“Lakini huo hautakuwa uungwana. Watachukuaje binti ya watu bila
wazazi wake?” Akaongea baba mtu akisikika
kulalamika. “Sasa inategemea na vile Sabrina
alivyowaambia baba. Inaonekana Sabrina yupo na huyo kijana Singida. Tokea
atokea hapo nyumbani, ahamie huko mpaka leo hajasikia ndugu hata mmoja
akimtafuta Sabrina, unafikiri hata huyo mwanaume atatufikiriaje mahusiano tuliyonayo
sisi na Sabrina? Hata akimwambia waendelee tu bila sisi, kwamba sisi hatujali,
unafikiri itakuwa shida? Ataolewa bila hata sisi na wala isimsumbue tena.”
Sabina akazidi kuwaumiza. “Tuwe tu wakweli jamani,
Sabrina ameishi hapo nyumbani kama mpita njia tu lakini si kama mmoja wetu.”
“Sio kweli Sabina. Ukiongea hivyo unakosea. Sabrina alionywa hapa kama mtoto anayechungwa
tu.” “Sawa mama. Mimi nipo kazini. Nitawapigia nikitoka.” Sabina akaaga.
“Au umpigie ujidai unauliza anaendeleaje?”
Sabina akacheka. “Sawa mama. Au mtulie hapohapo
nijaribu kumpigia. Lakini msiongee chochote. Ili mumsikie na nyinyi.” “Sawa.”
Hilo wakalifurahia sana wazazi wao. Sabina akapiga zaidi ya mara tatu, hakumpata
Sabrina. “Jamani, mimi narudi kazini. Sabrina simpati.
Atawatafuta atakapokuwa tayari.” Sabina akawaaga na kukata simu.
Walishajua kuolewa kwa Sabrina na mtoto wa Msindai, kutawaletea heshima kubwa
sana na pesa, hawakutaka kupitwa tena. Wasiwasi ukazidi kuwaingia siku
zilivyozidi kwenda.
Kwa Sabrina
& Jack
S |
abrina hakumtania Jack, akamfukuza chumbani. “Hakika hiyo siku yakufunga ndoa ifike haraka. Kwanza nitawaambia nyumbani sio ndani ya miezi miwili tena. Ndani ya mwezi nataka kuoa.” Sabrina akacheka na kumsukumia nje ya mlango wa chumbani kwake na kufunga malango. “Wewe nifungulie, nitalala kwa heshima kabisa. Nakukumbatia tu.” “Mimi sitaweza kukumbatiwa na wewe nikaridhika. Nitataka zaidi.” Sabrina akamjibu. “Mimi nitakuwa mwaminifu kwa Mungu, nitakukatalia.” Sabrina akazidi kucheka akiwa ndani chumbani, Jack nje ya mlango wao. “Unamuamsha Emma, wewe Jack! Nenda kalale acha kulalamika hapo nje kama mtoto mdogo.” “Sawa bwana.” Sabrina akaendeleza tabia yakumfukuza.
Kulikoungua
Mpini….
J |
ack
hakusubiri jumamosi. Ijumaa akaondoka na ndege ya mchana kwenda kuzungumza na
wazazi wake. Akamkuta mama yake uwanja wa ndege. “Mbona midomo imekukauka?
Umekula wewe?” Mama yake akaanza. “Sijala chakula cha mchana, si ulisema
utanipikia ndizi, au hukupata muda?” “Nimepika. Umekunywa maji lakini?”
“Nimekunywa mama, acha wasiwasi.” Wakaongozana mpaka kwenye gari mama yake
akimwangalia. “Mbona kama una wasiwasi?” “Mama!” “Nauliza tu. Kuna nini?” “Kwa
hiyo unataka nianze kukwambia hapahapa kwenye gari hata sijapumzika! Ndizi
zenyewe sijala.” “Umebadilika Jack wewe! Hukuwa hivi. Sisi tulikuwa tukiongea
mambo yetu bila kupanga vikao! Mimi nilikuwa mtu wako wakaribu sana. Naona
umepata mtu mwingine.” Jack akaanza kucheka.
“Mama
Msindai unazeeka vibaya wewe! Mbona unakuwa hivyo?” “Wala si kuzeeka! Wewe ndio
umebadilika. Week nzima nakubembeleza uniambie jambo moja tu! Ni nini hicho
chakuniambia mbele ya wengine wakati mara zote ulikuwa ukiniambia mimi kwanza?” Jack akatingisha
kichwa. “Sawa Jack.” “Mama, nimekuja kwa ajili ya kuzungumza na wewe, baba
pamoja na wengine. Kwa nini usisubiri? Yamebaki masaa machache sana.” Mama yake
akanyamza. Akajua ndio amemkasirikia.
“Basi
nakwambia lakini sio ushituke na kukasirika huku barabarani.” “Haya niambie.”
Jack akamwangalia, akatamani asubirie mpaka kaka yake atakapokuwepo ili
amsaidie, lakini mama huyo aling’ang’ania, mpaka Jack akasalimu amri. “Ni nini
mbona unasita?” “Sabrina ni mjamzito.” Mpaka Jack akamuona jinsi
alivyobadilika. Akanyamaza, na Jack naye akanyamaza. Hawakuzungumza tena mpaka
walipofika nyumbani. Kwa kuwa ilikuwa mapema, baba yake hakuwepo nyumbani ila
mschana wa kazi tu. Ndugu walikuwa wanafika hapo saa moja usiku kwa kikao.
Jack
akamuona mama yake anashindwa hata kumtizama. Wakaingia ndani, Jack hakuwa na
mzigo wowote. Akifikia nyumbani kwao, kila kitu kinakuwepo chumbani kwake. Huwa
anakwenda hapo na simu yake, pamoja na walet basi. Hata chaja nyingine ya simu
huwa anakuta hapo nyumbani kwao. Mama yake akapitiliza chumbani kwake, na Jack
naye akaingia chumbani kwake kumpigia simu Sabrina na kumtaarifu kuwa amefika
salama. Sabrina akagundua Jack amebadilika. “Nakuombea
hekima Jack. Mungi yupo na wewe. Hata katika hili atatupa suluhu. Ataingilia
kati.” Sabrina akamfariji. Jack akatulia kimya. “Sema
amina Jack.” “Amina.” Jack akaitika. “Na
usilazimishie mambo. Msikilize mama na ushauri wake, wape muda huku na sisi
tukiendelea kumsubiria Mungu.” Jack akatulia.
Sabrina
alijua kwa kuwa amemnyima penzi Jack, na anamuhitaji, akajua atapambana mpaka afanikiwe
kumuoa kwa haraka tofauti kama wangekuwa wakiishi kama mke na mume. Akajiambia
hiyo tamaa yake ndiyo itamfanya apambane mpaka amuoe. Akabaki akimtanguliza
Mungu mbele, kumbe na yeye ananufaika. Alijua Jack akiendelea kupata penzi,
atabweteka kama Emma, au Tino. Akakusudia safari hii lazima Jack amuoe. Maadamu
amemuonjesha na yeye akakiri kama Emma na Tino kuwa wamefurahia penzi lake,
akajiambia kwa Jack anayempenda hivyo, atapambana mpaka afanikishe. Sabrina akamtania
kidogo bila kumuuliza kinachoendelea hapo, na alijua mama yake ndio atakwenda
kumpokea. Akamtania tena kidogo, angalau Jack akaanza kucheka. Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jack
akatoka kukaa sebuleni, mpaka baba yake anarudi kutoka kazini saa 12 jioni,
mama yake hajatoka chumbani. Na Jack alikusudia kumuacha, ampe muda
wakufikiria. “Mama yako yuko wapi?” “Chumbani.” Mzee Msindai akashangaa kidogo.
Maana wawili hao, Jack akiwepo nyumbani hufuatana kila mahali mpaka chumbani.
“Mzima?” “Nafikiri anahitaji muda wakupumzika tu.” Baba yake akafikiria kidogo,
akaingia chumbani. Isivyo kawaida akamkuta anasoma kitabu chumbani. “Jack yupo sebuleni.”
Akaanza Mzee Msindai. “Mimi ndiye niliyemleta kutoka uwanja wa ndege.” Akajibiwa
hivyo, Mzee akajua kuna jambo. “Uliniambia.” Akamalizia mzee Msindai akiweka vitu
mezani. Akatamani kuuliza, akaona anyamaze tu. “Basi mimi nitakuwa naye hapo sebuleni.”
Akaaga, mkewe kimya. Akatoka.
“Kwema?”
Baba yake akamuuliza Jack aliyekuwa ameachwa sebuleni peke yake, hata hajawasha
tv, wala hasomi gazeti. “Kwema baba. Naoa.” “Uliniambia. Hongera sana. Binti
mweyewe ni wa wapi?” Akauliza huku akikaa. “Wazazi wake wanaishi Chalinze.”
“Kwa hiyo ni Mzaramo au kabila gani?” “Mama ndio mzaramo, lakini baba yake mtu
wa Songea.” “Kwa hiyo ni Wangoni.” Akamalizia baba yake. “Ndiyo. Ni mchanganyiko
wa mngoni na mzaramo.” “Sawa. Kwa hiyo mahari tunakwenda lipa Chalinze au
Songea?” Wakacheka. “Kwa wazazi, Chalinze.” Akamtania kidogo hapo. Akamwambia
anajua kucheza ngoma za Kingoni, kwa hiyo hatamtia aibu, atampatia tu mke. Jack
akacheka sana. “Sawa baba.” Jack akaitika huku akicheka. Baba yake akampa
historia za wangoni, akamtajia baadhi ya marafiki zake wangoni.
Wakaendelea
kuzungumza akimtania Jack, kuwa wangoni hasira zao kujinyonga. Kwa hiyo asije
muudhi mkewe. Jack akaendelea kucheka, mama yake yupo chumbani. Junior na mkewe
wakaingia. “Shikamoo baba.” Wote wakasalimia. “Marahaba. Umesikia tunakwenda
kuoa kwa wangoni?” Junior akakaa akicheka. “Kumbe ni Songea?” “Wazazi wanaishi
Chalinze.” “Hapo Chalinze tu, hamna shida.” “Hongera Jack. Naona mtoto wa mama
umekua.” Wakacheka sana. “Asante shemeji.” Wakaendelea kumtania Jack, mtoto wa
mama.
“Mbona
nimeona gari ya mama, yeye mwenyewe simuoni hapa? Au yupo jikoni?” Waziri
Msindai, Junior akiwa nyumbani, akauliza na kusimama. “Mama Msindai! Uko wapi?”
Akaita huku akimfuata jikoni. “Yupo chumbani.” Baba yake akamjibu. Junior
akaenda kugonga chumbani kwa mama yake. “Mama Msindai umelala? Nimekuja kula
ndizi, Jack aliniambia utampikia?” “Ingia.” Akasikia sauti ya mama yake.
Akaingia nakushangaa anasoma kitabu, wakati kipenzi chake ametoka Singida, yupo
sebuleni! Akajua ameshajua. Akaanza kumtania mambo mengine tu, lakini huyo mama
akaonekana mzito kweli.
Mara
akasikia sauti za dada zake nje. “Warembo wa Msindai wamefika mama. Twende
utukaribishe chakula. Mbona unakimbia wageni?” “Nataka kumalizia kitabu
changu.” Akajibu mama yake, macho kwenye kitabu. “Yameanza lini mama!?”
“Ulipomchukua mtoto wangu, na kwenda kumpeleka kutengeneza pete ya uchumba,
kumchumbia mwanamke aliyeshindwa maisha huko, ndio uzee anakuja kumalizia na mtoto
wangu! Wewe mtumzima ambaye nakutegemea uongoze familia, leo unampotosha mwanangu
mwenyewe nikiwa hai!” Watu wote nje wakanyamaza, maana mama yao alikuwa akiongea
kwa sauti ya juu na ukali sana.
“Jack bado ni mdogo sana. Anahitaji uongozi wetu. Leo unanyamazia kitu kama hicho, unajichukulia mamlaka yakumuozesha mwanangu! Ujasiri huo unapata wapi?” Mzee Msindai akaingia. “Kuna nini mama? Mbona ukali kwenye jambo la kheri?” “Hakuna jambo la kheri hata kidogo.” Jack na dada zake nao wakaingia hapo chumbani kwa wazazi wao. Mama Msindai anawaka kama moto. “Mtoto anahitaji kuelekezwa, yeye anamuongoza anavyojisikia yeye bila kuniuliza mimi! Anamsaidia kutengeneza pete ya uchumba kwa siri na kwenda kumvalisha mwanamke mwenye mimba, tena isiyo yake!” Kina dada wakakaa vizuri kusikiliza. Junior na Jack kimya.
“Huyo
msichana sio mgeni kwa Jack. Jack alishajaribu kumtongoza tokea wapo chuo.
Akamkataa. Amekwenda kuzunguka huko na wanaume, wamemtenda vibaya, wakambandika
mimba, ndio anarudi sasa hivi kwa Jack amlelee mtoto wake!” Mama Msindai
akasimama. “Muulizeni Jack huyu kama sio miezi kama mitano iliyopita
alimjaribisha tena huyo msichana, akamkataa, tena kwa kumwambia aendelee na
maisha yake! Sasa hivi anakubali ndoa kwa nini kama sio kukwama kimaisha tu?”
Mama akaendelea, wote kimya wakimsikiliza. “Junior wewe kama mtumzima, unajua
hilo, leo unakwenda kwa siri, tena ulikuwa hapa siku ya jumamosi, ukanyamaza
kimya ukiwa umempa mzigo mtoto. Ili akamvalishe pete huyo mama, bila kuniuliza
au kunishirikisha! Mnataka mtoto wangu aanze maisha kwa kulea watoto wa watu!
Yaani yeye anaanza ndoa na safari za kliniki sio kwenda kupumzika kwenye
mahoteli ya maana na mwanamke anayempenda! Mnamzeesha mwanangu mimi nikiwepo!
Haitawezekana Junior. Labda mnisubiri nikiwa nimekufa.” Kila mtu alikuwa
amenyamaza.
Junior
akakaa. “Naomba kuzungumza baba. Najua wote hamjui kinachoendelea, na sasa hivi
lawama zinaangukia kwa kaka wakati alikuwa akinisaidia tu.” “Anakusaidia nini
kama sio anataka kukuingiza matatizoni kwa makusudi tu? Yeye kwa nini hakuoa
mwanamke mwenye watoto, akaenda kuoa binti?” Mama Msindai akauliza kwa ukali
sana. “Nashauri utulie mama J, tumsikilize Jack mwenyewe.” Akaingilia Mzee
Msindai. Jack akainama kwa muda. Kisha akaanza taratibu. “Au jamani niwaombe
radhi kwa yote. Zaidi kaka. Naona nimekuingiza kwenye matatizo, bila kutarajia.
Niwaache muendelee na maisha yenu, na mimi nikaendelee na yangu.” Jack akasimama.
“Kwa
hiyo unaondoka?” Mama yake akauliza kwa ukali. “Ndiyo mama. Naondoka. Kwa kuwa
sipo tayari kukusikia ukimtukana na kumdhalilisha Sabrina, mwanamke atakayekuwa
mke wangu siku za karibuni sana.” “Haiwezekani!” Mama yake akapinga na
kumshangaza sana Jack mpaka akarudi. “Labda hujaelewa mama. Hata kwa kaka sikuwa
nimemuomba ushauri au kumpa nafasi ya kunishauri. Hivyo hivyo kwenu. Nimetoka
Singida kwa heshima ya familia kama kaka anavyosema kwa wote. Nimekuja kuwataarifu
kuwa, naoa. Sijaja kutafuta mke hapa nyumbani. Sijaja kupokea ushauri wa
nani nimuoe. Hilo naomba niwaweke sawa. Nipo hapa kuwataarifu naoa. Hatua
ya kutafuta mchumba nimeshamaliza na nimefunga.” Jack akawa mkali, na
kuwasimamia mpaka mama yake, wote wasiamini.
“Sijui kama mnanielewa? Baba!” Akamgeukia baba yake. “Nimekuja kuwataarifu kuwa, nimepata mchumba, NAOA. Hilo ndilo limenileta nyumbani jamani. Ni nani, yukoje, hilo nimeshafunga. Huko sitarudi tena. Nasikitika hajawa chaguo lenu, lakini mimi ninayemuoa ni chaguo langu, NAOA. Tena naoa ndani ya muda mfupi sana kuanzia sasahivi. Na kwa kuwa nawaona kama hamtakuwa na mimi kutokana na kile mnachokisikia juu ya mpenzi wangu, nafikiri hata ile miezi miwili niliyowambia, sitasubiri tena. Huo muda niliweka kwa heshima yenu tu. Maadamu hamtaki kuungana na mimi kwenye hili, mimi mwenyewe na marafiki zangu tutakwenda kulipa mahari, nitajigaramia harusi yangu mwenyewe, NAOA. Na ili nisiwakere na kuwatia aibu hapa mjini, nitafunga harusi yangu Singida. Kwa herini.” Jack akataka kutoka, baba yake akamuwahi.
“Subiri
kwanza Jack.” “Sitasubiri baba. Wewe hujui, lakini mama anajua jinsi
nilivyomsubiri Sabrina. Unafikiri mimi sikutani na wasichana warembo na wazuri?
Muulize kaka msichana aliyenikuta naye ijumaa iliyopita, yeye mwenyewe alijua
ndiye atakuwa mke wangu. Lakini hakuna atakayekuwa mke wa Jackson Msindai, kama
sio Sabrina. Ni bora nisioe, niendelee kutembea hovyo, nikifa na maradhi
itakuwa basi. Msitake kunichanganya.” Jack akawaka kabisa. Mtoto huyo wa mama
hajui jibu la ‘hapana’. Tokea mtoto, akitaka kitu, lazima apewe. Na mama
yake alihakikisha hilo lazima litimie. Akitaka kitu, Jackson alipata. Sasa leo
‘hapana’ kwa Sabrina wake, hapo ndipo walipomjua mtoto wao.
“Mimi ndiye ninayeoa, na ndiye nitakayeishi na
mke wangu. Nitaishije naye, ni juu yangu. Mbona watu wanaoa wanawake mabikra na
bado wanashindwana! Mimi ninaposema Sabrina ni mke wangu mnafikiri sijaona
wasichana wengine warembo? Mnafikiri sijalala na wanawake mabikra? Nimelala
nao. Wenye viuno vyembamba na makalio makubwa pia nimelala nao. Na..” “Jack
umekasira, unaongea maneno utakayojutia baadaye. Naomba utulie.” Kaka yake
akamuonya.
“Hapana
kaka. Hamuwezi kumzalilisha Sabrina mbele yangu. Hamjui alikopita. Mimi najua.
Sabrina hajashindwa maisha. Anayo pesa yake yakutosha tu. Mimi ndiye
niliyemfuata Sabrina Moshi, akiwa anaishi kwenye Villa nzuri tu. Sabrina hana shida
yakumfanya aolewe na mimi au anikimbilie. Hata leo nikimfukuza Sabrina nyumbani
kwangu, anaweza kujitegemea bila shida.” “Kumbe unaishi naye nyumba moja!?”
akauliza baba yake. “Ndiyo, na si kama mke wangu. Sabrina amemgeukia Mungu.
Anajutia kitendo chakutembea nje ya ndoa, sasa hivi anaishi maisha ya kimungu. Hata
nilipomuomba ahamie Singida tuje tuishi naye, akijua ninaye mpenzi wangu Pam,
alitaka akaishi kwake, mimi ndio nilijiona siwezi kuishi bila Sabrina.
Nakumbuka alikuwa hotelini, ikabidi nimfute Sabrina, na Pam akinitaka haswa!”
Jack akaendelea kuongea kwa Jazba.
“Nampenda
Sabrina kuliko nafsi yangu. Ananijua, ananielewa, na ananitia moyo kwa yale
ninayoyafanya. Hiyo miezi minne iliyopita nilipomuomba aje Singida niishi naye,
alikataa kwa aibu, kama hivi anavyosema mama. Aliniambia alikuwa akijisuta.
Hakutaka kuja kwangu halafu watu wafikie kujiuliza hichi anachoongea mama.
Sabrina ni binti mdogo tu. Amepata mimba, yeye akaamua kuitunza hiyo mimba
wakati mabinti wengine wanatoa! Hata mwanaume aliyempa mimba alimshawishi sana
aitoe. Akamwambia wataepuka aibu. Akampeleka mpaka kwa daktari kwenda kumtoa
huyo mtoto, ndio Sabrina akamuomba huyo daktari amdanganye huyo mwanaume kuwa
alimtoa mtoto, akamchoma tu sindano ya usingizi, yule mwanaume akaamini Sabrina
yupo kwenye maumivu yakutoa mimba. Mwanaume akaondoka, Sabrina akabaki na mimba
yake.”
“Sabrina
ni mwanamke ambaye hajui kukwepa majukumu. Unapompa tatizo Sabrina, anatafuta
ufumbuzi, hakimbii. Ni mwaminifu, ambaye japokuwa mimi pale chuoni walikuwa
wakinililia, mpaka wanachuo pale walikuwa wakipigana kwa ajili yangu, lakini
Sabrina alinikataa mimi kwa kuwa alikuwa kwenye mahusiano mengine. Tena wala
hakuwa kwenye mahusiano mazuri, alikuwa akinyanyaswa haswa. Lakini hakutaka
kumsaliti huyo mwanaume. Nitapata wapi mwanamke atakayesimama na mimi kama si
Sabrina?” Jack akaendelea.
“Kaka
alinikuta na huyo Pam. Mzuri, muulizeni kaka mwenyewe. Lakini Pam alikuwa akinikatisha
tamaa kwa kile ninachokiamini, na sababu nzima ya mimi kuwepo Singida! Nikiwa
na Pam, Sabrina akamsikia anavyonikatisha tamaa juu ya lile jimbo. Kuwa
sitaweza kwa kuwa mbunge wa sasa hivi ameshika sana watu. Na amefanikiwa sana.
Pam akanikatisha tamaa akiniambia maneno ya ukweli yakunivunja moyo. Sabrina
akanyamaza kabisa mpaka Pam alipoondoka. Sikutegemea hekima ya Brina. Akasubiri
hata yule kijana ninayeishi naye akaondoka akiwa amesikia yote aliyoongea Pam.”
“Nikiwa
nimekata tamaa kwa maneno ya kweli aliyokuwa ameniambia Pam, Sabrina
akanikumbusha mimi ni nani. Nikiwa hata sijui kama chuo alikuwa akinifuatilia,
kumbe amekariri na anakumbuka hata madogo niliyokuwa nikiyafanya chuoni, na
mimi kuyapuuza. Akanikumbusha mambo madogo yoote niliyoyafanya chuoni na
niliyoyabadilisha tokea nimefika pale chuoni kabla hata sijachaguliwa kuwa
raisi. Sabrina akanikumbusha moja hadi jingine kwakuwa tulianza naye mwaka wa
kwanza, ila yeye alisomea diploma ya miaka miwili, kwa hiyo aliniacha chuoni.
Sabrina akanikumbusha yote. Akaniambia mimi nilizaliwa kuongoza.” Kila mtu
akashangaa.
“Brina
aliongea hivyo bila kunipamba. Akasema uongozi na kutawala ndicho kipaji na
kusudi Mungu alinipa nije kutumika hapa duniani. Akaniambia ndio sababu kila
ninapofika, nikijaribu kitu, Mungu anaweka mkono wake hapo na kuhakikisha kusudi
la Mungu, wala si langu, la Mungu mwenyewe kupitia mimi linasimama na
kufanikiwa. Akanikumbusha uongozi mbovu nilioukuta pale chuoni ukiwa umeota
mizizi mirefu ya rushwa mpaka ya ngono, jinsi nilivyobadilisha hata kabla
sijawa raisi wa chuo. Sabrina akatembea na mimi hatua kwa hatua mpaka ile hali
yakushushwa moyo ikabadilika. Akanionyesha uwezo mkubwa ambao ninao ndani
yangu, na vile nilivyoruhusu mazingira yanipotoshe.”
“Kina
Pam na ugumu wa ile sehemu vilinifanya nikajisahau. Lakini Sabrina amenirudisha
kwenye mstari. Ndoto za kuja kuwa mbunge pale nilishazitupilia mbali. Muulizeni
mama. Jimbo lile nilishamwambia mama, haliingiliki. Hivi nilikuwa nikitafuta
uhamisho, nihame Singida! Miradi ya chama yote ilikuwa imekufa. Lakini Brina,
ametumia cheo kidogo nilichonacho mimi, kuanza kuifufua. Halali akiweka mipango
ya kutumia dhamana niliyopewa na Mungu kwenye ule mji. Mimi kama mwenyewekiti
wa chama pale Singida, amenionyesha ni nini naweza kufanya. Tumeanza muda mfupi
tu, lakini kwa mawazo ya Sabrina, nimeweza kufufua vijana wa pale. Jumatano
nimekutana na vijana wote. Nimezungumza nao juu ya kutengeneza na kusajili
rasmi timu ya mpira wa miguu, kwa jina la chama. Wote wakakubali. Ndio jana,
nikisema jana ni jana, yule tajiri wa Singida, Patel, alikubali kukutana na
mimi, nimezungumza naye, amekubali kudhamini ile timu ya chama.” “Hongera
Jack.” Baba yake akampongeza.
“Asante
baba. Lakini ni Brina wangu baba. Hayo yote ni yeye. Mimi nakwenda kazini
asubuhi, yeye anaweka mipango. Yeye ndiye aliyenilazimisha kwenda kukutana na
Patel nikijua atanikatalia. Yeye ndiye aliyeweka appointment kwa Patel,
akaniambia lazima niende ili tujue kama ametoa jibu la ‘ndiyo’ au ‘hapana’ ili
tuendelee na wengine. Sabrina aliniandalia kila kitu cha kwenda nacho kwa
Patel. Ninavyozungumza hapa, Patel ameniandikia hundi ya pesa yote ya jezi ya
timu, mipira, nyavu, na usafi wa kile kiwanja. Yote hiyo ni kazi ya Brina,
jamani. Aliniambia lazima kuanza kama nilivyoanza chuoni. Chini kule ambako
watu hawapaoni na kupajali. Yule mbunge wa pale akija ananywesha watu pombe.
Lakini Brina akaniambia nianze kwa kukusanya vijana wa chama. Kuwaweka pamoja,
kuwaanzishia miradi, na kuwafanya wawe hai.”
“Brina
anahangaika kutembea juani na tumbo lake akinisaidia kupeleleza na kujua nini
nifanye ili kujiinua kwenye ule mji. Anatumia pesa yake mwenyewe wala si yangu
kwenye mambo yote hayo. Ananitia moyo na kuniombea bila kuchoka, tena akishika
mikono yangu na kuniambia mikono yangu ilishabarikiwa, wala sihitaji kuangalia
mazingira yanayonizunguka na watu wanaonikatisha tamaa, kwa kuwa hawajui kile
Mungu ameweka ndani yangu. Ni mimi kuchukua hatu. Huyo ni Brina jamani. Kesho
kocha niliyemtafuta na Brina, anaanza kuwafanyia mazoezi wale vijana kama timu
inayoeleweka, huku ninashugulikia jezi zao na kutafuta jinsi ya kusajili ile
timu ya chama ya vijana. Kwa pesa na uungwaji mkono na Patel, ndani ya muda
mfupi sana na Mungu akiweka mkono wake kama tunavyoomba na Brina, mtakuja
kushuhudia ile timu ikicheza na kushindana mikoani. Hayo yote ni Brina.”
“Ni
kweli mimi nilikuwa mwenyekiti wa tawi wa chama pale. Lakini nilifika pale
mazingira yakanikatisha tamaa. Nilikwenda na matarajio makubwa, nikaishia
kugonga mwamba. Mama huyu hapa ni shahidi jinsi nilivyokwa nikimlalamikia juu
ya Singida. Lakini nilikuja huku kustarehe na Pam, Brina ananihangaikia kundaa
vitu vya kufanya nikirudi kule. Narudi Brina akiwa amechoka, mimi nimetoka
kustarehe huku! Ameniwekea mipango mizuri sana. Waliompa nafasi kule Singida
wanampenda sana Brina. Nimemtambulisha kwa dada mmoja, mtumzima tu, ambaye yupo
na mimi kwenye ungozi, yule dada anamsifia Brina kwa hekima, utulivu na uwezo
wa kufikiri na kufanya mambo. Kesho anakutana na vijana wa kike wa chama pale,
ili kuzungumza nao. Lakini ameshafanya uchunguzi wa nini chakufanya akijua
madhaifu yao na nguvu zao. Mimi mwenyewe nilijaribu kumkatisha tamaa nikiwajua
wale wasichana, lakini jinsi alivyonieleza, mpaka huyo dada Imani mwenyewe
akashangaa.”
“Nampata
wapi mwanamke kama Brina jamani? Alianza akisimama na mimi kama rafiki tu,
akijua namuoa Pam. Brina akawa anatumia pesa yake kuendesha mambo pale, wakati
mimi nahangaika na Pam, tena wala hanidai. Ananipikia vizuri, ananifulia,
ananitandikia mpaka kitanda!” Wote wakacheka. Kasoro mama yake ambaye alipoa
kabisa.
“Natamani
mtoto anayembeba Brina awe wangu. Hakika namuona mjinga na kumuhurumia sana
mwanaume aliyemtelekeza Brina. Jamani kwangu naona ni bahati ya pekee. Kuna mtu
aliniambia bila hata kumjua Brina kuwa, ‘Chakuokota si chakuiba. Mwenye mali
ndio mjinga’.” Wote wakacheka. “Nina uhakika wa mtu wa kusimama na mimi
mpaka kifo changu. Nyinyi wazazi wangu mnataka nini kama sio kuniona nipo na
furaha?” Baba yake akakaa. Pakazuka ukimya.
“Mimi
naondoka, nakwenda kutafuta chakula, kesho niwahi ndege ya mapema sana narudi
Singida kuendelea na mipango yetu. Lakini nataka mjue kabisa, NAOA. Mungu
amenipa Brina niliyekuwa nikimtamani kwa muda mrefu, akiwa na mtoto. Mimi sijui
ni kwa nini, lakini, nimefanikiwa kumpata Brina, na mtoto wake. Ndiyo, naingia
kwenye ndoa nakuanza majukumu ya mtoto, lakini na mwanamke ninayempenda. Brina.
Mtoto atanitambua mimi kama baba yake, kwa kuwa baba yake alitaka auwawe.
Hamtaki. Kwangu nahesabu ndio mtoto wangu wa kwanza. Na samahani baba, atakuwa
ni Msindai kama kina Msindai wa kaka hapa. Nitamlea na kumpenda kama mtoto
wangu. Atakayetaka nimtambulishe kama ndugu, basi baada ya miezi mitano kuanzia
sasa, na mimi nitakuwa na mtoto. Sasa kabla ya hapo, nataka niwe nimemaliza
swala la kuoa, nipumzike na mke wangu ndipo tuje kwenye kulea.”
“Kaka
hausiki kwenye maamuzi yangu, ila alichofanya nikunipunguzia kuishi kwa
wasiwasi. Maana nilikuwa nikiishi na Brina, huku nikiwa sina uhakika kama
atanikubali tena. Kwanza amenikuta na Pam, pili ni alishakusudia kutulia
kabisa. Kutokana na kutendwa vibaya na wanaume hakutaka tena kujihusisha nao. Alikusudia
kutulia na mtoto wake tu, basi. Nilipomwambia kaka, alichosema na yeye ni kama asemavyo
Brina. Jibu litakuwa ‘ndiyo’ au ‘hapana’. Lazima nizungumze naye.
Na ili anione nipo serious na sifanyi mchezo kama kwa kina Pam, kwa kuwa
Sabrina ni mtu makini, akashauri kwake niende umbali mkubwa, niende na pete
kabisa sio maneno matupu wakati nimetoka kulala na Pam. Na akanitoa kabisa pale
hotelini nilipokuwa nimefikia na Pam, akanionya nisirudie tena huo mchezo,
popote na kwa yeyote. Kaka akaniambia ninayoyafanya sasa hivi gizani na watu
wakiwa kama hawaoni, yatakuja kunifuata baadaye nikiwa mwangani. Na akanionya
nisirudie tena kuwa na wanawake wawili kwenye maisha yangu. Akanitoa pale hotelini,
nikaenda kulala nyumbani kwake. Sasa hapo kosa la kaka ni lipi?” Jack akauliza
kwa ukali. Kimya.
Akatoka
kwa hasira. “Jackson!” Akasikia baba yake akimuita. Akarudi. “Ulitaka kuoa
lini?” “Haraka iwezekanavyo ili nianze kulala na Brina.” “We Jack!” Dada yake
mkubwa akamshangaa. “Naona hamnielewi kila ninachoongea, je! Nataka kuoa, na
mimi nitulie kama kaka. Hamtaki kuungana na mimi, basi.” “Nendeni mkale. Nyinyi
wote, nendeni, nipate muda wakuzungumza na mama yenu. Umesikia Jackson?” “Sawa
baba.” Akatoka, ndugu zake wakamfuata nyuma.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Naona
mtoto wa mama ameamua kuoa kwelikweli!” Dada yake wanayefuatana akamchokoza kwa
kunong’ona. “Achana na mimi Jena.” Wakaanza kucheka kimya kimya wakiongozana jikoni.
“Mimi nilishukuru kaka J, alivyokunyazisha. Maana nilisema leo moto umewaka
leo, tutajua yote! Mpaka kulala na mabikra!” Jena akaendelea walipofika jikoni.
Wote wakaanza kucheka. Junior akawa anatingisha kichwa kama anayesikitika huku
akicheka. “Naona mnataka kuniwekea usiku kwenye mipango yangu mimi! Sitaki mchezo.”
“Kwa kweli hilo umeliweka wazi mpaka na matusi!” Wote wakazidi kucheka taratibu.
“Sasa tusubiri mama awekwe sawa, tuanze mipango ya harusi. Ila kama akikataa, mimi
nitakuja kwa siri.” Dada mkubwa, Jacinta, akanong’ona. “Hata mimi nitakuja
mwenzangu. Ila Junior wewe sidhani kama utaweza kwenda.” Junior akanyamaza
kidogo.
“Hili
linalompata Jack, na mimi nilishapitia hapo ila kwa sura nyingine. Muulizeni Joy.”
“Mimi pia nakumbuka. Mpaka mama akapandisha pressure!” “Wewe unakumbuka
Jacinta.” Junior akakubaliana na dada yake. “Sasa wewe kaka alikukatalia nini
wakati Joy hakuwa na mtoto?” “Basi tu mama. Nahisi kama anakuwa hayupo tayari
kukutoa kwa mwanamke mwingine! Tazizo wala si mtoto. Mimi ninauhakika na hilo.”
“Sasa mbona alikuwa haishi kunisisitiza kuoa?” Jack akauliza. “Si kwa kuwa hukuwa
umemletea mwanamke bado! Sasa na wewe ulivyomwaga sifa za Brina hivyo, mwenzio
anaona anapokonywa.” Wakazidi kucheka.
“Mimi
aliyenisaidia kunifungua macho ni baba. Halafu ukumbuke mimi sikuweza kuwa
mkali kama hivyo wewe. Ilichukua muda sana. Kila siku anatoa sababu zisizoisha.
Ndio ikabidi sasa nimtoe kwa chakula cha usiku, ili tukazungumze sisi tu
wawili. Ikabidi nimuhakikishie mahusiano yetu hayatakaa yakaisha. Urafiki wetu
utabaki hivyohivyo na sitahama kwenda popote, nitakuwa naye hapahapa Dar.
Nikamuomba ampe nafasi Joy, amfahamu ndipo aamue. Nikamwambia Joy atampenda na
kumuheshimu. Wala hatatutenganisha. Ndio kidogo akatulia. Tukaja kufunga ndoa.”
“Ila kwangu haikuwa rahisi hivyo Junior. Mwambie mwenzio ukweli. Ilichukua muda
sana mama kunifungulia moyo.” Joy akaingilia.
“Nakumbuka
kuna kipindi Joy alikuwa haji hapa nyumbani.” Jacinta akaongeza, wakacheka.
“Alisema nimemuharibia pressure cooker yake kumbe ni msichana wake wa kazi!”
Wakazidi kucheka taratibu. “Niliondoka hapa nalia. Ndio Junior akaniambia zile
hasira sio za pressure cooker, nimpe tu muda. Na mimi nikamwambia sirudi tena
kwenu. Tulikaa muda kweli. Haji nyumbani kwetu na mimi siji hapa. Anakuja
Junior peke yake.” Wakazidi kucheka taratibu. “Sasa tusubiri tuone. Tena kwa
Jack, huyo anayemuita mtoto mpaka leo! Sijui!” “Mimi naoa, wala sitasubiri.”
“Lakini naomba mchukulie taratibu Jack. Tafadhali sana.” “Mimi sipo kama hivyo
wewe kaka. Mimi siwezi kusubiri. Mnataka Sabrina aje aolewe mimi nibakie kuitwa
shemeji!” Walicheka kwa sauti mpaka wakajisahau. “Msinitanie mimi kabisa.”
Wakazidi kucheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nani
Kashika Makali, Nani Kashika Mpini? Usikose Muendelezo Kujua Mizani Italemea
Wapi.
0 Comments:
Post a Comment