Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Makosa! – Sehemu ya 16. - Naomi Simulizi

Makosa! – Sehemu ya 16.

Kwa Sabrina & Jack.


Haikuwa rahisi kwa Sabrina kama alivyodhania. Hofu ya alipoachwa Moshi na Tino ikamrudia. Gafla akaona tumbo linazidi kuwa kubwa na yupo peke yake. Mpaka inafika saa saba usiku, hana usingizi ndio kama ameamka wakati alikuwa akizunguka huo mji siku nzima. Akageuka kulia na kushoto, hamna usingizi. Akaanza kusikia fujo kwa nje ya mlango wake. Watu wakipigana kama walevi. Matusi, fujo, akasikia muhudumu akiwaamulia na kuwaambia atawaitia polisi. Hofu ikazidi kumuingia Sabrina, akakaa na kuwasha taa kabisa.

          Huku kwa Jack nako ikawa hivyohivyo. Akafikiria sababu alizoambiwa na Sabrina zakumtoa pale. Akajiuliza analinda nini na anapoteza nini! Akahesabu hili na lile. Mipango waliyopanga na Sabrina. “Brina ananielewa mimi kuliko mtu mwingine yeyote.” Gafla hata mama yake mzazi akaona hamuelewi kama Sabrina. “Sabrina yupo Singida kwa ajili yangu mimi!” Jack akaona atakuwa mjinga kama asipochukua hatua. Akatoka kitandani na kuvaa kwa haraka, akatoka hapo kumfuata Sabrina hotelini.

          Alifika na kukuta hao watu bado wakipigana. Na walifahamiana. Jack akazungumza nao. “Mtaumizana bure muishie jela. Hata hiyo pesa mnayodaina haitawasaidia. Ona mnavyotokwa damu!” Sabrina akasikia sauti ya Jack akatoka kwa haraka.  Jack akamuona. “Rudi ndani Sabrina. Nakuja.” Sabrina akarudi ndani kwa haraka. Aliona kweli sio salama. Wawili hao waliokuwa wakipigana ni kweli walikuwa wakivuja damu. Polisi wakafika hapo. “Nafikiri tupo sawa jamani. Au mnasemaje?” Jack akawauliza wale waliokuwa wakipigana. Kwa hofu yakuwekwa ndani, wakaamua wakubaliane kuyamaliza kwa amani. Polisi wakaondoka, na hao vijana wakaondoka. Pakatulia.

          Sabrina akasikia hodi mlangoni kwake. Akajua ni Jack. Akafungua kwa haraka. “Nimekuja kukuchukua, turudi nyumbani.” “Sikujua kama hapa kuna baa, au wanakunywa usiku mpaka sasa hivi!” Jack bila kujibu akaanza kurudisha vitu kwenye gari, Sabrina amesimama akimwangalia asiamini anachokifanya. Akabeba mizigo yote, akakusanya na vichache vilivyokuwa juu ya meza, akaingiza kwenye moja ya begi la Sabrina, akapeleka kwenye gari. “Ulishalipia usiku wa leo?” “Bado.” “Twende.” Wakatoka hapo chumbani, akalipia mapokezi. Muhudumu akamshukuru Jack kwa kutuliza ule ugomvi pale. Jack akazungumza naye kidogo, wakarudi kwenye gari.

          “Nilijua utakuwa umeshalala!” Sabrina akaanza walipopanda tu garini. Jack akamwangalia na kuondoa gari pale. “Mwenzio sikupata hata usingizi kwa hofu yakubaki pale peke yangu. Nilijua ingekuwa tu rahisi, lakini inatisha Jack!” “Kwa nini hukunipigia sasa kama ulivyoahidi?” “Nilijua utakuwa umelala! Ndio maana sikuamini niliposikia sauti yako pale! Nikatoka kwa haraka kuhakikisha kama kweli ni wewe. Eti nimefurahi umekuja kunichukua!” Jack akatabasamu tu, akaendelea kuendesha.

          Hapakuwa mbali na nyumbani, baada ya kama dakika 10 hivi, usiku ule na hapakuwa na magari babarani, wakafika nyumbani kwa Jack. Ile hekaheka ya kuingiza mizigo ndani, Emma akatoka. Akaanza kusaidiana na Jack. “Bora umerudi, maana nimemalizia kile chakula usiku huu, nikajiambia maisha yakulala na njaa yanaanza upya.” Sabrina akaanza kucheka. “Wewe unanipendea chakula tu?” Sabrina akamuuliza. “Nilikwambia usimfanye Sabrina kijakazi wako.” “Lakini wote tunanufaika kaka. Au unafurahia kutoka kazini na kuja kuanza kutokosa samaki?” Wakaanza kucheka. “Kumbe Jack anatokosa samaki?” “Sina muda wa kukaanga mimi. Nikishabandika jikoni, nakatia nyanya na kitunguu, mchuzi tayari tunakula na wali. Muulize kama sio vitamu. Mwenyewe anajilambaga.” Emma akacheka kama anayeogopa kusema kitu. “Mbona husemi?” “Unamuuliza kwa kumtisha bwana!” “Ila huwa tunakula.” Emma akaongeza huku akicheka. Ukaendelea utani kidogo, wakamaliza kuingiza vitu ndani, Emma akarudi chumbani kwake, Jack akamfuata Sabrina chumbani kwake.

          “Nimefurahi umekuja kunichukua, Jack.” Akarudia tena Sabrina. Jack akacheka na kwenda kukaa kitandani. Sabrina naye akakaa. “Itakuaje Jack?” “Maisha na mipango yetu viendelee kama kawaida. Naomba tusiyumbe tena.” “Sawa.” “Nitazungumza na Pam, afike hapa mimi nikiwepo. Kama sipo, nyinyi si marafiki, asije ili utulie.” Hapo Sabrina akanyamaza. Wakakaa hapo kidogo, Sabrina akamsugua kidogo mgongoni kama kumfanya atoke mawazoni amtizame. Na kweli akamwangalia. “Nenda kalale, kesho kazini?” “Ni kweli.” Jack akanyanyuka na kuondoka. 

Jumatano.

          Aliamka asubuhi, akamuandalia kifungua kinywa kizuri, akamuwekea kwenye contena lenye mfuniko baada yakuangalia saa, nakuona ni saa 1:30 na bado hajatoka chumbani akaenda kumgongea. “Ingia.” Jack akamkaribisha. Akamkuta anavaa. “Nimepitiwa na usingizi. Alam iliita, nikazima.” “Nikusaidie nini ili uwahi kazini?” Sabrina akaanza kutandika kitanda wakati Jack akimalizia kuvaa shati. “Nimeshamaliza. Asante. Ulilala kweli? Maana nasikia harufu ya mayai!” “Nitarudi kulala. Niliamka kukuandalia kifungua kinywa.” “Asante kujali Briana. Nakushukuru. Halafu nipe namba yako hiyo mpya ya simu.” “Siikumbuki Jack. Nitakupigia.” “Hapana Brina. Unasema lakini hupigi. Sitaondoka hapa mpaka unipigie. Naomba nenda ukalete simu.” Sabrina akacheka na kutoka.

          Akampigia Jack akiwa chumbani kwake. Jack akapokea. “Mimi naitwa Sabrina.” Jack akacheka. “Haya, asante.” Akakata. Sabrina akarudi chumbani kwa Jack akiwa anamalizia kujiandaa, kisha wakatoka pamoja. “Ndio unapendeza hivyo kila ukienda kazini!” “Mimi muhasibu wa huu mji, Sabrina. Nahudumia watu wengi  wa hadhi tofauti tofauti, lazima niwakilishe wizara ya fedha vizuri. Kuwahakikishia pesa ya serikali ipo salama.” Sabrina akaanza kucheka. “Ndio mpaka nakunukia vizuri!” “Harufu hiyo unaipata wewe tu, mama.” Hapo Sabrina alikuwa amevaa tisheti ya Jack. Alitoka nayo usiku uliopita hotelini akiwa ndiyo aliyokuwa ameivaa wakati analala. Hata Emma alimuona ila akanyamaza.

           “Sasa hiyo tisheti ya tokea jana mama, itanuka. Badili. Zipo hapo ndani nyingi tu.” “Hii bado inaharufu nzuri tu. Ikiisha wala hutapata shida kunikumbusha, nitaitoa mimi mwenyewe.” Jack akambusu shavuni. “Acha niondoke sasahivi kabla sijachelewa kazini.” Akatoka, Sabrina akajishika shavu huku akimfuata nyuma. “Usisahau chakula Jack.” “Siwezi, ninanjaa! Jana sikula.” “Pole.” “Uache kunichanganya Brina! Naomba tulia hapa.” Jack akachukua chakula, nakutoka. Sabrina akabaki akifikiria alichosema.

          Lakini alifurahia sana kufuatwa na Jack. Kwamba Jack bado anamuhitaji! Alishampa njia zote za kufanikiwa. “Kama ingekuwa mtu mwingine si angeendelea tu na mchakato akaniacha pembeni kama kina Tino!” Sabrina akaendelea kumtafakari Jack huku akisafisha pale na kupaweka sawa. Akagundua Jack aliacha pesa pale alipochukua chakula. Akacheka. “Haya ndiyo aliyokuwa akiyasema Pam!” Asijue Pam aliongea akiwa ameiona pesa na kuichukua yeye.

          Akarudi kulala mpaka kwenye saa tano. Akakuta Jack alimpigia na kumuachia ujumbe. ‘Pesa ya matumizi ya hapo ndani umeiona? Niliicha jikoni, na wewe usiiache hapo.’ ‘Asante na samahani nilikuwa nimelala sikuona ulivyonipigia.’ Akarudisha majibu, Jack akapiga. “Afadhali kama ulirudi kulala. Unampango wa kutoka?” “Nitakwenda tu sokoni na kurudi. Vipi?” “Nataka nikukutanishe na yule dada. Anaitwa Imani. Ni dada mtumzima, anajiheshimu na hana mambo ya kitoto. Utampenda tu.” “Si ulisema utamwambia aje hapa nyumbani?” Akauliza Sabrina. “Kama utaona sawa.” “Kwenye saa nane nitakuwa nimesharudi. Nataka nijiandae sasahivi, nitoke.” “Nakutumia namba yake, na yeye nampa yako. Lakini nitamwambia saa nane awepo hapo.” “Sawa Jack. Uwe na wakati mzuri.” “Na wewe pia. Ila usizunguke sana!” Sabrina akacheka na kuaga.

Sabrina Na Kwa Jack.

M

ida ya saa nane wakati anapika, akasikia hodi. Akajua ni Imani. Akamkaribisha jikoni, wakaanza kuzungumza. “Mbona kunanukia hivyo? Unapika pilau?” Sabrina akacheka. “Mboga za majani hizo, nakaangia na kitunguu swaumu tu.” “Mambo ya pwani?” Wakacheka. Mazungumzo yakaanza. Na kweli alionekana ni dada anayeelewa mambo na huo mji. Akamweleza Sabrina mambo mengi sana, na watu na sifa zao hapo mjini. Akaeleza mengi akimtahadharisha awe makini na nani na yupi. Sabrina akawa makini akimsikiliza huku akipika. Akamuonya mengi na kumwambia mazuri ya huo mji na ubaya wake pia.

          Sabrina akauliza maswali mengi, mpaka inafika saa kumi kamili Jack anarudi nyumbani, Sabrina alishajua nini chakuanza kufanya kwenye huo mji. Jack akawafuata jikoni. “Hapa umeniletea jembe, Jack mdogo wangu. Naona nishindwe mimi mwenyewe!” Imani akamsifia Sabrina. Wakacheka. “Umeona eeh!” “Aah kabisa. Kwanza sio mapepe. Mdogo lakini anaonekana akili yake yakiutuuzima. Huyu hata ukiniacha naye siku nzima, hutanisikia nikilalamika.” “Nashukuru dada Imani kama umeona mtaendana. Hata yeye anataka mabadiliko na maendeleo.” Wakaendelea watatu hao wakizungumza, Sabrina akipika. Alionekana ana vingi vyakupika, lakini kwa haraka haraka, wakamuona akiepua na kuweka tu vyakula juu ya meza.

          “Dada Imani kula kidogo ndio uondoke.” “Hapana. Soda uliyonipa inatosha. Acha na mimi nikapike kwangu.” “Basi beba hata chapati tatu na wewe ukanywee chai asubuhi.” “Wala kesho hazifiki hizo mdogo wangu.” Wakacheka. Sabrina akamfungashia zile chapati, mara hodi mlangoni. Jack akatoka kwenda kuangalia mgeni, wakati Sabrina na Imani wakimalizia mazungumzo.

          “Unataka nini Pam? Mbona kama nimekueleza vizuri sana mchana?” Wakamsikia Jack akiongea. “Sijaja kukuudhi Jack. Nimekuja kumuomba Sabrina msamaha. Na ulisema nije hapa wewe ukiwepo. Nimesubiri muda wa kutoka kwako kazini, ndio nikaja hapa, nikijua wewe upo. Au nimekosea?” Kimya. “Niambie Jack. Kama nimekosea, nitaondoka. Sitaki kukuudhi wewe wala Sabrina. Sabrina mtu mzuri sana. Sitaki tukosane.” Sabrina akakunja uso. “Uzuri wangu ameujulia wapi na lini!?” Akajiuliza Sabrina akishangaa. “Sasa Sabrina mdogo wangu, acha na mimi nikaivishe kwangu. Maadamu umesema unapenda mlenda, kesho nitakupikia, ukija kwangu nakupa uje ulie ugali.” Sabrina akacheka. “Sawa dada yangu. Nisalimie watoto na shemeji.” “Zimefika.” Imani akaondoka na chapati zake. Akamsikia akisalimia tu na kumuaga Jack, akaondoka bila mazungumzo mengi kwa Pam.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sabrina akaendelea kupika. Alikuwa akisukuma na kuchoma chapati. “Pole na upishi Sabrina?” “Asante.” Akaitikia Sabrina bila hata kumtizama Pam. Akaendelea na mapishi. “Najua niliongea maneno ambayo nilivuka mpaka. Nikasema hata mambo yetu ya ndani ya kimapenzi, lakini...” “Hebu subiri kwanza Pam! Uliongea nini tena?” Jack akauliza kwa ukali. Sabrina kimya hata hakuwatizama. Akaendelea tu kupika. “Nahisi ni hasira sijui au pombe! Lakini nimejiambia napunguza pombe. Natulia kama ulivyonishauri.” “Pam! Acha kunizungusha na maneno mengi. Ulimwambia nini Sabrina juu yetu?” Pam kimya.

          Emma akaingia. “Bwana Sabrina akiwepo humu ndani, kunakuwa na neema ya ajabu! Naumwa Sabrina!” Sabrina akaanza kucheka. “Njaa?” “Kama upo huko tumboni. Nikaribishe tu huko jikoni.” “Hubadili nguo za shule?” Sabrina akamuuliza. “Sina nguvu. Kaka shikamoo.” “Wewe kila siku unanjaa, kwa nini huli mchana?” “Pesa ya chakula nimenunulia simu kaka yangu. Nasubiri mwisho wa mwezi, niombe tena pesa nyumbani.” “Simu yako ya zamani umehonga?” Jack akamuuliza, Emma akaanza kucheka. Wakajua kweli. “Sasa huo si ujinga wewe Emma?” “Wala hukukosea kaka. Lakini nishafanya, acha tu nije kula nyumbani. Asubuhi niliondoka na maandazi hapa, nikala njiani.” Wakamsikia Emma akicheka.

          “Shem leo hujashitua nini? Mbona kimya? Ile furaha yetu haipo!” “Siku hizi sinywi tena.” Emma alicheka mpaka Pam mwenyewe akaanza kucheka. “Sasa huamini?” Pam akamuuliza. “Acha muda ujibu hilo Shem. Mzima lakini? Naona umepoaa!” Akauliza Emma huku akiingia jikoni. “Mimi mzima tu. Nimekuja kutengeneza.” “Safi sana. Kutengeneza muhimu.” Emma akaosha mikono. “Mimi nipo tayari Sabrina. Natetemeka njaa.” “Chapati hizi za asubuhi.” “Hakuna zakuonja?” “Hapana Emma. Wewe kula chakula kipo mezani. Chapati za asubuhi.” “Zinanukia hizo!” “Umeambiwa chapati za asubuhi Emma, kale chakula.” Jack akaweka msisitizo. Emma akacheka na kutoka hapo jikoni.

          “Acha mimi nipige picha kwanza ndio nipakue. Viazi vya kukaangwa, mboga za majani zinanukia kama pilau, na maini!” Sabrina akaanza kucheka jikoni. “Sabrina udumu mama. Nguvu hiyo ya upishi izidi kukujaa. Ukipika chapati, upike za asubuhi na za kuonja usiku.” Wote wakacheka. “Haya, njoo uchukue moja.” “Mungu amenijibu kwa haraka! Sikutegemea.” “Ukimuendekeza huyo, atamaliza chakula chote leoleo.” “Nitakukatia na wewe kaka, wala mimi si mchoyo.” Kweli Emma akachukua chapati, akamkatia Jack. Wakala huku wakicheka. “Umeona mambo hayo kaka? Unalala usiku ukiomba asubuhi pakuche salama, ili ule chapati.” Sabrina akazidi kucheka. Emma akachukua chakula chake, akaelekea chumbani kwake. Pakazuka ukimya.

          “Kwa hiyo Sabrina umenisamehe?” Kwa kuwa Sabrina alishapewa habari za Pam na Imani, akajua ni hovyo tu. Akawa ameshamdharau kabisa. Hakumtofautisha na Kasandra, aliyemchukulia Emma, Emma akashindwa hata kumuoa. Akajua na yeye hana mwendo mrefu na Jack. Akawa sio tatizo tena. “Eti Sabrina?” “Mimi nilishakwambia tokea jana. Achana na mimi. Hunijui, sikujui. Tumekutana hapa kwa Jack. Acha kunifuatilia na kuniingilia, na mimi sitakuingilia kwenye mipango yako. Mimba niliyonayo na umri wangu, naishije hapa duniani na nitamuweka wapi mtoto wangu akizaliwa, havikuhusu. Usihangaike na mimi. Na tafadhali usiniingilie kabisa. Umenielewa Pam?” “Nilitaka kukusaidia tu.” Akajaribu kujitetea, Jack kimya.

          “Nilishawahi kukuomba msaada? Nani amekwambia nina shida mimi? Nishaishi na watu wa aina yako wengi tu. Nakuomba achana na mimi. Sijakuomba msaada, na sihitaji msaada wako. Nikihitaji, mimi mwenyewe nitakutafuta nikuombe. Usinipe msaada huku ukinitukana na kunidhalilisha. Nikija kuwafanyia kazi wewe na Jack sio kwa sababu nataka mnisaidie. Ni kwa kuwa na nyinyi mtanufaika na huduma yangu. Kama huoni kama utanufaika na mimi katika biashara yenu, inamaana hunihitaji. Sasa kwa nini utake kuniweka sehemu ambayo unajua hutanihitaji? Si ndio utaendelea kuninyanyasa?” “Sitakunyanyasa. Nitafanya kazi na wewe na tutaheshimiana.” “Basi mimi sitaki kuajiriwa na wewe.” Sabrina akaongea kwa kujiamini.

          Jack akajua alikasirika sana. “Sijui kama umenielewa Pam?” “Nimekuelewa na naomba msamaha.” “Sawa.” Sabrina akaendelea na shuguli zake, akawaacha wapenzi hao wamesimama hapo mlangoni jikoni. “Kwa hiyo si yameisha Sabrina?” “Yameisha. Kama unanjaa, kaa hapo mezani ule chakula.” Pam akacheka. “Mimi nilijua tu, mimi na wewe hatuwezi kukosana Sabrina. Nishakuelewa, sasa hivi nitakuwa makini na maneno yangu. Mwenzio mropokaji, halafu sipendi kumuudhi mtu ila huwa wakati mwingine napandwa na hasira, naongeaga ujinga mpaka baadaye najishangaa mwenyewe! Mimi najihisi sipo sawa mimi!” Mpaka Sabrina ikabidi tu acheke. “Kweli tena. Wananiambiaga watu. Lakini sasa hivi naacha kuropoka. Tena nikiwa na wewe best yangu, nitakuwa naangalia kila neno. Ukiona nimepitiliza, nishitue tu. Nataka tubaki kuwa marafiki.” Sabrina akaendelea kupika huku akimtafakari Pam jinsi alivyojirudi. Akahisi kuna anayetaka kuibiwa tu, si bure. Pam huyu si yule waliyekuwa naye jana yake akimtukana matusi mabaya vile! Akatulia tu kimya.

          Alipomuona Sabrina ametulia anaendelea na yake hapo jikoni, akachukua sahani, kweli akakaa mezani. “Vinanukia vizuri hivyo! Ngoja na mimi nionje japo kidogo.” Jack kimya. “Basi chakula kama hiki kikipata Safari baridiii.” Akajishitukia. “Au hata soda.” Akajirudi, Sabrina alipomsikia akacheka huko jikoni. “Ukitaka nitaenda kukuletea bia yako ya Safari.” “Nimeacha mwenzio. Sasa hivi sinywi pombe hata kidogo.” Akaongea akimwangalia Jack aliyekuwa ameinamia simu yake tu, kimya.

          “Mimi ningekuwa wewe Sabrina, ningekuja kufanya kazi na mimi.” “Mbona umenikazania, wakati ulisema vizuri tu kuwa huajiri watu wa karibu?” “Nakiona kama kichwa chako kitanisaidia maarifa?” “Umeniona wapi wakati uliniona mara moja tu, ukaja na matusi?” “Sabrina naye kwa kukumbushia mambo ya zamani!” “Ni jana tu wala si zamani!” “Basi, nimeomba msamaha. Ila chakula kitamu!” “Sasa usimmalizie Jack, na mimi ujue tupo wawili. Nakula sana.” “Sasa mbona hata huna tumbo wala mwili? Mtoto huyo unambembea wapi?” Sabrina hakumjibu, akanyamaza tu.

          “Kaa tule Jack mpenzi wangu. Tushasameheana, yamekwisha. Si ndiyo?” Jack akatoa macho kwenye simu yake, akamtizama na kurudisha macho yake kwenye simu akaendelea na alichokuwa akifanya kwenye simu. “Mwenzio Sabrina amenisamehe. Na tushakuwa marafiki. Nimeacha pombe na kuropoka, si ufungue moyo unisamehe tu?” Jack kimya. Akaondoka kabisa pale. “Naona na mimi niondoke kabla sijaharibu zaidi.” Akarudisha sahani jikoni, na yeye akaondoka. 

Alhamisi.

S

iku hiyo Sabrina akatoka mapema kumfuata Imani. Walikuwa na miahadi. Akampeleka mpaka kwenye jengo la chama. Akamzungusha kwenye miradi ambayo ilishakufa. Akamtembeza hapo mjini, ndipo akarudi nyumbani akiwa na picha kamili. Jioni aliporudi Jack, wakaanza kuzungumzia aliyoyaona na kuanza kushauriana nini chakufanya. Wakati wamekaa wawili hao wakiweka mipango yao na kuandika, simu ya Jack ikaita. Jack akaiangalia, alikuwa Ibra, akapokea. “Unamkumbuka yule mwanamziki Mganda unayemsifia maneno ya nyimbo zake?” Akamtajia jina. “Kafariki!?” “Hapana bwana! Weekend hii yupo jijini. Anatumbuiza. Njooni na Pam, hoteli juu yangu.” Jack akatulia. “Upo kaka?” “Nafikiria.” “Unafikiria nini kwenye tukio la mara moja kwa miaka, kaka!” “Ulitaka iwe lini?” “Ukitoka kazini kesho, mnaweza kuja na ndege ya jioni. Mimi na May tutawapokea. Tukale, kisha tutawapeleka hotelini. Kesho yake tena tutakuwa wote. Njoo uoshe macho mjini. Hujaona flyover kwa muda mrefu.” Jack akacheka. Ibra akampanga mpaka Jack akakubali.

          Akakata simu akabaki kama anayefikiria. Sabrina akaona amuache. “Ngoja nikaandae chakula cha usiku. Emma atarudi sasa hivi na njaa zake.” “Usimuendekeze, atakuwa anakulilia kila siku.” Sabrina akacheka na kuelekea jikoni. “Napika tu wali, nina kiporo cha mboga.” Jack akamfuata. “Ibra ametualika jijini. Unataka tuongozane?” Sabrina akacheka. “Wewe umealikwa uende na mpenzi wako, unataka kubeba na wapangaji pia! Nenda ukafurahie na wenzio. Mimi utanikuta hapahapa. Kwanza jumamosi nina miahadi na dada Imani.” Jack akabaki kimya.

          Mara Pam naye akaja, akiwa amechangamka kweli. “Ibra ameniambia.” Jack akamwangalia tu. “Si kuhusu safari ya Dar! Au amenidanganya hujakubali?” Akajirudi kwa haraka baada yakuona utulivu wa Jack usoni. “Nimezungumza naye.”  Akashangilia Pam. “Ameniambia na kina Ney watakuwepo. Lazima nipendeze, au unasemaje mpenzi wangu? Nikuwakilishe vizuri. Na safari hii tukienda sinywi pombe kabisa, ili nisikutie aibu kama vile Arusha.” Jack kimya. “Inabidi nikasukwe. Tunaondoka saa ngapi?” “Lazima niende kazini, kwa hiyo itakuwa jioni. Nikikosa ndege ya jioni, basi jumamosi asubuhi.” “Kesho tukalale Dar mpenzi wangu. Ibra amesema atatutafutia hoteli 5 star. Tukaoshe macho. Maswala ya tiketi niachie mimi, nimpigie simu Doto sasa hivi, atuangalizie ndege ya kesho. Nikipata mchana wa saa 8 je?” “Isiwe chini ya hapo Pam, tafadhali.” “Nimekuelewa. Sasa ngoja nikajiandae kwa safari.” Pam akatoka hapo na furaha zote.

Ijumaa.

K

wenye mida ya saa saba mchana Jack akarudi kutoka kazini. Akamkuta Sabrina amejilaza chumbani kwake. “Upo sawa?” Jack akauliza. “Mzima kabisa. Nimejilaza tu. Vipi, mbona mapema leo?” “Ile safari ni leo. Pam amepata ndege ya saa 9 na nusu.” “Sawa.” Jack akabaki akimwangalia. “Vipi?” Sabrina akamuuliza na kukaa. “Najisikia uzito!” Jack akalalamika. “Uzito wa nini tena?” “Kwenda kwenye hiyo safari!” “Nenda kafurahi na wenzako Jack. Unafanya kazi sana, halafu bado wewe ni kijana, unastahili mapumziko.” “Mbona wewe ni kijana na huendi?” Jack akauliza.

          “Jamani Jack! Kwanza mimi sikualikwa.” “Mimi nimekualika.” “Hapana Jack, sipo kwenye nafasi kama yako au yenu kwa sasa. Sina furaha moyoni yakusema nakwenda kusherehekea au kupumzika. Huku kuwa busy hapa na kuwaona nyinyi, kunanisaidia kuondoa hofu moyoni. Nipo kwenye wakati mgumu Jack, Mungu ndiye anayejua.” “Naweza kuelewa Brina.” “Sidhani Jack. Mimi mwenyewe sikuwahi hata kuhisi ninachojihisi sasa hivi. Natamani haya yote yageuke kuwa ndoto.” Sabrina akafikiria kidogo. “Umeshawahi kupatwa na ile hali ya moyo kupasuka? Yaani unakaa hivi, unasikia PAA! Kama kumeanguka chuma sakafuni!” Jack akamuhurumia sana.

          “Ndio hali ninayoipata. Nashukuru kumpata na dada Imani, namuona ni mtu mzima, anamipango inayonifanya nifikirie, nisikae nikijiwazia mimi na matatizo yangu. Mimi sio mtu sahihi sasa hivi kuwa karibu kama unataka kweli kupumzika na kustarehe. Badala yakuwafanya muwe na furaha, nitawafanya wote muwe na mawazo. Heri wewe uende ukafurahie na wenzako. Ukirudi hapa uwe na nguvu zakututosha wote, kuliko ubaki hapa. Unastahili kupumzika Jack. Nenda na ninaomba ukafurahie haswa. Safisha mawazo.” Jack akainama. “Twende nikakusaidie kujiandaa.” “Hamna kitu kikubwa chakubeba.” “Basi nenda angalau utoe hizo nguo za kazini, uvae kama unayekwenda kwenye kupumzika.” Jack akasimama na kutoka hapo.

          Pam alikuja kumchukua akiwa amependeza vilivyo. Sabrina mwenyewe akamsifia. Na vile anavyopenda kucheka, Pam akazidi kuvutia. Akamchokoza kidogo Sabrina kama anayejikomba, Sabrina akimwangalia tu. Jack alipotoka na kibegi chake, wakaondoka. Sabrina akarudi kulala mpaka jioni, akaamka kupika ili Emma akirudi akute chakula. Kwenye saa mbili usiku Jack akampigia. “Vipi?” “Huku tuko salama kabisa. Mlifika salama?” Sabrina akauliza. “Tulifika salama, tupo hapa hotelini tunajiandaa tutoke kwa chakula cha usiku, nilipiga kukujulia hali.” “Asante. Basi muwe na wakati mzuri.” Wakaagana na kukata. Sabrina alipoangalia muda na kuona ni saa mbili na walishazungumza, akazima kabisa simu. Akaiweka pembeni.

Jumamosi.

I

mani alifika hapo kwenye mida ya saa nne asubuhi, akamkuta Emma na Sabrina wakisaidiana usafi. Akamchukua Sabrina kama walivyokubaliana, wakaenda kuzunguka kufuatilia miradi mingine. Sabrina alimpenda Imani kwa kuwa alikuwa ni mzaliwa wa pale, anapafahamu sana mjini. Halafu akatokea kumkubali sana na yeye Sabrina. Ikawa rahisi kupanga naye mambo. Akawa akiulizia kwa nini hiki kilikufa, tatizo lilikuwa nini, kama kinaweza kufufuliwa, nini wafanye wasirudi nyuma tena, na nini kinahitajika. Hapo Sabrina akawa anaandika tu. Imani naye akawa amemfurahia umakini wake, wakajikuta wanaendana.

          Akarudi nyumbani akiwa hoi kwa kuwa Imani hakuwa na gari, walitembea mpaka miguu yake ikasalimu amri. Alikuwa amechoka, jua lote la siku lilimuishia mwilini. Hakuwa hata na nguvu ya kupika. Akaamua kununua chakula. Akarudi na chips yai kwake na kwa Emma. Wakala pamoja huku wakizungumza. Emma akamkaribisha kesho yake waende naye kanisani kwao, akakubali bila shida akaona itamsaidia kumtoa hapo nyumbani ambako angebaki peke yake na kujiongezea hofu tu akijikumbusha matatizo yake.

Jumapili.

A

subuhi kwenye saa nne, wakaondoka na Emma kwenda kanisani kwao. Nako mbali lakini wakatumia usafiri wa daladala. Ibada zakipendwa, zikavuta mpaka saa nane na nusu mchana. Emma akamwambia Sabrina anahamu na mbuzi choma, na anajua sehemu nzuri inayotengeneza na ndizi za kukaanga. Akampanga Sabrina kwa maneno mengi mpaka Sabrina akakubali. Wakaongozana wakitembea, jua kali mpaka wakafika. Wakatafuta sehemu nzuri wakakaa wao wawili. Ukaanza utani na utundu wa Emma. Sabrina anacheka kama anayetekenywa. Story za shule anakosoma na msichana aliyemuhonga simu zikaendelea na muda nao ukienda, hawana habari. Sabrina anacheka hana mbavu. “Nionyeshe picha yake.” “Ni mweupe huyo, dada!” Sabrina akazidi kucheka. “Wewe unapenda wasichana weupe?” “Mweusi sioi.” Sabrina akazidi kucheka. Akaonyeshwa msichana mwenyewe ni wa hapohapo Singida lakini Mnyiramba. Sabrina akamsifia. “Sasa utamleta lini nyumbani?” “Siku kaka akisafiri kama hivi, ukiniruhusu, nitamleta.” Sabrina akazidi kucheka. “Unamuogopa Jack?” “Nimekabidhiwa kwake, basi baba anakazi yakuulizia maendeleo yangu kwake mchana na usiku!” Wakaendelea kucheka hapo wakila mpaka giza likawakuta mtaani.

          Wakaanza kutembea taratibu hawana haraka wanarudi nyumbani. Wameshiba, hawana wanae muwahi. Vicheko, Sabrina akawa amefurahi kweli siku hiyo. Simu ya Emma ikaita. “Kaka huyo!” Sabrina ndio akili inamrudia, hana simu. “Pokea umsikilize.” Emma akapokea. “Uko wapi wewe?” Aliposikia sauti ya ukali, akaona amrushie lawama Sabrina. “Tulikwenda kanisani na Sabrina, akasema anahamu ya nyama choma, lakini akataka iwe ya mbuzi. Ndio ikabidi kumpeleka. Hapa ndio tunarudi.” Sabrina akakunja uso, akimtizama Emma. “Mko wapi?” Jack akauliza. “Tunatembea kutafuta daladala, leo si unajua ni jumapili daladala za shida?” “Kama unalijua hilo kwa nini hukumwambia mwenzio mkabeba mkaja kula nyumbani?” “Sabrina alitaka kula palepale, alisema hana hata nguvu yakutembea.” “Nisubirini hapohapo nakuja.” Akakata.

          “Wewe Emma! Nani aliyesema anahamu ya nyama choma ya mbuzi kama sio wewe?” “Hiyo sauti yake ilivyo ya ukali, nikaona nikupambanishe naye tu.” Sabrina akaanza kucheka. “Wewe si umetoka kanisani wewe?” “Huo sio uongo bwana. Nimeongeza kidogo tu kwenye ukweli. Sasa amesema anakuja kutuchukua. Hapo karudi nyumbani, katukosa, ndio maana ameamua kuja kutufuata. Kwanza kwa nini hajakupigia wewe?” “Simu yenyewe sijui hata ilipo!” Wakaanza kucheka. Wakatafuta sehemu wakakaa. Zikaendelea stori, wanacheka. Akagundua Emma anakwenda kanisani kupiga kinanda. Mtoto aliyekulia kwenye ulokole. Na nimpigaji mzuri tu, na huko kanisani pia alikabidhiwa kwa mchungaji. Kwa hiyo na huko nako baba yake anapiga simu kuulizia. Sabrina akazidi kucheka.

          “Asikwambie mtu! Nina mzee mkoloni, yule anayekwambia lala chini akuchape viboko.” “Emma!” “Wewe siku muulize kaka. Alishakuja kunitandika palepale.” Sabrina alicheka mpaka machozi. “Mbele ya Jack!?” “Kama natania, muulize kaka. Na kanisani sio ombi, wala hiari, ni lazima. Anapiga simu kila jumapili kuulizia kama nimekwenda, na kama niliwahi.” “Acha masihara Emma!” “We acha. Utakuja kumuona. Mwezi haupiti, atakuja kuja kunitembelea. Ongea yake yenyewe utafikiri nipo jeshini!” Sabrina alizidi kucheka mpaka machozi. Emma alikuwa mtundu wa maneno, alimfanya Sabrina acheke sana.

          Wakiwa katikati ya stori, wakaona gari ya Jack. Wakasimama. “Wewe kaa naye mbele, ngoja mimi nitulie nyuma kimya. Maana hiyo sauti yake, mimi namjua kaka, si kwema.” Wakawa wanaongea huku wakisogelea gari ya Jack. Sabrina anaendelea kucheka, Emma kimya. Sabrina akafungua mlango wa mbele akapanda, Emma nyuma. “Pole na safari.” Sabrina akaanza. “Asante.” Jack akaitikia kwa kifupi tu, akanyamaza. Wakatulia kidogo.

“Mlirudi saa ngapi?” “Ungetaka kujua hilo ungewasiliana Brina!” Akaanza Jack. “Umezima simu tokea juzi nakutafuta kwa simu sikupati bwana! Inakuwa kama umenifanyia makusudi!” “Tulizungumza juzi Jack, labda umesahau. Kumbuka ilikuwa usiku ukaniambia ndio mnatoka kwenda kupata chakula cha usiku. Umesahau?” Jack akamwangalia na kunyamaza. “Pole. Ulinitafuta sana?” Kimya. “Usikasirike bwana Jack! Mwenzio nilikuwa nakusubiri kwa hamu, nina habari njema kibao za kukupa. Jana tumezunguka na dada Imani. Halafu hukuniambia kama vijana walikuwa na eneo pale sokoni!” “Walishindwa biashara, wakaamua kuwa wanakodisha hilo eneo. Kwa hiyo pesa ya kodi ndio inachukuliwa, napo inalipwa kwa kuvutana kweli!” “Nimemwambia dada Imani tuangalie mkataba, tuone unaisha lini. Pale tunaweza kupatumia sisi wenyewe, na tukapata pesa zaidi ya kukodisha. Ni sehemu ya mbele kabisa ya soko! Tunaweza kuuwa ndege wawili kwa jiwe moja. Vijana wakapata ajira, na bado tukaingiza pesa.” “Sasa yote hayo kwa nini hukunitafuta na kuniambia?” Jack akauliza kwa kulalamika.

          “Nilitaka upumzike, ufurahie huko ili ukirudi uwe fresh. Kichwa chepesi, hata nikikwambia jambo, linaeleweka kwa haraka.” “Wala haijasaidia.” “Tena!?” Sabrina akashangaa. “Hakuja huyo mwanamziki wakiganda, unayempenda?” Kimya. Sabrina akawa hajaelewa. Akanyamaza mpaka wakafika nyumbani. Emma haraka sana akakimbilia chumbani kwake huku akimkonyeza Sabrina. Sabrina akamshika Jack mkono akamvutia chumbani kwake. Wakakaa.

          “Niambie nini kimekuudhi Jack?” “Unanipuuza sana Brina! Hunichukulii maanani. Nakuwa kama mtu baki tu, tena hata usiyenifahamu! Nikiwepo sawa, nisipokuwepo pia ni sawa!” Sabrina akabaki ameduaa. “Unawezaje kukaa siku nzima hata usinifikirie hata kidogo!? Siku nzima, Brina!? Na leo pia! Hata usiwe na wasiwasi kama siku nilipokwenda kula kama nilirudi salama, au la!? Hukutaka hata kuniambia usiku mwema! Mimi nisingekufanyia hivyo Brina. Sina nilichofanya huko ila kukupigia tu wewe simu. Njia nzima nimekuwa nikikupigia wewe simu! Nimefika hapa kama kwenye saa 6 mchana, sikukuti nyumbani wakati unajua wazi mimi narudi leo! Hujali nitafikaje nyumbani! Kama nitafika nikiwa na njaa au la! Unanipuuza Brina. Unanipuuza sana.” Sabrina akamkumbuka Tino, naye alichanganyikiwa hivyohivyo kwa kumkosa masaa machache tu. Akakumbuka alivyokuja kumbadilikia. Akatulia kidogo, akakumbuka huyo ni Jack, alikuwepo tokea Emma na Tino.

          Akarudisha hapo mawazo kwa haraka. “Nikikwambia ijumaa nililala kwa shida sababu ya hofu kwa kuwa wewe hukuwepo hapa ndani, utaamini?” Kimya. “Jana niliweza kulala sababu ya uchovu Jack. Nilitembea juani karibu siku nzima, nimerudi hapa na chips zangu na Emma, nilishindwa hata kupika! Nimelala kwa kupitiwa na usingizi nikiwa hapo kwenye kona, hata sikujifunika. Nimeamka usiku nikiwa nimeshika hiyo tisheti yako Jack. Uchovu na kukulilia ndiko kulinifanya niweze kurudi kulala tena. Ningekupigia, ningekuchanganya tu Jack. Nipo kwenye kipindi kigumu haswa, zaidi ninapokuwa peke yangu.” Sabrina akaendelea kujieleza machozi yakimtoka.

          “Kwa hiyo ninapopata kitu chakunichukua mawazo, najitahidi nisijikumbuke kwa muda. Ile ijumaa tulipoongea, kwa kuwa ilikuwa usiku sikujua kama utanitafuta tena. Nikajifariji kuwa angalau upo na wenzio mpo kwenye wakati mzuri. Nikaweka simu pembeni nikalala. Sikupuuzi Jack. Niamini kuwa wewe ndio mtu pekee umebaki kwenye maisha yangu, wewe ni shahidi wa hilo. Naanzia wapi kukupuuza Jack?”Jack akamvuta kama amlalie. Sabrina akajilaza hapo mapajani. Na yeye akajivutia mto, akauweka nyuma yake, akaegemeza mgongo. Wakatulia, Sabrina akijaribu kujifuta machozi.

          “Hata mimi nimejilaumu sana kuondoka. Nilifanya haraka kukuacha. Hapakuwa na ulazima wa kwenda, hasa kipindi hichi ambacho ndio umekuja tu, na mimi nikakuacha!” “Hapana Jack. Unayo haki yakufurahia. Huna sababu ya kujinyima raha kwa matatizo yasiyo kuhusu.” “Wewe unanihusu Brina. Kwa hiyo matatizo yako ni yangu. Hata nikijitahidi vipi kukwepa, najikuta unapoumia na mimi naumia tu. Siwezi kujisaidia, siwezi kukimbia. Upo kwenye moyo wangu, hujawahi kutoka tokea nakufahamu.” Sabrina alilia sana. Alilia, akalia akiwa amemuinamia Jack. Akajitoa na kuhamia kwenye mto wake, akajifunika na tisheti ya Jack, akaendelea kulia. Jack akamfuata tena akamrudisha lakini safari hii kifuani.

          Sabrina akajiweka vizuri akilia kwa majuto mengi akifuata wanaume wengine na kukwepa upendo mkubwa hivyo! Akajutia asijue chakufanya akiwa amebeba mimba ya Tino! “Naomba nisikilize Brina, tutakuwa sawa?” “Hapana Jack. Niambie kama mimi ndio nitakuwa sawa. Hakuna ‘tuta’ tena. Huu ni mzigo wangu peke yangu Jack.” “Nimerudi mapema kwa ajili yako Brina. Haupo peke yako na samahani nilikuacha. Sitarudia tena, kuanzia sasa tutakuwa wote.” “Sijui Jack! Ila ninachojua sitaki kukuingiza kwenye matatizo yangu.” “Nilishakwambia matatizo yako ni yangu. Sina jinsi nikakwepa. Nakupenda Brina, sina jinsi nikajisaidia. Siwezi kuficha na wala siwezi kudanganya. Nashindwa kuendelea kuvumilia. Nahisi nitachanganyikiwa kama sitakwambia ukweli.” Sabrina akahisi hajaelewa vizuri, akakaa kabisa.

          Akajifuta machozi, akakaa akamwangalia. “Siwezi kuvumilia tena Brina. Siwezi kuficha tena. Juzi usiku imebidi kuwaambia wote niliokuwa nao. Niambie kile unachotaka niwe, mimi nitakuwa, nikuoe na mimi nipumzishe nafsi yangu.” Sabrina hakuamini. Jack akatoa pete mfukoni. “Jana kaka alinisaidia kwenda kununua hii pete kwa ajili yako. Nimekisia tu size kutokana na wembamba wako, ukinikubali leo, hii pete ni yako Brina. Na ya ndoa inakuja kwa haraka. Huyo mtoto hatakuwa wako peke yako, atakuwa wetu.”

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

  • Jackson Msindai anataka kumaliza kabisa. 
  • Safari hii Sabrina amepata!? 
  • Wakiwa na mipango mingi mizuri mbeleni katikati yao, Yepi yanawasubiri kuyakabili! 
  • Kila hatua kwenye maisha ina changamoto yake. Je, Safari hii Jack atahimili mshindo ili kubaki na Sabrina, au Yatamshinda kama Tino aliyeanza kwa viapo vizito na ahadi nyingi halafu kuja kushindwa vibaya sana kungali mapema kabisaaa?
  • Nini kitaendelea kwa wooote? 
  • Mambo ya Simulizi hili ndio kwanzaaaa yanaanza, 

            Usikose muendelezo kuona mengi ya maisha wanakopitishwa viumbe wengine. 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment