Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 8. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 8.

 

Sabrina akamuona Tino anaanza kusinzia. Akajua amechoshwa na mapenzi waliyofanya, na siku hiyo ambayo kwake ilikuwa ngumu zaidi, akidhani amemkimbia. “Twende tukale kwanza ndipo turudi kulala.” Akamwangalia na macho ya uchovu bila ya kujibu. Akamuhurumia. “Laza kiti, ulale kidogo.” Bila kubisha akajilaza kabisa. Sabrina akaona ni heri akanunue chakula cha palepale hotelini. Wakarudi mpaka hotelini Tino bado amelala kitini. “Tino!” Akamgusa taratibu, akawa amelala, hana habari. Akashuka na kumfuata upande wake. Akaanza kumbusu. Akaamka akicheka. “Kwa uamshwaji huu, mimi naona niendelee kulala tu.” “Tumefika bwana. Twende.” Akatoka garini.

“Si nilishaoga? Au natakiwa kuoga tena?” “Hapana. Ila ule angalau milkshake. Kama ungekuwa hujachoka, ningeagiza viazi vya kupondwa na nyama.” “Nimechoka Sabrina. Acha nilale tu.” Walipofika chumbani Sabrina akampa milkshake, akaenda kusafisha mdomo na kubadili nguo, akapanda kitandani kama mfu. Sabrina alimalizia kuweka chumba sawa, akaoga tena akapanda kitandani. Kwake ilikuwa siku nzuri sana. Alijua ametengenezwa vizuri akapendeza. Anammiliki Tino. Mwili huo uliokuwa haujashikwa kwa muda mrefu, siku hiyo Tino akautendea haki na kuusifia. Max amemkubali na kumsifia. Kesho anapewa leseni ya kuendesha. Hapo alipo amelala kwenye hoteli nzuri. Na anauhakika wa kuendelea kulala pazuri. Pesa ya Tino ipo na Max amehalalisha kuitumia ipasavyo. Akajivuta mpaka kifuani kwa Tino, kama aliyekuwa akimsubiria, akashangaa Tino anamuweka sawa akiwa vilevile amelala, akamkumbatia vizuri. Sabrina akambusu hapo kifuani. “Asante.” Akashukuru Tino na kupotelea usingizini.

Tino&Sabrina.

A

subuhi aliamka akamkuta Tino ni kama anamsubiria. Sabrina akacheka. “Hivi wewe ni kiumbe gani ukilala usiku kucha hugeuki!?” Sabrina akacheka. “Hata nyumbani walikuwa wakinishangaa.” “Mimi nilikuwa nikilala nageuka sana mpaka nipitiwe na usingizi. Kuugua na kushindwa kujigeuza mwenyewe ndiko kumenibadili. Sasa nimeshangaa wewe, tokea nimeshituka usiku, asubuhi hii, upo hivyo hivyo mpaka unaamka!” “Nimeshazoea. Nikigeuka geuka ndio usingizi unaniisha. Ila nikitulia sehemu moja ndio nalala sana.” Akataka kujitoa pale kifuani.

“Subiri kwanza Sabrina.” Sabrina akatulia. “Jana wakati Max anazungumza na wewe. Sijui sikuwa nimesikia vizuri, au masikio yalipokea kile moyo ulitaka kusikia!” “Nini tena?” Sabrina akauliza. “Nikama nilisikia ukisema unanipenda!” Sabrina akacheka. “Nataka tu uhakika Sabrina. Au nataka kujua ukweli. Nishahangaika na haya mapenzi! Mpaka nikajuta kuzaliwa hivi nilivyo na Mungu kunipa hiki kipaji kinachoniingizia pesa. Si Lela wala huyo msichana uliyemsikia walishindana na Lela nikaishia kumuoa Lela ndio wanawake pekee niliokwisha kuwa nao. Na wala Lela si tapeli wa kwanza kwangu. Nishajaribisha huko chuo na mtaani ndipo nikaangukia kwa Lela. Mpaka nahisi nina laana! Sasa natamani kujua ulimaanisha au ni kwa kuwa Max alikubana?” Sabrina akajua Tino anamaanisha, si swali la kitoto. Ameamka na swali!

Akaamua kukaa kabisa. “Sijui umekuwa na wasichana wa namna gani Tino. Lakini kwani matendo yangu yameshindwa kuzungumza kabisa?” “Hapana Sabrina. Unakumbuka uliniambia huwa unafungwa na maneno yako?” Sabrina akapoa. “Iweje nipone, halafu uje ujione muda wa kuwa na mimi umekuishia, unahitajika Singida kwa Jack? Maana mpaka sasa Jack anakusubiri.” Sabrina akatulia kidogo akiwa amekaa. Akaegemea ukuta, akakuta Tino bado akimwangalia.

“Nakupenda Tino.” Akaanza taratibu. “Nilizungumza vile na Jack kama mipango yangu ya baadaye nikiwa sijui hatima yetu ni nini na wala sikujua unanichukuliaje kabla yakupona kabisa na baada ya kurudia maisha yako ya zamani. Kumbuka nililetwa nyumbani kwako kama mfanyakazi tu. Nisingeweza kuweka mikakati ya kuwa na wewe mpaka kifo Tino, wakati nikiwa sijui nafasi yangu kwako.” “Sasa hivi umejua?” “Kwa asilimia kubwa.” Akajibu taratibu Sabrina akimwangalia. “Hiyo ndogo iliyobaki ni ipi?” Sabrina akavuta pumzi kwa nguvu.

“Mimi kama binadamu kuna hofu Tino. Naomba unielewe. Kuna wakati naingiwa na wasiwasi najiambia labda ukipona kabisa, ukarudia maisha yako kama ya zamani pengine nakuzidi, unaweza kugundua mimi siye mtu unayenihitaji kwenye maisha yako!” “Sabrina?” “Naomba unisikilize tu Tino. Nikikuangalia hivyo ulivyo. Sura, pesa, nyumba na hata vitu nilivyovikuta ndani yako. Tuje aina ya mwanamke uliyeoa, napata picha wewe ni mwanaume unayependa vitu vizuri vyenye hadhi. Nimekaa na wewe huu mwezi ulioweza kujitegemea. Nimekuona jinsi unavyojijali wewe mwenyewe. Msafi sana. Kuanzia muonekano wako, nje na ndani. Unajali mwili wako kupita hata watoto wa kike wengi tu.” Tino akacheka kidogo.

“Kweli. Una aina fulani wa muonekano ambao nahisi unataka uwe hivyo ndio maana unajijali hivyo. Wakati wote, muda wote upo nadhifu haswa. Uwe unakwenda au unatoka mazoezini ukiwa unatokwa jasho au la, upo nadhifu. Nikikufananisha wewe na mimi, na vingi unavyomiliki, ni vitu viwili tofauti kabisa. Sasa najiuliza na kujitia hofu mimi mwenyewe, mwisho wa haya yote ni lini? Hilo moja.” Sabrina akaendelea.

“Pili, Tino. Nimekukuta umeshaanza maisha yako. Umejijenga. Unalalamika umeishiwa ukiwa na mamilioni ya pesa kibao benki.” Tino akakunja uso. “Niliona salio pale benki Tino. Nikakuona jinsi ulivyonyong’onyea ukisema umeishiwa wakati hakuna mtu ambaye ananizunguka ambaye anamiliki mahela kama hayo. Halafu najiuliza, umeshakuwa na misingi yako ya maisha. Huanzi maisha kama mimi. Si kama kina Jack tunao anza maisha, ndio wanatafuta kuwekeza. Wewe umeshakaa mtaani, unajua wapi utupie ndoano yako, ili upate pesa. Sasa naingiwa na hofu na kukosa ujasiri nikijiingiza kwako wewe unayeendelea na mimi ninayeanza, itakuaje? Hiyo pili.” Tino akacheka.

“Kumbe ni bora nimeuliza! Sasa hayo ningeyajuaje?” “Usinitoe kwenye mtiririko wangu. Nitasahau.” “Haya mama. Endelea.” Tino akamruhusu. “Tatu, hunijui Tino. Hunifahamu hata kidogo. Unaujua upande wangu mmoja tu. Ulio ona nikikusaidia na kukusimulia mimi mwenyewe. Hujui kama nimekudanganya au la. Hujui tabia zangu. Pengine nipo kama mmoja ya wasichana ambao ulishakuwa nao, wakakushinda! Lakini Jack ameona ubaya wangu wote. Sijifichi kwa Jack. Anaponiambia yupo tayari kuanza na mimi maisha, sina hofu kwa kuwa najua ananijua na bado amekubali kunipokea nikaanze naye maisha.” Akaona Tino amekunja uso.

“Ni nini tena!?” Ikabidi Sabrina amuulize. “Hukuniambia kama unakwenda kuanza maisha na Jack! Uliniambia mnakwenda kuanza biashara!” “Tino!” “Kweli Sabrina. Au mimi ndio sikuwa nimeelewa? Maana hivi leo kwenye mazungumzo ndio nasikia hiyo mipango yakuanza maisha pamoja!” “Ulielewa sawa sawa. Nilikwambia kwa sehemu tu, kutokana na mahusiano tuliyokuwa nayo wakati ule na kile tulichokuwa tukizungumza, nini kinafuata baada ya kutoka kukuhudumia wewe. Hata hivyo sikukubali mahusiano kwa asilimia 100.” “Japo sielewi kutokubali kwa asilimia 100 ndio nini, na mimi nitataka kujua kwa asilimia ngapi upo na mimi, ila kwa sasa nataka kujua ni kwa nini hukumkubalia kwa asilimia 100?” Sabrina akajua anayo kazi.

“Sabrina?” “Mmmh!” Akahema kama ameshachoka. “Naomba usinichoke Sabrina. Ninayo maana kubwa sana.” “Nakuelewa Tino. Na sijakuchoka. Ila sijui nikwambie nini!” “Ninachotaka ni ukweli kutoka kwako. Naona leo tumeanza vizuri. Angalau nimejua kinachoendelea moyoni au kichwani mwako. Nataka kujua kila kitu ili tukitoka hapa, tutoke tukijua tumesimamia wapi. Kwa hiyo tafadhali naomba unijibu tu.” Sabrina akavuta shuka na kujifunika vizuri.

“Nilikwambia tulikuwa tukiwasiliana na Jack tokea nitoke chuo. Sijui kama unakumbuka?” “Nakumbuka.” “Sawa. Lakini ubusy wa nyumbani na wakati mwingine mawasiliano yakawa magumu kwa sababu nilikuwa nikipokonywa simu anapewa mdogo wangu anayenifuata.” “Kwa nini!?” Tino akauliza kwa kushangaa kidogo. “Unakumbuka nilikwambia Emma alinipokonya vitu vyake vyote?” Tino akaitika kukubali. “Sasa simu ya mkononi niliyokuwa nayo wakati ule ni yeye alininunulia na ndio ilikuwa Iphone iliyokuwa imetoka mwaka ule. Kasandra alikuwa akiipenda sana. Kwa hiyo nayo aliichukua Emma, akampa Kassandra. Sikuweza kuwa na simu kuanzia hapo. Maana pesa ya matumizi niliyokuwa nikipewa nyumbani ilikuwa ndogo sana, na hapo ukumbuke pesa hiyohiyo ndogo niliyokuwa nikipewa nyumbani ndio nilikuwa nikitegemea na chakula, malazi na vitu vyangu vidogo vidogo vya matumizi mimi kama mtoto wa kike. Ilikuwa haitoshi kabisa. Nakumbuka wakati mwingine nilikuwa nakula mlo mmoja kwa siku. Nikafika hatua ikabidi nianze kutumia vitambaa kama pedi. Vikichafuka, nafua.” “Haiwezekani Sabrina.” Sabrina akacheka na kujifuta machozi.

“Kweli Tino. Nilimaliza ile shule kwa shida sana. Lakini Jack huyohuyo kuna kipindi akawa akininunulia chakula. Unakuta ni muda wa chakula cha mchana, akigundua nimebaki darasani sijakwenda kula na yeye anayo nafasi, alikuwa akininunulia chakula, ananipitishia darasani. Kwa ufupi niliishi hayo maisha, hata wazo lakununua simu nikawa sina sababu ya uwezo. Sasa Sabina alikwenda China, akawanunulia baba na mama zawadi za simu. Kwa hiyo zile za zamani wakawapa wale wadogo zangu wakiume wanao nifuata.” “Kwa nini sio wewe!?” “Mimi sijui Tino. Lakini sasa kwa sababu wao wapo shule za bweni hawaruhusiwi kwenda na simu shuleni. Kwa hiyo wakiwa shuleni ndio nakuwa namuomba baba au mama niazime kwa muda huo. Naweka line yangu, natumia. Na hapo ndipo nilikuwa naweza kuwasiliana na Jack mara moja moja, tena nikiwa na pesa, au Jack akijua nina simu ndio akawa akinipigia au kunirushia muda wa maongezi.” Sabrina akaendelea.

“Sasa heshima kwa Jack ikaongezeka, Tino! Kwa mabaya yote niliyomfanyia, lakini Jack hakuwahi kunikatia tamaa. Tokea tupo chuo yupo na yule msichana wake, akaonyesha kunijali sana mimi. Kwa hakika hata sijui walikubaliana vipi na msichana wake, lakini Jack aliendelea kunijali vizuri tu mpaka shule yangu ikaisha yeye nikamuacha chuoni. Na baada ya kumaliza pia tulipotezana kidogo, kisha tukarudi kuwasiliana. Lakini mazungumzo ya kawaida tu. Jack ni wale watu wanaojali Tino, mpaka kumfikiria mtu kama amekunywa maji au alipata usingizi wakutosha. Mstaarabu sana, halafu nafikiri Mungu alimuumba ili aje kuwa kiongozi. Ukimuona tu, utatamani akusimamie jambo lako. Amejawa na hekima, mtulivu halafu akizungumza tu hivi, utajua ni mtu anayefikiria na anauelewa na mambo.” Kwa uangaliwaji ule na Tino, akaona afupishe sifa za Jack.

“Kwa ufupi kutokana na alivyo Jack, nikaona na kujitahidi hata akili yangu ikubali mahusiano yetu yabakie ya ukaka na udada tu, si mapenzi.” “Kwa nini tena wakati amejawa sifa kibao!” Sabrina akacheka, akajua tayari Tino ameona wivu. “Mtu kama huyo si ataniona mimi mbambaishaji tu? Kwa nini nimkatae vibaya hivyo, halafu kwa nini gafla nijidai nampenda!? Hata yeye angejua ni kwa kuwa nimekataliwa na Emma! Nimeshindwa huko kwengine, ndio namfuata yeye! Yaani yeye anakuwa kama chaguo la pili! Nikaona sitamtendea haki. Jack anastahili msichana mzuri atakaye muenzi.” “Ilikuaje na yule msichana aliyekuwa naye chuoni?” “Sikutaka hata kuanzisha aina hiyo ya mazungumzo Tino. Ila tu katika mazungumzo yetu nikajua yupo peke yake, hana mahusiano ya kimapenzi. Ndio linapokuja sasa jibu lako, alinikaribisha nikaishi naye wakati nahamia Singida kuanza maisha. Hakunitongaza moja kwa moja ndio maana na mimi sikumpa jibu la moja kwa moja.” “Sijaelewa!” Tino akazidi kumbana.

“Aliniambia hivi, nisiwe na wasiwasi juu ya sehemu ya kuishi. Yeye anayo nyumba kubwa tu, hatajali kuishi na mimi kwa kuwa hisia alizokuwa nazo nyuma bado hazijabadilika. Kwa hiyo haitakuwa mbaya nikiungana naye kuanza maisha.” Tino akapandisha nyusi zote juu. Sabrina  akacheka kwa aibu. “Ndio na mimi nikamuuliza haoni itakuwa tatizo kwa mama mwenye nyumba wa hapo? Akaniambia mpaka hapo anaponikaribisha, hakuna mama mwenye nyumba, mimi naweza kuwa mama mwenye nyumba, endapo nikitaka.” Tino akabaki vilevile akimwangalia. Sabrina akacheka mpaka akajifunika na shuka usoni.

“Acha kuniangalia hivyo bwana Tino!” “Mimi nashangaa, kumbe naishi na wewe mwenzangu unasubiriwa kwa majukumu mazito hivyo! Haya, ukajibu nini na mkaishia wapi, na kwa nini?” “Kumbuka nilivyokwambia jinsi nilivyomkataa Jack. Sikutaka anione mbambaishaji, au sijui ninachotaka. Kwa hakika nilikosa ujasiri kwa Jack. Nilishamuumiza Jack. Sikutaka nije kumuumiza tena.” “Kwa nini, kwani wewe humpendi?” Sabrina akafikiria kidogo. Kisha akatoa jibu ambalo hata yeye alionyesha hana uhakika. “Sijui Tino. Sielewi ni nini kinanipata kwa Jack!” “Nini?” “Subiri kwanza. Hayo yakwenda kuishi kwake hakuniambia muda mrefu sana uliopita. Nafikiri ulishaanza kupona. Ukumbuke mipango mingine kati yetu iliendelea kabla hata hatujazungumzia sehemu ya kuishi. Kama biashara gani tukafanye pamoja. Masoko, wapi pakuhifadhia bidhaa, usafiri, ndipo sasa mimi nikamuuliza nitakapokuwa Singida nitaishi wapi? Nikamwambia labda aanze kunitafutia sehemu ya kuishi. Ndipo akaniambia kama nilivyokwambia. Sikumpa jibu la moja kwa moja kutotaka kuja kumuumiza. Nilimwambia aendelee kunitafutia, ili tuwe na chaguzi nyingi baadaye. Isiwe kwake tu. Kama nilivyokwambia, Jack ni mstaarabu. Akakubali bila shida. Tukaishia hapo nikiwa sijui kama kwanza nitakwenda, pili kama nikienda nitakwenda kuishi kwake.” “Kwa nini?” Tino akauliza tena.

“Nilikuwa sijui utapona lini na mtanihitaji mpaka lini, Tino! Binafsi nisingeweza kukuacha ukiwa bado upo dhaifu na pili, nisingeweza kung’ang’ania kubaki kama Da Lela angerudi na kuniambia niondoke amepata mtu mzuri zaidi. Kwa hiyo Jack nikamuweka huru na wazi. Nikamwambia endapo anapata mtu wakuanza naye biashara, aanze tu asinisubiri. Maana yeye alishasema hataweza kufanya biashara na kazi, huku akitaka kujiingiza kwenye siasa. Jack ni wale wanasiasa kwelikweli. Na anaonekana hata kuwepo Singida ni mkakati maalumu, kuja kugombea lile jimbo. Na ninavyomtizama Jack, hatashindwa endapo atapitishwa na chama tawala kuwa mgombea pale. Yupo vizuri sana na anafahamiana na wakubwa wengi. Kwa hiyo aliniambia kama ni biashara, atafanya kwa ajili yangu, lakini si kitu ambacho kipo kwenye mipango yake.”

“Kwa swala la kutokubali kuishi naye lilinijia baada ya kuishi na wewe Tino. Kabla ya hapo nafikiri ningemkubalia. Lakini ukumbuke tuliachwa wawili tu kwenye ile nyuma. Ukawa unanifuata kila mahali na kunionyesha unanihitaji sana kitu ambacho sikuwahi kukipata. Sijui kama unanielewa?” Tino kimya. “Taratibu nikaanza kujisikia hisia zinabadilika. Nikakuzoea sana, nikawa nafurahia vile unavyonifuata nakutaka uwe karibu na mimi. Tukikaa hata kwenye kochi tunakaa wote na unataka unishike mkono. Nikajitahidi nisiwaze vinginevyo nikashindwa. Sasa nikajiambia haitakuwa sawa kwa Jack. Eti niende kwake huku mawazo yapo kwako! Nikajiambia nisije nikaenda kwa Jack, tukaishia kuoana halafu tukawa na ndoa kama yako wewe na dada Lela! Naomba usinielewe vibaya Tino. Nilitaka uhakika wa mapenzi yangu kwa Jack kabla sijakwenda kumuumiza tena. Tukaishia kama nyinyi hivi.”

“Hapana. Nakuelewa Sabrina. Naelewa kabisa. Aliyokwambia Max wala hakuongopa. Hatukuwahi kuwa na ndoa nzuri, nafikiri ndio maana haikuwa ngumu kwa Lela kuniacha nikiteseka. Kwanza sijui kama ni kweli au hasira tu, kuna siku wakati ananitukana, nikiwa nimeshakuwa mgonjwa, aliniambia anashukuru Mungu alikuwa akitumia dawa zakuzuia mimba, ili asizae na mimi. Akaniambia ingekuwa aibu mara mbili hao watoto ambao angezaa na mimi eti wanione baba yao najinyea hovyo kama bata.” Sabrina akashituka sana mpaka akajikuta akijifunika mdomo.

“Wewe acha Sabrina! Wewe unafikiri ni kwa nini nataka kukusikia moyo wako? Lela alikuwa akianza kunitukana, utaondoka wewe. Utafikiri tulikuwa na uadui au kuna baya kubwa nililowahi kumtenda zamani, sasa ndio ananilipa kisasi.” “Basi na mimi ndivyo nilivyojua, mpaka ikabidi nimuulize da Sabina. Ndipo aliponiambia jinsi Lela alivyokupigania mpaka akabadili na dini, ukamuoa yeye!” “Nakwambia kama wakati ule ungeniambia Lela atakuja kuwa hivi, hata kwa pesa ningekukatalia.” Tino akaongea kwa kuumia sana.

“Ndio maana nataka kukusikia Sabrina. Nataka kujua kama kweli ipo hisia ya kweli au la! Sikutaka huku kukung’angania ndiko kukufanye unikubali, halafu historia ikajirudia!”  Tino akajiweka sawa.

“Kwa vyovyote unavyoniona nilivyo. Kwa sifa zote nilizokuwa nazo nje, haikuwa hivyo kwenye ndoa yangu na Lela. Imekuwa ni hili na lile mchana hadi usiku. Kwenda Club kwake ndilo jambo alilokuwa akifanya bila kuchoka kama mtoto mdogo anayekuwa. Maisha ya baa ndio ikawa kawaida yake na hilo kundi lao na dada yako Sabina. Anazunguka mtaani kama hana au aliyekataa jukumu lake la ndoa. Huna jinsi ukamfurahisha Lela. Akiamua kulalamika, hata zawadi utakayomletea, atalalamikia tena bila aibu. Haridhiki kwa maelfu wala mamilioni. Mlalamishi, na akianza kuongea ni mpaka akili inaganda kwa masaa, unashindwa hata kufikiria. Hakuna heshima wala utulivu. Mpaka nafikiri hili lililotokea, ilikuwa nilazima ili angalau nipate uwezo wa kuchukua hatua hii yakumuacha. Maana ni kama alishika akili zangu nikawa wala sijui chakufanya naye.” “Pole Tino.” Sabrina akamvuta mkono na kuanza kuuchezea.

“Ile nyumba na vyote ulivyoviona mle ndani vilishapoteza maana muda mrefu sana kwangu. Ilibakia jumba la maonyesho kwa Lela. Akileta mashoga zake kujitangazia utajiri mimi nikijifungia kule nyuma. Kama sio kufanya mazoezi, basi kuna chumba kwa ndani palepale ndipo nilikuwa napata utulivu, nakuchora. Kwa hiyo nilikuwa kwenye lile jumba, lakini maisha yangu yalikuwa kama sipo kazini nipo pale, basi ujue ndio nilikuwa kwenye kile nyumba cha nyuma. Wakati mwingine mpaka kulala, na kuamka asubuhi kurudi ndani kuoga, kubadili nguo na kwenda kazini.” “Kwa nini sasa!?” Ikabidi Sabrina aulize.

“Fujo na kelele zisizoisha. Ushauri wa kibabe wa nini nifanye kwa vitu ambavyo hata yeye mwenyewe Lela hana uelewa navyo! Ili tu nitengeneze pesa zaidi. Ukimwambia maswala ya mikataba niliyoingia na ugumu au madhara ya kuivunja, anabisha. Ukimuelekeza anapinga. Ndipo nikaja kugundua nazungumza mambo makubwa na mtu mwenye uelewa mdogo sana. Hajasoma na wala haelewi maadili ya kazi kwa kuwa kazi yake nikupokea simu kwenye ofisi yao na kuchapisha. Usinielewe vibaya. Lakini ndio ngazi ya Lela kimaisha. Mbali na urembo wa mwili wake anaojua kupita hata warembo wa mashindano, hana uelewa mwingine wowote. Hapo ndipo nikajithibitishia na kuamua kuacha kumjibu kabisa. Nikajiambia ni kama kumpigia mbuzi gitaa ili aburudike. Nikupoteza muda. Nikaachana naye. Nikawa nabaki nikimtizama tu anapoanza kuongea na kunitukana. Nikimaliza muda niliokuwa nimemuwekea kumsikiliza, naondoka. Hicho ndicho kilikuwa kikimuudhi zaidi. Maana starehe nyingine ya Lela ni kuongea. Sasa ukimnyima hilo, unamkera.” Tino akaendelea.

“Juu ya mali na nyumba na vilivyopo, vilianza kunitumikia na nikaanza hata kuvitumia, au hata yale makochi kuyakalia vile ni ulipokuja wewe na kuanza kuvitumia kwa ajili yangu. Ile amani na utulivu vilivyokuwepo pale ulipokuja, havikuwepo mle ndani tangia Lela aanze kuishi pale. Ulikuja navyo. Vilibaki kuwa kama thamani tu, mpaka pale ulipokuja wewe na kabla ya ndoa yangu na Lela. Huwezi kuamini kule kukaa kwenye ile meza ya pale jikoni, nilianza nikikufuata wewe japo ile meza niliinunua kwa pesa nyingi sana.” “Kwa nini!?” “Kwanza nilikuwa namkwepa Lela. Nisingethubutu kuingia jikoni yeye akiwepo! Na asipokuwepo alikuwa na dada anakuja na kuondoka pale kupika. Naye alikuwa akipika vibaya, Lela mwenyewe hakuwa hata akiweza kula chakula chake, anaishia kwenda kula baa tu ila msafi sana. Aliiwezea ile nyumba. Lakini kwa ninavyomjua Lela, ingekuwa shida kuja kuniona nakaa pale jikoni na yule dada yupo pale! Nikawa nakwepa kabisa.” “Mmmh!” Sabrina akaguna.

“Na kuhusu wasiwasi wako wakuanza na mimi niliyeanza maisha muda mrefu, naomba usiwe na wasiwasi Sabrina. Mimi sio mbishi sana.” Sabrina akacheka kidogo. “Najua nimekupita kiumri, lakini naamini hatutashindwa kuelewana. Uliza kila unapoona huelewi na toa ushauri kila unapopata wazo. Najua kwa sasa huna kazi, na unamahitaji yako binafsi, usiwe na wasiwasi. Kama nilivyofanya jana kukupa pesa ya matumizi yetu wote na yako binafsi, lakini tutatafuta njia nzuri ili uwe na pesa yako wewe binafsi na kwa kuwa tumekubaliana tutakuwa wote, tukiwa tayari kuanza kazi, nafahamiana na watu wengi tu, nitakusaidia kutafuta kazi. Kama ni biashara, basi fikiria kitu chakufanya. Kama ni hiyo alizeti, fanya lakini si na Jack.” Sabrina akacheka na kutoka pale kitandani.

“Unakwenda wapi sasa?” “Si tunasafiri leo? Mimi ndio dereva na sina leseni Tino. Acha nikashugulikie leseni ili tusafiri kwa utulivu, tusisimamishwe na trafiki huko barabarani.” “Sawa. Lakini naona tusifanye mambo kwa pressure. Hatujui kule kwenye leseni tutamaliza saa ngapi, na sitaki safari za usiku. Nitaongea na watu wa hapa kama tunaweza kuongeza siku moja. Tuondoke kesho asubuhi. Leo ukashugulikie leseni, halafu ununue simu yako, hiyo uirudishe simu ya watu. Wasijefikiria umetoroka na simu ya mdogo wako.” “Sitaki kurudi nyumbani Tino. Sipo tayari. Sio sasa hivi. Wataishia kunivunja moyo.” “Sio lazima ukarudi. Tutatuma kwa posta.”

Kimfaacho Mtu,….

T

ino akamsogelea pale, akaanza kupata busu la asubuhi. Sabrina naye akatulia hapo kama aliyekwisha patwa hamu naye. “Niambie kama unanipenda na umenichagua mimi. Sema tu, nataka kukusikia Sabrina.” Tino akaongea kwa kubembeleza. “Nakupenda Tino na nimekuchagua wewe, niwe kwenye maisha yako.” Sabrina akaongea kwa upendo. Tino akainama. Akamtoa kofia taratibu huku akimbusu. Akamfungua tena nywele. Akamwangalia. “Nilikwambia kama hizi nywele zimekupendeza?” “Nilitengeneza na kucha.” Tino akacheka. “Nimezisikia kifuani jana. Una vidole vizuri Sabrina.” “Ila mikono migumu mpaka huwa naona aibu wakati mwingine unapoiangalia na kuishika!” Akajikebehi mwenyewe. “Hiyo mikono ilinitoa kwenye mauti Sabrina. Ikanitakasa. Ilinilisha nikiwa siwezi hata kushika kijiko! Ikanivisha nikiwa nimeshikwa na baridi. Ilinibembeleza wakati nina maumivu. Ikaniliwaza ili nilale. Ilinikwangua mba uliokuwa ukiniwasha karibu kuchanganyikiwa, lakini si mikono yangu au ya Lela iliyoweza kufika kichwani na kunisaidia. Hii mikono.” Tino akaishika yote miwili. Akaibusu. Sabrina akajifuta machozi kwa bega.

“Hii mikono hii, ilifika sehemu ambayo wengine walishindwa kufika, wakanikimbia. Lakini yenyewe ilifika, ikanisafisha na kuponya madonda yangu yote. Mikono hii hii, ilihakikisha natoka pale kitandani ikisaidiana na haka kamwili kadogo, mpaka nikakushangaa!” Sabrina akacheka taratibu. “Mimi nikiwa nimekata tamaa, siku ile kwa mara ya kwanza ukapambana, hii mikono ikanitoa kitandani na kunikalisha kwenye makochi niliyokuwa nimenunua kwa pesa nyingi sana, lakini sikuwa na bahati yakuyakalia.”

“Hii mikono hii, ndiyo iliyoanzisha safari ya mazoezi ikisaidiwa na hiyo midomo.” Akamvuta na kumbusu midomoni. “Nakumbuka ulinikuta nimekasirika. Nimetupa vile vimipira vya mazoezi sakafuni. Pale nilikuwa nimejaribu mpaka nikaamua niache tu. Uliokota ile mipira kwa kutumia hii hii mikono. Ukanishikisha na kufunganisha nguni yangu ndani ya ngumi yako. Ukanisaidia siku ile na karibia juma zima mpaka nikaweza kushika vizuri. Ukanisindikiza mazoezini na kunisaidia kubeba vifaa vya mazoezi kupitia hiihii mikono. Wakati Mungu akiiumba hivyo, na kuruhusu ipite kwenye shuruba, alikuwa akinitazama mimi.” Sabrina alifurahi sana.

“Aliiandaa hii mikono kwa ajili yangu akijua siku moja Costatino  mimi, aliyenichukulia wazazi, akaninyima ndugu na marafiki wa kweli, nitaihitaji. Kwa hiyo wakati Mungu akikuumba wewe, na kila unachokichukia mwilini mwako, alikuwa akinifikiria mimi huku duniani.” Akamvutia karibu, akaibusu tena na tena hiyo mikono, akarudi mwilini kwa Sabrina. Hata Sabrina alijua Tino anafurahia anachokifanya hapo. Alihakikisha anamfurahisha Sabrina vilivyo ndipo wakatoka hapo baada ya kujiandaa. Sabrina alifua nguo zake alizonunua usiku wakati anaoga. Alizipiga pasi asubuhi ili zikauke vizuri, akavaa. Ungependa kumwangalia Sabrina na kamwili kake kadogo akiwa anatembea na Tino. Gafla hadhi yake ikapanda. Sabrina huyu ni wa Tino. Ameambiwa pesa si tatizo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walianzia kwenye leseni. Wakafanya taratibu zote, wakaambiwa waifuate baada ya masaa mawili. Wakati wanasubiri huo muda, wakaamua kwenda kutafuta simu yakutumia Sabrina na kurudisha kwa kuituma kwa njia ya posta ile simu aliyoazimwa nyumbani kwao. Sabrina alifurahia sana simu aliyokuwa amenunuliwa. “Hii nimeipenda. Huwa napenda sana simu kubwa. Emma ndiye aliyekuwa akipenda iPhone.” “Nimefurahi kama umeipenda.” Wakafanikisha mambo yao wakiwa wanaongozana kila mahali kama kumbikumbi.

Walipomaliza na kupata leseni, wakampigia simu Max kushukuru. “Nashukuru kaka. Lakini Sabrina anataka kukushukuru yeye mwenyewe pia.” Max akacheka, Sabrina akapokea simu. “Nimefanikiwa, nataka kukushukuru, asante.” “Mimi naona shukurani hiyo inifikie uso kwa uso.” Sabrina akacheka. “Tino hajala vizuri kaka yangu. Na tumekuwa na siku ndefu, nataka akale na apumzike.” “Hata kwetu tunapika na kuna makochi.” “Unataka tuje nyumbani!?” Akamwangalia Tino na kumpa simu. “Kama mmeivisha, sisi tunakuja.” Akadakia Tino. “Mpaka sahani zimeshaanza kuandaliwa, mkifika tu tunahamia mezani.” “Asante kaka. Mwambie shem tunakuja matumbo matupu.” Wakataniana kidogo na mkewe pia, wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Ukikaribishwa nyumbani kwa Max, ujue ni mkewe. Hapo anataka kukuona.” Sabrina akaingiwa hofu. “Tino!” “Ni watu wazima, wenye msimamo wa maisha. Mkewe alimchukia Lela kwa kuwa alimuona ni mchezaji sana. Usiogope. Ninauhakika  mtaelewana tu. Wanandoa nzuri sana. Watoto wazuri, utapenda kuwepo kwao.” Sabrina akaanza kukanyaga mafuta kuelekea Mbagala Mwisho, nyumbani kwa Max.  Njiani kwenye mataa, Tino alishaomba mabusu ya hapa na pale, Sabrina akicheka kila wanapopigiwa honi nyuma kuwa waondoe gari.

Sabrina alikuwa akicheka sana. Mara Tino aingize mkono ndani ya gauni kifuani amchezee matiti au chini mapajani huku akiendesha. Sabrina alikuwa akicheka kama anayetekenywa. Mwishoe Tino akashika ambako uvumilivu ukamshinda Sabrina. Akatafuta sehemu, akaegesha. Giza lilishaingia. Sabrina aliyenyimwa mwili. Hana nyama za kumzuia kujikunja popote. Akaruka upande aliokuwa amekaa Tino, akalaza kiti na kumkalia. Mabusu yakaendelea hapo, akachukua mkono wa Tino akauweka kifuani ndani kabisa akamshikisha matiti yake. Akapotelea kwenye ulimwengu mwingine, akatoa penzi zuri sana hapo hapo barabarani ndani ya gari, Tino alifurahi sana. Hakutegemea kupata penzi barabarani hasa kutoka kwa Sabrina! Kwa harakaharaka alionekana mshambamshamba, asiyejua kinachoendelea, lakini akianza jambo, utashangaa sana.

 “Mungu wangu wewe mtoto! Utanimaliza. Kwa mwendo huu!” Sabrina akacheka wakati akimsafisha, na kurudishia zipu ya suruali. “Acha kunichezea matiti ukiwa haupo tayari, unanifanya nashindwa kuvumilia nakubaka hata barabarani.” Akambusu Tino mdomono, na kurudi kwenye kiti cha dereva huku  wakicheka.

 Nyumbani Kwa Max.

Walifika nyumbani kwa Max wakiwa wamejawa furaha. Sabrina akashangaa hilo jumba na mazingira yake. “Hapa bado ni Mbagala?” Sabrina akanong’ona. Tino akacheka. “Acha utundu Sabrina. Twende.” Wakashuka garini, wakamuona Max na mkewe mlangoni. “Nisalimiaje?” Akauliza Sabrina wakati wanawasogelea. “Mpe shikamoo. Ni dada mtu mzima. Na acha kuogopa.” Tino akajibu kwa sauti ya chini. Sabrina akacheka. “Nilishaanza kuandaa sare za msiba wako.” Mke wa Max akamtania Tino bila hata tabasamu usoni. “Mtasubiri sana.” Akajibu Tino, Sabrina akiwa anafuata nyuma nyuma.

Walipofika karibu ya wenyeji wao, Tino akamgeukia na kumshika mkono Sabrina akawa kama anamsogeza karibu ya wenyeji wao. “Shikamooni.” Akasalimia Sabrina akiwa bado ameshikwa na Tino. “Marahaba Sabrina. Hujambo?” Akaitika mke wa Max kwa kumfahamu. “Sijambo.” Akatoa mkono na kumpa. “Karibuni ndani. Tino pole kwa matatizo.” “Nashukuru Mungu nipo nimesimama hapa.” “Na umshukuru haswa kwa kuwa ni kweli amekuhurumia. Na nafikiri hutapata nafasi nyingine kama hiyo. Nahisi hata mbingu zilichoka na wewe kwa kuchezea nafasi nyingi sana walizokupa zakumkomesha Lela kabla hajakudhuru, ukashindwa. Kwa hiyo safari hii uitumie vizuri. Na uweke kikomo haswa.” Mama Kundi akawa akizungumza akimwangalia Tino kwa kuweka msisitizo. Tino akanyamaza tu.

“Nimesikia mnanjaa. Karibuni ndani mle.” “Asante. Twende Tino.” Akaongea kwa upole Sabrina. Wakaingia ndani. “Wala usimuhurumie huyo. Anatakiwa kuchangamka. Amezidi! Mimi mpaka nilimkataza asimrudishe yule kichaa wake humu ndani. Hajui anaongea na nani wala kina nani wanamsikiliza. Akifika hapa mdomo wake unajaa nyumba nzima mpaka watoto wangu wanashindwa kukaa hapa, wanakimbilia chumbani! Hawatatoka mpaka wawasikie hawa wawili wameondoka! Mdomo kama chiriku! Na akiongea na mwenzie huyo, utafikiri yeye ndio kasoma, anapesa, halafu huyu ndio mkewe. Ana amri, halafu akili hana. Mpaka mimi nikamwambia  wazi kabisa, anavutia akiwa ameufunga ule mdomo wake. Akiufungua tu, hana tofauti na mpumbavu yule wa mwisho kabisa. Akataka kunijibu, nikamwambia neno litakalotoka mdomoni kwake, hata kama ni ‘asante’ nitampiga vibao mpaka alie.” Sabrina akashangaa Max na Tino wanacheka.

“Ndio akanyamaza, akachukua pochi yake hapa, akamuamuru bwana huyo uliyemshika mkono, waondoke. Ndio nikawaambia nisiione sura yake tena hapa kwenye nyumba yangu. Na kweli hakurudi.” Sabrina akawa hajui chakusema. “Njoo mezani mwaya mtoto mzuri ule. Nimesikia hata unasalimia ‘shikamoo’!” Mpaka Sabrina akacheka. Meza ilikuwa imeandaliwa vizuri. Pasafi sana.

Wakamuona mama Kundi anacheka peke yake. “Wamemkomesha Tino, naona ameamua safari hii kutafuta katoto kadogo, tena sio shangingi la hapa jijini! Chezea kifo wewe!” Akaendelea kucheka, Max na Tino wakiangaliana na kucheka taratibu. “Ndoa ya kanisani haivunjiki shem.” “Mbona safari hii unaivunja kama sio unaogopa kifo?”  Mama Kundi akamuuliza na kuendelea. “Na kwa taarifa yako huyo mkeo wa kanisani ni mjamzito. Na nimesikia walikuwa wakijenga na huyo mwanaume wake huko Kigamboni. Nasikia walinunua eneo karibu kabisa ya bahari jinsi walivyokuwa wakichezea pesa yako bila huruma! Unaambiwa Lela ndiye anayemwaga mamilioni ya pesa bila kufikiria. Sasa hapo wanasubiria pesa yako ya mwisho, wamalizie mjengo wao. Hapa tunapozungumza wanaishi kwenye apartment za Ocean road kule, ujue wapi pesa yako inapoishia. Fikiria zile apartment jinsi zilivyo aghali! Wanalipa kwa dola! Huingii mle ndani mpaka watu wa ndani waruhusu uingie. Muulize kaka yako leo karudishwa getini. Eti Lela amelala, amekataza walinzi wasiruhusu mtu yeyote asifike kwenye apartment yao. Kamwanaume kake kanatamba mjini kuwa kamekula Bingo ya miaka. Anavuta pesa kwenye ATM inayotema dola! Na Lela kaacha kazi, analea tumbo.” “Kazi ya nini wakati mshahara wangu ulikuwa unaingia kila tarehe 15 ya mwezi?” Akaongea Tino kwa hasira wakati Sabrina anamuwekea chakula.

“Ulimfuga mwenyewe yule Tino! Ulimwachia kupita kiasi mpaka nikahisi amekuloga wewe!” “Mbona ulishamwambia na yeye mbele yangu na wageni wote waliokuwepo siku ile ulipomwambia utampiga!” Mpaka yeye mwenyewe akacheka. Wakakumbushana yaliyotokea siku hiyo kulipokuwa na tafrija hapo kwenye nyumba yao, wakaalika wageni mbali mbali, Tino na Lela nao wakahudhuria. Lela akaanza tabia yake yakumuendesha Tino mbele za watu mpaka mke wa Max, mama Kundi, akashindwa kuvumilia. Akalipuka yeye kama mama yake mzazi Tino. Mwishoe akaishia kuwafukuza wote wawili mbele za watu. Wakazidi kucheka. “Ila hilo la ushirikina niliropoka siku ile kwa hasira. Nafikiri alishanikera sana mpaka nikashindwa kuhema. Sijui kalelewa wapi yule kiumbe! Hana adabu hata ya kinafiki!”  Akamalizia mama Kundi kwa mshangao.

“Natamani kuiona sura yake atakapopokea talaka yake!” Akaongeza Max. “Mimi namsubiria tarehe 15 atakapokimbilia benki, halafu akute akaunti ilishafungwa. Na pale ofisini nimewaambia hata asiruhusiwe kuingia getini. Wamtaarifu kabisa kuwa nimesema sio mke wangu tena, hana mamlaka yeyote juu yangu. Madai yangu yote hayahusiki tena na yeye. Nikawaambia wakimpa habari zangu zozote, nitawashitaki tena. Akiuliza chochote, wamwambie majibu atayapata kwa mwanasheria wangu!” Alishangilia mke wa Max kama ameokota alumasi wengine wakicheka, Sabrina akiendelea kusikiliza tu bila nyongeza.

“Max mume wangu, mimi naenda kuacha kazi kule wizarani.” “Halafu ndio iweje!?” Mumewe akamuuliza. “Naenda kuombe kazi ya ulinzi huko ofisini kwa kina Tino, ili niweze kumpokea Lela siku akienda kudai pesa.” Wote wakacheka. “Huyu yupo likizo, naona amechoka kukaa nyumbani. Anataka arudi kazini.” Max akamzungumzia mkewe, mkewe akacheka. “Ndio maana nikashangaa mbona leo mpo nyumbani mapema!” “Huyu ndiye aliyenitoa kazini. Wala msingenikuta hapa.” Akajibu Max. “Nilitaka kumuona Sabrina, na sura ya Tino. Nione jinsi ulivyokomweshwa na Lela. Ndio nikamwambia Max nitapika, mje wote tupate mlo wa pamoja kabla nyinyi wawili hamjaondoka hapa mjini.” “Tunashukuru kutualika. Nyumbani kwako kuzuri na pasafi sana.” Sabrina akaongea kwa heshima. “Asante mwaya. Sina mtoto mdogo ndio maana unapaona hivi.” Akamalizia mama Kundi.

Ushauri wa Mke wa Max.

W

akaendelea kula, lakini wakimsoma Sabrina vile anavyomuhudumia Tino kwa upendo. “Nikuongeze kidogo?” Tino akawa kama anafikiria. “Kidogo tu. Sitakuwekea kingi. Halafu tukifika nitakuongezea na shake. Lakini naomba nikuongeze kidogo tu.” Akaendelea kunong’ona Sabrina akimbembeleza Tino kula, lakini Max na mkewe wakiwasikiliza na kuendeleza mazungumzo. Tino akakubali. Akamuongezea tena kidogo. “Ukimaliza hicho tena, basi.” Akambembeleza Tino kama mtoto. Tino akaanza kula tena, taratibu tu, Sabrina akiangalia kama anajimwagia, anaokota chakula, na kumkumbusha kujifuta kama kimemwagika nje ya mdomo. Wakala hapo mezani, mpaka wakamaliza.

Sabrina akasaidia kutoa vyombo mezani na kusafisha. “Naweza kuvisuuza mara moja hapo kwenye sinki.” “Hapana. Dada atavisafisha. Naona yupo chumbani. Atashuka tu muda sio mrefu. Nenda kapumzike. Nashukuru.” Sabrina akaweka vyombo vyote kwenye sinki wakarudi sebuleni na mke wa Max.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Sasa mimi nataka niwashauri jambo.” Akaanza mke wa Max. “Zaidi wewe Tino.” Wakajiweka sawa. “Na hili nimemwambia Max. Lela ni mjanja sana. Japokuwa ametapanya pesa kwa kiasi hicho, akipokea tu talaka, atataka mgawane kidogo alichobakisha, wakati mwenzio amejenga kwake na mwanaume wake. Sasa, ili na wewe ule jasho lako nashauri hiyo pesa iliyobaki, sijui ni kiasi gani, lakini iwekeze. Chakwanza, nunua nyumba ila si kwa jina lako.” Akaendelea.

“Max aliponiambia habari za Sabrina na vile alivyomsoma kwa haraka, na mimi nakubaliana naye, Tino.” Sabrina akaanza kutetemeka. “Sabrina anakupenda na kukujali. Huyu ambaye hakukukimbia wakati wa shida, yupo na wewe mpaka sasa, huyu ndiye atakayekusitiri. Popote mnapokwenda, hakikisha unanunua jumba zuri na sehemu nzuri ambayo hata ukiamua kuja kuiuza baadaye, utapata faida. Lakini isiwe kwa jina lako. Ili mkiamuriwa na mahakama mgawane kila kitu, basi uwe na sehemu ya kuishi. Kingine, usisubiri huo mkono. Lazima maisha yaendelee na pesa iingie. Fungua biashara itakayokuingizia pesa. Acha yale maneno yako yakuwa mkono wako ndio utajiri wako. Mungu amekufungua macho kuwa anaweza kuchukua huo mkono lakini akakuacha wewe. Sitaki kukuogopesha, lakini usipopona?” Sabrina akamuona Tino amebadilika mpaka rangi.

“Kweli Tino. Wewe bado mdogo. Usipoangalia, utakufa masikini wakati Mungu amekupa nafasi. Anachokwambia shemeji yako najua kinaogopesha, lakini naomba usipuuze hata kidogo. Kama Mungu aliyekupa hicho kipawa cha uchoraji, anajua sasa hivi huwezi kukitumia, na unayo pesa, tafadhali jiambie ni njia nyingine Mungu amekupa kukutajirisha kwa njia ingine. Ipi! Ni wewe kufikiria.” Tino akabaki kimya akiangalia mkono wake huku akiusugua.

“Na hata kama utapona, lazima uwe na kitega uchumi zaidi ya kimoja. Si umetuona mimi na Max? Maisha yalitupitisha pagumu, wewe ni shahidi. Pamoja na uzima wetu, shule tulizokuwa nazo na hatukuugua, ilitulazimu kufikiria mara mbilimbili ili kuepukana na ile aibu ya kukopa na kuomba pesa mpaka kwako wewe. Nafikiri unakumbuka ada ulizokuwa ukiwalipia watoto wetu hapa!” Tino kimya. “Ile hali isingebadilika bila sisi kuongeza kitega uchumi kingine. Kwa hiyo Tino. Naomba niangalie na uache kujionea huruma.” Mama Kundi akaongea kwa ukali kidogo, Tino akamwangalia. “NILAZIMA kuanza biashara. Umenielewa?” Mama Kundi akaweka msisitizo.

“Kwa aina hii ya mwanamke uliyekaa naye hapo pembeni, kama hutafanya ujinga ukamfanya akukimbie, huna utakalojaribu ukashindwa. Sijui kama unanielewa?” “Nimeelewa.” Tino akakubali. “Sasa na wewe Sabrina, lazimisha hiyo isiishie kwenye kula. Weka msisitizo kwenye maisha pia. Changamka, hapo ulipomkuta Tino pasiwahi kurudi chini ila kwenda juu. Mshauri mwenzio na weka msisitizo kwenye mambo muhimu. Tino si mbishi. Namfahamu mpaka moyo wake. Mkijaribu na kushindwa, msikate tamaa. Jaribuni tena na tena mpaka mpate kitu cha maana kinachoeleweka. Na utulie, sio ukabadilishwe na mazingira. Endelea na moyo huo huo wa uvumilivu bila kukata tamaa. Kazi ndio imeanza, usije kubweteka. Umemaliza la ugonjwa, atakuja tatizo Lela ambalo nimeambiwa umekubali kusimama na mwenzio, si ndivyo?” “Ndiyo.” Akakubali Sabrina.

“Hilo la muhimu na la msingi sana. Sasa wakati unamkabili Lela, unafikiria kitu gani chakufanya, sio kuanza kupoteza pesa kwenye kununua dhahabu na mapochi ya garama wakati kuna kitega uchumi kitakachokusaidia kuendelea kukuongezea pesa. Sijui kama unanielewa Sabrina?” “Nimeelewa dada.” “Sikatai uvae vizuri, lakini sio ndio unawekeza pesa zote kwenye muonekano kama Lela. Utaachwa vibaya kama Lela, maana namuhurumia sana yule msichana. Mwanaume aliyenaye sio kwamba anampenda. Muhuni tu wa mjini, yupo na Lela sababu ya pesa. Akishaona Lela ameachwa hana pesa, sijui kama atabaki naye. Sasa na wewe akili kichwani. Wekeza kwanza ndipo uvae. Unanisikia?” “Nakusikiliza na nakuelewa. Si ndio Tino?” Akamshika mkono Tino kama kumtoa mawazoni maana ni kama alihama kabisa pale kimawazo.

Tino akamwangalia. “Tino?” Sabrina akamwita taratibu. “Nimeelewa Sabrina! Hata hivyo si ulishakuwa na mawazo ya biashara? Nikufikiria tena kwa upya na kuchukua hatua kwa haraka.” Tino akaongea kwa upole. “Tutakuwa sawa Tino. Naomba usiogope. Taratibu tu, tutafanikiwa. Sawa?” Sabrina akamwambia kwa upole. Tino akabaki kimya. “Naamini tutakuwa sawa dada yangu. Tukikwama tutauliza.” Akaongea Sabrina akimwangalia mke wa Max. “Hapo umenifurahisha. Uthubutu tu, ndio unao takiwa. Na kama tayari na mawazo yalikuwepo, pesa ipo, kwa nini mshindwe?” Akawatia moyo kwa mifano mingi, mpaka Tino akatulia. Wakaaga na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Chungu na Tamu. Sabrina katikati. Tino amempata ila kila mtu anamtahadharisha na Lela. Vita ipo mbeleni. Kila mtu anajipanga kivyake. Itakuaje? Usikose muendelezo kujua nini kitajiri.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment