Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 15. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 15.

Kwa furaha aliyoiweka moyoni mwake, Jack akamsogelea karibu na kumkumbatia kwamuda. Akamsikia akicheka. “Nini?” “Napenda hiyo harufu yako! Utanifanya nilale nikiwa nimesimama hapahapa!” Jack akacheka. “Halafu lile koti lako limeanza kupungua harufu bwana!” Jack akacheka sana. “Kwa hiyo hulitaki tena?” “Bado kidogo. Na ni kwa vile sina jinsi. Ningeshalifua nikurudishie.” Jack akajua ni huo ujauzito. “Nikupe nini sasa? Lipo jingine safi. Nikutolee?” “Sasa silitakuwa likinukia sabuni sio wewe!” Jack akazidi kucheka. Akavua tisheti aliyokuwa amevaa. Palepale mbele yake, akabaki na singlendi ndani. “Haya, hiyo hapo.” Akamkabidhi. Sabrina alifurahi, mpaka akamshangaza Jack. Aliinusa hiyo tisheti akiwa amefunga macho.

          “Sabrina!” “Acha nikalale. Sasa hivi hapa nitalala haraka bila shida. Hii harufu inanifanya nalala vizuri sana, sijui kwa kuwa ni wewe Jack?” “Mimi nimefanya nini!?” Akamshika mkono na kumvutia chumbani kwake. “Hujui ulichokifanya kwangu Jack. Pale uliponitoa, nilikuwa sina shida ya pesa, wala nisingekuwa na haraka yakuondoka maana yule mwenye ile sehemu alimwambia Tino, asiwe na wasiwasi naweza kuendelea tu kuishi pale. Hata hivyo kwa wakati huu hana wateja wengi wa kupahitaji pale walipokuwa wamenipa. Lakini hofu! Niliingiwa na hofu ya ajabu.” “Ulikuwa ukiogopa nyumbani?” Jack akamuuliza.

          “Kila mtu na kila kitu kwa ujumla wake. Aibu, nazungukaje na tumbo kubwa baba hajulikani? Au halina baba, baba anajua nilishaua kiumbe! Halafu nafikiri na uchungu ule wakumuuguza sana Tino, halafu kuja kunigeuka vile!” Akaongea kama ambae bado haamini alichofanyiwa na Tino. “Hivi unajua Tino aliniacha hospitalini!? Japokuwa sikuwa nikiumwa, lakini ile dawa ya usingizi na dripu mkononi, ilinifanya nionekane kama mgonjwa, Jack. Tino aliweza kuniacha, wakati mimi nilikuwa naye kila wakati, silali mchana wala usiku kwa kumuuguza! Kwanza hakuwa hata akikubali nimuache peke yake hata kwa lisaa! Nilikuwa nikimbemba kumtoa kitandani, namuingiza kwenye gari kwenda kununua vitu!” “Kwa nini sasa!?” “Alikuwa akiogopa naweza kuondoka, nisirudi tena. Anyway, vile kukwambia sitakuja huku, na bado ukanifuata na kunichukua, nahisi nafsi yangu na akili imekubali wewe ndio kimbilio langu. Sasa nikihisi uwepo wako hata kwenye nguo, nalala vizuri sana.” Jack akabaki ameinama.

          “Nenda kalale. Kesho uamke na akili safi. Ukichelewa kupata kifungua kinywa, beba.” “Naona nitafanya hivyo, ili nilale zaidi. Usiku mwema Sabrina.” “Nawewe Jack.” Jack akatoka, Sabrina akatoa nguo zote kwa haraka, akavaa ile tisheti aliyopewa na Jack, akakimbilia kitandani kulala. Ilikuwa na harufu yakutosha ya Jack, akalala kwa haraka sana.

Jumanne.

A

subuhi wakati anaenda kazini, Jack akagonga tu mara moja na kuingia chumbani kwa Sabrina akiwa na kikombe cha chai na maandazi mawili ameshika mkononi. Sabrina akacheka. “Sasa kwa nini huweki kwenye sahani?” “Nimeona aibu. Pale jikoni kusafi sana. Nikaona heri nichafue kikombe kimoja tu, ukiamka upakute vilevile pasafi.” “Mstaarabu wewe! Lakini usiwe unafanya hivyo. Mimi nipo tu nyumbani kwa sasa, sitashindwa kusafisha vyombo. Na chakula cha mchana nikufungashie?” Jack akafikiria.

          “Unaona shida kwenda na chakula?” “Hapana. Wenzangu huwa wanabeba na kupasha. Naona kama nitakuongezea usumbufu! Heri hicho chakula kibaki cha jioni.” “Hapana bwana Jack. Mimi furaha yangu nikuona unakula vizuri na unashiba, sio unaacha chakula ndani unakwenda kuteseka nje!” Jack akacheka huku akila. “Kama ndio hivyo basi nakwenda kujichukulia cha mchana nikale kazini.” “Hutaki nikusaidie?” “Ulivyojifunika vizuri hivyo! Wewe lala tu, nitafanya mwenyewe.” Sabrina akamtizama Jack kwa kumfikiria. Wanaume wawili alioishi nao walimtumia bila kuchoka wala kumfikiria. Aliwatumikia mchana na usiku. Kuwapikia na kuwafikishia chakula mpaka mikononi mwao, na bado hawakumuenzi. Jack anathamini kila kitu anachomfanyia na anamfikiria na yeye! Ikamgusa sana Sabrina.

          “Sasa unawaza nini hapo? Mimi nimekuja tuongee kabla sijaondoka.” Sabrina akacheka, Jack akakaa kabisa hapo kitandani. “Unataka kuzungumza nini?” Akauliza Sabrina akikaa na yeye vizuri. Jack akashangaa amevaa ile tisheti yake. Akacheka moyoni, lakini alifurahi sana. “Swala la simu. Tutakuwa tukiwasiliana vipi au watu watakuwa wakiwasiliana vipi na wewe? Nataka kukutambulisha kwa baadhi ya watu. Naanza ule mchakato mwenzio, silali.” Sabrina akacheka. “Safi sana. Hakuna kulala mpaka kieleweke. Nitatoka kwenda kuregista namba mpya. Naamini baadaye nitakuwa hewani. Hilo usiwe na wasiwasi, ila nikushauri kitu Jack?” Jack akakaa.

          “Nakusikiliza.” “Naomba usinielewe vibaya au ukaona navuka mipaka.” Jack akabaki akimtizama. “Najua upo kwenye mahusiano na Pam. Lakini kwa jinsi nilivyomsikia jana, yupo kwenye timu pinzani. Huyu mbunge wa hapa kwa namna fulani ni kama wanafahamiana. Na pengine wanafahamiana kwa muda mrefu. Nashauri mipango yote ya nini tufanye, ibaki kwako tu kwa sasa, ili kwanza usiuze mipango yako nje. Huwezi jua akiwa na wenzake huko nje atazungumza nini!” “Zaidi huko baa ambako wanakutana.” Jack akaongeza akionekana kama anakerwa.

          “Hilo moja, la pili acha watu waone tu vitu vizuri vinatokea. Utashangaa ile imani utakayojenga hata kwa Pam mwenyewe. Kuna watu ukiwaambia mambo makubwa mapema, wanaweza kukukatisha tamaa kwa sababu ya kutokukujua, au hofu zao wenyewe, au hata wivu tu. Lakini ukifanya jambo kimyakimya, halafu likaja kutoa matunda mazuri, unajikuta unavuta watu wengi kwako kuliko kuwapoteza mwanzoni kabisa. Kingine, usiposema mipango yote hata kwa wenzio huko chamani, utajipunguzia upinzani usio na sababu. Tutembee hatua kwa hatua bila haraka. Ibaki sisi tu tukitia tiki mpango mmoja hadi mwingine, huku tukitathimini matokeo.” Jack akamwangalia Sabrina kama asiyeamini kama ni yeye.

          “Sisi tu ndio tujue kama tumefikia lengo. Wapi tumekosea, nini chakuongeza. Kwa muda gani na kwa umakini gani. Nani aingie kwenye lipi na kwa kina gani. Sijui kama umenielewa?” “Sana, Sabrina wangu. Nakushukuru mama. Naona nazidi kukuhitaji.” “Chamwisho.” Wakacheka. “Naomba kila mpango tuuwekee muda. Mipango isiyo na muda wa kuutendea kazi, huwa inabaki kuwa mipango tu. Utashangaa siku zinazidi kwenda, hakuna kinachofanyika.” Jack akasimama na kumbusu shavuni.

          “Wewe unanifaa Sabrina. Asante mama.” Sabrina akafurahia busu la shavuni asubuhi hiyo. “Haya mabusu yakiendelea hivi, nahisi nitakuwa nikifikiria zaidi.” Wakacheka. “Naomba ukiamka baadaye, ushugulikie swala la simu kisha nipigie, halafu nitakutumia kila kitu tulichoandika jana, unisaidie kuanza kupanga muda.” “Sawa. Unafikiri muda gani huyo msichana wa chama atakuja hapa?” “Ni dada mkubwa kidogo. Ukinipigia, nitakujulisha.” Jack akaaga na kutoka.

           Sabrina alirudi kulala. Kama kwenye mida ya saa nne hivi akaamka tena njaa ikumuuma. Akaamua aoge ndipo akale. Akaoga vizuri, akajitengeneza na nywele alizokuwa amesukwa Dar, akajipenda. Mbele ya kioo, macho yakatua tumboni kwake. Akajishika tumbo lake, akapotelea mawazoni. Tumbo hilo dogo kabisa kama mgongo, lilishaanza kutokea mpaka analiona kwa nje. Mwezi wa kwanza na wa pili kwenda watatu, bado lilikuwa dogo kabisa. Muda ulivyozidi kusogea, akaona ukuaji pia unaongezeka. Akajishika tena, akahesabu, akagundua anasogea mwenzi wa nne. “Ni haki yake kukua.” Akajiambia na kuamua kutoka. 

Pam tena.

A

kashituka sana alipofika jikoni na kumkuta Pam. “Umenishitua!” Sabrina akajishika kifuani. “Nilipiga hodi, labda hukusikia.” Sabrina akajua amedanganya. Alikuwa chumbani muda wote na hapo sio pakubwa kiasi hicho kushindwa kusikia hodi. “Kwema lakini? Naona upo jikoni, lakini huli.” “Kwani siruhusiwi kuwepo jikoni?” Sabrina akamtizama. “Nini?” “Swali dogo tu na la kawaida Pam. Mbona unapaniki? Kaa tule.” Sabrina akampita. “Unanjaa ya chakula cha mchana au kifungua kinywa?” Sabrina akamuuliza. “Mimi nishapata supu ya asubuhi. Nimekuja hapa tuzungumze.” Sabrina akamtizama, kisha akaendelea na alichokuwa akifanya.

          “Mbona umenitizama halafu ukanipuuza?” Sabrina akacheka. “We Pam! Acha kujiudhi asubuhi hii. Kaa tuzungumze. Mwenzio njaa inauma.” Akamtizama tena vizuri akagundua hayupo sawa. “Mbona kama umekuja na jazba? Kwema kipenzi cha Jackson Msindai?” “Naona huyo Jack anataka kunichanganya mimi.” Sabrina akacheka. “Unataka kuzungumza nini na mimi?” Akaona yake na ya Jack hayamuhusu. “Naona nikuajiri tu pale kwenye biashara yangu.” Sabrina akabaki akimtizama. “Ndio nakupa kazi Sabrina, ili utoke hapa ndani. Changamka! Wewe vipi?” Sabrina akatoa chakula alichokuwa akipasha moto kwenye microwave.

          “Njoo tuzungumze hapa wakati nakula.” Wakahamia mezani. “Nakusikiliza, au na wewe umezira kama Jack?” Sabrina akajua Jack amemkatalia asimuajiri tena. “Mimi niliheshimu sana ile sababu yako ya mwanzoni kabisa Pam. Uliongea kama mfanyabiashara haswa!” “Eti eeh?” “Sana. Na katika hilo nikakuheshimu zaidi. Sasa kwa nini tena unarudi kinyumenyume?” Pam akajichekesha. “Naona Jack ni kama alichukia juu ya hilo. Leo asubuhi naona nampigia, hapokei. Nikamfuata mpaka kazini kwake, wala hakuwa busy! Namuuliza mbona hapokei simu zangu, ananiambia alipanga kunirudishia baadaye.” Sabrina akaendelea kula kama hamsikii.

          “Baadaye kwenye mazungumzo ndio nakuja kumsikia akisema eti jana nilikuja hapa nimelewa! Eti jana nilikuwa nimelewa kiasi chakushindwa kujielewa mimi?” Akamuuliza Sabrina swali, Sabrina akabaki amemkodolea macho. “Nakuuliza wewe Sabrina? Maana ameniambia nilikuja hapa nimelewa nakuanza kuzungumza mambo ya ajabu! Nilidanganya sikunywa pombe baa, sijui nilimwambia mwanzo nilimtuma kijana! Wakati hata sikusema wapi niliponywea pombe!” Sabrina akajua tayari amejichanganya.

          “Kwanza hata sikuwa nimelewa! Bia tatu ndio zakunilewesha mimi!” Sabrina kimya, akiendelea kula. “Kwanza nilikunywa na pesa yangu. Sijahongwa, jasho langu. Sasa hasira za nini?” Sabrina akamtizama na kuendelea kula. “Wewe unastarehe yako, mimi yangu na yeye hivyohivyo. Kama yeye anavyofurahia kwenye mapenzi, ndivyo...” “Woooo!” Sabrina akashituka sana. “Unavuka mipaka Pam.” “Naongea ukweli. Yeye Jack hanywi pombe. Starehe yake ni...” “Tafadhali hasira zisikufanye ukazungumza mambo ya ndani sana. Namuheshimu sana Jack. Sihitaji kujua mambo yenu ya ndani. Naomba turudi kwenye yanayotuhusu mimi na wewe. Tafadhali sana.” “Mbona sijaongea kitu cha ajabu!” Sabrina akamshangaa sana Pam.

          “Nini sasa? Mbona unashituka vitu vidogo sana? Mapenzi kitu cha kawaida sana. Nini cha ajabu? Kwani wewe hujui kama mimi na Jack tunafanya?” “Kuhusu kazi, nashukuru kwa kutaka kunipa kazi, lakini nafikiri ulikuwa sahihi tokea mwanzo. Nilikuelewa vizuri sana. Nafikiri tubaki kuwa na urafiki tu, tusiharibu kwa shida ya muda mfupi. Mimi nitapata tu kazi sehemu ingine.” “Sasa na mimba hiyo nani atakuajiri?” Sabrina alishituka, akabaki akimtizama.

          “Mimi nakuhurumia wewe mwenyewe na mtoto! Unahitaji kujipanga haswa mama. Jukumu ulilochukua lakuzaa wakati maisha yenyewe yanapiga chenga! Huna hata pakuweka kichwa chako wewe mwenyewe, na kazi huna! Unafikiri utamuweka wapi huyo mtoto? Utamtegemea Jack mpaka lini? Unapopewa msaada, pokea ili ujikwamue na wewe. Utakuwa mtu wakuachiwa hivi vipesa mbuzi kila siku, mpaka lini?” Akamuonyesha pesa na kikaratasi alichokuwa ameshika mkononi. Hata Sabrina hakuwa ameelewa.

          “Mtegemea cha ndugu, hufa masikini.” “Mbona kama unalazimishia huo msaada kwangu?” Sabrina akamuuliza akiwa ameumia sana. “Nataka kukusaidia.” “Mimi sio mtoto mdogo Pam. Nishaishi na watu wa aina yako wengi tu, najua huwa wanayo hila nyuma yake. Sasa wewe nia yako ni nini hapa? Mimi sitegeki kipuuzi.” “Mimi sijakuona mtoto. Mtoto anaweza kubeba mimba?” Pam akaongea kwa kupaniki. “Mimi nataka kukusaidia tu, naona mnaniziria!” “Unisaidie kwani nimekuomba msaada? Hunijui sikujui, unataka kunisaidia kivipi?” “Mimi nakufikiria wewe. Utakaa hapa mpaka lini?” “Inakuhusu nini wewe?” Sabrina akambadilikia, akawa ameshapandisha hasira.

