Kimya. Naye Ezra akabaki amenyoosha mkono akimtizama usoni. “Jelini?”
“Jelini?” “Ndiyo.” “Kwenye simu zote mbili au simu moja tu?” Akashindwa kabisa kujibu. “Unaanza kunitia wasiwasi Jelini!” “Ni simu zote.” Akajibu kwa haraka. “Ila sasahivi imeingia kwenye simu moja. Inamaana huo mwingine uliingia muda gani?” “Nilitaka tukifika nyumbani ndio tuzungumze vizuri. Sio kuzungumza wimawima. Na jana usiku ulisema mnataka kuwahi kulala. Sikutaka kukuchelewesha kwa kuanzisha mazungumzo ambayo pengine yangechukua muda mrefu.”
“Muda wangu wote uliobaki hapa duniani, nimekupa wewe Jelini. Na wewe unajua. Wewe ni furaha yangu. Wewe ni dharula yangu ya kwanza. Wewe ni kipaumbele changu. Wewe ni kila kitu changu. Inapofika kwenye kuchagua chochote, wewe kwanza.” Jelini akashindwa hata cha kujibu.
“Nakupenda. Na maisha yangu yapo wazi mbele yako. Sitaogopa kusema, na sitakuficha kwa yeyote yule. Linapofika swala lolote linalokuhusu wewe, kila kitu kitasimama kwa ajili yako. Si mchana, si usiku. Unanielewa?” Jelini akatingisha kichwa kukubali na kumkabidhi simu ya kwanza. Akaipokea na kurudi kukaa vizuri ili asome.
Kisha akatoa simu ya pili. Akamgusa nayo kwenye mkono pale alipofikia. Akageuka. “Hii ni jana usiku.” Akamkabidhi simu ya pili. Ezra akawa na simu zote mbili. Kimya kwa abiria wote, hata Junior safari hii hakuingilia. Akawa kama Emelda tu, ndugu mtizamaji na msikilizaji. Maana ni kama Ezra alibadilika kabisa na hakutaka kusubiri wakazungumze kwa faragha kwanza. Akaonyesha wazi hataki kuchezewa, awekwe wazi kieleweke. Palepale ndani ya gari, mbele hata ya wageni! Junior akaendelea kukanyaga mafuta.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akamuona Ezra amesoma mpaka akabadilika sura. Akatulia kimya kabisa akiangalia nje ya gari. “Umenikasirikia Ezra?” Jelini akauliza kwa upendo ila sauti ya hofu. Ezra akavuta pumzi kwa nguvu na kunyamaza. Kimya. Na yeye akaamua kunyamaza. Kimya gari nzima hakuna aliyemuongelesha mwenzie na hapo bado Ezra alibaki na simu za Jelini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Walipofika Tegeta, Jelini akamuomba Junior amshushe aende dukani kwake akaangalie mambo yanavyokwenda. “Nilifikiri tunakwenda wote nyumbani!” “Acha mimi niishie hapa. Nimalizie nao kazi na kufunga mahesabu. Tutawasiliana.” Akaonyesha ni lazima ashushwe. Mpaka hapo hakuwa amejua msimamo wa Ezra kwani alikuwa kimya tokea asome zile jumbe. “Basi acha nikupeleke mpaka dukani kuliko kukushushia hapa barabarani.” “Asante, japo kwa hapa ni kama nimeshafika tu.” Junior akasisitiza mpaka akamfikisha. Akashuka na Ezra naye akashuka.
Akamfungulia nyuma ili atoe mzigo wake na kumkabidhi simu zake. “Ulinidanganya Jelini!” Alipofunga buti na kujiridhisha wapo wenyewe, ndipo akamwambia. “Najua. Na samahani. Ila yote nafanya kwa sababu nakupenda Ezra. Nahofia kukupoteza.” “Lakini si kwa kunificha!” “Nakuahidi kurekebisha. Nitatengeneza mimi mwenyewe.” “Unatengenezaje!?” “Kwa kutokimbia kivuli changu. Acha nitengeneze kwanza, ndipo nikutafute. Lasivyo nisipoweka kikomo, tutafika pabaya zaidi ya hapa tulipoishia leo. Mimi najua ninachozungumzia. Muwe na usiku mwema.” Akachukua sanduku lake na kuondoka bila ya kugeuka nyuma. Wao wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alivyotulia tu baada ya kupitia kila kitu hapo dukani, akabaki akiwaza jinsi alivyoachana na Ezra. Alijua hayupo sawa, ameshatibuka na anamlaumu kwa kumficha. Na jinsi anavyomjua Colins, akajua hatatulia mpaka kweli wakutane. “Ni kweli siwezi kukimbia kivuli changu mwenyewe.” Jelini akawaza akimfikiria Colins. Na akajua mwisho wa yote, ni kumkorofisha kabisa Ezra, na kuishia pabaya zaidi. “Bora ni rekebishe ndipo tuendelee na Ezra. Nikilazimishia hivi, nitampoteza kabisa.” Akiwa na hisia za hofu akaendelea kupanga hili na lile, na kuchukua maamuzi mwenyewe.
Akamtumia ujumbe Colins. ‘Naomba tukutane usiku wa leo.’ Akamtajia hoteli ambayo alifikiri ni wazi na salama kwake. Bila ya kuchelewa, Colins akajibu. ‘Nashukuru Jelini. Nakuahidi sitachelewa.’ Jelini akarudi nyumbani. Akamkuta mwanae. Akazungumza naye na kumpigia simu mama yake.
Akamwambia wamerudi kutoka safari, ila atatoka anakwenda kukutana na mtu sehemu. “Kuna jambo lazima nirekebishe kabla sijaendelea kuharibu.” “Ni nini tena!?” “Acha nirekebishe kwanza, ndipo nitakwambia. Ila sitachelewa kurudi.” “Sawa. Ila naomba umakini Jelini mama yangu mzazi. Tusianze tena hekaheka. Maana tumepumzika kwa muda mrefu kweli! Naomba tusianze tena.” “Nimebadilika mama jamani! Sio mambo mabaya.” Hapo akawa ameshaanza kukasirika. Mama yake akajua. “Mbona husemi sasa, unasema nusunusu tu?” “Nikirudi nitakwambia, ila sio sasahivi. Na usianze mama.” Akaweka msisitizo, mama yake akaona amuache. Akaanza kujiandaa.
Colins&Jelini
Mida ilipofika akatoka Jelini aliyependeza haswa. Akaendesha mpaka nje ya hiyo hoteli, akatafuta sehemu ya kuegesha, akaegesha gari yake na kumpigia simu Colins. “Umefikia wapi?” “Nilishafika. Nipo ndani nakusubiria.” Akamuelekeza upande aliokuwa amekaa. “Basi na mimi nakuja.” Giza lilishaingia nje. Akajivuta taratibu mpaka ndani.
Wakati anaingia ili kufikia sehemu aliyomwambia yupo, ilikuwa lazima kupita sehemu ya kuogelea ambayo jioni hiyo wengi hupenda kukaa kuzunguka hayo mabwawa wakiwa kwenye meza zao wakila na kunywa.
Sasa wakati akipita ni kama moja ya meza alimuona Kemi na Love wakiwa wamekaa na watu wengine. Akashituka sana ila akapita bila kuendelea kuwatizama. Lakini sauti zilikuwa zao kabisa wakiwa na wanaume pia kwenye meza yao. Ila macho ya wanaume wengi yalimpokea na kuwa yakimsindikiza mpaka akapotelea sehemu ya pili ambako ni kama Colins alijitenga na makundi ya watu. Mwishoni kabisa mwa hoteli, karibu na baharini. Mida hiyo mawimbi ya bahari tu ndiyo yaliyokuwa yakisikika eneo hilo alilokuwa amejitenga.
Alimkuta amekaa peke yake, mwisho kabisa na meza chache zilizokuwa upande huo. Patulivu sio kama kule alikowapita kina Love. Alisimama alipokuwa akimsogelea. Japokuwa hakuwa amerudisha mwili kabisa lakini alipendeza na kuvutia. Vile alivyo mweupe, halafu akavaa nguo nyeupe tupu mpaka kofia nzuri sana ya rangi hiyo, ikamkaa vizuri. Ndevu zilishaota. Zikatengenezwa kwa ustadi. Katikati ya weupe wa ngozi yake na mavazi meupe, zile ndevu nyeusi zilimpendeza na kumfanya avutie zaidi.
Jelini akatabasamu kwa kuridhika alipomuona vile. “Naona umepona kabisa.” “Mwili bado kidogo. Ndio maana sizembei mlo hata mmoja. Hapa nishamaliza kikombe kikubwa cha maziwa. Nilikuwa nikikusubiri tuagize wote chakula baada ya mimi kupata supu.” “Hata mwili haunekaniki vibaya. Na umependeza na kofia pia.” “Naficha kipara.” Wakakaa.
Wakabaki wakiangaliana. Jelini akacheka na kuinama kama anayefikiria. Akaja muhudumu. Akaagiza juisi ya embe. Na Colins yeye akataka aletewe supu kwanza kabla ya chakula. Muhudumu alipoondoka, Jelini akaanza. “Nimekuja kuitika wito.” “Nakushukuru.” Akaanza.
Upande Wa Colins.
“Unakumbuka siku ya mwisho ulikuwa umenisamehe ukanikaribisha nije kwako siku inayofuata?” “Nakumbuka.” “Usiku uleule James alipomiambia umenisamehe nikataka kuja angalau kukuona. Lakini James akanikatalia na kunishauri nisubiri mpaka kesho yake, nisije vile nikiwa dhaifu.” Jelini akakunja uso.
“Nilikuwa kama mgonjwa Jelini! Chakula hakipiti kwa sababu ulinikasirikia. Nikadhoofu sana. Kufupisha habari ndio ukakubali tukutane na ukamwambia James hata wewe ulishapatwa na hamu na mimi. Ndio tukakubaliana kesho yake nije kwako tokea asubuhi. Lakini Jelini, nilishakuwa nimepanga na James hatua za kukuchumbia ili nikuoe kwa haraka.” Jelini akawa haamini.
“Najua sasahivi itakuwa ngumu kuamini, lakini muulize James. Nilishamwambia anisaidie kupanga harusi kabisa. Na ilikuwa baada ya kuzungumza na wewe siku ile, juma lilelile nikatafute pete nikuvalishe, nije kutoa mahari…” “Unatoaje mahari na wazazi ambao walikuwa hawanitaki?!” “Nilishapanga nikuoe, wao waje kuungana na sisi baadaye hata kama ni baada ya miaka 20. Sikutaka kuwasuburi wakubaliane na mimi ndio nikuoe. Nilijiambia tutajua baada ya safari, lakini sisi lazima tuone. Na hata James atakuwa shahidi yangu katika hili.”
“Nakumbuka kwa mara ya kwanza nikaweza kulala vizuri nikijua kesho yake nakuja kuonana na wewe, tuwekane sawa, yaishe tuendelee na ukurasa wetu mpya. Na nilipanga niachane na ratiba zote za wazazi tubakie sisi tu na maisha yetu, kwani hata nyumba nilishamaliza kuikarabati na kupandisha ukuta wa kujitenga na nyumbani kwa wazazi.” Kinywaji kikaletwa. Jelini alipenda sana juisi ya pale na yeye Colins akaletewa supu yake.
Akaanza kuinywa hiyo juisi bila ya kuichelewesha. Colins akaendelea baada ya kuagiza chakula alichoomba kifike baada ya nusu saa, Jelini yeye akaomba aletewe tena juisi ileile wakati anamletea chakula. Hakutaka kula chochote zaidi ya hiyo juisi tu.
“Sasa asubuhi yake ukumbuke ilikuwa siku ya jumapili. Familia huenda kanisani. Wakati nataka kutoka mlangoni, wakanivamia wazazi wangu, Love, Kemi Kasa na huyo mtumishi wao. Nikawaambia kama kuna kikao, kiendelee wakati mwingine, mimi nina haraka. Ikawa kama kuna kuvutana. Mashitaka yaleyale juu yako, hakuna jipya. Ila msisitizo ikawa ni kwamba wewe umeniloga, lazima niombewe, nikombolewe.” Jelini akabaki akisikiliza tu.
“Kukazidi kuvutana. Mimi nikiwaambia sina shida ya hata kama umeniloga, waniache. Wazazi wakalazimisha maombi. Ukazidi uvutani usioisha. Mwishoe mama akanisihi akisema, maadamu yule mtumishi yupo pale, sio vibaya kufanya maombi ya pamoja. Nikaona waniombee tu ili kwanza mama aridhike wajue mimi sina mapepo na pia niokoe muda, wanipishe nije kwako. Yakaanza maombi. Kumbe yule hakuwa mtumishi, ni mganga tu. Mwishoe akanifunika kitambaa usoni, kuanzia hapo ufahamu ukapotea kabisa mpaka siku naombewa na wewe ukiwepo. Mengine yote ni kama ndoto.” Jelini kimya.
“Kwa hiyo ndio hivyo.” Akaweka msisitizo akitaka kumsikia Jelini. “Jelini?” “Pole Colins. Pole sana.” “Unajua sicho ninachotaka kukusikia. Nilitaka uusikie na upande wangu pia, ujue nilikuwa na malengo juu yetu, ila wamenikatili vibaya sana.” “Naomba na wewe unisikilize Colins na ukumbuke. Haya yaliyotokea kwenu ni muendelezo wa visa vilivyokuwepo kwenu tokea zamani. Hakuna jipya.” “Kweli Jelini!?” “Niambie jipya ni lipi Colins! Sema walichobadili ni njia ya kukuzuia tu. Au wewe umesahau?!” Jelini akawa ametulia tu.
“Sio watu hawahawa wanakuja na sababu zilezile za sisi kutokuwa pamoja ila kwa njia tofauti tofauti?” Akaendelea. “Sio wazazi hawahawa walifanikiwa tokea mwanzo, kukuchagulia kwenda kwa Love usije kwangu niliyekuwa nikikusubiria? Na ulitii. Kwani pale ulikuwa umeharibiwa akili?” “Hunitendei haki Jelini!” “Si ubishe! Maana ndio watu haohao, ukiwa na akili zako timamu, si ndio walikuzuia tena usinisindikize hospitalini nikaishia baa na kina dada Doro! Sasa kilichobadilika ni nini kama si mbinu tu ila watu ni walewale, sababu ni zilezile ambazo huwa unarudi nazo na mimi nakusikiliza, tunaendelea.” Kimya.
“Na unaposema nimeshindwa kukusubiri, ni lini na wapi!? Na hebu niambie kwako natakiwa kuwa nakusibiri mpaka lini? Maana huu mchezo si wa mara moja na wala hauna dalili ya kuja kuisha. Leo tumekaa hapa, mwanamke wako naye amekaa pale nje!” Colins akashituka sana. “Haiwezekani Jelini!” “Sina sababu ya kusingizia maana mimi sinufaiki kwa chochote ila kuishia kuwa muhanga wakati wote.”
“Mbaya zaidi yupo na Kemi ambaye alishafanya jaribio la wazi kabisa la kutaka kuniua!” Akazidi kumshitua Colins. “Kivipi?!” “Sikutaka kusema. Ila kwa kuwa naona bado wananifuata na kunichafua kila mahali yeye na Love, japo Kemi nilimsamehe hata Kasa alipomtuma mwanasheria wake, mimi nilikubali yaishe. Lakini Kemi ndiye aliye niumiza hapa kichwani kwa kunitega kwa mguu kwa makusudi.” Colins alizidi kushituka.
“Halafu alivyo mshenzi, aliponiumiza akajua baba yake atamkamata, akamtafuta kaka yake kwa haraka ili aingie kwenye security camera za kwenye ile kampuni ya baba yake kufuta like tukio kwa haraka ili baba yake asimkamate. Na kweli Kevin alifuta. Lakini Kasa anaakili ya haraka sana. Akawahi lakini akaambiwa na mfanyakazi wake kuwa ilishafutwa. Yaani hicho kipande kwa muda huo mzima kuanzia naingia ofisini kwao gorofa ya juu mpaka naondoka, hakipo. Yaani ikawa siku ile ni kama mimi sikuwepo kabisa pale kwenye ofisi ya baba yao. Bila yakupoteza muda alimpigia Kevin huyohuyo na kumwambia airudishe kwa haraka sana.”
“Kasa aliwaadhibu wote wawili kwa vile alivyo amua yeye, ikiwemo kumfukuza kazi Kemi. Na pia kutaka Kemi aniombe msamaha. Lakini mimi nilisamehe kwa kuwa Kasa alikuwa upande wangu! Tofauti na wewe Colins. Kasa hakuwahi kuruhusu mtu wala kitu kituingilie mpaka aliposhindwa mwenyewe na bado anasema kuwa Kemi huyuhuyu alimpa madawa ya kumlevya, akaishia kulala na yule mwanamke. Sasa Kemi huyuhuyu ndiye ameungana na Love mpaka amemfanikishia na kwako, kwa kufika umbali mkubwa sana.”
“Kuwa na ubinadamu Colins, kweli ulitaka mimi nibaki kwenye mahusiano ya namna hii. Mimi na wewe, mpaka lini?” Kimya mpaka Colins akabadilika sura. “Kuwa tu mkweli Colins. Wewe ulitaka mpaka nini kitokeee ndipo uridhike? Kifo changu? Maana Colins, ni walewale waliokuwa wakikusababishia tokea mwanzo, na kujawahi kuwashinda, nikafanikiwa mimi kukupata wewe! Haijawahi tokea hata mara moja Colins! Wakati wote wewe unasababishiwa na kushindwa!”
“Sababu ni zilezile! Kweli unataka niache mahusiano yakueleweka, turudiane, halafu tuendeleze mchezo uleule!?” “Nitakuwa makini, na safari hii hata wazazi nimeshawaweka sawa.” “Kwa kufanyaje? Tafadhali niambie tu. Maana kwa upande wa Love tu, yupo hapa tulipo na shoga yake. Sijui kama amekufuata au imetokea tu! Hatujui maana mimi ndiye niliyechagua hapa. Ana jinsi gani yakujua ulipo, mimi sijui!”
“Haya, tukija kwa wazazi wako, niambie kile kitakachobadilika. Maana walikuja nyumbani wakamtusi mama yangu na mimi kwa wazi kabisa. Neno kwa neno kama ambao walikuwa na hoja wameandaa kuja kuwakilisha. Mbele ya mtoto wangu aliyekupenda sana Colins, na bado Jeremy alikuwa akiamini lazima utarudi. Akaacha zile treni akitaka mtu asiziguse mpaka siku utakayorudi akuonyeshe. Siku wazazi wako na bibi pamoja na babu yako wanakuja kututusi, ilimsumbua Jeremy, alikuwa haelewi, anakazi yakumuuliza bibi yake bila ya kuridhika.” Hapo Colins alikuwa mwekundu kupitiliza.
Na yeye Jelini akaendelea taratibu tu. “Sasa unaposema utadhibiti wazazi wako, na donda mlilomwachia mama yangu na mwanangu? Kwamba leo ndio nikukimbilie, nimuache mama ambaye wakati wote hubaki na mimi wakati wewe ukiwa kwenye sababu zako kama hizi! Kweli Colins?!”
“Haya, tufanye nakurudia, wewe unauhakika gani kwamba hao uliowataja au unao watajaga wakati wote, hawatarudia tena!? Unasema utakuwa makini. Kwa njia gani ambayo ilikushinda mwanzoni sasahivi uweze!? Tafadhali niambie Colins.” Kimya.
“Au basi niambie, ili niwe kweli ninakupenda, ni mpaka uone nakufa kwa ajili yako ndipo uridhike na kusema ni kweli nilikupenda!?” Kimya, Colins kawa mwekundu haswa. “Umeondoka karibia mwaka! Nimekusubiri Colins. Muulize shem. Tena kwa kujikana haswa huku picha zako na maisha yako yakianikwa kwa makusudi! Lakini mimi nilikusubiri nikiwa na msamaha wako!”
“Huyu Ezra nilishamkataa mwanzoni nikiwa nakusubiria wewe, na hata yeye nilimwambia. Sikutaka nijichanganye ili usije rudi, ukanikuta tena na mtu. Muulize Ezra kama utaweza. Nilimkataa kwaajili yako Colins. Nilikaa nikikusubiri muda wote huo kwa mateso na upweke mwingi mno! Sasa kweli ulitaka nisubiri mpaka nizeeke kabisa, halafu waje waniambie siwezi kuzaa ndipo uridhike? Maana wewe unaweza kupata mtoto hata ukiwa kikongwe! Unaweza kuoa hata ukiwa na miaka 70. Lakini sivyo kwangu!”
“Mimi si msichana mdogo kusema nina muda bado! Nishazaa, na umri wangu umekwenda Colins. Kweli unataka mwenzio bado niendeleze mchezo wa kukusubiri tu kila wakati ukija na sababu tofautitofauti!?” “Safari hii tunaoana kabisa na kuanzisha familia.” “Halafu ndio inakuaje?! Eti Colins? Huu mchezo wa kusabahishiwa na hao watu wako ukija kuendelea huko kwenye ndoa? Unapotea tena, unaniacha na mimba, unakuja kurudi na sababu zako kama hivi, hapo mtoto pengine ana mwaka. Unasababishiwa tena, unapotea tena.”
“Halafu mleaji ni nani? Kama si mimi mwenyewe na mama yuleyule ambaye hanichoki! Na ambaye wazazi wako walishamtusi! Sasa ndio eti anabaki kunisaidia kulea watoto ulioniachia, ukiwa wewe unaendeleza maisha huko walipo kukusababishia kuniacha! Maana wazazi wako hawataki hata kunihisi mimi na mtoto ambaye wanasema nilimzaa mtaani tu! Na hayo nayo waliyasema siku ile walipokuja nyumbani, mbele ya ndugu zangu, akiwepo na Jeremy mwenyewe! Tena bila hata huruma kwa mwanangu!” “Samahani sana Jelini. Samahani kwa hilo.” “Itasaidia nini sasahivi? Niambie ukweli Colins. Itamsaidia nani? Sio wewe uliyeyasema hayo! Hata ukiomba msamaha, haibadilishi ukweli. Bado nabakia Jelini yuleyule mwenye historia mbaya ya nyuma, na siwezi kubadilisha. Nina mtoto nilizaa nikiwa shuleni ambaye hata wazazi wako wanajua ni umalaya tu. Nimeishi baa. Siwezi kubadilisha hayo!”
“Lakini huko nilipokwenda, nimepokelewa Colins. Makosa yangu ya zamani, eti wanasema ndio nguvu yangu ya sasa. Napendwa na kuheshimiwa bila manyanyaso! Sasa kweli Colins unataka nitoke huko, nije tuanze tena mchezo uleule! Ni lini tutaweka kikomo? Au ndio mpaka wewe useme? Mimi natakiwa nitulie tu mpaka uamue wewe?!”
Kisicho Ridhiki, Hakiliki.
Chakula alichoagiza Colins kikaletwa pamoja na juisi ya embe aliyoagiza Jelini. Wakati muhudumu akimpangia Colins chakula chake, Jelini akachukua ile juisi iliyoletwa. Alipokunywa kama funda mbili tu hivi na kutulia, akaanza kusikia tumbo linavuruga. Akaona aende chooni maana ilikuwa embe! Akajua imeshalainisha kila kitu humo tumboni, ajiwahi.
Chakula alichoagiza Colins kikaletwa pamoja na juisi ya embe aliyoagiza Jelini. Wakati muhudumu akimpangia Colins chakula chake, Jelini akachukua ile juisi iliyoletewa. Alipokunywa kama funda mbili tu hivi na kutulia, akaanza kusikia tumbo linavuruga. Akaona aende chooni maana ilikuwa embe! Akajua imeshalainisha kila kitu humo tumboni, ajiwahi.
Akiwa anatembea hali ikazidi kuwa mbaya. Ikabidi akimbie kabisa watu wakimwangalia mpaka Colins akashituka. Jasho jingi likaanza kumtoka ndipo akajua sio embe linalomvuruga, kuna LAZIADA.
Akajua kuna mchezo ameshachezewa. Haikuwa hali ya kawaida. Kwa haraka sana akampigia simu Ezra. Na yeye akapokea kwa haraka kama aliyekuwa ameshikilia hiyo simu mkononi, maana iliita mara moja tu na kupokelewa. “Nisaidie Ezra. Nahisi nimepewa sumu kwenye juisi ya embe. Nipo hoteli.” Akamtajia. “Sio mbali na kwako. Hapa nakimbilia chooni, najifungia kabisa wasije nidhuru zaidi, lakini natokwa jasho jingi, tumbo linavuruga.” Kisha simu ikakatika kitu kilichomtia hofu zaidi Ezra. Maana aliita mara kadhaa. “Jelini! Jelini? Jelini?” Kimya.
Huku kwa Jelini akaingia chooni na kweli akajifungia na kukaa chooni. Alihara kama bomba. Wazo la haraka la kujitapisha ile juisi likamjia. Akajiingiza vidole makusudi ili kutapika ile juisi yote. Akawa na kazi ya kutapika huku jasho likiendelea kutoka kama aliyekuwa akimwagiwa maji! Baada ya muda akaanza kuona ginza, kizunguzungu, akaanguka na kuzima kama mshumaaa.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mapenzi&Pesa!
Kuna Wasiokubali Kushindwa, Kufa Kupona.
Mwisho wa Jelini ni Upi? Utabiri wake mwenyewe umetimia?
0 Comments:
Post a Comment