Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 18. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 18.

 

Na Jack alimjua mama yake, mfikiria kwa upana na urefu, kikubwa, si msahaulifu. Kwa hiyoakajua wazi hawezi kumpa majibu mepesi. “Nilipomkaribisha huku, nilimwambia juu ya kufanya naye biashara. Sijui kama unakumbuka?” Jack akamuuliza mama yake kwa upole. “Nakumbuka sana tu, sijasahau chochote.” Mama Msindai akaweka msisitizo hapo, kumkumbusha Jack anazungumza na nani.

“Sasa kipindi kile alikuwa amepata kazi ya muda mfupi. Nakumbuka hata wewe nilikwambia mama. Nikakwambia amesema hana uhakika itaisha lini, kwa hiyo amenishauri niendelee tu.” “Alipata kazi gani?” Mama yake akauliza. “Alikuwa akimuuguza mtu. Wakahamia kwa matibabu KCMC, alipopata nafuu akamuacha Sabrina, Moshi akiwa amemruhusu na kumlipa. Kwa hiyo Sabrina aliponiambia yupo Moshi anatafuta kazi, akijua ameshanichelewa mimi, pengine nilishaanza biashara na mtu mwingine, ndipo nikamfuata. Mimi ndiye nilimfuata Sabrina, Moshi na kumuomba aje na mimi huku. Nilimfuata ijumaa iliyopita. Amekaa hapa kama week moja ndio jana nimemuomba nimuoe.” Mama Msindai kimya akisikiliza.

“Sabrina ananielewa mama yangu. Huku kuishi naye hapa kwa juma moja tu, tena kama rafiki wala si mpenzi, nikiwa bado na Pam, nimegundua kwa nini moyoni nilikuwa nikimsubiri Sabrina.” Jack akaendelea taratibu. “Inamaana anamfahamu Pam!?” “Alikuwa akiishi hapa huku akimjua Pam kama ndiye mpenzi wangu na akaheshimu hilo. Ila mimi mwenyewe ndio nimeshindwa mama yangu. Sabrina ananikamilisha kwa namna ya ajabu sana.” Jack akaanza kumsimulia mambo aliyomshauri na jinsi alivyomtia moyo akiamini kile anachokipenda Jack, mama yake akimsikiliza tu.

“Kama ukitaka kuniona ninafuraha daima, nisaidie nimuoe Sabrina.” “Kwani mimi nimekataa! Ninachotaka upate mtu anayekupenda Jack, sio mtu ambaye atakutumia tu. Yaani awe ameshindwa huko maisha ndio ukawa wewe kimbilio! Mambo yakimnyookea mbele ya safari, anakukimbia.” “Sio Sabrina mama. Ninauhakika na Sabrina. Akiamua kusimama na wewe, au akisema ‘ndiyo’ kwako, hayumbishwi. Unakumbuka chuoni?” “Nakumbuka.” Mama Msindai akajibu. “Ule ndio wakati ambao nilimpenda Brina zaidi, mama. Japokuwa nilikuwa na sifa zote. Wengine wakinitetemekea, lakini Sabrina alinikataa sababu alikuwa kwenye mahusiano mengine, tena sio hata kwamba yalikuwa mahusiano mazuri, ila bado aliyaheshimu hakutaka kumsaliti mwenzie kwa ajili yangu.” Jack akaendelea.

“Sabrina ana msimamo, mama. Halafu kingine kikubwa, anaheshimu maamuzi yangu na anataka niwe na furaha. Amekuja kuishi na mimi hapa, akijua nipo na Pam kwenye mahusiano, akaliheshimu hilo japo alikuwa akitamani kama angerudisha miaka nyuma, wakati ule angekuwa hayupo kwenye mahusiano, akanikubali.” “Umejuaje Jack mwanangu?” “Ameniambia mwenyewe mama. Brina mwenyewe aliniambia tena hata kabla yakuniambia niendelee na maisha yangu hivi karibuni tena. Kuna siku alinitumia ujumbe, sema sikukuonyesha. Alikuwa bado yupo kwao. Aliniambia kama angekuwa na uwezo wakurudisha miaka nyuma, angerudisha mpaka siku aliyosema ‘ndiyo’ kwa mwanaume aliyekuwa naye siku mimi nikimtongoza chuoni, ili aseme kwake ‘hapana’, ili wakati ule mimi namtongoza, angekuwa hana mtu, ili anikubali mimi. Akaniambia kabisa, lakini hawezi tena, na anasikitika amechelewa. Nakumbuka sikuujibu ule ujumbe, na wala sikuuzungumzia hata na yeye mwenyewe, yaani leo ndio nakwambia wewe.” Jack akaendelea taratbu akimuaminisha mama yake.

“Na ndio baadaye nilipokuja kuwa naye kwenye urafiki tu wakawaida, ndio nikaja kugundua wakati ule akinikataa mimi sio kwamba alikuwa kwenye mahusiano mazuri sana. Lakini nilimsikia akikiri alikuwa kwenye manyanyaso makali sana huko kwa huyo mwanaume mwingine, lakini hakumsaliti mpaka yule kaka mwenyewe alipoamua kumuacha, ndipo Sabrina akachora mstari kwenye hayo mahusiano, hata yule kaka alipomrudia na kumuomba msamaha akitaka kumuoa, Sabrina alimkatalia. Lakini hakumsaliti. Sabrina anamsimamo mama. Akisema ‘ndiyo’ yake ni ndiyo, sio mbambaishaji. Ukiwa naye, unauhakika na mtu wa kusimama na wewe kwa hakika.” Jack akaendelea, mama yake akimsikiliza tu.

“Nampenda Brina, mama. Kama ukitaka kuniona nafuraha wakati wote, nipe baraka zako nimuoe Brina wangu. Ni mwanamke niliyekuwa nikimsubiria kwa muda wote huo, na wewe unajua. Tafadhali mama yangu.” “Lini unataka kuoa?” Mama yake akamuuliza. “Haraka iwezekanavyo. Sitataka harusi kubwa na ya garama sana. Tuna mipango mingi sana mimi na Brina, na yote hiyo inahitaji pesa. Hatutaki kupoteza pesa kwenye harusi wakati tunaweza kutumia hiyo pesa kusaidia maisha ya watu huku. Brina amepitia miradi mingi ya chama ambayo imekufa. Amenishauri mimi kama mwenyekiti wao, niifufue tena. Tumeshauriana njia ya kuifufua, tumepiga mahesabu tumeona tutahitaji pesa nyingi. Sasa najua watu ambao nitaomba michango yao kwenye hili la chama, ndio haohao nao tutawachangisha kwenye harusi. Sasa ndio maana tunaona tufanye kitu kidogo cha pesa ndogo kutoka kwetu sisi wenyewe. Kisha baada ya harusi tutafanya harambee kubwa ili kupata hiyo pesa.” Akamsikia mama yake anacheka taratibu. Akajua amegusa moyo wa mama yake.

“Sasa hiyo ndiyo roho ya uongozi. Kufikiria wengine sio wewe tu. Sasa hiyo harusi itafanyika huku au huko?” “Nafikiria huko nyumbani ambako ndugu wengi wapo huko.” “Umpigie simu na baba yako umtaarifu ili tuanze mipango. Umemwambia Junior?” “Nimezungumza naye, na yeye ndiye aliyenisaidia kutafuta pete ya uchumba. Na kuniambia nisisubiri tena. Nimwambie Sabrina kwa wazi ili nijue kwa hakika kama ni wangu au niendelee na maisha yangu.” Jack akaharibu bila kujua. “Kumbe umeshachumbia!?” Mama yake akaulizi kwa kulalamika akishangaa sana kwamba amepitwa!

“Sikujua kama Sabrina angekubali, mama!” “Sawa.” Jack akajua ameumia. “Sikutaka ujue kama nimekataliwa tena mama yangu. Nilijua ungeumia.” “Mimi ni mama yako Jack. Na hatujawahi kufichana jambo lolote. Unafikiri mimi ndio napenda kusikia tu habari njema kutoka kwako halafu mbaya uwe unaumia mwenyewe?” “Basi nisamehe mama yangu. Sitaki kukuudhi na sitaki tukosane hasa kipindi hichi ninachotaka kuoa. Si unakumbuka ulivyokuwa unataka nioe?” “Naona mambo yenyewe yameanza kwa vificho vificho! Nakuwa kama mtu wa pembeni tu!” “Mama!” “Naelewa, wala silalamiki. Nishaelewa kuwa mambo ya muhimu kama kuchumbia, unamuhusisha kaka yako. Mnaenda kutafuta naye pete. Mimi ambaye nilikuwa nakuombea, na kukutafutia wasichana, japo umekuwa ukiwakataa, na sikuwahi kulalamika wala kuchoka, ukaniacha, nakuja kusikia tu kwamba umechumbia! Tena kwenye stori tu! Lakini naelewa.” Jack akajua kumeshaharibika, si kitu kidogo kama alivyodhania mama yake atachukulia.

“Kaka alisema safari hii niende umbali mkubwa zaidi mama. Hata sikuwa na wazo lakuchumbia. Alinikuta hotelini na mwanamke.” “Pam?” “Si unaona hata Pam unamjua! Mimi sikufichi mama yangu kipenzi.” “Mmmh!” Akaguna kwa kulalamika. “Mama! Nilimuaga Brina nakwenda mapumzikoni na Pam! Hebu fikiria mama yangu, halafu nije kumuomba kumuoa! Sikujua kama angenikubali.” “Narudi kwenye pointi yangu ile ile Jack. Wewe ndio katoto kangu kamwisho. Sitakiwi kusikia mambo kutoka kwa watu. Mimi ndio natakiwa kuwaambia watu mambo yakiziwanda wangu! Sio vinginevyo.” “Nisamehe mama yangu kipenzi. Nimekosa.” Jack akambembeleza hapo kama dakika tano mbeleni ndipo marafiki hao wapenzi wakapatana.

“Kuna kitu kingine nitakuja kukwambia mimi mwenyewe siku ya jumamosi. Hicho nichamuhimu sana. Nataka nikwambie tukiwa tunaangaliana machoni.” “Ni nini?” “Mama Msindai!” “Nidokeze tu.” “Hapana mama. Nataka kukwambia nikiwa nakutizama hivi. Sio kwa simu.” “Basi mimi sitakaa kwa amani. Nitakuwa nikiwaza tu. Mpaka jumamosi kote huko!” “Mama, kwaheri. Nitakuona jumamosi.” “Nikupikie nini ukija?” “Nina hamu na ndizi za nyama. Weka nazi nyingiii.” Mama yake akacheka, wakaagana.

Jack kwa baba yake.

K

wa baba yake hakuchukua hata muda mrefu. Akampongeza sana na kumwambia itamuongezea heshima kwenye jamii. “Hata mtu akitaka kukupa majukumu mazito, anakuwa na imani na wewe kwa sababu anakuona umekuwa mtu mzima. Ni uamuzi wa busara sana.” “Asante baba. Lakini nataka kuoa hivi karibuni. Ndani ya miezi miwili.” “Kwa nini haraka hivyo!? Umeshamfahamu huyo mwenzio!?” Hapo Mzee Msindai akashituka kidogo. “Tokea nipo chuoni nilikuwa naye na tukaendelea kuwasiliana. Kwa hiyo namfahamu vizuri tu.” “Ooh! Kama ni hivyo huna sababu yakuendelea kusubiri. Nitazungumza na Junior, ashauri tufanye nini kwa harusi hiyo ya muda mfupi, lakini iwe nzuri.”  Mzee huyo alishamjua Jack na mama yake. Akajua jambo litakapomfikia yeye, basi limeshapita kwa mkewe na lina baraka zake. Hata akitaka kupinga, mkewe hawezi kukubali. Lazima atamlazimisha mpaka hilo jambo la Jack alipitishe, lakini si kwa watoto wao wengine. Na ukimsikia huyo mama akisema, ‘mtoto anataka au mtoto amesema’. Familia nzima wanajua anayezungumziwa hapo ni Jack.

Mzee Msindai hakuwa na mengi sana. “Asante baba. Na mimi nitakuja huko jumamosi.” “Hiyo itakuwa vizuri, ili tuzungumze na kupanga pamoja.” Wakazungumza kidogo tu, wakaagana. Akawa amemaliza kwa wazazi, kwa upande mmoja kuwataarifu juu ya harusi tu wala si ujauzito wa Sabrina ambao si wake. Lakini mama yake alishaanza wasiwasi juu ya Sabrina! Jack akajua kutakuwa na ugumu zaidi atakaposikia ni mjamzito. Jack akabaki akiwaza hapo kwenye kochi, Sabrina chumbani.

Kwa kaka yake.

B

aada ya kujiuliza na kujijibu kwa muda mrefu pale, akaishia kujiambia nilazima amuoe Sabrina tu. Akaweka hasara na faida za kumuoa Sabrina akiwa na mwanae, faida zikazidi. Akajiambia mvua inyeshe jua litoke, atamuoa tu Sabrina. Akaamua  kumpigia simu kaka yake ili kumtaarifu kila kitu na malalamishi ya mama yake. Kaka yake akacheka. “Mama hataki ukue yule! Na wala hataki kusikia umekua! Anakuona kama mtoto wakulilia nyonyo, ambalo analo yeye tu. Kila kitu umlilie yeye kwanza, kiziwanda wake. Na hataki akushiriki na yeyote yule!” Jack akaendelea kucheka. “Lakini naomba swala la Brina kuwa mjamzito naomba hilo nimwambie mimi kwanza. Anaweza kuanguka kwa mshituko.” “Kabisa. Ni heri akusikie mwenyewe. Mimi sitakuwa na maelezo yakutosha.” Wakanyamaza kwa muda. “Nampenda Brina, kaka yangu. Ananikamilisha kwa kila eneo la maisha yangu.” “Hata kama ni harusi ya haraka, lakini tutakuandalia harusi nzuri tu, mshindwe wenyewe.” Jack kusikia hivyo, akafurahi sana. Alimjua kaka yake. Akisema atafanya jambo. Huwa anasimamia mpaka likamilike. Akamshukuru na kukata.

Kili Kazi Na Malipo Yake.

J

ack akaamua kumfuata chumbani. Akamkuta amepiga magoti pembeni ya kitanda amejifunika na mto kichwani analia kimyakimya. Akasikia tu akivuta kamasi ndipo akajua analia. Akaenda kukaa pembeni yake. Kitandani na kutoa mto kichwani. “Naomba tuzungumze Sabrina.” Sabrina akajifuta machozi, lakini akabaki amepiga magoti vilevile akiendelea kujipangusa uso. “Haya maswali uliyoyasikia, hatuwezi kuyaepuka. Yatakuja na yatataka majibu. Leo nimebabaika sana kwa kuwa sikutegemea swali kama hilo kutoka kwa mama ambaye ananifuatilia kwa karibu sana. Kila siku asubuhi nikitoka hapa nyumbani kuelekea kazini, lazima kumpigia na kumsalimia kumtaarifu nimeamka salama na ninakwenda kazini.” Sabrina akabaki akisikiliza.

“Maswali yake kwangu ambayo najua itakuja kuwa ngumu sasa hivi ni kama yale ya mama kwa mtoto wake wa miaka 5. ‘Umekunywa maji, na kwa kiasi gani? Umekumbuka kuweka chandarua? Umekumbuka kubadilisha mashuka weekend hii? Umekumbuka kupata kifungua kinywa? Kuna vumbi sana huko, usisahau kunywa maziwa.’ Hayo ndio mahusiano niliyonayo na mama hata nilipokuwa chuoni ilikuwa hivyo hivyo. Anaweza akaja hapa Singida kunitembelea ofisini, anaanza kunifunga tena kamba za viatu miguuni.” Sabrina akashangaa sana. “We Jack!” “Wewe utamuona tu. Mpaka kina Ibra wanamfahamu na ilibidi niwaambie wamzoee tu. Pale chuo alikuwa akija, anaanza kunichomekea shati vizuri, tena mbele za watu.” Sabrina ilibidi acheke tu.

“Sasa unasemaje?” “Namuacha tu. Sasa nisemeje? Na anafanya bila hata kujijua. Upo mbele ya marafiki, unamtambulisha, anaanza kukutengeneza hiki na kile kama mtoto mdogo. Ilimradi mikono yake iwepo mwilini mwangu. Zawadi zake ndio utachoka. Yeye ndio atakumbuka kuninunulia soksi na nguo za ndani. Sasa amenilemaza hata sijui kununua hivyo vitu. Leo ananiambia ameninunulia soksi, ila alisahau kunipa. Sasa hapo inaweza ikawa kweli au nia nirudi tena nyumbani, anione tu.” Sabrina akajua hapo kazi atakuwa nayo.

“Akipiga simu, ile tu nikipokea simu nikimwita mama, anajua kama nipo sawa au la. Na hajui kuachia jambo, atakukera mpaka umwambie kila kitu. Kwa hiyo anafahamu asilimia 89 ya kila kinachoendelea kwenye maisha yangu. Siwezi na sijui kujificha kwake. Mbaya zaidi akiwa amenipigia nikiwa na hasira, au jambo limeniumiza, ndio najikuta namwambia yeye kila kitu kama kujituliza. Kwa mara ya kwanza tokea nazaliwa ndio leo naanza kuona athari yake. Narudije nyuma na kutengeneza malalamishi yangu juu yako Brina, kuwa hunipendi mimi?” Sabrina akaumia sana.

“Kumbe ulishamwambia kama sikupendi?” “Wala sitakudanganya Sabrina. Ulipobadili mpango wa kuja huku, nikiwa nimeshamwambia mama naandaa nyumba Brina anahamia Singida, nataka kuweka mazingira yakumkaribisha aje aishi kwangu. Nikahangaika usafi wanyumba. Hata hii rangi unaona ya ukutani nilipaka upya kwa ajili yako. Nikabadili nyavu za madirisha na kuweka hayo madirisha ya Aluminium unayoyaona na kujengea mafeni ya juu kila chumba. Yote hayo mama alijua nafanya kwa ajili yako. Kuja kupata ujumbe wako eti huji tena, umeamua kuanza maisha yako huko, mimi niendelee tu na biashara nisikusubiri tena, ikaniumiza sana. Nilishindwa hata kulala Brina. Nilikuwa nikikusubiri online usiku kucha angalau kukupata nikuulize ni nini nilikosea! Nini kimekufanya ubadili mawazo kwa kazi itakayokuja kuisha, na huna kazi nyingine! Kumbe mimi nasubiri huku, wewe ulishani block! Mimi sijui kama umeni block, najua upo matatizoni. Ndio Ibra akanielewesha kuwa mtu akikublock Whatsapp huoni profile picha yake kama alikuwa anayo, na simu ukipiga humpati.” Sabrina akajisikia vibaya sana. Akainama.

“Sasa siku ile uliponitumia ujumbe na kunibock, katika hangaika hiyo ya kukusubiri online, mama naye akaniona nipo online usiku, akanipigia. Nikamueleza ukweli, kuwa nimekata tamaa na nimejua wewe hunipendi kimapenzi labda urafiki ambao nikionyesha naingia ndani sana ni kama nakuogopesha unanikimbia. Nikazungumza na mama karibu usiku kucha maana Ibra alishaniaga akasema yeye analala sababu ya kazi kesho. Nikakaa na mama kwenye simu mpaka nikalala. Simlaumu anapoonyesha wasiwasi sasa hivi. Anayo haki yakuhoji. Na lazima niwe na majibu ya wazi. Mama anayo haki Brina. Nilimtwisha malalamiko yangu, sasa hivi hata kama nimetengeneza na wewe, siwezi kumpuuza tena.” Sabrina akakaa.

“Naelewa Jack, na wala sikulaumu. Makuzi yako na yangu yapo tofauti sana. Wewe umelelewa ukiwa karibu sana na familia, zaidi mama. Mimi imekuwa tofauti. Kadiri nilivyoendelea kukua, ndivyo nilivyozidi kuwa mbali na familia, zaidi mama. Nimekuwa ni mtu ambaye ananilalamikia sana. Amekuwa akinipa maneno machungu mno jinsi ninavyomkatisha tamaa kwenye kila kitu. Nafikiri nilikwambia jinsi alivyoumia baada yakujua sipo tena na Emma ambaye alijua nikimaliza chuo pengine angenioa. Bila kujua sababu, mama aliumia sana na kulalamika kwa wazi hata mbele za wale wadogo zangu wa kiume ambao kwanza niliona ni wadogo zangu, pili ni wakiume Jack. Anataka kuwafundisha nini kwa kuachwa kwangu! Sasa ikawa hivyo hata kwa Sabina na yule kaka yangu. Wakipiga simu hizo ndio zikawa habari wanazopewa. Nimesoma kitu cha ajabu, na mwanaume pia nimeshindwa kumtunza. Akawa akinilalamikia kwa kila mtu, hakuna ninachoweza kufanya vizuri kwenye maisha na ikawa sasa nafikiri imemuingia akilini, hata nimfayie kitu gani kizuri pale nyumbani, hawezi kushukuru kama akijua ni mimi nimefanya, lazima atatoa kasoro tu.” Sabrina akaendelea taratibu tu.

          “Hiyo kitu ikawa inaniumiza sana na kunimaliza nguvu kupita kazi nyingi nilizokuwa nikifanya pale nyumbani. Nikawa sina kimbilio, na simu kama nilivyokuwa nikikwambia wakati ule ulipotaka kuniletea simu. Ilikuwa napata mawasiliano pale wadogo zangu wanapokwenda shule. Kwa hiyo ninapokuwa nao nyumbani, wale wadogo zangu ambao nao wakajifunza kunidharau kwa kejeli kutoka kwa mama aliyekuwa akinifananisha nao. Kuanzia matokeo shuleni, kuwa wao wanaakili kuliko mimi na utendaji kazi wao pale nyumbani na uwezo mkubwa wakufikiria walio nao kuliko mimi mjinga.” “Sabrina! Alikuwa akikwambia hivyo!?” Jack akaumuuliza kwa kuumia.

“Kabisa Jack. Tena si kwa kujificha, mbele yao. Tusi lake kubwa ilikuwa, ‘mjinga kabisa wewe’. Kwa hiyo hata wale wadogo zangu walikuwa wakiniita mjinga. Utasikia wakiniambia, ‘wewe si mjinga tu’. Hapakuwa na heshima hata kwao. Sasa ukumbuke hapo wao ndio nilikuwa nikiishi nao. Baba kunichapa hata mbele yao lilikuwa jambo la kawaida sana tu. Nikitumwa sehemu nikachelewa, au ng’ombe wakimwaga maziwa, watasahau yote niliyofanya mazuri siku hiyo, nitachapwa mbele ya wale watoto, tena na matusi juu. Zaidi nikichelewa kurudi nyumbani hapo baba alikuwa akinitandika, anasema nimeanza mambo ya wanaume, nataka kuleta watoto pale ndani wasio na baba. Nilikuwa natoka kwa shida Jack! Hata kusuka ilibidi nijifunze kujisuka mwenyewe, tena usiku maana kwanza sikuwa na hela, pili muda sikuwa nao. Kwahiyo ukisema niende nikimaliza kazi, ni jioni. Kusukwa mpaka nimalize, tayari giza limeshaingia, nikirudi nyumbani ni kuchwapwa.” Sabrina akainama.

“Unaona huu upande wa kushoto? Kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Nywele zake ni nusu ya upande huu kwa kuwa nilichelewa kurudi nyumbani, nilikwenda kusukwa rasta za mabutu, siku karibu na ya chrismasi. Nikasema angalau siku hiyo na mimi nipendeze. Kina Sabina na kaka walikuwa na wao wanakuja nyumbani. Ndugu wa vijijini walikuwa pia wanakuja. Nikasema na mimi angalau nijipendezeshe. Sikuwa na wasiwasi kwa kuwa kulikuwa na watu kutoka kijijini, nasaidiwa kazi pale. Nikatoka kwenda kusuka. Rasta huwa zinachukua muda mrefu kusukwa. Basi kipindi hicho nikasema ndio kipindi muafaka kwenda kusukwa kwa kuwa kuna watu pale nyumbani, kama kuna kitu chakufanywa, basi watatumwa wao. Lakini ikawa kinyume kabisa. Sitasahau jinsi nilivyodhalilika siku ile Jack. Nilitoka nyumbani mchana, nikarudi saa moja usiku.” Sabrina akainama, akamuona anacheka kwa kuguna.

“Nilipokelewa mlangoni. Ngozi ya kichwa ilikuwa ikiuma sababu ya kuvutwa wakati wakusukwa. Mama akanishika kichwa na kunivutia ndani. Mbele ya wadogo zangu na wageni. Jack, nilichapwa kama mbwa. Hapo hapo akanikata huu upande wote, akaniambia anione sasa kama nitapata sababu ya kwenda kuzurula. Hapo wadogo zangu wanacheka na kushangilia.” “Haiwezekani Sabrina. Kwani hukuomba ruhusa?” “Jack, natokaje kwenye ile nyumba bila kuomba ruhusa? Tena sio mimi, Sabina ndiye aliyeniombea. Niliomba simu ya mama mdogo, alikuja hapo nyumbani kwa ajili ya sikukuu, nikampigia Sabina. Nikamuomba hela ya kusukwa, na nikamuomba aniombee ruhusa kwa baba, nikasukwe. Tena baba akiwa na mama wakasema, kama nikimaliza shuguli zangu zote, ndio niende. Nikafanya shuguli zangu zote, ndipo nikaenda. Kaka anakuja nyumbani na Sabina, wanakuta upande mmoja nywele zipo nusu. Na mimi pale nyumbani ndio wananisifia kwa nywele nzuri. Zinakuwa kwa haraka, halafu laini. Nikifumua hizi nywele utaona. Ni ndefu sana japo zimepishana. Sabina akashangaa sana. Akaniuliza kwa nini nipo vile! Wale wadogo zangu wakawa wanasimulia pale mbele za watu huku wanacheka. Nakumbuka kaka alikasirika sana nakushindwa hata kuvumilia. Akaongea palepale tena kwa kugomba sana. Ilibaki kidogo awachape wale watoto ila akawakemea sana. Lakini na yeye siku zilipoisha akaondoka kama Sabina ambaye ni kama Mungu mtu pale nyumbani, nikaachwa na watu walewale, maisha yangu yakaendelea vilevile.” “Daah!” Jack akashangaa sana.

“Tuache hayo, lakini ile hali ikanifanya nianze kumuuliza Mungu ni kwa nini mimi anaruhusu kudhalilika kiasi hicho na nipitie hapo? Katika kuendelea na hayo maswali, ndipo nikakutana na Yesu. Jack, Yesu yupo. Mwenye nguvu na mamlaka yake.”  Mpaka Sabrina akaanza kutokwa na machozi. “Nikataka kumfahamu Mungu aliyeniumba. Yale manyanyaso, yakanifanya nitumie bibilia ya baba, nikaanza kumsoma na kutaka kumtambua Mungu. Kumbuka sikuwa na rafiki wala mawasiliano mpaka wale watoto waende shule ndio angalau ulikuwa unaweza hata kunipata kwa simu tena mama akifurahi. Nikimuudhi, ujue napokonywa simu. Siwezi kukaa nao sebuleni kuangalia tv, ni jikoni kama nimemaliza kazi. Hapo ndipo nikakutana na Yesu. Bila kuhubiriwa na mtu, mimi mwenyewe tu.

Anyways.” Sabrina akajifuta machozi vizuri. “Mambo hayakubadilika pale nyumbani. Lakini nikapata nguvu za ajabu sana Jack. Furaha ambayo sikuwahi kuwa nayo. Amani na utulivu nikimsubiria Mungu bila malalamiko huku nikimkumbusha ahadi zake kwenye bibilia juu yangu. Sikumwambia mtu kitu kinachoendelea kwangu, lakini nikawa najitahidi kufanya kazi bila kuchoka. Lengo likawa limebadilika sasa, nafanya kwa bidii ili Mungu anione wala si wazazi tena. Hata wakinitukana, nikawa sina shida. Ilimradi nimefanya kwa uaminifu, Mungu wangu ameniona, nikawa sijali. Ila nilimwambia hivi Mungu, kwa kuwa nafanya sana kazi. Nataabisha huu mwili, nikamsihi Mungu asiruhusu kuchapwa tena. Na kweli Jack, ikawa kama muujiza kwangu. Wakati mwingine mama au baba unakuta ametoa kabisa mkanda kiunoni ili anichape, moyoni naanza kumlilia Mungu na kumkumbusha, basi unashangaa baba anagari kunichapa. Anarudisha mkanda wake kiunoni, au kama ni mama, ananitukana tu, nakuishia kutupa fimbo.”

“Napo hayo maisha yakaendelea, nakumbuka nikamuomba tena Mungu anisaidie kulainisha mioyo ya wazazi, waniruhusu kwenda kwa Sabina, angalau nikapumzike kidogo. Nayo hiyo ni habari ingine, tuache. Ila Mungu akafanya. Lakini nilipofika kwa Sabina, ili nipumzike, rafiki yake ambaye ni mke wa Tino aliponiomba nikamsaidie kukaa na mumewe. Nikisema kukaa, namaanisha kukaa haswa. Hakutaka hata nimguse Tino. Alikuwa amemfungia kama mnyama. Alinifungulia tu mlango kunionyesha alipomfungia, yeye mwenyewe yule dada alikimbia. Chumba kilikuwa kinanuka Jack! Sio kinyesi tu, yaani kama kitu kilichooza. Lela alikuwa anakwenda kupumzika na mwanaume wake, na kina Sabina. Sasa ili watu wasimuone amemtelekeza mumewe, akataka mtu wakuwepo pale ili tu awaambie watu hajamuacha Tino peke yake nyumbani, amemuachia mtu wakumuhudumia. Lengo lake sio Tino apone, ilikuwa ni aendelee kuwa mdhaifu vile vile ili yeye aendelee kula pesa ya Tino.” Sabrina akamuelezea mkasa wa Lela na Tino kwa kifupi ila kwa undani, Jack akabaki ameshangaa na kuumia sana.

“Sasa kwa nini naye Tino alioa mwanamke wa namna hiyo akijua hana mapenzi ya dhati kwake?” Sabrina akacheka. “Unamuona hivyo alivyo Pam?” Jack akanyamaza asijue kwa upande upi. “Basi uzuri aliokuwa nao Pam, ndio kama Lela, sema yeye Lela ni mwembamba zaidi juu halafu Pam mwili wake mnene zaidi. Mweupe kama anakwenda kuwa muarabu hivi, halafu mtoto wa mjini anayejua kujitengeneza. Ukimwangalia Lela, hutachoka kumtizama Jack. Mzuri kama hivyo Pam, na maneno mengi hivyo hivyo kama mapacha sema angalau Pam huwa angalau akiteleza anajirudi, ila si Lela. Lela ni mkatili, katili ambaye hana aibu. Msafi na anapenda vitu vizuri. Nafikiri hapo ndipo walipoendana na Tino. Tino ni msafi kwa kumwangalia. Kitu kisocho na hadhi hanunui wala hamiliki. Hiyo nyumba yao ni safi Jack, imepangiliwa mpaka vijiko vipo vimewekwa kwa mstari na kwa ukubwa wake. Masufuri na miko vimepangwa hivyo hivyo.” “Kama wewe huko jikoni?” Sabrina akacheka. “Ilibidi niige Jack. Wewe mwenyewe utaona aibu jinsi kulivyo pangiliwa. Kila kitu kipo sehemu yake wakati wote. Ukiingia ndani kwao, hakuna mbu wala nzi, utafikiri upo nchi nyingine. Wewe fikiria mpaka bafuni na chooni ni pakavu!” Wakacheka.

“Sasa aliponiacha Lela huku akiniambie nisihangaike kabisa na mumewe, mimi nikaingiwa huruma. Nikajiambia Mungu ananiona pale nilipokuwa nimekaa tu sebuleni wakati kiumbe chake kinaangamia ndani. Nikasema hapana. Nipo pale kwa sababu. Mungu hakuwa amenipeleka pale kwa bahati mbaya. Ndipo nikaingia kwenye kile chumba na kuanza kumsaidia Tino. Mashuka aliyokuwa nayo kitandani yalikuwa yameganda kwenye vidonda. Uzuri au ubaya godoro liliwekwa plastiki. Kwahiyo uchafu na unyevu haukuwa ukienda kwenye godoro, mashuka yanafyoza kinyesi na mikojo, vinaishia mwilini mwake. Alijawa madonda ya kuungua, sina jinsi nikakueleza ukaelewa. Halafu Tino alizaliwa na mama mwitaliano. Kwa hiyo ni mweupe haswa, na ana manywele kila mahali. Nikisema kila mahali, ni mwili mzima.”

“Nikaanza kazi yakumsafisha yeye kwanza, na kitanda chake. Alikuwa na kila kitu lakini hakuna wakumsaidia kuvitumia. Alikuwa akitetemeka baridi, maumivu na homa ilikuwa juu sana. Nilikuja kumtoa manywele mwilini, nahisi yalijaa mfuko. Hapo ni kuanzia shingoni tu mpaka unyayo. Maana ananywele mpaka vidoleni.” Jack akashangaa kidogo. “Alikuwa akitisha Jack, kama mnyama wa porini. Kama una roho ndogo, Tino niliyekutana naye mimi siku ya kwanza, usingemsogelea. Alikuwa akitisha sana. Nikaanza kumpa chakula na kumuhudumia bila kumsikia mkewe aliyeniambia nisihangaike naye yupo mtu huwa anamuhudumia, kumbe muongo. Nimekaa hapo nikimuhudumia Tino bila kuona yeyote mpaka aliporudi siku ya jumatatu usiku maana nilikwenda pale kwao siku ya jumamosi, na yeye akaondoka siku hiyohiyo na kurudi jumatatu usiku. Ninachotaka kusema, niliendelea kumsaidia Tino si kwa ajili ya Tino mwenyewe, ila Mungu. Muda wote huo namuhudumia Tino, wala hakuwa akizungumza.” “Kwa nini?” Jack akauliza.

“Tino ni wale vijana walioumbwa na Mungu wazuri sana kwa muonekano. Halafu anajipenda na kujijali kupita nitakavyokwambia hapa. Stoke aliyokuwa ameipata, ilimfanya mdomo upinde. Alikuwa akiongea mate yanamwagika, halafu maneni yanatoka kwa shida. Nafikiri hiyo ikamkatisha tamaa yakuzungumza, halafu hakuwa na nguvu kabisa sababu ya ukosefu wa chakula. Mimi mwenyewe nilikuwa nikimuhudumia siijui sura yake anafananaje. Alijawa ndevu uso mzima na nywele.” “Hata hukuona picha!?” “Huwezi amini Jack, hapakuwa hata na picha. Nilipomuuliza mkewe hakutaka kunipa akanijibu hata hajui zilipo. Nilikuja kumfahamu sura alipopata nafuu, nikaamua kumpeleka kwa kinyozi kwa kuwa alikuwa na mba ule ambao ngozi ilikuwa inatoka kichwani. Ndipo nikashangaa uzuri wa yule kijana.” Sabrina akafikiria kidogo, Jack akimtizama.

    Anyway, turudi kwenye hili ninalotaka kukwambia. Nilipokuwa nikimuhudumia Tino, nilifanya kama nafanya kwa Mungu wangu kwa asilimia 100. Hapakuwa na mapenzi wala sikujua kama kunanitakachopata. Kama nilivyokwambia tuliachwa peke yetu hata pesa aliyonilipa mkewe, nilianza kuitumia kwa matumizi ya pale nikiwa sijui atarudi lini, huku nikimuomba Mungu na pale asiniache. Tino apone, aendelee na maisha yake na mimi nije huku kwako. Na ninaomba niwe mkweli Jack, lengo lakunileta huku kwako tokea mwanzo ilikuwa nikuja kujikwamua kiuchumi wala si mapenzi.” “Nilijua hilo.” Jack akajibu.

“Kabisa. Kwanza nilishakuonea aibu. Hata Tino nilimwambia. Nitakwenda kwa Jack sio kwa mapenzi kwa kuwa kwanza nakuonea aibu. Nilikukataa vibaya sana. Halafu nikajiuliza swali kama alilokuuliza mama yako. Na Tino nikamwambia. Jack ni mtu mzuri sana na mstaarabu mno. Nikamsimulia jinsi ulivyonisaidia bila kinyongo chuoni nilipoachwa na Emma kwa fedheha kubwa vile. Ukanirudishia heshima pale chuoni, ukahakikisha namaliza chuo. Nikamwambia Jack anastahili mwanamke atakayempenda kwa dhati na kumuheshimu. Nikamwambia Tino, hata iweje, siwezi kurudi tena kwa Jack na kumwambia nampenda! Nikamwambia atajua namdanganya. Ni kwa nini nilimkataa tokea mwanzo, na kwa nini sasa hivi nirudi tena nimwambie nampenda? Nikamwambia tokea chuo aliponisaidia, nilishajiambia hata ikitokea anaachana na yule msichana wake wa pale chuoni, sitajisogeza sababu nilishamkataa hata yeye alishaendelea na maisha yake. Anao wasichana wake.” “Lakini mwishoni nilikukaribisha na kukwambia zile hisia nilizokuwa nazo chuoni bado zipo, Brina! Au hukuelewa?” Jack akauliza.

“Ni kama nilielewa, lakini kwanza nilijikatisha tamaa Jack. Nikasema labda hisia zakutaka kunisaidia tu au..” “Hisia za kutaka kukusaidia! Come on Brina!” “Najua Jack, lakini kumbuka na aibu pia. Na kujiuliza na kujiona sitakutendea haki. Kumbuka hapo nilishamuona Lela na Tino wanavyoishi, tena hata Tino nilimwambia. Jack ni mtu mzuri sana. Nasita kukurudia sasa hivi sababu ya ugumu wa maisha na mazingira yangu nikiogopa kurudi nyumbani. Nikaja kwako nikakukubalia unioe, halafu badaye nikakutenda kama Lela wake! Nakumbuka mpaka Tino akanyamaza. Nikamwambia ingekuwa mtu mwingine, wala nisingejivunga, ila sio Jack. Nikamwambia Jack namthamini sana, siwezi kuja kumuumiza. Na yeye baadaye nilipomueleza juu ya kilichompata yeye sitaki kikupate na wewe kupitia mimi, akasema anaelewa aina ya ndoa aliyo nayo. Ni kweli.”

Anyway. Tukaendelea na Tino mpaka tukaondoka naye pale nyumbani. Tino akanipa kitu pekee kilichonifanya kumkimbilia Mungu, na baadaye kumuacha huyo Mungu.” “Kitu gani?” Jack akauliza. “Kunihitaji kwa hali ya juu. Tino alinionyesha hawezi kuishi bila mimi.” “Ambayo ilikuwa ni kweli.” “Kweli kwa uhalisia kuwa alinihitaji nimtumikie sio kama nilivyojiaminisha Jack. Tino alikuwa akinililia nisimuache popote. Hakuwa akitaka niwe naye mbali hata kwa nusu saa! Akanipa kile ambacho hata Emma hakuwahi kunipa. Tino akajaa kwenye maisha yangu na kuniahidi kuwa na mimi daima. Akasema hatutashindwana. Yeye sio mbishi japo ni mkubwa kwangu na amenitangulia kimaisha. Tino alikuwa akiniweka kifuani Jack. Usiku nilale akiwa ananisikia. Tukikaa, anataka japo nimshike. Mpaka analilia penzi langu! Nikalewa, nikamsahau Mungu wangu, nikarukia mapenzi nikijua wazi Tino ni mume wa mtu, na bado hajaachana na mkewe! Na wanayo ndoa ya kanisani.”

    “Haikuchukua muda mrefu kubadilika au uhalisia kujitokeza. Lela akarudi anamtaka mumewe, Tino anataka mali. Mtoto niliyebeba akaonekana itamsababisha asishinde kesi na kumchelewesha maishani. Hana muda na mtoto kama nilivyokwambia alikuwa na mipango yake. Haya, mimi naye sikuwa muhimu kama nilivyodhania. Mengine unayajua, nilikusimulia. Ninachotaka kukwambia Jack, kipo kitu Mungu alinipa, na nikakipoteza kwa Tino. Hakuna mtu atabadilisha maisha yangu isipokuwa mimi mwenyewe. Matusi ya mama yangu mzazi na maneno yake mazito kama fungu la kokosa, yalinifanya nikarudi kwa Mungu nikamsihi anisamehe pale nilipokosa, anisamehe na anibatilishie kile mama yangu anatamka kwangu. Mimi sio fungu la kukosa. Nikamkumbusha Mungu maandiko yoote aliyoahidi juu yangu. Na wote tunamjua Mungu si mwanadamu hata aseme uongo. Ahadi zake ni kweli daima. Hajawahi kushindwa hata siku moja, na wala hana mpango wakuja kuanza kushindwa kwangu. Mimi ndio tatizo Jack.” Jack akabaki akimsikiliza.

“Nikikusimulia jinsi nilivyoishi na Emma, unaweza kudhani nilikuwa mjinga. Kuna mambo alikuwa akinifanyia yule kiumbe, mpaka naona aibu kusimulia. Ni manyanyaso ya namna yake. Niliacha anitumie na kuninyanyasa vile atakavyo huku nikikataa wanaume wazuri kama nyinyi. Nikajifunga kwake tu, kama niliyechukuliwa ufahamu. Haya, kama ambaye sina akili, nikijua wazi kabisa nafanya kosa, nikashindwa kusubiri malipo yangu kutoka kwa Mungu baada yakufanya kwa uaminifu kwa Tino ambaye ni mtoto wake, nikaamua kujipunja kwa kujilipa mimi mwenyewe. Nikaona Mungu atanichelewesha, nikajilipa mwenyewe. Nikajilipa kirahisi sana, na shetani akapata mlango hapo hapo wakunifedhehesha.” “Acha kumwita mtoto ni fedheha Brina. Usirudie hiyo kauli.” Mpaka Sabrina akalia.

“Hapa nilipo Jack, sipo kwa kuwa nina mkosi wala kauli za mama yangu ni kweli kwangu. Naanza kuamini natoa mwanya mimi mwenyewe wa kukosea. Somo nililofundishwa kwa Tino, halijatosha, jana nikiwa hata sijatengeneza kwako, hatujapanga, wewe si mume wangu Jack, lakini ona nilivyokimbilia mapenzi! Natoa wapi kibali cha kulala na wewe wakati wewe bado si mume wangu!?” Jack akashituka sana hakujua kama kibao kitakuja kupindukia kwake.  “Nani amenikabidhi wewe kama ni mume wangu? Baraka za Mungu nimezipata wapi katika hili? Wakati gani nimerudi kwa Mungu nikamuuliza Mungu juu ya hili? Sio wewe uliyenitoa Moshi, Jack. Ni Mungu. Nilikaa pale ndani siku tatu bila kula wala kunywa, nikimlilia Mungu anisamehe na anitoe kwenye ile hali. Nikamlilia Mungu nikimsihi aniguse tena, anipe tena nafasi ya nyingine na nikamuahidi safari hii nitaitumia vizuri.” Sabrina akajifuta machozi.

Ndoto ya Sabrina Akiwa Shidani, Mfungoni….

“Siku ya tatu kwenye mfungo wangu, nikiwa na hili tumbo usiku nikiwa nimelala nikaota ndoto hii. Nilikuwa nimekodisha gari kama hiace. Daladala kwa matumizi yangu mimi. Sasa nikawa natumia na nimepewa na dereva. Dereva anafanya kile ninachomuamuri kwa kuwa kwa wakati ule gari ilikuwa chini ya mamlaka yangu. Sasa kufika maeneo kama ya pale fire, Dar. Nikawa tumeegesha hilo gari. Wakaja kina mama wakawa wanapanda. Mimi nikawaambia shukeni, hili gari sio kwa bishara, nimekodi kwa matumizi yangu. Wakanishawishi sana huku wakitia huruma, kuwa niwapeleke mpaka hospitali ya Muhimbili, watanilipa. Nikagairi safari zangu na mipango, nikawapandisha kwenye gari huku nikijua navunja sheria. Haikuwa gari ya biashara, ila nikawapanga ili trafic wasituone ndani. Tukawapeleka mpaka Muhimbili, lakini njiani nikaamua kukusanya sasa pesa kwa kila abiria.” Sabrina akacheka.

“Kila niliyemsogelea kumuomba nauli, alinipa kikaratasi kimechapishwa na mamlaka kuwa hatakiwi kutozwa nauli. Wengine ni watoto, kwa hiyo ni wanafunzi, wengine eti ni watu wazima, ambao hawana kazi kwa hiyo eti mamlaka au serikali imewapa kibali cha kutotozwa nauli, wasafiri bure. Mmoja tu akanilipa, wakati basi lilikuwa limejaa watu. Nikawashusha nikiwa nimeumia sana, kuwa nimewapeleka na kuwafikisha pale halafu mimi sikufaidika! Ikaniuma sana, nikawa namwambia yule dereva, yaani nimelipwa na mtu mmoja tu tena aliyekuwa amekaa nyuma kabisa, wengine wote hawajanilipa! Nikahesabu garama niliyolipa kuwafikisha pale. Kutumia mafuta yangu, gari yangu na mpaka kuvunja sheria na sikulipwa ila mmoja tu tena ambaye alikuwa kimya kabisa! Nikashituka kutoka usingizini, nisijue maana ya ile ndoto kabisa.” Jack akabaki kimya akitafakari.

“Naweza nikawa sikupatia tafsiri nzima ya hii ndoto lakini mimi nikachukulia gari ni huu mwili wangu ambao ni kama tumeazimwa tu Mungu. Tukifa huu mwili tutauacha mavumbini. Huu mwili ni mavumbi Jack. Unatuponza tu kumkosa Mungu kwa mahitaji yake mengi yasiyoisha. Nikajiangalia maisha yangu na jinsi nilivyokwenda umbali mrefu kuwekeza kwenye maisha ya watu. Nikaanza na Emma. Sijisifii Jack, lakini nilimbemba Emma bila kuchoka. Siku uliponifuata pale chuoni, ukanikuta nimekaa peke yangu, nilikuwa nikimfikiria Emma na kule nilikopita naye bila kuchoka huku akininyanyasa sana. Kile alichokifanya pale chuoni kuninyang’anya vitu halikuwa jambo geni kwangu kufanyiwa na Emma. Sema alivuka tu mipaka kufanya hadharani, ila yupo rafiki yake alikuwa anajua ubaya anaonitendea Emma na kumvumilia mpaka akawa ananishangaa ananiuliza tatizo ni nini! Kwa nini namruhusu Emma kunitenda vile!”

“Haya, nikakumbuka jinsi wanavyonitenda nyumbani huku nikiwatumikia kupita kiasi. Wadogo zangu wakiwa likizo, mama alikuwa akiniambia niwafulie nguo kwakuwa wao wamechagua kusoma, basi mimi niwafulie, wao wasome au waende tuition, wakati mwingine nawafulia wao wakiwepo tu hapo hapo nyumbani hata hawasomi. Nikamkumbuka Tino. Vile nilivyomtoa kwenye hali ya kufa. Nikahangaika naye kwa garama kubwa nikitumia nguvu zangu, utu wangu, kwa garama kubwa mpaka yakumkosa Mungu wangu, na mwishoe ninaishia tu mimi kuumia na kukosana na Mungu ambaye ananipa faraja nikiwa naachwa peke yangu!”

“Nakumbuka baada ya hapo nikamuahidi Mungu kuwa, endapo atanitoa kwenye ile hali ya upweke, akanipa nafasi ingine tena, sitamkosea. Nikamlilia mno nikimuomba msamaha. Nikamwambia narudi kwake nikiwa kwenye hii hali ya ujauzito usio na baba, nikamwambia yeye ndio atakuwa baba wa huyu mtoto. Atanificha aibu yangu, nikamkabidhi huyu mtoto. Nikamwambia anitunzie, anisomeshee. Isitokee anataka kusoma popote, akakosa ada, kwa kuwa nitamdai yeye kwa kila hitaji la huyu mtoto. Amlinde asiugue na wala asinipokonye. Mimi niondoke kwenye huu ulimwengu nimuache akitumikia kusudi la kutungwa mimba yake. Nikamlilia sana Mungu, nikamaliza mfungo wangu, nikiwa sijapata jibu lolote.”

“Nakumbuka siku ya tatu yake, nikaamka nikiwa nakukumbuka mno. Nikalia kwa uchungu. Nikarudia ujumbe wa mwisho niliokutumia. Nikalia sana. Usiku nikasema niku unblock tu, angalau niione sura yako pengine nitalala. Maana nililia sana siku hiyo nikikukumbuka na kuumia kwa nini nimempoteza mtu mmoja tu ambaye alikuwa faraja yangu! Ndio nikaku unblock Whatsapp na kila mahali. Hapo ndio nikamuona Pam kwenye profile yako.” “Ile picha aliweka Pam mwenyewe, wala sikuwa nikijua kama ilikuwepo. Yaani wewe ulinishitua nakunifanya nijiulize ulitoa wapi ile picha, ndio baadaye nikagundua ulitoa kwenye profile yangu. Na nafikiri aliiweka jioni ileile nilipokuwa naye. Kwa hiyo hata uliponiambia hongera, nikaanza kujiuliza umejuaje habari za Pam na ile picha wakati sijawahi hata kukwambia! Ndipo wakati tuna chat nikaona hiyo picha.” Jack akaongea kwa kujitetea kidogo.

Anyway, wewe ukanikaribisha tena huku. Nilikataa sababu ileile. Nilikataa nini na sasa hivi nakubali nini? Aibu! Nikajiambia ni kama ninakufuata sasa hivi kwa kuwa nimeshindwa huko kwengine, nakukimbilia wewe! Nikasema hapana. Kwanza itakuwa nikukuchanganya tu, upo na mpenzi wako na mimi nakuja na tumbo langu! Nikamkumbusha Mungu kuwa huyu mtoto ni wake, siwezi nikampa mtu mwingine mzigo. Sasa kule kunifuata kwa nia ya kutaka uwe tu na mimi si kwa mapenzi, kuwa utanisaidia kutafuta kazi, nikakubali kiharaka bila wasiwasi.” Sabrina akakaa vizuri.

“Unakumbuka ule usiku umelala na mimi pale Moshi na kunikumbatia?” Jack akatoa tabasamu. “Mungu ndiye anajua Jack.” “Na mimi nataka kujua.” Sabrina akacheka. “Nilijuta, kwa nini sikukubali tokea siku ya kwanza.” Jack akacheka. “Kuna jinsi ulinishika Jack, nikapata ulinzi wa ajabu. Harufu yako ikawa kama ndio kitu pekee nilichokuwa nikikihitaji au nakikosa wakati wote. Kwa miezi yote niliyokuwa nikilia na kulala usingizi wa mang’amung’amu, lakini siku ile nikaanza kulala. Na kila wakati ninapokuwa na nguo yako nalala bila shida. Sikujali tena kuwa unaye mtu wako, ila ile kujua nitakuwa na wewe huku, kukanifanya nitulie kabisa, nikajiambia sitatembea kesho. Nikajiambia nitatembea kwa hatua, ila sio mbali na wewe na ndio maana nilikuwa tayari kutafuta chumba hapahapa Singida ilimradi niwe na wewe karibu lakini sio mbali na wewe tena. Nikajua wewe ndiye ninayekutaka na ndiye ninayekuhitaji. Nikamshukuru sana Mungu. Hata siku ile ya jumapili ndio ilikuwa sababu ya mimi kwenda na Emma kanisani. Nilikwenda kumtolea Mungu sadaka ya shukurani. Kimya kimya. Nikamwambia Mungu asante. Kwanza, kwa kunitoa kwenye ile hali ya upweke kule nikiwa sijui nitakwenda wapi, na kunirudishia Jack japo si kama mpenzi, lakini kama mtu wa karibu yangu sana. Nikatoa ile sadaka ya shukurani jana.”

“Wala si mwenzi uliopita Jack. Jana! Ni jana ndio nilikumbuka makuu Mungu aliyonitendea. Mimi Sabrina ninapakuishi, nina Jack, kama haitoshi, nina milioni za pesa benki! Zangu mimi! Natoka na kurudi nitakavyo! Sina wakuninyanyasa wala sina maombi yakutopigwa!” “Ndio maana ulikuwa mkali kwa Pam?” Jack akamuuliza na kumfanya Sabrina kuanza kucheka. “Nilijiapia sitafungua mwanya kwa yeyote kinitumia na kuninyanyasa tena Jack. Nilijiapia na kumwambia Mungu, chochote nitakachofanya sasa hivi, kiwe kwa ajili ya kujenga ufalme wake na nitamdai yeye wala si wanadamu wasio na shukurani na ambao wanabadilika.”

“Uliponikuta nimepiga magoti hapa nikilia, wala si kwa alilosema mama Msindai, Jack. Mama yupo sahihi kabisa. Hata mimi nilishajiuliza hilo swali. Mimi nilikuwa nikitubu Jack. Hakika nimemkosa Mungu wangu na nimejichukia kwa nini nakuwa narudia kosa mara kwa mara! Namtaka Mungu anifanyie nini ili nimtangulize yeye? Sijui imani yako Jack, lakini mimi najua kwa hakika tulichofanya mimi na wewe ni dhambi. Mimi si mkeo Jack. Mungu hajanipa wewe. Mbaya zaidi hatujaweza hata kujibu maswali ya watu wa karibu kama mama yako, tumekimbilia kitandani! Sio sawa kwako Jack.” “Mimi sijutii Brina. Ninahamu na wewe kupita nitakavyokwambia au tulivyofanya. Ndio maana imekuwa ngumu kukuachia asubuhi ya leo, mpaka uliponiambia njaa inauma. Unaladha ya ajabu sana! Matiti yako mazuri, natamani kukushika kila wakati ndio maana pale kwenye kochi nilikuwa sitaki ukae, unilalie tu ili mkono wangu uchezee hayo matiti yako.” “Bwana Jack!” Akamsukuma kwa nguvu.

“Mimi nasema ukweli kile ninachojisikia.” “Tunamkosea Mungu Jack. Usifikiri nakwambia hivi kwa kuwa sijakufurahia! Nimekufurahia sana tu. Hata sasa hivi nakutaka tena. Si unakumbuka mimi ndiye niliyemwambia hata dada Imani asije leo, nitamtafuta kesho?” “Nakumbuka.” “Kwa sababu nilitaka uendelee kunifanyia uliyokuwa ukinifanyia Jack, lakini si sawa. Kazi ya mwili ndio hiyo. Kutaka zaidi na zaidi, na wala hautosheki. Hali ninayojisikia hapa, ni kama ulinigusa miezi mingi iliyopita, nina ukame sana, kumbe asubuhi tu.” “Basi tuagane.” Jack akamgusa. Sabrina akamkwepa.

“Hapana Jack. Tunakaribisha laana na mkosi kwetu. Tuko kwenye wakati mgumu kuliko unavyodhani. Vita inayokukabili wewe sasa hivi, huwezi bila hekima ya Mungu. Na ninakuhakikishia Jack, neno, ‘nampenda Brina’ tu, halitoshi kwa familia yako inayokupenda na kukujali. Unamuhitaji Mungu. Na huwezi kumsikia Mungu ukiwa umemkasirisha. Naomba tuache huu mchezo wa furaha ya muda, huku tukikimbia uso wa Mungu tunaye muhitaji. Mbali na hili la ndoa tu, kwenye huu mji tunamuhitaji Mungu ili atupe kibali, na uweze kushinda. Wenzako wanakwenda kwa waganga, lakini wewe nilazima umlilie Mungu na ajidhihirishe haswa. Naomba tutubu tumrudie Mungu. Nimekuhakikishia mimi nipo hapa, sina ninapokwenda na wala sina nitakayemkubali isipokuwa wewe. Lakini endapo mama akashindwa kunipokea, sitakuwa na namna ingine.” Jack akainama.

“Umenielewa Jack?” Jack akanyanyua kichwa na kumtizama. “Umesema mama akishindwa kuelewa ndio umesema itakuaje?” Jack akauliza. “Mimi ninajua Mungu hashindwi na chochote Jack. Kama amefanya kwangu kwa hayo niliyokusimulia, atashindwaje kwako? Na kama mimi ni mke ambaye Mungu alikusudia uwe na mimi, hili jambo atalisimamia, mpaka likamilike. Tutaomba pamoja kabla hujakwenda kuzungumza na wazazi, na mimi sitawapigia simu wazazi mpaka wewe utakapoweka sawa mambo yako. Usiogope, unapomruhusu Mungu aingilie kati jambo, huwa anayo namna yake, utashangaa na amani tutakayotembea nayo.” “Kwa hiyo mapenzi ni mpaka wazazi wakubali?” “Acha hizo Jack. Mpaka ndoa.” Jack akatoa macho.

“Brina!” “Si tumekubaliana tunamtaka Mungu, na nguvu zake pamoja na hekima zake katika maisha yetu?” “Daah!” Jack akawa ameshachoka. “Basi hiyo ndio garama ndogo sana yakulipa ili kumpata Mungu.” “Sio garama ndogo bwana.” “Naomba upige magoti nikuombee Jack. Acha kulalamika. Hutakufa.” Akapiga magoti. “Lakini Mungu aliona usiku wa jana nilivyolala vizuri?” Akaendelea kuhoji Jack akilala kama mtoto mdogo. Sabrina akaanza kucheka.

“Yeye Mungu si anatuwazia yaliyo mema? Sasa mbona mema yamekuja na wewe unaleta kipingamizi?” “Mema yapo Jack. Lakini yawe yako. Sio kila jema unakimbilia. Mimi sio mkeo, Mungu hajakupa bado. Akikukabidhi siku ile kanisani, ruksa. Utaendelea kula mema tu. Unafikiri mimi ndio sikutaki?” “Mimi naona hunogewi kama mimi.” “Ningefika mara zote hizo kabla yako?” Jack akacheka sana. “Mimi mpaka nikawa nashangaa. Kidogo tu, tayari!” “Sio kidogo Jack. Ile hali yakujua nashikwa na Jack. Mwanaume anayenipenda na aliyenivumilia muda wote huo! Ukanipokea nilivyo, nini kinanizuia unaponigusa nisifike?” Jack akajisikia vizuri.

“Basi nikienda nyumbani nawaambia mwezi ujao nataka kuoa. Siwezi kuendelea kusubiri. Kama hawana pesa, basi. Lakini nakuoa Brina. Hii raha niliyopata jana na leo, nataka niimiliki.” “Basi tumwambie Mungu. Tushikane mikono tumwambie Mungu. Tutubu na kumwambia tunahitajiana sana tena kwa haraka, atusaidie.” Sabrina akamshika mkono Jack akaanza kuomba. Akatubu kwa ajili yake na Jack. Akaomba baraka na ulinzi kwao. Akaombea mipango yote waliyonayo. Mpaka anamaliza, Jack ametulia. “Kwa maombi haya naona kweli dhambi itakaa mbali.” Sabrina akacheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hapo ndipo walipo Jack na Sabrina. Vita ya ndani na Ya nje. Watamkabili vipi Mama Msindai? Jack ameonjeshwa tu, anataka kujenga mzinga. Ameahidiwa yote ni mpaka ndoa, huku mama bado hajamuweka sawa.

Nini Kitaendelea?

Usikose Mazito ya Mbeleni.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment