“Sasa
lazima ukazungumze tena na mama yako Jack. Najua hata wewe hutafurahia kuwa
kwenye harusi bila yeye. Usikubali hasira zikukoseshe kitu muhimu sana. Tulia,
nenda kazungumze na mama yako. Upate baraka zake, tuanze mipango.” Jack
akasimama akiwa anacheka. Kila mtu akacheka kimya kimya. Akarudi chumbani kwa
mama yake.
Jack arudi
tena kwa mama yake.
A |
kaenda
kupiga magoti pale alipokaa mama yake. Akaanza taratibu tu. “Nampenda Brina,
mama. Hii kuishi naye kwa huu muda mfupi, nimeelewa ni kwa nini moyo wangu
umekuwa ukimtamani na kuwa tayari kumsubiri. Brina ni wangu mama. Hata yeye
amekiri amefanya kosa. Anajutia kupita kiasi. Amejawa hofu juu ya huo ujauzito,
ingekuwa mtu mwingine angetoa mimba, ila sema Brina ameumbiwa uwezo wa kubeba
matatizo na kuyatatua. Hajui kukimbia matatizo. Naomba umkubali mama yangu,
najua utampenda sana. Amekuwa akiwa na manyanyaso sana. Ningetamani kama angeonja
hata nusu ya mapenzi unayonipa mimi, ili aje awe mama mzuri hata kwa watoto
wangu.” Jack akaendelea taratibu.
“Naomba
mpe nafasi. Mfundishe yale yote ambayo unatamani kuona mke wangu ananifanyia,
na vile ambavyo unataka wajukuu wako wafanyiwe.” “Unajuaje kama anafundishika?”
Mama yake akauliza. “Katika yote, Brina ni jasiri sana, ila mnyenyekevu mno. Na
ndio maana kwa muda mfupi sana ameweza kusoma ule mji, na kuweza kuelewana na
watu. Ukitaka kuniona nikiwa na furaha wakati wote, basi nimuoe Sabrina, na
wewe ubaki kwenye maisha yangu. Nikiwa na nyinyi wawili, hapo nimekamilika.”
“Naona yeye sifa zake zimezidi! Umesema mimi nilikuruhusu uue ndoto zako lakini
Sabrina akakukumbusha wewe ni nani!” Jack akacheka. Akamkumbuka kaka yake.
Akajua kweli hayupo tayari kumuachia.
“Kwanza
lazima ujue mama, hata Sabrina aweje, hawezi kuchukua nafasi yako kwenye moyo
wangu.” Akamuona anaanza kucheka. “Sikudanganyi kukupamba, ni kweli mama yangu.
Wewe ndio best wangu. Kile nichokisikia sikichuji, nakuletea kama
kilivyo. Nisamehe kushindwa kukushirikisha maswala ya pete, ni kwa kuwa
sikutaka kukuumiza kama Brina angenikataa. Alishanihakikishia kuwa hataki
mwanaume tena. Halafu kitendo chakuniona mimi na Pam, nakuendelea kumuheshimu
Pam kama wifi yake, nacho kikanikatisha tamaa japo alishakiri kwangu anatamani
arudishe siku nyuma, turudi kuwa chuoni halafu nimtongoze tena. Aliniambia
anajuta sana, na anaumia lakini hana jinsi. Mungu amemuumba hivyo. Kusimama na
mtu mpaka huyo mtu mwenyewe aseme basi. Sabrina hatanikimbia katika shida wala
raha. Atakuwa wangu mimi tu, sio kama kina Pam.” “Kwa hiyo unataka kuoa lini?” Jack
akakaa.
“Ninahamu
yakuishi naye kama mke wangu kabisa, mama. Naona sitaweza kusubiri tena. Brina
amesema amefanya makosa mengi sana akimkosea Mungu. Amejiapia kurudi kwa Mungu
na kumtanguliza Mungu kwenye kila kitu. Hataki hata nimkumbatie sana!” Mama
yake akaanza kucheka. “Kweli mama. Sasa unafikiri nitasubiri mpaka lini?
Nisaidieni nioe jamani! Tafadhali mama yangu. Na wala sitaki mambo mengi.
Harusi tu.” “Uliniambia. Lakini lazima iwe nzuri. Kiziwanda tena!” Wakawasikia
wanacheka huko chumbani. Wakajua wameshapatana. “Naona harusi ipo.” Jena
akanong’ona. Wakacheka kwa sauti ya chini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakasikia
mlango wa chumbani kwa wazazi wao unafunguliwa, kila mtu akavuta simu yake,
wakijidai hawakuwa wakiwasikiliza ila wapo kwenye simu zao. “Inabidi tugawane
majukumu.” Mama Msindai akaaza. Jacinta na Jena wakaanza kupiga vigelegele.
“Mama mkwe kakubali!” “Mmbea wewe Jena!” Wakaanza kucheka. “Harusi
inamaandalizi mafupi sana lakini nataka mziwanda apate kitu kizuri kama Junior.”
“Kweli mama.” Junior bila kinyongo akaitika na kumfanya mama yake ajisikie vibaya.
“Unisamehe Junior mwanangu. Nahisi nilikuwa kwenye mshituko.” “Usijali mama J. Wewe
nipe majukumu, mimi na marafiki zangu tuanze kazi, tuandae harusi nzuri tu.” Marafiki
wa waziri nchini, lazima wafanye kitu kizuri.
“Basi,
naona wewe ushajigawia majukumu. Mchango wangu na mama yenu, utatuambia.” “Sawa
baba. Lakini kikao cha kwanza lazima Jacinta, Jena na Joy muwepo ili mtoe
mawazo yenu. Na nitaanza kuwapigia simu watu wachache ninaojua watafanya mambo
kwa haraka ili tusipoteze tena muda hapo.
Kukiwa na bajeti najua pesa haitakuwa tatizo. Kwani kunasehemu maalumu mnataka
harusi yenu ifanyike?” “Hapana kaka yangu. Brina amesema ndogo tu ili
tusiwachoshe hao marafiki zenu tutakao wahitaji tena kwenye harambee ambayo tunaiandaa.”
Wakacheka.
“Wanandoa
hawa wanamipango!” Jacinta akaongeza. “Lakini mmenifurahisha sana Jack.
Endeleeni hivyo hivyo. Mtafanikiwa mapema sana kuliko wengine wanao anza siasa
kwa kuchelewa, tena wakiwa wamejawa tu tamaa. Utajikuta upo kwenye vikao vya
baraza na wazee wakubwa kabisa, wewe ndio mtoto. Na hiyo ni kwa kuwa umejiandaa
mapema bila kuchelewa.” Baba yake akampongeza. “Asante baba. Hata kaka Junior
ameniambia hivyo hivyo.” “Lakini nataka niwatoe wasiwasi wewe na Sabrina.
Harusi ni kitu kinachofanyika mara moja tu. Hakirudii. Mnahitaji kumbukumbu
nzuri. Msiwe na wasiwasi juu ya pesa. Harusi ni harusi, na harambee ni
harambee. Haviingiliani.” “Ni kweli kabisa.” Jacinta naye akaunga mkono.
Wakazungumza na kupanga mengi. Akaachiwa yeye Jack jukumu la kutafuta tarehe ya
kupeleka mahari, ili waanze vikao vya harusi. Akakubali siku hiyo ya mahari
ndipo atamchumbia Sabrina upya. Wakamaliza hapo, Jack akiwaambia kesho yake
atakuwa na majibu yote. Wote wakashangaa. “Kweli umeamua kuoa!” Jack akacheka
na kusimama kwenda kumpigia simu Sabrina.
Jack Kwa
Sabrina.
“Mbona umelala mapema!?” “Si wewe haupo? Emma naye amewahi kuingia
chumbani. Ameenda kujisomea, kesho anamtihani.” “Pole.”
Jack akamuhurumia kwa upweke. “Hata hivyo nahitaji
kupumzika mapema. Kesho nitakuwa na siku ndefu sana. Asubuhi tutakuwa na wanawake.
Na jioni nilimuomba dada Imani kama tunaweza kuwepo mpirani angalau siku ya
kwanza tuone inaendaje. Naona na mumewe amefurahia huyo! Amesema tutaongozana.”
Jack akalipokea hilo vizuri sana. “Nakushukuru kusimama
na mimi, Brina.” “Karibu Jack. Utafanikiwa tu. Mimi nina imani na wewe ndio
maana nahangaika hivi.” Jack akatulia kidogo akimtafakari Sabrina.
“Vipi na wewe huko? Nilikuombea kabla sijalala. Najua utapambana na
ugumu huko. Lakini nimemuomba Mungu kusudi lake lisimame.”
Sabrina akaongea kwa upendo. “Nashukuru kwa maombi.
Naona sasa hivi kazi imebaki kwako. Wanataka kujua lini wazazi wako watakuwa
tayari kupokea mahari.” “Mungu wangu Jack! Wamenikubali!?” “Hata wangekataa,
ningekuoa Brina. Wewe ni wangu. Unanikamilisha mama.” Sabrina hakuamini.
“Nakuhitaji mimi kwanza kabla ya wengine. Piga simu kujua ni lini wapo tayari
ili tuweke mipango. Na mama ameomba hiyo siku ya mahari nikuvalishe tena peke
ya uchumba, yeye akiwepo.” Sabrina hakuwa akiamini. Akabaki akifuta machozi.
Jack akajua analia. “Nakupenda sana Sabrina. Mungu atatusaidia hata hili litakamilika tu vizuri. Wapigie simu baba na mama tujue wanasemaje.” “Leoleo au kesho?” Sabrina akauliza akifuta machozi. “Kama unaona ni usiku sana, basi iwe kesho. Hamna shida.” “Acha nijaribu Jack. Nahisi huu ni wakati wa Mungu kwangu. Sitaki kusubiri tena.” Jack akacheka. “Haya, nasubiria majibu.” Akakata simu.
Sabrina kwa
wazazi.
S |
abrina akawapigia
simu nyumbani kwao kwa kutumia simu ya baba yake. Haikuta sana ikapokelewa. “Sabrina mama?” Mpaka Sabrina akashituka. “Ni mimi Sabrina, baba, sio Sabina.” Akajaribu
kujitambulisha akihisi baba yake amekosea. “Sabina
alitupa namba yako. Hata leo mama yako alikupigia kutaka kujua unaendeleaje,
lakini hukuwa hewani.” “Ndiyo.” Sabrina akaitika hivyo asijue amwambie
nini baba yake ambaye hawakuwa na mahusiano mazuri kabisa.
“Sijui mama yupo karibu hapo?” Akauliza.
“Nipo nakusikia tu. Hujambo?” “Sijambo, shikamoo mama.”
“Marahaba. Unaendeleaje?” Sabrina akasita
kidogo. Akashindwa hata chakujibu, akaona aendelee tu na yake. “Nafikiri Sabina aliwajulisha. Nimepiga simu kuwataarifu nataka
kuolewa.” Akamsikia mama yake anapiga vigelegele. Akacheka. Akajua ndio
wamekubali. Asijue hiyo simu ilikuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu sana mpaka
wakakata tamaa wakijua ataolewa bila wao. “Hongera sana
Sabrina.” “Asante baba.” “Hongera mama. Hongera mnooo.” Mama yake naye
akampongeza Sabrina kwa furaha. Sabrina akacheka. “Sasa
huko ukweni wanataka kujua kama mtakuwa tayari kupokea mahari, na mpo tayari
kwa lini?” Sabrina akaenda kwenye pointi moja kwa moja.
“Sisi tupo tayari mama. Hiyo ni heshima kubwa sana. Kwani wewe
unataka iwe lini?” Mpaka Sabrina akashangaa huo
ushirikiano. “Ingekuwa mapema tungeshukuru. Tunataka
kufunga ndoa haraka. Mkitoa orodha ya nini kinahitajika kwenye mahari, nikawapa
na tarehe ambayo mpo tayari kupokea hiyo mahari, nafikiri itatusaidia sana
kurahisisha mambo.” “Hilo halina tatizo kabisa. Nilishaanza kuulizia na kuomba
ushauri kwa wenzangu waliotangulia kuozesha, naona hata kesho nitakuwa
nimekamilisha.” Sabrina hakuamini. “Wewe ni Mungu. Badala yako hakuna mwingine.”
Sabrina akaongea moyoni.
“Nashukuru sana baba. Na kingine, mwenzangu alinichumbia tukiwa
wenyewe tu. Lakini mama yake ameomba wakija kutoa mahari, tuvalishane pete ya
uchumba. Kwa hiyo itakuwa kama tafrija ndogo hivi. Sijui kama ni sawa?” “Mmmh!
Sabrina mwanangu, huko tuliposikia unaolewa ni pakubwa mama. Na hali ya hapa
nyumbani ni kama unavyoijua. Tutaweza kweli?” “Msiwe na wasiwasi mama. Ninachotaka
ni baraka zenu tu na utayari. Garama nitagaramia mwenyewe.”
Hawakuamini kama ni Sabrina aliyeondoka hapo mchovu, anarudi na uwezo wote huo! “Kama ni hivyo ni
sawa. Baraka zetu zote unazo, na utayari upo mama. Mtoto wa kwanza kuolewa! Acha
tuhangaike.” Sabrina akacheka taratibu.
“Kwa hiyo kama kesho mtatoa hiyo orodha ya mahari, lini mtakuwa mpo
tayari kupokea ili niwaambie wajipange?” “Maadamu utatuwezesha mama, wewe ndio
tukuachie mpango mzima. Uongoze vile utakavyo, tutawaambia kina Sabina
watusaidie kuandaa tu ili ukija hapa na wakwe zako ukute mambo mazuri.” “Basi
nitawaambia waje kutoa hiyo mahari hata jumamosi ijayo.
Mnisaidie tu hiyo orodha kesho, ili wajiandae.” Akamsikia mama yake
akishangilia sana. Sabrina akacheka na kuaga.
Kwa Jack.
Hapo
hapo akampigia simu Jack. “Nimekaa palepale nilipokuwa
nimekaa wakati tunazungumza mwanzo, nakusubiria.” Sabrina akacheka. “Niambie huko ukweni?” “Huwezi amini Jack! Nahisi kweli Mungu
ameamua kusimama na sisi. Wamepokea hilo jambo vizuri! Nimepokelewa kwa
mapenzi, wanasema walikuwa wakisubiri simu yangu, na baba akaanza kufuatilia
mambo ya mahari. Ameahidi kesho atakuwa amekamilisha, atanitumia.” Jack
akafurahi sana.
“Lini watakuwa tayari kupokea sasa?” “Waliingiwa na hofu ya maandalizi
ya hiyo tafrija, sababu ya pesa. Wakaniambia kwa sasa hawapo vizuri kifedha.”
“Ungewaambia sisi tunahitaji tu kibali. Kila kitu tutagaramia wenyewe. Wasiwe
na wasiwasi.” “Nimewaambia Jack. Nimewaambia pesa za maandalizi yote
nitawatumia wakishanitumia hiyo orodha ya mahari.” “Afadhali. Hapo
umenirahisishia sana. Sasa unafikiri hata jumamosi ijayo wataweza kupokea
ugeni?” Mpaka Sabrina akacheka. “Nini?” “Ni kama tunawaza pamoja! Na mimi nimewauliza hivyo
hivyo, wamesema nikiwawezesha, hapatakuwa na shida.” “Saafi sana. Mbona naona
Mungu amekusudia nipate mke!” Wakaanza kucheka wawili hao, wasiamini
kinachowatokea.
Jackson Kwa
Kina Msindai.
J |
ack akarudi kwa familia yake. Akwapa habari njema. Wote wakapokea vizuri bila shida. Tena na mama Msindai ndio akawa mstari wa mbele, akitaka yeye na mumewe wasimamie mahari nzima. “Nyinyi mkipata hiyo mahari mnitumie mimi. Mimi na baba yenu ndio tutahangaikia hilo. Tutawapigia simu watu baadhi watusindikize ukweni.” “Nashukuru baba. Ila ningeomba ifikapo jumatano nipate idadi ya wote watakao kwenda ili kusaidia maandalizi kule kwa kina Brina.” “Mimi nina ombi moja jamani.” Akawahi Joy mke wa Junior. Wote wakamgeukia. “Naomba ukaniombee kwa Sabrina, na mimi kiziwanda wangu asimamie harusi.” Kila mtu akaanza kucheka. Walimjua mtoto wa Junior na Joy anavyopenda urembo.
Wakaanza
kumkumbuka huyo mtoto na kama atapata hiyo nafasi. “Kama namuona mwanangu yule.
Simu zake zitaanza, utamsikia. ‘Anti, si unajua nilivyo
na nywele nzuri! Sasa uniongezee na vibanioa vizuri sio kama hivi alivyoniletea
mami’.” Jacinta akafanya wacheke sana. “Hana adabu kabisa. Halafu wakati
wote utamsikia mwenyewe anasema eti nikitaka kujua mambo mazuri ya nywele, nimuulize
anti yake. Eti yeye amerithi nywele kutoka kwa Anti yake. Na wala sie mie mama
yake!” Wakazidi kucheka. “Sidhani kama Brina atakuwa na tatizo. Na endapo
ukitusaidia na wa kiume, utamrahisishia zaidi. Ana mambo mengi huyo, nafikiri
karibu na harusi itabidi nimtoe kule Singida. Atakuja kwenye harusi amechoka
sana.” Wote wakacheka. “Kweli. Ana mipango isiyoweza kusubiri. Nimeongea naye
sasa hivi, ratiba yake ya kesho ishajaa!” “Kweli huyo ni wakumtoa huko. Arudi
baada ya fungate. Na umsaidie, ikifika karibu ya siku ya harusi, mpunguzie
majukumu.” Mama yake akatoa hilo wazo, kila mtu akashangaa wasiamini kama ni
yeye kwa Sabrina. Wakazungumza hapo, wakaweka mipango mingi, yote ikawa sawa.
Mahari ya
Sabrina.
J |
ack
alimsindikiza Sabrina uwanja wa ndege siku ya alhamisi. Alitaka kuwahi jijini
ili akajisafi angalau aendane na anakoolewa. Hata siku ya mahari akitokea, basi
ajiwakilishe vyema. Kwa kuwa bado hakuwa amewaelewa vizuri watu wa kwao, na
hawakuwa wamerudisha maelewano vizuri, na kwa Sabina nako Sabrina hakutaka kuja
kukutana tena na Lela aliyeambiwa alikuwa akimtafuta, wawili hao wakakubaliana
kwa wakati huo ni heri Sabrina afikie tu hotelini. Kwanza kumfanya atulie na
jambo la mahari liishe kwa usalama bila kutibuliwa yeyote na chochote.
Alipotua uwanja wa ndege wa Mwalimu JK, akachukua
taksii mpaka hotelini maeneo ya Sinza ambako alijua angetumia muda mrefu huko
akijisafi. Alifika mapema tu hotelini na kuelekea saluni moja kwa moja. Akawaomba
wamtengeneze nywele kama walizokuwa wamemtengeneza akiwa na Tino. “Hizo
tutakesha dada yangu.” “Tunaweza kumalizia kesho au hotelini.” Hilo
wakalifurahia kujua hana haraka. Kama alivyofanyiwa wakati ule. Kusukwa huku akitengenezwa
miguu na kucha za mikono ndivyo na siku hiyo nayo akafanyiwa hivyohivyo.
Sabrina akaanza kusukwa ikiwa ni saa kumi jioni. Uzuri alikuwa ameshaosha na
nywele, wasusi wawili. Kazi ikaanza. Kila wakati akitumiana ujumbe na Jack,
wakizungumza hili na kutaka kujua kama anakunywa maji au chakula ilimradi tu
Sabrina awepo naye kwenye simu.
“Mgongo vipi?” “Nipo sawa Jack. Nimejiegemeza vizuri, usiwe na
wasiwasi.” “Nikuone.” “Acha haraka bwana Jack! Nataka nimalize, ukija kulipa
mahari ujutie kulipa ndogo.” Jack alicheka sana. “Acha masihara! Ndio utapendeza hivyo?” “Sijaja mjini kucheza
mimi. Utachanganyikiwa ukiniona.” Jack akazidi kucheka. “Sawa mama. Acha na mimi nijiandae, vizuri. Ukiniona, ujute
kuchelewa kuolewa na mimi.” Sabrina alicheka mpaka machozi. “Usiniletee mchezo.” Sabrina akazidi kucheka. “Nishakuwa na hamu na wewe.” “Hata mimi. Lakini ndio mpaka
jumamosi.” “Najuta kukubali ondoke mapema. Eti nimebaki namsubiria Emma, mimi! Kweli?
Hakika sikubali, natoka.” “Kaa hapo kwenye kochi
utulie. Baada ya nusu saa nitakupigia tena.” Wakaendelea kupigiana mpaka
saa tano usiku Jack akalemewa na usingizi. “Nenda
kalale. Kesho kazini, Jack.” “Nakuonea huruma kukuacha peke yako.” Jack
akaongea na miyayo akiwa kitandani. “Usijali. Lala. Tutaongea
kesho. Kwanza nakaribia kumalizwa.” “Sawa mama. Nakupenda Brina.” “Na mimi
nakupenda Jack wangu.” Wakacheka kidogo, Jack akalala.
Ijumaa.
Kwa
kuwa walichelewa kummaliza, alirudi hotelini saa saba usiku, akiwa hoi. Alilala
mpaka saa nne asubuhi siku ya ijumaa. Akiwa bado kitandani akampigia Jack.
Wakazungumza kwa muda mrefu tu, Jack akiwa kazini anamalizia siku na yeye aende
Dar jioni hiyo. Alikuwa akiondoka na ndege ya mwisho kabisa hapo Singida. “Nitakupitia hapo hotelini.” “Wewe si umesema mama yako
anakuja kukupokea halafu unamtoa kwa chakula cha usiku!?” Sabrina
akamuuliza. “Mara moja tu.” “Hapana Jack bwana! Wewe
umeweka mipango na mama Msindai, tulia. Ungetaka ungeweka mipango na mimi.” “Brina
naye! Nakuja tu kukuona!” “Wewe unataka mama yako aje anione kabla ya mahari?”
“Basi bwana. Lakini tumekubaliana jumamosi tunaondoka wote.” “Ndiyo, leo
nakwenda kulala nyumbani. Kesho narudi huku, jumapili tunarudi Singida, si ndio
hivyo?” Wakazungumza kidogo, wakaagana.
Sabrina Arudi
Nyumbani.
J |
ioni
Sabina alipotoka kazini, akampitia pale hotelini. “Sabrina umebadilika!
Umenikalia kitajiri tajiri!” Sabrina akacheka sana. “Kweli Sabrina! Umebadilika
sana, halafu ukapendeza mpaka unavutia! Umeongezeka kidogo na ukapendeza.”
Hakumgundua kama ni mjamzito. “Asante. Namshukuru Mungu dada yangu. Vipi wewe?”
“Mimi mzima, lakini nashangaa kwa nini hukutaka kufikia kwangu! Kwani
nilikuudhi nini?” Sabrina akacheka na kupandisha mizigo yake kwenye gari. “Hiyo
ndio nguo yakuvaa kesho?” “Ndiyo, nilikwenda kuinunua leo. Nimezunguka mpaka
nimeipata hii. Imenigarimu lakini nimeipenda sana.” “Inaonekana ni ya garama
hata jinsi ilivyowekwa!” Bado Sabina hakuwa akiamini kama ni Sabrina. Kucha ndefu
halafu safi. Amevaa vizuri juu mpaka chini. Nywele za mawimbi madogo yaliyojaa,
akaziachia, zikaanguka mpaka katikati ya mgongo. Zilikuwa rangi ya dhahabu
ambayo imetulia. Ukilinganisha na rangi ya Sabrina mwenyewe, ukweli alipendeza.
Sabina akabaki akimwangalia asiamini kama ni Sabrina.
Wakiwa
njiani Sabina akatamani sana kusikia moyo wa Sabrina aliyekuwa amenyamaza
kimya. “Nilikuudhi nini mdogo wangu?” “Wala dada. Ila nilikuwa na mambo mengi,
sikutaka kukusumbua. Kwa mfano jana usiku nilirudi hotelini kwenye saa saba usiku,
sababu yakusukwa. Na ndio maana nilichukua hoteli karibu na sehemu niliyosukwa.
Halafu pia nilijua leo nitazunguka sana mitaa ile ya pale Sinza kujinunulia
vitu vyangu. Kwa hiyo Sinza ikawa sehemu sahihi kwangu. Hukunifanyia lililo baya
dada yangu. Mbona ningeshakwambia?” Sabrina akaongea kinyenyekevu tu.
“Afadhali
kama kuna amani kati yetu. Sitaki tukosane.” Sabrina akacheka taratibu. “Kaka
atakuwepo?” “Alishaingia mapema tu, tokea jana. Baba alimuomba awahi ili
wasaidiane mambo ya pale. Wameniambia pesa ulizokuwa ukiwatumia zimewasaidia
sana.” “Afadhali kama ni hivyo.” Simu ya Sabrina ikaanza kuita.
“Nipo njiani kuelekea nyumbani Jack. Vipi wewe?” “Ndio namsubiria
mama amalize kujiandaa, tutoke. Weka video basi nikuone.”
Sabrina akacheka. “Ni giza Jack, huwezi kuniona.”
“Unanifanyia kusudi Brina!” “Hakika ni giza Jack. Piga kwa video uone kama
utaniona.” “Basi nakuamini mpenzi wangu. Ulikula jioni hii?” “Nilipata
mishikaki pale karibu ya hotelini, hapa nilipo tumbo limejaa. Nimekaa kwa shida
sababu ya shibe.” Jack akacheka. “Lakini ndio
vizuri.” “Simama mwangani unipigie kwa video nione ulivyopendeza wakati unamtoa
mama Msindai. Sio uniabishe.” Jack akacheka sana. “Ukiniona, mate yatakutoka.” Sabrina akacheka sana,
Sabina akiwasikiliza. “Jinsi ulivyopendeza baba
watoto?” “Si mchezo.” “Basi piga kwa video nikuone mpenzi wangu.” Jack
akakata.
Baada
ya muda akampigia kwa video. “Jack wewe! Ndio mpaka
suti!?” “Suti bila tai, mama. Namtoa mke wa mtu kwa dinner, lazima nimtendee
haki.” “Baba nimekukubali. Umependeza sana. Sasa na nywele ulinyoa lini?”
“Sitaki masihara mama. Nakwenda ukweni.” Sabrina alicheka mpaka machozi.
“Kwa hiyo hayo maandalizi ya ukweni?” “Kumbe! Tena
nasindikizwa kuchukua mke na Mzee Msindai mwenyewe, kijana wake mkubwa, mama
Msindai mwenyewe, na dada zangu! Lazima niwakilishe ukoo vizuri.” “Mwenyewe huyo
Jack!” Sabrina akamtania. “Sina mchezo mimi.”
