa
kuingia vipindi vya asubuhi maana nilipitiwa na usingizi mida ya saa 12 asubuhi,
kwa kulia na mawazo. Niliamka nikiwa nahasira, ndipo tukakutana pale kantini
nikiwa natafuta chakula, na hasira, huku bado nina usingizi. Nahisi hasira kwa
Emma, nikakumalizia wewe Jack. Najua sikuwahi kukuomba msamaha kwa aibu, lakini
naomba unisamehe. Nilikuwa nikikufuatilia sana tu.” Jack akacheka kwa
kuridhika.
“Haya nimesamehe.” “Kwani bado ulikuwa
umeumia!?” “Sana Sabrina! Kwanza sikutegemea. Kumbuka wakati ule ndio nilikuwa
gumzo pale chuoni! Wasichana walikuwa wana..” “Kupigania.” Akamalizia Sabrina
na kucheka. “Sio kupigana bwana.” “We Jack! Unakumbuka wale wasichana wa Certificate
walipigana wakisema mmoja alimwambia mwenzie anakuja kukutongoza, akasikia yeye
ndio akaja akakuwahi?” Jack akaanza kucheka. “Usicheke. Si ni kweli?” “Walikuwa
watoto wale.” “Na wale wasichana wa masoko? Wauza sura?” Jack akazidi kucheka.
“Umekumbuka eeh?” “Sasa ndio hayo yakawa yananishangaza Brina! Sikuwa na msichana
pale chuoni. Eti nikaonyesha nia kwako, na wewe ukanitolea nje kwa dharau vile!
Hakika sikuamini!” Sabrina akafikiria kwa kutulia kama anayejaribu kuvuta
kumbukumbu, akakumbuka aibu aliomsababishia Jack na kuumia zaidi.
“Daah! Nisamehe Jack. Najua ingekuwa
mtu mwingine na niliyokufanyia, asingeweza hata kunihifadhi hivi! Nisamehe tu,
na endelea kunivumilia. Lakini nakuhakikishia nimejifunza Jack. Na ninaona ndio
maana Mungu amenipa na huyu mtoto ili nitulie.” “Mtoto ni baraka Sabrina, sio
adhabu ili utulie. Na wewe sio kwamba hukutulia. Ni hukubahatika kupata mtu
ambaye amekuthamini. Nahisi ni kwa kuwa hawajui uthamani wako.” Sabrina
akamwangalia, akainama. Akataka kupotelea kwenye mawazo yake akawa kama
amekumbuka kitu cha msingi zaidi ya kujihuzunisha mawazoni.
“Nilichotaka kukukumbusha Jack, ni
hiki alichokuwa akikizungumza mpenzi wako leo, Pam. Hakina tofauti na kile
ulichopitia chuoni. Mazingira ni yaleyale, tabia za viongozi wa hapa au
wananchi wa hapa ni vilevile kama chuoni.” “Lakini wakati mwingine najikatisha
tamaa Sabrina! Najiambia kule ilikuwa chuo, sio huku uraiani!” “Hata kidogo
Jack. Unajuaje kama Mungu alikuwa akikuandaa kwa ajili ya nyadhifa za juu
zaidi?” Akajiweka sawa. “Ulikuwa mwaminifu kwa kidogo Jack. Kwa nini usimdai
Mungu kwa hilo ili akuaminishe kwa kikubwa?” Jack akamtizama kwa macho
yaliyoanza kupata tumaini.
“Wakati
nipo hapo jikoni nasafisha, nikakumbuka jinsi ulivyoanza chuoni, kidogo tu. Kwa
ujasiri kuhakikisha watu wa mikopo wanapata pesa yao kwa haraka na kihalali
bila hongo. Ulihangaika wewe mwenyewe, unakwaenda mpaka bodi ya mikopo Dar.
Ukajua tarahe na muda ambao pesa zinatolewa. Ukamuomba mkuu wa chuo dhamana
yakuongozana na waziri wa fedha na kumsaidia majukumu hayo ili kuhakikisha
wanachuo wanapata pesa yao kwa wakati.” “Unajua niliomba kikao na mkuu wa chuo
pamoja na Dean of students?” “Nilisikia. Nikasikia mpaka akaitwa
waziri wa fedha kwenye kikao. Akataka kupinga, akaitwa na raisi pamoja na
makamu wake, ukajenga hoja mpaka ukapitisha hoja zako zote, mkuu wa chuo
akaamuru kuwa kuanzia siku hiyo utaratibu wako uliopendekeza utafuatwa.
Unakumbuka furaha na shukurani za wanachuo waliokuwa wakifuatilia mikopo?” Jack
akacheka.
“Sasa nani anaweza kufanya hayo kama
siye mtu aliyeumbwa kutawala? Wewe umeletwa hapa duniani kutawala Jack.
Nikipaji chako. Na kwa kuwa Mungu amekupa huo uwezo, akaweka ndani yako,
hutapata amani mpaka utimize hilo.” Sabrina akainua ujasiri ndani ya Jack.
“Tafadhali usije kujisahau wewe ni nani, Jack. Uwezo wako mkubwa wakufanya
mambo na shule uliyopitishwa na Mungu pale chuoni. Usisahau sababu ya kukatishwa
tamaa na maneno ya watu wasiokujua na kuelewa uwezo wako. Fanya mambo kisha
waje waone, sio ukubaliane na vitisho vyao.” Akamuona Jack anavuta pumzi kwa
nguvu kama aliyesafisha kifua.
“Nashukuru Sabrina. Kumbe ndio maana
moyo wangu ulikuwa ukitamani sana uje huku!” Sabrina akacheka. “Nina wazo
Jack.” “Niambie, nakusikiliza.” “Kwa
sasa hapa kwenye hili jimbo si yupo mbunge wa chama pinzani?” “Tena amekaa hapa
muda! Na wala si kijana kama anavyosema Pam, ni mtu mzima tu, sema anapenda kujiweka
kama kijana.” “Sawa. Hilo wala si tatizo. Naomba wewe anza kama ulivyofanya
chuoni.” “Nifanye nini sasa? Maana mimi mwenyekiti tu wa vijana wa chama chetu
hapa Singida. Nitafanya nini Brina?” “Njoo hapa sebuleni kwenye makochi. Mgongo
umeanza kuuma kwenye hicho kiti.” “Pole.” Wakahamia sebuleni.
“Ehe!” Jack akataka aendelee. “Lazima kubadili
hiyo ya mwenyekiti wa vijana tu. Wote tunajua wewe ni zaidi ya hiyo ‘tu’.
Unaweza ukafanya mambo mengi sana kwenye huu mji, kupanua hiyo ‘tu’. Kwa
kuwa kwanza uwezo unao, wewe kama Jackson Msindai. Mzawa wa hapahapa Singida
huko vijiji sijui vya wapi sijui!” Jack akacheka. “Isanzu.” “Sasa! Hapa kwenu
Jack. Upo viwanja vya nyumbani. Unayo sababu yakutaka vitu vizuri vitokee
nyumbani. Kwa hiyo sababu ipo, nia unayo. Sasa nini chakukushinda?” Akamuona
amefunguka uso.
“Nipe wazo nianzie wapi?” Jack akaomba ushauri lakini akiwa
amehamasika. “Cha kwanza, si mnalo jengo la chama hapa?” “Kubwa tu, sema halipo
vizuri.” “Hilo hilo Jack. Omba utawala kuwa ukilitumia. Wewe kama kiongozi wa
vijana hapa, lazima ulete mabadiliko. Omba wafadhili waje wafundishe ujuzi
tofautitofauti. Wewe ni Msindai, jina lako kubwa sana hapa nchini. Umetoka
kwenye familia inayojielewa na ni wa tawala. Wapo watu wengi tu wangependa kuja
kutoa mafunzo mafupi mafupi kwa vijana wa hapa. Iwe kwa kupenda sifa au msaada
kweli. Makanisa na taasisi za watu binafsi. Sijui vitengo vya madawa ya
kulevya. Waombe waje wawe wanatoa mafunzo kwa vijana. Badala yakunywesha watu
pombe, tufanye kampeni ya kukusanya pesa. Tufungue mradi mkubwa pale, vijana wa
chama waache kulalamika njaa, tuwaajiri palepale. Wanajiingizia pesa, na mfuko
wa chama unaingiza pesa.” “Yes!” Jack akashangilia sana.
“Sabrina nimekukubali.” Sabrina
akaanza kucheka. “Kuna watu wanakodisha mashamba. Kodisha wewe kwa jina la
chama. Waambie vijana walime huko. Haya, tumia kujulikana kwako vizuri. Itisha
au tufanye harambee, watanzania hawahawa, wanazo pesa Jack. Tufungue miradi ya
visima. Huku kunasifika kwa shida ya maji. Kingine, tuandae tamasha kwenye
hoteli nzuri tu. Anza kazi yakuandikia barua viongozi wa nchi. Muombe hata
raisi aje kuhudhuria hilo tamasha la vijana. Wafanye maonyesho, kisha tuombe
hiyo hela. Uone kama hutaleta mabadiliko hapa Singida, kisha nchini.” Jack
akapiga magoti mbele ya Sabrina, akamlalia magotini.
Sabrina akampapasa kichwani taratibu. Jack
akatulia kwa muda akisikilizia mikono ya Sabrina kichwani mwake, kisha akamwangalia.
“Nakushukuru sana Sabrina. Asante kwa mawazo mazuri na mazito. Tunaanza
kuyafanyia kazi haraka hata kabla ya uchaguzi kukaribia. Wewe utakuwa msaidizi
wangu.” “Sina hata kadi ya chama mwenzio!” Wakacheka. “Nakupa usiku huuhuu.”
Jack akasimama kwa haraka kuelekea chumbani. Akatoka na kadi moja ya chama.
Sabrina akacheka. “Kweli wewe mwenyekiti! Unatunza kadi za chama mpaka
nyumbani!” “Jaza, weka saini kabisa.” Sabrina akawa anajaza, Jack akarudi tena
chumbani kwake, akatoka na laptop.
“Umechoka sana au tunaweza kuandika
kidogo?” Sabrina akamshangaa Jack. “Mpaka umenifurahisha Jack. Unafanyia kazi usiku
huu!” “Na kesho nikitoka kazini, nakuja kukuchukua nikupeleke ukapaone pale
kwenye kituo cha chama. Hakuna hata anayepajali wanasema jengo limekaa kushoto,
tena mbali na mjini! Vijana huwa wanakaa tu nje. Huwa nakwenda kukaa nao na
kuzungumza tu. Hamna chamaana.” “Tena kumbe unayo mahusiano nao?” “Kuna siku za
weekend huwa tunacheza soka.” Sabrina akafurahia sana. “Nilisema mimi,
umezaliwa kutawala Jack! Unao uwezo mkubwa sana.” “Nashukuru kunitia moyo na
kuniamini Sabrina. Nilikuwa nakuwa nao tu, lakini sijui jinsi ya kuwasaidia.”
Akawasha kompyuta.
“Nafikiri tuanze kufikiria biashara ya
kuweza kuwafanya wajihusishe.” “Pesa?” Akauliza Jack. “Naomba tusianze na
tatizo la pesa, tuanze na wazo kwanza. Biashara gani ya haraka kwa kipindi
hiki? Na isiwe ya mafuta. Hutaki kumuumiza Pam. Ulimkuta kwenye biashara yake,
muache hapo.” “Sawa. Hapo naona hiyo itakuwa hekima. Labda kwanza kabisa
tukifanye imara kile tulichonacho. Kwa mfano timu yetu ya mpira tuliyo nayo
tuisajili kabisa, tuipe jina halafu nitafutie mfadhili. Vijana wanacheza hao
Sabrina, ni hivyo wapo vichochoroni.” “Sawa sawa. Anza basi kuandika hilo. Hiyo
itakuwa njia nzuri sana ya kuwaweka pamoja na kuvuta wengine.” Wakaandika juu
ya timu. Jack akawa na majina ya baadhi ya matajiri wa hapo mkoani Singida,
wafanyabiashara wakubwa ambao alijua wangependa kujulikana wanagusa jamii huku
wakijitangaza.
“Na wanawake lazima kuanzisha kitu
Jack.” “Kama nini? Mimi nimekuwa karibu na vijana wa kiume zaidi.” “Mara nyingi
sisi kupika kunatukutanisha kwa haraka. Sasa tukikutana hata mara mbili au
tatu, itatusaidia kutuweka pamoja.” “Basi nikutambulishe kwa dada mmoja naye ni
kiongozi mwenzetu.” Jack akatoa wazo. “Yaani hilo litakuwa la msingi zaidi.
Ndipo nitaweza kujua kwa haraka.” “Basi nitamwambia kesho mchana aje hapa
mzungumze.” “Wazo zuri.” Wawili hao wakaandika usiku huo na kujiwekea mikakati
yao mpaka wakaridhika. Wakazima taa za hapo sebuleni na jikoni, wakaongozana upande
wa vyumbani.
“Nimekwambia
nakushukuru sanaaaaa?” Sabrina akacheka na kusimama karibu kabisa na mlango wa
chumbani kwake. “Karibu. Na nina uhakika utafanikiwa Jack, kwa kuwa wewe
hujajichagua, ni Mungu ndiye amekuchagua. Wakati wote amekuwa akisimama na wewe
kuhakikisha kusudi lake linatimia kupitia wewe.” Jack akamwangalia Sabrina kama
anayemshangaa. “Kumbe ndio maana moyo wangu ulikuwa ukikutamani sana Sabrina!
Umebeba majibu yangu mengi!” “Na mimi nimefurahi tupo wote Jack.”
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sabrina
Ametua jijini Singida na ameanzisha jambo ndani ya Moyo wa Jack, anataka kugusa
jamii. Mungu alimpa Karama ya kufufua hata vyenye muelekeo wa kufa. Safari hii
ni Jack, baada ya Tino, Emma na nyumbani kwao ambao wote walishindwa kutambua
juhudi zake na kumdharau vibaya sana.
Sasa safari
hii yupo kwa Jack Msindai wa Pam.
Itakuaje? Huku nako vitakwendaje?
Usikose
Muendelezo Kumuona Sabrina na Kwa Jack naye. Vile anavyoanziaga padogo sana,
lakini hugeuza mambo na kuwa kama Mkuyu.
Safari hii Kosa Kwa Tino, Faida Kwa Jack.
Na
Kosa kwa Pam, Uwanja wa Sabrina Kufanya yake
ambayo Mungu huweka mkono wake.
Itakaje?
0 Comments:
Post a Comment