“Nyamaza nikwambie kitu, Jelini. Usilie.” “Mimi nilijua tu! Yaani jambo zuri tu likitaka kutokea
kwangu lazima kuna kitu kinajitokeza! Sijui ni mkosi gani! Na mimi namjua
Colins. Hivi amepona! Atasumbua tu.” “Usilie. Nisikilize.” Junior
akazidi kumtuliza, Ezra kimya.
“Mimi nimekusikiliza
mazungumzo yako.” “Hujamsikia yeye! Colins hajuagi
jibu la hapana, Junior. Huu usumbufu
wala sio wa leo tu. Kila mtu anatujua mimi na Colins. Na usifikiri kuna
muendelezo! Huwa tunaishia hivyohivyo kila siku. Anachotaka ni kuniponza tu.
Anitoe kwenye pumziko, tuanze tena hekaheka zetu.” “Usimruhusu. Wala
usilegeze kamba. Hivyo ulivyoamua, simamia hapohapo, baada ya muda ataelewa na
kuheshimu maamuzi yako akijua safari hii umeamua kutulia. Unanisikia?”
“Sasa
akipiga tena? Na tena?”
“Mimi nitazungumza naye.” Ezra akadakia, na kumfanya Jelini akae kwa haraka. “Kweli Ezra?!” “Sibahatishi mimi Jelini. Nimeamua
kuwa na wewe, hatanitisha kijinga hivi. Na wala sitakuacha kwa ajili yake.
Mbona nilikutongoza nikijua yupo na nikama hakuwa ameondoka moja kwa moja kwenye
picha!” Jelini akakunja uso.
“Mimi nakufuata Jelini.
Nakufahamu vizuri sana. Nilishakuwa na habari zenu zote tena kamili. Najua
tabia yake, najua jinsi mlivyokuwa karibu. Najua Jelini. Wala usiogope, pengine
iwe tu kama umeamua kurudiana naye.” “Hata nikikuacha wewe sasahivi, nikisema
namrudia. Nakuhakikishia kwa asilimia 100, ukija kunitafuta baada ya miaka hata
miwili baadaye, utanikuta na historia hiihii Ezra. Mimi mwenzio kilio changu,
hata yeye Collins nilimwambia, nataka mwanaume kama hivyo wewe.”
“Uliyetulia, wangu wa
peke yangu.” Junior akacheka. “Usicheke bwana Junior!” “Wewe tulia, wala
usipaniki.” “Lazima Junior. Mimi nitampata wapi mwanaume kama Ezra, kama sio
anataka aniponze mwenzie!” “Usiwe na wasiwasi. Na mimi nakuhitaji Jelini.
Siwezi kukuacha kirahisi hivyo.” Junior na Emelda wakaanza kusikia kissing
hapo nyuma.
“Haya, Ezra. Naona
usingizi wa Jelini umeisha, zamu yenu kukaa hapa mbele.” Walicheka sana. Mpaka
Emelda aliyekuwa ametulia akacheka. “Maana nyinyi hamtamaliza. Naegesha gari,
muhamie mbele, na sisi tupumzike.” “Mwaya Junior! Sasa si nilikuwa nimeshituka
ndio natulia taratibu?” “Wewe hutamaliza Jelini. Na hivyo umekumbatiwa hapo!
Tutafika mpaka Songea bado hujatulia, unataka ubembelezwe tu. Njooni mbele.”
Junior akatafuta sehemu nzuri, akaegesha, na kutoka kabisa garini.
“Wala zamu yangu ya
kulala ilikuwa haijaisha, nikaamshwa!” Jelini akawa analalamika huku akihamia
mbele. “Usijali. Utalala vizuri hotelini.” Emelda na Ezra wao hawana mbavu.
“Junior saa zingine anakuwa upande wangu, saa zingine nakua simuelewi!” “Wewe
wangu Jelini. Upande uliopo ndipo nilipo.” “Mmmmh!” Akaguna, safari ikaendelea.
Emelda na yeye ikawa zamu yake. Ila aibu!
Mwanga nje japo vioo vyote vya gari vilikuwa vyeusi kasoro cha mbele ya gari.
“Njoo upumzike hapa.”
“Na wewe umechoka.” Emelda akamjibu kwa kunong’ona wasisikike. Junior akavuta
mto na kuuweka kama Ezra, utafikiri aliona! “Lala hapa.” Akapigapiga mto.
Emelda naye akajinyoosha kwenye kiti hicho cha nyuma na kumlalia. “Unanukia
vizuri! Umebadili harufu kabisa!” Jelini akafurahia kuona Junior ametambua, ila
akanyamaza kimya ili Emelda mwenyewe apate sifa kwa mpenzi wake.
“Jelini
alinisindikiza. Nikanunua aina hii ya lotion, shower gel yake na body spray.
Ila garama!” “Naona garama yake inaendana na harufu. Nzuri sana na imetulia.
Nimependa. Asante Jelini.” “Mpenzi wako ndio mchaguzi mzuri. Amechagua
mwenyewe, wala sio mimi.” “Naona hii ndio itabakia kuwa harufu yako.
Nimependa.” “Asante.” Akaanza kumchezea vinyweleo vya nywele chini ya shingo
alipokuwa amejilaza, pembeni ya sikio lililokuwa juu. Taratibu bila papara
Emelda alikuwa akisikia raha! Akajiweka vizuri na kuanza kusinzia.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kukatulia kwa muda
kuwapa nafasi na wao walale. Kama kawaida ya Jelini kunyamaza muda mrefu
hawezi. Akaanza. “Ujue Colins atarudi tena?” “Nafahamu.” Ezra akajibu bila
wasiwasi. Jelini akamwangalia vizuri. “Namaanisha hatatulia mpaka apate
anachokitaka. Hajui jibu la hapana.” “Nafahamu. Ila safari hii itabidi akubaliane
na jibu la ‘hapana’. Hata kama kwake ni msamiati mgumu, ataumeza
hivyohivyo. Nilijua angerudi, ila sikujua ni lini, kwa sababu niliambiwa bado
anajiuguza.” Jelini akashangaa sana.
“Naijua historia yako
na yake vizuri tu. Najua jinsi linapofika swala lako vile alivyo. Jasiri.
Na hana umbali ambao ataogopa kufika ili kukufikia. Najua.” Jelini akazidi
kushangaa.
“Ezra!” “Mimi nilitaka ukiri wako tu na kujua
msimamo wako. Maadamu umeamua kubaki na mimi. Tena sio kwa kulazimish…” Kisha
akasita. Akawa kama amegutuka kitu.
“Au umelazimishwa
kuwa na mimi?” “Hapana Ezra! Mimi nakupenda wewe. Na nakutaka wewe. Nataka
tubaki wote.” Jelini akaongea kwa upendo. “Nimehangaika! Hivi ndio kwa mara ya
kwanza, nimetulia na kufanya jambo la kueleweka likaonekana. Inamaana hata hilo
najua, unajua.” Akawa kama anamuuliza.
“Najua Jelini.”
“Umenipenda nilivyo Ezra. Kwenu sijifichi wala sijibaraguzi. Wazazi wako
wananipenda. Haya, Junior ananipenda na kuniheshimu. Sijapata hiyo hali kwa
yeyote! Kila mahali nilipokuwa na mahusiano, nimepambana na changamoto.
Kwengine mpaka kutishiwa kifo, ilimradi tu mahusiano yamekuwa na vipingamizi.
Ila sio kwako Ezra. Nimeamua kutulia na wewe.” “Unamaanisha kwa Kasa?”
Hilo lilimshitua Jelini, akashindwa hata kumtizama. Akanyamaza kimya.
“Ninapokwambia
nakufahamu Jelini, si kwa kubahatisha. Nakufahamu. Ndio maana nilipokusogelea
mara ya kwanza, ukaonekana hunitaki. Nilikuacha kabisa.” Jelini akaanza kulia
tena. “Uliniacha Ezra, wakati mwenzio nilikuwa
matatizoni.” Akawa kama analaumu. “Ukawa
unanipuuza kabisa.” “Kwa sababu nakupenda kwa dhati na nilikuwa nina
mpango na wewe wa muda mrefu, mpaka uzee wetu kama si kifo. Si kucheza na hisia
zako tu na kukuacha katikati, Jelini. Nakuhakikishia kipindi kile, kama
ningeendelea kukufuatilia, ungenichukia kabisa. Muulize Junior, hata
yeye nilimwambia. Ningegeuka kero kwako, na ningekupoteza kabisa.”
“Hapana
Ezra.”
“Jelini! Nakwambia ukweli. Kwa sababu hata wewe mwenyewe umetoka kukiri kwa
Colins. Ulikuwa na sababu zote ulizomtengenezea na bado ulikuwa na msamaha
wake mkononi. Ukimsubiria. Hata mimi mwanzoni uliniambia kabisa.
Hukutaka kujichanganya, ili akirudi asije kukuta na mtu. Si ni kweli?”
Akanyamaza.
“Hukuwa tayari si
kwangu tu, kwa mwanaume yeyote yule. Na najua umezoea kufuatwa na wanaume. Kila
mmoja akikwambia maneno yanayofanana. Nilikupa muda kwanza ukamilishe swala la
Colins wewe mwenyewe bila kuingiliwa. Kisha pia nilitaka kukupa
nafasi unifahamu. Kwa sababu nilijua kwako nilikuwa mgeni. Ungenikubali tokea
mwanzo, nilitegemea ungenifahamu tukiwa kwenye mahusiano ya mwanzoni.
Nisingeharakisha kukuchumbia kama hivi, mpaka uwe na uhakika na mimi. Lakini
uliponikataa, nikaa..” “Sikukukataa Ezra!” Jelini akakanusha kwa upole.
“Basi niseme
ulivyoanza kunikwepa. Au hapo pia si sawa?” “Nilikuwa kwenye wakati mgumu!”
“Basi kwa mimi kulitambua hilo, nikaamua kukuacha. Huoni mara ya pili
ilivyokuwa rahisi?” “Sasa mimi nina uhakika inakuja na ya tatu ndio
maana nina wasiwasi Ezra! Namfahamu Colins. Walisumbuana sana na Kasa.
Sitaki akutibue. Halafu ukanipa tena muda kama ulivyofanya ile mara ya kwanza.”
“Siwezi, kwa kuwa
sasahivi nimeshajua umeamua kutulia na mimi. Hiyo inanipa ujasiri. Na wewe wala
usipaniki. Ushauri niliompa Emelda ndio na wewe nakupa. Shetani ni ‘kama’
simba aungurumaye. Ni kelele tu. Akishaona haupaniki. Huogopi.
Umemaanisha. Na yeye atatulia. Sasahivi anachotaka kukwambia ni yupo.
Amerudi. Anakuhitaji. Lakini wewe ukimuonyesha uliposimama ni sahihi, na
hutatetereka, unamaanisha, yeye mwenyewe atachoka. Kwa hiyo
usiogope wala usipaniki. Hata akikupigia tena, tulia kabisa.”
“Unauhakika? Maana mimi
namjua Colins. Anajua kukazania jambo na ananjia zake hizo! Kama una roho ndogo
hutamuweza. Baada ya Kasa kama kutoka kwenye picha, akahamisha
usumbufu wake. Alikuwa akiwasumbua kina Jema na shem! Mchana, alfajiri na
usiku, hakuna kuhema. Hata na kwa huyo Kasa kwenyewe napo ni kama akawa
hajaridhika. Mara amvamie usiku kwa hili na lile. Na ukumbuke Kasa ni wale
Mafia, wanao ogopewa haswa na kulindwa kama raisi wa nchi.
Lakini haikuwahi kumtisha Colins.”
“Alikuwa asiponiona
au nisipopokea simu zake, anavamia kwa Kasa hata usiku mwingi tu, na
hapo hataondoka mpaka aamshiwe Kasa mwenyewe, kitu ambacho si cha
kawaida hata walinzi wake walikuwa wakiogopa. Lakini yeye alitafuta njia
yake yakuwa akiamshiwa huyo Kasa. Sasa angalau kwa Kasa alikuwa amkimmudu. Kasa
ni mkorofi na katili haswa. Watalumbana wakitishana kwa hili na lile mpaka
aridhike Kasa hajanisikia kwa muda wote huo ndio anaondoka. Ndio maana
nakuhofia wewe.”
“Nakupenda Jelini. Na
nimekusudia uwe mke na mama wa watoto wangu. Hakuna umbali na garama nitashindwa
kulipa kwa ajili yako. Kwa kuwa sipo tayari kufika umbali niliofika na wewe na
mwanamke mwingine. Ndio linakuja ombi langu kwako, usije nibadilikia.”
“Wala huna haja ya kuniomba Ezra. Mimi mwenyewe nakutaka. Nikiwa na wewe
nakuwa na furaha mpaka moyo wangu unatulia! Sijawahi kuwa kwenye mahusiano na
mtu, nikatulia hivi. Si kwa Colins wala Kasa, ambaye sijui umeambiwa nini juu
yake!” “Vyakutosha kuelewa kilichokuwa kikiendelea kati yenu.” Jelini akazidi
kunyong’onyea.
Ezra akamtizama vile
alivyopoa. “Nakupenda wewe Ezra, na sidanganyi.” “Na mimi nakupenda Jelini.
Tutulie. Yote hayo yatapita na tutabaki sisi tu, tena salama.” Jelini akavuta
pumzi kwa nguvu na kuzishusha, akajituliza kitini. Safari ikaendelea
akitafakari.
Japokuwa walimuacha
Emelda na maswali mengi, lakini akavutiwa vile Jelini alivyo na ujasiri wa
kueleza hisia zake kwa Ezra. Akarudi kulala baada ya ukimya mwingine huku
akibembelezwa kwa kupapaswa. Akajua hata Junior hakuwa amelala, alikuwa
akisikiliza. Na yeye akampapasa kidogo magotini pale alipokuwa amemlalia. Akitumia
kucha zake alizobandika kama kumbembeleza na yeye, ndipo akapotelea usingizini.
Walisimama mara ingine. Wakajisaidia na kununua chakula. Wakajaza tena mafuta,
Ezra akakanyaga mafuta mpaka walipofika Songea.
Songea.
Bado ilikuwa mapema
tu. Walitafuta hoteli nzuri ya hali ya juu hapo mjini. Wakachukua vyumba
vitatu, vyenye vitanda viwiliviwili. Wakashusha mizigo yao, ndipo wakamtafuta
Mika ambaye alisharudi shuleni. Akawaelekeza alipowaacha Mateo na mama yao.
Ukweli ilikuwa sehemu
duni sana. Nyumba ya kulala wageni iliyopo sehemu duni, lakini sivyo ndugu hao
walivyopaona. Walijawa shukurani, na furaha ya ajabu. Huyo mama alikuwa dhaifu,
mwili usio na nyama kabisa kama ambaye hakuwa akipata mlo wa kutosha. Lakini
wazi alionyesha kujawa na furaha baada ya kumuona Emelda! Kila wakati alikuwa
akimshika popote pale, hata gauni lake! Ilimradi tu kutaka awe naye karibu japo
hakuwa mzungumzaji kabisa. Mkimya zaidi ya Emelda. Ndani ya dakika tano za
salamu na kumjulia hali akawa yeye amemaliza kabisa, macho kwa Emelda muda wote.
Walikuwa wamemletea
dawa za maumivu. Emelda akampa nyama za kuchoma na ndizi walizokuwa wamenunua
njiani pamoja na soda kisha akampa dawa. Mateo alikuwa akila kwa uchu, ungejua vyakula
ni vigeni kwao.
Walikubaliana mlo
mzuri wa pamoja uwe usiku baada yakutoka shuleni kwa Mika. Wakatoka hapo
chumbani kumpisha Jelini na Emelda kumsaidia kumuweka sawa huyo mama. Kwa
sababu ukweli alikuwa na hali mbaya kama alivyohisi Emelda tokea mwanzo. Hata
harufu hapo chumbani haikuwa safi. Wawili hao wakaanza kazi ya kumsafi huyo
mama baada ya kumpa vitu vizuri vya kuogea na Emelda kumuosha mpaka nywele.
Akampaka mama yake mafuta
vizuri mpaka unyayo. Nywele ikawa kazi ya Jelini. Akamfunga vizuri baada ya
kukausha. Kwani alikuwa amesuka mabutu/vitunguu tu. Na Mateo naye alimletea
nguo na viatu. Akamwambia mdogo wake na yeye akaoge tena kwa kujisugua vizuri.
Hakuwa mbishi wote walikuwa wakimsikiliza sana Emelda. Akafanya hayo kwa
haraka. Akabadili angalau akaonekana na afadhali.
Baada ya muda mama
Emelda akatoka nadhifu mpaka Ezra na
Junior wakashangaa. Safi. Na huo ni msasa wa muda mfupi, siku ya kwanza
tu! Inamaana Emelda amerithi ngozi ya shukurani kutoka kwa mama yake. Mavazi
pia waliyokuwa wamemnunulia yalikuwa mazuri na Emelda alimjulia mama yake kwani
alileta vinavyomuenea. Hata sendozi walizokuwa wamemnunulia, nyepesi kutokana
na afya yake, asusumbuke kutembea navyo. Akapendeza.
“Sisi tunapenda vitu vizuri kama hamjui.”
Jelini akajisifia akijua wamevutiwa na mama Emelda. Emelda mwenyewe alijawa
furaha, akawa na kazi ya kucheka tu. Hali waliyomkuta nayo muda mfupi huyo
mama, sio kama hapo. Akawaka.
Songea Boys.
Safari ya shuleni kwa
kina Mika ikaanza wakiwa wamembebea vitu vingi tu na zawadi alizokuwa
amaenunuliwa na dada yake tokea Dar. Walikuta akiwasubiria hata bwaloni
hakwenda kula. Alifurahi sana kumuona Emelda, kama mama yao tu mpaka wote
wakashangaa. Walionekana ni familia duni, lakini wanahitajiana sana. Upendo ule
wadhati.
Ila pia akashangazwa
na hali ya mama yake. “Umeshaanza kupendeza mama!” Akamtania mama yao huku
amemshika dada yake mkono kama asikimbie. “Na Mateo umependeza sana.” “Nimevaa
vitu vipya vyote!” Wakacheka na kuwapisha kwa muda kama kuwapa faragha kama
familia. Wakateta yao ndipo wakaomba pamoja.
“Sisi kesho
tunageuza.” Junior akawa akimuaga Mika. “Sina jinsi ya kukushukuru au
kuwashukuru mkaelewa. Asanteni sana.” “Usijali kabisa.” “Aisee siamini! Kumuona
mama yangu hivyo! Najisikia raha! Asanteni sana.” Akazidi kushukuru huku
akiwasindikiza.
Junior Kwa Shemeji Yake.
Wakati kila mtu
ameingia garini akajifanya amekumbuka kitu. Akamuita na kusogea pembeni. “Sijui
Emelda alikutambulisha vipi juu yangu?” Mika akawa kama hajaelewa vizuri. Ila
akajibu kwa kuuliza. “Wewe si ndio kaka mkubwa kwenye familia anayofanyia kazi!?”
“Ndiyo lakini nimetokea kumpenda Emelda, nataka kumuoa.” Mika akabakia akimwangalia
kama ambaye taarifa imegoma kupenya akilini kwake.
“Niliona nikutaarifu na
wewe, na nitazungumza na mama pia. Lakini nakusudia kumchumbia kwa kumvalisha
pete ya uchumba juma hili. Ilikuwa wazazi waje huku kujitambulisha kwa mama
yenu au kwenu kabla sijamvalisha pete, lakini ndio ikatokea hili.”
Akimaanishana hayo mafuriko na ugonjwa.
“Nakufanya mama
aondoke nyumbani. Lakini lengo lilikuwa ni kumfuata huku mama. Tujitambulishe
na kueleza nia yakutaka kumuoa Emelda kwanza.” “Unamaanisha Emelda huyu dada
yetu!?” “Ndiyo.” Akawa kama haamini kabisa.
“Yeye mwenyewe Emelda
anajua?!” “Kama nampenda?” Akashindwa kujibu hilo. “Nimeshamwambia na hata
swala la kuwa nataka awe mke wangu, anajua ila nimemficha ni lini nitamchumbia.
Nataka kumfanyia kitu kizuri sana. Afurahie siku nitakayo mvisha pete.” “Kwamba
unataka kumfanyia Emelda surprise?!” Alihakikisha anaweka jina la dada
yake kama ambaye anatafuta uhakika kwa Junior. Kujua hapo wanamzungumzia
mtu huyohuyo mmoja ambaye wote wanamfahamu! Akamfanya Junior acheke ila
akakumbuka anazungumza na msomi. Kijana wa kileo. Anaelewa mambo ya surprise.
“Ndiyo. Natamani kama
ungekuwepo na wewe.” “Bado siamini! Nahisi kama sielewi! Unamzungumzia
Emelda huyuhuyu, dada yangu mimi?!” Na kweli alionekana bado yupo kwenye
mshituko. “Ndiyo. Ni Emelda. Simfahamu Emelda mwingine, Mika. Najua dada yako
ni mke Mungu aliyemtunza kwa ajili yangu.” Hapo hakujua aseme nini tena.
Akabaki kimya kama aliyepotea pale kabisa kimawazo. Junior akaona amuache tu. Wao
wakaondoka kurudi kwenye hoteli waliofikia wao. Waliwahamishia hapo kwenye
hoteli yao.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati kila mmoja
ameingia kuoga kutoa uchovu na kujisafi, pamoja na kubadili nguo walizokuwa
wamevaa siku nzima safarini ili wakutane kwa chakula cha usiku. Ezra na Junior
wakiwa chumbani kwao. Emelda na Jelini chumba kingine. Mama Emelda na Mateo
chumba chao. Emelda akakimbilia kuoga yeye wa kwanza na kuvaa kwa haraka,
akatoka kukimbilia chumbani kwa mama yake akimwambia Jelini ampigie akiwa
tayari.
Mtafutaji Asiyechoka.
Jelini anatoka kuoga,
akasikia jumbe zinaingia kwenye moja ya simu yake. Akaangalia ndani ya pochi. Akatoa
ile iliyoonekana ina jumbe. Akafungua. Akakutana na picha zake alizokuwa
akivalishwa pete ya uchumba. Akashituka kidogo na kuangalia namba maana haikuwa
na jina. Mara ujumbe ukaingia.
‘Mimi kwa
akili zangu timamu. Bila kushurutishwa na mtu au kwa mambo ya kuharibiwa akili,
kwa hakika ningekusubiri Jelini. Nisingemvisha pete ya uchumba mwanamke
yeyote yule, hata aweje, isipokuwa WEWE. Na nisingempa mtu yeyote nafasi
yako moyoni mwangu. Kwa sababu moyo wangu utabakia na nafasi yako pekee, daima.
Hapana hata mwanya wakuingiza mwanamke mwingine. Uliwezaje Jelini?!’ Jelini alipigwa
ganzi, akajikuta anakaa kitandani na taulo bichi.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kina Ezra walimaliza kujiandaa,
wakapendeza na kutoka vyumbani kwao kuwasubiria wachumba sehemu ya mapokezi.
Walikubaliana muda. Wakasubiri. Wakamuona Emelda, mama yake na Mateo
wakiwasogelea. “Tumeona hapa wana vyakula vizuri tu. Naona tupate chakula
hapahapa. Itatusaidia pia kuokoa muda. Tupate usingizi mzuri, kesho tuondoke
muda mzuri tukiwa hatujachoka.” Junior akamwambia Emelda. “Sawa. Ni wazo zuri.”
“Jelini yuko wapi?”
Ezra akauliza. “Nilimuacha chumbani! Nilipoona muda unakwenda hanipigii kama nilivyomwambia
akiwa tayari anipigie, nikajua amenisahau. Ndio maana tukaja huku moja kwa moja.
Lakini nilimuacha muda tu anaingia kuoga!” Ezra akampigia. Simu zake hazikuwa
hewani. Akakimbilia chumbani kwake akiwa na funguo za ziada alizokuwa nazo
Emelda.
Aligonga mara moja na
kufungua. Hakumkuta hapo chumbani, akajua yupo bafuni. Akagonga kidogo. “Jelini?
Upo sawa?” “Nakuja sasahivi. Nipe kama dakika 10 tu. Samahani nimechelewa.
Nakuja sasahivi.” “Basi nakusubiria hapo nje ya chumba.” “Sawa. Sitakawia.
Samahani.” “Usijali.” Ezra akatoka.
Baada ya muda akatoka
Jelini ambaye hata hakuwa amejitengeneza kama kawaida yake. Halafu ametulia
isivyo kawaida yake. Ezra akamtizama, akahisi kuna kitu hakijakaa sawa. “Kwema?
Mbona kama umekosa raha?” “Nahisi ni uchovu wa safari tu. Ila nipo sawa.” Kwa
mara ya kwanza akamdanganya. Ezra akamtizama, akajua ni zaidi ya hapo,
ila akamuacha tu wakielekea walipo wengine.
Wakatafuta meza na
kukaa, kila mtu akaagiza chakula chake, Emelda akamsaidia mama yake kuagiza
chakula na kinywaji. Maana alimjua, asingeweza kuchagua hapo mbele ya watu
halafu vishakuwa vyakula vingi sana. Hajui chakufanya na hiyo menu. Akamsaidia kuchagua,
muhudumu akiwa anandika. Yeye Jelini akaomba tu juisi akisema bado anajisikia
kushiba sana. Kwamba alikula nyama nyingi kuliko wao huko njiani, kisha
akatulia.
Kwa kuwa yeye ndio
mara zote anawafanya wote wazungumze. Kama changamsha genge, na kwa kuwa
akawa amepoa kuliko kawaida yake, akafanya wote watulie. Pale pakawa kimya.
Na yeye akawa amepotea kabisa kimawazo. Ezra akamuona hayupo pale kabisa.
Akajua kuna kitu hakipo sawa.
Vyakula vikaletwa.
Kila mmoja akapata chake, wakaomba na kuanza kula. Jelini bado yupo mbali
kabisa. Ezra akamtingisha kidogo kama kumrudisha pale. “Naomba tule wote hiki
chakula. Wameweka nyama nyingi.” Ndipo kuangalia, akagundua chakula
kilishaletwa pale. Akatoa tabasamu la kujilazimishia. “Utashangaa mimi
niliyesema sisikii njaa ndio nakula kukuzidi wewe.” “Usijali. Kipo kingi na
tusipotosheka nitaongeza kingine.” Wakaanza kula pamoja. Angalau wakamaliza kwa
amani hapo.
Kabla hawajaagana
kwenda kulala, maana walikuwa wakidamka tena alfajiri sana kurudi jijini. Walipomaliza
kula, wakamuomba Mungu kwa pamoja, ndipo wakatawanyika. Jelini hakutaka
kujichelewesha kabisa. Akaaga yeye wa kwanza kuwa anawahi kulala. Ezra
akamsindkiza mpaka chumbani kwao, ili kupata naye muda kujua kulikoni.
Wakawaacha kina Emelda na Junior.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Kuna nini Jelini?
Mbona umekosa raha gafla?! Tumekuboa?” “Hapana Ezra! Hakuna chakuniboa. Nahisi
nimechoka tu. Acha nilale, nikiamka naamini nitajisikia vizuri. Wala usiwe na
wasiwasi.” “Kama kungekuwa na tatizo, ungeniambia?” Ezra akamuuliza tena
ila safari hii swali la moja kwa moja kama aliyehisi anamficha kitu.
“Ningekwambia Ezra! Tafadhali usiwe na wasiwasi.” Akamtizama kwa kutoridhika.
Hapakuwa na mazingira aliyoweka ya kutaka mikono wala kiss kama
alivyomzoea. Na yeye hakutaka kulazimishia. Akamuaga na kumuacha alale. Lakini
mpaka anapotelea usingizini, Emelda alikuwa hajarudi hapo chumba.
Safarini Kurudi Dar.
Safari ya kurudi Dar
ikaanza. Safari hii Junior na Ezra walikaa mbele. Hakuna kukumbatiwa. Jelini
akabaki amepoa hapo viti vya katikati alipokuwa amekaa na Emelda pamoja ma mama
yake. Mateo alikaa nyuma kabisa. Kimya mpaka Ezra akamgeukia. Akamkuta ametulia
kimya anangalia nje, hajalala.
“Usingizi?”
Akamuuliza. Akatingisha kichwa kukubali. Akamuomba Mateo aliyekuwa amekaa nyuma
yake ahahamie kiti kingine. Akamwambia arudishe kiti nyuma, alale. Bila ya
maneno mengi. Akajinyoosha na kujifunika, hapohapo akalala.
Waliendesha mpaka
nusu ya safari, wakasimamisha gari. Wakanunua tena chakula ili wakale ndani ya
gari, wakaongeza mafuta ya gari, Junior akasema hajachoka, anaendelea
kuendesha. Safari ikaendelea. Jelini akala na kurudi kulala.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa amelala tena,
wanakaribia jijini. Pochi ameweka katikati ya miguu. Ikaanza kunguruma, kama
kuna jumbe zimeingia. Ikanguruma kila mtu akasikia maana kulikuwa kimya haswa.
Wote walikuwa wamelala kasoro Junior na Ezra. Waliweka mziki kwa sauti ya
chini. Kwa hiyo simu yake iliweza kusikika ikinguruma pochini.
Akavuta kiti ili akae
wima. Akaokota pochi katikati ya miguu yake kwa haraka ili isiendelee kunguruma
na kusumbua. “Samahanini.” Akanong’ona akiomba msamaha kwa waliokuwa wamelala.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ilikuwa simu ya
kwanza, Colins aliyotumia kumpigia, sio ile aliyomtumia ujumbe usiku uliopita.
Ikawa kama anamwambia popote ulipo, nakuona na kukufikia maana alimtumia picha
walizokuwa na Ezra nje ya hotel siku ile ya jumamosi, ufukweni, alipokuwa
akimbembeleza baada ya kupishana na mama yake, alipomtoa Jeremy arudi nyumbani.
Mama yake alimuacha akiwa
hayupo sawa. Ezra akabaki akimbembeleza. Akapata na denda la muda mrefu
tu mpaka akamtuliza. Basi hizo picha zikatumwa hapo na kumshitua sana Jelini. Zilionekana
kwa vizuri tu, kama mtu aliyewapiga picha kwa karibu kabisa. Jelini akashangaa.
Maana walikuwa sehemu ya kuegeshea magari. Jua lilishazama mida hiyo lakini
bado kulikuwa na mwanga kiasi, lakini hakumuona mtu ambaye alikuwa hata na
dalili ya kuwapiga picha!
Ujumbe nao ukaingia. ‘Naumia, sina jinsi ya kufanya. Najiuliza na kusononeka kama
na yeye umempa ahadi kama zangu!! Na je, kwake unapatwa na hisia kama
zile ulizoniambia unapata ninapo kukumbati na kupata midomo yako!! Najiuliza
usiku kuchwa, nakushindwa kuamini, Jelini wangu! Yupi ana viapo vyako
vya kweli, na yupi amedanganywa!’
‘Maana
ninachojua mimi, mapenzi ya kweli, huvumilia. Haijalishi muda Jelini.
Mimi ningekusubiria kama nilivyokusubiria kwa Kasa bila ya kuchoka, japo maisha
yako na wewe yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Na nilijua mpaka huwa ulikuwa
ukihamia kwake siku za weekend. Lakini nilikusubiri Jelini. Tena
nilisubiri bila ya kukukatia tamaa. Nikijua wewe ni wangu tu. Na kwa kuwa nina
mapenzi ya dhati na wewe, sikuhesabu mabaya japo nilishuhudia maisha uliyokuwa
ukiishi na Kasa. Nilikusubiri Jelini. Wewe uliwezaje kunikatia
tamaa!?’ Gari
zima lilikuwa kimya wakati akisoma jumbe zake. Ezra akamgeukia kama kusoma
sura.
Kabla hajairudisha
simu kwenye pochi, Ezra akamuwahi. “Na mimi naomba kusoma.” Jelini alishituka,
akaanza kutetemeka. Akashindwa kujibu, midomo ikitetemeka, akitafuta neno
sahihi la kuzungumza na kushindwa. Ikawa kama amefumaniwa! Ezra akageuka vizuri
na kunyoosha mkono kabisa, kama anayepokea. Jelini akabaki amekufa ganzi.
~~~~~~~~~~~~~~~
Usiku uliopita
alimwambia Ezra, ni uchovu
tu! Leo anataka kusoma jumbe! Inamaana mwishoe atagundulika
kuna mawasiliano ya siri yanayomnyima raha, yanaendelea. Kwamba Jelini yu majutoni tayari!
NI
NINI KITAENDELEA?
-
Je, Jelini atatoa simu, siri ifichuke? Au atakufa na
tai shingoni?
-
Je, ng’ang’ania ya Colins imefanikiwa kupenya moyoni kwa Jelini na kumkumbusha
penzi la kale?
-
Nani atafanikiwa
kumuingiza Jelini kanisani?
Au ataishia kama mama zake kitu alichokwepa Jema kwa garama zote?
-
Junior naye amekusudia kumuoa Emelda, kipingamizi Hope amepokea chake
nakuonekana ni kama ameridhika
nakutoelewa uchochezi wa wifiye. Uchumba wa
Junior & Emelda ukitangazwa?
- Edwin aliyeliwa vyake kwa muda
mrefu Je?
MENGI
MAZITO YANAENDELEA.
0 Comments:
Post a Comment