Sabrina akazidi kucheka. Akamsikia mama yake akimuita.
“Wewe nenda.” “Basi nitakupigia kabla hujalala.” “Ukichelewa ujue
ndio kesho. Leo nimezunguka sana. Nipo hoi!” “Si nilikwambia uletewe gari hapo
hotelini ukaniambia hutazunguka sana wewe!” “Nilipatwa tamaa yakuzunguka.
Lakini nipo sawa. Nenda kafurahie na mama. Nisalimie.”
Sabrina akawa anaaga. “Na mimi nakusalimia Jack.”
Sabina akaingilia. “Habari yako?” “Nzuri. Nimetaka
kukusalimia tu.” “Nashukuru sana. Muwe na safari njema.” “Asante. Tutakuona
kesho.” “Kabisa. Kesho mapemaa, nakuja kuchukua mke wangu.” Sabrina
akajisikia vizuri sana. Akacheka. “Sawa Jack.
Hutanyimwa.” Wakaagana na kukata.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Umebahatika
Sabrina, anaonekana anakupenda!” “Namshukuru Mungu.” Sabrina akajibu kwa kifupi
tu, akanyamaza. Sabina naye akaona anyamaze. Akapigiana simu na marafiki zake,
wakawa wanacheka njia nzima, huku akiwaambia jinsi anavyowasubiria kwa hamu
kesho yake, nyumbani kwao kwenye tafrija ya mdogo wake, huko Chalinze. Sabrina
kimya anasikiliza tu, akajua kumbe kutakuwa na ugeni mkubwa. Akaendelea
kuzungumza na rafiki zake, Sabrina akaanza kusinzia. Mwishoe akajivuta nyuma na
kulala. Alilala asijue yuko wapi.
Akiwa
usingizini akasikia vigelegele, akashituka sana, akakaa. Akakuta mama yake,
mama zake wadogo, bibi na wageni wengine wa hapo mtaani, marafiki wanazunguka
gari wakiimba na vigelegele. Kumbe walishafika nyumbani. Sabrina akashangaa
sana. Hata hakutegemea. Akakaa vizuri akishangaa. Akamwangalia Sabina. “Wote
hao wamekuja kwa ajili yako Sabrina. Jikaze, weka tofauti zetu pembeni angalau
uonyeshe umethamini wanachokufanyia.” “Hata sikutegemea dada!” “Basi ndio
hivyo. Yote hiyo ni kwa ajili yako tu. Wasamehe wazazi, wape nafasi yakukusherehekea.”
Sabrina akageuka dirishani, bado walikuwa wakicheza sana na kushangilia. Kama
waliokuwa wakiwasubiri wao tu. Hali ya kuwa bibi harusi ikamjia. Akajisikia
vizuri, angalau kwa mara ya kwanza na yeye Mungu akampa kicheko. Akajisikia
machozi yakimtoka. Mama yake akafungua mlango kwa furaha, akatoka. Wakaimba
hapo wakimzunguka. Akafunikwa na khanga nyingi tu, ndipo wakamuingiza ndani kwa
nyimbo na shangwe. Wakacheza hapo, wakamwingiza ndani kabisa chumbani kama bibi
harusi kweli kweli.
Wakaendelea
kuimba kidogo, akamsikia baba yake akiwashukuru wote na kuwakaribisha tena
kesho yake, mchana. Wakapiga vigelegele, wakatawanyika. Mama, bibi na mama zake
wadogo wakaingia kwenye hicho chumba walichomuingiza. Wakapiga vigelegele hapo,
Sabrina akicheka. Alimuona jinsi mama yake alivyofurahi. Wakampongeza na
kumsifia jinsi alivyopendeza. Stori zikaanza, wakiwa wamejawa vicheko. Sabrina
akapotelea mawazoni wakati vicheko vikiendelea, Sabina naye akiwepo katikati yao
akiwa amechangamka kwelikweli.
Saa
sita usiku ndio watu wakaanza kutoka hapo chumbani kwenda kulala. Ndio angalau
Sabrina akamuomba dada yake akamletee pochi yake aliacha kwenye gari, maana
alikataliwa kabisa kutoka hapo chumbani mpaka kesho yake baada yakulipiwa
mahari. Sabrina akaleewa mizigo yake, akakuta Jack alipiga kama mara 7. “Jack
naye! Sasa mara 7 zote hizi kama nyumba inaungua moto!” Akajisemea moyoni.
Akamtumia ujumbe. ‘Pole mpenzi wangu. Nilipokelewa hapa
kwa shangwe, ndio wageni wanaondoka. Hata sikutegemea.’ Hapo hapo Jack
akapiga simu.
“Hujalala tu!?” “Nalalaje wakati sijajua kama mke wangu amefika
salama au la! Umenitia wasiwasi nimeshindwa kulala.” “Pole mpenzi wangu.”
Sabrina akamuelezea shamra shamra alizozikuta hapo nyumbani. “Sasahivi ndio nimeomba niletewe mizigo yangu kutoka kwenye
gari, ili nipate simu nikutaarifu mpenzi wangu kama tulifika salama. Pole.”
Akampamba hapo, Jack akatulia na kuanza kucheka. Akauliza habari za matembezini
huko alikokwenda na mama yake, akamwambia atamtumia picha ajionee mwenyewe.
Wakazungumza tena hapo wakicheka ndipo wakaagana.
Jumamosi
siku ya mahari ya Sabrina.
J |
umamosi
aliamshwa na kelele nje. Kina mama waliokuja kupika kwa ajili ya ugeni. Wakawa
wakicheka na kupiga vigelegele kila mara. Sabrina akaangalia saa ya simu, akakuta
ni saa nne kwenda saa tano, Jack alishampigia mara moja na kumtumia ujumbe, ‘ukiamka nipigie’. Akampigia. “Umeamka
salama?” “Mimi mzima. Vipi?” “Najua unauchovu wa kusukwa, kutembea na safari.”
“Nipo sawa Jack. Asante kujali.” “Karibu. Kuna kitu chochote unataka nikujie
nacho? Chochote kile.” “Naomba vinywaji mpenzi wangu. Naona wamepata wageni
wengi, watahitaji vinywaji. Soda na maji.” “Hapo utanisaidia.” Kumbe
Sabina alikuwa akiwasikiliza.
“Sawa, na nini tena?” “Labda niulize, halafu nitakujulisha.” “Iwe mapema
mama. Mzee Msandai huwa hajui kuchelewa popote. Anataka tuanze safari kwa muda
tuliopanga.” “Nitakupigia sasa hivi.”
Wakaagana. Wakati anatoka kwenye chandarua, akamuona dada yake amekaa hapohapo
chumbani. “Mbali na soda, walete nini? Naomba uwaulize hata kina mama au baba.
Nini kinahitajika?” Sabina akatoka kwa haraka. Baada ya muda akarudi. “Nafikiri
kila kitu kipo labda disposable plate, vijiko, uma, napkins na vikombe. Ili
shuguli ikiisha kusiwe na kuosha sana vyombo. Na wasivunje vyombo vya mama.”
“Sawa.” Sabrina akampigia simu Jack.
“Pole mpenzi wangu.” “Wala usijali mama. Niambie.” “Naomba msaada na
wa sakani, vijiko, vikombe, napkins na uma vile vya disposable.” “Sawa. Na nini
tena?” Jack akauliza kama visivyotosha. “Ni hivyo tu mpenzi wangu. Na hivyo vinywaji.” “Na wewe
binafsi? Hamna kitu unataka pengine umesahau? Kina Jena wanaweza kukununulia
kama ni vitu vya kike.” “Nashukuru. Lakini nina
kila kitu ninachohitaji kwa leo. Nakushukuru kwa kujali mpenzi.” “Basi nitakuona
baadaye.” Wakazungumza kidogo, wakakata.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku
hiyo Sabrina akahudumiwa kila kitu kikimfuata hapohapo chumbani kama bibi
harusi haswa. Nyumba ilijaa shamra shamra, vigelegele kila wakati. Lakini yeye
alibaki kimya tu akicheka na kutoa tabasamu bila kuweka neno. Mama yake akajawa
na shuguli! Akakuta kweli pesa yake ilifanyiwa kazi. Kulinunuliwa vyakula vingi,
nyumba ikawa inanukia tu kwa vyakula. “Naomba umwambie baba, azingatie muda
aliowaambia wageni. Ni watu wanao kwenda na muda sana.” Sabrina akamtuma dada
yake. Sabina akatoka kwenda kuweka mipango sawa. Hilo likapokelewa.
Kufika
saa sita mchana, rafiki wa Sabina kutoka mjini nao wakaingia. Kelele na fujo.
Wakatengeneza kundi lao hapo nje, wakaanza kunywa pombe walizokuja nazo kutoka
mjini. Shamra shamra, Sabrina asiamini kama yeye ndio amekusanya watu wote hao.
Akaenda kuoga na kuanza kujiandaa. Saa 9:30 jioni Jack akapiga simu kumtaarifu
wameshafika Chalinze. Sabrina hakuamini. “Mlisema saa 10
mama.” Jack akamkumbusha. “Basi kaka anakuja
kuwapokea.” Sabrina akakata. Akawaambia wageni wamefika, anaomba
wakapokelewe barabara kuu. Kaka yake akaondoka na gari ya Sabina. Kutoka
nyumbani kwao mpaka barabara kuu ni kama nusu kilometa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada
ya muda kidogo wakaona gari ya Sabina inakuja na magari mengi nyuma mpaka
wakaingiwa hofu. Idadi waliotoa na magari yao wakidhani ni familia ya kujazana
kwenye gari moja. Waliweka turubai nje, wakapanga vizuri kwa kiustadi viti walivyokodi
na meza zake. Sabina wakisaidiana na marafiki zake walitandika hizo meza na
viti wakavalisha vitambaa vyake. Japokuwa ilikuwa nje, lakini pakavutia. Kwa
asili Sabina alikuwa akikumbuka nyumbani. Kwa hiyo hawakuwa na nyumba ya
kifahari, lakini ilikuwa nyumba nzuri tu hapo kwenye huo mtaa au kijiji cha
mjini kidogo wanapoishi. Na nje walimwaga kokoto kuzunguka eneo la mbele ambako
pia walizungushia michongoma kwenye eneo hilo kubwa sana la wazazi wao, kuzunguka
nyumba nzima na shamba lao ambalo lipo nyuma ya hiyo nyumba yao ya kawaida tu, baba
yao akiweka ulinzi kwenye mifugo yake. Kwa hiyo hapakuwa na mwaya wa mifugo ya
mtu mwingine kuingia kwenye eneo lao, hata mwizi.
Watu
wa lile eneo wakabaki wakishangaa aina ya magari yaliyokuwa yakiingia hapo
ndani, kaka yake Sabina ndiye aliyekuwa akiwaelekeza kwa kuegesha. “Sikutegemea
kama watakuwa wengi hivi!” Baba yao kina Sabina akaingiwa na hofu. Gari ya
kuchukua video na kamera ikiwa na wataalamu wake maalumu na wenyewe walifuatana
na kaka yake Sabina. Wakaomba sehemu ya umeme. Wakaanza kufunga mitambo kwa
haraka kabla hata watu hawajashuka kwenye magari. Wao ndio walikuwa wa kwanza,
nyuma ya gari ya Sabina. Ndipo msafara
wa magari mengine ukafuata. Kama waliokuwa wakisubiriana, walipoingia wote na
kuegesha wote magari, wakashuka wote kwa pamoja. Habari zilishamfikia Sabrina
chumbani kuwa amekuja kuposwa kitajiri.
Wenyeji
wakaenda kuwapokea na vigelegele. Moyo wa Sabrina ukajawa furaha ya ajabu huko
ndani akijua Jack amefika. Wakakaribishwa mpaka eneo maalumu. Walionekana watu
wa maana watupu. Waliokuwa wakiwaona kwenye luninga na kuwasikia kwenye vyombo
vya habari, siku hiyo wakazi hao wa Chalinze wakapata fulsa ya kuwaona kwa
macho. Sabina alimnunulia mama yake nguo nzuri tu na alishamwambia atengeneze
nywele. Akamjia na baba yake na shati zuri na suruali. Kwa hiyo wazazi nao
walipendeza.
Dada
zake Jack wakachangamka. Walipofika tu, wakamkabidhi kaka yake Sabina kila kitu
walichoagizwa na Sabrina, na kuongeza vyakula. Walikuja na mpishi maalumu na
gari yake iliyokuwa imebeba vyakula. Mbuzi wawili ambao walishachomwa tayari, na
hawakuwa wamekatwa. Walichomwa na vichwa vyao. Wakapabwa vizuri kitaalamu. Kuku
wakuchomwa kwenye masinia makubwa sana wakawa wamefunikwa vizuri wakionekana
jinsi walivyopambwa ndani kwa ustadi. Hawakuamini. Angalau hofu ikatulia kuona
kutakuwa na chakula chakutosha huo ugeni mzima. Vinywaji ndio vilikuwa vingi
mno mpaka wakashangaa. Wakajua wamejiandaa kwa hakika.
Wachukua
video na wapiga picha walishaanza kazi yao kurikodi kila tukio. Waliwapisha
wageni wao kwenye viti, wale wa pale waliwekewa mikeka. Mzee Msindai na kijana
wake mkubwa, Junior, au waziri Msindai kama walivyozoea kumsikia kwenye vyombo
vya habari, ndio waliokuwa mstari wa mbele. Walipoletewa vinywaji kama
ukaribisho, Mzee Msindai akakataa. “Sisi tumekuja kuchukua mke. Jackson amesema
hapataliwa wala kunywewa hapa, mpaka apewe mke wake.” Mzee Msindai akaanza.
Watu wakapiga vigelegele sana. “Sasa kabla hatujatulia, tunataka kujua tupo
sehemu sahihi! Hapa ndipo alipo Sabrina? Sabrina tuliyekuja kuoa leo?
Tukishakamilisha taratibu zote, Jackson akasema huyo mtakayemtoa hapa ndio
Sabrina wake. Tukamalizana kimila, hapo hata mkitupa tu maji, tutaridhika.”
Watu wakazidi kushangilia.
Wageni
upande wakina Msindai wakaanza kuimba, “Tunataka, mke wetu! Tunataka mke wetu!”
Ule wimbo uukavuma pale. Wasomi hao wakachangamka. Kina Jacinta walikuja na
marafiki zao nao wakawasaidia kuimba na kucheza mpaka ikabidi Sabrina atolewe. Sabrina
alitolewa akiwa amependeza sana. Wote kwa pamoja wakasema, “Waoooo!” Na
kusimama kwa heshima wakipiga makofi, nakuzudi kushangilia bila hata kumzunguka
au kumgusa Sabrina. Kwa mbali walishangilia sana wakimpongeza Jack.
Kama
waliokuwa wamejipanga, wakamuona Jack anamsogelea. Kama kumpa nafasi
wakashangaa wote wanarudi nyuma kabisa kwenye viti, wote wakanyamaza kabisa,
wakazi hao wa Chalinze wakishangaa tu. Milio ya picha ndio ikazidi kusikika
wakati Jackson akiendelea kutembea kumsogelea Sabrina aliyekuwa amesimama juu
barazani kwao, sehemu maalumu waliyokuwa wameiandaa kwa ajili ya maharusi hao.
Jackson alikuwa amependeza sana, kama alivyomringishia Sabrina, na Sabrina naye
akijua ndio kwa mara ya kwanza anakwenda kukutana na kina Msindai, hakujikosea.
Wachukua
video nao walionekana ni makini. Hawakuwa wakikosea wala kuharibu utaratibu.
Walikuwa wakitembea na Jackson huku wakimpa nafasi. Jack alikwenda mpaka pale
aliposimama Sabrina, akapiga magoti. Kimya kizito kikatanda.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usikose kuwa na Sabrina kwenye wakati wake.
Usisahau, kila HATUA/BARAKA kwenye maisha, IPO CHANGAMOTO
YAKE.
Endelea kufuatilia.
0 Comments:
Post a Comment