          “Nakuuliza, inakuhusu nini Pam? Unafikiri Jack ameniokota mimi? Acha kujidai kama umechanganyikiwa! Kama umezoea kuropoka huko, sio kwangu. Shika adabu yako. Na maisha yangu na ya mtoto wangu hayakuhusu. Usitake kunichanganya.” Sabrina na wembamba wake akamsimamia Pam na umbile lake, akanywea. “Kwanza potea.” “Hapa ni nyumbani kwa mpenzi wangu. Huwezi kunifukuza.” “Sasa unamuona Jack hapa? Hayupo Jack wala Emma. Usitake kuniharibia siku kwa maneno yako yakipuuzi.”  Sabrina akasimama na kuondoka hapo. Akachukua pochi yake na kutoka kabisa hapo ndani. Alikuwa na hasira, karibu arukwe na akili. Akatoka hapo asijue hata aendapo.

Kwa Jack.

H

uku nyuma Pam akapaniki. Akampigia simu Jack. Akaanza kwa kulia sana kuwa Sabrina amemtukana. Ubaya ni kuwa Pam ni mropokaji na ni muongo wakupitiliza. Jack alimjua hivyo. Akaongopa hili na lile, Jack akiwa ametulia tuli akijua atajua tu ukweli kilichotokea kati yao, kutoka kwa Pam yeye mwenyewe. Pamela akaongea yote mpaka akajikuta anaongea na ya ukweli. “Umefanya nini Pam!? Nilikwambia nini hukusu kufika hapo nyumbani na kuanza kuongea bila kufikiria?” Jack akamuuliza taratibu tu. “Mimi nilikuja kuzungumza naye maswala ya biashara, yeye ndio amepaniki!” Akabadilika tena. “Si umetoka kuniambia wewe mwenyewe kuwa ulikwenda kumpa kazi, akakataa akisema uamuzi wako wa mwanzoni ni sahihi?” Jack akamuuliza taratibu tu.

          “Sio hivyo moja kwa moja!” “Nilitoka kukwambia nini juu ya kumpa Sabrina kazi? Si nilikwambia umuache? Kwa nini ulimfuata nyumbani?” “Hapa ni kwako Jack. Na mimi ni mpenzi wako. Nipo huru kuja muda na wakati wowote. Sabrina sio wakunizuia au tangia lini imekuwa nahitaji sababu ya kufika kwako?” Pam akambadilikia na Jack. “Sabrina yuko wapi?” Jack akauliza akiwa ametulia tu. “Kwani mimi ni mlinzi wake?”  Akauliza kwa kiburi na kukata simu. Kimeshaumana kwa wanawake hao wawili, Jack katikati yao.

Nyongo Mkalia Ini.

S

abrina hakuwa na simu. Jack akabaki ameinama akifikiria. Tayari walikuwa na mipango na Sabrina ambayo hakutaka ivunjike. Akaaga pale ofisini, akatoka kurudi nyumbani kwake. Akakuta kile kikaratasi alichokuwa amemuachia Sabrina cha maelezo na pesa ya matumizi kimetupwa sakafuni, karibu na meza ya chakula. Akajua Pam ndio amechukua hiyo pesa. Akaingia chumbani kwa Sabrina, hakuwepo ila mizigo yake ilikuwepo. Hilo likamfariji. Akatoka nje huku akimuita, hakuwepo. Akabaki amekaa pale sebuleni akili ikishindwa kufanya kazi. Ilikuwa saa 8 mchana, mwajiriwa huyo wa serikali, amekaa nyumbani na si kazini. Akakaa hapo mpaka saa 12:30 jioni ndipo akamuona Sabrina anaingia. Akabaki kimya akimwangalia.

          Sabrina akaenda kukaa pembeni yake. “Nimepata sehemu ya kuishi Jack. Kwa sasa nimepata hoteli. Bei yake ni nafuu. Nitakuwa hapo mpaka nitakapokamilisha vitu vya ndani.” Jack akabaki akimtizama. “Nimenunua line. Simu ipo hewani. Tutakuwa tukiwasiliana na naomba tuendelee na mipango yetu kama kawaida. Nafikiri kesho ni siku nzuri kunikutanisha na huyo dada. Tutapanga vizuri. Kuna mambo nimeyafikiria leo, naona yataendana na haya mazingira ya hapa Singida. Nitakushirikisha kwa karibu nikishazungumza na huyo kiongozi mwenzako utakayenikutanisha naye, na kumsikiliza.” Kimya, Jack akimwangalia. Mwishoe Sabrina akainama akifikicha mikono. Pakatulia kimya. Mwishoe Sabrina akaona aondoke pale. Akanyanyuka kurudi chumbani kwake kufungasha.

          “Hivi unajua ni kwa muda gani nimekuwa nikikusubiri Sabrina?” Sabrina akageuka. Jack alikuwa amesimama mlangoni. “Eti Sabrina?” “Lakini mimi nipo hapa kwa ajili yako Jack! Na nitasimama na wewe mpaka kieleweke. Ila naomba fikiria Jack, haya si mazingira ya mimi kuwepo na hii hali yangu. Sitaki tuharibu mahusiano kati yako na Pam, pia kati yangu na Pam. Maadamu unajua mimi ni wako tu, na hutanipoteza, acha nikakae kwangu tu. Nishateseka na kuhangaika na haya maisha, wewe ni shahidi. Sijapumzika hata mara moja! Nimechoka Jack, nataka kupumzika. Angalau mara moja tu maishani. Naomba uwe na mimi katika hili. Nisaidie nipumzike.” Jack akatulia.

          “Siondoki kwa kuwa namuogopa Pam, au nitamshindwa kummudu! Namuweza sana tu. Lakini sitaki fujo. Naomba nipumzike Jack. Na najua wewe unaweza kunipa hiyo nafasi. Ukiniruhusu nikaondoka hapa kwa amani, ujue utanipa utulivu mimi, Pam, wewe mwenyewe na Emma pia. Hutaharibu jina lako hapa mjini. Utabaki ukiheshimika. Ila nikiwepo mimi hapa, tutaharibu sifa yako na hutakuwa na utulivu wa kufikiria. Utakuwa mtu wa kupigiwa simu juu ya mashitaka yangu kila wakati. Ila kukiwa na amani, tutafanya mambo yetu kwa utulivu.” Kidogo Jack akatulia.

          “Nilifurahia jinsi tulivyokuwa tukiishi hapa, Brina! Naona kama napokonywa tonge mdomoni!” “Naumia Jack, naumia sana. Nina majuto ambayo sijui nikwambie nini! Natamani kurudisha muda nyuma lakini najua nimechelewa Jack. Nimechelewa. Hapa navuna matunda ya maamuzi yangu. Acha nisikuharibie na wewe, wote tukakosa kimbilio. Naomba nisaidie usafiri wa mpaka hotelini.” Wakaanza kusaidiana tena kuweka vitu kwenye gari, mpaka wakamaliza.

          Wakaondoka pamoja. Akampeleka mpaka hotelini, akashuka garini ili kumsaidia kushusha mizigo yake yote na kuingiza kwenye chumba alicho kodi. Akafanya hilo zoezi mpaka akamaliza kuingiza vitu vyote hapo chumbani, kisha akakaa kitandani na kuinama. Sabrina akaenda kukaa pembeni yake, akamuegemea. “Tutakuwa sawa Jack. Na hapa sio mbali na mjini. Tunaweza kuonana hata kila siku.” “Daaah!”  Jack akasikika akilalamika. Wakatulia hapo kwa muda. Kimya kila mtu akiwaza lake. Sabrina akamuwekea mkono mgongoni akaanza kumkunakuna mgongoni taratibu kama kumtuliza. Mwishoe Jack akamwangalia. Wakabaki wakiangaliana huku Sabrina akiwa amemlalia begani.

          “Mtoto anazidi kukua Jack. Nafikiria kuanza kuulizia hospitali nzuri, nianze kliniki.” “Mimi najua kila eneo hapa mjini. Kwa nini huniulizi mimi!?” Sabrina akacheka. “Basi naanza upya. Naomba unishauri wapi nianze kliniki.” “Unataka kuanza lini?” “Naona hili juma lipite kwanza, lijalo.” “Sawa.” Jack akarudi kuinama. “Unawaza nini sasa?” Jack akamwangalia na kurudi kuinama. “Nyumbani kuna chakula. Nenda ukale, upumzike. Nitakupigia kesho.” “Sawa.” Akasimama Jack, nakuondoka bila kuongeza neno.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          Akiwa njiani simu ya Pam ikaingia. Akapokea. “Vipi?” Jack akauliza taratibu tu. “Safi, nilijua utakuwa umenikasirikia.” Pam akaanza kucheka hovyo, Jack akajua ameshalewa. “Uko wapi Pam?” “Ndio nafunga hapa ofisini, nitoke.” Hapohapo Jack akabadili njia na kuelekea ilipo ofisi ya Pam ambako ndiko kwenye biashara yao. Hapakuwa mbali. “Jack?” “Nakuja hapo. Sipo mbali, ndio nakata kona.” “Lakini sasahivi mimi sipo hapo.” Jack akakanyaga breki kwa hasira. “Kwa nini udanganya bila sababu Pam!?” “Kwani mimi nimekudanganya nini sasa hivi?! Si nimekwambia ukweli kuwa sipo ofisini!? Nimetoka muda si mrefu. Tena nilifikiria kuja kukuona nyumbani. Au umekasirika?” Jack akavuta pumzi kwa nguvu. “Naomba kukuaga kwa sasa Pam. Tutazungumza baadaye.” “Kwa hiyo hutaki nije nyumbani, ndio umezira?” “Usiku mwema.” Jack akakata na kuamua kwenda tu pale ofisini kwenye biashara yao.

          Alimkuta mlinzi na kijana mmoja wa wale ambao huwa hapo wakisaidiana na Pam. Akakaa hapo wakazungumza kidogo. Akauliza maswali, akaona mambo sio mabaya. Akaondoka kurudi nyumbani. Hiyo ilikuwa jumanne, Sabrina alifika hapo jumamosi, lakini akaona kumeshabadilika. Hapafai tena. Akaingia na kukaa sebuleni. Akawasha tv. Emma akatoka chumbani na kumsalimia. “Vipi mtihani?” “Duuuh! Naona nisiongee kaka. Sabrina sikumkuta, yuko wapi?” “Aliondoka.” Emma akatulia kidogo kama ambaye amepata habari asizokuwa amezitegemea. Kisha akaona aulize tena. “Ameondoka ndio moja kwa moja au atarudi?” Kabla ya Jack kujibu wakasikia mlango unafunguliwa bila hodi, wakajua ni Pam tu.

          Emma akaanza kucheka. “Taratibu na mlango huo Shem, mbona rahisi tu kufungua?” Wakamsikia Pam akicheka nje. Emma akaenda kumfungulia. “Naona leo unataka tulale mlango wazi!” “Lango lenu bovu hili bwana! Mpenzi wangu yupo?” “Yupo, karibu.” Emma akampisha mlangoni. “Unajua pale nilipokwambia nafunga, nilijichanganya. Ndio Zena akanishitua sasa hivi kuwa nilijichanganya wakati nazungumza na wewe. Eti badala ya kukwambia nimeshafunga pale nimeondoka, nikakwambia ndio nafunga. Nahisi kuchoka.” Emma akacheka na kuelekea jikoni. “Nimetoka pale sasa hivi nimemkuta Jona bado yupo, na alisema ulitoka asubuhi kwenye saa tano, ukarudi kwenye mida ya saa nane. Hukukaa sana, ukaondoka.” “Naye atakuwa mbeya huyo Jona! Yeye anaangalia muda wa kila ninachofanya?” Pam akakaa.

          “Acha kuongopa bila sababu Pam! Wewe ni mtumzima na hadhi yako. Kwa nini kudanganya vitu visivyo na sababu?” “Naona wewe bado unahasira na mimi juu ya huyo Sabrina. Kama amekwambia mambo mengine, ujue amekudanganya. Na sijui nia yake nini! Mimi sikumwambia jambo baya zaidi ya kumkumbusha yeye ni mjamzito asiye na kazi anatakiwa kujifikiria.” Jack alishituka sana. “Umemwambia nini!?” “Nishakwambia. Kama na wewe huelewi basi. Mimi nampa kazi, ananiletea maringo wakati anakula na kulala hapa kwako bure tu? Atasubiri vijisenti vyakupewa mpaka lini? Siku ukiondoka bila kuacha pesa kama leo? Atafanyaje?” Pam akaanza kuongea.

          “Nilichofanya ni kumkumbusha yeye ni nani, na asijilinganishe na visichana vidogo ambavyo havina majukumu! Au asikusikilize wewe mwenye ajira yako ya maana. Atakaa hapa mpaka lini? Mwishoe atakuja kujifungulia hapahapa wakabaki yeye na mtoto wake wakikuangalia wewe kwa kila kitu! Sasa mimi namwambia ukweli, anapaniki! Najua ukweli unauma. Lakini lazima mmoja wetu amfungue macho.” Emma akatoka jikoni taratibu kwa kunyata akarudi chumbani kwake. Jack alibaki kama amepigwa ganzi, akimwangalia Pam, asiamini kama yale ndio maneno aliyompa Sabrina.

          “Sasa unashangaa nini!? Ni nini cha ajabu na cha uongo nilichozungumza kwake!? Kama unadhani na safari hii nimeongopa, naenda kumuita azungumze hapa mbele yako.” Pam akasimama. Akaenda kugonga chumbani kwa Sabrina kwa muda, kimya. “Sasa kama ameninyamazia,  hataki….” “Sabrina alishaondoka.” Jack akaamua kumkatisha kumpunguza maneno. Pam akarudi pale sebuleni.

          “Yaani ameondoka kabisa sababu ya mazungumzo madogo vile! Basi hana kifua na hataweza kuishi na watu.” “Naomba nyamaza Pam. Tafadhali acha kuzungumza bila kufikiria. Nyamaza kabisa.” Hapo Pam pombe ikaanza kuisha taratibu. Jack huyu hajawahi kukutana naye. Jack amemgombesha! Akashituka mpaka usoni akionyesha hakutarajia. “Unaongea na kujadili kila jambo bila kupata muda wakuchuja mambo! Kwa nini ulikuja hapa nikiwa nimekuonya kabisa usizungumze tena na Sabrina maswala ya kazi?” “Nia nikutaka kusaidia Jack!” Pam akawa mtulivu.

          “Kivipi? Ulitaka kumsaidia vipi mtu ambaye haitaji msaada wako? Sabrina hana shida Pam. Nimemtoa kwenye Villa nzuri na za kisasa kuliko hapa. Yupo hapa kiundugu tu akitaka watu. Nilimuombea kazi ili asikae mpweke, au yeye alitaka kazi ili asikae tu bure! Na haya nilikwambia Pam, lakini wewe ukaja kumvamia na maneno mengii, ukitaka afanye unavyotaka wewe wakati wewe mwenyewe hata hujui unataka nini?” “Unanitusi Jack!” “Kivipi na wakati wewe mwenyewe ndiye uliyetuambia sisi hatujui biashara, wewe mjua biashara huchanganyi biashara na mahusiano na ndio maana umefanikiwa sana. Au umesahau?” Kimya.

“Sabrina akasema amekuelewa kabisa. Leo unarudi tena kumpa kazi ileile uliyomkatalia kwa sababu za kimsingi, tena nikiwa nimekukataza, halafu unampa maneno makali! Ulitaka nini kitokee Pam?” “Naomba nisamehe Jack.” Jack akasimama na kuondoka pale, alipokuwa amekaa na Pam.

          Pam akamfuata chumbani. “Nataka kupumzika Pam. Na wewe umekuwa ukinywa nafikiri karibu siku nzima. Naomba uondoke, ukapumzike nyumbani kwako, tutazungumza kesho. Tafadhali sana.” “Lakini mimi sijalewa Jack! Nimekuja tulale leo.” “Hapana, asante. Naomba urudi kesho ukiwa hujakunywa pombe kabisa. Kama hutaweza kesho, haina haraka. Utakapokuwa tayari kuweka bia chini ili uje tuzungumze, ni sawa. Naomba unipishe nipumzike.” Pam akamwangalia na kutoka. 

 Kwa Pam!

W

akati wote msamaha na kumbembeleza Jack kwa kumpa penzi huwa vinasaidia. Safari hii alimfukuza bila hata kuuma maneno! Pam alitoka hapo akiwa na mshituko, pombe yote ikamwisha kwa hofu. Alipofika tu garini akampigia simu Ibra. Rafiki kipenzi wa Jack tokea chuoni. Kama kawaida yake Pam akaanza kwa uongo mwingi. Akaongea mengi asiseme ukweli, Ibra akimsikiliza usiku huo. “Naona gafla amenibadilikia!” “Hapana Pam. Mimi namfahamu Jack, sio kigeugeu. Lazima ipo sababu, tena kubwa na ya msingi. Sifa kubwa na ya kwanza kwa Jack ni mvumilivu wa kupitiliza. Wewe si nilikwambia mbele yake tulikuwa tukimwambia hana moyo?” “Nakumbuka, lakini mimi nakuhakikishia Ibra hakuna kitu kibaya nilichofanya cha ajabu. Labda iwe ushauri alionipa ambao sikuutendea kazi. Tena kwa faida yao wenyewe.” Pam akaanza kwa kujirudi sasa.

          “Ukisema ‘yao wenyewe’, unamaanisha na nani?” Ibra akauliza taratibu tu. “Si unakumbuka biashara ambayo tunafanya naye?” “Hiyo ya mafuta ya alizeti?” “Ndiyo. Ile niliyokuwa nikifanya mimi, yeye akaongeza tu mtaji. Sasa akamuombea Brina kazi hapo. Mimi nikamwambia...” “Subiri kwanza Pam, ukisema Brina, unamaanisha Sabrina!?” Ibra akauliza asiamini alichosikia. “Ndiyo Sabrina, lakini Jack mwenyewe anamuita Brina.” Ibra akajua tayari. “Sabrina yupo Singida!?” “Alikwenda kumtembelea Moshi siku ya ijumaa, akarudi naye jumamosi. Akasema..” Pam akaongea mengi sana. Akijichanganya kwa hili na lile lakini Ibra akajua ameshampoteza Jack.

          Akaongea sana, Ibra akaona hatalala na kesho yake alikuwa na majukumu ya alfajiri na mapema. “Nisikilize Pam. Umeshasikia ule usemi wa kila mwanadamu anao udhaifu wake?” “Najua. Lakini sio Jack! Tafadhali naomba zungumza naye. Nisaidie kunibembelezea. Jack sio wakunifukuza mimi! Hata penzi amekataa! Sijafanya kitu cha ajabu jamani! Nia ilikuwa kumsaidia huyo Sabrina. Maneno niliyomwambia Sabrina ni ushauri tu.” “Sasa hapo ndipo ulipovuka mpaka, na sijui kama kuna kurudi nyuma tena.” Ibra akawa kama na yeye amekata tamaa.

          “Kama hujawahi ona udhaifu wa Jack, basi ndio ujue ni Sabrina.” Pam akawa hajaelewa. “Mimi sijui amekwambia nini juu ya Sabrina! Lakini udhaifu wa Jack, ni huyo Sabrina. Kama huamini, kata simu sasa hivi mpigie Ney, au Felex wale tuliokuja nao mwezi wanne, tukaenda nao Arusha na wewe ukiwemo. Wale wanamjua sana Jack, tulikuwa karibu sana chuoni na tulikuwa kwenye uongozi mmoja. Wote tulifanya kazi chini ya uongozi wake Jack. Wewe nenda moja kwa moja kwenye swali, waulize udhaifu wa Jackson Msindai ni upi? Halafu utapata jibu lako.” “Lakini mimi sijakosa Ibra! Labda tu kama ananitafutia sababu.” “Kule kutokufanya alichokwambia yeye juu ya Sabrina, hilo nikosa ambalo kwake hataweza kulifumbia macho.” Ibra akawa muwaza kwake na kuendelea.

          “Hakuna anayejua anachokiona kwa Sabrina, au kile anachojisikia, lakini huwa hajiwezi kwa huyo Sabrina na hajitahidi, wala hajidai. Ashapita kwingi sana na huyo Sabrina, akambeba sehemu ambazo kila mtu alikuwa akimshangaa. Mpaka mkuu wa chuo alishamuuliza ni nini anachopigania hivyo, lakini hakuna aliyepata jibu. Nina uhakika hata Sabrina mwenyewe haelewi hiki ninachokwambia. Lakini nilishamwambia hata msichana mmoja aliyekuwa na mahusiano na Jack pale chuo, Sabrina akiwepo kwenye picha. Aliponisikiliza, mambo yake yanaendelea vizuri tu mpaka leo.” “Ulimwambia nini sasa?”  Akauliza Pam akiwa ametulia.

          “Maana mimi namtegemea sana Jack kwenye hii biashara Ibra. Nilikuwa siuzi Dar na mikoa mingine. Lakini kwa ajili yakufahamika kwake yeye Jack na hilo jina lake la Msindai, sasa hivi soko langu kubwa lipo Dar kwa ndugu zake na marafiki zao. Sitaki kupoteza mahusiano na Jack.” “Sasa hilo ungelijua mapema na ukaona uzito wake, ungekuwa makini Pam. Umecheza sana na Jack akikuvumilia, lakini sasa hivi sijui!” “Au ni kwa sababu ya huyo Sabrina?” “Sabrina alikuwepo kwenye moyo wa Jack miaka mingi tu. Mwenzio aliyekuwa kwenye mahusiano na Jack, alitaka kuharibu kama wewe hivyohivyo mimi nikamuwahi. Muulize Ney. Nilizungumza naye, Ney akiwepo na akamthibitishia. Alipofuata ushauri wangu, japokuwa hakuolewa na Jack, lakini walikuwa wapenzi mpaka tumemaliza chuo, na Jack amemuunganisha na wakubwa hapa mjini, yule msichana anakazi nzuri sana hapa jijini. Yote hayo ni Jack, kwa kuwa alifanya na kupenda kile anachokipenda Jack. Akatulia, yake yakamwendea sawa, sasa hivi maisha yake safi sana hapa jijini. Lakini wewe Pam, pombe.” Hapo Ibra akamgeuka.

          “Sikuwa nimelewa Ibra! Nilikunywa kidogo tu.” “Mimi si nilikuona Arusha Pam. Ukiwa baa, kunywa kidogo yako wewe sio kidogo kwa wengine. Sijui kama Jack alikwambia siku ile tulipokwenda mziki, ulivua chupi mbele yetu.” Pam akashituka sana. “Hapana Ibra, unanisingizia!” “Inamaana Jack hakukwambia!?” “Hapana Ibra!” “Basi mpigie simu Ney muulize na hili ili kuthibitisha. Ulilalamika mbele yetu wote kuwa chupi uliyovaa inakubana. Hapohapo ukaivua wakati Ney alikushauri ukavulie chooni. Tena alitaka kukusindikiza kabisa. Unakumbuka kumjibu, kwani ni nani asiyejua kama wewe umevaa chupi? Unakumbuka?” Pam kimya.

          “Si nilikwambia udhaifu wa Jack? Sasa uone basi. Yote hayo aliyanyamazia, na mkaendelea kama kawaida. Lakini kumtibua tu Sabrina, leo amekufukuza. Ndio uamini ninachokwambia sasa. Umevuka mpaka ambao huwa haruhusu yeyote yule auvuke. Jack yupo Singida kwa malengo. Hayupo huko mbali na jiji kwa bahati mbaya. Alikusudia, mpaka nahisi aliomba aletwe huko. Yupo sehemu sahihi kabisa. Ila kilichokuwa kikipungua ni watu. Maadamu Sabrina amekubali kuja kuishi Singida, hataruhusu uharibu hilo kwa lolote, maana hapo utakuwa unaua na ndoto zake.” “Ndoto gani?” Akauliza Pam.

          “Kama wewe umekuwa na Jack muda wote huo hujazijua ndoto zake, ujue hutakaa ukamfahamu tena Jack ambaye ni muwazi kama kitabu. Na kwa kusisitiza tu kabla sijakuaga, hivyo unavyomuona Sabrina hivyo. Pengine umemlinganisha na hivyo wewe ulivyo, ukampima kwa vipimo vyako vyote ukamdharau. Lakini sivyo amuonavyo na kumchukulia Jack. Huyo Jack alikuwa akihutubia maelufu ya wanafunzi wa pale chuoni. Wote tunakuwa ukumbini pale. Anaongea pointi za msingi kama unavyomjua Jack. Watu watampigia makofi mpaka maprofesa na mkuu wa chuo watampongeza, lakini yeye atamwangalia mtu mmoja tu, Sabrina. Akiona hamwangalii wala kuonyesha anamsikiliza, muulize Ney. Hiyo siku inakuwa imeharibika vibaya sana. Hata umsifie vipi, yeye mwenyewe ataanza kutoa kasoro alichoongea, na wakati kila mtu alikipitisha tena kwa shangwe. Alikuwa akifika kwenye kuhutubia wanachuo wote, namaaniasha maelfu tuko pale, kabla hajaanza kuzungumza, yaani hajakaribishwa yeye kama raisi wa chuo, macho yake yataangaza ukumbi mzima mpaka ajue ni wapi Sabrina amekaa, ndipo utamuona anazungumza kwa ujasiri na kujiamini. Lakini si vinginevyo.” “Mmmh! Basi nahisi nimeshamkosa huyo Jack na biashara zake!” Hapo Pam akajisalimisha.

          “Naona sasahivi umenielewa ninachomaanisha.” Ibra akajua ameelewa sasa. Akili yake imetulia, hatimaye ameshika. “Heri ningelijua hilo mapema! Maana ile siku ya jumapili alipomuombea kazi pale kwenye ile biashara, kuna jinsi nilimzungumzia huyo Sabrina, nikamuona amebadilika kabisa mpaka nyumbani Sabrina aliposema sababu yangu ni ya msingi na yeye anaiheshimu, ndipo nikamuona kidogo ametulia, lakini hakurudi kuwa sawa kwangu. Jumatatu yake mpaka mimi ndio nikamtafuta! Sasa unaponiambia hivyo, sidhani kama kuna kurudi tena nyuma. Kuna jinsi amenibadilikia!” “Sijui bwana Pam! Usiku mwema.” “Naomba usinitelekeze Ibra. Nisaidie.” “Kivipi tena Pam? Wewe unataka kunikosanisha na Jack.” Ibra akataka kujitoa mapema.

          “Hata kama mapenzi hayawezekani, basi asijitoe kwenye biashara pia. Nitaaibika hapa mjini. Biashara zilikuwa haziniendei vizuri. Ameingia yeye kwenye biashara nimepata wateja wengi, mpaka Dodoma pia napeleka! Ana watu wengi sana Jack, sitaki kumpoteza.” “Ninavyomjua Jack sio mtu wa visasi. Hawezi kukuharibia biashara.” “Basi njoo weekend hii na msichana wako tutokeni. Twendeni tena hata Arusha. Safari hii nitatulia, sitakunywa pombe kabisa. Na nitamuomba msamaha yeye na Sabrina.” “Subiri kwanza nizungumze na  May, nitakujibu kesho.” “Nashukuru Ibra. Na naomba wewe ndio uzungumze na Jack. Mimi nikitoa wazo la kwenda kupumzika Arusha, hawezi kukubali.” “Nitakujibu kesho.” Wakaagana. Lakini Pam akiwa amekata tamaa kabisa. Baada yakusikia uzito wa Sabrina kwa Jack, na vile alivyomkashifu kwa Jack! Akajua ndio maana hata siku ya jumatatu hakumtafuta na wala hakujibu jumbe zake mpaka alipompigia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Maji kutibuka kotekote. Mkosa! Nini kitaendelea? 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment