Sabrina & Tino.
Walitoka
hapo Tino akiwa mtulivu sana. Sabrina akamuacha kabisa mpaka walipofika hotelini. Wakaoga, wakati wapo kitandani akaona amuulize. “Niambie wasiwasi
wako upo wapi, Tino.” “Huu mkono Sabrina. Maisha yangu yote yanategemea huu
mkono. Itachukua miaka kama hii niliyonayo kunijenga kisoikolojia kuwa naweza
kuishi bila huu mkono. Ndio kila kitu changu! Ndio unaonipa pesa na faraja.
Kwenye kuchora pekee ndipo kulikokuwa kukinifanya hata kuweza kuishi na Lela
nyumba moja na nikaweza. Hata nikiwa nimekasirika vipi, nikianza kuchora, akili
zangu zinazama huko. Siko mpweke tena. Hakuna tatizo linasimama nikiwa nachora.
Huu mkono ulikuwa kila kitu changu tokea mdogo naishi na baba pamoja na yule
mke wake. Huwezi kunisikia nikilalamikia kitu nikiwa na huu mkono. Sijui maisha
mengine bila huu mkono!” Tino akaongea kwa masikitiko.
“Mtu
akiniambia nianze kufikiria maisha mengine mbali ya huu mkono!” “Hudhani kama unaweza
kufanikiwa....” “Mbali na huu mkono!?”
Akamkatiza na kuuliza kwa kuhamaki. “Nataka kusema zaidi ya kuchora.
Unaweza kutafuta faraja mbali na uchoraji Tino. Watu wana mafanikio, amani na
furaha na hawachori!” “Kwa kuwa Mungu ndivyo alivyo waandikia hivyo. Mungu
amenipa kipawa hiki kwa sababu Sabrina. Huu mkono umeniketisha na wakuu wa nchi
mbali mbali. Umenitoa nchi nyingi sana hapa ulimwenguni. Kuna kipindi
nilikwenda Italy kwa familia yangu upande wa mama, nilikwenda kumuona jamaa
mmoja anachora, aliziona kazi zangu, alishangaa sio ile yakujisifia. Akanichukua
tukaenda naye Ufaransa akitaka nikakutane na kazi za watu wengine kwenye
maonyesho ya picha za wachoraji mashuhuri. Kwa kukiri yeye mwenyewe, alisema
hakuna hata kazi moja inayopita ujuzi wangu.” Tino akakaa.
“Sabrina, huu mkono wangu wa kulia umebarikiwa! Si kwa kujisifia, ni kwa kile kipaji Mungu ameweka ndani yangu. Kama isingekuwa mkataba wa hii kazi kunifunga, ningekuwa nikifanya naye yule jamaa. Nilitaka mkataba wangu huu uishe, nijiongeze. Mbali yakuchora ramani za majengo, nilifikiria hata kuhamia Italy, au Ufaransa. Nisome kidogo tu kupata leseni kule, niendelee na kazi. Hapa najiona nimerudi nyuma haswa.” Sabrina akaona hana jinsi akambadili mtazamo kwa haraka ila kuungana naye, matokeo ndiyo yatambadili. “Basi tukatafute ushauri huko KCMC. Tuone watakachotuambia.” Usiku huo wakalala, bila mapenzi.
Moshi.
W |
aliondoka
jijini Dar asubuhi na mapema kabla hata jua halijachomoza. Wakiwa njiani
alimsikia Tino akiwasiliana na mtu.
Baada ya mazungumzo ya muda, wakitaniana kidogo, akamsikia Tino akimwambia, “Huu ndio ule wakati wakulipa deni yako Swai. Nitakuwa mjini
kwako kwa muda, lakini sitataka mtu alijua hilo.” “Unamkimbia nani?” Wakataniana
tena kidogo, akaendelea. “Nahitaji hifadhi mjini
kwako.” Akamalizia hivyo. Wakataniana kidogo, akamsikia anasikiliza. “Yaani hapa nipo njiani.” Akaongeza Tino. Mwishoe
akamuona amefurahia, akamshukuru sana na kukata.
“Yesss!”
Akashangilia Tino. “Umeona jinsi huu mkono unavyoniketisha na wakuu na kunipa
mengi hapa duniani?” Sabrina akamgeukia kidogo na kurudisha macho barabarani
kuendelea kuendesha. “Huyu Mzee alikuwa rafiki yake baba. Wakati nipo chuoni
baba alimleta kwangu na kumuombea nimtengenezee ramani nzuri sana ya hoteli.
Bila shida, nikamchorea ile ramani. Akaipeleka kwa mjenzi wake. Huyo mtu
alikuwa na kampuni kubwa tu ya ujenzi. Alirudi kwa baba, akasema yule mjenzi
alimshangaa sana kuwa amepata wapi ramani kama ile. Wakamsifia sana. Sasa
akataka kunilipa pesa nyingi, nikamwambia anisaidie ada ya mwaka ule tu. Badala
ya baba kunilipia, yeye ndio alipe. Akashangaa akasema mbona nikidogo hivyo,
nikamwambia nyingine nitakuja kudai wakati mwingine.” Tino akaendelea akisikika
kuhamasika haswa.
“Sasa
tokea wakati ule, akiwa na kazi zake na matajiri wenzake, walikuwa wakinipa
mimi. Ile nyumba yangu ya Kunduchi nimejenga kwa kazi zake alizokuwa akinipa na
marafiki zake. Kazi za pembeni tu sio ile kampuni. Ana mahoteli huko
Kilimanjaro, Dar na Mwanza. Ila apartment anazo mbili tu, Dar na Moshi. Sasa leo
ndio nimemkumbushia deni ya kazi ya kwanza kabisa. Ametupa sehemu ya kuishi
kwenye moja ya apartment zake hapo Moshi. Sijawahi kufika, lakini huwa anapenda
vitu vizuri. Naamini patatufaa kwa muda tutakao kuwa hapo Moshi.” “Hongera
Tino.” Sabrina akatamani kuuliza juu ya ushauri waliopewa na mkewe Max,
wakununua nyumba mbali na ile ya Kunduchi, akaona anyamaze kwanza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walifika
jioni kukiwa kumeshakuwa na baridi. Walisimama mara kadhaa njiani. Lakini
Sabrina aliweza kuendesha bila shida. Walielekea moja kwa moja kwenye hizo
apartment. Zilizojulikana kwa jina la Luxury Villa. Kwa hakika zilikuwa nzuri.
Walifika hapo wakakuta sehemu ya Mapokezi wanayo magizo yao. Wakasindikizwa
mpaka kwenye hiyo sehemu yao waliyopewa. Chumba kimoja, sebule na jiko. Ukitoka
baraza la mbele uliweza kuona sehemu ya kuogelea, nyuma bustani nzuri. “Hakika
hapa ni pazuri!” Akakubali Sabrina. Tino akatoa simu na kumpigia huyo mmiliki,
Swai. Akamshukuru kwa mapokezi mazuri, wakataniana tena kidogo wakaagana.
“Nashukuru
Sabrina. Asante kuwa na mimi. Nashukuru kutembea na mimi.” Shukurani hizo
zikaendelea. Usiku uliopita walilala bila mapenzi, lakini usiku huo Tino alitoa
shukurani zake zikisindikizwa na penzi zito kwa Sabrina. Kwa uchovu, Sabrina
akalala kama nusu mfu. Aliamka asubuhi ya saa nne, Tino ndio anatoka mazoezini.
“Najua hata huko hospitalini wataniongezea mazoezi ya kitaalamu zaidi. Acha na mimi nikazane.” Katika
hilo Sabrina akawa mtu wakutia moyo tu, kwa kuwa alijua hakuna jinsi
angemwambia Tino vinginevyo wakaelewana.
Wakatulia
hapo juma la kwanza. Wakifurahia kuwa mbali na Lela na purukushani za jiji la
Dar. Mapenzi kila wakiangaliana, bila kuchoka. Mazoezi mengine Tino
aliyamalizia mwilini kwa Sabrina wakicheka na kufurahia bila ya kujali kesho.
Ukweli walikuwa na wakati mzuri zaidi Tino ambaye kwa mara ya kwanza maishani
ni kama amepata faraja ya kweli. Sabrina alikuwa akimjali sana. Akimfariji bila
kuchoka. Akimuona amepotelea mawazoni, basi Sabrina atamuongelesha kwa hili na
lile, mpaka watacheka. Kufuatana ndio ilikuwa kila mahali. Sabrina akiwa jikoni
akipika basi ujue Tino atakuwa naye hapo jikoni akimwangalia jinsi anavyompikia
hivyo vyakula vya kumpa nguvu huku akimuongelesha mpaka amalize kupika na
kulishana.
Palipo Amani, Uharibifu nao Hunyemelea.
W |
akati Sabrina na Tino wakiendelea kufurahiana wakithibitishiana walikusudiwa kuwa pamoja tokea mwanzo, kufutana machozi kwa haja, naye shetani alikuwa kazini akipanga yake. Huko kwa Max akakutana na Lela halisia. Alidhani wanamfahamu Lela, kwamba vile Lela alivyo ndivyo amemaliza, lakini akaja kukutana na Lela mwingine, aliyemjia kivingine kabisa, tena akiwa amejipanga vilivyo, tena na mwanasheria aliyekuja na hoja za nguvu mpaka Max mwenyewe, mtaalamu wa kesi, akasalimu amri na kuwakimbia kwa kuwaambia waahirishe kicho kikao chao, yupo na majukumu mengine, wapange wakati mwingine wa kukutana.
Baada ya Lela na wakili wake kuondoka
ofisini kwa Max, Max alibaki akitafakari kwa kina alichokisikia kutoka kwa
Lela. Kila alivyopanga hoja zake kumkabili Lela, tatizo lililokuwa limebaki ni
Sabrina. Utetezi wake mkubwa Lela ni kumleta Sabrina nyumbani kwake kwa ajili
maalumu ya kumlea mgonjwa, mumewe. Akajitetea kwa machozi kuwa hajawahi
kumtelekeza mumewe, ila kumpa huduma bora bila ya kujali garama ambazo zilikuwa
juu sana. Lela alisema alimuacha na msichana msomi kama Sabrina aliyempa pesa
nyingi na usafiri kabisa ili chochote kikitokea, aweze kumkimbiza mumewe
hospitalini. “Kama mimi ningekuwa nimemtelekeza
mume wangu au simjali, ningemuachia msichana kama Sabrina ambaye nilimlipa
mshahara mkubwa vile, pamoja na usafiri?” Akauliza Lela akilia kwa
uchungu sana.
“Kama nia yangu ni kumuangamiza huyo Tino, ningemuacha kweli kwenye
mikono salama na nyenzo za kumsaidia?” Ushahidi
wa ujumbe kutoka kwa Sabrina mwenyewe akisema Lela alimuachia mgonjwa, tena
baada ya kulipwa huo mshahara anaosema Lela ni mkubwa sana, wa miezi mitatu, Lela
alikuwa nao. Ujumbe alioandika Sabrina kwa Lela akidhani utamfunga Lela ndio
ukawa msaada kwa Lela. Ubaya wa ule ujumbe wa Sabrina haukuwa na kiasi cha pesa
alicholipwa na Lela kama mshahara wake, kwa hiyo Lela akataja pesa anayotaka
yeye. Ambayo ilikuwa kubwa ya kushangaza. Akasisitiza kwa masikitiko kwamba hicho
ndicho kiasi chote alichokuwa amemlipa Sabrina, na akawaambia ndio waamini
jinsi kumuuguza Tino ilivyokuwa ikimgarimu.
Akaendelea
kujitetea akitumia ujumbe huohuo wa Sabrina juu ya kuwatelekeza. Lela alikuja
na uthibitisho wa ugonjwa wake mpaka wa kutoka kwa daktari aliyekuwa
akimuhudumia maradhi ya pressure yaliyosababishwa na kumuuguza huyohuyo Tino
kabla hajalemewa na kutafuta msaada wa Sabrina. Lela alieleza kuwa alikuwa
akiugua kwa muda mrefu ila kukosa muda wa matibabu yake sababu ya kumuuguza
mumewe ambaye kwa asilimia kubwa ndiye aliyechangia maradhi yake mpaka kulazwa.
“Nilipompata Sabrina, tukakubaliana anisaidie
kumtunza Tino, ndipo nilipokwenda na mimi hospitalini.” Lela akaeleza
mengi kwa machozi akionyesha Tino ndiye amekosa fadhila.
Nani wakutolewa muhanga….
M |
ax
akaendelea kuwaza akipanga hoja zake kutokana na kile alichokizungumza Lela na
Tino ambaye ndio mteja wake kwa wakati ule. Kila alipopanga hoja zake, bado tatizo
likabaki ‘Sabrina’. Kwamba akimtoa Sabrina pichani, na yeye akatunga
yake ya kumfundisha Tino kujitetea mahakamani, lazima kushinda tu maana itakuwa
ni maneno yake Tino dhidi ya Lela. Ikabaki jinsi ya kumtoa Sabrina kwa Tino.
Max akajua haitakuwa rahisi Tino kumuachia Sabrina. Kwanza Tino alishasema ni
bora apoteze kila kitu kuliko kumuingiza Sabrina matatizoni. “Huyu Sabrina
hawezi akaninyima pesa ndefu namna hii!” Max akawaza akipigia mahesabu pesa
atakayolipwa na Tino. Akajiambia nilazima amuendee kwa hoja za kueleweka. Ipi? Kazi
ya kuanza kumpeleleza Sabrina, kumjua yeye ni nani ili kumfitini kirahisi,
ikaanza.
Max akampeleleza Sabrina kutaka kujua
ni msichana wa namna gani, ikashindikana kwa sababu Sabrina si mtoto wa mjini,
hana kashfa, hajulikani na yeyote yule. Akajua Lela mwenyewe ndiye atakayempa
habari za Sabrina. Kwa kuwa Lela ni muongeaji sana, Max akaandaa maswali
yakumchomekea hapo katikati wakati akijieleza ili akiwa anaongea yake, na yake
yajibiwe. Na kweli. Bahati kwa Max hasara kwa Sabrina. Max akampigia Lela akiwa
amejiandaa na maswali yake, na kweli Lela aliyajibu kwa undani mpaka Max
akaridhika kuwa amepata nondo za kumtosha kusuka yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku
inayofuata kwa Max ambayo ndio alipanga azungumze na Tino ndio ikawa siku ya
Tino kwenda KCMC kumuona daktari kwa mara ya kwanza. Sabrina na Tino waliamka
na furaha, wasijue linalowasubiri mbeleni. Tino alikuwa na tumaini kubwa kwa
daktari atakayeenda kumuona kana kwamba ndio alikuwa anakwenda kupokea upanyaji
wake wa huo mkono wa kulia aliokuwa akiutegemea sana. Moyo ulijawa furaha, hata
akaomba penzi la asubuhi kabla hawajatoka maana hakuwa amekwenda mazoezini.
Sabrina akiwa ametoka tu bafuni na taulo lake, akaliachia na kuanguka sakafuni
mbele ya Tino. Tino akapiga magoti mbele yake kwa haraka, akamshikilia hips
zake kwa nguvu, midomo ikaanza kutembea mwilini kwa Sabrina. Akiwa amesimama vilevile,
midomo ya Tino ikatulia sehemu ambayo Sabrina akasalimu amri akafanikisha bao
la furaha. Akacheka sana, asiamini. Tino akamuinamisha kitandani na yeye
akafaidi penzi ndipo wakatoka.
Huyo
huyo Mzee Swai akamtambulisha kwa daktari ambaye alikubali kuwaona bila
kusubiri muda mrefu. Baada ya siku 5
mbeleni, Sabrina akamsindikiza mpaka KCMC. Mzee Swai alimwambia yule daktari
kuwa Tino ni kijana wake aliyeachiwa na marehemu baba yake. Kwa hiyo amuhudumie
kama ni kijana wa Swai. Na kweli, alimpokea akiwa mcheshi. Akamuhoji maswali kadhaa.
Akaangalia pressure yake. Akamwitia mtu wa kufanyia ule mkono mazoezi.
Wakamwambia hakuna dawa yakumpa ili mkono upone, ila akiendelea hivyo bila kuwa
na pressure ya juu, mazoezi ya ule mkono na viungo kwa jumla, baada ya muda
ataona mabadiliko. Hilo halikumfurahisha Tino ambaye aliuliza maswali mengi
akitaka kuona kama kuna njia ya haraka ya kuponyesha ule mkono. Wakapewa siku
za kwenda mazoezini wakaondoka, Tino akiwa hana furaha hata kidogo.
Sabrina
akidhani wamemaliza siku kwa habari mbaya, ili usiku atafute jinsi ya kumtuliza
mpenzi wake, kwenye saa 12 jioni Max naye akapiga simu. Tino alipoona tu simu
ya Max, akapokea kwa haraka. “Mambo yametibuka Tino.
Lela amerudi kivingine.” Tino akakaa kwa haraka pale alipokuwa amejilaza
kochini, macho kwenye luninga, amekumbatia mkono wake hata hamuongeleshi
Sabrina aliyekuwa amekaa kochi la pembeni yake. “Nini!?”
Tino akauliza kwa mshituko sana. “Amekataa kusaini
talaka. Anasema yeye bado anakupenda. Aliondoka nyumbani akiwa mgonjwa, akaona
asimlemee msichana wa kazi aliyekuwa amemleta pale nyumbani akuhudumie wewe.
Akaonelea yeye akauguzwe kwa rafiki ambaye ni kama ndugu. Ameleta uthibitisho
wa siku alizokuwa akienda hospitalini. Anaonekana pressure ilikuwa ikimsumbua.”
“Haiwezekani Max!” Tino akashangaa sana.
“Huwezi amini Tino, amekuja ofisini kwangu na wakili wake. Lela
analia, anasema umekosa fadhila. Amepatwa pressure kwa kukuuguza wewe.
Yeye ameondoka akiwa amekuachia msichana mzuri kabisa, ambaye ni Sabrina ili
akuuguze wewe, halafu huku nyuma umemfungia nyumba!” “Na maswala ya pesa?”
Akauliza Tino. “Anaakili sana Lela. Ameonyesha ujumbe
wa Sabrina aliomwandikia. Ubaya ule ujumbe wa Sabrina haukuwa na kiasi cha pesa
alizotaja kulipwa na Lela. Kwa hiyo Lela ametaja yeye kiwango kikubwa sana cha
pesa ambacho alimwachia Sabrina akidai ilikuwa ni kwa ajili ya mshahara wake
Sabrina akimlipa kwa muda mrefu ili asije kukukimbia maana wafanyakazi walikuwa
wakikukimbia sababu ya jukumu zito la kukulea wewe na kumuacha yeye akihangaika
na wewe peke yake. Anasema sasa, alipompata Sabrina ndipo akaona amtie moyo kwa
kumlipa pesa nyingi ili akae na pia akamuachia pia pesa ya matumizi, lakini
anasema Sabrina ndio hakuelewa, alidhani pesa yote hiyo ni ya mshahara tu.
Ambacho hicho kiasi alichotaja Lela, ni kingi sana Tino. Kwa kipindi hicho
mpaka sasa, kinatakiwa kiwatoshe.” Max akamtajia Tino hicho kiasi
alichosema Lela alimpa Sabrina. “No way!” Tino
akahamaki kwa sauti.
“Muongo kabisa, anamsingizia Sabrina. Mimi ni shahidi wa Sabrina.” Tino
akatetea, Max akajua bado yupo upande wa Sabrina, lazima kuongeza nguvu. “Sasa hayo ni maneno yake Sabrina dhidi ya Lela maana hata
wewe hukuhesabu pesa alizomkabidhi Sabrina.” Tino akatulia. “Pesa yote si alimkabidhi Sabrina na Sabrina ndio alikuwa
akitoa za matumizi ya pale nyumbani?” Max akauliza. “Ndiyo lakini…” “Sasa ndio nakwambia, huwezi kusema wewe ni
shahidi wa Sabrina kwa imani tu, Tino! Ni mpaka uwe ulizihesabu hizo pesa na
kuthibitisha. Na hilo watakubana nalo mahakamani. Kuwa makini kwa kila
unachozungumza.” Hapo Tino akapoa.
“Na kuna jambo nitakwambia baadaye tukiwa wawili. Ila kuhusu pesa za
benki hata hajagusia kabisa ila kulalamika garama za kukuuguza wewe zilikuwa
juu sana. Ila nilizungumza na yule muhasibu, anasema tarehe 15 juzi, Lela alimpigia
simu akimuulizia mshahara wako. Alipozikosa nafikiri ndipo alipokimbilia
nyumbani kwenu.” “Sema kwangu.” Tino akamkatisha kwa
hasira. “Kisheria ni kwenu wote wawili, Tino.”
Max akamuweka sawa na kumuumiza Tino zaidi.
“Sasa alipofika Kunduchi, ndipo mlinzi akamkatalia kuingia mlangoni.
Nafikiri sasa ndipo akafungua simu yake, akatafuta mwanasheria, na huyo
mwanasheria anaonekana amejipanga Tino. Lela amerudi akiwa na lawama sana na
wewe.” “Huo ujauzito niliosikia anao?” Tino
akauliza. “Mimi sikuona tumbo. Kama anayo mimba basi
bado haijatokeza au ilitoka. Ila hivi ninavyokwambia Lela anataka ndoa yake.
Anakulaumu wewe ndio unamkimbia baada ya kukuuguza kwa miezi sita mchana na
usiku mpaka yeye ndio ameugua.” “Haiwezekani Max! Haiwezekani!” Tino
akasimama. Sabrina aliishiwa nguvu, hata kusogea alikuwa hawezi tena.
“Kwa kifupi nakusubiria wewe. Na kwa sasa inaonyesha wewe ndio
unamuacha bila kosa. Na unamjua Lela, atakuwa ameshachafua kila mahali.” “Hilo
sijali. Juu ya ile nyumba yangu?” Akauliza
Tino. “Hapo lazima ucheze kwa makini sana Tino.
Ukionekana wewe ndio unamuacha bila makosa, kuna athari zake.” “Leo ni siku
mbaya sana kaka. Naona kila kitu kipo vibaya. Kila ninapoenda habari ni mbaya!”
Akalalamika Tino. “Mimi ninachoshauri ni utulivu na
umakini. Lela bado hajajua kama upo na Sabrina. Hilo moja.” Hapo Tino
akashituka.
“Na kama upo naye, mpoje naye! Upo naye hapo karibu?” Max
akauliza kama anayetaka kumteta Sabrina. Tino akakubali kama Sabrina yupo hapo.
Max akaendelea akisikika amegairi alichotaka kuzungumza. “Kwa hiyo muwe makini sana kusiibuke sababu ingine tena itakayomfanya
akakushinda. Maana hakuna uthibitisho kama Lela alikuwa kwa mwanaume, maana
hana ujauzito wala uthibitisho. Anasema alikuwa akiuguzwa. Kama alifukuzwa kazi
kwa kuugua, tena anasema wewe ndiye uliyesababisha maradhi kwake, unajukumu
lakumtunza kama mke mpaka kuhitimisha.” Tino akatupa simu kwenye kochi kwa
hasira na kuingia chumbani. Sabrina alibaki ametoa macho kwa mshituko.
Kisicho Riziki,
Hakiliki.
S |
abrina
akabaki amekaa hapo kwenye kochi kama aliyepigwa sindano ya ganzi baada ya kama
dakika 10 akamuona Tino ametoka na nguo za mazoezi. “Naomba uwe makini Sabrina.”
Tino akaongea akitaka kupita ila akasimama kama kuweka msisitizo. Sabrina
akamgeukia. “Kwenye nini?” “Kama ulivyosikia. Lela hana mimba. Max anasema ikitokea
sisi tunaharibu, atashinda.” “Unamaanisha nini sisi tusiharibu?” Sabrina
akauliza taratibu tu. “Katika kila kitu, lakini zaidi kwenye mambo ya ujauzito.
Hakikisha hushiki mimba.” “Hudhani kwamba hilo angalizo limechelewa?”
Sabrina akauliza akiwa ameshakasirika na yeye. Tino akashituka sana. “Inamaana
umeshashika mimba tayari!?” Akauliza kwa kuhamaki sana kama ambaye alikuwa
akibakwa na Sabrina.
“Sijui!”
Sabrina akajibu akiwa anamtizama. “Hapana Sabrina. Sipo kwenye wakati ambao
naweza kulea. Angalia afya yangu. Sijui hata mwisho wa maisha yangu utakuwa
vipi! Mkono ambao ndio nautegemea maishani ndio huo nimeambiwa hakuna tiba ili
upone kwa haraka. Huyo mtoto atakuja kwenye mazingira gani!?” Sabrina akabaki
akimtizama. “Yaani la ugonjwa halijaisha, tunaingiza watoto! Tutampa sababu
Lela kunishinda.” “Hebu subiri kwanza Tino. Acha kunichanganya tafadhali. Mbona
gafla inakuwa ni kama unatoa lawama kwangu!? Halafu unaposema Lela atakushinda,
unamaanisha unalinganisha thamani ya nyumba na watoto!?” Sabrina akauliza.
“Tafadhali
fikiria Sabrina, hata mara moja tu kama mtumzima na uliyesoma.” Sabrina akatoa
macho kwa kumshangaa. “Huyo mtoto tutamuweka wapi? Hapa tulipo sisi wenyewe
tumehifadhiwa! Hatima yangu na Lela ni kama ulivyosikia. Unafikiri itakuaje?” “Subiri
kwanza Tino. Maana naona unazidi kuwa mkali na mwishoe utapandisha pressure kwa
kitu ambacho kilishatokea.” “Inamaana umesha shika mimba?” “Tafadhali Tino,
naomba utulie. Kumbuka hata mwezi haujapita tokea tuanze kukutana kimapenzi.
Kwa hiyo sijui. Naomba tusiazime matatizo ya kesho leo, ukajikuta unaongea
mambo ambayo utakuja kujuta baadaye.” “Siwezi kujuta. Hili naomba ulizingatie
Sabrina. Sina mazingira yakuanza na watoto sasa hivi. Nipo kwenye wakati mbaya
sana kwenye maisha yangu.” Tino akachukua simu yake pale alipokuwa ameitupa kwa
hasira. Akamuona amesoma ujumbe fulani uliokuwa umeingia, kisha akaondoka bila
kuaga. Akamuacha Sabrina amepigwa na butwaa asiamini alichokisikia kutoka kwa
Tino.
Kwa Tino..
Max
alimuomba akiwa peke yake ampigie ili wazungumze. Akaelekea gym akiwa na hasira
na maumivu rohoni akampigia akijua wazi huko alipo Sabrina hatasikia. Max
akapokea kwa haraka kama ambaye alikuwa akimsubiria yeye. “Sasa mimi sina habari nzuri sana Tino na nina sikitika sina
jinsi nyingine ya kufanya ila kukwambia tu. Ili ujue chakufanya. Au nikupigie
wakati mwingine, tuzungumze vizuri?” “Tafadhali niambie tu. Hii siku ishakuwa
mbaya.” Tino akaongea kwa jazba.
“Nimepata
tetesi kutoka kwa mtu wa karibu sana wa Lela ambaye wapo kundi moja na dada
yake Sabrina. Nimesikia huwa wanakuwa baa na sehemu za starehe pamoja, ila
sitakutajia jina lake. Lakini mimi kama kaka yako, nimeona nikwambie tu, wewe
mwenyewe uamue na ujue jinsi ya kujipanga kuanzia sasa.” “Juu ya nini tena?”
Tino akauliza. “Sabrina. Kumbe huyo binti yupo hapo kwa
malengo tokea mwanzo kabisa. Nasikia kumbe dada yake yupo karibu sana na Lela.
Anajua jinsi ulivyo na pesa na jinsi Lela anavyoichezea pesa yako. Sasa nasikia
dada yake alipoona Lela anafaidi na hakutunzi, ndipo akaona mwanya. Akaamua
kumuunganishia mdogo wake. Nasikia Sabrina maisha yalikuwa yamemshinda kabisa
huko nyumbani kwao. Ndio dada yake akamuita mjini. Akamueleza juu yako, ndio
Sabrina akakubali kuja kupambana kufa na kupona akikuonyesha anakujali kwa hali
na mali ili ukipona tu, akubane.” Tino akaumia sana maana ni kweli hata
Sabrina alimwambia maisha yalikuwa magumu sana kwake, hakufanikiwa kupata ajira
baada ya kumaliza chuo, akabaki nyumbani akisaidia kazi za nyumbani.
“Hawa mabinti
wawili hawa, Sabrina na dada yake, nasikia kwao ni huko Chalinze. Wanahali ya
ushirikina sana kwao. Huyo aliyeniambia ambaye wapo kundi moja kwenye starehe,
nasikia anasema huyo dada yake huko kazini hawawezi kumgusa jinsi
alivyojizatiti. Hata viongozi wake wanamuogopa. Akitaka jambo lake huko kazini,
nasikia anajisifia kuwa ni lazima liwe hata kwa numba. Ndio maana ana safari
nyingi za kikazi za nje ya nchi kuliko wenzake wote huko kazini, kumbe ni kwa
kuzisuka kiushirikina. Sasa tetesi zilizopo, nilizosikia eti wana mpango
wa mambo mawili. Sabrina kujishikisha mimba na kutumia mbinu za uchawi kukubana
mpaka ndoa.” “Basi nimeshachelewa kaka. Nahisi ameshashika mimba.” Tino
akaongea kwa kuumia sana akikumbuka juhudi za Sabrina kwake akidhani ni upendo
kumbe nia ni kuja kula pesa yake! Tino akabaki akitingisha kichwa kama ambaye
haamini.
Max
akafanikiwa kupata moyo wa Tino. Akajua yupo upande wake. “Sasa ujue huyo atakuangamiza. Akizaa tu huyo mtoto, ukitoka
kwenye tatizo Lela, unakuja yeye ambaye atakuwa amekuzalia na mtoto.”
Tino akakaa kabisa. “Na Lela akishajua tu kama umekuwa
na mahusiano naye, ndio ujue utakuwa umepoteza kila kitu, wanawake hao
watakuacha barabarani.” “Sijui nina
mkosi gani kaka yangu! Kwa Sabrina nilijua nimepata, na nikamuamini sana, kumbe
ni tapeli mtupu! Amekuja kwangu na maneno ya kitapeli, akinionyesha ananijali,
kumbe macho yake yapo kwenye mali zangu!” Tino akaumia sana.
“Ila nafikiri
kwake huyo hatujachelewa. Tunaweza kumtoa kwenye picha kirahisi sana akiwa
hukohuko Moshi kabla hajaja huku kuungana na dada yake. Acha nijipange mimi
kwanza, ndipo nikupe na wewe muongozo. Ila kuanzia sasa, jitahidi sana kumkwepa
na kuwa naye makini ili.” Max akaendelea kumtia hofu mpaka akaridhika
kwamba hata Tino akirudi kwa Sabrina, hakuna kutengeneza tena. Yeye ndio
ameshika masikio ya Tino sasa. Alipojiridhisha ndipo, akaaga akiwa amemuacha
Tino ameishiwa nguvu kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mpaka
Tino anarudi, Sabrina alikuwa amebaki hapohapo alipokuwa amekaa. Tino akaingia
kuoga, akatoka, Sabrina amebaki hapo hapo. “Nataka tukatafute ushauri wa
madktari. Kama imetungwa, kabla hajawa mtoto, tutafute dawa ili uanze kupata
siku zako kama kawaida.” Sabrina alishangaa na kuumia sana. “Unamaanisha kutoa
mimba! Yaani kuua mtoto sababu wewe na Lela hamjafikia muafaka!?” “Unang’ang’ania
nini wakati wewe mwenyewe umesema haijafika hata mwezi!? Inamaana hajakuwa
mtoto bado. Tafadhali kuwa mtu wakufikiria Sabrina. Hata mtoto wa darasa la
saba ataelewa hili. Huyo sio mtoto, itakuwa donge tu la damu. Unataka aje kuwa
mtoto halafu aje aishi wapi? Mazingira gani!? Fikiria.” Sabrina alimtizama Tino
akatingisha kichwa kwa kuumia sana. Huku akimshangaa. “Kwanza, kama mimba
imetungwa tayari, hakuna cha donge, huyo ni mtoto. Na naomba nikutoe wasiwasi
Tino. Uzuri ni kwamba kama ni mimba imetungwa, itakuwa kwangu sio kwako. Mwambie
Max anayekufundisha jinsi ya kuishi, kuwa wewe upo huru kuendelea na maisha
yako kama kawaida.” Sabrina akaondoka kuingia chumbani kwao, bafuni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sabrina
alikuwa kwenye mshtuko wakupita kiasi. Hakutegemea kama Tino angembadilikia hivyo!
Na ni kweli alijiachia. Akajishika tumbo nakuanza kufikiria mara ya mwisho
kupata siku zake. Akili ikawa ilishachanganyikiwa. Hakukumbuka. Akaanza kulia
kwa hofu. ‘Itakuaje kama nimeshika mimba?
Nitakwenda wapi na nitafanya nini?’ Hofu ikazidi kumuingia.
Akakumbuka alivyoondoka nyumbani bila kuaga ila kuwafikishia ujumbe kupitia
Sabina.
“Nitakwenda wapi?” Sabrina
akazidi kuwaza huku akilia. “Jack!” Akamkumbuka Jack. Kijana aliyemvumilia na
kumsubiri bila kuchoka. Ukaribisho aliompa kwenda kuanza upya. Makazi na
malazi. Akakumbuka ujumbe wa mwisho aliomtumia na kumblock bila kutaka kumsikia
anamjibu nini. Akaendelea kujiachia kwa Tino bila kufikiria. Akazidi kuumia.
Akakumbuka mazungumzo kati ya Tino na Max. Akajua lazima Tino atarudi kwa
mkewe. “Kweli mimi fungu la kukosa!” Sabrina akazidi kujikatia tamaa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment