Ndoa Ndoano...Mapinduzi Kila Kona
T |
ino
alimaliza, Sabrina asijue. Alibaki ameinama akifikiria. Akawa amezama kabisa
kwenye mawazo. “Mungu wangu! Nimejiingiza kwenye nini hiki?” Sabrina
alibaki akiwaza huku amejiinamia, akizungusha simu yake. Akatolewa mawazoni na
mkono wa Tino akimshika. “Siwezi nikaruhusu uingie matatizoni Sabrina. Nakuahidi
hakuna atakayekulaumu wala kukulalamikia kwa lolote.” “Naogopa Tino!” “Hata
iweje, sitakubali uingie matatizoni. Ni heri nipoteze kila kitu ila sio wewe.
Naomba usifikirie kunikimbia. Nakuhitaji. Ukibadili tu mawazo, ukaondoka leo,
sitakuzuia, ila ujue utanirudisha kule uliponitoa, na safari hii sitasimama tena.”
Tino akaongea kwa upole akibembeleza.
“Siwezi
kukuacha Tino. Ila nahisi kama da Lela amejipanga zaidi! Kwa nilivyozungumza na
Sabina, hawa watu wawili wanaonekana wamekusudia kupata pesa yako kwa namna
yeyote ile. Pengine alipanga kurudi na kukumaliza, sijui. Leo agutuke hana pesa
yakuendelea kuwa na huyo mwanaume wake, maana alivyoniambia Sabina ni kama huyo
mwanaume anampendea pesa Lela. Na Lela nasikia anampenda sana huyo mwanaume,
kwa anayomfanyia kitandani. Sabina anasema Lela ni kama amechanganyikiwa kwa
huyo kijana. Amemnunulia gari na amempangishia nyumba nzuri sana, tena ya pesa
nyingi. Wanaishi maisha ya hali ya juu sana. Kila weekend wanahamia hotelini.
Sasa niambie hayo maisha watakubali kuyaachia hivi hiv!” “Najua hawawezi
kukubali, na ndio maana na mimi najipanga.” Tino akajaribu kujiweka sawa.
“Maisha
yamenipa nafasi nyingine kupitia wewe. Nahitaji muda wa kupona kabisa. Na
siwezi bila wewe. Ukiondoka tu sasa hivi, ujue ndio nimekwisha. Nivumilie tu
nipone kabisa, ndipo niweke kikomo na Lela. Nitakulinda kwa kila niwezavyo.
Sitakuacha ukapata shida kifedha na....” “Naomba nikukatishe Tino. Najua
umekuwa ukitumiwa kwa uzuri wako na fedha pia.” Tino akatulia. “Najua. Sabina
ameniambia. Ameniambia kuwa hata Lela alikutoa kwa mwanamke mwingine kwa
kupambana haswa. Najua. Lakini sio mimi Tino. Nina shida na pesa, lakini nataka
kuanzia mwanzo naomba unielewe, sipo na wewe kwa ajili ya pesa yako. Maombi
yangu ni kukuona unasimama na kuweza kujitegemea.” “Basi jua bado sijaweza
kujitegemea Sabrina.” Tino akahakikisha hilo anaweka sawa na wazi kwa Sabrina.
“Bado
Sabrina. Hata kama unaniona natembea na kufanya mazoezi, ujue zipo nyakati
naingiwa hofu kabisa. Nashindwa hata kulala, wakati mwingine naota nikiwa
nimefungiwa kwenye kile chumba gizani. Kitu pekee kinachonifanya nitulie na
nirudi kulala, ni pale ninapofungua macho na kuona taa inawaka na wewe upo pale
na mimi. Na ndio maana ulipotaka kurudi kulala chumbani kwako hata siku ile Lela
alipokuwepo pale, nilikutaza usiondoke kurudi kulala chumbani kwako, uendelee
kuwepo na mimi. Najawa hofu bila wewe. Naomba Lela asifanikiwe na kwako pia.”
“Hawezi Tino.” “Unauhakika? Maana Lela anajua kutumia kila njia ili kunifanya
niwe chini ya himaya yake. Mpaka kwa vitisho. Sasa nataka kujua kama unao
uhakika?” Sabrina akatingisha kichwa kukubali.
“Ila
tuwe makini Tino.” “Ndio maana nataka tutoke kabisa hapa. Tuende sehemu ambayo
hakuna atakayetufahamu ila mimi na wewe tu. Nitaanza upya kabisa matibabu
yangu, na daktari mpya. Tutaishi mimi na wewe tu mpaka niwe na uhakika nimepona
kabisa ndipo nitarudi huku na kumalizana kabisa na Lela.” Sabrina akataka kujua
juu ya hatima yake na yeye, akaona awe mpole. Tino alikuwa amekaa mbele yake,
kijana anayevutia, anamlilia anamuhitaji. Yeye Sabrina! Sabrina akalainika
kabisa. Akajiambia atajua mbele ya safari.
“Sawa.
Ila naomba tusiongozane wote polisi au kwa mwanasheria wako Tino. Kwenye mambo
kama hayo naomba nisionekane kimbelembele. Nitazungumza na watu wa hoteli kama
wanausafiri au nitakuitia taksii.” “Sawa. Nitakukuta hapa hotelini?” “Si
umesema tunaondoka kesho?” “Hapana. Naona nimalizane na haya mambo, tuondoke
kesho kutwa.” “Basi naomba wakati unashugulikia hayo mambo mimi nikabadili hizi
nywele. Sitachelewa kurudi. Nitafumua usiku wa leo, kesho nikienda ni kusuka
tu, nakurudi.” Akamuona Tino ameinama.
“Sitakawia
kurudi Tino. Nilivyo hivi sio sawa. Hata nywele zinanuka?” “Kweli utarudi
Sabrina?” Sabrina akashangaa wasiwasi wake. “Kwa nini nisirudi Tino!?” “Labda
umeingiwa hofu kusikia mpaka mambo ya polisi!” “Sio mimi Tino. Nipo na wewe kwa
kuwa mimi nimekubali. Huwa ninashida nakufungwa na ahadi zangu mwenyewe.
Ingekuwa sio hivyo, ningeshaondoka pale kwako muda mrefu sana. Kumbuka
tuliachwa mimi na wewe tu pale, bila pesa huku Jack akiniita Singida. Si ningekuacha
na kukimbilia Singida? Lakini nilibaki na wewe nikiwa sijui mwisho wake.
Nimekuahidi nitakuwa na wewe mpaka tukubaliane, ujue nitafanya hivyo.” Tino akabaki
kimya.
“Unajua
ni kwa nini Emma, alinibembeleza sana anioe?” Kimya. Tino akamwangalia. “Nikwakuwa
nilimvumilia Emma, nikikwambia nilipopita naye yule kiumbe, usimuone anakuwa
kama mwehu akihesabu siku. Ni kwa kuwa anajua wazi, hakuna mtu anaweza
kumvumilia kama mimi. Na sikuchoka mpaka yeye mwenyewe aliponiacha kinyama. Na
ndipo muda huo tukiwa tumeachana, sio wakati tupo naye, kipindi aliponiacha ndipo
nilipochoka, na kupigia mstari mahusiano ambayo hayakuwepo. Na ndio maana
alipotaka turudiane huku akituma marafiki zake wambembelezee nilikataa Tino.
Nikajisikia sina chakumpa tena Emma. Simu ya mwisho, Emma alilia Tino. Akiomba
msamaha na kukiri yote aliyonitenda mabaya, nikiwa hata sijamlalamikia hata
mara moja ila kunyamaza na kumuacha tu. Alikiri na kutubu kwa machozi.
Akakumbuka siku alizokuwa na shida, nikasimama na yeye. Misiba niliyohudhuria
kwao mpaka kifo cha mama yake kilichomuathiri sana, nikasimama naye mpaka
akaweza kurudi kazini. Maana alipatwa kama depression akaacha kwenda kazini
kabisa. Akawa hawezi hata kutoka ndani. Kitandani tu, mimi nikimuhudumua.”
“Nilipoona
atapoteza kazi, nikaamua kumwandikia barua yakumuombea likizo ya dharula, nikaipeleka
mimi mwenyewe ofisini kwao, yeye hana habari kwa kuomboleza. Kuja kurudi
kazini, meneja wake mwenyewe akamwambia ile kazi bado ipo kwa sababu nilikwenda
nikazungumza nao, nikajaza fomu za likizo na kuandika barua pia ndio maana
anayo ile kazi. Hakuamini Emma. Sikwambii haya kwa kujivunia, ila
kukuhakikishia kuwa, nikikuahidi kitu, jua nitafanya.” Sabrina akaendelea kwa
upole tu.
“Jack
nimezungumza naye na kumwambia nitamtafuta baada ya mwezi na siku chache
kuanzia sasa. Hiyo itakuwa miezi mitatu tangia tukubaliane.” “Ulikubaliana na
Lela, Sabrina. Sio mimi. Huo muda ni wako wewe na Lela.” “Tino! Ulitaka nikae kwa
muda gani!?” “Ulisema mwenyewe mpaka tukubaliane.” Sabrina akabaki akimwangalia.
“Naomba usifikirie kuondoka sasa hivi, naomba jipange kuwa na mimi katika kila
khali.” “Mpaka lini Tino!?” “Mpaka tutakapokubaliana vinginevyo.” Sabrina akabaki
kama asiyepata jibu lake kwa hakika, na Tino alijua ila na yeye ni kama
alipatwa na kusita. Akashindwa kuwa muwazi zaidi ya hivyo.
“Unaenda
wapi sasa?” “Naanza kufumua nywele ili kesho nisikawie saluni. Uje unikute humu
ndani, usipandishe pressure nikichelewa.” Tino akacheka tu, Sabrina akahamia
bafuni. Baada ya muda Tino akamgongea. “Nakwenda mazoezini. Wana gym nzuri sana
huko chini.” “Unataka nikusindikize?” “Hapana. Malizia tu.” “Sasa usinogewe
ukachelewa kurudi Tino. Mimi nakujua. Uje tulale mapema, kesho uamke na
nguvu.” Akamsikia akicheka huku
anaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada
ya mazoezi alirudi, akaoga akatoka kukaa sehemu yenye makochi hapohapo chumbani
akiangalia tv, wakati Sabrina akioga na yeye. Alipomaliza akatoka na kumfuata
Tino. “Nywele zimeshakauka?” “Ndio nilikuwa nafunga mabutu huko bafuni.” Akakaa
chini kabisa kwenye miguu yake, akaipakata na kuanza kuifanyia masaji. Tino
akajiegemeza kwenye kochi vizuri. Sabrina akaendelea kuiminya taratibu huku
akipitisha vidole katikati ya vidole vyake vya miguu. Tino akawa ametulia
kabisa. Sabrina akaendelea kwa muda, taratibu tu. “Twende ukalale kitandani
Tino.” “Daah! Hivyo unavyonifanyia najisikia vizuri!” Sabrina akacheka.
“Hamia
kitandani ukalale. Bado huo mwili unahitaji muda wa kutosha kupumzika.” Tino
akarudi bafuni kusafisha meno, Sabrina akazima tv na taa kwenye ile sehemu
pembeni ya sehemu ya kulalia, akaenda kukaa kitandani sehemu ya miguuni huku
taa za hapo pembeni ya kitanda zikileta mwanga wa kiasi hapo kitandani. Tino
hakutaka kurudi kulala gizani tena, ilikuwa lazima alale angalau taa ndogo
ikitoa mwanga. Akatoka bafuni na yeye akapanda kitandani. “Njoo ulale hapa.” Tino akionyeshea pembeni yake. “Sio unanitaka
huku miguuni ili nikufanyie masaji!?” Akauliza kwa aibu kidogo akicheka.
“Hapana. Nakutaka hapa.” Tino akapigapiga ubavuni kwake upande wa kushoto.
Sabrina akaangalia huku na tabasamu la soni, usoni.
Tino
alikuwa amelala chali. Kijana huyo aliyemtoa mate hata Lela! Ngozi nzuri. Ndio
ametoka saluni kufanyiwa usafi wa nywele na ndevu. Akatengenezwa vizuri na
ukweli alivutia kumtizama. Halafu yupo na Sabrina! Msichana wa kawaida kabisa!
Hana mambo mengi makubwa kwenye mwili wake. Kwanza ni kama alinyimwa mwili.
Hana rangi ya mwili ya kuielezea na kumsisimua mtu. Ni msichana wa kawaida
kabisa. Mpaka awe na wewe, umfungulie mlango kwenye maisha yako, ndipo
atakayokufanyia, utashindwa kusahau. Amemuacha msomi Emma, mwenye ndoa na
mtoto, kubaki akihesabu siku tangia aondoke kwenye maisha yake. Sasa Tino
anamwita kulala ubavuni.
Akaweka
miguu ya Tino pembeni, akajivuta upande alipoitwa. Hakujua alale chali, au
ubavu. Ubavu wa kulia au kushoto! Akacheka tena alipofika hapo. Alishalala na
Tino, lakini wakati wote alilala miguuni. Leo amekaribishwa ubavuni! Akanyanyua
mashuka, akaingia ndani, akajivuta mpaka hapo ubavuni, akajilaza kugeukia
ukutani. Akamsikia Tino naye akimgeukia. Akamuweka sawa lile chuka mabegani.
“Sasa hiyo khanga kichwani, utalala vizuri kweli?” “Inabidi. Kesho nitaenda
kuzisuka ili nilalie kofia laini ya kulalia.” Akahisi akimchezea vinyweleo vya
chini ya ile khanga, kwenye shingo karibu na kichwani. Sabrina alisikia raha ya
ajabu, akatulia kabisaa.
“Nakushukuru
Sabrina. Asante kwa kila kitu. Na ninaamini kila kitu kitakuwa sawa.” “Naamini
hivyo Tino.” Sabrina akaitika taratibu. “Geuka nikwambie kitu.” Sabrina
akageuka na tabasamu usoni. “Nini?” Akauliza
taratibu akiwa amelala wakiangaliana. Tino akapitisha kidole juu ya nyusi zake.
“Ukiwa hivi pembeni yangu, najihisi naweza kila kitu.” Sabrina akacheka
taratibu akifikiria. “Mbona kama huamini?” “Najua upo kwenye kipindi kigumu
Tino.” “Kwa hiyo unaamini nakutumia tu, nikipona ndio basi?” “Sitegemei kitu
cha tofauti kutoka kwako Tino. Nipo hapa kama mfanyakazi tu.” “Wote tunajua
hiyo si kweli Sabrina!” Akapinga Tino.
“Ulinitumikia
kabla ya kulipwa. Na ulilipwa mshahara aliochagua Lela, na bila kukuomba ulitumia
hiyo pesa yote kunihudumia mimi. Tena kwa vitu vilivyokugarimu, ulivyojua
vitaniongezea mimi nguvu. Umenilea kwa
upendo japo ulishauriwa unidharau kama wengine waliomsikiliza Lela. Walianza
wengi tu hapo mwanzoni. Wakavunjwa moyo na Lela mwenyewe kwa namna moja au
nyingine. Kila mfanyakazi aliyemleta kwangu, alihakikisha anamfitini na mimi
kwa kuhakikisha ananihudumia mimi kama takataka. Waliobaki kwa siku mbili tatu
alianza kuwanyima mshahara ili waondoke.” “Haiwezekani Tino!” Sabrina akashangaa
sana.
“Kabisa.
Wewe si wa kwanza. Na usifikiri ni bahati mbaya. Anafanya kwa kusudi kabisa, kuvunja
mahusiano yangu na kila kiumbe anayetaka kunikaribia ili yeye ndiye abakie akinimiliki
na kujinufaisha zaidi na zaidi bila kutosheka. Lakini wewe ulibaki ukiwa huna
pesa wala ahadi yeyote ile, Sabrina. Kwa hiyo upo na mimi najua sio kwa sababu
ya kazi.” Sabrina akashindwa kumwangalia. “Nitalienzi hilo daima
Sabrina. Sitakaa nikasahau.” “Tumshukuru Mungu alinileta kwa wakati na kunipa
uwezo wakufanya kitu sahihi mpaka ukawa hivyo.” “Niamini nikikwambia sisahau
kumshukuru Mungu, Sabrina. Hapakuwa na jinsi ya mimi kutoka pale isipokuwa
Mungu kukutumia wewe. Ukawa jasiri kuliko wanaume wote waliopita pale na
kunizunguka. Uliweza kummudu Lela na kelele zake zote wakati aliweza kuwamudu
mpaka jamaa, ndugu na marafiki zangu! Nikabaki vile peke yangu mpaka ulipokuja
wewe. Nakushukuru Sabrina. Nataka ujue namaanisha.” “Najua Tino. Karibu.” Akataka
kumbusu midomoni, kwa haraka sana Sabrina akakwepesha akainama kama ambaye
hajaelewa.
Pakazuka
ukimya kama Tino na yeye amepigwa na bumbuwazi. Lakini Sabrina akaweka mkono kifuani
kwa Tino. Alikuwa amevaa singlendi. Nguo ndogo ya ndani ya juu, baadhi ya
nywele za kifuani zikawa zipo kwa nje. Taratibu kwa makini akaanza kupitisha
vidole kama kutaka kuzirudisha ndani ya ile nguo nyepesi aliyovaa Tino.
Alifanya hivyo kuzunguka juu ya kifua. Alipofanikiwa kuziingiza zote, Tino
akashangaa anazitoa tena kwa vidole, taratibu. Tino akacheka nafsini kwake. Akajisahau
hapo kifuni kwa Tino akichezea hizo nywele za kifuani na kumthibitishia Tino ni
kweli aliziacha hapo kwa ajili yake. Alifanya hivyo kwa muda, Tino akiwa
ametulia kimya mwishoe akaona ametulia, mkono umebaki hapo kifunia. Akajua
anasinzia. Sabrina akasikia busu juu ya kichwa chake, akapotelea usingizini
hapo ubavuni kwa Tino mkono kifuani.
Akiwa
katikati ya usingizi akasikia. “Sabrina!” Alikuwa Tino akimuamsha. Akaamka. “Nataka
kwenda kujisaidia. Samahani, utarudi kulala.” Sabrina akajisogeza pembeni na
kutoa mkono kifuani. “Nikuletee chupa? Nilikuja nayo.” “Sitaki kukusumbua. Acha
niende tu chooni.” “Sio usumbufu.” Sabrina akatoka kitandani na kwenda kuleta
chupa aliyokuwa akiitumia Tino akiwa mgonjwa hawezi kutoka kitandani. “Mbona
kama hujalala!?” Sabrina akamuuliza maana alionekana kama ambaye hajapata hata
lepe la usingizi! Lakini Tino akatoa tabasamu tu bila yakujibu. “Acha kuwaza
bwana!” Sabrina asijue kinachomsibu mwanaume huyo aliyemchezea nywele za kifua.
Bila kuwaza, akajisahau kama Tino sio mgonjwa kama vile alivyokuwa zamani, akamfunua
shuka taratibu akiwa ameinama pale kitandani, wakati anataka kumtoa suruali
ndipo akaelewa kwa nini halali. Akasita, Tino akimtizama. “Huyu si alipatwa
na stoke! Nguvu za kiume anazipata wapi?” Akajiuliza Sabrina akiwa
anababaika pale mbele ya Tino.
“Au
ulitaka ukajisaidie chooni?” Ikabidi Sabrina aulize. “Nilifikiri hutaki
nisumbuke!” Akajibu Tino taratibu tu. Sabrina akajua amefanya kusudi kukubali
chupa ya kujisaidia pale kitandani ili amuone. Ikabidi akae pembeni yake.
Taratibu akamtoa ile pensi aliyokuwa amevaa ya kulalia. Akatamani afunge macho
baada ya kushusha nguo ya ndani Tino naye akimsaidia kunyanyuka ili ashushe
zile nguo kirahisi. Tino ametulia kimya akajua anamtizama. Inabidi sasa ashike
na kulengesha kwenye chupa. “Inabidi kunyoa na hizi nywele Tino. Unatisha
huku.” Sabrina akamshika vizuri, akaweka kwenye chupa, baada ya sekunde chache
kweli Tino akakojoa mkojo wa kutosha tu. Sabrina akatingisha kuhakikisha hakuna
mkojo tena. Kama kawaida yake, akatamani usiku huo abadili na kumwacha kama
wanaume wengine, lakini alishamzoesha kumkausha kabisa kama mtoto wa kike, tena
yeye mwenyewe akimpa sababu ya kwa nini anafanya hivyo. “Ili lisikudondokee
hata tone la mkojo Tino, ukatonesha vidonda.” Sabrina mwenyewe ndiye
aliyeanzisha na kumzoesha kumfuta baada ya kujisaidia haja ndogo. Usiku huo
amwambie amepona! Akaona hapana, akashika tena na kukausha taratibu, Tino
akimwangalia tu bila hata kutaka kumsaidia.
Alipomaliza
chupa akiwa ameeweka chini ikabidi kurudishia nguo ya ndani na ya juu. “Nimeyataka
mwenyewe! Sijui nilikuwa usingizini!” Akajisuta Sabrina wakati akirudishia
nguo. Akamfunika. “Nakwenda kumwaga mkojo.” “Asante.” Akashukuru Tino lakini
Sabrina akajua anamcheka moyoni. Alifika bafuni usingizi umepaa. Akaanza
kucheka kila akikumbuka. “Mmmh! Tino si mchezo.” Akasifia Sabrina akiwa
bafuni. “Sijui ndio ananifikishia ujumbe kuwa yeye bado mwanaume!” Akaendelea
kuwaza akiwa bafuni, mwishoe akaona atoke tu.
Anarudi kulala ubavuni au chini
miguuni! Akaanza kujiuliza Sabrina. Mkono kifuani, au arudi kugeukia ukutani!
Akakubaliana na hilo wazo. Akamzunguka na kwenda kulala ukutani. Na yeye bila
hila akamgeukia. “Nilijisikia vizuri vile tulivyokuwa tumelala kabla sijakuamsha!”
Akaanza Tino huku akimchezea tena shingoni. Sabrina akasikia kucheka. Pia
alihisi kitu kimemgusa sehemu za chini. Hakujibu. “Utafanya nijutie kukuamsha.”
“Naona kama nakufanya hupati usingizi Tino. Nakubana sana.” Akaongea huku akijigeuza, kumgeukia yeye. “Sidhani
kama nakosa usingizi kwa kubanwa, nahisi ni hizi juisi za virutubisho unazonipa
ndizo zimeondoa uchovu.” “Si ni kitu kizuri? Au nipunguze aina hii ya matunda!
Nilisoma wakasema ni nzuri kwa kukurejeshea nguvu. Ndio maana nilikuwa
nikikusaigia vingine kwenye chakula na kusaga unakunywa kama juisi.” “Sasa
upunguze tena nirudi sina nguvu! Huoni ni afadhali kunambadiliko sio unanishika
nakuwa kama mtoto mdogo wa kiume!?” Sabrina alicheka sana mpaka akajificha hapo
ubavuni.
“Eti
Sabrina?” Sabrina hakutoa kichwa. “Mimi nilijua utafurahia kuwa kazi yako imezaa
matunda! Halafu mwenzangu unataka unirudishe kama joka la kibisa!” “Bwana Tino!
Mimi simaanishi hivyo. Nilikuwa naongelea kukosa kwako usingizi.” “Huko
kunasababishwa na kunyimwa busu, wala si vinginevyo.” Sabrina akazidi kucheka
usiku huo. “Wewe Tino umepona bwana! Acha mimi nikauze alizeti.” Tino na yeye
akaanza kucheka. “Mimi naona unakimbia matokeo yako wewe mwenyewe!” “Tulale
bwana Tino!” “Basi rudi hapa kifuani.” Sabrina akajitoa pale alipojificha.
“Unamaanisha nilale kabisa hapa juu?” “Vyovyote vile utakavyo wewe.” “Bwana
Tino! Utanifanya nishindwe jinsi ya kulala.” “Basi mimi nafunga macho. Njoo
Sabrina wangu.” Akiwa anacheka, akajirudisha. Lakini safari hii nusu ya mwili
kifuani. Akamsikia akipitisha vidole kidogo tena juu ya kifua chake, na yeye akamkumbatia
vizuri, wakalala.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati
Tino akifanya mazoezi asubuhi hiyo, Sabrina akajua uzunguni hapo kwenye hiyo hoteli,
hatapata mtori. Alibeba chupa za chai, akapanda gari bila kuoga akaenda kutafuta
baa ambayo atapata mtori, na mchemsho. Akanunua na kurudi kwa haraka. Tino anarudi
chumbani kutoka mazoezini, akakuta mtori na milk shake ametengenezewa na
Sabrina. Akacheka. “Vinavutia kwa macho na matokeo yake pia siyo mabaya.” “Mimi
wala sikusikilizi Tino. Naomba ule ndio ukaoge, uondoke ukiwa umeshiba.” Tino
akawa anacheka. “Ninavyoringiwa Tino mimi!” Sabrina akawa anacheka tu huku na
yeye akila.
Walikula
Sabrina akamwambia yeye ndio atangulie akaoge. “Ile ahadi ya usiku ya kunyolewa
sijui bado ipo!?” “Mimi nilikuwa usingizini wala sikuwa najua nini nafanya.”
Tino akacheka sana huku akielekea bafuni akichechemea bila fimbo yake. “Bisha
tu Sabrina. Ila ujue uongo nao ni dhambi kama dhambi nyingine zote.” Sabrina
akazidi kucheka.
Alioga
Tino akatoka msafi na amependeza. “Urudi Tino, sio ukafichwe huko.” “Wewe si
hunitaki bwana! Sasa wivu wa nini?” “Tino!” “Narudi mama, niende wapi mimi
watakaponipokea kama kwenye mikono ya Sabrina wangu?” “Ndio mimi nakushangaa.
Urudi hapa.” “Nitakuwa nakupigia ili ujue nilipo, sasa na wewe sio kina Jack
wakubadili mawazo, unikimbie.” Sabrina akacheka sana. “Nikauze alizeti?” “Ndio
naona unapotaka kukimbilia huko! Rudi hapa, kama ni hizo alizeti, tukauze
wote.” “Singida huko?” “Mbona nitakufuata tu, nani hataki starehe
yakukojoleshwa?” Sabrina alicheka mpaka akaishiwa nguvu.
“Hakika
Tino umepona wewe! Twende tukauze alizeti.” “Kwani mimi nitakataa! Nakufuata
popote uendapo.” Sabrina akazidi kucheka. “Lakini hivyo sivyo nilivyoambiwa juu
yako Tino! Mimi niliambiwa wewe mpole sana Tino. Huwezi hata kuzungumza!” “Kwa
wanao niudhi.” “Kwa hiyo Sabina alikuwa anakuudhi?” “Najua amekwambia sana tu.
Yeye hajaolewa, hashituki yupo club na mke wa mtu mpaka asubuhi hata hashituki
wala kumshauri mwenzie arudi nyumbani! Na yeye Lela, Sabina akamfanya kama
Mungu wake, huna unalomwambia juu ya Sabina. Kidogo tu, utasikia hata Sabina
kasema! Nikaona wote wananichezea akili, nikaachana nao wote wawili na kundi
lao wote.” Sabrina akafikiria kidogo.
“Hivi
Sabina anapenda starehe eeh!” “Kwani wewe humjui dada yako?” “Sio sana Tino.
Hata huko kwetu Sabina ni kama Mungu mtu. Anaheshimika sana kwa elimu aliyopata,
kazi nzuri aliyonayo na alipofika kwenye maisha. Kujenga nyumba kama ile na
kununua gari ya kifahari vile! Huna utakachosema nyumbani juu ya Sabina.”
“Najua kwenye hiyo NGO anayofanya kazi ya mambo ya reseach, analipwa pesa
nzuri sana. Sasa eti ndio Lela, sekretari wa kampuni ya kawaida, alikuwa
anakimbizana naye, wakati mwenzake analipiwa mpaka safari za nje ya nchi!
Asimuone Sabina ana kitu, hata kama mwenzie amerudi nacho kutoka kwenye safari
zake za nje ya nchi, mbona na yeye Lela atanunua! Utadaiwa hiyo pesa mpaka
uitoe tu.” Sabrina akanyamaza.
“Nenda kasuke upendeze Sabrina wangu.” Sabrina akacheka kinyonge, akasimama. Akajiweka sawa kidogo na kupasafisha pale, wakatoka. Akamshusha Tino kituo cha polisi, yeye akarudi Sinza kwenye saluni alizozoea.
Kwa
Sabrina.
S |
abrina akafika
saluni akiwa amepewa pesa yakutosha. Akaambiwa na Tino asuke atakacho, ilimradi
yeye aridhike. Sasa kufika saluni, akakutana na mitindo mipya, nywele mpya
zimeingia mjini. Akaanza kubabaika. Msichana aliyempokea akaanza kuuza biashara.
“Kwa rangi yako hiyo, urefu wa nywele zako na kasura hako, hii nywele ndio
itakufaa.” “Wewe umenena, lakini ili awake vizuri, changanya na goldi kidogo.”
Mwenzake akadakia. “Msije mkanifanya kinyago na rangi yangu jamani!” Sabrina
akawatahadharisha. “Sasa unataka rangi gani?” “Nyeusi.” “Hee!” Kila mtu
akahamaki. “Kwa unauzee gani?” “Unaficha mvi?” Kila mmoja akaongea lake.
Sabrina
katokea shamba. Akajiambia labda mambo mapya. “Usimtie shemeji vishawishini
mdogo wangu. Upo naye, lakini macho yapo kwa warembo wa nje! Wewe bado mdogo.
Mwili wako mzuri hujaharibika na machips ya mjini!” “Bwana mtoto kama mzungu!
Hana hata nyama ya mgongo!” Sabrina akaanza kucheka asijue kumbe na mwili wake
unaweza kuja kusifiwa siku moja. Akamwagiwa sifa hapo wee, mwishoe akakubaliana
na staili waliyomchagulia. “Nywele ndefu bebi! Shemeji apate kwa kushika.”
Wakaanza upya maneno ya kumpamba, Sabrina hana mbavu kwa kucheka. Akaambiwa kwa
aina hiyo ya nywele, lazima wasusi wawe watatu ili wamalize mapema. Nywele
akaambiwa zile 100% human hair. Kutajiwa bei, akapima na muda atakao kaa nazo,
akaona ni sawa.
Kazi
ikaanza ya kusukwa. Nywele ndogo ndogo mpaka urefu wa nywele zake, kisha
zinaachwa. Na mawimbi juu. Sabrina akaomba atengenezwe kucha za miguu, na
asuguliwe nyayo. Huku anasukwa, huku anaoshwa miguu iliyokuwa bandani kwa ng’ombe
ikikanyaga kinyesi cha ng’ombe takribani miaka mitatu! Sabrina amerudi kwenye
viwanja vya mjini, acha asuguliwe nyayo na kutolewa uchafu kwenye kucha.
Akasafishwa vizuri na kwa kina, na kupakwa rangi. Kwa asili alikuwa na kucha
ndefu. Kwa hiyo hakubadikwa. Hata mkononi alitaka apakwe tu rangi. “Mambo si
hayo mdogo wangu!” Wakaanza kumsifia tena. “Ukirudi leo lazima shemeji
akusahau.” Sabrina akazidi kucheka huku akisukwa.
Akajisahau
Sabrina kwa raha ya kurudi mjini. Akapita muuza nguo. Kila mtu akachangamkia.
Wengine wakataka mkopo, wateja wengine wakakimbilia ndani kujaribu. Sabrina
akabaki ametulia kimya, wasusi wawili waliingia ndani kujaribu nguo. “Sasa hizi
zilizobaki za ‘miss world’ wetu, hizo hapo dada.” Akamsogezea Sabrina, akacheka
huku akizipokea. Anaanza maisha mapya, nguo zote aliacha kwao. Kwanza
alishazichukia. Ndio zile anazomnyanyasa nazo Emma. Akajiambia hazitaki tena,
ndio mwanzo wa muonekano wa Sabrina mpya anayefanya maamuzi magumu. Akachukua
baadhi alizopenda, akaingia ndani na yeye kujaribisha. Zote akapenda. Akalipia,
na kwenda kuziweka kwenye gari ili asisahau. Akarudi kukaa kuendelea kusukwa.
Kwa Tino.
T |
ino yeye
siku yake iliharibika mara tu aliposhushwa kituo cha polisi na Sabrina na
kumpigia simu kabla hajaingia kituoni na kumkosa. Akampigia kama mara tatu,
Sabrina hakupokea. Akajiambia labda atarudisha simu yake, asiingie ndani,
akabaki amesimama hapo nje ya kituo cha polisi akijua Sabrina atampigia, lakini
wapi. Lisaa likapita Tino yupo nje ya kituo cha polisi anasubiri simu ya
Sabrina. Baada ya nusu saa nyingine, Max akampigia kumuuliza amefikia wapi.
“Nipo hapa kituo cha polisi Osterbay.” “Upo na nani?”
Akauliza na kuzidi kumchanganya Tino. “Iweje Sabrina awe ndio amenitoroka!”
Akawaza Tino. “Nitabaki peke yangu!” Gafla akapata panic attack.
Hofu kubwa ya gafla ikamwingia. Kutoka kufungiwa kwa muda mrefu gizani, leo
yuko peke yake mwangani! Tena na hofu ya kuuwawa na mkewe pamoja na mpenzi
wake! Halafu anajikuta peke yake! Akazidi kuingiwa hofu. “Tino?” Max akaendelea kutaka kujua. “Nipo peke yangu.” Akamuhurumia. “Basi nakuja sasa hivi ili tusaidiane.” “Nashukuru kaka.”
Baada ya kama dakika 25 nyingine ndipo Max akawasili. Akamkuta amesimama nje
juani, jasho linamtoka, simu sikioni. Akamuona amekuwa mwekundu. Akajua
anazungumza na Lela.
Akamuona
anarudisha simu mfukoni. “Kwema? Nimefurahi kukuona kwa macho, sasa hivi
nasadiki kama ni wewe.” “Kwema kaka.” Wala hakuonekana kama ni kwema.
Wakapeana, hugi la kiume, akabaki akimshangaa. “Ushamaliza ndani?” “Bado
sijaingia.” Akashangaa kidogo. “Twende tuingie.” Wakaongozana, Tino akitumia gongo
upande mmoja. Amepoa kama siye waliyezungumza jana wakipanga mipango. Wakafika
mapokezi, macho kwenye simu. Ikabidi askari aulize. “Niwasaidie nini?” Kimya
kama aliyegairi. “Tino!” Max akamshitua. “Unajua nini, haina maana tena. Hata
wakiniua kesho, hivi nilivyo ninafaida gani? Ni heri waje hata usiku huu
wanimalize nipumzike.” Tino akatoka pale. Max na yule askari wa mapokezi
wakabaki na mshangao wakimsindikiza kwa macho.
Ikabidi
Max amfuate nje. “Ni nini kinaendelea Tino?” “Juu ya nini?” Tino akauliza kwa
ukali. “Kwa nini unakuwa mnafiki na kushindwa kuniambia? Tatizo ni pesa au
nini? Kama unataka nikulipe na kwa kuniambia ukweli basi nitajie garama zake.” Max
akapandisha nyusi zote juu kwa mshituko. “Umeniona nachechemea hapa. Mdomo bado
haujarudi kama nilivyokuwa. Mkono wangu nashindwa hata kuandika sentensi nzima.
Leo nakuja kudai nyumba! Ili nani aende akaishi hapo? Mimi peke yangu! Hivi
unajua mimi ni yatima na sina ndugu? Ndugu na marafiki niliowategemea ni kama
nyinyi mlinitelekeza, nimebaki peke yangu. Nataka nyumba na mali ili vinisaidie
nini? Si ni heri nife yaishe huyo Lela na mwanaume wake waishi hapo na watoto
wao? Kama ulitegemea na leo nikulipe, sina kazi ya kukupa. Katafute wateja
wengine. Acha nikafe mbele ya safari. Jiandae na malipo yako makubwa ya mwisho
baada ya kifo changu wakati ukimsaidia Lela. Lakini mimi sina kazi.” Tino
alimfunga mdomo yule Max, akatembea akichechemea mpaka akavuka barabara Max akimtizama.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment