Ibada ya sifa ilianza
kwa nguvu zote Junior akiwachangamsha kwa kuimba wakicheza mpaka wazee. Walizidi
kushangilia pale mchungaji alipokwenda kukamata gitaa la bezi. Alijua kulipiga,
ungejua ya kale ni mali. Ikawa ibada nzuri sana, ila watu wakahisi lazima kuna
jambo jema. Si kawaida yao hao watatu kuongoza ibada ya sifa ni mpaka wawe na
jambo maalumu. Kwa hiyo hapo jukwaani akawepo mchungaji na vijana wake hao
watatu. Akiwepo Noah kiongozi wa kila siku. Ungemuona mama mchungaji, ungejua
tu, ni Junior ndiye anayeongoza ibada na mumewe amemkumbusha mbali. Alikuwa
akicheza na vigelegele kila mara.
Ukafika wakati
mchungaji, akasimama. “Nina matangazo mawili muhimu kabla ya kuleta neno.”
Kimya. “La kwanza ni la kusitisha uchumba.” Akaangalia waumini wote wakahamaki
wakinong’ona. “Nimepata nafasi ya kuwasikiliza wote hawa wawili, wamefikia
muafaka kwa amani kabisa. Kila mmoja amekubali kuendelea na mwenzie kama
mtumishi, lakini si katika safari ya ndoa. Wao wapo na amani na makubaliano.”
Kimya kila mmoja akiwa na shauku ya kujua ni nani.
“Hope ni binti
yangu,..” Wakashangaa sana na minong’ono kuzidi. Ndipo wakajua Ester
hakusambaza habari. Kwamba watu hawafahamu. Basi mchungaji akaiweka vizuri,
kabla hapajapoa na ndipo akatangaza uchumba wa Ezra na Jelini. Watu walishangaa
sana, ila kushangilia pia. Wakaitwa mbele.
Walizidi kushangilia
pale Jelini alipokuwa akisogelea madhabahuni. Ukweli alipendeza mno. Gauni la
heshima alilokuwa amevaa na rangi zake, vito vya thamani alivyokuwa amevaa!
Ungetamani abaki umtizame tu. Umbile lake lilikaa vizuri kwenye hilo gauni! Kwa
hakika walipendeza.
Picha zao zikaanza
kurushwa kwenye screen kubwa ya
kanisa. Wao wawili wakiwa pamoja ndipo tukio zima la siku ya ijumaa
wakivalishana pete. Ilipendeza sana.
“Sasa hapa ni
kuwaombea tu. Kama mlivyoona mpaka video yao fupi, walishavalishana pete. Na nimeambiwa
hiyo pete kidoleni kwa Jelini, kutoka ni mwiko. Hataki nayo kabisa.”
Jelini akaficha mikono nyuma, akikataa kwa wazi kabisa. Kichwa na mabega
vikimsaidia. Watu wakaanza kucheka wakishangilia. Ezra akajisikia kupendwa! Na hivi alishalizwa hapohapo!
Halafu safari hii anachumbia mtoto mkali, Jelini! Alijawa sifa huyo! Cheko
njenje.
“Basi, mama. Leo ni siku yako. Nataka
ufurahie. Hakuna wakutoa hiyo pete. Sawa Ezra?” “Kabisa. Itaongezeka tu lakini
si kutoka.” Wakashangilia watu kwa vigelegele. Mama mchungaji mpaka madhabahuni
akishangilia kwa furaha.
“Acha tutamke baraka
kwenye safari yenu ya uchumba.” Wakapiga magoti, lakini Ezra hakutulia. Akageuka
akiamtafuta Junior mpaka akampata kwa macho. Akamuita kabisa, akaenda na yeye
pale mbele, ndipo akili ya Ezra ikatulia. Wazee wakawasogelea. Wakaombewa, na
pongezi kisha ibada kuendelea.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mama mchungaji
aliandaa tafrija nzuri sana tena ya kisasa. Jelini na Ezra walipendeza kana
kwamba ndio siku ya harusi yao. Maana Jelini alirudi tena nyumbani kubadilisha,
akavaa nguo ya usiku iliyokuwa imekaa vizuri haswa, kisha Ezra akavaa shati
linalofanana rangi na hilo gauni. Wakavutia. Cheko wakati wote. Mpaka usiku
walipomaliza.
~~~~~~~~~~~~~~~
Jelini na Emelda
wakapanga kukutana mida ya saa nne asubuhi ya siku inayofuta. Wakafanye
manunuzi ya safari. Ila shida ya Jelini ni kumnunulia vitu vya maana zaidi vya kuvaa,
maana alishamuona aina ya vitu anavyovaa haviendani na hadhi aliyoingia,
mwanamke wa Junior. Akataka kumnunulia vitu vizuri na vya kisasa kutokana na
uwezo wa Junior. Ukweli Junior alimshukuru.
Maandalizi ya safari
kwa wanne hao, yakanoga. Maana na Jelini aliruhusiwa kwenda nao huko Songea. Wakatawanyika
wakiwa wamehamasika kwelikweli. Hatimaye hilo juma likaisha.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mume wa Ester
alishapiga simu tokea asubuhi na kumtaarifu mchungaji wasingeweza kufika
kanisani kwani Ester ni mgonjwa. Mchungaji akawapa pole na kukata simu bila ya
kuongeza kitu. Ester alipoambiwa baba yake alitoa tu pole na kukata simu,
ikamuuma sana na kujua hakuwa akitaniwa tena. Hata kwenye tafrija nyumbani kwao
akashindwa kuhudhuria. Ikabidi huo uongo uendelee tu bila mumewe kujua ukweli.
Jumatatu
Emelda akabakia
yuleyule. Kudamka kufanya shuguli zake, kama hajachumbiwa na Junior! Akafanya
yake mpaka kuandaa mboga za mchana ili mama Leti akifika asipate shida. Mida ya
saa nne Jelini akawa ameshafika kumchukua. Akaingia mpaka chumbani kwake kuona
alicho nacho.
“Kwa nguo za ndani na
sidiria nakupa 80. Sio mbaya. Ila vya nje vyote, twende tukasake. Mpaka
sanduku. Halafu na vya mama. Akiingia kwenye gari anakuja mjini, mambo yake
safi.” “Basi huyo ndiye nina wasiwasi naye Jelini! Wamemtoa kwenye matope, hana
nguo. Sidhani kama atakuwa kwenye hali nzuri. Kichwa mpaka mguu! Ila nimembebea baadhi ya nguo.” “Usijali.
Tunamsafi kuanzia kichwa mpaka miguu, sisi wenyewe, hapohapo hotelini kabla ya
safari.” Wawili hao ushoga tayari.
Na vile alivyomchukulia,
haikumuwia ngumu kumzoea na kumwambia chochote hata kama alichoona kwa wengine
ni fedheha kusema, lakini kwa Jelini alikuwa huru kuzungumza naye. Alishamsoma
Jelini na kumuelewa kwa haraka sana. Japokuwa anaonekana wa thamani, lakini
anathamini mtu na si kile alichonacho. Akajikuta amemwamini kwa haraka.
Hapo Emelda alikuwa
na mihela, alishatumiwa na Junior tokea usiku uliopita. Naye alijitutumua
kumuonyesha ni bora kuliko Edwin. Akatoa pesa ya nguvu, tena ndefu kwa huyo
Emelda. Na kumwambia akiishiwa huko kwenye manunuzi yake na Jelini, asisite
kumwambia. Atamrushia kwa haraka.
Wakatoka hapo
wakaanzia kusuguliwa miguu. Kwa mara ya kwanza Emelda akatengenezwa kucha zote,
tena kitaalamu. Nywele akabanwa vizuri ndipo safari ya manunuzi ikaanza. Jelini
mpenda vizuri. Kumwaga pesa kwenye kitu atakacho si mbahili. Emelda akawa
mpole.
Akiona kitu ni garama
sana, anamwambia atalipia yeye. “Nina hela Jelini, ila nazibania.” “Basi acha
mimi nilipie. Mimi sitaki uvae matambaa ya ajabu ajabu halafu tunatokea mahali
sisi wote wanne, wewe uonekane tofauti! Hivyo sitajisikia vizuri.”
Emelda akacheka. “Mwenzio ninapenda vitu vizuri. Bora nisinunue kitu kizuri
kama sijafika bei, mpaka niikusanye hiyo pesa, ndio nikanunue kuliko kununua tu
kitu bora.” Ikabidi Emelda ajiachie. Ukweli alimfaa. Akamnunulia vitu kuanzia
anaamka asubuhi mpaka anakwenda kulala.
“Na ubadili harufu
yako. Inamaana kuanzia sabuni unayoogea mpaka kitu unachopaka mwilini mwako.
Kwanza una rangi nzuri sana.” Hapo napo akawekeza ndipo akamrudisha nyumbani
akiwa mpaka na masanduku ya maana ya safari. Ndipo na yeye akarudi kazini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa kina Junior
wao wakashugulikia ruhusa, wakapata bila shida. Wakapanga kuondoka kesho yake.
Siku ya jumanne. Maandalizi yakaanza. Wakiwa ofisini wanatuma watu wawafanyie
hiki na kile ilimradi kukamilisha hiyo safari kwa haraka. Watoto hao wa
mchungaji safari za kwenda kuhubiri mbalimbali walishazoea. Walishajua njiani
wawe wana beba nini chamuhimu cha kuwafaa njiani na huko waendako. Basi
maandalizi yakaendelea na kutaarifu wazazi pamoja na Jelini na Emelda kuwa saa
9 alfajiri ya siku ya jumanne, wanaondoka jijini kwenda Songea.
~~~~~~~~~~~~~~~
Jelini yeye
alishazoea safari kama hizo wakiwa wanakwenda kwa bibi yao, migombani. Maisha yalipowabadilikia
ndipo wakaanza kwenda na gari yao. Lakini walikuwa wakipanda mabasi tu. Kwa
hiyo alijua ni nini kinahitajika kwenye gari wakiwa njiani. Akawasiliana na
Ezra ili wasirudie kununua vitu. “Mito, mablangeti mepesi ya kujifunikia kwenye
gari, maji na vitu vidogovidogo vya kula na kunywa, hivyo niachieni mimi. Najua
kuviandaa na ninavifaa vya kutunzia.” Huo ukawa msaada mkubwa kwao.
~~~~~~~~~~~~~~~
Sasa ikawa furaha yakupitiliza
kwa Emelda aliyezoea mabasi akienda kwao tena peke yake. Safari hii anarudi na
Junior! Tena wanakwenda kumchukua mama yake na mdogo wake! Halafu anasindikizwa
na watu wa maana, na yeye anarudi kitajiri! Siku hiyo alifanya kila kitu hapo
ndani. Mpaka kupitiliza. Alikuwa na nguvu ya ajabu.
Watu wanatoka
makazini na Junior kufika hapo, alishaivisha kila kitu mpaka vitafunwa vya siku
inayofuata. Nyumba ni safi, amemuachia mama Leti vyombo watakavyolia usiku huo
tu kuja kusafisha kesho yake. Lakini mpaka nguo alishafua.
“Na wewe upate wa kukutunza hivihivi Emelda
binti yangu.” Maneno ya mama mchungaji kwa Emelda kila wakati. “Amina mama.
Mwenzio napokea halafu natunza kwenye hazina yangu.” Ndio majibu yake Emelda.
Japokuwa habari ilishabadilika, ni mkwe, tena wa Junior, mama mjengo!
Yeye hakubadilika. Akaongeza juhudi akijua hapo ndipo atafikia mama
yake.
Safari ya
Songea.
Saa 9 alfajiri wakawa
getini kwa kina Jelini, wote watatu wakimsubiria kwenye gari. Akatoka na mama
yake. Wote wakashuka garini kumsalimia. “Naombeni taratibu na umakini huko
barabarani jamani. Mrudi kama mnavyoondoka hapa.” Mama Jema akasihi. Wakaomba
wote watano, ndipo safari ikaanza.
Waliamua kuchukua
njia fupi ya masaa 10 na dakika kama 40 hivi kama wangeendesha moja kwa moja
bila kupumzika. Wakitokea hapo Dar, kupitia Lindi, Tunduru mpaka Songea. Ezra
alikaa nyuma na Jelini ili amlalie alale, Junior dereva, Emelda akakaa kiti cha
mbele pembeni ya Junior. Akampa na yeye mto wake na blangeti, kisha akauweka
mto mwisho kabisa ya alikokaa Ezra, akamlalia kwa kukumbatia. Ezra alikuwa
akisikia raha vile alivyomshika, kama Jelini mwenyewe.
Alimkumbatia vizuri,
uzalendo ukawashinda. Wakaanza kunyonyana bila kupumzika kama wenye uchu
na kusahau kama kuna watu mle ndani. Na kigiza kikawasadia faragha. Ezra
alimkumbatia kwa furaha zote, na hivi ni Jelini wa mikono! Akawekeka vizuri kissing ikaendelea kwa kujinafasi.
Waliposikia Junior ameongeza
sauti ya redio, wote wakacheka na kuacha. “Mnatunyanyasa kihisia!” Emelda
alicheka mpaka akajifunika. “Mwaya Junior sijui yukoje!” Ezra hana mbavu. “Wewe
si umesema unausingizi sana. Mbona hulali?” Junior akamuuliza nakufanya
wazidi kucheka. Utani ukaanza. Stori. Jelini maneno mengi usingizi ukapaa.
Akaanza.
“Mwenzio sasa hivi
nina mchumba, Junior.” “Hongera sana.” “Mwaya Junior! Sasa wewe unamjua mchumba
wangu?” “Basi mama. Acha tuanze upya. Una mchumba Jelini?” Ezra na Emelda
hawana mbavu. “Ninaye mchumba, tena sio mchumba wa siri. Sasahivi kila mtu
anajua nimechumbiwa.” “Eeeh?” “Kabisa. Tena mashoga zangu wameniambia kama ni
karata, mie nimelamba dume.”
Walicheka. Walicheka sana.
“Bwana mashoga wa
Jelini!” Emelda akaongeza. “Wale wote mitambo.
Tena pale jana niliwasihi watulie, kwa kuwaambia pale nyumbani kwa mchungaji. Hakuna
fujo. Maanti zangu wa mjini wale. Wananipenda sana. Pale walikuja kumuona huyo
mchumba wangu mimi.” “Wakakusifia?” Junior akaendelea kuuliza akimchokoza.
“Kwanza wanasema mchumba
wangu hajawahi kuingia kwenye anga
zao wote wale, inamaana kweli ametulia.” Ezra akawa hajaelewa. “Yaani
wale sehemu zote za dhambi hapa jijini, wapo.” Walicheka mpaka kuchoka.
“Huna jengo la starehe wale ukawakosa. Kwa hiyo wakisema hujaingia kwenye rada zao, inamaana hata nyumba za
kulala wageni hamjawahi kupishana. Mziki, baa, popote kunakohusu ya siri, hawajakuona mpenzi wangu. Halafu
sasa wakasema wewe dume la nguvu.
Muulizeni Emelda alikaa nao jana, alikuwa na kazi ya kucheka tu akiwashangaa.”
“Wamesema watamfanyia
Jelini kitchen party ya nguvu, mpaka
mji mzima wajue Jelini katoka sokoni, wasimsumbue, ili church boy asife
kwa pressure.” “Mimi ndio church boy?” Ezra akamuuliza Emelda. Hawana
mbavu. “Ndivyo wanavyokuita kwa sababu hawakuoni mtaani.” Wakamsikia akiaanza
kucheka tena kama aliyekumbuka kitu.
“Nini sasa?” Junior
akamuuliza. “Yaani siimpatii picha hiyo kitchen
party yao! Mama mchungaji sithubutu kumualika.” “Kwa nini!?” Wote
wakauliza kwa pamoja. “Hakika hamtaki kujua. Wale! Nikiwaambia ni mitambo, ni
mitambo ya bangi. Nitashindwa kuja kumuangalia mama mchungaji usoni baada ya
kiyo kitchen party yao. Wataniharibia mahusiano bure na mama mkwe. Bora
hiyo iwe ya wao tu.” “Na mimi nataka Jelini jamani! Mbona unaanza kunitenga?”
Emelda akalalamika.
“Emelda naye! Sasa
harusi yetu si ni moja! Umesikia hawa mabwana harusi washasema tunasimamiana,
kila kitu kimoja. Sasa siku hiyo nikiwa bibi harusi si na wewe ni bibi harusi?”
“Subiri kwanza Jelini? Kwamba utamkaribisha na yeye?” Junior akauliza. “We
Emelda, si ulinisikia nikiwaambia jana kuwa sisi ni wake wa twins, wanafanya kila kitu pamoja?”
“Labda ndio kipindi mama aliniita. Mimi sijasikia.” “Wewe wangu Emelda wala
usijali. Nitakachofanyiwa mimi, ujue na wewe utafanyiwa. Na mama pamoja na Jema
nishawaambia.” Kidogo wakaingiwa wasiwasi hao wanaume wawili.
“Wao wamechukuliaje?”
Ezra akauliza. “Mimi nilivyowasoma ni kama walitegemea eti! Hawakushangaa.
Walichosema ni kama mimi. Wanahisi itapendeza sana. Bado hawajaipatia picha
vizuri. Ila ujue Emelda tutafanyiwa kitchen
party mbili. Ya kanisani,
na hiyo ya mtaani ambayo wataisimamia maanti zangu. Hiyo mama mchungaji
na wale marafiki zake wa staarabu, hiyo hapana.”
“Ila nashauri msimnyime
moja kwa moja. Mwambieni kwanza. Naweza pata picha aina ya kitchen party unayozungumzia Jelini. Mama ameishi uswahilini au
tumeishi huko kwa muda mrefu sana. Ana aina hiyo ya marafiki, hawaendani na wa
pale kanisani kabisa. Na hajaachana nao. Maana huwa anahudhuria mambo yao mpaka
sasa.” “Anajua kucheza taarabu yule!” Ezra aliongeza nakufanya wacheke sana.
“Haiwezekani!”
“Utamsikia akitoka kwenye hizo shuguli zao. Ataimba na kucheza taarabu, baba
anamuangalia, anamwambia anamkumbusha mbali.” “Basi kama ndio hivyo, yale mambo
mengine atakua anayajua pia. Jema atazungumza naye tuone atasemaje.” Stori
zikaendelea.
Mrejesho Wa Edwin.
“Halafu wewe Emelda
nimesahau kukuuliza. Mbona jana tumekaa wote kwenye ibada nzima hukwenda kwa
watoto? Ujue Jeremy anakupenda! Amemwambia bibi yake kama wewe utamfundisha
kule kanisani, anarudi kwenye madarasa ya watoto.” Junior akamwangalia. “Kwamba
jana ulikuwepo ibadani hukurudi kwa watoto?!” “Sikurudi.” Akawa kama amemaliza.
“Mwaya Emelda!”
Jelini akalalamika na kufanya wacheke. “Ongea bwana! Sasa hivyo ndio jibu gani
hilo?!” “Mwenzio sikutaka kuyaanzisha hayo mazungumzo mpaka turudi Dar. Na hivi
Junior ndio dereva, nilikuwa nataka tuzungumze tukirudi, tena akiwa ametulia.”
“Basi mimi siwezi kusubiria tena. Bora tu utusimulie.” “Mimi mwenyewe nataka
kujua sasahivi. Siwezi kusubiri kama
hivyo Jelini.” Junior akaongeza.
“Jana kulikuwa na
hekaheka nyingi pale kanisani na nyumbani ndio maana sikukwambia kwa urefu,
Junior. Lakini Edwin hakuchukulia zile taarifa vizuri.” Wote wakakaa
sawa. “Ilikuaje!? Na uanzie mwanzo, Emelda. Maana nishakuona unapenda kufupisha
stori.” Jelini akafanya wote wacheke. “Jelini!” “Ni Emelda huyo! Anzia kuanzia
unaanza mazungumzo mpaka mwisho.” Emelda akafikiria akaona awaambie tu bila ya
kuwaficha.
“Niliwahi kama
kawaida. Nikamuomba tuzungumze. Nikamwambia moja kwa moja kuwa, jana yake, siku
ya jumamosi, nimegundua dada Ester hakurudisha jibu sahihi la ujumbe
aliomtuma.” “Emelda bwana! Mstaarabu mwenyewe! Ehe?” Walicheka sana. “Sasa wewe
ungesemaje?” “Mimi wala nisingemzungusha hivyo. Ningemwambia tu mimi sikutaki.”
Walicheka mle ndani, mpaka basi.
“Endelea sasa Emelda
bwana!” “Nikamwambia mimi nilimjibu dada Ester siku ileile aliponiambia, kuwa
‘hapana’. Kwa kuwa mimi namuona yeye kama mtumishi
mwenzangu tu. Tunaweza fanya kazi vizuri pale kanisani, lakini si kwenye
maswala mengine. Alibadilika! Sijawahi muona Edwin hivyo! Akawa kama
analalamika ila kwa hasira. Na katika moja ya malalamishi yake alisema yeye
anajiona ni kama amekuwa akitumiwa vibaya, ila hajui ni kwa maslahi
ya nani.” “Kivipi!?”
“Sikumuuliza kwa kuwa
nilikuwa na jibu tayari, na sikutaka tuende huko maana Junior alishanikataza.
Kwa hiyo nikamuacha ili azungumze, nimsikie.
Ila akamalizia kwa kusema yeye hawezi tena kufanya kazi na mimi.” Wote
wakashangaa.
“Haiwezekani Emelda!”
“Kweli tena Junior. Kwa hiyo akasema kama mchungaji anavyosema ile si
huduma ya mtu mmoja. Wote tupo shambani kama watenda kazi, basi nichague. Kama
nataka kubaki, yeye aondoke, au yeye abaki mimi niondoke.”
“Haiwezekani!” Na Ezra naye akahamaki kama mwenzie. Emelda akacheka na
kuendelea.
“Sasa yeye ndio
kiongozi wa ile huduma pale. Anaandaa kila masomo na kupanga nani awe wapi.
Nikaona bora mimi ndio niondoke. Lakini najua ananihitaji sana pale. Sio watu
wengi wanapenda kuwepo pale zaidi muda wa ibada. Kila mtu anataka kuwa ibadani.
Na mara nyingi sana tunaweza jikuta tumebakia sisi wawili tu au watatu. Ila
nimemwambia akinihitaji tena, anijulishe, mimi sina shida ya kufanya naye kazi.”
Akashangaa Junior ametulia kimya.
Akamwangalia kama
anayetaka kujua anafikiria nini. Wote kimya. “Ndio hivyo.” Akawa kama
anayemwambia Junior. “Mimi naona tufanye kama alivyotushauri Ezra. Vita zingine
ni za kunyamaza tu. Nyamaza tu tuone mwisho wake.” “Mmmh!” Junior akamwangalia
na kumuuliza. “Nini?” “Eti mimi nakuhisi
kama umefurahia vile!” Yeye na Ezra wakacheka kwa pamoja, Emelda akapata jibu
lake.
“Nilijua tu. Lakini
nyinyi sio watu wazuri jamani! Ile huduma inahitaji watu.” “Debe limevuja,
nafuu kwa mchukuzi. Mwache. Ila nitaanza kuifuatilia kwa karibu, tukiona
analemewa, tutatangaza pale kanisani kwa anayeweza kujitolea.” Stori
zikaendelea, wakiendelea kukanyaga mafuta.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakasimama kwenye
mida ya saa nne asubuhi, sehemu kupata kifungua kinywa. Wakawa wamejawa furaha
muda wao hao wanne wa pamoja. Wakala vizuri, Jelini alipomaliza, akasema ndio
muda usingizi umemlemea. Ilikuwa Ezra ampokee mwenzie kuendesha, lakini ikabidi
tena akae naye nyuma ili alale. Na ile shibe, kukumbatiwa na kufunikwa vizuri,
akalala kama katoto kachanga.
Zilipendwa!
Alilala mpaka simu
yake ilipozidi kuita kwenye pochi yake. Ezra akamsaidia kuvuta pochi. “Naomba
nitolee tafadhali.” Akaitoa Jelini akiwa amemlalia bado ana usingizi. Ezra
akaitizama ilikuwa namba tu haina jina. Akamkabidhi, Jelini akiwa bado na
usingizi. “Huyu sijui nani!” Akaipokea akiwa bado amejilaza hapo kwa Ezra,
amekumbatiwa kama katoto na kujifunika mpaka kichwani.
“Jelini!” Jelini alishituka,
hakutegemea kabisa. “Colins!?” “Nimekuamsha nini?”
“Nilikuwa nimelala.” “Pole na samahani sana. Sikutaka kukusumbua.” “Hamna
shida. Unaendeleaje? Ulipona?” Mapigo ya Ezra yalishabadilika. Mwili
ulishakufa ganzi.
“Namshukuru
Mungu nimepata nafuu kubwa sana. Kwa asilimia 85 ni kama nimepona. Asante
kwako. Nakushukuru Jelini. Bila wewe nisingetoka kwenye ile hali.” “Usijali.
Hata kama isingekuwa mimi, Mungu angekutumia tu mtu mwingine Colins.”
“Alishawatuma wengi tu lakini wakanipuuza. Wazazi hawakuwa wakijua kitu
chakufanya na mimi, mpaka ulipokuja wewe. Ulichokifanya kwangu ni deni ambalo
najua sitaweza kukulipa daima. Nashukuru. Asante.” “Karibu.” Jelini akajibu
lakini alishaanza kuingiwa na hofu kila akifikiria mazingira aliyopo.
Inamaana Ezra
anasikiliza na Junior pia. Hofu. “Jelini!” “Bado nipo.”
Akaitika. “Nina kitu nataka kukwambia. Tafadhali naomba
tukutane.” “Mimi sitaweza Colins.” “Sitatulia mpaka unisikilize.” “Wewe unataka
kunitia matatizoni Colins. Mimi hivyo sitaki. Mwenzio sasahivi nimechumbiwa.
Sitaki tena yale maisha ya kumangamanga kama uliyonikuta nayo na kuniacha nayo.
Mimi sitaki.”
“Kwa nini
unakataa wito, na hujui ninachokuitia!?” “Haki wewe unataka kuniponza Colins.”
“Sio nia yangu. Tafadhali nisikilize. Nisikilize tu.” “Basi ongea hapa
sasahivi, mimi nakusikiliza.” “Jelini!?” “Mimi najijua mimi na wewe Colins.
Hakuna cha maana kitatokea kati yetu, hata nikikupa nafasi ingine, zaidi ya
kuniponza mwenzio, niachike huku na sitapata mimi mwanaume kama Ezra. Unataka
kuniponza tu.”
“Kwani yeye
huyo Ezra hazungumzi na watu wengine?” “Anazungumza nao, lakini sio kama hivi mimi
na wewe. Hata kama ingekuwa mimi nisingekubali.” “Unajuaje?” “Basi kwa juhudi
hiyohiyo uliyohangaika mpaka ukapata namba yangu hii mpya, fanya hivyohivyo kwa
Ezra. Tafuta namba yake, kisha mwambie unachoniambia sasahivi. Ezra akikubali,
mimi nitakuona. Sitaonana na wewe bila baraka zake. Usitake kuniponza. Na kwa
heri.”
Kabla hajakata akamuwahi.
“Jelini!
Jelini!” “Ni nini Colins!? Mbona mimi unanifanyia hivyo wakati wewe nilikuacha
ukaishi na Love bila kuwaingilia? Sijawahi kukufuata ofisini wala kwenu.
Nilikuacha tu nikabaki nikikusubiria kama mjinga vile! Sasa sasahivi mbona
unanifanyia fujo?!” “Sifanyi fujo Jelini. Nataka unisikilize. Si unisikilize
tu?” “Nakusikiliza ongea sasahivi lakini si sehemu ya faragha mimi na wewe.
Hapana, Colins. Hilo halitatokea. Kwanza najua unachotaka kuniambia.”
“Ni nini?”
“Unataka kuja kunipa sababu zako kama ulivyozoea kunipa sababu ya kwa nini ulipotea.
Utasema ni Love na wengine kibao ndio wamekusababishia, na sio wewe.” “Kwa nini
unaniwekea maneno mdomoni?” “Wewe bisha kama sicho unachonitafutia Colins.”
“Hayo ni maneno yako wewe.” “Umeona? Basi kwa taarifa yako, nilishakutafutia sababu
zote. Na zote nilikuwa nazo na misamaha yake. Nilikuwa nikisubiri
tu urudi, nikusikilize halafu nikwambie nimekusamehe tuendelee na ule
mchezo wetu wa kuzungushana bila la maana.”
“Nimekaa
muda wote kama mjinga, nikikusubiria wewe, huku Love akisambaza picha zenu kwa
kila anakojua nitaona, akisaidiwa na Kemi ili tu kuniumiza.
Ulikuwa mzima tena nyingine ukiwa unaenda kazini kabisa. Nyingine mpo na
familia zenu zote mbili. Yaani yako na wazazi wa Love. Mpo kwenye wakati
tofauti tofauti wafuraha tu. Yote hayo alikuwa akisambaza kuonyesha mnafuraha na mnabaraka
za pande zote mbili. Nyingine mpo na Love na marafiki zenu huko kwenye nyumba
yenu Kigamboni na picha nyingine nyingi tu.”
“Na bado
nilikuwa nikikusubiria mpaka Mungu akanihurumia. Nilikuwa silali bila dawa za
usingizi. Sasa hivi unataka kunirudisha kwenye yale maisha, wakati Mungu
amenitoa huko kwa upendo. Sitaki tena Colins. Kama msamaha, nilishakusamehe.
Wala huna haja yakunitafuta na kujieleza.”
“Huo ni
upande wake Love. Na alifanya kusudi kunikomoa mimi akijua hata nikirudi kama
hivi, utakuwa na hasira na mimi kama hivi, utakataa hata kunisikiliza. Kwani
utapungua wapi ukinipa muda mfupi tu kunisikiliza?” “Wewe ni shahidi. Tulikuwa
na muda wote ulimwenguni. Hapakuwa na Ezra wala yeyote kutoka upande wangu aliyekuzuia
kuwa na mimi. Ukabaki ukicheza na hisia zangu. Sasahivi na mimi nimepata mtu
anayenipenda na kunithamini. Mtu wa maneno yake. Ezra ni mtu mzuri sana.
Unataka kumtibua, anione mimi sio mtu wakutulia, aniache.”
“Mwanzoni
umesema huna jinsi ya kunilipa. Basi mimi nakupa jinsi ya kunilipa Colins. Uniache
kabisa, hayo ndio yatakuwa malipo yako kwangu.” “Usinichangulie jinsi ya
kukulipa Jelini. Bado nafikiria jinsi yangu ya kukulipa. Na nia yangu sio
kukuchanganya. Nakusihi nipe nafasi unisikilize.” “Sitaki. Na ingekuwa mtu
mwingine, hii simu ningeitupa sasahivi, lakini najua hata nikinunua simu ingine
na namba mpya, utanipata tu. Mimi nakuacha Colins, na wewe naomba niache.”
“Unajua siwezi.”
Colins akaongea bila ya kumumunya maneno, tenana uhakika.
“Basi
mtafute Ezra, uzungumze naye. Mimi usinipigie tena.” “Siwezi kuruhusu Ezra awe
katikati yetu, Jelini. Alitukuta mimi na wewe. Halafu eti mimi ndio nimuombe
yeye ruhusa ya kuzungumza na wewe! Hata kidogo. Kama yeye ni
muungwana ataelewa tu. Alikupata kwa sababu mimi nilikuwa matatizoni. Lakini si
vinginevyo. Na yeye anajua hilo na wewe ni shahidi. Ulinikuta kwenye hali mbaya
nikiwa sina ufahamu wangu. Ulitaka nifanyaje na wewe uliambiwa ukweli wote,
Jelini? Walinitoa kwangu nikiwa sina akili zangu. Baada ya hapo yote nimefanya
yapo kama ndoto tu kwenye kumbukumbu zangu. Sikumbuki hata maisha niliyoishi na
Love huko Kigamboni. Na wewe ni shahidi yangu. Umeambiwa na kunitoa kwenye ile
hali. Kweli ndio unataka kuniadhibu mimi kwa makosa ya watu wengine? Ulitaka
mimi nifanyaje kwenye hali kama ile?" Akauliza na kuendelea bila ya kusubiri
jibu.
"Naandaa
mazingira mazuri tutakayoweza kutulia na kuzungumza vizuri kwa utulivu bila
muingiliano wowote.” Jelini akakata. Na kuanza kulia kwa hofu
akimkumbuka Colins aliyemudu kumfuata mpaka Kasa, akajua wazi Ezra mstaarabu
atasumbua tu. Kimya gari zima kikisikika kilio chake AKIFIKIRIA hayo mazingira
anayaandaa wapi na vipi! Safari hii atafanyaje! Colins hajui jibu la hapana.
Hayo yote yakamtia wasiwasi Jelini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Asilimia 85 za kupona kwa Colins zimemtosha kurudi kwa Jelini.
Na amemuhakikishia hawezi kumuacha &
anaandaa mazingira mazuri ya kukutana naye tena.
Kwa njia gani ikiwa Jelini amemkatalia Waziwazi?
Nini kitaendelea?
USIPITWE.
0 Comments:
Post a Comment